Simulizi : Sitaisahau Facebook
Sehemu Ya Tano (5)
John alikuwa ananiona? Nilijiuliza.Lile joto likazidi. Abiria wakashuka garini.Kuna kitu hapa!! Mapambano mapya!! Nikajisemea huku nikiendelea kumzuia John.John sasa akanizidi nguvu.Akanitoka. Akashuka chini. Nikajaribu kumkimbilia.Huko nikamkuta akiwa anafanya jambo la ajabu. John alikuwa anajarfibu kuisukuma gari kwa kuitikisa.Ajabu! Ikaanza kutikisika kweli. Mtikisiko ule ukawashtua wengi. Sasa vilio vikaanza kusikika. Kila mtu kuitetea nafsi yake.Watu wakashuka upesi kwa kugombania mlango. Basi likaanguka.Lilipoanguka John akatazama mahali. Na mimi nikageuza jicho kutazama. Yalikuwa makaburiMakaburi yaliyo na historia ya kushangaza. Makaburi ambayo yalimtoa nishai mchina alipojaribu kupitisha umeme juu yake. Umeme ukagoma kuwaka.Haya yalikuwa makaburi ya Kiyeyeu.Yalikuwa yanafuka moshi wa dhahabu!!Vita!!Mayowe yakatawala, akinamama wakiwa wamesahau watoto wao na wanaume nao wakiwasahau wake zao sasa kila mmoja alikuwa akiipigania nafsi yake. Sikuwa katika umoja na akina Jesca tena! Hapa sasa kila mwenye macho hakungoja kuambiwa tazama!!Makaburi yale mawili yaliendelea kufuka ule moshi wa rangi ya dhahabu.Wenyeji wa kijiji kile walikuwa katika taharuki kubwa sana huku wakizungumzia juu ya kukasirika kwa mizimu.Nani sasa aliyeikasirisha? Walijiuliza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Vilio vilisikika tena kutokea gizani. Watu wakakimbilia huko. Waliporejea ilikuwa taarifa ya mama mmoja aliyekuwa anakimbia ameshambuliwa na kitu kisichofahamika na hatamaniki tena. Amekufa!!Hali ikatulia kwa muda. Akajitokeza mzee mmoja wa makamo akitembea kwa kutumia mkongojo.Huyu hakuogopeshwa hata kidogo na hali iliyokuwa inaendelea. Alisimama mbele ya kundi na kuanza kusema anachokifahamu, alielezea historia fupi ya makaburi ya Kiyeyeu na majanga yanayotokea iwapo wazee wale waliolala katika makaburi yale wakikerwa na jambo. Hapa sasa akafikia kusema kuwa kuna mtu mmoja katika msafara alikuwa ameikasilisha mizimu!!Ni lazima abaki ili kuwanusuru wenzake. Kama akiendelea mbele basi litatokea balaa kubwa zaidi ya hili. Alizungumza kwa sauti ya juu na kila mmoja aliweza kusikia. Sauti yake na umri wake vilikuwa vitu viwili tofauti!!“Hivyo kama unajua una lolote la kuikera mizimu hii ni heri ubaki nyuma kuwanusuru wenzako.” Alizungumza kisha akatuachia mtihani wa kuamua aidha kujitokeza ama la!Maneno yake niliamini kabisa yalikuwa yanamlenga John. Nilijisikia uchungu sana, John alitakiwa kubaki nyuma. Yaani harakati zangu zote hizo zinaishia hapa!! Niliumia sana.Niliangaza huku na huko. Sikumuona John!! Nilitaka kumuita lakini niliamini kuwa hawezi kunisikia.Kimya kilitawala akisubiriwa mtu huyo ambaye ameikera mizimu aweze kujitoa kundini. Hakuna aliyejitokeza.Mzee akaendelea kusubiri!! Bado hakujitokeza mtu yeyote.Kimya kilikatishwa na sauti ya mwanaume akipiga mayowe. Tukageuka nyuma kumtazama. Alikuwa amejishika shingo yake huku akipiga kelele. Mara damu zikaanza kumtoka puani, masikioni na mdomoni. Badala ya kumsaidia kila mtu akawa anamuogopa!!Hatimaye akaanguka na kutulia tuli! Alikuwa amekata roho!!Kina mama wakapiga kelele sana, wanaume wakabaki kushangaa.Yule mzee wa kimila akaipaza tena sauti yake, “Kama asipojitokeza mtu huyu majanga yataongezeka. Mizimu inakasirika.”Sasa watu wakaanza kusemezana huku wakisisitizana kuwa mtu huyu ajitokeze ili mizimu itulie. Bado hakuweza kujitokeza mtu yeyote.Zikaanza kutolewa hirizi miilini mwa watu, lakini yule mzee wa kimila akapinga kuwa hizo ndio tatizo.Waliokuwa na dawa za kienyeji wakatoa. Bado haikuwa tiba.Kiza kinene kikatanda kama dalili ya mvua. Mwanga mkali ukamulika bila kutoa kelele. Watu watatu wakasalimia na ardhi.Ilikuwa radi!! Na walikuwa maiti tayari.Roho ikaniuma sana, nikajiona mimi ndiye muhusika. Nikatamani John atokezee nimtangaze kuwa ndiye chanzo. Lakini John hakuwepo tena!!Vile vifo vya radi ya ghafla vilimshtua kidogo yule mzee.Mara akabadilika sura na kuwa kama aliyekasirika!!Akatoa amri ya watu kujipanga msitari. Amri ikasikilizwa. Wanaume na wanawake mstari mmoja, mistari ilipopangwa ndipo nilimuona John. Na yeye alikuwa amepanga mstari. Akaanza kupita na kufanya kile anachokijua mwenyewe. Alimfikia John, na yeye akamuona akamshika mkono. Ina maana John anaonekana? Nilijiuliza.Nikiwa katika hali ya mashaka ya kila kinachoendelea. Mara yule mzee mkongwe alinifikia, alikuwa anatabasamu, mgongo wake uliopinda ulimfanya awe ameinama na kuwa mfupi sana!!“Shkamoo babu.” Nilimsalimia.“Marahaba mjukuu wangu.” Alinijibu kwa ukarimu sana.Kisha akanishika mkono.Alipofanya hivyo kwa wasafiri wengine hakutumia muda mrefu, lakini kwangu ni kama alitumia sekunde nyingi.“Unaitwa nani binti.”“Isabela!!”“Nani alikwambia unaitwa Isabela.” Aliniuliza huku akinitazama usoni.“Naitwa Isabela mzee.” Nilitaharuki kutokana na maswali ya mzee huyu.“Hilo sio jina lako binti.”“Sio jina langu?”“Na litakugharimu sana na kuwaumikza wengine katika maisha yako.” Kauli nzito za mzee huyu zilinishangaza.Isabela sio jina langu? Ni miaka zaidi ya ishirini tangu nipewe jina hilo. Sasa leo ananiambia kuwa hilo sio jina langu? Maajabu haya.“Hautaendelea na safari hii…kuwaepusha wenzako na mabalaa yasiyowahusu.” Alininong’oneza. Nikahisi ubaridi ukinipenya mwilini, mapigo ya moyo yakapungua kasi. Nikakata tamaa.Mimi tena? Sio John!! Maajabu haya.“Kama unao upendo waruhusu wenzako waende zao. Janga lako haliwahusu hata kidogo.” Alinisihi. Nikatikisa kichwa kukubali. Huku nikiamini kwa asilimia kadhaa kuwa tatizo ni John na yule mzee hajui kitu.Mzee akawatangazia watu kuwa tatizo limekwisha. Na kweli nilipokubali tu waondoke zao. Nilipogeuka makaburini. Ule ukungu haukuwepo tena.Abiria wakaingia katika basi lile la ziada lililokuja kutuchukua.Tofauti na mawazo yangu. Kuwa John atazuia basi lisiondoke baada ya yeye pia kuwa mmoja kati ya abiria. Haikuwa hivyo. Basi liliwaka vyema. Na kutoweka!!Ilikuwa usiku mnene lakini kinyume na taratibu za usafiri Tanzania, basi lile lilisafiri usiku. Hayakusikika malalamiko ya kubanana tena. Kila mmoja alitaka kutoweka eneo lile. Hata madereva na makondakta wote walikuwa waoga.Nilibaki na yule babu!!! Akina Samson, Jesca, na Jenipher walitaka kubaki na mimi lakini kwa maneno ya yule babu kuwa mzigo wangu hauwahusu. Niliwaruhusu waende zao huku nikiwapatia pesa nyingine ya ziada.“Nendeni mkautangaze ushuhuda huu popote pale. Msifiche hata moja lililotokea. Hata kama sitafika huko mtakapokuwa. Naamini sisi ni washindi.” Niliwaeleza. Wakalia kwa uchungu. Samson akagoma kabisa kuondoka lakini hatimaye alikubali kuondoka.Nilibaki na mzee yule tukizungumza. Alinieleza juu ya jina langu. Akadai kuwa hakuwa akijua nilikuwa naitwa nani lakini Isabela halikuwa jina langu.“Rejea nyumbani ukalitafute jina lako. Jina lako limepotea ama limefichwa. Na ukiendelea kuamini kuwa wewe ni Isabela basi maisha yako yatakuwa ya tabu sana. Utawatesa wenzako nawe utateseka sana.” Alinieleza yule babu.“Unaweza kwenda kupumzika nyumbani kwangu. Kesho upatafute nyumbani kwenu. Ukalitafute jina lako.”Tuliongozana na yule mzee hadi nyumbani kwake. Hapo tulipokelewa na mbwa wengi sana waliomlaki bwana huyu kwa furaha.Wahehe na mbwa!! Niliwaza.******Nililala katika mkeka. Ni kama nililala kwa sekunde kadhaa hatimaye pakapambazuka.Mzee akaniamsha, akanisihi sana nihakikishe Napata jina langu halisi na hapo nitaendelea na maisha yangu vizuri.“Jina langu ni nani?” nilijiuliza kwa sauti akanisikia.“|Hata mimi silijui lakini ni lazima ulipate ili kuzikwepa laana za ukoo wako. Fuatilia historia yako vyema mwanzo hadi mwisho. Historia ya kweli ipo kwa mama…kamuulize mama yako. Wewe ni nani? Lakini nakukumbusha kuwa wewe sio Isabela”Mzee alinisindikiza hadi njia ya mabasi.“Usizungumze na mtu yeyote, kwa usalama wako na abiria wenzako.” Alifanya kunisemesha kwa sauti hafifu. Nikamsikia na kumwelewa.Basi likapita. Nikapanda!! Mzee alinilipia nauli huku akichukua fursa ya kuzungumza na kondakta.Safari ya kurejea Makambako. Safari ya kwenda kulitafuta jina langu. Jina lililopotea.Kaka aliyekuwa pembeni yangu alikuwa anaongea maneno mengi sana. Lakini sikuwa namjibu chochote.Hatimaye tukaifikia Makambako!! Nikashuka garini nikaikanyaga ardhi ya Makambako kwa huzuni sana!! Hatua kwa hatua nikaanza kuelekea nyumbani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/SIRI SIRINIMwanamke wa makamo ambaye sasa mvi zilikikaribia kichwa chake chote alikuwa anafagia uwanja. Alikuwa akiimba nyimbo anazozijua yeye huku akionekana kuzifurahia. Nilimtazama kwa makini. Nikatamani ningekuwa nimekuja kwa mazuri huenda ningemshtua kisha tukacheka wote. Lakini nilikuwa nimekuja kwa mengine magumu sana.Huyu alikuwa ni mwalimu Nchimbi. Mama yangu mzazi.Nikanyemelea. Akashtuka akageuka.“Belaaa….Belaaa mwanangu.” Akautupa ufagio, akanikimbilia, akanikumbatia kwa nguvu. Joto lake likaupenya mwili wangu ulio dfhaifu. Nikaamini kuwa nilikuwa nimemkumbuka sana. Chozi likanitoka. Nikamkumbatia kwa nguvu zaidi.“Karibu mwanangu…mbaya wewe..yaani kimya kimya au uliongea na Suzi..wabaya sana nyie.” Alilalamika nikajilazimisha kutabasamu.Tuliingia ndani. Tukafanya mazungumzo ya hapa na pale. Hadi tulipokatishwa na nyimbo nyingine kutoka kwa mlevi. Huyu alikuwa baba yangu mzazi. Asubuhi sana alikuwa anatokea kilabuni.Sijui alilala huko? Nilimuuliza mama./“Hamna sema ameamkia huko.”“We Helena wewe…Aaah!! Suzy..ina maana haunioni uje kunipokea…si ku hizi hamsalimii watu!!” alizungumza kilevi. Macho yake hayakumwezesha kujua iwapo mimi ni Isabela.Akapita akiacha nyuma harufu ya pombe kali. Akaingia chumbani.Baada ya kelele za hapa na pale akasikika akikoroma!!!Nilijikaza sana na sasa nikaamua kumueleza mama kilichonileta pale nyumbani.“Mama hivi hili jina la Isabela ni nani alinitungia.”“Mbona wauliza hivyo mwanangu.”“Nipe jibu mama..ama ukoo wangu ni upi.”“We mtoto umekuwaje lakini.”“Nijibu mama.”“Mbona kila kitu kipo wazi..ukoo wako ni huu wa baba yako, na jina hilo ni mimi na baba yako tulikupatia.” Alinijibu.Niliondoka sebuleni nikaenda chumba cha wasichana nikajinyoosha. Nikapitiwa na na usingizi.Nilikuja kushtuka nikiwa na njaa kali.Nikaliendea jiko.Nikajihudumia vilivyokuwepo, kisha nikareje chumbani.Majibu ya mama yalikuwa hayajaniridhisha hata kidogo.Nitamuuliza baba pia!! Huenda kuna kitu anajua.Kwa nini aliniita Isabela.Nikasinzia huku nikiwa nimejiahidi hivyo kichwani mwangu.*****Asubuhi na mapema nilikuwa wa kwanza kuamka. Nilihitaji kumuwahi baba akiwa katika akili zake vyema kabisa.Kabla hajalewa!!Niliwahi na kujifanya naosha vyombo.Hatimaye nikasikia mlango wa chumbani unafunguliwa. Baba akatoka.“Aaah!! Bela mwanangu…lini tena umetuvamia wewe…umemaliza mitihani lakini.”“Nimemaliza..shkamoo baba….”`aliijibu salamu. Tukabadilishana mawazo na hatimaye kama kawaida yake akaniomba pesa.“baba kabla ya hilo…nahitaji kukuuliza kitu.”Alinisikiliza kwa makini, nikamueleza kile nilichomueleza mama. Baba alionekana kushtushwa na habari hiyo. Alijaribu kujiweka sawa lakini nilikuwa nimemsoma.“Fanya hivi…nipatie hiyo pesa nikirejea tutaongea ni stori ndefu kidogo..si unataka kujua maana ya Isabela na kwanini tulikuita hivyo..nifanyie kwanza nienda kupata supu kidogo.” Alijaribu kukwepesha mada.Niliheshimu maamuzi yake. Nikaingia ndani nikarejea na pesa kidogo nikampatia. Akatoweka.Moyoni nilipata matumaini makubwa sana!! Niliyaamini yale maneno ya yule mzee.Sasa mimi ni nani kama sio Isabela? Na kuna siri gani inazunguka hapa. Nilijiuliza. Wa kunijibu alikuwa ni baba.Nilisubiri sana. Hadi pale ilipokuja taarifa kuwa baba amekutwa mtaroni. Hana jedraha lakini haijafahamika bado kama anapumua ama amekufa!!Hii ilikuwa ni habari ya kushtua sana.Mimi na mama tukakimbia kuelekea hospitali ambayo tulielezwa kuwa amelazwa.Bahati mbaya zilikuwa mbio za kuwahi upepo.Baba yangu hatukuwa naye tena!! Kifo cha utata. Hakuwa amelewa. Alikutwa na ile pesa niliyompa.Hakika mimi sio Isabela, na kuna siri mzee wangu amekufa nayo!! Nilizungumza na nafsi yangu.Jina langu ni nani sasa? Na kwa nini waliniita Isabela?****Ulikuwa msiba wa mtu maskini hata utata ungegubika vipi bado angezikwa na kusahaulika. Ndivyo ilivyokuwa kwa baba yangu.Licha ya kifo chake kuwa na utata hapakuwa na la ziada alitakiwa kuzikwa.Msiba huu ulivuta watu wengi kiasi kutokana na jina la mwalimu Nchimbi ambaye ni mama yangu. Mwalimu!! Hivyo wanafunzi walijaa sana.Historia fupi ya marehemu ilisomwa.“….marehemu ameacha mjane na watoto wanne..mmoja wa kiume na watatu wa kike….Sebastian John, Suzan John, na Helena John.” Alimaliza kutaja majina ya watoto wa marehemu.Sauti za kuguna zukatawala ghafla, watu wakawa wanaulizana hao watoto wanne mbona hawajatimia? Kina mama wakashindwa kumezea wakauliza palepale.Ujumbe ukamfikia msomaji baada ya kijana mmoja kuagizwa.Msomaji akaanza kupekua hapa na pale. Kimya kikatanda!!!“Anaitwa Isabela John huyu hapa.” Shangazi yangu alipaza sauti akanitambulisha ili kuondoa ile sintofahamu. Nikanyoosha mkono juu. Watu wakageuka na kunitambua.Tendo lile la watu kugeuka kuniangalia likanifanya nipatwe na aibu kidogo. Inakuwaje mimi jina langu linasahaulika?Sikuuliza!!! Nikauchuna.“Kwa hiyo mtoto wa nne ni Isabela John….samahani sana kwa mkanganyiko huu.” Aliomba radhi yule msomaji. Waungwana hawakulalamika.Alipotaka kuendelea kusoma yanayoendelea katika risala hiyo akawa anatawaliwa na kigugumizi. Hali hii sasa ikaanza kuwakera watu. Lakini kabla hili halijapita akaanza kupiga chafya.“Samahani!” akaomba radhi tena.Haikukoma, ikaongezeka chafya ya pili, mara ya tatu ya nne, chjafya mfululizo. Akaachia lile karatasi lililoandikwa risala. Hali ikaonekana dhahiri kuwa si nzuri!!Akajikunja kunja huku akionekana kuzitafuta pumzi zake. Mwili ukakosa muhimili akaanguka chini.Wale waliokuwa na ghadhabu sasa ikawalazimu wakimbilie kutoa msaada. Msoma risala akatulia akiwa amejishika kifuani. Akafanana na ile maiti ya baba iliyopo katika jeneza.Baadhi ya wanaume wakamchukua garini.Tuliosalia tukaendelea na taratibu nyingine, hatimaye tukazika. Watu walikuwa wanajiuliza kimemsibu nini yule bwana. Hakuna hata mmoja aliyeweza kutoa majibu hata mimi pia nilikuwa katika sintofahamu.Siku iliyofuata asubuhi na mapema la mgambo likalia. Msoma risala alikuwa amepoteza maisha!!!*****Suala la baba kuondoka na siri kubwa aliyotakiwa kunieleza lilikuwa ni jambo lililoutafuna sana mwili wangu. Nilikuwa najiuliza bila kufikia muafaka.Maisha yaliendelea. Chuo kilikuwa kimefungwa jijini mwanza na nilikuwa nina kumbukumbu kuwa niliomba ruhusa maalumu kabla ya mitihani haijaanza. Hivyo nilitakiwa sasa kufuatilia iwapo mtihani umekaribia ama la.Nilitafakari nani wa kumuuliza. Nikamkumbuka Maria. Nilijilazimisha kuamini kuwa yale ya mimi kumuona katika pori nchini Zambia zilikuwa ni ndoto tu.Nikajaribu kuvuta kumbukumbu za wapi nimewahi kuhifadhi namba yake sikupata jawabu. Hilo nalo likawa tatizo.Nikafikia uamuzi wa kwenda katika huduma za internet cafĂ© sio mbali sana kutoka nyumbani kwetu. Wakati huo sikuwa na nywele kichwani hivyo nilikuwa nimejitanda ushungi.Nilifika kwa wakati muafaka nikapata nafasi, nikatazama yaliyonipeleka kisha nikalipia huduma ile.Wakati nasimama niweze kutoka nikagonganisha macho yangu na mtu ambaye niliamini kuwa haikuwa mara yetu ya kwanza kuonana. Alikuwa ni msichana mnene. Nikavuta kumbukumbu lakini sikulipata jina lake.“Mambo…” nilimsalimia, akatabasamu kisha akanijibu.“Ujue nilidhani nakufananisha. Nilikuangalia wakati unaingia ujue nikahisi nimekufananisha.”“Na mimi hivyo hivyo!!” nilimuunga mkono.Tukasogea nje na kupiga stori za hapa na pale.Wakati wa kuagana ndipo tukakumbuka kuulizana majina.“Naitwa Isabela.”“Mh!! Isabela!! Ulibadilisha jina ama..maana nakumbuka walikuwa wanakuita nani vilee.” Alijaribu kuvuta kumbukumbu. Mimi nikawa namtazama tu! Nilibadilishaje jina sasa mimi.“Hata sijabadili mbona.” Nilimwelewesha. Akazidi kupinga.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Hatukufikia makubaliano, akapigiwa simu akaniaga huku akisisitiza kuwa nimemdanganya jina. Mimi sio Isabela.Nilimsindikiza kwa macho hadi akatokomea. Nilijitazama iwapo nilifanana na mmoja kati ya ndugu zangu lakini hakuna niliyefanana naye ambaye ningeweza kumtupia lawama kuwa watu wananifananisha naye.*****Kile kitendo cha yule dada kuonekana kana kwamba amenifananisha kisha akakataa kuwa jina la Isabela si la kwangu nilikipuuzia na kumchukulia yule dada kuwa amepoteza kumbukumbu zake kwa kuwa miaka imepita mingi sana.Nilivyotoka pale moja kwa moja nikaenda nyumbani kwa dada Suzi kwani tangu nirejee Makambako sikuwa nimeenda kumsalimia mume wake na familia kwa ujumla zaidi ya kukutana msibani.Nilimkuta yupo nyumbani akiwa na familia yake jikoni wakiandaa chakula.Alinipokea vyema tukasalimiana kisha nikataka kumsaidia kupika.“Kuliko kunisaidia kupika ni heri unisaidie kumbeba huyu mwanao.” Alizungumza huku akijitoa mtoto aliyekuwa amembeba mgongoni. Nikampokea na kumbeba.Ghafla mtoto akaanza kulia taratibu kisha anaongeza kilio.“He! Haka nako lini tena kameanza kuchagua watu.” Nilimuuliza dada. Hakunijibu zaidi ya kuguna akimaanisha kuwa huenda ni jambo la kawaida.“We dogo wewe..mama yako mdogo huyo.” Alisema akimaanisha kumweleza yule mtoto mdogo wa mwaka mmoja. Japo hakumuelewa.Mtoto akazidi kutoa kilio.“Hebu mchukue mwanao nadhani ana kisilani cha usingizi.”Nilimkabidhi dada Suzi mtoto wake, cha ajabu hakunyamaza zaidi ya kuongeza kulia. Sasa Suzi akashtuka na kulichukulia uzito hili suala ambalo mwanzo ulikuwa kama mzaha fulani hivi. Alimkagua mwanae kama amechubuka mahali. Hakuna kitu!Huenda basi ameumwa na mdudu, hata hilo pia halikuwepo!!!Mapishi yakakoma kwa muda. Mtoto analia kwa sauti ya juu sana. Machozi yanamtoka kwa wingi mno. Hatari!!Ilianza dakika moja na sasa zilikuwa zinatimia sitini, yaani saa zima bila kilio kukoma. Mtoto alikuwa analia sana.Majirani wakakisikia kilio hicho kikuu wakajongea pale nyumbani kwa Suzi. Na wao pia wakashangaa.Suzi akajaribu kumpa titi mtoto aweze kunyonya, akalikataa. Kila mmoja alijaribu kumbeba bila mafanikio.Kimbilio lililofuata likawa hospitali.Huko napo hapakuwa na nafuu yoyote. Madaktari walimfanyia uchunguzi na kurejea na majibu yasiyoridhisha hata kidogo. Walisema kuwa mtoto hakuwa na ugonjwa wowote ule. Hivyo hawakuwa na msaada wowote ule.Tulirejea nyumbani. Tulipofika huku kila aliyetazama tukio hili akiwa katika mfadhaiko wa hali ya juu na kuegemeza imani zao katika mambo ya kishirikina. Ni hapa na mimi nilijishtukia na kuanza kuamini kuna jambo. Lakini jambo lenyewe ni mimi!!Niliamini kuwa ni mimi baada ya kuyakumbuka maneno ya yule mzee kule Iringa. Aliyeniambia nisipofuatilia jina langu basi nitasababisha majanga mengi sana popote nitakapokuwa.Usiku mzima mtoto alikuwa analia. Na kama hiyo haitoshi mara mkono wake wa kushoto ukaanza kujikunja. Suzi naye akawa analia sasa maana hakuwa na njia nyingine.Baba wa mtoto alipigiwa simu akiwa safarini kuelekea Songea akalazimika kuhairisha safari, mama yetu alikuwa hapo nyumbani pia.Suzi alikuwa Amelia sana na alikuwa amewaacha walokole wenzake wakimwombea kwa namna zote mtoto yule. Lakini hali iliendelea kuwa tete.Mtoto huyu akifa itakuwa juu yangu!! Niliwaza na kufikia maamuzi.Dada Suzi alikuwa mtu pekee ambaye angeweza kunisaidia katika hili. Maana tayari tulikuwa tunamtambua kuwa alikuwa mwanamke wa kipekee aliyeweza kuhifadhi siri nzito nzito.Huenda hata siri aliyokufa nayo baba nayo angeweza kuwa nayo!! Nikarusha karata yangu.Nikamfuata dada Suzi nje alipokuwa amekaa chini ya mti akilia kwa juhudi zote.“Da Suzi.” Nilimuita, akageuka akanitazama na macho yake mekundu yaliyovimba kutokana na kulia kwa muda mrefu.“Nahitaji kuzungumza nawe dada.”Alinitazama tena bila kusema lolote.“Kuna jambo nahisi….”“Nini?”“Naweza kuwa najua chanzo cha tatizo hili.”Suzi akageuka mzima mzima akanitazama kwa umakini kabisa akisubiri niseme neno.Sikuwa na haja ya kumueleza kuwa ile ninayotaka kumwambia ni siri, nilikuwa namuamini sana.“Suzi…” nilianza kumuelezea kwa kirefu na mapana juu ya maisha niliyopitia, nikamueleza juu ya ile mimba ya maajabu ambayo mwisho wake ulikuja baada ya kukatwa ilea lama ya 666 katika makalio yangu, nilimueleza pia juu ya Dokta Davis na pesa zake haramu, ndoto za maajabu zote pia nilimuelezea.Dada Suzi alinisikiliza vyema sana nilipokuwa namueleza juu ya makaburi ya Kiyeyeu huko Iringa na jinsi nilivyokutana na babu nisiyemfahamu aliyenieleza kuwa jina la Isabela sio jina langu. Natakiwa kulitafuta jina langu.Alishangazwa na kukwama kwa basi letu hadi pale niliposhuka mimi, kifo cha mwanaume aliyekuwa anasoma risala ya marehemu baba pia alishangaa nilivyomweleza kuwa yawezekana ni moja ya majanga niliyoyasababisha.“Hata baba alikuwa ameniahidi kunieleza jambo fulani lakini ajabu kabla hajaweza kunieleza ametutoka. Nahisi ni yaleyale. Najua dada yangu hauamini mambo haya lakini niamini mdogo wako.”Nilimsisitiza na ili kumfanya aamini tuliingia ndani nikamfunulia kovu langu. Hapo sasa aliweza kuniamini.“Kwa hiyo mwanangu anaweza kufa pia.” Aliniuliza kwa wasiwasi.“Sijui nisemeje lakini kiukweli naogopa sana…” nilimjibu.“Sasa Bela mimi nafanyaje hapa katika hili.”“Dada kama unaweza kujua lolote lile kuhusiana na mimi tafadhali nieleze tumuokoe mtoto. Hana makosa hata kidogo.” Nilimsihi Suzi. Kilio cha mtoto kilikuwa juu kama kilivyoanza na alikuwa anazidi kujikunja mkono.Suzi alinitazama usoni kama anayesoma kitu fulani kwangu.“Bela…yapo baadhi ninayoyajua….nitakueleza, sio kwa imani za kishirikina hapana!! Nakueleza kwa kuwa ni lazima uyajue. Kama mwenyezi Mungu amenipa pigo hili ili nikueleze siri hii basi nakueleza. Lakini jitahidi kuwa na moyo mgumu.” Nilianza kutetemeka kwa maneno hayo ya dada, hakika nilikuwa namuheshimu kwa kuwa na siri nzito nzito.Kabla ya kunieleza aliniongoza katika sala. Nikamfuatisha hadi alipomaliza.Sasa uwanja ukawa wake nami nikawa katika zamu ya kusikiliza.“Siri hii hata aliyenieleza hajui kama alinieleza.”“Kivipi?”“Mzee alikuwa amelewa siku hii. Na pesa ya kulewa nilimpa mimi. Baada ya kulewa akawa anasemezana nami kwa njia kama ya kupitiwa ama hajui anazungumza na nani.”Nikakubali kwa njia ya kichwa.Suzi alinielezea juu ya upendo wa baba kwa mama yangu ulivyomlazimisha kufanya jambo hili la ajabu. Tendo la kuiba mtoto na kumpatia mama bila yeye kujua.“Aliiba mtoto…kivipi?”“Baada ya mimi kuzaliwa mama alizaa mtoto mwingine, akafariki dunia akiwa tumboni. Siku chache kabla ya kuzaliwa. Baada ya hapo akashika mimba nyingine tena. Alipojifungua tu mtoto akafariki tena.” Alinieleza dada Suzi, taarifa ile ya pili ikanisisimua kuliko ile ya kwanza, maana nilikuwa naifahamu hiyo kuwa iliwahi kutokea. Hii ya pili sikuwa naifahamu.“Baba akazungumza na manesi, akawapatia pesa nyingi ambazo ziliwafanya wasahau wajibu wao. Wakakiuka maadili wakaiba mtoto na kumpelekea mama halafu yule mtoto aliyekufa akapelekwa wanapojua wao.”“Kwa hiyo mama alipozinduka?”“Akajikuta ana mtoto wa kike….akaamini ni mtoto wake wa kumzaa.”“Kwa hiyo mama anajua kuwa hayo yalitokea?” niliuliza kwa hamaki.“Si yeye wala ndugu mwingine anayefahamu jambo hili. Kama nilivyokwambia hata mimi baba alinieleza akiwa amelewa.”“Sasa huyo mtoto mwingine yupo wapi sasa hivi? Na anaitwa nani jamani”Ndiye huyu mbele yangu, anaitwa Isabela.”Nilipiga yowe la mshtuko!! Suzi akawahi kuniziba mdogo na kunikanya kuwa niwe mtulivu kama kweli nimeamua kuichukua siri hiyo. Nikajilazimisha kutulia.“Isabela…wewe sio mtoto wa familia hii ya mwalimu Nchimbi, mimi sio dada yako wa damu, mwalimu sio mama yako na hata marehemu pia hakuwa baba yako.” Alisema Suzi huku akiwa amenitazama usoni moja kwa moja. Nikashtushwa na kauli hiyo. Nilitegemea kuwa Suzi atabadili kauli hiyo huenda amesema kimakosa, lakini hakubadili.Mapigo ya moyo yakaenda kasi sana!! Nikatamani ile iwe filamu na itamalizika baada ya muda fulani. Lakini hali ikaendelea kuwa kama ilivyo.“Dada Suzi, kwahiyo mimi…eeh!” nilikuwa nimepegawa.“Hiyo ndiyo siri Isabela. Haya je inahusika kwa namna yoyote na tatizo la mwanangu???”“Dada yawezekana kweli yahusika sana. Kwa maana hiyo mimi sio Isabela. Hili jina alinipa nani.”“Baba na mama….namaanisha mwalimu Nchimbi na marehemu mume wake.”“Basi mimi sio Isabela. Mama yangu na baba yangu watakuwa wapi Mungu wangu!!” nilijiuliza huku nikijikuna kichwa changu pasipo kuwashwa.Wakati najikuna kichwani zikarejea zile kumbukumbu za kudekezwa sana na mwanamke huyu ambaye sasa naambiwa kuwa sio mama yangu. Upendo wa dhati alionionyesha tangu nikiwa mdogo ulizidi kunifanya kimya kimya nipingane na kauliza dada yangu. Lakini ule uwezo wa dada kutunza siri ulinirejesha kuamini kuwa ule ni ukweli.“Kwa hiyo inakuwaje.” Alinishtua Suzi na kunifanya nikumbuke kuwa tulikuwa na tatizo.Natakiwa kulipata jina langu na ukoo wangu!! Nilimwambia Suzi.*****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Kama ilivyokuwa kwangu ndivyo ilivyomuwia mwalimu Nchimbi ugumu sana kuweza kuamini alichokuwa anaelezwa na dada Suzi. Alimanusuru azimie kama zisingekuwa jitihada za dada Suzi kulegeza maneno makali na kuyafanya laini.Hatimaye mama aliyekuwa mbishi kipindi chote cha maziungumzo alikubali kwa shingo upande kuwa mimi sio mwanaye.Kwa kuokoa maisha ya mtoto wa dada Suzi ambaye alikuwa analia mfululizo tuliamua kwa pamoja kushirikiana kulitatua tatizo hili.Hospitali!! Hapa ndio tulianzia kumtafuta mama yangu. Ilikuwa hospitali ya serikali na ni miaka mingi sana ilikuwa imepita. Kila kitu kilikuwa kimebadilika, hakuwepo wa kuweza kutusikiliza na kutusaidia.Mtoto akiwa amebaki nyumbani, sisi tukiwa katika hekaheka hizi ndipo mama alipokuja na wazo la kumwendea mkunga ambaye alimzalisha. Mama alikiri kumkumba mama huyo ambaye ni mstaafu tayari.Hakuna aliyelalamika kuhusu kuchoka. Tulitembea kwa miguu. Tulipofika maeneo ambayo mama alihisi kuwa ndipo anaishji yule mkunga tulianza kuulizia. Ilituchukua muda mfupi tu kuweza kuyapata makazi yake.“Ameenda sokoni lakini atarudi muda si mrefu.” Msichana tuliyemkuta pale nyumbani alitujibu.Tukajiweka katika mkeka tulioukuta pale nje na kumsubiri.Kama tulivyoelezwa mama huyo mkongwe kiasi alifika, kwa kumtazama alionyesha kuwa ujanani alikuwa mrembo sana lakini mwenye maringo.Licha ya uzee huo bado alikuwa na maringo kiasi katika sauti yake.Alitukaribisha huku akiwa amesimama kwa namna ya kutusikiliza shida yetu ni ipi.Kila mmoja akamwachia mama jukumu la kuzungumza.“Naitwa mama Isabela au …” kabla hajamaliza kujitambulisha ilisikika sauti kutokea dirishani, “Shakamoo mwalimu!!”“He! We ni nani tena unanisalimia umejificha…” alisema mama kwa kitetemeshi cha ualimu.Yule mkunga akasaidiana nasi kutazama mlangoni. Akatoka msichana kwa makisio ni umri wa miaka kumi na moja.Akamsalimia mama kwa kupiga magoti.Kabla ya kujibu mama akaanza kuvuta kumbukumbu.“Eliza….nimekosea!!!” alimkumbuka jina lake kwa usahihi.“Mjukuu wangu huyu, kumbe ni mwanafunzi wako.” Yule mkunga aliyekuwa amesimama akasema huku sasa akikaa. Mwanafunzi yule akawa ameujenga urafiki kati yetu.Tukakaribishwa ndani!!!Baada ya utambulisho mama alianza kujielezea juu ya jambo lililotuleta. Alianzia mbali sana hadi akalifikia lengo letu.Mama yule kwanza, alishtushwa na taarifa hiyo kisha akasema kuwa hajui lolote kuhusu tukio hilo.“Kwa hiyo una uhakika kuwa nilizaa mtoto na akawa hai?” mama alimuuliza akiwa amemkazia macho. Mkunga akawahi kukwepesha macho yake, nikamsoma na kugundua anatudanganya.“Sikumbuki..ujue nimewazalisha akinamama wengi sana…hakika sikumbuki.” Alijitetea huku akiwa na hofu.Aliusimamia uongo wake huo hadi pale nilipoamua kuyaingilia mazungumzo haya, hasira ilikuwa imeanza kunitawala.Nikarusha karata yangu!!!“Mama mimi nadhani nimpigie simu yule baba aliyeshuhudia tukio hili, najua nikimpigia atakuja na yule askari. Kwa hiyo tutaufahamu ukweli.”Yule mama akatowa yowe la hofu huku akizungumza kikabila cha kwao, hakika alitaharuki kusikia polisi.“Mwanangu…usipige simu subiri tunayazungumza haya yanaisha.”Uwanja ukawa wake akazungumza.Kama dada Suzi alivyosimuliwa na marehemu baba juu ya uwepo wangu katika familia ile ndivyo ilivyokuwa kwa nesi huyu ambaye mara kwa mara alitusihi tuyamalize kindugu.“Na mama yangu ni yupi?” nilimuuliza ghafla akashangaa.“Sikuelewi unaniuliza mimi au?”“Ndio nakuuliza wewe…..mimi ni huyo mtoto azliyeibiwa.”Akakodoa macho yake kwa hofu. Nikaiskia hasira ikinichemka sana nikatamani kumrukia.“Kwakweli mimi sijui labda Gloria ndio atakuwa anafahamu.”“Gloria ndio nani?” mama alimuuliza.“Tulikuwa naye..huyo ndiye aliyenishawishi.*****Hatukupoteza muda, tulimpa nafasi kidogo ya kujiandaa tukaondoka kuelekea kwa huyo aliyemuita Gloria. Haikuwa safari ndefu sana, tulitumia taksi.Na yeye tulimkuta vilevile akiwa yupo katika uzee.Baada ya salamu mbili tatu. Moja kwa moja ikawa zamu ya yule nesi kumueleza mwenzake juu ya tukio la miaka zaidi ya ishirini iliyopita.Kama ilivyokuwa wakati tunamueleza na yeye alileta ujanja wa kutaka kumruka mwenzake lakini alipothibitishiwa kuwa akileta udanganyifu yupo shahidi na polisi pia. Naye akanywea!“Tunachohitaji kujua ni kitu kimoja tu!! Mama aliyeibiwa mtoto ni nani.” Nilikoroma kwa hasira. Suzi na mama wakawa wakimya.“Ni Dina….Dina yule…..”“Dina ni nani na anakaa wapi.”“Dina ni kichaa…eeh! Mungu nisamehe mimi nisamehe…” alianza kulia yule mwanamke.” Hakuna aliyembembeleza.Neno lake la kuwa Dina ni kichaa liliniacha njia panda, ina maana mama yangu ni kichaa na anaitwsa Dina? Hapana haiwezi kuwa!!! Nilipinga kimya kimya.Baada ya kutulia tena akatueleza juu ya kichaa aliyepewa mimba miaka mingi iliyopita. Mimba iliyotaka kuchukua uhai wake kwa sababu ya kukosa matunzo. Ilikuwa kama bahati diwani wa kata hiyo ambaye alikuwa mwanamke alipata kukutana na kichaa huyu. Wakati huo mimba ilikuwa na miezi saba. Huruma ilimshika kutoka na na imani yake ya kiroho..”“Ooh!! Jesus jesus!!” Suzi alinong’ona huku akiwa kama anasali.Akaendelea yule mama. “Basi akafika mwenyewe hospitali na kutoa amri ya mwanamke yule kusaidiwa. Hatua za haraka zikachukuliwa. Mwanamke akaanza kukamatwa kinguvu na kupelekwa kliniki. Baadaye akafungiwa kabisa bila kutoka hospitali. Hatimaye miezi tisa ikatimia akajifungua bila kufanyiwa upasuaji. Mtoto wa kike!!!!Wakati anajifungua mtoto huyu ndipo ilipatikana biashara hii ya kuiba mtoto. Hakika hali ilikuwa ngumu sana kiuchumi. Utawala wa serikali ya awamu ya kwanza ulikuwa umechachamaa sana hivyo kwa pesa tuliyotangaziwa na yule kijana ambaye simkumbuki jina mimi na mwenzangu hatukuweza kuikataa.Pia tuliamini kuwa yule kichaa asingeweza kumlea mtoto wake. Hivyo kwa huruma tukamchukua yule mtoto na kumuuza.”Simulizi ile ilinisisimua sana!! Nilikuwa natetemeka kwa kila neno alilotamka yule mwanamama. Nilijihisi kama nusu mwanadamu nusu nimekufa!!Kimya kikatanda. Kila mmoja akiwaza lake. Mimi nikizidi kuamini maneno ya mzee yule wa Iringa. Kuwa lile halikuwa jina langu na wala haukuwa ukoo wangu.“Mama yangu yupo wapi?” hatimaye niliuliza.“Kwa kweli ni siku ya nne hivi sijamuona lakini huwa anapatikana stendi na majalalani.” Nikasisimka tena kusikia maneno haya. Mama yangu anaishi majalalani!!!Niliumia.Hapakuwa na jipya tena kwa pale. Kwa kuwa huyu mama alikuwa anamtambua Dina ilimlazimu kuzunguka nasi siku nzima kumtafuta.Siku ya kwanza hatukufanikiwa kumuona.Siku ya pili majira ya mchana baada ya kuzunguka siku nzima bado kimya. Tukapewa taarifa za juu juu kuwa aliingia katika gari ya kwenda Mbeya.Huo ukawa mwanzo wa safari nyingine.“Tulimshusha Uyole.” Kondakta alitueleza baada ya kufanikiwa kulipata lile gari alilosadikiwa kupanda mama yangu.Wakati huu nilikuwa mimi na mama pamoja na yule mkunga. Dada Suzi alirejea nyumbani kwa ajili ya kulea mtoto ambaye sasa kilio kilikuwa kinapungua na kidogo alikuwa ananyonya.Safari ya kwenda Mbeya ikafuata. Tukaweka kituo Uyole. Kama vile chokoraa tulianza kuzurura huku na huko bila mafanikio. Yule mkunga ndiye aliyekuwa anaulizia mara kwa mara maana ni yeye alikuwa anaujua muonekano wa huyo Dina.Siku mbili Uyole bila mafanikio. Mama alikuwa amechoka dhahiri lakini asingeweza kusema, nadhani kwa kuwa aliamini nipo katika matatizo pia ni kama mwanaye wa kumzaa, maana hata titi lake nilikuwa nimenyonya.Siku ya nne inakuja habari nyingine kuwa Dina alionekana sokoni. Asubuhi na mapema tukafunga safari kuelekea Uyole sokoni.Tulisubiri kwa masaa kadhaa.Kelele za akina mama zilitushtua, walikuwa wanahangaika huku na huko kutaka kushuhudia jambo huku wengine wakiwa wanakimbia.“Yule pale Dina!!” mkunga alipiga kelele huku akitujelekezea kwa kidole.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Mwanamke mnene, akiwa na malapulapu mwilini alikuwa akiwaponda watoto na mawe. Huku akiwa na fimbo mkononi. Alikuwa anajongea eneo la soko. Jambo hilo liliwapagawisha akina mama na sasa walikuwa wanapiga kelele.Nilimtazama mwanamke huyu anayesadikiwa kuwa ni mama yangu. Mara ghafla nikajikuta nipo wima, nikakimbia mbio mbio. Umati ulikuwa unashangaa na hata mwalimu Nchimbi alibaki kunitazama tu asijue la kufanya.Macho yetu yalipogongana nikaona kitu!!Ni kama kioo mbele yangu na nilikuwa najitazama.Damu nzito kuliko maji!!!Sikuogopa mawe aliyoshikilia, mavazi yake machafu!!Nikamsogelea na kumkumbatia.Maajabu!! Na yeye akanikumbatia huku akizungumza kabila nisilolielewa. Kimya kikuu kikatawala!!Hakuna aliyetusogelea.“Mama!!” nilinyanyua kinywa changu na kumuita!!“Su…Subira…..” aliniita kwa mshangao.Alipotaja jina hilo. Nikajikuta kama nasukumwa chini. Nikaanguka kama mzigo.Nikajikuta katika filamu ya ajabu huku mimi nikiwa wa ajabu zaidi.Nilikuwa napambana na mamia ya watu. Na sasa nilikuwa ana kwa ana na Dokta Davis. Alikuwa ananiogopa sana, nami sikuwa na huruma. Nikiwa na panga kubwa mkononi. Nilimkaribia na kumfyeka.Nikatazama maadui wengine wanaonikabiri na wao nikawatenda nilichomtenda Davis.Likafuata pambano kuu la kupambana na joka la maajabu.Lilinisumbua lakini kila liliponijeruhi na mimi niliondoka na kipande kimoja cha mwili wake.Pambano lilikuwa kali hadi walipotokea viumbe weupe sana wakaniweka kando kisha wakalimaliza joka.Kisha wakakiteketeza kijiji kile cha maajabu. Lakini cha kushangaza mimi sikuungua kabisa.Moto ulipokwisha nikajikuta nimesimama peke yangu. Uchi wa mnyama. Nilikuwa nimechoka na nilikuwa natokwa jasho.Ule ujasiri niliokuwanao ukayoyoma na sasa nikawa naogopa.Mara ghafla…”Mamaaaaaa!!” nikapiga kelele kubwa na kutaka kukimbia.Nilipojaribu kufanya hivyo nikakabiliana na kamba ngumu zikiwa zimeifunga mikono yangu na miguu. Nilikuwa natokwa jasho sana.Niliangaza huku na kule bila kupata majibu.Mara kundi la watu likafika pale chumbani.Wote walikuwa wakinishangaa. Nikamuona mwalimu Nchimbi.“Mama ni nini hiki…mbona nimefungwsa hivi.” Niliuliza huku nikiwa nashangaa.Mwanaume mmoja nisiyemtambua akaanza kunielezea juu ya vurugu nilizokuwa nafanya licha ya kupigwa sindano ya usingizi.“Ni ugonjwa wa kushangaza sana.”Alinielezea tukio zima la kuanguka baada ya kukumbatiana na kichaa ambaye alitoweka pia baada ya mimi kuanguka.“Mama yangu!!” niliwaza!! Kisha nikatabasamu na akili ikiwa imerejea sawia.Nilipofunguliwa kamba niliwaelezea juu ya yote yaliyokuwa yananikabili katika maono yangu ya ajabu.“Nimeikamilisha kazi!!!” hatimaye nilitamka hayo.Tulikuwa hospitali ya mkoa ya Mbeya. Baada ya siku nne niliruhusiwa kuondoka. Niliambatana na mwalimu Nchimbi.“Naitwa Subira!!” nilimweleza mama.“Najua!!” aliniambia, nikashangaa.“Umejuaje.”“Ulisisitiza sana wakati ukiwa umepoteza fahamu zako.”Nilitabasamu naye akatabasamu.*******Mtoto wa dada Suzi alikuwa halii tena japo mkono wake ulibaki kuwa vile umejikunja.Amani ikautawala moyo wangu!!!Taarifa pekee iliyoniumiza ni juu ya kifo cha mama yule kichaa aliyekufa baada ya kugongwa na gari.Japo nilipata nafasi ya kusikia neno moja tu kutgoka kwake lakini alikuwa amenisaidia mengi mno.Familia yangu ilimzika kwa heshima zote kama ndugu.Baada ya kuyaweka haya yote pembeni niliirejesha akili yangu jijini Mwanza.Mama alikopa pesa nikasafiri kurejea chuoni.Safari ilikuwa njema sana.Maria akawa mwenyeji wangu jijini Mwanza. Akanielezea juu ya yote yaliyotokea. Hapakuwa na lolote baya, zaidi ya maajabu ya kanisa fulani kudai limemtoa John msukule kutoka gamboshi.Nilitabasamu na kukiri kuwa dini imegeuka biashara. Lakini sikumwelezea Maria juu ya yote tuliyoyapitia.“Jesca na Jenipher je?” nilimuulizia na kutegemea jibu la maajabu tena.“Kumbe mwenzangu na wao hawakufa..eti vilizikwa vinu badala ya watu!! Dunia ina mambo.” Alijibu.“Kwa hiyo bado wapo chuo.”“Hapana hawapo kwa sasa. Lakini Jesca yupo mtaani.’“Amakweli dunia ina mambo…” nilimuunga mkono.Maria hakujua lolote lile kuhusu yaliyonisibu mimi. Na alikuwa kama anayenifahamisha juu ya yaliyotokea huku akiamini kuwa ile ruhusa niliyoomba ndio iliyonifanya nitoweke ghafla.“mwenzangu na mimi siku moja sijui nikaota madudu gani. Wacha nipagawe..” Maria alinisimulia alichokiota na kilikuwa sawa na kilke kichotutokea msituni.Maria hakujua kama ni kweli alikuja kule msituni!!!“Nilipiga kelele wewe nikamuita Mungu, mama na mizimu yote!!” aliendelea kusimulia.Baada ya mazungumzo hayo marefu. Niliingia kuoga.Baada ya kuoga nikiwa katika kutafuta nguo ya kubadilisha nikakutana na kadi ya benki. Nikaitazama huku nikiweka mbali kabisa tamaa.Nilipokuwa nimebadilisha nguo, nikaanzisha moto mdogo nyuma ya nyumba na kuviteketeza baadhi ya vitu ambavyo nilihisi vitakuwa vinanikumbusha juu ya Dokta Davis. Nilitaka kuiteketeza kadi ya benki pia lakini nikakumbuka kuwa ilikuwa pia kwa ajili ya matumizi ya chuoni. Nikaghairi zoezi hilo.******Baada ya wiki moja nikapata fursa ya kukutana na John!! Nilikutana naye akiwa anaelekea kanisani.“Bwana asifiwe dada..Bela.” alinisalimia huku akionekana kutokumbuka lolote.Nikamjibu, tukabadilishana naye mawili matatu. Akaenda zake huku akinisihi kuwa akitoka kanisani atanitafuta.Niliondoka pale nikiwa natabasamu na kujipongeza kwa vita ile kuu ambayo nimeibuka kuwa mshindi. Vita ambayo nimepoteza kipande kidogo tu cha nyama yangu lakini kwa ukombozi wa mamia ya watu..kutoka katika milki ya Shetani na chapa yake ya 666.Japo sikutaka tena kurejea katika mtandao huo lakini nilikiri kwa kila neno la lugha ninayoifahamu kuwa kamwe SITAISAHAU facebook.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/MWISHO