Search This Blog

Sunday 19 June 2022

KISU CHENYE MPINI MWEKUNDU - 5

 





    Simulizi : Kisu Chenye Mpini Mwekundu

    Sehemu Ya Tano(5)



     Inspekta Beda alipofika bado hakumjali. Kama alivyofanya mama Beda, naye akaamua kuondoka pale ndani. Akatoroka na mwanae Vero na Sara ambaye alikuwa na umri wa miezi miwili tu. Lakini wakati anatoroka alikuwa anasumbuliwa na tumbo ambalo alihisi kuwa ni sumu baada ya kudokezwa na Vero wakati tukio limeshatokea.



    *****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Veronika akaacha kusimulia na kumgeukia Sara ambaye alikuwa analia. “Nafikiri sasa utakuwa umejua kwanini nimemuua Lucy.”

    “Kuhusu Lucy nimejua, bado sijajua mama yangu na bibi yangu ilikuwaje na pia ningependa kufahamu kwanini ulimuua mama Pili”

    “Swali zuri, lakini kwanza naomba nikueleze jinsi nilivyoingia kwenye maisha ya uchangudoa mpaka nikafikia uamuzi wa kuwa muuaji na kumuua mama Pili.” Akatulia kidogo na kumkazia macho mdogo wake ambaye alishaanza kumuamini na kumuelewa dada yake.

    “Habari ya mama na bibi naomba niiweke kiporo kwanza. Katika kutafuta maisha ndipo nikahamia kwa mama mmoja mfanyabiashara aliyekuwa anaishi Kawe. Nikafanya kazi za ndani huko huku wewe ukiwa mgongoni kwangu nililazimika kuwaongopea kuwa sisi ni watoto yatima bahati yule mama hakuwa mdadisi......”

    “…….Nikakaa kwa yule mama hadi ulipotimiza miaka mitano nikaagana na yule mama baada ya kupata ahadi ya ajira yenye malipo zaidi kutoka kwa mama mwingine ambaye alikuwa nyumba ya jirani, sikujua nasema sikujua kumbe yule mama alikuwa nyoka kabisa tena nyoka mwenye sumu kali kwani sikuwa wa kwanza kuangukia katika mikono ya mama pili kupitia ushawishi wa huyu mama.”

    “…..Namkumbuka vizuri yule mama anaitwa mama Mwazani naye pia yupo kwenye mpango wangu akipona bahati yake, huyu ndiye aliyenikutanisha na mama Pili huku akifahamu fika lengo la mama Pili. Nakumbuka siku aliyonipeleka mama Pili alifurahi sana. Akampa pesa ambazo zilikuwa ni ujira wake kwa kunipeleka pale. Sikumbuki ni miaka mingapi nilifanya kazi kabla ya kuingizwa rasmi kwenye mtandao wa machangudoa. Ninachokumbuka huu ni mwaka wa tano au wa sita toka niingie kwenye biashara hii.”

    “Lakini dada hujanipa sababu za kutosha za kumuua Mama Pili.”

    “Bado sijamaliza mdogo wangu, nina sababu zaidi ya moja za kumuua mama Pili….”

    “……Kama unakumbukumbu ukiwa na miaka saba uliwahi kutekwa na wanaume watatu wakakufanyia mambo machafu ambayo yalikuathiri sana kisaikolojia ule ulikuwa ni mpango wa mama Pili na alilipwa pesa nyingi sana, pili tulikubaliana akusomeshe, nasikitika hajatekeleza nasikia uchungu mdogo wangu kama si kukufundisha mwenyewe basi hata kusoma na kuandika ungekuwa hujui. Tatu ni yeye ndiye aliyenilazimisha kwa nguvu kuingia kwenye biashara ya ukahaba kwani alitafuta watu wakanifungia chumbani kwa kushirikiana na mwanae Pili.(kipande hicho akashindwa kujizuia akatulia kidogo na kujifuta machozi ambayo yalikuwa yanamwagika kwa wingi) Vile vile naomba ufahamu kuwa nilipofika pale niliwakuta mabinti wengine ambao alikuwa anajinufaisha nao kwa mtindo huo, cha kusikitisha zaidi ni pale alipomlazimisha binti mmoja kutembea na mwanaume ambaye ni muathirika wakati akijua wazi. Baada ya kuathirika kutokana na matunzo duni yule dada alisumbuliwa na homa za mara kwa mara. Mama pili hakutaka kuingia gharama tena akatumia njama ya kumuwekea sumu na kumuua. Kijana yule yule ambaye alimlazimisha yule binti akanilazimisha na mimi pia. Nikakataa lakini wakatumia ubabe kuhakikisha nafanya mapenzi na yule kijana kwani alilipwa pesa nyingi. Ndio maana nilipoenda kupima nilikuwa na uhakika mkubwa kuwa majibu hayatakuwa mazuri kwa sababu yule kijana alilazimisha kufanya mapenzi bila kinga.”

    Akatulia na kumkazia macho mdogo wake ambaye alikuwa makini kumsikiliza dada yake.

    “Naomba tulale nina kazi ya kufanya kesho.” Alimaliza kisha akajivutia shuka akalala.

    “Samahani lakini kwa usumbufu huyo kijana unamfahamu vizuri?”

    “Ndiyo. Anafanya kazi kampuni ya mafuta BP mtaa wa jamhuri, sitaki swali tena mdogo wangu nimechoka pengine unataka kujua jina lake anaitwa Samson Masanja.” Hakuongea tena akajivutia shuka akalala.



    ********



    Alitembea kwa wasiwasi mkubwa kwani eneo alilokuwepo ni eneo analofahamika sana. Pia aliogopa kwa sababu alikuwa anatafutwa na polisi. Kilichomsaidia hakuacha alama yoyote ya picha ambayo ingewafanya polisi waitoe magazetini na kuhatarisha maficho yake. Alishaifikia nyumba ile aliyokusudia. Hakuwa na haraka. Akabana sehemu ambayo ilikuwa inatumika kuhifadi magunia ya mkaa. Ilikuwa ni siku ya tatu anakuja kujificha hapo bila kufanikisha kulipata windo lake. Akakaa hapo kwa masaa mawili bila kutokea kile alichokitarajia. Akiwa amekata tamaa ndipo alipoushuhudia mlango ukifunguliwa. Akamtazama vizuri aliyetoka. Ni yeye. Aliwaza kwa furaha huku akijiandaa kwa shambulizi.

    Pili aliingia chooni baada ya dakika chache akatoka. Hakufika mbali. Vero akampiga kwa gongo zito kichwani akataka kudondoka lakini vero akamuwahi ili asitoe kishindo. Kisha akammalizia kwa kudidimiza kisu che mpini mwekundu upande ambao alihisi kuwa ndiko yaliko makao ya moyo. Akamshikilia taratibu hadi alipohakikisha mwili wake ameulaza chini. Moyoni alifurahi sana jinsi alivyoifanya kwa umahiri mkubwa kazi hiyo.

    Taratibu akaondoka eneo la tukio. Tofauti na wale wengine huyu alimuua kwa utulivu zaidi. Mama Mwazani ndiye aliyenileta huku sasa ni zamu yake. Aliwaza huku akiondoka kifua mbele baada ya kutekeleza jukumu lile. Akapita kwenye vichochoro mbalimbali ambako alipishana na makahaba aliowafahamu sana. Hakuna hata mmoja aliyeweza kumtambua Vero. Alijitahidi kubadilisha mwendo na chochote ambacho kingemfanya mtu aweze kumtambua.

    Salum, mpenzi wake Pili alikuwa amechoka kusubiri kule ndani. “We pili vipi huko nje?” Aliuliza kwa hasira kidogo. Alipoona hajibiwi ndipo alipoamua kutoka nje. “He. Vipi tena mpenzi.” Alishtuka baada ya kumuona Pili akiwa amelala chini. Kwa kuwa kulikuwa na giza akaingia ndani na kuchukua kibatari.

    “Damu.” Alishituka salum kabla ya kutimua mbio akiogopa ushahidi ambao ungekuja baada ya kuonja mvua ya makofi pengine na virungu kutoka kwa polisi.



    * * *

    Kachero Dadi Kasweyaga alikuwa anajiandaa kunyofoa laini yake ya mtandao ambao unafahamika ofisini kwake ili aweke ile inayofahamika zaidi na ndugu na marafiki. Ilikuwa ni kawaida yake kwa siku anazochoka kubadili laini kwa kuchelea kupigiwa usiku. Leo ilikuwa ni moja ya siku hizo. Wakati anataka kuzima ikaingia simu. Safari hii ilipigwa na bosi wake Inspekta Beda.

    “halloo habari afande.”

    “Nzuri za nyumbani.”

    “Salama kwani umemaliza likizo afande?”

    “Ndiyo na hivi ninavyoongea nakuhitaji ofisini kuna dharura.”

    “Sawa afande.” Akajibu huku akijifanya kuchekacheka kumbe alikuwa amekunja uso kwa hasira. Akamkazia macho mkewe mama Tunu. Akasikitika kwani alikuwa anakaribia kuanza safari yake ambayo imemfanya awe pamoja na mama Tunu.

    Akainuka kitandani kivivuvivu.

    “Vipi baba Tunu.” Mkewe alishituka usingizini baada ya purukshani za mumewe wakati anajiandaa kuondoka.

    “Kuna imejensi nimeitwa ofisini.”

    “Mh. Haya .” Alinung’unika mkewe huku akiinuka kutoka kitandani kwenda kufunga mlango.



    Akafungua mlango na kutoka, mkewe akaubamiza mlango kwa nguvu kitendo kilichomfanya kachero atambue kuwa mkewe kakasirika.

    Hakuishi mbali sana na kituo cha polisi cha Buguruni. Akatembea moja kwa hadi kituoni.

    “Vipi peter kumbe na wewe umeitwa?” Aliuliza kachero Dadi baada ya kumkuta koplo Peter Mkwabi akiwa pale kituoni.

    “Ee. Kuna mauaji mengine afande.”

    “Yanafanana na yale ya kwanza.”

    “Siyo kufanana tu. Aliyeuwawa safari hii ni mtoto wa yule mama.”

    “Nini? Ina maana Pili naye kauwawa?”

    “Yes. Tofauti na mauaji ya kwanza safari hii muuaji katumia kitu kizito kisha akamalizia na kisu kama kilekile.”

    “Kina mpini mwekundu nacho?”

    “Ndiyo afande, ni muuaji wa ajabu kabisa kwani kitu alichotumia kilitosha bila kuhitajika kile kisu. Nilikuwa nakusubiri kwani afande yuko eneo la tukio.”

    Kwa kuwa kulikuwa na hatua chache kutoka kituoni hadi eneo la tukio walilazimika kutembea kwa miguu.

    * * *

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hasira kali ilikuwa inarindima katika kichwa cha Inspekta Beda. Aliapa kumuua kwa mkono wake mtu aliyemuua Lucy. Lakini alishangazwa na kitendo cha muuaji huyo kufanya mauaji hayo kwani hakuwa na uhusiano wowote na familia ya mama Pili. Alijaribu kuchunguza kama kuliwahi kuwa na uhusiano fulani kati ya Lucy na familia ya mama Pili lakini akagundua hakuna uhusiano wa aina hiyo.

    Ripoti ya wataalamu wa vidole ilikuwa mbele yake. Bado ilionyesha kuwa muuaji wa watu wote watatu alikuwa mmoja. Anataka nini? Hili lilikuwa swali gumu kabisa lililopita kwenye kichwa cha Inspekta Beda. Alisaga meno kwa hasira. Haikuwa kawaida kwake kufanya kazi siku tatu kabla hajapata ufumbuzi au mwelekeo wa ufumbuzi lakini safari hii mambo yalionekana kutatanisha.

    Hata pale alipotajiwa Vero ndiye muuaji hakuweza kufikiria kabisa kuwa Vero huyo atakuwa ni mwanawe wa kumzaa ambaye amemtelekeza. Vero wake alikuwa mpole mwenye huruma. Huyu anayemsoma kwenye faili ni Vero kahaba tena muuaji. Hakuipa akili yake nafasi ya kupitisha wazo juu ya mwanawe.

    Akiwa kwenye lindi la mawazo simu ya kiganjani ikaita. Akaitazama vizuri. Ilikuwa inapigwa na Kachero Dadi, akashtuka kwani alishazoea simu za kachero yule mara nyingi hazikuwa na taarifa nzuri.

    “…. Kama yale ya kwanza lakini safari hii ni Kawe…”

    “…Nilipigiwa simu na mkuu wa kituo cha huku kwa sababu alipata taarifa kuwa tumeshikilia upelelezi wa mauaji yanayofanana na haya.”

    “Uko wapi sasa?”

    “Niko Kawe nimeshamaliza uchunguzi.”

    “Umegundua nini?”

    “Kuna uhusiano wa karibu kati ya mama Pili na marehemu.”

    “Mh. Haya mauaji yanaweza kuwa ni ya kisasi.” Aliongea Inspekta huku akishusha pumzi.

    “Vipi kuhusu Vero umejaribu kuhoji hapo.”

    “Ndiyo. Vero alikuwa house girl nyumba ya jirani huyu mama ndiye aliyemtoa na kumpeleka kwa mama Pili.”

    “Enhee. Angalau mwanga naanza kuupata huyo Vero alitokea wapi?”

    “Hapo pana ugumu afande kwani aliyemwajiri Vero kwa mara ya kwanza kwa sasa ni marehemu.”

    “He. Na yeye kauwawa?”

    “No. Huyu amekufa kwa ajali ya gari wakati anaelekea Morogoro.”

    “Duh. Mbona mambo yanazidi kuwa magumu?”

    “Sana. Maana huyu vero hafahamiki kabisa ni mtu wa aina gani maana anakuwa kama mzuka.

    Inspekta Beda aligonga meza kwa hasira. Matumaini ya kumpata muuaji yalikuwa madogo. Ili muuaji apatikane ilitakiwa aeendelee kuua jambo ambalo lingekuwa hatari zaidi. Vitu viwili vilimfanya Inspekta aone ugumu uliopo wa kumpata muuaji, Kulikuwa hakuna picha yoyote ya muuaji pia alikuwa hajulikani hata ndugu yake mmoja ambaye wangeweza kumdadisi mambo kadhaa. Ilikuwa ni ajabu kwake kwa mshukiwa kutojulikana kabisa hata maelezo ya awali.

    Alipitia kumbukumbu mbalimbali za kipolisi lakini bado hakufanikiwa kupata lolote kuhusu Vero. Katika orodha ya wahalifu aliyokuwa nayo wanawake walikuwa watatu tu tena wawili kati yao walishauwawa na Polisi wakati wa jaribio la kupora gari la mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya kiasia.



    “Vipi dada umemaliza kazi?” Aliuliza Sara huku akimkazia macho dada yake.

    “Angalia idadi ya visu kwenye begi.” Alijibu huku akijilaza pale kitandani.

    Sara alifungua begi la dada yake na kuanza kuhesabu idadi ya visu vilivypo.

    “Viko vinne.”

    “Wanaume wawili wanawake wawili.” Aliongea huku akijilaza kitandani na kujipongeza kwa jinsi alivyomuua mama Mwazani kule Kawe na kuwaachia kazi ngumu Polisi. Wakati akiwa pale kitandani akafungua Mkoba wake na kuchungulia akiba iliyopo. Ilikuwa inatosha kuendesha maisha yake kwa mwezi mmoja zaidi. Hizi zilikuwa fedha alizozipata baada ya kumuua Lucy. Akatabasamu. Alishanogewa na mchezo wa kifo. Alitamani kuua zaidi na zaidi…….

    Vero aliamka saa 1.21 akafungua mkoba wake kwa mara nyingine akatoa simu ya marehemu Lucy kisha akaiwasha ile. Ilipowaka tu ukaanza kuingia mfululizo wa meseji ambazo hazikupungua saba. Akafungua na kuanza kuzisoma. Moja ilimvutia zaidi. …… Lucy rafiki yangu uko wapi ukifungua simu naomba unipigie nime kumiss sana kila nikikutafuta hupatikani. Habiba. Akaamua kuijibu ile meseji. …… Pole Habiba mwenzio nishakufa siku nyingi naandika nikiwa kaburini jitahidi kuwafanyia wema binadamu wengine huku mambo ni magumu kuna mateso makubwa sana… Akaituma. Ukaja mlio ambao ulimuashiria kuwa meseji imepokelewa. Baada ya dakika kumi ikaingia meseji nyingine. ….Acha utani Lucy hayo masihara siyo mazuri….. Yalikuwa ni majibu ya ile meseji ya Vero. Kama huamini chukua hii namba ya mama kisha umpigie umuulize, sasa siwezi kuendelea kwani malaika wa adhabu yuko mbele yangu subiri niadhibiwe kama nitapewa tena nafasi nitakupigia…… Alijibu ile meseji kisha akazima simu.

    Moyoni alicheka kwa mzaha alioufanya. Alijua wazi jinsi gani yule binti atachanganyikiwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa mama mzazi wa Lucy. Lucy ni marehemu kweli lakini hii meseji kutoka kaburini kiboko…. Alicheka tena safari hii kwa sauti huku akimshangaza Sara ambaye muda mwingi alikuwa kimya akitafakari kuhusu mlolongo wa maisha yake.

    “Vipi mbona unacheka.”

    “Acha nicheke mdogo wangu.” Alisema kisha akamsimulia kuhusu zile meseji.

    Wote wakacheka.

    “Leo utaenda?”

    “Hapana, waliobaki natakiwa kuwa makini kwanza kuna wanaume wawili halafu Koku na mama yake.”

    “Kwa nini usiwasamehe.”

    “Hapana mdogo wangu, machungu ya ubaya wao hayawezi kuondoka kama wataendelea kuwa hai. Tone la mwisho la damu ndilo litakalo nifanya nijisalimishe mbele ya mikono ya sheria.”

    “Kwa hiyo utafanyaje kuhusu waliobaki?”

    “Natakiwa kupumzisha kichwa changu kwa siku mbili zaidi nikitafakari nini cha kufanya.”

    “Sawa.” Aliongea Vero kwa upole zaidi.

    “Halafu kwa nini unapenda kutumia kisu chenye mpini mwekundu?” Aliuliza Sara.

    “Ni rangi ambayo ninapoiona inanikumbusha wajibu wangu kwani ni rangi ya hatari pia kuna dhana kuwa ni rangi ya ukombozi, ndio maana nchi nyingi zilizokombolewa kwa vita bendera zake ni nyekundu.”

    “Mh. Dada una mambo, ungekuwa mwanasiasa sijui ingekuwaje.”

    “Mungu aninusuru, siasa ni kitu ambacho sitaki kukisikia kabisa katika maisha yangu.”

    “Kwanini?”

    “Sijaona watu madhalimu na wanafiki wakubwa kama wanasiasa usinitajie kabisa nasikia kichefuchefu.”



    * * *

    “Enhe. Amesema alikuwa anaongea kutoka kaburini?” Alihoji tena kachero Dadi huku Inspekta ambaye alikuwa kando yake akiwa amefura kwa hasira. “Ndiyo.” Alijibu Habiba huku akitoa ile simu yake na kufungua sehemu ya meseji.

    “Uliwahi kuongea naye.” Aliuliza tena kachero.

    “Hapana. Kwani baada ya kuniambia kuwa malaika wa adhabu amefika alizima simu.”

    Kachero Dadi alitamani kucheka lakini akajizuia kwa kuwa Inspekta alikuwa kando.

    Inspekta akaichukua simu ya yule binti, akaanza kusoma ile meseji. Akatikisa kichwa.

    “Sidhani kama huyu mtu ni mwanamke.”

    “Kwanini?”Aliuliza kachero

    “Si kawaida kuwa na mwanamke mjanja namna hii ambaye haogopi hata polisi.”

    “Umejuaje kuwa haogopi polisi?”

    “Angekuwa mtu mwenye woga asingethubutu kutumia simu ya marehemu wakati anajua wazi kuwa anatafutwa.”

    “Unajuaje kama muuaji ndiye anayetumia simu ya marehemu?” Aliuliza kachero.

    “Angekuwa mtu mwingine angetoa laini kisha akapachika ya kwake habari zingekuwa zimeisha.”

    “Mh. Aliguna kachero huku akikuna kichwa.”

    Baada ya dakika chache simu ya Inspekta ikaanza kuita. Akaangalia jina kabla ya kupokea. Moyo ukamlipuka kwa hofu.

    “Shikamoo baba.”

    “Wewe nani?” Alifoka Inspekta badala ya kujibu.

    “Ina maana toka niende kaburini mmeamua kufuta hata namba zangu?” Uliuliza upande wa pili.

    “Kwanza niambie wewe ni nani?”

    “Mimi ni Lucy baba.”

    “Uko wapi?”

    “Niko makaburini hapa Kinondoni nimepewa upendeleo wa kipekee kuongea na binadamu wenzangu.”

    “Sikiliza wewe ndama, siku nikikutia mikononi mwangu utajuta kuzaliwa.”

    “Usijitukane baba kama mimi ni ndama basi wewe utakuwa ng’ombe kamili kwa sabau wewe ndio baba yangu na hilo la kujuta kuzaliwa lisikupe tabu kwani siwezi kujuta mara mbili nimeshajuta na huku niliko bado naendelea kujuta, naona malaika anakuja kuniuliza maswali….”

    “Wewe usikate…” Alishachelewa kwani simu ilikatwa.

    “Mruhusu huyo binti aende kwani ishakuwa balaa hapa.” Aliongea Inspekta huku akiegemea kwenye kiti chake. Hakuna aliyetaka kujua Inspekta alikuwa anaongea na nani kwani simu yake ilikuwa kwenye mfumo wa ‘loud speaker’ Kachero alikuwa hoi kutokana na kujizuia na kicheko baada ya tukio lile la simu kutoka kaburini.

    “Unafikiri kwa nini ameamua kukupigia?” Aliuliza kachero huku akizidi kupata mateso ya kubana kicheko kilichokuwa kinamvizia.

    “Siwezi kujua lakini muuaji ni mtu anayejua nini anachokifanya.”

    “Una maana gani?”

    “Jinsi nilivyoongea nae ni wazi kuwa anajua anachokifanya pia kuna fumbo zito nahisi liko ndani yake…..”

    “….. kuna uwezekano mkubwa wa mahusiano kati ya mama Pili na Lucy, siwezi kujua ni uhusiano gani lakini nahisi upo kwani watu wote watatu aliowaua wana uhusiano isipokuwa huyu Lucy ambaye kuna kitu kama uhusiano ambao ulijificha.”

    “Tutawezaje kufahamu hilo.”

    “Ni vigumu kwani marehemu wameondoka na siri hii.”

    “Kwa upande fulani nataka kukubaliana na wewe hasa nikifikiria kitendo cha muuaji kuondoka na Lucy toka ofisini kwake hadi pale alipouwawa.”

    Simu ya Inspekta ikaanza kuita tena. Akaiangalia tena ile namba, safari hii alikuwa mkewe.

    “Enhe.” Aliuliza huku akijitayarisha kusikia taarifa za kuchukiza tena.

    “Kapiga tena yule mtu anatusalimia sana na anasema eti karibuni atatufuata tujumuike wote kaburini.”Aliongea mkewe. Inspekta alisikiliza bila kuongea lolote. Kuna nini mbona huyu muuaji anatuchezea sana? Alijiuliza Inspekta.

    Kama aliyezinduka usingizini akauliza.

    “Anasemaje nani atamfuata?” Aliuliza Inspekta huku hali ya hasira ikiwa imepotea kwani aliona wazi kuna tishio la mauaji mbele yake.

    “Atatufuata sisi.”

    “Achana nae mpumbavu bado kidogo nitamtia mikononi.”

    “Huuu.” Mkewe alishusha pumzi kisha akakata simu.

    “Unaona jinsi muuaji anavyonichezea?” Aliuliza Inspekta.

    “Mh. Afande hata mimi huyu mtu ananitatanisha sana.”

    “Ngoja niende nyumbani nikaongee na mke wangu huenda kuna kitu atakuwa anafahamu.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    * * *

    “Mbona unachukua visu viwili.” Aliuliza sara.

    “Huenda nikafanya mambo kulingana na idadi ya visu.’

    “Mh. Dada unatisha huogopi?”

    “Matatizo yanaondoa uoga.”

    “Mbona watanzania wana matatizo mengi lakini ni waoga.”

    “We hujui tu. Akitokea mpumbavu mmoja tu akawahamasisha waandamane ili wachome moto ikulu wataandamana tu kwani hawana cha kupoteza ndio maana ukichunguza waandamanaji wengi ni watu wenye maisha magumu hata siku moja huwezi kumshawishi tajiri aandamane.”

    “Mh. Dada una maneno kama msomi.”

    Akaweka visu vyake vizuri kwenye mkoba wake. Akampungia mkono mdogo wake akaondoka. Tofauti na mauaji mengine aliyoyafanya safari hii aliondoka akiwa na hofu kubwa. Wakati anataka kutoka mle ndani akakumbuka kitu. Ilikuwa ni hatari kwake kuondoka namna ile. Alijua wazi kuwa kulikuwa na ugumu mkubwa wa kazi iliyomkabili mbele yake.

    “Mbona unarudi? Aliuliza Sara.

    “Natakiwa kubadilisha mfumo wa kazi kwani iwapo nitaendelea na mfumo wa kawaida naweza kujikuta kwenye mikono ya dola kabla ya kumaliza kazi.”

    “Kivipi.”

    “Utaona.”

    Akarudisha vile visu kwenye begi kisha akaondoka na kwenda maeneo ya dampo.



    Akaanza kupekua pekua hatimaye akazipata nguo chafu zilizochanikachanika ambazo asingeweza kuvaa zaidi ya mwendawazimu. Akazichukua na kuziweka kwenye mfuko wake wa nailoni. Akatembea hadi sehemu alipolikuta gofu la nyumba. Akaangalia pande zote kuhakikisha usalama, hakukuwa na mtu aliyemuona wakati anaingia mle ndani. Akaingia na kuvaa yale mavazi. Chizi. Alikuwa kichaa kamili kama si ngozi yake ambayo bado ilikuwa na mng’ao wake wa kuvutia. Hakutaka chohote kimuumbue akatoka nje haraka, akatembea mpaka pale alipoona yamemwagwa mabaki ya mkaa. Hakutaka kujiuliza akaanza kujipaka vumbi lile la mkaa. Sasa alikamilika kama kichaa, akazidi kujitia uchafu kila alipouona………



    * * *

    “Mama aomba maji, mimi aa njaa ataka kula.” Kichaa aliendelea kumkera mke wa Inspekta ambaye tayari alikuwa na mawazo mengi kutokana na simu ya ajabu aliyoipata. Huku bado moyoni akiendelea kuuguza kidonda cha kufiwa na mwanae ambae alimpenda sana.

    “Njoo unywe na uondoke kabisa sitaki kukuona hapa unatia kichefu chefu.” Alilalamika mke wa Inspekta Beda. Akaanza kutembea kwa haraka kwenda ndani kumchukulia yule mwendawazimu maji ya kunywa. Mwendawazimu akiwa mwenye njaa na kiu alimfuata mama yule huku udenda ukimtoka hovyo. Mama Lucy akaingia kwenye chumba ambacho ndoo za maji zilikuwa zinahifadhiwa. Akafunua moja ya ndoo zilizopo mle chumbani. Hakuwahi kuchota yale maji. Mlango ukafungwa nyuma yake. Alipoangalia nyuma yake alisimama yule mwenda wazimu akiwa na bisu kubwa lenye mpini mwekundu. Ule udenda uliokuwa unamtoka haukuwepo tena.

    “We. Kichaa unataka nini?” Aliongea Mrs Beda kwa Kihoro.

    “Roho yako.” Alijibu yule kichaa kwa mkato.

    “Unanikumbuka?” Aliuliza yule kichaa huku akimkazia macho mama Lucy kwa namna ambayo ilimtisha.

    “Ha..ha..hapa..pana sikujui toka humu ndani.” Alifoka mama Lucy kwa ukali uliochanganyika na woga.

    “Unakumbuka kuna siku uliwahi kushirikiana wewe Lucy , Koku na Fred kununua sumu kwa ajili ya kumuua mtu fulani?”

    “Hapana.” Alikataa huku akionyesha mshituko mkubwa zaidi.

    “Najua unakumbuka vizuri sana, pengine ambacho huwezi kukumbuka ni kuwa mimi ndiye Vero mtoto wa yule mama na pia ni mtoto wa Inspekta Beda.” alitulia na kumwangalia yule mama ambaye alitokwa na haja ndogo kutokana na woga uliomkuta.

    “Sitaki niamini kuwa kuna mambo ya kishirikina umemfanyia baba yangu hata akaitelekeza familia yake lakini nataka nikudhihirishie kuwa nilikuwa nimejificha sehemu fulani siku mliyokuwa mnapanga kumuwekea sumu mama yangu. Ingawa miaka mingi imepita bado kumbukumbu yangu haiwezi kufutika mpaka pale sura yako na wenzako zitakapofutika kwenye uso wa dunia, pia naomba uelewe wazi kuwa mimi ndiye muuaji wa Lucy………” Hakumaliza hotuba ile ambayo haikuwa rasmi kwani yule mama alianguka kutokana na mshituko mkubwa alioupata. Haikuwa kazi kubwa kwa Vero bila huruma akakipitisha kisu katika shingo la yule mama. Damu zikamwagika na kutapakaa eneo lile. Hakukihitaji tena kile kisu. Akakiacha kisu pale pale.



     Damu zikamwagika na kutapakaa eneo lile. Hakukihitaji tena kile kisu. Akakiacha kisu pale pale. Akaichukua simu ya yule mama ambayo alikuwa ameivaa shingoni kwa kamba maalum. Akatafuta namba fulani fulani. Akaipata namba ya Koku. Akaanza kupiga namba ikawa inaita bila kupokelewa. Bahati ilikuwa upande wake ile simu ikakatwa kisha ikatumwa meseji niko getini nakuja.

    Mjinga amejileta mwenyewe. Aliwaza Vero.



    Akasimama nyuma ya mlango kwa umakini mkubwa. Koku akafungua mlango huku macho yake yakiwa kwenye simu. Alikuwa anaandika meseji. Hakupata nafasi ya kumaliza kuandika meseji kisu kikali kikapenya kwenye shingo lake. Akatapatapa bila kupiga kelele, hatimaye akakata roho.

    Akamshukuru Mungu kwa kumaliza kazi ile salama. Kazi iliyobaki hakuiiona kuwa kubwa sana kwani hata kama asingeimaliza bado alikuwa na furaha ya kumaliza robo tatu ya kazi yake. Akaandika meseji akamtumia Inspekta Beda.

    Bado wawili tu utapumzika.

    Akaanza kuondoka mle ndani taratibu lakini kabla hajafika getini akasikia mlio wa gari nje. Akarudi haraka ndani. Akaanza kuchungulia dirishani. Mungu wangu. Alishituka Vero baada ya kumuona Inspekta Beda akifungua geti huku akiwa ameongozana na askari wengine wawili. Nimekwisha.



    * * *

    Hofu iliyokuwa imetanda katika jiji la Dar es salaam ilianza kupungua baada ya taarifa za kukamatwa Vero. Magazeti karibu yote yalibeba taarifa hizi za kusisimua. Waandishi wa magazeti walikuwa na kazi ya ziada kuripoti mauaji haya. Watu sita walikuwa wameuwawa katika staili inayofanana, kilichosisimua zaidi ni mauaji ya familia ya Inspekta Beda. Hata waandishi walishindwa angalau kutia uongo kuwa mauaji haya yanahusiana na jambo lipi.

    Gumzo kubwa katika vijiwe vya kahawa lilikuwa ni juu ya muuaji huyu ambaye hutumia kisu chenye mpini mwekundu. Miongoni mwa watu waliokuwa kwenye wakati mgumu ni kachero Dadi Kasweyaga ambaye katika maisha yake ya kazi hakuwahi kukutana na tukio kama hili. Leo kidogo alikuwa kwenye ahueni baada ya Vero kukamatwa.

    Watu wengi walikuwa maeneo ya polisi chang’ombe wakijaribu kuchungulia ili waweze kumwona mwanamke aliyetikisa jiji la dar es salaam. Kukamatwa kwake kulikuwa gumzo kwa sababu alikuwa msichana mpole ambaye hakutegemewa kuweza kulitikisa jiji kubwa namna hii. Hofu ilikuwa imepunguwa watu wengi walikuwa na furaha.

    “Umesema unaitwa nani?”

    “Veronika Charles.”

    “Nataka kujua kwanini umefanya mauaji ya kutisha na kulitikisa jiji.” Aliendelea kuhoji Kachero Dadi.

    “Mimi?”

    “Kumbe naongea na nani?”

    “Nimemuua nani?”

    “Ebo. Unajifanya kushangaa sio?”

    “Unajua mnanichanganya sana mimi nimeuwa mtu.” Alishangaa Vero.

    “Swala sio kukataa kama umeua au hujaua tunachotaka kujua kwanza kwa nini ulimuua mama Pili kisha utamaliza kuhusu hao wengine.”

    “Mama Pili ninayemjua ni mmoja tu ambaye ni jirani yangu pale kinondon naye ni mzima.” Aliendelea kukanusha Vero. Kiasi fulani kachero Dadi aliaanza kushangazwa na jinsi huyu mwanamke anavyoongea kwa kujiamini huku akiwa na uhakika wa asilimia mia kwa kauli zake. Lakini asingeweza kusahau jinsi mwanamke huyu alivyokuwa mjanja kiasi cha kuwachachafya na kuwakejeli kwa kutumia simu.”

    * * *

    Huyu hakuwa na furaha. Taarifa za kukamatwa kwa Vero hazikumfurahisha hata kidogo. Alijua kuna makosa yamefanywa na polisi. Ni kweli aliyekamatwa ni Vero lakini si Vero muuaji ambaye anasakwa na jeshi hilo. Pengine ni jina tu ndio ambalo limemponza. Halafu alihisi kuwa huenda alipita eneo la tukio muda mfupi baada ya mauaji. Akaanza kurudiwa na fikra juu ya tukio lile.

    Baada ya kumuona Inspekta anakuja na askari wawili aliamua kujificha nyuma ya sofa lililoko pale sebuleni. Askari walishtushwa na mauaji yale lakini Ghafla, Inspekta akatoa amri mlango ufungwe askari waingie vyumbani waanze kumtafuta muuaji. Hapo Vero alijua kuwa amekwisha. Lakini akajiwa na wazo la ghafla. Akaiwasha ile simu ya marehemu na kuamua kujaribu bahati yake kwa kupiga namba ya Inspekta.

    Inspekta alipokea haraka haraka huku akipatwa na mshangao mkubwa.

    Akiwa kule nyuma ya sofa Vero aliamua kucheza karata ya mwisho, ilikuwa ni karata hatari kwani hakuwa na uhakika kama pale sebuleni kulikuwa na mtu amebaki au la.

    “Hallow afande nimefurahi sana kupishana na wewe wakati unaenda nyumbani kwako nafikiri umeshajionea mambo niliyoyafanya Mungu akipenda nitarudi tena kesho kuja kummalizia aliye baki.” Inspekta akapatwa na mshituko baada ya kupata simu hiyo. Akakosa umakini.

    “Nafikiri utafurahia kazi nzuri niliyoifanya hapo ndani kwani itakupa changamoto kubwa zaidi na kuchangamsha akili yako.” Akatulia kidogo kisha akakata na kuzima simu.

    “hallow twendeni haraka muuaji yuko nje tunaweza kumuwahi.” Wakatoka haraka haraka baada ya kupewa taarifa ya simu ile.

    Hakuwa na muda wa kupoteza hiyo ilikuwa karata yake ya mwisho. Walipotoka tu naye akatoka mle ndani. Akapita palepale getini. Akaanza kuimba na kutukana hovyo baada ya kutoka mle ndani. Hakuna aliyemjali, chizi nani angejishugulisha naye?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipofika mbele kidogo akamkuta Inspekta na wenzake wakimuhoji dada mmoja ambaye ni wazi alikuwa katika mizunguko ya kawaida. Akapishana nao bila kutiliwa mmashaka. Akashangaa kuona yule dada akifungwa pingu. Mwendawazimu huyooo akatokomea.

    Saa mbili na nusu usiku akaingia ndani ya gofu lile ambalo alificha nguo zake. Akabadili na kuvaa hijabu nzuri iliyomfanya afanane na mwanamke wa kiarabu au kisomali. Akatabasamu, ni wazi alikuwa anasherehekea ushindi wake Mkubwa alioupata. Alijishangaa hata yeye mwenyewe. Ni wapi alipata uwezo wa kufanya mambo makubwa kama yale.

    Akatembea taratibu kuelekea kule gesti. Alisikia raha, raha kubwa kabisa ndani ya moyo wake. Vilibaki visu viwili tu. Ilikuwa lazima avitumie.

    Aliingia chumbani na kumkuta Sara akiwa amelala.

    “Vipi mbona hujafunga mlango?” Aliuliza Vero.

    “Nilitaka usipate shida ya kubisha hodi.”

    “Kuwa makini, usirudie tena ni hatari.” Aliongea huku akipekua kwenye begi lake na kutoa taulo.

    “Vipi umemaliza?”

    “Bado wawili mmoja nitahitaji msaada wako.”

    “Kivipi?”

    “Nahitaji umvute hadi hapa ili nimalizie kazi yangu.”

    “Nitawezaje dada?”

    “Wanaume ni watu dhaifu sana tofauti na unavyofikiri, ukitumia nguvu watakushinda. Maneno mazuri tena yanayosindikizwa kwa sauti laini ya mahaba ni silaha tosha ya kumshawishi hata mkuu wa majeshi akainuka kitini na kukupigia saluti?”

    “Unafikiri wanaume wote ni dhaifu kiasi hicho?”

    “No. kuna wanaume wachache wenye uwezo mkubwa kifikra. Hawa ni hatari sana kwani huwezi kuwaangusha kwa maneno wala tabasamu lako lakini hawa ninaowakusudia ni walewale wa kawaida……..”

    “Samahani dada visu vimebaki viwili lakini nimegundua cha tatu ambacho si chekundu kama vile vingine….” Akamkatisha kabla hajamaliza kuongea.

    “Hicho sikutaka ukione lakini kuna shujaa mwanamapinduzi ambaye atakuwa wa mwisho kuuwawa kwa mkono wangu.” Alijibu na kuondoka huku akionekana wazi kutotaka maswali zaidi kuhusu hilo.

    * * *

    Fred alikuwa na huzuni kubwa kutokana na kifo cha mama yake na dada zake. Mara nyingi aliogopa kulala mle ndani peke yake kwani Inspekta hakurudi nyumbani kutokana na uzito wa majukumu yaliyomkabili. Mara nyingi alirudi nyumbani na kulala mchana kisha kukesha kazini usiku. Vitu viwili vilimpa moyo Fred, kwanza muaji alikuwa anaua wanawake tu pili alikuwa amekamatwa. Haikumwingia akilini kuwa muuaji anaweza kuendeleza tena kazi yake.

    Akaingia ndani na kukaa pale sebuleni. Mama yake alikuwa amezikwa yalibaki maombolezo tu. Alijua wazi kuwa ni yeye ndiye mrithi wa Inspekta Beda, lakini wazo moja lilimtisha je. kama Inspekta ataoa si itakuwa balaa. Akaanza kulia upya.

    Kilio chake kikakatishwa na mtu aliyekuwa anagonga mlango. Akafungua mlango. Akaingia msichana mwenye hijabu nyeusi.

    “Habari kaka Fredi.”

    “Nzuri za nyumbani.” Alijibu Fred huku akijaribu kukumbuka ni wapi alimuona huyo msichana bila kupata jibu.

    “Vipi mbona pako kimya sana Koku nimemkuta?” Swali hilo likazidi kumshangaza fredi kwani aliyekuwa anauliziwa hapo alikuwa marehemu.

    “Wewe ni nani?.” Aliuliza Fredi kwa mshangao mkubwa kabisa.

    “Hee. Mara hii umenisahau kaka Fred, mimi ni rafiki yake naitwa Mary nilikuwa masomoni Uganda.”

    “Duh. Samahani sana unajua nilikuwa najiuliza mbona sura yako kama niliiona mahali fulani, yaani si ngeni kabisa tena nilihisi kuwa kama nilikuona hapa nyumbani.”

    “Miaka miwili tu niliyokaa Kampala umenisahau hivi, ningekaa miaka kumi si ingekuwa balaa.”

    “Samahani sana Mary lakini Koku amekufa.”

    “Koku amekufa.” Alishituka akaanza kulia. Akalia kiasi ambacho Fredi alishikwa na huruma akaanza kumbembeleza. Kwa kisingizio cha kumbembeleza akawa anamshika maeneo ambayo kimaadili hakuruhusiwa. Kosa. Alishituka baada ya kuona yule mwanamke akiwa ameshikilia kisu chenye mpini mwekundu. Alikuwa anatafuta namna ya kujiokoa lakini alishachelewa kwani hakupewa muda wa kufikiria zaidi kisu kile kikapenya kwa nguvu upande wa kushoto wa kifua chake.

    “Naitwa Veronika Beda.” Alitamka huku akimkazia macho fred ambaye alikuwa anatapatapa kuipigania roho yake. Ingawa alikuwa anakata roho alishituka baada ya kutajiwa jina hilo. Wakakutanisha macho yao. Alitaka kuongea kitu… aliendelea kujaribu kuongea akaishia kwenye miguno ya mauti… Macho yake yakapoteza nuru ya uhai. Akakata roho.

    Akaangalia saa kubwa ya ukutani. Ilikuwa saa nane na nusu mchana. Akashituka, muda wa Samson Masanja kutoka kazini ulikuwa umekaribia. Akajikagua mwilini akagundua matone ya damu ambayo yalimezwa na weusi wa nguo yake. Hakuna ambaye angeweza kugundua kuwa ni matone ya damu kwani yalikuwa na rangi nyeusi kama nguo yenyewe.

    Akatembea hadi kituo cha magari ambacho kinajulikana kwa jina maarufu Studio. Akapanda daladala lililokuwa linaelekea Kariaoo. Kijana aliyekaa naye siti moja alijaribu kumchombeza kwa hili na lile lakini alikuwa kimya hakumjibu chochote na wala hakumsikia kwani mawazo yake yalikuwa hatua kadhaa nje kabisa ya daladala. Yule kijana alianza kuongea maneno ya kashfa. Vero akageuka wakakutanisha macho yao. Hakuendelea tena kuongea. Sura ya Vero ilitisha. Ilikuwa sura yenye ujumbe mzito ambao yule kijana alishindwa kuutafsiri lakini alijua ni ujumbe hatari. Sura ambayo haikutaka mchezo wala utani. Haikuwa sura ya kawaida ya kike. Yule kijana alijikuta akikosa amani pale alipokaa. Alitamani gari lifike ateremke. Alishaona balaa.

    Baada ya kuteremka Vero alitembea kwa kasi huku akikatiza mitaa mbalimbali ya Kariakoo. Baadae akafika katika viwanja vya mnazi mmoja, akaendelea kutembea kwa kasi huku akijitahidi kuwa makini na magari katika kituo cha mnazi mmoja. Akavuka salama, akaingia mtaa wa Jamhuri.

    Akatembea kwa kasi hadi alipokifikia kituo cha mafuta cha BP.

    “Habari yako dada.”

    “Nzuri nikusaidie nini?”

    “Naweza kumpata Samson Masanja.”

    “Mh. Wiki ya pili sasa Samson kalazwa katika Hospitali ya Amana.”

    “Unaweza kunielekeza chumba alicholazwa?”

    “Ukiingia pale Receiption uliza VIP wakikuelekeza nenda chumba namba 9 ndiko alikolazwa.”

    Akaondoka huku akimshukuru yule dada.



    DUKA LA VIFAA VYA HOSPITALI. Maandishi hayo yalimvutia Vero ambaye moja kwa moja aliingia mle dukani.

    “Hili shilingi ngapi?” Aliuliza huku akishika koti jeupe la hospitali.

    “Elfu kumi na tano.” Alijibu yule muuzaji huku akilitoa lile koti kwa mti maalum.

    “Nipatie hilo.” Alisikika huku akitoa kiasi alichoambiwa.

    Akaliweka kwenye mfuko wake kisha akaondoka.

    Baada ya nusu saa alikuwa maeneo ya Ilala. Akaingia moja kwa moja pale hospitali. Akatembea moja kwa moja hadi mapokezi.

    “Habari dada.”

    “Salama nikusaidie nini?”

    “Naomba unielekeze VIP.”

    “VIP ni huku (huku akinyoosha kidole) lakini kwa sasa huruhusiwi kwa sababu huu si muda wa kuona wagonjwa.” Alijibu yule dada wa mapokezi ambaye kabla ya kufika Vero alikuwa anasinzia pale dirishani.

    Vero akaondoka pale dirishani na kuelekea upande alioelekezwa. Bila kujali onyo alilopewa. Yule dada wa mapokezi hakumwangalia Vero wakati anaingia kule viliko vyumba vya VIP. Hakuingia moja kwa moja. Akaingia chooni na kuvaa koti lile jeupe ili asiweze kusumbuliwa kwani korido ilikuwa ndefu mpaka kukifikia chumba namba 9.

    Alipishana na manesi wawili ambao walionekana kuwa busy huku wakitoka chumba kilekile alichotaka kuingia. Akaingia mle chumbani. Chumba kilikuwa na vitanda viwili lakini mgonjwa alikuwa mmoja.

    “Samson.” Aliita Vero

    Mgonjwa dhaifu aliitika kwa sauti yenye mikwaruzo.

    “Nani.” Aliuliza mgonjwa huku akikohoa.

    “mimi ni Vero unanikumbuka?”

    “Sogea nikuone macho yangu hayaoni mbali.”

    Vero akasogea karibu na mgonjwa.

    “Umenikumbuka?” Aliuliza Vero huku akianza kuingiwa na huruma kutokana na hali ya samson Masanja.

    “Bado.”

    “Unamkumbuka mama Pili, yule mama wa Buguruni ambaye alikuwa anafuga machangudoa?” Aliuliza huku huruma aliyokuwa nayo ikianza kupotea. Akamuona mgonjwa akishtuka kidogo.

    “Sina muda wa kupoteza mimi ni mmoja wa watu ambao kwa kutumia fedha zako uliweza kutuambukiza virusi, Nimekuja kuchukua roho yako. Kwani hustahili kifo cha kiungwana kama hiki cha hospitali.” Alimaliza na kuchomoa kisu chake chenye mpini mwekundu.



    *****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa anakaribia kupatwa na wazimu kwa mshituko alioupata baada a kifo cha Fredi. Veronika alikuwa amekamatwa. HUYU ANAYEFANYA MAUAJI NI NANI? Lilikuwa swali lisilojibika. Alifungua tena tepu ndogo ambayo ilikuwa imerekodiwa wakati makachero wanamuhoji Veronika.

    “Nimeshindwa sasa kama munataka kunua niueni tu…..” Alifoka Vero kwenye kinasa sauti kile. Akasimama na kuanza kuzunguka zunguka huku akikuna kichwa chake.

    Ni muda huu ambao akili yake ilikuwa kama imerudi. Akaanza kumkumbuka mkewe Vick na mama yake. Alishangaa kugundua kuwa siku zote hizo hakupata hata fursa ya kujiuliza wako wapi.

    Upweke uliotawala kwenye nyumba yake ulimfanya atokwe na machozi mara kadhaa.

    UKO WAPI MAMA. Aliwaza huku akimkumbuka mama yake mzazi, mama ambaye alikuwa na huruma ya kweli mama ambaye aliyatoa maisha yake kwa ajili ya manufaa ya mwanae. Alianza kutokwa na machozi baada ya kuikumbuka familia yake.

    Akakumbuka kuwa mkewe alikuwa mjamzito. Amejifungua? Au ameolewa na mwanaume mwingine? Akainama pale mezani. Upweke ulikuwa unamsulubu fikra zikarudi nyuma akakumbuka jinsi alivyomfokea mkewe mpaka akaamua kutoroka. Aliowathamini wote wamerudi mchangani.

    Wakati akiwa kwenye dimbwi la mawazo simu yake ikaanza kuita. Akaitazama ile namba akazidi kuchanganyikiwa. Namba ya marehemu Lucy ndiyo iliyoingia.

    “Hallow habari Inspekta.”

    “Ongea unachotaka kuongea.”

    “Bila salamu?”

    “Haya nzuri ongea.”

    “Nataka ufahamu kuwa mimi ni muuaji mwenye huruma kama mama yako mzazi. Kama una kumbukumbu mama yako aliwahi kwenda mahali kumuokoa dada ambaye alikuwa anakaribia kuambukizwa virusi vya ukimwi na mumewe. Hivyo kwa kufuata moyo nzuri wa mama yako na mimi napenda kumuokoa huyo dada munayemshikilia hapo. Moja napenda utambue kuwa mimi ndiyo Vero, pili naona kazi zenu hamfanyi kitaalamu hivi askari wakubwa kama nyinyi mnashindwa kuoanisha alama za vidole za mtu munayemshuku na zile zilizoko kwenye visu, huyo dada mnamuonea tu kama unakumbuka vizuri siku ya tukio ulipishana na mwendawazimu ambaye ndio mimi, pia napenda kukufahamisha kuwa tayari nimemaliza kazi kwa mtu wa mwisho nenda chumba namba 9 upande wa VIP katika hospitali ya Amana.”

    Simu ilikatwa Inspekta akainua simu yake ya mezani. Akiwa amechanganyikiwa kabisa akampigia kachero Dadi kasweyaga.

    “Hallow vipi afande.” Ilisikika simu upande wapili

    “kuna mauaji mengine Amana.”

    “Tumeshapata taarifa na maiti yake pamoja na ile ya Fredi zote ziko hospitali ya Taifa ya Muhimbili nilikuwa nakuja kukupa taarifa.”

    “Halafu naomba huyo Vero aachiwe nafikiri mahojiano na aina ya matukio yanayotokea hahusiki kabisa.” Alimaliza Inspekta kisha akaegemea kiti chake tena.

    Akili yake ilifanya kazi kuliko uwezo wake wa kawaida. Swali moja alilojiuliza ni kuhusu muuaji ambaye ameweza kutoa historia ya maisha ya mama yake siku za nyuma. Huyu mtu ni nani na anataka nini. Hilo ni swali lililopita katika kichwa cha Inspekta. Akatoa simu yake akajaribu kupiga katika namba za Lucy. Simu ilikuwa inaita.Hatimaye ikapokelewa.

    “Enhe.” Iliuliza sauti kwa dharau kidogo.

    “Nataka kujua ni kwanini umefanya mauaji mengi kiasi hicho?”

    “Kwa kuwa muda wangu wa kuishi umekwisha nitakufahamisha kila kitu.”

    “Tutaonana vipi?”

    “Unakumbuka vizuri pale ulipokulia?”

    “Una maanisha nini?”

    “Unaikumbuka ile nyumba ya mbagala ambayo ilikuwa ya marehemu baba yako?”

    “Ndiyo nakumbuka vizuri.”

    “Tukutane pale saa 12.30 Jioni.”

    “Sawa.” Simu ikakatwa.



    * * *

    Huku hofu ikiwa imeutawala moyo wake Inspekta alitembea Taratibu kuelekea eneo walilokubaliana kukutana. Alipapasa mfuko wake wa kushoto. Bado bastola yake ilikuwepo. Alikuwa amedhamiria kuua ingawa alijiuliza sana kwa nini muuaji ametaka wakutane eneo lile. Siku hii hakuvaa sare zake za kazi. Alipofika eneo lile la kihistoria kwake akashangaa kuona jinsi lilivyochakaa huku likiwa limezungukwa na majumba makubwa ya kisasa.

    Nyumba yao ilikuwa imeanguka upande mmoja. Alipoangalia vizuri ndipo akashtuka baada ya kuwaona mabinti wawili waliokuwa wamekaa kwenye gogo lile la mnazi ambalo alikuwa anapenda kukaa miaka mingi iliyopita.

    “karibu.” sauti tulivu ya Vero ilimkaribisha.

    Ulikuwa mshtuko wa mwaka. Asingeweza kumsahau Vero kwani alifanana sana na mama yake mzazi. Aliyemshangaa pale ni yule binti mwingine ambaye alifanana na mkewe Vick.

    “Vero. Unafanya nini hapa?” Aliuliza Inspekta huku akionekana wazi kuchanganyikiwa na kusahau dhamira yake ya kumuua muuaji.

    “Baba, si unamtaka muuaji. Niko mbele yako nifanye utakacho lakini kabla ya yote naomba nikusimulie kila kitu kuhusu mauaji yale.” Huku machozi yakimtoka akasimama na kuanza kumsimulia Inspekta.

    “…….. kutokana na ile sumu mama yangu aliishi siku chache hatimaye akapoteza maisha akaniacha mimi, Sara na bibi yetu ambaye alipoteza maisha kutokana na kuzidiwa na homa za mara kwa mara ambazo zilisababishwa zaidi na ukosefu wa chakula bora. Baba tazama hayo makaburi….” Inspekta akaangalia kule alikoelekezwa kidole. Ndio kwanza akagundua kuwa kulikuwa na makaburi mawili. Hilo la kwanza ni la mama yangu Vick ambaye alikupenda akayapigania maisha yako kwa nguvu zake zote lakini ukamtesa na kumnyanyasa na hilo la pili ni la mama yako mzazi, amekufa hata mazishi yake hujahudhuria………. Narudia tena mimi ndio muuaji na sababu zangu nishakueleza.”

    Sara na Inspekta walikuwa wanamwaga machozi. Sara alikuwa analia kwa kuliona kaburi la mama yake. Inspekta alikuwa analia kutokana na mjeledi aliopigwa katika maisha yake.

    “Baba sioni tena thamani ya kuendelea kuishi mimi ni muathirika yanipasa kumfuata mama na bibi, naomba umtunze huyo sara….”

    “Hapana mwanangu usiniache peke yangu….” Inspekta alilia kama mtoto mdogo huku akimbembeleza Vero ambaye alikuwa ameshika kisu mkononi.

    “Hapana Vero mwanangu usifanye hivyo dawa ya ukimwi ishagunduliwa mwanangu.” Alibembeleza Inspekta huku akimnyooshea mkono mwanawe asithubutu kujiua.

    “Dada utaniacha na nani kama utakufa.” Sara naye alilia akimbembeleza dada yake asijiue.

    “Usijali Sara nimekufikisha mbele ya baba yako atakutunza mimi naondoka.”

    “Veroooooooooo.” Aligumia Sara kwa uchungu wakati akimshuhudia dada yake akididimiza kisu kifuani kwake mwenyewe.

    Damu ziliruka zikarukia kwenye blauzi nyeupe ya Sara. Vero alikuwa anakata roho huku akimwangalia mdogo wake kwa macho yaliyojaa huruma. Sara aliinama pale alipolala dada yake na kumshikilia mabegani huku akilia kwa uchungu.

    “Kwanini dada, kwa nini ufe.” Aliendelea kulalamika Vero.

    Inspekta naye aliendelea kulia kwa sauti kubwa. Huku akimwangalia mwanae alivyokuwa anakata roho. “Sara.” Aliita Vero. “Nakk…..kk..mh….” Haijulikani alitaka kuongea nini akakata roho.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MWISHO



0 comments:

Post a Comment

Blog