IMEANDIKWA NA : RAYMOND MWALONGO
*********************************************************************************
Simulizi : Siri Ya Furaha
Sehemu Ya Kwanza (1)
Wakati wa majira ya saa sita mchana, hali ya hewa ilikuwa shwari katika jiji la Dar es salaam lililotawaliwa na jua kiasi. Watu walionekana wakiwa katika mihangaiko yao ya kujitafutia riziki katika kipindi hicho cha mwezi wa kumi na mbili. Akili zao zilikuwa zimetawaliwa na mawazo juu ya sikukuu za mwisho wa mwaka ambazo walipaswa kuzigharamia ili kwenda sawa na utamaduni wa kila mwaka. Lamos Maputo, akiwa kijana miaka thelathini na saba alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa katika pilikapilika za mihangaiko hiyo ya mwisho wa mwaka. Akiwa mwenyeji wa Shinyanga, tayari alikuwapo jijini na familia yake kwa miezi kadhaa akijitafutia riziki.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ugumu wa maisha kwa kipindi cha miaka mingi ndio uliomchanganya Lamos kwani hata wakati huo alionekana akiongea peke yake. Alikuwa amebeba kikapu kikubwa ambacho kilikuwa na samaki ndani yake aliowanunua eneo la Feri, Posta. Huku akiwa katika mavazi duni, kikapu hicho kilionekana kikichuruzika maji ambayo yalikuwa yakiendelea kulowanisha shati lake alilokuwa amevaa. Kodi ya nyumba, afya ya mwanae pamoja na biashara yake iliyokuwa inasuasua ndivyo vitu vilivyosababisha awe anaongea peke yake barabarani. Wakati huo alikuwa amepewa siku tatu tu ili akamilishe kodi ya nyumba aliyokuwa amepanga Kimara, huku akielezwa kuwa angefukuzwa kama angeshindwa kutimiza agizo hilo. Mwanaye pekee Veronika alikuwa na matatizo ya kiafya kwani naye alikuwa uvimbe mkubwa kichwani mwake. Mtoto huyo aliyekuwa na mwaka mmoja alimchanganya zaidi Lamos kwani uvimbe wake ulikuwa ukiongezeka siku hadi siku.
Tayari madaktari wa hospitali ya taifa ya Muhimbili walishamweleza kuwa kama angendelea kumchelewesha mwanaye kufanyiwa upasuaji basi ubongo wa mtoto huyo ungeweza kuhalibika na mwishoe mwanaye angekuwa hana akili timamu. Jambo hilo Lamos hakuhitaji litokee kabisa kwani alimpenda sana mwanaye huyo pekee lakini hakujua jinsi ambavyo angeweza kupata kiasi cha shilingi laki tano kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo la upasuaji.
“ sijui hizi samaki nitauza leo….Vero naye ahh! Kodi ya nyumba” alisikika Lamos akiongea kwa nguvu huku akivuka barabara ili apande magari yaliyokuwa yakielekea Kimara. Alikuwa akivuka barabara bila hata kuangalia magari yaliyokuwa yakipita huku akiwa hana hofu hata kidogo. Ghafla zilisikika kelele za wapita njia ambao waliliona gari moja la mizigo lililokuwa likijongea kwa kasi eneo alilokuwapo Lamos aliyekuwa akivuka barabara kuu taratibu. Mbali ya kelele hizo zilizopiwa na watu, Lamos hakusikia na juhudi za dereva pekee ndizo zilizoonekana kwani alifunga breki kali ya gari hilo lililoburuzika huku mlio mkubwa wa breki za gari hilo ukisikika.
Wakati huo ndio Lamos alishtuka, gari hilo lilikuwa tayari kando yake kidogo kwa sentimeta chache huku likiwa limemkosa. Dereva wa gari hilo alishuka akiwa na hasira, alionekana kama alitaka kumpiga Lamos ambaye hakujali jambo kwani alianza kuondoka taratibu eneo hilo kama hakukuwa na tukio lililokuwa limetokea. Mwonekano wake ndio uliompa hisia dereva huyo aliayeamini Lamos alikuwa hana akili timamu. Hata watu waliokuwa karibu na eneo hilo walitarajia kuona akiomba msamaha lakini hakufanya hiyo. Mwishoe dereva wa gari hilo aliondoka na gari lake eneo hilo huku akiwa na jazba.
Lamos hakuwa na hofu huku akionekana mtulivu kama hakuna jambo lililokuwa limetokea. Tayari alikuwa katika daladala iliyokuwa ikielekea Kimara ambako alikuwa akielekea.Gari alilopanda lilianza kuondoka eneo la feri huku abiria waliokuwamo katika gari hilo wakionekana kumshangaa Lamos ambaye alikuwa mbali kimawazo na alionekana kutojali ajali iliyotaka kutokea. Baada ya saa moja waliwapo maeneo ya Kimara Mwisho eneo ambalo Lamos alikuwa akiishi, alionekana akishuka huku akiwa amebeba kikapu chake cha samaki mikononi.
“we baba…! uwe mwangalifu jamani” alisikika mwanamke mmoja wakati Lamos akipita kando ya siti aliyokuwa amekaa. “wewe mwanamke usinifanye mtoto mdogo mimi najua ninachofanya niwe mwangalifu wa nini?” alilalama Lamos akioenkana kukerwa na kauli aliyoambiwa. Abiria wengine waliamua kuingilia jambo hilo kwa kumtuliza Lamos ambaye aliweka kikapu chake chini na kuanza kumkalipia mwanamke huyo. Hasira zake zilimfanya aanze kuelezea matatizo yake ya familia, jambo lililowaudhi abiria hao waliokuwa wakimtuliza ili ashuke.
Baada ya dakika moja aliamua kushuka huku akionekana kuendelea kuongea peke yake juu ya jambo hilo. Abiria wengi walibaini kuwa Lamos hakuwa sawa kutokana na mambo aliyokuwa akiyafanya. Lamos alianza kuvuka barabara huku akiwa amejitwisha kikapu chake cha samaki lakini pia hakuwa ameangalia magari huku akiendelea kuongea. Kulikuwa na pikipiki iliyokuwa katika kasi ikiwa upande wa barabara ya magari yaingiayo jijini. Pikipiki hiyo ilikuwa imeongozana na gari moja dogo la kutembelea, dereva wake alishtuka baada ya kumwona Lamos akiwa katikati ya barabara. Alijaribu kufunga breki za pikipiki yake kwa nguvu lakini jambo hilo halikusaidia kwani pikipiki hiyo iliishia kwenye mguu wa kushoto wa Lamos ambaye hakuiona pikipiki hiyo.
Watu kadhaa waliokuwa karibu na eneo hilo la barabara walistuka kwa namna tofauti huku wengine wakionekana kupiga kelele ikiwa ni baada ya kumshuhudia Lamos akirushwa umbali wa mita kadhaa toka eneo la ajali huku akiwa anapiga kelele kama mtoto mdogo. Dereva wa pikipiki hiyo pia alirushwa umbali wa mita kadhaa toka eneo hilo na magurudumu ya pikipiki hiyo yalionekana yakizinguka kwa kasi huku pikipiki ikiwa inajizungusha eneo hilo. Watu walijongea kwa kasi eneo la tukio wakiwa na shauku ya kuwaangalia wahanga wa ajali hiyo. Dereva wa pikipiki hiyo alionekana akiwa amekaa eneo aliloangukia huku akiwa na michubuko kadhaa hata watu walipofika eneo alilokuwapo aliwawaeleza hakuwa na maumivu sana.
Hali ilikuwa tofauti kwa Lamos ambaye mguu wake wa kushoto ulionekana dhahiri ukiwa umevunjika, damu ilikuwa ikimvuja pia kichwani katika majeraha aliyokuwa ameyapata. Alikuwa na majeraha mengine mengi sehemu tofauti za mwilini mwake na zaidi kwa wakati huo alikuwa amezimia. Watu waliofika kumwangalia waliamua kumsogeza kando ya barabara wakiwa na lengo la kutafuta gari la kumwahisha hospitali. Baada ya dakika moja, yeye pamoja na dereva wa pikipiki walipakizwa katika gari moja la dogo lililokuwa la mpita njia na safari ilianza wakielekea hospitali. Wakati zoezi hilo likiendelea watu wengine walikuwa wakinufaika nalo kwani baadhi yao walionekana wakiokota samaki ziliokuwa za Lamos huku wengine wakitaka kupigana kabisa.
Baada ya dakika arobaini, gari lililowabeba lilionekana likiwasili katika hospitali kuu ya taifa ya Muhimbili na wauguzi wakishirikiana na wapitanjia waliowapeleka majeruhi hao walisaidiana kuwapeleka katika chumba maalumu ili wapate matibabu ya awali. Watu waliowasindikiza majeruhi hao wakiwa nje ya chumba hiho walionekana wakilisimulia tukio la ajali hiyo huku wakimtaja Lamos kuwa ndiye aliyekuwa na makosa kwa kuvuka barabara bila kujali usalama wake dhidi ya vyombo vya moto vilivyokuwa vinapita.
* * * *
Mama Vero kama wengi walivyomzoea katika mtaa aliokuwa akiishi maeneo ya Kimara Mwisho, alikuwa mkewe mpendwa wa Lamos. Mbali na ugumu wa maisha waliokuwa nao katika familia yao hakuthubutu kufikiria kurudi nyumbani kwao wilayani Kahama, mkoani Shinyanga. Alikuwa akiamini wangefanikiwa siku moja na mume wake katika maisha yao. Wakati huo, majira ya jioni alikuwa katika mawazo tele huku akiwa amemshika mwanaye Veronika ambaye alionekana akiwa na uvimbe katika kichwa chake. Alikuwa akiwaza juu ya matatizo yaliyokuwa yakiikabili familia yao likiwapo tatizo la uvimbe wa mwanao kichwani. Jambo jingine lililokuwa likimuumiza kichwa lilihusina na kodi ya nyumba kwani aliamini haingeweza kupatikana ndani ya siku tatu walizokuwa wamepewa.
Siku hiyo alikuwa akishangaa kwani mumewe hakurudi nyumbani majira ya mchana kumwangalia mwanao aliyekuwa anaumwa kama ilivyokuwa kawaida yake kufanya hivyo kila siku. Alikuwa ametulia chumbani kwao kwani hakupenda kutoka nje ambako wanawake wenzie wapangaji walikuwa na majungu juu ya kushindwa kwao kumtibu mwanao na kulipa kodi. Alikuwa hajala kitu kwa siku nzima zaidi ya uji ambao alikuwa akimlisha mwanaye. Majira ya saa moja na nusu aliitwa na mpangaji mmoja nje ambaye alimweleza kuwa alikuwa na mgeni. Alitoka nje akiwa na shauku ya kumwona mgeni ambaye alikuwa akimhitaji.
Mara baada ya kutoka nje alionesha dhahiri mshtuko baada ya kumwona mjumbe wa nyumba kumi wa mtaa huo ambaye alikuwa namfahamu. Alianza kuhisi mjumbe huyo alikuwa amepewa jukumu la kuwatoa nje ya nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi baada ya kushindwa kulipa kodi. Alijongea taratibu eneo alilosimama mjumbe huyo ambaye alionekana akiwa mnyonge pia. “pole sana mama mumeo amepata ajali na muda huu yupo Muhimbili amelazwa” ilikuwa sauti ya mjumbe huyo mara baada ya kusalimiana na mkewe Lamos.
Taarifa hiyo ilimumaliza nguvu mwanamke huyo ambaye alikaa chini kabla ya kuanza kulia kwa uchungu. Mjumbe huyo akishirikiana na wapangaji kadhaa walichukua jukumu la kumtuliuza kutokana na mshtuko aliokuwa ameupata. Baada ya nusu saa alitulia na kutambua kuwa jambo hilo lilikuwa limeshatokea na alielewa ujasiri ndiyo pekee uliopaswa kupewa nafasi katika matatizo waliyokuwa nayo. Aliamua kuelekea chumbani kwao na kumchukua mwanaye kabla ya kumbeba. Alikuwa akiwaza kuelekea Hospitali ili kwenda kumwangalia mumewe. Jambo lililoanza kumtatiza tena lilihusiana na nauli hakuwa na fedha hata kidogo. Uoga ulikuwa ukimwingia kila alipofikiria kuwaomba msaada wa fedha wapangaji wenzie. Baada ya muda mrefu wa kufikiri alipuuzia hofu yake, aliamua kwenda kuwaomba fedha wapangaji ili aweze kuzitumia kwenye usafiri wa daladala kuelekea Muhimbili. Ilichukua dakika kadhaa kwa wapangajia hao walioonesha dharau kumchangia mkewe Lamos kiasi cha shilingi elfu moja. Alishukuru kwa msaada huo kabla ya kuanza kuondoka kuelekea katika kituo cha daladala. Alikuwa tofauti na watu wengi waendao kuwaangalia wagonjwa kwani hakuwa na kitu chochote alichobeba huku akiamini Mungu angemtangulia hata juu ya chakula cha mgonjwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Majira ya saa tatu kasoro alikuwa katika wodi la wanaume huku mapigo yake yakimwenda mbio kwa shauku ya kutaka kumwona mumewe. Alikuwa ameshaelezwa kuwa alikuwapo katika wodi hilo la nne, kitanda namba ishirini na tano. Baada ya kutembea kwa muda mfupi alikifikia kitanda hicho kabla ya kumwona mumewe akiwa na majeraha sehemu nyingi za mwili wake na zaidi alionekana akiwa amevunjika mguu wake uliokuwa umezungushwa na bandeji maalumu. Lamos alishtuka kumwona mkewe kabla ya kutoa tabasamu la mbali, wakati huo alikuwa ameshazinduka baada ya kuzimia. Mkewe alianza kulia kwa uchungu na Lamos ndiye alionekana akimtuliza. Naye alikuwa amechanganyikiwa kwani hakujua hatma ya maisha yao. Baada ya muda mfupi alitulia na walionekana wakiongea huku mwanao akiwa amelala wakati huo. Pembeni ya kitanda alichokuwa amelala Lamos kulikuwa na vyombo vya chakula vilivyoashiria kuwa alikuwa amekula muda mfupi uliokuwa umepita. Jambo hilo lilimpa faraja kidogo mkewe ambaye alivuta pumzi ndefu.
Baada ya mazungumzo ya muda mfupi mkewe aligundua kuwa mumewe alinunuliwa chakula na mtu aliyemgonga na pikipiki ambaye hakuwapo hospitali hapo wakati huo. Mara baada ya kupata matibabu katika majeraha yake machache aliyoyapata mmiliki wa pikipiki aliyemgonga Lamos alihurusiwa kuondoka hospitalini hapo. Alikuwa ameahidi kurudi kumwangalia Lamos siku iliyofuata. Akiwa amekata tamaa juu ya suala zima la kula chakula mkewe Lamos alipata faraja majira ya saa nne, wakati ambao mumewe alikuwa amelala. Alimwona mama mmoja akipita na chakula kilichokuwapo kwenye sahani na alionekana kama alikuwa anaenda kukitupa.
“samahani mama unakipeleka wapi hicho chakula?” alisikika mkewe Lamos akimuuliza mama huyo. “…Aah! mgonjwa wangu ameshindwa kula kwa hiyo nataka nikitupe kitaharibika” alisikika akimjibu mama mmoja wa makamo ambaye alimpa nafasi mkewe Lamos kukiomba chakula hicho ambacho alipewa.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao hospitalini hapo kwa muda wote waliokuwapo.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao hospitalini hapo kwa muda wote waliokuwapo. Mara kadhaa mmiliki wa pikipiki aliyemgonga Lamos alikuwa akiwatembelea ingawaje hakuwasaidia sana kifedha. Wodi walilokuwapo kwa wiki moja, watu waliwatambua na kila chakula kilichokuwa kikibaki walikuwa wakiwapatia kwani hawakuwa na fedha hata kidogo za kununua chakula. Wakati huo walikuwa wakifikiria kuondoka hospitali hapo ili warudi nyumbani kwao walikopanga maeneo ya Kimara Mwisho. Waliwaza jambo hilo kwa vile gharama za matibabu zilikuwa zikiongezeka kadri siku zilivyokuwa zikisogea na jambo hilo lilikuwa likiwaongeza hofu kwani hawakujua jinsi ambavyo wangelipa gharama hizo.
Lamos aliamua kumwomba kijana aliyemgonga kwa pikipiki amsaidie kumlipia gharama hizo za hospitali kwani hakuwa na msaada mwingine. Ndugu zake wengi walikuwapo mkoani Shinyanga ambao hawakuwa na mahusiano mazuri. Wachache waliokuwapo jijini hakuwa na mawasiliano nao na alitambua haingekuwa rahisi kusaidiwa. Kijana aliyemgonga kwa pikipiki alijitahidi kutafuta fedha ambazo hatimaye alilipia hospitali kabla ya Lamos kuhurusiwa kuondoka akiwa amekaa wiki mbili hospitali hapo. Walimshukuru sana kijana huyo hasa baada ya kuutambua ukweli kwamba Lamos ndiye alikuwa chanzo cha ajali iliyotokea. Kijana huyo alifanya ubinadamu baada ya kugundua Lamos hakuwa na msaada wowote. Alikodi pia teksi aliyohitaji impeleke Lamos na mkewe maeneo ya Kimara walikokuwa wakiishi.
Hatimaye waliondoka hospitalini hapo huku Lamos aliyepewa gongo la kumsaidia kutembea akiwa na faraja kidogo. Ndani ya gari yeye na mkewe walikuwa watulivu huku wakionekana kama walikuwa wakiwaza jambo. Hivyo ndivyo ilivyokuwa vichwani mwao walikuwa wakiwaza jinsi ambavyo wangekabiliana na matatizo waliyokuwa nayo.
Akiwa amevunjika mguu Lamos alitambua kuwa alihitaji fedha za kulipa kodi ya nyumba na zaidi fedha kwa ajili ya upasuaji wa uvimbe uliokuwapo kichwani kwa mwanao kwani ulikuwa ukiongezeka siku hadi siku. Hakujua hatma ya mambo yote hayo jambo lililomfanya ashike kichwa chake mara kadhaa.
Kuna wakati kila alipowaza kuwa alikuwa akielekea nyumbani kwake, moyo wake ulikuwa ukishtuka kwa hofu. Alikuwa akimtambua mama mmiliki wa nyumba aliyopanga kuwa hakuwa mtu mzuri hata kidogo. Aliamini mama huyo angeendelea kumdai kodi ya nyumba hata akiwa katika hali yake hiyo ya kuumwa. Baada ya dakika arobaini na tano za kutembea na gari barabarani hatimaye walikuwa wakijongea taratibu na katika nyumba waliyokuwa wamepanga. Mioyo yao ilikuwa ikiripuka kwa hofu hata amani waliyokuwa nayo kidogo ilianza kupotea.
Mkewe Lamos ghafla alianza kutokwa na machozi kabisa wakati wakiwa mita kadhaa kuifikia nyumba waliyokuwa wamepanga. Alikuwa ameiona taswira ya nje ya nyumba hiyo ambayo hakuifikiria hata kidogo. Mwonekano uliokuwapo nje ya nyumba hiyo ndiyo uliomchanaganya kabisa hata Lamos ambaye pia alishtuka kwa kushika kichwa chake. Vyombo vyao vyote vilikuwa vimetolewa nje ya nyumba hiyo huku vikionekana kama vilikuwapo eneo hilo la nje kwa siku kadhaa. Jambo lililowaumiza zaidi vyombo hivyo vilikuwa vimenyeshewa na mvua katika kipindi hicho ambacho mvua ilikuwa ikiendelea kunyesha jijini Da es salaam.
Mara baada ya kushuka katika teksi hiyo ya kokodi waliishia kukaa nje huku mkewe Lamos akiendelea kulia ilhali Lamos mwenyewe akionekana kuchanyanyikiwa. Walikuwa wakishangaa jinsi watu wa eneo hilo walivyokosa utu wa kushindwa kuwahifadhia vitu vyao. Walikosa jibu la kumzungumzia mama aliyekuwa akimiliki nyumba hiyo ambaye alishindwa kuwa na uvumilivu. Baada ya kukaa eneo hilo la nje kwa muda wa saa moja waliweza kuyatambua mambo kadhaa likiwapo lililomhusu mama mwenye nyumba hiyo. Alikuwa ameondoka asubuhi ya siku hiyo akielekea Moshi, mkoani Kilimanjaro. Waligundua unyama wa mama huyo aliyewakataza wapangaji wengine kutojaribu kumhifadhia Lamos vitu vyake vilivyokaa eneo hilo la nje kwa siku tatu. Alikuwa amefunga chumba alichokuwa akikaa Lamos na familia yake na tayari kulikuwa na mtu mwingine aliyekilipia aliyetarajiwa kuhamia eneo hilo muda wowote. Wapangaji na watu kadhaa waliokuwa wakikaa karibu na nyumba hiyo walikuwa wakiogopa kujaribu kutoa vitu vya Lamos kwani waliamini kuwa mama mwenye nyumba hiyo alikuwa mshirikina. Kwa muda wa miaka kadhaa alikwisha wapangisha nyumba yake watu tofauti na alikuwa tabia za kuwadhalilisha kwa namna hiyo wapangaji walioshindwa kulipa kodi. Viongozi wa eneo hilo walikuwa wakimwogopa pia mama huyo jambo lililowafanya wasiingile mzozo wowote na wapangaji wake.
Mbali na mambo hayo ambayo Lamos aliyafahamu, hayakubadilisha hata kidogo taswira ya moyo wake kwani alikuwa akimchukia kila mtu aliyekuwa katika nyumba hiyo. Wote aliwaona hawakuwa na utu na hakuhitaji msaada wowote kutoka kwao. Hata ilipotimia saa moja jioni wapangaji hao waliwaita Lamos na mkewe ili walale katika vyumba vyao lakini walikataa msaada huo. Lamos alipandwa na hasira juu ya msaada huo na alionekana akiwatukana mara kadhaa. Jambo hilo liliwafanya wapangaji hao watulie katika vyumba vyao.
Lamos alikuwa amebakiwa na shilingi mia saba tu, hakuwaza kula hata kidogo kama ilivyokuwa kwa mkewe. Ila aliwaza kutumia fedha hizo kumnunulia chakula mwanao, hivyo ndiyo alivyofanya. Alimtuma mkewe akanunue juisi pamoja na mkate na baada ya dakika kadhaa alirudi. Mara baada ya mwanao kula walionekana wakiongea juu ya jambo ambalo wangelifanya siku iliyofuata hasa baada ya mambo kuwa magumu. Walibaki wakijifariji katika eneo walilokuwa wamekaa huku wakiwa wamejifunuka shuka wakati huo mwanao alikuwa amelala na eneo hilo lilikuwa tulivu kwani watu wengi walikuwa wamelala. Hawakujua jambo ambalo wangelifanya siku iliyofuata kwani walishindwa kwa kuanzia kutatua matatizo yao.
Majira ya saa sita usiku walianza kuchanganyikiwa baada ya mingurumo ya radi kuanza kusikika huku kukiwa na kila dalili za kunyesha kwa mvua. Walibaki wametulia eneo hilo wakitamani mvua hiyo isinyeshe kutokana na karaha waliyokuwa nayo wakati huo.
Kadri dakika zilivyozidi kusogea ndivyo dalili za mvua hiyo kunyesha zilivyozidi kuongezeka. Hatimaye mvua ilianza kunyesha taratibu huku Lamos na mkewe wakibaki wanatazamana. Walikuwa wamekata tamaa na walionekana kuwa tayari kwa jambo lolote ambalo lingeweza kutokea. Baada ya dakika kadhaa mvua hivyo iliongeza kasi huku ikiwa imechukua taswira mpya kwani ilikuwa ya mawe. Walibaki wametulia eneo hilo huku wakiwa wamejiegesha katika upande mmoja wa kabati lao kubwa. Mvua hiyo ilikuwa ikiwanyeshea kidogo kutokana na kabati hilo lililokuwa linawazuia.
Walikuwa wamemfunika mwanao kwa mashuka yote yaliyokuwapo ili asiipate karaha hiyo ya mvua iliyokuwa ikiendelea. Tayari mguu wa Lamos ulionekana ukiwa umelowa ikiwa pamoja na nguo walizokuwa wamevaa. Wapangaji kadhaa walionekana wakiwaangalia kupitia madirisha yao, waliingiwa na huruma lakini Lamos na mkewe walishawaeleza kuwa hawahitaji msaada wowote. Mvua hiyo ya mawe iliongezeka maradufu jambo lililomfanya Lamos amweleze mkewe waondoke eneo hilo. Lamos alionekana akivuta gongo lake tayari kwa kuondoka na mkewe wakiwa na mwanao ambaye alikuwa ameamka huku akiwa amenyeshewa na mvua pia na zaidi alikuwa analia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati wakijiandaa kuondoa kuna upepo wa nguvu ulivuma na kabati lililokuwa pembeni yao lililonekana likiyumbayumba. Mwishoe lilianza kuanguka, likielekea eneo walilokuwa wamekaa. Ghafla walishtushwa na mlio uliotokea kichwani mwa mwanao mara baada ya kabati hilo kutua kichwani mwa mtoto huyo. Lamos alichanganyikiwa kusikia mlio huo uliotokea kichwani kwa mwanao na alihisi kuwa huenda mwanao wangempoteza kabisa usiku huo kwani alikuwa na uvimbe mkubwa kichwani mwake. Walilisogeza haraka kabati hilo pembeni na eneo walilokuwapo kabla ya kusimama wakiwa na lengo la kuondoka. Wakati huo mwanao alikuwa akilia kwa sauti kubwa kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata. Sauti aliyokuwa akiitoa ndiyo iliyommpa shaka zaidi Lamos kwani hakuwahi kusikia toka kwa mwanaye huyo. Alielekeza mkono wake wa kulia na kumshika kichwani kabla ya kugundua mwanaye huyo alikuwa akitokwa na damu eneo hilo la kichwani. Hata alipouelekeza mkono wake mbele ya macho yake, kwa mwanga hafifu uliokuwapo aligundua mwanao alikuwa akitokwa na damu kwani mkono huo ulikuwa na damu.
Walitembea taratibu wakiondoka eneo hilo kwa vile Lamos hakuweza kutembea haraka kwa kutumia gongo lililomsaidia kutembea huku akiwa amevunjika mguu wa kushoto. Baada ya dakika ishirini wakiwa wamenyeshewa sawasawa walikuwa wakijikinga mvua hiyo katika kituo cha daladala. Ni wakati ambao waligundua uvimbe wa mwanao ulikuwa umepasuka huku mtoto huyo akitokwa damu pamoja na usaha. Hawakujua hatma ya mtoto huyo aliyekuwa akiendelea kulia, mkewe Lamos naye alionekana akitokwa na machozi pasipo kujitambua.
Walikaa eneo hilo la kituoni mpaka asubuhi wakati ambao mvua ilikuwa imetulia. Waliamua kurudi eneo lililokuwa na vyombo vyao, wakati huo Lamos aliwaza jambo. Alihitaji kuongea na mjumbe wa nyumba kumi ili amsaidie katika tatizo alilokuwa nalo na zaidi la mwanaye. Alitekeleza zoezi hilo kwa kwenda kuongea na mjumbe wa eneo hilo ambaye alimwahidi kuchangisha fedha kwa wakazi wa eneo hilo ili mwanae Lamos afanyiwe upasuaji haraka iwezekanavyo. Baada ya zoezi hilo Lamos aliamua kurudi katika eneo lililokuwa na vyombo vyake, nje ya nyumba aliyopanga awali huko aliungana na mkewe. Wakiwa na faraja kidogo walikuwa wakisubiri fedha ambazo waliamini mjumbe wa nyumba kumi angewachangisha watu wa eneo hilo.
Wakati wakiwa eneo hilo Lamos alikuwa amewasha redio yake ndogo na alikuwa akisikiliza kituo kimoja cha redio. Majira ya saa nne asubuhi wakati akiendelea kusikiliza matangazo ya kituo hicho cha redio alisikikia tangazo moja aliloamini lingebadili maisha yake kwa wakati huo. Lilikuwa ni tangazo lililomhusu mganga wa jadi aliyekuwa akitokea katika jiji la Vadodara nchini India ambaye alikuwapo nchini akiwa amefikia mkoani Morogoro. Mganga huyo aliyepelekea tabasamu la mbali katika paji la uso wa Lamos alikuwa akihusika na magonjwa mbalimbali. Pia alikuwa akihusika kumwezesha mtu kuwa tajiri, jambo hilo ndilo lililomvutia Lamos na alianza kuingiwa na ndoto ambazo hakuwahi kuzifikiria katika maisha yake.
Wazo la kufuata utajili kwa mganga huyo kutoka India hakumhusisha hata mkewe ambaye bado alikuwa kwenye majonzi ya matatizo yao. Lamos moyoni alijenga nia ya kuwa tayari kwa masharti yeyote ili awe tajiri. Majira ya saa moja jioni mjumbe aliyekuwa amewaahidi kuchangisha mchango kwa ajili ya upasuaji wa uvimbe wa mwanao alifika. Alikuwa amefanikiwa kuchangisha kiasi cha shilingi laki mbili ambazo bado hazikutosha kitu. Kutokana na maelezo ya awali ya madaktari walihitajika kuwa na kiasi kisichopungua laki tano.
Lamos alimshukuru kwa mchango huo mjumbe wa nyumba kumi huku akimweleza kuwa siku iliyofuta wangeenda katika hospitali kuu ya taifa ili kuangalia uwezekano wa kufanyiwa upasuaji kwa mwanao huyo. Wakati akitoa shukurani hizo alikuwa na mawazo tofauti na yale ambayo mkewe na mjumbe walikuwa nayo. Alikuwa akiwaza kuzitumia fedha hizo kumwahi mganga wa jadi Kamaraj Sankar kutoka nchini India ambaye alikuwa akizunguka sehemu tofauti duniani. Aliwaza kufanya jambo hilo kwani alikuwa akitambua kuwa mganga huyo alikuwa nchini kwa siku saba tu na baada ya hapo alikuwa akielekea India.
Lamos alimshukuru kwa mchango huo mjumbe wa nyumba kumi huku akimweleza kuwa siku iliyofuta wangeenda katika hospitali kuu ya taifa ili kuangalia uwezekano wa kufanyiwa upasuaji kwa mwanao huyo. Wakati akitoa shukurani hizo alikuwa na mawazo tofauti na yale ambayo mkewe na mjumbe walikuwa nayo. Alikuwa akiwaza kuzitumia fedha hizo kumwahi mganga wa jadi Kamaraj Sankar kutoka nchini India ambaye alikuwa akizunguka sehemu tofauti duniani. Aliwaza kufanya jambo hilo kwani alikuwa akitambua kuwa mganga huyo alikuwa nchini kwa siku saba tu na baada ya hapo alikuwa akielekea India.
Mkewe Lamos alikuwa na shauku ya kuona mwanao anafanyiwa upasuaji siku iliyofuata na aliamini jambo hilo lingempa amani moyoni mwake. Kuhakikisha jambo hilo alimweleza mumewe wampigie simu daktari ambaye aliwapa maelezo ya fedha zilizokuwa zikitakiwa kwa ajili ya upasuaji wa mwanao. Walitekeleza zoezi hilo na daktari huyo aliwaeleza kuwa iliwapasa watatute kiasi cha laki tatu ili kukamilisha malipo ya upasuaji huo. Mkewe Lamos alichanganyikiwa zaidi kusikia maelezo hayo lakini Lamos ambaye moyoni alipoteza utu kwa mwanaye alimuondoa shaka. Alimweleza kuwa siku iliyofuata wangeenda na mwanao hospitali ili afayiwe upasuaji na fedha ambazo zingebaki wangemalizia baada ya upasuaji.
Wakati akieleza hayo Lamos alikuwa akiwaza kumtoroka mkewe na mwanaye siku iliyofuata ili aelekee mkoani Morogoro. Baada ya mikakati yao juu ya upasuaji wa mwanao siku iliyofuata waliamua kwenda katika nyumba ya kulala wageni baada ya kuhofia kunyeshewa na mvua kama ilivyowatokea.
Majira ya saa nne usiku baada ya chakula, mkewe Lamos na mwanae walikuwa wamelala katika nyumba moja ya wageni iliyokuwapo maeneo ya Kimara. Lamos alikuwa bado hajalala huku akifikiria jinsi ambavyo angeenda kuupata utajiri kutoka kwa mganga wa jadi bwana Kamaraj kutoka India. Upendo aliokuwa nao kwa mwanaye na mkewe kwa miaka kadhaa ulikuwa umepotea ghafla kwani alikuwa amechoka maisha ya karaha. Alipitiwa na usingizi majira ya saa tano na nusu usiku lakini ilipotimia kumi na moja alfajiri alikuwa ameshtuka kutoka usingizini. Ni wakati ambao alianza kushuka taratibu toka katika kitanda cha nyumba hiyo ya kulala wageni huku akiwa amemwacha mkewe na mwanaye kitandani hapo.
Alivaa shati lake kwa utulivu ambalo lilikuwa limetundikwa nyuma ya mlango wa chumba walichokuwapo. Baada ya zoezi hilo alionekana akijipapasa mifuko yake ya suruali kabla ya kubaini kuwa alikuwa na fedha zote. Alibeba gongo lake lililokuwa likimsaidia kutembea baada ya kuvunjia mguu, mbali na gongo hilo alibeba funguo za chumba hicho. Alitembea taratibu kabla ya kufanikiwa kutoka katika chumba hicho, baada ya zoezi hilo aliurudisha mlango wa chumba hicho taratibu kabla ya kuufunga kwa funguo alizozichukua. Alianza kutembea taratibu akitoka katika nyumba hiyo ya kulala wageni. Alipolifikia eneo la mapokezi ambalo halikuwa na mtu wakati huo aliziweka funguo hizo mezani. Hatimaye aliongoza moja kwa moja mpaka barabara kuu ielekeayo Morogoro.
Alikaa barabarani kwa muda wa robo saa kabla ya kupata gari lililokuwa likielekea mkoani Morogoro. Mara baada ya kuingia katika gari hilo na kukaa katika siti aliyoipata alijihisi akipata amani moyoni mwake kwani aliamini mwanzo wa mafanikio yake ulikuwa umefika. Akiwa njiani alikuwa akirifikiria jina la Kamaraj Sankar, mganga wa jadi kutoka India ambaye aliamini angebadili maisha yake. Majira ya saa tatu kasoro alikuwapo katika kituo kikuu cha mabasi cha mkoani Morogoro. Wakati huo aliutumia kuwauliza watu kadhaa juu ya mganga huyo kutoka India. Zoezi hilo halikuwa gumu kwani mganga huyo alikuwa ameshapata umaarufu wa kutosha ndani ya siku tano alizokuwapo. Hiyo yote ilitokana na watu wengi kusafiri kutoka sehemu tofauti za Tanzania ili kwenda kutatua shida zao.
Mganga huyo alikuwa amefikia katika msitu mmoja uliokuwa karibu na safu za milima ya Uruguru. Lamos aliamua kukodi teksi ili impeleke katika msitu huo, jambo hilo lilifuata baada ya kugundua kulikuwa na foleni kubwa kwa mganga huyo ambaye alibakiwa na siku mbili za kuwapo nchini. Teksi aliyokodi iliondolewa kwa kasi katika kituo hicho cha mabasi kabla ya kufuata barabara iliyoelekea katika safu za milima ya Ururguru. Baada ya saa moja Lamos alikuwa katika foleni kubwa ya watu walikuwa wakienda kumwona mganga wa jadi bwana Kamaraj Sankar kutoka nchini India. Walikuwa katika kivuli cha msitu uliokuwa katika eneo hilo ambalo lilikuwa tulivu huku zikisikika kelele za watu pamoja na zile za ndege waliokuwa msituni.
Lamos alikuwa amebakiwa na kiasi cha shilingi laki moja na nusu ambazo aliamini zingemtosha katika tatizo alilokuwa nalo. Katika foleni hiyo kulikuwa na wagonjwa kadhaa ambao pia walihitaji kumwona mganga huyo wa jadi. Hakukata tamaa kutokana na karaha zilizokuwapo katika foleni hiyo na hakuwa tayari kuondoka bila kuonana na mganga huyo aliyekuwa akitoa huduma yake katika hema kubwa lililotengenezwa eneo hilo huku akiwa na wasaidizi wengi. Magari zaidi ya hamsini ya kifahari ya matajiri toka sehemu tofauti waliokuwa na nia ya kukutanana na mganga huyo pia yaliyomwongeza hamasa ya kuhakikisha anatimiza adhma yake.
Majira ya saa kumi na mbili kasoro jioni ndiyo alikuwa akitembea na gongo lake taratibu akijongea katika eneo alilokuwa amekaa mganga huyo ndani ya hema hilo. Kulikuwa na wasaidizi wake wengine zaidi ya kumi ndani ya hema hilo ambao wote walikuwa wahindi lakini msaidizi mmoja ambaye alikaa karibu na mganga huyo alikuwa mwafrika. Hatimaye Lamos alifika eneo alilokuwapo mganga huyo ambaye alimhurusu akae huku wakiwa wanatazana. Alimtazama msaidizi wake aliyekuwa mwafrika na kwa ishara ya kichwa alimhurusu amuulize kitu Lamos. “shida yako ni nini?” lilikuwa ni swali toka kwa msadizi wa mganga huyo toka India. “ nahitaji utajiri…” alijibu Lamos haraka huku akionekana akijiweka sawa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Msaidizi wa mganga huyo ambaye Lamos alianza kuhisi alikuwa Mtanzania alionekana akizungumza kwa lugha aliyohisi ni ya kihindi akimwambia mganga huyo huduma ambayo Lamos alikuwa akiihitaji. Mganga huyo alimweleza jambo msaidizi wake huyo ambaye alisikika tena “ unaulizwa utayaweza masharti utakayopewa..?” “ndiyo nitayayeza.. yoyote yale” alijibu tena Lamos. Baada ya kutoa jibu hilo msaidizi wa mganga huyo alimweleza tena mganga huyo bwana Kamaraj Sankar. Hatimaye Lamos aliambiwa aweke kiasi cha shilingi laki moja na elfu ishirini katika kitambaa cheupe kilichotandikwa na msaidizi wa mganga huyo wa jadi. Aliona kama bahati yake kwani alikuwa na kiasi cha shilingi laki moja na nusu pekee. Bila kupoteza muda aliweka fedha hizo alizoambiwa katika kitambaa hicho cheupe. Mganga huyo alikiviringisha kitambaa hicho kikiwa na fedha hizo kabla kukitupia katika boksi dogo lililokuwa pembeni yake.
Baada ya sekunde kadhaa Lamos alishtuka kuona moshi ukitoka katika boksi hilo alilotupia fedha hizo. Zilipita sekunde kadhaa tena kabla ya moshi huo kupotea, mganga huyo wa jadi aliuelekeza mkono wake wa kulia katika boksi hilo kabla ya kutoa karatasi moja. Aliinyanyua karatasi hiyo iliyokuwa imeandikwa `Goldern Watch` maandishi ambayo Lamos alifanikiwa kuyasoma pia. Maandishi hayo aliwaonesha wasaidizi wake wa kihindi waliokuwa wamesimama pembeni kidogo na eneo hilo walilokuwa wamekaa.
Baada ya sekunde kadhaa msaidizi mmoja wa kihindi aliipeleka kwa mganga huyo saa moja ambayo ilikuwa ikivutia sana kwa mwonekano huku ikiwa ya dhahabu. Mganga huyo aliipokea kabla ya kuonekana akimpa maelezo msaidizi wake wa kiafrika aliyekuwa kando yake. Baada ya dakika moja maelezo hayo yalikuwa yamekamilika.
Msaidizi wa mganga huyo aligeuka na kuanza kumpa maelezo Lamos juu ya jambo la kufanya. Alielezwa kuwa ilimpasa aitupe saa hiyo porini kwa nguvu huku akiwa amefungwa kitambaa usoni. Saa hiyo alielezwa kuwa ilipaswa itafutwe kama Lamos angeshidwa masharti ambayo angepewa na ilipaswa itafutwe pia kama angeamua kuachana na utajiri wa masharti ambayo angepewa. Saa hiyo ndiyo ingekuwa dawa kwa Lamos kurudi katika maisha ya kawaida.
Lamos alikubaliana na maelezo hayo na wasaidizi wa mganga huyo walijongea na mmoja wao alimfunga kitambaa ambacho hakikumruhusu kuona. Walianza kutembea naye akiwa ameishika saa hiyo ya dhahabu aliyokuwa amepewa huku akisaidiwa na gongo lake pamoja na wasaidizi hao. Walitembea kwa muda wa dakika kadhaa huku Lamos akitambua kuwa walikuwa nje kabisa ya hema walilokuwapo. Eneo hilo lilikuwa na miti mingi ambayo mingine matawi yake yalikuwa yakimgusa usoni. Lamos alielezwa aitupe saa hiyo katika eneo hilo ambalo hakulitambua. Alitekeleza jambo hilo kwa kuitupa saa hiyo kwa nguvu zake zote na aliamini aliitupa kwa umbali mrefu kutoka na nguvu alizotumia. Hatimaye akisaidiwa tena na wasaidizi wa mganga Kamaraj Sankar alirudishwa tena katika hema alilokuwapo huku akiwa bado hajafunguliwa kitambaa usoni. Mara baada ya kukaa katika eneo alilokuwapo awali ndani ya hema hilo, wasaidizi wa mganga huyo walimfungua kitambaa walichomfunga na alielezwa jambo lililokuwa likifuata lilikuwa masharti ya utajiri ambao angepewa.
Lamos alitikisa kichwa akiashiria kuelewa jambo hilo huku akiwa mtulivu akisubiri masharti hayo, msaidizi mmoja aliipeleka karatasi nyingine iliyokuwa na masharti kwa msaidizi wa kiafrika ili amsomee Lamos. “Sharti la kwanza, toka leo mpaka mwisho wa maisha yako huhurusiwi kuoa wala kufanya tendo la ndoa” alisikika msaidizi huyo na Lamos alitikisa kichwa akiashiria kuelewa jambo hilo baada ya sekunde kadhaa za kutafakari. “Sharti la pili, kama una mtoto wa kike au wa kiume basi ukifa atarithi mali zako katika misingi ya masharti haya, yaani asioe au kuolewa lakini pia asifanye tendo la ndoa”. Lamos alitikisa kichwa tena akiashiria kulielewa sharti hilo. “onyo ukikiuka masharti hayo au mwanao atakaye kurithi basi utafilisika na kuwa mwehu, hivyohivyo kwa mwanao, kama utashindwa masharti hayo utapaswa uje uitafute saa uliyoitupa eneo hili wewe au mwanao na ukiipata umtafute bwana Kamaraj Sankar popote Duniani na ndiye atayetengua makubaliano haya” alimaliza msaidizi huyo na Lamos alitikisa kichwa kuashiria kuelewa masharti hayo aliyopewa kwenye karatasi pia.
Hatimaye Mganga huyo wa jadi alioenekana kuelewa kila jambo lililokuwa limekubalika. Alielekeza mkono wake katika boksi moja kati ya maboksi kadhaa yaliyokuwapo. Alitoa dola kumi na mbili za kimarekani zilizokuwa sawa na elfu kumi na mbili za kitanzania kwa wakati huo. Alielezwa fedha hizo azitumie kuanzisha biashara yeyote na ndani ya mwezi mmoja angekuwa tayari mmoja wa matajiri. Alielezwa kama angeyafuata masharti aliyopewa angeweza kuwa tajiri mkubwa Afrika na mwishoe dunia ingemtambua.
Lamos aliondoka akiwa na furaha huku akiwaza utajiri tu mbali ya masharti aliyopewa, aliona si kitu kwani alikuwa amechoshwa na karaha za maisha. Mara baada ya kutoka katika hema hilo alibahatika kupata msaada wa kusafiri kwa kutumia gari la mtu mmoja ambaye alikuwa akitokea kwa mganga huyo. Wakati huo alikuwa akiwaza kuanza biashara ndani ya mkoa huo wa Morogoro na baada ya mafanikio aliwaza kuhamia jijini Dar es salaam. Muda wote alikuwa na furaha huku akijipapasa mifuko yake kuangalia dola kumi na mbili alizokuwa amepewa. Siku hiyo alipanga kulala katika nyumba ya kulala wageni na siku iliyofuata aliwaza kuanza kufanya biashara. Aliwaza kwenda benki siku iliyofuata kabla ya jambo lolote kwani huko alihitaji kubadilisha dola hizo kumi na mbili za kimarekani alizokuwa amepewa.
Kama alivyopanga siku iliyofuata asubuhi na mapema mara baada ya kuamka alielekea benki akijikongoja na gongo lake na mara baada ya kubadilisha dola hizo za kimarekani na kupata elfu kumi na mbili za kitanzania aliongoza katika maduka ya jumla ya mkoani hapo. Alinunua soksi pamoja na leso, baada ya kupata vitu hivyo akitumia fedha zote alizozibadilisha, alielekea eneo la kituo cha mabasi. Ndoto za kuwa tajiri alioziona zikijongea kwa kasi tofauti na alivyotarajia kwani ndani ya saa moja alikuwa amemaliza vitu hivyo. Jambo lililomshangaza zaidi hakuwa akitangaza bidhaa zake kama walivyofanya wenzie. Alikuwa ametulia sehemu moja aliyokaa kwa vile mguu wake ulikuwa bado haujapona huku akitumia gongo kutembea . Baada ya vitu hivyo kuisha aliamua kwenda kununua tena, wakati huo ilikuwa kama awali tena, majira ya saa sita alipohesabu fedha alizokuwa nazo mara baada ya kuuza bidhaa hizo kwa mara ya pili aligundua alikuwa na shilingi laki moja na elfu ishirini. Fedha hizo zilikuwa zaidi ya mauzo ambayo alikuwa ameyafanya, jambo hilo lililompa hamasa ya kuamini ndani ya siku kadhaa angekuwa tajiri. Aliamua kwenda kununua tena bidhaa hizo na wakati huo aliongeza nyingine huku akiwa na imani ya kuziuza kama ilivyokuwa awali.
* * * *
Ndoto za kuwa tajiri alioziona zikijongea kwa kasi tofauti na alivyotarajia kwani ndani ya saa moja alikuwa amemaliza vitu hivyo. Jambo lililomshangaza zaidi hakuwa akitangaza bidhaa zake kama walivyofanya wenzie. Alikuwa ametulia sehemu moja aliyokaa kwa vile mguu wake ulikuwa bado haujapona huku akitumia gongo kutembea . Baada ya vitu hivyo kuisha aliamua kwenda kununua tena, wakati huo ilikuwa kama awali tena, majira ya saa sita alipohesabu fedha alizokuwa nazo mara baada ya kuuza bidhaa hizo kwa mara ya pili aligundua alikuwa na shilingi laki moja na elfu ishirini. Fedha hizo zilikuwa zaidi ya mauzo ambayo alikuwa ameyafanya, jambo hilo lililompa hamasa ya kuamini ndani ya siku kadhaa angekuwa tajiri. Aliamua kwenda kununua tena bidhaa hizo na wakati huo aliongeza nyingine huku akiwa na imani ya kuziuza kama ilivyokuwa awali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
* * * *
Mkewe Lamos aliumia sana baada ya kugundua kuwa Lamos alikuwa ametoroka na kumfungia na mwanaye katika nyumba ya kulala wageni waliyokuwa wote. Jambo hilo lilimfanyaa alie muda wote huku akiwa amechanganyikiwa na zaidi akiwa hajui hatma ya mwanaye ambaye alikuwa uvimbe kichwani. Uvimbe huo ndio uliomwongeza majonzi kwani ulikuwa ukiongezeka kadri dakika zilivyozidi kusogea na zaidi mtoto huyo alikuwa ameishiwa nguvu na alitoa macho kama mtu aliyekaribia kufariki. Wakati huo wa majira ya saa nane mchana mkewe Lamos alikuwa akizunguka zunguka katika mitaa ya Kimara Mwisho huku akiwa amembeba mwanaye. Alikuwa akiogopa kumwendea tena mjumbe wa nyumba kumi ambaye aliwasaidia kuchangisha fedha kwa watu wa mtaani kwao. Aliamini mjumbe huyo asingemwelewa hata kidogo kwa vile fedha hizo alizochangisha mumuwe alikuwa ametoroka nazo.
Majira ya saa tisa mchana akiwa amechanagnyikiwa alipata wazo, aliwaza kwenda kuomba msaada katika kanisa moja la kikistro lililopo maeneo ya Kimara Mwisho. Hakupoteza muda alianza kutembea kwa haraka akielekea katika kanisa hilo na aliamini wachungaji wa kanisa hilo wangemsaidia. Baada ya robo saa alikuwa akijongea katika mlango wa mbele wa kanisa hilo, kabla hajaufikia alimwona mchungaji mmoja mwenye asili ya Ujerumani akitoka katika kanisa hilo. Alimwita kwa nguvu mchungaji huyo aliyemfahamu kwa vile alikuwa akiabudu katika kanisa hilo. Mchungaji huyo alishtuka baada ya kuitwa na alipogeuka alimwona mkewe Lamos ambaye alionekana hakuwa sawa. Nguo zake zilikuwa zimelowa jasho huku akiwa hajavaa hata viatu, nywele zake zilikuwa zimevurugika na alionekana kuhitaji msaada wa jambo.
“mama tatizo yako nini mpaka iko katika hali hiyo” alisikika mchungaji huyo mwenye asili ya Kijerumani kwa Kiswahili kisicho fasaha.
“mwanangu baba! mwanangu anaumwa sana…… ona baba uvimbe alionao kichwani” alisikika mkewe Lamos huku akimwonesha mchungaji huyo uvimbe ambao mwanaye Veronika alikuwa nao kichwani. Mchungaji huyo alimsogele mtoto huyo kabla ya kumshika kichwa akiuchunguza uvimbe huo. Alionesha kushtuka sana baada ya kuuona uvimbe uliokuwapo kichwani kwa mtoto huyo, jambo lililomshtua zaidi ilikuwa harufu ambayo iliitoka katika uvimbe huo. “imefanya nini hii mtoto jamani, mama nenda kwa gari pale mimi iko kuja” alisikika mchungaji huyo huku akimwonesha mkewe Lamos gari lililokuwapo karibu na eneo walilosimama.
Mkewe Lamos alitembea kujongea katika gari hilo na mchungaji huyo alielekea kanisani na baada ya dakika moja alitoka akiwa amebeba ufunguo wa gari mkononi mwake. Mchungaji huyo alikuwa akitembea haraka huku akimwonesha ishara mkewe Lamos ili azunguke upande wa pili wa gari. Mara baada ya kuingia kwenye gari hilo, mchungaji huyo akiwa na mkewe Lamos aliliwasha gari hilo na kuliondoa kwa kasi eneo hilo la kanisani. Mawazo aliyokuwa nayo yalihusiana na kumwahisha hospitali mtoto huyo ambaye aliamini alikuwa katika hali mbaya kiafya.
Akiwa kimya alionekana akigeuka mara kadhaa kumwangalia mtoto huyo ambaye bado alikuwa ametoa macho. Mkewe Lamos alikuwa mtulivu na hakujua hospitali waliyokuwa wakielekea wakati huo. Moyoni alikuwa na shauku ya kufika haraka hospitali ili madaktari waweze kuokoa maisha ya mwanae. Baada ya dakika arobaini gari la mchungaji huyo lilikuwa likiegeshwa mbele ya hospitali ya Aga Khan. Kasi ambayo gari hilo lilifika nayo hospitali hapo ndiyo iliyowapa shauku hata wauguzi ambao waliwahisha kitanda chenye maitairi eneo hili huku wakiwa wanaamini mgonjwa aliyekuwa amefikishwa eneo hilo alikuwa mtu mzima.
Mchungaji huyo mwenye asili ya kijerumani ndiye aliyekuwa wa kwanza kushuka katika gari hilo akifuatiwa na mkewe Lamos. “nesi iko msaidia hii mtoto tafadhari….” Alisikika mchungaji huyo baada ya kumchukuwa kwa kasi mtoto huyo kutoka kwa mkewe Lamos. Muuguzi aliyeelezwa kauli hiyo alijongea haraka na kuushuhudia uvimbe uliokuwapo kichwani kwa mtoto huyo ambao ulimshtua hasa kutokana na vile ulivyokuwa ukitoa harufu. Mbali na jambo hilo alishtushwa na jinsi mtoto huyo alivyokuwa ametoa macho huku akiwa mtulivu kama vile alikuwa katika nyakati za mwisho kabisa za maisha yake.
Mambo hayo aliyoyagundua kwa sekunde chache ndiyo yaliyomfanya muuguzi huyo amchukue mtoto huyo kabla ya kuanza kukimbia naye akielekea eneo la ndani ya hospitali hiyo. Nyuma yake alikuwa akifuatwa na mkewe Lamos pamoja na mchungaji ambao nao walikuwa wakikimbia. Baada ya kukimbia kwa muda mfupi walizuiliwa na muuguzi mmoja wakati wakijaribu kumfuata muuguzi aliyembeba mtoto ambaye alikuwa ameingia katika chumba cha upasuaji. Walielezwa wakae katika viti vilivyokuwa karibu na eneo hilo ili wasubirie taratibu ambazo zingefuata. Wakati huo ndiyo ambao mchungaji huyo aliutumia kumhoji mkewe Lamos juu ya maisha yake na matazizo aliyokuwa nayo mwanaye. Mkewe Lamos alijitahidi kumweleza mchungaji huyo juu ya maisha yake huku akitokwa na machozi kwa uchungu. Alimweleza kila kitu likiwamo suala la imani yake kwamba alikuwa ametorokwa na mumewe kutokana na ugumu wa maisha na matatizo waliyokuwa nayo.
Mchungaji huyo alionekana kuumia sana, alimfariji mama huyo kwa kumwahidi kumsaidia kadri ambavyo angeweza. Baada ya nusu saa wakati wakiwa wanaendelea na mazungumzo yao ilhali mchungaji huyo akionekana kumfariji mkewe Lamos, alijongea muuguzi mmoja ambaye hakuwa na furaha na kuwaeleza kuwa walihitajika katika ofisi ya daktari mkuu. Bila kupoteza muda walisimama haraka wakiwa na shauku ya kutaka kujua jambo ambalo daktari huyo alikuwa amewaitia. Wakiwa wanatembea kwa haraka, walikuwa wakiongozwa na muuguzi aliyewaita. Hatimaye waliishia kuingia katika ofisi ya daktari mkuu aliyekuwa akihusika na matatizo ya vichwa. Mara baada ya kuketi katika viti walivyooneshwa daktari huyo alianza kwa kuwaambia kuwa upasuaji dhidi ya mtoto waliyemfikisha ulikuwa umeanza. Walielezwa kuwa walifanya vyema kumwahisha mtoto huyo kwani alikuwa na maumivu makali ya kichwa ambayo yangeweza kumwondoa uhai wake muda wowote.
Aliwaeleza upasuaji huo uliokuwa wa saa tano ungegharimu kiasi cha shilingi milioni moja zaidi aliwapa imani kuwa mtoto huyo angepona vizuri. Baada ya maelezo ya kina waliyoyapata kutoka kwa daktari huyo, mchungaji huyo aliyejitambulisha kwa jina la Sigismund Leopold aliahidi kugharamia matibabu ya mtoto huyo. Baada ya kuelezwa taratibu za kufanya malipo, hatimaye walihurusiwa kutoka katika ofisi hiyo ili wasubirie upasuaji huo ukamilike. Mara baada ya kutoka mchungaji Sigismund alimweleza mkewe Lamos amsubirie hospitali hapo ili afuatilie uwezekano wa kupata fedha za matibabu ili walipe siku hiyo hiyo.
Alimwachia mama huyo kiasi cha shilingi elfu ishirini ili azitumie kama kuna jambo lolote lingejitokea. Mkewe Lamos alishukuru kwa kila jambo ambalo alikuwa amesaidiwa na mchungaji huyo ambaye aliondoka hospitalini hapo. Moyoni alikuwa amepata faraja kidogo mbali ya matatizo ambayo mwanaye alikuwa nayo aliamini angepona na zaidi alikuwa na imani juu ya msaada alioahidiwa. Kila alipomfikiria mumewe hakupata jibu kwani alikuwa bado hajaelewa kama alikuwa ametoroka na kumsaliti au la! Kuna wakati alikuwa akihisi mumewe angemrudia kutokana na upendo aliokuwa nao kwake lakini kila sekunde iliyozidi kwenda ndiyo ilimkatisha tamaa na alijikuta akianza kuamini alikuwa ametelekezwa na mumewe.
Baada ya masaa matano kama walivyoelezwa upasuaji dhidi ya mwanaye ulikuwa umekamilika huku akiwa amelazwa katika chumba maalumu. Wakati huo mchungaji Sigismund Leopold alikuwa amerudi na tayari alikuwa amekamilisha malipo ya upasuaji huo. Ni wakati ambao mkewe Lamos alikuwa ametawaliwa na faraja ambayo aliikosa kwa muda mrefu. Baada ya wiki mbili mwanaye Veronika alikuwa amepona kabisa huku akiwa na afya njema. Hakuwa na jambo la kufanya zaidi ya kutoa shukrani rukuki kwa mchungaji Segismund ambaye hakuhitaji kuishia hapo katika kumsaidia kwa vile tayari alishaelewa kuwa Lamos alikuwa ameitoroka familia yake.
Kutokana na afya aliyokuwa nayo mtoto huyo hatimaye walihurusiwa kuondoka katika hospitali hiyo. Mchungaji huyo aliongozana nao mpaka katika eneo ambalo awali mkewe Lamos alikuwa akiishi na mumewe kabla ya kutoroka. Lengo lao lilikuwa kwenda kuangalia uwezekano wa kuvipata vyombo vya mama huyo ambavyo vilitolewa nje baada ya kushindwa kulipa kodi ya nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi awali na mumewe. Taswira waliyoipata katika eneo hilo lililokuwa na vyombo hivyo iliwakatisha tamaa kwa vile vyote vilikuwa vimeibiwa. Vyombo vichache vilivyokuwapo vilikuwa vimeharibika sana kutokana na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha kiasi.
Mchungaji Sigismund aliamua kwenda kumpa mkewe Lamos chumba kimoja kilichokuwa cha kanisa na lengo lilikuwa aishi eneo hilo kwa muda mfupi wakati akiangalia uwezekano wa kumsaidia zaidi. Alishukuru kwa msaada huo alioupata kutoka kwa mchungaji huyo ambaye alionesha nia ya kumsaidia zaidi na mwanaye. Baada ya wiki mbili alimpangishia mama huyo vyuma viwili na mwanae katika eneo hilo la Kimara Mwisho na zaidi alimfungulia duka dogo la mahitaji katika kituo cha daladala cha eneo hilo. Akiwa na amani zaidi furaha hakuwa na jambo la kufanya zaidi ya kumshukuru mchungaji Sigismund kwa msaada wake. Alikuwa akiabudu na kumshukuru Mungu juu ya kila jambo alilomtendea katika kanisa la kikistro alilokuwa akitumikia mchungaji Sigismund. Wakati huo alikuwa akiwaza juu ya maisha yake na mwanaye na kila mwanaume aliyemuhitaji alimchukia kwani alikuwa anamfananisha na Lamos Maputo, mwanaume aliyemterekeza na mwanaye.
* * * *CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya miezi sita Lamos Maputo akiwa amepona mguu wake, hakuwa yule wa awali tena kwani alikuwa na duka lake maeneo ya Kariakoo jijini Dar es salaam huku akiwa na mafanikio ya kutosha ikiwapo nyumba aliyokuwa nayo Sinza. Mbali na vitu hivyo alikuwa tayari na gari la kutembelea huku hofu ya maisha ikiwa imepotea. Alikuwa akifikiria kuwa tajiri zaidi ya alivyokuwa wakati huo kwani alishaahidiwa na mganga wake kuwa angeweza kuwa tajiri mkubwa Tanzania na Afrika kwa ujumla na zaidi alihakikishiwa kuwa angeweza kuwa kati ya matajiri wakubwa wa Dunia.
Hakuwa na fikra za kuwa na mwanamke tena katika maisha yake, kila mara alipowaona wanawake alikuwa akiwaogopa na hakupenda kuwa nao karibu. Alikuwa akihofia kuvunja sharti la kwanza la kutokuoa na kufanya mapenzi alilopewa na mganga wake ambalo hakutaka kulivunja katika maisha yake. Hata mkewe ambaye awali alikuwa akimpenda sana hakumhitaji tena mara kadhaa alikuwa akimfikiria mwanaye ambaye hakujua kama alikuwa hai au la! Alikuwa akihofia uhai wa mwanaye huyo kwani pindi alipomtoroka akiwa na mama yake alimwacha akiwa katika hali mbaya kiafya. Jambo hilo ndilo lilimfanya awe mtulivu na hakujaribu kufikiria kufuatilia ukweli juu ya mwanaye. Alifanya hivyo kwani alikuwa akihofia kugundua kama mwanaye alikuwa amefariki. Alielewa jambo hilo lingemuumiza sana katika maisha yake kwa vile mtoto huyo ndiye alipaswa kuwa mfariji wake pekee kwa sababu hakuwa na uwezo wa kupata mtoto mwingine katika maisha yake kutokana na masharti aliyopewa.
Watu wengi walikuwa hawamwelewi vizuri Lamos Maputo ambaye hawakubahatika kumfahamu mkewe hata watoto wake. Alikuwa akiishi peke yake katika nyumba yake aliyokuwa nayo maeneo ya Sinza. Watu pekee waliokuwa karibu na bwana Lamos walikuwa walinzi wa kampuni ya ulinzi ya ‘Ultimate Security’ ambao mara kadhaa walikuwa wakipangwa kulinda nyumba yake. Muda wote Lomos alionekana akiwa na kiu ya maisha kwani alikuwa hapatikani dukani kwake huku akijitahidi kutafuta uwezekano wa kupanua biashara yake katika mikoa tofauti. Mbali na mambo hayo alikuwa akisafiri mara kadhaa kuelekea jijini Hong Kong nchini China ambako alikuwa akinunua bidhaa alizokuwa akiziuza dukani kwake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment