IMEANDIKWA NA : FAKI A. FAKI
*********************************************************************************
Simulizi : Niliua Kwa Kukusudia
Sehemu Ya Kwanza (1)
Kabila langu ni Mkwe.re. Nilizaliwa katika Kijiji cha Mdaula, Chalinze, miaka ishirini na nne iliyopita. Wazazi wangu walinipa jina la Tunu. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikuwa mtoto wa kwanza katika familia ya mzee Rajab Athumani. Tulizaliwa wawili tu mimi na mdogo wangu aliyeitwa Inana. Tulipishana kuzaliwa kwa miaka mitatu.
Nilipofikia umri wa miaka saba nilipelekwa shule nikaanza darasa la kwanza. Mpaka ninafika darasa la nne Inana alianza darasa la kwanza. Wakati nipo darasa la saba Inana alikuwa darasa la nne.
Sikutegemea kuwa ningefaulu kwenda sekondari lakini ukweli ni kuwa nilifaulu nikaanza masomo ya sekondari. Wakati nipo kidato cha tatu na Inana akiwa darasa la sita wazazi wetu walifariki dunia ghafla kutokana na ajali ya gari.
Umauti uliwakuta kwa pamoja wakiwa katika basi wakitokea Morogoro. Basi hilo liligongana uso kwa uso na lori la mafuta. Basi lilipinduka mara tatu. Baadhi ya abiria wakiwemo baba na mama yetu walikufa hapohapo.
Huo ukawa mwisho wa masomo yetu. Mimi nilikomea kidato cha tatu, Inana alikomea darasa la saba. Hatukuwa na ndugu wa kutuhudumia wala kutuongoza. Ndugu waliokuwepo hawakutujali. Tukawa tunaishi kivyetuvyetu mimi na mdogo wangu.
Nilikuwa ninatoka asubuhi kwenda Chalinze kutafuta vibarua ili tupate pesa za kutuwezesha kuishi. Nilikuwa napata vibarua vya kufua mashuka kwenye magesti mbalimbali na ninaporudi nyumbani jioni tunaanza kupika na mdogo wangu.
Kwa muda wa miaka mitatu tukawa tunaishi kwa kuhangaika. Mwisho nikawa namchukua mdogo wangu na kwenda naye Chalinze kufanya naye vibarua.
Ile nyumba tuliyokuwa tunaishi pale Mdaula ilikuwa ya udongo. Wakati wa mvua ilikuwa
inavuja. Iliendelea kuvuja na mwisho ikaanza kubomoka kidokidogo. Hatukuwa na uwezo wa kuijenga kwa sababu pesa tulizokuwa tunapata ziliishia kwenye chakula tu.
Katika msimu mmoja wa masika nyumba yetu ilibomoka yote na kubakia chumba kimoja tulichokuwa tunalala sisi ambacho kuta zake zilikuwa zimejaa matundu. Mtu akipita nje unamuona.
Usiku mmoja tulikuwa tumechutama kwenye pembe moja ya chumba chetu. Mvua ilikuwa inanyesha na chumba kizima kilikuwa kinavuja. Tulikuwa tumejifunika shuka moja lililokuwa limeloa maji tukiisikiliza mvua. Godoro lilikuwa limeloa chapachapa. Ndani ya
chumba kulikuwa kumejaa vidimbwi vya maji hadi uvunguni mwa kitanda.
Ghafla ukuta wa upande mmoja wa chumba ukaanguka. Kwa bahati njema uliangukia nje. Kama ungeangukia ndani ungetuua.
Ulianguka kwa kishindo kikubwa. Mimi na Inana tulishituka tukajua tumeshakufa. Tukataka kukimbia lakini hatukujua tukimbilie wapi kwani mvua bado ilikuwa ikinyesha kwa nguvu na ilikuwa usiku. Tukabaki palepale.
Kwa vile kulikuwa wazi, ubaridi ulikuwa ukitupiga na vile tulivyokuwa tumeshaloa tulikuwa tunatetemeka kwa baridi. Inana alikuwa akiweweseka.
"Vumilia mdogo wangu. Yote yatapita. Hakuna lisilo na mwisho," nikamwambia kumfariji.
Inana akanitazama. Mdomo wake ulikuwa wazi. Meno yake yalikuwa yakichezacheza na uso wake ulijaa michirizi ya maji.
"Ukuta umeshaanguka dada'ngu, tutafanyaje?" Akaniuliza kwa sauti ya kutetemeka kama mwenye homa.
"Itabidi tuuzibe kabla hakujakucha."
"Tutauziba na nini?"
"Tutafunga nguo ambazo hatuzitumii. Tusubiri mvua iache."
Mvua ilipoacha tukatoa maji yaliyokuwa yamejaa mle chumbani. Tulikuwa tunayachota na kuyamwaga nje. Tulipomaliza tulikamua nguo zetu zilizokuwa zimeloa tukaenda kuzianika.
Baada ya hapo tukaanza kazi ya kuuziba ule ukuta. Tulichimbia tena miti ya ukuta huo kisha tukaanza kufunga nguo ambazo zilikuwa hazitumiki tena.
Kwa vile godoro nalo lilitota hatukuweza kulala tena. Tulikaa kwenye fumbati za kitanda na kuanza kuzungumza.
"Inana, mimi naona nitafute nauli niende Dar. Hali ya hapa Mdaula imeshakuwa ngumu," nilimwambia mdogo wangu.
"Huko Dar utaenda kwa nani?" Inana akaniuiza.
"Naenda kutafuta kazi hata kama ni kazi ya ndani.""Huo mpango wa kazi atakufanyia nani huko Dar?"
"Nitatafuta mwenyewe, jiji nalijua. Unafikiri tutaendelea kuishi maisha haya hadi lini?"
"Kila kitu kinakwenda kwa mipango dada. Lazima upange utafikia kwa nani ili uanze kutafuta hiyo kazi na pia tujue kwa upande wangu itakuwaje.""Mimi nikienda Dar, wewe utaendelea kubaki hapahapa. Asubuhi unakwenda Chalinze kutafuta vibarua jioni unarudi. Mimi nikifika Dar nitatafuta jamaa yeyote nifikie kwake. Kazi za ndani ziko nyingi nitapata tu. Nikishapata nitakufanyia mpango na wewe uje Dar."
"Huyo jamaa ambaye utafikia kwake ni nani?"
"Kuna yule mama tuliyekuwa tunamuita shangazi ambaye aliwahi kufika hapa wakati wazazi wetu wako hai na pia kuna siku nilikwenda Dar na baba tukafikia kwake.""Anaishi wapi?"
"Anaishi Buguruni."
"Ana nyumba yake?"
"Ana banda lake la uani, anaishi na watoto wake.""Ni sawa. Sasa cha muhimu ni kutafuta nauli ya kwenda huko Dar."
"Ndiyo nataka nianze huo mpango wa kuweka pesa."
Asubuhi kulipokucha jua lilichomoza kama vile usiku hakukuwa na mvua. Baadhi ya majirani waliouona ukuta wetu umewekewa matambara ya nguo baada ya kuanguka usiku walikuja kutupa pole.Siku ile nilipanga niende Chalinze peke yangu, Inana abaki pale nyumbani kwa vile tulikuwa tumeanika nguo zetu pamoja na godoro lililokuwa limeloa.
Pia tulikuwa na wasiwasi kuwa mvua ingeweza kunyesha mchana na chumba chetu kikaporomoka tena, hivyo tuliona ni vizuri mmoja wetu abaki.Nikapanda basi hadi Chalinze. Kulikuwa na gesti kama tano hivi zinazonipa kibarua cha kufua mashuka, taulo na mapazia. Kila siku nilikuwa ninakwenda kwenye gesti tofauti. Kama leo nikienda kwenye gesti mojawapo, kesho ninakwenda kwenye gesti nyingine.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya wiki moja huwa nazirudia tena gesti hizohizo. Nilikuwa ninapata vishawishi vingi kutoka kwa wanaume lakini nilikuwa siwatilii maanani. Nilikuwa nikijali zaidi kazi yangu na maisha yangu.Kulikuwa na gesti moja ambayo niliihama kwa vile kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa akinisumbua mara kwa mara akitaka tufanye ngono. Alivyoniona nafanya vibarua vya kufua mashuka akaona angeweza kunipata kirahisi. Hapo gesti sikufika tena.
Sikuwa na muda wa kufikiria mapenzi. Nilikuwa na maisha magumu sana. Sikuwa na furaha yoyote na sikuona kitu chochote ambacho kingenipa starehe zaidi ya kibarua kilichonipatia pesa ya kula mimi na mdogo wangu.Nilikuwa msichana mzuri wa umbo na sura. Mwenyewe nilikuwa najua hilo. Uzuri wangu ulipotea kabisa kutokana na ile shida ya maisha iliyotokana na kufa kwa wazazi wetu na kutuacha bila mtu wa kututazama.
Nilipofika Chalinze nilishuka kwenye basi, nikawa navuka barabara kwenye alama za pundamilia ambapo gari husimama kupisha wapita kwa miguu wavuke barabara.Nikaona Toyota Prado linakuja nikadhani lingesimama kunipisha. Prado halikusimama. Dereva wake alifunga breki miguuni kwangu, nikajaribu kurudi nyuma mbio ili kulikwepa. Prado likasota na kunigonga, likanitupa chini.
Aliyekuwa akiendesha gari hilo alikuwa Mwarabu aliyechanganya na uswahili. Alikuwa mtu mzima aliyevaa suti na tai. Alishuka haraka na kunifuata. Alipoona nilikuwa nagaragara chini huku damu ikinitoka midomoni alipata hofu akanibeba na kunipakia kwenye gari lake.Watu walioona tukio hilo walianza kupiga kelele za kumshutumu Mwarabu huyo kwa kutosimama kwenye alama za pundamilia na hivyo kunigonga. Watu wakawa wanakuja mbio.
Mwarabu baada ya kunipakia alijipakia haraka na kuliondoa gari kwa kasi.
"Umeumia sana?" akawa anaendesha huku ananiuliza.
Nikamkubalia kwa kichwa. Mdomo niliuona mzito na damu ilikuwa ikiendelea kutoka midomoni. Nilikuwa nimeikinga kwa mikono.Mwarabu alinipeleka Hospitali ya Chalinze. Akaeleza kuwa alinigonga kwa bahati mbaya. Alitoa pesa akawapa madaktari na kuwaambia wanishughulikie haraka.
Kweli penye udhia penyeza rupia. Mwarabu alipotoa pesa hakuulizwa kama alikwenda kutoa ripoti polisi wala kutakiwa kwenda polisi kama ilivyo kawaida.
Kwa bahati njema madaktari waliponichunguza kwa kutumia picha za X-Ray waligundua kuwa sikuwa nimepata athari kwa ndani isipokuwa mguu wangu wa kulia ulishtuka na ulipata michubuko kwenye goti.
Kadhalika jino langu moja lilivunjika kipande na nilijing'ata ulimi, ndiyo sababu damu ilikuwa ikinitoka midomoni.
Hata hivyo, mguu wangu ulioelezwa kuwa ulishtuka ulianza kuniuma na kuvimba.
Madaktari walinifunga dawa sehemu niliyopata michubuko. Nikapigwa sindano ya kutuliza maumivu kisha nikapatiwa dawa ya kuchua mguu.
Wauguzi walianza kunichua palepale. Nilikuwa napiga kelele wakati wa kuchuliwa kutokana na maumivu niliyokuwa nikiyasikia.
Baada ya kushughulikiwa yule Mwarabu alikuja katika chumba nilichokuwa nimelazwa akaniuliza: "Unaishi wapi?"
"Ninaishi Kijiji cha Mdaula, hapahapa Chalinze," nikamjibu.
"Ulikuja hapa Chalinze kwa nani?"
"Huwa ninakuja kufanya vibarua, jioni ninarudi."
"Unafanya wapi vibarua?"
"Kwenye magesti."
Nilipomwambia hivyo Mwarabu alishituka akaniuliza: "Unafanya kibarua gani?"
"Kibarua cha kufua mashuka."
"Sawa. Sasa itabidi nikurudishe nyumbani uuguze mguu wako, ukipona utaendelea na kazi yako."
"Sawa. Nirudishe," nikamwambia nikiwa nimekunja uso.
Nilipopata ruhusa pale hospitali, Mwarabu alinipakia kwenye gari lake. Alinipakia katika siti ya mbele. Nikawa nazungumza naye.
"Usikasirike msichana," aliniambia huku akiendesha.
"Ile ajali ilitokea kwa bahati mbaya. Kwanza nashukuru hukuumia sana."
"Jino langu limevunjika na mguu wangu unauma," nikamwambia.
"Hebu fungua mdomo."
Nikafumbua mdomo wangu. Akalitazama jino langu lililobaki kipande.
"Lingetoka lote ningekununulia jino la bandia lakini limebaki kipande, samehe. Litakuwa alama yako."
Nikamtupia jicho kali yule Mwarabu. Aliponiona nimechukia alitabasamu.
"Nakutania tu. Pole sana. Usichukie."
Sikumjibu kitu.
"Mguu wako umeshituka kidogo. Jichue hiyo dawa asubuhi na jioni, utapona," aliendelea kuniambia.
Mwarabu alinipeleka hadi kijijini kwetu Mdaula. Alipolisimamisha gari mbele ya nyumba yetu aliniuliza: "Unaishi kwenye kibanda hiki?"
"Ndiyo."
Mwarabu akashangaa.
"Wazazi wako wako hapa?"
"Wameshakufa."
"Unaishi na nani?"
"Mdogo wangu."
Wakati huo Inana alikuwa amesogea karibu na gari.
"Huyo ndiye mdogo wako?" Mwarabu akaniuliza.
"Ndiyo."
Mwarabu akamtazama Inana.
"Hujambo?" alimuuliza.
"Sijambo. Shikamoo!" Inana akamsalimia.
"Marahaba. Nimemleta dada yako, nilimgonga na gari kwa bahati mbaya. Nimempeleka hospitali na ameshapata matibabu."
Inana akashituka.
"Dada umegongwa?" akaniuliza.
"Hakuumia sana. Ni mguu tu umeshituka na jino lake limevunjika kipande," Mwarabu akadakia.
Nikafungua mlango wa gari ili nishuke. Mwarabu akaniambia: "Subiri."
Alitia mkono ndani ya koti lake akatoa vitita vya noti. Alinipa kitita kimoja akaniambia: "Hizo ni shilingi laki moja, zitakusaidia kwa siku utakazouguza mguu wako."
"Asante," nikamwambia.
Alichomoa tena shilingi elfu ishirini akampa Inana.
"Na wewe chukua hizi."
"Asante baba," Inana akamshukuru.
Nikashuka kwenye gari.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Haya kwaherini. Nitakuja kukuangalia kesho." Mwarabu aliniambia niliposhuka kwenye gari lake.
"Haya. Asante," nikamjibu.
Mwarabu akaondoka zake.
Nikaingia chumbani kwetu mimi na mdogo wangu. Niliketi kwenye fumbati za kitanda. Inana akaniuliza.
"Ni kweli dada umegongwa na gari?"
Nikalivua gauni nililokuwa nimevaa, nikauweka mguu wangu kitandani.
"Unaona nilivyoumia?"
Inana akautazama mguu wangu huo uliokuwa umevimba na kufungwa dawa kwenye goti.
"Haa! Dada mguu umevimba sana. Alikugongaje?"
"Mpuuzi sana yule mzee. Mimi nilikuwa navuka kwenye alama za pundamilia, yeye hakusimama. Alijifanya ana haraka sana, akanigonga. Jino langu pia limevunjika."
"Maskini dada yangu! Hebu nilione."
"Polisi walikuja?"
"Hawakuwahi kuja. Alinibeba mwenyewe kwenye gari akanipeleka hospitali. Aliwapa pesa madaktari ili asiambiwe aende polisi."
"Lakini amefanya ubinadamu, amekuleta hadi hapa nyumbani na amekupa pesa na mimi amenipa pesa."
"Pesa za kudhalilishana hizi. Kama mguu wangu hautapona nikamlilie nani?"
"Lakini madaktari si wamekwambia haukuvunjika?"
"Madaktari wenyewe wameshapewa pesa, si wanaweza kudanganya tu. Mguu umevimba namna hii halafu wananiambia haukuvunjika, eti umeshtuka tu."
"Haukuvunjika dada, kama ungevunjika usingeweza kukanyaga."
Nikanyamaza kimya kumfanya mdogo wangu naye atafakari kidogo kisha tukaendelea na mazungumzo.
"Umeshakula dada?" Inana akaniuliza.
"Nimekula wapi hata chai sikunywa mdogo wangu."
"Sasa nikakutayarishie chai au nipike ugali kabisa?"
"Pika ugali, chai ya nini tena, muda huu itakutia joto uanze kutokwa na majasho!"
"Haya. Subiri nikanunue unga."
Inana akatoka nikabaki peke yangu mle chumbani nikifukuza inzi wasitue pale nilipowekwa dawa.
Ndani ya moyo wangu nilikuwa naipigia hesabu ile laki moja niliyopewa. Licha kwamba niliumizwa, pesa hizo nilizopewa zilikuwa kama mkombozi wetu.
Tulikuwa tuna mahitaji mengi yanayotaka pesa. Lakini nikajiambia tusizitumie pesa zote hizo, tubakishe kiasi kwa ajili ya akiba yetu kwani lolote linaweza kutokea katika mwili labda kulikuwa na kiungo kingine kimedhurika.
Niliposikia Inana anawasha moto, nikamuita.
"Abee dada," Inana akaniitikia.
"Ebu njoo."
Inana akaja na kusimama mbele yangu kwa shauku ya kutaka kujua nilichomuitia.
Nikamuuliza: "Unapika ugali na mboga gani?
"Kuna kisamvu kilichobaki jana na kambale wa kuchoma. Ulitaka niongeze nini?
"Basi vinatosha."
"Subiri uji uchemke ndiyo utie unga na uji usiwe mzito sana. Ugali unaweza kuoza."
"Dada kwani lini niliozesha ugali?"
"Nakukumbusha tu usijisahau kwa sababu nimeshakusikia umeanza kuimba."
"Nikiimba ndiyo najisahau?"
"Sana!"
Inana akacheka na kuondoka.
Baada ya nusu saa tu alileta sahani ya ugali mle chumbani.
Akarudia bakuli la kisamvu na sahani ya chumvi, ndipo akaleta maji ya kunawa mikono.
"Siku zote nakuambia ukiweka chakula, weka maji ya kunawa kwanza kisha ya kunywa. Mara nyingi wewe unasahau maji ya kunywa," nikamwambia.
Samahani dada nimejisahau kidogo."
"Nimeshakuzoea. Nakukumbusha tu."
"Sawa dada."
Inana akaninawisha kwa ukarimu mkubwa sana kisha na yeye akanawa. Akaomba kisha tukaanza kula huku kila mmoja akionekana kufurahia utamu wa kisamvu kilicholala jana.
Tulipomaliza kula, Inana akaondoa vyombo na kuniuliza;
"Dada usiku tule nini?"
"Utanunua mchele na maharage, uangalie kama mkaa utatosha ubandike maharage sasa hivi," nilimuagiza Inana ambaye kwa wakati huo nilimuona msaada mkubwa kwani sikuwa na uwezo wa kufanya chochote zaidi kuuguza mguu pamoja na jino langu.
"Sawa dada," alinijibu huku akimalizia kuondoa vyombo.
Siku zikazidi kusonga mbele huku nikiendelea kuuguza mguu wangu pamoja na jino, hata hivyo niliendelea kumshukuru Mungu kwa kunipa nafuu.
Siku zote hizo sikuwa na uwezo wa kurejea tena Chalinze kwenye vibarua vyetu, siku zote mdogo wangu Inana ndiye aliyekuwa anaenda kwenye vibarua, japo nilimhurumia, lakini sikuwa na jinsi kwani nilikuwa mgonjwa.
Hata hivyo, siku zote za kuuguza mguu wangu pamoja na jino, yule Mwarabu hakuwahi kuja kunijulia hali hata siku moja licha ya kuahidi.
"Sasa dada tutaendelea kuishi maisha haya ya tabu hadi lini?" Inana aliniuliza usiku mmoja wakati tukijiandaa kulala.
"Kwa sasa tupo gizani, tuendelee kumuomba Mungu huku tukifanya kazi kwa bidii, ipo siku asubuhi yetu itafika," nilimjibu Inana kwa maneno ya kumtia tumaini licha ya hali yetu ya maisha kuwa mbaya kila kukicha.
Wiki moja baadaye, nikawa nimepona kabisa mguu wangu pamoja na jino, nikawa natafakari cha kufanya baada ya hapo.
"Inana…" nilimuita mdogo wangu.
"Bee dada..."
"Nataka nizungumze na wewe."
"Nakusikiliza dada."
"Kwa sasa nimepona, hivyo kuna jambo nimeamua kufanya naomba ukubaliane na mimi japo unaweza kuumia," nilifungua mjadala wa mazungumzo hayo.
"Mmh! Kitu gani tena hicho dada?" Nana aliniuliza huku akinikazia macho kwa shauku ya kujua ninachotaka kumueleza.
"Inabidi wewe ubaki hapa mimi niende nikahangaike huko Dar es Salaam," nilianza kumueleza Inana ambaye tayari alikuwa ameshaanza kuonesha wasiwasi kabla hata sijamalizia mazungumzo yangu.
"Dar es Salaam!" Inana akahamaki.
"Ndiyo, si unaona hali hii ya maisha tunayoishi kwa sasa?" nilimuuliza Inana kwa sauti ya kumshawishi akubaliane na dhamira yangu.
"Sasa utafikia kwa nani, ulishawahi kufika Dar hata siku moja?"
"Unamkumbuka mama Shufaa?" nilimjibu huku nikimtupia swali.
"Mama Shufaa…" Inana alirudia jina hilo huku akivuta kumbukumbu vizuri.
"Ndiyo dada, nimemkumbuka."
"Anaishi Dar es Salaam sehemu moja inaitwa Buguruni Malapa."
"Unapafahamu?"
"Nitaulizia."
"Umepanga kuondoka lini dada?"
"Kesho," nilimjibu huku nikimtazama machoni.
Tulizungumza mengi, lakini mwisho mdogo wangu alikubali kubaki kijijini hapo aendelee kuhangaika na vibarua nami nikajaribu karata yangu huko Dar.
Siku iliyofuata, nilidamka mapema na kujiandaa kwa safari ambapo niliondoka saa mbili na kufika stendi ya Ubungo jijini Dar es Salaam majira ya saa nne asubuhi nikiwa na furushi langu chakavu la nguo chache nilizokuwa nimebeba.
Kwa kuwa nilikuwa na kiasi fulani cha pesa, nilipanda basi hadi Buguruni Malapa ambapo nilianza kazi ya kumuulizia mama huyo ambaye kutokana na shughuli zake za kubangaiza za mama ntilie alifahamika sana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Unaona kile kijumba kibovu pale?" alinielekeza mama mmoja wa makamo baada ya kumuulizia kama anamfahamu mama Shufaa.
"Ahsante sana mama," nilimshukuru mama huyo na kuelekea kwenye kibanda hicho.
Baada ya kufika, nilimkuta Mama Shufaa japo alinishangaa kutokana na hali yangu lakini alinipokea na kunipa hifadhi ndani ya kijumba hicho kibovu.
Nilimuelezea hali halisi ya maisha yetu baada ya wazazi kufariki dunia na kwamba nipo hapa Dar es Salaam kutafuta vibarua.
Mama Shufaa ambaye kiukoo ni shangazi yetu, alinipa pole na kunishauri kuwa nijaribu kutafuta kazi za ndani maeneo ya Sinza na Kijitonyama wanakoishi watu wenye uwezo kifedha.
Kesho yake asubuhi niliamka, baada ya kujiandaa nikapanda basi la kuelekea Sinza ambapo nilianza kazi za kugonga kwenye mageti ya watu kutafuta kazi za ndani.
Niligonga mageti mawili lakini sikufanikiwa.
Nikiwa nimekata tamaa kabisa, niliona nyumba moja iliyokuwa na geti kubwa, nikajiambia nijaribu kuulizia hapo, nikishindwa basi nirudi Buguruni hadi kesho tena.
Nikiwa najiandaa kugonga kwenye nyumba hiyo, ghafla lilikuja gari kwa kasi na kufunga breki karibu kabisa na miguu yangu, nilipoliangalia vizuri, alikuwa ni yule mwarabu aliyenigonga siku chache zilizopita.
Haraka akashuka na kuja hadi karibu yangu, tukasalimiana.
"Habari yako," alinisalimia huku akijaribu kuniangalia kwa umakini sana.
"Nzuri tu, za kwako."
"Salama, sijui wewe."
"Aah, salama lakini kama nakufananisha hivi, tuliwahi kuonana Chalinze?," yule mwarabu aliniuliza akijaribu kuvuta kumbukumbu.
"Ndiyo, mimi si ndiye ulinigonga yaani umenisahau mara hii?," nilimjibu na kumuangalia usoni, tayari alijawa na aibu kwa mbali japo hakutaka kuonesha dhahiri.
"Kumbe niko sahihi, maana nilikuwa nakufananisha tu!"
"Ni mimi bwana."
"Ehe sasa mbona uko hapa, ni kwa ndugu yako?"
"Hapana, niko hapa Dar tangu jana natafuta kazi," nilimjibu kwa kumkazia macho na kumuuliza kwani na yeye yupo Dar?"
"Mimi naishi hapa Dar, kule Chalinze kuna biashara zangu kama sheli za mafuta na nyinginezo.
Sasa unatafuta kazi gani?," aliniambia kisha akanitupia swali hilo.
"Yoyote, niko tayari kufanya," nilimjibu kwa ujasiri uliochanganyika na hofu kwa mbali.
"Oke, mimi nina hoteli yangu lakini kwa sasa hakuna nafasi kabisa, sijui nitakusaidiaje?," alisema yule mwarabu lakini kwa sauti ya upole na ya chini mno.
"Mmh!," niliishia kuguna huku nikiinamisha uso.
"Sasa sikiliza, naomba kesho uje hotelini kwangu," alisema na kuchomoa waleti yake ambapo alinipa shilingi elfu kumi kama nauli.
"Sawa, sasa huko hotelini ni wapi?," nilimuuliza kwa utulivu huku moyo wangu ukinienda pupa, sijui ni kwa minajili gani.
"Unapafahamu Mwananyamala?"
"Hapana, ni wapi?"
"Wewe kesho panda basi lolote la Mwananyala, waambie wakushushe Kwakopa, ukifika ulizia hoteli inayoitwa Riyama Hotel, ni hapo."
"Sawa."
"Lakini naomba uje kuanzia saa nne hadi sita, kwa muda huo utanikuta, sawa?"
"Sawa," nilimjibu kisha tukaagana.
Baada ya kuachana naye, sikuwa na ajizi zaidi ya kurudi Buguruni kwa shangazi mama Shufaa. Sikuona sababu ya kuendelea kutafuta kazi kwani nilikuwa na matumaini ya kupata kibarua cha riziki kwa mwarabu yule ambaye niliamini kabisa asingeweza kunitosa.
Nikapanda basi kuelekea Buguruni, njia nzima nilikuwa kimya. Kichwa changu kilijawa na mawazo mengi sana. Kuna wakati nilimfikiria mdogo wangu Inana, lakini sikuwa na jinsi ya kumjulia hali na kumjuza ninavyoendelea. Sikuwa na simu, iliniuma sana.
Nilifika majira ya adhuhuri na kumkuta shangazi akifua.
"Za huko utokako?"
"Salama tu."
"Vipi maendeleo, umefanikiwa?"
"Mungu amesaidia, unakumbuka jana nilikuambia niligongwa na gari kule Chalinze siku za hivi karibuni?"
"Ndiyo, nakumbuka ulinisimulia imekuwaje?"
"Nimekutana na aliyenigonga," nilimjibu na kuketi karibu naye.
"Hee, imekuwaje?," Shangazi aliuliza kwa hamaki na kunitazama kwa shauku ya heko.
"Tulisalimiana tu, nikamueleza shida yangu ndipo akaniambia niende kwenye hoteli yake Mwananyamala kesho."
"Mungu ni mkubwa sana."
"Kuna chakula humo ndani, waweza kulituliza tumbo lako."
"Ahsante."
Siku hiyo nilishinda kwa furaha kubwa nikiamini kuwa hatimaye mwanga wa mafanikio ulianza kuonekana japo kwa mbali sana.
Usiku sikupata usingizi mapema. Nilikuwa nawaza na kupanga mambo mengi sana, lakini kubwa nililoliwaza ni kwenda kumfuata mdogo wangu huko kijijini nikishafanikisha kazi.
Sijui nililala saa ngapi, nilishtuka asubuhi na kumsaidia shangazi kazi kidogo, kisha nikajiandaa kwenda huko Mwananyamala. Nilipanda basi hadi Ubungo ambako niliunganisha hadi Mwananyamala eneo moja linaloitwa Peace.
Nikaulizia Kwakopa na kuoneshwa. Nikauliza pia hoteli hiyo ya Riyama. Nayo nikaoneshwa na kwenda nikiwa na hofu.
Nilipofika, nikamuulizia yule mwarabu ambaye hadi wakati huo sikuwa nimelikariri kabisa jina lake. Hata hivyo, nilikuwa sikumbuki kama aliwahi kunitajia jina.
"Ndiyo, yupo nimwambie nani?," alikuwa ni mhudumu wa mapokezi hotelini hapo.
"Mwambie yule msichana wa Chalinze," nilimjibu huku nikiendelea kushangaa uzuri wa hoteli hiyo ya kifahari.
"Haya, twende nikupeleke ofisini kwake," yule dada alisema nami nikamfuata.
Tulifika hadi ofisini kwa huyo mwarabu na kumkuta akiwa bize nyuma ya kompyuta.
"Oh! Karibu sana," aliniambia lakini sura yake ikiwa imepoteza kabisa uchangamfu.
"Ahsante sana," niliitikia kwa unyenyekevu mkubwa.
Baada ya kusalimiana, niliketi kwenye kiti kizuri na cha thamani kilichokuwepo ofisini hapo.
Zilipia karibu dakika tano bila kusemeshana chochote na huyo mwarabu, nikaanza kuingiwa na wasiwasi juu ya msaada wa kazi nilioahidiwa.
Baada ya ukimya huo Mwarabu alifungua kijaluba cha bati kilichokuwa juu ya meza yake. Ndani ya kijaluba hicho kulipangwa sigara. Niliziangalia kwa pembeni mwa macho nikagundua zilikuwa aina ya Embassy.
Alichomoa sigara moja akaipachika midomoni mwake kisha akaokota kibiriti cha gesi.
"Samahani," akaniambia kabla ya kuiwasha sigara iliyokuwa midomoni mwake.
Sikujua alinipa samahani ya nini, samahani ya kutaka kuvuta sigara katika ofisi yake mwenyewe au alinipa samahani kwa kujua kuwa angenitia moshi?Vyovyote ambavyo alifikiria niliona samahani yake haikuwa na maana yoyote kwangu. Ukimya wake wa takriban dakika tano ulikuwa umenipotezea muda wangu mwingi.
Alikuwa ameniacha njia panda nikiwa sijui nitaelekea wapi, kwenye kupata kazi au kuambiwa nije siku nyingine.Simu yake ya mkononi iliyoonekana kuwa na thamani kubwa ambayo ilikuwa pale juu ya meza, ikaita. Akaitupia jicho kisha akanyoosha mkono na kuichukua.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipotazama namba iliyokuwa inaita alitabasamu. Akapuliza moshi wa sigara yake bila kujali kuwa moshi huo ungenifikia mimi na kuniumiza.Akaipokea ile simu huku akiondoka kwenye kiti.
"Hallo Gulam!" alisema wakati akielekea kando ya dirisha.
Nilimtupia macho nikamtazama kwa nyuma. Makalio yake yalikuwa yamepigwa papi na suruali yake ilikuwa imeshuka chini ya kiuno. Mara kwa mara alikuwa akiipandisha. Alisimama kando ya dirisha na kujinyoosha.
"Ndiyo, nilishazipeleka benki," akasema kwenye simu na kuongeza;
"Zilikuwa milioni mia moja."
Alisita kidogo, akavuta sigara na kupuliza moshi kabla ya kuendelea.
"Zilikuwa pesa taslim si hundi."Nilishukuru alivyoondoka pale kwenye kiti kwani moshi wote ungekuwa unaniingia mimi.
"Bado namdai milioni hamsini," akasema kwa mkazo huku akionesha ishara kwa mkono wake. Akaongeza;
"Nazihitaji pesa hizo. Nataka nifanye ukarabati wa hoteli yangu. Umenielewa?"
Mwarabu huyo akasikiliza simu kisha akasema; "Sawa." Aliushusha mkono uliokuwa na simu, akarudi kwenye meza.
Kitu cha kwanza aliizima sigara kwenye kizimio kilichokuwa juu ya meza ikiwa imebaki nusu. Alikuwa akivuta kitajiri sana. Hata hivyo hali ya hewa iliyokuwa kwenye ile ofisi ilikuwa imeshaharibika."Sasa sikiliza," akaniambia huku akiketi. "Unaitwa nani?"
"Naitwa Tunu Rajab."
Alichomoa kalamu kutoka mfuko wa koti lake akaandika jina hilo kwenye karatasi iliyokuwa juu ya meza.
"Una umri gani?"
"Umri wangu!" Nikasema huku nikifikiria."Umri wako ndiyo."
"Nina kama miaka 24 hivi."
"Ulisoma hadi darasa la ngapi?"
"Niliachia kidato cha tatu wazazi wangu walipofariki."
"Hukuwa na kaka zako wa kukuendeleza?""Mimi ndiyo mtoto wa kwanza."
Naweza kukutafutia nafasi nzuri baadaye lakini kwa sasa nitakuweka katika sehemu ya mazingira ya hoteli. Yaani kuangalia usafi. Nadhani nikisema usafi unanielewa?"
"Hebu nifafanulie.""Kuna siku utakuwa unalimalima kwenye bustani. Kuna siku utakuwa unafua na kuna siku utapiga deki. Utakuwa pamoja na wenzako."
"Sawa."
"Mshahara wako utakuwa shilingi laki moja na nusu."
Nini kitaendelea?Usikose kufuatilia usiku wa leo.....
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment