Search This Blog

Monday, 20 June 2022

KIZUIZI - 4

 





    Simulizi : Kizuizi

    Sehemu Ya Nne (4)



     “Nitayalia pesa haya mabwege mpaka yakome” alisema kwa sauti ya chini huku akigida soda kidogo iliyosalia katika chupa.

    Mtihani wake wa kutaka kugundua iwapo kweli yule ni James ama la ukawa umefanikiwa.

    Akajiona mtu mwenye bahati kupita wote duniani, akaupinga vikali ule usemi wa bahati haiji mara mbili kwani kwake yeye sasa ilikuwa ni bahati nyingine kati ya nyingi zinazojileta kila siku katika maisha yake.

    Jose akasahau kuhusu kuliwa pesa nyingi katika kamari, akarejea nyumbani akiwa na furaha. Sasa aliamini kuwa anaweza kubuni mradi mwingine wa kufanya na James huku akiendelea kumtumia mkewe kama chombo cha starehe, na banda la kutoa na kuweka pesa kama ofisi tu.

    Sekta tatu muhimu sana.

    Nani kama Jose B waukweli??CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ***



    Emmy alidamka alfajiri na mapema akiwa amefanya maamuzi na sasa alitaka kufanya utekelezaji. Alioga na kisha akaizimisha simu yake inayotambulika kwa mumewe. Akatia kadi nyingine asiyoitumia mara kwa mara.

    Alifanya hivi ili kuua ndege watatu kwa wakati mmoja.

    Kwanza kumhangaisha mumewe kama alivyohangaika yeye baada ya James kuizima simu yake, pili aweze kukutana na Jose B na kumalizana naye bila usumbufu wa kupigiwa simu na Lameck amb aye walikuwa na ahadi ya kuonana na mwisho alitaka kuukoleza uongo wake alioumwaga ofisini kwao kuwa anaumwa sana, hivyo hakutaka kusumbuliwa ili ajipange vyema kujibu lawama iwapo zitatolewa.

    Emmy alikuwa na namba zote kwa ambao anaweza kuwapigia.

    Majira ya saa moja asubuhi akatoweka, hata Gloria ambaye ni wifi yake hakujua kama ameondoka.

    Mtu wa kwanza kuwasiliana naye alikuwa ni Jose B waukweli, akitumia namba ile mpya.

    Wakakutana nyumbani kwa Jose B.

    Emmy alimlilia sana Jose B na kumweleza juu ya kipigo ambacho alikipokea usiku kutokana na ujio wake. Jose alikuwa anapenda sana sifa na pia kunyenyekewa ilikuwa ni dhahabu kwake. Sasa Emmy alikuwa anamnyenyekea. Jose B akabweteka akajihisi yu katika dunia ya peke yake. Akamsikiliza Emmy na kumwonea huruma.

    Siku hii hakumtumikisha ile adhabu ya kinyanyasaji.

    Emmy akaondoka na kuelekea nyumbani kwa Lameck.

    Wazo likiwa ni lile kuwa anaenda kumueleza Lameck kila kitu kisha waone ni kipi wanafanya ili waweze kujiokoa na janga lililopo mbele yao.

    Maji yalikuwa yamezidi unga.

    Emmy akiwa na mavazi ya baibui ambayo ni maarufu sana katika visiwa vya Zanzibar na pia siku za ijumaa katika jiji la Dar es salaam. Aliwasili katika nyumba ambayo Lameck anaishi.

    Tayari walikuwa wamewekeana miadi ya kukutana asubuhi hiyo.

    Akagonga mlango. Kimya

    Akajaribu tena huku akilazimisha tabasamu ambalo atalitumia kuurejesha urafiki wao wa ujanani na utotoni.

    Hadi tabasamu likafifia usoni bado mlango haukufunguliwa.

    “Vipi dada...unamcheki luteni?” sauti nzito iliuliza. Emmy akageuka, akakutana na mtu mwembamba, hakuamini kama ni yeye aliyeuliza lile swali.

    “Unamcheki luteni?” ilikoroma tena ile sauti.

    “Namuulizia Lameck.” Emmy aliuliza kwa uoga kiasi.

    “Ametoka asubuhi kama saa mbili hivi. Wewe ulikuwa na miadi naye?”

    “Ndio alijua nitakuja.”

    “Basi kuna dharula amekimbia hospitali mara moja. Kuna jamaa yake amekumbwa na maswaibu.”

    “He, nani tena?”

    “Hakunipa neno jingine zaidi ya hilo.” Ilijibu sauti nzito kwa msisitizo.

    Emmy alikaa kimya kwa sekunde kadhaa akaitoa simu yake akapiga namba za Lameck.

    Ilichukua sekunde kadhaa simu kuanza kuita.

    Ikatokea hali ya kukera na kuzidi kuifanya siku hii iwe ya kuchukiza. Simu iliita katika chumba cha Lameck ambacho ndani hapakuwa na kiumbe hai yeyote. Bila shaka Lameck aliisahau simu yake ama aliiacha kwa maksudi nyumbani. Emmy akaporomosha tusi zito kwa lugha ya kiingereza.

    Sauti nzito hakuelewa nini kinaendelea.

    Emmy hakutaka kuuliza swali tena. Akaaga



    ***



    Majira ya sasa sita mchana Emmy akiwa amefadhaika kabisa alirejea nyumbani, hata kabla hajalifikia geti Gloria alitoka mbio kumkimbilia.

    Emmy akashangaa haikuwa kawaida ya Gloria hata kidogo kukurupuka akimuona, ni kweli hakuwa ameaga asubuhi lakini isingeweza kuwa sababu ya kukimbiliwa kiasi hicho.

    “Wifi, kaka...kaka....”

    “Kaka?... amefanyaje?” Emmy aliuliza.

    “Anko Lameck hajasema lakini ...sijui tu....kuna tatizo wamekutafuta sana. Anko alikuwa na wasiwasi sana...” Gloria alizungumza huku akirusha mikono huku na kule.

    Hakika palikuwa na tatizo.

    Emmy akasikia tumbo likimuunguruma, akakumbuka kuwa hakuwa ametia chochote tumboni tangu asubuhi. Nguvu zilikuwa zinauaga mwili.

    Gloria akaendelea, “amesema ukifika nikwambie kuwa wapo hospitali.”

    “Hospitali gani??”

    “Hakuitaja jina..” Gloria alijibu huku akiwa na hofu zaidi ya Emmy ambaye ni wifi yake.

    Msiba! Hisia hizi zilimshambulia ghafla Emmy, akahisi kuna taarifa nzito za msiba. Emmy

    hakuhisi kitu kingine bali kifo cha mume wake mpenzi.

    Atakuwa amekufa kwa sababu ya wivu wa mapenzi. Emmy alifikiria.

    Mapigo ya moyo yakaongeza mwendokasi huku jasho nalo likitiririka kwa fujo.

    Emmy akajihisi yu hatiani, hatia ya mauaji ya mumewe. Mume aliyemuachia kitoto tumboni.

    Kimuhemuhe!



    WAKATI Emmy akihaha bila kuujua ukweli walau hospitali ambayo Lameck na James watakuwa wamejihifadhi, katika chumba ingine mwanamke alikuwa akijizuia kucheka baada ya kuwa amecheka kwa muda mrefu.

    Alikuwa na uhuru wa kucheka kwani shughuli yake aliyoikusudia hakutegemea itakuwa na vituko kiasi kile.

    Badala ya hasira sasa alikuwa ana furaha.

    Hakika alikuwa na kila sababu za kumfanya acheke.

    Hakutegemea kucheka, hiyo ni kweli. Alishalia kwa kipindi kirefu na kuapa kuwa chozi lake lazima liondoke na roho ya mtu ama watu wengi.

    Hakika roho kadhaa zilikuwa zimetoweka tayari, ile roho iliyotakiwa zaidi ikawa imesalia. Na hii ndiyo iliyomfanya acheke.

    Alimfikiria Kindo, akautafakari uongo wake na kuuweka katika mzani wa ukweli. Ule ukweli ukazidiwa kwa kiasi kikubwa na upendo.

    Kindo alikuwa muongo aliyepitiliza.

    “Kindo akanilaghai Kinte na Kakele ni ndugu zake? Kindo ...Kindo...hapana aisee... wanaume.. wanaume si viumbe wa kuwaamini” alijisemea huku akitikisa kichwa kama mtu anayekataa, kisha akaitwaa sigara yake, akajionea huruma mapafu yake kabla hajaiwasha, akatamani asikikute kiberiti mahala pake ili ashindwe kuivuta sigara ile lakini haikuwezekana, kiberiti kilikuwepo, akaitia mdomoni akaiwasha huku akiikariri sauti ya daktari ikimsihi aache matumizi ya sigara kwani imemuathiri sana. Akapuuzia.

    Wakati anaupuliza ule moshi hewani akaukumbuka wema wa Kindo wakati anamtongoza, akafanya tabasamu hafifu kisha katika mzani wa wema akaipima na roho yake mbaya. Wema ukazidiwa ujazo na roho hii chafu.

    Yule mwanamke akakunja ndita, akajikamua atokwe machozi. Hayakutoka.

    Akairudisha sigara yake mdomoni, akabaini kuwa ilikuwa imezimika.

    Akaiwasha tena.

    Akataka kuivuta akaanza kucheka, akawa anacheka huku anakohoa.

    Alicheka mpaka machozi yakawa yanamtoka.

    Alikuwa amekumbuka ghafla tukio lililotokea usiku uliopita, baada ya kumuona Kindo baada ya miaka kadhaa.

    “Bwege ni muoga aisee...yaani hadi mkojo?” alisema kisha akatulia kidogo, akaendelea tena kucheka.

    Mwanamke huyu alikuwa anajiuliza wazo la kumtisha Kindo alilitoa wapi. Kilikuwa kitendo cha ghafla sana alichokiamua.

    Alimfuatilia Kindo tangu alipoingia katika baa ile, akiwa na wasaidizi wake alimuhesabia chupa alizokunywa, akamcheka baada ya kusinzia.

    Wenzake walitaka wamalize kazi palepale. Akawazuia wasifanye vile.

    Hisia za mapenzi mazito ambayo yalizua janga baadaye ziliibuka, akamuonea huruma Kindo. Akasitisha zoezi hilo.

    Kindo alikuwa amebadilika sana, hakuwa mwembamba sana kama zamani, sasa alikuwa na afya huku kitambi kikibisha hodi katika tumbo kiweze kuchukua nafasi.

    “Anafaidi aliyeolewa naye.” Alikiri katika nafsi yake.

    “Mamu mimi sikuwa na bahati na nitakufa bila bahati...nitakufa nikirandaranda..chanzo ni Kindo.” Alinung’unika peke yake.

    Wazo la kumvagaa Kindo lilimwingia lakini akahofia kufadhaika na baadaye kulainika mbele ya bwana huyu.

    Akafikia maamuzi ambayo sasa yanamchekesha hadi anatokwa machozi.

    Mamu alimngojea kindo alipotoka nje ya baa ile wakati anatafauta usafiri, huenda wa kurejea nyumbani kwake, Mamu akazipima kumbukumbu zake iwapo anajua lolote kuhusu yaliyotokea ama la anahusika.

    Mamu alimuagiza kijana ambaye waliandamana naye. Siku hii hawakuwa wameziba nyuso zao na walipendeza kuwatazama.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nenda ukamwambie hivyo halafu uondoke..” Mamu aliagiza. Kijana akafanya alichoambiwa akamfikia Kindo.

    “Samahani braza..” Kindo akageuka huku akiwa na hofu kwa mbali, kikaratasi mkononi.

    “Sema ..” alikoroma.

    “Kuna mdada na kaka moja wanakuita katika meza ile...”

    “Ni akina nani?”

    “Kinte na Kakele.” Alijibu kwa sauti tulivu.

    Yowe likamtoka kijana huyu mwenye dalili za kitambi, pembeni palikuwa na mfereji wa maji machafu.

    Akazidiwa nguvu na hofu ya matukio mawili ya ghafla yaliyojitokeza.

    Kwanza ujumbe ukiwa na majina, Bibiana na Deo na sasa anaambiwa kuwa anaitwa na Kinte na Kakele.

    Kindo akaweweseka na kushirikiana kikamilifu kwa kukumbatiana na ule mfereji..

    Alfajiri inafahamika kuwa aliye katika mfereji ule ni James mume wa Emmy.

    Ustaarabu wa vibaka uliwawezesha kupiga namba za simu. Kwanza walipiga katika namba iliyoandikwa ‘Wife’ haikuita, hii ilikuwa namba ya Emmy ambaye alikuwa amebadili kadi tayari kwa shughuli maalumu.

    Namba ya ‘Babamkwe kijana’ ndiyo ilipatikana, wakampa maelezo juu ya tukio hilo.

    Lameck akaghairi kila alichokuwa amepanga kufanya kwani alijua kuwa iwapo James amepatwa na matatizo basi hata Emmy ambaye walikuwa wamepanga kukutana naye asubuhi hiyo aisngeweza kufika.



    Akajiandaa upesi akatimua mbio huku akisahau simu yake moja.

    Simu ambayo Emmy alifika na kupiga ikaita katika chumba.

    Sasa wapo hospitali na Emmy hajui lolote.

    Kizungumkuti.



    ***



    Simu ya Emmy iliita akiwa anahaha huku na kule kumsaka mume wake, namba ya Lameck iliendelea kutopokelewa.

    Akapokea upesi, ilikuwa namba ambayo haikuwa mara ya kwanza kuiona lakini haikuonyesha jina.

    Akapokea na kusikiliza sauti upande wa pili.

    Lameck alikuwa amepiga. Emmy akakumbuka kuwa aliwahi kuifuta namba ile baada ya kuacha kupatikana kwa kitambo kiasi fulani.

    Akamuelekeza hospitali moja iliyopo maeneo ya mnazi mmoja katikati ya jiji la Dar es salaam. Emmy akachukua taksi upesi. Akatoa malekezo, dereva akawa anapafahamu.

    Safari ikaanza. Emmy akiwa na wasiwasi mkubwa. Alihisi huenda mumewe amejinyonga kutokana na hali ya sintofahamu iliyojitokeza nyumbani, hakuamini hata kidogo kuwa anaweza kumkuta James yu hai.

    Hatimaye aliwasili, baada ya kuwa amemlipa dereva alitembea upesi upesi huku akibofya namba za simu. Lameck akatokeza hata kabla simu haijaanza kuita.

    “Jimmy amekuwaje tena....vipi yupo wapi?” Emmy aliuliza maswali mfululizo.

    Lameck alimtuliza na kumweka katika matumaini. Alimueleza kuwa James amerejewa na fahamu tayari alikutwa katika mfereji akiwa hajitambui.vibaka walimpora simu na pesa alizokuwanazo ambazo hata yeye hakumbuki ni kiasi gani.

    “Alikuwa amelewa sana....” Lameck alimalizia.

    Emmy alisikitika kusikia mumewe amekutwa mferejini. Alijitundika katika msalaba wa hatia na alikuwa tayari kuhukumiwa lakini angeificha wapi aibu yake??

    Swali zito.

    “Naweza kwenda kumuona.” Emmy alimuuliza Lameck. Badala ya kujibu Lameck alimshika mkono na kumwongoza katika chumba alichokuwa amelazwa James.

    “Mh. Kihospitali kidogo hichi napotea chumba, au uzee.” Lameck alijisemesha huku akikiendea chumba kingine. Emmy akiwa kandoni mwake.

    Huko napo akawa amepotea tena.

    “Mh. Hapana bwana ni kilekile.” Alijisemesha tena huku akiwa anakosa umakini.

    Emmy akafuata tena.

    Hakuna mtu!! Lameck akastaajabu.

    “Au atakuwa chooni huyu..lakini sasa hivi ametoka huko.” Lameck akaongea kama anayemshirikisha Emmy jambo asilolijua. Kimya.

    Emmy akaanza kufukutwa na hisia kuwa Lameck kuna jambo anamficha juu ya mume wake, hisia ngumu za kuamini kuwa James amekufa zikarejea kumshambulia, sasa zikamvuruga. Akaanza kutetemeka.

    Lameck naye akakumbwa na sintofahamu. Akamwendea daktari.

    Baada ya mazungumzo akarejea akiwa ametaharuki.

    Emmy alipoona hali ya lameck, akaanza kulia. Akaamini katika mawazo yake. James amekufa.

    Hatia yote juu yake. Emmy akaamini kuwa amemuua mumewe.

    Akatamani kuropoka chanzo cha James kutoweka nyumbani na kwenda kulewa, lakini hofu ya kuisaidia polisi upelelezi ikamkabili na kuwa kizuzi, akasita.

    Kizuizi juu ya kizuizi.....



    ****



    ILIANZA kama utani na sasa ikawa kweli kwamba James hakuwa katika hifadhi yoyote ile katika hospitali ile. Hakuwa uani wala katika chumba cha daktari. James hakuwa popote pale.

    Emmy akahisi mumewe yu katika chumba cha kuhifadhia maiti. Jambo lililomshangaza kila mtu, lakini kwa kuwa alikuwa katika taharuki hawakumuuliza.

    Ile hali ya kutomuuliza wala kumweleza lolote Emmy juu ya mahali ambapo mumewe anaweza kuwepo ama nini kinaweza kuwa kimemsibu ilimvuruga akili binti yule. Umri mdogo ukiongezea na hatia zinazomkabiri kwa kutunza siri mbalimbali zilimfadhaisha . Akalegea na kuisalimia sakafu taratibu, hakuna aliyekumbuka kumdaka asianguke vibaya.

    Emmy akapoteza fahamu.

    Akaanza kusafiri katika nchi ya giza, nchi yenye giza nene. Akiwa yeye na malaika wake wanaomlinda.

    Kiuhalisia tayari alikuwa kitandani akipepewa na kutafutiwa huduma ya kwanza.



     MZIGO!. Tena ulikuwa mzigo usiokuwa na maana hata kidogo. Kwanini akae na mzigo usiokuwa na maana wakati mzigo anaouhitaji upo mahali fulani salama?? Ulikuwa utoto kubeba mzigo wa mchanga na kuuacha ule wa dhahabu ukiwasubiri watu wengine waweze kuukwapua. Huo ulikuwa ni ujinga, na mtu afanyaye ujinga kwa maksudi anaitwa mpumbavu.

    Mariam akafadhaika kujitambua kuwa yu mpumbavu sana anayepoteza wakati na kuwa mpumbavu aliyekomaa.

    Mariam aliwaza sahihi, hakika alikuwa anachelewa maksudi kumaliza kinachotakiwa kumalizwa.

    Grace alikuwa ni mzigo usiokuwa na maana zaidi ya kulala na kulala tena bila faida yoyote.

    “Kwanza huyu bwege kumbe hata haumii kwa sababu huyu sio ndugu yake, pumbavu kabisa sijamkomoa huyu natunza tu limzigo hapa” Mariam sasa alikuwa amekasirika, hakuwa akitabasamu tena.

    Ghafla akainyanyua simu yake akawapigia vijana wake.

    “Chukua hiyo takataka muirudishe tulipoitoa” Mariam aliamrisha. Vijana wakatii, hapakuwa na takataka nyingine zaidi ya Grace. Hawakuwa na maswali.

    Mara akapiga tena Mariamu.

    “Nisubirini twende wote saa moja usiku.” Amri ikatoka, vijana wakatii.

    Majira ya saa moja kama walivyokubaliana, Grace akiwa amefungwa kitambaa usoni tangu afike katika chumba kile alikuwa ameandaliwa tayari kwa ajili ya kurejeshwa nyumbani. Mariam alifika kwa wakati. Gari mbili zikaongozana kuelekea nyumbani kwa James.

    Zilisimama umbali wa mita kadhaa, hapakuwa na watu wengi katika eneo lile.

    “Ole wako upige kelele, unaiona hii bunduki; itatawanya kichwa chako mara moja.” Kijana mwenye lafudhi ya kisukuma alimtisha Grace ambaye sasa alikuwa amefunguliwa kitambaa usoni.

    “Mwambie baba yako anasalimiwa sawa...” kijana yule aliufikisha ujumbe ambao alipewa na Mariam kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi.

    Grace akatembea huku akitetemeka akiwa haamini kama ni kweli ameachiwa ama n’do anatolewa kafara baada ya hatua kadhaa. Alilifikia geti huku akitetemeka. Akabonyeza kengele ya mlangoni.

    Baada ya dakika kadhaa akasikia vishindo. Hakuwa mtu mmoja bali kundi la watu.

    “We nani?” ikasikika sauti ya Lameck.

    “Ni mimi Grace babu.” Sauti ilijibu huku ikitangaza waziwazi hali ya uoga.

    Geti likafunguliwa mara moja huku mtutu wa bunduki ukiwa mbele.

    Mwanajeshi kamili alikuwa akijihami kwa lolote lile ambalo lingeweza kutokea kwa wakati ule. Grace alipoingia ndani alianza kulia huku akiwa amemkumbatia Lameck, Gloria naye uvumilivu ukamshinda akaangua kilio.

    Kilio ambacho kiliwakumbusha kuwa James ambaye ni baba mwenye nyumba naye hakuwa akijulikana alipo. Emmy ambaye alikuwa mama mwenye nyumba naye alikuwa hoi hospitalini baada ya shinikizo la damu kupanda, ikawa balaa juu ya balaa.

    Lameck pekee ndiye alikuwa jasiri japo moyoni aliingiwa na sintofahamu juu ya nini kinaendelea katika familia ile.

    Kuna kipindi alitamani James apotee jumla ili aweze kufanikisha suala lake lake la kumchukua mtoto ambaye yupo katika tumbo la Emmy, lakini aliyafutilia mawazo hayo. Ile heshima anayoonyeshwa na Lameck ilimfanya ajisikie aibu kwa mabaya anayomuwazia.

    Lameck akaamua kuwa upande wa mkombozi na si mteketezaji.



    ***



    MAALIM Shaban, kijana ambaye alikulia na kulelewa katika misingi nyoofu ya dini ya kiislamu. Alikuzwa kimaadili. Na akayatii maadili yale. Jina lake la Shaban Hassan lilifupishwa baada ya kijana yule kutupiwa heshima ya maalim na vijana wenzake kutokana na utii wake.

    Alikulia katika njia imara hadi alipomaliza kidato cha sita.

    Imani ikaanza kupotea baada ya kushindwa mitihani ya kidato cha sita na kuamua kutafuta ajira. Suala la kutafuta ajira halikuwa jepesi katika mkoa wa Pwani, vijana wenzake walikuwa wavuvi na Maalim alihitaji kazi ya kukaa ofisini.

    Akaamua kukimbilia jiji la Dar es salaam baada ya kupewa baraka na mama yake mzazi.

    Akapokelewa na ugumu katika jiji, japo alikuwa anaishi kwa mjomba wake lakini maisha tegemezi yalimsumbua akili.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipouzoea mji akaamua tena kutafuta ajira. Sasa alikuwa tayari kwa ajira yoyote.

    Kampuni ya G&E DRY CLEANERS ilikuwa inahitaji mfanyakazi, tangazo hili likafungua njia kwa Maalim kukutana na bosi wake.

    Akapata ajira ya kuchukua nguo chafu katika ofisi mbalimbali na kisha kuzisambaza tena baada ya kuwa zimefuliwa.

    Haikuwa kazi nyepesi, ni kazi iliyohusisha kuendesha pikipiki, kukwepa magari kadhaa ili kufika kwa wakati katika ofisi ambazo zinahitaji huduma.

    Maalim alihimili.

    Mshahara ulimkatisha tamaa lakini angefanya nini?

    Mazoea yake na wakurugenzi kadhaa katika ofisi mbalimbali yakampatia kibarua kingine katika ofisi nyingine. Walau kipato kikaongezeka na kazi za kuendesha pikipiki zikapungua.

    Katika ofisi mpya alifanikiwa kupata kitengo cha kompyuta ambayo aliifahamu tangu akiwa kidato cha tano.

    Utundu wake katika kompyuta na uaminifu wake ukamfurahisha mkurugenzi, akaamua kuzungumza naye.

    Maalim akajieleza ugumu wa maisha anaopitia, mkurugenzi akamuelewa na kumuahidi kuwa atamsaidia.

    Baada ya miezi miwili akapewa taarifa ya kushtukiza. Alikuwa ameitwa katika usaili, ofisi kuu ya mtandao wa simu unaojulikana sana Tanzania. Maalim hakuamini, bosi akamwambia kuwa ameamua kulitimiza hilo kabla hajajikita katika kutayarisha mambo kadha wa kadha kuhusiana na ndoa yake.

    Kabla James hajafunga ndoa na Emmy, Maalim alikuwa anaanza kupata uzoefu katika kiti cha kuzunguka katika ofisi kuu ya mtandao huo wa simu.

    Maalim akafarijika na mshahara, akamuona James kama Mungu mtu kwake.

    Akazidi kumtii Mungu kwa wema anaomuonyesha, akamweka James katika mikono yake.

    Maalim alistahili alichokipata kwani alikuwa mtulivu na mvumilivu.

    Katika siku zote za kazi Maalim alikuwa mkweli na hakupenda kudanganya, kila mtu alimuamini kwa hilo. Japo aliwakera baadhi ya wanaopenda kupitia njia ya nyuma lakini hakujali hilo alichotazama ni kuuegemea ukweli.

    Sasa Maalim anajikuta katika siku mbovu kupita zote, siku ambayo kwa wengine ingeweza kuonekana kama ni baraka.

    Maalim alitakiwa kufanya jambo nje kabisa na kanuni za ofisi.

    Siri za mteja zinabakia kuwa siri vinginevyo mpaka kwa kibali kutoka polisi na sababu maalum inayoeleweka.

    Kwa wateja wa kawaida Maalim angeweza kuwajibu mara moja kuwa haiwezekani, lakini huyu aliyehitaji kupewa siri za mteja alikuwa mtu mwingine kabisa hakuwa mtu wa kawaida.

    Huyu alikuwa Mungu mtu. James.

    Kijana aliyemtafutia kazi hii ambayo imempa heshima na maisha mazuri sana.

    Maalim Shaban alipokea simu ya James akiwa mjini Mwanza alipokwenda kushughulikia suala la kiufundi katika ofisi ya kule.

    Sasa yupo jijini Dar es salaam baada ya kuruka na ndege kuliacha jiji lile.

    Simu ya ajabu sana ambayo ilimsisitiza kuichunguza namba fulani ya simu na kumpatia kila swali atakalouliza.

    “Lakini kaka haturuhusiwi huku ku...” kabla hajamaliza alikatishwa, “Kuna shilingi milioni tatu za harakaharaka fanya hivyo” James alisema.

    Maalim akashusha pumzi kwa nguvu zote. Hakutegemea shambulizi kali kama lile. Ni kweli lichwa ya kuwa anaheshimika bado hakulipwa kiasi kama kile kwa mwezi.

    Maalim akafanya dua kumpinga pepo wa tamaa asimwingie.

    “Nahitaji kujua kama anawasiliana na mke wangu, meseji zote anazotumiana na mke wangu, yupo wapi kwa sasa, na ikibidi watu anaowasiliana nao kwa sana. Fanya hivyo kisha utanipa taarifa.” Alimaliza James kisha akakata simu bila kungojea shauri lolote kutokea upande wa pili.

    Sasa Maalim hajielewi ni nkitu gani afanye kwa siku inayofuata akishaingia ofisini. Ni kweli alikuwa na uwezo wa kujibu maswali yote aliyouliza James, tena hata kwa dakika tano tu. Lakini ni kinyume na kanuni ambazo alitia sahihi yake tena mbele yake huyo James ambaye sasa anamshauri azisahau na kumpatia pesa ili azivunje.

    Maalim alitambua fika taarifa atakayoitoa, sio tu itakuwa kinyume na taratibu za ofisi, bali taarifa hiyo inaweza kuzua tafrani, kuhusishwa kwa mke wake na umuhimu wa kuzifahamu meseji wanazotumiana wawili hao. Pia alihitaji kufahamu huyo bwana ni wapi anapatikana.

    Damu ikimwagika ipo juu yangu! Maalimu alijionya huku akisokota ndevu zake fupi.

    Masaa yalienda kwa kasi sana, Maalim hakuwa na jibu lolote la kuweza kumshawishi James akatishe alichoomba. Akiwa hajakaa sawa simu yake iliita ikimaanisha ujumbe umeingia.

    Maalim aliona uvivu kuusoma ujumbe ule, ilikuwa kawaida kwa simu yake kuingia ujumbe mara kwa mara, aidha kutoka kwa mama yake, wajomba, kaka zake, wadogo zake, babu na bibi.

    Wote lao moja tu. Kuomba msaada, tena wakiweka na kauli za ukali iwapo wasipotimiziwa.

    Maalim amekulia katika maadili ya kimaalim, basi akaendekea kuishi kimaalim akawa anajibana na kutuma chochote anachoweza.

    Isingekuwa vile huenda hata angekuwa na chumba cha kuvutia. Chenye mambo kadhaa ya kisasa, lakini tofauti na kompyuta yake ndogo hakuwa na jingine la kustaajabisha.

    Mara ukaingia ujumbe mwingine tena.

    Usumbufu! Maalim akajisemea. Akaitwaa simu akafungua ujumbe wa kwanza.

    Mtumaji alikuwa amehifadhiwa kwa jina la Kaka Rashid. Maalim Shaban akaukunja uso wake na kufanya swala fupi kabla ya kuifungua.

    “Mdogo wangu usione kwamba nakusumbua, hapana yaani huku chuo siwezi kufanya mitihani bila kumalizia hiyo pesa. Tafadhali sana nijali kwa hili nimalize hii Diploma” Maalim akabofya mahali pa kujibu ujumbe, kisha akajishangaa maana hakuwa na cha kumjibu kaka yake ambaye hawakuzaliwa tumbo moja. Ni kaka wa ukoo.

    Kichwa kilikuwa wazi ajibu nini. Mara simu ikaita ilikuwa namba mpya. Akaitazama kabla ya kupokea, na akaipokea kisha akakaa kimya bila kusema lolote.

    “Unajidai napiga simu zangu hupokei, sikia tulikuambia kuwa ukienda mjini utasahau familia yako tazama sasa, babu yako anaumwa unajida upo bize huko mjini, Maalim nakuapia kuwa maiti yako yatatupwa na utakosa wa kukuzika wallah nakuapia. Wewe unakataa kuja kumwona babu yako, aliyekushonea kaptula za shule mpumbavu wewe ulikuwa unatembea matako wazi wasichana wanakucheka.......nasemaje sitakupigia simu tena....na ukae huko hadi mzee ajifie mwenyewe. Vihela vyako vinakuzuzua, tutaona.” Maneno makali kutoka kwa shangazi yake yalipenya na kufanya mfano wa karaha katika moyo wake, akauma meno yake, baadaye akagundua kuwa alikuwa anatetemeka na jasho lilianza kumtoka.

    Utata!



    Maalim akajikaza akaufunua ujumbe mwingine mpya akitarajia kukutana na kero zilezile.

    “Nyingine nitakutumia kesho nikitoka benki.”

    Ujumbe kutoka kwa James, ujumbe ambao haukueleweka, Maalim akahisi kuwa James alikosea kutuma ujumbe ule. Akaupuuzia.

    Zoezi likiwa halijamalizika, akatazama ujumbe uliosalia, akaufungua. Hapa hapakuwa na namba ya mtu bali jina la kampuni ya simu.

    Milioni moja na laki nane zilikuwa zimeongezeka katika akaunti yake.

    Akashtuka sana. Akaangaza huku na huko.

    Alikuwa peke yake.

    Mtumaji wa zile pesa alikuwa ni James mwenyewe. Pesa za utangulizi kwa ajili ya biashara aliyotangaza kwa Maalim. Biashara ya kuzijua siri za mkewe.

    Kizungumkuti kikamkabili Maalim, hakika alikuwa na shida na pesa. Lakini hakutaka kwenda nje ya kanuni.

    Kabla hajapata jibu. Shangazi alipiga kwa namba yake ambayo mwanzoni Maalim alikuwa hapokei. Maalim akakata na kufanya kitendo asichokitarajia.

    Akazinukuu zile namba pembeni kisha akatumia huduma za kutuma pesa kwa njia ya simu. Shilingi laki nne taslimu.

    Shangazi hakupiga tena simu zaidi ya kutuma ujumbe wa kumshukuru Maalim kwa pesa zile huku akimwombea kwa Mungu amzidishie zaidi na zaidi.

    Pesa komesha ya kila kitu!

    Kaka mtu naye aliyelalamika kupungukiwa ada akatumiwa kiasi alichohitaji.

    Maalim anakuja kushtuka ameyafanya hayo anakumbuka kuwa alitakiwa kufanya malipo kwa kukiuka kanuni za kampuni na pia kwa mwenyezi Mungu.

    Wasiwasi ukatanda.



    ***



    Jose B waukweli alikuwa anafunga mahesabu ya mwisho wa mwezi katika ofisi yake.

    Kwa mahesabu ya harakaharaka alikadiria kuwa alikuwa na siku nyingi tangu Emmy aondoke nyumbani kwake bila kumpatia malipo yake.

    Akaipanga siku hiyo aweze kufanyanae mawasiliano ili aweze kupata haki yake kulingana na makubaliano.

    Alipofikiria jambo hilo akafanya tabasamu kidogo kisha akasonya.



    “Kaka naweza kutoa pesa...”

    Jose B akanyanyua uso wake na kukutana na sura nadhifu, yenye asili ya kipemba.

    Hakumtilia maanani

    “Shilingi ngapi?”

    “Milioni moja kamili.?”

    Jose B akanyanyua kichwa chake na kumtazama vizuri, alikuwa na hofu kijana yule, kama si hofu basi ulikuwa wasiwasi.

    Ana nini huyu? Alijiuliza.

    “Aaah. Milioni hakuna lakini lakini sita ipo.” Hatimaye Jose alijibu huku mawazo yake yakiwa juu ya kijana yule badala ya kuwaza biashara. Tabia ya kuzaliwa ilikuwa inamtafuna.

    Kijana yule akabofya tarakimu kadhaa... kabla hajaendelea Jose akaingilia kati, “una kitambulisho?” kijana akatikisa kichwa kukubali.

    Jose B akamruhusu akaendelea kutoa pesa, baadaye akamkabidhi kitambulisho. Jose B akakitazama kwa makini, akamtazama na mtoaji, hakika alikuwa ni yeye.

    Akamhesabia pesa zake akamkabidhi huku roho ya kiherehere ikimsukuma kujua zaidi.

    Ningekuwa nimefunga hapa, ningemfuatilia huyu jamaa. Jose B aliwaza huku akisikitika kumkosa yule mpemba.



    ***CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Lameck alimaliza kumsikiliza Emmy kwa masikitiko makubwa. Uchungu aliokuwa anaubeba Emmy ulikuwa mkubwa kupita umri wake na ilikuwa lazima aanguke na kupoteza fahamu.

    Hali ya kuwekwa utumwani na kijana mdogo kabisa kulimtia hasira Lameck, akakunja ndita. Emmy alikuwa ameamua kumweleza kila kitu Lameck hasahasa baada ya kusikia kuwa Grace aliyekuwa ametekwa alikuwa amerejeshwa.

    Emmy alimsimulia hadi hisia zake mbaya juu ya kuhusika kwake kumteka Grace, Lameck akamfariji na kumwambia asijali.

    Emmy akakiri kuwa Jose B amewahi kumwingilia kimwili lakini kamwe hakusema kuwa mara ya kwanza hakulazimishwa na mtu.

    “Siri ya kujua kuwa mimi nilifanya mapenzi na wewe alipewa na nani?” Lameck aliuliza. Emmy hakuwa na jibu lakini alisisitiza kwamba huyo Sam wa pili anajua kila kitu kama kilivyokuwa.

    Lameck akahisi kuwa huenda ni yule rafiki yake aliyempokea Emmy siku ya tukio n’do anashirikiana na Sam wa pili kumzunguka yeye na Emmy.

    Mwanajeshi akaunganisha hasira za kupoteza maungo ya uzazi vitani na hili tukio hasira ikamkaa sawa kichwani.

    Baada ya kumrejesha Emmy nyumbani akatoweka kuelekea nyumbani kwake.

    Kitimtim!



     KITENDO cha kushuhudia machozi ya Emmy na sauti ya ubembelezi wakati akimueleza kuhusu Jose B, kilimpagawisha Lameck. Hasira zikiwa zinachemka

    kichwani alitoweka mpaka nyumbani kwake.

    Hata kabla ya kubadili nguo zake ambazo alikuwa amezivaa kwa siku mfululizo, Lameck alielekea katika nyumba ambayo aliamini ulikuwa mwanzo mzuri wa shughuli yake kabla ya kumkabili Jose B moja kwa moja.

    Alimkuta Kipande.

    Alikuwa amejipumzisha. Sam akamuamsha kwa fujo.

    Kipande cha mtu kikaamka.

    Lameck akafikisha shutuma zake kwa bwana Kipande juu ya kuvujisha siri za yeye (Lameck) kufanya zinaa na Emmy. Kipande akashangazwa na taarifa hiyo.

    Ni kweli alikuwa anafahamu juu ya suala hilo, lakini hakuwahi kumwambia mtu yeyote yule , aliyoyaona yaliishia palepale.

    “Lameck, mara yangu ya mwisho kuongea na huyo hawara wako ni siku ile umenipa namba nikampigia. Tena alikata hata bila kumaliza kunisikiliza.” Alijibu kwa jazba Kipande.

    Neno hawala likamchanganya Lameck, akahisi kudharauliwa. Hakuwa tayari kushuhudia Emmy akifanyiwa dharau.

    Kwa hiyo anamuita Malaya kwa kuwa wanamtumia na yule mshenzi eeh! Lameck alijisemea. Kisha pasipokutarajia Kipande akafanyiwa shambulizi la ghafla, teke kali mbavuni.

    Kipande kile cha mtu kikainamia upande mmoja.

    Teke jingine likarushwa, Kipande akajikunja kurudi nyuma, Lameck akamkosa.

    “We bwege unamuita Emmy Malaya unamjua wewe...yaani Kipande unaenda kushirikiana na yule bwege kumlaghai Emmy na kumtesa kijinsia. Kipande nilikuamini ujue…” Lameck alilalamika,

    Kipande naye akawa amekumbwa na hasira kwa kesi ya kusingiziwa.

    “Kipande Sam wa pili ni nani?” Lameck aliuliza kwa jazba. Kipande ambaye bado alikuwa anaugulia maumivu hakujibu lolote bali alimkazia macho mekundu Lameck.

    Aliendelea kuuliza bila kupata majibu.

    “Ngoja nikamuulize huyo bwege mwenzako....” Lameck akasema huku akianza kuondoka.

    “Bwege mwenyewe n’do maana Sudani walikuhanithi.” Kipande alijikuta akitokwa na maneno yale makali.

    Lameck akashtushwa na kauli ile. Kipande amejuaje kuhusu siri ile, ghafla akageuka. Alikuwa radhi kutukanwa kila tusi lakini sio kukumbushwa tukio la kupoteza uanaume wake katika vita nchini Sudani.

    Mwanaume akageuka mbiombio akisindikizwa na hasira kali akamvaa Kipande. Safari hii akamkuta Kipande akiwa wima.

    Mtu yule mnene ambaye kwa kumtazama unaweza kumweka katika kundi la watu wazito na wasiojua lolote, alijichepua upesi kando bila Lameck kutarajia akajikuta akisalimiana na sakafu. Akaamka upesi, akajirusha mzimamzima bila kanuni maalum, Kipande akawa mtulivu akamdaka mguu, akaukunja kisha akamfyatua teke tumboni. Lameck akapiga yowe la uchungu.

    Kipande akasitisha mapambano baada ya kuona amemzidi Lameck mbinu. Lameck akaendelea kuugulia akiwa chini.

    Vita hii ilikuwa ya kimyakimya, hakuna mashabiki waliokua karibu ili waweze kuachanisha hali ikiwa mbaya kwa upande mmoja.

    Kipande akatoweka na kumwacha Lameck peke yake.

    Mtihani mkubwa. Nani amevujisha siri ya uhanithi wake? Hili swali liliambatana na maumivu makali aliyokuwa anaugulia Lameck pale chini. Ule munkari wa kumtafuta

    Jose B ama Sam wa pili ukashuka kwa kiasi kikubwa. Kuvuja kwa siri hii kukawa kizuizi kingine kikubwa sana. Laiti kama Emmy akigundua suala hili, huu ungekuwa mwanzo wa kudharauliwa na madai yake juu ya kumpa mimba walipokutana yatatupiwa mbali na watakaosikia.

    Tangu lini hanithi akampa mtu mimba??

    Uongo uliopitiliza.



    *****



    MAALIM Shaban akiwa ofisini alikuwa makini kabisa na mkoba wake mdogo ambao ndani yake kulikuwa na zaidi ya shilingi milioni mbili. Maalim alikuwa akibofya kompyuta yake kwa umakini, mapigo ya moyo yakienda kasi sana.

    Akaingiza namba za simu alizopewa huku akitetemeka.

    Joseph Boniphace Kasanzu.

    Hayo yalikuwa majina matatu ya mmiliki wa namba ile.

    Maalim akatabasamu, akafikiria kitu kwa muda, aliwahi kuliona jina hilo la ‘Boniphace Kasanzu’ mahali, haikuwa mara ya kwanza, akafikiri kidogo mara akapata jibu, akajisahihisha kuwa yule amjuaye yeye alikuwa Sam Boniphace Kasanzu.

    Akapuuzia.

    Kilichofuatia ni kubaini iwapo simu hii imehifadhi namba za mke wa James, Emmy!

    Hakika zilikuwepo, Mama Kijacho. Lilikuwa limehifadhiwa hivyo. Shaban akatabasamu. Akaingia katika jumbe fupi fupi walizokuwa wanatumiana.

    Utata!

    Palikuwa na kila dalili ya wawili hawa kuwa katika mkataba hatarishi, mkataba kati ya Emmy na Joseph. Maalim akashusha pumzi. Akarekodi mambo kadhaa pembeni.

    Alikuwa amemaliza kila ulizo alilotajiwa na James.

    Nafsi ikaanza kumsuta kama ilivyofanya awali. Dalili za kuisababisha ndoa ya James ivunjike zikamtawala. Akafumba macho na kumfikiria Emmy ni uchungu kiasi gani atajibebea, huzuni ikamtawala na kujiona yu mkosefu mara mbili.

    Akiitoa siri hiyo, ameenda kinyume na kanuni za mkataba.

    Akiendelea kuificha, atakuwa anashuhudia uongo jambo ambalo imani yake haimruhusu.

    Imani na kanuni zikatua katika mzani.

    Imani ikaizidi kanuni uzito.

    Liwalo na liwe! Alijisemea.

    Ghafla akashtuka tena kuwa alikuwa amechukua malipo kwa ajili ya kazi hiyo.

    Imani ikampiga kikumbo cha fadhaa. Akapatwa na aibu.

    Nimekula rushwa.

    Maalim akajiegemeza kichwa chake katika kiti chake cha kuzunguka. Mambo kadhaa yakapita kichwani mwake. Akaitwaa simu yake akamtumia James ujumbe mfupi sana.

    “Network inazingua sana bro. Ikikaa poa nakupa majibu yote”

    Maalim akajiingiza tena katika dhambi ya uongo. Akazidi kughafirika.

    Ujumbe alioutuma alihitaji kujipa muda wa kufanya maamuzi sahihi.

    Maamuzi yatakayomwacha na amani katika moyo wake.

    James akakubali kusubiri hadi mambo yatakapokuwa shwari.



    ***



    Wakati James anavuta subira kupatiwa majibu ili aingie kazini rasmi. Upande mwingine, mwanajeshi aliyejeruhiwa alikuwa anakaribia kabisa sehemu ambayo alikuwa ameelekezwa. Alikuwa amevaa miwani ya jua ilhali jioni nyeusi ilikuwa inammulika.

    Akalifikia geti na kubofya kengele. Hakupata majibu yoyote.

    Alijaribu tena na tena hakupata jawabu.

    Akajiweka pembeni, akangoja kwa muda zaidi. Akaamua kuuliza hatimaye baada ya kiza kuzidi kutawala eneo lile.

    Watu wawili wa kwanza hawakufahamu lolote. Lameck akasonya baada ya kukumbuka kuwa anayo namba ya Jose B.

    Akaipiga namba ile kwa kutumia namba yake inayojulikana na wachache.

    Jose B akapokea.

    Mahali alipokuwa palikuwa na kelele.

    “Nipo casino nitakupigia nikitoka.” Jose B alijibu kwa tabu bila kuwa amesikia lolote.

    Lameck ambaye hakuwa mgeni wa jiji la Dar es salaam hasahasa maeneo ya Magomeni, aliifahamu baa kubwa ambayo ndani yake ilikuwa na casino la kuchezea kamari. Akayakubali machale yake yaende huko.

    Hasira za kupewa kipigo na mwanajeshi mwenzake zilikuwa zimemtawala.

    Akajikongoja upesi kabla Jose B hajapiga simu.

    Akajiweka jirani na maeneo ya mlango wa kutokea akimtazama kila mtu anayetoka na kuingia.

    Muda ukazidi kwenda, masaa mawili yakapita.

    Lameck akaamua kupiga tena simu.

    Aliweka sawa sikio lake ili aweze kusikia jambo ambalo aidha lingempa moyo wa kuendelea kusubiri ama la akajipange upya.

    Muziki!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muziki aliousikia katika simu ni huohuo ulikuwa unapiga katika ukumbi ule.

    Lameck akatabasamu na kuzidi kujenga tumaini la kumpata mbaya wake.

    Baada ya nusu saa simu yake iliita. Alikuwa na Jose B ambaye jina lake limehifadhiwa kama Sam wapili.

    Mwanajeshi aliyejeruhiwa akazungusha macho upesi kama yu katika vita kubwa ya kutisha, akawapigia mahesabu watu wawili waliokuwa wamejikita katika kutumia simu zao. Mmoja alikuwa bonge..........mwingine alikuwa na umbo kama aliloambiwa.

    Bila shaka mwingine alikuwa Sam wa pili.

    Lameck akachepuka upesi akapishana na watu kadhaa akajongea na kuwa jirani kabisa na kijana huyu ambaye alionekana dhahiri kuwa pesa imemtakatisha.

    Lameck akachukua simu yake ya siku zote. Akampigia Emmy.

    Emmy alipopokea akamwambia maneno machache.

    “Mpigie..mwambie alipo pana kelele ajisogeze kando.. nahisi ni yeye”

    Alisema hayo na kueleweka kwa Emmy pekee.

    Baada ya dakika mbili yule kijana akiwa anatabasamu alielekea nyuma ya baa ile upesi huku akiwa anatabasamu. Lameck naye akatabasamu, akaanza kumfuatilia bila yeye kujua.

    Lameck alijifanya anatafuta mtandao wa simu. Yule kijana hakuweza kugundua lolote. Mwanajeshi akajipanga kwa ajili ya shambulizi la mwisho. Shambulizi ambalo litamuweka yule kijana katika himaya yake.

    Kadri alivyozidi kumsogelea ndipo mbinu zikazidi kuyoyoma. Atamkamata vipi?

    Hakuwa ametembea na kitambulisho, na iwapo atamkamata kibabe basi kwa namna yoyote ile hatafanikiwa kuondoka naye bila watu wengine kutambua hilo. Pia licha ya kumwona kuwa ana mwili mdogo.

    Wazo la uwezekano wa kuwa na silaha mahali pale ni mkubwa.

    Kwa utaratibu wa kucheza kamari, vijana wengi huwa wanatembea na silaha ndogondogo ambazo ni hatarishi sana. Hufanya hivi kwa kinga binafsi.

    Lameck akaingiwa kigugumizi.

    Kigugumizi ambacho kilimkera.

    Ningekuwa vitani, ningemrukia na kuigeuza shingo yake, wallah hakuna ambaye angejua. Tatizo namuhitaji akiwa hai. Lameck alijisemea huku akimtazama yule kijana kwa jinsi anavyozungumza kwa shangwe katika simu ile.

    Lameck asiyekuwa na maamuzi thabiti wakati anaendelea kusubiri, likatokea tukio la ghafla ambalo liliifungua akili yake na kuamua nini cha kufanya.

    Yule kijana aliyekuwa anashuka tambo mbalimbali katika simu. Alivamiwa na kikundi cha watu wanne.

    Mmoja alimkwapua simu.

    Hata kabla hajajua nini cha kufanya mwingine alimrukia na kumkaba.

    Hakuweza kupiga kelele.

    Wale wawili wakaanza kumpekua mifuko yao.

    Iliwachukua dakika tatu kuisalimu amri.

    Lameck akitumia viungo vyake vichache aliwasambaratisha mara moja wale vijana. Kuja kustaajabu Jose B alikuwa ametoweka tayari baada ya mshikemshike huo.

    Lameck alibarikiwa machale, hasahasa katika mambo ya kivita.

    Aliifuata njia ambayo aliamini kuwa Jose B ama Sam wa pili huenda ameelekea.

    Sasa ikawa kama filamu ya mapigano ya kimyakimya, filamu ya kimafia.



    *****



    Kadri alivyozidi kumsogelea ndipo mbinu zikazidi kuyoyoma. Atamkamata vipi?

    Hakuwa ametembea na kitambulisho, na iwapo atamkamata kibabe basi kwa namna yoyote ile hatafanikiwa kuondoka naye bila watu wengine kutambua hilo. Pia licha ya kumwona kuwa ana mwili mdogo.

    Wazo la uwezekano wa kuwa na silaha mahali pale ni mkubwa.

    Kwa utaratibu wa kucheza kamari, vijana wengi huwa wanatembea na silaha ndogondogo ambazo ni hatarishi sana. Hufanya hivi kwa kinga binafsi.

    Lameck akaingiwa kigugumizi.

    Kigugumizi ambacho kilimkera.

    Ningekuwa vitani, ningemrukia na kuigeuza shingo yake, wallah hakuna ambaye angejua. Tatizo namuhitaji akiwa hai. Sam alijisemea huku akimtazama yule kijana kwa jinsi anavyozungumza kwa shangwe katika simu ile.

    Lameck asiyekuwa na maamuzi thabiti wakati anaendelea kusubiri, likatokea tukio la ghafla ambalo liliifungua akili yake na kuamua nini cha kufanya.

    Yule kijana aliyekuwa anashuka tambo mbalimbali katika simu. Alivamiwa na kikundi cha watu wanne.

    Mmoja alimkwapua simu.

    Hata kabla hajajua nini cha kufanya mwingine alimrukia na kumkaba.

    Hakuweza kupiga kelele.

    Wale wawili wakaanza kumpekua mifuko yao.

    Iliwachukua dakika tatu kuisalimu amri.

    Lameck akitumia viungo vyake vichache aliwasambaratisha mara moja wale vijana.

    Kuja kustaajabu Jose B alikuwa ametoweka tayari baada ya mshikemshike huo.

    Lameck alibarikiwa machale, hasahasa katika mambo ya kivita.

    Aliifuata njia ambayo aliamini kuwa Jose B ama Sam wa pili huenda ameelekea.

    Sasa ikawa kama filamu ya mapigano ya kimyakimya, filamu ya kimafia.

    Lameck akiongozwa na machale yake aliendelea kutimua mbio, hatimaye akaona kivuli kikipepea gizani, akaongeza mwendo ili aweze kukivikia. Kile kiwiliwili kikaacha viatu, sasa ikawa riadha kweli.

    Lameck alikaza mwendo, mara kile kiwili wili kilichokuwa kimya wakati wote kikaanza kupaza sauti ya kuita mwizi.

    Ilikuwa ajabu sana, mwizi kumfukuza mtu aliyemuibia tayari. Kwa hali ya kawaida mwizi huwa mbele mfukuzaji nyuma lakini huyu mtu alikuwa anashangaza watu anavyopiga kelele.

    Walipotazama mbele hawakuona mtu. Wakapuuzia wakamwacha aendelee kupiga kelele.

    Mpiga kelele alikuwa ni Jose B waukweli, baada ya kuwa amepata ajali ya kukimbizwa na mbwa kisha kugongwa na pikipiki hakuwahi kupata mushkeli wowote ule. Sasa alikuwa katika mshikemshike. Kukimbizwa na watu alioamini kuwa ni vibaka ambao tayari walikuwa wamepora simu yake.

    Jose alivyoona hapati msaada na nguvu zimeanza kumwishia mwilini, akajikuta akivamia ukumbi wa starehe na kuvuruga utaratibu wote uliokuwa pale.

    Alikuwa anahema juu juu na hakuweza kueleweka kile alichokuwa anasema.

    Walinzi waliwahi kuirejesha amani kwa kumtwaa Jose B na kuondoka naye, hakuwa na viatu alisalia na soksi pekee miguuni. Jasho lilikuwa linamtoka na hakuwa na amani.

    Lameck ambaye tayari alikuwa akivinjari eneo lile alilifuatilia kwa ukaribu tukio hilo la kushtukiza. Macho yake makali yaliwasindikiza wale walinzi hadi mahali walipomweka Jose B.

    Lameck hakusubiri zaidi, kilio cha Emmy kilisikika kikijirudiarudia katika akiili yake. Morali ikazidi kupanda.

    Lameck akajisogeza hadi jirani na walipokuwa watu hawa watatu wakimuhoji Jose B aliyekuwa anasisitiza kuwa alikuwa anawakimbia vibaka ambao walikuwa wameikwapua simu yake kabla ya kusaidiwa na msamaria mwema ambaye hawafahamiani.

    “Wakati wakiendelea kupigana mimi nikaanza kukimbia n’do baadaye nikasikia mtu akinikimbiza tena” Alijieleza Jose B huku akihema juu juu.

    Walinzi walimuelewa na hakuwa kwenye utani hata kidogo.

    Wakamruhusu aondoke zake.

    Akawasihi wamsaidie kutafuta taksi, wakamfanyia msaada huo.

    Akajiweka ndani ya taksi na kuamuru iondoke.

    Safari ikaanza.

    Lameck aliona dalili zote za kumpoteza kijana yule zinajongea. Akaingia katika taksi nyingine na kumwamuru dereva aifungie tela taksi inayoondoka.

    Dereva akataka malipo mara mbili. Lameck akamkubalia.

    Baada ya dakika kadhaa Lameck alikuwa anatembea kwa miguu kumuwahi muhusika wake ambaye alikuwa ndio kwanza ameshuka kutoka katika taksi. Palikuwa na hali fulani ya kutoelewana kati ya mteja na mwenye taksi.

    Jose B hakujua kuwa katika patashika ile ya kuvutwa na wale walinzi waliweza kumpekua na kuondoka na pesa zote. Sasa dereva anataka kulipwa.

    Lameck alingoja pembeni kidogo akijifanya hana ajualo. Jose b akaingia ndani kisha akatoka na pesa akamlipa yule mwenye gari.

    Gari liliondoka kwa kasi Jose B akafanya kosa kulisindikiza kwa macho.

    Ghafla akajikuta katika mikono imara.

    Hakuweza kufurukuta na akapewa onyo kuwa akipiga kelele anauwawa.

    Mtihani mwingine.



     Majira ya saa nne usiku James alikuwa amekaribia eneo ambalo alikuwa anaelekezwa kwa njia ya simu kila baada ya dakika chache.

    Hasira ikiwa inamchemka tele, alitamani sana kumwona mtu ambaye anamkusudia. Habari rasmi za kuwa amewahi kuwasiliana na mkewe japo alifichwa juu ya maongezi yao zilikuwa zimempagawisha sana. Alitamani kuua mtu.

    “Sogea kusini, angalia kasikazini, rudi nyuma kidogo. Hapo hapo tulia” ilikuwa sauti tulivu ya Maalim Shaaban akimuelekeza James mahali ambapo simu ile ilikuwa inapatikana.

    Maalim alikuwa ofisini hadi muda ule, ilikuwa kawaida yake kukesha ofisini siku ambayo ataamua na kuchukua ruhusa.

    “Nampigia simu huku. Simu ipo hatua tano kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini. Kuwa naye makini. Akiinyanyua tu simu ndo huyo. Napiga.”

    James akajiweka makini sana. Mara kushoto kwake simu ikaanz akuwakawaka. Mwenye simu akawa anaishangaa badala ya kuipokea.

    James akacheza na wakati. Alipoanza tu kutoka nje aweze kuipokea ama kufanya analojua. Na yeye akatoka nje.

    Teke moja la mbavu, yule kijana ambaye alikuwa ameanza kulewa akalainika. Kikafuatia kipigo cha kimyakimya mpaka akalainika.

    Sura hii alikuwa anaiona kwa mara ya kwanza katika maisha yake. Alijaribu kuifananaisha na ile ya Jose B lakini haikufanana hata kwa mbali.

    Lakini simu ilikuwa ya Jose B waukweli.

    Huyu watakuwa wanafahamiana. Alijisemea James kisha akaendelea kumkaba yule kijana ambaye hakupata walau nafasi moja ya kujibu mashambulizi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Jose yuko wapi?” James aliuliza hatimaye.

    “Simjui.....simjui mimi..” alijitetea yule kijana, James hakutaka kumuelewa. Alimpiga kiganja cha mgongoni, kijana akalainika lakini akaendelea kujitetea.

    Raia walipita kama vile hakuna tukio linaloendelea, maana ilikuwa kawaida kwa mambo kama hayo kutokea katika mazingira yale. Na isitoshe wengi wao walikuwa wanamfahamu yule kijana aliyekuwa anapokea kichapo, walimfahamu kwa tabia zake za kuchomoa chomoa wateja na kukwapua simu. Walimpita.

    James akamsogeza muhanga wake pembeni akajaribu kujenga lugha ya kirafiki huenda ataambulia jambo lolote. Haikuwezekana, kijan a hakuwa anajua lolote juu ya Jose.

    “Simu hii ni ya nani?” aliuliza.

    “Nimekwapua kaka.” Jibu la kijana yule likamshtua James. Alitaka kuliamini lakini moyo ukasita akahisi anachezewa shere. Akamtishia mambo mengi yule kijana lakini ukweli ukabaki kuwa hakujua lolote kuhusu mwenye simu bali alikuwa amekwapua tu.

    Usiku wa James ukaisha vibaya tena. Badala ya kumnasa James ameishia kumnasa kibaka.

    James akaamua kuondoka na ile simu.

    Mara simu ya Maalim ikaingia.

    “Naona sasa upo naye.” Maalim alimwambia James.

    James akashusha pumzi akakosa cha kuongea akakata simu.



    Maalim Shaban akiwa hana hofu tena baada ya kuamua kufanya kazi ile kwa ujira mkubwa. Alijiaminisha kuwa dhambi zote ni sawa mbele ya Mungu. Kwa usemi huu akaamua kuwa kama ni dhambi iwe dhambi tu. Akauvua umaalim akauweka kando.

    Akachukua simu yake akapiga namba fulani.

    Ikaita kwa muda mrefu kisha ikapokelewa.

    “Mambo dada....za siku....samahani kwa kukupigia simu usiku.”

    “We nani?”

    “Huwezi kunifahamu lakini nina jambo dogo la kushirikiana nawe.”

    “Kama hutaki kusema wewe ni nani basi sihitaji kukusikia.”

    “Ah ni sawa kama hutaki kunisikiliza lakini nina wasiwasi mume wako amekutana na Joseph Boniphace.”

    “Who is Joseph Boniphace and who the hell are you?” sauti ya kike ikitapika kwa hasira ilisikika.

    Maalim akatabasamu kisha akasema, “Namba zake hizo nakutajia kama unazifahamu lakini kama hauzifahamu nakutakia usiku mwema.” Maalim akataja namba za Jose B.

    “Samahani umesema mume wangu amekutana naye wapi? Wamezungumza nini?” ilikuwa sauti ya Emmy alikuwa amesimama wima katikati ya chumba kanga ikiwa imeuacha mwili, alikuwa anatetemeka.

    “Sijui.” Maalim alijibu kisha akaendelea, “ila nilipenda tu kukushirikisha. Maana hadi sasa wako pamoja”

    Emmy akawa kimya kama aliyechanganyikiwa.

    “Kuna mambo mengi sana umeyafanya na huyo kijana na baada ya muda mfupi mumeo atayafahamu. Nasisitiza kuwa atayafahamu yote kama yalivyo ni hilo jambo linaloniumiza sana. Nikaamua nikushirikishe.”

    Emmy kimya.

    “Kwa hiyo kama hautajali nikutakie usiku mwema ama la tuzungumze jambo.”

    Sauti ya Emmy ikasikika akilia kama mtoto. Moyo wa maalim ukalipuka kwa uchungu, imani yake kali ikajiunga upya huruma ikamjaa.

    Pesa nimechukua, kanuni za kampuni nimevunja, eeh Mungu nipe mwangaza katika hili. Alifanya dua kimya kimya kisha akamtia moyo, “Usilie dada nitakusaidia kwa usiku huu lakini hakikisha kesho tunaonana.”

    “Unanisaidiaje kaka. Pliiz nakuomba kama ipo ndani ya uwezo wako nisaidie.”

    Usijali hakitaharibika kitu mpaka tukutane siku inayofuata.

    Simu ikakatwa.

    Emmy alibaki ameduwaa, hakutegemea simu kama hii usiku mnene namna ile na kuelezwa jambo zito namna hii.

    “Mungu wangu kama James amegundua kuwa nilizini na Sam nimekwisha mimi. Nitaificha wapi aibu yangu, huenda amemwabia pia juu ya Lameck.” Emmy alijiuliza huku akisikia dhahiri maumivu ya kichwa yakimsulubisha.

    Akiwa katika hali hiyo ikaingia simu nyingine tena.

    Kutazama alikuwa ni Lameck.

    “Eeeh Mungu saidia asiwe naye kapigiwa simu kama yangu.” Emmy akajiseme kisha akapokea simu ile.

    “Nipo na yule bwege hapa. Nimempiga sio siri.” Lameck alisema kwa utulivu.

    “Nani?”

    “Sam wa pili.” Lameck akajibu.

    Emmy akaruka pembeni kama aliyeona nyoka mkali asiyekuwa na subira katika kung’ata.

    Muda si mrefu anaambiwa kuwa Sam wa pili yupo na mumewe muda ule na wakati huohuo anaambiwa kuwa Lameck yupo naye na amempiga sana.

    Emmy akakata simu akaizima kabisa.

    Hali ilikuwa tete.

    Ina maana Joseph na Sam wa pili ni watu wawili tofauti ama. Na kama ni tofauti sasa huyu Jose ametoa wapi meseji zangu na kumwonyesha James.

    Halafu na namba ya simu inafanana na ya Sam.

    Mauzauza haya.

    Emmy alibaki ameduwaa, hakutegemea simu kama hii usiku mnene namna ile na kuelezwa jambo zito namna hii.

    “Mungu wangu kama James amegundua kuwa nilizini na Sam nimekwisha mimi. Nitaificha wapi aibu yangu, huenda amemwabia pia juu ya Lameck.” Emmy alijiuliza huku akisikia dhahiri maumivu ya kichwa yakimsulubisha.

    Akiwa katika hali hiyo ikaingia simu nyingine tena.

    Kutazama alikuwa ni Lameck.

    “Eeeh Mungu saidia asiwe naye kapigiwa simu kama yangu.” Emmy akajisemea kisha akapokea simu ile.

    “Nipo na yule bwege hapa. Nimempiga sio siri.” Lameck alisema kwa utulivu.

    “Nani?”

    “Sam wa pili.” Lameck akajibu.

    Emmy akaruka pembeni kama aliyeona nyoka mkali asiyekuwa na subira katika kung’ata.

    Muda si mrefu anaambiwa kuwa Sam wa pili yupo na mumewe muda ule na wakati huohuo anaambiwa kuwa Lameck yupo naye na amempiga sana.

    Emmy akakata simu akaizima kabisa.

    Hali ilikuwa tete.

    Ina maana Joseph na Sam wa pili ni watu wawili tofauti ama. Na kama ni tofauti sasa huyu Jose ametoa wapi meseji zangu na kumwonyesha James.

    Halafu na namba ya simu inafanana na ya Sam.

    Mauzauza haya.

    Lameck alivyojaribu kupiga simu tena na tena bila kupatikana akazifuga hasira zaidi.

    Akarejea katika chumba ambacho alikuwa amemuhifadhi Jose B.

    Akamkuta akiwa amenyong’onyea katika hali ya kuhuzunisha. Akamtazama kwa jicho la chuki kisha akamuweka sawa kwa kumnasa kibao cha kushtukiza, Jose B akatokwa na yowe la kustaajabisha. Lameck akashtuka kiasi fulani, alisahau kuwa alikuwa amemnasa kibao.



    “Ni kipi unajua kuhusu Emmy na mimi?” Lameck aliuliza akiwa amechukia.

    Jose B akajiweka tayari tayari kupokea pigo jingine, hakujua ajizibe wapi usoni ama katika viungo vingine.

    Lameck akafanya mambo mawili kwa pamoja, kwanza akafanya kumkabili Jose kama alivyotarajia. Jose B lakini hakumkabili badala yake akafanya lile la pili baadaye, akabadili aina ya shambulizi.

    Akamkumbuka yule mwarabu aliyemfyatua risasi na kuuacha uanaume wake nchini Sudan.

    Akakunja uso kwa hasira akamdaka Jose B, mkono mmoja ukazikamata korodani zake vilivyo, mkono mwingine ukaikamata shingo.

    Jose B akatokwa yowe la uchungu huku akisihi kuwa atasema kila kitu.

    Lameck akasita kumwadhibu kijeshi, akasimamisha lile zoezi. Jasho likiwa linamtiririka.

    Hakika Joseph Boniphace alikuwa amekamatika. Uchungu wa kulikimbia jiji la Mwanza kwa tamaa ya pesa za bwelele ukaanza kumchekea.

    Picha mbalimbali akiwa na furaha baada ya kuwa anaumiliki umbea zikaanza kupita katika kichwa chake, alikuwa anathema damu kana kwamba muda wowote ule anaweza kuiaga dunia.

    Lameck hakuwa na wasiwasi alitambua vyema kuwa kwa kipigo kile, Jose B atainusa jehanamu na si kuingia moja kwa moja.

    Na ilikuwa hivyo.

    Katika kufikiria mikasa mbalimbali aliyopitia, Jose B akaukumbuka ujanja ambao ameutumia kwa watu wengi na kufanikiwa kuwafanya watumwa kwake.

    Alikumbuka madhaifu yanayowatawala watu mbalimbali, akajikuta anafanya tabasamu hafifu ambalo halikuonekana kutokana na kipigo kikubwa alichokuwa amepokea. Badala ya tabasamu Jose B akafanana na mwanadamu mwenye sura mbaya kupita wote duniani.

    Hata Lameck hakujua iwapo Jose B alikuwa katika kutabasamu.

    “Sasa nakusikiliza neno kwa neno, ukiupindisha ukweli wowote ule nakumalizia. Na hakuna ambaye atajua kuwa umekufa maana nitakusagasaga humu humu ndani.” Lameck alikaripia.

    Jose B, akatishika kusikia kifo, lakini pia akapata la kujibu.

    “Naweza kukueleza kila kitu, lakini lazima tuelewane utanipatia bei gani....” Jose B waukweli akazungumza kwa shida sana.

    “Unasema?”

    “Una shilingi ngapi?”

    “Shilingi nikupe mimi kwa ajili gani? Mpumbavu wewe!!”

    “Nikueleze kila kitu.....”, akasita kisha akaendelea, “Maana tukiongea tu haina maana. Umeshanipiga sana na pia unaweza kuniua.”

    “Unamaanisha nini? Nitakuua kijana, nitakusambaratisha.” Lameck alikaripia.

    Jose B akafanikiwa kuisoma tabia ya Lameck kuwa alikuwa anamchimba mkwara, hakuwa katika kumaanisha. Akafanya tabasamu hafifu tena. Akachukiza.

    “Ninachokusimulia nakiuza......usipokinunua kwangu wenzangu aidha watakuuzia wewe na usipokinunua watawauzia wengine. Ni siri ya kule Zamzam Ubungo. Siri inayotanuka na kufikia katika kuzini na mke wa mtu, mwisho wa siri hii ni aibu ya karne. Yule mwanamke kama ulikuwa hujui alikuwa ni mtoto wako.” Jose B akajitoa muhanga akaongea kwa sauti inayotia huruma sana na inayoonyesha kukata tamaa moja kwa moja.

    Lameck akataka kufanya shambulizi jingine lakini akagundua kuwa kuna maneno makali sana yalikuwa yamemfadhaisha kutoka kwa Jose.

    Neno baya lilikuwa kwamba siri hii haikuwa kwa mtu mmoja, waliijua na wenzake pia.

    Laiti kama Jose B angekuwa ni mwanajeshi pia wa kambi ya upinzani ama jambazi mzoefu, Lameck asingeshtushwa kamwe na maneno yale kwani huwa maneno ya kumzubaisha mtu kisha kupata sintofahamu ya kufanya maamuzi na hatimaye kujikuta anafanyiwa shambulizi.

    Lakini Jose alikuwa lofa tu asiyejua hili wala lile. Lameck akaingiwa na kigugumizi.

    Akili yake ikafanya mahesabu ya upesi upesi, akamvaa Jose B bila kusema chochote, lakini safari hii hakumpiga, alimpekua ipasavyo, lengo likiwa kuitafuta simu ya mkononi.

    Hakuambulia kitu.

    Akaghafirika alipomkumbuka kibaka aliyeikwapua wakati Jose B anazungumza na Emmy.

    “Kesho asubuhi tunaenda kwa hao jamaa zako mmoja baada ya mwingine. Tumeelewana.” Lameck alitisha, Jose B ambaye alikuwa amezoea ule mkwara hakutishika.

    “Umenielewa wewe fala?” alikaripia tena.

    “Nimekuelewa kaka.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mlango wa chumba alichohifadhiwa ukafungwa kwa nje.

    Kilikuwa chumba kimojawapo katika nyumba ya rafiki yake Lameck ambaye ni mwanajeshi mstaafu kilikuwa chumba maalum kwa ajili ya watu maalumu, mstaafu huyo alikifanya rasmi kwa ajili ya waharifu ambao wanakatiza mbele yake. Kwa kuwa serikali ilikuwa bado inamuhitaji sana, kuna baadhi ya waharifu walikabidhiwa kwake na kwa namna yoyote ile walikiri makosa yao ama la waondoke wakiwa si timamu tena..

    Mzee Sadiki hakuwa mtu wa mchezo. Watoto wake walilitambua hilo, na ilikuwa bora kuukimbia mji kuliko kuadhibiwa na mzee huyu.

    Ni mzee huyu aliyemshawishi baba yake Lameck kumwingiza mwanaye jeshini. Mtoto ambaye sasa ni rafiki yake mkubwa.

    Na sasa anakitumia kile chumba ambacho walikiogopa utotoni kumwogopesha Jose B waukweli.

    Jose B waukweli akalala pale. Hakuamini kinachotokea.

    Alilala akiwaza asubuhi atampeleka wapi Lameck ili kujitoa katika kizuizi hicho, kizuizi cha kifo.



     Maalim Shaban aliisumbua akili yake mara moja kisha akafanya ‘mak-taimu’ akabofya vitufe kadhaa akaiona simu ya Jose B.

    Maalim akafanya jambo ambalo ni la kawaida sana kwake, akaifungua ile namba akatazama yote ambayo yalikuwa na madhara kwa yule mwanamke aliyeongea naye katika simu.

    Kisha akafanya jambo ambalo ni la kawaida sana katika kitengo alichokikamata, akaifungia ile namba usiku uleule isiweze kutumika kwa matumizi yoyote.

    James bila kujua, licha ya kumkosa Jose na kujikuta akimkamata kibaka mzoefu alijipa moyo kuwa atapata mawili matatu kutoka katika ile simu.

    Hakujua kama mtaalam Maalim Shaban alikuwa amevuruga kila kitu na pale alikuwa ameshikiria kopo tupu.

    Hilo lilikuwa jambo la mwisho la kuiharibu siku yake hiyo kabla hajajitupa kitandani katika hoteli aliyokuwa amejihifadhi.

    Akasinzia akiwa hana matumaini yoyote ya kujua kuna nini kati ya Jose na mkewe.

    Mtihani.

    ***



    Mgogoro mkali wa nafsi ulikuwa unamuhangaisha mwanamke aliyekuwa anagida mvinyo, alikuwa akijiuliza kama mawazo yake ni sahihi ama la.

    Ni kweli alikuwa ameanza kulewa, lakini hakuamini kuwa ulevi ule unaweza kumletea hali ile ya kufananisha mambo. Hakuwa mwepesi kiasi hicho kuchanganyikiwa akiwa amelewa.

    Mara yake ya mwisho kulewa chakari ilikuwa siku ambayo alipona katika tundu la kifo na hatimaye kurejea mtaani.

    Alilewa kwa sababu alikuwa akimlaani Kindo, alilia sana kwa upofu wake katika mapenzi ulivyomwingiza katika shimo la miiba, shimo ambalo matokeo yake ya mwisho huwa kifo. Lakini bahati ya kipekee ikamwangukia, sasa yu hai tena na amekaribia kuonana na Kindo auelezee uchungu wake kwa vitendo.

    Kwa kuyakumbuka haya Mariam akakiri kuwa hakuwa amelewa ila kuna jambo halisi alikuwa ameliona na kamwe asingeweza kulala bila kuling’amua kimarefu na mapana.

    Swali likawa kwanini amfananishe wakati muda ulikuwa umepita tangu waonane? Halafu hakuwa mtu wake wa karibu sana kwake. Tatizo hakumbuki ile sura aliwahi kuiona wapi. Hilo likawa tatizo jingine

    Wenzake walikuwa wamekerwa na kitendo cha bwana yule kuwavurugia utaratibu wao mezani.

    Walimlaani huku wakitukana matusi ya nguoni bila kupeana nafasi ya nani aanze kutukana na nani afuatie.

    Pombe zikawapa nguvu zaidi ya kutukana.

    Mariam alikuwa mkimya akilazimisha kumbukumbu.

    Baada ya dakika kadhaa aliaga kuwa anaenda uani, hakujibiwa na walevi waliokuwa wakishindana kutukana matusi mazito ya nguoni kwa kijana ambaye hakuwa pale.

    Mariam hakuwa anaenda mahali alipoaga kuwa anaenda. Alienda kufuatilia anapopelekwa yule kijana ambaye alikuwa ametaharuki.

    Mariam akafanikiwa kumwona tena. Sasa alitanabai kuwa yule alikuwa ni kijana ambaye alimtembeza kona zote la jiji la Mwanza na hatimaye akafanikiwa kuuondoa uhai wa baba yake Jame na pia mdogo wake James.

    Hatua ya awali kabisa ya kulipiza kisasi.

    Mariam anakumbuka jinsi kijana yule alivyokuwa mcheshi na mkarimu. Pia asiyependa kingi bali wastani. Tabia za kijana huyo mara mbili tatu ziliwahi kumweka Mariam katika hali asiyoweza kuielezea kwa wepesi, hakujua kama hisia zake za mapenzi zilikuwa zinaibuka upya kutoka huko zilipolala ama la? Lakini alihisi kuna jambo. Hakuwahi kusema lolote japo alifarijika kuwa karibu na yule kijana.

    Kuna wakati alijaribu kumvalia nguo za kumtega lakini cha ajabu kijana hakuonyesha tamaa zozote.

    Au domo zege? Aliwahi kujiuliza Mariam siku moja. Sasa amemwona tena.

    Hakumkumbuka jina lakini alikumba maneno mawili ‘wa ukweli’ maneno aliyoyasikia wakati fundi viatu alipokuwa akitoa wasifu wa bwana mjua mengi ambaye angeweza kumtembeza kila kona ya jiji la Mwanza huku akimpa maelezo juu ya sehemu hizo.

    Mariam akafanya tabasamu dogo kiasi.

    Tabasamu la furaha baada ya kufanikiwa kutambua kuwa kamwe huwa halewi kizembezembe.

    Tabasamu lile halikudumu kwa muda mrefu.

    Mariam alishuhudia jinsi wale walinzi walivyompekua na kuchukua pesa zake zote.

    Mariam akataka kusema neno lakini akasita. Hakutakiwa kuwa na papara.

    Ile hali ya kuibiwa akaamua kuitumia kama nafasi ya kipekee ya kulipa fadhila.

    Akamshuhudia kijana akipanda katika taksi.

    Naye akavuta subira kidogo akapanda taksi nyingine. Akaamuru imfuate kwa mbali aliyetangulia.

    Mwenye taksi akafuata maelekezo.

    Baada ya mwendo wa dakika tano, tayari yule dereva mwenye macho mekundu akagundua kitu.

    Kuna gari ilikuwa inawafuata kwa nyuma.

    Akamshtua yule dada.

    “Mh..hapana hawawezi kuwa wanatufuata sisi.” Alipinga Mariam bila kuonyesha wasiwasi.

    “Nina uzoefu na kufungia watu mkia...hii gari imetufungia mkia.” Alisisitiza huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa anasema.

    “Waache wapite sasa.” Mariam alisema kwa hasira.

    Maneno Maneno, dereva huyu mkongwe katika kituo cha Magomeni mikumi akatii amri, kwa mbinu zake za kiueledi akafanya kitu.

    Akazuga ameharibikiwa na gari yake. Akaegesha pembeni.

    Taksi ya nyuma ikawapita.

    Baada ya dakika mbili, mchuano ukaendelea.

    Teksi ya Mariam ikawa nyuma. Mbele wakatanguliwa na teksi mbili.

    Hatimaye teksi ya kwanza ikasimama.

    Mariam akamuamuru dereva amwache mbali kabisa.

    Maneno akatii amri, akamshusha akalipwa kilicho chake, akangoja kifuatacho.

    “Nisubiri.’ Mariam alimwambia.

    Mariam akiwa na kirairai cha kumshangaza Waukweli akiwa na pesa ya kumlipa yule dereva taksi. Anakutana na jambo jingine la ajabu.

    Anamshuhudia yule kijana akikwapuliwa na mtu mwingine kwa fujo.

    Macho yakamtoka pima.

    Akajificha nyuma ya mti mdogo na kuangalia kilichokuwa kinaendelea.

    Mara akashtukia akivutwa ghafla.

    Kisha akazibwa midomo.

    Hofu ikatanda. Hakuweza kurukaruka.

    Alipotanabaishwa na hisia kuwa aliyemshika alikuwa mtu salama.

    Pumzi zikamtoka kwa fujo.

    “Nilikwambia yule anafuatilia kitu.” Ilikuwa sauti ya Maneno.

    Kisha akaendelea, “Hii ndiyo michezo yangu twende zetu.”

    Akamvuta Mariam garini. Sasa akaifungia mkia gari iliyomteka yule kijana.

    Gari ambayo alikuwemo Jose B waukweli na Mjeshi Lameck.

    Mpambano mahususi.



    Kwa usiku ule ilikuwa ngumu sana kuweza kufanya msaada wowote ule, Mariam akafahamu mahali ambapo Jose B amehifadhiwa.

    Akamuamuru yule dereva amrejeshe kule katika ukumbi wa starehe.

    Dereva akatii.



    ****



    Usiku ulikuwa mgumu sana kwa James. Alipanga na kupangua vitu kichwani mwake.

    Maadui wawili alioamini wamemzunguka na wamekuwa kizuizi katika maisha yake hawakuonekana. Hii ilikuwa ni adhabu kubwa sana, kupambana na watu wanaokuona na wewe huwaoni.

    Kitendo cha kutumiwa ujumbe ambao una majina mawili ya Deo na Bibiana ambao ni marehemu ilimsababisha atambue kuwa Jose B anamfuatilia kwa ukaribu na anamwona kila nyendo zake.

    Hata kabla ya dakika nyingi kupita mara anafuatwa na mtu ambaye anamfikishia ujumbe kuwa anaitwa na watu wawili Kinte na Kakele.

    Hapa hakumbuki kama alijibu chocjote lakini alijikuta hospitalini.

    Majina haya aliyeyafahamu alikuwa ni marehemu baba yake, marehemu Bibiana, marehemu Deo na marehemu Mariam.

    James akashtuka akakaa kitako.

    Ina maana kuna mmoja amefufuka ama mzimu wake umerejea katika uhai?

    James akakilaza kichwa chake katika kona ya kitanda na kuendelea kufanya tathmini.

    Baba, Deo, Bibiana. Hawa wote walizikwa na alilitambua hilo. Wawili kati yao aliwaondosha kwa mkono wake ilimradi tu wasiweze kumharibia mipango yake ya kufunga ndoa na Emmy.

    Lakini Mariam pekee ndiye hakuzikwa.

    James alijaribu kukumbuka namna ambavyo alishirikiana na baba yake katika kumtokomeza Emmy ili mipango yao iweze kwenda barabara. Ilikuwa njia ambayo kwa mwanadamu wa kawaida kupona inakuwa ngumu sana.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walimnyanyasa sana, walimpa kila aina ya mateso, mwisho wakamtupilia mbali.

    Mbali asipopajua na alikuwa katika hali ya kufa.

    Na ilikuwa lazima afe. Ni hivyo walivyojithibitishia.

    Baba na mwana wakafanya fitna wakamtokomeza mwanadada yule kwa maslahi yao binafsi. Wakaamini kuwa wameua.

    Siri ikabaki mioyoni mwao.

    James akiwa katika kuyawaza hayo akakitazama kidole chake ambacho kina mchubuko usiokwisha ambao sasa unaitwa kovu.

    Akaikumbuka pete ambayo Mariam alimvisha baada ya kuwa amebadili dini na kuwa mkiristo akitokea katika familia ya kiislamu iliyomgomea katakata kubadili dini.

    James akafumba macho na kuukumbuka upendo wa dhati kutoka kwa Maria. Akakkiri kuwa ulikuwa upendo wa kipekee.

    Lakini lengo lao na baba yake lilikuwa tofauti sana. Ilikuwa ni zaidi ya penzi.

    Mpango wao usingeweza kuimalika iwapo wasingeusuka vyema. Ndipo wakaamua kuwashirikisha Kinte na Kakele. Kwa lengo maalum.

    Kuisaka pesa.

    Hawakuutaka umasikini tena.

    Mkoa wa Kigoma ulikuwa umewawia mgumu sana. Pasipo elimu walikuwa hawana maana kabisa.

    Kindo na baba yake waliingia mjini humo kwa kufuata masharti ya mganga wa jadi kutoka jijini Dar ambaye ni mmanyema mkazi wa Kigoma.

    Mganga aliyewapa sharti la kutoa mtoto aliyepo tumboni kafara ili mambo yaweze kuwanyookea. Kindo alitakiwa kumjaza mimba mwanamke kisha zoezi lifanyike. Hapa ni baada ya kumaliza sharti la kwanza, sharti la kuitoa roho ya mama mzazi wa Kindo.

    Kindo akakutana na Maria.

    Lengo likiwa kumjaza mimba kisha hata kabla mtoto hajakomaa tumboni waweze kumtoa kafara. Maria akapenda kweli. Mwisho akabadili dini.

    Wakati baba na mwana wakiendelea kungoja mtoto bila mafanikio.

    Hatimaye ndoa ikafungwa kutokana na msukumo wa Maria, ndoa hii ilihusisha watu wachache sana kanisani, lakini hatimaye wakavishana pete.

    Maria akiwa bado hajashika mimba.

    Ndoa yenye utata. Ndoa ambayo mwanamke hakujua kwa nini imefungwa alidhani ni mapenzi lakini baba na mwana pamoja na mshemeji na mawifi feki walitambua kwa nini imefungwa.

    Akiwa katika ndoa hii ya kimasikini Maria akanogewa na penzi ambalo kwa kindo lilikuwa mzigo.

    Siku moja Maria akamita mumewe chumbani na kumuuzia siri.

    Madini.

    Maria alikuwa na madini aliyoyahifadhi kwa kipindi kirefu sana. Ni madini aliyoyakwapua kutoka kwa baba yake mzazi aliyekuwa anashughulika na uchimbaji wa madini. Mzee alihaha kwa muda mrefu sana kuyasaka lakini hatimaye akasema bora liende.

    Akaendelea na shughuli zake kama ilivyo ada.

    Hakuweka hisia kuwa yawezekana Mariam anaweza kuwa alifanya kitu kama kile. Japo alikuwa mtoto wake wa kambo hakumfikiria vibaya.

    Hakujua kama kikulacho kinguoni mwako.

    Siri hii ilitoka baada ya Kindo kumsihi mkewe kuwa anatakiwa kupelekwa hospitali kwa ajili ya kutazamwa tatizo lake la kutozaa.

    Maria alijisikia vibaya sana kuishi katika ndoa muda mrefu bila kushika mimba. Kuna kipindi aliamini kuwa huenda ni laana za wazazi baada ya kuamua kubadili dini ili aolewe na Kindo. Lakini yote alimwachia Mungu.

    Zilihitajika pesa kwa ajili ya kufanikisha jambo hilo. Hawakuwa na pesa.

    Maria akaifungua siri yake na kuuweka kando ule usemi wa hakuna siri ya watu wawili.

    Kindo akaipokea kwa shangwe siri ile.

    Akaingoja siku ya kuonyeshwa madini hayo.

    Tanzanaiti. Madini ghali kabisa yanayopatikana katika nchi ya Tanzania.

    Kindo akamshirikisha baba yake, wakafikia shauri kuwa wamdhulumu Maria na kumtokomezea mbali.

    Kwanza hana kizazi. Na hawakuwa na lengo na ndoa hiyo bali walikuja Kigoma kusaka pesa. Pesa ambayo ingepatikana kwa kumtoa kafara kiumbe ambaye angejiunda katika tumbo la Maria.

    Kafara ya kumtoa mama yake na James haikufanya kazi vyema.

    Hawakuupata utajiri. Mama akaiaga dunia.

    Hii ya sasa nayo ikataka kuleta sintofahamu.

    Sasa wamekutana na utajiri halisi.

    Baba na mwana wakishirikiana na wapambe wawili wakaungana kumdhulumu Maria kisha kuukimbia mji wa Kigoma.

    Kinte na Kakele walihusika katika kuyatafutia soko madini yale.

    Baada ya soko kupatikana. Baba na mwana wakakumbwa na pepo la tama. Wakaamua kumweka mbali na dunia Maria.

    Wakaamua kumuua.

    Kisha baada ya hapo akiwa ametoweka wawadhulumu akina Kinte na Kakele.

    Mpango ukasukwa ukafanikiwa. Maria akarubuniwa akaingia mkenge.

    Wakamfanya walivyotaka.

    Baada ya kuhakikisha kuwa Maria hawezi kupona, wakarejea mkoani. Na kuanza kujiandaa kuuacha mji. Akina Kinte na Kakele hawakujua kama kuna mambo mengine makubwa yamefanywa nyuma yao bila kushirikishwa.

    Wakakimbilia jijini Mwanza.

    Huko Kindo akajibadili jina na kuwa James, Kinte akawa Bibiana na Kakele akabaki kuwa Deogratius. Kilichofanyika jijini Mwanza Bibiana na Deo walikilaani mpaka walipoiaga dunia. Maisha magumu waliyoyapitia katika mji huu yalikuwa fundisho tosha kuwa kamwe usimwamini mwanadamu. Anabadilika wakati wowote.



    James aliaga kuwa anaenda kuyauza madini yale jijini Dar es salaam.

    Wote wakaibariki safari yake. Safari ndefu ambayo ilimchukua James miaka mpaka aliporejea tena.



    Lilitangulia kwanza jina lake kanisani akitangazwa kuwa anataka kufunga ndoa.

    Ni hapo Deo na Bibiana walipoamua kulipiza kisasi.

    Wakapanga kumwekea kizuizi kuwa anafunga ndoa kwa mara ya pili wakati mke wake wa kwanza bado yu hai. Kitu ambacho hakikubaliki katika kanisa.

    Jose B waukweli akainasa siri hii ya kizuizi akaiuza kwa James hatimaye akawaua, bibiana na Deo ilimradi tu aweze kumuoa Emmy ambaye alikuwa bado bikra.

    James akiwa na furaha na kuamini kuwa Maria ndiye alikuwa na matatizo ya uzazi baada ya Emmy kushika ujauzito, yanazuka mengine ya kutisha. Kuna roho ilikuwa hai ikimfuatilia maisha yake.

    Mariam.

    Nafsi ya James ilimsuta ikimwambia kuwa ilikuwa haki yake kuadhibiwa tena adhabu kali kwa roho kadhaa zinazomlilia. James akayafumba macho yake kwa namna ya kujuta.

    James akakiri kimya kimya kuwa vita hii ilikuwa inaelekea kumshinda.

    Akaamua kumshirikisha mtu ambaye atakuwa na uwezo wa kuihifadhi siri yake kwa muda mrefu bila kuitoa na ambaye anaweza kumpa ushauri ulionyooka tena wa kiume.

    Lameck.

    Yes. Bamdogo Lameck. Yule ni kamanda haswaa na kamwe hawezi kuniangusha.

    Alijiaminisha James na kujikuta akitabasamu kwa mara ya kwanza kisha akajifunika shuka akaanza kuutafuta usingizi.

    James alikuwa na haki ya kutabasamu maana mwanajeshi aliyefuzu kamwe huwa hana roho ya kuropoka na kuziacha uchi siri anazohifadhi.

    Mara nyingi huwa yu radhi kufa na siri zake kuliko kuziacha hai duniani huku akiamini kuwa lazima atakufa.

    Lameck akawa chaguo sahihi la James.

    Lakini laiti kama angejua....................

    James akasinzia akiwa amepitisha wazo hilo la kuonana na Lameck aweze kumweleza siri zake na kisha kushauriana ni kitu gani wanaweza kufanya ili kuepushia mbali janga lile ambalo linakomaa kila kukicha na kuonekana kutapakaa katika kina kirefu kisichofikika kirahisi.

    Usingizi ni usingizi tu, haijalishi umelala ukiwa na mawazo ama ukiwa vyema kichwani.

    James alishtushwa na simu majira ya saa tatu asubuhi, na alikuwa na lengo la kuamka saa moja asubuhi hapo awali.

    Namba ya Maalim Shaban.

    Akaipokea baada ya kuwa ameweka sawa koo lake.

    “Jitahidi kadri uwezavyo usitoke maili hamsini na simu hiyo kuna jambo nalifanyia utafiti. Kuwa na subira. Asante.” Maalim alitoa agizo katika namna ambayo hakuhitaji pingamizi lolote....

    “Lakini.....sikia...” James alitaka kuweka pingamizi, hata hakusikika simu ikawa imekatwa.

    Akaghafirika lakini hakuwa na la kufanya.

    Akapiga kite cha ghadhabu. Akajilaza tena kitandani.

    “Mita hamsini? Upumbavu kweli huu, lakini hebu ngoja......kwa Lameck nitaenda baadaye” alikata shauri.

    Akaivuta shuka.

    Usingizi ulipoanza kumpitia, akakumbuka kero ambayo atakumbana nayo baada ya dakika kadhaa kupita.

    Kero kutoka kwa wahudumu wa hoteli ile. Alitambua fika kuwa majira ya saa nne na ikizidi sana saa tano asubuhi, atagongewa mlango kwa ajili ya kupisha usafi ufanyike.

    James akasimama, akajinyoosha akiwa na bukta yake fupi. Akatoka nje ya chumba, bahati nzuri akakutana na muhudumu.

    “Naendelea kutumia chumba hiki, na sitahitaji usafi kwa leo.”

    Muhudumu akafikisha taarifa sehemu husika.

    James akarejea chumbani. Akaitwaa simu yake akampigia Lameck.

    Simu ikaita mara mbili Lameck akapokea baada ya kusalimiana ikakatika bila kuwa wameelezana chochote. Alipojaribu kupiga tena haikuwa hewani.

    Tanesco hao.....aliweka matazamio yake James; akajiegesha tena.

    Wakati James anajiegesha tena huku akianza kutumikia kifungo cha kukaa eneo lisilozidi umbali wa mita mia tokea hapo alipo. Mambo kadha wa kadha yalikuwa yanaendelea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



     Lameck alikuwa ameamka tayari na kulitembelea bafu, sasa alikuwa anajiandaa kumchukua Jose B waukweli ili aweze kumpeleka kwa wenzake ambao wanahusika na mpango huu wa kumchezea shere na kuyatia mkosi maisha yake.

    Ile hali ya Emmy kukata simu na kisha kutoweka hewani moja kwa moja hata alipojaribu kumpigia tena na tena hakuwa akipatikana. Lameck akatilia mashaka, lakini akajipa matumaini kuwa mchezo ulikuwa umekaribia kuisha.

    Lameck alimkuta Jose akishangaa huku na kule.

    “Kwa hiyo unanidanganya kuwa jina lako ni Jose bado.....” Lameck alikoroma.

    Jose B akainua kichwa akamtazama.

    Alikuwa amekata tamaa, shingo yake ilikuwa imejiegemeza upande wa kulia na kusababisha kichwa kikichukua mhimili wake katika ukingo wa ukuta.

    Jose B alimtazama Lameck kwa jicho lililomsihi asimwadhibu tena kwa kipigo cha aina yoyote.

    Hakika Jose B alikuwa amepatikana.

    “Ulisema jana utanipeleka leo kwa wenzako.wakati ndio huu, tunaenda....na ole wako unilaghai.” Lameck alitishia kama kawaida yake. Mara simu yake ikaita, akaitazama akaona jina la James. Akaikata na kuizima. Hakutaka kuzungumza lolote na mtu yeyote hadi pale ambapo atakamilisha mipango yake.

    Lameck alitamani kuwa anaangalia saa katika simu yake ili afanye mambo kwa wakati. Na isingewezekana bila kuiwasha simu.

    Akajipekua na kujikuta na kadi ya simu. Hakutaka kujiuliza ni ya nani ama ni lini aliiweka katika mifuko ya nguo yake. Kwani alikuwa na kawaida ya kuwa na namba nyingi tofauti tofauti.

    Akaitia katika simu akaiwasha.

    Ewalaa, mambo yakawa barabara katika mstari.



    “Ni wapi tunapoenda.”

    “Kinondoni B maeneo ya Aika Bar.....”

    “Mwingine anapatikana wapi?”

    “Huyo wa Kinondoni atatusaidia kuwafikia wengine niamini.”

    Lameck akamtazama Jose, hakika alikuwa anamaanisha alichokuwa anasema. Lameck akamnyanyua na moja kwa moja akamwingiza katika gari ambayo iliandaliwa rasmi kwa ajili ya shughuli hizo. Walikuwa wawili tu.

    Lameck alikuwa mkimya akimsikiliza Jose anavyotoa maelekezo ya kufika eneo husika.

    Taratibu mwendo wa ile gari ukapungua baada ya maelekezo ya muda mrefu kutoka kwa Jose.

    “Una uhakika na maelezo yako?”

    “Asilimia zote bosi....”

    “Kwa hiyo baada ya kukata kushoto tunaelekea wapi?” aliuliza katika namna ya udadisi.

    “Tukikata hapo tutakutana na geti kubwa rangi ya udhurungi, ni hapo hapo anapatikana mwenzangu. Niamini kuwa sina ninachokudanganya.”

    Alijitetea Jose B ambaye alikuwa ameunganishwa mkono wake mmoja na pingu ambayo iliunganika na mlango wa gari hilo.

    “Anaitwa nani jamaa.....”

    “James lakini jina la kikazi ni Jimmy Mapesa.” Jose B alitoa mchanganuo mfupi unaoeleweka.

    Lameck akajikaza kijeshi, lakini hakuweza kuyazuia mapigo ya moyo kuongeza kasi yake.

    Mtu anayeelezewa ni yule James ambaye anamfahamu fika.

    James. Mtoto wake kiukoo.



    Akaanza kutetemeka midomo yake, Jose B na pingu yake mkononi akaanza kujitangazia ushindi katika vita hii.

    “Unamaanisha wewe unashirikiana na James?” Lameck akauliza swali la kijinga.

    “Ni bosi wangu ni yeye anayeniweka mjini.” Jose alijibu.

    Karata yake ilikuwa sahihi sana.

    Lameck akakosa muelekeo, akashusha kiti cha gari, kikawa mfano wa kitanda, akajinyoosha huku akitokwa na matusi mfululizo.

    “Ujue mambo mengine yanachanganya sasa wewe na James kivipi mnashirikiana sasa....ujue mnanichanganya.” Alitokwa maneno haya kama aliyepagawa.

    “Kwani unamfahamu?” Jose B akadadisi kinafiki.

    Bila kutarajia, Lameck akanyanyuka upesi kwa sekunde kadhaa akawa amemnasa vibao viwili vya nguvu Jose B. Yowe la mshtuko likamtoka kijana yule, akatamani kujikuna kwa mikono yote lakini mkono mmoja ulikuwa umefungwa pingu.

    Akajikuna kwa mkono mmoja.

    Lameck alikuwa ameegemea siti akipiga mluzi kana kwamba si yeye aliyetoka kufanya tukio lile la kumshambulia.

    Honi kali za magari zilimkurupua na kugundua kuwa ile ilikuwa njia ya magari kupita.

    Akalisogeza mbele gari lake na kuyapisha magari mawili yaliyompigia honi.

    Akatafuta mahali akaliegesha.

    Sasa Lameck akawa katika sintofahamu. Mara akavamiwa na wazo la kumshirikisha Emmy juu ya siri hii inayozunguka na kutafuna wahusika wachache lakini ikiacha balaa kubwa.

    Emmy alikuwa mtu sahihi sana kwake, kwani aliamini kuwa hajui lolote juu ya uhusiano wa karibu kati ya Jose B na mume wake.

    Pia aliiona hatari ya kifo cha Emmy katika siku za karibuni.

    James alikuwa akimuhesabia siku Emmy ili aweze kumuua. Haya yalikuwa mawazo ya Lameck.

    “Huyu mtoto kumbe mafia kiasi hichi? Yaani siku zote anaongea na mimi wakati anajua kuwa nimefanya mapenzi na mkewe? Mh jamaa hatari huyu. Sasa ana mpango gani ?” alijiuliza.

    Hakuwepo mtu wa kumjibu.

    “Huyu lofa anaweza kumuua Emmy na mtoto wangu katika tumbo lile.” Aligutuka baada ya kupata wazo hili.

    Alipolitafakari likaanza kumtesa palepale.

    Akakumbuka kuwa hana uwezo wa kuzaa tena baada ya risasi matata nchini Sudani. Picha ya mwarabu ikajijenga katika kichwa chake. Mwarabu alikuwa anatabasamu huku akiwa na ile bunduki.



    Lameck akafumba macho na kujilaani kwa kitendo cha kumsaidia yule binti ambaye alimpelekea kukumbwa na dhoruba kali.

    “Laiti kama ningekuwa na uwezo wa kuzaa ningejiondokea zangu nikajifiche mahali kuikwepa aibu hii.” Alisema kwa sauti ya chini.

    Jose B alikuwa ameupiga marufuku mdomo wake usiweze kusema lolote. Lakini akili yake ilikuwa katika sherehe ya kujipongeza kwa kupata wazo la kumpeleka Lameck kwa James.

    Jose B alifahamu fika kuwa wawili wale ni ndugu na mbaya zaidi anahifadhi siri zao wote.

    Hivyo kwa kukutana kwao lazima wote wangegeukana naye angepata upenyo wa kuwa mshindi.

    James angejiuliza iwapo siri yake ya kuwaua Bibiana na Deo ipo hai kwa watu wengine huku Lameck akikosa muhimili kwa kuwa Jose B akitapika siri ya kumfumania na mke wa

    James basi utazuka ugomvi mkali utakaohusisha mapigano yasiyoweza kuachanishwa kirahisi na mwisho wa siku atapata upenyo wa kutoroka.

    Sasa anaanza kuziona dalili za ushindi.

    Lameck ameanza kuchanganyikiwa.

    Lameck akiwa vilevile amefumba macho mara akachezwa na machale. Akayafumbua.

    Ana kwa ana na gari la James. Lilikuwa linarudi kinyumenyume liweze kukata kona na kuondoka.

    “Funga kioo fala wewe.” Alitokwa na kauli chafu Lameck. Jose B naye kwa uoga akajaribu kufunga. Akakumbana na pingu.

    Lameck akatuliza akili kidogo, akabofya kitufe. Vioo vyeusi vikajifunga vyenyewe.

    Gari ikageuza na kuwapita kwa fujo huku ikipiga honi kadhaa.

    Mwendeshaji alikuwa mwanamke ambaye nywele zake zilikuwa zimekaa hovyo tofauti na anavyofahamika kwa kuwa nadhifu.

    Uso wake nao ulikuwa katika hali ya mashaka. Na haikuwa kawaida yake kuendesha gari kwa fujo.

    Jina lake la kuzaliwa aliitwa Emiliana John. Na sasa ameolewa anaitwa Emmy James.

    Ni huyu ambaye Lameck ametoka kumuwaza muda si mrefu.

    Lameck akabofya jina la Emmy na kumpigia simu.

    Hola.

    Hapakuwa na salio katika simu yake.

    Akakumbuka kuwa alibadili kadi yake ya simu muda mfupi uliopita.

    Akapiga kite cha ghadhabu kisha akamkazia jicho Jose B.

    “Kwa hiyo unasubiri nini hapa wewe mwanaharamu.” Alimuhoji kwa shari.

    Jose B kimyaa.

    “Wewe na huyo James wako wote ni kenge tena wapumbavu, mnafatilia maisha yangu. Sasa nenda kamwambie hivi hiki ni chuma kingine. Chuma cha pua. Nina jeshi kubwa nitawasambaratisha nasema, nitaanza na wewe nakupasua kichwa anafuata yeye naua mimi. Mnajifanya wajuaji sasa ole wenu mwende kumgusa Emmy, nasemaje kipigo nilichokupa jana...kamsimulie huyo bwege mwenzako, na kile kitanzi ulikiona pale ndani nitakunyonga nasema....umenielewa we kunguru?” Lameck alipayuka kama kichaa, hakutunza neno lolote, alikuwa ameghafirika. Akamtukania Jose b mama yake mzazi, akamtukania ukoo wake.

    Ama kwa hakika alikuwa amechanganyikiwa.

    “Yaani mkamguse Emmy? Mbona nitaua mtu hadharani. Si mnajua kifo hakijaribiwi?” Sasa aliongea kama anajisemesha mwenyewe huku akijaribu kutabasamu..

    Jose B hakuwa mwanasaikolojia lakini aliipata picha ya ni jinsi gani upendo una nguvu kupita maelezo. Ama kwa hakika Lameck alikuwa katika mapenzi mazito na Emmy.

    “Sasa anampendea nini wakati ni ndugu yake?” Jose alipata nafasi ya kujiuliza.

    Akawaza biashara nyingine wakati yu katika matatizo yaliyoletelezwa na biashara.

    Ama kwa hakika umbea umenikaa damuni. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Jose B akakiri kuwa alikuwa mshakunaku, mpenda kujua mengi.

    “Toka mbele yangu mpuuzi wewe...” akawaka Lameck, akiwa amejisahau kama amempiga pingu Jose. Mara akaweka kiti chake sawa.

    Matusi yakiendelea kuporomoka bila kukoma, mara anawatukana matrafiki wanaomsimamisha, mara anawatukana wanaomnyima saiti akitaka kuovateki, matusi mazito kwa wanaomnyima nafasi akitaka kutanua, Lameck alitukana sana, matusi ambayo baadaye yakawa burudani kwa Jose B. Hayakumtisha tena.

    “We kuku wa kisasa usiyewika, telemka chini upesi, upotee hapa. Na ukaifikishe taarifa kama ilivyo. Na kaa ukijua wewe ni marehemu mtarajiwa, yaani ukimgusa Emmy na wewe nakuua.” Lameck, akaifungua pingu, akaufungua mlango na kumkanyaga Jose B, akaangukia nje.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaufunga mlango kisha akaendelea na nyimbo zake za matusi mazito mazito.

    Akamalizia na kiitikio cha kumtukania James mama yake mzazi tena. Lameck alikuwa amechanganyikiwa.

    Aibu kuu ilikuwa inamngoja.

    Lakini atafanya nini? Je akimbie na kumwacha Emmy matatani akiwa na kiumbe chake tumboni ama aendelee kubaki na aibu kuu. Aibu itakayosafiri na masalia ya heshima yake na kumwachia dharau kubwa.

    Mtihani.



    *****



    Emmy aliendesha gari lake kwa mwendokasi mkubwa, akiwa na msongo wa mawazo juu ya mambo anayoyapitia. Alihitaji kumsikia Maalim alikuwa na lipi la kusema.

    Makutano yao yalikuwa, Yombo Vituka Mwisho wa lami, eneo lililojitenga nje kidogo ya jiji la Dar es salaam linalozidi kutanuka siku hadi siku.

    Maalim aliamua kukutana na Emmy eneo la mbali na mji kwa kiasi fulani ili aweze kujiweka mbali na watu ambao wanaweza kuwa karibu na James. Maalim akayafanya mambo yake kwa usasa zaidi.

    Alianza kwa kumwekea Kizuizi James. Alikuwa amempigia simu na kumpa maelekezo ya uongo, maelekezo ya kukaa sehemu moja mpaka atakapopewa taarifa ya mpya.

    Kizuizi hicho kilikuwa kimetatuliwa.



    Emmy alikutana na Maalim, sura haikuwa ngeni kabisa. Aliwahi kuiona mahali.

    “Mambo sista.” Maalim alisalimia.

    “Safi hali..” alijibu kwa utulivu Emmy huku akiendelea kutafakari ni wapi aliwahi kuiona sura ile.

    “Poa karibu...” alikaribishwa katika baa ndogo isiyokuwa na watu wengi.

    Emmy kama msukule, akafuata njia.

    “Nimewahi kukuona mahali.” Emmy aliamua kuukata ukimya.

    “Hata mimi nadhani tumewahi kuonana.” Maali Shaban alijibu.

    “Ni wapi?”

    “Hapa hapa mjini nadhani.”

    “Naitwa Maalim Shaban.”

    Emmy akafanya tafakari, akapata jawabu ni wapi aliwahi kuonana naye. Ni katika ofisi ya mume wake. Maalim alikuwa ameajiriwa pale.

    Wakaketi.

    Maalim akaanzisha mazungumzo. Emmy akawa msikilizaji. Maalim akaanzia mkasa wa meseji katika simu ya Jose B, akaeleza jinsi mumewe anavyofahamu mambo kadhaa kuhusu Jose B. Na hisia zake juu ya uhusiano kati ya Emmy na Jose.

    Emmy alikuwa anasubiri kwa hamu kujua hitimisho la ni wapi James yupo na ni maamuzi gani amechukua baada ya kuigundua siri ile. Emmy alijikaza japokuwa alikuwa anatetemeka kwa hofu ya kulisikia hitimisho.



    Maalim akatiririka yote ayajuayo kisha akakwama na kubadili mazungumzo kabla hajasema lolote jingine la ziada ambalo lilitakiwa kuyafikia masikio ya Emmy na kuichangamsha akili yake.

    “Nayaweka maisha yangu katika utata, sijui ni kipi kimenisukuma na kukueleza haya. Lakini nadhani ni sauti iliyo ndani yangu imenilazimisha. Mimi ni muumini safi wa dini ya kiislamu, kuna mambo kadhaa naenda kinyume na siwezi kujizuia kama mwanadamu..” akaweka kituo na kumtazama Emmy usoni.

    Emmy akakwepesha macho yake na kutazama chini. Maalim akaendelea, “Nasikia una mimba.” Maalim alizngumza, hakujulikana iwapo anauliza ama ametoa tu kauli.

    Emmy akabashiri kuwa Maalim atakuwa na jibu tayari.

    Hakujibu chochote.

    “Nadhani damu hiyo ya kitoto kichanga imenisukuma mimi maalim kujiingiza katika mchezo nisioufahamu mwanzo wake na hata nikikuomba unieleze bado utayaficha mengi sana.”

    Emmy kimya usikivu ukimtawala.

    “Nimemzuia James asiijue siri hii ya wewe na yule kijana Joseph wa Boniphace”

    “Jose?” emmy akauliza.

    “Wewe unamwita Sam n’do huyo ninayemzungumzia.”

    “Nimejiweka pabaya katika maisha yangu maana simjui Jose, James wala wewe sikujui kiundani. Nimejikuta tu naitetea ndoa yako. Sasa basi kuna kitu unatakiwa ufanye upesi. Halafu unatakiwa kuwa msiri na jasiri, usiyaropoke haya kwa mtu yeyote yule. ”

    “Kitu gani?”

    “Pesa ili niondoke zangu katika jiji hili niende nyumbani kupumzika kidogo. Sihitaji kumsaidia James kwa lolote tena wala wewe. Nilichofanya kimetosha kuyaweka maisha yangu matatani na pia nimejaza mdudu wa mashaka katika akili yangu.”

    “Milioni tatu tu. Itaniweka pazuri walau.”

    Emmy akafanya tathimini, akajihisi yu katika mtego wa kudhulumiwa, lakini sura ya Maalim haikuwa na chembe ya unafiki, na haikuwa mara ya kwanza kuonana naye. Emmy akaifikiria na ndoa yake akaogopa kucheza pata potea katika hili.

    Maalim akaisoma akili ya Emmy, akanyanyua simu yake akampigia James na kuweka sauti ya juu. James alikuwa analalamika kuwa simu haionyeshi chochote kile na hata zile meseji alikuwa hajaziona. Maalim akamuuliza maswali kadhaa ya kumchimba. James akakiri kuwa hajui lolote.

    Emmy akashawishika japo nusu kwa nusu. Na amani ikarejea tena baada ya kugundua kuwa mume wake yu hai. Akaamua kuuvaa mkenge, japo akiba yake kiasi fulani ilikuwa imetetereka lakini aliwafahamu wafanyakazi wenzake ambao wanaweza kumsaidia upesi.

    Wakakubaliana na kuagana.



    ****



    MFEREJI uliopo pembezoni mwa barabara ulimpokea Jose B baada kuukosa muhimili aliposukumwa na yule mwanajeshi kutoka katika gari.

    Jose B alijaribu kuyahimili maumivu makali, akajikongoja na kusimama. Akakumbana na umati wa watu kila mtu akishangaa kivyake. Jose naye akashangaa.

    Wanaume wawili wakawa wepesi kuliko wengine, wakaingia katika mfereji na kumchukua Jose B. Akiwa bado hajui nini kinaendelea alifikishwa katika gari dogo, hakuwa na timamu zake. Bado aliona maluweluwe.

    Gari ikatoweka, wananchi wakishangaa.

    Jose B akawa katikati ya vijana wawili asiowajua.

    Sasa akili ilikuwa timamu. Akapatwa hofu. Akahisi yu katika jaribu jingine.

    Wazo la kwamba amechezewa mchezo ya yule mjeshi likavamia kichwa chake, akaanza kutetemeka. Hakuna aliyemsemesha.

    Mara jicho lake likatua katika kioo kilichokua juu ambacho dereva anaweza kukitumia kutazama abiria wake.

    Jose B akaona macho angavu ambayo hapo kabla aliwahi kukutana nayo mahali. Hakujikita sana katika kufanya tathimini ya ni wapi amewahi kuiona. Lakini alijiaminisha kuwa huenda hata ni mteja wake wa kutoa na kuweka pesa.

    Wazo hilo la kwamba huenda sura hiyo aliwahi kuiona katika banda lake la kutolea pesa likaambatana na wazo kuwa atakuwa ametekwa na sasa anaenda kukombwa pesa zake zote za akiba.

    Jose B akajutia kuja jijini Dar es salaam.

    Baada ya muda mrefu wa ukimya hatimaye gari ilisimama. Mbele ya nyumba ambayo haikuwa ya kutisha sana na haikuwa ya kimasikini sana.

    Jose B akasaidiwa kushuka huku akiwa anachechemea.

    Mara akageuka mwanamke akiwa anatabasamu.

    Sura hii Jose B aliwahi kuiona. Sasa kumbukumbu zikamvamia kwa kasi. Akamkumbuka.

    Walionana jijini Mwanza, wakati akimzungusha huku na kule kulitambua jiji hilo la miamba.

    Tatizo hakumkumbuka jina.

    “Pole sana wa ukweli.” Alizungumza yule mama kuonyesha kwamba anamfahamu kijana yule vilivyo. Jose akaanza kurejewa na amani. Akakaribishwa ndani.



    ***



    ***



    Wakati Jose B akiokolewa na Mariam, mwanamke ambaye walikutana jijini Mwanza.

    Huku upande mwingine Lameck alikuwa nakaribia kuwa mwehu, kila aliyemkwaza aliambulia mvua ya matusi bila kujalisha amemkwaza kwa maksudi ama bahati mbaya.

    Baadhi yao waliomkwaza na makofi yalikuwa haki yao.

    Lameck alikuwa anapagawa taratibu.

    Alipokuwa amejituliza chumbani kwake, mara ghafla akatambua kuwa hakutakiwa kulala, aibu ilikuwa inajongea kwa karibu sana.

    Lameck alifikiria mengi akaamini kuwa Emmy alikuwa mtu pekee wa kuweza kumshirikisha jambo hili zito ili wajue nini cha kufanya maana hili janga walilizua wao na sasa linasambaa kwa kasi. Tatizo simu ya Emmy haikuwa inapatikana.

    Akasimama akavaa nguo zake akaambatanisha na bastola yake kiunoni kwa ajili ya ulinzi wake mwenyewe, akatoweka.

    Moja kwa moja hadi nyumbani kwa Emmy. Akajivika ujasiri na kujifanya hana hofu japo moyo wake ulikuwa unapwita kwa kasi. Hakujua kwa nini Emmy hakuwa akipatikana kwenye simu hivyo hakujua kama James atakuwa ameanza kumuadabisha kwa uovu aliomfanyia ama la.

    Ilikuwa saa tatu usiku. Kwa kuwa anafahamika pale kuwa ni ndugu hakupata usumbufu akaingia ndani. Alikuwa ametanguliza machale mbele.

    Akamuulizia Emmy akaambiwa kuwa yu ndani amelala.

    James yeye alikuwa hajarejea nyumbani bado.

    Jibu hili likamfariji na kumpunguzia hofu bwana Lameck.

    “Naomba ukamuite.” Aliagiza. Grace akasimama na kuelekea katika chumba cha Emmy.

    Baada ya dakika kumi, Emmy alifika katika sebule, Grece akampiga kope Gloria, wakaelekea chumbani kwao. Sebule ikabaki na watu wawili tu. Emmy na Lameck.

    Emmy hakumtazama usoni Lameck, alimwonea aibu kiasi fulani na alikuwa na hasira bila kujua kwa nini amekasirika.

    “Emmy”

    “Bee.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nisikilize kwa makini sana.”

    “Nakusikiliza we ongea tu....halafu huyo Jose nani sijui yuko wapi ...sijui Sam.”

    “Nimemtupa huko aende zake ni mpumbavu sana.”

    “Ehee.” Akaguna na kumtazama usoni.

    “Sikia Emmy hutakiwi kulala hapa. Upo katika hatari kubwa.”

    “Hatari? Hatari ipi.”

    “Unaishi na muuaji. Muda wowote unauwawa.”

    Emmy akajiweka sawa, akaegemeza shavu katika kiganja chake, macho yake ya kurembua yakamtazama Lameck.

    Lameck akasimulia kila kitu kuhusu Jose B na uhusiano baina ya Jose na James.

    “Wanajuana?” Emmy akashangaa.

    “Ndio na wanafahamu kila kitu kuhusu sisi. Yaani unajua maana ya kila kitu eeh...n’do hivyo kwa hiyo James alikuwa anatafuta upenyo tu aanze kukuua wewe kisha mimi.” Lameck aliongea kwa kunong’oneza.

    Emmy akapaliwa na mate, akakohoa huku akijigonga gonga kifua. Akarejea katika hali ya kawaida.

    Taarifa ya kwamba anaweza kufa muda wowote ilimchanganya kuliko taarifa nyingine zozote zile.

    “Tena anamchukia sana huyo kiumbe tumboni mwako, mi nilikwambia ukabisha haya yako wapi sasa kumbe mumeo mwenyewe mtu mbaya sana. Halafu Emmy aibu inayokuja ni kubwa sana ujue. Aibu kubwa mno. Ni aibu ambayo itasababisha hata maiti zetu watu waogope kuzitazama usoni. Mtu na baba yake? Mh.” Lameck alizidi kuweka mkazo. Emmy akaishia kukodoa macho.

    “Ujue yaani kwa hiyo una maanisha....yaani mh..” akajiuma uma Emmy.

    “Mimi nimeamua kuondoka, bora nikaanze maisha kwingine lakini sihitaji kushuhudia maiti yangu ikionewa aibu kwa kweli. Na upande wako mimi sijui lakini ni lazima atakuua tu. Tena atakuua kwa mateso” Lameck alizungumza neno kifo kama neno la kawaida kabisa.

    Emmy akazidi kuchanganyikiwa. Akasisimka kusikia kuwa ni lazima atauliwa na mume wake. Tena kifo cha mateso.

    “Unaniacha Lameck wakati....wakati...tumefanya...nanii”

    “Sio kwamba nakuacha maamuzi yapo mikononi mwako hadi sasa hivi.” Kama ni kuondoka ama kubaki.

    “Tunaenda wote Lameck.” Emmy alinywea na kuamua kukabidhi maisha yake kwa Lameck.

    “Alfajiri sana. Nipigie simu. Hatutakiwi kuendelea kuweka rehani roho zetu na muuaji tunamjua.

    Walimaliza mazungumzo na Lameck akatoweka.

    Emmy aliingia chumbani kwake, akajirusha kitandani. Akatazama katika kabati akakutana na suti na nguo mbalimbali za mume wake.

    Akashtuka kama ameona jinamizi. Akaliendea kabati akaamua kulifunga.

    Alipogeuka kurejea kitandani akautana na ukuta ukiwa na picha kubwa ya James siku ya harusi yao. Akatokwa na yowe la hofu.

    Akakiendea kitufe cha kuzima na kuwasha taa, akazimisha.

    Giza likatawala.

    Emmy akagaagaa kitandani, akamfikiria Jose B, akamlaani kimya kimya kwa kuuchezea mwili wake ilhali akijua fika kuwa anamuuza kwa James na wao ni kitu kimoja kabisa.

    Machozi yakamtoka.

    “Hivi inachukua dakika ngapi kuua?” alijiuliza bila kupata jibu.

    Aliamini fika kuwa Jose B si mwanadamu na stahili yake ni kuuwawa.

    “Nimemfungulia biashara, nimempangishia nyumba nzuri. Kumbe ananizomea tu.....ina maana hata msibani alipokuja alikuwa ananichora tu hayawani yule.”

    Kilio cha kwikwi kikaendelea kutawala.

    Emmy aliusikia moyo wake jinsi ulivyokuwa ukipashika kwa joto la uchungu. Machozi yakaendelea kuilowanisha shuka.

    “Ila Mungu atanilipia tu, kama nimeipigania ndoa yangu kwa njia zisizokuwa sahihi Mungu anisamehe, nimejaribu sana, nimejaribu kupigana mimi, nimeuacha mwili wangu uchezewe na baradhuli, nimetumia pesa nyingi kuiamarisha ndoa hii. Tazama sasa kumbe na mtoto sio ridhiki yangu huyu. Naenda kumzalia baba yangu mtoto. Aibu gani hii...” alilalamika sana huku akiendelea kulia.

    Baadaye akapitiwa na usingizi hadi alipokuja kuamshwa majira ya saa nane na nusu usiku.

    Usiku wa mauzauza, usiku ambao ulibadili kila kitu katika maisha ya yake.



    ***CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog