Search This Blog

Sunday 19 June 2022

BOMU LA KARAFUU - 3

 







    Simulizi : Bomu La Karafuu

    Sehemu Ya Tatu (3)



    10 - Mateso



    Kile kivuko kilitia nanga kisiwani Chumbe ambapo magari, pikipiki, baisikeli na wenda kwa miguu walitoka kivukoni kuelekea pwani, kila mmoja akiwa na harakati zake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yale magari mawili ambamo walikuwemo Barshid na wenzake na lile lililokuwa na wale vijana na mateka wao Pei yalitoka pale kwa kasi na kuelekea upande wa kaskazini mwa kisiwa kile. Wakati wote huo bado Pei alikuwa hajazinduka, lakini alikuwa akipumua na hivyo kuwaondoa hofu wale vijana kuwa huenda angekuwa kesha poteza uhai.



    Baada ya kwenda umbali wa kama kilomita ishirini na tano hivi kutoka ufukweni, lile gari liliingia kulia likipita kwenye barabara nyembamba, katikati ya kiunga cha mikarafuu iliyokuwa imeshikamana vyema mithili ya msitu. Katika kiunga hicho ambacho kwa kukisia kingefikia kiasi ekari kumi hivi, ilikuwemo pia minazi na miti na mazao mengine.



    Kiasi kilomita mbili kutoka barabara kuu kulikuwa na geti ambalo liliunganisha pande mbili za uzio wa seng’enge. Ile Toyota ilipokaribia geti lilifunguliwa na vijana wawili waliokuwa wamevalia sare ambazo zilifanana kidogo na zile za askari wa mgambo. Wote walikuwa na silaha aina ya SAR. Yale magari mawili yalipita bila kusimama huku wale vijana wakiinua mikono yao kama ishara ya kupiga saluti, kisha wakafunga geti.



    Mwendo wa kilomita moja hivi zaidi kulikuwa na geti lingine kama lile la mwanzo, lakini hili liliunganisha uzio wa kuta mbili za matofali ya udongo. Ukuta huo kwa pande zote, kulia na kushoto haukuonekana mwishilio wake na ulikuwa mrefu, sehemu ya juu kukiwa na nondo zilizochongwa mfano wa misumari, zikiwa sehemu zimenyooka na sehemu zimepindishwa.



    Na mara hii pia asikari wawili waliovalia sare kama zile za wale wa mwanzo walifungua geti na kutoa salaam ya saluti magari yale yalipopita.



    Kuanzia pale kwenye geti kwa ndani kulikuwa na barabara pana iliyowekwa kokoto zilizoshindiliwa baraabara. Pande zote mbili za barabara hiyo zilikuwa wazi kukiwa na manyasi mazuri yaliyopandwa na kutunzwa vizuri. Hali kadhalika, kulikuwa na miti ya mikaratusi na maua ya aina mbalimbali.



    Mwisho wa barabara hiyo kuliwa na jumba kubwa la ujenzi wa kizamani, kama yale majengo ambayo yapo hadi sasa maeneo ya mji mkongwe, Unguja. Upande wa kulia, pembeni mwa jumba hilo kulikuwa na banda la wazi ambalo lingeweza kuhifadhi magari zaidi ya manne, na wakati huo lilikuwepo gari moja aina ya Toyota Hilux Pickup likiwa limeegeshwa.



    Yale magari mawili yalisimama mbele ya lile jumba na waliokuwemo wakatoka, isipokuwa Pei, ambaye bado alikuwa hajarudiwa na fahamu.



    Kati ya wale waliotoka kwenye ile Toyota, yule mgeni kutoka Visiwa vya Ngazija pamoja na mtu mwingine wa makamo, ambaye ilielekea ni baba wa Burshid waliingia kwenye lile jumba, wakiwa wamefunguliwa mlango na askari mwingine aliyekuwa kavaa sare.



    Wale vijana, Burshid na Osmun pamoja na wale wawili waliokuwa kwenye gari alilokuwamo Pei walisimama kando kidogo ya yale magari.



    “Sikia Dondwi, mchukueni huyo jamaa mpelekeni kule bandani. Mfungeni kamba na hakikisheni hafurukuti, tutakuja kumshughulikia hivi punde,“ Burshid alimwagiza mmoja wa wale vijana.



    “Sawa bosi, kuna lingine?“ yule aliyeitwa Dondwi aliuliza.



    “Hapana, ila hakikisheni mnakuwa nae hata kama mmemfunga kamba. Sisi tuna mazungumzo kidogo ndani, tutakuja huko mara tu tukimaliza,“ Burshid alisema.



    “Sawa bosi,“ Dondwi alijibu.



    Burshid na Osmun waliingia kwenye lile jumba wakiwaacha Dondwi na mwenzake wakisaidiana na wale madereva na walinzi wawili wakishughulika na kumtoa Pei kutoka kwenye gari.



    Walimbeba mzobe - mzobe hadi kwenye banda moja kubwa lililokuwa nyuma ya lile jumba. Ndani ya banda hilo kulikuwa kumesheheni marobota mengi yaliyojaa karafuu zilizokaushwa. Kwa kukisia haraka haraka, zingefikia hata tani mia moja, marobota hayo yakiwa yamepangwa kwa ustadi mkubwa, yakiwa yameshonana kulia na kushoto na kuacha njia nyembamba katikati.



    Upande wa kulia unapoingia kwenye banda hilo kulikuwa na kijichumba cha ukubwa wa kama futi nane kwa nane ambacho kilijengwa kwa kutumia mbao laini, na hakukuwa na mlango. Mle ndani mlikuwa na meza moja ndogo na viti vitatu vya mbao. Kulikuwa pia na kabati moja dogo la mbao la milango miwili.



    Wale vijana walimwingiza Pei kwenye chumba hicho kisha wakamkalisha kwenye kimoja kati ya vile viti vitatu, kiti ambacho kilikua pembeni kwenye kona. Katika ile hali ya kumsukasuka tangu walipomtoa kwenye gari hadi mle bandani, Pei alianza kurejewa na fahamu. Walipomketisha kwenye kile kiti na kuanza kumfunga kamba, maumivu yalimfanya ashituke.



    “Anhaa, umezinduka eenh, safi sana, basi poa, tulia tukupe starehe unayostahili,“ mmoja wa wale vijana alisema, huku wenzake wakicheka.



    Pei hakujibu lolote kwani bado fahamu zilikuwa hazijamrudia sawasawa. Kila walipokuwa wakikaza zile kamba, mwili wake ulishtuka kwa maumivu, na ni hali hiyo ndiyo iliyomzindua pia akili ambapo taratibu aliihisi hatari iliyokuwa ikimkabili.



    Ukiwauliza wale ambao wapo kwenye kazi za ukachero, watakueleza kuwa moja ya mafunzo magumu waliyopitia ni yale yenye kuhusu jinsi ya kuuwezesha mwili kukabiliana na mateso ya kila aina, wenyewe kwa lugha ya Kiingereza wanasema “endurance to torture and pain.“ Ni jinsi ambavyo mtu anaweza kuvumilia matezo na maumivu yanayotokana na mateso hayo.



    Kila kiungo cha mwili wa Pei kilizinduka kutokana na ukweli uliomshukia kuwa sasa alikabiliwa na mateso na kwamba anahitajika kuwa na uvumilivu wa hali ya juu. Na si hivyo tu, bali pia kutafuta haraka njia ya kujinasua kutoka kwenye mateso yanayomkabili. Alikumbuka moja ya kanuni za mafunzo aliyopitia kuwa endapo angekabiliwa na kufungwa kamba mwilini, basi ajitahidi kutunisha misuli ya maeneo ambayo kamba hiyo itapita wakati anafungwa.



    Hii ni kanuni yenye maana rahisi kwamba baada ya kufungwa kamba ukiwa umetunisha misuli, basi baadaye utaweza kulegeza misuli yako na hivyo kulegeza kamba ulizofungwa na hivyo pengine kukupa nafasi ya kujikwamua. Na ndivyo alivyofanya Pei. Alitunisha misuli kwa namna ambayo wale vijana hawakugundua alichokuwa akikifanya, na hasa kwa vile wao hawakupitia mafunzo kama hayo. Basi walipoona Pei analalamika kila walipokaza kamba, wakadhani kuwa zinambana barabara, kumbe sivyo ilivyokuwa.



    Lakini pamoja na kwamba Pei alitumia ujanja huo, bado mwisho wa siku haikumsaidia sana. Kweli baada ya kufungwa aliweza kulegeza kamba na kupunguza maumivu, lakini kitendo kwamba mikono ilifungwa barabara kwa nyuma ya kiti, na kila mguu ulifungwa pamoja na tendegu moja la kiti ilimfanya asiweze kufurukuta. Kibaya zaidi ni kwamba baada ya kumfunga ni vijana wawili tu waliotoka, wengine wawili walibaki wakimlinda.

    Wakati huo tayari alikwishapekuliwa, ambapo vitu alivyokuwa navyo ikiwemo simu yake ya mkononi, saa, pochi iliyokuwa na pesa kidogo na viatu alivyokuwa amevaa vilichukuliwa. Katika kupekuliwa huko, waliomteka walidhani wangepata japo fununu ya kuwa yeye ni nani, lakini Pei hakuwa na kitambulisho wala karatasi yoyote ambayo ingeweza kuwafahamisha yeye alikuwa nani. Kibaya zaidi ni kwamba hata simu yake sehemu ya majina ilikuwa tupu, na wala hakukuwa na orodha ya simu zilizopigwa au kupokelewa, wala sehemu ya ujumbe mfupi haikuonyesha sms zilizotumwa au kupokelewa au kuhifadhiwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kukosekana kwa yote hayo kuliwakadhibisha sana wale vijana, hasa Burshid ambaye alionekana wazi kuwa alikuwa ndiye kinara wao. Hali hiyo ilimuingiza Pei kwenye mateso makubwa. Baada ya wale vijana kwenda kumfahamisha Burshid kuwa mateka wao alikwishafungwa na yuko tayari kwa usaili, Burshid na Osmun walikwenda kule kwenye ghala. Mkononi Burshid alikuwa na mkia wa taa, ambao kwa kuutizama tu ulikuwa unaogopesha kwa kuwa ulikuwa mnene na wenye magamba yaliyochanua, makali.



    Kufika tu pale alipokuwa kafungwa Pei, Burshid alimzaba kofi la uso ambalo lilimchana mdomo na damu ikaanza kumtiririka.



    “Hiyo ni salaam tu. Unauona huu, bila shaka unaujua kuwa ni mkia wa taa, na unafahamu unaathari gani ukitandikwa nao. Ukitaka usalama wako usinilazimishe kuutumia, nijibu maswali yangu kwa kadri nitakavyokuuliza, vinginevyo...teh-teh-teh, ndugu, utajuta kuzaliwa. Unaitwa nani na umetumwa na nani kutufuatilia?“



    Huku mdomo ukiwa unatoa damu, Pei alikaa kimya akawa anamtazama Burshid bila kupepesa jicho. Burshid aligeuka kuwatazama wenzake huku akiwa na tabasamu la dharau, kisha kwa spidi ambayo Pei hakuitarajia, Burshid aligeuka akainua ule mkia wa taa juu na kisha akaushusha kwa nguvu nyingi mara mbili, ukatua kwenye mabega ya Pei, ukachana shati na ngozi. Yalikuwa ni maumivu makali ambayo yalimfanya Pei atoa ukelele mkubwa. Damu ilianza kumchuruzika kutokea pale ule mkia wa taa ulipomchana mabegani.



    “Narudia tena. Unaitwa nani na nani kakutuma utufuatilie?“



    “Sijui unachokizungumza...sijatumwa na mtu, mmefanya makosa kunileta huku...sihusiki na.....“



    “Nyamaza! Usitufanye sisi wajinga, tunajuwa ulikuwa unatufuatilia tangu jana kule Hoteli ya Ufukoni. Kwa usalama wako, jibu maswali yangu, la sivyo bora uswali sala yako ya mwisho.“



    “Sijui unachokizungumza......“



    Burshid alisogea hadi kwenye kiti alichofungwa Pei, akaupeleka uso wake karibu kabisa na uso wa Pei.



    “Bro, nadhani huthamini maisha yako, basi kwa taarifa yako utaongea na utanieleza ninachotaka kufahamu, na.....“



    Hakumalizia alichotaka kusema kwani Pei alivurumusha bonge funda la mate yaliyochanganyika na damu, likatua kwenye macho ya Burshid na kumfanya asiweze kuona kwa sekunde kadhaa. Kitendo hicho kiliwakasirisha wengine wote waliokuwapo pale, basi Pei alipokea kipondo si cha kawaida, ambapo kila aliyekuwepo alimpiga alipopataka na kwa namna aliyoitaka. Mwisho wa yote, Pei akiwa bado amefungwa kwenye kiti alikuwa sakafuni, hajitambui kabisa, na laiti kama isingekuwa Mzee Mudrick na yule mgeni kuingia ghalani, basi bila shaka Pei angekata roho.



    “Inatosha, mwacheni!“ Hiyo ilikuwa ni sauti kali ya Mzee Mudrick.



    “Hapana, haitoshi baba, amekataa kusema lolote, na isitoshe amenitemea mate usoni,“ Burshid alilalama akiwa ameinuwa juu ule mkia wa taa akitaka kuendelea kumlabua Pei.



    “Inatosha, akirudiwa na fahamu mtaendelea kumbana, ataongea, ikishindikana wakati huo basi itakuwa ni msiba wake,“ Mzee Mudrick alisema, na akasikilizwa.



    Kiti alichofungwa Pei kikainuliwa wima, mwenyewe akiwa hana fahamu. Alikuwa hatamaniki, mwili mzima ulitapakaa damu na uso ulimtutumka ukawa mithili ya bumunda. Mzee Mudrick, mgeni wake na wale vijana wakatoka na kumuacha Pei akiwa kusikojulikana katika hali ya kuzimia.









    11-Mbaroni



    Majira ya saa sita na nusu hivi, maafisa wanne kutoka Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KKMZ) au maarufu kama SIAFU waliingia ofisi za BIKANGA, wote walikuwa wamevaa kiraia. Kiongozi wao alikuwa Mkuu wa kikosi hicho, Kessi Kussi (KK).



    ‘‘Cheichei,” Kessi Kussi alimuamkua Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi Mtendaji wa BIKANGA, ambaye alikuwa ni Zamoradi, shogake BeBe.



    “Cheichei....karibuni,“ Zamoradi aliitikia ile salama na akawakaribisha.



    “Asante sana. Mimi naitwa Kessi Kussi ni Mkuu wa KKMZ, na hawa ni maafisa wenzangu. Tunahitaji kumuona Mkurugenzi, tumemkuta?“ Kessi Kussi alisema.



    “Yupo, lakini anajiandaa kwenda masjid. Mlikuwa na miadi naye?“ Zamoradi aliuliza.



    “Hapana, hatuna miadi, lakini ni muhimu tuonane nae sasa,“ Kessi Kussi alijibu.



    “Ngoja nimuulize kama atawaona.“

    Zamoradi aliinua mkono wa simu ya mezani na kisha kutofya vitufe kadhaa kwenye simu, ilipoitikiwa alisema:



    “Samahani Mkurugenzi, Bwana Kessi Kussi kutoka KKMZ yupo hapa anahitaji kukuona.“



    “Mbona sina miadi naye na najiandaa kwenda msikitini. Hawezi kuja baada ya saa nane, nitakuwa nimerudi,“ Mkurugenzi alijibu.



    “Nimewaeleza kuwa ulikuwa unajiandaa kwenda masjid, lakini wamesema ni muhimu wakuone sasa,“ Zamoradi alijibu.



    “Mbona unasema wamesema, kwani wapo wangapi?“ Mkurugenzi aliuliza.



    “Wapo wanne,“ Zamoradi alimfahamisha.



    Mkurugenzi alikaa kimya kidogo, akajiuliza kulikoni? Hata hivyo alijipa moyo kuwa huenda ni shughuli za kawaida za kikazi, ingawa alifahamu kuwa mara nyingi KKMZ wanapotembelea ofisi za mashirika, au hata za watu binafsi huwa kuna jambo.



    Lakini ghafla moyo wake ulimshtuka, akawaza:



    “Isijekuwa hawa wamenusanusa kuhusu hili dili na yule Mngazija? Hizi pesa...mnh, nimefanya jambo la kijinga kutoziondoa mapema hapa ofisini. Lakini sidhani kama wamekuja kwa hilo, wamejuaje? Aah, nisijipe ugonjwa wa moyo bure!“



    Baada ya tafakari hiyo akasema: “Sawa, waingie.“



    “Haya, karibuni,“ Zamoradi aliwakaribisha Kessi Kussi na wenzake.



    “Asante,“ Kessi Kussi alisema.



    Waliingia ofisini kwa Mkurugenzi ambaye walimkuta akiwa ameketi kwenye kiti nyuma ya meza yake kubwa iliyokuwa imesheheni majalada na makaratasi mengine yaliyokuwa yamezagaa bila mpangilio maalum. Walipoingia, alisimama na kuwakaribisha.



    “Assalaam Alleikum, karibuni mketi,“ Mkurugenzi alisema, huku naye akiketi kwenye kiti chake.



    “Wa-Alleikum salaam. Samahani kwa kuja bila taarifa, lakini jambo lililotuleta ni la muhimu sana, hivyo tunaomba utuwie radhi,“ Kessi Kussi alimweleza.



    “Bila shaka, naona huu ni ugeni mzito, karibuni sana,“ Mkurugenzi alijibu.



    “Asante. Mimi naitwa Kessi Kussi, ni Mkuu wa KKMZ, na nimeongozana na hawa wenzangu,“ Kessi Kussi alifanya utambulisho kwa upande wake.



    “Sawa, ingawa hatujawahi kukutana lakini nakufahamu kwa jina tu kutokana na mawasiliano ya simu na pia ya kiserikali. Mimi naitwa Swadif Hinda, ni Mkurugenzi Mtendaji wa BIKANGA,“ Mkurugenzi naye alijitambulisha.



    “Ndugu Swadif, nami pia nakufahamu kwa njia hiyo. Naomba, tusipoteze muda. Ujio wetu hapa tunafuatilia taarifa tuliyonayo kwamba unahusika na magendo ya karafuu, na..“

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kessi Kussi hakumaliza alichokuwa anataka kusema kwani Mkurugenzi Swadif alinyanyuka kwenye kiti chake kama vile mtu aliyechomwa na msumari.



    “Sawa, ingawa hatujawahi kukutana lakini nakufahamu kwa jina tu kutokana na mawasiliano ya simu na pia ya kiserikali. Mimi naitwa Swadif Hinda, ni Mkurugenzi Mtendaji wa BIKANGA,“ Mkurugenzi naye alijitambulisha.



    “Ndugu Swadif, nami pia nakufahamu kwa njia hiyo. Naomba, tusipoteze muda. Ujio wetu hapa tunafuatilia taarifa tuliyonayo kwamba unahusika na magendo ya karafuu, na..“



    Kessi Kussi hakumaliza alichokuwa anataka kusema kwani Mkurugenzi Swadif alinyanyuka kwenye kiti chake kama vile mtu aliyechomwa na msumari.



    “Nini..nani, mimi? Magendo gani? Mimi sina uhusiano wowote na magendo ya karafuu,“ aling’aka.



    “Tafadhali keti chini Ndugu Swadif, keti chini unisikilize,“ Kessi Kussi alisema.



    “Sawa, lakini hizo tuhuma zinanishangaza sana. Magendo na mimi wapi na wapi?“ Mkurugenzi Swadif alisema, lakini kidogo sauti yake ilionyesha kupoteza makali.



    “Tulizonazo ni taarifa tu Ndugu Swadif, na ndio maana tumekuja hapa ili tuongee nawe na kupata ukweli wa jambo hili, kwa hiyo ni vyema ukatoa ushirikiano unaostahili,“ Kessi Kussi alisema, huku wale aliofuatana nao wakiwa wapo kimya kabisa.



    “Sawa, nakusikiliza,“ Mkurugenzi Swadif alisema, akaegama kwenye kiti chake na kufumbata mikono yake kifuani.



    “Ndugu Swadif, una pesa zozote hapa ofisini kwako hivi sasa? Tafadhali tueleze una fedha kiasi gani na umezipataje, kama unazo,“ Kess Kussi alisema akiwa ametulia kwenye kiti.



    Na safari hii pia Mkurugenzi Swadif alisimama wima kama vile aliyekuwa kakalia kaa la moto.



    “Sikilizeni jamani, masuala ya mimi kuwa na pesa ni masuala binafsi, na silazimiki kumweleza yoyote juu ya hilo. Tafadhalini, kama hamna lingine naomba mniruhusu nitoke niwahi msikitini,“ Mkurugenzi Swadif alisema huku akiwa anatoka kwenye meza yake na kufanya kama vile anayetaka kutoka nje.



    Kess Kussi na wenzake nao wote walisimama na kuweka kama kizuizi fulani hivi, jambo ambalo lilimfanya Mkurugenzi Swadif arudi nyuma ya meza yake, akabaki amesimama akiwatazama.



    “Sikiliza Ndugu Swadif, sisi hatukuja hapa kucheza, tupo kazini. Ikiwa hutaki kutueleza ni kiasi gani cha fedha ulicho nacho hapa ofisini kwako na maelezo ya ulikozitoa, basi tutafanya upekuzi,“ Kess Kussi alisema.



    “Hapana, sitaruhusu upekuzi wa aina yoyote, na wala sitaeleza kuhusu pesa nilizo nazo kwa sababu hilo haliwahusu,“ Mkurugenzi Swadif alisema akawa ananyoosha mkono akitaka kuchukua simu yake ya mkononi.



    “Tafadhali usiguse chochote hapo mezani kwako. Tusingependa kutumia nguvu katika jambo hili, lakini ukitulazimisha tutafanya hivyo na itakuwa mbaya sana kwako,“ Kessi Kussi alimtahadharisha.



    Mkurugenzi Swadif alirudisha mkono na kisha kurudi nyuma na kukisuma kiti chake, almanusura angeanguka, hasa pale alipoona mmoja wa wale maofisa alioongozana nao Kessi Kussi akiwa ametoa bastola iliyomlenga.



    “Basi, basi, mnaweza kufanya upekuzi kama mnavyotaka, lakini kuna pesa zangu nimezihifadhi humu ofisini, ni zangu, za halali kabisa,“ Mkurugenzi Swadif alisema.



    “Ni shillingi ngapi?“ Kess Kussi aliuliza.



    “Sio shillingi ....ni dola za Marekani...dola elfu kumi na...hapana elfu ishirini na tano,“ Mkurugenzi Swadif alisema, huku akionyesha wazi kuwa wasiwasi mkubwa ulimtanda.



    Kessi Kussi na wenzake walitupiana macho ya mshangao waliposikia thamani ya fedha alizozitaja Mkurugenzi Swadif.



    “Dola za Marekani elfu ishirini na tano, fedha hizo kwa hesabu ya haraka haraka ni shilingi zetu za madafu milioni ishirini na nne na ushee! Ndugu Mkurugenzi umezipataje fedha hizo, wewe ukiwa kama mtumishi wa umma,“ Kess Kussi alimuuliza.



    “Nimezipata kutokana na biashara zangu na.....aah, kwa kifupi ni pesa zangu,“ Mkurugenzi Swadif alisema, huku akimeza funda zito la mate na akionekana wazi kutokwa na kijasho chembamba kilichoanzia kwenye paji la uso.



    “Tafadhali zitoe hizo dola tuzione,“ Kessi Kussi alisema.



    “Zipo hapo kwenye kabineti, zichukueni,“ Mkurugenzi Swadif alisema.



    “Hapana, ni pesa zako, kazitoe mwenyewe, na ni vyema uharakishe, tuna kazi nyingine zinatusubiri,“ Kessi Kussi alisema huku sauti yake ikiwa kali kidogo.



    Bila kusema lolote zaidi, Mkurugenzi Swadif aliondoka kwenye meza yake akaenda hadi lilipokuwa kabineti la chuma la kuwekea makabrasha, akalifungua na kutoa mkoba mdogo wa ngozi ambao ulionyesha kutuna kutokana na vilivyokuwemo.



    “Ni hizi hapa,“ alisema akijaribu kumkabidhi mkoba huo Kessi Kussi.



    “Ufungue huo mkoba ili tuone hizo fedha,“ Kessi Kussi alimwamrisha.



    Mkurugenzi Swadif alifungua ule mkoba ambao kweli ulijaa noti za dola za Marekani.



    “Hizi hapa,“ Mkurugenzi Swadif alsiema huku sauti yake ikizidi kugwaya.



    “Zitoe zote uzihesabu,“ Kessi Kussi alimwamrisha.



    “Zipo zote, sina haja ya kuzihesabu,“ Mkurugenzi Swadif alisema huku akijaribu kufunga ule mkoba.



    “Nimesema zitoe zote uzihesabu tuhakikishe kama zipo kamili kama ulivyosema,“ Kessi Kussi alisema kwa sauti kali.



    Mkurugenzi Swadif alitoa mabunda ya zile noti ambayo yalikuwa yamefungamanishwa kwa mpira, “rubber band.“ Wakati alipotoa bunda la kwanza, juu yake kulikuwa na karatasi nyeupe iliyofungamanishwa na zile pesa. Haraka haraka, akaichomoa ile karatasi na kutaka kuichanachana, lakini hakuwahi, Kessi Kussi alimkataza kwa sauti kali kabisa.



    “Heei, acha, usiichane hiyo karatasi, lete tuone nini kimeandikwa juu yake,“ Kessi Kussi aliamuru.



    “Hapana, haina kitu, ni karatasi tu,“ Mkurugenzi Swadif alisema kwa sauti iliyonywea, huku akijaribu tena kuichanachana.



    “Nimesema usiichane, iweke juu ya meza,“ Kessi Kussi aliamrisha huku akimsogelea Mkurugenzi Swadif, ambaye kwa mkono uliokuwa ukitetemeka dhahiri aliiweka ile karatasi juu ya meza.



    Kessi Kussi na mmoja wa wale maafisa wengine walisogea na kuiangalia ile karatasi na wakagundua kuwa ilikuwa na majina manne ambayo yaliwashitua sana. Yalikuwa ni majina ya vigogo, wawili kutoka Wizara mbili za Serikali, mmoja kutoka jeshi la polisi, na mmoja kutoka kikosi cha SIAFU. Isitoshe, mbele ya kila jina kulikuwa na namba iliyoonyesha dola za marekani.



    “Mnh, Bwana Swadif, kwa hiyo huu ndio mgao wa hizi fedha siyo?“ Kess Kussi aliuliza.



    Mkurugenzi Swadif hakujibu. Mwili mzima ulikuwa ukimtetemeka, alibaki kajiinamia.



    “Ok, zihesabu hizo pesa,“ Kessi Kussi alimwamrisha tena.



    “Lakini...hizi, aah, zipo sawa tu,“ Mkurugenzi Swadif alisema.



    “Zihesabu tuhakikishe,“ Kess Kussi alimweleza kwa sauti iliyokuwa imekaza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati Mkurugenzi Swadif akiwa katika zoezi la kutoa zile fedha ili azihesabu, simu ya mezani kwake iliita, akasita kutaka kwenda kuipokea.



    “Iache iite, endelea na shughuli yako, na harakisha muda umekwenda,“ Kessi Kussi alimwamrisha tena.



    Ile simu iliita ikakatika, kisha ikaita tena ikakatika. Mara mlango wa ofisi yake Mkurugenzi ukagongwa. Mmoja wa wale maafisa aliufungua kiduchu akatoa kichwa kuona nani aligonga, akamwona Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi.



    “Samahani, kuna simu ya Mkurugenzi kutoka Wizarani, wanasema ni ya muhimu,“ Katibu Muhtasi Zamoradi alisema.



    “Waambie hawezi kupokea simu kwa sasa, wapige baadaye,“ yule afisa alimwelekeza.



    “Lakini...“ Zamoradi alianza kulalama.



    “Mama, hakuna cha lakini, wajibu hivyo, na usigonge tena mlango,“ yule afisa alisema kwa sauti kali kidogo, kisha akaufunga ule mlango.



    Mkurugenzi Swadif alikuwa katikati ya kuhesabu zile fedha huku Kess Kussi na wenzake wakifuatilia kwa makini. Alipomaliza na kuthibitika kuwa kweli zilikuwa dola za Marekani elfu ishirini na tano, akaufunga ule mkoba, ikiwa ni baada pia ya kurejesha kile kikaratasi kilichokuwa na majina ndani ya mkoa ule.



    “Hizi hapa,“ akawa anataka kumkabidhi ule mkoba Kessi Kussi.



    “Ni zako, utazibeba mwenyewe. Nyanyuka twende,“ Kessi Kussi alimweleza.



    “Mnanipeleka wapi jamani. Hizi pesa ni zangu za halali,“ Mkurugenzi Swadif alilalama.



    “Tunakokupeleka utakufahamu tukifika, na suala kuwa pesa ni zako za halali au si za halali litajulikana hukohuko,“ Kessi Kussi alisema huku akiashiria waondoke.



    “Basi, subirini jamani, naomba nimwachie maagizo sekretari wangu,“ Mkurugenzi Swadif aliomba.



    “Muda huo hatuna, utampa maagizo au kuwasiliana na yeyote umtakaye tukiwa huko twendako,“ Kessi Kussi alisema huku akiwaashiria wale maafisa aliofuatana nao waondoke.



    Alichoruhusiwa kuondoka nacho kutoka pale ofisini kwake ilikuwa simu zake mbili za mkononi na ule mfuko uliokuwa na pesa, ambao alikuwa kaushika kama vile mtu anavyoshika chetezo chenye makaa ya moto.



    Walipotoka walimkuta katibu muhtasi wake, Zamoradi, akiwa wima na mwenye wasiwasi. Kwa hali aliyomuona nayo bosi wake wakati akitoka ofisini kwake akiwa kawekwa mtu kati na wale maafisa wa KMKZ, alijuwa wazi kuwa mambo hayakuwa shwari.

    “Vipi Mkurugenzi, mbona hivi?“ aliuliza.



    “Ah, mama, siwezi kusema lolote kwa sasa, nitakupigia simu. Naomba ukae kimya kwa sasa, endelea na kazi zako,“ Mkurugenzi Swadif alijibu.



    “Anachosema ni kweli mama. Endelea na kazi zako kama kawaida, tusingependa kusikia lolote juu ya kuondoka kwetu na Mkurugenzi. Lolote likisikika tutajuwa ni wewe na utajiweka katika hali mbaya, umesikia?“ Kessi Kussi alimweleza kwa sauti kali kidogo.



    “Ndiyo, ndiyo...nimeelewa. Sitasema lolote,“ Zamoradi alijibu kwa sauti iliyojaa wasiwasi, kisha akawapisha wakatoka.



    Baada ya wale maafisa wa KKMZ kutoka pale ofisini, na alipowachungulia na kuhakikisha wameondoka kwa kutumia gari la KKMZ, uvumilivu ulimshinda Zamoradi, akainua simu.



    Alibonyeza vitufe kadhaa na simu ilipopokelewa upande wa pili, ikawa:



    “Beli, hapa kumetokea jambo kubwa, hapa nilipo nguvu sina.“



    “Jambo gani Zamo?“



    “Bosi wangu kakamatwa na watu wa KKMZ.“



    “Kakamatwa? Imekuwaje, Zamo?“ BeBe ambaye alikuwa anajua kilichokuwa kikiendelea aliuliza.



    “Hata sielewi Beli. Wajua muda mfupi tu tangu uliponipigia na kuniuliza kama bosi wangu yupo walifika wale maafisa wa KKMZ. Au unalijua jambo hili Beli?“



    “Sikiliza Zamo. Umeshamweleza mtu mwingine yeyote kuhusu tukio hilo?“



    “Hapana, ni wewe tu niliyekupigia?“



    “Sawa, tafadhali kaa kimya, endelea na shughuli zako. Hili jambo ni zito. Jioni tukikutana nitakueleza nini kimetokea, sawa mpenzi.“



    “Sawa, Beli, lakini...“



    “Aa-aah, tulia Zamo, usitake kujua mengi kwa wakati huu, yatakuchanganya.“



    “Mnh...aaah, sawa Beli.“



    “Ok, tutaonana baadaye.“



    Mara baada ya kuzungumza na Zamoradi, BeBe alimpigia simu Mkuu wa KKMZ, Kessi Kussi a.k.a KK, na mazungumzo yakawa:

    “Halo Mkuu, nina taarifa kuwa mkurugenzi wa BIKANGA yupo mikononi mwenu, ni kweli?“



    “Aah, tena ni vyema umenipigia A5, ni kweli tunaye. Tafadhali njoo Hoteli ya Ufukoni baada ya kama masaa mawili hivi. Nimeongea na MB, atakuwa pamoja nasi wakati huo. Vipi unataarifa zozote kuhusu Pei?“



    “Hapana Mkuu, bado sijawa na mawasiliano naye, lakini naamini bado yupo mikononi mwa hawa waendesha magendo. Napanga mkakati wa kwenda kumwokoa na nashauri tulizungumzie hilo tutakapokutana.“



    “Vyema A5, sijui yupo katika hali gani hadi sasa, maana jamaa hawa ni makatili wa kupindukia.“



    “Aah, ndiyo misukosuko ya hizi kazi zetu, lakini hisia zangu zinaniambia kuwa bado yupo hai, ingawa kwa vyovyote vile watakuwa wamemtesa sana.“



    “Ok, basi tuonane Hoteli ya Ufukoni baadaye.“



    “Sawa Mkuu.“



    Mazungumzo hayo yaliishia wakati BeBe na dereva Kaku walishafika Michenzani. BeBe alimwagiza dereva amfuate baada ya dakika arobaini na tano. Alipandisha juu, akaingia kwenye flati ya shogake Zamoradi ambako haraka haraka aliunganisha kinasa sauti walichokuwa wamekitega usiku kule chumbani kwa yule Mngazija. Kama matarajio yake yalivyokuwa, zilisikika sauti za wale vijana na yule mgeni wao.



    Yote waliyoyazungumza yalithibitisha wazi kuwa lile lilikuwa kundi la sehemu ya mtandao wa waendesha magendo ya karafuu. Mipango ya jinsi ya kuvusha kiasi kikubwa cha karafuu ilipangwa, ambapo pamoja na kutoa fedha nyingi za kununua karafuu hizo kwa njia ya magendo, zilitengwa pia fedha za kuwahonga baadhi ya maafisa wa ngazi za juu serikalini, ikiwa ni pamoja na idara na taasisi muhimu.



    BeBe alishangaa sana aliposikia nyadhfa na majina ya waliotajwa kugawiwa hongo hilo. Hakujua kwa wakati ule kuwa KK naye alikuwa na orodha hiyo ya baadhi ya viongozi. Alipokwisha kusikiliza mazungumzo yote yaliyonaswa na kile kinasa sauti, alikirudisha kwenye kifuko chake na kisha akatayarisha zana za mapambano ambazo alipanga kuzitumia usiku katika harakati za kwenda kumuokoa Pei, na pia kuwatia mbaroni wale waendesha magendo.



    Aliporidhishwa na maandalizi yake aliingia bafuni kuoga, wakati huo ikiwa tayari muda wa kukutana na Wakuu wake ukiwa umekaribia. Alipotoka nje akiwa amebeba begi dogo lakini lililokuwa na vifaa muhimu, alimkuta dereva Kaku akimsubiri. Walikwenda moja kwa moja hadi Hoteli ya Ufukoni.



    “Ni vyema ukajitayarishe maana jioni hii kutakuwa na safari ya kwenda Chumbe. Nifuate hapa saa kumi na moja jioni,“ BeBe alimwagiza dereva Kaku.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sawa mama. Jambo moja, nina silaha ya moto ambayo naimiliki kihalali, ni bastola, je niwe nayo?“



    “Bila shaka, itakuwa vizuri maana lolote linaweza kutokea na hiyo silaha ikawa na manufaa makubwa.“



    “Sawa, basi tutaonana baadaye.“





    “Ni vyema ukajitayarishe maana jioni hii kutakuwa na safari ya kwenda Chumbe. Nifuate hapa saa kumi na moja jioni,“ BeBe alimwagiza dereva Kaku.



    “Sawa mama. Jambo moja, nina silaha ya moto ambayo naimiliki kihalali, ni bastola, je niwe nayo?“



    “Bila shaka, itakuwa vizuri maana lolote linaweza kutokea na hiyo silaha ikawa na manufaa makubwa.“



    “Sawa, basi tutaonana baadaye.“









    12 – Aibu



    Walipoachana, BeBe aliingia hotelini na akapanda hadi ghorofa ya pili ambako alikwenda moja kwa moja chumba #26. Aligonga mlango, na alipoitikiwa aliufungua akaingia. Ndani alimkuta MB akiwa peke yake ameketi kwenye sofa, juu ya meza ndogo iliyokuwa pembeni mwa sofa hilo kulikuwa na glasi iliyojaa aina fulani ya juisi.



    “Habari Mkuu,“ BeBe alitoa salaam.



    “Nzuri A5, vipi mambo?“



    “Si mazuri sana, lakini tumepiga hatua.“



    “Ni kweli. Pamoja na kuwa hatuna uhakika na hali ya Pei, lakini hatua hii mliyofikia si mbaya, ni nzuri. KK yupo njiani na wanakuja na Mkurugenzi wa BIKANGA. Tunataka tujue mbivu na mbichi juu ya jambo hili.“



    “Mpango mzima ukoje, Mkuu?“



    “Aaa, kimsingi tunataka tumshawishi huyo mkurugenzi awapigie simu wale walioorodheshwa kupewa hongo ya zile dola 25,000, waje hapa kuchukuwa mgao wao.“



    “Ni mtego mzuri wa kuwanasa, lakini atakubali?“



    “Nadhani atakubali maana hivi sasa amechanganyikiwa, na sisi tunataka kutumia hiyo hali ya kuchanganyikiwa kwake ili tuweze kuwatia mbaroni hao jamaa zake?“



    “Sawa Mkuu, ni mpango mzuri. Hapa ninayo tepu ya mazungumzo yao walipokuwa wakipanga mikakati yao ikiwa ni pamoja na huo mgao wa fedha. Mkuu, umeamini hisia zangu za mwanzo kabisa juu ya kuwapo kwa wasaliti ndani ya SIAFU?“



    “Ndiyo, zilikuwa ni hisia sahihi kabisa, hata KK ameshtushwa sana kuona kuwa mmoja wa wasaidizi wake wa karibu yumo kwenye ile orodha ya mgao.“



    Wakiwa katika maongezi hayo, mlango uligongwa na kufunguliwa sawia. Aliingia KK akiwa pamoja na mmoja kati ya wale maafisa wawili aliokwenda nao kule kwenye ofisi za BIKANGA. Pia aliingia Mkurugenzi Swadif, ambaye alikuwa amefungwa pingu mikononi.



    “Karibuni mkae,“ MB aliwakaribisha.



    Wote walipokuwa wameketi, huku Mkurugenzi Swadif akijaribu kuficha mikono yake yenye pingu, MB alianzisha maongezi.



    “Ndugu Swadif, hatuna haja ya kupoteza muda. Bila shaka unaelewa kuwa umejiingiza katika matata makubwa na ni juu yako kufanya kila unaloweza ili kujinasua. Sisi tupo tayari kukusaidia kama utakuwa radhi kutoa ushirikiano tunaouhitaji kutoka kwako.“



    Mkurugenzi Swadif alimeza funda la mate, kisha akasema:



    “Ni ushirikiano wa namna gani, na mtanisaidiaje niondokane na balaa hili?“



    “Kukusaidia kwetu kutategemea ushirikiano wako. Kikubwa tunachotaka ni kuwatia mbaroni hawa watu wote wanne walioorodheshwa kwenye mgao wa zile pesa. Bila shaka wewe ambaye ndiye uliyekutwa na fedha hizo ndiye pia ambaye unatakiwa kuwafikishia mgao wao, siyo?“



    “Ndiyo.“



    “Sawa, sasa tunataka uwapigie simu mmoja baada ya mwingine, waambie waje hapa hotelini kuchukua mgao wao.“



    “Halafu wakishakuja itakuwaje?“



    “Hilo tuachie sisi. Utakachotakiwa kufanya ni kumkabidhi kila mmoja bahasha yenye mgao wake, na utakuwa umekamilisha jukumu lako.“



    “Bado hujanifafanulia mimi hiyo itanisaidiaje. Je nikitoa ushirikiano huo mtaniachia huru?“



    “Ukweli ni kwamba hutaachiwa huru, lakini kuhusika kwako kutashughulikiwa kwa namna tofauti.“



    “Aah, hiyo haitanisaidia na.....“ Mkurugenzi Swadif alianza kulalama, lakini hakufika mbali.



    “Sikiliza Ndugu Swadif, usitusumbue. Fahamu kuwa tunatumia njia hii nyepesi kwako kwa sababu tu za kiungwana, vinginevyo tungetumia njia tofauti ambayo kwa hakika ingekuwa mbaya sana kwako. Tafadhali, usitufikishe huko,“ KK alifoka akiwa amesimama akimkabili Mkurugenzi Swadif.

    “Ni kweli Ndugu Swadif, tunao uwezo wa kutumia njia mbaya sana za mateso kupata taarifa tunazozihitaji kutoka kwako, lakini tumeona hilo tuliache kwa sasa, hata hivyo usipotoa ushirikiano basi tutalazimika kutumia njia hizo, na kila nikikuangalia kamwe hutaweza kuhimili hata chembe ya njia tunazoweza kutumia,“ MB naye alisisitiza.



    “Basi, sawa, nitawapigia, lakini nawaombeni jamani mnisaidie....aah, kwa namna yoyote ile maana maisha yangu naona yanavurugika,“ Mkurugenzi Swadif alisema huku akiwa na dalili za wazi za kububujikwa na machozi.



    Zoezi la kuwapata wale wote waliokuwa kwenye orodha ya ule mgao wa hongo lilikamilika vizuri, na ilikuwa ni aibu kubwa kwa wahusika. Kilichofanyika ni kwamba baada ya kuwapigia simu wahusika wote na akaongea nao, Mkurugenzi Swadif aliachwa peke yake pale kwenye sebule ya chumba alichofikia Mkuu wa BUNDI, Momaa Bulo a.k.a. MB. Mkuu huyo pamoja na Mkuu wa kikosi cha SIAFU, Kessi Kussy wakahamia chumba cha kulala, akiwemo pia BeBe na yule afisa mwingine wa SIAFU.



    Mkurugenzi Swadif alipewa maelekezo ya jinsi ya kuwapigia simu wale wote waliokuwa kwenye orodha ya mgao na awaombe wafike pale Hoteli ya Ufukoni wakachukue mgao wao.



    “Wakishafika wote, utampa kila mmoja moja kati ya hizo bahasha tulizokupa ambazo juu zimeandikwa majina yao na zinapesa tulizozitia alama zetu. Wote wakishapokea bahasha zao utaagana nao. Yatakayofuatia tuachie sisi,“ Mkuu wa SIAFU, KK alimpa maelekezo Mkurugenzi Swadif.



    “Sawa, nimekuelewa,“ Mkurugenzi Swadif alisema.



    “Tafadhali hakikisha sauti yako na yote utakayoyatenda yaonekane upo katika hali ya kawaida ili usiwashitue. Kumbuka, kufanikiwa kwa zoezi hili ndiko kutakokusaidia katika jambo hili,“ Mkuu wa BUNDI, MB alimfahamisha.



    “Nafahamu, nitajitahidi,“ Mkurugenzi Swadif alisema.



    Mtu wa kwanza kupigiwa simu na Mkurugenzi Swadif alikuwa ni Kaimu Kamanda wa kitengo cha Wanamaji cha SIAFU, Gamati Saamur, ambaye kwenye ile orodha ya mgao wa hongo alikuwa nambari mbili. Mkurugenzi Swadif alifanya mawasiliano hayo akitumia simu yake ya mkononi. Mazungumzo yalikuwa hivi:



    “Bwana Saamur, Assalaam Alleikum.“

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ohoo, wa-Alleikum Salaam Mkurugenzi, umzima?“



    “Naam, ni mzima wa afya, sijui weye?“



    “Mie sijambo, vipi mbona sauti yako inaonyesha kupooza, umzima kweli weye?“



    “Hapan-shaka. Je twaweza kuonana mara moja hapa Hoteli ya Ufukoni, nina mzigo wako.“



    “Kuonana tunaweza kuonana, lakini vije upo huko hotelini?“



    “Aah, hiyo isikupe taabu, nipo pamoja na mgeni wetu, nipo pia pamoja na jamaa zetu. Tutakuwa na maongezi kidogo.“



    “Basi shwari, Mkurugenzi, ni njiani naja.“



    Mazungumzo na wengine yalikuwa katika mtiririko kama huo, na wote waliitikia mwito baada ya kupata maelezo kama hayo Mkurugenzi Swadif aliyompa Bwana Saamur. Waliofuatia walikuwa ni Mwenyekiti Mtendaji wa bodi ya BIKANGA, Bwana Mwinyikusi Saadini na Kamanda wa Kitengo cha Uchunguzi cha Jeshi la Polisi, Bwana Pesha Kalima. Kidogo kulikuwa na mabishano na Katibu Mwandamizi wa Wizara ya Mazao ya Biashara, Dk. Hinga Patani, ambaye kitendo cha kuitwa hotelini hakukiafiki.



    “Kwa nini usiniletee huo mzigo ofisini kwangu kama ilivyo kawaida?“



    “Nakuelewa Katibu lakini mazungumzo na huyu mgeni wetu ni mazito na yenye mwelekeo mzuri, na tumeona ingekuwa vyema tusifanyie ofisini. Wajua tena mambo ya maofisi yalivyo.“



    “Huo ni wasiwasi usiokuwa na msingi, hapa ofisini kwangu kuna faragha ya kutosha.“



    “Naelewa Katibu, lakini kwa hili la leo naomba utuwie radhi, hatutakuwa na muda mrefu.“



    “Ok, nipeni kama dakika kumi hivi, lakini hakikisheni hatuchukui muda mrefu, nina majukumu mengine.“



    “Sawa Katibu.“



    Baada ya kama nusu saa hivi, wote waliopigiwa simu na Mkurugenzi Swadif walikuwa wamefika pale hoteli ya Ufukoni. Walipokuwa wamekusanyika sebuleni mwa chumba #26 na mwenyeji wao, maongezi yakawa:



    “Samahani, nimekuiteni hapa hotelini na kuwakatizia shughuli zenu. Imenilazimu kufanya hivyo kwa vile kuna mzigo wenu unaotokana na yale ambayo tulishayazungumza wiki kama mbili hivi zilizopita. Na bila kupoteza zaidi muda, naomba niwakabidhi kila mmoja fungu lake,“ Mkurugenzi Swadif aliwaeleza.



    “Sawa Mkurugenzi, lakini mbona safari hii utaratibu umebadilika? Wajuwa kutukusanya sote mahala kama hapa kunaweza kuzua maswali kwa baadhi ya watu?“ Huyo alikuwa ni Katibu Mwandamizi wa Wizara ya Mazao na Biashara, Dk. Hinga Patani.



    “Nakubaliana nawe Dakta, lakini imebidi kuwe na mabadiliko haya kwa vile baada ya kupata kile kilichopo tutakuwa na maongezi kidogo na wale jamaa zetu,“ Mkurugenzi Swadif alisema.



    “Wako wapi hao jamaa, mbona uko peke yako?“ Hilo liliulizwa na Kamanda wa Kitengo cha Uchunguzi cha Jeshi la Polisi, Bwana Pesha Kalima.



    “Wapo, tukimaliza hili zoezi nitawaita,“ Mkurugenzi Swadif alijibu.



    “Sawa, kamilisha ulilotuitia, muda unakwenda,“ Katibu Mwandamizi wa Wizara ya Mazao na Biashara, Dk Hinga alisema, huku sauti yake ikionyesha wazi kuwa bado alikuwa amekerwa na kitendo cha kuitwa pale hotelini.



    Wakati Mkurugenzi Swadif akizichambua bahasha zilizokuwa na mgao, alipata swali kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya BIKANGA, Bwana Mwinyikusi Saadini.



    “Subiri kwanza, je mgao ukoje, ni kama tulivyokuagiza kuwa safari hii waongeze kiwango?“



    “Ndiyo, wameongeza. Badala ya dola elfu nne zile za mgao uliopita, mgao huu wameongeza hadi kufikia dola elfu tano,“ Mkurugenzi Swadif alijibu.



    Wengine wote pale ndani walitikisa vichwa kwa namna ya kuridhika na jibu hilo, ndipo Mkurugenzi Swadif akagawa zile bahasha kila mmoja kwa jina lake. Walipoangalia kilichokuwamo ndani ya bahasha na kuridhika na walichokiona kila mmoja aliweka bahasha yake kwenye mfuko ama wa suruali au wa koti lake.



    Jambo ambalo hawakulifahamu kwa wakati ule ni kwamba mazungumzo yao yote si tu yalikuwa yakisikilizwa na wakuu wa SAIFU na BUNDI, pamoja na maofisa wengine waliokuwa chumba kingine, bali pia kinasa sauti kilikuwa kikiyarekodi. Pamoja na MB, KK na BeBe walikuwepo pia maafisa kutoka Taasisi ya Kupambana na Rushwa Zanzibar (TAKURUZA), ambao waliitwa mahsusi kwenda kuwatia mbaroni wale waliopokea hongo ile.



    Basi kule chumbani walipohakikisha wale mabwana kila mmoja kapokea bahasha yake, walitoka kwa mlango mwingine na wakaingia chumba walichokuwamo Mkurugenzi Swadif na wenzie.



    “Tulieni hapo hapo mlipo, mpo chini ya ulinzi.“ Hiyo ilikuwa ni sauti ya Bwana Hingu Naima, ambaye alikuwa Mkuu wa TAKURUZA.



    Ama kwa hakika hali pale ndani ilikuwa ya kushtusha mno, na ilikuwa ni aibu kubwa kwa wale viongozi wa kutoka Wizarani, SIAFU na BIKANGA. Hakukuwa na utetezi wa aina yoyote, bali wale waliopokea mgao walimtupia macho ya lawama Mkurugenzi Swadif, bila shaka wakimlaumu kwa kuwachoma. Hata hivyo, walikuja kujua baadaye kuwa wote, pamoja naye, walikuwa ndani ya kikaango kimoja kilichokuwa kikitokota maji ya moto.

    Basi shughuli ikawa imehamia kwa maafisa wa TAKURUZA ambao walithibitisha kuwa kila mmoja wa wale watuhumiwa alikuwa na ile bahasha ambayo ilikuwa kithibiti kuwa walipokea rushwa. Palepale wote wanne walifungwa pingu za mikononi na kisha wakaondoka na maafisa wa TAKURUZA. Pale ndani walibaki MB, KK, na Mkurugenzi Swadif.









    13 - Mbaroni



    Ingawa kitendo cha kuwatia mbaroni wale maafisa wanne kilikuwa cha mafanikio makubwa, bado hali ilibakia tete. Suala kwamba Pei bado alikuwa mikononi mwa wale waendesha magendo halikuwa zuri na ilibidi kuwekwa mikakati ya kwenda kumwokoa na pia kuwatia mbaroni wale waliomteka.



    “A5, nakupongeza kwa kazi nzuri hadi hapa tulipofikia, lakini bado ipo kazi kubwa zaidi mbele yetu,“ huyo alikuwa KK.



    “Nashukuru Mkuu, nami pia bado sijaridhika hadi tujue Pei ana hali gani huko aliko, na ndio maana nikaomba huyu Mkurugenzi Swadif tubaki naye,“ BeBe alijibu.



    “Mnhuu, A5, nadhani nafahamu ni kwa nini umetaka tubaki naye, lakini hebu eleza mwenyewe fikra zako.“ MB alimuuliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mkuu, nimeona tuwe naye kwa muda kwa vile yeye anayo mengi ya kutueleza kuhusu huko aliko Pei, kwani naamini kwa ukaribu alionao na hawa jamaa, kwa vyovyote atakuwa ameshafika kule waliko kisiwani Chumbe,“ BeBe alijibu.



    “Upo sahihi kabisa A5, fikra zako zimelingana na nilichokuwa nikikifikiria, huyu ndugu kwa vyovyote atakuwa anafahamu ni wapi wamekwenda kisiwani Chumbe,“ MB alisema.



    “Ndiyo Mkuu, na si hivyo tu, kwa vile ameshafika huko, basi atatueleza hali ya mazingira ya huko yalivyo, ikiwa ni pamoja na ulinzi uliopo. Hii ni muhimu kwetu kwa ajili ya kupanga vyema mashambulizi,“ BeBe alisema.



    “Sawa kabisa A5, nami pia nilipata wazo kwamba huyu bwana anaweza kutupa taarifa zaidi kuhusu hawa jamaa zake waendesha magendo. Ndugu Swadif, umeelewa tunachohitaji kukifahamu?“ KK alimuuliza.



    Kwanza Mkurugenzi Swadif alisita, akawa kama asiyetaka kujibu, lakini bila shaka alihisi kuwa hakuwa na pakukwepea, ikabidi aseme ukweli.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog