Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

MACHO YA BUNDI - 4

 





    Simulizi : Macho Ya Bundi

    Sehemu Ya Nne (4)



    Nakuambia simuachi mwanangu ng’o, mwanamke wako asiyezaa asije kumuua mjukuu wangu.”

    “Unasemaje?” nilisema nikamvamia na kumkaba koo akawa anahema kwa shida. Mume wangu alijitahidi kutuachanisha lakini mikono yangu ilikuwa kama ina sumaku.

    Baadaye nilihisi kwamba naweza kuua hivyo nilimuachia na Mei akaanguka chini huku akiwa ametokwa na macho kama vile ameaga dunia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilijifanya kama vile sijali lakini akili yangu ilikuwa haijatulia. Nilidhani nimeshaua. Nilirudi nyuma na kujiuliza kimoyomoyo je nikimbie au nifanye nini.

    Wakati nawaza nini cha kufanya, Mei alipepesa macho nikajua kuwa hajafa. Mume wangu alikimbilia jikoni na kuchukua maji katika ndoo, alimwagia na akapata nguvu ya kukaa.

    Alikuwa akiniangalia bila kusema chochote. Baadaye alipata nguvu na kuketi kwenye kiti cha plastiki kwa kuwa nguo zake zilikuwa zimelowa aliona siyo vema kukaa kwenye kochi.

    “Naomba gari haraka sana nitoke katika nyumba hii,” alisema huku akimuangalia mume wangu.

    Haikuchukua muda mlinzi aliyekuwa ameagizwa kutafuta gari akawa amefika na gari dogo ambalo halikuwa la kukodishwa lilikuwa ni la mtu binafsi.

    “Mzee nimelikuta gari hili tu pale stendi ya taksi. Sikupatana naye bei.”

    Nilimuona mume wangu akienda kuzungumza na yule dereva wa lile gari kisha akachukua masanduku ya nguo za Mei na kuyapakia kwenye gari hilo.

    Sikuwa na wasiwasi kwamba sasa anaondoka kwa kuwa nilimuonjesha kidogo ukali wangu na naamini aliamini kwamba sasa hapa nyumbani kwangu hapakaliki.

    Niliona kama wanachelewa na mimi niliinuka na kuchukua kapu la viatu na kwenda kulitupa ndani ya gari lile.

    Mume wangu hakutaka kumruhusu Pili aondoke na mtoto wake mchanga, aliwasihi abaki ili amlee hapa nyumbani, lakini mama yake alikataa katakata akidai kuwa naweza kuwadhuru.

    “Unamtaka huyu mtoto au humtaki?”

    “Namtaka.”

    “Sasa kama unamtaka kwa nini hutaki kuniruhusu kuondoka naye.”

    “Mimi nina imani kuwa atalelewa vyema na mama yake pamoja na huyu mke wangu mkubwa.”

    “Kama alitaka kuniua dakika chache zilizopita una uhakika gani kuwa atakaa vizuri na mwanangu Pili na mjukuu wangu?”

    “Amesema mara kwa mara kuwa mwenye matatizo ni wewe na siyo Pili ndiyo maana nakuomba muache mwanao akae hapa isitoshe ni mke wangu sasa.”

    “Sawa ni mke wako, lakini kama kuna mtu ambaye mimi na hata yeye hana imani naye tutafanyaje?”

    “Mama mimi nipo chini ya miguu yako nakuomba muache hapa nyumbani ondoka wewe tu.”

    Mei hakukubaliana na mume wangu na akaamua kuondoka na mwanaye pamoja na mjukuu wake.

    Tulibaki mimi na mume wangu tunaangaliana. Hakuna aliyesema neno kwa takribani dakika tano baada ya watu wale kuondoka.

    Nilikuwa mimi ndiye kwa kwanza kumuuliza mume wangu sababu za kung’ang’ania Pili abaki.

    “Mimi sioni kama kuna tatizo kati yako na Pili, mwenye matatizo ni Mei.”

    “Lakini haya yote umejitakia mume wangu. Wewe ndiwe chanzo cha haya yote.”

    “Mke wangu huko tulishavuka, tukaelewana tusirudi nyuma tena, tujadili hili lililopo mbele yetu.”

    Nilimuangalia mume wangu huku nikitokwa na machozi. Nilijaribu kusema jambo lakini ulimi ulikuwa mzito.



    MUME wangu aliamua kujilaza kwenye kochi kisha kunitaka niwe karibu naye ili aniambie jambo. Nilipomsogelea alisema nisijali kwani maneno ya yule mwanamke, yaani Mei yasinitie wazimu.

    “Kwa nini amenidhalilisha?”

    “Yule Mei japokuwa ni mkwe wangu sitataka akanyage hapa tena.”

    “Unasema kweli?” nilimuuliza mume wangu.

    “Nakuapia. Hakanyagi hapa. Ninachowaza ni mtoto wangu tu maana bado ni mdogo na najua hana uwezo wa kumtunza.”

    “Nikuambie jambo?”

    “Sema.”

    “Yule amefanya hivyo kwa kuwa anataka mtoto wako amfanye mtaji, yaani apate matumizi ya kila siku kupitia mwanao…”

    “Thubutu, hapati kitu hapa!”

    Mara tulisikia breki ya gari ambalo lilisimama nje ya nyumba yetu. Nilichungulia na kumuona Mei akitoka huku uso ukiwa umevimba.

    Aliingia ndani bila kubisha hodi.

    “Nimegeuza gari. Njiani nimemuuliza Pili kama umetoa fedha za matumizi ya mtoto akasema hujatoa, nikamuamuru dereva ageuze gari.”

    Tuliangaliana mimi na mume wangu kwa kuwa hayo tulikuwa tukiyazungumza dakika kama mbili zilizopita. Mume wangu aliinuka na kukaa kwenye kochi huku akiwa amekunja uso, aliniangalia nami nikakunja uso.

    “Lakini Mei kwani wewe ni mke wangu? Hayo mambo angefanya Pili siyo wewe.”

    “Mimi nahusika mia kwa mia, kwani Pili anakwenda kukaa kwa nani?”

    “Pili kwenda kukaa kwako ni wewe umejitakia, kwani mimi nimeshindwa kumlea?”

    “Kwa maana hiyo unataka kuniambai hutoi?”

    “Kwako Mei sitoi hata senti tano. Hapa umemchukua Pili kwa nguvu hata muda wa kumpa hizo fedha ingekuwa saa ngapi”

    “Kwani kutoa fedha kunahitaji winji, kalete hizo fedha tuondoke zetu.”

    “Nakuambia nenda kwenye gari na ukabaki na mtoto kisha mtume Pili aje hapa nimuelekeze cha kufanya.”

    “Yaani unaniamuru kwamba niende nikamchukue mtoto ina maana unanigeuza mimi ni yaya siyo?”

    “Hapana.”

    “Sasa kwa nini unasema niende kwenye gari nikampakate mtoto, unanivunjia heshima Bwana Chinchi kuwa umemzalisha mwanangu?”

    “Huyo ni mke wangu, wewe ulitaka nizae na nani?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Na huyo mkeo wa kwanza.”

    Baada ya kusema hivyo alinitibua nikasimama na kutaka kumuendea pale alipokuwa amesimama lakini Chinchi mume wangu akanizuia.

    “Hebu niache, nikamfundishe adabu huyu pimbi.”

    “Nani pimbi.”

    “Wewe pimbi, sasa hivi umeponea tundu la sindano na umerudia tena kosa lilelile, sasa nakuua kabisa.”

    Wakati nasema hivyo Pili aliingia ndani huku akiwa na mtoto wake.

    “Mama, sasa hivi ulikuwa umezimia na unarudia tena kutaka kugombana na mama mkubwa, unafanya vibaya mama.”

    “Sifanyi vibaya, mimi napigania haki zako, huoni kwamba huyu bwana anataka kukutesa?”

    “Hapana mama, mambo yangu na huyu bwana tuachie wenyewe tutayamaliza.”

    “Acha kunifundisha cha kufanya, kosa mimi unadhani huyu bwana angekuoa, si angeendelea kukaa na huyu mwanamke tasa hapa ambaye anajaza choo tu!”

    Maneno hayo yalinifanya nitoke jikoni huku nikiwa nimeshika panga, hasira zilikuwa zimenikaa barabara kichwani. Haraka kama umeme mume wangu alinishika huku akipiga yowe:

    “Salome utaua, utaua mke wangu…”





    Mume wangu alikuwa na nguvu kuliko mimi, alishika panga na kuninyang'anya lakini wakati huo Mei alikuwa ametimka na kuwa nje ya nyumba yetu lakini alikuwa bado anabwabwaja maneno.

    "Unataka kunichinja kwa kuona nafaidi siyo, huwezi kuniua mimi wewe kwa sababu ya kupigania haki ya mwanangu. Huniwezi kwa lolote," alisema Mei.

    Pili baada ya kuona vurugu hiyo alitoka nje na kumsihi mama yake waondoke kwa ahadi kwamba kesho yake angefika na kuonana na mume wetu.

    Binafsi nilimuona Pili ana adabu na anastahili kuwa mke wa pili kwa mume wangu.

    Ni kweli kwamba sijazaa na mume wangu licha ya kuishi naye miaka minne sasa na Mei ambaye nilimshirikisha tangu wakati wa uchumba tulipokuwa tunakutana na Chinchi Masasi Hoteli anajua.

    Mawazo yalinijia na kujiuliza sababu za Mei kutaka kuvunja ndoa yetu wakati nimekubali mtoto wake Pili aolewe na mume wangu.

    ***

    Ni miezi miwili sasa tangu tuwatimue Pili na mama yake Mei. Nilimshauri mume wangu kwamba ampangishie nyumba badala ya kwenda kwa Mei na akafanya hivyo.

    Siku moja nilikuwa na hamu ya kwenda kumuona mtoto na nilinunua nguo kadhaa kama zawadi za kichanga.

    Tulikwenda na mume wangu nyumbani kwa Pili na kumkuta akicheza na mwanaye maana tukiwa nje tulisikia akimbembeleza kwa nyimbo za kwao za Kimakua.

    "Kinomvelhelha mwana wa numwane (namsindikiza mtoto kwa mama yake), mwanalolha nounlha, mwanalolha noulha mwana noulha, chiichii unanchia (mtoto huyu analia, mtoto huyu analia, chichiii kwanjiwa)".

    Ndiyo wimbo aliokuwa akiimba Pili pale sebuleni. Tulikuta kuna viatu nje ya nyumba nikahisi inawezekana mama yake alifika pale.

    Tulibisha hodi na kukaribishwa. Tulipoingia tukakuta kumbe aliyekuwa akiimba wimbo ule ni Mei na wala siyo Pili.

    "Karibuni, karibuni," alisema Pili.

    Tulisalimiana wote na kwa mara ya kwanza Mei alionekana kuchangamka, aliacha kabisa makeke yake ya siku zote.

    Nilitoa zawadi zangu kwa mtoto na Pili alizifurahia japokuwa mama yake hakuwa na furaha sana.

    Nilizikunjua nguo zote ambazo zilikuwa kwenye kisanduku kidogo na kumpa Pili. Mei hakuchangamka kabisa, hali iliyonishangaza.

    Baada ya mazungumzo mafupi tuliaga bila kula chochote kutokana na kumhofia Mei ambaye alijifanya yupo bize jikoni.

    Tuliingia kwenye gari na kutoweka nyumbani kwa Pili, ajabu ni kwamba mara tu baada ya kufika nyumbani bundi alipita karibu na uso wangu, akatua katika dirisha la chumba chetu cha kulala macho yake yalikuwa yaking'aa, ghafla nikaanza kutapika.

    "Nini tena Salome, una malaria?" aliuliza mume wangu.

    Sikumjibu na hali ilizidi kuwa mbaya. Mume wangu akaamua kunikimbizia hospitali baada ya kuniona nanyong'onyea na kuishiwa nguvu kutokana na kutapika sana.



    Tulipofika hospitali haraka sana niliingizwa kwenye chumba cha daktari akaamua nifanyiwe vipimo.

    Nilienda maabara ambapo nilipimwa damu kuchunguza malaria na kuona kama sukari ipo sawasawa mwilini.

    Nilichukuliwa damu nyingine kwa ajili ya kupimwa kama nina taifodi.



    Baadaye karatasi za vipimo zilipelekwa kwa daktari ambaye aliniita chumbani kwake ili kunisomea majibu, mume wangu Chinchi nilimuacha akiwa amekaa kwenye benchi.



    "Mama matokeo ya vipimo yanaonesha huna ugonjwa wowote," alisema daktari huku akigeuzageuza ile karatasi aliyopewa na kuniangalia.

    "Sasa kama sina ugonjwa wowote kwa nini natapika sana?"

    "Kwani katika mwili wako unajisikia kuumwa chochote licha ya kutapika?"

    "Hapana."CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Sasa vipimo vinaonesha huna ugonjwa mama."

    "Ushauri wako ni nini sasa kama mtaalamu?"

    "Yule aliyekuleta ni nani wako?"

    "Ni mume wangu."

    "Unaonaje tukimuita ili nikueleze tulichogundua?"

    "Umegundua nini wakati umesema sina ugonjwa?"

    "Huna ugonjwa lakini una jambo zito?"

    "Zito? Nini tena, niambie mimi si ndiye mgonjwa?"



    Moyo wangu ulienda mbio na kujiuliza hawa jamaa wamegundua kuwa nina ngoma? Sasa kama nina ngoma kwa nini wanataka kumuambia mume wangu badala ya kunijulisha mimi kwanza?



    Maswali hayo nilijiuliza moyoni huku nikumuangalia daktari aliyekuwa akitabasamu.



    "Usitabasamu daktari, niambie kama nimeathirika nijue. Sasa unataka kumuambia mume wangu bila mimi kujua kwanza kwa nini? Huwa mnasema kabla ya mtu kuambiwa kuwa ana ngoma, anapewa ushauri nasaha, sasa mbona hufanyi hivyo?"



    "Sikiliza Salome. Nimekuambia huna ugonjwa wowote lakini wewe unakazania kwamba labda una ngoma, sasa kama ungekuwa na tatizo hilo kwa nini nishindwe kukuambia wakati maadili ya kazi yanasema hivyo?"



    "Nashangaa, swali hilo jiulize wewe."



    Wakati nikitafakari la kufanya daktari huyo alishika kiwiko cha simu yake ya mezani na akampigia nesi.

    "Nesi huyo mzee aliyekuja na huyu mama mwambie aingie ndani," sikusikia upande wa pili alijibu nini.

    "Ndiyo ni huyo aliyekaa kwenye benchi ana ufunguo wa gari mkononi."

    Sekunde chache baadaye mume wangu aliingia katika chumba cha daktari na kunikuta nikiwa natokwa na jasho.

    "Amezidiwa, niambie daktari amezidiwa?" alisema mume wangu huku akionesha wasiwasi mkubwa.

    "Hapana, nimekuita kuna jambo tumegundua."

    "Jambo gani tena daktari!"

    "Huyu ni mkeo?"

    "Ndiyo."

    "Napenda kukuarifu kwamba, hana ugonjwa wowote unaomsumbua isipokuwa

    "Isipokuwa nini,kwa nini anatapika mfululizo?"

    "Mzee wangu ungesubiri basi nimalize kutoa maelezo."

    "Sawa. Nakusikiliza."



    "Mzee tulia nikupe habari."

    "Haya sema sasa."

    "Mzee kwani mlikuwa na mpango wa kupata mtoto hivi karibuni?"

    "Unasemaje?"

    "Hukusikia?"

    "Rudia!"

    "Nimekuuliza mlikuwa na mpango wa kupata mtoto hivi karibuni?"

    "Kwa nini unaniuliza hilo swali?"

    "Jibu kwanza swali huwezi kupandanisha maswali."

    "Nijibu kwa nini unaniuliza hivyo?"

    "Mkeo ni mjamzito!"

    "Siamini!!"

    "Mkeo ni mjamzito ndiyo maana anatapika. Haumwi chochote."

    "Salome, Salome, nakupenda sana."

    Alinikumbatia tukiwa tumesimama wima. Nilishindwa kuvumilia, nilitokwa na machozi na kuanza kulia kwa kwikwi. Mume wangu naye alibubujikwa machozi hali iliyomfanya daktari kushangaa.

    "Jamani, kwa nini mnalia?"

    "Ni hadithi ndefu sana, hatuamini hiki unachotuambia," alisema mume wangu na kuanza kumsimulia mkasa wote uliotaka kusambaratisha ndoa yetu.

    "Basi Mungu alisikia kilio chenu, mama una ujauzito na kwa kuwa una miaka thelathini na tatu itakubidi uwe karibu sana na hospitali ili upate uangalizi wa karibu wa madaktari. Unajua ukipata ujauzito ukiwa na umri kama wako kunahitajika uangalizi wa karibu."

    "Daktari wangu atakuwa wewe," nilisema huku machozi yakiendelea kulowanisha mashavu yangu.

    Tulitoka ndani ya hospitali hiyo tukiwa na furaha kubwa sana. Hakika tulijiona kama vile tumefunga ndoa leo.

    Tulipofika nyumbani kijana wetu wa kazi alitushangaa kwani mara tu baada ya kushuka kwenye gari tulikumbatiana na kuingia ndani.

    Nilipoingia, nilikwenda moja kwa moja kuchukua shampeni isiyo na kilevi na kuifungua. Nilimmwagia yote mume wangu, naye akaenda kuchukua yake akafanya kama nilivyofanya mimi.

    Nilifungulia muziki sauti ya juu tukawa tunacheza na mume wangu. Tulikatizwa na Mei aliyefika ghafla na kugonga mlango.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nini tena? Mei nilikuambia usije tena hapa?" alifoka mume wangu.

    "Nimekuja kukuarifu kuwa mwanao mgonjwa."

    "Kwa nini Pili asinipigie simu na ukaamua kuja wewe?"

    "Hakupiga kwa sababu naye analia baada ya kuona mtoto kazidiwa."

    Mume wangu aliingiza mkono mfukoni na kumpa shilingi elfu arobaini.

    "Nenda mpelekeni hospitali na kama atakuwa na tatizo lingine, Pili anipigie simu, tafadhali sana sitaki uje hapa nyumbani. Nasema sitaki."

    Mei hakujibu chochote, alinyakua zile fedha, akatoka nje na kuingia kwenye gari lililomleta, akatoweka.

    Mei baada ya kupewa fedha alikwenda moja kwa moja kunywa bia jirani na nyumba waliyopangishiwa na mume wangu.

    Tulijua hayo baada ya kumshauri mume wangu apige simu kwa Pili kujua hali ya mtoto.

    "Mama alikuja huko? Mbona amerudi sasa hivi na amesema anakwenda kutuliza mawazo kwa kupata bia mbili tatu, alikuja kufanya nini?"

    "Kwani mwanao haumwi?"

    "Haumwi. Mzima nacheza naye hapa."

    "Mjinga sana mama yako."



    "Vipi ujinga wake ni upi?"

    "Kaja hapa akasema eti mtoto mgonjwa na ana hali mbaya."

    "Mama kasema hayo?"

    "Ndivyo alivyoniambia na nimempa shilingi elfu arobaini baada ya Salome kunishauri."

    "Jamani mama ananishangaza sana, alikuwa na shida ya fedha za kunywea akaona aje kukudanganya."

    Mume wangu alikata simu.

    Tuliamua siku hiyo kwenda kula chakula cha jioni katika hoteli moja inayoitwa Kem, ni hoteli ya kisasa ambayo hata mwanamuziki Diamond aliwahi kuja kufanya vitu vyake.

    ***

    Miezi ya kujifungua ilifika na siku hiyo nakumbuka ilikuwa saa tisa usiku niliposikia maumivu makali sana ya tumbo.

    Nilimwamsha mume wangu na kumpa taarifa ya kuugua kwangu.

    "Kama ni hivyo ni vyema tuwahi hospitali."

    "Sawa."

    Nakumbuka wakati tunahudhuria kliniki tuliambiwa tuandae pamba, glovu, wembe, kanga na zagazaga nyingine ambazo manesi walisema zitatusaidia siku ya kujifungua.

    Nilimuambia mume wangu Chinchi achukue begi langu ambalo lilikuwa na vifaa hivyo na haraka sana akavikimbiza na kuviweka kwenye gari.

    Nilijikokota kutoka nje ya nyumba yetu kwenda pale lilipokuwa gari, niliona kama vile lipo maili mbili kwa jinsi nilivyokuwa nasikia maumivu.

    "Ngoja nikusaidie," alisema mume wangu huku akinishika mkono.

    Ghafla tukiwa tunatoka nje ya nyumba, yule bundi ambaye huwa tunamuona mara kwa mara aliruka na kusimama kwenye dirisha letu.

    "Mume wangu unamuona yule bundi anatuangalia?"

    "Achananaye huyo na wala usimfikirie!"

    "Nisimfikirie kwa nini wakati huwa anatoka na kusimama katika dirisha letu?"

    "Nimekuambia achananaye, mara ngapi tunamuona na hakuna chochote kinachotupata? Mungu mkubwa."

    "Sawa lakini ni lazima tupitie kwa Padri Kalo akatuombee."

    Alinikokota hadi kwenye gari na yeye kuliwasha. Tulikwenda moja kwa moja hadi kwa Padri Kalo ambaye alishangazwa sana kusikia tunamgongea usiku ule.

    "Mzee Chinchi kwani kuna nini usiku wote huu?" alihoji Padri Kalo.

    "Tafadhali sana toka nje, tuna dharura."

    Padri Kalo alitoka huku akiwa kavaa kanzu akaambiwa na mume wangu kuwa tumepitia tu kwake tunahitaji maombi.

    "Mke wangu hajisikii vizuri, naomba umfanyie maombi kabla ya kwenda hospitali."

    Alianza maombi yake: "Mungu tunakuomba malaika wako wamlinde mama huyu na wabaya wote waliomzunguka. Nakuomba uwe karibu naye wakati wote akiwa hospitali ambako anakwenda kujifungua ili ajifungue salama na aijaze dunia kama wewe mwenyewe ulivyoamuru enzi ya babu yetu Adamu na bibi Hawa. Tunaomba haya tukikutanguliza wewe Mungu. Amin."

    Tuliondoka kwa padri kwa mwendo wa kasi huku tumbo likiniuma sana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog