Search This Blog

Sunday 19 June 2022

KISU CHENYE MPINI MWEKUNDU - 1

 





    IMEANDIKWA NA : AHMED MUSSA MNIACHI





    *********************************************************************************



    Simulizi : Kisu Chenye Mpini Mwekundu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



     kipupwe kiliufanya mji wa Dar es salaam uchangamke zaidi. Hali hii iliwakera wauza soda na maji baridi. Waliofurahia ni wenye Vilabu vya pombe na nyumba za kulala wageni ambazo si rasmi maarufu kama ‘Gesti bubu’. Hali ya hewa ilikuwa ni baridi ya wastani ambayo iliwavutia wengi. Hali hii ya baridi iliwafanya wanywaji wengi kuongeza kipimo cha ulevi. Miongoni mwa mitaa maarufu ambayo ilifurika watu katika kipindi hiki ni Buguruni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Karibu kabisa na soko kubwa la Buguruni kuna baa maarufu inayoitwa Sewa.Umaarufu wa baa hiyo unatokana na biashara maarufu ya mwili ambayo hufanywa na makahaba ambao hujulikana zaidi kama dada poa.

    Kulikuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu wa rika tofauti isipokuwa watoto. Wachache walifika hapo ili kupata kinywaji tu. Wengine walifika hapo kupata huduma za makahaba ambao hulifanya eneo hilo kuwa maarufu na lenye mvuto wa kipekee ukilinganisha na maeneo mengine ya Buguruni.

    Eneo hili lina makahaba wengi ambao hujiuza kwa bei nafuu. Wapo watu wenye ndoa zao ambao ni wateja wazuri wa biashara hii ya ukahaba, hivyo kulifanya eneo hili kuwa na msisimko mkubwa. Ni eneo la ajabu kwa sababu wateja wake wengi ni wale ambao hulilaani na kuliona halifai mchana, wanapokuwa kwenye vijiwe vya kahawa au wanapochangia hoja zinazoibuka kwenye daladala lakini kumbe ni wateja wazuri linapoingia giza.

    Watu wengi walikuwa wamekaa kwenye Baa hii wakiwa na malengo yanayofanana, kama si kujiuza basi ni kununua. Wanaume wengi walikuwa wamekaa kwenye viti huku wakichagua huyu na yule katika namna ambayo usingeweza kugundua. .....Jinsi walivyowaita wanawake wale ilikuwa ni sanaa nyingine aina yake. Wapo waliomwita waliyemtaka kwa ishara ya kukonyeza, wapo waliojifanya kwenda nje kisha kumgusa waliyemhitaji kwa namna ambayo hakuna ambaye angeweza kugundua zaidi ya yule aliyeguswa, pia walikuwepo wale ambao waliweza kuwakabili wale makahaba katika staili ambayo wengi iliwashinda, hawa ni wale ambao kama aibu inatokana na mishipa fulani wao ilikuwa imekatwa au haipo kabisa pia kuna ambao waliwasubiri eneo ambalo walihisi mwanga wa taa usingewaadhiri, hawa walivizia maeneo yenye giza kabla ya kuanza chombezo zao.

    Walitumia njia ya kuongea nao moja kwa moja huku wakiomba wapunguziwe bei tena kwa sauti ambayo hata mtu aliyeko pembeni angeisikia.

    “Hili ndio tatizo lenu, kikifika kipindi cha baridi au mvua basi mnatupandishia bei.” Alilalamika mmoja wa watu hao baada ya kuona bei imeongezeka kidogo muda huu wa baridi.

    Ghafla, akaingia mwanamke ambaye kwa dakika kadhaa aliteka hisia za wengi. Alikuwa ni mwanamke mrefu mwenye sura nzuri ambayo ilipambwa vema na wanja na vipodozi vingine.



    Alivaa gauni fupi la kijani ambalo liliruhusu nusu ya mapaja yake kuwa nje. Alikuwa na miguu iliyojaa vizuri na kuwafanya wanaume kadhaa wameze mate kama mtu anayeona ndimu ikiliwa mbele yake. Rangi yake ilikuwa ni maji ya kunde ingawa sehemu ya mapaja ilikuwa nyeupe kadri ulivyokuwa unaelekea kule lilikoishia gauni. Viatu vyake vyeusi vya mchuchumio viliendana vema na gauni lile ambalo nafasi iliyotakiwa kuwa na mikono mirefu au mifupi ilikuwa imepita mikanda ambayo ililishikilia vema gauni lile. Sehemu ya kifuani iliruhusu robo ya matiti ambayo yalijaa vema kuwa nje. Ili mradi kila mwanaume mle ndani alichagua sehemu iliyomvutia na kukazia macho. Wapo waliokodolea macho kifua, wapo waliovutiwa na miguu, wapo..wapo… walikuwepo tu, kwani wanakosa?



    Alitembea taratibu huku akisindikizwa na macho ya wanaume wenye uchu wa fisi. Kwa mshangao wa wengi akachagua meza iliyokuwa tupu. Kwa mtu aliyemtazama vema mwanamke huyu angegundua dosari moja tu. Hakuwa na furaha. Alionekana kutatizwa na jambo, jambo hilo lilimfanya awe na mawazo mengi kiasi cha kutotamani mteja kwa siku hiyo. Akiwa na uzoefu wa miaka saba kwenye kazi ya ukahaba kwa mara ya kwanza alijikuta akikataa wateja jambo ambalo liliwavutia zaidi wateja na kuwafanya wapandishe dau. Haikuwa rahisi kumnasa kwa siku hiyo. Mmoja wa ‘machangudoa’ wenzake ambaye kiumri alionekana kuwa ni mdogo kwake hakuivumilia hali hiyo, akaingiwa na mashaka. Huyu alionyesha kuwa na ukaribu zaidi ya ule wa kuwa wote nimakahaba.

    “Vipi dada Vero unaumwa leo?” Aliuliza yule binti.

    “Hapana mdogo wangu nimechoka, nimechoka kujiuza.” Aliongea waziwazi na kumfanya yule msichana abaki mdomo wazi kana kwamba ni kitu cha mwisho ambacho alitegemea kukisikia.

    Akamtazama Vero usoni, akapatwa na mshangao baada ya kuona Vero akitiririkwa na machozi.

    “Una nini dada Vero?” Aliendelea kuuliza yule msichana ambaye kiumri alikuwa kati ya miaka kumi na nne na kumi na saba. Badala ya kujibu Vero akaendelea kutiririkwa na machozi. Hali hiyo ikamfanya yule muulizaji kutokwa na machozi pia .

    Akajikuta akilia bila kujua kinachomliza dada yake.

    Hali ile ya huzuni kwa makahaba wale ikazusha maswali mle baa. Kwa kuogopa kuendelea kuvuta zaidi hisia za watu. Veronika akaondoka huku akisindikizwa na msaidizi wake katika kilio.

    “Dada unalia nini.” Aliendelea kuuliza yule binti.

    “Usilie Sara mdogo wangu hiki ni kilio changu we nisindikize tu.”

    “Hapana dada, kilio chako ni changu sijisikii raha kuendelea na biashara wakati wewe unalia, wewe ndio mlezi wangu dada, wewe ndio kipenzi changu, wewe ni baba wewe ni mama siwezi dada bila wewe siwezi chochote, kumbuka nilipokuwa………..” Hakumaliza chochote alichotaka kuongea kikakatishwa na kilio walichoangua wote wawili.

    Safari yao ikawafikisha nyuma ya baa ya Kimboka maeneo ya Buguruni sheli. Wakafika kwenye nyumba moja ambayo ilikuwa inauzwa pombe za kienyeji. Mama mmoja mnene ambaye alikuwa muuzaji akaja kuwalaki. Walikuwa tayari wameshafuta machozi na kujitahidi kadri ya uwezo wao kuficha ile hali ya kilio.

    “Vipi wanangu mbona mmerudi mapema leo?” Aliuliza yule mama huku akifunga vizuri kifuani kanga ambayo ilianza kulegea.

    “Tumechoka mama tumeona leo tupumzike mapema” Alijibu Vero huku akiingia ndani akifuatiwa na mdogo wake ambaye alikuwa amejawa na maswali juu ya kipi kilichokuwa kinamliza dada yake. Hakuwahi kuingia ndani. Mama Pili , yule mama mnene muuza pombe akaenda kumzuia mlangoni huku akikaza vizuri kanga yake ambayo ilikuwa inakaribia kufunguka.

    “Hivi nyinyi watoto mna wazimu eeh. Eti tumechoka.” huku akibana pua yake.

    “Mnafikiri kama si hiyo kazi mtaweza kuchangia vipi gharama za hapa ndani?”

    “Mama siku moja tu.”

    “Siku moja tu. Nisikilize we mwana tena nisikilize vizuri. Nasema lazima urudi bila mchango huwezi kulala hapa.” Aliendelea kufoka Mama Pili huku akifunika vizuri sehemu ya kanga ambayo ilikuwa inakaribia kuyaacha maziwa yake makubwa nje.

    “ Sawa mama kama siwezi kulala mimi naondoka.”

    “Ondoka. Tena ondoka na hii takataka yako.” Huku akimnyooshea Sara kidole.

    “Tuondoke mdogo wangu.”

    “Tunaenda wapi dada?”

    “Kusikojulikana.”

    “Kwanini tusimuombe msamaha yule mama tukaendelea kukaa pale.”

    “Hapana mdogo wangu yule Mama si mtu mzuri yaani miili yetu ndio kitega uchumi chake, haiwezekani.” Aliongea huku akiendelea kutokwa na machozi. Mama Pili alikuwa ameshika moja ya nguzo za nyumba yake huku akiwaangalia ndugu wale ambao waliokuwa wanatokomea gizani. Hakuamini kama wangeondoka kweli. Wangeenda wapi nao ni mateka wake? Hili ndilo alilolijua siku zote lakini leo mambo yalikuwa tofauti. Alisubiri dakika kadhaa kuona kama wangerudi kumuomba radhi na kumnyenyekea kama alivyozoea lakini haikuwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    * * *

    Saa 11.00 waliamshwa na sauti za kipaza sauti iliyokuwa inasikika kutoka msikiti wa jirani na pale walipolala. Waliamka kwenye baraza ya nyumba ile iliyoko Tabata Matumbi ili wasije wakakutwa na wenye nyumba. Baridi ilikuwa kali ikawatesa. Mbu walikuwa wachache kutokana na baridi lakini nao walijitahidi kuongeza mateso kwa ndugu hawa wawili.

    ***

    ‘Ko.ko.ko.ko…..’ Saa 2.16 viatu vya Veronika, vilikuwa vinashirikiana na sakafu ya korido ya kituo cha afya cha Tabata shule kutoa mlio usio rasmi. Nyuma alikuwa anafuatwa kwa karibu na mdogo wake Sara , mpaka muda huo alikuwa hajafahamu kilichomleta dada yake pale kituo cha Afya.

    Kadri walivyokuwa wanaelekea upande fulani ndivyo alivyozidi kuhisi sababu ya dada yake kuja huku.

    Kupima, si uzito kipimo ambacho wakazi wengi wa Jiji la Dar es salaam hukipenda huku wakijidanganya kuwa ndio kithibitisho cha ubora wa afya zao. Ingekuwa uzito wangepima hata Buguruni. Kilikuwa ni kipimo ambacho ‘mabrazameni’ na ‘masistaduu’ wengi hawataki hata kukisikia, wanandoa nao hususani wanaume hukiogopa na badala yake husubiria majibu kutoka kwa wake zao pale wanapokuwa waja wazito. Ukimwi. Hakuamini kama dada yake yuko kwenye foleni kwa ajili hiyo.

    “Biashara yenyewe ya kujiuza kwa nini aje kupima?” alishindana mwenyewe na mawazo yake.

    Wakati akiwa kwenye mawazo hayo ghafla. Vero akamgeukia, akaanza kumnong’oneza sikioni. Ingekuwa foleni ya kawaida watu wangetega masikio ili kujua Vero na mdogo wake wananong’ona nini, Lakini hapa yaliwashinda. Foleni ya kupima, hususani kwa mtu anayepima mara ya kwanza si mchezo. Kila mmoja alikuwa kwenye hali nzito ambayo aliijua mwenyewe tu kwenye nafsi yake. Hakuna aliyekuwa na muda wa umbeya hapo.

    “Sikiliza mdogo wangu, nimekuja kupima nataka kujua afya yangu, kama unataka twende tuingie pamoja, sikulazimishi ni hiyari yako.” Ukawa ni wakati mwingine wa Sara kushindana na nafsi yake.

    “Niende nisiende?.” Lilikuwa ni swali gumu lililopita kwenye nafsi yake. Ingawa alikuwa na umri mdogo wa miaka kumi na minne lakini alifahamu vema matatizo yanayotokana na maambukizi ya virusi hivyo hatari.

    “Ah. kwa nini niogope? Kama kufa mbona kuna wengi wanaokufa kwa magonjwa tofauti.? Lazima nipime”. Akakata shauri.

    “Niko tayari dada.” alinong’ona baada ya kukubaliana na nafsi yake kuwa kuna umuhimu wa kupima, akaungana na dada yake kwenda kuchukua kadi kwa ajili ya vipimo.

    Hatimaye zamu ikafika.

    “Namba kumi na tatu aingie, kumi na nne ajiandae.” Ilikuwa ni sauti ya muuguzi ambaye alikuwa na vikadi maalumu vya foleni kwa waliokuja kupima. Vero aliitazama tena kadi yake akahakikisha kuwa ilikuwa namba kumi na tatu namba kumi na nne ilikuwa ni ya mdogo wake sara.

    “Twende.” Alimuhimiza kwa sauti ndogo.

    “Ni zamu yako.”

    “Twende tu.”

    Wakaingia kwa pamoja. Kilikuwa ni chumba cha wastani ambacho kilikuwa na meza moja ndogo ambayo nyuma yake kulikuwa na kiti cha daktari na kitanda cha kulaza wagonjwa wakati wa vipimo. Pia kapu dogo la plastiki ambalo lilikuwa limehanikizwa kwa mabomba ya sindano, mikasi, nyembe na vifaa kadhaa vya tiba.

    Meza ile ilikuwa imefunikwa kwa kitambaa cha kijani huku juu yake kukiwa na kifaa cha kupimia joto, mapigo ya moyo na vingine vingi.

    “Jina.”

    “Naitwa Veronika Beda.”

    “Umri.”

    “miaka ishirini na moja.”

    “Una mume?”

    “Sina.”

    “Huyu ni nani?”

    “Ni mdogo wangu tumekuja kupima sote anaitwa Sara Beda.”

    “Pamoja au kila mmoja atachukua majibu peke yake?”

    “Pamoja.” alijibu Vero huku akihisi kubanwa na pumzi kwa woga.

    “Karibuni sana kwenye huduma zetu rafiki za upimaji kwa hiyari.”

    “Ahsante” Wakajibu kwa pamoja.

    “Kwanza nikupongeze kwa uamuzi wa busara ulioufanya au mlioufanya. Watu wengi wanashindwa kufahamu umuhimu wa huduma zetu rafiki ambazo zinakufanya hata ukikutwa na maambukizi kuishi kwa uhuru na matumaini.” Akatulia kidogo na kumeza mate huku akiingiza mkono kwenye kiboksi kidogo ambacho kilikuwa na baadhi ya vifaa.

    Kazi ikaanza.



     * * *



    Giza lilichukua nafasi yake. “Leo tutalala wapi dada?”

    “Usijali mdogo wangu nina akiba ya kutosha tutalala gesti halafu kesho tutaanza kutafuta chumba.” “Mbona jana tumelala nje kama hela ilikuwepo?” “Jana ilikuwa jumapili tusingeweza kupata chumba, unakuwa kama mgeni wa Buguruni siku za wikiendi” “Kwani imekuwaje mpaka umemkimbia yule mama?”

    “Usijali mdogo wangu ngoja tufike nitakusimulia kila kitu.”

    Akiwa na begi lake begani Veronika aliwaza mambo mengi. Matokeo ya vipimo hayakumuumiza kichwa, kuna mambo yalimuumiza kichwa.

    Hakuona thamani ya kuendelea kuishi lakini ilikuwa lazima atimize mambo fulani yaliyokuwa yanapita kichwani mwake. Usidhulumu usidhulumiwe, Nimedhulumiwa. Aliwaza huku akijihisi kutaka kulia.

    Walikuwa eneo la Buguruni sheli wakavuka barabara na kujichanganya na kundi la watu waliokuwa wanasubiri daladala za Tabata, Ubungo na kwamnyamani. “Dada mbona sikuelewi leo?” “Kwani Vipi?” “Kwanini tunazurura tu bila kunielewesha wapi tunaelekea?” “Leo nina furaha sana mdogo wangu usiwe na wasi wasi tunaenda hapo Matumbi tu.” “Una furaha mbona matokeo ya vipimo si mazuri.” “Nafurahi matokeo yako ni mazuri wewe ndio mimi.”

    “Hivi kwanini hujashituka ulipoambiwa kuwa umeathirika?” “Kwa sababu nilijua siku nyingi kuwa itakuwa hivi.”

    “Ulijuaje?

    “Ni hadithi ndefu nitakusimulia kesho.” Wakaingia kwenye gari linaloelekea Ubungo. Wakashuka Tabata Matumbi. Sara alikuwa hamuelewi kabisa dada yake. Mambo aliyoyafanya kwa Mama Pili siku iliyopita mpaka siku hii ambayo amechukua uamuzi nzito wa kwenda kupima bado yaliendelea kumtatanisha. Hii ilikuwa ni siku nyingine ambayo Vero aliendeleza mlolongo wa tabia za ajabu ambazo hakuwahi kumuona nazo. Wakatembea taratibu wakipita vichochoro mbalimbali vya mitaa ya Tabata Matumbi.

    Ni mitaa ambayo ilitafsiri maisha ya wakazi wake. Usingetembea hatua kumi kabla haujakutana na vidimbwi vidogo ambavyo vina maji machafu yenye harufu mbaya. Taka taka za mkaa ambazo zilimwagwa hovyo zilizidi kuchafua mandhari ya mtaa huu.

    USANGI GUEST HOUSE maandishi hayo yaliyokolezwa kwa rangi nyekundu yalimvutia Vero. Akafuata mshale unaolekeza kule iliko nyumba hiyo ya kulala wageni. Haikuwa nyumba yenye mvuto, kuta zake zilikuwa zimechakaa na kufanya ramani zisizo rasmi ambazo zilitokana na uchafu. Hata rangi yake iliyopigwa mwanzo ilikuwa haijulikani tena. Wakaelekea moja kwa moja hadi ndani sehemu yenye kidirisha kidogo kilichoandikwa MAPOKEZI. “Kuna vyumba.” “Vipo.” “Akaandikisha jina kwenye lile daftari, Zubeda Mwandege kazi mfanyabiashara Kutoka Tanga kabila Msambaa.” Alimaliza maelezo yake na kumkabidhi yule dada wa mapokezi daftari lake.

    “Chumba namba 9” alisema yule muhudumu huku akimuonyesha Vero kiliko kile chumba kwa kidole. Vero na Sara wakatembea taratibu kuelekea kwenye chumba chao. Walilakiwa na kitanda cha futi nne kwa sita. Baada ya kuingia mle chumbani akafungua begi lake na kuanza kukagua tena yale matokeo ya vipimo vya H.I.V aliyoyapata kule Tabata. Akatikisa kichwa kama anayekubali kitu fulani. Akaendelea kupekuwa begi lake. Kuna kitu alikuwa anatafuta. Bado Sara alikuwa anaendelea kushangazwa na vituko vya dada yake. Alikaa kimya akimwangalia dada yake wakati anapekua begi lake. KISU.? Alishituka Sara baada ya kumuona dada yake akiibua kisu kikubwa chenye mpini mwekundu. Alishituka kwa sababu hakikuwa kisu cha kawaida. Asingengeweza kuchukua kisu kinachofanana na upanga mdogo kwa ajili ya kukatia nyanya. Pamoja na mshituko huo bado hakutaka kumuuliza dada yake.

    “Mdogo wangu naomba ulale tutaonana kesho Mungu akipenda.” “Unaenda wapi dada?” “Naenda kuua mtu.” Alijibu kwa mkato huku akichomeka vema kiunoni kile kisu kikubwa ambacho hakikuwa na ala.

    Akageuka na kumkazia macho mdogo wake.Alitisha. Hakuwa vero mpole ambaye alizoeleka katika macho ya Sara. Huyu alikuwa ni mwingine kabisa ambaye alibeba sura ambayo ilimbabaisha Sara na kumfanya ashindwe kuuliza chochote alichokusudia.



    * * *



    Miguno na vilio vya mahaba viliendelea kusikika kwenye chumba cha mama Pili. Ilikuwa ni tabia ya mama huyo kujifariji na wateja wake wa pombe kwa malipo madogo. Hakujali umri wa mteja wake, alichojali ni pesa tu.

    Leo ni siku ambayo kijana mdogo kabisa bila soni wala haya anapewa huduma na mama Pili. Vero alikuwa amesimama nje ya chumba hiki huku moyo wake ukienda mbio. Kupitia tundu lililokuwa kwenye pazia aliweza kuona kila kilichofanyika kwani kibatari hakikuzimwa. Kijana yule aliendelea kuonyesha ufundi kwa mama Pili. Vero alikerwa sana kwani aliona anapotezewa muda wa kutimiza dhamira yake. Baada ya subira ya muda mfupi hatimaye wakamaliza ushenzi wao.

    Kwa mshangao Vero akamuona mama pili anatoa pesa na kumpa yule kijana kama malipo kwa huduma ile ya ngono.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ahsante mama.” Alisikika yule kijana.

    Mpuuzi mkubwa huna akili mpumbavu, unamwita mama mtu uliyefanya naye upumbavu huo, hujui thamani ya mama? Aliwaza vero kwa hasira Huku akichomoa kisu na kukishikilia vema mkononi. Dhamira yake ilikuwa moja tu kuua, hakuwa na utani alikuwa amedhamiria kuua. Hasira na hamu ya kutekeleza mauaji ilimfanya akishikilie kwa nguvu zaidi kile kisu. Mama pili ndiye alikuwa namba moja katika orodha ya watu aliokusudiwa kuwaua. Yule kijana akafunga vizuri zipu ya suruali yake akaondoka. Wakati anaondoka Vero akazunguka nyuma ambako kulikuwa na dirisha maalum ambalo alilifahamu vema kwani lilikuwa muhimu sana. Mara nyingi walikuwa wanatumia dirisha hilo kuwakimbia polisi na maafisa wa afya ambao hufanya ukaguzi wakati wa magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na mengineyo. Akaingia haraka ili amuwahi mama Pili kabla hajamaliza kuvaa.



    * * *



    “Ngo. Ngo. Ngo.” “Ingia.” Alisikika mama Pili baada ya kusikia mlango ukigongwa. Vero akaingia ndani moja kwa moja. “Enhe. We malaya umefuata nini?” Aliuliza mama Pili baada ya kumuona mgongaji. Vero hakujibu alizidi kumkazia macho yule mama. “Nakuuliza wewe malaya umefuata nini hapa kwang…….” Chochote kilichotaka kuzungumzwa kilinyamazishwa na kitendo cha ghafla kilichofanywa na Vero.

    Alimrukia kwa ghafla na kumuangusha kitandani kisha akamziba kwa mto uliokuwa pale kitandani. Kwa kasi akachomoa kisu alichoweka kiunoni akakididimiza kwenye titi la kushoto la mama huyu. Mama Pili akakurupuka kwenye hifadhi ile ya mto akaanza kugumia kwa uchungu wa kutokwa na roho. Kilio cha kutokwa na roho kilikuwa kikubwa kikafika nje. Vero alielewa haraka hatari inayotaka kutokea. Haraka haraka akakimbia na kukiacha kisu kile pale kifuani. Damu zilikuwa zinaruka kama mpira unaovujisha maji. Wakati anatoka akapishana na mtu ambaye alikuwa anakuja mbio akifuatiwa na watu wengine walioonekana kulewa chakari. Akapishana nao huku akipigana nao vikumbo. Bila kuonekana na yeyote akapita kwenye dirisha lile la dharura akamezwa na kiza cha usiku. Kama kivuli akatoweka eneo lile.



    * * *



    Saa 2.30 ilimkuta koploPeter Mkwabi akiwa nyumbani kwa mama Pili. Sambamba naye alikuwa kachero Dadi Kasweyaga ambaye hakuvaa sare za kazi kama Yule mwenzake. “Umesema unaitwa nani?” Aliuliza kachero yule huku akiandaa kalamu na daftari lake ndogo.

    “Pili Bundala.” “Una uhusiano gani na marehemu.”

    “Ni mama yangu mzazi.”Akatulia kidogo na kumwacha yule dada afute machozi. “Unaweza kujua ni nani kamuua mama yako?” “Sijui.”

    “Kuna yeyote ambaye unamuhisi?” “Hakuna” “Mligunduaje kuwa kauwawa?” “Tuliingia ndani akiwa anakata roho kwani kabla alipiga makelele ambayo yalitushtua, katufia mikononi…..” Aliongea akasindikiza maongezi hayo kwa kilio kidogo cha kwikwi. “Nani alikuwa mtu wa mwisho kutoka kabla ya shambulizi la marehemu.” “Suma.” “Anaishi wapi?” “Sifahamu anakoishi lakini anauza sigara huko barabarani.” “Baada ya Suma kutoka kuna mwingine aliingia.” “Hakuna.” “Mlijuaje kama marehemu yuko kwenye matatizo.” “Tulisikia kilio kikubwa ambacho kilitushitua wote hapo nje.” “Mlichukua muda gani toka kusikia hicho kilio kufika eneo la tukio.” “Muda huo huo tuliinuka na kukimbilia ndani.” “Toka kuondoka kwa Suma mpaka kusikia kilio hicho ulipita muda gani?”

    “Kama dakika tano hivi.”

    “Nani alikuwa wa kwanza kuingia ndani?”

    “Mzee Bundala.” “Baba yako?” “Hapana yeye ni jirani tu.”

    “Suma alikuwa anafanya nini huko ndani?”

    “Walikuwa faragha na mama.”

    “Faragha ya aina gani?” Hakujibu.“Walikuwa wapenzi?” Akaitikia kwa kichwa huku akiona haya.

    “Hakukuwa na mzozo wowote kati ya marehemu na mpenzi wake kabla ya kifo chake?”

    “Hakukuwa na mzozo na hata alivyoondoka alikuwa mwenye furaha.”

    “Huwezi kuhisi kuwa Suma ndiye aliyemuua mama yako?”

    “Hapana.”

    “Kwanini unakanusha wakati yeye ndiye mtu wa mwisho kutoka kabla ya kifo chake?”

    “Hilo linanishangaza hata mimi kwani Suma hakuingia na kisu mle ndani.”

    “Una uhakika gani?”

    “Sijamuona nacho.”

    “Iwapo alikificha.....”“Alikuja akiwa amevaa fulana ambayo ilimbana na suruali yake pia ilikuwa imebana, laiti kama angeficha na jinsi kilivyo kikubwa kile kisu lazima kingeonekana kwani alikuwa amechomekea na suruali aliishusha kiasi cha nusu makalio.”

    “Ahsante kwa majibu yako, naweza kukuhitaji baadae kwa mahojiano zaidi.”

    “Sawa.” Alijibu Pili kwa sauti yenye majonzi.



    * * *



    Suma kijana mchezesha kamari na muuza sigara alikuwa anaonja ladha ya kuisaidia polisi. Alikuwa amefungiwa mahabusu baada ya kuulizwa maswali kadhaa. Ni wazi hakuhusika na walishaibaini hilo, tatizo ni jinsi ya kutoka mle ndani. Alikuwa anaonja ladha chungu ya wapenda rushwa ambao walipenda hata haki ya kupumua basi mtu ailipie, Suma hakutolewa alikuwa anasubiriwa mtu mwenye uchungu na ndugu yake aje kutoa chochote Kachero Dadi Kasweyaga alikuwa amekaa muda mrefu pale kituoni kuvizia ndugu wa Suma ambaye atatoa chochote. Hakutokea ndugu wala nani.

    “Mtoe huyo mshenzi, ukome kufuata wanawake watu wazima. Mtoto mdogo unavamia miguberi.” Alifoka kachero Dadi Kasweyaga baada ya kukata tamaa na kufeli mpango wake wa kujipatia rushwa. Siku moja ilitosha kumtia adabu Suma muuza sigara. Pamoja na maisha yake kijiweni na kujichanganya na vijana wakorofi wauza bangi alikuwa hajawahi kuingia huku. “Vipi afande unamwachia muuaji?”Aliuliza Koplo Peter huku akicheka “Mwache aende ananizingua tu hapa.” Alijibu “Vipi una ripoti kutoka hospitali?” Aliuliza tena Konstebo. “Ripoti ni ya kawaida isipokuwa wataalamu wa vinasaba ndio wameleta ripoti inayonichanganya kidogo.” “Kivipi?” “Inahisiwa kuwa muuaji ni mwanamke kwani kumekutwa na mabaki ya rangi za kucha kwenye kisu?”

    “Lakini hata wanaume siku hizi wapo wanaopaka rangi za kucha.”

    “ Pia imeokotwa hereni eneo la tukio.”

    “Afande hata wanaume nao huvaa herini na hatuna uhakika kama kweli hiyo hereni iliachwa na muuaji au mtu mwingine tofauti?” Alijibu Koplo na kumfanya kachero akae kimya akitafakari. “Lakini afande ile hereni ni ya kike sio zile za kiume.” “Usinichekeshe, hakuna hereni za kiume zoteni za kike.’

    “Na wale wanaovaa?” “Waulizwe.”Akachukua note book yake akaanza kuipitia.

    “Mzee Bundala anatakiwa kuhojiwa.” Aliongea kachero baada ya ‘kuipitia note book’ ile.

    Saa 7.35 ilimkuta kachero Dadi Kasweyaga akiwa katika eneo la tukio. Akawapita kina mama waliojitanda kwa kanga pale nje akaingia ndani. Huko ulikuwa unafanyika utaratibu wa mazishi ikiwa ni pamoja na michango mbalimbali.

    Akawasalimia wazee waliokuwa wanashona sanda. Kisha akaonyesha kitambulisho chake na kuomba kuonana na wahusika.

    “Naomba kuonana na mzee Bundala kama yupo hapa.”

    “Katoka kidogo ameenda kununua karafuu maiti huko nje, msubiri atakuja sasa hivi?”

    Kachero akakaa kwenye stuli akimsubiri Mzee Bundala. Wakati akiwa pale kwenye stuli akapata fursa ya kuisanifu nyumba ile. Nyumba ile kuukuu ilikuwa na vyumba vitano. Vyumba vyote vilikuwa na waombolezaji, wengi wakiwa ni ndugu jamaa, marafiki na bila shaka wateja wa pombe zile za kienyeji.

    Mara, wakaingia wazee wawili ambao walikuwa wamebeba mfuko mweusi wa nailoni.

    “Mzee Bundala mgeni wako huyo.”Alisikika mzee mmoja huku akichukua ule mfuko mweusi kutoka kwenye mikono ya mzee bundala.

    Wakatoka mle ndani na kutafuta sehemu ambayo haikuwa na waombolezaji wakasimama hapo.

    “Naitwa kachero Dadi kasweyaga natokea kituo cha polisi Buguruni.” Alianza kachero baada ya kusalimiana kisha akatoa kitambulisho chake.

    “Samahani kwa usumbufu mzee kuna mambo machache nataka kukuuliza.”

    “Uliza baba hakuna tatizo” alisisitiza mzee Bundala.

    “Naomba unielezee kwa ujumla mazingira ya mauaji yalikuwaje.”

    Maelezo yake hayakuwa tofauti sana na yale ya Pili.

    “Inasemekana wewe ni mtu wa kwanza kuingia ndani baada ya tukio.”

    “Ni kweli baba.”

    “Hakuna mtu yeyote uliyemuona anatoka katika chumba cha marehemu?” Aliuliza kachero Dadi.

    Hapo ikawa kama aliyemzindua mzee Bundala.

    “Kweli nimekumbuka kuna msichana nilipishana nae mlangoni tena alitoka mbio lakini sikumzingatia kwa kuwa nilifikiria afya ya marehemu kwanza.”

    “Unaweza kukumbuka sura yake?”

    “Hapana kulikuwa na giza ninachokumbuka ni kuwa huyo msichana alikuwa mrefu wa wastani.” Alijibu Mzee Bundala.

    “Ahsante mzee Bundala unaweza kwenda lakini naomba uniitie mtoto wa marehemu.”

    “Pili?”

    “Eee, kwani anao wengine?”

    “Wapo lakini si wakazi wa Buguruni na hawakuwepo siku ya tukio.”

    “Hao siwahitaji, namuhitaji huyo Pili.”



    Baada ya dakika chache pili akawa mbele ya kachero yule.

    “Unasema mzee Bundala ndiye mtu wa kwanza kuingia siyo?”

    “Ndiyo.”

    “Ulipita muda gani toka kuingia kwa Bundala na kufika kwenu kwenye eneo la tukio?”

    “Ni vigumu kukadiria muda kwani tuliachana hatua kama kumi kwani mwenzetu alituzidi mbio.”

    “Hamkuwahi kukutana na mtu yeyote ambaye alikuwa anatoka ndani?”

    “Hapana sijakutana na yeyote na jinsi ilivyo ndogo ile korido lazima ningemuona.”

    “Haiwezekani kuwa aliyefanya kitendo hicho akawa ametokea mlango wa uani?”

    “Haiwezekani.”

    “Kwanini?”

    “Kwa sababu tulikuta mlango ukiwa umefungwa kwa ndani kama angekuwa amepitia huko angeacha mlango wazi.”

    Kachero akakuna kichwa huku akitafakari zaidi.

    “Zaidi ya huo mlango kuna sehemu nyingine ya kutokea nje?”

    Hapo Pili akatulia kidogo akiwaza jinsi ya kujibu swali lile. Kidogo alishituka. Kachero akaugundua mshituko ule, akasubiri kwa hamu kidogo kusikia nini ataongea Pili.

    “Hujajibu swali langu Pili.” Alisikika kachero baada ya Pili kunyamaza kwa muda mrefu kidogo.

    “Ipo sehemu nyingine ya kutokea lakini ilizibwa kwa viroba na ni sisi wenyewe tu ndio tunaoifahamu.”

    “Unaweza kunipeleka kwenda kuiona hiyo sehemu?” Akaitikia kwa kichwa.

    “Sawa.” Alijibi huku akiongoza kwenye chumba hicho.

    Wakaongozana na kachero kuelekea kule ndani. Wakaingia chumba ambacho kilikuwa na mitungi mingi ya pombe. Chumba kile hakikuwa na mlango. Kilikuwa karibu na chumba cha mauaji. Ndiyo kwanza akagundua kuwa kile kiroba kilichotumika kuzibia pale kilikuwa kimepasuliwa katikati na kubaki kama pazia lenye pande mbili.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mh.” Aliguna Pili baada ya kugundua tukio lile.

    “Hili dirisha liliwekwa hapa kwa nini?”

    “liliwekwa hapa kwa dharura kama itatokea tukavamiwa na majambazi basi hapa ndiyo sehemu nzuri ya kutokea.”

    “Unataka kuniambia hakuna watu wa nje wanaoifahamu sehemu hii?” Aliuliza Kachero.

    “Hakuna.” Alijibu kwa mkato huku akionyesha wazi kuchoshwa na maswali ya kachero.

    “Hakuna mtu yeyote ambaye anaifahamu sehemu hii lakini yuko nje ya haya makazi?”

    Akainua kichwa juu kujaribu kuvuta fikra.

    “Yupo.” Alijibu kwa mkato kisha akaendelea.

    “Anaitwa Vero.”

    “Vizuri, tutampata vipi huyo Vero?”

    “Sijui.”

    “kwanini?”

    “Kwa sababu alifukuzwa na mama hivyo hakupata fursa ya kuaga.”

    “Mh.” Aliguna kachero huku akitikisa kichwa kuonyesha kubaini kitu.

    “Kwanini alimfukuza?”

    “Sifahamu kwanini .” Kachero alibaini kuwa anaongopewa. Haikuingia akilini kwa mtu ambaye alikuwa anaishi humo ndani ashindwe kufahamu ugomvi wa mama yake na huyo mtu.

    “Unaweza kuniambia mama yako alikuwa na uhusiano gani na huyo Vero?”

    “Sifahamu.” Alijibu. Uongo mwingine. Aliwaza Kachero huku akijua wazi kabisa kuwa kuna kitu anafichwa.

    “Unamfahamu ndugu yeyote wa Vero?”

    “Hapana.”

    “Ahsante, naona niishie hapa ila kama nitakuhitaji tafadhali nitaomba utoe ushirikiano wa kutosha.”



    II

    Saa 8.43 Sara alikuwa macho. Aliwaza mengi kuhusu dada yake. Kuna wakati alijikuta akilia. Milango ya gesti ilikuwa imefungwa hivyo uwezekano wa Vero kurudi usiku ule haukuwepo. Kilichomtisha zaidi hakujua anaenda kumuua nani na baada ya hapo atamuua nani mwingine. Alijaribu kuutafuta usingizi ili mawazo yale yaweze kupotea lakini ilishindikana. Saa 9.48 usingizi ukamchukua. Akalala.

    Akashituka saa 3.33. Ilikuwa baada ya kusikia mlango ukigongwa. Akafungua ule mlango. Mwanamke mrefu alikuwa amesimama mlangoni.

    “Samahani nilikosea chumba.” Aliongea yule dada huku akiinua macho juu ya mlango kuhakikisha kama alikuwa amekosea kweli.

    Wakati anataka kufunga mlango akamuona mwanamke mwingine ambaye alikuwa amejitanda kanga. Alimjua, Isingekuwa rahisi kwa Vero kujiweka katika mazingira ambayo yangemfanya Sara ashindwe kumfahamu. Alimpokea dada yake kwa kumshika mkono akaingia naye chumbani.

    Sara aliangukia kitandani akataka kulala. Kabla hajafanya lolote mlango ukagongwa tena. Dada wa mapokezi alikuwa mlangoni. Hakujua kabisa kama Vero aliondoka usiku wa kuamkia siku ile kwani wakati anaondoka yule dada alikuwa chumbani kwake.

    “Samahani dada.” Aliongea yule dada huku akionyesha mshituko kidogo.

    “Bila samahani.” Alijibu Vero huku moyoni akishangazwa na mshituko ulioonyeshwa na muhudumu.

    “Kwa kawaida kukaa hapa ndani mwisho ni saa nne hivyo kama munataka kuongeza muda nawashauri mulipie mapema.” Alimuelewa akatoa kiasi alichohitaji. Yule dada akaondoka kwenda kule chumbani kwake. Baada ya dakika chache akarudi akiwa na lile daftari.

    “Nimeandika kila kitu naomba uweke saihihi yako.” Yule dada aliongea huku akionyesha wazi kuogopa kumuangalia Vero usoni. Baada ya kupiga sahihi yake yule dada akaondoka haraka.

    Akachukua kioo kidogo akaanza kuikagua sura yake. Kweli yule dada alikuwa na kila sababu ya kumuogopa. Iwapo yeye mwenyewe alijiogopa baada ya kuiona sura yake kwenye kioo ingekuwaje kwa mtu mwingine? Alikuwa anatisha. Macho mekundu na sura iliyobeba ukatili ni miongoni mwa vitu alivyosadiki kuwa vilimtisha yule mhudumu. Hata angekuwa nani lazima angeona mabadiliko yale. Aliingia ndani akafunga mlango.

    “Umemuua nani?” Aliuliza Sara baada ya kumuona dada yake akilala kitandani bila kubadili nguo.

    “Mama Pili.” Alijibu kwa mkato huku akijivutia shuka.

    “He! Kakukosea nini dada?” Aliuliza Sara huku naye akionyesha hofu ya wazi

    “Niache nipumzike muda wa kujua ukifika utajua kila kitu kuna mambo mengi unatakiwa kuyafahamu.” Alijibu Vero huku akifumba macho.

    “Dada huoni kama utatafutwa na polisi kama kweli umefanya mauaji.”

    “Ni kweli nitatafutwa lakini naomba Mungu nisikamatwe mpaka nitakapokamilisha kazi yangu.”

    “Ina maana kuna mwingine amebakia?”

    “Sio mwingine, wengine, naomba ukatishe maswali yako nahitaji kupumzika bado nina kazi kubwa mbele yangu.” Safari hii sauti yake Ilikuwa kali na ya amri zaidi. Sara akanyamaza, na kumwacha dada yake apumzike kama alivyoamrisha.



    * * *



    Jumanne tulivu. Lucy alimaliza saa za kazi za siku hii kwa furaha kubwa. Furaha hiyo ilisababishwa na ujio wa mchumba wake ambaye alikuwa masomoni huko Norway. Alitarajiwa kuwasili Dar na ndege ya saa 12 Jioni. Aliamua kuwahi mapema maeneo ya airport. Akaangalia kwenye simu yake ilikuwa inaonyesha saa 9.40. Akatoka nje ya ofisi zile za kampuni ya simu zilizoko mtaa wa ohio. Moja kwa moja akaingia kwenye gari lake. Wakati anataka kufunga mlango akazuiwa na mtu aliyekuwa anampa ishara ya mkono kuwa amsubiri. Yule mtu alipofika karibu simu ya Lucy ikaanza kuita, Kabla ya kumsikiliza yule aliyemsimamisha akapokea simu kwanza.

    “Poa shoga.”

    “Mwenzangu, ndo naelekea airport nimeambiwa anawasili jioni.”

    “Ahsante.” Alijibu huku akishukuru kwa alichoambiwa na mpigaji wa simu.

    “Habari anti.”

    “Nzuri sijui nikusaidie nini?”Aliuliza Lucy huku akionyesha wazi kutomchangamkia huyu dada

    “Samahani anti mi naomba unipe lifti.”

    “Unafika wapi?”

    “Majumba sita.”

    “Majumba sita?”

    “Ndio ni pale maeneo ya uwanja wa ndege karibu kabisa na kituo kinachoitwa posta.”

    “Ahaa. Sawa ngoja nikuache pale airport nafikiri pale ni karibu kabisa na nyumbani. Yule dada akaketi siti ya nyuma ya dereva.

    Baada ya mwendo wa nusu saa wasimamishwa na taa za barabarani zilizoko katika makutano ya barabara ya Pugu na Mandela.

    “Ah, hizi taa nazo.” Alilalamika Lucy.

    “Usilalamike sana dada Lucy.” Mtu aliyempa lifti aliongea.

    “Eh. Kumbe unanifahamu.” Alishituka Lucy baada ya kusikia jina lake likitajwa na mtu asiyemfahamu. Akageuka.

    “Umenisahau?” Aliuliza yule mtu.

    Lucy akageuka akashangaa kumuona abiria wake akiwa amejifunika kanga kama mpishi anayeogopa kuchafuka kwa masizi.

    “Mbona sikufahamu.” Aliongea huku akionyesha hofu kubwa pengine kwa kudhani kuwa anaongea na jini.

    “Naitwa Veronika Beda.”

    “Whaaat?” Alishituka Lucy akataka kuinuka kwenye siti akimbie. Hakuwahi, mkono wa kulia wa Vero ukazunguka kwenye shingo ya Lucy mkono wa kushoto akautumia kudidimiza kisu chake kwenye titi la kushoto la Lucy. Damu ikaanza kumwagika. Akakiacha palepale kisu chake chenye mpini mwekundu.

    Akatumia ile kanga kufuta matone ya damu yaliyorukia mkononi. Matone mengine yalizuiwa na kanga kuifikia blauzi yake. Akaanza kumpekua marehemu, akaangaza macho mle ndani akauona mkoba wa Lucy. Akaufungua. Akaziona, zilikuwa nyekundu nyekundu tupu. Hakutaka kuhesabu akazishindilia kwenye nguo ya ndani. “Wasalimie Kuzimu.” Aliongea peke yake wakati anateremka kwenye lile gari. Hakuna aliyeona, Vioo tinted wangeonaje?

    Alivuka barabara akafuata njia inayoelekea buguruni Chama. Ile kanga yenye matone ya damu aliiacha kwenye gari. Alitembea taratibu kuelekea Buguruni Chama.

    “Hee. Shoga huonekani?” Alishitushwa na sauti ya mtu aliyemfahamu. Alimtambua, alikuwa Zabibu msichana ambaye walikuwa wote kwenye kijiwe cha ukahaba.

    “We acha tu shoga, mama Pili amenifukuza nyumbani kwake lakini sina kinyongo huu mguu ni wa kwake naenda kumsalimia.”

    “Mh. Shoga sahau kabisa.”

    “Kwanini ?”

    “Hivi ninavyokwambia unatafutwa kila kona eti unahusika na mauaji ya mama Pili.”

    “Eti nini, mama Pili amekufa?” Alijifanya kushitushwa na taarifa ya kifo cha mama Pili lakini ukweli alishitushwa na taarifa ya kutafutwa kwake na polisi. Alishangaa kwanini polisi waliweza kumbaini mapema kiasi kile. No, Lazima nifanye kitu kujiokoa. Aliwaza



     Alivuka barabara akafuata njia inayoelekea buguruni Chama. Ile kanga yenye matone ya damu aliiacha kwenye gari. Alitembea taratibu kuelekea Buguruni Chama.

    “Hee. Shoga huonekani?” Alishitushwa na sauti ya mtu aliyemfahamu. Alimtambua, alikuwa Zabibu msichana ambaye walikuwa wote kwenye kijiwe cha ukahaba.

    “We acha tu shoga, mama Pili amenifukuza nyumbani kwake lakini sina kinyongo huu mguu ni wa kwake naenda kumsalimia.”

    “Mh. Shoga sahau kabisa.”

    “Kwanini ?”

    “Hivi ninavyokwambia unatafutwa kila kona eti unahusika na mauaji ya mama Pili.”

    “Eti nini, mama Pili amekufa?” Alijifanya kushitushwa na taarifa ya kifo cha mama Pili lakini ukweli alishitushwa na taarifa ya kutafutwa kwake na polisi. Alishangaa kwanini polisi waliweza kumbaini mapema kiasi kile. No, Lazima nifanye kitu kujiokoa. Aliwaza

    “Kwa hiyo unanishauri vipi shoga?”

    “Usiende kwani watakusumbua mpaka uje kutoka utakuwa umesota rumande si chini ya mwaka mmoja.”Alitikisa kichwa kukubaliana naye.

    Akavuka upande wa pili wa barabara. Alikuwa anacheza kamari mbaya katika maisha yake. Alikuwa amesimama kwenye kituo cha daladala katika eneo ambalo alifahamika sana. Moyo ulikuwa unaenda mbio, kituo hiki hakikuwa mbali sana na baa maarufu ya kimboka. Nyuma ya baa hii ndiko iliko nyumba ya mama pili. Pale aliposimama aliomba Mungu asije kuonwa na mtu yeyote anayemfahamu.Mungu alikuwa upande wake akaingia kwenye gari linaloelekea Mwenge bila kukutana na yeyote wanayefahamiana.



    ****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hasira ilikuwa inarindima kwenye kichwa cha kachero Dadi Kasweyaga. Alikuwa hajakamilisha uchunguzi wa mauaji ya mama Pili analetewa tena taarifa ya mauaji ya mwanamke mwingine. Akiwa kwenye gari ndogo la polisi alitafakari mambo mbalimbali bila kupata majibu. Mauaji ya safari hii yalikuwa na uzito wa kipekee. Aliyeuwawa ni mtoto wa Inspekta. Hili lilimchanganya zaidi. Aliogopa sana kubaini kuwa muuaji ni mmoja kwani alijua kazi itakuwa ngumu zaidi. Ugumu aliouona ni uhusiano wa mtu wanayemshuku na mauaji haya ya Lucy. Hakuona dalili ya kahaba huyo anayeitwa Vero kufahamiana na Lucy.

    Watu wengi walikuwa wamezunguka eneo la tukio na kusababisha foleni kubwa ya magari. KoploPeter Mkwabi alikuwa eneo la tukio akiandika maelezo kutoka kwa trafiki aliyekuwa eneo lile. Walipeana mikono na koplokisha akaenda kuchungulia mle kwenye gari. “My God, mpini mwekundu tena.” Aliongea kwa sauti aliyoisikia mwenyewe huku akishangaa jinsi bisu lenye mpini mwekundu lilivyohitimisha uhai wa mrembo yule.

    “Enhe ilikuwaje?”Kachero alimgeukia yule askari mwenzake wa kitengo cha usalama barabarani na kumrushia swali hilo.

    “Baada ya taa za magari kuruhusu nilishangaa kuona hili gari likiwa limesimama tu na kusababisha foleni kubwa, dereva mmoja wa lori baada ya kuona anachelewa akashuka na kuja kwenye hili gari na kuwa wa kwanza kuliona tukio hili.”

    “kuna yeyote uliyemuona akiteremka ndani ya hili gari”

    “Kwa mujibu wa maelezo ya Dereva wa lori kuna mwanamke aliteremka.”

    “Mwanamke?” Kachero alishituka . Mpini mwekundu halafu mwanamke tena. Mauji haya ambayo yalifanana yalimchanganya kachero. Taarifa za mwanzo zilimpa moyo kuwa angefanikiwa kumnasa muuaji lakini hizi zilikuwa za aina yake. Haiwezekani muuaji akawa mwendawazimu anayeua ovyo. Inakuwaje mtoto wa Inspekta tena anayefanya kazi kwenye kampuni kubwa ya simu yenye malipo mazuri ahusiane na changudoa huyu ambaye hata hafahamiki katokea mkoa gani?

    Yalikuwa ni maswali yaliyopita kichwani mwake huku yakikosa kabisa majibu.

    “Naomba ufanyike utaratibu hii gari iondolewe hapa na hii maiti ipelekwe hospitali.” Aliongea kachero huku akiingia kwenye gari.

    Akaendesha gari kwa kasi hadi mitaa ya Ohio. Akasimamisha gari mbele ya lango la kuingilia kwenye kampuni ya ile ya simu. Akapiga honi kama mara tatu. Akaja mlinzi ambaye alikuwa na sare za rangi ya kijivu. Kabla hajaongea chochote akachomoa kitambulisho chake na kumwonyesha.

    “Karibu.” Alikaribisha yule mlinzi baada ya kugundua anaongea na nani.

    “Ahsante.”

    “sijui nikusaidie nini afande.” Aliuliza yule mlinzi.

    “Unamfahamu Lucy Limo afisa uhusiano wa kampuni hii?”

    “Ndiyo namfahamu mzee na tumeshapata taarifa yake kwamba ameuwawa.”

    “Sijauliza swali la kuuwawa hapa jibu vizuri tafadhali.” Alisikika kachero kwa ukali Kisha akaendela.

    “Huwa unaingia zamu saa ngapi?”

    “Saa sita mchana natoka saa kumi na mbili jioni.”

    “Mbona hii ni saa moja hujatoka?”

    “Mwenye zamu kachelewa kufika hivyo siwezi kuondoka mpaka afike nikabidhi lindo.”

    “Vizuri. Kwa hiyo uko hapa kabla marehemu hajaondoka.”

    “Eee.” Alijibu huku akiitikia kwa kichwa.

    “Wakati anaondoka marehemu aliongozana na nani?”

    “Kuna mwanamke mmoja ambaye alimuomba lifti.”

    “Huyo mwanamke alitokea wapi?”

    “Hilo siwezi kufahamu afande lakini mimi nimeripoti kazini yeye alikuwa amekaa paleee.” akaonyesha kwa kidole sehemu ambayo alikaa huyo mtu.

    “Hukumtilia mashaka?’

    “Hapana.”

    “Kwanini hukumtilia mashaka wakati ni sehemu yako ya kazi.”

    “Alikuwa nje ya mipaka yangu.”

    “Lucy aliondoka saa ngapi hapa ofisini?”

    “Saa 9.40.”

    “Ulijuaje?”

    “Huwa tunaandika muda wa kuondoka.”

    “Unataka kuniambia huyo aliyeondoka na Lucy alikaa hapo nje kwa zaidi ya masaa matatu?”

    “Bila shaka mkuu.”

    “Ahsante kwa majibu yako unaitwa nani?”

    “Amani Kombo.”

    “Kwa heri ndugu Kombo, nikihitaji msaada zaidi nitakutafuta.”

    Akajitoma kwenye gari lake akaliwasha na kuondoka.



    * * *

    Alifungua chupa ile ya maji baridi yenye ujazo wa lita moja na nusu akaanza kuyanywa.

    “Umekula?” Aliuliza huku akimkazia macho Sara ambaye alikuwa anaanza kumuogopa dada yake baada ya kupata taarifa ya mauaji ya mtu wa pili.

    “Nimekula dada, hapo nje wanauza chips na vyakula mbaimbali.”

    Aliongea huku machozi yakimtoka. Vero aliligundua hilo. Hakutaka mdogo wake ahuzunike.

    “Sara mdogo wangu, huna sababu ya kulia kwa haya ninayoyafanya, wewe bado ni mdogo kuna mambo mengi sana huyaelewi. Najua unaniona kama niliyechangnyikiwa lakini akili zangu ni timamu kabisa na ninajua ninacho kifanya. Wewe ni mdogo wangu wa tumbo moja. Baba na mama yetu ni mmoja. Nakumbuka baadhi ya siku uliwahi kuniuliza mama yetu yuko wapi, pia uliwahi kuniuliza kuhusu baba, babu, bibi na ndugu wengine. Kwa kuwa natafutwa na polisi sijui kama nitaweza kuwakwepa siku zote hivyo naona nikueleze ukweli wa maisha yako na haya mauaji ninayoyafanya. Baba yetu amezaliwa katika familia ya kimaskini sana. Akiwa na miaka minne baba yake mzazi ambaye ndiye babu yako alifariki dunia. Hapo maisha yalikuwa magumu sana kwake. Akasoma kwa shida hadi alipofika darasa la saba. Mungu akamjalia akafanya mtihani.Kisha akakaa nyumbani kusubiri matokeo ya darasa la saba……………….”



    ****



    MIAKA KADHAA ILIYOPITA



    Matokeo ya darasa la saba yalikuwa yametoka. Matokeo haya yaliwafanya baadhi ya wakazi wa Mbagala kuacha shughuli zao na kujikusanya kwenye mbao za matangazo katika shule mbali mbali zilizoko katika kitongoji hiki cha manispaa ya Temeke. Mkusanyiko huu ulikusanya rika mbalimbali ; Watoto, vijana na wazee.

    Hofu ilionekana wazi katika nyuso za baadhi ya watoto na wakubwa. Ajabu. Wapo wale walioonekana kuwa na furaha kwa kukosekana majina fulani tu.

    “Je. Si nilikwambia mtoto wa mzee Mbonde hawezi kufaulu.” Alisema Mama mmoja huku akionekana wazi kufurahia matokeo hayo. “Hee, usiniambie shoga Halima naye kafeli.” Mama mwingine alidakia huku akionyesha mshangao. “kila siku mwanangu ana akili darasani, kiko wapi?” Aliendelea kuropoka yule mama . “Heeee. Afadhali maana hata maji tusingekunywa.” Alishabikia mama wa tatu ambaye muda wote alikuwa kimya.

    Beda Sanga alikuwa amesimama nyuma ya ubao ule. Jina lake lilikuwepo lakini hakuwa na furaha yoyote. Aliliangalia kwa mara ya pili jina lake. Beda Sanga, Shule atokayo Mzinga Kongowe Shule aendayo Benjamin Mkapa. Hakujua kama acheke au alie, akabaki ameganda hapo mpaka mtu mmoja alipomvuta shati.

    “Tupishe wenzako kama umefeli si usubiri matokeo ya pili?” akamtazama yule mtu bila kusema lolote. Akatoka na kukaa chini ya mwembe.

    Waliotoka kwa furaha aliwaona, waliohuzunika aliwaona hata wale waliolia aliwaona. Hakujua alistahili kuwa kundi gani katika makundi hayo. Alie, acheke au anune? Bado hakuwa na jibu ingawa alishaingia kwenye kundi la watu waliohuzunika. Kwanini asihuzunike? Michango ya shule ya msingi ilimshinda, shati la shule lilikuwa kuukuu ambalo limtofautisha na wenzake pale shuleni. Mara ngapi alirudishwa nyumbani kwa kuvaa kandambili? Kukosa hela ya muhogo na aisikrim kwake ilikuwa kama wimbo wa taifa. Amlilie nani? Mama yake mfagia barabara au baba yake ambaye alishatangulia kaburini? Dunia inamuadhibu kwa kosa gani? Akashindwa kuvumilia hatimaye machozi yakaanza kumtoka.

    Akainuka pale kwenye mwembe. Hakuna aliyejali wala kuthamini kilio chake, machozi yake yalienda bure kabisa. Haikuonekana thamani halisi ya machozi wala haikuonekana thamani ya kilio chake. Alilia utotoni mama yake akajua mwanangu ana njaa akampa ziwa, alidondosha machozi utotoni kwa kipawa alichopewa na Mungu mama yake akajua anaumwa tumbo akampeleka zahanati. Leo hii amemaliza darasa la saba bado kilio hakijaisha. Hakuna anayemuelewa au hakuna anayetaka kumuelewa. Nani yuko tayari kusikiliza kilio cha mtu mwingine. Labda ni huyo mama yake anayefanya kazi ya kufagia barabara huku akitumika kama ngao ya serikali ya ongezeko la ajira. Ajira? Ndio huo ndio mtaji halisi wa maskini, Maskini hahitaji pesa bali nguvu zake tu.

    Alitembea taratibu hatimaye akajikuta maeneo ya Mbagala rangi tatu. Hakupanga kwenda huko. Mawazo na simanzi ilimfanya ajikute akiwa eneo hilo lenye purukushani nyingi.

    “Aaa, vipi Beda.” Sauti ya mtu aliyekuwa mbele yake ilimshitua.

    “Safi Frank mambo vipi.”

    “Poa.” Alijibu yule kijana mwenye beseni la ndizi ambaye alikuwa hirimu yake.

    “Vipi ulienda kuangalia matokeo?”

    “Aaah. Achana na habari za matokeo bwana sitaki hata kusikia.”

    “Kwanini?”

    “Hii ndiyo kazi yangu nisome tena nataka nini?” Beda akatikisa kichwa bila kuongea lolote. Akaachana na kijana yule ambaye walisoma darasa moja.

    Hakufika mbali akashikwa bega na kijana mwingine ambaye alikuwa na furaha kubwa

    “Bedaaa.” Yule mvulana alimshika Beda kwa nguvu huku akimtikisa.

    “Shule yetu mimi na wewe tu ndo’ tunaenda Benjamin.” Akajilazimisha kucheka ili kuficha huzuni aliyokuwa nayo. Hakuongea lolote, Angethubutu kuongea tu angebainika. Hata hivyo aliamua kuachana na rafiki huyo mwenye furaha kwani aliogopa angeangusha machozi.

    Akaenda hadi barabarani. Huko akamkuta mama yake akiwa amevaa ovaroli nyekundu na kofia ya bluu. Puani alikuwa ameweka kifuniko kama vile vya wavuvi wa samaki. Huyu hakuzuia maji kama wale wavuvi. Alikuwa anazuia vumbi ya barabarani. Aliendelea kufagia bila ya kumuona mwanae ambaye alimsimamia nyuma huku akimtazama kwa huzuni

    “Mama Beda, mwanao humuoni?” Aliuliza mama mtu mzima ambaye Beda angeweza kumwita bibi.

    “Yuko wapi?” Aliuliza mama Beda huku akijua wazi kuwa anafanyiwa shere. Akageuka. Akamwona mwanawe akiwa amesimama nyuma yake. Hakuwa na furaha. Alimjua vema mwanae, hakuwa katika hali ya kawaida.

    “Vipi Beda unasemaje mwanangu.” Aliongea mama yake kwa sauti ya upole na kubembeleza.

    “Matokeo mama .”

    “Uhuu.” Alishusha pumzi ndefu mama Beda huku akimshika mwanae mkono.

    “Haya niambie matokeo yamekuwaje?”

    “Nimechaguliwa kujiunga na shule ya sekondari Benjamin Mkapa”. Lilikuwa ni pigo lingine kwa mama Beda. Akajishika kiuno huku akiachia lile fagio aliloshika mkononi lianguke.

    “Mh. Makubwa. Yunifomu, Vifaa vya masomo, ada na nauli juu….” Aliongea peke yake .

    “Vipi Mama Sanga mbona hivyo.” Aliuliza yule mama mtu mzima.

    “Mwenzangu makubwa madogo yana nafuu, eti Beda kafaulu.”

    “Pole Mwaya, majukumu ndo’ yanaanza hivyo.” Aliongeza yule bibi.

    “Mwenzangu ndo nimechanganyikiwa hapa hata sijui niingilie wapi.”. Maneno ya mama yake yakaanza kumliza tena Beda. Huyu ndiye mtu pekee ambaye angeweza kumsaidia. “Tangulia nyumbani nakuja.” Alisikika mama Beda kwa sauti ya kukata tamaa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog