Search This Blog

Sunday 19 June 2022

AJIRA TOKA KUZIMU - 5

 





    Simulizi : Ajira Kutoka Kuzimu

    Sehemu Ya Tano (5)



     Mamamia akamnyanyua, na hapo akina Brenda na Beatrce wakawasili. Brenda akamweleza Tembo kwa kifupi kisa na mkasa na nini hatma yao!!

    Tembo akapagawa!!!

    Hofu ya kifo ikamwingia na yeye…

    Upesi zikachukuliwa pikipiki na kuelekea nyumba aliyokuwa akiishi Tembo zamani, nyumba ambayo Tuntu alimpatia ajira kewa mara ya kwanza. Kwenye kile kitanda alitakiwa akatoe vitu ambavyo vcinatakiwa kuchomwa moto, likiwemo na lile godoro alilokuwa amelilalia siku hiyo.

    Tembo akaongoza msafara… wakaifikia nyumba yakiwa yamebaki masaa mawili tu Tuntu ainuke tenma na kuwapa adhabu kuu.

    “ANAYEISHI HUMU AMEFIWA AMESAFIRI KWENDA MSIBANI….” Wakapewa jibu hilo na mpangaji mwingine.

    Wote kwa pamoja wakachoka, na lilikuwa limebaki saa moja na dakika kadhaa!!!



    *****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    SIMU ya Athumani au maarufu kama Bichwa haikuwa inapatikana. Muda ulizidi kwenda na mganga akizidi kupiga simu kuwa hapatakuwa na namna ya kumkwepa Tuntu iwapo atainuka kabla godoro halijachomwa moto. Na makorokoro yaliyoko chini ya kitanda hayajaondolewa.

    Bichwa ndiye alikuwa mmiliki wa chumba kile baada ya Tembo kuhama. Na taarifa ilikuwa kwamba ameenda msibani kijijini kwao, simu haikuwa inapatikana. Tembo alitamani walau atokee jirani mmoja ambaye atamkumbuka kuwa aliwahi kuishi katika chumba kile lakini haikuwa hivyo. Kila mpangaji alikuwa mgeni machoni pake.

    Wasichana wakawa wanamtazama Tembo aweze kufanya maamuzi ya busara ili waweze kulikwepa janga lililopo mbele yao.

    “Kama vipi tuvunje!!” Tembo akatamka kwa sauti ya juu huku akiwa haonekani kujiamini hata kidogo. Mamamia akakubaliana na wazo la Tembo, lakini wakati huohuo mpangaji mmoja akatoka katika chumba chake. Alikuwa mama mtu mzima akiwa ameifunga kanga yake katika mtindo wa lubega.

    Macho yake makubwa yakawatazama akina Tembo, akalamba midomo yake kisha bila kutoa salamu yoyote akaanza kuporomosha maswali na kashfa hata asiwape nafasi moja ya kujibu.

    Lafudhi yake pekee ilitosha kumtambulisha kuwa alikuwa mzaramo. Kama hiyo haitoshi mama huyo alipaza sauti juu akamuita mwenzake kwa jina la mama Zulfa.

    Huyu sasa alikuwa kiboko zaidi yake, alidandia treni kwa mbele lakini moto wake ulikuwa wa ajabu.

    “Kione kifupiii eti nyooo tuvunje kama vipi, mi nimekisikia tu nikawa nangoja nini kitafuata, uvunje mlango kwa misingi gani. Kama mnadaiana ni nyie hukohuko, Athumani katukabidhi chumba chake kikiwa kimefungwa na atatkikuta hivihivi kikiwa kimefungwa, ona na kile kingine kimepauka miguu kinaunga mkono eti nyoo tuvunje, mwone manyonyo yake hovyooo, mijitu sijui ya wapi hii. Hata salamu haitoi. Ona litumbo lake, tena mtupishege msije kuwa mnataka kuzalia katika hiko chumba cha Athumani wa watu…..” mama mtu mzima alizidi kuropoka na hapo yule kiboko yao akampokea sasa.

    “…ona mimacho yake imerendemka kwa husda mnazotaka kuleta kwa Athumani wa watu. Mbona hamkuja alipokuwa hapa, mmetegea ametoweka nd’o vitumbo mbele, na kianaumne chenu lisuruali linazidi mwili. Mwone shati lake kama kaja mjini na lifti za magari ya mkaa vile mweusii, likipara ka tako la mtoto mdogo vibaka wakubwa nyie….” Yule dada asiye na haya huku akipoandisha macho na kushusha aliwapayukia akina Tembo.

    Tembo, Brenda na Beatrice walibaki kuduwaa wasijue na kufanya, lakini Mamamia alishavurugika kichwani. Na yale matusi yakamchanganya zaidi, akachomoka upesi akamvamia yule dada aliyedandia treni kwa mbele. Akamdaka vyema shingo yake.

    Tembo akabaki kushuhudia timbwili. Yule mama mtu mzima akajisogeza aweze kuingilia, Mamamia akamuona… akamdaka ile kanga yake upesi akaivuta ghafla.

    Ebwana eeh!! Tuliokuwepo nd’o tulifaidi zaidi, wewe msomaji endelea kupatia picha katika maandishi.

    Shanga kama nane katika kiuno cha yule mama zikaonekana, akashindwa aidha ayazibe manyonyo yake ama azibe huko chini. Akimbie ndani ama aendelee kusimama.

    Mamamia akaendelea kutoa kipigo kwa dada mvamia treni kwa mbele. Kilikuwa kipigo cha kimyakimya lakini kitakatifu.

    Muda ulizidi kwenda kasi, ugomvi nao ukachukua dakika zaidi.

    Mamamia alikuwa na wazo kichwani mwake, wazo hili lilikuja wakati anapigana na yule mwanadada. Akajaribu bahati yake ya mwisho kabisa kama kweli aliwazalo litafanya kazi.

    Upesi akamuachia yule dada pale chini, akamvamia yule mama mwenye mwili mkubwa na shanga zake kiunoni.

    Aliamini kabisa kuwa yule mama akiwa na timamu zake hawezi kummudu, hivyo akiwa yu uchi hajielewi elewi nd’o ilikuwa nafasi ya kipekee.

    Mamamia akamrukia na kumsukumia katika mlango wa chumba cha Athumani bichwa.

    Kama vile ameyaona yaliyo mbele yake, ikawa vile. Mlango wa nyumba ya uswahili ukaporomoka kwa uzito wa yule mama kibonge.

    Zilikuwa zimebaki dakika takribani dakika kumi na tano mambo yaharibike.

    Baada ya kuangukia mle ndani mlango ukiwa umevunjika ndipo likazuka balaa jingine la mwaka.

    Chumba kile kilichofungwa kwa kufuli kabisa, ndani yake pakitegemewa kuwa tupu. Haikuwa hivyo!! Kitu kikakurupuka kisha zikasikika kelele kuu za kiume.

    “Mamaaaaaaa….”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Si Mamamia wala yule mama kibonge wa kuwa uchi aliyekuwa jasiri katika hili. Kila mmoja akapiga mayowe, lakini aliyeogopa zaidi alikuwa mama kibonge. Kwani alikuwa anatazamana ana kwa ana na Athumani Bichwa ambaye anasadikika kuwa amefiwa na ameenda msibani.

    Kwa hiyo moja kwa moja mama kibonge akaamini kuwa ule ni mzimu wa Athumani, tena mzimu wenyewe ulikuwa umevaa chupi tu.

    Mama kibonge akazirai pale pale.

    Athumani bichwa yeye akawa ameduwaa hata asikumbuke kuwa yupo na kichupi tu.

    Mamamia alivyotoka mbio, akina Brenda nao wakataka kuunganisha naye lakini Tembo akawahi kumdaka mkono.

    “Tembo kuna mzimu humo…. Mzimu una chupi tu….” Mamamia akapayuka, mashuhuda wengine waliokuwa pale kushuhudia ugomvi ule wakavutiwa na maelezo yale, wakaanza kujisogeza pale katika kile chumba hata yule dada aliyepewa kipigo na Mamamia naye akasogea jirani. Wakati huu akiwa mpole sana.

    Wengi wao waliogopa kuingia mle ndani kutokana na kusikia habari za mzimu wa Bichwa ndani ya chumba chake. Lakini Tembo na wenzake walilazimika kuingia kwa sababu walihitaji sana kutoa makorokoro chini ya kitanda ili yasije kuwakuta mabaya mzimu wa Tuntu ukiamka tena.

    Tembo na akina Mamamia wote wakaingia, yule dada mnyonge wa Mamamia naye akaunga tela akatazame huo mzimu pia amtazame na shoga yake ambaye alikuwa amepoteza fahamu.

    Hakujua kama anajiingiza katika mkumbo asioujua.

    “Bichwa…..” Tembo akamuita jamaa aliyekuwa ameduwaa na kichupi. Athumani hakugeuka alibaki kuwa ameangalia chini tu huku akiwa ameganda kama sanamu.

    Upepo mkali ulivuma kupitia madirishani, ilikuwa ni kama dalili ya mvua. Wasshabiki walikuwa wameongezeka nje ya mlango lakini wakihofia kuingia ndani ya kile chumba. Hadi pale mjumbe wa nyumba kumi kumi alipoingia mle ndani kujua kulikoni.

    Hata yeye alikuwa ameingia wakati mbaya sana. Ni bora hata asingefika kabisa.

    Mvua kubwa ikaanza kunyesha….. mvua iliyodumu kwa dakika takribani kumi na tano tu kisha ikakoma.

    “Wewe Bichwa imekuwaje upo ndani ya chumba hiki na umefungiwa kwa nje?” mjumbe akamuhoji Bichwa….. safari hii Bichwa alikuwa amevaa nguo zake huku akiwatoa hofu kuwa yeye sio mzimu bali kuna madeni alikuwa anayakwepa nd’o kisa cha kujifungia ndani kwa mtindo ule. Akamtaja na aliyemfungia kuwa ni rafiki yake.

    Zile kelele za umati hazikusikika tena. Mjumbe akaamini kuwa mvua ile itakluwa imewakimbiza pale. Mama kibonge naye alikuwa amezinduka, hivyo ndani ya chumba kile wakawepo watu nane. Wanaume watatu na wanawake watano.

    “Mi naomba nikapumzike jamani…..” Mama kibonge akaomba, mjumbe akawasihi kuwa hakuna ambaye anatoweka pale hadi wajue namna ya kuukarabati mlango wa Athumani.

    Wakati huo zilishapita dakika zaidi ya arobaini tangu ule muda walioungoja utimie na haukutimia. Brenda akahisi yule mganga ni mwongo kabisa aliyewaingiza katika aibu kuu. Akatamani kumpigia simu amkaripie lakini akajipa muda zaidi mpaka atakapokuwa peke yake.

    “Nitaukarabati mimi..” Mamamia akamaliza mzozo. Hilo likapitishwa na kila mmoja akatakiwa kuondoka. Hapo ndipo lilipotokea la kutokea.

    Wanane hawa walipotoka nje ya kile chumba wakajikuta katika mji wasioufahamu, mji ulikuwa umechangamka sana kila mmoja na shughuli zake huku wakizungumza lugha waliyoijua wao tu. Vitu walivyokuwa wanauza hata havikueleweka eleweka, lakini walikuwa na furaha sana.

    Mjumbe akataka kurudi katika chumba cha Athumani Bichwa kwa uoga lakini akafadhaika kabisa.

    KILE CHUMBA HAKIKUWEPO TENA………badala yake akakutana na watu wakiwa wametingwa na biashara zao za bidhaa zisizofahamika.

    “Tuko wapi hapa eeeh!” Mjumbe akamuuliza Tembo ambaye alikuwa amekodoa macho na mdomo wake ukiwa wazi. Hakujibiwa!!

    “Tembooooo……we Munyama weweeee!!! Munyama mukubwa kamba fedha… baba lao hiloooo…” ikasikika sauti kwa mbali ikimwita Tembo kwa manjonjo makubwa.

    Tembo akaona hii nd’o nafasi ya kupata mwenyeji na kumuuliza hapo ni wapi na imekuwaje wapo hapo.

    Tembo akatilia maanani sauti ilipotokea….

    Naam! Akakutana na sura aliyokuwa anaifahamu vyema kabisa… hamu ya kumjua mwenyeji wake ikakoma. Akaanza kutetemeka wakati mwanadada yule mwenye tabasamu pana usoni akizidi kumsogelea.

    Alikuwa ni ASIA DIGITALI!!

    Mungu wangu tupo kuzimu!!! Tembo akajisemea, Brenda akamsikia.

    “Unathemaje Hathani…hapa kudhimu….. mama weee” Kithembe akapagawa, na hapo mkojo wa moto kabisa ukapenya katika chupi yake.



    “Karibu kwangu Tembo…..” Asia alizungumza huku akiwa anarembua macho yake. Mchomo wa wivu ukapenya katika moyo wa Brenda ila alipokumbuka kuwa yupo kuzimu hofu ikarejea. Lakini akakiri kuwa hakika alikuwa anampenda Tembo.

    Asia alimshika mkono Tembo na kuongozana naye hadi katika chumba kikubwa chenye uwazi sehemu kubwa na sehemu moja ikiwa na meza pamoja na viti. Tembo na wennzake wote wakaketi.

    “Wanadamu wapumbavu sana ninyi….. pumbavu kabisa nasema.” Asia alikuwa kama anayezungumza peke yake!! Hakuna aliyemjibu wote walikuwa wanatetemeka.

    “Ooooh!! Halafu mimi naye nasahau kabisa kuwa ninyi ni wageni wangu hata maji sijawakaribisha…. Tembo waulize wenzako kinywaji gani wanapendelea kwanza. Au ngoja… kila mmoja ataje kinywaji anachopendelea…. Ila zisiwe pombe tu maana hapa haziruhusiwi kabisa.” Asia akazungusha macho yake kwa wageni wake.

    “Mama Ashura….” Akaita, yule mama mwenye shanga kiunoni akaduwaa Asia amemjuaje. Asia hakujali akamalizia, “Unatumia kinywaji gani…”

    “Chochote tu mama yangu!!” akajibu kinyonge huku akiifinyafinya mikono yake.

    “Na wengine mliobakia…” akahoji. Wote wakatoa jibu kama la mama Ashura kasoro Brenda ambaye alileta kizaazaa.

    “Mi thinywi kitu….”

    “Unasema….” Asia akamuuliza kwa sauti ya upole.

    “Thinywi chochote.. “

    “Kwanini haunywi..”

    “Thjithkii tu….”

    Asia akatulia huku akimtafakari Brenda na ile ongea yake.

    “Thjithkii kunywa chochote..” Kamuigiza anavyoongea huku akiwa ameibana pua yake.

    Asia akaondoka huku akizidi kusikitika na kusema ‘wanadamu…wanadamu…’

    “Tembo huyu ni nani?” hatimaye Mamamia alimuuliza, Tembo akajikohoza kidogo kisha akamjibu kuwa anaitwa Asia. Jina hilo lilikuwa geni kwa Mamamia. Akataka kuuliza zaidi lakini akamwona Asia akitembea kwa maringo na nyuma yake wakifuata watu wanne na sahani kubwa.

    Wakalitua katika meza… harufu isiyoeleweka ikatawala eneo lile.

    Asia akatabasamu kisha akaunyanyua uso wake na kuwatazama wageni wake zamu kwa zamu. Walikuwa wameduwaa tu, labda walikuwa wanaishangaa ile sahani kwa jinsi ilivyokuwa kubwa.

    “Funua!!... wewe hapo nd’o utafunua na utawapakulia wenzako chakula” aliamrisha Asia kisha akamnyanyua Brenda kwa mkono mmoja akasimama wima, akamtanguliza mikono yake ikashika ule mfuniko. Asia akamwamuru afunue!!

    Ebwana eeh! Tembo akaruka kule, Mamamia huko, Brenda huku na wale wageni wengine kila mmoja akajitetea kivyake kwa mayowe makubwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “He! Sitaki kuamini yaani kumbe waoga hivyo… kweli nyie hamna njaa kabisa. sasa nini cha kuwaogopesha hapa hebu acheni ujinga njooni mezani jamani….” Asia ambaye kwa mara ya kwanza alizama katika kicheko kikubwa sana hatimaye alizungumza.

    Hakika kila mmoja alikuwa na haki ya kupagawa, kwenye ile sahani kubwa ya maajabu alikuwa amelala yule mganga wa jadi ambaye alifanya jitihada za kutaka kumtokomeza Tuntufye Kanyenye kwa kumtoa kafara Asia Digitali.

    Bora ungekuwa ni mwili wenye uhai….. huu haukuwa na uhai na ulikuwa umetapakaa damu haswa. Brenda akawa analia kama mtoto mdogo!!

    “Wanadamu wapumbavu sana nyie, ona sasa mmenikasirisha bure tu mimi.” Asia alilalama kama hafurahii kinachoenda kutokea na kinachoendelea kutokea.

    Kisha ghafla akachomoa upanga unaowaka kwa makali yake. Sasa hakuwa katika kucheka tena.

    “Mnaupenda utajiri wa bure bure bila kujua namna ya kuuheshimu pumbavu nyie…” Asia akabwata kisha bila mtu yeyote kutarajia aliruka juu na kutua juu ya mwili wa yule mama kibonge.

    “kiherehere chako kuja pasipokuhusu kimekuponza…” alisema hayo kisha akauzungusha ule upanga mara moja kwa nguvu ya ajabu.

    Mkono mmoja ukachomoka. Mama akapoteza fahamu!! Damu ikaruka juu kama bomba lililo pasuka.

    Brenda aliyekuwa jirani na yule mama akapiga mayowe makubwa huku Mamamia yeye akiuziba mdomo wake.

    “Hassan Tembo…….. naitwa Tuntufye Kanyenye, Tuntu. Nipo hapa kukufanya uchukie uhai wako, nipo hapa kukufanya uchukiwe na hao uliowapatia ajira, watakuchukia sana na watakutesa sana lakini amini kuwa hautakufa kirahisi. Na kama ukifa basi nitakufuata hukohuko utakapoenda pumbavu wewe….. halafu na wewe hapo” akamgeukia Brenda, “Yule mpumbavu aliyekupeleka kwa huyo mganga mkashirikiana kutaka kuniangamiza mtasaidiana naye kujuta. Nitakung’oa mikono, miguu na hivyo vimatiti vyako kifuani….shenzi kabisa!!” uso wa Asia ulikuwa umeiva haswa wakati anatoa karipio hili, panga linalochuruzika damu likiwa mikononi mwake. Hakuwa katika masihara tena!!

    Hapa ndipo Tembo akatambua kuwa huyu hakuwa Asia bali Tuntu katika mwili wa Asia. Kifo chake akakiona kipo jirani kabisa kufika.

    Tembo naye akajikojolea!!

    Kwa mkono mmoja, Asia akaushika mguu wa yule mama aliyekatwa mkono. Akaanza kuuburuta kuelekea katika pori dogo mbele yake.

    Wakabakia viumbe saba wanaotetemeka ajabu!!

    Pakiwa kimya hakuna hata mmoja anayemsemesha mwenzake!!

    Alichoahidi Tuntu katika mwili wa Asia kikaanza kutimia.

    Mateso bila chuki!!

    Yule mganga ambaye alionekana kuwa amekufa tayari alinyanyuka kutoka katika ile sahani kubwa, mwili wake ukiwa unachuruzika damu.

    “Brenda we Brenda wewe…” mganga akamuita Brenda huku akijiweka sawa katika ile sahani.

    Brenda akaanza kurudi kinyumenyume mara ajikwae aanguke anasimama tena. Wengineo walikuwa wanagugumia tu kwa hofu ya maajabu yake.

    Mwili ule ukashuka na kuanza kutambaa ukimfuata Brenda.

    Mamamia akaiona hatari ya mdogo wake kufa ilikuwa karibu sana.

    Akaangaza huku na kule akaokota jiwe ili aweze kumbamiza nalo yule kiumbe.

    “Mamamiaaaa tupa tupa hichooo…” Tembo akapiga mayowe Mamamia akaduwaa, na kutazama alichokuwa amebeba.

    Kilikuwa kichwa cha mtu!! Kilichofuata hapo ulikuwa mtafutano kila mmoja anakimbia kuelekea anapojua.

    Mwishowe wakajikuta mbele ya Asia Digitali.

    “Huo ni mwanzo nilikuwa nawafanyia pashapasha…. Kumbe kukimbia mnajua vizuri kabisa…….”



    Asia alitoweka akiwaacha akina Tembo katika sintofahamu ya hali ya juu.

    Alikuwa ni Mamamia aliyeunyanyua mdomo wake na kuanza kumlaumu Tembo moja kwa moja, kisha Brenda na Beatrice wakaungana katika kulaumu.

    Tembo alitamani sana kuwaeleza kuwa hakuna alilokuwa nafahamu hadi wakati ule lakini wote walikuwa na hasira kali katu asingeweza kuwabadili.



    Ile hali ya wenzake kuwa na hasira ilimsababisha Tembo awe kama ametengwa kila mmoja akimuona kuwa ni adui yao. Na wengine wakafikia hatua ya kusema huenda yeye na tuntu lao ni moja katika mpango huo.

    Hali ile ya kutengwa ikampelekea Tembo kujikuta akiunda urafiki na kiumbe aliyejiita Maziku. Huyu ndioye kiumbe peke waliyemkuta huko walipoaminishwa kuwa ni kuzimu na mtu aliyeitwa Tuntufye Kanyenye.

    Hali hii ilizidisha chuki kwa wenzake ambao walizidi kuamini kuwa Tembo hayupo katika suluba ya nafsi kama wanayoipata wao.



    LAKINI ni Maziku huyu huyu ambaye badala ya kuwaacha wageni hawa wa kuzimu wapigwe njaa na kubaki na uchaguzi mmoja tu wa kula nyama ya watu na damu. Aliwasaidia kupata majani majani japo yalikuwa machungu sana walilazimika kula hivyohovyo kuliko nyama za watu.

    “Mwenyekiti atawaua mmoja baada ya mwingine” Maziku ambaye hakuwa amewahi kuzungumza hata siku moja alimweleza Tembo.

    Tembo akashtushwa na kauli ya Maziku na ajabu zaidi ule uwezo wake wa kuzungumza ambao hakuwa akiujua.

    “Unashangaa kuwa nazungumza… mimi sikukatwa ulimi mdogo wangu!! Nilikuwa mtiifu sana baada ya kugundua sina la kufanya.”

    “Nini sasa kilikuleta huku…”

    “Tamaa, hata nyie najua ni tamaa tu imewasukumia huku hakuna jingine…” Maziku alijibu.

    “Kwa hiyo sisi tunakufa!!” Tembo alihoji na kabla Maziku hajajibu aliuliza tena, “Na hapa ni wapi tulipo…”

    “Hapa ni kuzimu…. Hapa hamtoki nd’o mmeshafika.” Maziku alijibu kwa utulivu, kisha akamalizia, “Jamaa ana hasira sana na wewe… ujue siku anakuchagua kukupa kazi tulikuwa wote… akakuamini sana lakini umemwangusha sana… atakuua yule..”

    Tembo alipagawa mno kusikia kuna habari za kukatwa ulimi na kuuwawa. Na mbaya zaidi hapakuwa na namna yoyote ya kutoka kule kuzimu.

    :Maziku… niombee msamaha.”

    “Ukithubutu kumwomba msamaha nd’o umempa ruhusa ya kukuua, Tuntu akusamehe. Jambo la msingi Tembo….” Akasita Maziku akamsogelea Tembo sikioni, “Unatakiwa kupambana naye, anakuogopa sasa hivi maana ulimzika wewe na ilibaki kidogo utukomboe wote, Tembo wewe ni shujaa sana. Pambana utukomboe…’

    Tembo alifadhaika baada ya mtu aliyetegemea kuwa atamsaidia na yeye akadai kuwa Tembo nd’o mtu wa kuwasaidia wote.

    “Hata jamaa zako wanaokuchukia wote watakupenda ukitukomboa…” alizidisha makali ya motisha ile. Tembo akabaki kujishangaa, ataanza vipi kupambana na mtu mwenye uwezo mkubwa kama Tuntu, ataanza vipi kufanya ukombozi.

    Ni kama Maziku alijua ni kitu gani Tembo anawaza. Akaongezea kauli nyingine iliyoamsha akili ya Tembo.

    “Sikia Tembo wenzako sisi hapa ni kama misukule tu, wewe mwenzetu unazo nguvu. Ukifanya mapenzi tu na mwanamke unakuwa na nguvu kama yeye japo kwa muda.”

    Tembo akainama chini akakumbuka namna alivyofanikiwa kurejea katika hali yake japo kwa muda mfupi baada ya kuingiliana na Asia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Lakini kama alivyokuonya hakuna kurudia kumwingilia msichana mmoja mara mbili….. na hii utaifanya mchana kama huu maana nd’o muda ambao anakuwa ameenda kuzurura duniani kusaka watu wake.” Maziku alimaliza kisha akatoweka akimuacvhya Tembo katika mtihani wa namna yake.

    Kuingiliana na msichana kimapenzi halikuwa tatizo, shida ilikuwa kurudia mara mbili. Yaani kwa kuwa aliwahi kulala na Brenda na Mamamia, atakiwi tena kugusa hapo. Hivyo waliobaki ni yule mama mtu mzima aliyekatwa mkono ama yule mwanadada mcharuko naliyedundwa na Mamamia.

    Namuanzaje sasa!!! Tembo alijiuliza huku akivutavuta majani yaliyokuwa miguuni kwake.

    “Ingekuwa usiku mi ningemlazimisha kwani nini?” akajiuliza kwa sauti ya juu kidogo.

    “Kaka!” sauti ya kike ikamtoa katika mawazo mazito aliyokuwanayo. Akageuka kutazama akakutanisha macho na huyu mwanamke mcharuko asili ya uzaramoni aliyedundwa na Mamamia walipokuwa ulimwenguni.

    Tembo akabaki kuduwaa, yule binti akaketi jirani naye.

    “Yule mkaka anayetupatia chakula amesema unaniita…”

    Maziku, Maziku keshaanza wakati sijajiandaa!!! Tembo alilalamika huku akijiweka vyema na kujivika uanaume wake tena akiamua kuamini maneno ya maziku kuwa ni sahihi na hii ilikuwa nafasi ya dhahabu.

    “Mi namweleza kama ilivyo aaargh!!” akaghafirika Tembo kisha akaanza kumweleza yule mwanamke juu ya harakati zao za kujikomboa. Akamweleza zaidi hadi kufikia suala la yeye kutafuta nguvu za kukabiliana na yule Tuntu wa Kanyenye.

    “Kama haupo tayari basi tungoje atuue kwa mateso ya kutukata kiungo kimoja kimoja hadi tunakata roho.. si umeona alivyomkata yule mama pale…” Tembo alikazia baada ya yule mwanamke kuonekana akipinga kabisa ile hali.

    Kusikia juu ya kifo cha mateso yule dada akauliza swali, “Sasa tunafanyia wapi…. Mchana huu…..” swali hilo likamfanya Tembo apepese macho kisha akaenda mahali alipokuwa Maziku. Akamuuliza juu ya hilo.

    Maziku kwa shangwe kuu akamchukua Tembo na yule dada asiyemjua hata jina hadi katika kipori kidogo akawaacha huko.

    Upesi upesi na kwa tahadhari kubwa Tembo akataka kumvamia yule dada… na hapo likatokea tukio lililomfadhaisha Tembo kupindukia.

    Tembo alikuwa hajiwezi tena, hakupata hamu ya tendon a hata maungo yake hayakuweza kufanya kazi.

    Tembo akabaki kulia kama mtoto mdogo.

    Yule dada akalazimika kuvaa nguo zake na kumwacha Tembo kichakani, Maziku akaenda akiwa na furaha akiamini Tembo amefanya mambo tayari. Akamkuta akiwa analia.

    “Maziku…. Siwezi kufanya lolote tena…..” akataka kuzungumza zaidi upepo mkali ukavuma.

    “Mwenyekiti amekuja aisee…..” Tuntu akamkurupua Tembo….. lakini9 kabla hawajapiga hatua yoyote Tuntu ndani ya mwili wa Asia digitali alikuwa mbele yao.

    Kama kawaida alikuwa anatabasamu.

    “Nilivyokuacha uongee nadhani unaongea hadi yasiyokuhusu sasa…. Haya sema mengine ya mwisho, mwambie upesi maana unaungana na wenzako katika ulimwengu mbaya wa wasiooongea… na wewe Tembo usidhani kuwa nitakukata ulimi wewe. Utajikata mwenyewe kwa meno yako.

    “Tembo.. nipiganie naenda kukatwa ulimi…. Nisaidie Tembo.” Maziku huku akiwa anatetemeka kabisa na macho ameyakodoa alimweleza Tembo.

    Tuntu alipiga hatua nne kubwa akamfikia Maziku na kumnyanyua juu juu. Kisha akachomoa kisu kidogo na kikali katika upande wa nguo yake.

    Tembo akafadhaika na kutaka kujizuia kushuhudia mwanadamu akikatwa ulimi.

    “naanza na huyu halafu ni wewe utakayefuata…. Nakukata masikio yako yote mawili na ninakuahidi Tembo kuwa mimi ni jeuri zaidi yako. Utakula sikio lako moja baada ya jingine!!” Tuntu alifoka.

    Ubaridi ukapenya katika mwili wa Tembo akasisimka masikio!!!

    Maziku akanyanyuliwa juu na kisu kikawekwa tayari!!!



    Kwa mara ya kwanza tangu afike eneo hilo asilolijua na akiaminishwa kuwa ni kuzimu Tembo akakumbuka kuwa hajawahi kuomba msaada wowote ule kwa mtu asiyeonekana bali kila siku huwategemea wanadamu na kama ilivyoandikwa basi hujikuta wanamwangusha.

    Tembo akafumba macho kwa sekundfe kadhaa.

    “Allah! Mbele zako hakuna mchafu wala msafi linapokuja suala la dua. Nimekukosea sana bila kujua kwa kipindi kirefu. Nigeuze shujaa sasa na nipate kuusimulia ulimwengu.” Alipomaliza hapo bila kungoja muujiza wa macho kwa macho alisimama wima.

    Akaenda kwa kasi na kumvamia Tuntu ambaye alikuwa ameufungua mdomo wa Maziku kwa ajili ya kuukata ulimi wake.

    Akamzaba kibao kimoja bila uoga. Tuntu akamwachia Maziku huku akipigwa na butwaa.

    Tembo akamuangalia Tuntu kama anayeangaliana na msichana mwingine tu. Akamuona kuwa ni Asia na hana uwezo wa kumfanya lolote jambo, japo alimzidi urefu.

    Mara Tuntu akauchomoa upanga mkubwa, Tembo akaanza kutetemeka lakini akajiaminisha kuwa ni heri kufa akiwa amejaribu kumtegemea Mungu kuliko fedheha waliyotarajia kuipata ikiambatana na mateso makali. Kabla Asia hajamfikia Tembo, Maziku naye alijirusha akamkwaa miguuu yake akatua chini kama gunia la mahindi.

    Tembo akamsogelea na kumpa amri moja kuu iliyomstaajabisha. Wala Tembo hakujua ametoa wapi ujasiri wa kuitamka.

    “Una machaguo mawili, aidha kutuacha huru tuondoke ama Mungu wetu atakuangamiza kwa mateso makali….”

    Tuntu hakujibu lolote alibaki ametulia tuli pale pale.

    Tembo alianza kumtikisa, hakuna dalili yoyote ya kuinuka. Wakasaidia na Maziku lakini bado hali ilikuwa vilevile.

    “Amekufa…..” Maziku alimweleza Tembo. Jambo ambalo Tembo hakuamini linawezekana kuwa jepesi kiasi kile.

    Baada ya dakika kumi na tano likazuka vurumai jingine.

    Maziku ndiye aliyeanza kukumbana na dhahama hiyo. Akaanza kupigwa vibao bila kumwona mtu anayempiga. Tembo na yeye akiwa ameduwaa tu akashtukia Maziku akinyanyuliwa juu na kitu kisichoonekana na kisha akaachiwa na kutua chini bila kuhitaji ushahidi wa ziada iwapo amekufa ama la maana alitua juu ya jiwe na kupasuka pasuka.

    Mamamia akasikia akipiga kelele baada ya sekunde kadhaa. Tembo akatimua mbio kuelekea zinapotokea kelele, kama ilivyokuwa kwa Maziku. Mamamia alikuwa akijaribu kujikinga uso wake mara mgongo wake huku akilia.

    “Nipe macho eeh Mungu unayetupigania sasa…..” aliomba Tembo kwa imani huku akitambua hayupo wa kuwasaidia zaidi ya Mungu aliyewaumba.

    Muujiza!! Ndo jambo pekee Tembo aliloweza kusema. Kabla hajachukua hatua.

    Aliweza kumuona Tuntu, safari hii hakuwa tena katika mwili wa Adia. Huyu alikuwa yule Tuntu aliyemjia ndotoni.

    Upesi wakati anamkaba Mamamia, na yeye akajikongoja upesi kuelekea alipokuwa.

    Akafika na kumnasa kibao kikali cha mgongoni.

    Tuntu akaduwaa kuwa Tembo alikuwa ameweza kumuona Tembo.

    “Kila mmoja asali kwa imani yake, la sivyo tunakufa wote. Kila mmoja aombe kwa juhudu huku akiamini…” Tembo akawahusia wenzake kwa kuhamasisha. Wakati huo alikuwa akikabiliana ana kwa ana na Tuntu.

    Nguvu za Tuntu zilikuwa kubwa lakini aliweza kuhimili vishindo. Wenzake wakaanza kusali wajuavyo wengine kwa sauti na wengine kimya kimya.

    Amakweli Mungu wetu ana nguvu na akiitwa huitika.

    Tuntu alilainika na kuishiwa nguvu, wale aliowakata ulimi wote wakarejewa na ufahamu wao zaidi na hawakumuogopa. Wakamvamia wakiwa na mapanga na marungu mikononi ambayo huwa wanayatumia kufanyia shughuli za kulima mashamba ya wachawi duniani.

    Wote wakiwa wanaunguruma kwa hasira walimfikia Tuntu aliyekuwa anakabiliana na Tembo.

    Kilichotokea pale kilikuwa kipigo kitakatifu.

    Oparesheni, ondoa shetani.

    Tuntu alijaribu kila namna akawaita miungu wake lakini hawakusimama mbele ya jina kuu kupita yote duniani na mbinguni.

    Mungu!!

    Alipigwa hadi akalainika, Tembo akarejea kuwa Munyama mukubwa lakini katika namna nyingine. Safari hii katika ulimwengu wa kishujaa kweli.

    “Haya imetosha!!” akaamrisha… wote wakaacha…. Akamsogelea Tuntu pale chini. Akamtazama na kugundua kuwa alikuwa katika hatua za mwisho kabisa za kukata roho.

    “Tembo….. nisamehe mjukuu wangu…” alizungumza.

    “Wahi duniani… wahi uwaambie watu ukweli…. Wahi waujue ukweli..” alisisitoza yule wa kuitwa Tuntu.. Tembo akabaki katika mshangao tu. Yule mtu hakuzungumza tena chochote. Akatulia tuli.

    “Tembo…. Tembo… we Hathani, hapa mbona ni Chamandhi jamani.. uwanja wa timu ya Adham ule pale…..” Brenda ambaye alikuwa kimya na mwenye uoga kwa muda mrefu alizungumza huku akistaajabu. Wenzake wote wakageuka wote wakabaki midomo wazi waliolijua eneo lile la Chamanzi.

    Hapakuwa kuzimu bali walifumbwa macho yao kishetani!!

    Kigiza kilianza kuingia wakati Tembo akiongoza kundi la watu zaidi ya sitini kutoka katika mji wa giza.

    Tembo alikuwa shujaa wa kweli katika hili. Wale wasiweza kuzungumza baada ya kukatwa ndimi zao walibaki kutabasamu na kuunguruma tu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mama mwenye mkono mmoja hakuwa na maumivu tena lakini alikuwa akiugulia kuupoteza mkono wake, lakini hakujuta sana kwani ilikuwa heri kupoteza mkono wake kuliko uhai.

    “Tutalala kwa bibi yangu… anakaa maenmeo ya huku huku na akisha asubuhi tutajua nini cha kufanya….” Tembo jemedari alikuwa akiliongoza kundi, nani angeweza kumpinga.

    Wakatembea hadi katika nyumba kubwa iliyozungukwa na uzio wa miti ya miiba. Tembo akagonga hodi mara kadhaa mlinzi akafungua.

    Kwa jinsi alivyokuwa amechafuka mlinzi hakuweza kumtambua hadi alivyomulika na tochi.

    Tembo ana nywele kichwani tangu lini?? Mlinzi alijiuliza.

    “Na hawa akina nani?” Mlinzi akahoji.

    “Ni ndugu zangu hawa wote na watalala kwa bibi yangu…” alijibu. Mlinzi akasita akafunga geti kwanza kisha akaenda ndani kutoa maelezo hayo.

    Bibi akaruhusu Tembo afunguliwe!!

    Tembo na wafuasi wake wakaingia ndani.

    Wakangoja nje wakati Tembo aliingia ndani kwenda kukutana na maajabu ya mwaka.

    Bibi alikuwa ameketi kitandani na aliyekuwa amelala alisemekana kuwa ni mgonjwa!!

    “Ni babu yako…”

    “Babu? Babu gani tena mwingine zaidi. Babu yangu alikufa zamani..” Tembo alistaajabu. Bibi akashusha pumzi kidogo, akamtazama Tembo usoni kwa masikitiko kiasi.

    “Babu yako…..” bibi akashindwa kuendelea.

    Yule mgonjwa kitandani aliyekuwa amefunikwa shuka gubi gubi akazungumza.

    “Mwambie, mwambie tu usiogope……”

    Bibi akaduwaa kwani ni muda mrefu ulipita bila mgonjwa yule kuzungumza.

    “Babu yako hakufa, lakini alipewa cheo huko kwa wenzake.”

    “Wenzake gani sasa??” alihoji Tembo.

    “Wachawi!!”

    “Nini bibi??? Yaani unamaanisha kuwa babu ni mchawi?? Mbona balaa leo lanikumba mimi.” aliuliza huku akiwa wima.

    Kama aliyeshtuliwa kutoka usingizini, yule mgonjwa aliinuka kisha akajifunua shuka lake.

    “Naitwa TUNTUFYE KANYENYE!!!!”

    Tembo akaingiwa na ubaridi mkali kupindukia, akajihisi uoga kukutana na mtu ambaye anaamini alikutana naye kuzimu.

    Akaanza kutetemeka, lakini mzee yule akabaki kumwaga risala.

    Akaomba msamaha na mengineyo kisha kumwomba Tembvo aitangazie jamii nzima bila uoga wowote.

    “Nilijua umri wangu umeenda sana nikaambiwa nikabidhi mikoba yangu kwa mwana ukoo, nikakuchagua wewe. Lakini bahati mbaya ama nzuri umekuwa shujaa na umeshinda vita hii. Hakika si utawala mzuri kumtumikia shetani. Tazama leo nakufa huku nikiwa nahitaji kuishi. Amakweli mungu wa kweli ni Mungu wenu nyinyi aliyeisimamisha miungu yote iliyotaka kuwachinjia mbali. Mungu wenu ni Mungu mkuu na kama ningeipata nafasi ya kuishi hakika ningeinama na kumsujudia yeye.” Alizungumza kwa hisia kali huku akimtazama Tembo.

    Baada ya hapo hali ikawa mbaya, akalala na hakuamka tena.

    Akafa kwa amani baada ya kumfumbua macho Tembo kuwa ni yeye aliyetakiwa kurithi mikoba ya kuzimu.

    ****

    KIHITIMISHO!!!

    ILIKUWA kama babu alivyohitimisha Tembo alijiweka hadharani na kutangaza juu ya muujiza huo. Akamsifu Mungu kwa maajabu yake na nguvu zake za kipekee.

    Akajitolea kumtumikia katika ujana wake hadi uzee wake.

    Somo la Tembo likawafungua wengi wasiokuwa na imani. Likawajaza nguvu zaidi waliokata tamaa.

    Pesa alizozipata kwa njia ya kichawi sasa akazipata kihalali kabisa. katika ushuhuda wake zilichangwa milioni nyingi kwa ajili ya wale wahanga wa kukatwa ndimi zao. Wakapatiwa makazi.

    Tembo akabakia kuwa Munyama Mukubwa sio kwa ajili ya pesa tena bali kwa jinsi alivyoishinda AJIRA TOKA KUZIMU.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MWISHO





0 comments:

Post a Comment

Blog