IMEANDIKWA NA : RAYMOND MWALONGO
*********************************************************************************
Simulizi : Muuaji Aliyebakia
Sehemu Ya Kwanza (1)
Ilikuwa Ijumaa ya tarehe kumi mwezi Desemba ambayo hali yake ya hewa ilikuwa tulivu kabisa. Nyakati hizo za asubuhi mambo hayakuwa shwari katika nyumba ya mzee Kibudo ambayo watu kadhaa walikuwapo nje wakilia kwa huzuni juu ya kifo cha mzee huyo aliyeuawa na watu ambao hawakujulikana. Watu hao wa kijiji cha Magugu wilaya ya Babati mkoani Manyara waliungana na familia ya mzee huyo katika tatizo hilo la msiba. Maswali mengi yalikuwapo vichwani mwa watu juu ya mtu aliyefanya mauaji hayo kwa mzee huyo aliyekuwa mkarimu licha ya utajiri wake aliokuwa nao kijijini hapo. Jeshi la polisi lilifanya uchunguzi juu ya kifo cha mzee huyo na mwishoe familia yake ilihurusiwa kufanya mazishi wakati wahusika wa tukio hilo wakiendelea kupelelezwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hatimaye mzee Kibudo ambaye ilielezwa kuwa aliuawa kwa mapanga alizikwa, tukio hilo lilishuhudiwa na mkewe na watoto wake watatu pamoja na ndugu na jamaa waliofika msibani hapo. Mara baada ya msiba huo familia ya marehemu Kibondo ilikuwa ikisubiri maelezo yeyote kuhusiana na wauaji wa mzee huyo lakini hakuna taarifa zozote zilizopatikana kutoka jeshi la polisi. James Kibudo ambaye alikuwa mtoto wa mwisho wa marehemu ndiye pekee alifanikiwa kupata nafasi ya kusoma katika shule moja mkoani Arusha. Kaka yake mkubwa alikuwa akiwasaidia wazazi wake kazi za shamba na uchungaji wa ng’ombe vitu vilivyomfanya mzee Kibudo kuwa na uwezo kifedha kijijini hapo.
Baada ya msiba huo James aliondoka nyumbani kwao kurudi shuleni mara baada ya kuagana na familia yake akiwamo dada yake aliyetarajiwa kuolewa. Kichwani alikuwa na mawazo juu ya mtu aliyehusika na mauaji ya baba yake jambo lililomkosesha raha mara kadhaa. Alitamani jeshi la polisi lifanikishe kukamatwa kwa watu hao na sheria kali juu yao ichukuliwe. Katika nyakati tofauti aliwasiliana na familia yake kwa njia ya simu akiulizia jitihada zilizofanywa na jeshi la polisi lakini jibu lilibaki kuwa watuhumiwa wa mauaji hayo hawakupatikana.
Mwezi mmoja baadaye James akiwa amebakiwa na siku chache ili shule yao ifunge kwa ajili ya likizo fupi, alishtushwa na ujio wa mjomba yake shuleni kwao. Jambo lililompa hofu ni hali ya wazi aliyoionyesha iliyompa hisia za tatizo nyumbani kwao. Mjomba yake huyo hakumweleza kitu zaidi ya kumwambia kuwa ajiandae kwa ajili ya safari kuelekea kwao, baada ya kubisha kwa muda mfupi akitaka kujua sababu ya kufanya hivyo alikubali na kujiandaa. Safari ilianza kuelekea kwao, muda wote wa safari James alikuwa na mawazo akiwa haelewi jambo lililokuwa limetokea hali iliyopelekea aanze tena kumuuliza mjomba yake huyo. Baada ya kuona usumbufu ulizidi alimjibu kwa ufupi kuwa kulikuwa na matatizo nyumbani kwao hivyo uwepo wake ulihitajika.
Baada ya safari hiyo ya masaa kadhaa walifika kijijini kwao Magugu, walianza kutembea taratibu kuelekea nyumbani kwao muda wote alikuwa na hofu akiwa haelewi kilichokuwa kinaendelea. Hofu hiyo ilimzidi na kujikuta akianza kulia baada ya kuona kundi la watu wakiwa wamezunguka eneo la nyumba yao na kelele za vilio zikiendelea.Alijitahitidi kutembea lakini miguu yake ilimwishia nguvu na hatimaye alianguka chini kabla ya kusaidiwa na watu waliokuwapo eneo hilo la msiba. Alipelekwa mpaka ndani na kuwakuta ndugu zake kadhaa waliomtaka atulie na kujipa ujasiri kama mwanamme. Walianza kwa kumweleza kuwa familia yake yote ilikuwa imeuawa usiku wa siku hiyo. Jambo hilo lilimfanya James kulia kwa uchungu baada ya kuelewa yeye pekee ndiye alikuwa amebakia katika familia hiyo zaidi hakuelewa chanzo cha mauaji hayo yaliyofanywa.
Kama kawaida polisi walifanya uchunguzi wao juu ya tukio hilo na kuondoka na vielelezo wakiahidi kufanya upelelezi zaidi. Hatimaye miili ya wanafamilia hao waliouawa kwa kukatwa na mapanga ilizikwa kijijini hapo. James alijawa na mawazo juu ya muuaji wa familia hiyo na wazo la kuhakikisha muuaji anapatikana linamkaa zaidi kichwani mwake. Akili yake ilikuwa tayari kuua katika kulipiza kisasi kwa mtu yeyote ambaye angethibitika kuhusika na mauaji hayo. Wakati huo alikuwa kidato cha nne akiwa amebakiwa na miezi kadhaa ya kumaliza shule, baada ya likizo aliondoka akirudi shule akitarajia kupata taarifa za wauaji kutoka jeshi la polisi.
Mali za familia hiyo ya marehemu Kibudo zilianza kusimamiwa na mdogo wake ambaye hakubahatika kuwa na mtoto katika maisha yake. Zaidi alikuwa ni mtu mlevi ambaye pia hakuwahi kuoa. Alichaguliwa kusimamia mali hizo wakati James akisubiriwa amalize shule ili akabidhiwe, hiyo yote ilitokana na hofu waliyokuwa nayo ndugu wa familia hiyo ya kuuawa iwapo wangesimamia mali hizo. Ndugu wengi waliogopa hata kulala katika nyumba hiyo ya marehemu mzee Kibudo wakihofia kuuawa.
George Kibudo alisimamia mali hizo katika misingi mibovu kutokana na tabia yake ya ulevi aliyokuwa nayo. Baada ya miezi mitatu James alirudi kijijini hapo na kuungana na baba yake mdogo huyo kusimamia mali hizo akiwa ameshamaliza kidato cha nne. Tatizo lililomsumbua kichwani mwake lilihusiana na kutokamatwa kwa mtu aliyehusika na mauaji ya familia yake. Pia aliingiwa na hofu juu ya sababu ya mauaji hayo, lakini jambo lililokuwa kichwani mwake siku zote aliamini baba yake hakuwa na kosa lolote alilomfanyia mtu. Aliamua kuanza upelelezi wake kwa utulivu kumfuatilia mtu aliyehusika na mauaji hayo kwani aliamini alikuwapo kijijini hapo. Alianza tabia ya ulevi ambayo awali hakuwa nayo lengo likiwa ni kuwa karibu na watu ili kufanikisha upelelezi wake.
Baada ya kipindi kifupi alibaini baba yake alishawahi kufanya biashara ya pamoja na mzee mmoja aliyejulikana kwa jina la Samola miaka mingi iliyokuwa imepita. Katika biashara yao hiyo walimalizana kwa kufikishana mahakamani baada ya kushindana katika kugawana n`gombe walizokuwa nazo. Baada ya mzozo huo wa kugawana n`gombe kumalizwa na mahakama, baba yake hakuwa na uhusiano wa karibu na mzee huyo ambaye alifilisika miaka kadhaa baada ya kugawana kwao. Upelelezi huo uliompa shaka ndiyo ulimfanya James amweleze baba yake mdogo aliyeishi naye wakati huo ambaye alipinga kuhusishwa kwa mzee huyo katika mauaji hayo ya familia yao.
Waliendelea na shughuli zao za kila siku, wakati upelelezi wa James dhidi ya muuaji wa familia yake ukiendelea. Siku moja akiwa amelewa akirudi nyumbani kwao akitokea eneo lililouza pombe za kienyeji ikiwa yapata saa saba usiku, James alishtushwa na kelele zilizotoka nyumbani kwao za mtu aliyeonekana alikuwa akipigwa. Kutokana na hali ya kulewa aliyokuwa nayo hakuingiwa na hofu zaidi ya hasira zilizompanda akiamini kuna watu walikuwa wakifanya mauaji. Alichomoa panga lake aliloliweka kwenye koti ambalo siku zote alikuwa akitembea nalo akihofia usalama wake, alianza kukimbia kwa kasi akielekea nyumbani kwao huku akipiga kwa sauti ya juu kelele ambazo hazikueleweka.
Mara baada ya kuukaribia mlango wa nyumba yao, aliwaona watu wawili wakitoka kwa kasi, mmoja akiwa na shoka na mwingine akiwa na panga. Alisimama pembeni kidogo na mlango wao akiwa anatafakari afanye nini, punde kidogo alitoka mtu mwingine kwa kasi ndani kwao akiwa amebeba panga mkononi. James alitoka mbio akimfukuza mtu huyo aliyekimbia kwa kasi ya ajabu, baada ya kuwa mita kadhaa nyuma akimfukuza akiwa anahisi hawezi kumkamata aliamua kurusha panga lake lililompata sawasawa mtu huyo shingoni. Mtu huyo alianza kukimbia kwa kupepesuka kabla ya kuishia kuanguka, James alimsogelea na kuanza kumpiga kwa mateke.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mtu huyo alianza kujiviringisha chini akipiga kelele baada ya panga lililompata kutoka shingoni na damu nyingi ilikuwa ikimtoka. “leo utasema anayewatuma kufanya unyama…” alisikika James ambaye alikuwa na hasira. Akiwa anaendelea kumpiga mtu huyo katika eneo hilo la giza huku akili yake ikiwa haijatulia kutokana na kulewa kwake alishtushwa na kitu kizito kilichotua begani kwake. Alianguka chini wakati mkono wake wa kulia akielekeza kwenye bega lake la kushoto na kushika panga lililomkata sawasawa. Akiwa anapiga kelele kwa maumivu aliwashuhudia watu wawili wakimbeba mwenzao aliyemkata shingoni na kuanza kuondoka naye kwa kasi eneo hilo wakielekea katika vichaka vilivyokuwa karibu na eneo hilo.
James akiwa anaendelea kulia kwa maumivu aliyoyapata, kundi la watu lilikuwa likielekea kwa kasi eneo alilokuwapo baada ya watu hao kusikia kelele zilizopigwa kwa muda mrefu. Hatimaye walifika eneo hilo na kumchukua kabla ya safari ya kumpeleka hospitali kuanza, wakati huo James aliendelea kulia pasipo kuelezea jambo lolote lililokuwa limetokea. Watu hao waliomchukua ambao walikuwa majirani walitoka kutoa msaada baada ya kuamini kuna mauaji yalikuwa yakifanyika katika nyumba ya marehemu Kibudo. Walikuwa wamebeba zana mbalimbali na zaidi kwa pamoja walikuwa na shauku siku zote za kumfahamu mtu aliyekuwa akifanya mauaji katika familia hiyo.
Waligawana kwa wengine kwenda kumpeleka James hospitali wakati wachache walibaki wakijadiliana juu ya matukio hayo yaliyokuwa yakiongozana. Mmoja wao alimkumbuka George Kibudo, baba yake mdogo na James jambo lililowapa hisia za kuanza kumtafuta kwa vile waliishi pamoja. Waliingia katika eneo la sebule la nyumba hiyo wakiwa wamebeba taa za mafuta kutokana na ukosefu wa umeme eneo hilo. Walishtushwa na mauaji yaliyokuwa yamefanyika sebuleni hapo dhidi ya George, alikuwa ameuawa kikatili na damu nyingi ilikuwa imemtoka ikiwa imezunguka eneo alilokuwapo. Wanawake walioshuhudia tukio hilo walianza kulia kwa sauti huku wakitoka eneo hilo la sebuleni ambalo mauaji hayo yalikuwa yamefanyika dhidi ya George.
Watu waliokuwapo nje nao walipata shauku ya kuona kilichokuwa kimetokea ambao nao pia hawakuwa na hamu ya kumtazama George mara mbili kwani alikatwa mapanga kila eneo la mwili wake. Siku iliyofuata ndugu na jamaa walifika nyumbani hapo kwa marehemu mzee Kibudo wengi wakiwa na mshtuko baada ya taarifa za mauaji hayo. Ndugu wachache ambao awali walipendekezwa kusimamia mali hiyo ya marehemu mzee Kibudo walionekana wakijisifu kwa kukataa kwao kutokana na hofu ya kutokea kwa mauaji ambayo awali walikuwa nayo. Bado kulikuwa na kitendawili juu ya muuaji wa familia hiyo na wachache walihisi huenda James alipata ufumbuzi kidogo. Baada ya uchunguzi wa jeshi la polisi mwili wa bwana George Kibudo ulihurusiwa kuzikwa, siku iliyofuata zoezi hilo lilifanyika ambalo pia lilihudhuliwa na James ambaye alikuwa amepata matibabu ya awali.
Muda wote wa mazishi James alikuwa na hasira juu ya mtu aliyehusika na mauaji hayo, mkono wake wa kushoto ulikuwa ndani ya koti lake baada ya kufungwa ili usichezecheze. Bado hisia zake zilikuwa zikimtuma na kuamini mzee Samola alihusika na mauaji hayo. Mbali na mahudhurio ya mzee huyo katika misiba ya ndugu zake bado hisia zake zilibaki palepale. Jambo lililompa taabu ni uwezo wake wa kufikiri alioufanya ili kumkumbuka mtu aliyefanikiwa kumkata na panga shingoni lakini hakufanikiwa kumkumbuka. Aliamini hiyo yote ilitokana na kulewa kwake siku hiyo ya tukio zaidi alipanga kuhakikisha mtu aliyehusika na mauaji hayo anagundulika na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Baada ya mazishi hayo askari wa upelelezi walimwita James kando na kuhitaji kujua mambo kadhaa yaliyohusiana na tukio zima lililopelekea kuuawa kwa baba yake mdogo.
James alitoa maelezo yake kwa askari hao ingawaje hakuhusisha hisia zake juu ya mzee Samola, alipanga kufanya upelelezi yeye mwenyewe juu ya mzee huyo. Askari hao ambao pia waliahidi kufanya upelelezi walimweleza pia kuwa wangetoa taarifa katika zahanati na hospitali ili mtu aliyeumia shingo asipatiwe msaada wa matibabu pasipo maelezo ya kutosha. Baada ya siku tatu, katika kikao cha familia James aliwaomba ndugu zake kadhaa wamsaidie kusimamia mifugo na mashamba ambavyo vyote vilikuwa vya marehemu baba yake. Hakuna hata ndugu mmoja alithubutu kukubali kumsaidia kusimamia mali hizo kwani kila mmoja alihofia uhai wake akiamini angeuawa. James alijitahidi kuwaeleza ndugu zake juu ya mwenendo wa marehemu baba yake akiwahakikishia kuwa alikuwa mtu mwema lakini hakuna hata ndugu mmoja aliyethubutu kuamini. Wengi walikuwa wameiingiwa na hofu hata watu wazima hawakuwa tayari kumsaidia.
Aliendelea kusimamia mwenyewe mali hizo akiwatumia watu aliowaajiri kama vibarua. Baada ya wiki moja akiwa katika matembezi yake ya jioni, wakati ambao pia mkono wake ulikuwa haujapona alimuona mzee Samola kwa umbali katika eneo ambalo liliuzwa pombe za kienyeji. Aliendelea kutembea akiwa hana wazo la kumsalimia mzee huyo ambaye alikuwa akimtazama kwa makini na hatimaye alimwita James. Alitiii wito kwa kuanza kutembea kuelekea eneo alilokuwa amekaa mzee huyo, mara baada ya kumfikia na kumsalimia, aliketi katika kiti kilichokuwa upande wa pili uliotazamana na mzee huyo. “Kijana pole sana kwa matatizo yaliyokukuta, naomba ujipe moyo” Aliongea mzee Samola akiwa ameinamisha kichwa chake chini.
“aah! mambo ya kawaida tu haya mzee, mimi nimeshatulia” alijibu James akiwa amemkazia macho mzee huyo. “Askari wanaendeleaje na upelelezi?” Aliuliza tena mzee huyo swali ambalo James hakuchelewa kulijibu.
“upelelezi unaendelea vizuri na tunatarajia watuhumiwa watafunguliwa mashtaka ndani ya mwezi huu” alijibu swali hilo na kumpandisha mzee Samola hofu ya waziwazi aliyoigundua kutoka kwa mzee huyo. James mara baada ya kumjibu aliaga na kuanza kuondoka akimwacha mzee Samola akiwa na nia ya kuwafahamu watuhumiwa wa tukio hilo lakini James alimweleza alikuwa na haraka wakati huo.
Akilini aliingiwa na hisia za kuamini ya kuwa mzee Samola alihusika na mauaji ya familia yake kwa namna moja au nyingine, zaidi alihitaji ukweli juu ya hisia zake upatikane. Aliamua kuanza kurudi nyumbani kwake ili akapange jambo la kufanya kuhakikisha anaupata ukweli unaomhusu mzee Samola. Mara baada ya kufika nyumbani kwake alikaa sebuleni akiwa anawaza jambo la kufanya, punde alisikia sauti ya mwanamke akipiga hodi jambo lililomfanya afungue mlango na kumkaribisha. Alikuwa ni mwanamke aliyemfahamu kwa sura lakini hakutambua alikaa maeneo gani kijijini hapo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kuzungumza kwa muda mfupi, mwanamke huyo ambaye alionekana kutokuwa na furaha alimtaka James waongozane naye nyumbani kwake. Alimweleza kuwa kulikuwa na jambo muhimu ambalo alipaswa kulitambua. James bila uoga alikubali na mara baada ya kufunga mlango wa nyumba yake walianza kutembea na mwanamke huyo kuelekea nyumbani kwake. Hatimaye walifika nyumbani kwa mwanamke huyo baada ya nusu saa ya kutembea, alikuwa akiishi katika nyumba iliyokuwa eneo la peke yake, waliingia katika nyumba hiyo na James alikaribishwa kiti na kuketi.
Mwanamke huyo alianza kwa kuhitaji utulivu wa James juu ya yote ambayo alidai yangetokea siku hiyo, jambo ambalo aliahidi kulitekeleza. Alianza kumwelezea juu ya mume wake ambaye alidai alikuwa amefanya mambo ya kusikitisha, wakati akieleza hayo mwanamke huyo alikuwa akilia. Jambo hilo lilimfanya James ahitaji kujua kuhusu mambo ambayo mume wake huyo aliyafanya, mwanamke huyo alisimama na kumwambia amfuate. Alitimiza jambo hilo na walianza kutembea kuelekea chumba cha pembeni alichohisi kilikuwa chumba cha kulala, alikuwa na shauku ya kujua jambo ambalo lingetokea. Mara baada ya kuingia katika chumba hicho James alimshuhudia mwanamme mmoja aliyelala kitandani akiwa amezungushiwa vitambaa shingoni mwake.
Kwa akili ya haraka aliamini mtu huyo ndiye aliyefanikiwa kumdhuru kwa panga siku ya mauaji ya baba yake mdogo.Alibaki na shauku ya kutaka kujua mtu huyo alitaka kumweleza nini. “Denis nimekuja na James unayemhitaji” aliongea mwanamke aliyeongozana naye mara baada ya kuingia kwao. Mwanamme huyo aliyemgundua muda huo kuwa aliitwa Denis alianza kunyanyuka taratibu, “James karibu sana bwana” alisikika akiongea kwa taabu mara baada ya kuketi katika kitanda chake. Baada ya salamu alianza kwa kumwambia kuwa alimwita ili kumweleza mambo yaliyohusu mauaji ya familia yake.Jambo hilo ambalo awali James alilihisia lilimfanya moyo wake ulipuke kabla ya kuanza kutokwa mishipa usoni iliyotokana na hasira, hali hiyo haikugundulika na wenyeji hao. “mtu anayehusika kwa aslimia zote ni mzee Samola…..” alitulia kidogo wakati mapigo ya moyo ya James yakiwa yameanza kwenda mbio.
“yeye ndiye aliyemuua baba yako kwa mkono wake akidai alidhulumiwa mali” Aliongea mwanamme huyo kwa sauti ya chini na polepole, alionekana alipatwa na tatizo lililopelekea ashindwe kuongea vizuri
“yeye ndiye aliyemuua baba yako kwa mkono wake akidai alidhulumiwa mali” Aliongea mwanamme huyo kwa sauti ya chini na polepole, alionekana alipatwa na tatizo lililopelekea ashindwe kuongea vizuri.
Wakati huo James alikuwa ametoa macho akimwangalia mwanamme huyo aliyesimulia mauaji ya familia yake.
“nimeamua nikueleze kwani siamini kama nitapona na zaidi nahitaji msamaha wako kwani nilihusika katika mauaji ya mara ya pili ya familia ya…” kabla hajamalizia sentensi hiyo James alimvamia na kuanza kumpiga ngumi mfululizo mwanamme huyo akitumia mkono wa kulia ambao hakuumia.
“James usimpige, usimpige kama nilivyokuomba kuwa mtulivu naomba utulie” alipiga kelele mwanamke aliyempeleka hadi eneo hilo jambo ambalo alitii. Alikuwa akitokwa na jasho kama alinyeshewa na mvua wakati huo mwanamme huyo alikuwa akikoroma mara baada ya kupigwa.
James aliondoka eneo hilo kwa kasi akiwa haelewi la kufanya hasira zilimpanda na aliweza kumuuwa mzee Samola kama angekutana naye njiani, alielekea nyumbani kwake ili kwenda kufikiri jambo ambalo alipaswa kulifanya. Aliamua kupiga simu kituo cha polisi cha wilayani Babati, askari walimwahidi kufika katika kijiji hicho cha Magugu ndani ya nusu saa.. Baada ya dakika arobaini na tano gari la askari lilifika nyumbani kwake hapo na aliwaongoza mpaka nyumbani kwa bwana Denis baada ya kutoa maelezo ya muda mfupi. Walimkuta akiwa amezidiwa sana ingawaje aliweza kuwathibitishia kuhusika na mauaji ya familia ya mzee Kibudo akiwa anatumwa na mzee Samola.
Walimchukuwa na kuanza safari ya kumpeleka hospitali ya wilaya ili akapatiwe matibabu, mara baada ya kufika katika hospitali hiyo madaktari walielezea uwezekano mdogo wa kupona kwake kwani kidonda chake kilichimbika sana. Hiyo yote ilitokana na aina ya dawa ya kienyeji aliyokuwa akiitumia, alikuwa akihofia kukamatwa kwake akienda hospitali jambo lililomfanya atumie dawa hizo. Askari mmoja alielezwa amlinde mgonjwa huyo na gari hilo la polisi liliondoshwa kwa kasi na kuanza kurudi kijijini Magugu. Askari hao waliokuwa wameongozana na James, lengo lao kubwa lilikuwa ni kwenda kumkamata mzee Samola aliyehusishwa na mauji ya familia ya mzee Kibudo kwa kiasi kikubwa. Mara baada ya kufika nyumbani kwake mzee huyo alishtushwa na ujio wa askari hao jambo lililowapa imani juu ya kuhusishwa kwa mzee huyo na mauaji hayo.
Askari hao walimkamata mzee Samola na kumpakia kwenye gari la polisi, wakati hayo yakiendelea watoto wake pamoja na wajukuu kadhaa walikuwa wakilia kwa uchungu juu ya tukio hilo lililokuwa likiendelea. Hata majirani walishtushwa na tukio hilo kwani walimtambua mzee Samola kama mtu mwema, vilio vyao hivyo havikuwazuia askari kutekeleza kazi yao kwani waliondoka na mzee huyo. Walimpeleka kituo cha polisi cha wilaya hiyo ya Babati na mashtaka dhidi yake yalitarajiwa kufunguliwa siku iliyofuata. James aliruhusiwa kurudi nyumbani huku moyoni akiwa na amani ambayo aliikosa katika kipindi kirefu. Mawazo yake yalimtuma kuhakikisha haki inatendeke katika kesi ambayo ilitarajiwa kufunguliwa hakutaka aina yeyote ya upendeleo. Alihitaji mzee Samola ahukumiwe adhabu ya kunyogwa kwa vile alifanya mauaji katika familia yake, alikuwa tayari kuua endapo mahakama ingeshidwa kufanya kazi.
Jioni ya siku hiyo James alipigiwa simu na mtu ambaye namba yake haikuonekana aliyemweleza awe mwangalifu kwani alikuwa akitafuta matatizo. Alipuuzia kauli hiyo na kuamini ilitoka katika familia ya mzee Samola. Siku iliyofuata askari walimfuata kijana Denis aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya wilaya wakihitaji maelezo zaidi, lakini alikuwa amezidiwa na kushindwa kuongezea jambo lolote. Masaa machache baadaye hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi na askari waliwaomba madaktari wajitahidi kuokoa maisha ya kijana huyo ili atoe maelezo yaliyohusiana na kesi ya mauaji. Hiyo yote ilitokana na mahojiano ya awali ambayo askari walifanya na mzee Samola aliyekana kuhusika na mauaji ya familia ya mzee Kibudo.
Hatimaye kesi iliyohusu mauaji ilifunguliwa dhidi ya mzee Samola na kijana aliyeitwa Denis ambaye pia alikuwa bado hajapona. Wiki tatu baadaye kijana huyo alipata nafuu baada ya jitihada kubwa zilizofanywa na madaktari na alikuwa na uwezo wa kupanda kizimbani. Jambo hilo lilikuwa faraja kwa James ambaye muda wote alikuwapo na askari hospitalini hapo ili kumlinda mtuhumiwa huyo. Baada ya hali ya mtuhumiwa huyo kuwa nzuri kiasi alimtaja mtu mwingine ambaye alikuwa mtoto wa mzee Samola kuwa alihusika pia na mauaji ya familia ya mzee Kibudo. Kijana huyo aliyeitwa Frank alikamatwa na kuongeza orodha ya watumiwa waliobakiza siku chache kupandishwa kizimbani.
* * * *CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jackson John Samola alikuwa mtoto wa nje ya ndoa wa mzee Samola ambaye alikuwa katika harakati za kutafuta maisha jijini Nairobi nchini Kenya. Katika maisha yake aliishi mkoani Shinyanga na mama yake na hakuwahi kuishi pamoja na baba yake mzee Samola. Alimheshimu baba yake huyo kwa vile alikuwa akimtimizia mahitaji yote aliyokuwa akiyahitaji wakati akiwa shule. Jambo hilo lilimjengea tabia ya kumtembelea mara kadhaa baba yake huyo mkoani Manyara. Akiwa bado yuko jijini Nairobi alishtushwa na taarifa alizopewa na ndugu yake aliyemweleza kuwa baba na kaka yake walikuwa wakishtakiwa kwa kosa la mauaji. Jambo hilo lilimchanganya sana na hakuamini kama ni kweli walikuwa wakijihusisha na mambo kama hayo.
Aliwaeleza ndugu zake wajitahidi kufanya kila waliwezalo kuhakikisha baba na kaka yake wanashinda kesi hiyo. Kutokana na kubanwa kwake na kazi aliamua kutuma fedha ili ziwasaidie katika kutoa rushwa ikibidi ili baba na kaka yake wasigandamizwe katika kesi hiyo. Ndugu zake walijitahidi kufanya jitihada mbalimbali ikiwamo ya kujaribu kumuua kijana Denis aliyetarajiwa kuelezea uovu huo lakini jitihada zao zilishindikana. Hatimaye kesi hiyo iliposomwa kwa mara ya kwanza watuhumiwa hao walionekana kuhusika na mauaji ya familia ya mzee Kibudo na hukumu ya kifo ilitolewa dhidi yao.
James alifurahishwa na tukio hilo lililofanywa katika misingi ya haki, watu wengi waliohudhulia kesi hiyo walihuzunika ingawaje ukweli ulijieleza kuwa watu hao walikuwa na hatia. Jambo kubwa ambalo liliwafanya watu kuhuzunika ni imani waliyokuwa nayo awali kuwa mzee Samola, mwanaye pomoja na Denis walikuwa wakionewa. Watu wa kijiji cha Magugu waligawanyika pande mbili kwa wale waliofurahia kutendeka kwa haki na wengine wachache waliungana na familia ya mzee Samola iliyokuwa na hasira juu ya hukumu hiyo. James akiwa nyumbani kwake jioni ya siku hiyo lilifika kundi la wazee na kuhitaji kuongea naye, jambo ambalo alilitii.
Wazee hao waliokuwa upande wake walimtaka ahame kijiji hicho haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha yake, wazee hao walimweleza juu ya mbinu za mauaji ambazo lazima zingepangwa na familia ya mzee Samola dhidi yake. Watu walizidi kuongezeka katika kikao hicho cha ghafla na zaidi ndugu zake waliungana na wazee hao wakidai walichoka kushuhudia mauaji dhidi ya familia yao. James alikubali ushauri huo na siku iliyofuata aliondoka akielekea mafichoni mkoani Arusha akiwa amewapa jukumu ndugu zake kuuza kila kitu alichokuwa nacho kijijini hapo. Alihitaji wamuuzie n`gombe zaidi ya mia aliokuwa nao na mashamba yote, fedha hizo alitaka zimsaidie kwenda kuanza maisha sehemu nyingine. Jambo hilo lilianza kutekelezwa na vitu hivyo vilianza kuuzwa kijijini hapo na sehemu nyingine tofauti.
Familia ya mzee Samola iliyokuwa na hasira iliweka kikao juu ya jambo la kufanya wakati watoto wa kiume wa mzee huyo walidai walimsubiri mwenzao kutoka Nairobi nchini Kenya ili wajue jambo la kufanya. Siku tatu baadaye kijana Jackson John Samola aliwasili kijijini hapo akiwa na hasira juu ya tukio lililokuwa limetokea, alikaa na kaka zake wengine ambao kwa pamoja walijadiliana. Mtu aliyeonekana kusababisha hukumu ya kaka na baba yao hakuwa mwingine bali ni James Kibudo huku kaka zake Jackson wakihitaji kulipiza kisasi.
Kilichowachanganya zaidi ni taarifa walizozipata kuwa mtu huyo alikuwa ameondoka kijijini hapo“msipate taabu kaka zangu, kama mtu huyu yuko katika dunia hii niachieni kazi, miaka hata kumi na tano itapita lakini adhabu yake iko palepale” alisikika akiongea Jackson akiwa na hasira. Kupitia elimu yake aliwaeleza kaka zake kuwa huo haukuwa muda muafaka wa kulipa kisasi kwani ingekuwa rahisi kwa wao kugundulika jambo ambalo walimwelewa.
Baada ya kuuzwa kila kitu kilichokuwa chake kijijini kwao Magugu, James alielekea jijini Dar es salaam akiwa na lengo kubwa la kwenda kunzisha biashara hilo liliwezekana kwani alikuwa amepata kiasi kikubwa cha fedha. Ndugu zake aliwaeleza wagawane mashamba kadhaa ambayo hakuyauza na kichwani mwake hakuwa na wazo la kurudi kijijni hapo akihofia kuuawa kama aliyokuwa amepewa ushauri. Moyoni alijiona hana kosa na alichoshukuru zaidi ni haki iliyokuwa imetendeka juu ya wauaji wa familia yake.
* * * *
Baada ya miaka kumi James alikuwa miongoni mwa matajiri wakubwa jijini Dar es salaam kupitia biashara tofauti alizokuwa nazo. Hakuwahi kurudi kijini kwao hata siku moja ingawaje ndugu zake walimtembelea mara kadhaa. Tayari alikuwa ameowa na alibahatika kupata watoto wawili wakiume, mambo yaliyojili miaka kumi iliyokuwa imepita alianza kuyasahau na aliwaza maendeleo zaidi. Wakati huo alikuwa na marafiki zake kadhaa ambao baada ya mikakati yao tofauti ya kujikwamua kimaisha waliamua kuanzisha kampuni ya utengenezaji wa vyombo vya ndani.
Taratibu zote zilifanyika na kampuni hiyo iliyosajiliwa kama JAJHO Company Limited ilianza kufanya kazi. Kampuni hiyo iliitwa hivyo ikitokana na kifupisho cha majina yao ambayo yalikuwa James,Amos,Jackson,Hamis na Onesmo. James ndiye alikuwa na hisa nyingi zaidi ya aslimia arobaini akifuatiwa na Jackson mwishoe wengine. Katika kipindi kifupi cha biashara kampuni hiyo ilionekana kukubalika na watu walionyesha uzalendo kwa kununua bidhaa zake zilizotengenezwa hapahapa nchini. Jambo hilo lilikuwa faraja kwa James aliyekuwa kiongozi wa kampuni hiyo kutokana na hisa nyingi alizokuwa nazo, lakini pia wenzie walionyesha furaha juu ya mafanikio hayo.
Mafanikio yake ndiyo yalimfanya James awapeleke mapema watoto wake nchini Marekani kwa ajili ya masomo. Walianza masomo katika shule iliyokuwa Chicago katika jimbo la Illinois iliyoitwa American Academy School iliyochukua watoto wa shule ya msingi mpaka sekondari. Moyoni hakuwa na shaka akiamini alikuwa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika maisha yake.
Jackson wa kampuni hiyo ya JAJHO Company Limited hakuwa mwingine bali ni Jackson John Samola ambaye lengo lake lilikuwa ni kulipiza kisasi kwa James. Hakuwahi kukutana na James zaidi ya kumuona kwenye picha kwa vile hakuishi katika kijiji cha Magugu ambacho James aliishi awali. Watu wote waliomiliki kampuni hiyo walikuwa rafiki zake na walikubaliana naye kuhakikisha wanamuua James. Lengo lao lilikuwa ni kusubiri kampuni hiyo ikue na James kuwa na kiasi kikubwa cha hisa na hatimaye kufanikisha zoezi la mauaji. Hakuna mtu aliyekuwa akijua siri hiyo zaidi yao wanne, Jackson siku zote za maisha yake alikuwa akiamini James angekufa kizembe na tayari alinasa katika mtego wake.
Baada ya mwaka mmoja Jackson na wenzake waliona ni muda muafaka wa kuuawa kwa James wakati ambao walikuwa na mafanikio makubwa katika kampuni yao. Walikuwa wakitafuta mbinu mbalimbali za kuhakikisha wanamuua James na mwishoe walipata jibu la kufanikisha zoezi hilo. Jackson alipendekeza kuwa waandae ziara ya kufurahia mafanikio yao wakiwa na familia zao na mwishoe waiangamize familia ya James. Aliwataka ziara hiyo ifanyike nchini Kenya kwa vile aliifahamu vizuri nchi hiyo na ingekuwa rahisi kufanikisha mauaji hayo. Wamiliki hao wa kampuni hiyo mbali na James walimheshimiana sana na Jackson na walikuwa tayari kumsaidia malipizi ya kisasi. Hawakuwa watu wema kwani walishawahi kufanya kazi za ujambazi na kwao kuuawa kwa James waliamini kungewapa kipato kikubwa kupitia hisa ambazo zingeongezeka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kikao chao hicho cha awali walichokifanyia nyumbani kwa Jackson, walipanga Amos ambaye alikuwa miongoni mwa wamilikiwa kampuni hiyo atoe maoni ya ziara hiyo katika kikao chao cha kampuni kilichofanya kila mwisho wa wiki. Kama ilivyokuwa kawaida yao kuwa na kikao siku ya Ijumaa, James alijumuika na wamiliki wenzie wa kampuni hiyo katika kikao. Mara baada ya mambo muhimu kuzungumziwa Amos alitoa maoni ya kufanyika ziara nchini Kenya wakiwa na familia zao katika kumaliza mwaka huo na kufurahia mafanikio yao. Jambo hilo lilionekana kupokelewa vizuri ingawaje James hakulifikilia kabla alikubaliana na wenzake kufanyika ziara hiyo mwishoni mwa mwaka. Wakati huo ilikuwa ni mwezi wa kumi na ziara yao ilipangwa kuanza mwishoni mwa mwezi wa kumi na mbili.
Makubaliano hayo yalionekana kuwa faraja kwa Jackson na wenzie walioamini kuwa mipango yao ilielekea kukamilika. Kila siku iliyokuwa ikienda walikuwa wakiendeleza vikao vyao vya siri vya kukamilisha mauaji hayo hiyo ilitokana na umaarufu aliokuwa nao James. Tayari alikuwa na jina kubwa hivyo mauaji dhidi yake yalihitaji usiri mkubwa ili kushindikana kwa jitihada zozote za upelelezi. Jackson bado alijijengea tabia ya kuwaeleza kaka zake kuwa mambo mazuri yalikuwa hayahitaji haraka akiwahakikishia kukamilisha malipizi ya kifo kama James alivyochangia kunyongwa kwa baba na kaka yao.
Siku sita kabla ya ziara ya wamiliki wa kampuni ya JAJHO Company Limited, James alipokea taarifa za mwanae mmoja aliyekuwa akisoma American Academy School. Alielezwa mwanae huyo wa kwanza aliyekuwa na miaka tisa ambaye aliyeitwa Geofrey alikuwa akipatwa na homa za mara kwa mara jambo lililowafanya walimu wa shule hiyo wamshauri mwanae huyo arudishwe Tanzania. James hakushangazwa sana na taarifa hizo kwani alilitambua hilo kwa vile mwanae huyo alikuwa akipatwa na maradhi tofauti tokea utoto wake. Alikubaliana na walimu kuwa mwanaye huyo arudishwe Tanzania lakini mdogo wake aliyeitwa Robert alitakiwa kubaki nchini humo kuendelea na masomo. Alielezwa mwanaye angefika Tanzania baada ya wiki moja, hiyo ilitokana na ratiba ya ndege ambayo alikatiwa tiketi. James aliyaelewa maelezo hayo lakini aligundua mwanaye angefika yeye akiwa ziarani nchini Kenya, Alipanga kuacha taratibu zote za mapokezi ya mwanaye zikiwa sawa.
Hatimaye siku ambayo wamiliki wa kampuni ya JAJHO Company limited waliipanga kwa ziara ilifika na waliamua kutumia usafiri wa gari lengo lao kubwa likiwa ni kupita katika vivutio tofauti vya nchi katika kanda ya kaskazini. Asubuhi ya siku hiyo James alifika na gari lake katika ofisi ya kampuni akiwa na mkewe ambaye walipendana sana tayari kwa ziara hiyo. Katika ofisi za kampuni yao zilizokuwapo maeneo ya Posta tayari wamiliki hao walikuwa wamefika na alikuwa akisubiriwa Hamis na familia yake ambao walikuwa hawajafika. Lilikuwa limeandaliwa basi maalumu kwa ajili ya safari hiyo na wamiliki hao walionyesha furaha wakisubiri safari hiyo ianze. “mzee hata mtoto tu, inakuwaje?” aliongea Jackson akimuuliza James katika hali ya utani kwani alielewa watoto hao walikuwa masomoni nchini Marekani.
“acha hizo bwana kwani hujui wako wapi?, ila mwanangu Geofrey yuko njiani akirudi tutapishana naye” aliongea James akijibu utani huo.
Baada ya dakika kadhaa Hamis alifika ofisini hapo akiwa na familia yake na safari ilionekana ilikuwa imesha kamilika. Waliingia kwenye basi lililokuwa limeandaliwa na safari ilianza wakiwa wamepanga kupitia hifadhi ya taifa ya Serengeti na mwishoe walipanga wapitie mkoa wa Mara wakielekea nchini Kenya. Walimtumia dereva mmoja ambaye alikuwa akiaminika sana na kampuni hiyo, James hakuwa na hofu kwani alishamwandaa mtu wa kumpokea mwanaye siku mbili zilizofuata hivyo aliamini mambo yote yangekuwa kama yalivyopangwa. Hawakuwa na haraka kwani siku hiyo walilala Moshi mjini wakiwa na lengo la kupata maelezo ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro siku iliyofuata.
Walitekeleza zoezi la kutembelea hifadhi hiyo siku iliyofuata na baada ya maelezo mafupi yaliyohusu mlima huo waliendelea na safari wakipitia hifadhi ya Serengeti na siku tatu baadaye walikuwa nchini Kenya. Walitumia siku mbili kutembelea maeneo tofauti ya jijini Nairobi na siku ya tatu walielekea Machakos kwa ajili ya kuendeleza ziara yao wakiwa na furaha tele juu ya tukio hilo. Walifikia katika hoteli ya kifahari ambayo walikuwa wameikodi kwa ajili yao kwa siku kadhaa wakiwa sehemu hiyo. Kila familia ilipewa vyumba vyake na kila hitaji lilikuwa likitimizwa na wahudumu wa hoteli hiyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment