Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

HATIA - 1

 





    IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA





    *********************************************************************************



    Simulizi : Hatia

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Safari nzima hakutaka kuzungumza na mtu yeyote hivyo alikuwa amepachika ‘earphone’ masikioni mwake ili hata asiweze kusikiliza watu walikuwa wanazungumza nini mara chache sana alipata nafasi ya kusikia mawili matatu hasahasa pale wimbo ulipokuwa unaisha na kuachia nafasi ya wimbo mwingine kuingia, katika kibegi chake kidogo alikuwa na takribani betri nne zilizokuwa zimechajiwa usiku uliopita ili asipatwe na usumbufu wa kuzimikiwa simu katika safari yake hiyo ndefu kiasi ya kuelekea wilayani Serengeti mkoa wa Mara.

    Hivi wazazi wangu ni wendawazimu…sasa waliniita Michael ili iweje kwa nini hawakuniita hata Masumbuko?. Alijiuliza kijana huyu mrefu wa wastani ambaye umbo lake kwa kumtazama ungemkadiria kuwa na miaka ipatayo thelathini lakini kiukweli ndio kwanza siku tatu zilizopita alikuwa ametoka kusheherekea kutimiza miaka ishirini na tano siku ambayo ilianza vizuri sana asubuhi kwa kupokea jumbe tofautitofauti kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki waliokuwa wanaikumbuka tarehe hiyo. Karibia kila mmoja alimtakia heri na fanaka katika maisha yake, huku wakikumbuka pia kumtakia aishi miaka mingi. Kuna ujumbe mmoja alioutegemea lakini hadi wakati huo hakuwa ameupata!!!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Joyce atakuwa ameisahau hii siku au kuna tatizo jingine?? Michael alijiuliza baada ya kutouona ujumbe wake kati ya jumbe zote alizopokea. Kwa kuwa Joyce hakuwa akikaa mbali sana na mtaa anaoishi Michael jijini Dar es salaam, basi Michael alitumia fursa hii kwenda kumpa surprise rafiki yake huyo wa kike tangu utotoni japo hawakuwahi kuvuka urafiki na kuwa wapenzi lakini ndipo walikuwa wanaelekea. Alitaka kuifanya siku hii iwe ya kukumbukwa.

    Michael alikuwa anatabasamu njia nzima, kwani aliamini kuwa ile hali tu ya kumkumbusha Joyce tukio hili ni lazima atamrukia na kumkumbatia, kitendo ambacho kwa Michael ni zaidi ya zawadi, lile joto la kipekee la binti huyo lingeweza kumchangamsha na kujisikia kweli amezaliwa siku hiyo.

    Utajuaje, huenda pia atanibusu?? Alijisemea Michael kisha akafanya kicheko kidogo cha kujilazimisha. Kisha akatikisa kichwa kama vile kuna jambo alikuwa analikataa.

    Sasa alikuwa ameufikia mlango. Akalazimika kunyata ili amshtue Joyce, na hatimaye apokee lile kumbatizi maridhawa.

    Alichokikuta Michael nyumbani kwa akina Joyce ndicho kilibadili ghafla mipango yake ya kufanyia mazoezi ya vitendo (field) katika jiji la Dar es salaam na kuamua kuelekea mji mdogo wa Mugumu Serengeti mkoa wa Mara bila kutarajia. Hakujua kwa nini ameuchagua mji huo lakini alijikuta katika maamuzi hayo. Maamuzi ya kuishi mbali na uchungu ule. Wivu wa kimapenzi ulimsulubisha na kumpelekesha kwa kiasi kikubwa.



    “Lakini kwani nilikuwa nimemtamkia kuwa nampenda?...mimi ni mpuuzi huenda labda ndio maana hakushtuka nilipomkuta.” Alijiuliza Michael huku akijaribu kunywa maji ili kulegeza donge la hasira lililokuwa limemkaba kooni .

    “Hivi ninachokasirika ni nini hasa wakati hajui kama nilikuwa namtaka?...ah!! huu ni upuuzi hakika.” Alijiliwaza Michael huku akishindwa kuyanywa yale maji na kuyafunika kisha kuendelea kupata burudani ya muziki baada ya muda alipitiwa na usingizi alikuja kushtuka baada ya mwanamama aliyekuwa pembeni yake kumlaumu kuwa alikuwa anamlalia kila anaposinzia.

    “Unasema??.” Aliuliza kwa sauti ya juu Michael baada ya kuwa ameathiriwa na sauti kali ya muziki masikioni.

    “Unanilalia bwana!!!.”

    “Ah!! Samahani…” Wakati huu alikuwa ameondoa ‘earphone’ masikioni mwake. Safari ilikuwa inaendelea, safari ya kutoka jijini Dar es salaam kuelekea Mwanza kisha mkoa wa Mara. Hii ndio ilikuwa mipango yake. Mipango ya kukimbia maumivu. Kuikimbia vita ya mapenzi badala ya kukabiliana nayo.



    Baada ya kuomba radhi alitaka kurejesha tena earphone masikioni lakini alisita kidogo baada ya kuvutiwa na vurumai iliyokuwa inaendelea kati ya makondakta wa hilo basi na mwanadada, kisa kilikuwa ni kukosa nauli kwa huyo dada huku akidai kuna mtu anamlipia yuko nyuma.

    “We mbona unasema kuwa kuna mtu analipa na sisi hatumuoni…nenda ukamguse basi mwambie alipe, yaani wewe umepandia njiani halafu unasema kuna mtu anakulipia, acha kutuzingua basi na ujanja wa kizamani. Hakuna lifti siku hizi ujue” Kondakta mmoja alibwatuka kwa ghadhabu akionyesha dhahiri kukerwa na maneno ya yule dada aliyekuwa hajakaa kisafari ndefu kabisa.

    “Ebwana anayemlipia huyu dada yuko wapi?? Sisi tunamshusha hivyo.” alitangaza kondakta lakini hakuna aliyejitokeza kubeba mzigo huo.

    “Mi sishukiiiii…sishuki, niacheni, niache hukooo, sitaki kushukaa.” Alilia yule dada kwa sauti ya juu huku akiwa ameng’ang’ania mkono wa yule kondakta hapo ni baada ya gari kuwa limesimama ili ashushwe. Kila mtu alikuwa na shughuli zake hakuna aliyejishughulisha na sakata hili kwa asilimia kubwa. Waliojaribu kujishughulisha walikuwa wakitabasamu ama kucheka huku wengine wakiongea sauti za chinichini. Haikujulikana wapo upande upi.

    Michael alikuwa bado anaangalia hilo vurumai linavyoendelea, kitendo cha huyo dada kilimkumbusha adha ya usafiri katika jiji alilokuwa ametoka la Dar es salaam lakini kikubwa zaidi ni umasikini unaotawala sehemu kubwa ya Tanzania, lakini kilichomuumiza ni unyanyasaji wa wanawake katika jamii jambo ambalo alikuwa analipinga na hadi kufikia kusomea masuala ya sheria na haki za binadamu akiwa mwaka wa pili katika chuo kikuu cha Dar es salaam na sasa alikuwa anaelekea katika field.

    Alikumbuka jinsi alivyokuwa anajisikia vibaya iwapo mzee wake anatokea kumnyanyasa mama yake. Ile hali ikajirudia tena baada ya sakata hili. Moyo ukamuuma!!!

    “Nipo naye huyo!!!.” Alitamka kwa sauti kuu Michael. Hakujua maneno haya aliyatoa wapi lakini aliyatamka kiufasaha na kusikiwa na kila abiria ndani ya basi hilo la Najimunisa wakati huo tayari tairi sita za basi hilo zilikuwa katika ardhi ya Dodoma. Watu wote waligeuka kumtazama kwa mshangao huku kondakta akitaharuki na uso wake haukutabasamu bali ulipambwa na ndita zilizomaanisha hasira.

    “Sasa muda wote huo ulikuwa wapi kujibu mbona mnaleta ujanja wa kishamba hapa..sasa ulitegemea nitamuacha huyu malaya wako asafiri bure au, acha hizo jombaaa!! Mbona tunatafutiana sababu za kutukana halafu mwishowe mnasema makonda wana matusi.” Kondakta ambaye kimabavu alimzidi Michael alitoa karipio.

    “Nauli ni shilingi ngapi??.” Badala ya kujibu lawama za yule Kondakta Michael kwa kujiamini kabisa aliuliza swali bila wasiwasi. Ilikuwa ni kama hakumsikia kipindi anabwatuka.

    “Sio ishu hizo kaka…nigei elfu ishirini na tisa hiyo.” Alijibiwa kwa jazba. Taratibu alijipekua na kutoa noti tatu za elfu kumi kumi akampatia akarudishiwa elfu moja.

    “Kakae kule nyuma na jamaa yako nafasi inatosha ile pale.” Alielekezwa yule binti ambaye bado machozi yalikuwa yanamtiririka mashavuni na kudondoka chini.

    Kwa kusuasua alienda na kujibanabana pembeni ya Michael wakati huo gari zima lilikuwa linaitazama filamu hii tamu ya kusisimua. Binti alipofika pale tayari Michael alikuwa amerejesha ‘earphone’ masikioni mwake na wala hakumjibu alipotoa shukrani ya msaada huo.

    Michael alitegemea kumuuliza maswali yule binti baada ya muda fulani. Lakini ajabu mdomo wake ukawa mzito.

    Alihofia kuwa kuanzisha kwake maongezi na msichana yule anaweza kuzua mambo mengine. Hakutaka kabisa kujiweka karibu na msichana kimaongezi, aliiona taswira ya Joyce katika uso wa kila mwanamke. Akampuuzia binti yule.

    “Mh!! Wanaume wanajua kutesa wanawake da!! Sasa hapo wamegombana nyumbani anauleta ugomvi wao kwenye usafiri ah!!! Ujinga kweli huu.” Alisikika abiria mmoja mwanamke wa makamo akilalamika lawama ambazo hazikupenya katika masikio ya Michael.

    “Pole dadangu!!!.” mwanaume mwingine upande wa kulia alimwambia yule binti naye akamjibu kwa kichwa.



    Muziki ulipomchosha Michael, akapekua begi lake dogo akaibuka na kitabu. Akakifunua ukurasa alioishia kabla ya kukifunika. CHUKI ndio lilikuwa jina la kitabu kile.

    Yule binti ambaye alikuwa mkimya, akajigeuza na kuanza kusoma ukurasa wa mbele wa kitabu kile. Umakini aliouweka ni kama vile kuna kitu alikuwa anafahamu.

    “Haa!!” akashangaa kwa sauti ya chini sana kama anajishangaa mwenyewe, Michael akasita kusoma lakini hakumtazama machoni, kisha yule binti akasema, “Huyu jamaa ametoa kingine mh!! Vipi ni muendelezo wa ROHO YA MWISHO au?” Aliuliza kwa furaha binti yule huku akionyesha kumjua vyema mtunzi wa kitabu kile cha hadithi. Kauli za dada huyu zikamgusa Michael, akajikuta akivunja kiburi chake cha kukaa kimya.

    “Hamna hiki kipo kivyake tu, ni kali kuliko ROHO YA MWISHO lakini hakifikii HILA” Alimjibu kwa uchangamfu baada ya kugundua kuwa yule dada naye alikuwa akimfahamu mtunzi wa hadithi ile wote walikuwa wakimzungumzia George Iron mtunzi wa vitabu vya HILA, ROHO YA MWISHO na riwaya yake ya kushangaza ya NILIKUFA JANA. Mwandishi aliyeikonga ipasavyo roho yake. Michael akataka kuzungumza mengi juu ya mwandishi huyu, lakini akajionya asiweke mazoea ya ukaribu sana na msichana huyu ambaye hakuwa akimfahamu hata kidogo.



    “Vipi hivi unaweza kuwa nacho kile cha HILA maana jamaa alitoa vichache halafu vikapotea kama vile hakutoa. Nasikitika sikupata bahati ya kukisoma.” Alijieleza kwa malalamiko yule dada lakini hakujibiwa na badala yake yule Michael alikichomoa kitabu cha HILA kutoka katika maficho ya begi lake dogowa, akampatia yule binti asiyemfahamu. Alionyesha kujisikia fahari sana kumiliki kazi zote zinazotolewa na mwandishi huyu.

    Kimya kikatanda baada ya kila mmoja kujikita katika kusoma simulizi.

    Urafiki wao ukaanzishwa rasmi na hobi zao katika kusoma vitabu.

    Michael akayasahau machungu ya Joyce kwa muda!!

    Akili yake yote ikajikita katika kitabu cha hadithi!!! Chuki!!

    Walipoviacha vitabu vyao, mazungumzo yalikuwa mengine. Hawakuwa wakimzungumzia tena mwandishi yule wa vitabu walivyomaliza kuvisoma.

    Wakajikuta wanajenga mazoea ya hali ya juu. Cha ajabu hawakuulizana majina. Kila mmoja alikuwa akimtegea mwenzake aanze kuuliza. Huku Michael akijiweka katika tahadhari ya kujikita katika maumivu mengine kwa kumwendekeza yule binti.

    Kadri muda ulivyokwenda ndivyo wawili hawa walikuwa kama wapenzi!! Huku yule binti akiifurahia zaidi hali ile.



    ******



    Basi lilikuwa katika mwendo mkali sana hapo likikaribia ardhi ya Shinyanga majira ya saa mbili kasorobo usiku, dereva ambaye tangu safari ianze alikuwa anazungumza mara kwa mara na abiria aliyekuwa pembeni yake alijikuta akifumba macho na kuyafumbua ghafla huku masikio yake yakijibiwa kwa kilio kikali kutoka upande fulani wa gari, ni uzoefu aliokuwa nao ndio sababu pekee iliyozuia gari lile lisipinduke baada ya kulivaa shimo ambalo hakuliona kwa kukosa umakini wakati wa kuendesha.



    Gari liliposimama, Michael alikuwa wima, macho yamemtoka pima huku chini akiwepo yule binti ametulia tuli huku akitoa kilio kwa sauti ya chini mno. Abiria kadhaa walisogea kule alipokuwa Michael na kumsaidia kushangaa huku hata mmoja hakuthubutu kumgusa yule binti kwa jinsi alivyokuwa amejikunjakunja katika hali isiyokuwa ya kawaida kabisa.

    “Gari ilipopiga lile bonde tulirushwa juu niliweza kumshuhudia akitua kwenye siti yake kwa kishindo halafu…sijui ni nini kimetokea baada ya hapo.” Alizungumza Michael baada ya maswali kumwangukia yeye juu ya kilichomsibu yule binti ambaye watu walimtambua kama mpenzi ama ndugu yake.

    “Mambo mengine kujitakia tu tazama sasa huyu wamegombana nyumbani amemnyanyasa kwenye gari hadi ameaibika ona sasa mwisho wake.” Alilalamika mwanamke mmoja aliyeonekana kuguswa sana na hilo jambo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Michael alitamani sana kujieleza kwamba hafahamiani na yule binti lakini aliamini kwamba hakuna hata mtu mmoja ambaye angeamini hivyo aliendelea kubaki kimya asijue la kufanya. Ile kauli aliyoitoa kuwa yeye yupo na yule binti tayari ikaanza kumuingiza matatani. Na hakuwa na ujanja wa kujinasua. Kauli ile ilisikiwa na wengi!!!

    Hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ujumla haikuwa mbali sana kutoka mahali basi hilo la Najimunisa lilipopatia hiyo tafrani, kwa maamuzi yaliyoafikiwa na kila abiria yule binti walimzoazoa kutoka pale chini na kumweka katika siti ya mbele ambayo ilikuwa na uwezo wa kupokea watu watatu, hakuwa akitokwa na damu lakini alikuwa akigumia kwa sauti ya chini sana, mwanamke mmoja alikaa pamoja naye kwa ajili ya kumsaidia huku Michael naye akiwa karibu yake.



    ******



    Hospitali ya mkoa wa Shinyanga ndio kwanza ilikuwa katika mgomo wa madaktari wakitaka mwenzao aliyewekewa zengwe na kufukuzwa kazi baada ya kushindwa kuokoa maisha ya mtoto wa Kigogo arejeshwe kazini hivyo hakuna huduma zilizokuwa zikitolewa pale licha ya madaktari kuwepo eneo hilo la Hospitali mjini Shinyanga. Kundi la wanaume wanne wakiwa wamembeba mgonjwa wao liliingia kwa uharaka wa kuhitaji huduma pale ndani, hakuna yeyote aliyewakaribisha zaidi ya ukarimu walioupata kwa mlinzi pale mlangoni huku akiwaonea huruma, kila mtu alikuwa bize sana na mambo yake binafsi yasiyoendana na mandhari ya hospitali.

    “Nesi nesi…” mwanamme moja aliita lakini alijibiwa kwa jicho kali kisha mwanamama huyo akatoweka. Kwa ujasiri waliamua kujitafutia wodi mojawapo na kumlaza yule binti kitandani kisha wakaanza kuhaha kuwatafuta madaktari ambao hata hawakuonyesha kujali. Mwanzoni walikuwa wanaume wanne pamoja na mwanadada asiyejitambua hata kidogo akiwa katika maumivu makali sana ambayo hakuhitaji kujieleza mwenyewe bali jinsi alivyokuwa ameuma meno na kuikunja sura yake lilikuwa jibu tosha, baada ya muda wakabaki watatu, wawili na hatimaye mmoja Michael!! Ndio alikuwa Michael peke yake pamoja na binti.



    Nafsi ya Michael ikaingia katika mgogoro mkali, mgogoro binafsi, maamuzi yalikuwa mengi lakini hakujua lipi ni sahihi. Akiwa katika wimbi la mawazo alisikia anaguswa begani.

    “Aah!! Kijana nimekutafuta kweli, ni zaidi ya saa zima sasa nilikuwa napita hapa lakini sijui kwa nini hii wodi nilikuwa naivuka.” sauti nzito kutokana na umri kwenda ilimweleza Michael ambaye alibaki kuduwaa ilikuwa mara yake ya kwanza kufika katika mkoa huu uliotawaliwa na jamii ya wasukuma halafu anatokea mtu anamfahamu.

    “Mimi?.”

    “Ndio wewe!!!.”

    “Aaah!!! Eheee.” aliuliza Michael ili apate kujua shida ya yule mtu.

    “Unawahi kusahau wewe, mimi ni yule mlinzi wa pale getini mwanangu poleni sana baba!!!! Pole sana” alijieleza yule mlinzi. Michael hakuwa na kumbukumbu kabisa kwamba pale kwenye basi walipofikia muafaka wa kumwahisha binti hospitali watu walichangachanga walichonacho na kufikisha shilingi laki mbili na nusu ambayo walimkabidhi, alipozipokea mkononi ndivyo hivyo hivyo alizishika hadi waliposhuka na kumfikia mlinzi wa geti, wakati anaandika jina lake katika kitabu cha orodha ya wageni ndio wakati huo huo aliziachia zile pesa na kuzisahau, jambo jema mlinzi huyu aliyejitambulisha kama mzee Matata aliona tukio hilo na kuokoa pesa za Michael na sasa alikuwa amempata kwa ajili ya kumpatia.



    Michael alishangazwa na uaminifu aliokuwa nao babu huyu wa makamo mrefu, mwenye mwili uliojengeka na ndevu zake zilizokuwa na mvi kiasi,

    “Kwa nini amenirejeshea hizi pesa??.” Alijiuliza Michael

    “Asante sana mzee wangu asante sana.” Michael alijaribu kumpatia kiasi fulani cha pesa lakini mzee Matata alikataa kabisa huku akimwonea huruma Michael kwa hali aliyokuwa nayo.

    “Ngoja niangalie kama utapata huduma walau ya kwanza maana huyu nani vile anaitwa??.”

    “Aaah!!! Mhh!! Huyu?? Anaitwa nanii Mariam eeh!!! Mariam.” alijibu Michael kwa kujiumauma

    Mzee Matata alipotoka Michael naye alifikiria kuondoka na kumwacha binti peke yake, akili ilikuwa imemruhusu lakini wakati anapiga hatua mlangoni aliisikia nafsi yake ikimtamkia neno ‘NIPO NAYE’ ambalo alilitaja pale ndani ya basi, nafsi pia ilimsuta kwa pesa aliyorejeshewa na mzee Matata, kwa kutoroka ilimaanisha kwamba amefanya dhulumati na kuweka maisha ya binti katika hatihati. Michael alizishusha pumzi zake kisha akarejea tena pale wodini kusubiria harakati za mzee Matata kama zitazaa matunda.





    Akiwa ni mtoto wa tatu wa mzee Akwino Msombe ni yeye pekee aliyejaaliwa kielimu hadi hapo alipofikia, jina Michael Msombe lilikuwa maarufu sana katika shule ya sekondari Musoma Technical alipomalizia kidato cha nne kutokana na umahiri wake katika kucheza mpira wa miguu, jina hilo likaendelea kupeta katika shule za Mara Secondary na baadaye Minaki kutokana na ubora wa Michael katika suala zima la uhamasishaji wa maendeleo na kuwa mshauri bora kwa wenzake hasahasa baada ya kufanya jitihada kubwa na kuunda tawi la FEMA katika shule yake.

    Katika chuo kikuu cha Dar es salaam Michael hakuwa akicheza mpira tena lakini aliendelea kuhamasisha hapa na pale lakini athari kubwa iliyopunguza uwezo wake wa kutimiza wajibu ilikuwa ni jinsia ya kike ambayo kwa mara ya kwanza alikuwa nayo karibu zaidi ya awali alipokuwa katika shule za wanaume watupu. Wasichana hawakuchelewa kutambua kitu fulani katika mwili wake, kijana aliyecheza mpira kwa kujituma miaka kadhaa iliyopita mwili wake ukiwa umejengeka vyema, mrefu wa wastani na rangi yake maji ya kunde ilimfanya aonekane mtanashati pindi anapochomekea shati lake la mikono mirefu katika suruali yake iliyopigwa pasi vyema, anapovaa jeans na fulana yake bado alionekana nadhifu, na hakuharibikia siku aliyojisikia kuvaa pensi kwani mguu wake ulistahili kuonwa na watoto wa kike.

    Hayo yote yalisindikizwa na jicho hadimu sana ambalo likimtazama mwanamke atajiuliza mara mbilimbili Michael anamaanisha nini?? Maskini Michael wa watu hakuyajua hayo yeye alikuwa akihisi huenda kizuri katika mwili wake ni kishimo kidogo (dimple) katika shavu lake la kuume jambo alilojitambia tangu utotoni.

    Akiwa na miaka 23 tu aliingia katika msukosuko wa kimapenzi wasichana wengi walimtamkia kwa midomo yao kuwa anawatesa lakini alichukulia ni utani hadi siku moja na yeye alipogundua nini maana ya kuteswa katika mapenzi. Ni siku ambayo alikutana na Joyce msichana ambaye walicheza naye utotoni na kisha kusoma wote shule ya msingi baada ya kumaliza shule ndipo rasmi wakapotezana baada ya Michael kuchaguliwa kujiunga Musoma tech kwa ajili ya kuendelea na kidato cha kwanza huku Joyce yeye akienda Nganza sekondari jijini Mwanza.

    Hapo chuoni walikutana mgahawani wakati Michael ananawa na Joyce anatafuta nafasi ya kukaa, kila mmoja alimshangaa mwenzake. ilikuwa ni furaha ya hali ya juu ambayo iliunda upya urafiki wao wa utoto na kuufanya wa ukubwani, kwa Joyce ilionekana kama imetosha lakini kwa Michael alitaka zaidi ya pale jambo lililomvuruga sana akili yake. Siku ya kuzaliwa kwake alitamani ibadilike kwani bila hivyo angeendelea kuumia miaka nenda miaka rudi. Kila siku hiyo inavyofika.

    “Kwanini Joy amenitenda hivi??.” alijiuliza kila siku.



    *****



    Baada ya kuamua kusubiri hadi kufikia kupitiwa na usingizi Michael alikuja kushtuka binti hayupo kitandani, mbio mbio akatoka pale wodini lakini hakujua hata ni wapi anaelekea. Madaktari wote walikuwa wamenuna ni nani utamuuliza swali akupe jibu lililomaanisha ukweli, huku na huko bila mafanikio hatimaye aliamua kumuuliza daktari mmoja nadhani jibu alilopewa kama mtu akiwa katika hali ya kawaida anaweza kutenda dhambi.

    “Samahani kaka si una namba yake huyo mgonjwa hebu mpigie umuulize yuko wapi.” sauti ya kike ilimjibu Michael donge zito la hasira likambana, ili kuliondoa akajisogeza ukutani akaruhusu machozi yamdondoke, alidhani yatatoka kidogo lakini yalimwagika mengi huku kwikwi nayo ikichukua nafasi yake. Alikuwa analia

    “Nchi yangu Tanzania…yaani mimi nimpigie mgonjwa simu aaah!!!.” alilaumu huku akijigongagonga kifua chake.



    *****



    Kutoonekana kwa binti na majibu mabovu aliyopewa na yule nesi yalimtia hasira sana Michael, ni mzee Msombe pekee aliyekuwa na uwezo wa kumtambua Michael (mwanaye) wakati anakuwa na hasira na si mwingine, Michael alitamani kumvaa yule nesi na kumchapa vibao lakini nafsi ikamsihi awe mtulivu. Kama vile mwendawazimu ama mtu aliyepoteza kitu cha thamani na sasa anakitafuta kwa udi na uvumba ndivyo ilivyokuwa kwa Michael alizurura pande tofautitofauti hadi akakata tamaa na kukaa chini bila kujua kama amekaa chini tena mbele ya mlango wa kuingilia chumba cha upasuaji.

    “Oya vipi wewe mbona umeziba njia??.” swali hilo ndilo lilimshtua na kutoka pale mara moja, wakati anaondoka hakuacha kuangaza huku na huko kama kuna uwezekano wa kumwona binti, pesa iliyokuwa mfukoni mwake ndio iliyomnyima amani laiti kama asingekuwa na ile pesa aliyochangiwa kwa ajili ya matibabu ya yule binti basi huenda angekuwa ametokomea tayari, lakini hata kama asingekuwa na hiyo pesa kauli iliyotoka katika kinywa chake bado ilimfunga ‘NIPO NAYE’…… “Hata!!!! Huyu ni ndugu yangu siwezi kumuacha!!!!” alijikuta akisema kwa sauti ya juu kijana huyu.

    “Vipi tena mjukuu wangu mbona upo hapa??? Kwani kuna mkeo hapa ndani amejifungua!!” alipokea swali hilo Michael huku akijipatia jibu lake kwa kutazama maandishi yaliyoandikwa mlangoni ‘Wodi ya wazazi’

    “Aaaah!! Mzee ni wewe, simuoni mgonjwa wangu mzee wangu.” alikuwa ni yule mlinzi aliyeiokota pesa na kumpatia Michael

    “Haaa!!!! Ina maana wakati tunamtoa pale wewe ulikuwa umelala, basi una usingizi mbaya.”

    “Mlimtoa wapi?? Saa ngapi??...eeeh!! mzee wangu.” aliuliza kwa wasiwasi.

    “Kumbe kweli ulikuwa unaota..yaani umetuambia kabisa tutangulie we tutakukuta mh!! Hebu tuachane na hayo…yule sijui mkeo ame…”

    “Aaah!!! Babu si mke wangu yule bwana” alikanusha kwa aibu aibu Michael

    “Yote sawa….kama nilivyokuhaidi nilimpata rafiki yangu mmoja hivi ni Daktari alinisaidia tukambeba hadi katika chumba kimoja hapo juu akampatia huduma ya kwanza kwa siri sana wenzake wasigundue……”

    “Ana tatizo gani?? Amepona???” aliingilia kati Michael

    “Tulia mjukuu wangu….yule binti ulisema sijui Maria eeh!!”

    “Eeh!! Maria anaitwa Maria.”

    “Tatizo alilonalo si kubwa sana lakini ni kubwa kwa upande mwingine…alishtuka kiuno”…(Michael akakunja uso kwa uchungu)

    Mzee akaendelea.. “Ilibaki kidogo tu avunjike jumla lakini daktari amejaribu na kukirudisha mahali pake..kinachotakiwa sasa ni mazoezi ili azoee hiyo hali na kurejea kuwa mzima tena” alimaliza

    “Sasa ina maana hayo mazoezi anafanya kwa siku ngapi…asante sana babu”

    “Anafanya kwa siku kumi na nne kama asipokuwa mzembe anapona hata kwa siku kumi” alielekeza yule babu

    “Yule sio mzembe mi namfahamu sana” alidanganya, kwani hata alikuwa hajawahi kuzungumza naye kwa kirefu huyo binti na kama hiyo haitoshi hata jina alikuwa hamfahamu

    “Haya sasa itambidi kesho afanye mazoezi halafu…..mh!!! una sehemu ya kuishi hapa Shinyanga au upo gesti??” mzee huyo mrefu mwenye lafudhi ya kisukuma alimuuliza Michael.

    “Kwa kweli mimi hapa ni mgeni sio siri nilikuwa naelekea naye Mwanza huko ndo nina wenyeji babu” alijieleza kwa upole sana Michael.

    “Hamna shaka nitazungumza tena na daktari yule rafiki yangu aangalie uwezekano wa kukupatia chumba mgonjwa awe anapumzika wewe utakuwa unalala gesti nadhani itakusaidia”

    “Yaani sana mzee wangu nashukuru kwa wema wako..”

    “Usijali hata mimi nina wanangu wanasoma huko Arusha na Manyara, nisipotenda wema kwa watoto kama nyie na wangu mimi nani atawatendea wema???”



    ******

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Joyce alishikwa na butwaa kali sana, si kwa sababu alimwona Michael alivyowafumania akiwa uchi wa mnyama na mwanaume mwingine ila ni kwa jinsi (Joyce) alivyowahi kumueleza Michael wakati wapo chuoni kwamba alikuwa akimchukia sana yule mwanaume ambaye leo hii amefumaniwa naye.

    “Mama yangu!!! Nitauficha wapi uso wangu mimi na tunaenda kufanya kazi sehemu moja dah!!!” alijiuliza bila kupata majibu. Hofu ilimtawala akashindwa hata kupiga namba za simu za Michael kwa kuhofia kuzidi kumkwaza.

    Michael hakuwa na mahusiano ya kimapenzi na Joyce binti wa miaka ishirini na nne mtoto wa mwisho wa mfanyabiashara ya mitumba Stanley Keto, lakini ilikuwa kazi rahisi kuhisi watu hawa walikuwa na mahusiano ni wao pekee walilijua jibu sahihi la fumbo hilo. Michael na Joyce walikuwa wanatamaniana lakini hakuna aliyemuanza mwenzake, hali hiyo ikamfanya Joyce aamini, kwa jinsi Michael alivyokuwa akiwavutia wasichana basi lazima atakuwa na mahusiano na msichana fulani hapo chuoni.

    Hisia zake hizo zikamsukumia na yeye kuamua kujivinjari na mwanaume mwingine, kwa muda mrefu alikuwa hajamkubalia Victor Nicholaus katika suala zima la tendo la ndoa lakini katika siku kuu ya kuzaliwa Michael Msombe akajikuta amemruhusu kaka huyo kuutawala mwili wake na ni katika siku hiyo Michael kwa macho yake anawafumania.

    Joyce alijua ni jinsi gani Michael aliumizwa na kitendo kile. Kosa kubwa alilofanya ni kukaa kimya kwa siku mbili akiamini hasira za Michael zitakuwa zimepoa, siku ya tatu Michael hakuwepo tena katika viunga vya jiji la Dar es salaam na hakujua ni wapi alipoelekea nani angemwelekeza!!!. Alivuta subira hadi muda wa kufanya field ulipofika lakini hiyo haikuwa suluhisho Michael hakuonekana na simu yake haikuwa ikipatikana.

    “Atakuwa ameweka ile namba nyingine lakini nayo sikuwahi kuichukua” hakuwa na ujanja mwingine Joyce kwani kwa marafiki pote hapakuwa na jibu la kuridhisha



    ******

    Siku tisa pekee zilitosha kwa binti kupona kabisa kiuno chake, ilibaki michubuko kadhaa tu katika paji la uso na mikononi lakini haikuwa na madhara makubwa sana.

    “Mkeo ni jasiri sana!!!!” daktari alimsifia Michael wakati anamuelezea jinsi yule binti waliyemtambua kwa jina la Maria alivyopona upesi. Michael alicheka kwa kujilazimisha, moyoni alikuwa anahofia kuhusu suala la pesa maana katika akaunti yake pesa ya field ilikuwa haijaingia bado, na mfukoni alikuwa na shilingi laki moja pekee na alijua ni lazima amlipe yule daktari, kwa kuwa alikuwa amezoeana na yule babu alimvuta pembeni kwa ishara kisha akamueleza kuhusu hilo tatizo lakini hata kabla hajamaliza mzee akaingilia kati

    “Michael mjukuu wangu mimi nimekusaidia kwa vyote hivyo ile hamsini uliyotoa kwa ajili ya dawa imetosha sana….”

    “Aah!! Babu kweli!!!”

    “Ndio wewe usijali…vipi safari lini sasa au tuko pamoja bado…umeionaje Shinyanga kwanza” mzee alimtoa hofu Michael

    “Shinyanga ni nzuri na mnaipendezesha wema kama nyie..kesho asubuhi nitadamka m na kuwahi gari za awali sana”

    “Ukipita Shinyanga usikose kuja kunisalimia” baada ya maongezi ikiwa saa sita mchana aliwaaga na kuwashukuru daktari na mzee Matata kisha akamchukua yule binti na kuondoka naye kwa mwendo wa taratibu.

    “Unajisikiaje??”

    “Nafuu sana asante Michael”

    “Nani amekwambia naitwa Michael”

    “Mzee Matata na daktari..”

    “Wamekudanganya!!”alijibu kwa ufupi Michael.

    Saa moja usiku Michael na binti walikuwa chumbani Michael hakuwa muongeaji sana licha ya binti kujisemesha kila mara, hata jina pekee bado Michael alikuwa hajamuuliza. Hakuwa na haja na kumjua kwanza aliona kama ni mikosi tayari katika safari yake.

    Tayari Michael alikuwa ameoga wakati huo binti akiwa nje hadi alipomaliza kuvaa ndo akamruhusu na yeye aingie kuoga wakati yeye (Michael) akatoka nje. Michael alitembea huku na huko bila sababu ilimradi binti amalize kuoga na kuvaa wapate kulala. Michael hakuwa na dalili zozote a kuwa na hisia na msichana huyu. Kile kitendo cha kumfumania Joyce kiliisulubu akili yake.

    “Nikirejea nampiga maswali kisha nampa nauli aende anapojua yeye.” Alijisemea wakati huo dakika ishirini zilikuwa zimepita. Sasa alikuwa ameamua kuutua mzigo huu Michael

    “Mh!! Hamalizi tu kuoga wanawake nao.” akiwa ametoka dukani kumnunulia binti mswaki alijisemea hivyo baada ya kuona kimya kikali kikiendelea.

    Simu ya mkononi ya Michael iliita, kumbe alikuwa ameisahau ndani ya chumba, hiyo ndiyo ilimlazimu kushusha kitasa chini na kuuruhusu mlango ufunguke haraka haraka akaingia ndani. Almanusura apoteze fahamu aliyatumbua macho yake, mdomo ukabaki wazi lakini sauti haikutoka, baridi kali ikaukumba mwili wake, miguu ikaanza kuishiwa nguvu hakuamini kilichokuwa kinatokea.

    Alisahau kwamba ni mlio wa simu yake uliomlazimu kurejea ndani bila kuruhusiwa na yule binti. Marumaru nyeupe iliyokuwa chumbani hapo ilikuwa imechanganyikana na wekundu, mwili wa binti ulikuwa uchi juu hadi maeneo ya mapajani, hakufanya maksudi kuwa katika hali ile lakini alikuwa hajitambui tena.

    Binti alikuwa amezirai, Michael alibaki amezubaa asijue wapi pa kuanzia, hakuchelewa sana kugundua chanzo baada ya akili yake kukaa sawa, binti alikuwa ameteleza wakati anatoka bafuni na kuanguka chini vibaya, Michael hakuweza kukisikia kishindo hicho kwani alikuwa ametoka mbali kidogo na eneo la mlango wa kuingilia chumbani hapo.

    “Binti!!!...binti!!!! we dada….” Aliita huku akijaribu kumtikisa kidogokidogo, hakupata jawabu lolote lile. Funda la hasira likitiwa hamasa na uoga aliokuwa nao lilimkaba na kujikuta akijuta kumsaidia yule binti kulipa nauli na kujitambulisha mbele za watu kwamba anafahamiana naye. Uvumilivu ukamshinda mtoto wa kiume akajikuta anamwaga chozi, ilianzia hasira kumkaba kooni, mara macho yakawa mekundu, kisha machozi yakatoka halafu kikafuatia kilio cha kwikwi. Michael alilia sana kwa mtihani mkubwa uliokuwa mbele yake hakuelewa ni vipi anapata suluhu kwa sasa.

    “Kaka…..kaka…..” sauti ya kike ilimshtua Michael kutoka katika kilio kikuu

    “Mh!!! Aah!! Binti…..umekuwaje…” aliuliza huku akijifuta machozi kwa kutumia viganja vya mikono yake.

    “Nikuulize wewe….aaaaah!!! ok! nimeteleza kutoka bafuni…kichwa kinaniuma jamani ah!” alilalamika kwa uchungu, Michael hakuamini macho yake kwamba binti alikuwa anazungumza huku akiwa amekaa kitako. Michael akamsogelea na kumsaidia kukaa vyema.

    “Pole sana pole…..unaweza kusimama????” aliuliza

    “Hapana kiuno kinauma sana sidhani kama naweza kusimama” jibu hilo lilirudisha mawazo upya kwa Michael lakini wakati huu hakuumia kama alivyoumia awali. Binti alijivutavuta kwa msaada wa Michael hadi akakaa kitandani kwa kujilaza maana hakuweza kukaa imara.

    Baada ya muda binti alipitiwa na usingizi na kumpa fursa Michael kuwaza ni nini atafanya kuepuka hilo janga alilolivaa mwenyewe.

    “Kesho sisafiri na huyu binti..wema wangu umetosha sasa, sibadili mawazo tena kama nilisema kuwa NIPO NAYE hilo neno nalifuta rasmi, mimi simjui bana!!! Nina matatizo yangu pia siwezi kubeba ya mwingine.” alijichukulia maamuzi hayo kijana Michael. Majira ya saa tatu usiku binti alikuwa ameamka tayari kutoka usingizini, kwa upande wa Michael bado alikuwa hajalala kwa sababu ya kuumiza kichwa juu ya uamuzi anaotaka kuuchukua.

    “Umeamka??” aliuliza swali ambalo alilitambua jibu lake

    “Eeh!!!”

    “Nikuletee chakula gani???”

    “Maji kwanza halafu chakula nichagulie”

    “Mh!! Wewe chagua bibie wala usiogope sawa eeh!!!” alijibu Michael

    “Haya chipsi na mishkaki, tia pilipili, tomato, ukwaju, saladi, chumvi, na nini vile ndimu eeh!!” aliongea haraka haraka kwa utani Michael akajikuta anatoa tabasamu huku akisugua viganja vyake katika mkono wa yule binti. Bila kuaga alitoka nje na kurejea baada ya nusu saa akiwa na chakula na maji, akamsaidia binti aweze kukaa kisha akafungua chakula, kwa akili ya kujiongeza akaanza kumlisha yule binti, kila macho yao yalivyogongana Michael alikuwa wa kwanza kukwepesha, alikuwa ni mwanaume mwenye aibu sana mbele ya wanawake huo ni udhaifu uliokuwa wazi kwake. Walitumia saa moja zima kula chakula hadi kukimaliza, Michael licha ya kumwonea huruma binti lakini azma yake ya kumwacha pale gesti ilikuwa palepale.

    “Michael wewe ni mwema sana asante sana kwa wema uliouonyesha kwangu…” sauti nyororo ya binti ilipenyeza katika masikio ya Michael..

    “Sijui nikulipe nini lakini ubarikiwe sana, naomba kitu kimoja nikuombe na ninaamini utanielewa.”

    “Kitu gani tena.”

    “Waonaje kama ukiniacha hapa uendelee na shughuli zako mimi nimekuwa mzigo mkubwa sana kwako angali u kijana mdogo tu, naomba kesho unitoe nje na uniache barabarani hapo heri niwe ombaomba maana ndio maisha niliyoyachagua tofauti na kule nilipokuwa, nia yangu ya kuondoka kule imefanikiwa huo kwangu ni ushindi mkubwa sana…” aliendelea kuzungumza huku akijilazimisha kutabasamu.

    Maneno ya yule binti yalimshtua sana Michael kwani alikuwa amepanga kumuacha kinyemela lakini anashangaa binti kwa hiari yake mwenyewe anaomba aachwe.

    “Kwa nini unaongea maneno hayo dada yangu, mimi bado sijakuchoka.” alidanganya Michael

    “Sijasema umenichoka wewe unadhani utaendelea kuwa na mimi hadi lini na wapi???.” swali hilo lilikuwa gumu sana kwa Michael kwani hakika jibu lake lilikuwa ni muda muafaka wa kumwacha yule binti.

    “Usiumie sana kaka Michael….wewe ni mwanaume wa kipekee, Mungu atakulipa katika njia zako utakazoenda nitakukumbuka sana na siku moja utakutana tena na mimi nikiwa salama mimi sitakusahau na hata wewe ukiniona usisite kuniita kwa nguvu zote JOYCEEEEEEEEE!!!!!! Mimi nitageuka”

    “Hah!! Kwani unaitwa nani wewe na huyo Joyce ni nani??.” aliuliza Michael huku akiweka kiuno chake vizuri pale kitandani.

    “Ooh!! Ulizoea kuniita binti mwone!! Naitwa Joyce mie

    “Unaitwa Joyce….we acha utani”

    “Utani gani mie Joyce jina langu la kuzaliwa kwani vipi??”

    “Kuna msichana mmoja anaitwa Joyce…”

    “Vipi wifi yangu nini??.” alidakia Joyce

    “Hapana alikuwa rafiki tu ndio maana nilishtuka kumbe na wewe ni Joyce…” alizungumza kwa uchangamfu mkubwa Michael.

    Kwa maongezi yao ya usiku uliopita Michael alijikuta akivunja kwa mara nyingine tena makubaliano yake na moyo wake, kwa kuwa Joyce alikuwa na uwezo wa kutembea japo kwa shida sana Michael aliongozana naye kuelekea kituo cha mabasi wakiwa katika teksi iliyowafikisha haraka, Michael akamsaidia Joyce wakapanda ndani ya basi la Mombasa Raha katika siti za mbelembele na safari ya kuelekea Mwanza ikafuata. Ubora wa barabara hiyo ya kuelekea Mwanza ulimpa ahueni Joyce kwani hakutoneshwa kiuno chake.

    “Nitakuacha Mwanza sawa.” ndilo neno la muafaka kati ya Joy na Michael waliloamua usiku uliopita. Safari ilionekana fupi sana kwa Michael kwani nafsi ilikuwa haijaridhika kumuacha njia panda Joyce ambaye kwa majina amefanana na binti aliyempenda wakati akiwa jijini Dar es salaam.

    Saa tano asubuhi safari ya masaa mawili ilikuwa imefikia kikomo katika stendi ya Nyegezi jijini Mwanza. Si Michael wala Joyce aliyekuwa anaufahamu fika mji huu uliotawaliwa na milima ya hapa na pale hivyo kila mmoja alimtazama mwenzake.

    “Tupeleke lodge yoyote iliyopo karibu na iwe nafuu kiasi.” alijieleza Michael kwa sauti ya chini mbele ya dereva ili Joyce asiweze kusikia.

    “Poa..” alijibu dereva kisha Michael na Joyce wakapanda safari ya dakika kumi ikawafikisha mbele ya lodge iliyojulikana kwa jina la DOUBLE G, baada ya kupewa pesa yake akatokomea yule dereva.

    “Chumba bei gani???...aah!! kwanza vyumba vipo??” aliuliza Michael

    “Vipo lakini subiri kidogo hebu…we nanii Dory, hivi chumba namba 18 kipo wazi au alilipia kulala yule bwana.” waliulizana wahudumu kisha likapatikana jibu kwamba kilikuwa wazi

    “Chumba kipo elfu kumi si mnalala au ni show time kama ni show basi elfu tano!!”

    “Hapana tunalala” alisema Michael huku akitoa pesa mfukoni na kulipia chumba.

    Hakuna aliyekuwa amechoshwa na safari lakini kutokana na kila mtu kuwaza la kwake walijikuta wakipitiwa na usingizi kila mmoja kwa wakati wake. Hadi saa moja usiku ndipo mkojo ulimwamsha Joy na yeye akamwamsha Michael.

    “He!! Tumelala hivyo…..” alijiuliza Michael wakati huo tayari Joy alikuwa ameingia msalani.

    Aliporejea Michael yeye alikuwa amevaa viatu vyake na alikuwa na kila dalili ya kutaka kutoka.

    “Wapi tena ndugu yangu jiji lenyewe hulijui tuachie sisi.” alitania Joy

    “Naenda kucheki benki kama mkopo umeingia si unajua tena…vipi twende wote”

    “Mimi sitoki humu ndani usije ukanipoteza bure” alijibu Joy, Michael akajiondokea.

    Dakika thelathini baadaye mlango uligongwa.

    “Hebu ingia au unadhani umepotea” alijibu Joy huku akikaa kitako na kuruhusu tabasamu jepesi limtawale na kweli kitasa kikashushwa wakaingia watu watatu waliojazia miili yao. Bunduki ndogo iliyowatangulia mkononi ilitosha kumnyamazisha Joy.

    Hakuna hata mmoja kati yao aliyefanana na Michael





    ****



    Michael alikuwa na furaha ya ajabu sana na alijiona ni mtu mwenye bahati kila mara, ndiyo alikuwa na bahati! Maana pale benki hapakumkatisha tamaa ila kumwongezea furaha tele, pesa ilikuwa imeingia katika akaunti yake pesa ya mkopo!

    “Huyu Joy huyu ana miujiza yake na nikifika lazima nimwambie baraka anazoniletea.” alisema Michael bila watu wengine kujua alikuwa anaongea nini, alipovuka barabara kuelekea upande mwingine akili ilimrudisha tena upande aliokuwa lengo ni kununua hiki na kile kwa sababu ya safari ya kesho yake safari ya kuelekea Mugumu Serengeti, alinunua vitu kadhaa wakati huo akiwa na jeuri ya pesa mfukoni mwake.

    “Joy, Joy, Joy…mh!! Ni msichana wa aina yake” alikiri Michael baada ya kufanya tathmini ya Joy akiwa si mgonjwa kama alivyo wakati huo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni mrefu kama mnyarwanda, si mweupe sana lakini weusi wake unatosha kumwona gizani na kwenye mwanga, midomo yake ina majeraha lakini kama ikipona ni mtego tosha kwa mwanaume yeyote asiye na subira, kifua chake ambacho Michael aliweza kukiona bahati mbaya alipokuwa ameanguka kutoka bafuni kilikuwa na mzigo mdogo wa embe dodo ambazo hazikuwa na mpango wa kuanguka katika siku za karibuni, tabasamu lake la nadra liliruhusu vishimo vilivyojificha kuchomoza na kuzidi kuing’arisha nuru ya uso wake. Hiyo ni picha ambayo aliijenga Michael akiwa katika manunuzi ya hapa na pale, mawazo hayo yalimpeleka katika ushawishi, ushawishi nao ukachipua upesi akajikuta anashawishika, kishawishi cha kuondoka na Joy kuelekea Mugumu Serengeti mahali ambapo hajawahi kufika kabla.

    “Nitaondoka naye…atapona mbele kwa mbele naamini atafurahi sana” alisemezana na moyo wake huku akirejea kule alipomwacha Joyce.

    Lakini anaelekea wapi huyu? Nisije nikajibebea matatizo!! Alijiuliza Michael huku akijionya..



    * * *



    Kaubaridi ka asubuhi asubuhi katika jiji la Mwanza maeneo ya Nyegezi karibu na chuo kikuu cha mtakatifu Augustino kaliwachochea wavutaji wengi wa sigara kununua pakiti kwa pakiti kukabiliana nayo huku wasiokuwa wavutaji wakipekua huku na huku kujua ni wapi waliyaacha masweta yao hapo ni baada ya kuingia hasara ya kununua miamvuli mipya kutokana na mvua iliyonyesha kuanzia alfajiri.

    Kijiwe cha Bob Soya cha hapo Nyegezi kona kilikuwa na wadau wengi sana, wachache walikuwa na uwezo wa kununua kete za bangi huku wengi wakisubiri za ‘kugongea’ kwa wenzao. Ushikaji uliwekwa pembeni kutokana na hali halisi ya hewa, kila mmoja alitamani moshi mkali wa madawa hayo uendelee kupenyeza ndani ya mapafu yake kisha kutoka nje kupitia pua na mdomo wake. Pusha aliifurahia sana hali hiyo ya hewa kwani aliuza kwa wingi sana bidhaa zake. Mteja mmoja peke yake ndio alikuwa hazungumzi sana, yeye na bangi, bangi na yeye huku muda ukisogea.

    Matusi makali makali yalizunguka eneo hilo ambalo lilikuwa jirani na nyumba ya kuishi watu. Matusi hayo mwishowe yakavunja amani iliyotawala kwa muda mrefu na kuzaa vita ndogo iliyosababishwa na ukosefu wa ustaarabu wa bwana mmoja aliyelazimisha kupewa kipisi cha bangi kwa ulazima huku akiwa hana pesa ya kukidhi hiyo haja yake. Ubabe wake uliwatetemesha wengi lakini leo alikuwa amempata kiboko yake.

    “Mkishagombana ndio mtapata zawadi ya ‘ndumu’ ama!!!” alizungumza yule mzee ambaye alikuwa kimya muda wote akivuta bangi kistaarabu. Wote waligeuka kumwangalia kwa sekunde kadhaa kisha wakataka kumpuuza na kuendelea kushabikia ugomvi.

    “Kaka, hebu wapatie idadi wanayotaka nitalipia..tuone kama watazimaliza” aliongea kwa jeuri akimtazama yule muuzaji. Amri hiyo ilipunguza makali ya ugomvi na kuuvunja kabisa, maadui wakawa marafiki na hasira kuwa vicheko. Huyu alikuwa ni mzee Robert Chacha, mfanyabiashara maarufu wa samaki katika jiji la Mwanza ambaye kutokana na kabila lake la kikurya isitoshe alikuwa mwanajeshi mstaafu alitokea kuwa maarufu kwa jina la ‘poti’. Ilikuwa mara yake ya kwanza kukifikia kijiwe hichi cha Bob Soya na hakuna aliyemtambua zaidi ya kujua kuwa ni mvuta bangi wa kawaida aliyezidiwa na baridi.

    Ndio Poti alikuwa amezidiwa na baridi hilo halikuwa na ubishi, lakini jeuri yake ya kukivutisha kijiwe kizima ndio ilimshtua kila mtu.

    “Shilingi ngapi jumla??” aliuliza Poti baada ya kila mmoja kuwa ameridhika na pia mzigo kumwishia muuzaji. Muuzaji alimtajia bei kwa uoga akidhani huenda ni bangi zilikuwa zimemchanganya huyu mzee na kujikuta anazungumza vitu asivyovijua lakini haikuwa hivyo, Poti alizama katika kibegi kidogo alichokuwanacho akakipekua kwa kubahatisha akachomoka na noti kadhaa zilizotosha kutibu njaa ya muuza.

    “Hiyo nyingine tunza…” alikataa kupokea chenchi aliyorudishiwa, akafunga kibegi chake na kutoweka.

    Alipoondoka nyuma aliacha gumzo huku kijiwe kikiwa kimesahau kuhusu ugomvi uliotaka kuibuka. Safari ya Poti ilikuwa haina uelekeo maalum ndio maana alijikuta akiishia katika nyumba ya kulala wageni ambayo alienda kwa minajiri ya kubadili nguo zake zilizolowana lakini kama bahati mbaya na nzuri kwake akamkuta msichana asiyekuwa na uelekeo ni huyo aliyemsindikiza chumbani kwenda kuwa jalala kwa muda, yaani kuuchukua uchafu wa Poti na kuuhifadhi. Ngono!!

    Poti alipofika ndani aligundua hiyo haikuwa tabia yake labda huenda ni bangi aliyovuta imemchanganya, badala ya kumtumia yule msichana aliyetegemea ujira baada ya kazi alimshangaza alipomlipa na kumruhusu kuondoka. Baada ya yule changudoa kuondoka Poti alibadili nguo zake na kupitia mlango wa nyuma akatokomea. Hakuaga mtu! Na kanini aage wakati hakuwa na mpango wa kutumia chumba hicho tena.

    Hicho kilikuwa chumba namba 18, chumba ambacho Michael na Joyce wake walikuwa wamekilipia kwa ajili ya hifadhi ya usiku mmoja bila kujua kama kilitumika siku hiyo hiyo.



    *****



    Mdomo wa bunduki uliokuwa umemuelekea Joy pale kitandani haukuwa umekosea njia hata kidogo, walikuwa ni walewale wavuta bangi waliopewa ofa ya kuvuta bure, tayari walikuwa wameusahau wema wa Poti kuwatoa katika baridi bila gharama yoyote sasa wanataka kujua ana nini katika begi wakiamini ni halali yao, ama kweli kijiweni hakuna rafiki wa kweli!!. Poti hakuwa pale ndani tena, walikuwepo watu wasiokuwa na hatia yoyote. Wangejuaje!!

    “We Malaya yuko wapi bwana yako????” sauti nzito ilimuuliza Joy pale kitandani wakati huo alikuwa anatetemeka na kuyasahau maumivu yaliyokuwa yanamkabili.

    “Sina….bwaaa..na!!!.” alijibu kwa kutetemeka sana Joyce. Kitako kimoja tu cha nguvu cha bunduki kiliiweka akili yake sawa

    “Bwana yako yuko wapi malaya wewe!!!.” sauti hii ilikuwa kali kuliko ya kwanza Joy hakutaka kuleta ubishi.

    “Ametoka kidogo….atarudi” alilazimika kujibu kwa hofu ya mtutu wa bunduki.

    “Soya….tumsubirie…..atarudi huyo fala muda si mrefu..” walinong’onezana wao kwa wao, wakati huu walikuwa wameutoa ule mtutu wa bunduki jirani na Joyce lakini alikuwa anatetemeka sana. Baada ya dakika kumi zilisikika hatua zikijongea katika mlango wa chumba namba 18. Majambazi watatu walijibanza nyuma ya mlango huku mmoja akiingia uvunguni mwa kitanda. Mlango ukarudishiwa kidogo.

    “Surpriiiiise!!!!!!!!” ukelele ulisikika kutokea nje ya mlango, ilikuwa sauti ya Michael ni Joy pekee aliyeitambua, moyo wake ukakata tamaa, alijua Michael alisubiri ajibu chochote. Laiti kama angejua kilichopo hapa ndani wallah!! Asingethubutu kuingia! Alijisemea Joyce huku Michael akiendelea kupiga kelele pale nje.

    Joy hakujibu chochote kile kwani alikuwa na hofu juu ya wale watu wabaya waliokuwa chumbani hapo. Sura zao hazikuwa na mzaha hata kidogo walimaanisha walichokuwa wamekifuata hapo ndani. Taratibu mlango ukaanza kufunguliwa kwa mguu kumaanisha kwamba kuna kitu mikono ilikuwa imebebwa hivyo kushindwa kutimiza wajibu huo.

    Uso wa Michael ulikuwa umechanua kwa tabasamu murua, hakuwa amevaa ile shati ya mikono mirefu aliyotokanayo nje, badala yake alikuwa ameitoa na kusalia na fulana. Wakati huu sasa aliweza kuyaonyesha maungo yake vyema, kifua kilichogawanyika katikati kutokana na mazoezi ya hapa na pale kilichomoza katika fulana iliyokuwa imembana hasa, suruali aina ya jinsi ilimchora miguu yake ilivyokuwa imara bila kuyumbishwa na matege ya aina yoyote kilikosekana kitu kimoja tu kukamilisha utanashati wa Michael, hakuwa akitabasamu! Ndio na hakupaswa kufanya hivyo maana Joy alikuwa ameyatumbua macho yake na kutokwa jasho kitu kibaya kilikuwa kimemtokea!! Taratibu bila kuzungumza chochote Michael ambaye alikuwa amesimama sasa mbele ya chumba hicho kimoja naye alimkazia macho Joy. Michael hakupaswa kusubiri kuambiwa akae chini, pigo moja tu katika mbavu zake lilimfanya ajikunje huku akitoa ukelele mdogo, akili ilikataa asikae chini lakini mwili bila ubishi ulilainika hatimaye akasalimu amri mbele ya Joy, mtutu wa bunduki ukafuata katika shingo yake, hofu ikaanza kutanda hofu ikamtawala na uoga ukachukua nafasi Michael akaanza kutetemeka. Dakika tano ziliwatosha kumpekua Michael na kufanikiwa kukutana na pesa kidogo tu kama shilingi elfu ishirini, badala ya kufurahia kidogo kilichopatikana bila jasho lao walipandwa na hasira.

    “Pesa zipo wapi????.” lilikuwa swali moja zito sana kwa Michael hakufahamu hawa watu wamejuaje kuwa ameingiziwa pesa za mkopo katika akaunti yake ndani ya dakika chache zilizopita. Maajabu!! Nani atakuwa amewatuma?

    “Nakuuliza wewe pesa ziko wapi?” hakuwa na cha kujibu Michael, pigo jingine la nguvu katika mgongo wake, akajikunja kwa uchungu kisha akajikunjua baada ya kugundua ameegemea sana katika mdomo ambao risasi hupitia kwenye bunduki iliyokuwa jirani na shingo yake.

    “Sina pesa mimi jamani ni mwanafunzi…..mimi mwanafunzi jamani…” alijitetea wakati huo Joy yeye yupo kimya. Jibu hilo lilikuwa karaha kwa watu hawa wabaya, waliendelea kumpiga Michael kwa awamu huku kwa maksudi wakiwa wameifungulia luninga iliyokuwa hapo ndani sauti ya juu hivyo mtu wa nje hakuweza kusikia kinachoendelea. Kadri jinsi Michael alivyojitetea ndivyo majambazi hawa walianza kupatwa na wasiwasi huenda wanamuhukumu mtu ambaye si sahihi

    “Kocha….una uhakika ni chumba namba 18……mbona humu tumekuta mwanafunzi!!!.....” Mawasiliano hayo kidogo yakafufua ndoto za Michael na Joy kupona dhidi ya watu hawa.



    ****



    Jitihada za Joyce Keto jijini Dar es salaam kumpata Michael hazikuzaa matunda, pale nyumbani alipokuwa akiishi Michael walidai kuwa aliondoka ghafla na hawafahamu alipo japo si mara ya kwanza kufanya hivyo. Rafiki zake Michael walimuelezea kwamba alikuwa katika hali ya unyonge sana kabla ya kutoweka bila kuaga. Majibu hayo yalimtia mashaka sana Joyce, aliogopa sana kuwaambia watu ukweli juu ya nini kilichotokea walipoonana na Michael kwa mara ya mwisho.

    Michael alikuwa amemfumania akiwa na mwanaume mwingine!! Hilo ndilo jambo aliloamini kuwa limesababisha kutoweka kwa Michael katika mazingira ya kutatanisha.

    “Lakini mimi sikuwahi kuwa na uhusiano na Michael licha ya watu wengi sana kuhisi mimi na yeye ni wapenzi.” aliwaza na kuwazua Joyce Keto. Ina maana alichukulia serious watu walipotuita wapendanao!! Alijiuliza. Aliogopa sana kumshirikisha mtu yeyote juu ya uhusiano wa kutoweka kwa Michael na tukio la kufumaniwa kwake. Kichwa kilimuuma sana kila alipojaribu kumpigia simu Michael na kuendelea kupata jibu lile lile kwamba namba anayopiga haipatikani.

    “Kama amejiua je???.” ghafla wazo hilo liliiteka akili ya Joyce. Mh!! Mtihani!! Alihitimisha mawazo yake kwa kupanda gari na kuelekea chuoni, foleni kubwa barabarani ilimtia hasira. “Ah!! Elfu tatu kitu gani bwana.” alijisemea huku akiomba kushuka kisha akakwea bajaji, ghadhabu yake ikapungua kidogo kutokana na kupata hewa ya kutosha. Dakika kadhaa zilitoweka Bajaji ikawasili katika viunga vya chuo. Joyce akashuka na kulipa pesa, kisha hatua kwa hatua akajikongoja taratibu hadi mbele ya ofisi alizokuwa amepanga kwenda.

    “Nimejaza namba ya simu ambayo si sahihi!!.” alijieleza Joyce mbele ya mkuu wa kitengo hicho.

    “Bwana eeh!! Mmezidi na nyie haya chukua uangalie mwenyewe wino wa kufutia huo hapo utajirekebishia, yaani watu wazima tunakuwa kama shule ya chekechea ah!!!” alizungumza kwa hasira mwanamke aliyekuwa katika kitengo hicho. Kwa Joyce huo ulikuwa ushindi mkubwa sana, ni jambo lililompeleka.

    “Huku wasichana huko wavulana” maelezo tosha kabisa kwa Joyce. Haraka haraka alianza kupekua katika majina ya wanaume 1…2….3….4….5…..alizihesabu namba hadi akafikia thelathini na tatu ‘Michael Msombe’!! moyo ulimpasuka na kumuongezea hamu ya kujua kilichoandikwa mbele yake, Mugumu Serengeti!! Mahakama ya wilaya kitengo cha kutetea haki zabinadamu. Ndio wapi sasa huku!!! Alijiuliza Joyce huku akirudia mara mbilimbili kulisoma jina hilo bila dalili yoyote ya kuliweka akilini mwake ipasavyo.

    Mkoa wa Mara!! Msamiati mwingine tena. Ili kuhifadhi kumbukumbu hiyo aliamua kuitumia simu yake kuandika kila alichoona ni kigumu kumeza kwa haraka haraka.

    “Michael ameenda wapi huku…hivi ni Tanzania…” alijiuliza Joyce.

    “Hivi wewe, mbona mzembe hivyo humalizi tu!! Unaboa bwana.” alilaumu yule mama aliyempa Joyce faili kwa ajili ya kufanya marekebisho.

    “Ah!! Samahani hivi ukitaka kuhama sehemu ya kufanya field unafuata process gani?” badala ya kujibu aliuliza swali jingine kwa kujikuta Joyce na kumtia hasira yule mama.

    “Hebu nipishe hapa ushanitia hasira….toka toka toka…tafadhali!” Joyce hakutaka shari huyoo akajiondokea, aliona nyumbani ni mbali sana akiwa ndani ya daladala alifungua simu yake katika sehemu ya internet akaenda google kisha akatafuta google map na kuandika Mugumu Serengeti, ilichukua sekunde kadhaa kutoa jawabu kwamba haikufanikiwa kupakua (load).

    Simu ya Joy haikuwa na salio la kutosha. Kompyuta yake ndogo nyumbani ilitumia sekunde chache ikaleta majibu ya kuridhisha.

    “Michael ndo ameenda huku kweli ama amelaghai pale ili nisifahamu alipoelekea??” kabla hajapata jawabu simu yake ya mkononi iliita, ilikuwa namba mpya kwake.

    “Haloo!!.” aliita

    “Haujambo mwanangu!!!.”

    “Sijambo, nani??” aliuliza Joyce

    “Mama yake Michael….” Moyo ulimpasuka Joyce kama vile amepigwa shoti ya umeme alitulia tuli

    “Shikamoo mama….shikamoo.”

    “Marahaba Joy, za siku mbili hizi mwanangu??”

    “Ni nzuri mama, sijui nyie.”

    “Sisi wazima kidogo, lakini huyo mwenzako hata kwenye simu hatumpati kulikoni.” aliuliza mama yake na Michael kwa sauti iliyosawazika.Kimya kilidumu kwa sekunde kisha Joyce naye akaelezea kutompata kwake hewani.

    “Nadhani yatakuwa matatizo ya simu tu si kawaida yake, nitaenda kwake kumuarifu kuwa unamtafuta” alisema tu kumridhisha mama huyo lakini ukweli ni kwamba Michael hakuwepo.

    Kwa jinsi Michael alivyomueleza Joyce juu ya uhusiano wake mzuri na mama yake tangu akiwa mtoto mdogo aliyetelekezwa na baba yake mzazi, Joyce aligundua kuna tatizo linataka kuibuka tena tatizo kubwa sana.

    “Lazima nifanye kitu mimi ndiye chanzo cha haya yote.” alijishauri.

    “Hivi kwani alinitambulishaje kwa mama yake!!!!.....nipo hatiani Joyce mimi” alijihukumu na kujibebesha hatia hii.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ile hali ya kuamini kuwa Michael alimtambulisha kwa mama na familia nzima kwa ujumla ilimtia katika kizungumkuti na kujutia kosa alilofanya la kujiachia kwa Victor na hatimaye kufumaniwa na Michael.sasa Joyce Keto alilazamika kumtafuta Michael ili aweze kumweleza hisia zake.



    Joyce hakujihangaisha kufanya mabadiliko katika sehemu aliyopangiwa awali kufanya majaribio yake. Kwanza hawatulipi!! Aliwaza hayo na kupata ujasiri zaidi.

    Siku nne baadaye alikuwa ndani ya gari akielekea katika mkoa asioufahamu hata kidogo, lengo likiwa kujitoa katika kitanzi cha hatia inayomkabili pia kuitimiza azma yake ya kuwa katika mahusiano na Michael.

    Mama yake Michael ndiye alimuumiza sana kwani Michael alikuwa ndiye mtoto wake wa pekee aliyezaa na mzee Msombe kabla ya kutelekezwa na kisha mzee Msombe naye kupotea ghafla katika mazingira ya kutatanisha. Michael ndiye faraja pekee iliyokuwa imebaki katika dunia ya mama yake.

    Kama amekufa itakuwaje!! Eeh!! Mungu muepushe!! Aliomba Joyce wakati safari inaendelea.

    Wkati akiwaza haya tayari michael alikuwa matatani!!!



    ****



    Matumaini waliyoyapata Joy na Michael kuwa huenda wale watu watawaacha kwa kugundua si watu sahihi hayakuwa sawa hata kidogo, kwani waliendelea kuulizwa maswali ambayo majibu yake yalikuwa magumu mno. Baada ya Michael kubanwa maswali huku akipokea kipigo hatimaye aliwakubalia kwamba ana pesa kiasi lakini katika akaunti yake.

    “Tunaongozana hadi hapo ATM, ole wako upige kelele aina yoyote ile mara moja nausambaza ubongo wako na wewe kuku hapo kitandani tulia hivyo hivyo nadhani unajua madhara ya kupiga kelele.” alifoka jambazi mmoja huku akimalizana na Michael na kumgeukia Joy.

    Wakati wakijiandaa kutoka, mara giza likatawala pale ndani. Umeme ulikuwa umekatika.

    “Weziiii……weziiiiii..tusaidieniiiiii” Joy alipiga kelele ghafla baada ya umeme kuwa umekatika na kusababisha ukimya pale ndani, sauti yake ilimshtua kila mtu hata Michael alishindwa kuelewa ni wapi Joy ameutoa ujasiri huu mbele ya mtutu wa bunduki, baada ya hizo kelele kimya kikuu kilifuata baada ya mshindo kusikika.



    ****



    HATIA



    Kituo kikuu cha polisi Mwanza, chumba cha mahabusu kilikuwa kimejaa sana lakini bado wengine waliendelea kuongezwa, kelele za mahabusu hazikuwakera polisi waliozidi kutoa amri kwa watuhumiwa waliokamatwa kuvua mkanda, saa, viatu na kuingia mahabusu. Majira ya saa mbili usiku aliingizwa mtuhumiwa mwingine

    “Mapulu!!! Mpeleke chooni huyo” sauti kali ya afande iliamuru. Mapulu alikuwa ni mahabusu aliyekaa siku nyingi sana katika kituo hicho, alikuwa na muda wa mwezi mzima hivyo alikuwa ni mzoefu sana na alitokea kuitwa ‘faza hausi’, huyo ndiye aliyewapokea mahabusu wapya na alizifahamu taratibu zote za hapo ndani. Alikuwa ni mjelajela kweli kwani haikuwa mara yake kufungwa na kuhusu kutiwa mahabusu ilikuwa ni kama kamchezo flani hivi hakuwa na hofu.

    Mahabusu aliyeingia alikuwa akilia kama mtoto mdogo licha ya umbo lake kuonyesha ujasiri wa hali ya juu.

    “Pumbavu!! Unamlilia nani hapa unadhani kwa mamako hapa, kuja huku nikupe chumba!!!” John Mapulu alimkaripia huyo mgeni huku akimzaba kibao katika mgongo wake, Mapulu alipokelewa na mahabusu wengine waliogundua kwamba huyo mgeni alikuwa dhaifu sana na ilikuwa mara yake ya kwanza kuingia mahabusu.

    Moja kwa moja alipelekwa bila kupinga katika mlango wa choo, harufu iliyompokea kuanzia mbali alitamani sana ardhi ifunguke ajitie humo ndani milele lakini hiyo ilikuwa ndoto ya linacha.

    “Umefanya nini mpaka umeletwa hapa ndani??” aliulizwa

    “Sijui hata!!!.” alijibu

    “Hujui!!! Kwa hiyo wamekuchukua tu…au huna sehemu ya kulala wamekupa hifadhi kwa leo???.” aliulizwa tena kwa kuzodolewa. Hakujibu kitu!.

    Hakika ilikuwa mara yake ya kwanza kuingia katika sehemu hiyo lazima ajisikie mpweke. Usingizi hakujua ataupatia wapi kutokana na ile harufu lakini alishangaa alipoamshwa asubuhi kwa kukanyagwa kanyagwa na watu waliokuwa wakielekea chooni, usingizi ulimpitia bila kujua.

    “Amka usafishe choo!!!!” aliamriwa na kijana ambaye laiti kama wangekuwa nje ya selo hiyo angeweza kumuita ‘dogo’ lakini nyuma ya chuma hizo hakuwa na ujanja alisimama na kufanya kama alivyoelekezwa mwili mzima ulikuwa unanuka!!

    “Michael msombe!!!” sauti ya afande iliita, lilikuwa jina geni pale ndani kila mtu akaanza kumuangalia mwenzake.

    “Michael!!” ilirudia sauti ile kwa ukali

    “Naam!!!!” ilisikika sauti kutokea chooni

    “John!! We mtu mbaya sana kumbe umemlaza chooni kweli” afande alisema kwa utani baada ya kumsikia aliyemuita akiita kutokea chooni.

    Suruali yake ya jinsi ilikuwa inamtelemka kutokana na kukosa mkanda wa kuikamata, macho yake yalikuwa yamevimba kwa kutokwa machozi sana huyu alikuwa ni Michael Msombe.

    Si kweli kwamba hakujua kwanini yuko pale ila ni uoga tu wa kuingia selo kwa mara ya kwanza ulimtetemesha. Michael alikuwa anatuhumiwa kwa kesi ya mauaji ya mtoto wa kike katika nyumba ya kulala wageni ya Double G jijini Mwanza. Kesi ambayo kwa asilimia kubwa haikuwa na ushahidi wa kumfunga lakini alikuwa ndani kwa ajili ya upelelezi, hakuwepo mtu anayemshtaki Michael tofauti na jamuhuri ya muungano ya Tanzania.

    “Huna ndugu yako umpigie aje akuwekee dhamana??” aliulizwa Michael baada ya kulifikia geti la chuma lililokuwa limefungwa imara.

    “Nilikuwa nasafiri!!!.”

    “Pumbavu, sijakuuliza kama ulikuwa unasafiri ama la..nimekuuliza una ndugu we fala nini??” alifoka askari, Michael akakosa cha kusema.

    “Mpuuzi wewe, nakuuliza unadengua unadhani mi nakutongoza au??? Haya utaozea humu ndani” maneno hayo ya afande yaliugalagaza vibaya moyo wa Michael, hakuwa na hatia lakini alinyanyasika. Michael alikuwa ameikariri vizuri namba ya mama yake mzazi lakini aliamini kuwa kwa kuruhusu mama yake apigiwe simu ilikuwa ni tiketi sahihi ya kumruhusu mama huyo mjane aitenge roho yake na dunia hii, mara chache sana Michael aliacha kujutia kitendo cha kumsaidia Joyce katika safari waliyokutana, Joy ameharibu mipango yangu yote!! Aliwaza lakini akayapinga mawazo yake baada ya kukumbuka huyo Joy anayemzungumzia yeye sasa ni marehemu si hai tena

    “0717..7….3…76..” aliitaja namba hiyo kwa askari wa zamu ambaye kidogo alikuwa mstaarabu.

    “Haya nitampigia….”

    “Tafadhali mwambie asimwambie mama” afande hakujibu akajiondokea. Zilikuwa ni siku tatu tangu atiwe selo, hata siku moja hakuwahi kupelekwa mahakamani kisa ushahidi haujakamilika.

    Mazingira ya selo yalikuwa magumu sana kuzoeleka kwa upande wake, japo alikuwa ameanza kupata marafiki ambao walikuwa wakimkaribisha chakula aliamini hapo si mahali sahihi kwake yeye, bado elimu yake ilimtia ushawishi kwamba watu wenye elimu hawatakiwi mahali pale.

    “Mbona sasa hawa wasio na elimu wameninyanyasa, lakini hata sikuulizwa nina elimu gani wakati naingizwa hapa ndani, kweli wanajali elimu hapa!!!! Hapana sidhani” alipata jawabu na kuanzia siku hiyo akaifuta dhana hiyo. Siku ikapita bila kumwona tena yule afande, wakati huu alikuwa halali tena kule chooni bali walilala wale wageni.

    Zilikuwa zimepita siku sita tangu Michael aingizwe pale ndani, walikuwa wanaingia wengine na kutoka lakini yeye hakuwahi kuja kutembelewa na ndugu yeyote yule. Ilifikia wakati baada ya John Mapulu ni yeye aliyekuwa anafuata kwa uzoefu pale ndani.

    “Hivi wewe huna ndugu!!!” John alimuuliza Michael siku hiyo wakiwa wanakula ugali na maharage ulioletwa kwa ajili ya mahabusu.

    “Ninao ila wako mbali.”

    “Huwa namsikia afande anasema uliua, je ni kweli??.”

    “Hapana kaka sikuua ila, kuna binti nilikuwa naye……” Michael alisimulia kila kitu jinsi alivyokutana na Joyce katika basi, maswahibu waliyoyapata Shinyanga na makubwa zaidi yaliyochukua uhai wa Joy hapo Mwanza. Michael alielezea kitendo cha Joy kupiga kelele kilivyowatia hasira majambazi na kufikia hatua ya kumpiga hadi kumuua.

    “Wewe sasa umekamatwaje??.”

    “Baada ya Joy kuwa ameuwawa niliwataarifu mapokezi, wao wakapiga simu polisi. Polisi walichelewa kuja lakini baadaye walikuja, walimchunguza Joy kwa macho kisha wakamwacha kama alivyo, kesho yake walikuja na daktari akamfanyia uchunguzi sijui alitoa majibu gani, baada ya siku mbili nikiwa mtaani nilipigiwa simu na watu nisiowafahamu….”

    “Ukawaeleza ulipo wakaja kukukamata…” alimalizia John kuonyesha kwamba anayajua sana mambo hayo.

    “Ni kweli na walinikamata kwa shari sana, walinipiga na kunitia pingu.” alimalizia Michael.

    “Ulifanya kosa kubwa sana kuwasubiri, baada ya tukio usingebaki…hawana dogo hawa wanapenda sana………mh!!! Umeandikisha shilingi ngapi katika PPR yako??”

    “PPR?? Ndo nini.” aliuliza Michael

    “Kikaratasi kilichoandikwa vitu ulivyoacha hapo kaunta kabla hujaingizwa lokapu”

    “Aah!! Elfu tatu”

    “Elfu tatu?? Hawakuachii hawa” alihamaki Mapulu. Michael akasononeka waziwazi na kukata tamaa. John akainuka na kuelekea katika chumba kingine.





    JOYCE NDANI MUGUMU SERENGETI



    Hapo kabla alizoea kuzisoama mbuga za Serengeti katika vitabu na kamwe hakuwahi kudhania kuna wanadamu wanaishi katika ardhi ile. Sasa alikuwa katika mji huu.

    Alifika siku ya ijumaa, hivyo alilazimika kusubiri kwa siku mbili zaidi ili aweze kwenda katika ofisi ya wilaya ambayo aliamini kuwa Michael anafanya masomo yake kwa vitendo huko. Joyce alikuwa haishi kujaribu kupiga simu ya Michael ambayo haikuwa inapatikana.

    Na wakati huo mama mzazi wa michael naye alikuwa haishi kumsumbua Joyce kumuulizia iwapo anajua lolote juu ya Michael alipo.

    Usumbufu aliokuwa akiupata kutoka kwa mama yake Michael kuhusu mwanaye ulimkosesha amani Joyce Keto sasa alikuwa ameeamua kubadili laini ya simu yake ili aweze kuwa na amani walau kiduchu wakati huo akifanya jitihada za kumpata Michael, kumwomba msamaha na kuanzisha rasmi penzi lao. Mara moja moja alikuwa akiiweka ile laini na kusoma baadhi ya jumbe zilizokuwa zimeingia kisha kuitoa katika simu. Kwa tahadhari kubwa!!

    Usiku huu wa jumapili alifanya hivyo tena. Ukaingia ujumbe.

    “Mwenye namba 0657727*24 amekupigia simu saa……” ulisomeka ujumbe katika simu yake.

    “Mh!! Atakuwa nani huyu jamani…mbona hii namba sina..au mama yake michael ametumia namba mpya” alijiuliza Joyce akiwa katika kitanda chake katika nyumba aliyopanga kwa muda. Haraka haraka alizinakiri zile tarakimu katika karatasi na kisha akatumia simu yake nyingine kupiga.

    “Hallow!!” upande wa pili ulipokea ilikuwa sauti nzito ya kiume.

    “Samahani kaka, nimekuta ujumbe wako kwamba ulinipigia simu lakini sikuwa napatikana” alijieleza Joyce

    “Hii simu wanatumia watu wengi, afande Matiko Mwanza hapa je kuna uhusiano wowote” aliuliza

    “Ahh!!! Sijaelewa.”

    “Labda kuna ndugu yako ni mahabusu maana hawa ndio wanapiga piga simu sana kwa ndugu zao, kwani hiyo namba yako ni ipi” aliuliza na Joy akamtajia naye akawa anaiandika.

    “Aaaah!! Kuna ndugu yako huku tena ana siku nyingi sana anaitwa Michael nani sijui” alijieleza yule afande kwa sauti ya ukali ikiwa na lafudhi ya ukuryani kwa mbali..

    “Nani Michael????......upo wapi afande wewe, kwani amefanya nini tena…aah!!! Umesema Mwanza” alijikanyaga kanyaga Joyce baada ya kupokea taarifa hiyo. Aliamini huyo ndiye Michael ambaye anamtafuta.

    “Mwanza kituo kikuu cha polisi…usiku mwema” aliaga na kukata simu.



    ****



    Joyce hakushtushwa sana na taarifa ya Michael kuwa mahabusu bali alikumbwa na furaha kubwa ya kusikia walau fununu kuhusu Michael.

    Siku iliyofuata Joyce aliiacha hoteli ya Girrafe na kukwea basi kuelekea Mwanza huku akiwa na matumaini tele.

    Furaha hii hakutaka kubaki nayo mwenyewe. Akamshirikisha mama yake Michael kwa kumuhakikishia kuwa Michael yupo salama na walitegemea kuonanan siku hiyo.



    Safari ilikuwa ndefu sana lakini hatimaye wakalifikia jiji la Mwanza hii ni baada ya kupanda mabasi mawili kwani basi la moja kwa moja halikuwepo siku hiyo. Hivyo walifika wilaya ya Bunda na kuchukua magari mengine yakawafikisha Mwanza.

    “Naitwa Joyce Keto….natokea….”

    “Sema shida yako…” alikatishwa na polisi aliyekuwa kaunta

    “Kuna ndugu yangu hapa anaitwa Michael Msombe nimekuja kumwona nasikia amekamatwa”

    “Anaitwa nani na amekamatwa lini???” aliuliza kwa hofu afande

    “Sifahamu….”

    “Haya subiri hapa dakika mbili…. Una uhakika wewe ni ndugu yake” alihoji Joy akatikisa kichwa kuashiria kukubali

    “Hakuna mtu kama huyo hapa” lilikuwa jibu la afande.

    “Hapa ndio central….” Aliuliza Joyce

    “Ndio hapa kwani hujui kusoma” alijibiwa kwa mkato na yule afande ambaye alionyesha kuwa hakupenda kuzungumza na Joyce.



    ****



    Taratibu Michael na John Mapulu wakawa marafiki ndani ya lock up, mara kwa mara walipiga stori za hapa na pale kuhusiana na maisha halisi huku simulizi za John zikimsisimua sana Michael ambaye hakuwa na jambo lolote lile la kutisha nje ya chuma hizo za mahabusu.

    “Mimi ni mbaya naua dakika yoyote ile kisha nasahau!!!!” alisisitiza John na kumwacha Michael mdomo wazi akiwa haamini kama yupo karibu na mtu wa hatari kiasi kile, japokuwa John hakuwa na mwili uliojaa sana lakini alikuwa na makovu mengi sana kuonyesha kwamba amebobea.

    “John Mapulu!!!!!” iliita sauti ya afande aliyekuwa ameikaza sura yake kana kwamba analinda mahabusu hata mmoja asitoroke, huku John akiamini sauti hiyo ilikuwa ni ishara kwamba mahabusu mpya ameingia hivyo aje kumpokea la! Haikuwa hivyo John baada ya siku nyingi alihitajika nje ya selo hiyo, labda kwa ajili ya mahojiano!!!, labda kupelekwa mahakamani, au kuachiwa huru kabisa!!! Hapana haiwezekani kwa muharifu kama huyu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Dogo kama nisiporudi mamlaka yote sasa juu yako, naweza kuwa napelekwa sehemu inaitwa ‘Sitaki maelezo’ huko ni hatari sana mdogo wangu hakuna mwanaume hata mmoja anayeweza kusita kutoa machozi, wanatesa vibaya sana na bila kujali lolote unaweza ukafa na usishtue jamii, na ujasiri wangu wote kule napaogopa sana, ukifanikiwa kutoka salama wewe si mwanaume tena!! Kule wananyanyaswa wenye makosa na wasio na makosa, hakuna huruma kule” kwa mara ya kwanza Michael akaisoma hofu aliyokuwa nayo John baada ya kuhitajika nje ya selo hiyo.

    Michael hakuwa na la kuongezea, moyo wake ulidunda mara mbili ya mwendo wa kawaida huko Sitaki maelezo aliwahi kupasikia tu kuwa ni kituo cha polisi cha Mkuyuni lakini maalumu kwa ajili ya mahojiano na watuhumiwa wa makosa ya jinai. Mh!! Hivi na mimi nina kosa la jinai eeh!!! Alijiuliza Michael na kuzidi kupatwa hofu.

    “John!!! Nakusubiri wewe!!!” alizidi kusisitiza afande, kwa unyonge John akaiangalia selo na kutoka nje, suruali aliyoivaa haikuwa na uwezo wa kukaa kiunoni. Alikuwa amekonda sana!!



    Michael alibaki mkiwa japo hakuna aliyethubutu kumsumbua kwa lolote amani haikuwepo nafsini mwake, huku akiwa anaamini fika kuwa John Mapulu hatarejea, muda wa saa tatu usiku akiwa amelaa baada ya kuwa wamehesabiwa alimsikia John akirudishwa pale mahabusu.

    “Kwa kesi niliyonayo sasa hivi wataninyonga!!! Sipo tayari kufa kwa sasa” ni maneno ya kwanza kabisa John kumnong’oneza Michael ambaye alikaa kitako kumsikiliza vyema.

    “Kwanini kaka unasema hivyo na imekuwaje umerudishwa hapa ndani??” alihoji Michael kwa mtindo uleule wa kunong’oneza.

    “Nitakueleza lakini kwa sasa hebu ngoja….watu wote wamelala hapa ndani??.”

    “Nahisi watakuwa wamelala ni muda mrefu sana tangu waache kuzungumza” alipojibiwa hivyo aliingiza mkono wake mmoja sehemu zake za siri na kuibuka na kitu ambacho Michael hakukifahamu si tu kutokana na giza hapana hakuwahi kukiona kabla.

    “Dogo umewahi hata siku moja kufikiria kuwa maisha yako yanaweza kuishia gerezani??.”

    “Hapana kwani vipi??.”

    “Vipi kuhusu kufanywa nyumba na mwanamme mwenzako??.”

    “Nyumba?? Ndio nini!!!” aliuliza kwa mshangao lakini kwa sauti ile ile ya chini

    “Kuolewa!!!”

    “Hapana na haitatokea…”

    “Ukienda jela utaolewa bila kupenda na mwishowe utazoea.” alijibu John huku akijikuna mgongo wake, Michael alibaki anashangaa kama aliyeambiwa mke wake ana mimba isiyokuwa yake.

    “Una maana gani??.”

    “Namaanisha utaolewa kama unapenda kwenda jela.”

    “Sipendi kwenda jela!!!.” bila kutarajia alijikuta anamjibu

    “Mimi pia sipendi kunyongwa hadi kufa ni heri nife kwa risasi…..hivi unafahamu kesi yako hukumu yake ni ipi??.”

    “Hapana sifahamu!!.”

    “Unapenda kifo cha aina gani??.” John alimuuliza

    “Mhh!! Sipendi kufa.”

    “Basi wao watakunyonga hadi ufe maana wewe uliua!! Utajisikiaje siku unahukumiwa??” aliuliza kama swali la kawaida kabisa

    “Lakini mimi sikunyonga!!!” alijitetea Michael bila kujua kwamba pale hapakuwa mahakamani, John Mapulu akacheka kwa sauti ya juu kidogo.

    “Mimi leo hii usiku natoroka sijui wewe mwenzangu” John aliyatamka hayo kama vile anayeaga kwenda msalani mara moja na kurejea tena baada ya muda mfupi tu.

    “Unatoroka!!! Kiaje mimi a a siwezi.” aligutuka Michael

    “Haya mimi nilikuwa nakuaga tu!! Kama vipi utamsalimia bwana mmoja anaitwa Dunga Dunga kama ukipelekwa gereza la Butimba na yeye anasubiri kunyongwa kwa hiyo utakuwa naye, yeye ni bingwa wa kuoa wenzake halafu yeye kuolewa hataki lazima atakuchangamkia ingizo jipya!! lakini kama akiwa amenyongwa tayari sina budi kusema alale pema peponi.” alimaliza kwa kucheka hasahasa baada ya kukumbuka kuwa amesema alazwe pema peponi. Muharifu kama huyu!!!

    “…….halafu kama wasipokunyongea hapa Mwanza basi wanaweza kukurudisha kwenu……huko Dar gereza moja hivi linaitwa Keko. ni heri ufanye sala kwa Mungu wako unayemwamini wakunyongee hapahapa Mwanza….” Aliongezea John.

    Mh!! Nifanye sala kwa ajili ya kuchagua mahali pa kunyongewa??!!! Alishangaa Michael.

    Michael alishikwa na hofu kuu ni kama John alikuwa ameshika kitanzi kwa ajili ya kumnyonga baada ya hukumu kupitishwa. Fundo la hasira lilimkaba kooni, alitamani sana kila mtu afahamu kuwa yeye hana makosa lakini hilo halikutokea.

    “Mapulu nimesema sipo tayari kufa….”

    “Umewahi kusikia mtu ananyongwa halafu anapona??.”

    “Hapana!!!”

    “Sasa wewe unasemaje hutaki kufa wakati upo tayari kunyongwa???” aliuliza kwa sauti iliyodhihirisha kukerwa na msimamo wa Michael.

    “Tuondoke wote John.”

    “Sio tuondoke sema tutoroke!!!.” John alimrekebisha Michael usemi wake. Michael akalazimisha kutabasamu. Wakalala!!



    Ni kama vile John alikuwa na saa ameitegesha, usiku wa manane kila mahali pakiwa kimya alisimama wima kwa tahadhari kubwa akawaruka wenzake kwa kunyata hadi akaufikia mlango wa stoo iliyokuwa inatumika zamani sana, kufuli lake lilikuwa kubwa lakini lenye muundo wa kizamani. Akachomeka kifaa alichomuonesha Michael baada ya kuingia, kwa muda wa sekunde kama tatu kufuli likasalimu amri.



    Mlango ulikuwa mgumu sana kufungua na ulielekea kumshinda John.nimuamshe Michael!!! Hapana. Alijiuliza kwa sekunde kadhaa kisha akaingia chumba kimoja akawaamsha watu wawili hawa walikuwa na kesi ya kukutwa na bunduki. Hakika John alikuwa hajakosea baada ya sekunde kadhaa mlango ulikuwa wazi.

    “John Mapulu!!!!!” ilisikika sauti kali ikitokea mlango mkuu wa kuingizia mahabusu, John na wenzake wawili walibaki wakishangaana kwani tayari walikuwa wamefungua mlango. Jonh aliwaonyesha ishara ya kukaa kimya nao wakatii.

    “John!!! mteja wako mpya huyu hapa….ingia huko nenda moja kwa moja huko mwisho” ilisikika sauti ya afande akitoa maelezo kwa mahabusu. Haraka haraka John alivyosikia mlango umefungwa aliwaacha wenzake wawili waliokuwa katika azma moja na kumuwahi huyo mahabusu mgeni asijue nini kinaendelea.



    “Lala hapo hapo wasikuzingue hao!!!” John alimkaribisha yule mahabusu mahali pazuri kabisa naye akashukuru na kujilaza.

    “Michael…..Mi…. amka wewe” John alimtikisa Michael na yeye akiwa na kumbukumbu sahihi kabisa alisimama wima na kumfuata John Mapulu.kuolewa!!kuteswa ….kunyongwa…hapana bora kutoroka!! Ni uamuzi alioufikia Michael akauvaa ujasiri.



    “Nikikamatwa nimekwisha!!!!” alijisemea Michael bila kumpa nafasi John kugundua kwamba alikuwa na wasiwasi mkubwa. Mlango ulikuwa wazi Michael akatangulizwa kisha wale wengine wawili ambao John alitokea kuwakubali ghafla kisha akajitosa ndani mwenyewe ukawa umebaki mlango mmoja pekee waweze kufika nje na kuwa huru.

    Kiongozi wa msafara akiwa ni John hivyo alisikilizwa kwa kila kitu. Wakati huu aliwasihi wenzake watulie tuli tena wakatii. Alifanya kitendo cha dakika chache kuvua suruali yake, kuchuchumaa chini kisha akapeleka mkono wake katika sehemu ya haja kubwa akaibuka na simu ndogo nokia 1100 ile ya tochi. Mchezo huu ni maarufu sana kwa wajelajela, unaitwa kupandisha na kushusha. Wafungwa hutumia maficho haya kuhifadhi pesa na simu ndogondogobila wasiwasi.

    Michael akakodoa macho lakini wale wengine hawakushangaa, nao pia walikuwa wajelajela. John akamsoma Michael usoni alivyoshtuka akajenga tabasamu bandia bila kusema neno lolote. Simu iliwashwa, ujumbe ukatumwa kisha ikazimwa baada ya kujibiwa ujumbe.



    “Dakika tatu zinazokuja tutakuwa nje, msiwe na papara zozote zile ili tufike salama!!!” alizungumza kwa kumaanisha John Mapulu, Michael alikuwa anatetemeka, alitambua kuwa hakuwa na hatia lakini sasa alikuwa anajiingiza katika hatia ya ukweli. Lakini kipi bora kunyongwa bila hatia au ukiwa na hatia!!! Alijiuliza lakini alikuwa amechelewa sana kupata jibu litakalompa maamuzi sahihi mlango wa pili ukawa wazi.

    “JOHN Mapulu….kuja hapa…kuja hapa haraka” ilisikika sauti ya amri ni sauti John aliyoifahamu ilikuwa sauti ya mpelelezi wa kesi yake Sajenti Romagi, mpelelezi aliyesifika kwa ukatiri wake



    Mkojo wa moto kabisa ulikuwa umeshapenya katika suruali ya Michael, alikuwa muoga kuliko wenzake hii ni kwa kuwa hakuwahi kuzoea hizo pilika pilika. John alisimama thabiti akakuna kichwa chake kutafuta maamuzi sahihi ama kurejea na kuitikia wito ama kuendelea na safari yao ya hatari kabisa. Hakutakiwa kupoteza hata sekunde kumi!!!! Tatizo!!!

    Hatia ya kutoroka ikaanza kumsulubisha palepale kabla hajatimiza lengo!!!



    “Twendeni!!!” aliamuru John, akafuatiwa nyuma na kundi la watu watatu wote wanaume lakini mmoja akiwa anatetemeka sana kama mwanamke huyo alikuwa ni Michael. mlango wa kutokea nje ulikuwa umefunguliwa na vijana ambao walikuwa wameziba nyuso zao kwa kutumia vitu kama soksi kubwa hivyo sura zao hazikuonekana. Hawakuzungumza kitu lakini John alielewa kipi kinachoendelea, upepo wa nje majira ya usiku ulipokelewa vilivyo na mapafu ya Michael na kumsahaulisha kosa kubwa alilokuwa amelitenda kosa la kutoroka!!!! Akiwa hajui la kufanya na wapi pa kwenda John Mapulu alimshika mkono wakaanza kutokomea taratibu kuelekea walipojua wao lakini Michael alikuwa kama kipofu anayefuata mkondo.

    Hatua kadhaa mbele Michael akiwa ameamini tayari wapo huru bila kupata usumbufu wowote katika giza walimkuta askari aliyekuwa lindoni akiwa amejiegemeza ukutani, John akamshtukia kuwa tayari alikuwa ameuchapa usingizi maeneo yale ilisikika harufu kali ya bangi bila shaka kabla ya kusinzia askari yule alivuta misokoto kadhaa ya mmea huu halali katika nchi ya Jamaika.

    Michael ambaye muda wote alikuwa anatetemeka alimshuhudia John akinyata kwa tahadhari kubwa na kumrukia yule askari kilichofuata ni kitendo cha John Mapulu kuwa juu ya askari huku mikono yake ikiwa imelikamata koromeo la huyu kiumbe barabara, baada ya dakika kadhaa akamwacha huru, licha ya kuachiwa huru hakuweza hata kusema neno. Alikuwa maiti!!!

    “Washenzi sana hawa!!!” alisema John kisha akampa ishara Michael amfuate, wale waliofungua mlango na akina John wakatoka walikuwa wamepita njia nyingine pamoja na wale wawili wenye kesi ya bunduki waliopata upenyo wa kutoroka pamoja na John baada ya kuamshwa wasaidie kufungua mlango. John tayari alikuwa na bunduki mkononi nani wa kumtisha kiumbe huyu hatari linapokuja suala la kutumia bunduki!!!! Michael alijiona muuaji na anayezidi kupotea njia pumzi za uhuru alizozikurupukia sasa zilikuwa zinamuwasha zaidi ya kawaida. Hatua kwa hatua, mtaa kwa mtaa, hatimaye walikuwa katikati ya kundi la raia wema ndani ya daladala zinazoelekea Nyakato Mecco nje kidogo ya jiji la Mwanza.

    Michael bado alikuwa kipofu!!!



    ****



    Geti dogo lilifunguliwa kidogo, baada ya kuhakikisha aliyetegemewa kuingia ndiye alikuwa mlangoni lilifunguliwa zaidi.

    “Mheshimiwa Mapulu!!!! Karibu nyumbani…..kama ndoto vile” sauti nzito ya kiume ilimlaki John aliyejibu kwa tabasamu hafifu.

    “Matha yupo au na yeye alikamatwa??” John aliuliza wakati huo ilikuwa yapata saa kumi adhuhuri.

    “Matha yupo lakini anakamuliwa na mshkaji mwingine” Alijibiwa kwa njia ya utani akaling’amua hilo akatoa kicheko kidogo.

    “Dogo langu hili, linaitwa Michael Msombe muite Dabo M,ukishindwa kabisa muite Dabo” John alimtambulisha Michael kama mtu ambaye anamfahamu siku nyingi sana. Akambatiza jina la Dabo.

    “Mambo vipi bro!!!” alisalimia Michael

    “Poa Dabo naitwa Bruno…karibu sana”

    “Asante sana” alijibu na geti likafungwa.

    Haikuwa nyumba iliyotangaza umasikini hata kidogo lakini ilionyesha matumizi mabaya ya pesa kwa samani zisizokuwa na shughuli maalumu kulundikana pale ndani, usiku ule hakuona mtu yeyote zaidi ya Bruno akahisi huenda wamelala wengine lakini haikuwa hivyo hadi panapambazuka hali ilikuwa hivyohivyo.

    Michael alishangaa lakini hakuuliza. Asubuhi yule John wa selo aliyekuwa akishindia kapensi kafupi kalikochakaa na wakati mwingine kumwacha uchi wakati akigombania vyakula walivyoletewa mahabusu wengine hakuwa yule tena alikuwa ameng’ara ndani ya nguo ya kulalia rangi nyeupe kabisa mkononi alikuwa na kikombe kikubwa kilichoongezwa uzito na maziwa yaliyokuwa ndani yake. John alikuwa tofauti sana hata rangi yake ilikuwa si ile iliyochafuka na kukosa maji ya kuoga walipokuwa selo.

    “Michael kuna mtu yeyote aliyekuwa anafahamu uwepo wako ndani ya selo??.”

    “Mh!!!! Hapana sidhani” alijibu baada ya kujaribu kufikiri

    “Una uhakika kuwa hujawahi kuja kusalimiwa???”

    “Hakuwahi kuja mtu yeyote pale kaka, we ulikuwa shahidi” aliendelea kusisitiza. John alitikisa kichwa ishara ya kukubali kisha akaifuata rimoti na kuitazama luninga kuubwa bapa iliyokuwa inamtazama kisha akaminya kitufe ikawaka, hakujishughuisha kuangalia ni chaneli ipi iliyokuwa inaupiga mziki wa zook, akajiondokea.

    “Michael!!! Una uhakika na unalosema???” aliuliza tena macho yake mekundu yakiwa yanautazama mdomo wa Michael.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Swali hilo likamshtua Michael kwa nini lilikuwa likiulizwa sana, safari hii akachelewa kidogo kujibu

    “Siku ile nilimpa namba za msichana mmoja yule afande sijui kama alipiga ama la lakini hakuwahi hata kuja pale mahabusu.” alijibu kwa sauti iliyokuwa na hofu

    “Nipe namba ya huyo msichana na kuwa makini sana wakati mwingine unapojibu swali sawa!!!” alifoka kidogo John na Michael akakubali bila kuzungumza chochote. Baada ya kumtajia akaondoka, jambo la kushangaza ni kwamba John akuuliza mara mbilimbili na wala hakuandika hiyo namba mahali popote pale, ni kama alikuwa ameipuuzia hata Michael aliamini hivyo.

    Siku hiyo ilipita huku Michael akipewa nguo za kubadilisha ambazo zilimkaa sawa kwenye mwili wake, japokuwa alikuwa na mawazo sana hakusita kukiri kwamba aliifurahia hali ya kuwa huru.



    ****



    Majibu ya askari aliyekuwa na wasiwasi mkubwa machoni mwake yalimkera na kumshangaza sana Joyce Keto, alishindwa kuelewa kwamba ni kweli aliyezungumza naye kwenye simu alikuwa ni askari ama ni mtu alimletea utani. Kwa ghadhabu aliondoka kituoni pale.

    Kwa nini nisimpigie simu huyo aliyejifanya askari!!! Alijiuliza Joyce huku akitembea kwa ghadhabu hakuwa na uhakika kama alikuwa akiyumba yumba ama la alichotambua ni kuwa alikuwa akisonga mbele. Moja kwa moja katika duka lililokuwa linauza vocha.

    “Nisaidie Tigo ya mia tano!!” alisema Joy na mwenye duka akampatia baada ya kuwa ameisugua. Bila ya kujua ni mara ngapi alikuwa ameingiza ile vocha bila kuwa na umakini aishtushwa na ujumbe uliomtaarifu kuwa namba yake ya simu ilikuwa imefungiwa kutokana na kuingiza namba zisizokuwa sahihi, Joy alitamani kulia, aliitazama simu yake kwa jicho la hasira kama ni yenyewe ilikuwa imefanya makosa hayo ili kumkomesha. Kwa mwendo wa kukata tamaa akaanza kuondoka lakini akasita tena na kurejea dukani.

    “Makao makuu ya tigo ni wapi, samahani lakini!!!”

    “Bila samahani malkia!!....” alizungumza kwa lafudhi ya kichaga na kisha akamuelekeza Joy wapi ambapo kampuni hiyo ya simu imeweka makao yake.

    “Asante sana….kwaheeri!!!” aliaga.

    Mwanzoni wazo lake lilikuwa kuondoka moja kwa moja na kuelekea hapo alipoelekezwa lakini njaa ilimkatisha kufanya hivyo, jicho lake liliangaza huku na huko kisha akajifikiria kwa muda pesa aliyokuwa nayo ilimruhusu kula wapi jibu likapatikana kuwa alitakiwa kula chakula cha bei poa sana ili mambo yaende sawia. Mama Fredi mgahawa jipatie chakula safi hapa.

    Maandishi hayo yaliyoandikwa kwa mkaa yalimfanya Joyce atabasamu kisha akajiambia “Mahali sahihi pa Joyce kupata chakula chake kwa siku ya leo.” akanyata na kuingia kwa mtindo wa kuinama hadi akapata nafasi yake. Bila hata kutaja ni chakula gani alikuwa anahitaji alishangaa mbele yake ukiwekwa wali uliochanganywa na maharage, nyama moja, mchicha na kipande kidogo cha bilinganya, hakutaka kuhoji aliamini huo ndio utaratibu wa mgahawa wa mama huyo aliyekuwa muongeaji sana. Huenda hata ndio sababu ya kuvuta wateja wengi sana katika genge lake.

    Baada ya kujiridhisha nafsi yake na chakula hicho kilichomgharimu shilingi elfu moja Joyce Keto alinawa mikono yake na kuondoka.

    “Ngoja niandae mahali pa kulala kwanza maana dalili zote zinaonyesha kuwa nitalala Mwanza, na huu ugeni nisije nikapata tabu baadaye.” alijishauri na kukubali ushauri huo akaanza kuhangaika huku na huko hadi alipopata nyumba ya kulala wageni iliyomgharimu shilingi elfu kumi ikiwa na choo na bafu ndani.

    Hakudumu sana katika chumba hicho baada ya kukizoea kwa dakika kadhaa wazo la kurejea tena Tigo lilimrudia, lakini kabla ya yote alijiweka maliwatoni na kuupasha mwili wake kwa maji baridi nguvu zikamrejea na uchangamfu ukachukua nafasi yake. Kosa dogo alilofanya Joyce liligeuka kuwa kubwa, ni baada ya kujiegesha kitandani na usingizi kumpitia. Alikuja kushtuka jioni ya saa kumi na moja.

    Tayari huduma alizotaraji kuzipata tigo hazikuwezekana palikuwa pamefungwa tayari.

    “Hee!! Saa kumi na moja.” alipayuka kwa nguvu akiwa pale kitandani lakini hakuwepo wa kumjibu hoja yake iliyokuja kwa mtindo wa kushtukiza. Alisimama kama anayetaka kuondoka ili awahi kitu lakini alirejea kivivu pale kitandani hakuwa na pa kwenda. Alijilaza pale alipotoka na kumkaribisha tena jinamizi wa usingizi lakini kabla hajachukua kiti na kuketi simu yake ya mkononi iliita. Ilikuwa namba mpya!! Mh!! Atakuwa mama yake Michael ama…sasa kwa nini atumie namba mpya…au!!!” alijiuliza bila kupata majibu, simu ikakatika!! Mara ikaanza kuita tena

    “Hallo!! Mambo vipi dada Joy” upande wa pili ulianza kubwabwaja

    “Poa nani mwenzangu samahani nilipoteza….”

    Mimi Fredrick, haunifahamu lakini” ilimkatisha sauti ile baada ya kueelewa kuwa alitaka kujitetea kwa kudanganya.

    “Wa wapi wewe??”

    “Mwanza nimepewa namba yako na Michael yupo matatizoni, umeenda kumwangalia polisi???” iliuliza sauti ile kwa utulivu

    “Nimeenda lakini sijamkuta….”

    “Wamekwambiaje kwani??”

    “Wamesema tu hayupo mi nikaondoka zangu”

    “Dah!! Hata sisi wametwambia hivyo..wewe upo wapi sasa maana sisi wenyewe wageni hapa Mwanza”

    “Mimi pia mgeni lakini nipo hapa Mitimirefu sehemu inaitwa Resting house, ukishuka tu hapa kituoni unapaona nadhani panafahamika” alijieleza Joy huku akiwa na furaha ya kupata wenzake katika vita moja. Alitambua kuwa ni kaka zake na Michael.

    “Haya kama tukiweza tutafika, kwa lolote lile tufahamishane sawa!”

    “Msijali nitapenda sana mkifika” alisisitiza Joy. Simu ikakatwa.

    Baada ya saa zima akiwa anafanya tafakari mbili tatu alishtushwa na mlango wa chumba chake kugongwa kwa utaratibu maalum.

    “Nani tena muda huu!!!” alijiuliza huku akiuendea mlango na kuufungua.

    “Una vitu vingine zaidi ya huo mkoba mezani??” lilikuwa swali kutoka kwa sura hizi mbili ngeni kabisa machoni mwa Joy.

    “Nyie ni akina nani??” aliuliza lakini hakujibiwa.

    “Tuondoke haraka eneo hili” aliambiwa

    “Twende wapi…nyie ni akina nani???”

    “Ndugu zake Michael, chukua vyako tuondoke”. Joyce akatii amri na kukusanya vilivyo vyake na kuanza kuondoka hadi kwenye gari ndogo aina ya corolla safari ya kuelekea asipopajua ikaanza.

    “Shem ujue nini yaani hii hali inashangaza sana mh!! Kumbe kweli anayekwenda jela si lazima awe na hatia…” baada ya kimya alikuwa ni John ambaye alikwa anajulikana kwa jina la Fredrick aliyeuvunja ukimya pale ndani. Mh!! Nimekuwa shem tayari!! Alijiuliza Joyce na kumalizia kwa tabasamu la kulazimisha bila kusema lolote.

    Baada ya mwendo kidogo John alitoa pipi na kuwagawia wote waliokuwa pale ndani, ni Joyce pekee aliyekurupuka na kuibugia pipi ile, baada ya sekunde kadhaa usingizi mkali ulianza kuyafumba macho yake alijaribu kupambana bila mafanikio kuidhibiti hali ile, dhahiri alionekana kutambua janja hiyo iliyokuwa imechezwa dhidi yake lakini haukuwepo ujanja wowote ule Joyce akapitiwa na jinamizi la usingizi mkali sana.

    Alikuwa amewekewa dawa za usingizi katika pipi!!!.

    Alikuja kushtuka masaa manne baadaye na kujikuta katika chumba kikubwa cha haja ambacho kilikuwa na hewa safi sana yenye ubaridi bila shaka palikuwa na kiyoyozi.

    Joyce alijinyoosha nyoosha huku akiyapikicha macho yake ili kujiweka sawa. Hapa ni wapi?? Alijiuliza, lakini kabla ya kupata jibu alisikia mlango ukifunguliwa kisha akaingia John ambaye alijitambulisha kwa Joy kama Fredrick.

    “Mambo vipi Joy naitwa John….jisikie huru upo nyumbani” John alijitambulisha kwa Joy ambaye bado alikuwa anashangaa.

    “Nimefikaje hapa….hapa ni wapi??” aliuliza Joyce, John ambaye alikuwa amevaa pensi pamoja na fulana kubwa iliouzidi mwili wake huku miguuni mwake akiwa na raba nyeupe.

    “Hapa ndio nyumbani kwetu karibu sana” alisema John huku akiachia tabasamu hafifu.



    *****



    Michael Msombe alikuwa ametekwa na sinema aliyokuwa anaangalia katika luninga kubwa iliyokuwa sebuleni, hakupatwa na ukiwa wowote kwa kuondoka John na Bruno. Mdadi ulikuwa umemshika pale jambazi kuu lilipokuwa likipigwa na nyota wa filamu hiyo ambaye alikuwa ni Jackie Chan, Michael alikuwa ni kama amezama na kuwa mmoja wa wahusika wa filamu hiyo hadi pale aliposhtuliwa na kikohozi cha kujilazimisha kutoka katika upande wa mlango wa kuingilia.

    Macho yake yalihama kutoka katika luninga na kuelekea pale mlangoni.



    Alikuwa ni msichana ambaye hakuna mwanaume ambaye angesita kumuita mrembo, nguo fupi aliyokuwa amevaa iliyaruhusu mapaja yake meupe kuchungulia nje, wepesi wa kitambaa cha nguo hiyo ulionyesha mchoro wa chupi aliyokuwa amevaa ikiwa katika mfumo wa bikini, kinguo cha juu saizi ya mtoto wa miaka minne kilihalalisha nusu ya tumbo lake kuwa nje. Matiti yake kifuani yalikuwa na uwezo wa kukinyanyua kinguo hicho kwa umbali mdogo sana huku ule mchomo wa mbele ukionekana kumaanisha kamwe hajawahi kunyonyesha.

    Sauti ya Michael ilipotea kabisa akajaribu kuilazimisha irejee ili aweze kumsalimia huyu kiumbe lakini iligoma kabisa. Akagundua kuwa alikuwa ameingiwa na tamaa.

    “Mambo!!!!” alisalimiwa Michael kwa sauti laini sana iliyopenya katika masikio yake kisha katika koo na kuilainisha sauti yake hatimaye akajibu

    “Safiii….karibu!!!” yule binti akaanza kusogea mahali alipokuwa ameketi Michael akimaanisha ameitikia wito, sehemu zake za nyuma zilikuwa zinatikisika kila hatua aliyopiga. Bila kutambua Michael akajikuta ameingia katika hisia nyingine na maungo yake kujikuta yakiinyanyua suruali yake, kwa haraka sana alichukua kitambaa kilichokuwa mezani na kujifunika lakini alikuwa amechelewa sana. Tabasamu zito kutoka kwa yule binti lilimpumbaza akabaki kama zoba.

    “Naitwa Matha….unanifahamu sijui???...lakini haunifahamu”

    “Yeah!! Sikufahamu nadhani”

    “Ni mchumba wa John..unamjua??”

    “Ndio John namjua!!!”

    “Wewe unaitwa Michael eeh!!!”

    “Umenijuaje kwani???” badala ya kujibu Michael aliuliza huku macho yake yakiendelea kumchunguza kwa chati binti huyu.

    Matha Mwakipesile alikuwa amepewa jukumu kubwa la kumfundisha Michael jinsi ya kutumia silaha mbalimbali, John alikuwa ameamua kumchukua rasmi Michael katika shughuli zake za ujambazi.

    Matha alimueleza Michael kwa utaratibu kabisa jukumu alilopewa, hali ya Michael iligeuka kuwa ya uoga sana hakuamini kuwa binti mrembo kama Matha anaweza hata kuwa na uwezo wa kushika bunduki sembuse kisu na kuua mtu. Mh!!! Usione ukadhani. Alisema kimya kimya Michael.

    Somo alilopewa na Matha halikuwa limemuingia hata kidogo, aliamini sasa alikuwa anapelekwa njia asiyoitaka hata kidogo. Kutoroka!!! Ndio wazo kuu lililomjia lakini atatoroka na kuelekea wapi. Akiwa bado katika mawazo hayo mara aliingia Bruno alikuwa mwingi wa furaha iliyojionyesha waziwazi, alimsabahi Michael kisha akaingia chumbani na kurejea tena baada ya muda mfupi akiwa amebadilisha nguo zake.

    “Bruno nahitaji sana kwenda nyumbani, nimekaa hapa imetosha nadhani mama atakuwa akinitafuta sana.” Michael alimwambia Bruno baada ya kuwa amekaa kitako.

    “John anakuja muda si mrefu utamweleza nadhani itakuwa vyema zaidi mi sijui lolote kuhusu wewe na John” alijibu kwa sauti iliyokuwa na uulizi ndani yake, Michael akatambua kuwa Bruno ameshtuka.



    Baada ya masaa kadhaa John alifika na baada ya kuzungumza pembeni na Bruno alimfuata Michael.

    “Nimeambiwa ombi lako si baya sana, lakini kabla sijakuruhusu naomba nikukumbushe kitu, unakabiliwa na kesi ya kumuua askari pale kituoni, una kesi kubwa ya kutoroka mahabusu hivyo umehalalisha kuwa ni wewe uliyemuua binti uliyekuwa naye nyumba ya kulala wageni, hizo ni kesi chache za halali zinazokukabili sijui kama zipo za ubakaji na wizi kwa kutumia silaha…kwa ufupi unarudi mtaani kupambana na hukumu ya kunyongwa baada ya fedheha ya kufanywa mke wa mtu gerezani….kama unaamini unaweza kupambana na haya yote peke yako mimi nitakusaidia nauli kesho uende mdogo wangu hata usijali.” alieleza John huku macho yake yakiwa yameutazama uso wa Michael aliyekuwa anaukwepesha uso wake kila anapogundua kuwa John anamwangalia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kumaliza kuzungumza hayo John aliyanyuka na kuondoka zake akimwacha Michael akiwa ameduwaa. Neno alilokuwa akilirudia mara kwa mara John kuhusu kuolewa na wanaume wenzake ni hilo lilimsumbua akili Michael hakuwa tayari hata kidogo kwa hiyo fedheha. Macho yalikuwa yamemtoka pima, aliingiwa na hofu ya kutoroka kwa mara ya kwanza!!.

    “John!!! Kaka John.” aliita Michael kwa nguvu wakati John akikaribia kutokomea.

    “Sema dogo!!!”

    “Naomba basi walau niwasiliane na mama najua ananitafuta sana mh!!.”

    “Polisi sio wajinga kama unavyodhani…wewe unamuwazia mtu ambaye kwa sasa anawasaidia upelelezi wa kujua wewe ulipo??? Wewe kumuona mama yako haina tofauti na kuonana na polisi” alijibu John Mapulu kisha akacheka. Neno hilo nalo likamshtua Michael na kuamini kuwa lilikuwa na ukweli ndani yake na mama yake huenda anaweza kumsaliti.

    “Kwa hiyo hata Joyce Keto anaweza kuwa anasaidiana na polisi?.” alijikuta akiuliza.

    “Tena kwa ukaribu sana…nakutakia safari njema Michael” alifungua mlango na kuingia ndani.



    Kesho yake Michael hakuondoka!!!!!



    ****



    Moshi wa bangi na sigara vilianza kuizoea damu yake, sumu ya maneno aliyokuwa akilishwa na John Mapulu sasa ilikuwa imesambaa ndani ya damu yake, aliwaona watu wote wanaomzunguka kuwa ni maadui hasa hasa askari.

    John alimwelezea Michael jinsi polisi wanavyoua raia wema hovyohovyo, alimpa mikasa mbalimbali ya kutisha hivyo kuikoleza hoja yake kuelekea kwenye ukweli. Taratibu Michael akaanza na sigara hatimaye akajiunga katika mkumbo wa wavuta bangi, kwa jitihada zote aliyapinga matumizi ya unga hilo pekee ndilo alilipigania hadi mwisho.



    Mwanzoni alikuwa msindikizaji katika shughuli walizokuwa wakienda kufanya akina John sehemu mbalimbali katika jiji la Mwanza kila baada ya shughuli alipewa nafasi ya kuuliza maswali mawili matatu. Kwa kuwa Michael alikuwa mwingi wa maswali hii ilimuwezesha kuelewa mambo mengi sana katika kipindi kifupi mno.



    Tayari alijua mbinu za kuvunja maduka, kuiba magari, na mbaya na kubwa somo la matumizi ya silaha lilikuwa limemkolea.

    John Mapulu hakuwa mtu wa masihala linapokuja suala linalomuhusu moja kwa moja, jambo hili hata Michael alilitambua upesi sana kadri alivyokuwa akiishi naye karibu. Mahusiano yaliyokuwepo kati yake na Matha (mpenzi wa John) katika kufundishwa jinsi ya kutumia bunduki yalikuwa yameanza kuvuka kiwango, nafsi ya Michael baada ya kumtamani Joyce Keto bila mafanikio ya kumpata, Joyce mwingine aliyefariki bila kuwa ameelewa azma ya Michael, sasa Michael alikuwa anamtamani Matha japo pia alikuwa hajamwambia, kila siku alikuwa akijizuia na kuuonya mdomo wake usije ukamponza.

    Aliamini kwa kumtamkia Matha kuwa anampenda ni sawa na kuanzisha vita na John Mapulu, vita kubwa ambayo wala hakuwa na ubavu wa kuicheza. Wakati fulani Michael aliamini Matha amewekwa karibu yake ili kumchunguza tabia zake hivyo alikuwa makini sana asiweze kuzionyesha hisia zake kwa mrembo huyu.



    Matha hakuisha kumvalia nguo za mitego Michael kila wanapokuwa wawili katika chumba maalumu cha mafundisho hayo.

    Siku hii jioni tulivu kabisa John na wenzake wakiwa wameingia katika tukio la kuiba pesa benki ambapo hawakutaka kuandamana na Michael kwa sababu ya uchanga wake katika masuala ya uharifu pia hawakuwa na mtaalamu wao wa kike Matha Mwakipesile aliyedai kwamba akili yake haikuwa barabara siku hiyo. Michael kama kawaida akiwa katika burudani yake ya kuangalia filamu, mwilini akiwa na pensi fupi na fulana iliyokatwa mikono alishtuliwa ghafla na ujio wa Matha pale ndani.

    “He!! Mwalimu vipi….pole aisee nasikia unaumwa??.” Michael alimuanza Matha ambaye kwa sasa walikuwa wamezoeana sana.

    “Mh!! Kakwambia nani??”

    “Ah!! Nimesikia tu!!!” alijibu huku akisimamisha hiyo filamu kupisha maongezi yake na Matha.

    “Ok!! Twende darasani” Matha alimwomba Michael naye akafuata bila ubishi, darasa alilokuwa akipewa na Matha lilimvutia kuipenda bunduki. Walipofika chumba hicho maalumu somo lilianza kama kawaida lakini hawakuchukua muda mrefu Matha akabadili hali ya hewa ya hapo ndani, ni wakati akimfundisha Michael jinsi ya kulenga shabaha akiwa kwa nyuma yake mkono wake wa kushoto ukiwa umekizunguka kiuno cha Michael, zoezi lilisimama ghafla baada ya wawili hawa kujikuta hawaitazami bunduki ila wanatazamana machoni wakiwa wametwaliwa na dalili zote za mahaba mazito.



    Mapigo ya moyo ya kila mmoja yalikuwa juu sana, taratibu bunduki ikatuliwa chini, Matha kwa kuutambua uoga wa Michael yeye mwenyewe akajitoa muhanga kusogeza papi (lips) za mdomo wake hadi zikagusana na za Michael, akaupenyeza ulimi wake katikati ya papi za Michael na yeye akaupokea taratibu. Michael alikuwa anatetemeka sana lakini baada ya ndimi zao kukutana akauvaa ujasiri, hapakuwa na godoro pale ndani hivyo wakajikuta katika sakafu iliyokuwa na vigaye, kivazi alichovaa Matha ni kama alimaanisha kitu kwani baada ya kuanguka chini alikigusa nacho mara moja mikanda ikaachia wawili hawa wakawa katika ulimwengu wa mahaba mazito.





    Matha yule ambaye ana uwezo wa kuua binadamu dakika yoyote ile katika mapambano sasa alikuwa amelala chali mshindi akiwa ni Michael katika kifua chake. Raha walizozipata waliweza kuzielezea wao peke yao maana hapakuwa na shahidi pale ndani zaidi ya mtutu wa bunduki. Hiyo ilikuwa ndiyo siku ambayo Michael kamwe hataisahau kwani ile hali ya kujiamni mbele ya John alihisi inapungua huku akihofia siri hiyo iwapo itavuja ni jinsi gani John atakisambaratisha kichwa chake.

    Kwa upande wa Matha hakuonyesha mabadiliko yoyote, hakuwa na uoga hata chembe, na siku iliyofuata alifika hapo nyumbani kwa ajili ya kumfundisha Michael. Darasa likageuka ukumbi wa ngono, Michael alipewa onyo kali.

    “Ukikataa tusiendelee kufanya nitamwambia John kuwa unanisumbua kimapenzi, usidhani kuwa atakuhoji kama ni kweli ama la…atakachofanya atachukua bunduki kama hivi na kukufyatua kichwa chako, kama akiwa na huruma sana atakuwekea sumu ufe usingizini….vipi upo tayari kufa??” Matha alimwambia Michael kwa sauti iliyojaa majivuno. Michael hakuwa tayari kufa hivyo akaingia rasmi katika utumwa wa ngono na mpenzi wa muuaji hatari, tena katika nyumba ya muuaji. Raha alizokuwa akizipata wakati wakipashana miili yao joto ilikuwa inayeyuka kila alipokuwa akimfikiria John siku akiugundua huo mchezo mchafu unaoendelea.



    *****



    “John leo nitampeleka huyu dogo kwa mafunzo ya shabaha kule pori!!! Usiku” Matha alimweleza John Mapulu ikiwa majira ya asubuhi baada ya kuwasili pale nyumbani kwa John.

    “Vipi lakini uelewa wake anaweza kuingia mzigoni?” Badala ya kujibu naye aliuliza

    “Kiaina lakini si wa kuingia mzigoni kwa sasa. Ni moto wa kuotea mbali akishaiva vizuri” Matha alimsifia Michael. Wakati huo na Michael naye alikuwepo pale sebuleni, hakutaka kumwangalia John wala Matha. John alianza kudhani Michael ameogopa sana kusikia habari za porini usiku, wakati Matha alijua kwa nini Michael hakutaka kuwatazama usoni.

    Msichana gani huyu hana hata chembe ya aibu!!! Aliwaza Michael.

    “Kwa hiyo twende wote ama utaenda na Bruno!!!” aliuliza John

    “Mwenyewe ninatosha hata usijali hatutachukua wakati sana, isitoshe Michael si mkorofi” alipanga maneno yake Matha kama karata na yakakubaliwa bila chembe ya wasiwasi na John.

    Wakaondoka



    *****



    Pori kubwa na zito ambalo Michael aliyepelekwa huku akiwa amefunikwa kitambaa usoni, hakulitambua hata kama asingekuwa na kitambaa usoni kwani alikuwa mgeni Mwanza. Walifika porini Michael akiwa na wazo moja tu la kutoroka kabla mambo hayajawa mabaya kwa upande wake, azma ya kuchangia mwili mmoja na mtu mkatili kama John ilikuwa inamtafuna kwa fujo, mwili wake ulioanza kunawiri kutokana na mlo safi na kamili aliokuwa anaupata pale kwa John sasa ulikuwa unaanza kufifia tena.



    Matha yeye ni kama raha hizo zilimkubali kwani alizidi kunawiri na kuongeza mvuto wake. Matha alisimamisha gari ndogo aina ya Cresta Michael akashuka na yeye akashuka, hakuwa na wasiwasi wowote juu ya Michael kwani alijiamini kupita maelezo katika suala la kujihami kwa kutumia viungo vya mwili mafunzo aliyoyapata kabla ya kuliasi jeshi la polisi miaka kadhaa nyuma. Nia ya Michael ilikuwa kutoroka lakini hakuona hata njia moja ya kuweza kumtoa pale katika lile pori.

    Nitazua mengine hapa!! Aliwaza na kusubiri kuona kilichokuwa kinataka kuendelea.

    “Michael!!!” Matha alimwita na kumtoa katika ndoto zake zisizo na mafanikio.

    “Naam mama!!!” aliitika kwa nidhamu.

    “Njoo huku mara moja!!!” Michael alitii amri, akamfuata Matha alipokuwa anaelekea, fikra zake ni kwamba alikuwa akienda kufundishwa huko kulenga shabaha. Alipokaribia aliamriwa kurudi kinyumenyume hivyo navyo akatii.

    “Simama!!” Matha aliamrisha, Michael akatii. Matha akamsogelea Michael na kumtia kitambaa usoni.

    “Vipi tena mama??.”

    “Ndio masharti ya kujifunza shabaha” Matha alitoa sauti ya amri lakini isiyokuwa na kujiamini ndani yake. Kimya kilitanda kwa sekunde kadhaa kisha Michael bila kuwa amejiandaa alichotwa mtama na kujikuta yu katika fundo la majani lililokuwa katika mfumo wa kitanda, kisha akafunguliwa kitambaa usoni, kabla hajasema lolote ulimi wa matha ulipenya katikati ya papi za mdomo wake, ule ubaridi wa ulimi wa Matha ukaubembeleza uoga wa Michael hadi ukasinzia na ujasiri ukaamka. Matha alikuwa kama alivyozaliwa na baada ya dakika mbili Michael naye alikuwa hivyo hivyo. Hii siku ilikuwa ya kipekee kwao kwani walikaa porini masaa mengi sana huku bunduki zikiwa pembeni kama nguo zilivyosahaulika na miili yao ikiwa imenatana.

    “Michael nataka uwe mpenzi wangu!!”

    “Unasemaje Matha??” aliuliza kama vile hajalisikia swali. Matha hakusema tena aliamini Michael amesikia.

    “Hivi unataka niuwawe ndio ufurahie???” Michael alisema kwa sauti iliyojaa hamaki.

    “Hautakufa…akuue nani???”

    “Matha unauliza aniue nani???...wewe umesema John anaua au sikukusikia??” alihoji Michael kwa ghadhabu, tayari alikuwa amejinasua kutoka mikononi mwa Matha.

    “Kama nisipokulinda utauwawa, laini nitakulinda” alijitetea Matha kwa sauti iliyojaa uhitaji wa mahaba.

    “Matha ujue unahatarisha maisha yangu, kwanini tusiuache mchezo huu, John hakupi nini kwani??” alilalamika Michael. Matha hakusema neno akaanza kulia, mwanga wa mbalamwezi ulimruhusu Michael kuishuhuda simanzi hii, hakuamini kama maneno yake ndo yamemkasirisha mrembo huyu, kosa kubwa!!! Alipojaribu kumbembeleza huku akisahau kuwa yu uchi alijikuta tena katika mahaba mazito ambayo baada ya hapo yalizaa tabia ya mara kwa mara kudanganya kuwa wanakuja kwa ajili ya mafunzo na kisha kuubadili uwanja wa mafunzo kuwa uwanja wa mahaba. Chumba cha nyumbani waliona hakiwatoshi!!

    Nachezea sharubu za simba!!!! Aliwaza Michael.

    Lakini angejitoa vipi katika msala huu!!



    ******



    Matha alikurupuka kutoka kitandani alipokuwa amelala na John, mbio mbio alikimbia kuelekea bafuni kuna jambo lilikuwa limemtatiza, lilikuwa jambo geni sana kwake. Alikuwa ana kichefuchefu cha ghafla, hakuwa anaumwa hapo kabla wala hakuwa amekula kitu kibaya usiku uliopita. Alifika na kutapika bafuni, kichefuchefu kikapungua hakutaka tena kurudi kitandani alioga kabisa na kuingia katika chumba kidogo cha mazoezi. Kichefuchefu kikamrudia tena safari hii hakutapika baada ya kukikabili kwa kulamba limao alilolitoa katika jokofu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kichefuchefu kikamkimbiza hospitali siku hiyo!!

    “Matha Mwakipesile ndo wewe eeh!!!.”

    “Ndio ni mimi dokta vipi malaria nini??.” alifanya utabiri usiokuwa sahihi.

    “Hapana hauna Malaria mwanangu..”

    “Mh!! Nini sasa hiki Mungu wangu.”

    “U mjamzito Matha!!!....mwezi mmoja.”

    “Dokta!!! Be serious!!!”

    “Ninamaanisha, vipi kwani hukutegemea au??.”

    “Yaani siamini maana ni wakati muafaka hii zawadi imekuja.” alijibu kwa uchangamfu Matha. Akaaga akaondoka!!!

    Alimanusra apate ajali njiani kwa papara alizokuwa nazo katika kuendesha gari kwa mwendo kasi ili awahi mahali. Hakuwa akienda kwa John lakini alikuwa akielekea kwa Michael aliamini kwa namna kubwa sana yeye ndiye muhusika wa hiyo mimba maana hawakuwahi kutumia kinga hata siku moja. Sijui walikuwa wakijiamini vipi!!!!

    Matha alikuwa na furaha tele kwani ni mwaka wa nne tangu awe na uhusiano na John Mapulu bila dalili zozote za kupata mtoto. Tangu amtoe usichana wake walipokutana katika msiba wa mama yake mzazi na Matha, uhusiano uliokomaa na kudumu kwa miaka hiyo tele, miaka iliyomhamisha Matha kutoka shuleni na kuingia rasmi katika ujambazi. Akiwa kama kipenzi cha John hakumjua mwanaume mwingine hadi anapoingia kati Michael Msombe.

    “Kumbe John hazai!!!” alisema kwa sauti ya chini kama vile kuna mtu pembeni yake alikuwa anamsikiliza.

    “Mbona sasa amekuwa mbinafsi kiasi hicho??? Kwa nini hakunambia kuwa ana matatizo, nimejihisi mpweke na kumlaani mama yangu kwa kunizaa mgumba!!! Namchukia John. Kama alinipenda kwa nini ameificha siri hii??” alilalama Matha bila kupata msaada wowote. Breki za gari yake zikafanya kazi yake alipolikaribia geti kisha injini ikazimwa baada ya gari kuwa limeingia maeneo ya Mecco ndani ya nyumba ya John aliyoishi na Bruno!!! John hakuwepo!!! Lakini Michael alikuwepo.

    “Michael!!!!.”

    “Nambie mpenzi wangu.” Kwa mara ya kwanza Michael akamwita Matha jina hilo kwa kujiamini. Matha akambusu shingoni kimahaba, wakati huo walikuwa katika chumba chao cha mafunzo ya kutumia bunduki.

    “Michael asante sana!!!!.”

    “Asante kwa lipi huishiwi visa wewe mke wa bosi!!”

    “Ah!! Sitaki mie hilo jina utaniudhi sasa hivi!!!” alilalamika kwa sauti ya chini Matha.

    “Basi samahani kipetito” Michael alimwambia Matha huku akichukua kichwa chake na kukilaza mapajani mwa Matha.

    “Michael nina ujauzito.” kama vile aliyepigwa shoti alijikuta akiruka kutoka mapajani mwa Matha na kusimama mlangoni kama anayetaka kukimbia. Matha akaubetua mdomo wake.

    “Matha unasemaaje??.”

    “Kwani ulikuwa unatumia kinga wakati tunafanya??.” Swali la Matha likamfadhaisha Michael akawa kama anayetaka kulia lakini chozi lilikuwa mbali sana, sura yake ikawa kama amepigwa ngumi.

    “Michael nimekwambia nina mimba yako!!!”

    “Sasa Matha hapo mimi nafanyaje unadhani??” alizungumza kwa upole Michael.

    “Nakusikiliza wewe!!!.”

    “Una uhakika kuwa ni ya kwangu???.”

    “Asilimia zote!!!! John hana uwezo wa kuzalisha” alijibu Matha kwa ujasiri

    “Fikiria kwa makini halafu utaniambia tunafanya nini???” alisema Matha kisha akambusu Michael katika papi za mdomo na kumwacha solemba. Mara akarejea na kumkuta Michael akiwa bado amesimama

    “Katika mawazo yako yote sahau kuhusu kufanya arbotion, I won’t!!!”



    *****



    Suala la Matha kumkumbusha Michael kuwa sahau kuhusu kitu kinaitwa utoaji mimba lilimchanganya zaidi Michael. Kila alipofikiria kuhusu tatizo la John la kutokuwa na uwezo wa kuzaa Michael alizidi kuchanganyikiwa kwani aliamini kuwa endapo John ataigundua mimba aliyonayo mpenzi wake (Matha) basi mshukiwa wa kwanza kabisa ni yeye (Michael) hilo halikuwa na kipingamizi chochote.

    “Na ikiwa hivyo basi nimekwisha mie!!!” Michael alisema kwa sauti ya chini huku kijasho kikipenya katika vinyweleo vya mwili wake kutokea kichwani na kuweka michirizi katika mashavu yake.

    Michael hakutafakari na kupata jawabu lolote la maana akaingia chumbani kwake akajiegesha kitandani. Akapitiwa na usingizi!!!

    Majira ya saa mbili usiku ndipo alishtuka, mang’amung’amu ya usingizi yalikuwa yakimyumbisha alikuwa akiyapikicha macho yake ili aweze kuona mbele vizuri wakati huo alikuwa anauendea mlango wa chumba chake aweze kuufungua na kutoka nje kiu kilikuwa kimemshika. Alipoufungua mlango ni kama alikuwa amemfungulia mtu ambaye bado alikuwa hajaomba kufunguliwa, Michael alikurupuka kama aliyekuwa amekabwa na jinamizi kisha ghafla akawa ameachiwa. Alikuwa ni John!!

    “Vipi dogo….” John aliuliza

    “Ahh!! Ni usingizi tu kaka vipi…aah!! Nilikuwa nimelala si unajua” alijibu pasipo kujiamini kijana huyu.

    “Jiandae tutoke!!!..nakupa kama dakika kumi na tano fanya fasta” John alimuamuru Michael. Wasiwasi ukamuandama Michael, hakujua huo mtoko ulikuwa wa kwenda wapi. John hakuwa katika mavazi ya kikazi, bali alikuwa ameitundika suti yake nyeusi iliyombana kiasi na kuonyesha kifua chake kilivyoachana katikati, kwa ndani alikuwa na shati jeupe, kiatu cheusi chini kilihitimisha kumfananisha John na bwana harusi na wala si jambazi mzoefu. Hivi tutakuwa tunaenda wapi?? Alijiuliza Michael.

    Hakuwa na wa kumpa jibu akaghairi kuliendea jokofu ili apate maji akapiga hatua kadhaa bafuni ili aweze kuoga, hata hivyo ubaridi wa maji ulimsababisha ajijengee hoja kwamba alikuwa msafi na kuhalalisha maamuzi ya kuacha kuoga. Badala yake akanawa uso kujitoa ile ladha ya usingizi usoni mwake, kisha akaliendea sanduku lake lililozuia zipu isijifunge kutokana na wingi wa nguo akatwaa jinsi ya bluu na fulana nyeupe akazitua katika mwili wake baada ya kuwa ametanguliza singlendi nyeupe kwa ndani, kisha akamalizia na raba iliyotawaliwa na weusi kiasi kikubwa na weupe ukichukua nafasi ndogo. Miwani aliyoivaa ilikuwa imempendeza sana kwani ilirandana na kiatu lakini usiku haukuwa wakati muafaka wa kuvaa miwani hiyo, baada ya kugundua hilo aliivua na kuirejesha mahali pake. Marashi!! Alikumbuka wakati anataka kutoka, haraka haraka alirejea na kupulizia kwa chati, aliporidhika akatoka na kuelekea sebuleni.

    Hakuwa na haja ya kujitazama kwenye kioo, alikuwa amependeza!!

    “Umejiandaa fasta sikutegemea maana nimekushtua sana!!!”

    “Nimekacha kuoga!!! Ndo maana nimewahi” alijibu Michael huku akikaa katika ncha ya sofa.

    “Twende zetu, huyu Bruno sijui atakuwa wapi muda huu??”

    “Hata sijui maana tangu nimelala dah!! Wewe wakati unakuja pale ndo na mimi nilikua naamka, masaa kama manne hivi nilikuwa mfu”

    “Shwari…tutampigia simu.” alijibu John huku akitangulia na Michael aliyetawaliwa na walakini akimfuata kwa nyuma hadi kwenye gari. Michael hakuingia kwanza alifungua geti gari ikatoka kisha akafunga ndipo akalifuata gari na kupanda.

    “Aaah!! Tafadhali bwana mdogo yaani mi nimekuwa dereva wako!!!” alizungumza John kimasikhara baada ya Michael kukaa siti ya nyuma, haikuwa mara ya kwanza Michael kumsikia John akisema hivyo, mara moja akahamia siti ya mbele. Kabla hajakaa John aliondosha pakiti ya sigara iliyokuwa imebakiwa na sigara tatu ndani yake, hiyo ilimaanisha kuwa sigara takribani kumi na saba zilikuwa zimezama na kutoka katika mapafu ya John. Alipenda sana sigara bwana John!! Michael bila kuomba alitwaa naye sigara moja akaiwasha na kuanza kupuliza moshi ndani na nje. Na yeye tayari alikuwa ameathirika japo sio sana na utumwa huu wa sigara.

    John alikuwa makini na usukani, kutokea pale Mecco alipinda kushoto kuifuata hoteli na bar ya Cheers kisha akakata kulia akiipita stendi ya Mecco na kuifuata barabara iendayo Nyakato sokoni, hapakuwa na masumbufu ya foleni za hapa na pale hivyo waliwahi sana kufika, baada ya kufika Nyakato sokoni gari ilikata kushoto baada ya kuwa imeingia barabara kuu ya Mwanza maarufu kama Nyerere road, gari liliondoka kwa mwendo mkali lakini salama kuelekea Igoma, NDAMA HOTELS ndipo kilikuwa kituo cha mwisho ambacho John alisimamisha gari lao dogo aina ya corolla. Wakati huo Michael alikuwa anamalizia kipisi kidogo cha sigara ya mwisho wakati wanashuka garini. John hakuwa katika hali ya uchangamfu hali hii ilizidi kumtia mashaka Michael.

    “Vipi ina maana amegundua kinachoendelea ama kuna jambo gani linaendelea hapa??” alijiuliza Michael wakati huo John alikuwa akiangaza ni wapi wanaweza kukaa kwa utulivu. Walipata mahali palipokuwa na utulivu walioutaka wakaketi.

    “Karibuni!! Karibuni sana” sauti ya muhudumu wa kike aliyetawaliwa na tabasamu bandia usoni maalum kwa ajili ya kazi aliwalaki wawili hawa.

    “Asante sana…tutakuita tukikuhitaji!!!” alijibu John bila kumuangalia binti huyu usoni. Binti hakujibu kitu bali tabasamu lake liliyeyuka ghafla akaanza kuondoka.

    “Hey!!....Mimi niletee Kilimanjaro, iwe ya moto tafadhali” aliamuru Michael

    “Naomba 1800….” Alijibu yule dada ambaye sasa lile tabasamu lililopotea ghafla baada ya kuambiwa ataitwa baadaye sasa lilikuwa limerejea maradufu. Michael hakujibu akamtazama John aliyekuwa ameinama, muhudumu akailewa maana hiyo akamsogelea John bila shaka ni yeye alikuwa na jukumu la kulipia bili.

    “Na mimi niletee Castle lite baridi, leta mbili kabisa.” John aliagiza huku akitoa noti ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi yule binti, akaondoka kwa furaha!! Bila shaka walipokea posho kutokana na idadi ya wateja walioweza kuwahudumia kwa siku.

    “Michael unamuonaje huyu binti!!!.”

    “Kivipi yaani.”

    “Muonekano wake tu!! Ni mrembo eeh!!.”

    “Kiasi chake, namaanisha yupo katikati!!” alijibu Michael huku akimtazama John na kulazimisha tabasamu ambalo halikujibiwa na John.

    “Wasichana wana mambo sana…..” kauli hiyo ikamgutua Michael kimawazo.

    “Kwanini wasema hivyo….” Aliuliza huku akijiweka sawa kwenye kiti chake, viwiko vya mikono yake vikiegemea mezani

    “Unajua unaweza kumpenda sana mtu halafu asitambue upendo wako, akatumia upendo huo kukuadhibu……lakini bado unaendelea kumpenda” alianza kujieleza John

    “Yeah!! Hiyo inawezekana lakini sijaelewa maana ya kauli yako ” aliuliza kwa hofu Michael wakati huu alitoa mikono yake mezani na kuifunga kifuani kwake

    “Michael si unajua kuwa wewe ni rafiki yangu sana?”

    “Naelewa hilo na ni kaka yangu pia kwani kuna nini??” Michael aliuliza huku akijutia kuuliza vile kwani hakutaka kusikia jibu litakalotoka, hatia iliusaga moyo wake, aliamini kwa maongezi hayo John kuna kitu alikuwa kama hajakigundua basi alikuwa amekihisi kati ya yeye (Michael) na Matha. Mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi, fulana yake iliyombana ilimwezesha mtu ambaye hata kama si mchunguzi wa masuala ya afya kuligundua hili.



    “Shiit!!! Nimeacha mguu wangu ndani ya gari!!!” John alijisonya baada ya kugundua amesahau bunduki yake garini, haukuwa utaratibu wake kutembea bila silaha. Lakini hakujisumbua kusimama na kuifuata. Kauli hiyo ilizidi kumtetemesha Michael.

    Ina maana ndio amekuja kunifichulia maovu yangu na kuniua hapahapa!!!! Mungu wangu, lakini nilimwambia Matha kila siku kuwa ananitia matatani ona sasa!!! Aah!! Ona sasa Matha!! Aliwaza Michael kwa uchungu na kuzitupa lawama kwa Matha kabla John hajaendelea kuzungumza

    “Eeeh!! Umeuliza kuwa nina maana gani, ujue Michael kuna wakati unafika lazima kila ukweli uwe wazi na uamuzi ufanyike mara moja, na uamuzi mgumu ni ule unaomuumiza aliyeuamua!!!” John aliendelea Michael akawa kimya, alikuwa amekodoa macho funda la mate alilotaka kumeza ni kama lilikuwa linataka kumshinda, koromeo lilionekana kuwa dogo lakini akajilazimisha likapita.

    Akayakumbuka maneno ya John Mapulu walipokuwa mahabusu!!!

    "Mimi ni mbaya...naua na kusahau mara moja!!"

    Mh!! nimeuawawa tayari.



    ****LAMBALAMBA HUMALIZA BUYU LA ASALI...Michael amemjaza mimba MATHA....mbaya zaidi hataki kuitoa.....itakuwaje?? kwa mara ya kwanza Matha anagundua kuwa John hana uwezo wa kuzaa.

    **** JOYCE KETO yupo wapi??

    ***Na John amempeleka Michael kumueleza jambo gani...JE?? NI SIRI IMEVUJA AMA!!!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog