Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

HATIA - 4

 





    Simulizi : Hatia

    Sehemu Ya Nne (4)





    Mark alishindwa kabisa kuelewa ni namna gani Adrian atamchukulia kutokana na tatizo lililokuwa mbele yake, lakini katikati ya mawazo akaanza kumuogopa Adrian akiamini kuwa ni mtu hatari sana kwake.

    Anamiliki bunduki!!! Hatari sana mtu huyu, alitaka kuniua au kumteka Nunda?? Mbona kizungumkuti!!! Alijiuliza Mark. Kisha akawasha redio kwa sauti ya juu kidogo ili iingilie kati mawazo yake yaliyomzonga kichwani. Haikuwezekana, akainuka na kutoka katika chumba chake akaenda katika baa iliyokuwa jirani akaagiza na kuanza kunywa moja baada ya nyingine.

    Lazima nifanye kitu hapa kabla ya hatari!!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *****



    Defao alizidi kujisahau na kujilinganisha na wafanyabiashara wenye majina makubwa jijini Mwanza, alikuwa hashikiki alitamani kuzimaliza kumbi zote za starehe na pia wanawake wote aliona kuwa ni haki yake kuwamiliki si mke wa mtu ama machangudoa wote alikuwa anawamezea mate na kisha mwisho wa siku alikuwa anatumia pesa zake na kuwapata.

    Alikuwa na wapambe wengi sana ambao walimuheshimu kutokana na pesa aliyokuwanayo, pesa iliyomsahaulisha kuhusu mgonjwa aliyemuacha nyumbani, pesa iliyomfanya amsahau kabisa Minja ambaye ndiye alikuwa amemchorea dili hilo!!!

    Defao akawa mwingine kabisa!!!!

    Defao akawa Defao kweli!!!

    Defao akiwa katika chumba cha kulala akiwa amesaliwa na takribani milioni moja na nusu alijikuta katika dimbwi zito sana la mawazo kumbukumbu mfululizo zikawa zinapita kichwani mwake baada ya kuwa ameangalia filamu katika luninga iliyokuwa imepachikwa katika ukuta wa chumba alichokuwa analala, filamu hiyo iliyoigizwa na masanii mashuhuri nchini Tanzania ilikuwa inazungumzia mapenzi bora lakini yanayoingia doa baada ya binti kupata ujauzito, ujauzito unakuwa karaha kwa mwanaume anaamua kuukataa. Aliukataa kwa sababu ya maisha yake magumu hakuwa anaweza kumuhudumia mtoto na mama yake.



    Defao akajikuta kwa mara ya kwanza anamkumbuka Joyce Keto, akakumbuka jinsi alivyombaka kisha akakimbia na kujificha. Akajutia nafsi yake akajiona yu hatiani. Nafsi ikamsuta akajihisi yupo dhambini, akawa amefikiria kutubu dhambi yake, dhambi iliyotiwa chachu na tabia zake za kubadili wasichana jijini Mwanza, akafikiria pia kutubu kwa Minja.

    Defao akawa ameamua kurejea mjini Singida. Aliamini kwa kiasi alichonacho Minja atamuelewa japo atalaumu sana. Pesa hiyo itatumika kiasi fulani kwa ajili ya matibabu ya mgonjwa. Je itatosha?? Hilo ndio likawa swali. Ghafla alipojiuliza hivyo akamkumbuka John Mapulu, akatamani kumwendea tena ili kudai kiasi kingine cha pesa.

    Defao akamchukulia John kuwa ni bwege asiyejitambua katika mapenzi, akamdharau sana kwa kudanganywa na mpenzi wake halafu akamcheka kwa kuwa mwepesi sana kutoa milioni kadhaa kumshukuru yeye kwa kumuibia siri juu ya mkewe.

    Akamsikitikia sana kwa kuwa John hakuwa na uwezo wa kuzaa, aliinama chini kisha akajisemea huu ndio wakati muafaka wa kuvuna tena kutoka kwa John!! Nitavuna kwa kuutumia udhaifu wake. Siri yake ya uhanithi itanipatia pesa zaidi ya hizi.

    Siendi Singida kwanza!!! Alifikia maamuzi ambayo aliyaona kuwa ni sahihi.

    Defao akawa ameamua kumfuata tena John Mapulu!!!

    Akapitiwa na usingizi akiwa na maamuzi hayo.



    *****



    “Puuuuu” gari aliyokuwa anaendesha Joyce Keto ilipitia bonde katika njia iliyokuwa ya kushangaza, bonde lile lilikuwa wazi sana.

    John akashangazwa sana na hali hiyo, Joyce alikuwa amefanya kosa kwa kukosa umakini barabarani, japo hakuwa na leseni ya kuendesha gari lakini alikuwa na uwezo mzuri wa kuendesha. Cha kushangaza tukio hilo Joyce alikuwa hajalitilia maanani, alionekana kuwa na hofu iliyojaa tele usoni mwake. Aliendesha gari kidogo kisha akaipaki.

    “Vipi Joyce!!!” John alimuuliza.

    “Mh!! Yule kama nani yule mh!!! Ila sio yeye” Hakueleweka alichokuwa akiongea Joyce, John akabaki anashangaa.

    Ilikuwa ni siku yao ya saba kwenda kliniki na siku hiyo Joyce aliendesha kuanzia safari ya kwenda na kurudi kwa uangalifu mkubwa kama kawaida yake lakini hapa palipokuwa wazi kabisa amefanya kosa ambalo John Mapulu alibaki kulishangaa.

    Joyce aliamini kile alichokiona kisha akaikataa imani yake!!! Hakuamini kama ni kweli.

    Baada ya dakika kadhaa Joyce aliondoa gari hadi wakafika nyumbani!!

    “Bosi kuna kijana amekuja kukutafuta anasema unamfahamu!!!”

    “Anaitwa nani?” John aliuliza huku akishusha kioo vizuri.

    “Amesema unayo namba yake lakini kama umeipoteza yeye anaitwa….nani…nani…Mafao sijui” mlinzi akawa amesahau jina la mgeni wa John. Joyce akacheka kusikia jina hilo, John naye akatabasamu akaitwaa namba akaingiza kwenye simu yake. Haikuwa imehifadhiwa hapo kabla akaihifadhi kwa jina la Mafao huku akitabasamu!!!

    Wakaingia ndani!!

    Huyo Mafao alikuwa ni Defao alikuwa amemfuata John nyumbani kwake badala ya kupiga namba yake , siku hii alikuwa amependeza sana na alifikia hatua ya kujilinganisha na John mwenyewe na pengine kumzidi.

    Hakumkuta akawa ameacha maagizo pamoja na namba za simu.

    Wakati anarejea mjini ndipo alipishana na gari ambayo ilikuwa imewapakia John na Joyce, Joyce akawa amemfananisha Defao, lakini hakuwa na uhakika kama alikuwa sawa ama la, ni wakati huo ambao alichengana na mahesabu ya kupunguza mwendo ili aweze kulivuka bonde.

    Defao hakulitilia gari hilo maanani yoyote akaendelea na shughuli zake.

    Alikuwa anasubiri simu kutoka kwa John!!!

    Kama kawaida akaingia katika baa mojawapo jijini Mwanza akaanza kupata moja baridi moja moto.



    Defao alipochangamshwa na zile pombe alizokuwa amegida kwa fujo kidogo, aliitazama simu yake hakuna mtu yeyote aliyekuwa amepiga simu.

    Dharau!!!! Akawaza Defao, kisha akabonyeza tena namba za simu alizoamini kabisa kuwa zilikuwa za John, John Mapulu, hazikuwa zinapatikana kama awali. Akawaza kurejea tena nyumbani kwa John lakini akaionya nafsi yake kwani ni kama alikuwa anaharakia sana mambo kuliko kuituliza akili yake na kuisuka mipango yake taratibu.

    Defao akajenga tabasamu lilioonyesha kukereka, akanyanyua chupa ya bia aliyokuwa anapiga katika mfumo wa tarumbeta. Akaipeleka mdomoni lakini akagundua kuwa ilikuwa imemalizika, akairejesha chupa kwa kasi ikakutana na meza ya mbao ikatoa mlio ulioshtua wachache. Akatazama kushoto na kulia akasimama na kuzinyanyua hatua zake kuuelekea mlango ulipo. Akawa ametoka nje.

    Hakuwa na pakwenda ambapo ni rasmi!!!

    Akaamua kurejea nyumba ya kulala wageni aliyokuwa amefikia!!!!



    *****



    Nia ya Matha ilikuwa kuuondoa uhai wa Joram ili amuepushie zogo la kuwa anamtumia kimwili bila mkataba maalum wa lini mchezo huo mchafu utafikia kikomo. Joram alikuwa ameiongeza idadi ya wanaume wanaoufaidi mwili wa Matha kutokea kuwa watatu na sasa walikuwa wanne, Joram alikuwa amejihalalisha kuungana na Michael, John Mapulu na Adrian Mhina.

    Matha akawa anamtazama Joram katika hali ya tofauti kabisa, alimchukulia kama mdhalilishaji, asiyekuwa na utu hata kidogo. Matha alikuwa anaamini asilimia zote kuwa Joram alikuwa ameshikilia mpini na yeye alikuwa upande wa makali. Joram alikuwa na silaha kubwa sana silaha ya siri!!! Jambo hilo lilimuumiza sana Matha ambaye hakutaka kuwa mtumiwaji kiasi hicho. Matha alikuwa anamzidi karibia kila kitu Joram, nguvu, cheo, ujanja na hata pesa. Tatizo lilikuwa moja tu!!! Siri!!

    Matha akawa ameamua kuua

    Kumuua Joram!!!

    Lakini wazo la kuua likawa mtihani mgumu sana.

    “Nitakuwa sijamkomoa kwa jambo analonifanyia kumuua ni adhabu nyepesi sana, atakufa mara moja……hapana lazima na yeye aumie” alibadili maamuzi Matha.

    Wazo lake likawa kumkomoa Joram.

    Akapiga akili kidogo tu akapata jawabu na hakutaka kupoteza muda sana kwani siku hii Joram alikuwa anahitaji penzi la Matha tena katika nyumba ya kulala wageni.

    Matha alifika kwa wakati eneo husika akiwa amevalia kama kawaida baibui lake kuweza kujificha kwa watu kisha alipofika chumbani aliliondoa na kusalia na nguo zenye kupendeza machoni hasahasa chumbani. Joram alimkumbatia kisha akambwaga kitandani.

    “Nina kiu Joram!!!” alisema Matha huku akiviondoa viatu vyake miguuni.

    “Nimeagiza chakula bila shaka muda si mrefu kitafika na maji pia nimeagiza. Alijibu Joram!!

    Baada ya dakika kadhaa mlango uligongwa, Joram akaenda kupokea chakula hicho.

    Matha akafakamia maji na kuyagida ipasavyo, Joram alitoka na kwenda kunawa mikono bafuni alitaka ale ashibe kwanza kabla ya kumnyanyasa Matha kijinsia.

    Alipotoka kwenda kunawa mikono ilikuwa nafasi ya kipekee kwa Matha alizama katika pochi yake akatoa unga mfano wa ndimu ya kusagwa akamimina katika chakula cha Joram.

    Bila wasiwasi wowote Joram aliporejea alichukua chakula kile na kutaka kumlisha Matha.

    “Mi siwezi bwana nimeshiba sana maji!!!” alikataa Matha. Joram akamuelewa akatupia pande lile la nyama mdomoni kwake.

    Matha akaanza kumuhesabia dakika, zilipofika tatu chambo katika ndoano ikaanza kuliwa na samaki.

    Matha akaanza kuhisi dalili za ushindi!! Ungaunga wa ‘doromee’ ukaanza kutenda kazi katika mwili wa Joram, Joram akalainika na kisha kuangukia kitandani.

    Ni wakati huo Matha alitoa taarifa kwa timu yake aliyokuwa ameiandaa kwa kazi moja tu kumuadabisha Joram bila kumuondoa uhai!!!!

    Shughuli ikaenda kama alivyopanga.

    Baada ya siku mbili jiji likatawaliwa na taarifa juu ya kulawitiwa kwa Joram!!!!!

    Ilikuwa ni taarifa iliyotapakaa sana jijini Mwanza kuhusu kulawitiwa kwa kijana mtanashati na mwenye nguvu. Taarifa hiyo ilisambaa upesi kutokana na mazingira ambayo muhusika alikutwa, ni jirani na mabweni ya shule ya sekondari!!!

    Joram alikutwa humo akiwa hajitambui kabisa, alikuwa yu uchi wa mnyama na pembeni yake palikuwa na pakiti za kondom zilizokwishatumika tayari. Wanafunzi makundi kwa makundi walizisambaza habari hizo katika hali ya ucheshi na wengine katika hali ya majonzi.

    Joram alichukuliwa na kupelekwa hospitali ambapo aligundulika kupewa madawa makali ya usingizi yenye athari kwa muda wa masaa ishirini na nne.

    Daktari baada ya kumpima aligundua kuwa hakuwa ameingiliwa kimwili yaani hakuwa amelawitiwa.

    Nguvu ya sauti ya daktari haikutosha kuwashawishi walioshuhudia tukio hili hivyo vyombo vya habari vikachukua ya daktari na wananchi wakibaki na mawazo yao ambayo kwa nafasi kubwa yalichukuliwa kuwa ni ukweli!!!



    ******



    Ilikuwa ni taarifa ambayo ilipokelewa kwa shangwe zote na Matha. Aliamini kwa skendo hiyo lazima Joram asalimu amri kwa mambo aliyokuwa anamfanyia.

    Ilikuwa kama alivyokuwa anafikiria, Joram alipozinduka na kupewa taarifa hizo za udhalilishaji alijidai kuwa hazijamshtua kumbe kichwani mwake alikuwa amechukua maamuzi mazito tayari.

    Joram akiwa na hatia yake moyoni hatia iliyoambatana na siri nzito juu ya John Mapulu na mpenzi wake Matha, alinyata usiku wa manane kutoka katika hospitali ya rufaa ya Bugando. Akatoroka kama vile anarejea baada ya muda mfupi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Haikuwa muda mfupi Joram akatoweka moja kwa moja bila kumuaga John wala Matha.

    Baada ya utafiti wa siku kadhaa taarifa kutoka hospitali zilikiri kuwa Joram ametoroka na haijulikani alipo. Taarifa hizo zilidumu kwa wiki kadhaa hadi pale jeshi la polisi wilaya ya Magu jijini Mwanza lilipotangaza kupatikana kwa mwili wa Joram ukiwa umeshambuliwa na wanyama lakini baada ya utafiti ilifahamika kuwa Joram alikufa kwa kunywa sumu.

    Hatimaye simulizi tamu ya kusisimua juu ya Joram ikawa imeishia hapo, Joram akawa ameiaga dunia.

    Matha aliipokea taarifa hii kupitia kwa mpenzi wake (John Mapulu). Usoni alisikitika huku moyoni akicheka, kicheko kikubwa sana kicheko cha ushindi. Ushindi wa chee!!

    Matha alikuwa amemuua Joram kiwepesi kabisa.

    Kifo cha kizembe!!!! Ni tafsiri aliyoifanya Matha.

    Hakika Joram aliuwawa kizembe.

    Matha akasalia na John, Michael na Adrian, huku tumbo lake likimkumbusha kuwa kuna kiumbe mwingine, kiumbe hatarishi zaidi anayetegemewa kuleta zogo kubwa zaidi.

    Mimba!!!!!



    ******



    Jambo ambalo mzee Keto hakutaka kulichukulia wepesi ni kifo cha mkewe mpenzi mama Joyce aliyezaliwa na kuitwa Mariana.

    Kujinyonga??? Hapana haiwezekani!! Alikataa kuamini kuwa mkewe aliweza kujinyonga kiwepesi kiasi hicho, hawakuwa wamegombana katika siku za karibuni wala watoto wao hawakuwa wamewakera.

    Alijaribu kuvuta kumbukumbu ya mazungumzo ya mwisho kati yake na mkewe, yote yalikuwa mazuri yaliyotawaliwa na upendo na amani tele. Hakupata kumbukumbu yoyote ile ya makwazo kati yao. Ndiyo Mariana alikuwa ni kutoka kabila la wahehe lakini hiyo haikuwa sababu tosha ya yeye kujiua.

    Ujumbe ujumbe ujumbe!!!! Akili yake ikakumbuka ujumbe alioucha Mariana. Ujumbe uliochukuliwa na askari. Akili ikapata ahueni ya kupata jawabu, akasimama wima akajisachi na kujikuta na senti kadhaa zilizokuwa zinatosha kwa nauli ya kumfikisha kituo cha polisi. Aliwapita watoto wake pamoja na watu wengine waliokuwa wamehudhuria msiba huo.

    Aliwasili kituo cha polisi Magomeni, na moja kwa moja akafikishwa kwa mpelelezi wa kesi yake hiyo isiyokuwa na mtuhumiwa.

    “Kuna ule ujumbe ningependa kuuona huenda una msaada wowote”

    “Sidhani maana una mafumbo matupu” alijibu yule mpelelezi huku akimpatia kikaratasi kilichokuwa na ujumbe.

    “Nimedhalilishwa nikiwa katika harakati za kumtafuta mwanetu bora nife!!!” aliyakariri maneno yale kwa sauti ya chini kama mara tatu huku akikiweka mezani kile kikaratasi.

    “Kweli hakuna maana yoyote!!!” aliunga mkono hoja, wakazungumza mawili matatu mzee Keto akaaga na kuondoka zake.

    Alifika na kujilaza kitandani, alikuwa amedhoofika sana na hakutaka kuzungumza na mtu yeyote. Akilini bado alikuwa anaimba ule wimbo aliousoma katika kile kikaratasi. Mara katikati ya wimbo akaikumbuka siku ambayo mkewe alishawishika kumtafuta mtoto wao kupitia katika imani za maombi ya kidini. Hapo hapo kama radi akamkumbuka mchungaji JK, alimkumbuka kwa kuwa alitangazwa sana katika magazeti mbalimbali ya jijini Dar es salaam. Kama vile ameshtuka kutoka katika ndoto ya kutisha Mzee Keto alisimama na kukaa kitako.

    Akachukua simu yake akataka kupiga lakini akagundua aliyetaka kumpigia yupo hapo hapo msibani.

    Alikuwa ni mama yake mdogo na marehemu mke wake. Ni huyo ndiye aliaga anaenda kwake kwa mara ya mwisho.

    “Huyu mwanamke alimfanya nini mke wangu!!!” alijiuliza mzee Keto. Hakutaka kuisumbua akili yake zaidi akasimama wima akatoka nje akasogea hadi jirani na yalipokuwa makundi ya kinamama. Akanyoosha mkono wake kisha akavikunja viganja mara kadhaa kumaanisha kuwa anamuita mtu, muhusika aliiona ishara hiyo akajinyooshea kidole kama ni yeye anaitwa, mzee Keto akatikisa kichwa kwamba hajakosea. Yule mwanamke akaacha kazi ya kuchagua mchele aliyokuwa anaifanya akajifuta mikono yake, akatafuta viatu vyake hakuviona akaamua kutembea pekupeku kumfuata mzee Keto, watu waliacha kufanya mambo yao wakaanza kumsindikiza mama yule kwa macho hadi alipomfikia mzee Keto.

    “Shkamoo mama!!!” alisalimia kikabila Mzee Keto

    “Marahaba!!” alijibiwa.

    “Samahani sana mama, Mariana alipokuja kwako mligombana chochote!! Na alifuata nini kwako usiku ule??” aliuliza kwa kujiamini.

    “Mimi?? Kwangu?? Lini baba” aliuliza kwa woga kidogo huku akijipiga piga kifuani.

    “Mh!! Kwani amekuja lini kwako??” aliuliza kimakosa kwani ni yeye alikuwa ameulizwa hilo swali.

    “Tangu mje wote siku ile hajawahi kuja tena kwangu??” alijibu yule mama safari hii kwa sauti tulivu.

    “Ina maana alienda wapi sasa?? Mh!! Hebu njoo ndani tuzungumze!!” aliamua kuituliza akili yake Keto.

    Mama yake mdogo Mariana akafuata kwa nyuma.

    “He baba wapi tena huko??” mama huyu alimshtua Mzee Keto baada ya kugundua kuwa alikuwa anampeleka chumbani kwake. Mzee Keto akashtuka akapatwa na aibu kisha akabadili uelekeo wakaenda sebuleni.

    Walizungumza mengi katika hali ya utulivu, Mzee Keto akazidi kufunguka akili yake. Mariana hakuwa amejiua kwa sababu ndogo.

    Wamemuua mke wangu!!! Aliwaza



    ********



    Furaha kubwa aliyokuwanayo Matha kwa kumteketeza Joram na ujanja wake katika njia nyepesi kiasi kile, Matha hakuridhika peke yake na ile furaha aliwafikiria Michael na Adrian katika jambo hili. Baada ya kuwa amempigia simu John Mapulu ili awe naye siku hiyo na John kukataa kata kata katika hali ya dharau. Baada ya hapo akawa na maamuzi mapya.

    Kwanza alitaka kupiga simu kwa Michael lakini akaghairi kwani alikuwa na safari ya kwenda kuonana na Bruno nyumbani kwa John maeneo ya Mecco, akaamini ataonana na Michael huko huko, kuhusu Adrian ilikuwa ni lazima ampigie simu ili aweze kujua kama wanaweza kuonana ama la.

    Alibonyeza namba za Adrian Mhina, simu ikaita haikupokelewa, akapiga tena ikakatwa na alipojaribu kwa mara ya tatu haikuwa inapatikana.

    Wivu!!! Akajitupa kitandani kwa nguvu, akaivurugavuruga shuka aliyokuwa ameitandika kitandani. Akatamani kulia machozi yakawa mbali sana, ile hali ya kutaka kulia na kukasirika kwa pamoja ikaifanya sura yake ikawa kama kinyago kilichochongwa kwa maksudi ya kuchekesha.

    Akiwa katika hali hiyohiyo mara simu yake ikaita, akawaza aidha ni John Mapulu, ama Adrian Mhina, akaichukua kwa haraka haraka akaitazama alikuwa ni Michael Msombe.

    Nini tena na huyu argh!! Akasonya akakata simu. Aliamini atapata kero nyingine tena. Wakati anairudisha ikaita tena, akaipuuzia akiamini kuwa ni Michael tena, ilipokatika ikaita tena, akaiendea kwa lengo la kuizima kabisa akakumbana na namba mpya. Akaitazama akaipokea bila kuongea mpaka upande wa pili ulipoanza kuzungumza. Ilikuwa sauti ngeni kwake.



    “Nakayange Mutukula naongea!!!”

    “ Nani?? Unasemaje??”

    “Mke wa John Mapulu!!” uliuliza upande wa pili akasita kujibu Matha badala yake akauliza.

    “Kwani vipi??”

    “Ningependa sana kuonana na wewe”

    “Ili iweje na kwa misingi ipi??” aliuliza kwa kiburi Matha. Upande wa pili haukutetereka.

    “Kwa ajili ya ndoa yako”

    “Ndoa yangu!!!” alihamanika Matha, sauti yake ikasikika ikianza kutetemeka.

    “Lini na wapi??” hatimaye alilegea.

    “Kesho mahali tutafahamishana” ilijibu kwa majivuno sauti nzito iliyotulia upande wa pili.

    “Umesema unaitwa??”

    “Eeeh!! Nakayange Mutukula” alijibiwa.

    Simu ikakatwa baada ya utambulisho.

    Mfuasi wa Joram, Joram hakufa na siri yangu!!! Alilalamika Matha huku akizungukazunguka chumbani mwake, alikuwa kama anayekaribia kuchanganyikiwa akatazama simu yake kwa hasira kama anayesubiri imjibu kitu. Mshtuko alioupata kwa simu hiyo ulisababisha ajihisi kama amepigwa teke na kitoto kilichoanza kukamilika tumboni. Maumivu matamu yakasikika kisha yakawa makali akakimbilia chooni!!

    Mpambano mpya kabisa!!!! Matha majaribuni!!



    *****



    Hali ya Matha kuruhusu hofu wakati akizungumza kwenye simu na Nakayange Mutukula ilimpa nafasi bwana huyu kuirusharusha miguu yake kwa kujitawala na kuamini kuwa tayari Matha alikuwa amesalimu amri.

    Ngao hiyo ya ujasiri ilimpa kiburi sana akazungumza anavyotaka, aliamini karata aliyoicheza ilikuwa sahihi sana. Na hata alipoikata simu yake alicheka kwa sauti ya juu isingekuwa muziki uliokuwa unapigwa nje na gari la matangazo huenda kicheko chake kingepasua ukuta na kufika nje. Alikaa kitako na kufanya ishara ya msalaba akibariki uovu aliotarajia kuufanya, uovu wa kuvunja amri kadhaa katika mfululizo wa kasi ya ajabu. Siku ya ahadi ilikuwa kesho yake, alipaona mbali sana kwani alitaka ndani ya siku tatu aweze kuwa amemaliza mchezo huo katika hali ya mafanikio. Jiji la Mwanza likaonekana kuwa jiji la mafanikio kwa mwanaume huyu, alikuwa anazipata pesa katika hali isiyokuwa na jasho lolote.

    Alihofia kujitambulisha kwa jina lake halisi kwa kuhofia kuwa huenda Matha tayari amewahi kulisikia mahali hivyo kumpa nafasi ya kujipanga katika kujibu mashambulizi ya maswali ya hapa na pale.

    Kwa jina hilo gumu alilolibuni aliamini kuwa Matha asingeweza kulielewa. Ilikuwa furaha kubwa akajifananisha na na muigizaji mashuhuri katika filamu akiwa katika nafasi ya kinara (steringi). Akiitendea haki nafasi hiyo kwa kigezo kuwa kinara hauwawi!!

    Aliangaza huku na huko akakutana na pakiti ya konyagi katika kona ya kitanda akaimimina katika glasi kisha akaichanganya na maji kidogo. Akaitazama glasi halafu akaimimina kwa fujo kinywani, sura yake ikabadilika wakati wa kuimeza. Akamaliza kwa kusema

    “Mimi ndio Defao bwana mwingine fotokopi”

    Defao akawa amemuingiza mkenge Matha, nia kuu ikiwa kujipatia pesa jina la Nakayange Mutukula likamchekesha akajiachia kwa kicheko kirefu kisha akajiweka chali tena kitandani akajiona tayari amemaliza kila kitu. Alijua kuwa lazima baadaye atasinzia na ilikuwa hivyo!!!

    Usingizi ukamtwaa!!!



    *****



    John Mapulu alishangazwa sana na ujumbe ulioingia katika simu ya marehemu Joram ambayo alikuwanayo yeye na alikabidhiwa kama ndugu wa karibu zaidi wa Joram. Alikuwa amesahau kabisa ni wapi alikuwa ameiweka simu ile hadi ilipokuwa imeingiza ujumbe ule, na laiti kama usingekuwa mlio mkubwa wa simu asingeweza kusikia.

    Ujumbe ule ulisababisha John aiwashe simu yake, simu aliyokuwa ameizima baada ya kuwa ametofautiana lugha na mpenzi wake (Matha), hii ilikuwa baada ya Matha kuhitaji kuonana naye wakati akiwa katika kipindi hicho kigumu cha kumpoteza msaidizi wake katika mazingira dhaifu lakini ya kutatanisha.

    Kifo cha Joram kilikuwa kimemkosesha raha kabisa, aliamini kabisa kuwa hakikuwa kifo chepesi kiasi hicho aliamini kuwa lazima kulikuwa na upande uliokuwa unahusika. Kuna jambo ambalo Joram atakuwa alifanya, jambo lililowafanya adui zake kumchezea mchezo huo mchafu ambao hata John alikiri kuwa angekuwa ni yeye angeukimbia mji!!!.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ujumbe huu ulioingia sasa unamfungua akili ulikuwa ujumbe ulioingia katika simu ya Joram bila ya Joram mwenyewe kuwepo.

    “Bwana Jo, kwa kuwa umepuuzia ujumbe wangu basi mi namwaga mboga na tusilaumiane katika hili kwani umekuwa wa kwanza kumwaga ugali” ujumbe ulimalizika hivyo, John hakujua hata ni lini ujjumbe huo ulitumwa lakini ni wakati huo ulikuwa umeingia.

    Saa nne usiku!!!

    Huyu ndiye anajua chanzo cha kifo cha Joram!!! Aliwaza John Mapulu huku akiinukuu ile namba katika kijitabu kidogo alichokuwanacho maalumu kwa namba maalumu. Kisha akachukua simu yake nyingine ya dharula akaipiga namba hiyo, huku akiwa hana mategemeo yoyote akashangaa namba ile ikaita kwa muda halafu mwenye simu akataka kupokea tu, John akawa ameikata.

    Laiti kama angetumia simu yake mwenyewe huenda angepata jawabu upesi!!! Hakufanya hivyo!!!

    Mh!! Ana maana gani huyu kuacha simu yake wazi hadi sasa wakati Joram tayari amekufa kama alivyoahidi kumkomoa??? Je ahofii usalama wake, na haioni hatari ya kuiacha namba yake hewani, mtu wa ajabu kweli!!! Alikiri John kisha akaikata simu yake na kuizima kwani namba ile nayo ilianza kumpigia.

    Wasiwasi kwa mbali ukamvaa John na kujihisi yupo katikati ya maadui ambao walikuwa wanajua nini wanachokifanya, maadui waliotoa onyo kwa kumwondoa duniani mpambe wake aliyeaminika katika kuitumia vyema bunduki, shujaa ambaye alikuwa haofii kilichokuwa mbele yake, mashuhuri aliyekufa kifedhuri!!! Joram!! Alikuwa amelishwa sumu. Kifo chepesi!!! Kifo cha kishamba!!!

    John hakutaka kulala pale nyumbani tena, akaenda kuuweka mgongo wake katika nyumba ya kulala wageni, hakumuaga mtu yeyote yule.

    Akiwa katika nyumba ya kulala wageni akapata wazo la kuingia katika mapambano mapema kabla adui hajamdhalilisha. Ghafla akiyawaza hayo mara kama sindano jina la Matha likapenya katika mwili wake katika namna flani ya kushtukiza halafu mara jina la Adrian Mhina likashtusha mishipa yake ya damu, akamtuhumu Adrian moja kwa moja kuwa ndiye muhusika wa jambo hili. Adrian amemuua Joram!!! Alifikiria hayo. Akaamini Joram ameuwawa kwa sababu ya mapenzi ya Adrian kwa Matha, Adrian alikuwa amemuua Joram kama onyo kali sana kwake ili ajue kuwa anao uwezo wa kumwondoa duniani.

    “Nani ametoboa siri kwa Adrian kuwa ni mimi nimemchezea mchezo akaswekwa rumande!!!” alijiuliza John huku akiamini kabisa Adrian ndiye muhusika mkuu katika mauaji ya Joram, akashikwa na hasira akahisi Adrian amemdharau sana kwa malipo hayo. Roho wa hasira akautia mwili wake baridi akaanza kutetemeka, baadaye jasho kali likamtiririka. Akakunja ngumi na kuugongagonga ukuta kama namna ya kupambana na hasira yake.

    John akamchukia Adrian na kukiri kuwa alikuwa amemdharirisha!!!

    Matha Matha Matha Matha!!! Huyu ndo alikuwa tatizo.

    Mapenzi yalikuwa yamemteka John, akakiri kuwa alikuwa hajiwezi tena katika mapenzi na ilikuwa lazima apambane!!!!



    *****



    Adrian aliamini kuwa Mark aidha alikuwa ametumwa na John ama ni kampani moja na John, kitendo kile alichomfanyia cha kumwingiza katika mtego na mkono wa dola kikamkaa na kumkwaza.



    John kwa kutumia huduma za kutuma pesa katika simu alitambua kuwa aliyetuma ujumbe katika simu ya Joram usiku uliopita alikwenda kwa jina la Gervas Kilinde. Akaamua kucheza pata potea akaamua kuingia katika tasnia ya uigizaji akaamua kumtumia tena yule mwanamke ambaye alimtumia wakati wa kumtia Adrian matatani, mwanamke aliyeigiza kuwa ameibiwa simu katika daladala.

    John aliamini kuwa mwanaume ana ufinyu sana wa mawazo pale mwanamke anapoingia kati.

    Mchezo ukachezwa, Gervas Kilinde ama Defao akaipokea simu kwa sauti nzito iliyoashiria usingizi bado.

    “Haujambo Gervas!!”

    “We nani??” aliuliza kwa shari kidogo.

    “Mh!! Au nimekosea namba wewe ni wa Kilinde”

    “Ndio ni mimi, we nani!!!”

    “Mamdogo wako!!”

    “Mamdogo??” aliuliza huku sauti yake ikizidi kusikika vyema.

    “Sijui nilikufananisha??? Au ni wewe maana kama nilikuona Mwanza kama siye basi watu mnafanana”

    “Mh!! Umesema mamdogo, mamdogo nani kwani?? Mi nipo Mwanza” alianza kuingia mkenge Defao.

    “Mh!! Nilikuacha bado mdogo yaani umekuwa mkubwa wewe, upo bado Mwanza au umeondoka??”

    “Nipo mama, kwanza shkamoo!!!”

    “Marahaba…wapi upo mi nipo huku Igoma”

    “Mh!! Unadhani mama naijua Mwanza basi!! Nimekuja tu kibiashara”

    “Kesho nasafiri, kama unaweza tuonane leo mapema maana ni miaka mingi na nimeamini kuwa damu nzito kuliko maji”

    “Sasa mimi ninatoka baadaye kidogo nitakupigia simu!!”

    “Kama saa ngapi mwanangu!!”

    “Asubuhi hii hii kuna mtu namsubiri anipigie simu nijue ninaonana naye saa ngapi kwanza”

    “Haya namba yangu ni hii hii”

    “Sawa mama nimefurahi sana umeniita jina langu maana siku hizi siitwi kabisa hilo jina”

    “Unaitwa nani tena he!! Miaka imepita”

    “Kweli miaka ni mingi, haya mama…samahani mama naomba ukate simu ananipigia huyu mtu nitakupigia” alizungumza kwa presha Defao.

    Mama mdogo akakata simu kama alivyoombwa.

    Gervas hakujitambulisha jina lake maarufu!!! Defao.

    Laiti kama Defao angejua hatari iliyopo mbele yake basi asingejieleza kinagaubaga kwa huyu mama, Defao alikuwa anajikabidhi katika mikono ya John Mapulu.

    Aliyekuwa amepiga simu wakati huu ni Matha!!

    Lengo likiwa kuhusu kukutana kwao!!!



    *****



    Kwaya mbalimbali zilikuwa zikitumbuiza katika namna ya kupendeza machoni, kila iliyoingia ilionekana kuwa bora zaidi ya ile iliyotoka, wasichana warembo waliosemekana kuwa wameokoka walikuwa wakipandisha na kushusha sauti kisha vijana watanashati wanaomjua na kumtii Yesu walichombeza kwa sauti ambazo si nzito sana wala nyepesi sana huku wakicheza kwa staili ambazo kama ingekuwa nje ya ukumbi ule zilifanana kabisa na zile za madansa wa miziki ya bongo fleva, staili za viduku na mapanga zilisababisha wakinamama wapige vigelegele na wanaume wachache wakipiga makofi.

    Kwaya ziliendelea kubadilishana kwa muda mrefu na burudani ilikuwa haichoshi kuitazama huku kila baada ya nyimbo moja zikisikika kelele zikisema ‘bwana asifiweee!!!’ na mamia ya waliohudhuria wakijibu ‘ameeeen!!’ sauti za wanawake zilimeza zile za akina baba na hata sauti za vilio vya watoto hazikuwa na nafasi.

    Baada ya masaa takribani mawili na nusu hatimaye aliingia mwanamke ambaye alitambulishwa kama mama mchungaji, ngozi yake ilikuwa ipo katika hatua za mwisho kuusaliti weusi wake wa asili aliozaliwa nao, miguu yake haikuwa ikifanana na rangi ya uso wake bila shaka alikuwa anatumia kemikali fulani usoni.

    Waafrika sisi!!!!!!

    Watu wote walisimama wima wakati huu aliposhika kipaza sauti mama huyu aliyekuwa na vito vya thamani karibia kila nafasi mwilini mwake.

    Mzee Keto alisimama lakini akiwa amechelewa, hakuwa akizijua taratibu.



    Mama mchungaji aliwasabahi kondoo wake katika namna ya kukariri vifungu vya biblia halafu akatumbuiza wimbo mmoja, wimbo usiokuwa na sauti maalum za kupanda ama kushuka. Alipoanza kuimba sauti yake ilisikika ikiwa inakwaruza, alipokelewa na kondoo wote katika sauti ya utulivu, Mzee Keto naye akiwemo. Baada ya dakika kadhaa ni mzee Keto peke yake ambaye hakuwa akipiga makelele katika kabila lisilofahamika, alijifanya kuwa amefumba macho huenda hata atapandwa na hayo maruhani lakini aliishia kufumbua macho na kukutana na visichana vidogo navyo vikiwa vinapiga mayowe ambayo hakuyaelewa. Hata waliokuwa wamelala walipayuka kadri wawezavyo. Alidhani kuna kitu wanapewa kuamsha mizimu hiyo lakini haikuwa hivyo. Alisikiliza huku na huko huenda atakutana na neno walau moja la kizaramo, kihehe, kisukuma, kipare na kichaga lakini wala hayakufanana akagundua siku hiyo alikuwa katika ibada ya nchi nyingine. Akakumbuka usemi wa cheza kadri mdundo unavyokwenda, ghafla akaanza kurukaruka huku na huko kama kichaa lakini kama yeye angekuwa kichaa basi waliokuwa pembeni yake ni vichaa zaidi maana walikuwa wanagalagala.

    Baada ya kurukaruka sana bila mafanikio ya kutokwa machozi aliambulia kutokwa jasho. Pambio lilivyokwisha alitaka kutoa leso aweze kujipangusa jasho lakini alisita baada ya kushuhudia umati wote ukitumia leso za aina moja tena hadi rangi zinafanana, zilikuwa na rangi ya kijani kibichi. Akajifanya hana haja ya kutumia leso yake kumbe alihofia kuitoa maana ilikuwa nyeupe akatumia kiganja chake kujifuta, alipomaliza aligundua alikuwa mmoja kati ya watu wachache ambao walikuwa wamesimama. Akakaa kiaibuaibu, alipounyanyua uso wake akakutana na sura ambayo haikuwa ngeni sana machoni pake, sura ya mchungaji, mchungaji maarufu, mchungaji Jacob Komanya au maarufu kama JK. Moyo wake ukapiga ‘paaaaa!!!’



    Akili yake ikamkumbusha kuwa fedheha zote anazopitia za kurukaruka na kutokwa jasho wakati umri umeenda lengo lilikuwa kukutana na mchungaji huyu lakini sasa alipomuona akaanza kumuogopa, alimuogopa sana kwani umati wote ulikuwa kimya wakati amesimama pale mbele.

    “Umati wote unamuheshimu…mimi nina jeuri gani ya kumtetemesha??” alijiuliza huku akizidi kumfanyia tathmini hasahasa katika shingo yake iliyojikatakata vipande dalili za afya njema na ile cheni nzito iliyopenyeza na kuonekana kidogo.

    “Mh!! Huyu siye niliyemdhania!!” alikiri Mzee Keto huku akikaa vyema katika kiti chake, akiwa amezama katika mawazo makali alishtushwa baada kuguswa na mkono laini katika bega lake, si mkono pekee uliomshtua bali kitambaa cha kijani kibichi. Kidogo apige kelele, lakini hapo hapo akazuga kuwa hajashtuka. Hakuulizwa chochote alipatiwa maji ya kuywa ya baridi kabisa, aliyapokea na alipogeuka kulia kwake karibia kila mmoja alikuwa amepatiwa huduma hiyo.

    Makanisa mengine starehe!!!!! Aliwaza. Hakuyafungua maji yale wakati ule ule aliyaweka kwanza katika miguu yake.

    Baada ya kuzungumza mambo mengi mara ilikuja hatua ya sadaka. Mzee Keto kamwe hatasahau jinsi alivyopukutishwa kila senti aliyokuwanayo mfukuno siku hiyo, cha kuumiza zaidi hata saa yake nayo ilitolewa sadaka.



    Nimelipia huduma ya maji hapa!!!! Alijisemea na kupiga kite cha hasira bila mtu yeyote kujua majuto yake.

    Kwa kuwa alikuwa ameamua kufuatilia ukweli juu ya kifo cha mkewe aliendelea kubaki hapo, ulifika wakati wa maombi.

    Kidogo mzee Keto acheke baada ya kusikia maombi juu ya wenye chunusi mara fangasi, mapunye, malengelenge, wanaotaka mume na mke, wanaotaka biashara zao zitoe faida, mikosi.

    Mganga wa jadi?? Mchungaji?? Alijiuliza katika hali ya kukasirika na kupuuzia. Hakupatikana wa kumjibu, lakini wakati akiyabwia maji yake alishtuka baada ya mlemavu wa miguu yote miwili kuyatupa magongo yake, maji yakampalia bahati nzuri hayakuleta madhara makubwa.

    Lazima mke wangu alishawishika hapa!!! Mchungaji JK hapana aisee!! Alikiri ujuzi wa bwana huyu japo kimya kimya. Wenye chunusi waliahidiwa zitaisha na hata wenye shida na wapenzi walipewa siku tatu tu watawapata wenzi wao.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kanisa la leo Mungu anajibu kwa apointment!! Safi kweli!!” alikejeli mzee Keto.

    Mchana kililika chakula cha kushiba, mzee Keto aliitumia fursa hiyo kupita kikundi kwa kikundi hatimaye alifanikiwa alichokuwa anataka, akawafikia “wapinga mchungaji” vijana hawa walikuwa waumini lakini hawakuwa wakimuunga mkono mchungaji kwa asilimia zote. Walikuwa na wasiwasi juu ya nguvu zake, kama vile hawasikilizi Mzee Keto akiwa bize na sahani lake la chakula alipata neno ambalo lilizungumzwa kama tetesi lakini ikapingwa.

    “Mchungaji JK ni mzinzi, na masharti yanamtaka awe hivyo” alisema kijana mmoja.

    “We we we we bora ukae kimya aisee acha kabisa kusema hivyo” mwenzake alimkatisha. Naye akatii akaacha.

    Mzee Keto akajiuliza maswali kuhusu tetesi hizo akapata uwiano wa kifo cha mkewe!!

    Mchungaji huyu ame…..amezini na marehemu mke wangu?? Alijiuliza kisha hakutaka kuendelea kula akaiacha sahani hapo, akajichanganya na makundi ya watu hatimaye akatoka nje. Akajihisi hatia ikikitekenya kichwa chake katika hali ya kukera akajigundua yu katika kumuabudu shetani wakati yupo kwenye gari akirejea kwake.

    Laiti kama angevuta subira na kuimalizia ibada hiyo, mchungaji JK alizungumzia kifo cha muumini mwenzao yaani Mariana ambaye alikuwa mke wa mzee Keto. Familia ya marehemu ilikuwa imetengewa pesa nyingi sana kama rambirambi na hiyo ilikuwa kawaida na sheria za kanisa hili.

    Harakaharaka za mzee Keto, familia ya Mariana, ikawa imelikosa bingo hili!!!

    Njia nzima mzee Keto hakuwa na amani aliwaza kuwa adui yake namba moja sasa alikuwa hadharani je atatekeleza vipi mpango wa kupambana naye kwa ajili ya kuujua ukweli hilo likabaki kuwa swali gumu. Akapiga moyo konde akaamini kuwa anao muda muafaka wa kuyafikiria hayo yanayomsibu.

    Akajipumbaza kwa kuusikiliza muziki unaopigwa katika daladala ile akasahau kwa muda kuhusu JK.



    *******



    Defao alikuwa katika hamu kubwa ya kuonana na Matha halafu ikaja hamu nyingine ya kuonana na mama yake mdogo. Akajisikia fahari kuwa jiji la Mwanza limempenda sana. Maamuzi yakawa ni nani awe wa kwanza kukutana naye. Kwanza alimfikiria Matha akaamini kuwa alikuwa na wakati mgumu sana wa kupambana na mawazo ya mama huyu mtarajiwa ili aweze kupata kiasi kizuri cha pesa hivyo kwa Matha alitakiwa kuandaa jumba la maneno ili kufanikisha hili, upande wa pili wa shilingi Defao akamuwaza mama yake mdogo, kwanza akamchukulia kama mtu asiyekuwa na umuhimu sana katika maisha yake lakini aliichukulia nafasi hii kama namna ya kipekee ya kujitafutia sifa kwamba ana maendeleo sana, Defao alitumia usemi wa mama yake mdogo huyo kuwa zilikuwa zimepita siku nyingi bila kuonana hivyo aliamini kabisa mara ya mwisho mwanamke huyo kumuona alikuwa katika mazingira magumu huko Singida, mazingira ya kimaskini yasiyotamanika, na pia hakuwa mtanashati.

    “Nafasi ya kipekee ya kuchota ujiko!!!” akafikiria kisha hata kabla ya kupata jibu la wapi ataanzia kwenda akawa anawaza huo ujiko anauchota kwa kutumia ngao ipi. Gari!!! Jibu lilijileta kichwani, nikiwa na gari atanikubali sana na pia baada ya kuzungumza nitampa shilingi kadhaa. Sitaki kuzungumza naye sana nitajidai niko bize kiasi ili akanitangaze vizuri huko aendako. Walizidi sana dharau hawa!!! Alijikuta akitoa sauti iliyotangaza nia yake. Sifa zikatoa jawabu, Sifa zikamsababisha achukue maamuzi, maamuzi ya kukodi gari kwa siku nzima.



    “Elfu thelathini, mafuta juu yako!!” hiyo ndio bei aliyotajiwa, hakuuliza mara mbili alitoa mara moja hicho kiasi akawalipa.

    “Na dereva utamlipa elfu kumi!!” alipewa maagizo. Laiti kama angekuwa anaujua mji Defao wala hakuwa na haja na dereva wa kulipia kwani alikuwa anajua kuendesha gari japo bila leseni.

    “Tuelekee wapi bosi!?.” Aliuliza dereva.

    “Wait please why are you, una haraka” alijaribu kukivaa kiingereza kwa pupa akawa ameishia katikati ya sentensi akajazilizia kiswahili. Dereva naye alikuwa wale wenzake na Defao hakuambulia kitu zaidi ya neno ‘una haraka’ akatulia.

    Defao alitoa simu yake akapiga simu ya kwanza…kisha baada ya mazungumzo mafupi akapiga ya pili nayo alizungumza kisha akakata.

    “Mecco na Igoma wapi panaanza!!”

    “Mecco na Igoma??” dereva naye aliuliza Defao akakereka akasonya. Dereva akajishtukia akajirekebisha upesi.

    “Mecco inaanza bosi!!.”

    “Twende Mecco katika mwendo wa kawaida tukikaribia yaani kikibaki kituo kimoja uniambie!!!” alitoa maagizo. Dereva akatii.

    “Una miziki ya West laifu.” alihoji Defao kwa mbwembwe.

    “Eeeh!! Nadhani itakuwemo..alijibu pasi kujiamini dereva huku akiiweka gari vyema barabarani.

    “Weka!!” aliamuriwa dereva, akawasha redio. Akaweka miziki ya bongo fleva kwa sauti ya juu. Defao akakunja uso wake kwa hasira lakini kimya kimya akamsamehe yule dereva kwani alikuwa hajaelewa kitu.

    “Punguza sauti!!” alimsihi. Akatimiziwa matakwa yake. Baada ya dakika kadhaa dereva akamkumbusha Defao kuhusu kituo.

    “Weka pembeni naomba niendeshe!!!” alizungumza kwa amri. Dereva akatii.

    Defao akakikalia kiti akajifunga mkanda, akachukua marashi aliyotembea nayo akajipulizia akawasha gari na kuiondoa taratibu huku akipiga simu ikapokelewa.

    “Nambie!!” aliunguruma.

    “Kama hujavuka bado mi nipo hapa Buzuluga simama twende wote Igoma si upo na gari lako”

    “Ndio nipo nalo aaahh!! Hebu ngoja nakupigia.” Akasita kumalizia akakata simu.

    “Buzulula ndo wapi??” alikosea kutaja jina hilo.

    “Buzuluga?? Buzulula” dereva alimrekebisha. Defao hakujibu kitu. Dereva akajiongeza!!

    “Ni vituo viwili nyuma hapo!!” alielekeza.

    Defao akasimamisha gari kituo cha Mecco, kabla ya kushuka akapiga simu.

    “Nimepapita kidogo narudi sasa hivi!!” alisisitiza kwenye simu. Wakati anakata simu, simu yake ikaita, hakutaka kupokea akakata halafu akapiga.

    “Nipo hapa kituoni mama yangu hii gari Spacio ya rangi ya maziwa!!!” alitoa maelekezo huku akijitanua kwenye usukani.

    Laiti kama angeujua ugeni huo ni bora angeanza na ugeni wa hapo Buzuluga alipopapita.

    Mwanamke wa makamo alilifikia gari hilo aliloelekezwa na Defao ama Gervas Kilinde. Defao alishuka haraka haraka akampokea kwa kumkumbatia.

    “Mh!! Gere huyooooo!!!! Marashi yako mazuri mwanangu”

    Sifa ya kwanza!!!!

    “Aah!! Kawaida mamangu!!! Kawaida sana” alizuga huku akitikisa funguo za gari.

    “Na gari lako Gervas mwanangu!!”

    Sifa ya pili!!!

    “Ndio la muda tu mbona!!!” alidanganya

    “Hongera mwanaweeee umenenepa jamani!!!”

    Sifa nyingine tena!!!! Defao akauona ufahari.

    “Karibu ndani ya gari tuzungumze kidogo basi walau unikumbushe sasa!!” aliomba Defao. Yule mama hakupinga akaingia ndani ya gari. Dereva alikuwa kimya akisikiliza mziki katika simu yake.

    Dakika mbili za maongezo zilikuwa zimetosha sana kumweka Defao matatani, kiumbe asiyekuwa na huruma alifika eneo lile, aliufungua mlango wa kushoto kwa dereva na kumsihi yule mama ashuke mara moja, yule mama akiwa anatetemeka akajitetemesha hadi mkoba ukabaki ndani ya gari. Aliyekuwa siti za nyuma akaamuliwa kukaa siti ya mbele, halafu nyuma akaingia mwenyewe kiumbe huyu matata sana. Haya yote yalifanyika kimya kimya kwani mdomo wa bunduki ulikuwa umeangaza tayari bila wananchi wengine kushuhudia. Ile hali ya wawili hawa kutetemeka ikampa picha kuwa hawakuwa wamejiandaa kwa shambulizi hili la ghafla sana. John Mapulu akajitangazia ushindi mapema alikuwa amemuingiza adui kwenye mkenge kwa njia nyepesi sana.

    “Nyasaka!!!” aliamrisha John, Defao hakuelewa kitu, akashtushwa kwenzi kubwa kichogoni pake!! Akataka kujikuna akasita.

    “Endesha kwenda Nyasaka!!” alitoa karipio huku safari hii akimpiga kwenzi yule dereva bila sababu.

    “Mimi sipajui huyu ndiye dereva!!!”

    “Haya haraka kwenye usukani.” Haraka haraka huku akitetemeka alitua katika usukani, hakuuliza maswali yake yale ya awali yaliyomkera Defao safari hii aliendesha moja kwa moja kuelekea Nyasaka.



    *****



    Matha alisubiri sana baada ya kuwa amempigia simu mtu aliyekuwa amejitambulisha kwake kama Nakayange Mutukula. Alikuwa makini sana akiangaza huku na huko ili awe wa kwanza kumtambua huyo mtu kabla yeye hajatambulika. Wazo la kumpigia simu Nakayange na kumtaarifu kuwa yupo hapo Buzuluga lilikuwa ni kwenda kumteketeza moja kwa moja. Matha aliona kama maadui wamekuwa wengi sana upande wake, haki aliyoona inawafaa kabisa ilikuwa ni kifo. Siku hiyo pia alikuwa amejiandaa kwa ajili ya kuua akiwa amevaa baibui ndani yake alikuwa amehifadhi kisu kikali kilichotandazwa sumu ya kuua upesi sana. Matha alikuwa katika kusubiri kwa mategemeo ya kumuona adui yake lakini haikutokea hivyo, wasiwasi ukaanza kumwingia akahisi kuna mtego anapangiwa ajiingize kichwa kichwa. Akaamua kupiga simu lakini wakati huu Nakayange Mutukula ambaye ndiye Defao hakuwa akipatikana kwenye namba yake.

    Simu ilikuwa imezimwa!!!

    Ni wakati huu ambao tayari alikuwa mikononi mwa John Mapulu.

    Defao hakuwa na ujanja wowote, na ilikuwa afadhali yake kwenda kwa John Mapulu kuliko Matha maana Matha alikuwa amepanga kummaliza wakiwa kwenye gari. Harufu ya kifo ikatawala pande zote.

    Matha alivyoona Nakayange hapatikani akachukua tahadhari akaondoka eneo lile, hakurudi kwake akaenda saluni kupiga stori hadi jioni bado Nakayange alikuwa hapatikani.

    Kengere za hatari zikamchangamsha kichwa chake akafikiria mengi sana kisha akawaza juu ya hatari kubwa iliyopo mbele yake. Hatari ya kuuwawa kwa mkono wenye nguvu, mkono wa John Mapulu.

    Alipotoka saluni alienda moja kwa moja Mecco nyumbani kwa John, akamkuta Michael Msombe. Kwa sauti isiyokuwa na raha akamwita katika chumba walichokuwa wanafanyia mazoezi ya kutumia bunduki.

    Michael alifika na kumshika Matha bega, Matha naye akaushika kwa juu mkono wa Michael, wakawa wamebadilishana joto la miili yao. Michael akakaa pembeni ya Matha, Matha akajilaza katika bega la Michael, Michael akaanza kumchezea chezea nywele zake, Matha akasikika akihema kwa shida, Michael hakushtuka alijua ni tatizo alilokuwanalo Matha akiguswa nywele zake. Akaacha!!!!

    Matha akarejea katika hali ya kawaida baada ya dakika kadhaa akaweza kuzungumza.

    “Maik nadhani ni wakati wa kusahau mambo mengi na kufanya maamuzi!!”

    “Maamuzi yapi mpenzi!!!”

    “Kuondoka kabisa eneo hili halitufai tena, tutauawa maadui wamekuwa wengi na mimba hii imekua” neno mimba lilimshtua sana Michael alikuwa hajalisikia siku nyingi sana. Akakaa vizuri uso wake uliokuwa na tabasamu muda mwingi likapotea taratibu.

    “Nahisi siri hii inaelekea kufichuka!” aliendelea Matha,

    “Nimejaribu kupambana sana Maik wangu, nimepigana sana juu ya amani yetu lakini nahisi sasa nimezidiwa naamini pona pona yangu na wewe ni kukimbia….nisamehe sana Maik nimekutia hatiani..nisamehe..” Alianza kulia Matha huku akimkumbatia Michael kwa nguvu sana.

    Joto la Matha likapenya katika mwili wa Michael, matiti yake ambayo bado yalikuwa na nguvu za kusimama peke yake yakamchoma choma Michael katika hali ya kuburudisha, kucha zenye urefu wa wastani zikatambaa na kumfinya finya maeneo ya uti wa mgongo na mbavuni, uso wa Matha ukawa unatiririsha machozi, Michael akajaribu kumbusu shavuni akakutana na ladha ya chumvi chumvi ya asili. Uvumilivu ukamshinda, ujasiri ukapungua akayaruhusu machozi na yeye yammwagike, hawakuwa na wasiwasi kwani chumba kilikuwa kimefungwa. Michael akauhisi kwa kasi kubwa upendo wa mama ambao ameukosa kwa siku nyingi sana. Upendo wa dhati aliuhisi katika lile kumbatizi alilofanyiwa na Matha.

    Matha alikuwa anampenda Michael!!!!!

    Michael akakubaliana na wazo la Matha, wazo la kutoroka, upendo wa ajabu ukajengeka juu ya mtoto aliye katika tumbo la Matha, Michael akaamini kuwa alitakiwa kucheza nafasi yake kama baba. Ghafla akaondoa hofu yake juu ya John, akaona alikuwa na kila haki juu ya Matha.

    Mipango ya haraka ikatakiwa kusukwa.

    Michael na Matha wakiwa wameungana kwa nia moja.



    ******



    John Mapulu aliwaongoza, Defao na yule dereva hadi katika nyumba yake maeneo ya Nyasaka, moja kwa moja waliingizwa katika vyumba viwili tofauti. Milango ikafungwa, vyumba vilikuwa vina mvuto sana japo hakuna sauti iliyoweza kupenya nje, Defao alikuwa amejikojolea tayari, hofu ilikuwa imemtawala sana hakuamini kama alikuwa katika hali ya kutekwa na hakuwa akimtambua huyu mtu aliyemteka ni nani. Mwili ulikuwa unakumbwa na baridi kila mara alipofikiria juu ya hatma ya kutoka mahali pale.

    Dalili za kifo zikaanza kujionyesha bila kificho, hakika alikuwa na ulazima wa kuwazia kifo maana alionyeshwa bunduki kabla ya kufikishwa hapo bila shaka mtu aliyewateka hakuwa mtu mzuri.

    Chakula kizuri kililetwa, Defao akafanya mgomo wa kula, akiamini kuwa amewekewa sumu, aliamini kwa kugoma kula chakula anaweza kuachiwa huru na kukikwepa kifo, mawazo hafifu kabisa!!!!

    Hakubembelezwa na mtu yeyote kula chakula kile, aliachwa akiwa anashangaa chakula kikachukuliwa.

    Giza lilipoingia hakuwa na mgomo juu ya kipigo baada ya kudai kuwa hamjui hata kidogo mtu aliyehusika na mauaji ya Joram.

    “Unamfahamu Adrian!!” lilikuwa swali jingine, Defao akasema hamjui.

    “Nani alikutuma kwa Joram??”

    “Simjui huyo mtu” alikataa Defao, ghafla mbavu zake ziliamishwa kidogo kutoka mahali pake, lilikuwa teke lenye nguvu sana, alitoa ukelele mkubwa sana huku akijaribu kupambana na maumivu yale. Kabla hajakaa sawa kiatu kigumu kiliukanyaga uso wake akajisikia ganzi halafu chumvi chumvi ikawa inapenya mdomoni mwake, akili ikiwa haiko sawa bado akakutana na vitu kama nyanya ya kopo vikimiminika katika vigaye vilivyokuwa hapo ndani, alianza kujiuliza vimetokea wapi kabla ya kugundua kuwa ni mdomoni mwake. Na ile chumvi chumvi ilikuwa damu yake.

    “Ulikuwa na dili gani na Joram??”

    “Baba mimi huyo simjui” alizidi kupinga Defao huku akilia kama mtoto na kitambi chake.

    “Umetokea wapi hadi kufika hapa??.”

    “Hapa Igoma.? Alijichanganya Defao, na kweli hakuwa akiujua mji.

    Majibu ya Defao hayakumshawishi kabisa John akaamini kuwa Defao alikuwa mtu jasiri sana ambaye anaweza kuficha siri za kambi yake, watu kama hawa John aliwatambua kwani naye alikuwa mmoja wao kati ya wanaume wanaovumilia suluba kama hizo katika kazi yake haramu ya ujambazi.

    Mjeledi!!! Akawa amefikiria juu ya adhabu nyingine kwa huyu bwana ambaye hata alikuwa hajamtambua jina. Laiti kama angejua jinsi Defao asivyoyajua yale yeye anayoyafikiria nadhani asingeumiza kichwa chake. Defao alikuwa ni bwege tu!!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mijeledi mitatu ya nguvu iliichana chana ngozi ya Defao, alilia kama mtoto akiwa ameuma meno kwa nguvu sana. Macho yake yalilegea akatoa kilio kingine cha uchungu mkali akapoteza fahamu. John Mapulu akamwacha hapo akaelekea katika chumba cha dereva.

    Dereva akasema hamjui huyo abiria wake.

    “Hata jina humjui??”

    “Simjui bosi wangu.”

    “Gari ya nani hiyo??.”

    “Pale Kirumba wanapokodisha kaka.” Alijibu katika njia ya kuijitoa hatiani.

    “Kwa hiyo mmetokea wapi kuja kule Mecco??.”

    “Kirumba huko huko.”

    Jibu hilo likamtibua John akili yake akawa kama kichaa tena, huyu anasema Igoma huyu anasema Kirumba.

    Wananidanganya!!!! Aliwaza John huku akiiuma uma midomo yake moja kwa moja akawa amemtia hatiani yule dereva. Ngumi nzito ya kushtukiza kutoka katika mkono wa kuume wa John ilitua katika kinywa cha yule dereva akatema jino moja na supu ya damu.

    John alipotulia kwa muda alishangaa kumwona yule dereva akimfuata kumkabili akiwa na bisibisi mkononi, hakushangazwa na uwepo wa ile bisibisi ndani kwani hakuwa amewakagua mateka wake.

    Aliitazama ile bisibisi kama kimswaki wanachotumia watoto. Dereva akakurupuka mzimamzima na kumrukia John Mapulu, mkono wake ukadakwa juu kwa juu akarushwa mzobemzobe, kabla ya kutua chini vizuri mfupa wa mkono ukalia ‘ko!’

    “Mamaa mkono wangu!!” akapiga kelele.

    Alipotua chini akiwa bado analalamika juu ya mkono wake, John alifanya shambulizi jingine la ghafla aliunyanyua mguu wake sole ya kiatu ikagandamizwa kwa nguvu katika mguu wa dereva mfupa mwingine ukalia ‘ka!’, maumivu ya mkono yakawa afadhali kuliko ya lile pigo la mguuni. Akapiga mayowe mengine.

    “Bado unayo mifupa mingine mingi, ukitaka kuondoka nayo utanieleza yule jamaa ni nani na nani amewatuma” alisema John, huku akitaka kuondoka, yule dereva akamtukana mama yake John, John akacheka kwa kejeli kisha akawa kama anataka kuendelea mbele.

    Hivi kanitukania mama yangu!! Alipata kumbukumbu, akarudi mbio mbio akaruka teke moja katika staili ya tik-tak likaufikia uso barabara, nguvu zikauzidi uso mwili ukafuata, dereva akajibamiza ukutani, akaanza kukoroma huku bisibisi ikiwa pembeni yake.

    John akatoka nje!!!



    ****



    Mzee Keto aliwaza na kuwazua juu ya adui yake ambaye kiuwezo alikuwa juu yake. Keto alikiri kuwa tofauti na umri hakuwa na chochote alichokuwa akimzidi mchungaji JK, jambo hilo lilimkera sana akajihisi anaonewa na yupo katika mpambano na mtu asiye na utu.

    Aliwaza kama anaye kiongozi yeyote yule serikalini aweze kumsaidia katika hili akajikuta anaambulia majina mawili tu ya ndugu zake mmoja alikuwa ni balozi wa nyumba kumikumi wakati mwingine alikuwa ni mtendaji wa kata tena kata yenyewe ipo huko vijijini. Keto akajenga tabasamu la bandia lililoibeba karaha yake kisha akasonya kana kwamba aliwadharau ndugu zake kwa vyeo walivyokuwanavyo serikalini. Aliwaona hawana maana, ndio hawakuwa na maana kwa sababu hawakuwa na la kumsaidia wakati ule, hawakuweza kupambana na JK.

    “Lakini huenda na wao wanawafahamu watu wazito huku Dar wanaweza kuniunganisha nao hebu ngoja…” alijisemea kisha akatwaa simu yake aweze kupiga.

    Simu iliita ikapokelewa, alikuwa ni Temba.

    Mzee Keto alijieleza kinagaubaga shida yake, bwana Temba akawa anasikiliza vizuri tu kisha akamjibu, “Aaah!! Shida yako hapo imepata dawa yupo kaka yetu mmoja hapo mjini ni kamanda..”

    “Kamanda…..anaitwa..” aliuliza kwa shauku mzee Keto.

    “Ndio ni Kamanda wa hawa mgambo wa jiji hapo anaheshimika sana” kusikia hivyo mzee Keto akakata simu na kuizima hapo hapo kisha akaanza kutukana matusi mbalimbali aliyoyajua na asiyoyajua. Majibu ya bwana Temba yalikuwa yamemkera. Mgambo wa jiji angemsaidia nini?? Mabango machafu pekee ndio yanayomuogopa mgambo wa jiji, hata machinga hawamuheshimu mgambo, leo hii kesi ya mtu hatari kama JK inapelekwa kwa mgambo wa jiji.

    “Mpumbavu sana huyu bwana Temba…au ndo anazeeka alaa!! Shenzi kabisa, wazee wengine bwana” alimaliza kwa kauli hiyo ya kishari zaidi. Laiti kama angekuwa mbele yake angemtandika kibao.

    Mzee Keto akaondoa shati lake akasalia kifua wazi, akahaha huku na huko akachukua taulo lake, akaelekea bafuni, baada ya kuwa ameondoa nguo zake akagundua kuwa hapakuwa na sabuni. Akavaa nguo zake akarudi chumbani hakutaka tena kuoga. Akajirusha kitandani. Akaanza tena kumfikiria mchungaji JK, alikuwa anaamini ipo bado mbinu ya kupambana naye. Akiwa katika kukata tamaa mara likaja wazo la akuanzaye mmalize na auaye kwa upanga naye atakufa kwa upanga.

    Mganga wa jadi!!! Mzee Keto akapata wazo hilo, akakaa kitako akaanza kulichambua na kuamini huko ndipo mahali sahihi kabisa pa kumkomesha mchungaji JK. Alianza kuwafikiria waganga mbalimbali hatimaye kura yake akaiangusha kwa mzee Manyaunyau, aliiangusha huku kwa sababu mzee huyu alikuwa anasifika sana na haikuwahi kutokea akashindwa jambo kwa waliowahi kupata huduma zake. Mzee huyu alikuwa kiboko ya wachawi, alirudisha mali zilizopotea alikuwa anakamata wezi na hata wale wasichana waliokuwa wanaenda Dodoma wakati wa bunge kwa ajili ya mawindo ya kuwapata wabunge kimapenzi aliwasaidia na kwa kiasi kikubwa walikuwa wanafanikiwa.

    Hakika walikuwa wanafanikiwa maana mara kwa mara walikuwa wanarejea kwake. Wagombea udiwani walisemekana kupitia kwake waziwazi huku wale wa ubunge na uraisi wakienda kisirisiri.

    Chaguo sahihi kabisa!!!! Alikiri mzee Keto.

    Akafikiria juu ya ni wapi atapata pesa ya kutosha ili kunogesha zoezi hili, hakuwa na pesa ya kutosha kwenye hazina yake, kabla ya kufikiria kuhusu kukopa akakumbuka michango ya rambirambi kwenye msiba wa mkewe. Alikuwa anafahamu taratibu zote za michango hiyo na alijua ni kwa jinsi gani ataichukua.

    Siku iliyofuata akawa amefanikiwa kuchukua pesa za kutosha akaongezea na hazina yake. Akapanda gari lake alipowasha likawaka lakini ‘geji’ ilikuwa chini mno, akateremka na kuamua kwenda kwa basi. Safari ya kwenda Msata!!! Msata kwa mganga. Mzee manyaunyau!!!



    ******



    John Mapulu baada ya kuwa ametoa kichapo kikali sana kwa Defao na yule dereva aliyejaribu kujihami kwa kurusha bisibisi, aliingia chumbani mwake akachukua simu aliyokuwa ameichukua kwa Defao wakati wapo ndani ya gari. Akaitazama mara mbili kisha akaiwasha. Kwanza alitaka kujua ni nani alikuwa akiwasiliana naye kabla ya kuja hapo alipotazama kwenye simu zilizopigwa akakutana na jina ‘Mama Jo’, na jingine lilikuwa ni ‘Mama mdogo Mwanza’, hiyo ilikuwa namba ya mama ambaye John alimtumia katika mtego wa kumnasa Defao.

    “Ina maana alikuwa akizungumza nini na mama yake Joram….au na yeye alitaka kumuua kama alivyofanya kwa Joram??” alijiuliza John bila kupata jawabu.

    “Huenda aliwahi kunipigia simu mtu huyu!!!” alijiuliza tena kisha akabonyeza namba zake katika simu hiyo akajipigia, akashtuka baada ya kuona jina katika simu yake linatokea kama ‘Mafao!!’.

    “Mafaoooo!!! Mafao!! Huyu ni nani kwani?” alijiuliza bila kuwa na majibu sahihi.

    Akavuta kumbukumbu kidogo akakumbuka ni lini alihifadhi hilo jina katika simu yake ni siku ile ametoka kumpeleka Joyce kliniki, alikumbuka kuwa ni mlinzi alikuwa amempa namba hiyo kwamba kuna mtu alikuja kumtafuta hapo anaitwa Mafao.

    “Mlinzi yupo nitamuuliza!!” alijisemea.

    Baada ya hapo akataka kuipiga namba hiyo iliyoandikwa mama Jo ili amjue ni nani, alitaka kupiga kwa simu yake lakini akaona ni sahihi sana akiitumia simu ya Defao. Akabonyeza ikaanza kuita ile inapokelewa tu simu ikalalamika ‘low battery’ ikazimika kabla hawajazungumza.

    John akafikiria kuhusu kuichaji lakini haikuwezekana hakuwa na chaja ya simu hiyo ‘Samsung SGH 707’. Akafura kwa hasira kali akaenda kwa mlinzi getini. Akamkuta amesinzia, akamnasa kibao akashtuka na kutaka kukimbia, akamkwida na kumtikisa kidogo akili zikasogeleana.

    John akaunda tabasamu bandia kabla ya kuzungumza, “Unamkumbuka Mafao”

    “Mafao, Mafao yupi kweli!!!” alihoji mlinzi. John akamkumbusha akawa amekumbuka. Akakiri kumkumbuka hata akimuona mbele yake. John akaondoka bila kusema lolote akaelekea chumba alichokuwa Defao. Akaufungua mlango akamkuta akiwa amezinduka tayari.

    “Unaitwa nani??” aliuliza kwa ghadhabu.

    “Naitwa Gervas….”

    “Jina jingine….”

    “Defao!!”

    “Safi kabisa….njoo hapa”

    Defao hakuweza kuinuka, John akamfata alipo akamnyanyua shingo yake, hakika Defao alikuwa hajiwezi, akamwacha akaelekea kwa dereva, alipoingia ndani akakumbana na pigo moja la mgongo lililomwachia maumivu, yule dereva alikuwa amemchoma na bisibisi, kichaa cha mbwa kikampanda John, akamtazama yule dereva aliyekuwa anataka kukimbilia nje akamuwahi akampiga ngwala, akasalimiana na vigaye akatoa kilio kikali. John akajirusha hadi pale alipokuwa adui yake akakutana na shingo yake, kabla hajafanya lolote yule dereva akamuuma mkono kwa meno makali. John akapiga kelele kisha akafyatuka kama mshale akaileta miguu yake yote miwili ikakikanyaga kifua cha dereva akakohoa kwa nguvu halafu tena akamrukia akaikamata shingo yake, akapiga kelele moja tu iliyoambatana na matusi kwa mama yake na dereva, alipomaliza na kumwachia kilichokuwa chepesi kilikwenda juu na kile kizito kikatua chini. Mwili ukaiacha roho ipae na wenyewe kutokana na kuwa mzito ukatua chini. Dereva akawa maiti!!!

    John hakuwa ameridhika alimbeba mzobe mzobe na kutoka naye nje





    ******



    Matha alikuwa katika tahadhari kubwa sana aliamini kuwa Nakayange Mutukula alikuwa ni mtu mbaya sana na alikuwa katika mbinu za kumuingiza matatani. Baada ya kuwa amejadiliana na Michael na kukubaliana kuwa ulikuwa umefika wakati wa kutoroka, alirejea nyumbani kwake Buzuluga ili kulimalizia swali la je? Wanatoroka vipi??

    Akiwa katika harakati za kupambana na majibu sahihi mara simu yake iliita, alipotazama aliona jina la Mutukula, kwanza akapata wasiwasi, kwa nini mtu huyu anampigia usiku wakati walikuwa na ahadi ya kukutana mchana, Matha akaipokea na kuusubiri upande wa pili uweze kuzungumza kwanza, kumbe upande wa pili nao ulikuwa unategea jambo hilo hilo. Upande wa pili alikuwa ni John Mapulu akiwa na simu ya Defao. John akajua anampigia mama JO, wakati huo Matha akijua anapigiwa na Nakayange Mutukula. Laiti wangejuana wapenzi hawa kuwa wanapigiana simu!!!!!!!.

    Baada ya Matha kusikiliza kwa muda mara alisikia upande wa pili ukipotea hewani, alipojaribu kupiga simu ikawa haipatikani. Ni wakati huo ilikuwa imekata chaji simu ile na John Mapulu hakuwa na chaja yake.

    Matha hakutaka tena kulala nyumbani kwake akawa ameamua kwenda kwa rafiki yake maeneo ya jirani.

    Hofu hiyo ikamwongezea ari ya kutaka kutoroka!!!

    Maji yalikuwa shingoni.



    *****



    Joyce Keto alikuwa wa kwanza kutambua kuwa John Mapulu hakuwa sawa usiku huo, John alikuwa na hasira na wala hakuwa na raha wakati akipata chakula cha usiku. Majira ya saa tatu na nusu!!

    “Na hapo umekuwaje tena bro!!” Joy aliuliza huku akilamba kipande cha limao.

    “Wapi tena, umesema” alishtuka John. Joy akaitambua hali hiyo.

    “Mkononi”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Aah!! Hapa hivi” alijibu John huku akijaribu kupanga kichwani majibu ya kumpa Joyce Keto.

    “Kuna mjinga mmoja amening’ata”

    “Na wewe ungemng’ata….akome” alijibu kitoto toto Joyce, John akatabasamu. Kisha akamuuliza Joyce, “Hivi unakumbuka siku ile tumetoka kliniki ukawa unaendesha gari??”

    “Ndio kwani vipi tena unataka niendeshe kesho tena”

    “Hapana una haraka kama nini…siku hiyo kuna mjinga alikuja kutaka kunidhuru hapa nyumbani”

    “Kiaje, ni nani kwani??” aliuliza.

    “We humjui lakini alikuja hapa wakati tunafika na yeye alikuwa ndo ametoka itakuwa tulipishana naye”

    “He!! Kwa hiyo ulimkamata!!!”

    “Unacheza na mimi tena??” alijitamba John huku akitafuna kipande kikubwa cha nyama.

    “Kasoro yule wa Singida aliyenibaka ndo umepuuzia” alilalamika Joyce, John akainama chini kujaribu kuikwepa hatia lakini aliponyanyua macho alikumbana nayo kutoka katika macho ya Joyce.

    John hakuwa na cha kujibu.

    “Ila naamini tutampata tu mjinga sana yule??” Joyce alimtia moyo John baada ya kumuona akiwa katika kuganda kimawazo. John alilijua hilo akatikisa kichwa juu na chini ishara ya kukubaliana na maneno ya Joyce.

    Baada ya chakula John alitoweka na Joyce akaingia chumbani kwake, alipoingia alianza kuwaza kuhusu mimba yake, akamuwaza baba wa mtoto na mara akamuwaza huyo mtu aliyekamatwa na John, akakumbuka kuwa ni mtu huyo aliyesababisha ashindwe kuliona bonde akawa amelifukia.

    “Mtu yule ni nani mbona sura sio ngeni…ni kama nimewahi kumwona mahali, ni wapi vile wapi wapi wapiiii!!” Joyce alikuwa akijiuliza huku akibinyabinya kichwa chake kama namna ya kukilazimisha kukumbuka.

    “Mh!! Hapana bwana nishamuona yule tena mara nyingi tu!!!” alisema kwa sauti Joyce, kidogo atoke kwenda kumwomba John amwone mtu huyo lakini akasita kidogo, akaisikiliza nafsi yake iliyomsihi awe na subira. Akajilaza lakini taswira juu ya mtu ambaye alitishia uhai wa John ikizidi kumwandama. Alijaribu kufikiri bila mafanikio.

    Kesho nitafanya juu chini nimwone mtu huyo huenda anaweza kuwa yeye!! Alimaliza hivyo akajilazimisha kulala.



    *****



    Mzee Keto alifanikiwa kuelewa njia kwa wepesi sana tofauti na alivyotegemea, kumbe ni maeneo hayo hayo alikuwa anapita akiwa anaenda kumtembelea rafiki yake wa siku nyingi tangu ujanani.

    Macho ya mzee Keto yalishangazwa na kibanda alichokitazama kwa mbali alishindwa kuelewa kama hapo ndipo alikuwa akipatikana mzee Manyaunyau, sifa zake hakika hazikuwa zikiendana na kibanda kile, haikuwa nyepesi kwa mtu anayesaidia wanasiasa wakubwa wakubwa kujichukulia nafasi serikalini kuishi eneo kama lile.

    Alizidi kusogea huku mawazo yake yakiacha kufikiria kuhusu kibanda kile bali ubora wa kazi za Manyaunyau. Mzee Keto hata kabla ya kukutana uso kwa uso akajikuta akimchukulia Manyaunyau kama mwanaume jasiri pekee aliyesalia mwenye uwezo wa kumsaidia.

    “Mi sijafuata nyumba hata hivyo” alijishauri mzee Keto huku akitoa tabasamu hafifu lisilokuwa na mpokeaji. Akiwa katika kutafakari juu ya atajieleza vipi kwa Manyaunyau ili aweze kumsaidia kumkomesha mchungaji JK, mara ghafla fikra zake zikakatishwa na honi za gari kutoka upande aliokuwa anaelekea yeye, kwa tahadhari alijiweka pembeni gari likapita kwa fujo na kutimua vumbi kali.

    Mzee Keto aligeuka na kulitazama huku akipikicha macho yake kujaribu kujitoa vumbi lililokuwa limefanikiwa kumwingia na kumsababishia karaha, lilikuwa ni gari la kifahari sana hata kama mzee huyu hakufanikiwa kulitambua modeli yake.

    “Kuna watu wana magari wengine sie tuna usafiri!!!” alikiri mzee Keto kisha akafanya tathmini tena juu ya Manyaunyau, akamchukulia tena kama shujaa, akajisemea kwa kusifu, “Huenda hilo gari limetoka ikulu, mkubwa wa nchi anataka huduma…huyu ndo Manyaunyau aisee.”.

    Hatimaye akiwa katika mawazo kemkem alikifikia kibanda cha mzee Manyaunyau, ilikuwa mara yake ya kwanza kuifuata huduma kama hii, hivyo hakuwa akizijua sheria zinazotumika huku. Alikuwa anatembea kama vile anaingia katika mojawapo ya vibanda vya matunda kwenda kujichagulia.

    “Weeeeee!!!!!” alishtuliwa na sauti ya kukoroma kama inayojilazimisha kuwa nzito wakati ni nyepesi. Akageuka huku na huko akakutana na mzee wa makamo akiwa na nguo ambazo zilimtambulisha ujuzi wake wa kuitwa mganga wa kienyeji. Macho yake mekundu yalikuwa yakimtazama mzee Keto kama vile alikuwa ni adui hatari kabisa ambaye laiti kama angeachiwa dakika moja tu angeleta maafa makubwa sana eneo lile, mzee Keto akawa wa kwanza kuyakwepesha macho yake lakini alipoyarejesha ili kujilazimisha ujasiri hakumwona yule mzee, halafu akiwa kwenye kuganda mara alihisi anaguswa begani, akakumbwa na mtetemeko kabla ya kugeuka akakutana tena na yule mzee safari hii alikuwa anacheka, alikuwa na meno machache kinywani, Mzee Keto akataka kukimbia lakini kabla hajaweza kutimiza azma akashangaa anapigwa bakora makalioni, akawa amekumbushiwa enzi za shule ya msingi alivyokuwa anaogopa kuchapwa sasa amekamatika uzeeni.

    “Vua viatu!!!!” aliamrishwa huku bakora ikiendelea kushambulia mwili wake, bahati nzuri viatu vile vilikuwa vinamzidi ukubwa kwa hiyo ilikuwa kazi nyepesi kuvivua. Alipofanikiwa kuvivua na kipigo kikasimama, yule mzee akaanza tena kucheka kwa sauti ya juu sana katika hali ya kukera mno. Mzee Keto akahisi amedhalilishwa sana lakini alilikemea wazo lake hilo kwani hakuna ambaye aliyemshuhudia wakati akipokea kile kichapo. Kwa ishara yule mzee akiwa bado anacheka alimuelekeza Mzee Keto mahali pa kwenda. Wakakifikia chumba kingine, mlangoni palikuwa na paka mkubwa akiwa amesinzia, kwa uoga wake mzee Keto akamfananisha na simba mdogo, akasita kusogea, mganga akaigundua hofu yake akamzaba kwa kutumia kiganja chake mkono wake maeneo ya mgongoni, mzee Keto akajikunja huku akijipa ujasiri, akampita yule paka akaingia ndani akafuatiwa na yule mzee.

    Ndani ya chumba kile akamkuta kijana umri kwa makadirio kama miaka arobaini. Yule mzee akamkabidhi kwa heshima zote kwa yule kijana, akainama na kuinuka mara tatu, Keto akawa anashangaa tu!!!. Kumbe yule mzee alikuwa ni msaidizi tu wa huyu kijana yule mzee hakuwa na heshima alizopewa kijana huyu, yule mzee hakuwa kama Manyaunyau, huyu kijana mbele ya Keto ndio alikuwa Manyaunyau. Hakuwa mkorofi kama yule mzee, hakuwa mtu wa amri bali mpole na msikivu. Alimsikiliza mzee Keto alipokuwa akijieleza shida zake na mwisho wa siku alitoa majibu ambayo yalimsahaulisha mzee Keto juu ya kipigo alichopokea kule nje, ghafla akajiona ni mshindi.

    “Usijali maombi yako yamekubalika…” Manyaunyau alitamka maneno hayo baada ya mzee Keto kuwa ametupia pesa nyingi katika kisonzo kilichokuwa katika chumba hicho. Baada ya hapo alipewa dawa za kutafuna, kufukiza na kuogea na nyingine ya kunuia alifungiwa. Alisisitizwa sana asitoke nje ya masharti, akakiri kuwa hatavunja masharti. Akapewa amri aondoke kinyumenyume hadi nje, mzee Keto kama mtoto mdogo akafuata masharti.

    “Nyauuuu!!!...” Paka alitoa mlio wa kuashiria shari, mzee Keto alikuwa amemkanyaga yule paka ambaye awali alikuwa amelala. Mzee Keto akakukuruka huku na huko, paka akakimbia. Mzee Keto akamaliza zoezi la kwanza bila kuharibu.

    Huko nje akakutana na yule mzee aliyemwadhibu, safari hii hakuwa akimuogopa tena. Alimkazia jicho kali lililojaa chuki hadi yule mzee akaanza kujichekesha.

    Mzee Keto akawa ameanza rasmi mpambano dhidi ya mchungaji JK, alipofika nyumbani alifuata masharti yote, alifukizia, akaoga na kunuia. Kisha akapata chakula na kuamua kupumzika kidogo lakini hiyo kidogo ikazaa kidogo nyingine hatimaye usingizi ukawa mkubwa akawa amelala jumla hadi asubuhi.



    *****



    Wazo la Joyce lilimsumbua sana usiku mzima, hapakuwa na jipya zaidi ya ile sura aliyokuwa anaifananisha kichwani mwake. Palipopambazuka alifuata kile ambacho akili yake ilikuwa inawaza, aliifuata ratiba yake kama kawaida huku akiifuatilia pia mienendo ya John Mapulu kwa ukaribu kabisa lakini katika tahadhari kubwa. Alihitaji kumfahamu huyo mtu aliye katika mikono ya John Mapulu kabla ya kumshirikisha mtu yeyote. John hakugundua kuwa Joyce alikuwa anafuatilia nyendo zake siku hiyo, na wala hakuwa na haja yoyote ya kuhofia kwani hata siku moja Joyce hajawahi kumwonyesha dalili zozote za kutaka kujua kuhusu nini anajihusisha nacho.

    Tofauti na siku nyingine siku hii joyce alikuwa na jambo, baada ya kustafutahi aliweka mkanda katika deki akawa anafuatilia kwa makini midundo ya kikongo ilivyokuwa inatendewa haki na akina dada na kina kaka katika muziki wa kundi la Wenge BCBG, alikuwa anatabasamu bila kujua kama anatabasamu. Kipande cha limao kilikuwa kimetulia pembeni yake kikisubiri kumfariji wakati wowote atakapokumbwa na kichefuchefu cha mimba.

    Kama kawaida John aliondoka majira ya jioni bila kumuaga Joyce. Joyce aligundua kuwa amebaki na nafasi kubwa ya kufanya kile alichokuwa amekusudia. Baada ya kigiza kidogo kuanza kuingia Joyce hatua kwa hatua bila uoga alitoka hadi nje akamkuta mlinzi akiwa katika dalili za kusinzia, akampita akazunguka nyumba ya nyuma akapanda taratibu kama asiyekuwa katika utafiti wowote akazimaliza ngazi akakifikia chumba. Akaukuta funguo ukiwa umekaa kipweke kabisa katika kitasa cha mlango mmoja akasogea kama mtu anayemnyemelea paka shume ambaye siku iliyopita alikuwa katika hatia ya kukwapua samaki aliyekuwa ameanikwa katika chana cha vyombo, sasa alikuwa amejisahau na alikuwa amerejea eneo la tukio huku akijifanya kuwa hakuwa na hatia. Joyce aliufikia ufunguo akautazama kishujaa lakini akaukamata kwa uoga kabisa ufunguo uliokuwa unaning’inia pale. Akataka kuutikisa ili uweze kutoa kizingiti na mlango ufunguke lakini akagundua kwamba alikuwa anatetemeka, akageuka nyuma kutazama kama kuna mtu alikuwa anafuatilia nyendo zake.

    Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa anamfuatilia. Akiwa katika kufikiria kama afungue ama asifungue akasikia sauti ya mtu kama anakohoa. Akataka kukimbia lakini akajikuta anashindwa kunyanyua mguu na baada ya kuhisi kuwa alikuwa anachanganyikiwa akajikuta ameukamata ule funguo akafungua na kujikuta yu ndani ya chumba. Macho yakamtoka pima!!! Mwanga hafifu uliokuwa pale ndani ulimruhusu kuyaona madonge madonge ya damu yaliyokuwa yamefanya utengano na kuunda kama ramani za milima na mabonde. Akataka kupiga kelele lakini akagundua koo lilikuwa limekauka, sauti haikutoka!!! Akajaribu kumeza mate lakini hayakuwa ya kutosha kulainisha koo lake.



    Akataka kukimbia lakini hofu ya kumshtua mlinzi ikamzuia akabaki ameganda akitetemeka. Mara kile kikohozi kikasikika tena, Joyce Keto akajihisi mbele yake kuna kitanzi na katika kitanzi hicho kuna shingo ya mtu akihangaika kupigania pumzi za mwisho bila mafanikio na baada ya yeye kukata roho itakuwa zamu yake kuwekewa kitanzi kile. Kwa uoga mkubwa akarudi kinyumenyume akaurudishia mlango akautia funguo na kuufunga, akauacha ule funguo ukicheza cheza pale mlangoni kwa staili isiyoeleweka lakini iliyovutia kutazama. Alipogeuka kuutazama akasikia kama unamuita vile, akajivisha ujasiri bandia akahitaji kujua ni kiumbe gani kilikuwa katika chumba cha pili.

    Maji ukishayavulia nguo….Joyce akajiuliza kimoyomoyo bila kutoa sauti. Akauvamia tena ule ufunguo akautoa mahali ulipokuwa na kugundua kuwa zilikuwa mbili. Akafanya makisio yake na kujipa jawabu kuwa ule mwingine utakuwa ni wa chumba cha pili. Akaukamata barabara akakiendea chumba cha pili. Akiwa katika kufungua, akakisikia kiumbe kilichokuwa ndani kikihema kwa nguvu sana, Joyce hakutaka kujiuliza mara mbilimbili juu ya ukali wa hicho kiumbe ndani ya chumba, akatimua mbio safari hii hakutaka tena kujua kama ule funguo ulikuwa unamwita ama la!!

    Joyce akiwa bado ametawaliwa na hofu alipunguza mwendo na alipiga hatua moja baada ya nyingine akamkuta mlinzi tayari akiwa katika safari ya usingizi. Joy akampita kwa kunyata, baada ya kuwa amempita aliendelea kunyata kwa staili ile ile ya kubariki usingizi wa mlinzi. Mara mlinzi alipiga chafya akiwa usingizini, Joyce akajikuta anashtuka na kupiga kelele kubwa. Mlinzi akashtuka kutoka usingizini akiwa na hofu na yeye akakumbwa na mshtuko mbiombio akakiacha kiti chake akakimbia. Joyce naye akakimbia mara mbili zaidi, kila mtu akawa anamkimbia mwenzake katika hali ya kushangaza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Joyce akawa amekuwa wa kwanza kupotelea baada ya kuwa amekimbia na kuingia ndani akiwa anahema juu juu, mlinzi naye bila kujua kitu anachokikimbia akawa amekimbia hadi nyuma ya nyumba, akiwa bado na zimwi la usingizi akihisi kuna jambo baya limejitokeza alikimbia hadi nyuma ya nyumba akakwea ngazi na kufikia vyumba vya juu. Akiwa na wazo la kujificha ili kukwepa hatari iliyopo mbele yake alipozitazama funguo zikiwa zinamchekea mlangoni aliamini mahali pale ndio palikuwa sahihi kabisa kwa ajili ya kujificha akakipita kama hakioni chumba cha kwanza ambacho hakikuwa na funguo akakifikia kile cha pili, alifika mara moja na kuzitekenya kiulaini kabisa zikampa upenyo wa kujitoma ndani ya chumba, akiwa hajui hili wala lile na akiwa kwenye kutetemeka alikutana na utelezi uliokitamani kiatu chake ukakivuta alipoking’ang’ania akawa ameuruhusu mwili wake wote kukutana na sakafu, sakafu ambayo ilikuwa imetawaliwa na mabonge mabonge ya damu. Hofu ikakutana na hofu kubwa zaidi, nafsi ikazidiwa ujasiri yale mafunzo ya ukakamavu aliyofunzwa enzi zake za mgambo hayakuwa na maana tena, mlinzi huyu aliyekuwa anakaribia kutimiza miaka hamsini japo hakuwa akiijua tarehe rasmi ya kuzaliwa kwake akawa amepoteza fahamu baada ya kupokea pigo moja bab kubwa usoni pake. Hakujua kama ni ngumi ama chuma, ni miaka mingi tangu akumbwe na pigo la namna hiyo, pale pale akawa ameziruhusu fahamu zake ziende likizo kwa muda usiojulikana.



    Ilikuwa ni kama jaribio la mwisho kwa Defao, kwani alikuwa hatimaye amejaribu kuipigania nafsi yake aliyoamini ilikuwa lazima itoweke kama akiwa mtulivu. Mateso yalikuwa yamezidi, kila kiungo kilikuwa kimeipata suluba kutoka katika viungo vya John Mapulu.

    Defao aliyekuwa muoga siku za awali sasa alikuwa ameamua kujaribu kupambana japo aliamini kuwa John alikuwa anatisha sana linapokuja suala la mapambano. Siku hii Defao akiwa ameshiba vizuri chakula maridadi alichokuwa ameletewa hapo ndani, alikuwa na wazo la kujaribu kufanya mapambano dhidi ya John, alikuwa ameamua kucheza pata potea. Akiwa na wazo hilo hilo siku nzima, ulifika wakati wa kutenda, ni wakati kigiza kikiwa kimeanza kuingia, mlango ulipofunguliwa akawa amemvamia mtu aliyeingia, akawa amempata barabara akamtandika ngumi moja kali ambayo alikuwa ameivuta kutoka mbali zaidi haijapata kutokea, katika ugomvi watoto huziita ngumi hizo ‘ngumi za kukopa’ yaani inavutwa kutokea mbali, mara nyingi hutumiwa na wale wenye uoga wa kupigana. Aliyepigwa ngumi hiyo hakutoa kelele, Defao akamrukia akaa juu yake akazidi kumjaza ngumi zile zile za kukopa. Mjeruhiwa hakupiga kelele zozote, Defao alipojiridhisha akiwa anatetemeka huku akiwa anachechemea akawa anatoka nje, aliamini kuwa amemuangusha chini John Mapulu.



    Joyce Keto akiwa amejifungia chumbani mwake, alianza kujishangaa kwanini alikuwa katika uoga mkubwa kiasi kile wakati hakuna mtu yeyote aliyekuwa amemuona wakati anaenda kule vyumbani.

    Akiwa katika fikra hizo mara taswira ya mtu yule aliyekuwa anamtilia mashaka zikaanza kumrudia, kwa sasa zilikuja kwa ukaribu zaidi.

    “Gervaaaas!!!.....” alijikuta anapiga kelele, alikuwa ameipata kumbukumbu halisi ya picha ya mtu huyo aliyekuwa anaisumbua akili yake. Huyu alikuwa ni mwanaume aliyekuwa amembaka miezi kadhaa iliyopita na kumsababishia ujauzito, Joyce aliapa kuwa akimtia Gervas (Defao), mikononi mwake basi atamtoa uhai kwa unyama aliokuwa amemfanyia. Sasa alikuwa amepata picha kuwa ni huyo huyo Gervas alikuwa amemuona siku kadhaa zilizopita akiwa anatokea kliniki. Ni mtu huyo huyo John alikuwa amemwambia kwamba alikuwa yupo mikononi mwake, hisia za Joyce zikamuwaza yule mtu aliyekuwa chumba cha pili, yule mtu aliyeunguruma na kumtisha hadi akakimbia. Hisia zikamtuma kuamini kuwa mtu huyo alikuwa Gervas. Ujasiri ukamuingia akawa ameamua tena kurejea kule vyumbani.



    Kabla ya kurejea alibadilisha nguo akawa amevaa suruali ya kitambaa kigumu, akavaa na raba za michezo zisizoteleza. Akapiga moyo konde akaondoka kwa ujasiri mkubwa kabisa kurejea kule vyumba vya nje. Mfukoni alikuwa na kisu kikali, alikuwa na hasira kwa mbali na alikusudia kummaliza Gervas iwapo ni yeye atakuwa katika himaya hiyo.



    Alipiga hatua za kunyemelea kama aliyeshika puto na anapita jirani na majani ambayo kama yakiligusa linapasuka. Alikuwa akitembea kwa tahadhari na uoga pia. Hakuwahi kuua maishani mwake, sasa alikuwa katika wazo hilo la mauaji. Hakika lazima atetemeke!!! Hakumkuta mlinzi, kiti alichokuwa amekalia kilikuwa kimebinuka sarakasi na kubakia hivyo hivyo kikihitaji msaada wa kukinyanyua. Joyce akakipuuzia na kuendelea na mawindo yake. Aliamini mlinzi atakuwa katika maficho yake akijijaza moshi wa sigara kifuani na kuutolea puani na mdomoni.



    Hatimaye alikifikia kile chumba alichoamini ndani yake kuna mtu na mtu huyo alijengeka kichwani mwake kuwa ni Gervas. Wasiwasi ukamjia, chumba kile kilikuwa wazi kabisa, Joyce huku akitweta alijipapasa akakikamata kisu chake katika mkono wa kuume.



    "Liwalo na liwe!!" alijiambia kisha akazidi kupiga hatua mbele akitanguliza mbele kisu chake. Kadri alivyozidi kuufikia mlango ndivyo wasiwasi ulizidi na miguu ikawa mizito kuendelea mbele. Lakini hakuwa na jinsi aliamua kuimaliza ile safari. Hatimaye akawa mbele ya chumba alichokusudia, macho yake yakiwa yapo wazi lakini uoga ulimfanya awe kama ameyafumba.



    Akanyata na sasa alikuwa ndani ya chumba, alikuta mfano wa mzoga ukiwa unapumua kwa tabu halafu ukiwa hauna hata namna yoyote ya mshtuko baada ya Joyce kuungana nao katika chumba kile. Joyce akaweka kisu chake tayari, kisha akaita, "Gere...we Gervas!!", hakujibiwa chochote akainama na kumtikisa huyo aliyekuwa hapo chini. Alipoona hajibu chochote akampiga teke la 'kike kike' bado ule mzoga haukuonekana kukereka na jambo hilo. Joyce akajitahidi kadri ya uwezo wake akaugeuza.



    Ghafla!!! ni kama alipigwa shoti!!!! alijikuta yupo nje hakumbuki kisu kilipoangukia bali alikuta anaingiwa na akili ya kukimbia. Miguu haikuwa mizito tena sasa aliweza kukimbia kwa kasi sana, akafika eneo la katikati ya mlango wa kuingia ndani na ule wa kutokea nje, Joyce akaona kama kuingia ndani ni kujitafutia balaa, akakimbilia nje.



    Uamuzi alioufikia Joyce ni kukimbia.

    Aliyoyashuhudia yalikuwa ni filamu ya kutisha iliyochezwa kwa muda mfupi. Chumba alichokuwa amekifungua muda mfupi uliopita na kukumbana na mabonge ya damu ambayo bila shaka yalitokana na kichapo alichotoa John kwa wabaya wake. Jambo ambalo kwa John kwake ilikuwa kawaida sana.

    Lakini hili la pili ndio lilimshangaza na kumuogopesha zaidi. Katika kile chumba alichosikia dalili ya mtu/kitu kupumua: hali iliyomwogopesha zaidi akakimbia sasa alikuwepo mlinzi wa getini katika hali ya kujongea katika mauti.

    Hofu ikatanda, ni saa ngapi yule mlinzi ametupiwa katika chumba kile na ni dakika ngapi zimetumika kumfanya apoteze hata uwezo wake wa kujitambua??

    Kiumbe hatari!! Hatari zaidi ya John Mapulu!! Aliwaza Joyce huku akizidi kukata mbuga bila kujua ni wapi anaelekea. Joyce sasa aliamini kabisa kuwa katika chumba kile ambacho awali alisikia dalili ya kitu kukoroma, basi ni kitu hicho kilichomsulubu yule mlinzi mzee wa getini, kitu hicho hakikulihofia rungu lake. Kitu hicho kilikuwa kimemsulubu mzee yule na sasa huenda ilikuwa zamu yake Joyce, kuhangaishwa hadi kutolewa uhai. Jambo ambalo Joyce hakuwa tayari kabisa kuona likitokea bila ya kumzaa mtoto wake aliyekuwa amebakiza miezi kadhaa tumboni.

    Joyce alizidi kukimbia gizani akitafuta mwanga ulipo. Siku hiyo ndio aligundua kuwa alikuwa mgeni sana wa eneo lililoizunguka nyumba hiyo aliyoamini kuwa ni mali ya John Mapulu. Joyce alijikuta akifanya jitihada za kupanda na kushuka katika matuta. Alikuwa katika shamba!!!



    Uoga ukazidi nguvu ujasiri, sasa akawa anatapatapa asijue pa kwenda. Akiwa katika mahangaiko hayo ya kutafuta njia ya kutokea alisikia kwa mbali dalili za uwepo wa kiumbe hai eneo lililozunguka, Mbwa!, Paka!! Alijiuliza Joyce ambaye aliwahofia paka kuliko mnyama yoyote maishani mwake. Akiwa katika kunyata nyata alishtuka ghafla, machale yakamcheza akayaheshimu akageuka nyuma, ana kwa ana akakutana na kitu kama mtu si mtu mnyama si mnyama akiwa hoi sana na akiwa anahema juu juu, Joyce alitaka kupiga kelele lakini mikono ikauzidi mdomo ujanja ikawahi kuuziba. Usiseme neno!!!!

    Hofu ilizidi kuchukua nafasi macho ya Joyce yalivyokitazama kiumbe kile cha maajabu. Uso wake ulikuwa umevimbiana hovyo hovyo huku ukitawaliwa na mabonge mabonge ya damu hapa na pale. Kwa mtazamo wa haraka kiumbe huyu ni kama alikuwa ametoka kufyonza damu ya kiumbe mwingine na sasa ilikuwa zamu ya Joyce. Miguu ikasahau wajibu wake wa kuubeba mwili, fahamu nazo zikakimbia majukumu yake, Joyce akalegea, giza likatanda akajikuta katika safari nyingine.

    Alikuwa amezimia.





    *****



    Adrian Mhina alikuwa amepanga mikakati na sasa aliamini ilikuwa imepangika. Mikakati ya kulipiza kisasi kwa John Mapulu kwa vitendo kadhaa vya kinyama alivyomtendea zamani na sasa. Kitendo cha kupokonywa mdomoni mpenzi wake wa kwanza (Matha), pili kubakwa kwa mpenzi na mchumba wa sasa Monica, kisha kama hiyo haitoshi suala la kuchezewa mchezo mchafu na kujikuta katika mkono wa dola kwa kesi ya kukutwa na risasi. Mambo hayo yote Adrian aliamini kuwa muhusika alikuwa ni John Mapulu.

    Roho ya kisasi ikachukua nafasi, Adrian kwa kutumia pesa za miradi ya baba yake na ya kwake anaamua kulipiza kisasi. Wakati huu alikuwa anajiamini zaidi na hakutegemea kufanya kosa la aina yoyote ile. Huku akimtumia kijana wa mjini Stallone, aliyekuwa maarufu kwa jina la Rambo kutokana na umahiri wake katika mapigano ya ana kwa ana na pia matumizi ya silaha .



    Stallone alikuwa akijulikana sana kwa jina lake lakini sio sura yake, ni watu wachache sana waliofanikiwa kuiona sura hii, Adrian alikuwa mmoja kati ya watu hao wachache. Haikuwa mara ya kwanza kufanya kazi na Stallone, kazi ya kwanza ilikuwa kumuadabisha Mark yule kijana ambaye Adrian alikuwa naye siku ile alipokamatwa na risasi katika mkoba wake. Zoezi hilo lilichukua siku tatu, na ukweli kuthibitika kuwa Mark hakuwa akijua lolote juu ya John Mapulu wala risasi zilizokutwa katika mkoba.

    Sura ya Stallone pekee ilimshawishi Adrian kutoa pesa iliyohitajika, Stallone alikuwa na misuli kila upande wa mwili wake, kichwa chake cha mviringo kisichokuwa na nywele kilikuwa na majeraha mengi ambayo sasa yalibakiza makovu tu. Hakuwa na dalili ya kutabasamu, na jicho lake lilikuwa tiba tosha kwa watoto wadogo wanaopenda kulia lia.

    Adrian aliondoka akiwa na matumaini makubwa sana ya kumkomesha John Mapulu.

    Katika kipindi hicho cha kusubiri majibu Adrian alijiweka mbali sana na Matha, alihofia Matha anaweza kutibua mipango yake yote iwapo John atagundua kuwa wanawasiliana hivyo Matha alivyokuwa anapiga simu haikuwa ikipokelewa.

    Na baadaye aliamua kubadili namba kwa muda!!!



    ******



    Michael Msombe na Matha walikuwa katika maandalizi ya mwisho kabisa ya kutoroka, hali ilikuwa imezidi kuwa tete. Mimba ya Matha ilikuwa imeanza kuonyesha dalili za waziwazi kuwa muda wowote ule itachungulia. Michael kwa upendo ulioanza kujengeka kwa Matha, kutokana na kumbebea kiumbe tumboni mwake alikubali kwa roho safi kutoroka ili kukaa mbali na John Mapulu. Kukaa mbali na HATIA.



    Yalikuwa yamesalia masaa arobaini na nane tu mkakati kabambe wa kutoroka uweze kutimia. Matha alikuwa tayari na pesa za kutosha kuwawezesha kufika jijini Arusha ambapo Matha alimwambia Michael kuna ndugu yake atawapokea huko na kuwahifadhi kwa muda kabla ya kuamua ni wapi wanaelekea.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Michael hakuwa na kipingamizi alikubaliana na Matha. Kichwani alikuwa jasiri sana ujasiri uliotokana na penzi kwa Matha na mtoto.

    Usiku huu majira ya saa nane na dakika kadhaa, Michael akiwa katika pumziko kitandani lakini akiwa hajapitiwa na usingizi. Alishtushwa na mlango wake kugongwa kwa nguvu sana, alisimama wima haraka akakitwaa kisu chake akakiweka tayari kisha akaufungua mlango na kumkabili mgongaji.

    Akaghairi na kukishusha kile kisu chini baada ya kukabiliana na John Mapulu. John akaunda mfano wa tabasamu kabla ya kuingia chumbani mle bila hodi.

    John hakuchelewa kuyaanzisha maongezi. Yalikuwa ni maongezi yaliyotangaza hali ya hatari, hatari kubwa.

    “Kuna bwege anatuwinda!!!” alianza kujieleza John huku Michael akimsikiliza, “Ni wale mafala waliomuua Joram, wamevamia anga zangu na kuondoka na watu wangu wawili halafu mmoja wamemuua pale pale na maiti yake wameyaweka katika mlango wa kuingilia…”

    “Wapi?? Mbona mi sijaona???” aliuliza kwa hamaki, Michael Msombe.

    “Sio hapa ni maskani ya kule Nyasaka niliwahi kukwambia…”

    “Kwa hiyo sasa inakuwaje hapa kaka…”

    “Wameanzisha…lazima tuyamalize…”, “Inatulazimu kuwafunza adabu” alisisitiza John, macho yake yakiwa yanang’aa sana, ikiwa ishara za hasira kali.

    Michael akabaki kutetemeka asijue la kufanya, John akaisoma hali hiyo akaongezea neno.

    “Wametoroka na Joyce, wale mabwege wanaweza wakamfanyia mambo ya kinyama sana…”

    “Joyce yupi tena??..nadhani nitakuwa simjui..”

    “Unamfahamu vyema kabisa ni Joyce…..K…Keto…yeah!! Joyce Keto..” Alizungumza kwa kusita sita Mapulu. Michael aliyakodoa macho yake kumtazama John, jina hilo lilikuwa limeanza kusahaulika katika masikio yake, ni jina la msichana aliyemsababishia kuwa hapo alipokuwa, sasa anasikia kuwa na yeye yupo katika kutekwa na wapinzani wa John.

    Ilikuwa ngumu sana kuelewa hadi John alivyomsimulia kila kitu kilivyokuwa kuanzia awali mpaka hapo walipofikia lakini neno moja tu ambalo John hakulisema, sio kwa kusahau bali kwa kuhofia urafiki wake na Michael.

    Suala la mimba!!!! Mimba ya Joyce Keto!!!!

    Somo likamwingia Michael ipasavyo sasa akawa tayari kukamata mtutu wa bunduki kwenda kumkomboa Joyce, msichana pekee aliyeamini kuwa aliwahi kumpenda hadi akapitiliza.

    “Lazima nimpate Joyce, nimweleze kuwa nampenda!!!” alijiapiza Michael huku akiagana na John Mapulu.

    Suala la kutoroka likaanza kuyeyuka kichwani mwake, kutoroka na Matha ni sawa sawa na kumuua Joyce, Michael hakuwa tayari kushuhudia damu ya Joyce ikimlilia.

    “Joyce mmoja alikufa mikononi mwangu sikufanya lolote la kuweza kumwokoa, na huyu wa pili akifa wakati uwezo ninao, ni LAANA!!!” alizidi kujipandisha mori, Michael.



    Michael hakuwa kwenye utulivu kabisa baada ya kupewa taarifa hiyo ya kushtukiza na John Mapulu, akiwa amebaki peke yake alikuwa akijiuliza mara mbili mbili. Alitaka asimuamini John na kuamini kuwa huenda ile ni mbinu tu lakini nafsi ilisita maana John alionekana kumjua Joyce vizuri.

    Hapana hakuna mbinu hapa!!! Alijihakikishia Msombe kabla simu yake haijaunguruma; akasimama akaiendea. Alikuwa ni Matha anapiga, yalikuwa yamebaki masaa machache kabla ya uamuzi wao wa kutoroka kutimizwa. Michael alijifikiria kuipokea simu ile kwa takribani sekunde thelathini, kisha akaipokea huku akiongea kwa hadhari kubwa sana.

    “Michael…Michael…tunatakiwa asubuhi tuondoke….”

    “Kwanini?? Mbona tumepunguza masaa Ma…” akajibu kwa wasiwasi huku akisita kumalizia jina la aliyempigia simu, kwa tahadhari ya kusikiwa na John.

    “Bwege ametuundia mbinu, sijui machale yamemcheza!!!”, alianza kujieleza Matha kwa utulivu kisha akaendelea, “Anataka tuingie kwenye mapambano fulani hivi, nahisi yatakuwa ya kutengeneza tu!!!” Matha alimaliza tuo ya kwanza na kumsikiliza Michael atasema nini.

    “Mh!! We kakwambia lini??” aliuliza Michael kama vile hajui chochote.

    “Usiku huu huu, na wewe anaweza kukwambia asubuhi.”

    “Ma….hebu ngoja asubuhi tutazungumza….” Alisema Michael bila papara.

    “Michael asubuhi ni mbali atatuzidi ujanja huyu na tutashindwa kuondoka, Michael pleeeease.” Alisihi Matha huku akiwa na dalili ya kulia.

    “Hapana naniii…haraka haraka haina baraka, subiri nimsikie kwanza halafu tutajua cha kufanya.”

    “Michael mpenzi wangu, mtoto Michael mtoto wetu, babangu nielewe tafadhali, atatulaani huyu mtoto, tukiingia kwenye mapambano tutamuua, Michael nakuomba Michael” Matha alizidi kulalamika. Maneno yake yakawa kama yana ncha kali kwa mbele, cha ajabu hayakulishambulia na kulijeruhi sikio badala yake yalienda na kuutekenya moyo wake katika namna ya kushangaza, akajisikia uchungu mkali.

    “Tutaongea baadae…” Michael Msombe akajibu bila kuelewa maana halisi kwa Matha juu ya hiyo baadaye kisha akakata simu bila kutilia maanani kilio cha kwikwi kilichosikika na kutoa mwangwi kwenye simu. Michael alizimisha simu yake, mapigo ya moyo yakawa juu sana, alikuwa hoi kimawazo akazihisi dalili zote za kuzimia. Huku Matha analilia kiumbe aliyeko tumboni mwake, huku kuna taarifa kuwa Joyce Keto yupo matatani.

    Michael akaibana misuli ya kichwa chake kilichokuwa kinaanza kuuma kisha akajiongoza hadi sebuleni akaliendea jokofu akatoa maji ya kunywa akayagida kiasi cha glasi mbili. Akapata ahueni akajilaza kitandani.

    Amsikilize nani na asimsikilize nani, nani mwenye umuhimu kati ya Matha na Joyce, kilio cha nani akisikilize!!!! Michael Msombe matatani.



    ******

    Jopo la Stallone baada ya utafiti wa hali ya juu sasa walikuwa wakimjua vyema John Mapulu, walimtazama kwa jicho la nje kama bwege mmoja aliyekuwa akimsumbua Adrian kwa kuwa tu ni dhaifu zaidi yake. Wafuasi wa Stallone hawakushtuka siku walivyomwona kwa mara ya kwanza.

    John Mapulu hakuwa na dalili zozote za kutisha!!!

    Baada ya Adrian Mhina kufanya malipo yale yaliyohitajika sasa ni utekelezaji uliokuwa unahitajika.

    Jopo la Stallone aliyejulikana zaidi kwa jina la Rambo, lilikuwa limeipanga siku maalum ya kwenda kumchukua John Mapulu na kumuadabisha na kisha kumfikisha mbele ya Adrian Mhina akiwa hai. Kwa udhaifu waliouona kwa John, Rambo hakuwa na haja ya kuandamana na vijana wengi, isingekuwa msaidizi wake wa karibu kulazimisha kwenda naye basi angeenda mwenyewe kumkabili John.

    Majira ya usiku wa saa nne bila hadhari kubwa sana, Rambo na mwenzake walikuwa katika geti kubwa la kuingilia nyumbani kwa John Mapulu maeneo ya Nyasaka. Hali ilikuwa shwari sana na tulivu kiasi cha kuwaruhusu ndege warukao angani kuitawala anga watakavyo kwa sauti zao nzuri zisizohitaji ala nyingine kuzipendezesha. Rambo akiwa anajiamini kabisa alitangulia mbele akiwa na silaha yake ndogo ya kisu mkononi huku bunduki ikiwa imehifadhiwa mbali kidogo. Lakini ambapo panafikika kirahisi.

    Geti lilikuwa limeegeshwa kidogo tu, Rambo akamtanguliza mwenzake aliyekuwa ameshika bunduki tayari kwa kumpasua yeyote atakayeleta kipingamizi katika zoezi hili.

    Walifanikiwa kuingia mpaka ndani, hapakuwa na dalili yoyote ile ya kuwepo mlinzi wala kiumbe hai. Rambo akaichomoa bunduki yake ndogo, msako ukaanza mara moja, ni kule kule walipoanzia ndipo walikifikia chumba kilichokuwa na kiumbe hai akiwa hajitambui. Rambo alimnyanyua juu juu akamtazama, hakuwa ameadhibiwa sana lakini ni kama aliangushwa vibaya, hakuwa anaweza kuongea. Rambo akachukizwa na hali hiyo, akaikamata shingo yake na kuizungusha kisha akamkokota kama gunia akamlaza getini.

    Ukafuata msako wa ndani ya nyumba, Rambo alikuwa mwepesi sana akazunguka huku na huko kila chumba, hapakuwa na dalili yoyote ya mtu. Rambo akajisikia hasira kwa mbali, ni kama John Mapulu alikuwa anamcheleweshea muda wa kufanya masuala mengine.

    Sasa walikuwa wamesimama nje ya nyumba hiyo karibu na mwili wa aliyekuwa mlinzi.

    “Tumsubiri au tuje siku nyingine???” Rambo alimuuliza mshirika wake. Hakupata jibu!!!

    Mshirika wake hakuwa na lolote la kujibu, badala yake alihifadhi silaha yake kisha akatoa pakiti ya sigara akachomoa moja na kuchomoa kiberiti akaiwasha. Akauvuta moshi mwingi ndani kisha akaupuliza hewani kwa mara ya kwanza, akauvuta tena na kuupuliza hewani huku akiusindikiza kwa macho. Akaonekana kuufurahia mchezo huu badala ya kuwa makini na nini kilichomleta pale. Rambo naye ambaye hakuwa mtumiaji mzuri wa sigara akawa anautazama ule moshi jinsi unavyopaa hewani katika namna ya kuvutia. Rambo naye akajisahau kuwa yupo eneo ambalo sio la kushangaa shangaa, lakini huenda dharau yao dhidi ya John Mapulu iliwapa viburi. Mshirika akazidi kuvuta sigara kwa juhudi kubwa ili mchezo ule uendelee kuwaburudisha.

    Huku zoezi la kutazama ule moshi angani likiendelea, mara jitu kubwa jitu lililokuwa linatisha sana kulitazama, lilikuwa kama limezidiwa na harufu ya ule moshi sasa lilikuwa limelewa ghafla na kuanguka chini kisha kikatoka kishindo cha namna yake. Rambo alikuwa chini, mshirika alipokuwa akijiuliza kulikoni, mara alishtushwa na pigo la kitu kizito katika mbavu zake, akaegemea upande mmoja kama anayeokota kitu ama anayesumbuliwa na kichomi. Kabla hajapata uwezo mzuri wa kusimama wima, alipokea zawadi nyingine tena safari hii ilikuwa katika paji la uso wake, na alipojaribu kufungua macho yake alikutana na yule jamaa bwege bwege waliyemuona siku kadhaa zilizopita sasa alikuwa sio bwege tena, bali tahira maana alikuwa anatabasamu wakati jitu zito likiwa linavuja damu likiwa limeikumbatia ardhi. Yule mshirika akathubutu kufanya kitendo cha haraka kuitoa silaha yake, mara akajisikia kama yupo katika anga safi ya kuvutia halafu baada ya sekunde chache akatua chini katika ile sakafu maumivu makali yakafuatia.

    “Amekutuma nani hapa!!”

    “Ady…Ady…” ndio neno la mwisho aliloweza kulisikia likitoka kinywani mwake kabla ya kunyamaza milele. John akasonya lakini tayari alikuwa ameupata mwanga.

    Kesho yake majira ya mchana vyombo vya habari vikatangaza kukutwa mwili wa aliyekuwa jambazi anayetafutwa siku nyingi, pembezoni mwa ziwa Viktoria ukiwa maiti. Hakuna aliyeamini kuwa Stallone Rambo hatimaye ameuwawa. Kifo cha mshirika wake hakikumgusa mtu yeyote zaidi ya ndugu zake. Hata jina kufahamika kuwa aliitwa Chriss ni baada ya wazazi wake kuomboleza.

    Taarifa ya kifo cha Rambo ilimshtua John Mapulu, hakuamini kama alikuwa amepambana na mtu hatari kama yule, japokuwa alikuwa ni mtukutu na jasiri alikuwa anamheshimu sana Rambo japo hawakuwahi kuonana hapo kabla. Sasa alikuwa amemuua.



    *****

    Adrian naye alizipokea habari hizi akiwa katika gari la baba yake akiwa anaelekea mahali ambapo Rambo alimwahidi kuwa siku hiyo mwili wa John ambao upo hoi kabisa utakuwepo, Adrian alikuwa mwenye furaha sana, katika akili yake alikuwa anaiona taswira ya Matha, alimtazama jinsi atakavyofurahi akimpigia simu siku hiyo baada ya kukaa kimya siku nyingi. Adrian aliamini kuwa kwa onyo atakalompa John hakika hatathubutu kuendelea kuwa na Matha.

    “Akileta ubishi mi naua kwani nini bwana!!” Adrian aliongea peke yake.

    Baada ya taarifa ile Adrian aliyumba kidogo aipeleke gari mtaloni kabla ya kuiweka sawa akapunguza mwendo na kuegesha pembeni. Habari ile ilisomwa kwa kirefu sana na ilikuwa na hadhi ya kuitwa habari kubwa. Adrian sasa akaisikia njaa ambayo tangu asubuhi ilikuwa ikimsumbua ikitoweka na kutwaliwa na hofu kuu moyoni.

    Mungu wangu!!! Kama Rambo alinitaja kuwa ni mimi nilimtuma itakuwaje…au sio John aliyemuua???....eeh!! Mungu saidia asiwe John maana…..Aliwaza Adrian huku akisikia kabisa mapigo yake ya moyo yakiwa juu sana.

    Ni siku hiyo aliyotegemea kabisa kuwa Rambo atamletea majibu juu ya John na ilikuwa ni hiyo safari aliyokuwa anaelekea huko kwa Stallone Rambo, sasa anasikia Rambo ni marehemu!!!!!!

    Mshtuko!!!!



    ******

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mzee Keto baada ya kuyamaliza masharti yote aliyopewa na yule mganga wa kienyeji sasa lilikuwa bado sharti moja tu ambalo lilikuwa kuu kabisa. Mzee Keto akiwa anamwamini kabisa mganga huyu maarufu kabisa katika jiji la Dar Es Salaam, sasa alikuwa anaenda kumkomesha mchungaji JK ambaye aliamini kuwa ni yeye aliyemtenda mama yake na Joyce hadi akafikia uamuzi wa kujinyonga.

    Jumapili hii ilikuwa zaidi ya jumapili nyingine, waumini walikuwa wengi sana, kulikuwa na wageni kutoka nchi za nje ya bara la Afrika waliokuwa wametembelea kanisa la Jacob Komanya, wageni wengine walikuwa wakitokea nchini Naijeria, nchi ambayo alichukua shahada yake.

    Kwaya mbali mbali zilitumbuiza na hatimaye ukaja ule wakati wa maajabu, maajabu ambayo yalikuwa kwa nia moja ya kushawishi waumini kutoa sadaka kubwa na kuwavuta wengi ambao bado walikuwa hawajajiunga na kanisa hilo.

    Mchungaji JK, alikuwa anatoa neno akikemea mapepo na sasa alianza kutetemeka.

    “Kuna shetani amemuingilia mpendwa mwenzetu…Hatutakubali hata kidogo aondoke hivi hivi, aleluyah!!!....shetani shetani…kwa nini shetani anatutawala kwanini lakini…” aliendelea kulalamika mchungaji JK, wakati huo waumini wengine walikuwa wakinena kwa lugha.

    Mzee mmoja naye siku hii hakuwa mgeni hata kidogo. Naye alijumuika kwa bidii zote kunena kwa lugha, alifanana na waumini wengine kwa kila kitu.

    “Mungu amenijalia talanta…talanta ya kulihubiri neno lake lakini akaniongezea uwezo wa kumtambua adui yangu, leo kuna shetani anataka kunitoa uhai…mtumishi wa Mungu natakiwa kuuwawa nikiwa katika himaya yangu, nikiwa katika hekalu la bwana, madhabahu yaliyobarikiwa!!!” alizungumza kwa hisia kali huku mkalimali akitafsiri kwenda katika lugha ya kiingereza. Wageni wale walioitambua lugha ya kiingereza wakapatwa na majonzi huku imani yao ikiendelea kuimalika kwa mchungaji huyu anayemiliki kanisa peke yake akiwa na vyeo mbali mbali kikiwemo cha uweka hazina.

    Mchungaji JK alizidi kuzungumza kwa kufokafoka mithili ya mpiga debe wa daladala za Dar es salaam, alikuwa akirudia maneno kadhaa kama mtu anayeyakariri, na sasa alikuwa anapiga hatua kulizunguka kanisa.

    Mzee Keto akaanza kutetemeka, maneno yale makali ni kama yalikuwa yakisemwa kuelekea kwake, alikuwa anatamani akimbie lakini hakuweza kunyanyua mguu wake kupenya umati huu mkubwa. Ile hatia ya kuingia katika kanisa hilo akiwa na dawa za kienyeji alizoambiwa kuwa zitamkomesha mchungaji JK ikaanza kumshambulia, Hatia ilikuwa inamsuta, akaanza kukiri kuwa mchungaji JK ni mtumishi wa Mungu na kwa vyovyote vile Mungu wake wa kweli atamuumbua mzee Keto hadharani.

    Hofu ikazidi na sasa mchungaji JK alizidi kumkaribia mzee Keto, mchungaji alikuwa anavuja jasho, wafuasi wake walikuwa bize wakimfuta kwa kutumia vitambaa vyeupe na vyekundu.

    “Nasikia nguvu za giza eneo hili..nasikia nguvu za giza eneo hili….Mungu ni mkubwa Mungu ni mkubwa!!! Nguvu za giza hazina nafasi katika himaya yake!!! Ooooh!!! Haleluyaaah!!” Alinena kwa fujo mchungaji, mzee Keto akajifanya amefumba macho, mikono yake ilikuwa inatetemeka.

    “Ni nani alinituma kwa Manyaunyau!!!” alijiuliza huku akiiomba mizimu ya mababu zake imwepushe na aibu iliyo mbele yake.



    Umati ukazidi kumfuata kwa macho mchungaji JK wakati akiwa ameweka kituo kidogo jirani na mahali ambapo mzee Keto alikuwa amesimama na waumini wengine.

    Mzee Keto aliyakumbuka masharti aliyopewa na mganga Manyaunyau na sasa alikuwa akishuhudia yale aliyoelezwa yakitokea mbele yake mchungaji JK alikuwa pembeni yake.

    “Akisogea tu angusha kitambaa chini…pale utakuwa umemaliza kila kitu..” maneno ya mganga yalikuwa yanajirudia rudia katika mfumo wa mwangwi kichwani mwa mzee Keto. Akajivika ujasiri huku akiwa anatetemeka akakichomoa kitambaa na kutaka kukidondosha chini. Ilikuwa ni kama mchungaji JK alikuwa akilisubiri tendo alilotaka kufanya mzee Keto na yeye aweze kugeuka, kile kitendo cha mzee Keto kudondosha kitambaa, kitambaa chekundu akakumbana na macho makali mithili ya Simba jike katika mawindo yalikuwa ni macho mawili ya mchungaji JK. Mzee Keto akaanza kutetemeka akataka kukimbia lakini mlango wa kutokea ulikuwa mbali sana, akafadhaika, sasa mchungaji JK alikuwa anapiga hatua katika namna ya majivuno, kanisa zima lilikuwa kimya, kiatu chake cha bei ghali kilikuwa kinasalimiana na ile ardhi yenye marumaru na kutoa mlio ambao haukuleta bughudha katika masikio ya waumini.

    Mzee Keto akazidi kutetemeka na sasa bila ridhaa yake alijikuta anakaa chini.



    ****



    ***MICHAEL katika wakati mgumu sana wa kufanya maamuzi aidhaaaa amfuate MATHA na penzi la wizi ama amuokoe JOYCE KETO kutokena na penzi la dhati!!



    ***MZEE KETO anashangaa dawa zake hzifanyi kazi mbele ya mchungaji huyu....Je? ni kipi kimesababisha iwe hivi...in maana JK ni mtumishi wa Mungu kweli!!!!!



    ***ADRIAN katika majuto ya kunzisha vita na JOHN MAPULU!!!



    ***JOYCE KETO yu wapi???

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog