IMEANDIKWA NA : Nasri Mgambo
*********************************************************************************
Simulizi : Kivuli (The Catching Shadow)
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa kashikilia nyaraka za kibenki mikononi mwake, kwa taratibu Johari alielekea chumba maalum cha maongezi cha benki yao. Chumba ambacho kilitengwa maalum kwa ajili ya kufanya maongezi na wateja wa hadhi kubwa wa huduma za kibenki zilizotolewa na benki ya National Investment Bank, ama NIB, ambayo ndiyo Johari alikuwa akiifanyia kazi. Moja ya majukumu ya Johari hapo benki ilikuwa ni kuonana na kufanya mazungumzo na wateja wakubwa wakubwa wenye uwezo na hadhi kubwa wa benki hiyo.
Ndani ya chumba alichokuwa akielekea mlikuwamo na bwana Jama Bhanji, ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu na mtu tajiri sana na aliyekuwa miongoni mwa wateja wakubwa kabisa wa benki ya NIB. Hivyo Johari alikuwa anaelekea kwenye mazungumzo na kumhudumia mteja mkubwa wa benki. Ndani ya hicho chumba bwana Jama Bhanji alikuwa kashikilia kikombe cha kahawa akiwa anainywa taratibu, huku macho yake kayarushia kwenye runinga ya kisasa iliyokuwamo ndani ya chumba hicho na ambayo kwa wakati huo ilirusha taarifa ya habari na wakati huo kiyoyozi kilipulizia hewa ya ubaridi kwenye chumba. Mara tu Johari alipofungua mlango wa chumba hicho na kuingia bwana Bhanji alitoa macho yake toka kwenye runinga na kumtazama Johari aliyeingia ndani ya chumba hicho, huku akiwa kajaza tabasamu usoni, akionekana nadhifu kwa suti aliyovalia.
Kwa bashasha Johari aliongeza tabasamu la uso wake na kuelekea kukaa kwenye kochi lililotazamana na kochi alilokaa bwana Bhanji, kisha akamkaribisha na kumwambia jinsi benki yao ya NIB ilivyo na furaha kuendelea kumhudumia mtu wa muhimu katika uwekezaji nchini. Maongezi yao yalihusisha mapitio ya faida za gawiwo ambazo bwana Bhanji alizipata kutokana na kuwekeza kwenye makampuni na miradi mbalimbali ambayo benki ya NIB ilimshauri mfanyabiashara huyo awekeze. Kwenye kikao hicho bwana Bhanji alijawa na furaha sana kwa maana miradi yote liyoshauriwa awekeze na watu wa benki hiyo ilikuwa imemuingizia faida nyingi sana na hivyo akamuahidi Johari kuwa ataendelea kutumia huduma za benki yao ya NIB na kufuata shauri za benki hiyo juu ya masuala ya uwekezaji.
Kikao cha siku hiyo na bwana Bhanji kilienda vizuri sana hivi kwamba Johari alisifiwa na wafanyakazi wezie na viongozi wake kazini kwa kuweza kushughulika na wateja wakubwa wakubwa wa benki hiyo, wateja ambao walikuwa wa hadhi kubwa na kila benki iliwalilia na kufanya jitihada kuwapata.
Johari alijawa na furaha na kujiona mwenye bahati na akili nyingi kwa kuweza kufanya kazi na kushughulika na watu wa hadhi ya juu. Alijivunia sana moyoni.
Kwa hakika Johari alikuwa ni mwanamke mwenye bahati sana. Alikuwa msomi, mrembo, mnyenyekevu, aliyependwa na watu kila mahala,maofisini, majirani na koote alikokwenda alipendwa, alikuwa na uwezo mkubwa kwa maana kazi yake ya benki ilimlipa vizuri na kumpa heshima. Na pia Johari alikuwa keshaolewa, na alimpenda sana mume wake ambaye aliitwa Malcom Munyisi. Malcom alikuwa akifanya kazi katika wizara ya mambo ya nje, kazi ambayo ilimfanya asafiri sana kwenda nje ya nchi katika nchi za ulaya, arabuni, uchina na hata amerika, Johari alifurahia sana kazi hiyo ya Malcom.
Hakika Johari alionekana mwenye bahati sana kwa wakati huo. Ila!, kama inavyosemekana miongoni mwa waswahili ya kuwa hakuna kizuri kisicho kasoro, basi ndivyo vivyo hivyo ilivyokuwa kwa Johari Chande Munyisi.
Na kichwani mwake Johari aliwaza sana mambo yaliyomtia kasoro. Pamoja na furaha zake na bahati zake alizo kirimiwa na mwenyezi mungu, katu hayakutoka kichwani mwake mambo yaliyomtia kasoro na aliyawaza sana.
Mambo yenyewe yaliyomtia kasoro yalianza kama miaka kumi na nne kabla ya wakati huo. Enzi ambazo Johari alikuwa binti yatima, mwenye maisha magumu ila binti aliyekuwa kajawa akili hivi kwamba alipata nafasi kujiunga na chuo kikuu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa ugumu wa maisha aliokuwa nao Johari kipindi hicho alichokuwa akisoma, alijikuta akiingia kwenye mahusiano na kijana mtukutu aliyeitwa ‘Kutu’. Kutu alimpenda sana Johari na alimpa kila kitu. Na akawa akimshawishi Johari ajiunge na kundi la kiharifu la kivamizi lililoitwa ‘mapanya’. Johari katu hakukubali kujiunga na kundi hilo la kiharifu.
Basi ikafika siku moja ambayo Johari alitimuliwa chuo na kuambiwa kuwa hatofanya mitihani ya mwisho wa ‘semester’ hadi atakapolipia ada ya chuo. Kitendo hicho kilimuuma sana na kumtia hasira, hivyo akafanya maamuzi mazito ya kuamua kujiunga na kundi la kiharifu la ‘mapanya’, ikiwa kama njia yake ya kujinasua toka kwenye ukata.
Hivyo kwa msaada wa bwana ake, Kutu, Johari alifanikiwa kujiunga na kundi hilo la kiharifu. Na akiwa ndani ya kundi hilo, haraka sana Johari alipata ada ya kulipa chuo na pesa nyingi za kufanyia mambo mengine. Na akawa mshirika mkubwa wa waharifu wa kundi hilo, ambalo lilifanya uharifu katika maeneo mbalimbali kwa kupora, kukaba na kuibia watu na kusaidia usambazaji wa madawa haramu ya kulevya.
Johari aliona kila kitu kinaenda sawa kwa kushiriki kwake kwenye uharifu wa kundi la ‘mapanya’. Mpaka usiku mmoja mambo yalipoanza kwenda kombo baada ya kuvamia nyumba ya mfanyabiashara mmoja wa madini mwenye asili ya kieshia.
Katika usiku huo mnene wa manane, kundi la ‘mapanya’ wakiwa wamevalia vinyago usoni, na silaha za bunduki, masime na mapanga, walivamia nyumba ya mfanyabiashara wa madini na vito vya thamani. Walifika na gari yao aina ya ‘Noah’, wakiwa kundi kubwa sana na waliojipanga wakiwa na uelewa wa ramani nzima ya nyumba ya mfanyabiashara huyo na walikuwa wakifahamu kila mahala ambapo vitu vya thamani vilikuwa vimefichwa kwenye nyumba mfanyabiashara huyo, tena walikuwa na funguo zao wenyewe za milango ya kila kona ya nyumba hiyo.
Bila huruma kundi la mapanya walimshushia mfanyabiashara huyo kipigo kikali mbele ya familia yake na kisha kuanza kupekua kila walipofahamu pana vitu vya thamani na kuanza kuchukua vitu hivyo.
Johari akiwa miongoni mwa waharifu wa kundi hilo la ‘mapanya’, tena mtoto wa kike pekee kundini, alishiriki vyema katika tukio hilo la kikatili. Na alishuhudia jinsi waharifu wezie walivyo mdhalilisha yule mfanyabiashara na mkewe mbele ya mabinti zao wawili. Alishuhudia jinsi yule mfanyabiashara na mkewe na mabinti zao walivyolazimishwa kulala kifudifudi kwenye sebule ya nyumba yao na kuzuiwa kutoa kelele za aina zozote na kupewa vitisho vya kukatishwa maisha dakika yeyote watakayo neng’eneka kwa namna yeyote ile. Mfanyabiashara wa watu alikuwa hoi kagalagazwa sakafuni, damu zikimtoka mdomoni na puani, alikuwa kakosa kabisa la kufanya zaidi ya kulia shahada kwa sauti ya chini, “la ilaha illa llah, la ilaha illa llah”, huku akiomba waharifu wabebe kila walichoona kinawafaa na kuondoka. Johari aliyekuwa kavalia kinyago alimuangalia mzee huyo na kuona jinsi alivyolia kwa mungu wake na kuwalilia wao, na mara akamuona Kutu akitoa bunduki na kumnyooshea mzee huyo na familia yake ili awaue.
Hapo sasa Johari alijikuta akiingiwa na huruma kidogo na akamuomba Kutu amwache mzee huyo na asimuue. Kutu ambaye alikuwa ni muharifu sugu alimtazama Johari na kuangua kicheko cha kishetani shetani kisha akafyatua risasi toka kwenye bunduki hiyo na kumuua mzee huyo. Hivyo Johari akashuhudia mzee huyo wa watu jinsi ambavyo risasi ilitawanyisha kichwa chake na kumpoteza uhai ndani ya sekunde, huku mke wa mzee huyo na mabinti zao wakishuhudia na walishindwa kujizuia na wakatoa ukelele wa kilio. Mara Kutu akawafyatulia risasi wote, huyo mama wa kiarabu na mabinti zake wawili na kuwaua.
Johari sasa hata kinyago akakivua hakuamini alichoshuhudia kikitendwa na Kutu. Johari alijikuta akitetemeka kwa kuogopa alichokiona. Macho yalimtoka na akajikuta kamvamia Kutu na kumhoji kwa hasira umuhimu hasa wa kuwaua yule mama na mabinti zake pamoja na baba yao mfanyabiashara. Kutu akamtazama Johari kwa jicho la ukali sana na kisha akamnyooshea bunduki na kumuwekea kichwani. Johari alikuwa na hasira sana wakati huo, hata hakuogopa hiyo bunduki aliyowekewa kwenye paji la uso. Tena wakati huo Johari mwenyewe alikuwa na bunduki yake mkononi. Mara wale waharifu wengine ambao hawakushtushwa na kilichotendwa na Kutu walikuwa washamaliza kubeba vitu vya thamani vya ndani ya nyumba hiyo, hivyo wakaamrisha Kutu na Johari waache upumbavu wao na kuamuru kuwa wote waondoke haraka toka kwenye nyumba hiyo. Hivyo wote wakiwamo Johari na Kutu walitoka nje haraka na Kurukia kwenye ‘Noah’ yao na ‘kuondoka’ pamoja na pesa na vito vya thamani walivyoiba.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usiku wa siku hiyo na wiki kadhaa zilizofuatia Johari alishindwa kulala kabisa kwa maana kila mara alipolala ilikuwa lazima aote juu ya ile familia aliyoshuhudiwa ikiuwawa na Kutu. Kwenye ndoto moja, aliota wanawake watatu waliovalia mavazi meupe na kujifunika hijabu wamelala kifudifudi kwenye sakafu huku damu zikiwavuja toka vichwani mwao na kuchafua nguo zao nyeupe, aliota akihangaika kuwapindua ili aone sura zao na kujua ni akina nani, ila ghafla waliamka wenyewe na kumtazama na aliona sura zao ni zile za yule mama na mabinti zake wawili waliouwawa na Kutu. Kila mara taswira za yule mama na mabinti zake zilimjia, mara nyingine aliota wakimlilia kwa uchungu mwingi, mida mingine alilala akahisi wapo nje ya dirisha la chumba chake wakimlilia. Kila mara Johari aliisikia sauti ya yule mzee aliyokuwa akiitoa muda mchache kabla hajauwawa, aliyasikia maneno ya shahada ya yule mzee, alisikia “la ilaha illa llah, la ilaha illa llah”, alisikia sauti hiyo ikianza kidogo na kisha kupanda na mara ikawa inageuka na kuwa kilio kikubwa cha mzee yule akimlilia.
Kama hiyo haikutosha, miezi michache baadae, Kutu alihusika katika ajali mbaya sana. Johari ambaye alikuwa na mahusiano na Kutu alipopokea taarifa alishtuka sana kujua kuwa Kutu alikufa kinyama kwa kuteketea kwa moto huku akijiona baada ya basi alilokuwa akisafiria kupata ajali na kusha kuwaka moto, tena katika hali isiyo eleweka abiria wote wa basi hilo waliwahi kutoka kwenye basi kasoro Kutu peke yake, ambaye alinasa kwenye basi na alichelewa kutoka hivyo akateketea kwa moto huku watu wakishindwa kumuokoa kutokana na ukali na ukubwa wa moto hivyo akafa akijiona. Johari alishtuka sana kwa taarifa ya kifo cha Kutu, alitetemeka na moja kwa moja alielewa huo ulikuwa ni mkosi.
Kama haikutosha waharifu wengine wawili wa kundi la mapanya walipata ajali mbaya sana na kufariki huku ndani ya wiki hiyohiyo waharifu watatu wa kundi la mapanya waliuwawa kinyama na maaskari walipokwenda kufanya uvamizi katika nyumba moja mitaa yenye ulinzi mkali. Waharifu wengine wakapotea hivyo Johari hakuwasikia wala kuwaona tena zaidi ya kuona matangazo kwenye vyombo vya habari wakitafutwa na ndugu zao.
Johari aliuelewa mkosi huo, kuwa ulitokana na Kutu kuua ile familia ya yule mfanyabiahara wa madini pamoja na familia yake. Ila kichwani mwake Johari alijiuliza sana mbona yeye hayamkuti ya kumkuta, na hivyo aliishi kwa hofu na wasiwasi. Ila hakupatwa na lolote japo ndoto aliendelea kuota ndoto za ajabu ajabu hadi usiku mmoja alipopata ndoto ya kutisha.
Usiku huo aliota akitembea na kukimbia kimbia katikati ya msitu mnene wa kutisha, akiwa na kiu, jasho likimtoka, nywele zikiwa zimemtimka, gauni lake likiwa chafu kwelikweli, huku akiwa kajawa na hofu, wasi na mashaka, na huku huku akisikia sauti za vilio na vicheko.
Mara akajikuta katokea nje ya msitu huo mnene ulioshonana na kuufikia uwanja mkuubwa. Katikati ya huo uwanja Johari aliona kuna watu wamekaa kwenye jamvi, wamevalia mavazi meupe. Walikuwa watu kama sita hivi.
Johari alipoangalia kwa makini aliona kuwa kumbe miongoni mwa wale watu walikuwamo yule mfanyabiashara aliyeuwawa, pamoja na mkewe na mabinti zao wawili, huku wakiwa pamoja na wanaume watatu wengine warefu sana na waliovalia mavai meupe.
Kwa hofu Johari alishindwa kuwakimbilia akabaki akiwaangalia hadi walipomuona na kunong’onezana jambo. Kisha moja kati ya wale wanaume watatu akainuka na kusimama na kumuelekea Johari huku uso kaukunja, alijongea hadi akamfikia, Johari alijikuta akiishiwa nguvu na kushindwa kusimama na kujikuta akipiga magoti mbele ya mwanamume yule.
Yule mtu alipomfikia Johari alisimama pembeni yake na kuanza kuongea kwa sauti ya kutisha, “Johari, Johari, binti mrembo uliyeingia kwenye majanga. Binti uliyekosa imani juu ya mungu wako akupaye riziki ukachukua maamuzi ya kujiunga na kundi la kiharifu ili kufanya maovu ulijiaminisha kuwa yangeweza kukuondolea ukata na kukuondoa kwenye lindi la umaskini”, aliongea mtu huyo huku mavazi yake meupe yakiwa yanang’aa hata yakaweza kuumiza macho ya Johari.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wezio wewe Johari, wezio wa kundi lenu la kiharifu, wamepata mikosi na kupoteza uhai wao na hakika nakwambia wao ni wa motoni. Hivi wewe muharifu unaweza kujua uchungu wa yule baba na mkewe kupoteza uhai na kuona mabinti zao wakiwa pamoja nao akhera?”, aliuliza huo mwanaume huku kaakimnyooshea Johari mkono awaone yule baba na mkewe na mabinti zake waliokuwa wamekalia kwenye jamvi pale kati uwanjani. Na kisha akaendelea kumwambia “Wewe Johari utabeba mzigo wa utasa, ujue uchungu wa kukosa mwana. Huo ndio utakuwa mtihani wako wa kukufunza kuwa na imani.Huo utakuwa ni mtihani ili kukurudisha katika mstari wa binadamu mtenda mema, nenda tenda kwa akili ikiwezekana tubu popote itapobidi na fanya toba, mungu atakusamehe na utakuwa miongoni mwa waja wema, ila ukiendekeza ubinafsi wako mikosi zaidi itakuwa yako”, alimaliza kuongea huyo mtu na kutoweka kisha wale watu wengine wote waaliokuwamo uwanjani wamekalia jamvi, akiwamo yule baba na familia yake wakatoweka pia. Baada ya kuamka toka kwenye ndoto hiyo, Johari hakuota tena ndoto mbaya mbaya. Ila kutokana na imani yake ndogo alipuuzia ndoto hiyo na hakutilia maanani nini hasa ilimaanisha kwenye maisha yake kuanzia wakati huo na akaendelea na maisha yake ya kawaida.
Baadaye Johari alihitimu elimu yake ya chuo kwa ufaulu wa alama za juu sana na hivyo akapata ufadhili wa kuendelea kusoma kwa ngazi ya ‘masters’ na kupata ajira, hivyo akabadilisha kabisa hali ya maisha yake na ya shangazi yake aliyeitwa Roda ambaye ndiye aliyemlea baada ya wazazi wake kufariki alipokuwa mdogo. Johari akaja kufahamiana na mtu aliyeitwa Malcom Munyisi na kupendana na kufunga ndoa. Kisha akajaliwa kupata nafasi muhimu ya kufanya kazi katika benki ya NIB, iliyokuwa moja ya mabenki makubwa nchini. Kwa ujumla maisha yake yalionekana yamekamilika, yaliyobarikiwa na mungu na ambayo kila mwanamke wa angeyatamani. Ila!, Johari aliishi katika ndoa na mumewe kwa miaka kumi pasina kupata mtoto, wala ujauzito wala dalili yeyote na ‘unukio’ wa ujauzito.
Johari alifahamu vizuri tatizo lake lilitokana na mkosi ‘aliojiokotea’ kutokana na maasi yake aliyotenda huko nyuma ila akiwa pamoja na mume wake walihangaika mahospitali kwa wataalam wa tiba za uzazi ambako tatizo lilionekana liko upande wake, tena tatizo lililowastaajabisha wataalamu kwa maana viungo na maumbile yake hayakuwa na kasoro yeyote ile iliyoeleweka kusababisha asishike ujauzito kwa sababu za kuelezeka.
Kadiri miaka ilivyokuwa ikienda Johari alizidi kuwa mwenye wasiwasi kuwa ipo siku eidha Malcom ama ndugu zake watazidiwa na hamu ya kuwa na mtoto kwenye familia na pengine hata kulazimisha ndoa yao kuvunjika, aliwaza sana juu ya jambo hilo na aliombea lisimtokee.
Kwa upande wa Malcom yeye alikuwa ni mtu mwenye mambo ya kizunguzungu, pengine ilitokana na maisha yake yaliyojawa na kwenda ulaya kila mara kila mwezi, hivyo yeye aliangalia tatizo la mkewe la kutopata ujauzito kama tu tatizo la kuendelea kulishughulikia na alizidi kuonesha mapenzi kwa mkewe. Ila sasa tatizo lilikuwa ni mama yake Malcom na mdogo wake wa kike aliyeitwa Snura, ambao wao walikuwa ni waongeaji na wenye mambo ya ukorofi sana.
Basi siku moja Malcom alimchukua Johari na kwenda nae kwao kwa mama yake kutembea. Siku hiyo walikuta kuna wajomba, baba wadogo, shangazi, mama wadogo wa Malcom wote wapo, kwa mshangao walioupata kwa kutotarajia uwepo wa ndugu wote hao, Malcom na Johari wakaambiwa kuwa hao ndugu wote walialikwa wajumuike siku hiyo kuzungumza mambo mbalimbali ya msingi ya kifamilia ikiwemo na kumshauri Malcom kwenye masuala muhimu ya kimaisha.
Wakiwa ndugu wote wamekaa chini ya mwembe nje ya nyumba ya kina Malcom, na Johari akiwa yuko hapo akijinyenyekeza mbele ya maongezi yao, mara mmoja wa wajomba wa Malcom akaanza kuongelea jinsi alivyojaaliwa kuwa na watoto watano wa kiume ambao aliwaita majembe na kuwasifu ni vidume hasa, na mara shangazi yake Malcom akadakia na kueleza jinsi ambavyo alijaaliwa kuzaa watoto saba na mwenyezi mungu na kushangaa hasa kwanini vijana wa kileo hawaelewi umuhimu wa kuwa na watoto mapema ilihali uhai ni mfupi.
Johari hakufurahia maongezi hayo aliona kabisa yanamsakama yeye na mumewe kwa kukosa mtoto.
Mara katikati ya mazungumzo hayo alifika binti mdogo, mzuri na aliyeonekana mpole na kuwaamkia kwa heshima na kujieleza kuwa kaja kumtembelea Snura, yani mdogo wa kike wa Malcom, mama Malcom kwa furaha sana alimkaribisha binti huyo na kumuelekeza aelekee huko nyuma ya nyumba kwenye jiko ambako Snura alikuwako akipika, na binti huyo akaelekea huko huku nyuma yake hapo chini ya mwembe ndugu zake Malcom walimtupia macho huku wakiwa na furaha na kuanza kumsifu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alianza baba ake mdogo Malcom kusifia, “kabinti kapoole, kazuuri, kanafaa kweli kuwa mke wa mtu ila laa!, vijana wetu wanaokoteza wanaacha mawari kama hawa mikoani”, akadakia mama ake mdogo Malcom, “tena kwa jinsi alivyo mpole binti huyu akiolewa wala hababaiki anazaa ‘fasta’, sio mijanamke mingine miaka dahali ‘no’ mtoto ‘no’ nini”, mama mdogo huyo aliongea kwa sauti. Maneno hayo yalikuwa wazi yakimlenga Johari. Mara akadakia mama ake Malcom, “Unajua enzi zetu mtu ukienda ukweni unafikia jikoni, unakaa huko unapika siku hiyo wakwe zako wanakula chakula ulichopika”, kisha akamuangalia Johari na wakaonana macho. Johari ikabidi ajibalaguze na kujiongelesha, “unajua mama mimi ni mpishi hodari tu sasa ngoja nika wakaangazie huko jikoni leo mle msosi niloupika mimi na mtaufurahia”, aliongea Johari na kujichekesha na kuinuka kwenda huko nyuma ya nyumba kulikokuwa na jiko, alijua lazima aondoke hapo ili kumuacha Malcom aongee na ndugu zake.
Hapo chini ya mwembe ndugu zake Malcom walimjiaa juu, wakimtamkia kuwa umri unaenda anahitaji mtoto, na kwamba kama mkewe hazai aachane nae aoe mwanamke mwengine. Malcom ambaye alijawa mambo ya kizungu, huku kavalia mawani yake, alikosa maneno ya kujibizana nao hao waswahili wa maneno akawekwa mtu kati wakimshambulia na kumuelimisha, aache ‘uboya’.
Wakati huo, huko jikoni alikokwenda kukaa Johari apike hapakuwa na amani, kwa maana Snura aligoma kupisha ‘mtu’ apike. Hivyo Johari akawa kakaa pembeni akimsaidia kupika kwa kumsogezea kopo la mkaa, mara amsogezee kopo la vitunguu na chumvi ama maji . Halafu mbaya zaidi muda wote Snura alikuwa anaongea na rafiki yake kana kwamba hawamuoni Johari, waliongea mambo yao ya kijijini ambayo Johari hakuweza kuchangia.
Ila kilichomuuma zaidi Johari ni pale alipokatiza kuku nje ya jiko hilo, kuku huyo mtetea alipita pamoja na vifaranga vyake. Basi Snura akaanza kumsifia huyo kuku, “Kuku si ndo huyu, kuku kuku kweli, kuku anatotoa vifaranga tunaona faida yake, mana raha ya kuku atotoe, sio kuku miaka nenda rudi kuku hatotoi, yani huyu kuku jinsi anavyototoa mfugaji anakupa raha ambayo hata binadamu mwengine hawakupi”, maneno hayo yalimuuma sana Johari pale alipoyaelewa maana yake, na alipoelewa kuwa kwa Snura, yule kuku ‘mdudu’ alikuwa na thamani kwa kutotoa kwake kuliko yeye Johari.
Ilimuuma hivi kwamba alilia njia nzima kwenye gari wakati yeye na Malcom wanarejea Dar es Salaam. Na Malcom alielewa kilichomliza mkewe, na safari hii alishindwa hata kumfariji, kwa maana hakuwa na pa kuanzia ndugu zake walifanya mambo ya kiroho mbaya bila kuficha safari hiyo.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment