Simulizi : Kivuli (The Catching Shadow)
Sehemu Ya Tano (5)
Basi bwana katika tabia ya Rashad kumfuatilia sana Johari, alijikuta akimfuatilia nyendo zake za kila siku ikiwamo kila alipokuwa akiwapeleka watoto zake shule. Lengo lilikuwa ni kujibana kwa pembeni na lango la kuingia shule na kisha kukaa hapo hadi Johari alipofikisha watoto zake shule, lengo lilikuwa ni kumpiga picha tu. Na baada ya kumpiga picha Johari, Rashad basi angefuraaahi na roho yake na kuangaliaangalia hiyo picha. Na Johari hakujua kuwa Rashad alikuwa akimfuatilia hadi kufikia hatua hiyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sasa bwana Rashad akaanza kufikiria sana kuwa kitu pekee kimfanyacho Johari akatae kuwa nae ni Malcom ambaye Johari alikuwa kaolewa nae na kuwa na watoto nae watatu. Rashad aliwaza kuwa kama ataweza kujenga mazoea na kupendana na watoto wa Johari basi angekuwa na nafasi kubwa ya kupendwa na Johari zaidi, na pengine kupitia ukaribu wake na watoto, Johari angeweza kuona urahisi wa kuachana na Malcom. Hayo mawazo yalikuwa ni finyu sana ila ndio hivyo Rashad alivyoamini.
Hivyo mchana mmoja wakati watoto wa Johari walipokuwa wanatoka shule wakisubiri dereva kuwafuata, Rashad aliwaendea na kuwasalimia na kujaribu kuongea nao. Watoto walikuwa wote watatu, Muujiza, Flora na Florian. Walikuwa wadogo, wazuuri waliochangamka na ajabu walikuwa huru na bila wasiwasi kuongea na Rashad ilihali hawakumfahamu. Rashad alifurahia sana kuongea na watoto wa Johari.
Ila sasa, kuna kitu ambacho kilianza ‘kumgonga’ akilini mwake. Katika hali isiyo ya kawaida, kupitia sauti za wale watoto, Rashad alijikuta anahisi kama anayesikia sauti za udogoni mwake. Kabisakabisa! Kichwani mwake alikuwa akisikia sauti ya kike ya mdogo ake wa kike, Sarha kila mara mtoto wa Johari, Flora alipoongea na alisikia sauti yake kwenye kila sauti iliyotoka mdomoni mwa Florian na Muujiza.
Ghafla kichwani mwake taswira za utotoni mwake zilimjia na aliona kabisa kuwa alikuwa sahihi kuwa sauti za wale watoto zilikuwa zinafanania kama za kwake yeye na Sarha walipokuwa wadogo. Na mara taswira za udogoni mwake zikamjia zaidi na kuona kabisa sura za watoto hao zilikuwa ‘kopiraiti’ na sura yake na Sarha kipindi wako wadogo.
Mara ghafla tawira na sauti hizo zilimtoka kichwani, na kusikia kauli za watoto wa Johari wakimuaga huku wakielekea kwenye gari iliyofika hapo kuwachukua na kuwarudisha nyumbani. Hapo akashtuka kuwa kumbe mawazo yake yalimuhama toka eneo hilo alilokuwako hivi kwamba hakugundua pale dereva wa kuwafuata watoto wa Johari alipofika.
Haikuwa hali ya kawaida kabisa. Wazo la ajabu sana lilimuingiza Rashad kichwani. Alijiaminisha kabisa watoto wa Johari walifanania kabisa na jinsi yeye na Sarha walivyokuwa kipindi wako wadogo.
Alipotoka eno lile la shule moja kwa moja alirejea nyumbani alikokuwa akiishi na huko akajikuta akitafuta picha ya zamani sana aliyopewa, picha iliyoonesha yeye na Sarha walipokuwa wadogo. Naam! bila ya kukosea, zile sura za watoto wa Johari zilirandana vyema na sura zao Rashad na mdogo wake kabisakabisa. “watoto wapo kama sisi tulivyokuwa wadogo”, alijiambia Rashad.
Sasa mawazoni mwake mawazo yakazidi kumzidia Rashad. Alijiuliza kwanini wale watoto wa Johari walifanana na familia yao. Alijiuliza kama wale watoto ni wake na sio wa Malcom kama ijulikanavyo. Alijuliza sana. Ila hakuwa na mtu wa kushea nae mawazo yake maana aliona kuwa Imran na mkewe Sarha wangepuuzia mawazo yake. Ila yaliyo kichwani mwake yalikuwa mazito hivi kwamba ilibidi amuelezee shemeji yake. Sasa Imran akatatizika zaidi. Alidhani Rashad kashaachana na habari za mwanamke aliyeitwa Johari, kumbe ndio kwanza alikuwa anakuja na habari mpya kuwa Johari ana watoto ambao yeye Rashad alihisi ni wa kwake.
“Kwa nini unafanya hivi shemeji yangu. Hivi unajua unachosema utasababisha kuleta mgogoro kwenye ndoa ya mdada wa watu”, aliongea Imran kumuomba Rashad aache habari hizo, ambazo hazikuyumkinika kwa akili ya kawaida.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Safari hii Rashad alimjia juu Imran wala hakumlazia damu, “Yani Imrani, nakuja kwako shemeji yangu, nakwambia kitu cha maana kama hichi wewe unanichukulia mimi nina matatizo ya akili”, alilalamika Rashad kwa hasira na kuanza kumvimbia shemeji yake. “Unanichukulia mimi ni mwehu, ilihali nina akili zangu timamu. Ninakwambia yule mwanamke ana watoto na wale watoto nimewaangalia vizuri na mimi naapia kwa mungu na mtume, wallahi wale wale watoto kwa jinsi walivyo tu ni wa kwangu, sio wa mume wa huyo mwanamke”, aliendelea kulumba Rashad tena kwa sauti kubwa. “wewe unaniletea habari za niongee vitu vyenye kuyumkinika akilini, inamaanisha unanichukulia mimi ni chizi mwehu. Na mimi nakwambia wewe na mkeo huyo Sarha, acheni mambo yenu ya madharau mimi niwaambiapo mambo naombeni muwe na heshima, naelewa niwaambiacho” aliendelea.
“Hivi nikiwauliza miaka zaidi ya kumi na kitu niliyoishi naranda mitaani mnieleze nillikumbana na nini mtaweza nieleza ninyi. Walau mwenyewe nakumbukakumbuka yaliyonisibu, sasa ndo nakwambia, yule mwanamke anaitwa Johari, nilitembea nae nilipokuwa chizi na nakwambia tena watoto alionao ni wa kwangu” alifoka Rashad, hivi kwamba mtu yeyote aliyekuwako nyumbani hapo angeweza kusikia kelele zake, zilizotoka hapo barazani walipokuwa wamesimama na kulumbana, mabishano yao yalisikika hadi ndani na kuwatoa nje Sarha na mama yake bi.Aisha.
Sarha na mama yake walitoka mbiombio na kuhoji ni nini kilikuwa kinajiri nje hapo. Ndipo Rashad akaanza kumwambia mama yake na dada yake kuwa ana watoto watatu aliozaa na yule mwanamke aliowaambia siku nyingi kuwa alikuwa na mahusiano nae kipindi yuko chizi.
Bi. Aisha kama walivyo Imrani na Sarha hakuamini na kutaka Rashad aache maneno yake. Rashad akawa akitumia nguvu kubwa akitaka wamuamini hadi akawa sasa analia, hatimaye mama yake, bi Aisha nae imani ikaanza kumuingia na kumwambia kuwa yeye kama mama yake anaelewa mwanae akiongea ni kwa vipi huuelezea ukweli na kwamba alikuwa keshamuamini, “mwanangu, ukielezacho huenda ikawa ngumu kwa mtu mwengine kuelewa ila mimi mama yako, sina shaka kabisa, nimekuamini kila unachokisema”, kwa kauli hiyo hata Imrani na Sarha ikabidi waamini kabisa kuwa huenda ni kweli Rashad alikuwa na mahusiano na huyo Johari kipindi yuko chizi na wakaamini kuwa huenda kweli watoto wa huyo mwanamke ni wa Rashad kweli.
Walau sasa moyo wake Rashad uliweza kutulia. Hatimaye walau mama yake, shemeji yake na Sarha walikuwa wakiamini alichokuwa akiwaambia.
Basi sasa Rashad akaamua kuonana na Johari. Na kama kawaida akamsubiria nje ya jengo la ofisi yake na kusimamisha gari lake pale Johari alipokuwa akitaka kuondoka, basi katika hali isio kawaida Johari alisimamisha gari na Rashad akapanda na kama kawaida Johari aliendesha gari hilo hadi Ocean road kisha akapaki gari pembeni na kumgeukia Rashad.
Alipomtazama aliona kuwa Rashad alikuwa na machozi uso wake wote. Mara akamuona Rashad akiingiza mkono mfukoni na kutoa picha mbili za ‘hardcopy’. Kisha akachukua moja na kumuoneshea Johari. Picha yenyewe ilikuwa ni ya familia yao, yani, Rashad, Sarha, Imrani na mama yao bi. Aisha.
Johari hakuelewa hao watu wa pichani na wala hakuelewa kilichomliza Rashad na akawa akiona kama analetewa uchuro garini mwake.
Ndio mara Rashad akafuta machozi yake na kuanza kuongea. “Unaona hawa pichani, hawa ndio familia yangu, mama yangu, shemeji na Sarha dada yangu”, aliongea Rashad na kumfanya Johari ashangae na kupayuka, “enhe, sasa ndio vipi yani?”, aliuliza Johari.
“Kwa mara ya kwanza, kwa mara ya kwanza, wameamini nilichowaambia kuwa niliwahi kuwa na mahusino na wewe”, aliongea Rashad. Maneno hayo yalikuwa kama bomu kwa Johari. Aliwaza kwa haraka na kujiuliza kama Rashad kaanza kushirikisha familia yake kwenye ishu ilokuwa inaendelea nini kilikuwa kinafuata.
“kwanini umewambia ndugu zako kuhusu sisi, hivi unajua unachofanya ni kuharibu maisha yangu” aliongea Johari kwa hasira na Rashad akajitetea kuwa ilikuwa lazima awaambie familia yake inayompenda.
“Johari najua humpendi mume wako kama unavyonipenda mimi, ndio mana ukadiriki kutembea na mimi hata nilipokuwa chizi na mimi nakwambia nakupenda pia, tena nakupenda sana, mimi niko radhi kukuoa hata ukisema unamuacha mumeo leo hii mimi nakuoa”, aliongea Rashad.
Kauli hiyo ilimtia hasira Johari na kuanza kupayuka jinsi alivyompenda mume wake na kuwa hawezi kuwa na Rashad na kujinadi kuwa tayari ana familia na mumewe, tena familia ya watoto watatu.
Kauli hizo za Johari sasa zilimuumiza Rashad na hivyo akjikuta akichukua picha ya pili na kumuoneshea Johari, “Ona Johari, huyo pichani ni mimi na mdogo wangu wa kike Johari.”, Johari aliangalia hiyo picha kwa jicho baya sana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ona Johari jinsi nilivyofanania nilipokuwa mdogo. Ona jinsi nilivyo fanana na watoto wetu, Muujiza, Flora na Florian”, aliongea Rashad sasa akimuangalia Johari machoni na kumshtua Johari kwelikweli na kufanya atoe macho. Hakuamini kama alikuwa kweli kamsikia Rashad akiwaita akina Flora kuwa ni watoto wake, alishtuka sana.
“Acha. Kushtuka Johari na kuogopa na usithubutu kujitia hujui hili, ukweli unaujua kuwa hawa ni watoto wangu.” Aliongea Rashad.
Johari alipanda hasira na kupayuka ila alishindwa kukana alichozungumza Rashad kuwa watoto ni wa Rashad na sio wa Malcom, akabaki akilia kwenye magari.
“Johari nakupenda sana. Mimi natamani umuache mume wako hata kesho, ili nikuoe. Hebu fikiri tutavyoishi kwa furaha, wewe mimi na wanetu watatu pamoja na mama yangu na Sarha, familia iliyokamilika kabisa.”, alimaliza kuongea Rashad.
Kwa akili za Rashad aliona kuwa kuna namna ya kumshawishi Johari kuachana na Malcom ili aolewe na yeye, ambacho Rashad hakutaka kukubali wakati huo ilikuwa ni ukweli uliowazi kwamba Johari alimpenda mume wake, tena alimpenda sana na aliipenda ndoa yake, na hakutaka Rashad awepo kabisa kwenye maisha yake.
Basi, jioni ya siku hiyo Johari alijifungia chumbani mwake na kulia sana. Alilia kwa kuogopa na kujiuliza nini kilikuwa kinaenda kutokea kwenye maisha yake. Aliogopa, kwa maana aliona jinsi Rashad alivyokuwa ‘serious’ kuwa anataka yeye Johari aachane na Malcom, tena alitaka waoane wao na zaidi ya yote alijua ukweli kuwa watoto watatu ambao Johari aliwalea na Malcom walikuwa ni wa kwake. Johari alihofia sana, na kujiuliza itakuwaje Malcom akijua ukweli.
Aliwaza sana Johari hadi usingizi ukamjia na kulala. Baada ya kulala, ndoto ya ajabu ilimjia. Katika namna isiyo ya kawaida Johari aliota anakimbia na kurandaranda mwitumi, huku nywele zake zikiwa zimetimka na mwili wake kujaa jasho, vumbi na kuchoka. Mara ghafla mwanamume mrefu sana, aliyevalia mavazi meupe mwenye mwili mkubwa alitokea mbele yake na kumshtua sana hivi kwamba akajikuta akipoteza nguvu na kushindwa kukimbia tena na akajikuta akisimama na kumuangalia yule mtu aliyemtokea. Mtu mwenyewe alikuwa amevalia mavazi ya kung’aa sana hata ya kamuumiza Johari machoni.
Mara yule mtu akaanza kuongea, “Kivuli humfuata mtu na huonekana na mtu pale awapo kwenye mwanga lakini nacho kila mara hupotea mwanga upunguapo na kuondoka, lakini mwerevu huelewa kuwa kivuli kitarudi tena na kuonekana kumfuatilia mtu kila mwanga utapokolea tena, basi vivyo hivyo ndivyo ilivyo mikosi itokanayo na maovu ya mtu, huonekana kisha hupotea na kufanya mtu aamini kuwa ayamepita ila baadae hurudi tena palepale kumtesa mtu”, alimaliza kuongea yule mtu.
Japokuwa Johari alikuwa akimuogopa huyo mtu kwenye ndoto alijikuta akipandwa na hasira na kumhoji, “unamaanisha nini, wewe jitu la kutisha, mbona unanizibia njia yangu niliyokuwa napita humu mwituni”.
Basi yule mtu akamjibu kuwa yeye hakuwa jitu la kutisha bali yeye alikuwa ni malaika wa mungu na kwamba alikuja tu kumkumbusha Johari kuwa alipewa mtihani, ili Johari atafute nusura ya mwenyezi mungu ila, ndio kwanza akaenda kwa waganga na kufanya ushirikina.
“Kwa maana hiyo, ule mtihani wa utasa ulioupata kutokana na maovu yako ya huko awali, ulipaswa ukufundishe kumtumainia tena mungu wako na kuzidisha maombi na dua kwake, ili akupe nusura na kukujaza imani yako, ila wewe umeenda kwa waganga na kumkufuru muumba wako, ama kwa hakika wewe ni miongoni mwa waja wale waliojichagulia wenyewe njia ya upotevu” na huyo mtu akaendelea kumwambia Johari kuwa, kukubuhu kwake katika kufanyia watu maovu kumefika tamati na kwamba nguvu za miujiza za wao malaika ndizo zilikuwa zinaingia kwenye vita dhidi yake Johari ili kuzuia uovu wake ulioota mapembe na kukomaa.
Basi hiyo ndiyo ilikuwa ndoto ya Johari.
...................................
Kwa upande wa Rashad ndugu zake walikuwa washamuamini alichowaambia. Ila sasa waliona ni mtihani wa aina yake uliokuwa ukimkabiri huyo mwanamke aliyeitwa Johari kwa maana walifahamu kuwa Johari alikuwa keshaolewa, walifikiria sana na kujiuliza, itakuwaje sasa mume wa huyo Johari atakapo jua ukweli juu ya mkewe.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ila yote kwa yote Rashad alifurahia sana jinsi walivyomuamini na kichwani mwake alijipa imani mia kwa mia kuwa ,hatimaye Johari atambwaga Malcom na kisha ataolewa nae yeye.
Kumbe kipindi Rashad akiwaza hayo, Johari nae alikuwa akiwaza yake. Si ya kutubu uovu aliowahi kufanya huko zamani ambao ulikuwa chanzo cha majanga yake yote aliyokuwa akipitia, wala si ya kukubalina na kila alilotamani Rashad, bali aliwaza namna ya kumpoteza Rashad. Johari aliwaza namna ambayo Rashad anaweza kufutika kwenye ramani. Na basi akapanga njama za kuagiza watekaji nyara wamteke Rashad, kisha wamtese na kumuulia mbali. Naam! hilo lilikuwa suala rahisi sana. Johari alikuwa na pesa za kutosha kumpoteza mtu.
Basi alifanikiwa kukodi watekaji nyara nao walimteka Rashad na kumpeleka mbali kwenye eneo la magofu ambako kulikuwa ni nje ya mji, karibu na mwituni na kusikokuwa na watu kabisa. Huko walimtesa sana kwa lengo la kumuua.
Mateso aliyopewa yalimfanya Rashad apoteze kabisa tumaini la kuishi na kujiona kuwa anakufa muda wowote. Hakukuwa na namna ambayo aliweza kujing’amua toka mikononi mwa watesi wake. Alijikuta akiishiwa nguvu na kuanguka kwa kuzirai huku watesi wake wakiendelea kumpa kichapo.
Hadi giza linaingia, huko alikokuwa akiishi Rashad, bwana Imran na mkewe Sarha na bi. Aisha walikuwa na wasiwasi mwingi, kwa maana toka mchana wake hawakumuona Rashad akirejea na wala hakupatikana kwenye simu walijawa na hofu kweli na wakashindwa hata pa kuanzia wakabaki wamejikusanya kwenye sebule ya nyumba yao huku wakisubiri labda angeingia hapo ndani muda si muda.
................................
Basi, Rashad alipoamka aliwaza kwa haraka sana kuwa lazima atafute mbinu ya kuwarubuni watesi wake. Nao watekaji nyara waligundua kuwa mateka wao kazinduka hivyo wakamuendea kwa ajili ya kummaliza.
Na Rashad alijua kuwa sasa walikuwa wanataka kummaliza kabisa hivyo aliamua kufanya maamuzi ya mwisho kabisa ya kutetea uhai wake. Na kujaribu kuwashawishi watesi wake kuwa yeye anatoka kwenye familia ambayo dada yake na shemeji yake wana uwezo sana. Hivi kwamba wanaweza kuwa na pesa zozote za kuwalipa, na hivyo Rashad akaomba wamueleze sababu za kumtekea, ndipo wakamwambia wametumwa na mwanamke anayeitwa Johari.
Rashad ilimuuma sana, hakutarajia hata mara moja kuwa Johari alikuwa na uwezo wa kumtumia yeye wateka nyara, tena mbaya zaidi watekaji waliotaka kumuua kabisa. Ilimuuma kwa maana yeye alidhani alikuwa na uwezo wa kumfanya Johari aachane na Malcom ili aolewe na yeye. Ila kumbe, Johari alikuwa hataki hilo kwa kiasi cha kujaribu kuthubutu kumtumia wauaji, ilimuuma sana.
Katika harakati za kujitetea Rashad akawaambia kuwa dada yake anaweza kutoa dau kubwa kuliko la Johari, hivyo akawapa dili kuwa wamuachie na dada yake atawalipa pesa nyingi zaidi.
Mara wale watesi wakacheka sana na kumuongezea kipigo na kumwambia kuwa hawana shida na nyongeza yeyote ya pesa, kwanza alikwisha waona sura hivyo wao waliona ilikuwa upumbavu wa hali ya juu kuamua kukubali dili alilokuwa akiwaofa kwa maana wakikubali na kumuachia lazima angetumia vyombo vya dola kuwapata na isitoshe walikuwa wameridhika na pesa za Johari.
Basi kwa kumuoneshea Rashad kuwa hawarubuniki, walimpigia simu Johari na kumwambia dili ambalo Rashad alitaka kuwapa pesa nyingi zaidi. Basi kupitia kwenye simu Johari alimrushia matusi Rashad na kujinadi kuwa yeye ndiye mwanamke mwenye pesa kuliko dada wa Rashad, tena ndiye aliyemiliki pumzi ya Rashad wakati huo, tena Johari akatoa kauli za kufuru, “hata mungu wako na malaika zake hawawezi kuokoa pumzi yako kwa sasa” alijinadi Johari, “yani ni kama vile iwe kheri unisujudie mimi kwa maana ndiye mmiliki wa pumzi yako” aliendelea kujinadi kishetwani shetwani kabisa. Kisha akakata simu.
Basi wale watesi waliendelea kumpiga Rashad hadi akapoteza fahamu tena na kumpa mapigo ya mwisho hadi ikafikia tamati wao wenyewe wakaona kuwa washaua. Rashad alikuwa kashakwisha.
Katika namna isiyolezeka wakati Rashad anapigwa na wale watesi mama yak, bi Aisha alikuwa akihisi maumivu mwilini na uchungu mwingi, ijapokuwa hakujua mwanae alikuwa wapi ama alikuwa na akina nani na bila kujua kuwa alikuwa katekwa alihisi kusikia maumivu na kutoa machozi, hiyo ilikuwa ni hisia ya kipekee hasa ambayo inasemekana huwa inawapata wa mama ama ndugu wenye mapenzi ya dhati sana, hivi kwamba bila kujua huhisi tabu zote apitiazo mtu wampendae kila awapo tabuni, hata kama hawajui hasa aliko.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati huohuo Johari akiwa kwwake alikuwa kajawa na furaha sana na mumewe. Wakati huo Johari alijiona kawini. Alijua Kuwa usiku huo Rashad alikuwa anakufa na kumuacha aishi raha mustarehe yeye na Malcom wake na watoto wao watatu. Johari alijawa na furaha usiku huo hivi kwamba watoto wake walipolala aliwasha muziki wa taratibu sebuleni kwake na kisha kufungulia shampeini na kumimina kwenye glasi na kisha kunywa pamoja na mume wake huku wakicheza ‘love songs’ kwa kukumbatiana na kwa mapenzi makubwa, Malcom alishangaa jinsi mke wake alivyokuwa kachangamka kupita maelezo. Na wakati huo Johari alifahamu furaha yake ilitokana na kujua ukweli kuwa usiku huo kauwawa Rashad, mtu ambaye alikuwa ndie kauzibe pekee kilichobaki katika kumfanya Johari aishi kwa kujiamini kwa asilimia mia na familia yake.
Basi, kule ambako, Rashad alikuwako wale watesi wake walikuwa wamempiga vya kutosha hadi wakaona kuwa wamemuua kisha wakaamua kuondoka.
Basi Rashad akiwa anaamini kuwa anakufa na kukata roho, aliona kuwa wale wateka nyara wameondoka na kumuacha kwenye baridi la usiku hapo kwenye magofu ili afe, na aliamini anakufa kweli. Na mara akazima, fahamu akapoteza na kuzirai kama mfu hata pumzi yake ilikuwa kama imempotea, ilikuwa ni mtu ambaye tayari kafa ila kumbe alikuwa bado yani Rashad alikuwa katika hali ambayo ilikuwa ngumu kuieleza, nusu mfu nusu mtu hai, ila aliyekuwa akielekea kufa kuliko kupona.
Mara njozi ikamjia, njozi kuwa katokewa na malaika akimwambia ajikaze, ajikaze asikate tamaa mwisho wake haujafika. Kwamba yeye yupo ili kumuangusha mwanamke aliyemuovu ambaye amechagua njia ya upotevu na kuacha njia iliyokuwa sahihi njia ya watu wema.
Mara malaika alimwambia Rashad awahi awahi na awahi kurejea ulimwenguni kabla milango iliyotenganisha uhai na ufu haijafungwa. Basi Rashad humohumo ndotoni akajikuta akianza kutimua mbio, mbio, mbio akikimbilia kwenye lango kuu lililotenganisha uhai na kifo ili aweze kutoka nje na kurudi kwenye uhai kabla lango hilo halijafungwa na yeye kujikuta kabakia kuzimu.
Basia ndani ya yale magofu ambayo Rashad aliachwa, hakuamka tena mpaka asubuhi jua lilipochomoza na kumuangaza humo ndani ya magofu na kumunguza kidogo ndio akaamka.
Japokuwa alikuwa na damu na maumivu mengi mwilini alijiona ana nguvu za kutosha hivi kwamba aliweza kujiinua. Hakika aliona kuwa ilikuwa ni muujiza wa mungu pekee uliomfanya awe bado mzima hadi wakati huo.
..............................
Asubuhi ya siku hiyo, Imrani na mkewe waliripoti polisi juu ya kupotea kwa Rashad. Na walikuwa wapo pamoja na mama yao bi. Aisha, ambaye alikuwa anashindwa kabisa kutulia, huku akikumbushia kuwa mwanae aliwahi kupotea kwa zaidi ya miaka kumi na kumlilia mungu aepushe mwanawe asipotee tena kama jinsi alivyopotea mwanzo.
Basi wakiwa wamekaa sebuleni mara walishaangaa mlango wa sebule hiyo ukifunguliwa na wakashangaa kumuona Rashad akiingia huku akiwa hoi, mwili umetapakaa damu na kujaa vumbi.
Wote walishtuka kumuona katika hali kama hiyo na kuogopa. Walijkuta wote wakiangua machozi ya mchanganyiko wa furaha ya kumuona karejea na pia majonzi kwa ile hali aliyokuwa nayo.
Basi baada ya kutulia Rashad alisimulia familia yake kuwa kilichotokea kilikuwa ni mipango ya Johari na kwamba alikuwa kanusurika kifo kwa mipango ya mungu tu. Ndugu zake walimuhurumia sana. Na kumuahidi kuwa hakika Johari lazima aozee jela kwa aliyoyafanya.
.........................
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Basi bwana, kwa upande wa Johari siku hiyo ilikuwa nzuri sana, tena ilikuwa jumamosi yani siku ya mapumziko. Hivyo mchana wa siku hiyo alibeba mume wake na watoto zao watatu na kuwatoa piknik, huko ufukweni mwa bahari kupunga upepo na kuota jua na kufurahia siku nzima. Ambacho Johari hakukijua hadi wakati huo ilikuwa ni kwamba Rashad alikuwa hajafariki kama jinsi wale watekaji nyara walivyomtaarifu kuwa walikuwa washamuaa. Tena hadi wakati huo anafurahia pikinik Rashad na ndugu zake walikuwa tayari washamshtaki polisi na wakati huo askari walikuwa wakimfuatilia na kumtia chini ya ulinzi.
Naam akiwa mwenye furaha na familia yake polisi walimjia Johari na kumuweka chini ya ulinzi na kumpeleka selo, huku nyuma akiacha mume wake, Malcom na watoto wao watatu.
.............................
Basi bwana, kesi ya Johari kutaka kumuua Malcom ilikuwa ni ya aina yake. Malcom hakuelewa kitu, yeye aliona kama mke wake anaonewa, kwanza hakuwa akimjua Rashad na wala hakufahamu hata chembe ya sababu ya kumfanya mkewe kudhamiria kumua Rashad. Hivyo pale alipoambiwa kuwa mkewe alikuwa akitaka kumuua Rashad kwa lengo la kuficha ukweli juu ya uhalisia wa baba wa watoto wa wao usijuliakane, Malcom alichanganyikiwa. Siku zote alijiona yeye ndiye baba wa watoto wa mkewe, na hakutaka kuamini madai kuwa Rashad ndiye alikuwa baba halisi wa watoto.
Pia kwa kuwa Johari alikuwa ni mwanamke mwenye cheo kikubwa na alijulikana na wengi, stori yake ilifikia waandishi wa udaku na hadi wale watangazaji wa redio. Ilikuwa ni hekaheka ambayo kila mtu mji mzima alikuwa akiifuatilia.
Johari alishindwa kabisa kujitetea na akakamatisha wale watekaji nyara aliowatuma kumteka Rashad, ambao nao walitumika kuwa ushahidi wa uovu wa Johari dhidi ya Rashad.
Basi watoto walipimwa DNA na kugundulika kuwa ni kweli walikuwa ni watoto wa Rashad na si wa Malcom. Naye Johari alihukumiwa kifungo cha miaka kadhaa kwa kosa la kujaribu kufanya mauaji ya kudhamiria, pia wale wateka nyara walihukumiwa.
Basi mwishowe Rashad na familia yake walipata haki yao ya kujualikana nani hasa ni baba wa watoto wa Johari na Johari akaishia jela kutokana na uovu wake.
......................
Basi mwaka mmoja baadae Johari akiwa jela alipata ugeni toka kwa Malcom. Johari alikuwa na michozi mashavuni kwa uchungu siku hiyo. Ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kwa Malcom kwenda kumtembelea toka afungwe. Malcom alikuwa hana hamu hata ya kumuona mkewe toka ajue ukweli kuwa watoto walikuwa ni wa Rashad.
Malcom mwenyewe sasa alikuwa kachoka na aliyeonekana kuwa na maumivu mengi ya moyo. Siku ambayo alikwenda kumuona Johari kwa mara ya kwanza alikuwa kaenda na fomu za kimahakama za kutiliana saini ya talaka na kumwambia Johari asaini kwa maana alikuwa anamtaliki ili aoe mke mwengine.
Baada ya Johari kusaini talaka hiyo Malcom huku akilia kwa kwikwi kabisa, Malcom aliingiza mkono mfukoni mwake na kutoa picha ya mwanamke aliyevutia sana na kumuonesha Johari.
Johari alipoangalia picha hiyo alimuona kuwa yule mwanamke alikuwa ni mjamzito, moja kwa moja akaelewa kuwa Malcom alikuwa akitaka kumuoa mwanamke yule wa pichani ambaye alikuwa akitarajia kujifungua na hivyo kumfanya Malcom kuwa baba wa mtoto wake halali kwa mara ya kwanza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kisha Malcom akaanza kumwambia Johari jinsi gani alihisi kupotezewa muda mwingi wa maisha yake, “miaka hii yote uliyoniaminisha nina familia yangu, mke na watoto, ingelikuwa najua kuwa wale watoto ni wa yule chizi wako hakika ningekuwa nimeachana nawe muda mrefu sana na kuwa na mke mwengine na kuwa na familia ya uhalisia na si ya kilaghai kama uliyonitengenezea wewe”, hatimaye aliongea Malcom maneno ambayo aliyahifadhi moyoni mwake kwa muda mrefu akisubiria kumwambia Johari. “Ila namshukuru mungu kuwa walau kanifungua macho kabla sijafa na kujua ukweli nikiwa bado ninawexa kuanza familia nyengine”.
Kisha Malcom akamwambia Johari kuwa alikuwa anafunga ndoa wikendi iliyokuwa inakuja na tena akaamua kumtajia jina la mkewe mtarajiwa, “Lulu, mke wangu mpya jina lake ni Lulu” kisha akamuaga, “bye Johari, I loved but your evil heart loved you most from the behind bars” halafu akaondoka, na kumuacha Johari akilia kwelikweli kwa kilio cha kwikwi, huku akimtzama jinsi alivyokuwa akiondoka kwenye hicho chumba cha kuongea na wafungwa.
MWISHO....................
0 comments:
Post a Comment