Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

HATIA - 3

 



    -


    Simulizi : Hatia

    Sehemu Ya Tatu (3)







    Matha bila kujua kuwa anafuatiliwa alielekea barabarani akaangaza hapa na pale akanyanyua mkono wake wa kuume akaita taksi, haraka haraka dereva aliyekuwa amemuona Matha aliifikisha gari yake Matha akaingia ndani.

    John akasubiri ile teksi ilivyoanza kuondoka naye akaingia katika teksi aliyokuwa amekodi.

    “Fuata gari hiyo!!” alitoa maelekezo hayo John, dereva akafuata maelekezo. Gari mbili zikawa zinafuatana bila gari ya mbele kuwa na habari juu ya hilo, John alikuwa amevaa miwani nyekundu kuziba macho yake yaliyokuwa mekundu sana, hakutaka kumtisha dereva.



    *****



    Adrian alikuwa amekaa nje ya duka kubwa la kuuza nguo maeneo ya Makoroboi, umeme ulikuwa umekatika na biashara haikuwa nzuri sana siku hiyo. Adrian alikuwa anaperuzi katika gazeti la michezo alilokuwa amenunua muda mrefu uliopita.

    Ubovu wa biashara wa siku hiyo haukumshtua sana Adrian kwani alikuwa na uhakika kuwa maduka mengine matano yaliyokuwa yamezagaa jijini Mwanza yangekuwa na biashara nzuri siku hiyo.

    Mzee Mhina Mboje alikuwa amemuamini sana kijana wake huyu wa pili kuzaliwa, japo aliwahi kuikataa shule alipokuwa kidato cha tatu lakini akili yake katika kutafuta maisha ilikuwa inavutia wengi sana na kuwapa wivu. Adrian sasa alikuwa anasimamia maduka yote ya baba yake huku lile la Makoroboi likiwa mali yake binafsi. Adrian aliwahi sana kujipanga kimaisha kwani tayari alikuwa ameondoka nyumbani miaka mingi iliyopita na kuamua kufanya maisha ya kupanga.

    Mwanzoni alikuwa anakaa na mdogo wake wa kiume lakini baada ya kuingia katika mahusiano ya kimapenzi aliamua kumrudisha mdogo wake nyumbani kwa wazazi ili aupate uhuru zaidi wa kujivinjari na binti huyu. Kwa kuwa ulikuwa upendo wake wa kwanza alikuwa akimsikiliza sana binti huyo ambaye alikuwa bado ni bikra, mapenzi yao ya kitoto toto waliyajua wao wenyewe. Adrian hakuruhusiwa kufanya lolote katika mwili wa huyu binti zaidi ya kumbusu shavuni tu na kuishia kucheza cheza.

    Adrian hakuruhusiwa pia kutangaza kwa mtu yeyote juu ya uhusiano huu eti kisa tu baba yake binti alikuwa mkali sana. Upendo wa dhati ukawa umejijenga.

    Ile hali ya Adrian kuukana uhusiano wake mbele ya watu ili kumfurahisha mpenzi wake huyo ilikuja kumgharimu sana. Akatokea mwanaume aliyekubuhu akamlaghai huyu binti ambaye ni Matha, alikuwa ni John Mapulu aliyemnyang’anya Adrian Mhina tonge mdomoni. Matha akahamishia upendo wake kwa John ambaye alikuwa ameitoa bikra yake. Adrian akabaki kama zezeta asijue la kufanya lakini hatimaye akazoea baada ya wawili hawa kuhamia sehemu nyingine kabisa mbali na yeye.

    Kumbukumbu juu ya Matha zikasahaulika pia kutokana na mchumba wake ambaye walikuwa wanatarajia kuoana baada ya mwezi mmoja kwani walikuwa na mwaka mzima tangu waishi maisha ya uchumba huyu alikuwa ni Monica Lewis, dada zake walikuwa wakimpenda sana na hii ndio ilikuwa chachu ya kumshawishi Adrian kuoa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mara kwa mara Monica alikuwa analala nyumbani kwa Adrian, na hata kabla ya kutambulishana kwa wazazi tayari Monica alikuwa ameshiriki katika tendo la ndoa na Adrian, ujanja aliofanyiwa na Matha miaka iliyopita hakutaka tena kumwamini mwanamke.

    Mwezi mmoja kabla ya ndoa tayari Monica alikuwa mjamzito, jambo hilo walilitambua wao peke yao, hawakutaka wazazi watambue hali hiyo ya wao kupata mtoto nje ya ndoa.

    “Mambo vipi kaka” alisalimiwa Adrian akiwa bado ameinamia gazeti lake.

    “Poa karibu!!” alijibu huku akiunyanyua uso wake. Hakutaka sana kumuangalia mtu aliyekuwa mbele yake kwa sababu alikuwa ameficha uso wake.

    “Unanikaribisha unanijua kwani??” aliuliza yule binti ndani ya baibui, Adrian akacheka.

    “Adrian!!! Za siku!!”

    “Mh!! Kwani we nani”

    “Matha!!! Jamani” alijitambulisha. Kumbukumbu ya sauti ile ya kupendeza ikarejea katika kichwa cha Adrian. Kabla hajajua la kufanya, Matha alimsogelea na kumkumbatia. Adrian hakuamini alichokuwa anakiona mbele yake, Matha akasikika kama analia, kilio hicho kikafuta hasira zote alizokuwanazo Adrian, joto lililopenya katika baibui na kumuingia Adrian likaibua hisia za upendo.

    Walikumbatiana kwa dakika nzima. Kisha baada ya kuachiana Matha alijifunua kidogo, Adrian akaona vishimo katika mashavu ya Matha.

    Upendo maradufu ukamvaa!!!

    Matha akawa katika majuto ya hatia iliyokuwa inamkabili kwa yote aliyomtendea Adrian miaka iliyopita. Kwa mbaali akausikia mguso wa kimapenzi kutoka kwa Adrian. Akaanza kupatwa na hofu huenda Adrian bado ana hasira, lakini haikuwa hivyo!!!!

    Walizungumza kwa dakika kadhaa kisha Matha akamwachia namba yake kijana huyu mwenyeji wa Tanga aliyekulia jijini Mwanza.

    Yote hayo yaliyokuwa yanatokea yalishuhudiwa na jicho kali lililokuwa nyuma ya miwani, jicho la John Mapulu. Alitamani kumfyatua palepale yule mwanaume lakini alijikaza, akauzuia wivu usipitilize. Akawa amemtambua mwizi wake akapanda teksi na kuondoka, wakati huo na wawili hawa walikuwa wameagana.

    Laiti kama angesubiri kidogo tu angepata kufahamu kuwa mpenzi wake huyo anakwenda kukutana na Minja anayeaminika kuwa alikufa usiku uliopita.

    Lakini John Mapulu hakuwa na subira.



    John alirejea nyumbani kwake, hakutaka tena kwenda kwenye tukio la ujambazi akili yake ilikuwa imechanganyikiwa kabisa. Uchungu alioupata Adrian miaka mitatu iliyopita sasa ulikuwa umemgeukia yeye.

    Wakati anamnyakua Matha mikononi mwa Adrian alijiona kidume sasa na yeye alikuwa katika majaribu ya namna ya kipekee.

    “Kama mwanzoni nilimchukulia Matha wake sasa wakati huu naitwaa roho yake, mshamba kama yule hawezi kumchukua Matha kirahisi hivyo, nitamuua!!!” aliapa John kwa sauti ya juu.

    Alikuwa kama amechanganyikiwa!!!

    Wivu ukawa unamtesa!!!



    ******



    “Tukutane hapo nje ya chuo cha biashara (CBE)”

    “Sawa dada” alijibu Minja. Matha akapiga hatua kadhaa akawa amefika hapo chuoni. Minja alikuwa ameanza kukasirika baada ya kuwa anapiga simu ya Matha halafu haipokelewi.

    “Ingia ndani!!!” Matha alimuamrisha Minja bila kumuangalia usoni. Hiyo ilikuwa ni mbinu ya kuepusha kama yupo mtu anawafuatilia asiweze kugundua lolote. Laiti kama angejua aliyekuwa anawafatilia tayari amepata jibu na kuondoka hata asingeweza kujihangaisha hivyo.

    Minja aliingia akaa katika meza moja, baada ya dakika mbili Matha naye akafika.

    “Samahani kaka naweza kukaa hapa?” alizuga, Minja akashangaa. Matha akajiongeza akakaa.

    “Chooni wapi kaka samahani” aliuliza kwa sauti ya juu ili majirani waweze kumsikia.

    Minja akashangaa tena.

    Matha akamuuliza mtu mwingine akaelekezwa akaenda uani.

    Aliporejea alikaa alipokuwa Minja. Aliamini kuwa tayari amewapoteza baadhi ya watu.

    “Ehee!! Kuna tatizo gani?”

    “Yaani sijui nisemeje”

    “Umeniita kufanya nini kama hujui la kusema” aliunguruma Matha, Minja akaogopa.

    “Usiku kuna mtu ameuwawa ndani kwangu” alijitutumua na kumueleza kila kitu kilivyokuwa. Matha akawa ameelewa kuwa dhumuni lilikuwa ni kuuwawa kwa Minja.

    “Laiti kama John angempata jana basi najua mambo yangekuwa mabaya……” aliwaza Matha huku walau hofu ya John kugundua tatizo hilo ikianza kupungua, lakini uwepo wa Minja jijini Mwanza ungekuwa bado ni tatizo. Matha hakuona tena haja ya kumuua Minja kwani alimuona kama hana hatia yoyote ile tena.

    “Unatakiwa uondoke haraka hapa Mwanza”

    “Sasa naenda wapi dadangu nisaidie”

    “Hujui pa kwenda, basi utaenda jela” alisema Matha, Minja akatetemeka kusikia hivyo.

    “Chukua hii, kesho uondoke!!!” Matha alimkabidhi Minja shilingi laki moja.

    Laiti kama angejua kuwa Minja kuna jambo zito analifahamu wala asingekubali aondoke hai jijini Mwanza.

    Asubuhi iliyofuata Minja akaondoka kuelekea Singida, alitegemea kufikia kwa rafiki yake ambaye waliwahi kufanya shughuli za udalali pamoja jijini Dar es salaam. Amani ikarejea moyoni mwake, akajihisi kuwa hana hatia tena. Akawa amesahau kuwa hatia humfuata muhusika popote atakapoenda.

    Hatia ilipanda naye katika basi kuelekea Singida!!!!

    Hatia haimuachi muhusika mpaka mwisho wa uhai wake, hatia huingia na mtu wake kaburini!!!



    ******



    Adrian aliwahi sana kufunga duka siku hiyo, aliikatisha ahadi aliyokuwa nayo ya kutoka jioni ya siku hiyo na mpenzi wake (Monica). Kitendo cha kumuona Matha kwa mara nyingine tena kilikuwa kimeamsha ari fulani katika nafsi yake.

    Alifika nyumbani kwake akaoga na kisha akaingia kitandani. Aliyawaza maisha yake na Matha miaka ya nyuma katika nyumba hiyohiyo hadi siku alipomsaliti na kuondoka na John. Zilikuwa ni hisia za kipekee zilizojawa na historia ambayo Monica hakuwa nayo kwani walikutana ukubwani.

    Ile hali ya kukosa nafasi ya kuitoa bikra ya Matha ilimtesa sana lakini bado aliona si bure anaweza kuthubutu kumtoroka Monica kisha walau afanye mapenzi na Matha kama njia ya kupunguza machungu aliyoyapata wakati ule.

    Adrian akaamua kumpigia simu Matha. Simu iliita kidogo ikapokelewa, alikuwa ni Matha katika sauti iliyochangamka sana. Adrian alilitambua hilo akajijengea kujiamini sana. Walizungumza mengi sana, na kuishia katika mazungumzo yaliyohusisha penzi lao la wakati ule. Mazungumzo hayo yaliibua hisia kwa kila mmoja, Matha akawa wa kwanza kulia, Adrian Mhina akaligundua hilo akajaribu kumbembeleza sana lakini kwa kuwa alikuwa yupo kwenye simu ilikuwa ni kazi bure.

    “Adrian nahitaji kukuona!!!!” Matha alijikuta akitamka kwa hisia kali. Adrian hakuamini alijua kuwa Matha anatania. Lakini kadri alivyorudia mara kwa mara ndipo aliamini kuwa alikuwa anamaanisha mpenzi huyu wa zamani.

    Kwa kuwa alikuwa ameoga tayari, alivaa pensi ambayo hupendelea kuivaa jioni, juu akavaa fulana iliyokuwa inambana na kuonyesha kifua chake jinsi kilivyokuwa kimejigawanya katikati, chini akavaa viatu vya wazi.

    Akachukua pochi yake, akatazama ndani yake palikuwa na kadi ya benki (ATM) na noti kadhaa za shilingi elfu kumi na elfu tano.

    Hizo zilimtosha kwa ajili ya kuchukua teksi iliyomfikisha maeneo ya PPF Tower, akazama katika mashine ya kutoa pesa akajitwalia kiasi alichotaka, kisha akapanda tena hiyo teksi iliyokuwa inamsubiri.

    “Tunaelekea wapi bosi!!!” alitamka yule dereva, Adrian akatabasamu kusikia anaitwa bosi, tabasamu lake likaruhusu meno yake yaliyoathiriwa na utafunaji wa vitu vyenye sukari kuonekana.

    “Millenium Hotel Nyegezi” alijibu kwa sauti nzito na tulivu.

    Safari ikaanza!!!



    Matha alikuwa anamaanisha alichokuwa anamwambia Adrian kwenye simu, picha za Michael na John Mapulu zilitokea mara kwa mara lakini hazikuweza kukizuia kivuli cha Adrian Mhina. Alijua ni kweli anafanya usaliti lakini, ile hatia ya kumtenda Adrian miaka kadhaa iliyopita ikawa inamuadhibu. Matha akajikuta anafanya maamuzi ya ajabu!! Maamuzi ya kuificha na kuifuta hatia hiyo kwa kumpa penzi Adrian.

    “John alimdhulumu Adrian, Michael amemwibia John, na Adrian anachukua kwa Michael….ah!! wote weziiii” alisema Matha wakati akiikaribia hoteli ya Millenium iliyopo maeneo ya Nyegezi jijini Mwanza.

    Matha alianguka kifuani mwa Adrian baada ya kuwa wameingia chumbani, Adrian alimpokea kwa kumbatizi lenye huba ndani yake. Machozi yakamtoka Matha na kukilowanisha kifua cha Adrian, Adrian hakuwa jasiri na yeye akatokwa machozi. Walikuwa wanavuta fikra za miaka iliyopita.

    Baada ya kuachiana, kila mmoja alimtazama mwenzake, halafu kwa pamoja wakautazama mlango kumbe ulikuwa unapiga kengele ya kuwapa taarifa ya kuwa upo wazi, wakatabasamu Matha akaenda kuufunga vizuri.

    Wakati anaenda mlangoni Adrian alipata fursa ya kumwangalia vizuri jinsi alivyokuwa ameumbika, hakuwa na shaka hata kidogo kuwa alikuwa na haki ya kumtoroka Monica siku hiyo na kuzini nje. Matha alikuwa ni mrembo haswaa, wakati anaufunga mlango aliinama kidogo, kikaonekana kicheni kinang’ara katika kiuno chake.

    Macho yakamtoka Adrian, alijua kuwa Matha alifanya maksudi kwani tangu zamani hizo alikuwa anafahamu ni kwa jinsi gani yeye (Adrian) ni mfuasi wa kiurembo hicho.

    Wakati Matha anarejea katika mwendo wa kunyata na yeye Adrian alielekea Matha alipotoka, akachomoa kikadi kilichokuwa pembeni kidogo ya mlango. Taa zote zikazima!!! Kiyoyozi kikawaka!!!

    Teknolojia ina mambo!!!!

    Akarudi kwa hisia za kupapasa akafika na kumkuta Matha bado amesimama. Akamkumbatia tena na kumbusu.

    “Asante Adrian!!!” alishukuru Matha kwa sauti ya kimahaba.

    Katika chumba hicho hakuongelewa Michael, John wala Monica.

    Kila mmoja alijua kuwa alikuwa anaiba!!!!



    *****



    Monica alikuwa anampenda sana Adrian sio tu kwa kuwa alikuwa na pesa na pia anatoka familia ya kitajiri la!! Moyo wa kujali aliokuwanao Adrian ulimvutia zaidi. Japo wasichana wengi walidhani kuwa Monica amefuata pesa kwa Adrian.

    Siku hii Monica alikuwa anataka kuzungumza na Adrian juu ya ndoa yao ambayo ilikuwa imekaribia na huo ujauzito aliokuwanao.

    Suala la kuitunza siri ya ujauzito huo ilikuwa imemchosha hivyo alihitaji kumshauri Adrian kuwa wawe wawazi.

    Adrian aliporejea tu kutoka Nairobi alipokuwa amefuata mzigo wa nguo mpya. Monica alimuomba waonane, Adrian akawa amempangia Monica siku hii ambayo alikutana na Matha. Ile hali ya Adrian kuhairisha ghafla miadi hiyo wakati yeye Monica akiwa amejipanga na kuwaaga wazazi wake ilimshtua na kumkera sana, alijiuliza maswali mengi.

    “Mara anaumwa!!! Sijui hajisikii vizuri!!!...kuna ukweli hapa au mume wangu amenichoka!!!” alijiuliza. Hakutaka kumwambia mtu yeyote kuwa Adrian amehairisha ahadi yake. Aliona aibu kwa wadogo zake wa kike ambao kila siku walikuwa wakimwonea wivu.

    Monica akawaza sana mwishowe akaamua kwenda kwa Adrian bila taarifa.

    “Isijekuwa ana kasichana leo hapo kwake….yaani sijui nitamfanyaje!!!” aliwaza Monica, wakati huo ilikuwa saa nne usiku.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kimya kimya huku mapigo yake ya moyo yakimwenda mbio aliifikia nyumba ya Adrian. Akanyata hadi mlangoni.

    Akatega sikio hakusikia lolote lakini pumzi zikipishana hapa na pale. Kabla ya kugonga mlango akaiondoa kanga yake aliyokuwa amevaa akabakia na kisketi kifupi sana, lengo likiwa kumtega Adrian.

    Akaikunja kanga na kuitia katika mkoba, akajaribu kufungua mlango ukawa haujafungwa, akausukuma taratibu ndani taa ilikuwa imezimwa, akapiga hatua mpaka ndani.

    “koh….koh….koh…” akakohoa baada ya kukutana harufu ya sigara, wakati anaiendea taa akasikia kitu cha baridi kabisa kikimgusa shingoni.

    “We Adrian wewe!!! Hebu acha ujinga…ina maana kumbe…..” kabla hajamaliza alisikia kitu kizito kikitua mgongoni mwake, hakikuwa chuma lakini mkono wa mtu, viatu virefu alivyokuwa amevaa vikamtegua mguu wakati anajaribu kutafuta balansi. Akapiga ukelele wa nguvu ukelele wa maumivu.

    Mara taa ikawashwa, hakuwa Adrian!!! Ilikuwa sura ngeni kabisa machoni mwake.

    “Shkamoo” alisalimia kwa uoga, akajibiwa kwa tabasamu feki, macho mekundu.

    “Wewe ni nani yake Ady” aliulizwa.

    “Nani mimi?” aliuliza na yeye il-hali wapo wawili tu hapo ndani. Akapokea pigo jingine usoni akatoa kelele tena. Kelele hazikuwa na msaada wowote kwani nyumba ya Adrian ilikuwa imejitenga sana.

    “Mke wake…naniii mchumba” alijibu Monica. Uso wake tayari ulikuwa mwekundu na alikuwa anajitahidi kuizuia damu inayomtoka isiendelee kutoka kwa kujilamba midomo.

    Jibu hilo lilikuwa baya sana mbele ya mtu aliyekuwa mbele yake. Mwanzoni alikuwa ameishikilia bunduki lakini sasa akaiweka kando akamvagaa yule msichana akamchania chania nguo zake, kisketi, bikini, sidiria na blauzi Monica akawa uchi wa mnyama. Lakini mbele yake alikuwepo mnyama mwingine John Mapulu. Kama vile simba anavyomvagaa swala ndivyo John alifanya akamvagaa na kuanza kumbaka Monica kwa kulazimisha, nguvu alizokuwanazo zilimshinda Monica ambaye alikuwa hajaandaliwa, maumivu yakamzidi damu nazo zikamvuja sana.

    “Nisamehe!!!”

    “Akusamehe nani?? Unajua Adrian yupo wapi na anafanya nini??” aliuliza John huku akiendelea kumbaka Monica.

    Baada ya kumbaka alimtembezea mwaliko wa kipigo kikali sana. Monica akapasuka pasuka.

    John hakuwa na huruma!!! Tayari alijua kuwa yu hatiani hivyo ongezeko la hatia nyingine kwake halikuwa tatizo. Maana hatia moja ukiongeza nyingine jibu bado ni HATIA.

    Alitambua kuwa ameua tayari!! Akavaa nguo zake na kutoweka bila kizuizi chochote, akimwacha Monica nusu mfu nusu hai.



    *****



    Matha na Adrian waliamka kwa ajili ya kujiandaa majira ya saa kumi na moja alfajiri.

    Wote walikuwa hawawezi kutazamana usoni. Hakuna aliyeweza kuzungumzia kuhusu usiku uliopita. Kila mmoja alijidai hajui kinachoendelea.

    Adrian aliwahi bafuni akabonyeza kitufe katika moja ya kona ya bafu maji yakaanza kupata joto, alipohakikisha joto hilo ni sahihi akaenda na kumchukua Matha wakaingia kuoga wote. Huko walikuwa kama watoto wadogo, mara wafinyane wamwagiane maji wabebane waogeshane ilimradi tu burudani.

    Walitumia saa zima bafuni na wote walitoka wakiwa na furaha.

    “Twende ukapaone kwangu najua umepasahau tayari, maana lile ghorofa la mzee Kimaro limevunjwa tayari yaani huwezi kupakumbuka”

    “Siwezi kupotea hata iweje, sasa nitakuja peke yangu kesho!!” aliahidi Matha katika hali ya kubishana. Adrian akakubaliana naye kwamba kesho ataenda mwenyewe. Waliagana kwa kukumbatiana pale chumbani kisha wakateremka na kwenda kupata kifungua kinywa halafu wakapanda teksi iliyomfikisha Matha hadi Buzuluga stendi na kisha kuondoka na Adrian kuelekea Isamilo.

    Wakapungiana mikono ya heri.

    Adrian alipoagana na Matha ndipo alipata upenyo kidogo wa kumfikiria Monica, kwanza alimchukulia kama msichana ambaye ameingilia mapenzi yake na Matha. Aliamini Monica ndiye alipaswa kuwa mpenzi wa John halafu yeye na Matha waendelee kama zamani.

    Suala la Matha kuwa bado hajazaa lilizidi kumtia hamasa Adrian na kuamini kabisa kuwa alipangwa kwa ajili yake kiumbe huyu. Uchungu wa bikra ya Matha kutolewa na mtu mwingine tayari ulikuwa umepoozwa usiku uliyopita, penzi alilopata kwa Matha lilikuwa limekifuta kidonda kile, wazo la kuendelea kuwa na Matha katika mapenzi lilivamia kichwa chake, likamyumbisha kimsimamo akaanza kuziona siku za kufunga ndoa na Monica zikizidi kusogea. Adrian akaanza kumuona Monica kuwa si mwanamke sahihi tena kwake.

    Adrian alitaka kumkwapua Matha, jumla jumla.

    Akiwa katika mawazo hayo akaikumbuka mimba aliyokuwa nayo Monica. Jambo hilo likamfadhaisha sana alijua hicho ndio kilikuwa kiunganishi baina yao.

    Naenda kumshauri aitoe!!!! Aliijiwa na wazo hilo la kishetani.

    Lakini kabla ya kumwambia aitoe hebu ngoja kwanza nikazungumze na mzee juu ya kuhairisha ndoa hii kwanza. Adrian aliwaza hivyo kwani alikuwa anaamini mzee wake alikuwa anampenda sana hivyo atamsikiliza na kumsaidia.

    “Hebu ingia huku Kirumba kwanza” Adrian alimwamuru dereva aende upande alioutaka. Huko ndipo alikuwa anakaa mzee Mhina na familia yake, hapo hapo nyumbani mzee Mhina alikuwa na ofisi yake ndogo.

    Adrian alifika na kuingia moja kwa moja ndani akawasalimia ndugu zake kisha akaenda kidogo kudeka kwa mama yake kabla ya kuingia ofisini kwa baba yake.

    “Simba hilooo!!!” alikoroma mzee Mhina akimsifia mtoto wake. Adrian alizipokea zile sifa kwa kicheko kidogo kisha akamsalimia mzee wake kwa kumshika mkono halafu akakaa.

    “Umetutenga sana simbaaaa!!!!”

    “Majukumu baba!!!!” alijibu Adrian.

    “Anakuja Monica tu, ana juhudi sana yule mtoto wangu” maneno hayo yaliyotoka katika kinywa cha Mzee Mhina yalimchoma sana Adrian kwani alijua ni kiasi gani familia yake ilikuwa inampenda Monica.

    “Monica akija ni sawa nimekuja mimi” alijibu kwa sauti ya chini Adrian.

    “Haya niambie mguu huo najua ni kwangu”

    “Ndio mguu huu kwako kuna jambo nahitaji tuzungumze kidogo ni kuhusu ndoa yangu mimi na Monica” Mzee Mhina akashtuka kidogo, akaacha kazi alizokuwa anafanya akaondoa miwani yake machoni akamtazama Adrian.

    “Umempiga mtoto wa watu eeh!!” alibashiri. Adrian hakujibu akatabasamu!!!

    “Bora ingekuwa hivyo tungeyamaliza wawili”

    “Nini sasa tatizo….”

    Kabla mzee Mhina hajamaliza kuzungumza alikatishwa na simu ya Adrian.

    “Ah!! Namba mpya hizi zinaniboa sana” alilalamika huku akijiweka sawa koo kwa ajili ya kupokea simu ile.

    “Adrian Mhina nani mwenzangu!!!”

    “Naitwa Jose kuna tatizo hapa kwako!!!”

    “Tatizo tatizo gani??” alihoji kwa mshangao mkubwa Adrian, mzee Mhina alikuwa makini kana kwamba alikuwa anausikia upande wa pili unavyojieleza.

    “Mkeo… ni mkeo…..hebu njoo” kauli hiyo ikamnyanyua kutoka katika kiti alichokuwa amekaa, akaanza kupambana na joto kali lililomkumba ghafla. Mzee Mhina naye akasimama wima na kumsogelea mwanaye.

    “Adrian nini kimetokea kwani”

    “Hata sielewi wananiambia mke wangu sijui, hebu ngoja niende baba”

    “Tunaenda wote hebu ngoja” mzee Mhina aliingia ndani akachukua funguo za gari lake akamuaga mama Adrian bila kumwambia lolote linaloendelea.

    Injini za gari zilizimwa mbali kidogo na nyumba aliyokuwa anaishi Adrian kwani umati ulikuwa mkubwa sana, Adrian alikuwa anatetemeka sana lakini mzee Mhina ukongwe ulimsaidia aliweza kupambana na presha ile.

    “Mungu Wangu sijui kama ni mzima yule” walisikika watu wakizungumza. Adrian aliyasikia hayo, mzee Mhina akawa makini amemshika mkono kwani aliamini kuwa kuna tatizo kubwa ambalo mwanae hawezi kulihimili.

    Na kweli hakuwa amewaza vibaya mzee huyu, punde tu baada ya kuuona mwili wa mpenzi wake Monica ukiwa umezungukwa na damu pande zote lakini ukiwa umesitiriwa kwa upande wa kanga Adrian alilegea na kupoteza fahamu palepale. Likaanza zoezi la kumpepea pasipo mafanikio.





    Baada ya polisi kumaliza utafiti wao na kutoa PF3 , mwili wa Monica ulipelekwa hospitali kwa kujaribu kuokoa maisha yake. Mzee Mhina alichukua jukumu lote la kusimamia shughuli hii kwani aliamini kuwa mwanae atazinduka baadaye bila wasiwasi wowote.

    Hospitali ya Sekoutoure (Seketule) ndiyo ambayo ilisimamia kidete kupambana na Israel asiitwae roho ya Monica. Juhudi zao zilizaa matunda kwani Monica alipata nafuu baada ya kuongezewa maji na damu mwilini huku akipumua kwa kutumia mtambo maalumu wenye hewa safi ya oksijeni.

    Mzee Mhina alikuwa makini sana na jambo hili, kwa kuwa aliambiwa mgonjwa anaendelea vizuri hakutaka kumfikishia taarifa mkewe alihofia kuvuruga amani nyumbani maana mkewe alikuwa muoga sana.

    Saa mbili usiku Monica alikuwa amerejewa na fahamu na alikuwa anapumua bila kutumia msaada wa mashine.

    Mzee Mhina alikuwa katika chumba cha daktari ili aweze kupokea maelekezo. Daktari alizungumza mengi ya kumtia moyo mzee Mhina kisha akafikia mahali akamweleza mzee Mhina jambo la kushtua.

    “Tunasikitika kwamba mimba yake imetoka”

    “Mimba!!! Mimba gani tena??” alihoji mzee

    “Mgonjwa alikuwa na mimba changa nadhani ni ya hivi karibuni labda wiki mbili hadi tatu”

    Mzee Mhina hakuwa na swali la kuuliza zaidi ya kumshukuru daktari kwa msaada wao mkubwa.

    Suala la Monica kuwa na mimba lilimshangaza sana mzee Mhina, kimoyomoyo akaanza kumlaumu Adrian kwa kumficha jambo hilo, alimchukulia kama mbinafsi sana. Aliamini ni yeye alimzuia Monica asimueleze kuhusu hilo.

    Ghadhabu ikampanda akaidhibiti kwa kupiga mluzi usiokuwa rasmi.

    “Monica mwanangu pole sana ni nini kilitokea” Mhina akamhoji mtoto wake huyo huku akimpapasa kiganja cha mkono wake wa kuume.

    “Adrian baba!!!”

    “Adrian…amefanyaje??”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa sasa siwezi kuzungumza” alijibu Monica. Baba akamuelewa!!!!



    Adrian alikuwa katika hali ya kawaida baada ya kuwa amepewa muda wa kupumzika kidogo.

    Sasa walikuwa, baba yake Adrian, Adrian na wazazi wa Monica. Wote walikuwa pale hospitali kumchukua Monica baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali. Lilikuwa jambo jema kuwa Monica hakuwa ameambukizwa magonjwa ya zinaa.

    Adrian alikuwa kimya muda wote akijiuliza ni nini kimemsibu mke wake huyo mtarajiwa.

    “Adrian nahitaji mazungumzo na wewe” Monica alimnong’oneza kwa sauti ya chini. Adrian akatikisa kichwa kuashiria kukubali.

    Mzee Mhina alikuwa makini na usukani huku nyuma gari ya baba yake Monica ikifuata. Safari hii iliishia nyumbani kwa akina Monica, Adrian alimkokota Monica hadi chumbani kwake. Hapo ndipo walikuwa huru kuzungumza.

    “Ulilala wapi Adrian” swali likatua katika kichwa cha Adrian, alikuwa hajajiandaa kujibu akaulizwa jingine tena, “Na ulilala na nani??” swali hilo likawa gumu zaidi ya lile la kwanza. Adrian akavuta pumzi ndefu huku akilitafuta jibu kwa jitihada zote.

    “Nililala kwa rafiki yangu mmoja hivi haumfahamu”

    “Ulilala naye?”

    “Nililala kwake kwani vipi??”

    “Adrian unanisaliti!!!” alisema Monica na kuanza kulia kilio cha kwikwi. Adrian akawa anambembeleza lakini akiwa na aibu kubwa sana, hatia ilikuwa inamsulubu ni kweli alikuwa amemsaliti Monica.

    “Yaani kweli Adrian mimi wa kunifanyia hivyo, nimekukosea nini??”

    Adrian hakuwa na la kujibu akamsisitiza Monica apumzike. Kabla monica hajakubaliana na ombi la Adrian kuwa alale, simu ya Adrian iliita, alikuwa ni Matha, akasita kupokea lakini hatimaye akapokea.



    ******



    Matha alikuwa ameufurahia sana usiku aliolala na Adrian. Alipata wasaa wa kukumbuka mengi ya nyuma enzi za utoto wake. Ilikuwa kumbukumbu ya kipekee. Baada ya kulala kutwa nzima usiku sana aliamua kumpigia simu Adrian.

    “Mambo baby Wangu”

    “Safi hali vipi…nipo na hebu nipigie baadaye kidogo” alijibiwa na simu ikakatwa. Akajiongeza kiutu uzima Adrian alikuwa na mpenzi wake.

    Wivu ukamshambulia lakini hakuwa na la kufanya. Akajifalagua hapa na pale hadi akalala tena.

    Adrian aliendelea kuzungumza na Monica hadi akaelezewa mkasa mzima ulivyokuwa.

    Akashindwa kumshuku mtu yeyote lakini kwa jinsi alivyozidi kuelezewa umbo la nje la muhusika akili yake ikahamia kwa John, John Mapulu.

    Alijiuliza amejuaje juu ya uhusiano wa ghafla aliokuwa nao yeye na Matha, akakosa jawabu. Akaondoa hisia zake potofu juu ya John.



    ****

    John hakurejea nyumbani baada ya tukio la kumbaka Monica, alielekea lilipokuwa eneo la tukio lao la wizi kwa kutumia silaha maeneo ya Imalaseko.

    Alishukia mbali sana na eneo la tukio bila kuwapa taarifa wenzake ambao waliamini kuwa alikuwa anaumwa.

    John akiwa na bunduki yake kiunoni ikiwa imefunikwa na shati kubwa alilovaa alikuwa na ghadhabu sana. Hasira yake alitamani kuimalizia kwa mwanadamu yeyote yule atakayekatiza mbele yake.

    Baada ya kumkosa Adrian nyumbani kwake ambapo alikuwa amepanga kumuua sasa alikuwa na shida na kichwa chochote kile.

    Alijibanza sehemu iliyokuwa na kigizagiza kidogo, mahali palipokuwa na kibanda ambacho mchana hufanya shughuli za kuuza nguo. Aliwashuhudia wenzake kwa jinsi walivyokuwa wanaingia ndani ya supermarket. Wawili walibaki nje kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, wakati huo walinzi wa sehemu hiyo tayari walikuwa katika foleni ya kusubiri kusomewa dhambi zao juu mbinguni. Tayari walikuwa wafu!!

    John alikuwa makini sana, jicho lake lilishuhudia gari ikija na kupaki mbali kidogo na supermarket, wakashuka watu kama kumi. Aliamini mambo yanaharibika, alitamani kupiga kelele lakini alikuwa anahatarisha maisha yake. Risasi mbili ziliwapata barabara wenzake waliokuwa wanaangalia usalama wa nje.

    Waliokuwa ndani hawakujua lolote kutokana na bunduki walizokuwa wakitumia maadui kuwa na viwambo vya kuzuia sauti.

    John akaamua kuiponya nafsi yake akatoweka eneo hilo kimya kimya.

    Hakika mambo yalikuwa yameharibika kwani siri ilikuwa imevuja na askari waliwahi eneo la tukio kwa ajili ya kuwakamata wezi.

    Haikuwa kazi rahisi lakini mwisho wa mchezo ni askari wawili na jambazi mmoja waliofanikiwa kubaki hai.

    Kituo cha polisi jijini Mwanza cha MWATEX ndipo alipohifadhiwa muharifu huyu. John alizisikia taarifa hizo kupitia vyombo vya habari siku iliyofuata. Hofu ya kutajwa na huyo mwenzake aliyesalia ilimtawala, John akawa si mtu wa kukaa nyumbani kwake tena wasiwasi ukawa ndiye rafiki yake. Alikuwa mzoefu wa kukamatwa na kuwekwa jela lakini hakupapenda hata kidogo hasa hasa kwa wakati huu ambao yupo katika vita ya kupambana dhidi ya wezi wa penzi lake.

    Hatia ikazidi kuzaana katika mwili wa John, hatia zote zilikuwa zinasubiri maamuzi yake. John hakuwa na maamuzi!!!

    Alikuwa anasikitisha sana!!!

    Michael aliigundua hali ya hofu aliyokuwanayo John, lakini siku aliyotaka kumuuliza ndio siku hiyo hiyo naye John alikuwa ameamua kumueleza Michael. Alimueleza juu ya suala moja tu la kuhusu wasiwasi wake juu ya kukamatwa na polisi wakati wowote.

    “Kwa hiyo sasa hapo tunafanyaje??”

    “Nahitaji unisaidie kama utaweza!!!”

    “Nitafanya nini sasa hapo kaka”

    “Nataka uende kule polisi ufatilie kama kweli Julius Machanya amehifadhiwa pale!!” alijieleza John.

    Michael alikuwa bado ana uoga lakini John alimtoa hofu, alimweleza jinsi ya kujua kama yuko pale. Michael alipata ahueni baada ya kuambiwa kuwa si yeye ambaye ataenda moja kwa moja bali na yeye atamtumia mtu!!

    Michael akatii siku hiyo hiyo akapata jawabu kuwa Machanya yupo pale kituo cha MWATEX.

    John hatimaye akawa amedhamiria kuzipunguza Hatia, hatia ya kwanza ilikuwa hii inayomtia wasiwasi hatia ya kutafutwa na polisi kwa kosa la wizi wa kutumia silaha.



    *****

    Adrian bado alikuwa anamuwaza Matha.

    Akiwa ndani ya gari kuelekea nyumbani kwao Kirumba alikuwa anafikiria ni jinsi gani atamtwaa Matha jumla jumla. Aliutambua upendo aliokuwa nao Monica kwake lakini kitendo cha kubakwa kilikuwa kinaanza kumuumiza kichwa.

    Laiti kama isingekuwa ujauzito!!!! Alisema kwa sauti ya chini Adrian.

    Alifika nyumbani na kumkuta baba yake akiwa bado hajalala.

    Mzee Mhina hakuwa amechangamka, na Adrian aliamini lazima iwe hivyo.

    “Adrian!!! Mbona ulinificha!!”

    “Nini baba??”

    “Kuhusu ujauzito wa Monica!!” alijibu huku akiwa amemkazia macho mwanae, Adrian akajihisi kufadhaika akainama chini akijidai kufikiria, alidhani Monica alikuwa amemweleza baba mkwe wake juu ya hilo. Alimlaani kwa kitendo hicho!!

    “Mony ndo kasema??”

    “Hapana sio yeye, ni daktari amenambia!!” alijibu mzee Mhina.

    “Unajua baba aaah!!! Mh!!! Nisamehe lakini ilikuwa bahati mbaya na hatukutaka wazazi wafahamu lakini aah!!!” alishindwa kujieleza.

    “Hilo sio tatizo…tatizo ni kwamba aliyembaka mkeo amesababisha mimba itoke” alitoa kauli hiyo huyo mzee. Kauli ambayo ilimshtua sana Adrian, kwanza alifurahia taarifa hiyo halafu baada ya kugundua kuwa damu yake ndio imepotezwa alianza kujiona mjinga. Akajihisi yupo katika hatia, hatia ya mauaji. Mauaji ya mtoto wake ambaye ilikuwa bado miezi mingi aweze kuzaliwa!!!

    Adrian akainama kwa muda mrefu!! Mzee wake akafika na kumpigapiga mgongoni kisha akamwacha sebuleni peke yake, yeye akaenda zake kulala.

    “Wamemuua mwanangu!!! Lazima nimsake muuaji!!!” aliwaza



    ******



    Hali ya hewa ya Singida ilikuwa imetulia sana, basi la Zuberi lilikuwa limesimama katika stendi ya Singida, abiria waliokuwa wamefika mwisho wa safari walikuwa wakiteremka kwa kufuata utaratibu usiokuwa maalum, kila mmoja alitaka kuwahi kushuka kabla ya mwenzake.

    Minja ambaye alikuwa ni mtu wa kulala safari nzima huku akiwa amejifunika usoni kwa kofia yake kubwa, aliwatazama jinsi abiria walivyokosa akili ya kujiongeza. Wakati akiwaona wenzake ni wajinga kwa kugombania kushuka garini, mara jicho lake likatua kwa mtu ambaye alikuwa mwenyeji wake katika mji huu wa Singida, haraka haraka alianza kuwapangua watu ili aweze kushuka kabla yao, wazo alilokuwa anawawazia likasahaulika na yeye akakubali kuwa mjinga.

    Jitihada zake zilizaa matunda japo aliwakera sana abiria wengine.

    “Aaaah!!! Defaooo!!!” alipiga kelele za furaha Minja baada ya kumuona rafiki yake ambaye alijipatia umaarufu kwa jina la Defao, kutokana na unene aliokuwa nao, unene ambao haukuwa wa utajiri bali unene wa kuzaliwa nao. Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Gervas!!.

    “Ahh!! Minja huyooo!!! Karibu kijijini kwetu!!” alijibu katika hali isiyokuwa ya kuridhisha, Minja aliligundua hilo lakini akamsogelea na kumkumbatia.

    Walitumia sekunde kadhaa kushangaana kabla ya Defao kumuongoza Minja hadi katika daladala ambayo iliweza kuwafikisha nyumbani kwa akina Defao maeneo ya Saba saba, nyumba ilikuwa imepooza sana. Nje walikuwepo watoto watatu hata wao nyuso zao zilikuwa zimejawa na simanzi huku macho yao yakitangaza njaa kali sana.

    Minja hakuhitaji Defao amvute pembeni kuweza kumtangazia dhiki iliyokuwa pale, mazingira yale yalimkumbusha hali iliyokuwepo katika familia ya marehemu rafiki yake bwana Rashid, mazingira aliyoyashuhudia siku chache kabla ya kifo chake. Kumbukumbu ya kifo ikawa imefanya shambulizi katika akili yake, ile hatia aliyoamini kuwa haikupanda gari ambalo alipanda kwa safari ya kwenda Singida sasa ikawa imeibuka, alikuwa amesafiri na hatia yake!!! Uso ukajawa na wasiwasi.

    “Vipi Minja….usisikitike rafiki yangu yaani nimepitia mengi ndugu yako…yaani afadhali umekuja” Defao alimweleza Minja huku akimpiga piga bega, hakujua kama Minja ameshtushwa na hatia inayomkabili.

    Minja hakujibu kitu, alitikisa kichwa kuonyesha kusikitika. Walipoingia ndani walipokelewa na harufu ambayo haikuwa ya kupendeza, kidogo Minja azibe pua zake lakini alisita akajikaza.

    “Karibuni!!” sauti ya mwanamke aliyekuwa na mvi hapa na pale katika kichwa chake iliwakaribisha akina Minja na Defao. Yule alikuwa ni mama yake na Defao.

    “Mama huyu ni Minja yule rafiki yangu niliyekupa taarifa zake!!”

    “Karibu baba, karibu tuuguze!!!” Alisema yule mama kinyonge, uso wake ulikuwa umepauka na alionekana kuwa na msongo wa mawazo.

    Minja alipata jawabu kuwa hapo ndani kulikuwa na mgonjwa.

    “Mama vipi amelala???” Defao aliuliza, mama akajibu kwa kichwa kuashiria kukubali!!

    Defao akamwongoza Minja wakatoka nje.

    “Minja ndugu yangu we acha tu, maisha yamenipiga kiukweli, hapa ndo nyumbani kwetu na yule ni mama yangu, hivyo vitoto hapo nje ni vya dada zangu walizalishwa wakiwa hapa hapa nyumbani ndo hao watoto tunalea!!!” alianza kujieleza Defao.

    Minja akawa msikilizaji!!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Pale ndani mshua anaumwa…si baba yangu ni kaka yake na mama, nishasahau kumwita mjomba tulizoeshwa hivyo” aliendelea. Bado Minja alikuwa anasikiliza.

    “Sasa hapa mzigo wote juu yangu!! Na sina hata kibarua maana kuna msala niliufanya hapa naishi kama digidigi tu!!!” alimaliza Defao kwa kumueleza Minja juu ya msala wa kumbaka binti wa mzee Bushir mzee ambaye alikuwa ni bosi wake wakati huo alikuwa ameajiriwa kama mlinzi.

    “He!! Ndio maana na wewe dada zako wakajazwa mimba!!!”

    “Hapana kaka si hivyo ila nilibaka!!! Yule mtoto hakika alinitega nikisema kunitega nadhani unanielewa, mimi unanifahamu huwa si mwepesi lakini kwa yule mtoto nilitenda unyama huo, ni hatia inayonisonga hadi leo kaka, maisha yangu yamekuwa magumu sana” alijieleza kwa sauti iliyoielezea kweli hatia yake, hatia iliyohitaji muafaka lakini muafaka wake ukawa mgumu sana.

    “Pole sana kaka, yametokea hayo tugange mengine sasa” alisema Minja huku na yeye akiikumbuka hatia yake, hatia ya mauaji ya rafiki yake Rashid.

    “Aaah!! Joyce nisamehe popote ulipo!!!” Defao alisema huku machozi yakimtoka, hakika alikuwa anajutia.

    “Joyce ndo nani tena??”

    “Ndiye msichana niliyembaka, anaitwa Joyce Keto. Sijui hata alipo kwa sasa!!” alijibu Defao, huku akizidi kububujikwa na machozi. Minja akamsihi ajikaze, akafanikiwa kumtuliza!!!

    Minja alikuwa bado anajiuliza juu ya hali ngumu aliyoikuta katika mji huo wa akina Defao. Hakika hali ilikuwa ni mbaya sana na hata pesa aliyokuwa nayo aliamini kuwa isingedumu kwa kipindi kirefu sana ingeisha na angeanza kuishi maisha ya kubangaiza. Ugeni wake katika mkoa huo ulimwogopesha zaidi.

    “Nitapata vipi pesa, udalali!! Umachinga!! Kuchimba mitaro!! Au au au…….yeah!!!” alikurupuka na kupiga kelele Minja. Deo akawa anashangaa, wakati huo alikuwa amenyamaza kabisa kulia.

    “Defao!!! Pesa pesa nje nje!!!” alisema Minja kwa furaha.

    “Pesa uipate wapi hapa Singida??” aliuliza Defao.

    “Pesa pesa kaka!!!! Nimeikumbuka pesa” aliendelea kusema Minja, furaha yake haikuwa ya utani. Defao alilisoma na kulielewa hilo.

    “Tulia basi unieleze!!”

    Minja alitulia na kuanza kumpa mkasa mzima Defao, alimpa mkasa uliosababisha yeye awe katika mji huo ghafla kiasi hicho. Alimueleza juu ya siri iliyopo kati ya John Mapulu na mpenzi wake Matha Mwakipesile. Minja hakusahau kumuelezea Defao juu ya pesa ambazo John anaweza kuwa anamiliki.

    Defao alipagawa baada ya kusikia habari hiyo, kutokana na shida alizokuwanazo aliamini huo ndio ulikuwa wakati muafaka wa yeye kufanikiwa tena kimaisha.

    Siku hiyo hiyo Minja alimpa maelekezo yote Defao jinsi ya kufika Mwanza na jinsi ya kumpata aidha Matha ama John Mapulu.

    Minja alikuwa anamchukulia John Mapulu kama mume mwema wa kawaida tu kamwe hakuwa anaufahamu upande wake wa pili.

    “Ukifika anza na yule John, yule ndo atakupatia pesa nyingi, huyo mke wake baadae, John akishatoa pesa tunamalizia na kwa mkewe” alieleza Minja.

    Harufu ya pesa ikatawala.

    “Tukizipata hizo tufungue hapa mtaani banda la Mpesa na Tigo pesa yaani hakuna kabisa hapa jirani kitu kama hicho halafu yanalipa hayo” Defao akiwa amechangamka kabisa alimueleza Minja. Kwa pamoja wakakubaliana.

    Siku hiyo walikunywa pombe kidogo, na nyumbani wakapeleka nyama. Ulikuwa mlo ambao ulikuwa umehadimika katika nyumba ile!!!!

    “Huyu ndiye mzee wangu anaitwa Sajenti Kindo” Defao alimtambulisha mjomba wake kwa Minja.

    “Kabla ya kuugua alikuwa ni sajenti huko Mwanza kwenu” Alimalizia Defao huku akificha juu ya suala la mjomba wake kukamatwa na kuwekwa ndani kwa kosa la kutoroka kwa mahabusu katika kituo kikuu cha polisi jijini Mwanza.

    Mzee Kindo alitolewa kwa msamaha wa raisi lakini alifutwa kazi kulingana na sheria na kanuni.

    Wazo lake la kumkuta mwanaye Joyce Kindo akiwa hai lilifutika baada ya kugundua kuwa tayari alikuwa anaitwa marehemu. Ni tatizo la ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu lilikuwa limemuweka kitandani, mshtuko alioupata ulimletea madhara makubwa. Huyu ndiye alikuwa Sajenti Kindo. Sajenti aliyekuwa zamu siku ambayo John Mapulu na Michael walipotoroka rumande.

    Minja aliachiwa jukumu la kuihudumia familia ya Defao wakati yeye (Defao) aliposafiri kwenda Mwanza, kwa lengo la kuonana na John Mapulu, lengo la kuvuna pesa bila jasho!!!

    Defao akaagana na Minja akapanda gari na kuondoka!!! Laiti kama angeyajua maovu na unyama wa Mapulu ni heri angebakia katika shida zake!!!!

    Hatia ya kumbaka Joyce Keto nayo ikapanda naye ndani ya gari.

    “Nikizipata hizi pesa nitampatia Minja fungu lake halafu namtafuta Joyce Keto, kama yupo hapo Singida nitatangaza ndoa..pesa ndo kila kitu!!!!” aliwaza Defao akiwa katika siti ya dirishani akihesabu miti jinsi inavyorudi nyuma kwa kasi!!!!

    Safari ya kwenda jijini Mwanza!!!





    ****



    Daladala inayokwenda Igoma jijini Mwanza ilisimama katika kituo cha Mwatex, akateremka mwanaume aliyekuwa amevaa miwani nyeusi. Kofia yake iliweza kuiziba miwani yake kidogo, alikuwa ni mrefu aliyekuwa na mwili uliothibitisha kuwa anafanya mazoezi, hakuwa akitabasamu wala hakuwa amenuna!!! Alilipa nauli yake kamili.

    Daladala ilipoondoka alitazama kushoto na kulia akavuka barabara na kuelekea kilipokuwa kituo cha polisi. Hakukiendea kituo moja kwa moja bali alipinda kidogo kushoto akakutana na uchochoro, akaangaza tena pande zote kisha akakaa chini. Akaunyoosha mguu wake ukawa umeiziba ile njia nyembamba. Akatoa sigara akaitia mdomoni akataka kuiwasha akagundua kuwa alisahau kiberiti nyumbani. Akaiacha kwa muda mdomoni kisha akaitoa tena na kuitupa, akajilaza katika majani akawa anasubiri kitu. Ilimchukua dakika takribani tano kupata jawabu la swali lake. Alihisi mguu wake uliokuwa njiani ukiguswa.

    Akasimama kwa ghadhabu, akaitoa miwani yake. Jicho jekundu likaonekana.

    “Samahani kakangu!!” sauti ya mwanamke ikamsihi mbabe huyu. Maneno yale yakamchefua akamsogelea alipo akamnasa kibao kimoja kisha kipigo cha nguvu kikafuatia, yule mama akapiga mayowe raia wema wakafika kumsaidia. Muharifu huyu bado alikuwa anataka kumpiga lakini wanaume wakamdaka na kumvuta kuelekea kituoni.

    Mwanamke alikuwa anavuja damu huku akigumia kwa maumivu!!! Wananchi wale wenye hasira wakajua wamefanya jambo la msaada sana kumkamata mbabe huyu ili sheria ichukue nafasi.

    “Unaitwa nani???” afande alimuuliza baada ya kuwa amemnasa vibao viwili.

    “John Daud!!!” alijitambulisha kishari shari!!!

    Akaamriwa kuvua mkanda, kofia, miwani ikachukuliwa, akavua soksi na viatu, akasachiwa akakutwa na shilingi elfu hamsini na tano, zikaandikwa katika kikaratasi (PPR) akapewa hicho kikaratasi na kuongozwa kuingia rumande.

    Alipoingia alitabasamu, tabasamu kutoka moyoni alikuwa amefanikiwa kirahisi sana kufika eneo la tukio kwa wakati. Mpango alioutaka ukawa umetimia. Safari ya kuingia rumande.



    Huyu hakuwa John Daud kama alivyojitambulisha huyu alikuwa ni John Mapulu. Alikuwa amefanikiwa kuingia rumande, lengo lake likiwa moja tu kummaliza rafiki yake ambaye alikuwa amekamatwa katika tukio la wizi Supermaket!! Aliamini kwa kumuua huyu atakuwa amejipunguzia hatia, inayomkabili.

    Hakuwa na wasiwasi wa kushtukiwa kuwa yeye ni John Mapulu aliyetoroka rumande katika kituo cha kati, kwanza alitambua kuwa wale askari waliokuwa zamu wote waliswekwa rumande na kama hiyo haitoshi, tatizo la takwimu Tanzania lilimpa hali kujiamini.

    John Mapulu akaichukua nafasi yake akakaa huku akiwa ameuficha uso wake, waliojifanya wenyeji walimzodoa lakini hakuwajibu chochote aliendelea kuinama hadi hapo kigiza kilipoanza kuingia.

    Punde baada ya kuhesabiwa idadi ya waliopo rumande kwa siku hiyo alihesabu muda kidogo mbele akaunyanyua uso wake, kisha mwili mzima akapiga hatua kuelekea chooni, akazuga kujisaidia haja ndogo, kisha akarejea na kupitia vyumba kadhaa, uzoefu wake katika maeneo kama hayo ulimpa ujasiri mkubwa. Ndani ya muda mfupi akawa amemuona Julius Machanya, ni huyu aliyekuwa anamtafuta!!!

    John alishuhudia jinsi alivyokuwa katika hali mbaya, alikuwa amezungukwa na damu zilizotokana na kipigo. Akamsogelea na kujilaza jirani naye!! Mahabusu wengine walikuwa wamekikimbia chumba hicho!! John akatumia mwanya huo kuikutanisha mikono yake miwili katika shingo ya July akaikaba kiujasiri akauondoa uhai wake. Kama jambo la kawaida kabisa!!!

    Hatia moja ikawa imepunguzwa kwa kufanya mauaji!!!

    Baada ya kumaliza shughuli hiyo John alienda hadi mlangoni na kumuita afande mmoja aliyemuingiza hapo ndani.

    “We mpumbavu unalala humu wakati una pesa?” afande akamweleza John!!!

    John akajidai kufikiri kisha akamuita tena.

    “Tuigawane basi!!!”

    “Haya hebu subiri!!! Unakaa kaa tu humu ndani wakati hakuna aliyekuja kukushtaki? Acha kuwa mjinga wewe, au unataka ukasimame na yule hawara yako mahakamani” alijibiwa, baada ya muda ulifunguliwa mlango akaruhusiwa kutoka akapewa shilingi elfu ishirini na tano nyingine askari wakaigawana.

    John Mapulu akawa huru tena!!!

    Hatia ya kwanza ikazikwa. Akajihisi yupo huru.

    Sasa ni zamu ya huyu mjinga Adrian ambaye anathubutu kunigusia Matha wangu!!! Alisema John huku akiwasha simu yake aliyokuwa amerejeshewa baada ya kutolewa rumande!!

    Akampigia Matha, wakapeana salamu na utani wa hapa na pale hadi salio likaisha. John akajisikia fahari!!! Chuki dhidi ya Adrian ikaongezeka hakutaka mtu yeyote amuibie mpenzi wake.



    ***



    Matha alikuwa ameanza kuipata amani ya nafsi baada ya Minja kuwa ameenda mbali na jiji la Mwanza. Aliamini kabisa hatia ya kubeba mimba nje ya uhusiano wake na John Mapulu ilikuwa imefichwa na Michael peke yake, kwani hata yule daktari aliyempima na kugundua kuwa yu mjamzito hakufahamu kama ile ilikuwa hatia bali alijua ni salama.

    Kukutana na Adrian Mhina na kufanya naye mapenzi kisha wote kuondoka wakiwa na furaha lilikuwa jambo jingine lililompa faraja na kuamini kuwa ameua hatia mbili kwa wakati mmoja. Akajisikia amani sana kuishi bila hatia, ilibaki hatia moja tu ambayo nayo haikumtesa sana kwani hakuwepo mtu ambaye amemshuku, hatia hii ilikuwa ni ujauzito aliokuwa ameuhifadhi katika mfuko wake wa uzazi. Hatia hii alijua itavuta subira kwani tayari alikwishagundua kuwa ana mwili mzuri ambao hauonyeshi ujauzito mapema, na pia hakuwa mtu wa kichefuchefu mara kwa mara.

    Mara akakumbuka hisia zilizokuwa zinajengeka haraka haraka juu ya Adrian, kwa hali halisi hazikuwa hisia za haraka haraka kwani hapo awali Adrian aliwahi kuwa mpenzi wake japo hawakuwahi kushiriki katika tendo la ndoa hadi pale walipofanya hivyo siku chache nyuma, tena kwa kuiba kwani Matha tayari alikuwa kwenye uhusiano na mwanaume mwingine.



    Matha alijaribu kupanga majina ya watu watatu ambao wote walikuwa naye katika uhusiano alijaribu kuzitafakari hisia zake kwa makini kwa kila mmoja. Alianza na John, akayakumbuka mema yote ambayo John Mapulu alimtendea, akahesabu maisha mazuri aliyonayo, bila John asingekuwa hapo alipo, akaupima upendo wa John akagundua ni upendo wa dhati kwani kamwe hakuwahi kumfumania wala kumhisia kwamba ana mahusiano na msichana mwingine.



    John ananipenda sana!!! Lakini John hazai!!! John hawezi kunipatia mtoto na mimi napenda sana watoto!!! John amenibadilisha na kuwa mrembo mkatili, John amenifanya niwe muuaji, John si mtu mzuri!! Ni kwangu tu ndo ananionyesha upendo, John alitaka kumuua Minja, John ameua watu wengi!! John hanifai japo ananipenda. Alifanya takwimu hiyo Matha akiwa kitandani kwake, akapiga kite cha hasira akakodoa macho yake kuiangalia picha ya John iliyokuwa ukutani akaitukania ile picha mama yake mzazi!!!



    Michael, huyu naye ni mimi nilimpenda, nadhani ni kile kifua chake, mwili wa mazoezi na tabasamu zuri ambalo huzaa vidimples, yupo nadhifu sana Michael, halafu ni mpole na anajua sana kunifanya nifurahie kuwa naye faragha, Michael hana pesa lakini Michael ana uwezo wa kuzaa, Michael amenipatia zawadi ya maisha yangu. Lakini Michael alitaka kunikimbia, Michael ni baba mbaya sana kwa nini alitaka kumkimbia mwanae, huyu hana mapenzi ya kweli, nadhani vitisho vyangu ndo chanzo cha kumpata kaka huyu. Michael wewe ni fala sana hujui kuwa John alinifanya kuwa muuaji naweza kukuua dakika yoyote??? Laiti kama nisingekuwa na mimba yako!!!!!! Alimaliza Matha kwa kukiendea kioo na kujitazama akalishika tumbo lake akajilazimisha kutabasamu, akaliendea jokofu dogo lililokuwa pale chumbani akachukua chupa ya maji akanywa.



    Adrian, Adrian, Adrian!!!! Sina la kusema juu ya uvumilivu wake. Alinivumilia hakuwa na papara ya mapenzi, tazama alikuwa na upendo wa dhati. Na hadi sasa hapo amesema kuwa hajaingia katika ndoa. Maisha yake ni mazuri sana, amejipanga. Hana roho mbaya kama ile ya John na ni mvumilivu sio kama Michael. Adrian ndiye mwanaume sahihi, lakini je ataweza kuwa nami na hii mimba??? Lilikuwa swali zito. Sitaki kuitoa na kamwe sitaitoa!!!! Aliapa Matha. Kisha akachukua kalamu na karatasi akaamua kupata jibu sahihi kwa kuwapanga kiherufi, Adrian, John, Michael. Adrian akawa ametangulia kwa kila hali. Matha akacheka peke yake kama mwendawazimu kisha akakichana kile kikaratasi, akakirukia kitanda akajilaza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *****



    Defao alifika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza, alikuwa makini sana hakutaka kuunda urafiki na mtu yeyote bali alifuata maagizo aliyopewa na Minja. Shati yake iliyokuwa imechomekewa kwenye suruali mpya aliyokuwa amenunuliwa na Minja pamoja na kiatu kilichong’aa aliwashawishi madereva wa teksi kumkimbilia na kumpa heshima za kumuita bosi. Defao hakuwajali aliziendea daladala zilizomfikisha hadi Mkuyuni karibu na gereza la Butimba, huko ndipo palikuwa na nyumba za kulala wageni zilizokuwa za hadhi nafuu ya Defao. Maelekezo haya alipewa na Minja.

    Alipata chumba cha bei nyepesi sana akalipia, akakikagua chumba kisha akatoka na kutafuta chakula cha bei nyepesi akaitibu njaa yake kisha akanunua vocha na kurejea katika chumba alichokuwa amelipia.



    Akavua nguo zake na kubakiwa na pensi, akaingia kitandani, akajaribu kuishusha chandarua lakini akagundua kuwa ilikuwa ina matundu mengi pia ilikuwa ina vumbi, akaghairi akakitupa kilipokuwa, akajilaza akachukua simu yake na kupiga namba alizohakikishiwa kuwa ni za John Mapulu, akaachia tabasamu pana baada ya kusikia simu inaita. Tabasamu lililojaa tumaini!!!

    “Nani mwenzangu!!!”

    “Defao….naongea na John Mafuru” Defao akakosea jina John hakung’amua hilo.

    “Eeh!! Unasemaje kwanza namba yako mpya huku”

    “Nina shida kubwa ya kuonana na wewe kwa siku ya kesho nina jambo la msingi nahitaji kukueleza”

    “Jambo gani??”

    “La msingi” alijibu Defao.

    “Nakupigia baada ya dakika tano ngoja niangalie ratiba”

    Defao akaikata simu na kusubiri apigiwe. Alifarijika kuisikia sauti ya John.



    John alikuwa amelala mapema sana siku hiyo, baada ya kuwa amezungumza mambo mawili matatu na Joyce Keto juu ya suala la kumuanzishia Kliniki ya mimba yake. John alikuwa amekubaliana na ombi hilo akaahidi kuwa atakuwa anampeleka.

    Simu aliyopigiwa ndiyo ilimuamsha kutoka usingizini. Akakaa akamfikiria huyo mgeni aliyetaka kuonana naye, akapatwa na wasiwasi kwani alikuwa na maadui wengi sana jijini Mwanza. Hakutaka kumfuata alipo bali alitaka huyo mgeni amfuate kwake ili aweze kupambana naye kama ni mtu mbaya. Baada ya kupata muafaka huo alimpigia huyo mtu simu na kumuelekeza jinsi watakavyoonana.

    “Lakini mkeo asiwepo!!!” alisema Defao baada ya John kuwa amemaliza kutoa maelekezo.

    Neno hilo lilimshtua John lakini akahisi ni mbinu ya kucheza na akili yake.

    Akatabasamu akazima simu akalala!!!



    Asubuhi aliwaandaa vijana wake watatu, vijana aliowaamini kabisa kuwa ni vijana mashuhuri na wana roho mbaya lakini kubwa zaidi walikuwa wanamuheshimu sana. Alimuandaa mmoja kuwa ndiye awe John Mapulu wakati wengine wawe walinzi wa kuhakikisha kama huyo mtu ni mbaya basi waweze kutoa shambulio ikiwezekana kummaliza kama atajibu mashambulizi ama kumchukua mateka ili aweze kuwaeleza ni nani amemtuma.

    Saa sita mchana, Defao alifika Nyasaka jirani na shule ya Jerry’s kama livyoelekezwa na John, akampigia simu , akapewa maelekezo ya mwisho akaiona nyumba.

    Lile jambo la kuiona nyumba ile lilimtia wasiwasi akaanza kumuogopa John, aliamini hakuwa na pesa za kawaida kama aliyesimuliwa na Minja mkoani Singida. Defao akairekebisha suruali yake akalisogelea geti, akabonyeza kengere kama alivyoelekezwa punde mlango ukafunguliwa.

    “Wewe nani??” mlinzi aliuliza.

    “Naitwa Defao ni…”

    “Nakutambua!!! Na nina taarifa zako” alimkatisha kisha akamfungulia mlango akaingia, wasiwasi ukazidi kumtawala Defao, akaanza kuwa muoga. Akachukuliwa na kupelekwa mahali palipokuwa na bustani ya kupendeza, akaiangalia ile bustani akatamani ingekuwa yake, akawaza kupata pesa nyingi bila jasho akapanga kuwa na yeye atafanya mambo ya kuvutia kama haya anayoyaona.



    Tamaa zikamuingia akaanza kufikiria jinsi ya kuchukua kiasi kikubwa zaidi ya Minja. Tamaa ikamshambulia ikamfanya ajione ana haki ya kupata mgao mkubwa. Wazo la kumchinjia baharini Minja likatulia tuli katika ubongo wake.

    Akiwa katika mawazo hayo, akatokea mwanaume mrefu mwenye suti iliyomkaa vyema katika mwili wake, haikuwa kubwa wala ndogo bali iliendana na mwili wake. Mkononi alikuwa ameshikilia glasi iliyokuwa na pombe kali. Alijongea hadi akamkaribia Defao.

    “Salama kaka, karibu sana!!!” alisalimia mwanaume huyu ambaye alijitambulisha kama John Mapulu.

    “Naitwa Defao!!!”

    “Hawajakuhudumia kinywaji??” aliuliza

    “Aaah!! Usijali bosi usijali” alijibu.

    Mwanaume huyu akakaa kitako, hakuwa John Mapulu bali Joram, huyu ndiye alikuwa ameagizwa na John Mapulu ili aweze kumtambua huyo mgeni.

    Joram hakuwa na wasiwasi, alikuwa amezungukwa na walinzi ambao walikuwa wamejificha na bunduki zao viunoni.

    “Ndio Defao…nakusikiliza!!” alisema Joram. Defao akaliweka koo lake sawa akajaribu kuzungumza kwa kujiamini lakini akawa anatetemeka sauti.

    Maelezo yake yalikuwa yamenyooka sana kama alivyokuwa ameelezwa na Minja. Joram alikuwa makini sana kumsikiliza Defao hadi pale alipomaliza.

    “Asante sana kwa taarifa kaka, asante sana tena sana….sasa chukua namba yangu hii nyingine nitakutafuta jioni, asante sana”

    “Lakini ni biashara hii ndugu yangu!!!” Defao alisema.

    “Kwani tulielewana bei gani kwa taarifa hii??” alihoji huku akidhani kuwa Defao alikuwa amewasiliana na Minja tayari kuhusu malipo.

    “Bado hatujazungumza!!”

    “Basi jioni nitakutafuta tuzungumze, kwa sasa hebu subiri kidogo” alinyanyuka Joram kisha akarejea na kibahasha kidogo akampatia Defao wakaagana kwa miadi ya kukutana jioni.



    “Vipi alikuwa na ishu gani huyo??” John alimuuliza Joram.

    “Aah!! Bwege tu huyo alikuwa anamuulizia Julius Machanya, nadhani ni ndugu yake” alidanganya Joram.

    “Mpuuzi aende akamuulizie kwa Mungu huko” alisema kwa jeuri John huku akimshangaa huyo Defao kwanini alitaka mkewe asiwepo wakati wa wao kukutana. Akapuuzia akaifuta namba yake!!!



    Joram alikuwa amepata siri nzito sana ambayo ilimsukumia kupata ujasiri wa kufanya jambo ambalo hakuwahi kuliota, baada ya kuondoka pale nyumbani kwa John alimpigia simu Defao kabla ya jioni wakakutana mahali akampatia milioni tatu, akijumlisha na zile za asubuhi jumla inakuwa milioni tatu na laki moja na nusu.

    Kwa Defao ilikuwa shangwe sana hakutegemea kupata pesa hizo kwa wepesi kiasi hicho, akazifunda katika suruali yake huku akimuahidi Joram ambaye yeye aliamini kuwa ni John Mapulu kwamba hataitangaza siri hiyo.

    Siku ya Defao ikapendeza sana akahama nyumba ya kulala wageni Mkuyuni akaenda zile za gharama ya juu kidogo. Upendo wake kwa Minja ukaanza kupungua hatua kwa hatua akaingiwa na pepo la dhuluma.

    Hakutaka kurudi Singida kwa wakati, akawatamani samaki wa Mwanza aina ya sato na dagaa watamu wa ziwa Viktoria. Miamba mikubwa mikubwa ikawa inazidi kumvutia machoni. Akapaona Mwanza patamu.

    Akaendelea kukaa!!!

    Jiji la miamba!!!



    *****



    Matha alikuwa anazungumza na Michael kwa njia ya simu ni siku nyingi zilikuwa zimepita bila wao kuonana. Yalikuwa majira ya saa nne usiku, wawili hawa walikuwa wanafurahia huduma za punguzo la bei katika mitandao ya simu hivyo walikuwa wanazungumza hata yasiyokuwa na maana.



    Mlango wa Matha uligongwa, akasogea akiwa na simu mkononi akaufungua, kipande cha mwanaume kikakingia ndani.

    Matha akakata simu ghafla, akamshangaa mgeni wake. Huyu alikuwa ni Joram!!! Kiuhusika alikuwa ni shemeji yake, lakini kikazi alikuwa ni jambazi mwenzake japo walipishana ngazi. Joram alikuwa wa kumuheshimu Matha kila siku!!! Lakini badala ya kumuheshimu ni mara nyingi Joram alipokuwa anabaki peke yake na Matha alikuwa akimtamkia maneno yaliyoonyesha kuwa alikuwa katika penzi zito.

    Matha hakuwa na hisia hata kwa mbali kwa mtu huyu!!!



    Harufu ya pombe ilimaanisha kuwa Joram alikuwa ametokea bar kunywa na kufika katika chumba cha Matha akiwa amelewa

    Joram alimsogelea Matha na kumkumbatia kwa nguvu, japokuwa alikuwa amelewa lakini bado alikuwa na nguvu. Matha hakuwa legelege alijitoa katika mikono ya Joram na kujiweka pembeni, Joram akamsogelea tena, machale yakamcheza Matha akaamua kujilinda. Mwilini mwake alikuwa amevaa kanga moja na ndani akiwa na chupi pekee, kifuani alikuwa na sidiria.

    Alimtazama machoni Joram kisha akaichokonoa kanga yake ikaanguka chini akazungusha mguu wake kama anavyofanya muigizaji wa filamu za mapigano Jean Claude Van damme. Mguu usiokuwa na kiatu ukatua barabara katika shavu la Joram akayumba lakini hakwenda chini. Matha hakulemaa akajirusha tena teke jingine safari hii Joram akaliona akakwepa lakini tayari mkono wa Matha nao ulishafika na kupangua kibao alichokuwa amekirusha Joram. Wakali wa mapigano ana kwa ana!!

    Kengere ya hatari ikalia katika kichwa cha Joram akahofia kuchafuliwa sura na mwanamke huyu, akaamua kuzungumza.

    “Matha!!! Achaaa”

    Matha akatulia akawa amejisahau kuwa chupi ipo hadharani.

    “Matha kuna jambo hapa!!! Kwanza vaa kanga” alisema Joram huku akitweta, Matha akavaa haraka haraka kanga yake.

    “Nisikilize kwa makini kwanza samahani kwa kuja usiku kwako lakini ilikuwa lazima iwe hivyo” alisita akavuta pumzi kisha akaendelea, “Unajua kwamba siri yako kidogo itoke leo??”

    “Siri gani??”

    “Kuwa u mjamzito!!!” alitamka maneno ambayo kwa Matha yakawa na ladha tamu ya mkuki kwa nguruwe….akakodoa macho.

    “Nani ana mimba nani kakwambia kama ni John anatania” alipagawa binti huyu, nguvu zikamwisha akajikuta anaogea ilimradi tu!!

    “Wala si John!!! Hata huyo John hajui, hapa nafahamu mimi, wewe, na aliyekupa mimba basiii!!!” alijibu kwa utulivu Joram. Matha alikuwa anamkubali sana Joram kwa kuficha siri, hivyo alimuamini pale pale. Joram alielezea picha yote ilivyokuwa. Kipindi hicho chote Matha alikuwa anatetemeka. Hakutegemea kama tatizo limeibuka upya!!

    “Kwa hiyo tunafanyaje Joram!!!” Matha akajaribu kuunda urafiki.

    “Nadhani unajua tunafanyaje, bila shaka unaamini kuwa mimi ni mtunzaji mzuri wa siri”

    “Nakuamini asilimia zote” alisema Matha, Joram akacheka kisifa sifa.

    “Safi sana nilidhani imani yako imeshuka!!!”

    “Kamwe haiwezi kushuka!!”

    “Basi hata siri ya kuwa mimi ni mpenzi wako wa siri nitaitunza!!” aliongea kimajivuno huku akiyanyanyua mabega yake juu, Ngoma za sikio la Matha zikataka kufyatuka kwa kusikia maneno hayo makali ya Joram.

    “Unamaanisha nini Joram?”

    “Kwani unadhani nimemaanisha nini?”

    “Yaani uwe mpenzi wangu”

    “Ooh!! Samahani sio mpenzi bali mzinzi mwenzako maana mpenzi ninaye” aligandamiza msumari mwingine Joram, Matha akaiuma midomo yake kwa ghadhabu, hofu ikachukua ubabe wake wa kurusha mateke. Akawa dhaifu!

    “Sidhani kama una maanisha Joram!!”

    “Aah!! Basi kama simaanishi ngoja niende, lakini wamuonaje John wewe, una hamu ya kufa?? Si unajua kufa hakujaribiwi” alisema huku akigeuka aondoke.

    “Joram!!!”

    “Yes!! Darling” alijibu Joram, Matha akataka iwe ndoto yeye kuitwa hivyo na Joram lakini ilikuwa ni hali halisi. Joram alikuwa anataka penzi, kichefuchefu kikachukua hatamu!!! Akakimbia bafuni akatapika kidogo.

    “Hivi ina miezi mingapi??” aliuliza Joram kwa mbwembwe. Huku akitabasamu.

    “Joram usizungumze na John lolote nitakupigia simu” alisihi Matha.

    “Jitahidi iwe kabla ya kesho jioni” alisema na kuondoka bila kuaga.





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kanisa la kilokole maeneo ya Mwenge jijini Dar es salaam lilikuwa limejaa watu wengi sana magari ya kifahari yalikuwa yamepangana na kuleta maana kuwa wafuasi wa kanisa hilo walikuwa ni watu wenye kipato cha juu, wale wa kipato cha chini hawakuwa na nafasi.

    Ndivyo ilivyokuwa lakini mle ndani ulipofika wakati wa kutoa ushuhuda waliokwenda pale mbele walikuwa watu wa hali za chini sana, Swali lilikuwa je ni wao pekee wanaopata miujiza hiyo ama kulikuwa na namna.

    Mamia ya waumini walikuwa wametega masikio ili waweze kusikia palikuwa na muujiza gani kwa siku hiyo.

    Mama mmoja akisaidiwa kutembea alisogezwa mbele ya madhabahu na kuanza kutoa ushuhuda wake juu ya mwanaye ambaye amepotea katika mazingira ya kutatanisha baada ya kwenda katika mji wa Mugumu Serengeti kwa masuala ya kimasomo.

    “Nilidhani mwanangu wamemuua, nimehangaika kwa waganga wengi sana hawakuweza kunipa jibu, sikuwa natambua kama lipo jibu la uhakika hapa duniani, sasa nimelipata jibu baada ya rafiki yangu kunikaribisha hapa kanisani nikakutana na mtumishi wa Mungu na kumuelezea alifanya maombi mazito juu yangu, kumbe mwanangu wanataka kumfanya msukule…” alishindwa kuendelea kuzungumza yule mama akaanza kulia akapepesuka akataka kuanguka chini mara akadakwa na watu waliokuwa wameandaliwa kwa shughuli hiyo.

    Sijui huwa wanaambiwa kabisa kuwa ataanguka!!!!

    “Bwana apewe sifaaaa” alipaza sauti mtumishi wa Mungu.

    “Ameeeeeeen!!!” walijibu kondoo wa bwana kwa sauti kuu. Mtumishi akapiga hatua kwenda kushoto kisha akaenda kulia halafu akarejea katikati, tabasamu pana likiwa mdomoni mwake, akatoa kitambaa chake cheupe akajifuta jasho usoni halafu kwa madaha akaliondoa koti lake, akatokea mtumishi mwingine akawahi kulipokea na kulihifadhi mahali salama.

    “Bwana apewe sifaaaa!!!!”

    “Aminaaaaaa”

    “Nilivisikia vyombo vya habari vikitangaza juu ya kupotea kwa huyu kijana nani nani!! Michael Msombe, kwa akili za kibinadamu wakasema huenda ameliwa na simba mara ameuwawa, nilicheka sana, hadi nikatokwa machozi. Mungu alizungumza na mimi, Mungu aliniambia ipo siku atawaonyesha ukweli kupitia mimi na hiyo siku ni leo, Bwana asifiweeee!!!!”

    “Ameeeeen!!!” watumishi walijibu kwa pamoja shairi hili lililokaririwa hata na wale malaya na majambazi. Shairi ambalo halikuwa na maana tena bali kwa wale wachache wenye imani thabiti. Shairi lililotumika kuwalaghai wenye shida.

    “Ndugu zanguni uchawi upo lakini katika jina lililo kuu jina la bwana hauwezi kusimama, mama aliwahi sana kutoa taarifa nipo napambana na hao wafalme wa Jehanamu, hawawezi tena kumfanya Michael kama wanavyotaka. Bwana anamuhitaji sana Michael kuliko wao wanavyomuhitaji haleluya haleluya!!!” alitia nakshi hizo mchungaji huyu ambaye tayari alikuwa ametumbua zaidi ya shilingi laki nane za mama huyu mjane, mama aliyekuwa yupo katika jitihada za kumsaka mwanae wa pekee, Michael Msombe.

    Maneno ya mchungaji huyu yalikuwa matamu lakini hayakuonyesha tumaini lolote lililo hai. Mama yake na Michael taratibu akaanza kuingiwa wasiwasi lakini hakuwa na jeuri ya kumtamkia mchungaji.

    Siku hiyo ya kutoa ushuhuda ndiyo siku ambayo waandishi wa habari nao walizinasa taarifa za mchungaji huyo wa kilokole kuthibitisha kuwa Michael amechukuliwa msukule. Bila kufanya utafiti magazeti ya udaku yakaandika, ilikuwa imepita miezi mitano tangu yaandike juu ya kupotea kwa wanachuo wawili Joyce na Michael katika mazingira ya kutatanisha. Polisi kama kawaida walitoa jibu la upelelezi unaendelea, upelelezi ambao haukupata ufumbuzi.

    “MICHAEL APATIKANA!!!!”

    “MWANACHUO ALIYECHUKULIWA MSUKULE AFUFULIWA NA JK”

    “MAAJABU YA NANE YA DUNIA!!! JK AFUFUA MTU”

    Vilikuwa baadhi ya vichwa vya magazeti!!!

    Taarifa hizo za magazeti ziliamsha akili katika familia ya akina Joyce jijini Dar es salaam, baada ya tafakari ya muda mzee Keto alipuuzia na kuona ni jambo lisilowezekana kumrejesha Joyce kwa maombi, jawabu hilo likakubaliwa na watoto wake wawili pamoja na mdogo wake.

    Alikuwa mama yake Joyce aliyeitwa Mariana ambaye hakukubaliana na jambo la kupuuza ushuhuda wa yule mama juu ya kupatikana kwa Michael, siku iliyofuata na yeye alifunga safari hadi Mwenge kumtembelea mchungaji huyo aweze kumueleza shida yake.

    Mariana alikuwa amejaliwa mwili mzuri sana, licha ya umri wake wa miaka arobaini na tatu (43), bado urembo wake ule wa enzi za usichana wake ulikuwa unaonekana. Alikuwa ni mwanamke wa mjini haswaa. Alivijua vipodozi na aliujali mwili wake, ilikuwa vigumu sana kuamini kwamba Joyce Keto alikuwa mtoto wake wa kumzaa.

    “Naitwa mchungaji Komanya!!”

    “Naitwa Mariana”

    “Bwana asifiwe!!”

    “Emen!!”

    Baada ya kusalimiana Mariana akiwa na mchungaji Komanya, alianza kujieleza shida iliyokuwa inamkabili, alisimulia jinsi Joyce Keto alivyopotea katika mazingira ya kutatanisha. Wakati wote aliokuwa anasimulia Mchungaji Komanya alikuwa anafumba macho na kuongea lugha zisizoeleweka huku akijipigapiga kifuani na kitabu cha dini alichokuwa ameshikilia.

    Mariana alipomaliza kujieleza, Komanya alifumba macho yake akaanza kusali kwa lugha za ajabu kisha akamsogelea Mariana na kumuwekea mkono juu ya kichwa chake. Akamwombea kwa dakika kadhaa kisha akaketi.

    “Mungu hakunipa macho ya kuona mbali, ila alinipa masikio ya kusikia vilio vyenu, ndugu zako wamekupinga sana, mume wako, watoto wote wameukataa ukweli, wewe ni jasiri sana!!!! Ooh!! My my my my!!!” Komanya alizungumza kwa hisia, Mariana akashtuka kwani alikuwa anaambiwa ukweli uliotokea nyumbani kwake.

    Imani ikajengeka!!! Matumaini ya kumpata mwanaye yakarejea!!!

    “Kwa kuwa familia haijakuunga mkono basi Mungu atafanya kitu juu yao, usiwashirikishe lolote hadi pale vitendo vitakapozungumza!!! Nakuhitaji kesho kutwa saa mbili usiku, lazima tufanye sala ya pamoja sala ya kuzivunja ngome za shetani!!!”

    “Hamna shida baba mchungaji!!” alinyenyekea Mariana.

    “Mungu akutangulie!!!! Nenda na amani!!” alimbariki akaondoka zake.



    ********



    Kanisa la Familia ya furaha, lilianzishwa kama sala ya familia jioni ambapo familia mbili zilikuwa zinakutana kwa maombi ya mwisho wa juma, familia mbili zikazaa tatu, nne na kuendelea hatimaye wakaamua liwe kanisa. Hapakuwa na mchungaji, bali zilikuwepo zamu za kuongoza ibada. Kila familia ilikuwa inatoa muwakilishi wa kuongoza ibada kila mwishoni mwa juma.

    Familia nyingi zikavutika na hatimaye wakaweka mahema kwa ajili ya kuwa wanafanyia ibada.

    Hapakuwa na kiwango cha sadaka bali michango ya hapa na pale. Kila kitu kilienda juu ya mstari.

    Familia ya mzee Komanya, ilikuwa na furaha sana katika wiki hii ya uwakilishi kwani tangu kanisa lianzishwe hawakuwahi kuweka mwakilishi mwanao wa pekee aitwae Jacob alikuwa masomoni nchini Nigeria ambapo alipelekwa kwa udhamini wa kanisa la Kirutheri.

    Siku hii mtoto wao alikuwa ndiye anayekwenda kuwakilisha. Wazazi wake walikuwa wamewatangazia watu wengi sana juu ya tukio hilo la mtoto kusimama mbele ya madhabahu.

    Siku ilifika umati ukawa umefurika, Jacob Komanya akasimama mbele ya jukwaa, sauti yake ikatikisa ngoma za waumini, mahubiri yake yakawavuta wapita njia, maombi yake yakawagusa wenye shida. Mkono wake ukawaangusha watu wenye mapepo. Madhabahu yakawa hayatoshi baada ya ibada kila mmoja alihitaji kumshika mkono. Jacob Komanya akageuka shujaa.

    Wazazi wake walishangazwa sana na uwezo wa mtoto wao. Siri alibaki nayo yeye mwenyewe!!!!

    Siri ya nguvu za giza, nguvu zenye masharti, masharti ya kuzini na wasichana wawili kila baada ya siku moja bila kuwarudia tena, masharti ambayo yaliziimarisha nguvu zake. Masharti yaliyomfanya JK aheshimike!! Masharti yaliyomuwezesha kuwa na sikio kali linalosikia mbali,

    Sikio kuu la kishetani!!! Sikio lililofanya watu waogope kumsema vibaya kwani alikuwa akiwasikia yote waliyosema.

    JK akapata heshima jijini Dar Es Salaam!!!

    Baada ya mwezi mmoja akateuliwa kuwa mchungaji mkuu, hakukawia kujipatia ‘a.k.a’ akajiita Mtume JK. Kanisa likatanuka upesi, wakajenga Mwenge kanisa kubwa ni huku Mama yake Michael na Mariana (mama Joyce) walizipeleka shida zao.

    Mama Michael umri ulikuwa umekwenda hivyo aliponea chupuchupu lakini Mariana alimvutia JK, akaingizwa rasmi kwenye hesabu.

    Masikini Mariana hakuyajua yote haya!!!



    ****



    Joram aliondoka pale nyumbani kwa Matha akiwa na tabasamu kubwa sana. Aliamini kwa karata ile kamwe hawezi kumkosa Matha katika futi sita kwa sita.

    Matha naye alibaki katika wakati mgumu sana.

    Wanaume watatu aliokuwanao katika mapenzi aliamini walikuwa wengi sana na lazima wangemuumiza kichwa sasa alipofikiria suala la kuongeza tena wa nne akili iligoma kabisa. Lakini alipofananisha matokeo, aliamua kumkubalia Joram.

    Sasa nikikataa halafu akimwambia John itakuwaje!!!, hakika bado sijajipanga kutoroka, na kumtoroka John sio suala dogo kabisa!! Moyo wa chuma ulihitajika kufanya jambo hili!! Litakalokuwa na liwe!!! Aliamua Matha. Akaichukua simu yake akampigia Joram.

    “Nimekubali lakini….”

    “Usijali nitaitunza siri kama kawaida yangu!!”

    Matha alizishangaa akili za Joram maana kila alipotaka kuzungumza tayari alishatambua neno la mwisho. Akazishusha pumzi, akatweta akamuaga Joram kiunyonge na kisha akakata simu!!

    Matha alipitiwa na usingizi na alipoamka alijishangaa kwamba yupo katika uhusiano na wanaume wanne, hakuwa na wasiwasi juu ya magonjwa lakini aliiangalia mimba yake iliyokuwa na miezi mitatu huku bado ikiwa ni mimba ya hisia kwani ilikuwa haionekani. Akajipiga piga kisha akatabasamu, akaifunga kanga yake vizuri akaingia bafuni, akaoga. Akarejea na kujiandalia stafutahi, chai ya rangi na kiporo cha wali akakipasha moto.

    Akastafutahi kimya kimya kwa amani finyu moyoni!!!

    Baada ya stafutahi akapokea ujumbe kwenye simu yake.

    “Baby kwa hiyo leo tunaonana!” ilikuwa namba ya Joram. Matha akahamanika, akamwona Joram kama anayevuka mipaka mapema akampigia akiwa na hasira, mkononi alikuwa ameshikilia fagio.

    Najua upo peke yako ndo maana nimetuma ujumbe huo!!!” aliwahi kuzungumza Joram. Matha hakuwa na la kusema akawa anahema juu juu.

    Joram akacheka kisha akakata simu!!

    Matha akaghairi kufagia akaenda bafuni, akataka kuoga akakumbuka tayari alikuwa ameoga, akapiga kite cha ghadhabu akatoka bafuni.

    Alipotoka akampigia simu Adrian ili waweze kuonana, alihitaji kuilazimisha furaha yake lakini bado alikuwa na simanzi, kuonana na Adrian ndio lilikuwa suluhisho pekee.

    Adrian alipeana na binti huyu miadi ya kukutana jioni.

    Majira na ya saa kumi jioni Matha alikuwa anaelekea kukutana na Adrian, akiwa ndani ya taksi, mara simu ikaita alikuwa ni Joram. Almanusura asipokee lakini alihofia kumkera mtu ambaye alikuwa ameishikilia dhamana ya amani yake.

    “Yes!! Joram”

    “Nipo hapa Golden Crest Hotel chumba namba 104 naomba uje”

    “Kufanya nini sasa hivi?” alihoji Matha. Joram hakujibu akakata simu. Matha akaumiza kichwa akawa katika jitimai la nafsi, hatia ikaanza kumtesa tena. Hatia aliyoamini Minja ameondoka nayo kwenda mkoani Singida sasa ilikuwa imerejea kwa kasi ya tofauti tena kwenye mikono ya mtu ambaye si wa lelemama. Mikono ya Joram!!!

    Matha akapiga akili ya haraka haraka, akaamua kumtumia ujumbe Adrian kuwa amepata udhuru wataonana baadaye, baada ya Adrian kuelewa japo kwa shingo upande alimpigia simu Joram akamwomba amuelekeze ni wapi anapoishi. Joram kwa sauti ya ujivuni akampa maelekezo Matha!! Baada ya maelezo aliondoka pale Golden Crest na kurejea nyumbani kwake.

    Baada ya nusu saa Matha alikuwa katika kitanda kimoja na Joram, hakupata raha yoyote ile kwani alikuwa na wasiwasi muda wote!!!

    Joram pekee ndiye alifurahia.

    “Joram pliz….”

    “John hatagundua usijali” alimalizia Joram, Matha akawa amemzoea na hizo tabia zake za ajabu.

    Baada ya kuoga akaaga na kuondoka!!!

    Safari ya kwenda kwa Adrian!!

    Alipokuwa na Adrian muda wote alikuwa amekilalia kifua cha Adrian, alijisikia amani sana katika mikono hii, alilia sana Adrian akawa anambembeleza, hakujua kwa nini malaika wake huyu alikuwa analia sana, hakujiuliza sana alichohakikisha ni kuwa anambembeleza.

    Usiku huo aliupitisha akiwa na Adrian, tayari alikuwa amemdanganya John Mapulu kwa njia ya simu kuwa alikuwa ameenda kumsalimia dada yake maeneo fulani nje kidogo ya jiji.

    Utu wa Matha ukawa unashuka kwa kasi sana alijiona kama hana umuhimu tena. Mtoto wake aliyekuwa tumboni pekee ndiye aliyebakia kuwa na umuhimu mkubwa.

    Umuhimu wa mtoto wake ndio ulisababisha apitie matatizo hayo laiti kama angekuwa hana umuhimu angeweza kuwa ameitoa mimba hiyo na kubakia bila msongo wowote wa mawazo.

    Matha akawa amefanya mapenzi na wanaume wawili, tena katika tofauti ya masaa machache.

    Matha alijua Joram kishaonja asali atataka kuchonga mzinga. Wakati anarejea Buzuluga nyumbani kwake wazo la kutafuta muafaka likamjia wazo kuu likawa ni kuua. Matha akanuia kumpa onyo lisilokuwa na nafasi ya pili kijana Joram.

    Roho ya kuua ikamwingia!!!

    Teksi ilimshusha, akalipia na kuingia ndani ya chumba chake!!

    Akalala!!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ****



    Michael alikuwa katika matembezi yake ya hapa na pale nje ya nyumba ya John, alikisogelea kibanda kinachouza magazeti akaanza kupitia vichwa vya magazeti mbalimbali.

    Macho yake yakavutiwa na gazeti la Ijumaa wikienda. Kichwa cha habari kilimshawishi akatoa pesa na kununua gazeti lile. Akarejea ndani upesi kwenda kuisoma habari ile. Kwanza alishtushwa na picha iliyofanana na mama yake, baadaye haikuwa inafanana alikuwa ni yeye na habari ilikuwa inamuhusu Michael mwenyewe, habari kwamba alikuwa amewekwa msukule na alikuwa ametambuliwa na Mtume maarufu jijini Dar kwa jina la JK yaani Jacob Komanya.

    Machale yakamcheza Michael, mchezo mchafu wa kitoto!!!! Alisema Michael huku akilazimisha tabasamu. Tabia za ajabu ajabu zilikuwa zimemuathiri na maneno ya John yalikuwa yamemkaa akaamini kuwa huo ulikuwa ni mchezo wa kumtia hatiani kirahisi.

    Kwa kipindi kirefu sana, Michael akawa amekumbuka kifo cha mwanadada Joyce Kindo ambaye alifia nyumba ya kulala wageni!!!

    Sikamatwi kirahisi!!! Alimaliza kwa kusema kisha akalihifadhi lile gazeti kwa ajili ya kuwaonyesha akina John pia!!!

    Hakuwa na wasiwasi!!!



    *******



    Mariana alirejea nyumbani akiwa na matumaini tele aliamini kuwa hatimaye alikuwa amepata suluhisho sahihi la kumrejesha mwanaye katika mikono yake.

    Hakumshirikisha mtu yeyote kama alivyoshauriwa na mchungaji JK baada ya maombi. Alibaki kimya akiisubiri hiyo siku ya miadi iweze kufika aonane na mchungaji kwa ajili ya maombi mazito. Kila mara alimuombea afya mtumishi huyo wa Mungu asiweze kukumbwa na lolote baya.

    Siku ya kwanza ikapita hatimaye siku ya siku ikafika!! Mariana akajiandaa na kumuaga mume wake kuwa anaenda kwa mama yake mdogo, mzee Keto hakupinga lolote alimuamini sana mke wake akampa ruhusa.

    Mariana akaelekea nyumbani kwa Mchungaji Jacob Komanya.



    Mariana alipishana na msichana rika la Joyce ambaye ni mwanae akitokea nyumbani kwa mchungaji majira ya saa moja na nusu. Yaani nusu saa kabla ya muda aliokuwa ameahidiwa na mchungaji kuwa wakutane.

    “Bwana asifiwe…mchungaji yupo!!” Mariana alimsalimia na kuuliza. Yule binti alimkazia jicho la wasiwasi kisha akamuuliza, “Una shida naye??”

    “Ndio nina miadi naye!!” alijibu

    “Mh!! Haya yupo wala hakuna mtu zaidi ya mlinzi mlangoni…kaombewe” alijibu kwa sanifu kisha akaondoka.

    “Mh!! Atakuwa na mashetani huyu!!! Haleluya bwana niepushe na roho hawa wachafu!!” alikemea mwanamke huyu aliyekuwa amevaa nguo sawa kabisa na wanawake wa nchini Nigeria.

    Taratibu akagonga geti na kufunguliwa mlango, mlinzi alikuwa bado anamkumbuka hivyo hakumuwekea kipingamizi. Haraka haraka akatembea na kuufikia mlango, akaugonga akatokea mchungaji akamfungulia.

    “Oooh!! Glory be to God, Mariana ni wewe!!! Bwana apewe sifa”

    “Ni mimi ameeen!!!” alijibu Mariana. Uso wa mchungaji haukuwa na furaha ya kweli na alikuwa na wasiwasi.

    Mariana hakujua kuwa binti aliyepishana naye nje ya geti alikuwa ametoka kulazimishwa kufanya mapenzi na mchungaji Komanya. Lakini mashetani yake yaliwazidi ujanja mashetani wa Mchungaji hivyo hakufanikiwa.

    Jacob Komanya, alikuwa katika mtihani mkubwa sana kwani kwa siku hiyo alikuwa amefanikiwa kuzini na msichana mmoja pekee jambo ambalo lilikuwa kinyume na masharti aliyopewa nchini Nigeria wakati akiwa masomoni.

    Mariana hakuwa na kiburi cha kumuuliza lolote JK, aliingia ndani. Akakaribishwa kinywaji akaachwa peke yake sebuleni. Baada ya muda mrefu kidogo mchungaji alirejea alikuwa amevaa suti nyeupe iliyoukamata mwili wake vizuri. Mguuni alikuwa amevalia kiatu cheupe aina ya ‘four angle’, kifuani alikuwa na cheni nzito iliyotengenezwa kwa madini ya dhahabu, ndevu zake zilizochongwa katika mfumo wa herufi O zilimfanya apendeze sana, Mariana alikiri unadhifu huo kimya kimya.

    “Tunaweza kwenda Mariana!!” JK alizungumza Mariana akasimama na kumfuata.

    JK hakumuaga mlinzi zaidi ya kuwasha gari na mlinzi kufungua geti. Ndani ya gari la kifahari aina ya Hummer, Komanya alikuwa anaendesha mwenyewe, Mariana alikuwa kushoto kwake ametulia tuli huku akijaribu kupitia maandiko hapa na pale.

    Tayari ilikuwa saa tatu usiku!!!

    Gari lilikuwa katika mwendo wa kawaida kutokana na foleni za hapa na pale lakini baada ya kuiacha Mbezi mwisho, mwendo uliongezeka kidogo hadi liliposimama maeneo ya Kibaha.

    Mchungaji alichukua kichupa kidogo kilichokuwa kimehifadhi utuli, akajipulizia kidogo kisha akatabasamu, Mariana naye akajibu kwa tabasamu lakini hilo lilikuwa tabasamu la mwisho kabla ya pepo la ngono halijampanda mama huyu, alijikuta anarembua macho yake, aibu zilikuwa mbali naye, alijisogeza karibu na mchungaji.

    “Jacob nahisi baridi!!!” alisema kimahaba, JK akatabasamu na kuifanya ile staili yake ya kunyoa ndevu kuonekana vizuri!!

    Hakujibu kitu badala yake aliwasha gari na kuendesha umbali mfupi. Akalifikia bango dogo lililoandikwa Kibaha Yetu Lodge, akakata kulia na kukanyaga mafuta tena akawa ameifikia nyumba hiyo ya kulala wageni.

    “Karibu baba!!!” alipokelewa kwa shangwe.

    “Nilipiga simu, mmepewa maelekezo tayari!!!” aliuliza.

    “Ndio chumba namba 18 kipo tayari!!!” alijibiwa na msichana aliyekuwa muhudumu wa pale.

    “Naona upo na mama mchungaji!!!” alitania yule binti!! JK akacheka kwa staha, Mariana akajisogeza karibu yake akamshika kiuno wakaelekea chumba walichoelekezwa.

    Haikuwa mara ya kwanza kwa mchungaji huyu kufika eneo hili!!!

    Bila kujitambua Mariana akazini na mchungaji, bila shaka hiyo ndio ilikuwa sala ya kumuombea Joyce Keto huko alipo aweze kurudi. Fahamu zilimrudia Mariana wakati wakiwa wamemaliza kufanya tendo, alimkasirikia sana mchungaji lakini JK hakuzungumza kitu zaidi ya kumwambia.

    “Nenda ukatangaze na ndoa yako ivunjike!!!” maneno hayo yalikuwa kama kisu kikali kwa Mariana, yalipenya kama ubaridi na kisha uchungu ukalipuka akaanza kulia, mchungaji akacheka kwa sauti ya juu kidogo huku akivaa nguo zake. Kicheko hicho kikawa shambulizi baya kwa Mariana akajiona amebakwa katika mazingira ya ajabu tena uzeeni.

    Akaondoka haraka haraka pale chumbani akiwa na akili ya kurejea jijini Dar es salaam. Alipofika barabarani akagundua kuwa hakuwa na nauli, mwenyeji wake alikuwa ni Jacob Komanya peke yake eneo lile. Mariana hakuwa na namna nyingine akarejea kwa aibu kubwa sana akakutana na JK anatoka mapokezi kukabidhi chumba.

    “Ulitaka kurejea Dar kwa miguu” aliuliza kwa dharau kuu JK, Mariana akapatwa na kigugumizi cha kujibu. Jacob Komanya akatoa pochi yake ya rangi nyekundu na nyeupe akachomoa noti sita zenye rangi nyekundu. Akawa amempatia Mariana shilingi elfu sitini za kitanzania.

    “Nahitaji elfu mbili tu!!” alileta jeuri Mariana huku akishindwa kumkazia macho mchungaji!!!

    “Na hiyo ya kutoa mimba atakupatia mume wako??” Jacob aliuliza swali lililomshtua Mariana, akawa amezidiwa ujanja alitamani kupiga kelele lakini hakuwa na ushahidi wa kumwezesha kufanya hivyo.

    Akasonya kwa hasira na kisha akajiondokea!!! Huku nyuma JK akacheka kidogo halafu akasikika akisema, “Naenda hapo Mlandizi kwenye maombi!! Twende wote basi!!!”

    Mariana hakugeuka!!!



    Mariana hakuweza kurudi nyumbani kwake kwani alikuwa amemuaga mume wake kuwa atachelewa sana kurejea hivyo aliamua kuchukua chumba katika nyumba za kulala wageni. Hakuwa na hamu ya chakula alilala hivyohivyo!!!

    Saa nne kamili asubuhi alifika nyumbani kwake, hakukuta watu zaidi ya mfanyakazi wa ndani alisalimiwa lakini hakujibu salamu hiyo, akaingia mpaka chumbani akajifungia.

    Punde tu baada ya kuufunga mlango, alianza kuisikia nafsi yake ikitamka neno HATIA, akajiuliza lina maana gani kwa wakati huo, macho yake yakatua katika mkono wake, akakutana na pete ya ndoa, kumbukumbu ya usaliti ikamchukua na kumlegeza akakaa kitandani bado alikuwa anaiangalia pete ile. Picha ya Mchungaji JK akiwa anatabasamu ikajijenga mbele yake, Mariana akauma meno kwa uchungu, kisha akazivuruga nywele zake, uchungu ukapita kipimo. Akapatwa na hasira kali chuki nayo haikubaki nyuma lakini hatia ya usaliti ndio ilitawala kichwa chake.

    Mzee Keto na upendo wake atanielewaje?? Alijiuliza Mariana, mara bila kutegemea, ule uasili wa kabila lake uasili usioaminiwa na watu wengi lakini ni uasili wa asili, uasili wa kurithi kutoka kwa chifu Mkwawa, ‘kuliko kudhalilika heri kufa!!!’, Mariana akajikuta akiwaza kujiua tena kwa kujinyonga. Maneno machache yalichafua karatasi, kanga yake ilimtosha kabisa muhehe huyu, Mariana akajinyonga chumbani mwake!!!

    Hasira, mfadhaiko na uasili ukawa umemuua Mariana. Hatia yake ilikuwa nzito kujibu kuliko kuikwepa. Mariana kitanzini akapanda na hatia yake.





    Kundi dogo la vijana lilikuwa limemzunguka kijana mwenzao ambaye alionekana kuwa katika hali tofauti kidogo ya maisha, walikuwa wanakunywa pombe huku wakilikubali kila jambo ambalo alikuwa akilisema kijana huyu.

    Alikuwa amevaa nguo zilizoonekana kuwa mpya lakini kwake hazikumkaa vyema, tumbo lake liliinyanyua shati yake na kuifanya kuwa fupi jambo ambalo liliruhusu mgongo wake kuonekana. Nywele zake zilizotoka kunyolewa siku kadhaa nyuma zilikuwa zinameremeta. Alikuwa anatoa noti kadhaa na kumlipa muhudumu, vijana wenzake walinyanyua glasi zao juu na kuzigonganisha ishara ya kumsifia, hakuna ambaye alikuwa amelewa.

    Mfukoni alikuwa na shilingi laki moja na nusu, elfu hamsini pungufu ya pesa alizokuwa amekuja nazo eneo lile la Villa Park akiwa ametokea nyumba ya kulala wageni aliyokuwa amehamia.

    Huyu alikuwa ni Defao akiwa ameisahau familia yake, akiwa amemsahau hadi Minja aliyekuwa amempa dili hilo. Defao alikuwa anaijaribu ladha tamu ya pesa, hakika ilikuwa tamu sana na ni ladha hiyo ambayo ilimuweka jijini Mwanza kwa siku kadhaa mbele.

    Heshima yake katika eneo la Villa Park ilikuwa juu sana, siku hiyo hiyo alipata mpenzi, akaondoka na kwenda kulala naye katika chumba alichokuwa amefikia. Ladha hiyo ya umaarufu ikamsahaulisha mengi akaisahau hatia yake ya kumdhulumu Minja mgao wake, pia hatia ya kuitelekeza familia yake ilikuwa imeenda likizo hakumkumbuka mgonjwa aliyekuwa mahututi. Defao alipachikwa jina la Papaa Defao na wanamuziki wa bendi baada ya kuwa amewatunza mara kwa mara katika nyimbo zao.

    Sifa zikaongezeka akapata wapambe.

    Kila penye wengi kuna jambo!!!

    Na hakuna rafiki mbaya kama rafiki anayepatikana wakati mtu ana pesa.



    ****



    Alidamka asubuhi akajikwatua na vipodozi mbalimbali akiwa mbele ya ‘dressing table’, akajigeuza huku na huko akauthaminisha urembo wake, akatabasamu.

    Alikuwa amependeza!!!

    Honi iliyopigwa ndio ilimkurupua kutoka pale na kuchukua mkoba wake mbio mbio akaanza kwenda nje, alipoifikia gari aliifuata ‘side mirror’ ya upande wa kulia mwa gari akautazama uso wake ambao ametoka kuuangalia sekunde chache mbele ya kioo kikubwa.

    “Mh!! Wasichana mna mambo?? Sasa huko ndani hujakiona kioo au” alizungumza kwa utani mwanaume huyu huku akiungurumisha injini ya gari yake, msichana huyu akajibu kwa kucheka huku akiweka sawa papi za mdomo wake kwa kuziumauma.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya hapo mwanaume huyu aliyekuwa amejiwekea hifadhi yake ndani ya suti nyeusi iliyokuwa ya hadhi ya juu alimfungulia mlango binti akajitosa ndani ya gari na kuubamiza mlango ukawa umejifunga.

    Kabla yule binti hajafika marashi ya yule mwanaume yalitawala ndani ya gari lakini kufika kwa yule binti kulivunja utawala wake, utuli wa yule binti ukachukua nafasi. Geti likafunguliwa John Mapulu akawasha gari, ilikuwa ni safari ya kumpeleka Joyce Keto kliniki ambayo aliamua amuandikishe hospitali ya Agha Khan ya jijini Mwanza kwani huduma zake zilikuwa nzuri sana tofauti na hospitali za serikali.

    Zoezi hilo liliwachukua muda wa nusu saa baada ya kufika. Joyce akapewa ratiba ya kuwa anahudhuria kliniki. John akaahidi kuwa anamleta kila siku iliyopo kwenye ratiba. Joyce akashukuru wakarejea nyumbani.

    Wazo la Joyce kuwatafuta ndugu zake halikuwepo hata kwa mbali, sumu aliyokuwa amepandikiziwa na John ilikuwa imeathiri akili yake na kujihisi hapo alipo ndio mikono salama zaidi na si kwingine.

    “Mh!! Mhehe ajiua, hawa nao kwa kutuandama!!!” alisema Joyce wakati huo gari ipo kwenye foleni, baada ya muuza magazeti kupitisha katika dirisha lililokuwa upande wake.

    “Hah!! Kumbe muhehe wewe mh!!” aliuliza John, Joyce hakujibu!!!

    Alitoa noti ya shilingi elfu tano, muuza magazeti hakuwa na chenji hiyo, na John naye hakuwa na pesa ndogo, mataa yakawa yameruhusu gari likaondoka.

    Joyce hakufanikiwa kununua gazeti lile, alitegemea atanunua mbele ya safari, akasahau hadi wakafika nyumbani.

    John akamuaga Joyce wakaahidiana kuonana jioni!!

    Laiti kama angefanikiwa kuisoma habari iliyokuwa kwenye gazeti basi angetambua kifo cha mama yake mzazi katika harakati za kumwokoa.



    *****



    Penzi alilopewa Adrian na Matha kwa mara ya pili lilikuwa bora kuliko lile la kwanza alisahau kabisa suala la ndoa yake na Monica, akawa ameamua kujizatiti kwa mpenzi wake huyu wa zamani hizo.

    Na ili ampate ilikuwa lazima na yeye amdhulumu John Mapulu. Atamdhulumu vipi?? Hilo ndio lilikuwa swali gumu.

    Nina pesa!!! Pesa ndio kila kitu!!! Nitamrejesha Matha kwangu. Alipata muafaka Adrian. Wakati huo alikuwa amerejea nyumbani kwake baada ya polisi kuwa wamekamilisha upelelezi wao dhaifu kama kawaida na siku hiyo hakuwa ameenda kazini kwani msaidizi alikuwa ametangulia tayari.

    Hatia ya kumsababishia Monica kubakwa ilikuwa imesahaulika, sasa alikuwa anaingia katika jaribio la kurejesha kile kilicho bora kwake.

    Adrian akafikiria kutumia pesa aliyokuwanayo kumpa John onyo, kumpa maumivu makali kama ambayo aliyapata yeye baada ya John kumpokonya tonge mdomoni. Hasira ikamsababishia kukihesabu alichotaka kukifanya kuwa kisasi halali.

    Akanyanyua simu yake akapiga namba fulani simu ikapokelewa.

    “Za siku kaka!!!”

    “Poa ndugu yangu, nina shida kidogo”

    “Nini tena??”

    “Namuhitaji Nunda”

    “Kuna mshenzi gani amekusumbua??”

    “Yupo mpuuzi nahitaji kumpa somo!!!”

    “Tuonane mchana dukani kwako”



    Adrian alikubali na kukata simu, akasimama na kuongoza mwili wake bafuni, akaoga kisha akajiandaa akaelekea Makoroboi kwa usafiri wa daladala.

    Mida ya mchana akafika rafiki yake wa shule ya msingi aliyeitwa Mark ambaye aliacha shule kitambo na kujiingiza katika vitendo vya kihuni. Alikuwa ameambatana na mwenzake.

    Adrian alitoa maelekezo yote, akaeleweka, kisha akawatajia jina la muhusika kuwa ni John Mapulu.

    “Nahitaji apigwe na apewe onyo la kuachana na mke wake!!”

    “Laki tano unusu!!” alitaja bei

    Adrian akakubaliana nayo akatanguliza nusu.

    Akawa ameingia rasmi katika vita ya kumgombea Matha!!!! Msichana aliyeamini kuwa aliumbwa kwa ajili yake.



    ****



    Baada ya siku mbili Adrian alipigiwa simu na Mark kuwa mambo yanakaribia kuiva hivyo wanatakiwa kukutana kwa ajili ya makubaliano ya mwisho baada ya utafiti.

    Adrian alijiona mshindi katika vita hii, akaacha shughuli zake na kufuata maelekezo, walikutana maeneo ya Nata, Adrian akaelezwa kwamba alitakiwa akutane na Nunda mwenyewe ili aweke kiapo cha siri. Adrian hakusita akakubali, hamu yake ilikuwa kumuona Matha akiwa huru ili aweze kumtambulisha kwa wazazi wake badala ya Monica.

    Walipanda daladala zinazoelekea Nyakato Sokoni ndani ya jiji la Mwanza, kila mtu alikuwa kimya hadi pale abiria mmoja aliposhtuka na kupiga kelele kuwa ameibiwa simu yake. Alikuwa ni mwanamama aliyekuwa na heshima zake kabisa kila mtu alimuamini, na jambo la kushtua zaidi ni pale walipojaribu kuipiga namba yake ikaita mara moja na kisha simu ikazimwa.

    “Sikubali mimi simu ya mume wangu jamani halafu mwizi yupo hapa hapa ndani sikubaliiiiii….” Alilia kwa uchungu yule mama kila mmoja akawa anamuonea huruma.

    “Dereva ingiza gari kituoni huu ushakuwa ujinga sasa!!! Mnawachekea sana na mnawajua” abiria mmoja aliyekuwa kimya muda mrefu alitoa tamko hilo, akaungwa mkono na wengi, taratibu daladala ikakata kushoto ikaingia kituo cha polisi maeneo ya mabatini. Abiria wasiokuwa na hatia walilalamika sana kupotezewa muda lakini je utajuaje huyu ana hatia na huyu yu salama.

    Gari lilipofika pale alishuka dereva peke yake, akaenda mapokezi na kutoa shtaka hilo, askari wawili wa kiume na watatu wa kike walipewa jukumu hilo la kukagua kila mmoja ili simu iweze kupatikana.

    Mark hakuwa na wasiwasi alikuwa akizungumza na Adrian kwa sauti za kunong’oneza, wote walikuwa na furaha.

    Askari aliamuru abiria wote kutelemka, likaanza kusachiwa gari, hakikupatikana kitu, baadaye abiria mmoja baada ya mwingine, wasichana kwa askari wa kike na wanaume kwa askari wa kiume. Zoezi halikuwa gumu sana kwani wengi wao hawakuwa na vifurushi. Na waliokuwa na vifurushi hawakuwa na dalili ya kuwa wezi wa hiyo simu, ndio hivyo alivyochukuliwa Adrian, kati ya abiria waliokuwa nadhifu basi alikuwa ameongoza. Kuanzia juu mpaka chini alikuwa anashawishi macho kumtazama.

    Kifurushi chake kidogo kilipekuliwa kwa wepesi. Askari hakuamini alichokiona, yeye pamoja na mwenzake wakajikuta wakihamaki, kutoka katika begi dogo la Adrian tofauti na uwepo wa pesa kulikuwa na risasi nne. Adrian hakuwa akiifahamu risasi ilivyo hivyo alibaki kutabasamu tu, harakaharaka akashangaa amerukiwa na askari mmoja akamnasa vibao halafu akamtia pingu mikono ikiwa kwa nyuma.

    Abiria waliruhusiwa kuondoka.

    Simu ilikuwa haijaonekana.

    Mark kama vile hamjui Adrian na yeye alitoweka!!

    Adrian matatani!!!



    Adrian aliingizwa katika chumba cha mahabusu akiwa haelewi nini kinachoendelea, safari yake aliyotegemea ya kwenda kumkomoa John Mapulu sasa ilikuwa imemgeukia yeye. Wasiwasi ukamtawala, ilikuwa mara yake ya pili kuingia katika mahabusu tena mara ya kwanza ilikuwa utotoni ambapo walikamatwa siku ya mkesha wa sikukuu ya krismasi wakiwa wanazurura. Hapo ilikuwa baada ya kuwa wametoroka kanisani.

    Asubuhi waliruhusiwa kurejea makwao. Hapakuwa na kesi na wala hawakupigwa makofi kama aliyokumbana nayo hapa.

    Wasiwasi ukazidi nguvu ushujaa wake, akafadhaika!!!

    Baadaye sana aliruhusiwa kupiga simu nyumbani kwao. Mzee Mhina akaipokea, akapewa taarifa, kama kawaida akawa mbinafsi hakumshirikisha mke wake japo alipaliwa na mate baada ya kupewa taarifa hiyo. Hakuyapenda mambo ya polisi kwani aliutambua usumbufu uliopo kule.

    Hakutaka kuendesha gari yake binafsi bali alipanda taksi hadi akafika pale kituoni.

    “Bunduki ya mwanao ipo wapi” askari mpelelezi wa kesi hiyo alimuuliza mzee Mhina wakati akijiweka sawa katika kiti kilichokuwa katika moja ya ofisi.

    “Bunduki!!! Bunduki gani” alihoji huku akishindwa kukaa vyema, alikuwa amekumbwa na mshawasha. Askari hakujibu lolote aliendelea kupeleleza mafaili yake huku na huko, na kupiga mluzi ambao haukuwa wa nyimbo yoyote ile bila shaka alikuwa ameutunga ghafla ili kumburudisha Mhina.

    “Kwani mwanangu amekamatwa kwa kosa gani??”

    “Jambazi!!”

    “Jambazi nani Adrian??” alihamaki. Askari hakujibu akakaa na faili mkononi akamkazia macho mzee Mhina kisha akajilazimisha kutabasamu.

    “Jambazi mwanao ilete hiyo bunduki tumalizane!!” alirudia maelezo yale askari huyu ambae alijulikana kwa jina la Moa. Baada ya kuhamaki sana na kulalamika kuwa hatendewi haki zake za msingi kama mzazi wa mtuhumiwa, Moa alisarenda akamueleza kinagaubaga kila kitu kilivyokuwa na baadaye akaitwa Adrian.

    Alikuwa peku peku, suruali kiunoni ilipakataa na shingo yake ilikuwa imerefuka, kwa masaa kadhaa Adrian alikuwa amekonda!!

    Hakukumbuka kumsalimia baba yake kutokana na hali iliyokuwepo. Aliamriwa kukaa chini kisha akaanza kuulizwa maswali akajieleza kila kitu kilivyokuwa huku akimtaja mara kwa mara Mark!! Lakini hakuisema njama aliyokuwanayo yeye na Mark dhidi ya John Mapulu!!

    Baada ya maelezo kuandikwa alirudishwa rumande dhamana ilikuwa haijatimia kimasharti.

    Kwa siku nyingine akawa amelazwa tena mahabusu.

    Siku iliyofuata ilikuwa jumamosi, mpelelezi wa kesi alikuwa na udhuru hakuja kazini, na siku ya jumapili si kawaida yake kuja kazini.

    Adrian akawa amesalia ndani ya kachumba kadogo ka mahabusu hadi siku ya jumatatu ambapo dhamana ilipitishwa akawa huru.

    Hewa ya uhuru iliyeyusha hofu aliyokuwanayo, japokuwa alinuka sana hakujali alifurahia kuwa huru.

    “Usimweleze mama yako chochote!!!” baba alimwambia mwana, lilikuwa neno la kwanza tangu awe huru!!!

    Adrian alijibu kwa kutikisa kichwa juu na chini mara kadhaa. Macho yake yalikuwa yamevimba bila shaka alipigwa kidogo na wakorofi wa jela aliowakuta pale mahabusu. Mzee Mhina akawasha gari wakaelekea nyumbani kwa Adrian.

    Baada ya kuoga na kupata chai nzito ya maziwa hatimaye kilikuwa kikao cha dharula.

    Baba na mwana!!

    Adrian alimueleza baba yake kila kilichotokea lakini hakutaka kuonekana mjinga mbele ya baba yake huyo aliyemuamini sana. Hakudiriki kumtaja John wala Matha katika mlolongo wa maelezo yake.

    “Una uhakika kuwa hujui lolote kuhusu zile risasi”

    “Nikwambie mara ngapi baba??” alihamanika Adrian, mzee Mhina akashusha pumzi kwa nguvu zote kisha akajiegemeza kichwa chake katika sofa.

    “Nitamalizana na yule mpelelezi japo anahitaji pesa ndefu sana kinyume na hapo ni mahakamani kisha hukumu kwenda jela” Adrian akapaliwa na chai aliyokuwa anaifurahia ladha yake mdomoni!!! Alikohoa sana kabla ya kukaa sawa.

    “Baba mpe hizo pesa mambo ya mahakamani tena aah!!” alilalamika Adrian. Mzee Mhina hakujibu kitu akawa ameaga na kuondoka!!

    Adrian hakuendelea tena kunywa chai, akaingia chumbani akajifungia na kuanza kumlaani Mark kwa kitendo cha kinyama alichokuwa amemfanyia.

    Ina maana alitaka nikafie huko huyu jamaa!!! Alijiuliza huku akikifinyafinya kitanda chake kwa kutumia makucha yake yasiyokuwa na urefu wa kutisha.

    Alilaani kwa kila namna na mwishowe fikra za ajabu ajabu zikaanza kumvaa akamwona Mark kama mnyama tena mnyama wa kutisha aliyefanya mbinu ili ammeze bila taarifa, mnyama asiyekuwa wa kufugwa, alimfikiria amfananishe na simba akagundua ni yeye alikuwa akiitwa simba na baba yake. Akaona jina lake haliwezi kufanana wala kutumiwa na mtu kama Mark.

    Mwishowe akaamua kumfananisha na JITU. Jitu lisilokuwa na utu, jitu ambalo linaipoteza amani kama ukilichekea lakini mwisho wa jitu ni kutumia makali ya upanga.

    Adrian akawa amejawa na fikra za kumteketeza Mark ambaye alikuwa amepewa jina la JITU.

    Wakati huo Matha alikuwa amesahaulika kidogo na John hakuwa kwenye fikra zake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *****



    John baada ya kuachana na Joyce tu, wazo lisilompendeza kabisa lilirejea kichwani mwake, wazo juu ya Adrian Mhina lilimkaba koo. Akasogeza gari pembeni ya barabara akazimisha, akatoa sigara katika koti lake akaipiga kiberiti na kuanza kupuliza moshi hewani kwa fujo, alikuwa anajaribu kukabiliana na ghadhabu iliyokuwa inachukua nafasi yake kwa kasi.

    Uso wa furaha aliokuwanao wakati yupo na Joyce ulikuwa umepotea, chuki ikachukua nafasi.

    John Mapulu akataharuki!!!

    Namuua huyu (……!`~) akamtukania mama yake!!!



    John alikuwa katika hasira zilizomaanisha alikuwa ameamua kumpotezea mbali Adrian kwa jambo alilohisi anafanyiwa naye. Hakuwa mtu wa kuweka ahadi asiyoitimiza.

    Alifanya mikakati yake na kamati yake ndogo. Aliamini kuwa Adrian hakuwa na haki ya kuyaonja mauti bali alitakiwa atikisike kwanza na iwapo ataleta ubishi ndipo iwe adhabu ya mwisho.

    Kwa kumtumia mama mtu mzima aliyekuwa anafanya shughuli za ukahaba pale mjini Mwanza John aliweza kuufanikisha mtego aliopanga kuuweka na aliamini kuwa utanasa.

    Kijana wa kazi Joram alikuwa kazini na mama huyu, walimfatilia Adrian siku hii kwa kila hatua aliyokuwa anaenda moja baada ya nyingine. Walimshuhudia tangu alipotoka nyumbani kwake na kuelekea hadi Nata ambapo walipanda daladala, ni katika mlolongo huo huo Joram alicheza kamchezo kadogo sana kakumzongazonga Adrian kisha kutumbukiza risasi tatu katika mkoba wake uliokuwa umeachia uwazi kidogo.

    Baada ya zoezi hilo ilikuwa zamu ya mama wa mjini kufanya maigizo ya kuibiwa simu, igizo lake likapata mashabiki wengi, gari ikaamuliwa kuingia kituoni.

    Adrian akawa ameingizwa hatiani!!!

    John akaendelea kuwa mshindi.

    Lawama zote zikamwangukia Mark.



    Mark alishindwa kabisa kuelewa ni namna gani Adrian atamchukulia kutokana na tatizo lililokuwa mbele yake, lakini katikati ya mawazo akaanza kumuogopa Adrian akiamini kuwa ni mtu hatari sana kwake.

    Anamiliki bunduki!!! Hatari sana mtu huyu, alitaka kuniua au kumteka Nunda?? Mbona kizungumkuti!!! Alijiuliza Mark. Kisha akawasha redio kwa sauti ya juu kidogo ili iingilie kati mawazo yake yaliyomzonga kichwani. Haikuwezekana, akainuka na kutoka katika chumba chake akaenda katika baa iliyokuwa jirani akaagiza na kuanza kunywa moja baada ya nyingine.

    Lazima nifanye kitu hapa kabla ya hatari!!!



    ***ADRIAN anahisi kuwa MARK ni mtu mbaya kwake...MARK naye anahisi ADRIAN ni mtu hatari anayemiliki Bunduki...wote hawajui kama kuna kichwa chenye jina la JOHN MAPULU katika mkasa huu......

    ****Mimba ya Matha bado ipo katika riwaya hii ya HATIA ....kumbuka ni mimba hiyo imeyaleta yote haya.....nini hatma yake.....NA VIPI YULE MCHUNGAJI FEKI?????

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog