Simulizi : Kisu Chenye Mpini Mwekundu
Sehemu Ya Pili (2)
“Mh. Makubwa. Yunifomu, Vifaa vya masomo, ada na nauli juu….” Aliongea peke yake .
“Vipi Mama Sanga mbona hivyo.” Aliuliza yule mama mtu mzima.
“Mwenzangu makubwa madogo yana nafuu, eti Beda kafaulu.”
“Pole Mwaya, majukumu ndo’ yanaanza hivyo.” Aliongeza yule bibi.
“Mwenzangu ndo nimechanganyikiwa hapa hata sijui niingilie wapi.”. Maneno ya mama yake yakaanza kumliza tena Beda. Huyu ndiye mtu pekee ambaye angeweza kumsaidia. “Tangulia nyumbani nakuja.” Alisikika mama Beda kwa sauti ya kukata tamaa.
* * *
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mvua ilikuwa imetulia na kuruhusu watu watoke majumbani mwao. Hali hii ilimuathiri sana mama Beda. Siku hiyo hakwenda kufagia barabara. Siku alizokuwa anapumzika ilikuwa kawaida yake kufanya biashara ndogondogo kama hii ya muhogo. Lakini leo alikuwa ameangukia pua, hakunusa wala hakupumua. Hakuna aliyekuja kununua muhogo zaidi ya watu watatu wa kwanza ambao walikuja kabla mvua haijaanza kunyesha.
Beda Sanga alitoka ndani ya nyumba ile ambayo haikuweza kuwasitiri vizuri kwa mvua kwani ilikuwa inavuja. Akajisogeza karibu na mama yake ili aweze kusikia lolote ambalo lingempa matumaini ya kwenda shule. Alijionea wazi ugumu wa biashara ya mihogo. Aliiona wazi huzuni iliyokuwa kwenye macho ya mama yake. Akakumbuka jinsi mama yake alivyoenda kuomba msaada kwa jirani yao ambaye ana uwezo kidogo. “Mama uliambiwa nini ulipoenda kwa mzee Uwesu.” Ilikuwa kama aliemtonesha, mama yake hakujibu badala yake akaanza kulia kilikuwa kilio kamili. Huku akiwa katika hali ya kwikwi akamwomba mwanae amsaidie kunyanyua vyombo warudishe ndani. Hakukuwa na biashara tena. Ilikuwa ni hasara tupu. Beda akaendelea kudadisi mama hakutaka kujibu. Akarudisha fikra jinsi alivyoenda kuomba msaada kwa mzee Uwesu.
“Baba mwanangu amefaulu naomba msaada wa mchango wenu kama inawezekana.” Aliyakumbuka vema maneno hayo ambayo aliyasema mara baada ya salamu.
“We mama usiniletee uchuro hapa kwani huko mnakofanya uchawi wenu hakuna michango. Kwa taarifa yako nakujua sana kuwa ni mchawi mkubwa hapa mtaani ndio maana huendelei, umemuua mumeo makusudi leo unakuja kutaka msaada kwetu?” Baada ya maneno hayo mama Beda akaondoka bila kuaga huku akilia. Hakutaka, hakutaka kabisa kumsimulia Beda mambo yale.
Usiku huohuo pamoja na kilio chake bado hakukata tamaa. Akaenda kwa Diwani wa kata yao.
“Hodi, hodi….” Alibisha hodi nyumbani kwa diwani. “Karibu..” Sauti ya kike ilijibu kutoka ndani. Akafunguliwa. “Karibu ndani.” Akamfuata yule binti ambaye mikono yake ilikuwa imelowa maji, bila shaka alikuwa anaosha vyombo muda huo. “Karibu ukae.” Alikaribisha binti yule ambaye alionekana wazi kuwa ni ‘house girl’. Akakaa kwenye moja ya sofa za thamani zilizokuwepo pale sebuleni. Akaruhusu macho yake yaisanifu sebule ile. Thamani ya kile kiti alichokalia tu ingetosha kabisa kutatua matatizo yake yote ya ada na vifaa vya shule. Alistaajabia ukubwa na uzuri wa sebule ile. Akastaajabu zaidi kuona samaki ambao walikuwa wanafugwa kwenye kabati maalum la vioo pale sebuleni. Hakumaliza kuisanifu sebule ile, diwani alifika pale sebuleni. Mzee Athumani Kipande diwani wa kata ya Charambe alikaa kivivuvivu katika moja ya viti vilivyokuwemo mle sebuleni. Alikuwa mzee mfupi mwenye mvi chache, mazingira ya nyumbani alipenda sana kuvaa msuli na kizibao.
“Karibu mama .” Aliita kwa mazoea tu kwani kiumri alikuwa mkubwa kuliko yule mama aliyekuwa mbele yake.
“Ahsante, Shikamoo.”
“Marhaba habari za nyumbani.”
“Nzuri kiasi baba.”
“Kwanini kiasi?”
“Ahh.” Alijikuta akishindwa kuongea na badala yake akaminyaminya vidole ambavyo vilikuwa vinatoa mlio kama vijiti vidogo ambavyo vilikuwa vinavunjikavunjika. Hatimaye akaamua kupasua jipu.
“Baba nimekuja unisaidie juu ya suala la mwanangu, amechaguliwa kujiunga na shule ya sekondari.”
“Msaada gani ulikuwa unahitaji?” Aliuliza diwani.
“Ili aweze kuanza masomo ninahitaji shilingi Elfu arobaini kwani tayari mwenyewe ninayo shilingi elfu ishirini.” Aliongea mama Beda huku hali ya kujiamini ikiongezeka.
“ Aaa, samahani mama unajua wiki hii kuna kundi la ngoma za kienyeji linakuja kutoka Botswana kwa hiyo akiba yangu nitaitumia huko mimi na familia yangu maana kiingilio kwa familia yote ni laki nne.” Akatulia diwani na kumwangalia mama yule kwa jicho lililokosa huruma. Moyoni mama Beda alilaani sana kauli ile, bora hata asingeambiwa.
Akanyanyuka pale kwenye kiti na kumuaga diwani wake.
Hizo zote zilikuwa kumbukumbu za siku mbaya ambazo zinapita katika maisha yake. Alisononeka sana moyoni. Ngalawa ya mawazo ikamfikisha kwenye mawimbi ya siku zile tamu ambazo alikuwa na uhusiano mzuri na diwani yule. Akakumbuka jinsi alivyoimba na kucheza ili diwani apate ushindi. Kumbukumbu zikamfikisha siku zile zenye ugwadu ambazo alipewa kitenge kipya cha waksi kutoka kwa mbunge mtarajiwa huku wakiongezewa na maji na soda kutoka kwa diwani wao. Akatikisa kichwa.
* * *
Ni siku nyingine. Saa 7.30 ilimkuta mama Beda akiwa na beseni lake la mahindi ya kuchemshwa maeneo ya Mtongani. Ilikuwa ni katika jitihada za kuhakikisha Beda anaenda shule. Kidogo siku hii ilikuwa nzuri kwake kwani alibakiza mahindi mawili tu. Akaendelea kuzunguka maeneo ya pale kituo cha magari, hatimaye akamaliza.
Akaanza kuhesabu kile alichokipata. Alikuwa na shilingi elfu kumi na nne na mia saba. Akatoa ile elfu kumi aliyonunulia mahindi, elfu nne mia saba akaweka kibindoni. Akatembea taratibu kuelekea nyumbani. Hakutaka kupanda gari kwani faida ilikuwa ndogo. Hatimaye chakara chakara za miguu zikamfikisha Mbagala rangi tatu. Bado mjeledi wa kashfa iliyotolewa na jirani yake uliendelea kumtesa ndani ya nafsi yake. Ina maana hapa mtaani ndivyo ninavyotafsirika, eti nimemuua mume wangu! Aliwaza na kusikia fundo likiushika moyo wake kwa uchungu.
Akatua beseni lake kisha akaingia ndani. Hakujua alifuata nini ndani akaamua kutoka. Hakugundua njaa aliyokuwa nayo kutokana na fikra nzito alizokuwa nazo. Akakaa chini ya mpera, bado jinamizi la shutuma za jirani yake liliendelea kumwandama. Fikra zake zikamfikisha kwa marehemu mumewe. Hawakuwa na maisha mazuri lakini asingeweza kushindwa kumlipia ada mwanae. Kitu kikamshika kooni. Akaanza kulia.
“Heheeeee. Mumewe kamuua mwenyewe leo anamlilia.” Kicheko cha Mama Suzi mke wa yule jirani yake kikamzindua. Akageuka na kumwangalia kwa hasira. Mama Suzi ambaye alikuwa anamwaga takataka kwenye kiwanja cha mama Beda akaondoka huku akishusha maneno ya majigambo. “Hunifanyi lolote nimeaga kwetu, umemuweza huyo huyo mumeo.” Aliendelea kumwaga maneno ambayo yalimuumiza vibaya mama Beda .
Mama Beda alishindwa kuvumilia akaokota chupa ya konyagi akaanza kumfuata jirani yake huyo. Mama Suzi akaanza kukimbia huku akiangusha ndoo ya takataka ambayo alibeba mkononi. Kwa nguvu zake zote mama Beda akairusha ile chupa.
* * *
Alitembea taratibu kuelekea kituo cha polisi Mbagala Charambe. Hakujua nini kimemsibu mama yake hadi akajikuta yuko kituoni. Moyoni alikuwa na maswali mengi sana. Hakujua ni kwanini furaha kwake kilikuwa kitu adimu. Hata jambo la kufurahisha yeye lilimtia uchungu. Mfano ulikuwa ni yale matokeo ya mtihani ambayo badala ya kumfurahisha yalimuhuzunisha. Angefurahi vipi wakati hakuwa na uhakika wa kusoma, halafu iweje leo akamatwe yule ambaye kidogo alimpa matumaini.
Alipofika pale mapokezi akamkuta yule bibi mfagia barabara akiongea na askari wa zamu. Ingawa aliwakuta wakiwa katikati ya maongezi aliweza kuelewa wazi kile walichokuwa wanazungumza.
“Kutokana na uzito wa kesi yake ndiyo maana tukaamua kumuhamishia polisi Chang’ombe.”
“huyu ndiye mwanae niliyekuwa nakueleza.” Aliongea yule mama huku akimkazia macho yule askari kama anayehitaji msaada zaidi.
‘‘Sawa mama lakini sina namna ya kukusaidia kwani suala lake limeshikwa na wazito.”
Yule bibi mfagia barabara akamgeukia Beda na kumwangalia kwa sura iliyokosa matumaini. Yule bibi akatoka mle kituoni lakini Beda hakutoka akaganda palepale kabla ya kuanza kuongea na askari.
“Shikamoo.” Alimwamkia askari aliyemkuta pale.
“Marhaba unasemaje?” Aliuliza yule askari kwa sauti nzito yenye ukali kidogo.
“Nimesikia mama yangu yuko hapa nimekuja kumuona.”
“Umesikia, umemsikia nani?” aliongea yule askari kwa sauti iliyojaa dharau na ujivuni.
“Nimesikia kutoka kwa majirani.” Alijibu
“Anaitwa nani mama yako?” Aliuliza yule askari
“Mrs Sanga.” Alijibu Beda.
“Ahaa, Yule mama aliyetaka kuua mtu?” Swali hilo likamshitua Beda hakuweza kulijibu.
“yule mama kesi yake ni nzito kahamishwa hapa yuko polisi Chang’ombe” Aliendelea kuongea yule askari. Beda akaondoka pale kaunta huku machozi yakimtoka.
Alipofika nje akaangua kilio kikubwa. Kilio chake kikakatishwa na mtu aliyemshika bega. Alipogeuka akamuona yule bibi ambaye mara nyingi alikuwa anafagia barabara na mama yake. “Usilie Beda mimi naenda kumuona mama yako huko Chan’gombe, yatakwisha tu.” Yule mama alimbembeleza Beda aache kulia.
“Kwani ilikuwaje?” Aliuliza Beda huku akifuta machozi yake.
“Kulikuwa na ugomvi na yule jirani yenu Mama Suzi, kamrushia chupa kwa bahati ikamkosa lakini hawakukubali wakaja kumshitaki huku kuwa amedhamiria kuua.” Beda akashusha pumzi kwa nguvu. Ulikuwa ni muendelezo wa machungu katika maisha yake.
* * *
Mbu na harufu za mikojo vilikuwa kero ya aina yake kwa mama Beda ambaye hakutarajia kupatwa na mkasa kama huo katika maisha yake. Ilikuwa kama ndoto pale Mama Suzi alipokuja na kuanza kumrushia maneno ya kashfa. Bila kutarajia alijikuta akiokota chupa na kumrushia. Ilikuwa ni bahati kwa Mama Suzi kwani chupa ilimkosa na badala yake ikapiga ukutani na kupasuka vipande vipande. Mama Beda alijua yamekwisha.
Siku ya pili akiwa kwenye maandalizi ya kuchemsha mahindi ndipo aliposhuhudia kile ambacho hakukitarajia. Askari wawili wakiongozana na mzee Uwesu walifika nyumbani kwake na kumkamata. Alielezwa wazi kuwa kosa lake ni kujaribu kuua. Alilia, akalia… Kilio chake kikapotelea hewani, hakuna aliyemjali alionekana punguani. Amlilie nani. Kwa namna ya kudhalilishwa akafungwa mikono yake kwa nyuma. Watoto wakamzomea, majirani wakamcheka. Mpeleke akaroge gerezani. Walichombeza safari yake hiyo. Hakuujua uchawi, hakumjua hata mganga wa kienyeji. Labda umaskini wake na yale macho yake yaliyobadilika na kuwa mekundu kutokana na kushinda kwenye jiko la kuni huku akibugia na kulizwa na moshi ule mkali. Alishakubali matokeo sasa alikuwa anasubiri kudra za mola wake.
Akapokelewa na kiza cha mchana kwenye chumba kidogo ambacho hakina hata dirisha. Baadae akatolewa bila maelezo yoyote na kupandishwa kwenye gari ambalo lilimfikisha polisi Chang’ombe. Akawekwa mahabusu. Makazi duni kabisa ambayo hakustahili kukaa hata mbwa. Hakutamani kuendelea kuishi, dunia aliiona chungu. Hakujua kama kulikuwa na tofauti kati ya dunia na jahannamu ule moto mkali ambao unaelezwa kwenye vitabu vitukufu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa kwenye lindi la mawazo mlango ukafunguliwa. Akatolewa kwa muda. Akashangaa baada ya kugundua kuwa ni mchana kweupe. Beda mwanae wa pekee alikuwa kaunta akihitaji kuongea na mama yake. Alitaka kuongea nini? Ilikuwa ni vigumu kufahamu kwani mtu na mwanae wakaangua vilio ambavyo vilidhihirisha jinsi askari wale walivyokosa huruma.
“Afande Marwa mrudishe ndani huyo asitupigie makelele hapa.”
“Sawa afande.” Amri ya mkuu ilipokelewa mama Beda akarudishwa tena kwenye chumba kile kibaya kuliko vyumba vyote alivyowahi kuingia. Akalia, akaliaa….. Sauti ikakauka lakini bado kilio kiliendelea. Kama alivyolia kwa sauti akashindwa kusikika sasa ilikuwa zaidi kwani alilia bila kutoa sauti. Alijua fika siri ya kifo cha mumewe, kumbukumbu hiyo ikazidisha kilio kisicho na machozi.
* * *
JIFUNZE!
“Mwenye pesa si mwenzako na kamwe masikini hathaminiwi katikati ya pesa. Pesa hubadili mioyo ya wema kuwa miovu, pesa hubadili ndio na kuwa hapana, pesa hununua utu na mbaya zaidi pesa hiyohiyo hurejesha utu! Isake kwa njia halali, jitume uwezavyo kuisaka. Ukiipata usiitumie kama fimbo maana utaitumia kuwachapa wenzako duniani lakini ipo hukumu inakungoja. Nawe utachapwa mara elfu ya ulivyochapa Duniani!!”…*
Ilikuwa ni wiki ya machungu kwa Beda, aliwaza mambo mengi. Umri wake mdogo haukuweza kuhimili mikikimikiki mizito, akaanza kusikia maumivu makali ya kichwa. Akapiga hatua kuelekea nyumbani kwa bibi mfagia barabara. Akafika maeneo yale ya Kimbangulile. Bibi mfagia barabara alikuwa amekaa nje kwenye nyumba yake ambayo ukiiangalia sana jinsi ilivyojengwa ilirandana na sura na umbo la mbwa mwenye lishe duni. Ilikuwa ni nyumba ya miti ambayo ilijengwa kwa namna ambayo ingekushawishi kuifananisha na mbavu za mbwa jinsi fito zilivyoizunguka na kujitokeza kama mbavu za mbwa aliyekonda.
“Bibi shikamoo.” Alisalimia Beda.
“Marhaba Beda, karibu sana.” Alikaribisha. Beda alikaa chini akajilaza kwenye mkeka ambao ulikuwa unasubiri amri ya mmiliki wake kuwa utupwe jalalani. Kichwa kilikuwa kinamgonga hivyo hakuhitaji maongezi zaidi ya kulala na kugaragara. Bibi mfagia barabara akashikwa na huruma akaenda duka ambalo lilikuwa jirani na pale nyumbani kwake.
“Unazo panado.” Alimuuliza muuza duka
“Zipo za Kenya na Tanzania” aliongea yule kijana huku akiyaweka mezani mapakiti yote mawili.
“Kwani bei zinatofautiana?” Aliuliza bibi mfagia barabara.
“Hizi za Kenya Bei yake ni kubwa kuliko hizi za Tanzania.”
“Haya, naomba hizo za Tanzania” Aliongea bibi mfagia barabara huku akitoa hela kwenye pembe ya kanga yake. Dawa alizohitaji zikafungwa kwenye gazeti bila kufuata utaratibu. Hakukuwa na maelezo zitumike vipi kana kwamba wote walikuwa madaktari.
Alitembea haraka kumwendea Beda ambaye hali yake haikuwa nzuri.
Alipofika akasimama kando yake akiwa ameshika kiuno“Amka umeze dawa.” Beda akajiinua pale kwenye mkeka mbovu na kuanza kujikung’uta mchanga uliokuwa kwenye shati lake.
“Usifikirie sana Beda mjukuu wangu mama atatoka tu.” Aliongea bibi mfagia barabara.
Alimeza zile dawa akalala tena pale kwenye mkeka.
*****
Mwezi mmoja ulikuwa umepita toka mama Beda awekwe ndani. Nenda rudi za kila siku zilimkatisha tamaa Beda. Kila walipokuwa wanatoka mara nyingi walikutana na mzee Uwesu yule jirani yao akiingia. Mzee Uwesu alikuwa ni mtu mwenye nafasi ya juu katika shiria la umeme Tanesco. Hili liliwatia mashaka kwani walihisi kuwa mzee uwesu aliamua kumkandamiza makusudi mama Beda kwa kutumia umaarufu na fedha alizokuwa nazo.
Siku ya pili Beda na bibi mfagia barabara walikuwa kituo cha polisi pale temeke Chang’ombe. Wakamwona yule askari anayeshikilia kesi yao.
“Habari baba.” Alisalimia yule Mama mfagia barabara kwa unyenyekevu ingawa aliyekuwa anamsalimia alikuwa sawa na mwanae wa kumzaa.
“Salama mama , niwasaidie nini?”
“Baba si unaju siku zote tuna kuja kwa ajili ya yule mtu wetu?”
“Enhe sasa, ngoja tuongee kiutu uzima. Munayo elfu arobaini? Kama ipo njooni kesho nitawasaidia sawa?”
“Sawa” Akajibu yule bibi bila kuwa na uhakika kama kweli ataipata hiyo elfu arobaini.
“Mwanangu Beda hii ndiyo dunia; Hakuna mwema aliyebaki, dunia imevaa joho la dhuluma na ukatili. Tulipe pesa mama yako atoke unafikiri utasoma?”
Yalikuwa ni maneno makali kama kisu kilichowekwa kwenye moto hata kikawa na rangi ya moto.
“Itakuwaje bibi?’ Aliuliza Beda kwa sauti yenye majonzi ndani yake.
“hivi nyumbani hakuwa na akiba yoyote?”
“Ninapafahamu alipokuwa anahifadhi hela zake lakini sijui kuna kiasi gani maana sijawahi kukagua.”
“Basi nenda ukaangalie kama kuna chochote utaniletea sawa?”
“Sawa bibi.” Alimjibu huku wakiingia kwenye daladala lililokuwa linaelekea Mbagala rangi tatu. Wote walikuwa kimya hakuna aliyeongea chochote mpaka Rangi tatu.
Walipofika Beda hakukumbuka hata kumuaga bibi mfagia barabara, akili yake ilikuwa pale alipokuwa anamuona mama yake akihifadhi fedha. Akatembea kwa haraka, uvumilivu ukamshinda akaanza kukimbia. Akakimbia, akakimbia…………
* * *
Mwanamke aliyekonda mwenye nywele chafu huku akiwa na ukurutu mikononi na sehemu zote ambazo ukurutu hupenda kujihifadhi alifunguliwa kutoka mahabusu ya polisi Chang’ombe. Alishachoshwa na dunia, alikuwa anasubiri siku ifike ajiondokee. Huenda nyumba ile ya mchanga ikamsitiri vema. Alijihisi kuichukia dunia. Alitamani angekuwa mti mchungu wenye matunda yasiyoliwa ili tu aepukane na adha ya binadamu. Hata hivyo alipingana na wazo hilo kwani miti michungu ndiyo ambayo hutumiwa kwa ajili ya dawa za maradhi mbalimbali hivyo angeendelea kumnufaisha binadamu. Akatamani bora angekuwa moto lakini akakumbuka umuhimu na matumizi ya moto. Basi bora ningekuwa ukoma au matende…… Akaridhika na wazo hilo la hatari.
Huyu hapa Sakina Msomba au Mrs Sanga ingawa mtaani anajulikana zaidi kwa jina la mama Beda. Alitoka mle ndani huku akitoa harufu ambayo ilimfanya mwanae Beda aangue kilio upya. Furaha ya kuachiwa huru mama yake ikamezwa na hali mbaya aliyomuona nayo. Hakuweza kumtazama mara mbili mama yake. Alikuwa mama mchafu aliyechakaa, anayejikuna na bila shaka mwenye chawa mwilini. Ilihuzunisha, ilitia uchungu pia ilisikitisha. Mama Beda akamtazama mwanawe jinsi alivyokuwa analia akatikisa kichwa, akamtazama bibi mfagia barabara akashindwa kuvumilia akaanza kuangua kilio. Kilio hiki kilisababisha baadhi ya watu wenye roho nyepesi ambao walikuja kwa matatizo madogomadogo kutokwa na machozi. Jinsi alivyokuwa huyu mama ingekuwa sababu tosha ya kumliza binadamu yeyote mwenye huruma.
Alitembea kwa kuchechemea. Hatimaye alikuwa huru, uhuru mchungu ambao hauna maana yeyote, katika fikra zake alijua kuwa uhuru wa kweli ni kifo. Angelala, angelala…… Asingeamka tena ingekuwa ni usingizi wa milele usio na kero.
Kutokana na harufu mbaya aliyokuwa nayo hata wenye daladala walikataa kumchukua. Ikalazimika kidogo kilichobaki wakodi teksi. Kweli wakakodi. Mwendesha teksi alikuwa anasonya na kujiona aliyekosa bahati kwa kumchukua abiria yule wa aina yake. Kweli alichukiza bado alitakiwa mtu aliyeshiba imani ya dini inayomjua Mungu muumba kuweza kuvumilia na kujua kuwa ule ni mtihani katika mitihani ya Mungu.
Wakafika pale nyumbani kwao. Nyumba ilikuwa imepooza. Majirani wakawa wanachungulia kwenye madirisha. Mama Juma tu ndiye aliyetoka kwenda kuwalaki. Naye huyu alikuwa na sehemu ya ubinadamu hakuweza kuvumilia kwa hali aliyomuona nayo jirani yake. Akaanza kulia huku akiweka sawa mtandio wake kichwani. Mama Salome alikuwa anawasili nyumbani kutoka kanisani akasikia kilio hicho, akaacha biblia mezani akakimbilia kule alikosikia kilio. Majirani hawa wawili ndio walioungana na mama Beda kwenye kilio kile.
“wallahi, mie n’lishasema mtaa huu hawamuogopi Mungu.” Aliongea Mama Juma kwa lafudi ya kipemba huku akionyesha wazi kusikitishwa na kitendo cha majirani kutokuja kumlaki mwenzao katika wakati ule mgumu. Mama Salome naye akaangua kilio.
“Jamani tumpeleke hospitali huyu.” Alipendekeza Mama salome huku akijifuta machozi yaliyotokana na kumhurumia jirani yake. Akatoa noti tatu za shilingi elfu kumi. Mama Juma akaondoka kwenda kuomba hela kwa mumewe. Aliporudi alikuwa ameongozana na mzee yule wa kipemba. Mzee Sudi Nassoro Bilali alipomuona mama Beda akajishika kichwa kwa dakika kadhaa. “Wallahi, hawa polisi hawana ubinadamu.” Akakunjua msuli wake. Ndani alikuwa amevaa kaptura ambayo ilivuka kidogo magoti. Akaingiza kwenye mfuko wa ile kaptura akatoa noti za shilingi elfu tano tano takribani nane akakabidhi kwa bibi mfagia barabara.
* * *
Wiki moja ya matibabu katika hospitali ya wilaya ya Temeke ilimrejeshea mama Beda Sura na hali ya kawaida ya kibinadamu. Angalau sasa aliweza kutazamwa bila kuwatoa watu machozi. Akiwa mwenye faraja kidogo baada ya idadi chache ya majirani kuja kumuona pale alipolazwa hospitali angalau sasa aliweza kuwaza juu ya mwanae Beda. Bado alikuwa na mtihani mwingine atasoma vipi mwanae.
Siku zikakatika mama Beda akawa mwenye afya nzuri. Akarudi tena mtaani kutembeza beseni la matunda na mahindi ya kuchemshwa. Biashara ilikuwa nzuri kias lakini haikuweza kukidhi mahitaji yote.
Alimaliza mitaa na kona zote za wilaya ya Temeke kusaka noti. Moyoni aliwaza akaona bora mwanae asingefaulu wangesaidiana biashara zile ngumu. Kwa kiasi fulani matokeo ya mwanae ilikuwa chanzo cha matatizo yote. Siku za nyuma hakuwa na mazoea kabisa na yule jirani yao mzee Uwesu, hata pale alipopita na gari yake alifunga vioo ili wasisalimiane. Matokeo ya mtihani yalimlazimisha kwenda kuomba msaada katika kasri ile ya shetani. Ndipo alipopokea mvua ya kashfa na matusi, haikutosha ukaanza uchokozi mkubwa uliomvurugia mambo yake yote.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
* * *
Alitembea taratibu akitokea dukani ambako alienda kununua majani ya chai. Alipishana na wanafunzi ambao walikuwa kwenye sare za shule tofauti tofauti wakigombea magari. Alijisikia uchungu sana alipobahatika kukutana na wanafunzi ambao alisoma nao shule moja. Walipendeza sana ndani ya sare zao mpya. Alijitahidi kutembea katika namna ambayo isingemkutanisha na wanafunzi wale. Kwanini huendi shule? Hilo ndilo swali aliloliogopa zaidi kwani lingeleta mlolongo wa kumbukumbu mbaya ambazo zingeweza hata kumliza. Hakutaka kulia, kama kulia alilia sana sasa alikuwa anasubiri matokeo tu. Aliamini kuwa kile kitakachotokea pengine ndicho alichokadiriwa na Mola jalali. Hakutaka kuwaza lolote juu ya mambo ya shule hakutaka kumuuliza tena mama yake kwani angemtonesha vidonda vya mahabusu ambako amekaa mwezi mmoja na siku kadhaa bila kusomewa mashtaka kisha kwa shilingi elfu arobaini tu akatolewa. Lilikuwa ni pigo baya katika maisha yake. Aliwaza mengi juu ya tukio lile, pengine yule mzee ana wivu kwani mtoto wake hakuchaguliwa kujiunga na sekondari. Akayapuuza mawazo hayo na kuendelea kupita njia alizoziona kuwa salama kwake kwani zisingemkutanisha na wanafunzi wenzake. Alikosea, tena alikosea sana. Alibadili mwelekeo akapita kichochoro ambacho alidhani kitakuwa salama zaidi. “Paaa.” Moyo wake ulishituka baada ya kukutana na Vick msichana aliyekuwa anakaa naye dawati moja. Alikuwa amevaa sketi ya kijani na shati jeupe. Chini alikuwa amevaa viatu vyeusi vya ngozi na soksi nyeupe. Alipendeza.
“Oooh, Beda huyo mambo.”
“Poa Vick” alimjibu msichana yule mpole. “Vipi shule badobado?” Kama alivyotarajia lilikuja lile swali aliloliogopa. Hakupenda kujibu swali lile lakini alikumbuka jinsi Vick alivyokuwa akimsaidia mambo mbalimbali pale walipokuwa darasani. Ni mara ngapi Vick amediriki kumnunulia peni na daftari. Hakuona sababu ya kuto mweleza ukweli. “Vick mwenzi sijui kama nitaendelea na masomo, we mwenyewe si unaifahamu hali yetu?” “Kwani Ada ni shilingi ngapi huko shuleni kwenu?” “Joining Instruction zinaonyesha kuwa ni shilingi elfu arobaini ukichanganya na mahitaji mengine madogomaadogo inafika elfu sitini.” “Siku zote hizo mama ameshindwa kupata hicho kiasi.’ “Alikuwa anakaribia kutimiza, angekuwa ashatimiza lakini akakamatwa na polisi mpaka kuja kutoka kiasi chote kilikuwa kimeishia kwenye matumbo ya polisi na amekaa huko mwezi mmoja na nusu.” “Mh. ilikuwaje mpaka akakamatwa?”
“walirushiana maneno na mama mmoja jirani ndipo kwa hasira yule mama akaenda kuripoti polisi kuwa Mama anamtishia kifo wakati si kweli na yeye ndiye aliyeanzisha ugomvi kwa kumwita mama mchawi.” Vick alimtazama kwa macho yaliyojaa simanzi. Ni wazi hakutaka kabisa kusikia Beda akikosa fursa hiyo adhimu ya kuendelea na masomo. Akainamisha kichwa chini. “Beda, pole sana kwa yote naomba niende shule lakini nitakutafuta.” alimaliza na kumpungia mkono Beda. Beda aliendelea kumkazia macho binti yule ambaye baba yake alikuwa na cheo kikubwa jeshini. Akaondoka huku akijilaumu kwa kuruka jivu na kukanyaga moto. Atanitafuta kwa lipi. Aliwaza jinsi binti huyu anayetoka katika familia inayojiweza kimaisha alivyoweza kumtembelea mara kwa mara wakati ule wanasoma. Akakumbuka hata pale aliponunuliwa vitabu.
Akaachana na mawazo hayo, akaamua kuongeza hatua ili asije kukutana na mtu mwingine. Aliogopa sana kama angekutana na Mrisho. Huyu alikuwa anamchukia sana Beda eti kwa sababu alikuwa anamzidi kwenye matokeo ya mitihani Darasani. Alijua wazi kuwa kama angesiki kuwa amechaguliwa na ameshindwa kuuendelea angecheka sana. Alimchukia sana Mrisho kwani ndiye aliyemuanzishia majina mengi mabaya darasani lakini hata hivyo majina hayo hayakuenea.
“We Beda unaenda wapi?” Akashituka baada ya kusikia sauti ya mama yake.
“He.” Akashangaa baada ya kugundua kuwa alikuwa ameipita nyumba yao hatua kadhaa. Alikuwa na mawazo mengi kiasi cha kukosa umakini na kutaka kupita nyumba yao. Alijishangaa hata yeye mwenyewe kwa tukio lile.
* * *
NUKUU!!
“HAO nd’o wanadamu, wanayatumia madhaifu yao wanajilinganisha na nyadhifa zao kisha wanakugandamiza! Mwanadamu kamwe si wa kumuamini kwa asilimia mia moja, maana anaweza kubadilika sekunde yoyote ile na kukufanya ufumbe macho na kufumbua ukidhani unaota mabadiliko yale… ishi na viumbe hawa kwa tahadhari, mwanadamu pekee wa kumuamini kwa asilimia zote ni WEWE MWENYEWE!!
Alijua wazi kuwa kama angesiki kuwa amechaguliwa na ameshindwa kuuendelea angecheka sana. Alimchukia sana Mrisho kwani ndiye aliyemuanzishia majina mengi mabaya darasani lakini hata hivyo majina hayo hayakuenea.
“We Beda unaenda wapi?” Akashituka baada ya kusikia sauti ya mama yake.
“He.” Akashangaa baada ya kugundua kuwa alikuwa ameipita nyumba yao hatua kadhaa. Alikuwa na mawazo mengi kiasi cha kukosa umakini na kutaka kupita nyumba yao. Alijishangaa hata yeye mwenyewe kwa tukio lile.
* * *
Ulikuwa usiku wa manane. Mvua zilizoambatana na radi na upepo zilikuwa zinanyesha. Beda alikuwa ametulia kitandani huku akiwa na hofu. Ilikuwa lazima awe na hofu. Kwanza hakuwa na imani na nyumba yao kama ingeweza kuhimili vishindo vya mvua ile, pili alisikia nyayo za mtu aliyekuwa anatembea karibu na dirisha la chumba chake. Hofu ikautawala moyo wake. Nani tena? Alijiuliza Beda kwa sauti iliyojawa na hofu.
Moyo wake ulizidi kupiga kwa kasi. Usingizi ulipotea ingawa alikuwa amejifunika shuka gubigubi. Ilikuwa lazima ajifunike.
Hisia kuwa kuna watu wanamchungulia kupitia matundu madogo ya nyumba ile ambayo ilijengwa kwa tope zilizidi kumtia hofu. Wazo la kujifunua ghafla ili kujua ni kina nani waliokuwa wanamchungulia lilipotea haraka sana.Alitamani sana kuwasha kibatari lakini hakuthubutu. Alijipa moyo kuwa huenda ilikuwa ni ndoto. Hakukubaliana kabisa na wazo hilo. Alikumbuka kuwa ni mara ya tatu sasa anashituka usingizini na kusikia nyayo za mtu nje ya chumba chake.
Sasa haikuwa ndoto tena kwani alisikia dirisha lake likigongwa. Mapigo ya moyo yaliongezeka kiasi cha kuweza kuyasikia mwenyewe. Liwalo na liwe, akajifunua. Hakuona mtu wala watu. Akaamua kutoka ndani. Akafungua mlango na kwenda kushuhudia kilichokua kinamsumbua. hakuna mtu. Akazidi kushikwa na hasira.
“Beda nipo hapa.” Akashituka zaidi baada ya kusikia sauti ya kike. Akataka kukimbia.
“Usikimbie mimi Vick.” Kweli ilikuwa sauti ya Vick. Alipoangalia vizuri akamuona Vick akiwa ameegemea ukuta wa nyumba yao. Alikuwa anatetemeka kwa baridi. Hivi ni Vick kweli au mzimu ule? Aliwaza Beda baada ya kuhisi kuwa ni jambo lisilowezekana Vick aje usiku wa manane tena wakati kuna mvua, radi na upepo mkali. Kilichomshangaza zaidi ni jinsi alivyoweza kutoka kwao kwani nyumba yao ilikuwa na geti kali. Akapiga moyo konde akamsogelea. Bado Vick alikuwa anatetemeka.
“Vick.”
“Bee.”
“Mbona usiku?”
“Nimekuja kukuletea hela ya ada.”
“Umepata wapi?”
“Nimeiba nyumbani.”
“Si ungesubiri asubuhi.”
“wakinikuta nazo!” Beda akashindwa kujibu. Sauti zao zilikuwa za kunong’ona. Bado Vick alikuwa anatetemeka kwa baridi. Beda akamshika mkono akaingia naye ndani. Vick akaingiza mkono wake kwenye sidiria yake ambayo ilikuwa imebeba matiti madogo machanga akatoa noti za shilingi elfu kumikumi akamkabidhi Beda. Ahsante sana Vick. Beda alimshukuru Vick kwa moyo wake wote. Kwa kuwa bado allikuwa anatetemeka Beda akashikwa na huruma. Akamvutia kifuani akamkumbatia huku akimfunika kwa shuka yake. Jinsi alivyokuwa na furaha ya kupata zile fedha hakuweza kugundua kuwa yule msichana alilowa.
“Ahsante sana Vick sina cha kukulipa.” Aliongea Beda kwa sauti iliyojaa shukrani ya kweli.
“Nikusindikize?” Aliuliza Beda.
“Hapana nasikia baridi naomba nilale hapa hapa nitaondoka alfajiri.”
“wazazi wako wakigundua.”
“Usihofu wote wamesafiri, wameenda msibani Mahenge”. Hakuwa na chaguo akakubali Vick alale pale. Vick alikuwa amelowa lakini akalala na nguo zake. Beda hakuona Shida kwani wakati ule Vick anakoroma Beda hakuweza kulala. Mawazo yake yalikuwa juu ya maisha ya shule.
Kitu kimoja kikamshangaza. Licha ya kupita kwenye kipindi kigumu na cha matatizo makubwa kitendo cha kukumbatiwa na Vick kilimpa faraja. Akashangaa, kwanini kukumbatiwa kumemsahaulisha matatizo kedekede aliyokuwa nayo. Akapuuza na kujivutia shuka.
* * *
“Vick, Vick… Amka uwahi nyumbani.” Alishituka kutoka usingizini.
“Niko wapi?” Alishangaa Vick, Beda akacheka baada ya kugundua kuwa Vick alidhani kuwa amelala nyumbani kwao. Alizidi kujishangaa baada ya kuona jinsi nguo zake zilivyolowa.
“Lakini Vick unajua unanishangaza sana.”
“Kwani vipi?”
“Umewezaje kutoroka bila kujulikana?”
“Nafikiri nimeshakueleza kuwa wazazi wangu wote wameenda msibani Mahenge”
“Hakuna mlinzi?”
“Hakuna.” Alijibu Vick kwa mkato huku akishika komeo la mlango. Akaondoka huku akimpungia mkono Beda.
Tukio lile lilimfungulia ukurasa mpya Beda. Alikuwa hajawahi kulala kitanda kimoja na msichana toka apate akili timamu.
Akatembea kwa kunyata hadi kwenye mlango wa chumba cha mama yake. Akatega sikio pale mlangoni. Akashusha pumzi baada ya kugundua kuwa mama yake alikuwa anakoroma.
Hajui kitu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alifurahia moyoni.
Baada ya kurudi chumbani kwake kitu cha kwanza ilikuwa ni kuhesabu zile noti alizopewa na Vick.
“Haaa.” Alishituka kwa mshangao. Zilikuwa fedha za kitanzania shilingi Elfu sabini. Hakuamini macho yake kama Vick anaweza kumfanyia mambo mazito namna ile. Akaruka ruka kwa furaha. Matumaini ya kwenda shule yalikuwa makubwa. Furaha yake iliendelea mpaka pale aliposhikwa na usingizi.
Beda akaamua kuwa muwazi kwa mama yake, aliamua kumsimulia tukio lote bila kumficha chochote. Na ndivyo alivyofanya. Mama Beda akajikuta anashindwa kumkaripia mwanawe kwani kwa kufanya hivyo angelazimika kuwa na fedha za kulipia karo.
‘Huu umasikini ni chanzo cha mambo mengi.’ Aliwaza huku akishindwa kujua iwapo ashukuru au asikitike kwa tukio lile.
* * *
Asubuhi saa 3.30 ilimkuta mama Beda akiwa katika viunga vya shule ya sekondari Benjamin Mkapa. Akaelekea moja kwa moja kule iliko ofisi ya waalimu.
Pale ofisini kulikuwa na walimu wachache, wengi walikuwa madarasani. Akawasalimia wachache waliopo.
“Samahani dada nimekuja kulipa ada ya mwanangu, sijui tunalipia wapi.”
“Fuata hiyo korido, kama anaanza nenda ofisi iliyoandikwa HEADMASTER kama alishaanza nenda upande wakushoto mbele kidogo ya ofisi ya kwanza kuna ofisi imeandikwa MALIPO.” Alimaliza kuelekeza yule mwalimu wa kike.
Akatembea kwa haraka huku kandambili zikipigapiga miguu yake. Akagonga mlango kwenye ile ofisi iliyoandikwa headmaster.
“Ingia.” Alikaribishwa na sauti ya kike. Akafungua mlango. “Habari yako.”
“Nzuri dada.”
“Mkuu ana mgeni tafadhali msubiri hapo kwenye kiti akiondoka utaingia.” aliongea yule dada ambaye alikuwa anachapa kitu kwenye Kompyuta. Baada ya kuangalia vizuri akagundua kuwa kulikuwa na chumba kingine mle ndani ambacho kilikuwa na maandishi mlangoni MKUU WA SHULE. Akakaa kwenye kiti.
Baada ya dakika kumi mlango ukafunguliwa. Akatoka mzee wa makamo ambaye bila shaka ndiye aliyekuwa anaongea na mkuu wa shule. Yule dada akamuashiria mama Beda kwa mkono kuwa aingie ndani.
Huku moyo wake ukiwa na furaha akaingia ofisi ya mkuu wa shule. Aipofungua mlango akamkuta mkuu wa shule akiwa ameenea kwenye kiti cha ofisi ambacho kilikuwa kinazunguka kama vile vya saluni. Alikuwa ni mzee mweusi mnene mwenye mvi. Uso wake ulikuwa mpana huku ukibeba mawani ya kusomea.
“Karibu.” Sauti yake ilikuwa nzito kiasi ilimtia hofu mama Beda.
“Ahsante, shikamoo.”
“Marahaba, enhe nikusaidie nini?” Mama Beda hakujibu badala yake akaingiza mkono kwenye mfuko wa nailoni ambao ulikuwa mkononi mwake. Akatoa makaratasi yaliyokuwamo mle ndani akamkabidhi yule mkuu. Mkuu akaweka sawa yale makaratasi akaanza kuyapitia moja baada ya nyingine. “Mbona umechelewa sana mama , hii nafasi naona kama imezibwa na mtu mwingine.” Lilikuwa ni pigo lingine akainamisha uso wake. Machozi yakaanza kumtoka. Mkuu wa shule akatulia hadi pale alipojifuta machozi kisha akaendelea. “Labda uende ofisi ya elimu wilaya wao wanaweza kukusaidia.” Huku akiwa na majonzi mapya akaondoka pale ofisini hakukumbuka hata kumuaga yule dada aliyempokea.
*****
Gervas Msangi aliinuka kwenye kiti akaanza kupekuwa hapa na pale akitafuta funguo afunge ofisi. Alihangaika kwa muda wa dakika tano. Hatimaye akaziona. Wakati anainuka pale kwenye kiti mlango wa ofisi yake ukagongwa. “ Vipi bosi mbona kama unataka kuondoka.” Alisikika Zena muhudumu wa ofisi ya elimu. “Eeeh, kwani vipi?” “Kuna kimeo huko chini unaweza kupata ya bia.” “Usinitanie Zena leo nimepigika kishenzi.” Aliongea kwa kiherehere. “Ngoja nikuletee.” akafungua mlango na kushuka chini. Baada ya dakika chache ofisi ya Gervas afisa elimu taaluma ikagongwa. “Ingia.” Alisema huku akijiweka sawa kwenye kiti.
“Habari yako.” Alisalimia Gervas baada ya kuona mama Beda amekaa kwenye kiti.
Wazo jipya likapita kichwani kwa Gervas. Aliweza kubaini kuwa huyu mama asingekuwa na chochote cha kumridhisha. Shetani akamkalia kichwani. Akatabasamu moyoni kwani mkewe alikuwa amesafiri.
“Enhe. Nikusaidie nini?” Aliuliza. Akampa zile fomu za mwanawe. akamsimulia hatua zote alizopitia mpaka kufika hapo. Pia akamuelezea sababu zote za kuchelewa isipokuwa ile ya kukamatwa na polisi.
Pale alipokaa Gervas alikuwa na wazo moja tu. Kweli alitaka kumsaidia huyu mama lakini na yeye alitaka kukidhiwa haja zake. Tamaa zilimshika zikamhamasisha. Alikuwa anatafuta namna mzuri ya kumshawishi yule mama ili aweze kukidhiwa haja yake. Ilikuwa ni kawaida ya afisa huyo kutofanya kazi bure bila kupokea chochote mpaka pale ofisini akapachikwa jina la mzee wa vimeo. Hiki kilikuwa kimeo kingine mbele yake. Lakini kwa jinsi alivyo alijua wazi kuwa huyu mama pamoja na umbo na sura nzuri alikuwa na dalili zote za maisha magumu. Umbo na sura yake vilimvutia. Duh. Lakini analipa huyu. Ibilisi aliendelea kumpigia matari kichwani.
“Sawa, nimekusikia na nimekuelewa. Nitakutafutia shule nyingine ambayo iko karibu kabisa na huko kwenu, umesema unatoka Mbagala eeh.” Aliuliza baada ya mambo kadhaa kupita kichwani mwake.
“Ndiyo baba.”
“Sawa iko shule moja ya sekondari pale headmaster ni rafiki yangu, tutampeleka huko.” Mama Beda akajawa na furaha.
“Ili tuweze kupanga vizuri nitahitaji kuonana na wewe jioni ya leo kwa sababu huu ni mpango mgumu kidogo tofauti na unavyofikiri.”
“Wapi?”
“Tukutane pale White park Kiwalani”
“Mbona sipajui.”
“We ukifika Kiwalani uliza tu iliko white park, ukija hapo nitakusaidia namna nzuri ya kufanikisha mpango wako maana nataka niifanye kazi yako haraka kwa sababu kesho kutwa nina safari ya kikazi mkoani.
“Ahsante baba.” Alisikika mama Beda huku akiinuka kwenye meza.
Maskini hakujua dhamira iliyojikita kwenye nafsi ya afisa elimu yule.
* * *
JIFUNZE/KUMBUKA.
“MAPENZI ni hisia zilizojikita chini kabisa ya moyo wa mwanadamu, mapenzi hayana wakati maalum wa kuanza kuonekana, mapenzi huja tu…. Mapenzi huisimamisha akili na kuleta ujasiri wa aina yake. Mapenzi yakisimama ni ngumu kwa mwanadamu mwingine kuyaamuru yatoweke kwa sababu mapenzi ni hisia zisizoonekana kwa macho bali vitendo. Vicky ametoroka nyumbani usiku wa saa saba, asijue kama yeye ni mtoto wa kike, asihofie mvua kubwa ya radi….. MAPENZI NI UPOFU!!”
“Tukutane pale White park Kiwalani”
“Mbona sipajui.”
“We ukifika Kiwalani uliza tu iliko white park, ukija hapo nitakusaidia namna nzuri ya kufanikisha mpango wako maana nataka niifanye kazi yako haraka kwa sababu kesho kutwa nina safari ya kikazi mkoani.
“Ahsante baba.” Alisikika mama Beda huku akiinuka kwenye meza.
Maskini hakujua dhamira iliyojikita kwenye nafsi ya afisa elimu yule.
* * *
Maridadi ni miongoni mwa nyumba za kulala wageni ambazo zina sifa ya kupokea wenyeji kuliko wageni. Iko karibu kabisa na reli ya Tazara. Watu wengi hupendelea kufika hapo nyakati za jioni. Gervas Msangi hakuwa mzoefu sana wa eneo hili lakini Ijumaa hiyo alijikuta akiwa mmoja wa wateja wa sehemu hiyo ambayo ilikuwa na baa. Hakuwa mlevi wa pombe, alikuwa na ulevi wake mwingine kabisa. Baada ya kukaa dakika kadhaa akijiburudisha na soda Gervas aliinuka na kuelekea mapokezi.
“Habari yako dada.”
” Nzuri shikamoo.”
“Ahsante, naweza kupata chumba?”
“Eeh. kulala elfu tano shoo taim elfu mbili.” Akatoa noti ya shilingi elfu tano akamkabidhi yule muhudumu wa gesti.
“Enhe, jina…”
“Carlos Tevez.”
“Nani.?” Aliuliza tena yule muhudumu kwa mshangao.
“Nimekwambia Carlos Tarimo.”
“Ahaa. Nilisikia Carlos Tevez.” Akacheka kidogo baada ya kugundua ameongopewa.
“Nitarudi baadae kidogo.” Alisema huku akiondoka baada ya kupiga sahihi kwenye daftari la kusajili wageni. Kabla hajafika mbali akarudi tena.
“Umesema chumba namba ngapi vile.”
“Namba kumi na moja.”
“Unaweza kunipatia funguo.”
“Hizi hapa lakini nakupa tu kwa kuwa nakuheshimu funguo zote zinatakiwa kubaki hapa receiption iwapo mteja atatoka nje ya eneo letu.” “Poa naenda hapo White parks nitarudi baada ya muda mfupi.” Akaondoka kwa haraka, alitamani apae.
* * *
Alikuwa na furaha kubwa baada ya kuahidiwa kusaidiwa na afisa elimu taaluma.
“Twende wote mama .” Alisisitiza Beda baada ya kutoa ombi hilo mara ya kwanza na kukosa jibu. “Kaa hapa nyumbani kwani nauli haitatosha.” Aliongea mama Beda kwa ukali kidogo.
Akafunga vizuri kanga yake ambayo nyuma ilikuwa na picha ya mgombea wa ubunge wa jimbo lake. Akahakikisha kuwa amejiaandaa vizuri kadri ya uwezo wake. Akaondoka na kumwacha Beda pale nyumbani.
****
Beda alikaa kwenye gogo la mnazi akamwangalia mama yake jinsi alivyokuwa anaondoka kuelekea Kiwalani. Moyoni alitamani sana waongozane lakini kigezo cha nauli kilichotumiwa na mama yake kilimkwamisha. Mama akatokomea…..
Ghafla, akazibwa uso na mtu asiyemfahamu. Akajaribu kupapasa kwa mikono yake.
“Sele..” hakupatia yule mtu aliendelea kumziba uso.
“Pita….” Bado hakupatia. Mtu aliyemshika akaangua kicheko. Akamtambua.
“Karibu Vick.”
“Ahsante, leo mama hayupo?”
“Mama kaenda Kiwalani.”
“Vipi mpango wa shule.”
“Ndio amefuatilia naona akirudi huko tutapata jibu kamili.” Alijibu Beda huku akisogea pembeni kidogo ili Vick naye akae.
“Vipi ulifika salama? Maana toka juzi hatujaonana” “Nashukuru Mungu nilifika salama.”
“Nilikukumbuka sana jana.” Aliongea huku akijishika shika vidole vyake.
“Hata mimi nilikukumbuka.” Aliongea Beda.
“Vile tulivyolala pamoja siwezi kusahau.”
“Utasahau tu.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nitasahau kama utanioa.” Hapo Beda akashindwa kuvumilia akaanza kucheka.
“Tutaoana kweli? Mbona una mawazo ambayo hayaendani na umri wetu?”
“Lazima niwaze kwani ipo siku na mimi nitakuwa mkubwa na chaguo sahihi ni sasa hivi.”
“Hatutakiwi kufikiria mambo ya ukubwani saa hizi.”
“Si kweli Beda mbona mwalimu anatuuliza ukiwa mkubwa unapenda kufanya kazi gani, huoni kama anatuuliza mambo ya ukubwani wakati sisi ni wadogo?”
“Kwa hiyo unasemaje?”
“Kama angeuliza unapenda kuolewa na nani ningesema Beda.”
“Kweli unanipenda?”
“Nakupenda sana Beda na natarajia siku moja utakuwa mume wangu.”
“uhhff.” Alishusha pumzi Beda.
“Twende ndani.”
“Kuna nini?” Aliuliza Vick.
“Twende we utaona tu.”
“Mh, haya.” Alisikika Vick huku wakiingia ndani.
* * *
“Kwanini umenileta huku gesti?” Aliuliza mama Beda. “Usiwe kama mtoto mpenzi.”
“Haa. Mimi mpenzi wako?”
“Usijali mimi nitakusaidia tu.”
“Sijahitaji huu uchafu nataka mwanangu asome?”
“Unajua toka siku ile niliyokuona kwa mara ya kwanza nilikupenda sana ndio maana sikuhitaji chochote zaidi ya penzi lako.”
“Kwa hiyo utanisaidia au hunisaidii?”
“Ukishanipa penzi nitakusaidia.”
“Hilo ndilo sharti lako?”
“Hilo tu.”
“Unaliona dogo, mbona sharti gumu sana.” Alilalamika mama Beda.
Mama Beda alikuwa hataki kabisa kuudhalilisha utu wake.
“Kwa hiyo utanipa hunipi?” Aliuliza Gervas
“Kwani siwezi kukupa fedha badala ya hicho unachohitaji?” Aliuliza.
“Hapana sihitaji fedha, mimi nina fedha zaidi yako” Aliongea huku akimshika shika kifuani.
“Aah, niache bwana.” Gervas hakuisikia kauli hiyo. Aliendelea kumvua nguo yule dada.
“Niache bwana.” Sauti ilikuwa imefifia.
Ndani ya dakika tano alikuwa na nguo ya ndani tu.
“Hapana hatuwezi kufanya bila kinga.” Alilalamika mama Beda.
“Tukifanya na kinga siwezi kuku saidia.” Aliongea Gervas kwa msisitizo.
“Naomba unijibu swali moja kabla hatujafanya lolote.”
“Uliza nitakujibu.”
“Mkeo yuko wapi?”
“Mke wangu amesafiri amejifungua wiki hiihii hivyo ameenda kwao kupumzika.”
“Naomba utumie kinga basi.”
“Siwezi kula pipi kwenye mfuko.”
“Mh…..” Aliguna mama Beda. Alihitaji msaada…………
* * *
“Ubwabwa mtamu, amepika nani?”
“Mimi.” Alijibu Beda.
“Mmmm, acha kujisifia amepika mama yako.” Aliongea Vick huku akijilamba vidole vyake.
“Ahsante kwa chakula kilikuwa kitamu sana.” Aliendelea kumwaga sifa Vick. Beda hakuongea chochote akatabasamu. “Naona muda umeenda wacha nirudi nyumbani.”
“Hautaki kusubiri umsalimie mama mkwe?” Hapo Vick akacheka mpaka jino la mwisho likaonekana.
“Nitamwona siku nyingine, wazazi wangu wamerudi leo baba alikasirika alikuwa anashangaa mbona hela zake zimepungua?”
“Hakukuuliza?”
“Hakumuuliza yeyote ana wasiwasi eti amepoteza kazini.” “Yaani, mama anatamani sana kuonana na wewe.”
“Usijali ataniona tu kama tutaendelea kuwa hai.” Akajibu huku akimvutia Beda upande wake. Akamkumbatia. Zilikuwa dakika mbili za hisia kali kwa kila mmoja.
“Kwaheri “
“Akaaga na kuondoka mle ndani huku akikimbia.” Huyo, huyoo….. Akatokomea gizani.
Beda akaanza kuingiwa na hofu baada ya kuona mama yake anachelewa kurudi.Hakuweza kulala. Mama yake alikuwa mtu wa matukio mabaya, hakuweza kusahau lile tukio la kuwekwa ndani mwezi mmoja na nusu. Aliogopa sana kwani hakuamini kama jinamizi la matukio mabaya limeacha kuiandama familia yao.
Alikuwa anaingia na kutoka ndani. Asingeweza kutulia usiku kama ule. Kuna nini tena? Alijiuliza bila kupata jibu. Aliangalia saa yake ya mkono ambayo mikanda yake ilishaharibika, ilisomeka saa 4.23 Mama yake alikuwa hajarudi. Akaamua kulala bila kufunga mlango wa kuingilia pale sebuleni.
* * *
Mama Beda alirudi nyumbani saa 6.30 usiku. Alikuta mlango ukiwa wazi. Akaingia ndani akiwa amechoka sana. Akachukua ndoo ya bafuni akajaza maji kisha akaenda kuoga. Alipooga akarudi na kukaaa kitandani. Machozi yakaanza kumtoka. Safari hii hakulia kwa ajili ya udhalilishaji aliojifanyia, kilichomsikitisha ni adhabu kubwa aliyompa yule afisa elimu. Yule alikuwa amejitakia mwenyewe mkewe Je. Hilo ndilo lililomtesa alimuhurumia sana mke wa Gervas ambaye kaenda kujifungua huko kwao.
Fikra zake zikampeleka miaka kumi nyuma. Akakumbuka jinsi mumewe alivyoiaga dunia. Akakumbuka jinsi alivyomuuguza muda mrefu. Akaanza kulia, alimhurumia mtu ambaye hamjui, mke wa Gervas Msangi ambaye amemchukulia mumewe. Akapapasa pale kwenye meza ndogo alikuwa anatafuta kiberiti. Hatimaye akakipata. Akawasha kibatari, akatembea kuelekea kule lilikokuwa begi la marehemu mumewe. Ndugu walimsusia kila kitu kwa madai kuwa yeye ndiye alimroga mumewe. Hakuwahi kutembelewa na ndugu upande wa mume hata siku moja baada ya kifo kile.
Ndugu zake walikuwa Kigoma adha ya usafiri iliwafanya washindwe kuhudhuria hata mazishi ya mumewe.
Alipekua lile begi akatoa karatasi mbili ngumu za rangi ya kaki. Akasoma karatasi ya kwanza kisha akaiweka mezani. Akachukua ile ya pili, haikuwa na maelezo tofauti na ile ya kwanza, tofauti ilikuwa ni majina yaliyotumika. Ile ya kwanza ilikuwa ni ya marehemu mumewe na ile ya pili ilikuwa ya kwake. Jina Sakina Msomba, Result HIV Positive. Alikuwa ni muathirika, alikumbuka vema jinsi alivyomuuguza mpaka mumewe anakufa mikononi mwake. Mumewe hakuwahi kutumia dawa za kupunguza makali hivyo alikufa mapaema. Alipoenda kuomba ajiunge akaambiwa CD4 zake zilikuwa zinatosheleza kwa wakati huo hakuhitaji kujiunga. Akaishi hivyo kwa muda wa miaka yote kumi. Baada ya kupata ile kashikasi ya kukamatwa na polisi hali yake ilibadilika ikawa mbaya.
Ndipo alipoanza dozi rasmi pale hospitali ya Temeke. Ni siri aliyoijua mwenyewe na madaktari tu. Leo amemuambukiza Gervas yule afisa elimu aliyekataa kutumia kinga. Hakuona sababu ya kumueleza ukweli amembembeleza mara nyingi atumie kinga hakutaka pia alijihisi kama aliyebakwa kutokana na hila aliyotumia afisa yule. Angefanya nini?
Wazo moja lilimtesa, mke wa Gervas hakustahili adhabu ile. Afanye nini kumuokoa? Lazima nimuokoe, siwezi kuacha mtu asiyehusika anapata adhabu asiyostahili, yule mumewe amestahili kwani ilikuwa vigumu kumpeleka PCCB, ningethibitisha vipi kuwa alihitaji rushwa ya ngono. Aliwaza mama Beda.
Nafsi yake yenye huruma haikutaka kusikia mwanamke mwenzake akipata mateso kwa sababu ya ufuska wa mumewe. Akalala akiwa na azma ya kumuokoa Mke wa Gervas. Nitamuokoaje? Ni swali lililopita kichwani mwake kabla hajapitiwa na usingizi.
* * *
Saa 1.30 Beda alienda kwenye mlango wa chumba cha mama yake. Akamsikia akiwa kwenye mkoromo wa usingizi . Akashusha pumzi kisha akakusanya vyombo alivyovitumia na Vick akakaa nje akaanza kuosha. Alikuwa na hamu kubwa ya kutaka kujua nini kimejiri kuhusu mpango wake wa kujiunga na masomo ya sekondari.
Aliendelea kuosha vyombo huku akiimba kwa mluzi. Alipomaliza alivianika kwenye uchanja kisha akarudi tena ndani. Wakati anaingia ndani akakutana na mama yake mlangoni. Alikuwa anapiga miayo ya uchovu.
“shikamoo mama .”
“Marahaba ngoja nioge mwanangu tutaongea vizuri nikirudi bafuni.”
Beda aliingia ndani na kusubiri kwa shauku kubwa.
Dakika za kuoga zilikuwa chache lakini Beda aliona kama siku nzima. Siku zilikuwa zinaenda wenzake walishaanza masomo. Akasubiri mpaka mama yake aliporudi. Mama yake akaingia chumbani akabadili nguo kisha akaja pale ambapo wenyewe walipatumia kama sebule. Kulikuwa na mkeka, kiti kimoja na kigoda tu. Beda aliona aibu pale alipokumbuka sebule alizotembelea kwa rafiki zake. Kidogo ilimshangaza kuona Vick mtoto aliyetoka kwenye familia yenye uwezo akiyakubali mazingira yale.
“Mama unabadili nguo mwaka nzima.” Alilalamika Beda
“Nakuja Beda mbona una haraka hivi?” Alisikika mama yake akiongea kutoka chumbani.
“Enhe, imekuwaje huko mama ?” Aliuliza Beda kwa kiherehere baada ya mama yake kutoka mle chumbani.
“Afisa elimu kanijazia hizi fomu tumebahatika kupata shule ya hapo jirani”
“Lini natakiwa kuanza?” Aliuliza Beda.
“Nikishapeleka hizi fomu nitapata jibu hukohuko.”
Aliondoka pale nyumbani huku akikabiliwa na mtihani mgumu kwa mke wa Gervas. Atampata vipi ili amweleze ukweli wa mambo. Iwapo atamueleza kweli haitamletea matatizo. Aliona wazi kuwa kuna hatari ya kushtakiwa kwa kueneza maradhi wakati anajua wazi kuwa yeye ni muathirika. Lakini kama angeweka wazi kweli angepata ule msaada? Angeupata vipi wakati Gervas alikataahata fedha. Kwanini Gervas ambaye kafunga ndoa kanisani atake liwazo lingine nje ya ndoa? Labda haya ni malipo mazuri ya usaliti. Hapana lazima nimuokoe mkewe, nitajibu nini mbele ya Mungu kama yule mwanamke atakufa kwa ajili yangu? Alijiuliza maswali mengi bila kupata njia sahihi ya kumnusuru mwanamke mwenzake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
**Tazama mama Beda anavyowakilisha mwanamke kama mtu mwenye huruma….. haikuwa nia yake kumwambukiza Gervas lakini anaamini anatakiwa kumwokoa mke wa Gervas..
HESHIMA KWENU WANAWAKE… Japo si wote wenye moyo kama wa mama Beda…
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment