Search This Blog

Monday, 20 June 2022

KIZUIZI - 1

 









    IMEANDIKWA NA :  GEORGE IRON MOSENYA





    *********************************************************************************



    Simulizi : Kizuizi

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Majira ya saa tatu asubuhi waumini waliokuwa wanatarajia kuingia katika misa ya pili walikuwa wameanza kujongea katika kanisa katoliki parokia ya mtakatifu Francis maeneo ya National jijini Mwanza. Ibada ya kwanza ilikuwa inakaribia kumalizika, kipengele cha matangazo mbalimbali ndio kilikuwa kinaimalizia hiyo ibada iliyokuwa inaongozwa na paroko wa kanisa hilo. Hali ya hewa ilikuwa ya ubaridi na waumini walikuwa wamejikunyata kila mmoja kwa namna yake huku wakiyapokea matangazo hayo.

    Mwanamama mfupi sana, nadhifu alikuwa mbele ya kipaza sauti akifuatisha mpangilio wa matangazo, aliyamaliza yale ya kawaida na sasa akayafikia mengine.

    Matangazo ya ndoa yalikuwa yanasomwa.

    "Bwana James Syaga wa parokia ya mtakatifu Kalolilwanga jijini Mwanza anatangaza kufunga ndoa na Bi. Emmy John wa parokia ya mtakatifu Joseph wilayani Kahama, hili ni tangazo lao la pili. Kwa yeyote mwenye kizuizi afikishe ofisini kwa paroko kabla ya tangazo la tatu" sauti ya mwanamama aliyekuwa anasoma matangazo ilisikika. Umri wake ulikuwa unafaa kuitwa bibi lakini alisoma kwa makini sana ukilinganisha na vijana ambao walikuwa na tatizo la kuchanganya herufi ‘r’ na ‘l’. Huyu hakukosea.

    Kanisa zima lilikuwa kimya, vilio vya watoto na vikohozi vya hapa na pale pekee ndio viliweza kuvuruga utulivu kiasi fulani. Ndege waliokuwa wamejenga viota vyao katika kanisa hilo pia walikuwa wanaruka hapa na pale huku wakiimba nyimbo zao nzuri za kuvutia.

    Mwanamama yule aliendelea kusoma matangazo mengine ya ndoa huku umakini ukiwa kwa hali ya juu kwa wale waliokuwa wanasikiliza, kwa wale wasiokuwa na ndoa wakawa wanajisikia aibu huku wenye ndoa wakijisikia fahari kuwa mfano kwa wengine.

    Tofauti na vilio vya watoto, kuna watu wazima wawili walikuwa wananong'ona kwa tahadhari ili wasiweze kusikiwa na mtu mwingine kuwa na wao wanachangia kuvunja utaratibu ndani ya kanisa, hasahasa padri aliyekuwa anaongoza ibada hii ya misa. Maana hakuwa na dogo, akikugundua unanong’ona alikuwa anakusema hapohapo.

    Wawili hawa mwanamke na mwanamume walikuwa katika mjadala mkubwa sana.

    "Ni Jimmy huyohuyo...haiwezekani Bibiana haiwezekani" Mwanaume alikuwa akimwambia mwenzake wa kike aliyeitwa Bibiana.

    "Wewe Deo, ndiye James huyo au watakuwa wamefanana majina?" Mwanamke ni kama hakuwa na uhakika bado.

    "Ni yeye bwana, mi namfahamu hadi huyo msichana anayetaka kumuoa...anachofanya sio sahihi." Deo alimjibu Bibiana kwa manung’uniko makubwa sana.

    "Kama ni yeye kweli, kesho naenda kwa Paroko, sikubali." alimaliza mazungumzo Bibiana huku uso wake ukitangaza chuki dhidi ya James Syaga. Chuki aliyoijua yeye na nafsi yake.

    Labda alitaka aolewe yeye? Labda ni chuki binafsi. Nani anayejua?

    Deo akamuunga mkono.



    ****

    Mazungumzo ya kunong'ona kati ya Bibiana na Deo ndani ya kanisa wakati matangazo ya ndoa yakiendelea yalimshtua kijana Joseph Boniphace ambaye alikuwa anaanza kupitiwa na usingizi baada ya kuwa amejikunyata kwa muda mrefu, mazungumzo hayo yalianza kama kero kwake, kwani yalikuwa yakimzuia kusinzia kwa amani, lakini kutajwatajwa jina la James na watu hawa kulichangia mshtuko wake wa pili. Kwa nini wanamtaja James?? Alijiuliza. Lazima kuna kitu hapa.

    Kwa tabia ya kupenda kujua yasiyomuhusu alitumia fursa hiyo kujitendea haki. Aliukemea ule usingizi nao ukamtii. Akayaamuru masikio yake kuwa makini, nayo pia yakamtii. Akaifurahia hali ile. Akayafumba macho yake kama vile amesinzia kumbe yu macho!!



    Tabia yake hii ya kupenda kujua mengi tena yasiyomuhusu ilimfanya apate umaarufu fulani usiokuwa na tija wala malipo, umaarufu wa kijinga katika vikundi vikundi alikuwa muongeaji mkuu, jambo gani limpite Jose asilijue? Skendo gani litapita mtoto huyu wa Boniphace pembeni na asilijue mwanzo hadi mwisho wake?? Kwa maisha yake hayo ya kujua kila kitu hatimaye akafupishwa jina lake kuwa Jose kwani kumuita Joseph ilionekana ni kupoteza muda lakini ili kumkumbuka mzazi aliyemzaa kijana huyu jina la Boniphace likafupishwa na kuwa B yaani Jose B.

    Jose B licha ya kujifanya kujua mengi, hakuwa muongo kila mara alikuwa na taarifa za uhakika, kwa hali hiyo watoto wa mjini wakawa wanamuita’wa ukweli’ na hatimaye likaunganika jina tamu kutamka lililoyapendeza masikio ya kila mtu kusikia Joseph Boniphace akawa Jose B Waukweli.

    Jina alilolipenda na kulitendea haki. Jose akawa Jose kweli.

    Jose alijifanya amesinzia kabisa lakini masikio yake yalikuwa wazi yakisikiliza kwa makini minong'ono hiyo kama yalivyokuwa yameamurishwa. Machale yakamcheza kuwa hayo mazungumzo hayakuwa tu ya kimbea ambayo yanaweza kumuongezea umaarufu bali yangeweza kutumika pia kama biashara kwake.

    Jose kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya kupenda kujua kila kitu akawaza kuyatumia mazungumzo hayo ya siri kujipatia chochote kitu. Jose akawaza pesa!!

    Japo hakuwa akimfahamu vyema huyo muhusika anayezungumziwa lakini aliamini akiweka jitihada atamfahamu.

    Kizuizi!! Alijiuliza, wanataka kumwekea kizuizi gani? Alikosa majibu. Na hata kama angekuwa na jibu bado hakumjua muhusika.

    Roho ilimuuma sana baada ya wawili hawa kukatisha maongezi yao. Aliumia kwa kuwa bado alikuwa hajapata stori iliyokamilika, lawama zake zilienda moja kwa moja kwa padri aliyeamuru waumini wasimame kwa ajili ya sala ya mwisho ya kufunga ibada. Jose B akahisi padri hakuwa ametenda haki.

    Lakini alifurahi kwa kuwa alipata vitu vitatu, jina la James Syaga, pili majina ya waliokuwa wakimteta (Deo na Bibiana) na tatu KIZUIZI!!

    "Hata hayo yanatosha!'' Alijisemea Jose B huku akiyakariri vyema majina hayo matatu kama vile anaenda kuweka majibu hayo katika mtihani darasani.

    Sasa alitamani misa imalizike aanze kuitumia taarifa hiyo, alihofia kuwa maneno mengi ya kukariri aliyokuwa akiyataja padri kwa kutumia kinasa sauti yangeweza kumuathiri na kumsahaulisha yale majina. Hivyo kila padri alivyokuwa akiwaamrisha kusema maneno fulani. Deo alijibu kwa sauti ya chinichini, ‘Deo, James, Bibiana na Kizuizi’. Kwa mtindo huu hakuna lililompotea kichwani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jose B, alijiona mwenye bahati sana kuwa wa kwanza kupata habari. Nitazidi kuwa maarufu!!! Aliwaza.

    Na pia nitapata pesa ikibidi.



    ***

    Maandalizi ya harusi yalikuwa yamepamba moto, simu ya James Syaga ilikuwa bize kila mara, vikao vilikuwa vinaendelea jijini Dar es salaam. Marafiki wa James hawakutaka kumwangusha kila mmoja alishughulika ipasavyo, jambo zuri kila mmoja alikuwa vyema kiuchumi.

    Milioni thelathini zilizuwa zimechangwa tayari katika vikao vitatu vya harusi. Na bado ahadi zilikuwa nyingi sana, na zilikuwa ahadi za uhakika. Kwani zilitolewa na watu wa uhakika.



    Emmy John alikuwa amechukua likizo ya majuma mawili kazini, sasa alikuwa ni mtu wa kujifungia ndani tu akisubiri kwa hamu kubwa kutimiza ndoto yake, ndoto ya kuolewa huku akiwa na usichana wake (bikra), ahadi aliyowahi kuwahaidi wazazi wake tangu akiwa katika umri wa balehe. Na kubwa zaidi ndoto ya kuolewa na James, mwanaume wa maisha yake. Emmy na James wote waliona kama siku hazisogei. Sasa tangazo la pili lilikuwa limepita, na lilikuwa limebaki tangazo moja waweze kuhalalishwa.

    James Syaga na Emmy John kuwa mtu na mke wake.

    Hiyo ndoto kila mtu aliyewafahamu wawili hawa alitamani itimie.

    Na kwa nini isitimie? Pesa zilikuwepo. James alikuwa na biashara zake na Emmy alikuwa mfanyakazi, tena anayelipwa mshahara mkubwa.

    Pande mbili za familia hazikuwa na vikwazo vyovyote juu ya ndoa hii. Familia ya Emmy ilimpenda sana James. Sasa nini cha kuzuia ndoto hii kutimia?? Hapakuwa na chochote!!!

    Wakati kila upande ukiamini kuwa hakuna kitakachoharibika. Kinaibuka kizuizi katika tangazo la tatu na la mwisho, kizuizi kipo maili nyingi sana kutoka jiji la Dar es salaam, Kizuizi kipo jijini Mwanza.

    Hakuna anayejua.



     “Ahaa!! Ok!! Naitwa Joseph Boniphace mzee wangu unanikumbuka??”

    Mzee Syaga akafikiria kwa wakati kisha akakiri kutomkumbuka Joseph, Jose B akatabasamu kisha akajisogeza zaidi kwa mzee Syaga.

    “Hata hivyo ni muda mrefu sana…anyway mimi rafiki yake na James, nimesikia anatajwa kanisani nikashtuka kweli ujue ni miaka hatujaonana!!” Jose B akaingiza kaujanja kake. Mzee Syaga akauvaa mkenge.

    Kwanza akacheka sana kwa majivuno kisha akamshika mkono Jose kama anamsalimia hivi.

    “Mwenzako ameamua kufunga ndoa kabisa, yaani nimefurahi kweli aisee…..amefanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi nimefarijika kwa kweli……” mzee Syaga hakuhitaji kumjua Jose zaidi akaanza kumwaga yake ya moyoni.

    Jose akajisikia mshindi tena katika raundi ya kwanza. Mwisho wa mazungumzo mzee Syaga akampatia Jose B namba ya simu ya James.

    Laiti kama angejua janja ya Jose B waukweli kamwe asingeitoa namba.

    Namba iliyozua balaa!!!



    Gauni la harusi na shela yake vilikuwa vimekaa vyema katika kiwiliwili cha mwanadada Emmy, ilikuwa mara yake ya kwanza kufanya hivyo mbele ya James.

    James hakuijutia milioni moja na laki mbili aliyompatia Emmy kwa ajili ya kununua shela hiyo. Hakika ilikuwa imempendeza sana.

    Hamu ya kumuoa Emmy ikazidi, wawili hawa wakawa wanatamaniana lakini wakajikaza na kuikumbuka ahadi.

    Mpaka ndoa!!!



    Wakiwa chumbani hapo, mara James alimsogelea Emmy akawa anamrekebisha gauni lake, katika kumrekebisha, kucha fupi za Jimmy zikakwangua shingo ya Emmy. Emmy akafanya malalamiko ya kimahaba, James akambembeleza naye pia kwa sauti ya kimahaba, mara wakajikuta wanatazamana usoni. Emmy akataka kuyakwepesha macho yake, James akawahi akamshika kidevu akamnyanyua wakawa wanatazamana, pumzi za Emmy zikaanza kupishana kwa nguvu, James akaligundua hilo, akazidi kumtazama Emmy. Emmy akajikuta anafumba macho akausogeza mdomo wake ukakaribia kukutana na wa James. Hakuwa akijielewa ni nini anafanya lakini alihisi yupo katikauhitaji wa kitu flani, hakika zilikuwa hisia za ajabu sana.

    James akaufungua kidogo mdomo wake ili aweze kumpokea Emmy, mara ghafla mlio mkali wa simu ya kichina ukawashtua, ilikuwa ni simu ya James. Emmy akajinasua kutoka katika mikono ya James huku akiona aibu.

    James akailaani ile simu kwa kukatisha uhondo huo, kwa shingo upande akaitoa simu na kuitazama.

    Ilikuwa namba mpya, hakusita kuipokea huku dhahiri akionekana kukereka.

    “James Syaga nazungumza hapa nani mwenzangu!!!” alihoji kwa ghadhabu kiasi fulani.

    “Joseph hapa, Jose…” upande wa pili ukajibu kwa kutetereka kiasi fulani.

    “Nadhani sikufahamu!!!” alisema kwa utulivu James huku akijaribu kuizuia ghadhabu iliyokuwa inamuandama kwa kukatishwa alichokuwa anataka kufanya.

    “Aaah!! Ndio lakini naitwa Jose….kaka kuna ishu nahitaji tuzungumze”

    “Unaweza kuzungumza.” Alijibu bila wasiwasi.

    “Upo peke yako??”

    “Tafadhali naomba uzungumze..suala la nipo peke yangu ama la hilo niachie mimi. Zungumza usemacho kijana” alijibu kwa jazba.

    “Ni biashara lakini…nd’o maana nahitaji uwe peke yako uweze kunielewa”

    “Aisee…unaweza kwenda moja kwa moja kwenye pointi yako ya msingi??” alitoa karipio, hasira ilianza kumzidia.

    “Una kizuizi katika ndoa yako..bila shaka haitafungwa kama hautafanya biashara na mimi”

    “Nini???” alishtuka Jimmy.

    “Kizuizi..kama ulivyonisikia” ilijibu kwa utulivu sauti ya pili.

    “Ki…..kipi” aliuliza huku akikosa utulivu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hicho unachouliza ndo biashara yenyewe niliyokwambia, biashara ya kizuizi”

    “Kimewekwa katika kanisa gani??” sasa alikuwa amejiweka mbali na Emmy wakati anaendelea kuzungumza.

    “Hata kulijua kanisa ni mojawapo ya hiyo biashara, kizuizi na kanisa vyote ni biashara.”

    “Ni nani wanaotaka kuniwekea”

    “Kukutajia wabaya wako pia ni kigezo kimojawapo katika biashara hii, yaani kizuizi, kanisa na wabaya wako vyote ni biashara kaka” ilijibu kwa utulivu sauti upande wa pili.

    “Upo wapi wewe.”

    “Ukitaka kunijua nilipo maana yake umeingia rasmi katika biashara je upo tayari au unataka tu kujua nilipo…”

    “Nipo tayari… nipo tayari kaka” wakati huu alizungumza kwa nidhamu kubwa.

    “Tukutane Mwanza!!!” sauti ilimjibu huku ikijiamini kisha simu ikakatwa.

    James Syaga akawa anatetemeka huku akijiuliza ilikuwaje akatokwa jasho jingi kiasi hicho. Wasiwasi ukatanda, hofu ikamtawala. Akazungumza machache na kumuaga Emmy.

    Hofu ikatembea naye njia nzima. Akafikiria na kubashiri baadhi ya vizuizi vinavyomkabili.

    Akakiri kuwa vyote havikuwa na uwezo wa kuizuia ndoa yake isifungwe, na vichache vyenye uzito vilikuwa siri yake. Sasa kulikoni hii simu kutoka huko inapotoka??

    Tafurani.....



    ***



    Jose B waukweli alijikuta katika maisha yake anawaza jambo ambalo hapo kabla hakuwahi kuliwaza. Utajiri!!! Na pesa zisizokuwa za jasho lake. Awali Jose B alikuwa akitumia tabia yake ya kujua mengi kutafutia sifa na umaarufu mtaani, ni yeye alikuwa wa kwanza kufahamu juu ya msiba mkubwa wa msanii maarufu wa filamu, ni yeye pia aliyeisambaza taarifa ya kuvishana pete ya msanii wa muziki Tanzania na aliyewahi kuwa mrembo wa Tanzania. Haya yote yalimwezesha kupata sifa kemkem. Hili la sasa lilikuja kivingine.

    Pesa.

    Ile hofu iliyomkumba James wakati wanazungumza kwenye simu ilimtia jeuri na hamasa zaidi. Akiwa katika moja ya chumba kimoja katika nyumba ya mzee Boniphace ambaye ni baba yake mzazi. Jose B alikuwa akikitazama kile chumba katika namna ya kukichoka, hakika ilikuwa lazima akichoke kwani kilikuwa hakina sealing board, hakikuwa na feni wala marumaru. Halafu kama hiyo haitoshi Jose alikuwa amezichoka karaha za kuishi na wazazi wake. Kila siku mama yake alimchukulia kama mtoto, alikuwa akimgombeza mbele ya wadogo zake bila kujali kuwa Jose alikuwa na umri wa miaka ishirini na tatu tayari. Jose akaanza kufikiria juu ya kuhama, ili apate uhuru wa kutosha uhuru wa kujivinjari na mpenzi wake Diana.

    Redio kubwa inayotumia santuri ‘CD’ iliyokuwa inamilikiwa na rafiki yake ilimuingiza katika matamanio. Naye akatamani kuwa nayo.

    Jose B akamgeuza James mtaji, huku Kizuizi kikiwa ngao yake kuu.

    Pesa nje nje!!! Akajisemeza na nafsi yake kisha akaachia tabasamu mwanana akajifunika shuka!!!



    ***



    James alikuwa katika sintofahamu, alijiuliza ni nani huyo anayetaka kuingilia mipango yake ya kufunga ndoa. Alijiuliza tena ni nani anayetaka kumtia katika aibu, aliwafikiria rafiki zake waliotoa michango yao, walivyoacha majukumu yao mengine na kuamua kuisimamia shughuli yake iende sawa.

    Leo hii anajitokeza mtu kumwekea kizuizi!! Hapana ilikuwa lazima achanganyikiwe.

    James aliwaza mambo kadhaa ambayo yangeweza kuwa kizuizi cha yeye kufunga ndoa. Hakika vizuizi vilikuwa vingi sana lakini karibia vyote vilikuwa ni siri yake. Hakuna mtu alikuwa akivifahamu waziwazi, hata mzazi wake hakuwa akielewa siri za mwanaye. Kasoro baba tu!!

    Baba hawezi kuvujisha siri zangu!! Alipinga palepale na kujizuia kumwazia vibaya baba yake.

    “Ni nani huyu amefahamu siri zangu???” alijiuliza James bila kupata jawabu.

    “Aliyepiga simu si mpumbavu ni mtu mzima na akili zake, lazima kuna jambo hapa, sitakiwi kupuuzia.” James alizidi kutilia mkazo suala hili. Huku akiwa makini katika usukani wa gari aliyokuwa anaendesha.

    James alipofika nyumbani kwake alipiga simu ya Jose. Ikapokelewa upesi. Wakazungumza mengi huku Jose akisisitiza kuwa hayupo tayari kufanya biashara kwa njia ya simu.

    “Hayupo tayari kufanya biashara kwenye simu????” alijiuliza James na kuzidi kupata mashaka juu ya uzito wa biashara hii iliyopo mbele yake. Kama haizungumziki kwenye simu basi ni jambo zito!!! Alikiri James.

    Pesa ni kila kitu!! Baada ya kumaliza mazungumzo na Jose, alipiga namba fulani simu ikapokelewa na mwanadada. Baada ya mazungumzo ya dakika tatu James akapata nafasi katika ndege ya kusafiri siku inayofuata kuelekea jijini Mwanza. Safari hii ilikuwa ya siri sana hakumwambia mtu yeyote yule kama atasafiri. Kwani alitegemea kurejea siku hiyo hiyo. Ama kesho yake mapema.

    “Nitakupigia simu kesho nikiwa Mwanza” James alimwambia Jose kisha wakaagana.

    Jose B alijirusha rusha kwa furaha pale kitandani, furaha yake ilikatishwa na chaga za kitanda kile kufyatuka, Jose akajikuta anasalimiana na sakafu mbovu ya chumba kile. Huku akiwa amekasirika sana alikirekebisha kitanda na kuulaani umasikini kwa lugha zote alizozijua.

    Usingizi ukampitia, mlio wa simu yake ukamshtua siku iliyofuata. Alikuwa ni James!!

    “Nambie bro!! nipo Mwanza tayari, tuonane wapi kaka” Sauti ya James ilisikika ikinyenyekea. Jose akatabasamu.

    “Poa nambie ulipo mi nakuja”

    “Kamanga feri huku..unapajua”

    “Mwanza ndo home kaka najua kila kona!” alijibu Jose kwa furaha.

    “Poa basi nipo pande hizi ukifika karibu na haya mawemawe makubwa nibip”

    “Shwari!!”

    ***

    Majira ya saa sita mchana Jose alikuwa amekaa katika meza moja na James. Ilikuwa mara yake ya kwanza kumuona.

    Kule kujiamini kwa Jose wakati anatoka nyumbani kuliingia katika mgogoro baada ya jicho lake kumwona James. James alikuwa na hadhi ya juu sana, na mwonekano wake pekee ulitosha kuutangaza ukwasi wake. James alionekana kuwa kati ya watanzania wachache wanaofaidi matunda ya nchi hii.

    “Yap!! Jose….ni biashara gani”

    “Kizuizi”

    “Kipi?”

    “Nitangazie dau tuanze biashara!!”

    “Wewe ndiye mwenye biashara kaka…anza!!” James alijibu bila kuwa na hofu yoyote.

    Jose B akazungusha akili upesi upesi akaona akitaja pesa nyingi ataonekana mwenye tamaa sana, pia akahofia kutaja dau dogo kwani angeweza kuonekana mwongo na asiyejua biashara. Akaifikiria pesa ambayo kwake itakuwa faida zaidi.

    “Milioni moja!!” akataja kwa uoga huku akijiuliza iwapo ni kubwa ama ndogo sana.

    “Nitakupa milioni sita….tumalize

    Biashara.” James alimjibu Jose. Soda aliyokuwa anakunywa ikampalia. Jose hakutegemea kusikia dau likipanda maradufu kiasi hicho. Ilikuwa ndoto kusikia pesa kama hizo. Isitoshe tangu azaliwe hakuwahi hata kumiliki shilingi laki moja.

    Jose akaamini ilikuwa siku ya muujiza kwake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Milioni mbili ikawekwa mezani ikiwa ishara ya kuanza biashara, Jose alizikusanya huku akitetemeka. Hakuhesabu badala yake aliziweka kwa fujo katika mfuko wake.

    Baada ya hapo Jose akageuka kasuku, akaanza kutiririka kila neno alilolifahamu. James akawa kimya anameza.

    Akasimulia kuanzia mkasa wa kanisani, tangu lilipotangazwa tangazo la ndoa.



    ****



    Bibiana alitamani sana kuwasiliana na paroko siku ile ile baada ya ibada lakini paroko akawa ametingwa na majukumu mengi hivyo akamwahidi kuwa amwone baada ya siku tatu yaani siku ya jumatano. Bibiana alipaona mbali sana lakini hakuwa na ujanja ilimlazimu kuvumilia.

    Mawasiliano baina yake na Deo yaliendelea kwani lao lilikuwa moja.

    Siku ya jumatano wakapanga waende wote kumwekea kizuizi James.

    Kizuizi cha kumzuia asifunge ndoa na Emmy.

    Ilikuwa siku ya jumanne, siku moja kabla ya kufika ile siku ambayo Bibiana alikuwa amepanga kumtembelea paroko kwa ajili ya kuweka pingamizi la James kufunga ndoa.

    Alikuwa ametoka kuhemea mahitaji kadhaa katika soko maarufu la ‘Mwendesha’. Ulikuwa ni mchana tulivu sana kwani asubuhi ya siku hiyo kimvua cha rasharasha kilikuwa kimenyesha.

    Alipofika nyumbani na kukitua kikapu chake, alipata ugeni wa ghafla. Walikuwa ni wanaume wawili waliopendezea katika suti zao, lakini walikuwa wameyaficha macho yao nyuma ya miwani. Mmoja alionekana kuwa mwenyeji kiasi eneo hilo huku mwingine akionekana kuwa mgeni.



    “Bibiana Michael!!!” alisikia sauti ikimwita, akajiweka vyema kuwatazama wageni wake huku akiunda tabasamu la kuwakaribisha wageni.

    Ghafla bila kutegemea alishangaa kukutanisha macho yake na mtutu wa bunduki, kabla hajafikiria kupiga kelele. Alikutana na macho makali kisha onyo!!!

    Akakaa kimya!!!

    “Nani yupo ndani??”

    “Peke…peke yangu!!!”

    Ishara ya kutangulia ndani ikamwongoza akaingia ndani.

    Bibiana akaketi kwa uoga mkubwa, wale wanaume hawakuketi, jicho la bunduki likaendelea kumtazama binti yule.

    “Bibiana…sina muda wa kupoteza. Unataka kumwambia nini paroko kuhusu ndoa yangu? Ujue wewe unajifanya kunijua sana, mimi kukutana na wewe huko vijijini kwenu isiwe tija ya kujifanya kunijua. Maisha yangu hayakuhusu Bibiana hujachangia chochote katika maisha yangu, tafadhali yaache yalivyo!!! Ok! Upesi nijibu..”

    Bibiana alikutana na macho makali ya James, alikuwa tofauti sana na yule James aliyemzoea miaka kadhaa nyuma. James huyu alitangaza ukatili waziwazi.

    Wakati Bibiana akitoa macho bila kujua cha kujibu. James alitoa ishara ya ghafla. Na pale pale likafanyika tendo la kushtukiza.

    Bibiana akalainika taratibu, akaanza kuliacha kochi alilokuwa amekalia, akasalimiana na vigaye vilivyokuwa ndani ya sebule yao bila kupenda. Akanyooka!!!!

    Kimya kikatawala!!!!



     Bibiana alikuwa ametishika haswaa na ujio wa ghafla wa James nyumbani kwake. Mwanzoni alidhani kuwa ilikuwa ni kwa nia njema lakini baada ya kushuhudia jicho la bunduki akatambua kuwa hapakuwa na amani tena.

    Kabla hajaelewa kwanini afuatwe na bunduki nyumbani kwake, nyumba ya kimasikini isiyokuwa na chochote cha kuweza kupora. Bibiana alijikuta ameelekezwa kwenda ndani, James asiyekuwa na huruma hata chembe usoni alimuuliza ni kitu gani alitaka kushtaki kwa paroko ili kuzuia ndoa yake isifungwe. Bibiana alijikuta anatetemeka badala ya kujibu kile alichokuwa anaulizwa.

    Hofu yake haikumsaidia lolote, alitakiwa ajibu ni siri gani alitaka kuipeleka kwa paroko. Neno moja alilotamka Bibiana lilitosha kumshawishi James aliyekuwa ameikamata vyema bastola yake aliyokuwa anaimiliki kihalali kabisa, kuminya kiwambo cha kuzuia sauti kisha akafyatua risasi iliyopenya vyema katika mbavu za Bibiana ikimweka katika ladha yenye ubaridi unaofurahisha kisha maumivu makali ya kushangaza na mwisho kuzitenganisha.

    Lile neno alilotamka Bibiana, James hakujua kama lilisikiwa na yule mtu waliyekuwanaye ama la. Kwa wakati huo hilo hakulijali sana badala yake alimfuta Bibiana zile sehemu walizoweza kugusana. Alifanya hivyo ili kuondoa zile alama za vidole ambazo zingeweza kumuingiza matatani iwapo upelelezi wa kina ungefanyika.

    Lakini kwa maisha duni ya marehemu Bibiana huo ulikuwa mwisho wa habari. Hakuna utafiti wa ziada ungeweza kufanyika.

    Siri kubwa aliyokuwanayo Bibiana ikampelekea kukumbana na mauti yake. Kizuizi kisichomuhusu kikaitwaa roho yake bila hiari yake.

    Bibiana akageuka hayati Bibiana!!!!

    Ukurasa wake katika kitabu cha simulizi ya maisha ya duniani kikawa kimefunikwa hapo hapo!!!



    *****



    Jose B hakuamini kabisa kama kwa maneno yake aliyompatia James yangeweza kuwa na thamani hata ya shilingi elfu kumi sasa alikuwa na shilingi milioni mbili mfuko mmoja na mfuko mwingine alikuwa na shilingi laki moja aliyopewa kwa ajili ya nauli yake kurudi nyumbani na pia kwa ajili ya kulipia taksi watakapohitaji kukutana tena.

    Jose B Waukweli, alikuwa akizidi kushangaa kuwa James hakuhitaji hata kujua huyo Bibiana anaishi wapi.

    “Yaani majina mawili tu yamenipatia milioni mbili???” alijiuliza Jose huku akiwa makini kabisa na mifuko yake wasije wakatokea vibaka na kumkwapulia mavuno yake. Mavuno ya kutibua siri.

    “Au jamaa alikuwa amelewa ametoa bila kujua???” hakuwepo wa kumjibu Jose B. Jose Waukweli. Akapuuzia maswali aliyokuwa anajiuliza, akazidi kukaza mwendo akafika kituoni akataka kupanda daladala lakini dhamira ikamsuta akahofia kukabwa na vibaka.

    Akanyata hadi zilipokuwa taksi.

    “Hadi Nyakato shilingi ngapi??” Jose akamuuliza dereva wa teksi.

    “Elfu sita kaka..” alijibiwa.

    Jose B wa ukweli akakumbwa na pepo la ubahili akaiona elfu sita nyingi sana. Akaomba kupunguziwa huku akijiapiza kichwani kuwa kama hatapunguziwa basi anaghairi kupanda teksi. Bahati nzuri akapunguziwa ikawa 5000, Jose akaingia ndani ya teksi, dereva akaondoa kuelekea Nyakato Sokoni.

    “Ningejua ningesema elfu nne...huenda angekubali.” Jose b aliwaza huku akijilaumu kukubali kulipa ile gharama ya elfu tano.

    Baada ya dakika kumi, Jose akashuka ndani ya teksi akiwa amemlipa dereva gharama aliyokuwa ameitaja.

    Hatua ya kwanza tu iliyokanyaga ardhi, Jose B akajihisi yu tofauti, alijihisi kama amekuwa mwepesi sana na ana uwezo wa kupaa, akajiuliza ni nini kinamfanya kuwa hivyo, upesi akapata jibu kuwa ni pesa.

    Jose alijitahidi sana kujiweka katika hali ya kawaida lakini haikuwezekana alitamani sana kumwambia mtu jambo lililomtokea lakini ubinafsi nao ukamkumba akagundua kuwa akimwambia mtu basi huyo mtu lazima atamwomba kiasi cha pesa. Naye hakuwa tayari kutoa chochote kile.

    Jose akaamua kubakia na siri yake. Akaingia hadi chumbani mwake akajifungia akafunga na madirisha akazima simu akazitoa pesa.

    Zilikuwa pesa halali kabisa!!!

    Jose hakumaliza kuzihesabu baada ya kugundua kuwa alikuwa anatetemeka hivyo kila mara kukosea mahesabu. Harakaharaka kama vile kuna mtu alikuwa anakaribia kuingia alizikusanya pesa zake na kuzihifadhi katika begi lake la nguo. Kisha akajinyoosha kitandani akajaribu kusinzia ikashindikana. Hakuwa na amani hata kidogo.

    Akiwa katika kugalagala kitandani, mara ghafla akaikumbuka sauti ya mdogo wake wa kiume akiwa anamlalamikia mama yake kuwa amerudishwa nyumbani kwa kuwa hajalipia pesa ya kiti na meza. Akaisikia sauti ya mama yake ikimjibu, “Subiri baba yako akirudi umwambie mimi sina pesa”, baba aliporudi Jose hakuwepo lakini siku iliyofuata mdogo wake hakwenda shule na siku ya pili yake pia ikawa hivyo hivyo.

    Jose akainuka upesi, akavaa kandambili miguuni mwake.

    “Frediiiiii!!!!.” Aliita kwa amri kuu. Sauti ikamfikia Fred ambaye ni mdogo wake.

    Hakuitika akaja kimya kimya.

    “Kwa nini hauendi shule siku hizi?” Akauliza. Fred hakujibu akatabasamu, ni kama hakutegemea swali kama lile ghafla kiasi kile. Haikuwahi kutokea hata siku moja kaka yake huyo akamuuliza juu ya mambo ya shule. Leo vipi?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nadaiwa pesa ya michango shuleni” alijibu kwa sauti isiyo na tumaini lolote..

    “Shilingi ngapi?.” Aliuliza kama mzazi.

    “Elfu ishirini.” Alitamka kwa sauti iliyoonyesha kukata tamaa na kuhisi kubughudhiwa na kaka yake. Kwa ishara za vidole Jose akamwita mdogo wake naye akamfuata kwa nyuma. Walipokikaribia chumba, Jose akamwambia asubiri kwa nje. Akatii.

    Baada ya dakika mbili!

    “Kesho nataka uende shule sawa!!!” Jose alizungumza huku akimkabidhi mdogo wake shilingi elfu thelathini. Fred alizipokea huku akiwa katika kutoamini maana tangu azaliwe ilikuwa mara ya kwanza kupokea pesa nyingi kama hiyo kutoka kwa kaka yake. Akashukuru mara mbilimbili akaondoka asimini kama ni kweli ama anataniwa!!.

    “Hiyo shule yenu inafundisha vizuri kweli ama?.” Aliuliza wakati Fred anaanza kuondoka.

    “Hivyo hivyo si unajua shule za serikali kaka.” Alijibu kwa unyonge.

    “Ok! Nitalifanyia kazi hilo” Alijibu kwa ujivuni huku akiwa ameridhika na kujaribu kusugua tumbo lake kana kwamba ana kitambi.

    Jose alikuwa kama anamiliki milioni mia.



    *****



    Emmy alishangazwa sana na safari ya ghafla iliyofanywa na mume wake mtarajiwa, lakini hakuwa na malalamiko yoyote kwani hiyo ilikuwa ni mara ya pili tangu wawe katika mahusiano kwa James kusafiri ghafla bila kuaga.

    Hali hiyo ya kutokuwepo kwa James ilimtia katika upweke. Kwani walikuwa wameahidiana kwenda ufukweni kujiliwaza katika siku hiyo. Hivyo Emmy hakujisikia kabisa kubakia nyumbani, lakini hakuwa na pahali pa kwenda.

    Akiwa katika chumba chake Emmy aliamua kupoteza mawazo kwa kuangalia filamu mbalimbali, nyingi zikiwa zinahusiana na maisha ya mahusiano ya kimapenzi na ndoa kwa ujumla. Kati ya filamu alizokuwa akiangalia nyingi zilikuwa zimeigizwa na wahindi.

    Akiwa amezama katika dimbwi la kutafakari filamu hizo, alisikia mlango wake ukigongwa.

    “Ingia!!” Aliruhusu.

    Aliyekuwa anagonga mlango alipojaribu kufungua haukufunguka, ndipo Emmy akakumbuka kuwa alikifunga kitasa kwa kutumia funguo. Taratibu akaichukua kanga yake akajifunga vyema na kuuendea mlango akaufungua. Alikuwa mama yake.

    “Mama nawe!! Ushanikatisha tena filamu yangu.” Alianza kudeka Emmy akimlaumu mama yake kuwa amemsumbua.

    “Sio mimi mamangu, una mgeni jamani na simu hata hupokei.” Alijibu mama yake Emmy huku akimfinyafinya Emmy mashavu yake laini kabisa.

    “Nani tena mama sasa hivi….nawe mbona umeng’aa hivyo unaenda wapi tena mama?? unataka kuniacha mwenyewe hivyo”

    “Mimi naenda kwenye ‘Vikoba’ mwanangu ushasahau?...ni Lameck amekuja” akamnong’oneza. Emmy akashtuka kidogo. Ni kama hakuitegemea taarifa hiyo kutoka kwa mama yake.

    “Yupo wapi?.” Aliuliza huku akiwa anatabasamu la mshangao

    “Sebuleni amejaa tele anakusubiria.”

    “Haya nakuja mama…” Aliaga Emmy na kurejea ndani. Akavaa vyema akajipodoa kidogo kisha akajongea sebuleni.

    Macho yake yakakutana na macho ya Lameck, wakajikuta wote wanatabasamu. Ilikuwa ni miaka mingi sana imepita tangu wawili hawa watengane.

    Lameck alikuwa ni baba yake mdogo na Emmy, lakini kwa umri waliendana kabisa, kwani Lameck alikuwa mtoto wa mwisho katika familia ya baba yake na Emmy mzee John Nchimbi. Lameck na Emmy walikua pamoja wakicheza wote, ile heshima ya baba mdogo ilisalia katika jina tu lakini kimatendo walikuwa ni walewale.

    Katika utoto wao walicheza michezo mingi sana ikiwemo ule wa kibaba na mama huku katika kombolela pia wakikumbuka jinsi walivyokuwa wanajificha pamoja.

    Baada ya kumaliza darasa la saba walichaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza, Emmy akatupwa Maswa shule ya wasichana huku Lameck yeye akipelekwa shule ya kata hapohapo jijini Dar es salaam.

    Huo ukawa mwanzo wa wawili hawa kupunguza ukaribu. Lakini kila likizo waliweza kuwa pamoja katika kusoma masomo ya ziada.

    Baada ya kumaliza kidato cha nne, walikutana tena jijini Dar es salaam. Katika kipindi hiki ndipo yalitokea haya yanayowafanya washangaane na kucheka kwa pamoja.

    Emmy na baba yake mdogo wakaanza kutamaniana kimapenzi. Walijaribu kuzuia hisia zao lakini hawakufanikiwa.

    Walipokuwa wakipata upenyo wakiwa wawili, walikuwa wanakumbatiana, na kubusiana huku kila mmoja akijisahaulisha juu ya udugu wao.

    Jambo ambalo hawakufanikiwa kulitenda ni kufanya tendo la ndoa kwani kila mara walipotaka kujaribu Emmy alikuwa analia kuwa anaumia kwa sababu kamwe hakuwahi kufanya tendo hilo, alikuwa ‘bikira’.

    Lameck hakutaka kulazimisha akawa anaacha. Alikuwa na huruma sana na hakupenda kumuumiza Emmy ambaye kwake alikuwa mtu wa karibu zaidi..

    Ngoja ngoja ya Lameck, mara matokeo ya kidato cha nne yakatoka, Emmy akarudishwa shule za wasichana Msalato Dodoma. Lameck hakufaulu, baba yake mzazi akaamua kumpeleka jeshini.

    Inapita miaka, mawasiliano yanapungua na sasa Emmy afisa mikopo katika benki ya serikali NMB anakutanisha macho na Lameck mwanajeshi kamili kambi ya Makambako Mbeya.

    Wanashindwa kujizuia kucheka wanalipuka kwa vicheko wanakimbiliana na kukumbatiana kwa takribani dakika mbili.

    “Hayooo!!!!” mama Emmy anawazomea kiutani alipowakuta wamekumbatiana. Wakajishtukia wakaachiana. Kila mmoja akiwa amebadilika usoni na kulengwa na machozi

    “Mi naenda hivyo Emmy…ngoja niwaache baba na mwana mbadilishane mawazo….shemeji baadaye..” aliaga mama Emmy na kuondoka akiwaacha nyuma Lameck na Emmy wakiendelea kushangaana.



    Siku hiyo ya kwanza waliyokutana hakuna aliyekumbushia mambo waliyofanya zamani. Ilionekana kana kwamba wote waliamini kuwa ule ulikuwa ni utoto ambao ulikuwa umepita na haukutakiwa kurudi kwa gharama yoyote ile. Kila mmoja alikuwa amepevuka na alikuwa anajitambua. Walizungumza mengi kisha Lameck akaaga na kuondoka.

    “Unakaa wapi siku hizi??.” Emmy aliuliza wakati Lameck anaondoka.

    “Nipo Makongo karibu na kambi ya jeshi kule.” Alijibu kwa utulivu.

    “Nitakuja siku moja kukutembelea.”

    “Karibu sana. unapajua lakini??”

    “Mhhh no!. si utanielekeza jamani...” alilalamika kizembezembe Emmy, sauti yake ikamsisimua Lameck.

    Lakini angefanya nini iwapo alikuwa ameamua kujizuia??



    ***



    James Syaga alitoweka eneo la National, akiongozana na bwana waliyefika naye nyumbani kwa Bibiana kisha kufanya mauaji ya kimyakimya. Waliingia katika gari waliyokuwa wameiegesha mbali kidogo kutoka alipokuwa anaishi marehemu. Huyu bwana waliye kuwa naye hakuwa akimfahamu hata jina ila aliunganishwa na rafiki yake kwa ajili ya kumpatia kampani awapo jijini Mwanza, kampani ya kupata silaha na kufanya mauaji ya upesi na kimyakimya Hasahasa ushirika wa kiusalama iwapo lolote baya linaweza kumtokea. James alichukua maamuzi haya baada ya kufikia maamuzi ya kumuua Bibiana ili kuondoa kero aliyotaka kumletea kwa kumwekea kizuizi. Kizuizi cha kukikwamisha ndoa yake aliyoiota kila siku ya kummiliki Emmy kama mke. Tena akiwa bikira.

    Wakiwa kwenye gari wanaondoka yule bwana alimuuliza James kitu cha kushtukiza ambacho hakukitegemea.

    “Kaka alichosema yule demu pale ni kweli ama?”

    James alitulia kwa sekunde kadhaa kabla ya kumjibu, alijua kuwa anamuulizia Bibiana, kitu ambacho hakutaka katu kukisikia

    “Tutazungumza tukifika” alitoa jibu fupi.

    Kichwani mwake James alichezwa na machale kuwa laiti kama atazungumza kitu chochote na yule bwana ni sawasawa na kuisambaza siri yake kwa mtu mwingine tena. Kichwani mwake akamwonea huruma sana huyu bwana asiye na hatia kwa kiherehere chake cha kutaka kujua yasiyomuhusu. Kutaka kwake kuijua siri yake alikuwa amejihakikishia tiketi yake ya mapema kabisa kutengana na ulimwengu. lilikuwa kosa kubwa kuyaruhusu masikio yake kusikia alichokisema Bibiana kabla ya kuaga dunia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa hivyo. James alizunguka sana na yule jamaa aliyeonekana kufurahia kuzitumbua pesa za bwelele katika hoteli za kifahari kula vyakula ambavyo hapo kabla alikuwa hajawahi kuvitia katika tumbo lake.

    Safari ya mwisho ilikuwa majira ya saa mbili usiku, palepale James alipokutana na Jose B wa ukweli, eneo ambalo alitoa kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kununua taarifa ya kuwekewa kizuizi. Taarifa iliyofanikisha kifo cha Bibiana.

    Yule bwana hakuwa akijua lolote lililokuwa mbele yake, tabasamu la James lilimhadaa na kujiona yupo salama. Eneo lilikuwa limetulia sana, hapakuwa na watu wengi kama inavyokuwa siku za mapumziko yaani jumamosi na jumapili.

    James alikuwa akimhesabia bwana waliyekuwanaye dakika za kuendelea kuishi.

    “Hivi ulisema unaitwa nani??” James alimuuliza.

    “Derick…aah!! Naitwa Derick…” alijitambulisha huku akijikunyata kupambana na upepo ulioleta kiubaridi kutoka ziwani.

    “Unaitwa Derick eeh!! Ok kamwambie Bibiana kisabengo chake kimemponza..” alijibu James.

    “Bibiana tena kwani…” kabla hajamaliza alijikuta ndani ya ziwa Victoria akijaribu kufanya juhudi za kulichafua ziwa hili maarufu Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa rangi nyekundu zilizokuwa zinamtoka mwilini. Maji ya ziwa Viktoria yakamshinda nguvu akazama mara ya kwanza na ya pili kwa kutapatapa. Alipozama mara ya tatu hakurudi juu.

    Samaki hawakuwa wakubwa kiasi cha kuugawana mwili wa Derick. Hatimaye kesho yake asubuhi wale wakongwe wa kukaa katika mwamba maarufu wa ‘Bismark’ wakagundua kuwepo kwa mwili wa mwanadamu eneo lile.

    Taarifa za kifo hicho zilichukuliwa katika hali ile ile ya ‘upelelezi unaendelea’.

    Magazeti ya Mwanza yakapata cha kuandika siku iliyofuata vifo viwili kwa kutumia bunduki. Huku Derick huku Bibiana.

    Chanzo hakikujulikana.

    Sasa nafsi ya James ilikuwa imetulia na aliamini kuwa suala lake la kufunga ndoa lingeendelea kuwa salama.

    Wazo la kumpigia simu Jose ili wamalize biashara ndio lilimfanya asifikie uamuzi wa kulala mapema badala yake akaamua kuonana na Jose usiku huo huo ili aweze kumalizana naye kwani habari aliyompa kwa kiasi kikubwa imemsaidia kuokoa ndoa yake.

    Bahati mbaya simu ya Jose haikuwa ikipatikana.

    James akaghairi kupiga simu uwanja wa ndege kwa ajili ya kuulizia nafasi ya kusafiri siku inayofuata.

    Usiku huo aliwaza mengi huku akimuunganisha Jose B kati ya wanadamu wanaotakiwa kufa ili aweze kubaki huru kabisa na ndoa yake ifungwe salama.

    “Nitampatia hiyo pesa kisha nitamuua…kwanza simjui asije kunigeuka tena huyu” alijiapiza James kabla hajalala.

    Akasinzia huku akimuwaza Jose B. Akiwaza jinsi ya kumuondoa duniani kimyakimya.



     Mawazo aliyokuwanayo Jose B sasa alitaka kuyabadili na kuwa vitendo kamili. Wazo lake la kuondoka nyumbani na kuishi maisha ya kujitegemea katika nyumba ya kupanga lilimfanya aamue kutembea huku na huku na madalali wakimwonyesha nyumba za hadhi aliyokuwa anataka.

    Jioni ya siku ya jumanne Jose alikuwa chumbani kwake. Daftari mezani kalamu mkononi akipiga mahesabu ya jinsi atakavyoanza maisha mapya. Akaanzia kodi ya nyumba yenye choo na bafu ndani, isikose marumaru, kitanda cha futi sita kwa sita, mziki mnene, godoro lenye hadhi ya kuitwa godoro, luninga bapa, nguo za kisasa, kabati kwa ajili ya kuzihifadhia hizo nguo, meza, viti, ‘dressing table’, makochi aina ya sofa ya kisasa. Kama hiyo haitoshi Jose B akawazia pia kununua ka-pikipiki kadogo kwa ajili ya mizunguko ya hapa na pale jijini Mwanza watoto wa mjini wanasema ka-kuuzia sura, na pia kumhamisha mdogo wake shule.

    Mshtuko!! Jumla ikazidi pesa aliyoimiliki, Jose akaumia sana. Malengo yake yakaanza kuingiliwa na kizingiti. Pesa ilikuwa haitoshi. Na hakuna hata kitu kimoja alichotaka kukikosa kati ya orodha aliyoiandika katika daftari lake.

    Ghafla wazo la pili likamvamia, akajiweka katika utulivu. Akafunika daftari lake akaanza kuiumauma kalamu yake. Ikajijenga picha ya mwanamke mrembo wa haja, akiwa na furaha sana, hakuwa peke yake alikuwa na wenzake watatu wote walikuwa wakimsikiliza huku wakiwa na dalili zote za kumwonea wivu. Alikuwa anazungumzia suala la ndoa yake ambayo inatarajiwa kufungwa hivi karibuni.

    Jose B naye akajiweka katika mazungumzo hayo japo hakutia neno lolote lakini alinukuu vitu fulani. Alipotoka katika mawazo hayo Jose B akaibuka na wazo la kujiongezea pesa.

    Pesa kutoka kwa mke mtarajiwa wa James. Ladha ya biashara aliyoianza kwa mafanikio ya kuuza habari ikawa imemkolea. Jose akawa ameamua kuangalia uwezekano wa kuiuza habari hii mara mbilimbili. Kwanza ameiuza kwa James na sasa alihitaji kuiuza kwa Emmy.

    “Ili iwe tamu zaidi lazima nikijue hicho kizuizi.” Alijisemea Jose B huku akijilaza kitandani. Jose akavuta kumbukumbu zake na kupata jawabu la ni wapi ataanzia, akamfikiria Bibiana ndiye atakuwa suluhisho la tatizo lake.

    “Huyu nikimpa kama elfu ishirini hivi lazima aniambie tu!!.” Alijiapiza Jose huku akimuwazia Bibiana kama mtu masikini sana ambaye hiyo pesa itakuwa kama almasi kwake.

    Uamuzi huo ukawa sahihi katika kichwa chake. Hatua iliyofuata ikawa kuzima simu. Hakuzihitaji tena hizo milioni nne zilizobaki mikononi mwa James kwani aliamini kuwa kwa kumuuzia mwanamke habari atapata malipo maradufu kwani aliwatambua wanawake kuwa ni dhaifu sana.

    Jose B Waukweli akaamua kuzima simu yake ili James asiweze kumpata hewani pindi atakapomtafuta kwa ajili ya kumaliza biashara.

    Ni wakati huo huo James alikuwa akijaribu kumpigia ili waweze kuonana kwa ajili ya kumalizia malipo na kuiondosha roho yake.

    Kuzima kwake simu kukaisalimisha roho yake.

    Laiti kama angeyajua mawazo ya James….

    Angejipongeza maradufu kutokana na uamuzi wake ule wa muhimu zaidi!!



    *****



    Chumba kilikuwa tulivu, hapakuwa na maongezi tena kama ni stori za utotoni zote walishazungumza tayari kama ni kukumbushiana jinsi walivyotengana yote yalikuwa yamewatoka vinywani. Habari za jeshini na ugumu wa kuwapa akina mama wasiojua kusoma wala kuandika mikopo yote walikuwa wamesimuliana na kila mtu kumpa pole mwenzake kwa ugumu wa kazi anayoifanya.

    Kuna jambo walikuwa wanalirukaruka hawalisemi lakini sasa mioyo yao ikaamua kuzungumza, macho yakainuka kuiwakilisha mioyo.

    Chumba kikawa kimya, sasa pumzi zao zikawa zinasikika zikipishana kwa kasi. Mjeshi akausahau ujasiri na afisa mikopo akauweka pembeni ule umakini wake akiwa kazini. Kazi ya kuhesabu pesa za wateja.

    Kumbukumbu zikarudi miaka kadhaa nyuma, elimu ya chuo kikuu ikakikimbia kichwa cha Emmy, mikikimikiki ya kwata za jeshi la wananchi Tanzania ikausahau mwili wa Lameck.

    Ubaba mdogo na u-mtoto wangu ukatoweka ghafla. Mapenzi yakang’ara machoni, subira ikajificha. Bwana harakaharaka akaibuka. Tamaa akaongozana naye, hulka akamwamsha shetani aliyekuwa amelala. Shetani akamuua uvumilivu ndani ya mwili wa Emmy, akamsahaulisha juu ahadi nyingi alizompa James. Hisia akapata uhai na utawala katika serikali ya miili miwili kwa pamoja.

    Macho ya Lameck yakajaa huba kuliko yale ya James. Emmy akaligundua hilo, bila kutarajia akajikuta anamsogelea Lameck. Lameck upesi upesi akajikumbusha mazoezi ya kubeba vitu vizito jeshini. Akambeba Emmy mzegamzega hadi chumbani. Kitanda kikawatazama kwa namna ya kuwahitaji sana, mashuka meupe yakawavutia wote.

    Emmy akiwa kama aliyepoteza fahamu akajikuta uchi wa mnyama juu ya kitanda kile. Baadaye……………

    Baada ya saa zima fahamu zikamrejea, shuka hazikuwa nyeupe tena bali kuna nakshi nyekundu zilikuwa zimejichora na kutia kinyaa kuzitazama!!

    Emmy hakuwa akiweza kutembea upesi. Alikuwa mfano wa mwanaume aliyefanyiwa tohara.

    Hakuna aliyemwangalia mwenzake usoni!!!!

    Bikra iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya James kwa kiapo cha ‘MPAKA NDOA’ ikavunjika mbele ya mjeshi kamilifu.

    Ndugu wa karibu kabisa!!



    ***



    Usiku wa mang’amung’amu ulimkumba Jose, alitamani asubuhi ifike upesi ili aweze kutimiza azma yake aliyoipanga ya kumwongezea kipato.

    Japo alichelewa sana kuupata usingizi lakini hatimaye usingizi ulimpitia na asubuhi aliyoihitaji ikafika.

    Aliwahi kuamka kabla ya wote pale nyumbani. Akafagia uwanja. Akajisafisha mwili na kisha akachomoa kwa tahadhari kubwa noti nyekundu nyekundu sita akaziweka katika pochi yake. Akaondoka.

    Saa mbili asubuhi akiwa na rafiki yake aliyempeleka mahali alipokuwa anaishi Bibiana, kauli mbiu ya ‘biashara asubuhi jioni mahesabu’ ndio chanzo cha kuwahi sana.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Eneo lilikuwa na watu wengi sana, ni kama aidha ilikuwa harusi ama msiba. Jose akajipenyeza kimyakimya katika umati wa watu matusi aliyotukanwa kwa sababu ya kuleta usumbufu wa kusukuma sukuma watu hakuyajali sana alichokuwanacho makini ni pochi yake mfukoni.

    Hatimaye alifika mbele kabisa. Akakutana na askari wakamzuia asiendelee zaidi.

    Maneno maneno ya watu yakamshtua. Kuna jambo la kushangaza lilikuwa limetokea pale nyumbani kwa akina Bibiana, kulikuwa kuna tukio la mauaji.

    Dakika kadhaa baadaye mwili ukatolewa ndani. Kwa kuwa Jose B alikuwa mbele aliitambua sura ya Bibiana.

    Mapigo ya moyo yakaenda kasi zaidi aliposikia kuwa ameuwawa kwa kupigwa risasi. Hofu ikatawala akatokomea eneo lile bila kukumbuka kuwa hakuwa amekuja peke yake pale.

    Jose alikuwa amekumbwa na taharuki kubwa sana. amani ikatoweka.

    Mtu wa kwanza kumuhusisha katika mauaji haya alikuwa ni James. Jose alizifikiria zile milioni mbili alizopewa kama malipo kwenye biashara ya kuuziana siri, siri ya kizuizi. Katika mawazo haya Jose akaisaliti ile dhana yake ya kwanza kwamba zile pesa zilikuwa chache sasa aliziona kuwa zilikuwa nyingi sana kwa ajili ya kununua habari ile. Tena alipokumbuka kuwa bei ya habari hiyo ilikuwa ni milioni sita, akajipa uhakika kuwa pana kitu hapo!!!! Milioni sita kwa ajili ya kununua habari???

    James ameua!!!! Alijiuliza Jose akiwa njiani kuelekea alipopajua yeye mwenyewe. Swali hilo likamfanya atetereke kimawazo. Maana jibu lake lilikaribiana na ndio!!

    Akajihisi yupo hatarini. Hatari ya kuuwawa. Kuuwawa kwa kuijua siri. Siri ya kizuizi!!! Na sasa siri ya mauaji.

    Nimemuua Bibiana!! Jose B alikiri….



    Kivipi Bibiana afe!!! Kivipi mh!! Hapana kuna kitu. Kizuizi kimemuua Bibiana” Jose alizidi kujiuliza kisha akaamua kujipatia jibu mwenyewe.

    Wakati akijipa uhakika kuwa huenda ni kizuizi kimemuua Bibiana, alijiaminisha kuwa kizuizi hichohicho kinaweza kumtia yeye matatani.

    Hatia ya kuwa mbinafsi na kutomshirikisha yeyote tangu mchezo huu unaanza ikaanza kumtafuna, alitamani japo angekuwa amewahi kumshirikisha mama yake, lakini haikuwa hivyo. Sasa mambo yanaanza kuwa magumu. Majuto yanachukua nafasi.

    Ile pesa ikaanza kuwa chungu hata kabla haijatumika kufikia nusu. Mipango ya kumtafuta huyo mke mtarajiwa ikaonekana kuwa batili. Hatia ikatambaa vyema na kujikita katika moyo wa kijana huyu mwembamba, mrefu wa wastani mwenye macho makavu ya mviringo, kichwa chenye nywele chache lakini kikiwa na siri lukuki na mdomo mdogo lakini wenye maneno mengi. Jose B waukweli.

    Mara akawaza juu ya kuukimbia mji.

    Wazo hili akalifutilia mbali mara moja na kujiona kuwa anatawaliwa na uoga usiokuwa na mantiki yoyote.

    Kwanza huyo James hafahamu ni wapi ninapoishi. Pili .......akazima simu yake kisha akamalizia.

    “Pili sipatikani kwenye simu. Atanipataje?”



    *****



    James aliamka mapema sana lakini hakubanduka kitandani. Jose B, bado alikuwa hapatikani kwenye simu.

    James aliamini kuwa Jose ameingiwa kiwewe kwa kuzipata pesa nyingi kiasi kile kwa pamoja, kwa mtazamo wa waziwazi alimwona Jose kuwa alitetemeka sana baada ya kupokea pesa zile za malipo, akaamini kuwa Jose atakuwa amejichimbia katika vilabu mbalimbali vya pombe akifaidi maisha ya kipekee ambayo kamwe hajawahi kuyapitia. James akampuuzia Jose B na kufikiria kwamba hana athari zozote katika mpango wake wa kufunga ndoa.

    James akazihesabia zile pesa alizompatia Jose, kwa maisha yake ya kimasikini hakika ingemchukua muda mrefu sana kuweza kuzimaliza. Mwanzo wa kuzimaliza zile pesa ndio ungekuwa mwanzo wa kutafuta mbinu za kupata pesa nyingine. Wakati huo ukifika tayari tangazo la tatu litakuwa limepita, na hapo James atakuwa amefunga goli la kisigino!!!!

    James akampuuzia Jose. Akajichukulia pointi zote upesi upesi na kujichukulia kuwa yeye ni mjanja kuliko Jose.

    “Kesho narejea Dar!!!” akajihakikishia James, kisha akaitwaa simu yake na kumpigia Emmy. Simu iliita mara ya kwanza haikupokelewa, mara ya pili hali ikawa ileile.

    “Katakuwa kanaoga ka-Emmy kangu!!!” alijisemea huku akiinuka kitandani.

    Naye akaelekea maliwatoni kukidhi haja zake.



    ***



    Almanusura hisia za James ziwe sahihi juu ya mchumba na mke wake mtarajiwa. Alihisi kwamba yu bafuni anaoga lakini hakuwa anaoga bali alikuwa anaugulia maumivu makali baada ya kuruhusu bikra yake itolewe na mwanajeshi sasa alikuwa anakandwa na mjeshi huyohuyo ili kupunguza adhabu ile ya kuchechemea huku akisingizia kuwa alikuwa ufukweni anaogelea mawimbi yakamchukua vibaya na kumrusha juu, akatua juu ya kitu kigumu.

    Aliporejea kutoka bafuni alikuta simu yake inawakawaka ishara ya simu iliyokosa majibu. Alipotazama kidogo aitupe chini, aliogopa alichokiona, lilikuwa jina la James ambalo alikuwa amelihifadhi kwa jina la kubuni la ‘Sweet husband’ jina hili lilikuwa likimfanya atabasamu siku chache nyuma sasa likaanza kumkosesha amani.

    Kile alichomuahidi James hakikuwepo tena. Aibu kuu.

    Sasa Emmy anaitazama ile simu kama mdudu wa kutisha ambaye akiguswa analeta madhara makubwa. Akatamani ampigie lakini hakuwa tayari kusikia jibu la mume mtarajiwa kuwa yupo njiani anakuja Dar es salaam.

    Wakati huo lilisalia tangazo moja tu ndoa iweze kuthibitishwa na kanisa.

    Ile subira aliyokuwanayo na matamanio makubwa ya kufunga ndoa yakaanza kuyeyuka. Akauona uchungu mkubwa ukimkabili baada ya kuifunga ndoa.

    “Au nisingizie kuwa ilitoka katika ajali ya wimbi la bahari?? Lameck ameniponza Lameck.” Alitafakari.

    Akiwa bado ametulia bila kujua ni dakika ngapi zimepotea akiwa hajafanya maamuzi, simu yake iliita.

    Alikuwa Lameck. Hofu nyingine tena.

    Kwanza aliona aibu kwa kitendo alichofanya na baba yake huyo, kisha akajivunja mshipa wa aibu akapokea.

    “Unaendeleaje kipenzi changu.” Sauti nzito ya Lameck ilimnong’oneza Emmy.

    “Lameck...acha kuniita mimi jina hilo tafadhali.” Alijibu kwa ukali Emmy

    “Nimeongea na mama amenambia upo chumbani peke yako na James bado hajarudi, kuna ubaya gani kwani mamii.” Lameck alibembeleza. Emmy akapagawa na mauzauza ya huyu bwana.

    “Lakini ninakaribia kufunga ndoa. Lameck please hebu tufanye kama hakuna kilichotokea ndugu yangu. Nakuomba nakuomba sana!! Lameck utaniharibia mwenzio” Emmy alisihi huku akijaribu kuizuia hasira yake.

    “Mimi sio muigizaji mamii, siwezi kabisa kujifanya sijui kilichotokea...Emmy si unajua nilikupenda nawe ulinipenda hapo kabla na hadi sasa...”

    “Ndio nakupenda Lameck lakini umeniharibia ujue...”

    “Kivipi?”

    “Jamaa anajua kuwa mimi ni bikra. Sa itakuwaje?”

    “Hayo ndo maneno sasa, kumbe hasira zote hizo ni hilo tu...njoo kesho home kwangu”

    “Kufanyaje sasa. Kufanyaje Lameck wakati tumeharibu tayari!!”

    “Njoo utafurahi.”

    Walimaliza maongezi baada ya makubaliano. Emmy alikubali lakini kwa shingo upande. Majuto yalikuwa yamemzidi nguvu.

    Akiwa bado anatafakari kidogo juu ya wito wa kwenda kwa baba yake mdogo, simu ikaita tena, sasa alikuwa James. Mume mtarajiwa.

    Hofu mpya ikajengeka. Lakini hakuwa na budi, akalainisha koo kwa kukohoa kisha akapokea simu akiulazimisha uchangamfu.

    “Vipi mpenzi umelala....” Sauti nzito ya James iliuliza.

    “Wala sema nilikuwa nawatch kideo sikuisikia simu yako...”

    Lile neno kideo likamshambulia ghafla James aliyekuwa ameketi kitandani, hakushtuka kwa sababu tu mpenzi wake alikuwa amejikita katika kutazama luninga, lakini lile neno kideo liliambatana na jambo jingine la muhimu sana. Ukiondoa KI linabaki jina DEO…..

    Mdomo ukawa mzito, Emmy aliendelea kukazana kuita ‘halo..halo..’ lakini hapakuwa na majibu. Mara simu ikakatwa.

    Emmy hakufanya jitihada zozote za kupiga simu, kwanza ilikuwa faraja kukwepa kuzungumza na James mazungumzo marefu..

    Akajirusha kitandani aweze kufanya mtihani wa kuwaza na kuwazua.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati Emmy akijirusha kitandani, James alikiacha kitanda akasimama wima akakumbuka kuna tatizo kubwa anakaribia kuliacha jijini Mwanza. Deo.

    Huyu kijana na yeye alikuwa bega kwa bega kumfitini asiweze kufunga ndoa na Emmy John. Kuondoka huku akiiacha roho hii ikifurahia hali ya hewa ya jiji la Mwanza lilikuwa kosa ambalo mwisho wa siku litamfanya aaibike hadharani na kukosa nafasi ya kipekee ya kuwa mwanaume wa kwanza kushirikiana na Emmy.

    Safari aliyotaka kuiandaa kwa ajili ya siku iliyofuata akalazimika kughairi. Alikiri kuwa anafanya haya yote kwa ajili ya mtu anayempenda kwa dhati, tena muaminifu kwake.

    Laiti kama angejua ukauzu aliofanyiwa na Emmy, huenda angeubadili uelekeo.

    James akakiri tena kuwa alikuwa akimuhitaji sana Jose B waukweli ili aweze kumfanikishia mipango ya kuonana na Deo.

    Atampata wapi? hilo likawa swali.

    Katika simu ya mkononi hakuwa anapatikana.

    James akaulazimisha usingizi. Hatimaye akapitiwa.

    Usingizi ukapaa majira ya saa kumi alfajiri na kuelekea kwa wengine, ukawa umemtupa mkono James.

    Akabaki kugaagaa kitandani akijiuliza ni namna gani anaweza kukabiliana na Deo pamoja na Jose B kimya kimya bila kuwa hata na mawasiliano nao??

    Akakosa jibu. Akasimama akaliendea begi lake dogo akatwaa tembe mbili za dawa akameza. Zilikuwa za kutuliza maumivu ya kichwa.

    Hakika James alikuwa amezidiwa.

    Akiwa katika kufikiri zaidi akakumbuka kuwa ameuwa watu wawili tayari, na wala hawakumuumiza kichwa na wala hakujuta.

    Kifo cha bwana mpenda kujua yasiyomuhusu kule ziwani hakikuwa na uzito sana. Lakini kifo cha Bibiana hiki kilikuwa cha kipekee, aliamini kitawavuta watu wengi sana, akakiri kuwa Deo kama patna wa marehemu Bibiana lao likiwa moja lazima atahudhuria mapema sana katika msiba huo na huenda hatabanduka hadi maiti ifukiwe kaburini na kama hiyo haitoshi hata matanga atayangoja.

    Pata potea. James akarusha karata kuwa huenda anaweza kupata hisia juu ya Deo katika msiba huo ambao utashangaza zaidi ya kuhuzunisha.

    Akaamua kuwahi mapema kabisa, miwani yake nyeusi machoni, kofia kubwa kichwani na ile hali ya hewa ya ubaridi akajificha ndani ya koti kubwa jeusi. Ilikuwa ngumu kumfahamu.



     Jose B akiwa katika nyumba ya kulala wageni ambayo alijihisi ni salama zaidi ya nyumbani kwao alikuwa katika kizungumkuti cha namna yake, alikuwa anahangaika kuamini iwapo ni kweli James ndiye muuaji ama ni hisia zake potofu? Alitamani awashe simu na kumpigia amuulize lakini akasita akagundua swali lile ni gumu sana na pia ni zito.

    Na kabla ya kuuliza akaamua kufanya ubashiri, iwapo Jose ndiye muuaji kweli kisha akasikia swali hili. kwanamna yoyote ile lazima atamsaka kwa udi na uvumba aweze kumteketeza asiweze kuisambaza siri hii zaidi.

    Kizuizi.

    Jose alipofikiria kuhusu kufa akapatwa mshtuko, hakuwa tayari kufa.

    Asubuhi alidamka na wazo la kijasiri, akaamua kwenda msibani huku kauli mbiu ya ‘Penye wengi pana mengi’ ikimuongoza na kujiaminisha kuwa lazima atagundua kitu cha ziada. Jose B akasahau kuhusu hatari inayomkabili, akatawaliwa na tabia yake ya kujua mengi hata yasiyomuhusu akaamua kufuata kiguu na njia kuelekea katika msiba wa Bibiana.

    Hakujua kama James naye alikuwa katika msafara huohuo.



    Laiti angejua...............



    *****



    EMMY JOHN alimuaga mama yake mzazi kuwa anaelekea ufukweni kupunga upepo na rafiki yake kwani hawezi kuishi kipweke bila uwepo wa James.

    Mama alimsikitikia mwanaye, akamruhusu huku akimtia moyo kuwa muda si mrefu mume wake atarejea.

    Aliyoyazungumza mama yalipenya kama upepo wa kawaida tu usiokuwa na maana. Emmy hakuwa akimuwaza James hata kidogo.

    Mawazoni mwake Lameck alijikita, kwa kuwa alimuahidi jambo jema. Kumsaidia kuificha aibu.

    Emmy akatoweka, safari ya kuelekea nyumbani kwa Lameck.



    Chumba cha Lameck kama ilivyo kawaida kilikuwa hakipo katika mpangilio mzuri sana kuonyesha kwamba hakuna mwanamke wa kukipendezesha. Kilifanania kama kawaida ya vyumba vya wasiooa na wasiojali, Emmy alikikuta katika mpangilio huo huo.

    Alikiri katika nafsi yake kuwa hakikuwa chumba cha kuvutia lakini bado hakufanya jitihada za kukiweka katika hali ya usafi, labda kwa sababu sio hicho kilichomleta katika nyumba hiyo.

    Lameck alimpokea Emmy kwa bashasha na kimuhemuhe cha namna yake, licha ya Emmy kujaribu kuvaa mavazi ya kawaida sana lakini bado alimteka Lameck ambaye alishindwa kusema neno lolote kwa sekunde kadhaa.

    Baada ya kimya kirefu hatimaye aliweza kumkaribisha Emmy, huku akitumia jina mpenzi jambo ambalo lilimkera Emmy lakini hakuwa na budi kukubali kwa shingo upande hasahasa akizingatia kuwa mchezo huo waliuanza zamani sana na hakuna aliyekuwa amemshawishi mwenzake bali ilitokea tu ikawa hivyo.

    “Ulisema hofu yako ni nini?” Lameck alimuuliza Emmy huku akimkazia macho. Emmy akaona aibu kujibu, Lameck akajiongeza.

    “Njoo huku hebu.” Lameck akakoroma, Emmy akasimama kama anayeongozwa na mitambo na kumfuata, walielekea chumbani.

    Kitandani palikuwa na kikopo kidogo cheupe pamoja na kitu mfano wa ndimu na vikorokoro vingine asivyovijua Emmy.

    Mahali pale palifanania eneo la mganga wa jadi.

    Emmy akatumbua macho akingoja kumsikia Lameck.

    “Hii unaikamua katika haya maji ambayo nitakuwa nimeyachanganya na huu ungaunga maalumu, kisha unachukua kitambaa unachovya kidogo unakandakanda hukoo (akimwonyeshea sehemu zake za siri), fanya hivi asubuhi kabisa na usiku bila kukosa. Na ukimaliza lala kidogo kwa dakika thelathini ukiwa umejinyoosha….. ” Lameck alitoa maelekezo hayo kama daktari bingwa wa magonjwa ya kike.

    Emmy alitamani kuuliza maswali zaidi lakini hakuwa akijiamini sana. Akaipokea ile dawa akaitia katika mkoba. Yale majimaji yalikuwa ni ‘Shabu’ dawa ya kutakatisha maji na kuua vijidudu, ni mfano wa ‘Waterguard’ na kile kipande kilichofanana na ndimu kilikuwa ndimu yenyewe. Dawa kamili kutoka kwa mganga mashuhuri.

    Bwana Lameck.

    Walizungumza mengi, kisha Emmy akatoweka. Tumaini likiwa dogo sana!!



    ****



    JOSE B waukweli alifika mapema sana msibani, alijiweka mbali sana. Hakutaka kuonekana kujihusisha sana na ule msiba, ni mengi yalikuwa yamekizonga kichwa chake. Alihitaji sana kuyafahamu kwani yalimuumiza kuliko huo msiba.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mara ajipitishe dukani mara ajiunge katika vikundi vya vijana wanaobadilishana mawazo, huku napo alichombeza kisha akahama tena na kujiunga na wazee wanaojadili ya kwao kuhusu msiba huo, hapa akachota kidogo pia. Alipogundua hakuna kubwa walilofahamu kuhusiana na kifo cha Bibiana aliwafananisha na wanadamu waliopitwa na wakati huku wakijiona wanaenda na wakati.

    Katika hangahika ya huku na kule hatimaye alipata kitu kilichomvutia na kumfanya aachane na mengine yote yahusianayo na msiba huo.

    Akaanza kumfuatilia kiumbe huyu ambaye bila kujijua alikuwa anahitajika sana kwa kipindi hicho. Jose B hakusema neno lolote na kiumbe yule aliyetawaliwa na huzuni kuu.

    Akienda kushoto Jose B naye aliketi kushoto. Aliporejea kulia Jose B naye alifuata, hatimaye yule kiumbe alisimama na kujizungusha huku na kule, Jose naye akafanya hivyo lakini kwa tahadhari kubwa sana asiweze kugundulika.

    Yule bwana akiwa katika huzuni ileile sasa aliambaa katika umati kisha akaifuata barabara ya lami, akatoweka bila kuaga.

    Jose B naye akatoweka bila kuaga vilevile.

    Akaendelea kumfuata mtu ambaye mara ya mwisho alionana naye kanisani, alikuwa pamoja na marehemu na alikuwa akizungumzia juu ya kizuizi. Kizuizi ambacho kilipenya katika masikio yake na kisha akakigeuza biashara ambayo sasa ilikuwa imempatia pesa lakini kabla ya kuitumia ile pesa yanatokea yakutokea. Bibiana anauwawa!!

    Sasa Jose B anataka kujua kuna siri gani nyuma ya haya mauaji. Anamfuatilia Deo.

    Deo hajui kama anafuatiliwa. Hadi nyumbani kwake, anapotaka kuingia ndipo anasikia akiitwa kwa jina lake fasaha “Deogratius”. Akageuka, akakumbana na sura ngeni machoni pake, akakutana na Jose B waukweli.

    Mbea, mnafiki, mwongo, msema chochote katika sherehe na kondakta wa daladala. Hawa viumbe hawawezi kuhangaika iwapo wataamua kuwa madalali. Huwa na maneno mengi matamu tena yanayoshawishi, Jose B alikuwa mmoja kati yao alikuwa na virusi vya unafiki, uongo na umbea. Alipovichanganya vikazaa tabia ya ‘ushakunaku’.

    Ana kwa ana na Deo. Jose B akaanza kurusha karata zake huku akijifanya kumjua sana Deo.

    “Ujue tangu msibani mi nakutazama nikajisemea huyu ndiye ama siye.”

    Deo akaiva akaisahau huzuni akatekwa na maneno ya Jose B na sasa walikuwa katika chumba kidogo kilichopunguzwa joto na feni aina ya ‘pangaboi’. Deo akizidi kufahamiana na Jose B.

    Baada ya kufahamiana Jose B akaleta mada juu ya kifo cha Bibiana.

    Hapa Deo akainamisha kichwa na kufanya aina ya kumbukumbu huku akiunganisha meno yake kwa huzuni kuu.

    Hakutaka kusema lolote juu ya msiba huu zaidi ya kukiri kuwa hata yeye alishangazwa sana.

    “Nimesikia sikia wale wazee wanadai ishu iliyomuondoa Bibiana ni Kizuizi” Jose aliongea kwa kunong’ona.

    “Kizuizi? Kivipi yaani.....”

    “Hata sijui lakini...hivi kwani alikuwa anataka kufunga ndoa huyu Bibiana maana nimesikia sijui kawekewa kizuizi sijui....” Jose B akampiga Deo chenga ya mwili, Deo akalainika.

    “Mh..Bibi hakuwa hata katika uchumba sema kuna ishu moja hivi lakini sidhani kama James anaweza kufanya jambo la kipuuzi kama hilo....”

    “James ndo nani?? Yaani kufa mtu we unasema upuuzi!!” Jose aliuliza.

    “Kuna mshkaji mmoja anataka kuoa....Bibi alitaka kumuwekea kizuizi.......lakini hata kwa paroko hakufika ndo amekufa.....James hawezi kuhusika...sawa jamaa ni katili lakini sio kiasi cha kuua..... namjua James namjua sana mimi!! Hata yeye ananijua” Deo alijibu huku akiamini Jose B hakuna anachoambulia. Na wakati huo alikuwa akijiuliza ni wapi aliwahi kukutana na kiumbe huyu.

    “Unajua nini Jose...ngoja tumzike kwanza Bibiana halafu sisi tutakaa tuzungumze juu ya hili ujue sisi wanaume tutaangalia nini cha kufanya.. kama ni kweli James lazima awajibishwe” Deo alimaliza maongezi ambayo Jose B alitamani yaishe siku hiyo hiyo yote. Alitamani kumchombeza Deo ili aendelee kuzungumza lakini alihofia kuwa haraka zake zinaweza kumkosesha baraka. Akakubaliana na Deo kisha wakaagana.

    Waliimaliza siku huku wakipeana ahadi za kukutana msibani siku inayofuatia. Jose B alimuachia shilingi za kutosha ili kumnunua Deo bila yeye kujua kama ananunuliwa.

    Jose B aliondoka huku akijiaminisha kuwa kwa makali aliyoyaonyesha lazima siku inayofuata Deo atamwaga siri yote juu ya kizuizi.

    Laiti kijana huyu angepewa nafasi ya upendeleo kujua yatakayotokea baada ya masaa machache huenda angemlazimisha Deo aseme yote juu ya kizuizi, lakini Jose naye ni mwanadamu kama wanadamu wengine hakuyajua yanayotokea baada ya dakika moja.



    SIKU YA BALAA JIPYA!!



    Kama ilivyo kawaida alifika msibani mapema, siku hii alikuwa amebeba pesa nyingi zaidi na zawadi ndogondogo kwa ajili ya kumnunua Deo reja reja.

    Alitegemea kuwa Deo atawahi kutokea kama alivyomuahidi lakini haikuwa hivyo. Alitamani kumpigia simu lakini akakumbuka vitu viwili, kwanza hakuchukua namba yake ya simu na kubwa zaidi bado hakuwa tayari kuwasha simu yake ambayo aliamua kuizima tangu kifo cha kushtukiza cha Bibiana kitokee.

    Jose akaendelea kuivuta subira isiyokuwa na dalili ya heri.

    Saa sita mchana hatimaye. Bado Deo hakuonekana.

    Jose akiwa bado anaduwaa mara aliguswa began a mzee wa makamo kiasi kikubwa.

    “Kijana....poleni sana. Nawe upo hapa kumbe.” Alizungumza kwa sauti murua ya kizee.

    Jose B akamtazama kwa dakika chache huku akiilazimisha sura ile kujichora katika ubongo ambao kazi yake ni kukumbuka. Hatimaye akamkumbuka.

    “Shkamoo mzee....” alimsalimia mzee yule.

    “Marahaba....poleni..ulianza kunisahau.” Aliuliza.

    “Si unajua tena mambo ya msiba.” Alijaribu kujitetea.

    “Alikuwa muumini safi sana hakika!!” alisema yule mzee

    kisha akatabasamu akampiga begani ishara ya kumpooza.

    “Ngoja nizungumze na kijana wangu mara moja hapa.” Aliaga yule mzee. Jose b akakiri kimoyomoyo kuwa yule mzee alifanana sana na mtoto wake wa kiume.

    “Duuh yaani hadi kutembea wanafanana aisee.” Alijisemea huku akiunda picha ya James na ya huyu mzee.

    Mtu na baba yake.



    Yule mzee alipotoweka, Jose B naye akatoweka baada ya subira kuwa shubiri kwake. Akaamua kuelekea nyumbani kwa Deo ili kutazama kulikoni.

    Kwa mwendo wa miguu akaona anachelewa akaamua kukodi pikipiki impeleke.

    Dakika tano akawa amefika, akamlipa mwenye pikipiki akaondoka zake ndipo akaanza kuiendea ile nyumba.



    Mlango ulikuwa umeegeshwa, haukuwa umefungwa. Jose B akamlaani Deo kimoyomoyo kwa kuchelewa kuamka kiasi hicho, akamuweka katika kundi la wazembe maradufu wanaobweteka kwa kupata visenti kidogo.

    Akaizuia hasira yake ili asiweze kumsemea mbovu kijana mwenzake. Akaunda tabasamu la bandia kabla ya kubisha hodi.

    Kimya!!



    Akajaribu tena. Kimya!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hili bwege linalala kama limekufa.” Akashindwa kujizuia akatukana.

    Hakubisha hodi tena akausukuma mlango, ukafunguka akaingia, akakumbana na giza, feni ikiwa inazunguka.

    “Oyaa....” Aliita kisharishari.

    Kimya!!

    Akapapasa kilipo kitufe cha kuwashia akakipata, akawasha taa.

    Lahaula!! Macho yalipouzoea mwanga ule, akakumbana na kitu ambacho kilimfanya alemae kwa muda kama aliyepigwa shoti ya umeme.

    Dimbwi kubwa la damu kitandani!! Damu ilitapakaa kila kona ya mwili ule kitandani, kasoro usoni tu…..

    Visu vitatu viligawa nafasi katika mwili wake, kimoja kikibaki tumboni, kingine mbavuni na cha tatu chenye mpini mkubwa kilijihifadhi upande wa moyo.

    Haikuhitajika elimu ya chuo kikuu kutambua kuwa Deo alikuwa maiti. Aliyekufa kifo cha kushtua!!

    Jose B alirudi kinyumenyume baada ya kurejewa na fahamu kiasi, akaangusha bila kutarajia kile kifurushi alichopakata mkononi, akageuka na kutimua mbio.

    Jirani na nyumba aliyokuwa akiishi Deo palikuwa na mbwa, Jose B hakujua ni kwa kiasi gani alitoa vishindo vikubwa, mbwa wakavutika na vishindo hivyo, ni kama waliambizana, mbwa wawili wanaojua nini maana ya kulinda wakaanza kumkimbiza Jose B.

    Mshikemshike...



    Mbwa wale kama walivyo mbwa wengine walibweka kwa sauti za juu wakati wanamkimbiza Jose B, hali hiyo ilizua utata katika akili ya Jose katika kufanya maamuzi. Akaongeza mwendo ili asiweze kudhurika na wale mbwa.

    Sauti zilizosikika pekee katika masikio ya Jose zilikuwa za wale mbwa wenye hasira, kiatu kimoja kikiwa kimechoropoka mguuni Jose alibakiwa na kiatu kimoja tu huku mguu mwingine ukiwa peku.

    Umakini wa Jose katika kuwakwepa mbwa ukamsababisha asiweze kuisikia honi iliyokuwa inapigwa na pikipiki iliyokuwa inakuja katika kona kali, Jose akaifikia kona, akajaribu kuwahi kuruka upande mwingine baada ya kukutana ana kwa ana na pikipiki ikiwa katika mwendo wa kasi.

    Akili yake ya kuhama upande ikafanana na ya yule dereva nay eye akahamia upande aliorukia Jose katika jitihada za mwisho za kumkwepa.

    Balaa!! Wote wakajikuta upande mmoja, ana kwa ana tena!!.

    Mlio mkubwa ukasikikakisha kimya kikatanda.

    Jose kimya, dereva kimya abiria aliyekuwa amebebwa naye kimya.

    Kiza kikubwa kikatanda.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog