Search This Blog

Sunday 19 June 2022

BOMU LA KARAFUU - 1

 





     IMEANDIKWA NA : ISSA J. SEMTAWA





    *********************************************************************************



    Simulizi : Bomu La Karafuu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Msichana mpelelezi machachari, tishio la wahalifu, Belinda Bernadoe, au BeBe kama anavyojulikana sana katika ulimwengu wa upelelezi, anapata telegramu ambayo inamkatizia likizo yake na kumtaka aende Zanzibar mara moja. Huko kuna kazi nzito ambapo Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KKMZ) kinapambana vikali na waendesha magendo ya karafuu.

    Ingawa baada ya kupata fununu ya kuwapo kikundi sugu cha waendesha magendo, KKMZ kimeweza kuokoa shehena kubwa ya karafuu, lakini bado karafuu zenye thamani ya mabilioni ya fedha zinaendelea kuvushwa na kuuzwa nje ya Zanzibar kwa magendo. Hali hii inaathiri vibaya uchumi wa Taifa.

    Hatimaye ‘BUNDI,’ kikosi maalum cha Wizara ya Usalama wa Taifa kilipewa jukumu la kuisaidia KKMZ kuyakomesha magendo hayo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ama ilikuwa kazi nzito iliyoambatana na mauaji ya kutisha. Kwa ujasiri na hekima, BeBe alililipua ‘Bomu la Karafuu.’

    Soma ushangae, ufurahi na uburudike. Kumbuka, hii ni hadithi ya kutunga ambapo majina na matukio yote si ya kweli na wala hayahusiani moja kwa moja na mtu yoyote. Endapo itatokea kuwapo kwa kushabihiana kwa majina ya vitu na watu, basi itakuwa ni kwa bahati mbaya, na si kwa kukusudiwa.

    1 – Telegramu

    Saa nne asubuhi tarishi wa Posta aliegesha baisikeli yake nje ya duka la Mzee Bernadoe kijijini Sega, yapata kilomita tatu kutoka mjini Muheza. Alitoa lesso kutoka mfuko wa shati lake akajipangusa jasho usoni, shingoni, na makwapani, kisha akairejesha mfukoni.

    Alionekana kuwa amechoka kwa jinsi alivyokuwa akihema kwa harakaharaka, shati lake likiwa limetota jasho mgongoni na makwapani. Licha ya umbali wa kilomita tano uliopo kati ya Muheza na kijiji cha Sega, kukiwa na vilima vidogovidogo, ni dhahiri jua kali la asubuhi ile lilimuongezea taabu ya uchovu katika safari yake.

    Wakati huo wa asubuhi, duka la Mzee Bernadoe lilikuwa limefungwa. Kama ilivyo kawaida ya maisha ya vijijini, maduka mengi hufunguliwa mchana baada ya watu kurejea kutoka makondeni. Hata hivyo, watoto wa makamo madogo hubaki majumbani wakiangalia nyumba na vitu vilivyoanikwa, kama vile makopa, unga na vinginevyo.

    Kama kawaida ya watoto, hawana dogo. Yule tarishi wa Posta alipoegesha baisikeli yake pale barazani kwa Mzee Bernadoe, watoto walimkimbilia kutoka kila upande wakamzunguka. Wote walimwamkia wakawa wanaitazamatazama ile baisikeli yake iliyokuwa na mfuko wa Posta juu ya kitako cha nyuma. Wengine wakubwa kidogo, walisoma maandishi yaliyoandikwa kwenye bati lililokuwa katikati ya magurudumu, la mbele na la nyuma. Maandishi hayo ya rangi nyekundu yalisomeka “Post Office Muheza.”

    Baada ya kujifuta jasho, yule tarishi aliuliza: “Wenye hili duka wapo?”

    Sauti zaidi ya kumi za wale watoto ziljibu: “Hawapo.”

    Wakati uleule wakawa wanamzongazonga kijana mmoja mvulana wa umri wa miaka sita hivi. Wakawa wanamsukumia mbele yao.

    Yule tarishi wa Posta ambaye wakati huo alikuwa ametoa bahasha ndogo ya rangi ya kaki kutoka kwenye ule mfuko wa Posta, alikisoma kitendo kile cha yule kijana aliyekuwa akisukwasukwa na wenzie. Akahisi kuwa yule kijana bila shaka ile nyumba yenye duka ndipo kwao.

    “Wewe nyumba hii ndipo kwenu?” alimuuliza yule kijana ambaye sasa alikuwa kasimama mbele karibu naye.

    “Ndiyo,” alijibu.

    “Unamfahamu dada aitwaye Belinda?”

    Hata kabla yule kijana hajajibu, tayari sauti kadhaa za wenzie zilijibu:

    “Ni dadake huyo.”

    Yule kijana akaishia kutabasamu tu. Yule tarishi akataka apate uhakika, akamuuliza:

    “Ni dadaako kweli?”

    Yule kijana akajibu: “Ndiyo, ni dadaangu.”

    “Hivi sasa yuko wapi?” yule tarishi wa Posta alimuuliza.

    “Kaenda shamba na mama,” kijana alijibu.

    “Huko shamba ni mbali sana kutoka hapa?” tarishi wa Posta aliuliza.

    Na mara hii tena sauti kadhaa za wale vijana zilijibu kwa pamoja: “Sio mbali.”

    “Nenda kamwite dadaako, mwambie kuna barua yake ya haraka kutoka Posta,” yule tarishi aliagiza.

    Hata kabla yule tarishi hajamaliza kutoa maagizo hayo, kikundi cha vijana wapatao nane wa umri kati ya miaka mitano na sita, wavulana na wasichana walichomoka mbio wakaelekea upande wa mashariki mwa kijiji cha Sega ambako kulikuwa bondeni. Yule kijana ambaye dada yake ndiye aliyekwenda kuitwa naye alizitimua mbio pamoja na wenzake. Walimwacha yule tarishi wa Posta akiwa na kikundi cha vijana ambao bado miguu yao haikuwa na nguvu za kutimua mbio.

    Kule walikokimbilia wale vijana ndiko kulikokuwa na mashamba ya wengi wa wanakijiji cha Sega. Siku za nyuma eneo lile lilikuwa ni sehemu ya mashamba ya mkonge. Baada ya kampuni iliyokuwa ikiyamiliki kushindwa kuendeleza kilimo cha zao hilo, mashamba yaligawiwa kwa wananchi wa eneo hilo, kikiwemo kijiji cha Sega. Familia ya Mzee Bernadoe ilibahatika kupata shamba la ekari nne, ambamo walipanda mahindi, mihogo, michungwa, minazi, na mazao mengine ya msimu na ya kudumu.

    Msichana Belinda na mama yake waliliona lile kundi la wale vijana walipokuwa wakienda mbio, huku wakikatiza mashamba ya wanakijiji wengine kuelekea kwenye shamba lao. Kama ilivyokuwa kwa wanakijiji wengine waliopitwa mbio na wale vijana, Belinda na mama yake nao walishikwa na butwaa. Waliacha kupanda mahindi wakasimama kama walivyofanya wanakijiji wengine kuangalia zile mbio za wale vijana zingeishia wapi.

    Tangu lile kundi la vijana likiwa mbali, macho makali ya Belinda yaliweza kumuona mdogo wake wa kiume akiwa miongoni mwa wale waliokuwa mbele. Belinda alihisi moyo ukishituka, si kwa woga, bali kwa hisia kuwa kundi lile lilikuwa likiwajia wao na kwamba mbio zile zilikuwa za ujumbe uliomhusu yeye.

    Sauti za “nyie wana uko kaya kuna mbwai?” zilisikika kutoka kwa akina mama waliopitwa mbio na wale vijana. Hilo ni swali katika lugha ya Kibondei lenye maana: “enyi watoto huko nyumbani kuna nini?”

    Lakini wale vijana hawakujibu wala kusimama, bali waliendelea kukimbia hadi walipofika pale waliposimama Belinda na mama yake.

    “Haya, kuna nini huko nyumbani?” Belinda alimuuliza mdogo wake, ambaye alikuwa miongoni mwa vijana watatu waliowafikia kwanza.

    “Ku….kuna…kaja m..mtu..wa…ana..kuita,” yule kijana alijibu mkatomkato, huku akitweta.

    “Ku..una mtu wa Po..sta,” kijana mwingine naye alidakia.

    “Kasema ku..kuna barua ya ha..haraka sa..ana,” msichana mmoja naye aliongeza.

    “Sasa hebu tulieni, elezeni sawasawa, mbona mnagombea kusema kama mnagombania chakula,” Mama Belinda aliwakemea baada ya kuona kila mmoja alitaka aseme yeye.

    “Ni barua ya haraka, alikuwa nayo mkononi,” yule mdogo wake Belinda alisema, kidogo akawa sasa amejaza pumzi za kutosha ndani ya mapafu yake.

    “Kaja na baisikeli ya Posta,” kijana mwingine aliongezea.

    Belinda alimtazama mama yake, akatikisa kichwa.

    “Likizo imekwisha. Hiyo lazima itakuwa ni telegramu, naitwa nirudi kazini,” alimweleza mama yake.

    “Labda ni barua ya kawaida, wewe huwajui hawa watoto, jambo dogo kwao ni kubwa,” mama Belinda alisema, lakini sauti yake ilionyesha kupwaya kwa wasiwasi.

    “Haya, chukueni hayo majembe na mbegu twende nyumbani,” Belinda aliwaeleza wale vijana.

    Ilizuka rabsha ya kugombania majembe na kikapu cha mbegu, kidogo tu wangemwaga mbegu kama Mama Belinda asingeingilia kati akakichukuwa kile kikapu akamtwisha kichwani mmoja wa wasichana waliokuwepo. Mdogo wake Belinda na mvulana mwingine waliwahi majembe, na msafara wa kurudi kijijini ukaanza.

    Kila walipopita shamba la watu wengine, Belinda na Mama yake waliulizwa kuna nini nyumbani, mbona wamefuatwa. Nao walijibu kifupi tu kuwa kulikuwa na mgeni. Vijana wengine hawakuvumilia ule mwendo wa polepole, wao walitimua mbio kwenda kumpasha habari yule tarishi wa Posta kuwa Belinda na mama yake walikuwa njiani wakirudi.

    Belinda na mama yake walipofika nyumbani walimkuta yule tarishi wa Posta ameketi kwenye msingi wa baraza ya nyumba upande uliokuwa na duka. Vijana kadhaa bado walikuwa wamemzingira, wengine wakiwa bado wameizunguka baisikeli yake.

    “Karibu ndugu,” Belinda alimkaribisha yule tarishi ambaye alipowaona alisimama.

    “Asante, poleni na shughuli za shamba. Shikamoo mama,” yule tarishi alimwamkua mama Belinda.

    “Marahaba baba, pole na mwendo wa jua kali,” mama Belinda alisema.

    “Asante sana. Nimeleta telegramu hii ya haraka. Bila shaka ni yako kama wewe ndiye Belinda Bernadoe,” yule tarishi alisema huku akimpa Belinda bahasha ya telegramu ambayo juu iliandikwa “HARAKA SANA” kwa wino mwekundu wa kalamu yenye maandishi manene.

    “Imefika, Belinda ndiye mimi,” Belinda alisema huku akipokea ile telegramu.

    “Sawa, naomba uniwekee saini yako kwenye hiki kijitabu,” yule tarishi wa Posta alisema akatoa kijitabu kidogo cheusi kilichokuwa na nembo ya Shirika la Posta na Simu Tanzania. Alifunua kurasa mbili tatu, akampa Belinda na kumuonyesha mahali pakutia saini. Belinda alitia saini kisha alirejesha kalamu na kijitabu kwa yule tarishi.

    “Asante dada. Sijui naweza kupata maji ya kunywa?” yule tarishi aliuliza.

    “Bila shaka kaka. Mndolwa, kamletee mgeni maji ya kunywa,” Belinda alimwagiza mdogo wake.

    Baada ya kunywa maji, yule tarishi aliaga akapanda baisikeli akaondoka. Kundi la vijana wa kike na wa kiume wakateremka naye mbio bondeni kuelekea Muheza.

    Belinda aliingia ndani akakaa kwenye sofa sebuleni. Alichana bahasha na kutoa karatasi ndogo iliyokuwa na ujumbe ambao haukuwa mrefu. Yalikuwa ni maneno saba tu:

    “BeBe, tumia ndege, tukutane Zanzibar kesho, MB.”

    Baada ya kuusoma ujumbe huo, Belinda alishusha pumzi akatikisa kichwa. Aliwatazama mama yake na mdogo wake ambao walikuwa wameketi kwenye masofa pale sebuleni.

    “Mnhuu, kuna habari gani?” Mama Belinda alimuuliza bintie, sauti yake ikionyesha shauku kubwa.

    “Ni kama nilivyohisi mama, likizo yangu imekatizwa. Hii telegramu inatoka kwa mkuu wetu kazini, ananitaka niwe Zanzibar kesho. Bila shaka kuna kazi muhimu huko Visiwani,” Belinda alimweleza Mama yake huku akimpa ile karatasi yenye ujumbe.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mama Belinda aliusoma ule ujumbe kisha naye pia akazishusha pumzi, akasema:

    “Loo, hii kazi yako! Nilikuonya lakini Belinda kuwa kazi hii mwanangu si kazi ya wanawake ukanibishia. Haya sasa, utaolewa kweli wewe? Huyo mwanamume atakayekubali uwe ukisafiri ghaflaghafla namna hii utampata wapi? Haya, likizo haijesha, bado tunahamu nawe, sasa ona unatakiwa uondoke. Ni kazi gani hii lakini?” mama Belinda alilalama.

    “Aah, Mama, kazi hii ni nzuri tu, tena wako wanawake wengine wengi wanaoifanya duniani kote. Kama nikuolewa nitaolewa tu, mbona bado muda upo. Labda baada ya miaka kumi ya kazi ndipo nitaanza kufikiria kuo…”

    Belinda hakumalizia usemi huo, maana ingawa mwenyewe aliyasema hayo katika hali ya mzaha tu, mama yake alikuja juu.

    “Wee, huna akili kweli wewe. Hivi miaka kumi unaiona michache eee? Labda hutaki na sisi tujivunie wajukuu kama wenzetu. Wenzio wanalilia kuolewa, wewe kila mchumba humtaki, eti oooh kazi yako haikuruhusu uolewe! Basi mpaka tufe ndio uta…..”

    “Aa-aah, maneno gani tena hayo? Kuna nini kinachosubiri watu wafe?” Sauti nzito ya Mzee Bernadoe ilikatiza usemi mkali wa mama Belinda.

    “Si wewe hapo unayemuendekeza mwanao. Kila akija likizo haimaliziki, kuolewa hataki na wewe baba yake unaona ndiyo sawa tu. Haya sasa, hata majuma mawili hajamaliza kaletewa telegramu aende haraka Zanzibar. Ni kazi gani hii?” Mama Belinda aliendelea kulalama.

    “Amaa, sasa waliona ni tatizo hilo? Huyu yupo kazini masaa ishirini na manne, hata akiwa likizo anaweza kuitwa kazini wakati wowote,” Mzee Bernadoe alimweleza mkewe huku naye akikaa kwenye sofa.

    “Kwa hiyo unakubaliana naye kuwa haolewi mpaka miaka kumi ipite?” Mama Belinda alimuuliza mumewe kwa sauti kali kidogo.

    “Ikiwa mwenyewe ameamua hivyo sawa, wacha alitumikie taifa,” Mzee Bernadoe alijibu.

    “Na hao wajukuu utawaona lini? Wenzetu wote wa rika letu wanao wajukuu. Sisi mwanetu mkubwa na wa kike pekee ni huyu naye hataki kuolewa. Wewe waliona jema hilo, tufe bila kuona wajukuu zetu? Mimi katu siyawezi hayo. Sifi bila kushika mwanaye huyu. Lazima aolewe ningali hai!” Mama Bernadoe alisisitiza.

    “Aah, Mama, hiyo miaka kumi nimesemea mzaha tu, nitaolewa hivi karibuni,” Belinda alijaribu kumliwaza mama yake.

    “Hata ukiolewa baada ya miaka kumi mama, sisi tunachoomba ni uhai utakaokuwezesha kulitumikia vyema taifa na kuendesha maisha yako na kusaidia nduguzo. Huyo Mama yako analilia wajukuu, mbona mimi babu yenu marehemu Mzee Mndolwa alikufa bila kuwaona nyie wajukuu zake. Kama wajukuu watapatikana tukiwa bado tuhai sawa, la sivyo basi si bahati yetu. Haya hiyo telegramu iliyoleta ujumbe iko wapi?” Mzee Bernadoe aliuliza.

    Kumbee, wakati watoto wengine walipokimbilia shambani kumwita Belinda, huku nyuma wengine walikwenda shuleni kumpasha habari mzee Bernadoe kuwa nyumbani kwake kulikuwa na mgeni. Kwa jinsi taarifa hiyo ilivyokuwa nusunusu, Mzee Bernadoe ambaye alikuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Sega, aliharakisha kurejea nyumbani.

    Kutoka shuleni hadi nyumbani kwa Mzee Bernadoe ulikuwa mwendo wa robo saa. Alipofika nyumbani ndipo alipowakuta Belinda na mama yake wakiwa katika ule mzozo juu ya kazi yake binti yao.

    Baada ya kusoma ujumbe uliokuwamo ndani ya ile telegramu, Mzee Bernadoe aliikunja akamrejeshea Belinda.

    “Sawa, naona kama kawaida ya siku zote, hii telegramu haitoi hata fununu kidogo ya kazi unayoitiwa huko Zanzibar. Au unafahamu kuna kazi gani huko Visiwani?” Mzee Bernadoe aliuliza.

    “Hata, sifahamu Baba, lakini mpaka kufikia hatua ya kunikatizia likizo yangu, basi bila shaka kuna kazi nzito sana huko,” Belinda alijibu.

    “Mnhuu, vyema. Hatuna la kusema zaidi ya kukuombea mafanikio na salama. Nitapenda kupata angalao telegramu yako ukiwa huko Visiwani. Usituweke katika hali ya wasiwasi,” Mzee Bernadoe alimuasa binti yake.

    “Wasiwasi gani tena. Wewe si unaifurahia kazi yake hiyo ya hatari. Hata akifa huko si utaona ni sawa tu?” Mama Belinda alisema kwa hamaki kidogo.

    “Aa-aah, mambo ya kufa yajia nini tena? Usimtilie mtoto nuksi. Hata kama akikaa hapa kijijini kama ni kufa si atakufa tu. Nenda kajiandae kwa safari yako Mama,” Mzee Bernadoe alisema huku akiketi vizuri kwenye sofa ili aweze kuyakabili mashambulizi zaidi ya mkewe.





    “Mnhuu, vyema. Hatuna la kusema zaidi ya kukuombea mafanikio na salama. Nitapenda kupata angalao telegramu yako ukiwa huko Visiwani. Usituweke katika hali ya wasiwasi,” Mzee Bernadoe alimuasa binti yake.

    “Wasiwasi gani tena. Wewe si unaifurahia kazi yake hiyo ya hatari. Hata akifa huko si utaona ni sawa tu?” Mama Belinda alisema kwa hamaki kidogo.

    “Aa-aah, mambo ya kufa yajia nini tena? Usimtilie mtoto nuksi. Hata kama akikaa hapa kijijini kama ni kufa si atakufa tu. Nenda kajiandae kwa safari yako Mama,” Mzee Bernadoe alisema huku akiketi vizuri kwenye sofa ili aweze kuyakabili mashambulizi zaidi ya mkewe.

    *****

    “Habari za asubuhi mabibi na mabwana. Rubani Misti Sheki na wana anga wenzake, tunawakaribisha katika ndege hii aina ya Fokker Friendship Nambari TC 505 inayoelekea Pemba kupitia Zanzibar. Safari yetu hadi Zanzibar itachukuwa muda wa dakika ishirini na tutaruka juu umbali wa futi 2800 kutoka usawa wa bahari. Tafadhali rekebisheni viti vyenu wima na fungeni mikanda yenu tayari kwa kuruka…….”

    Belinda aliyasikia nusunusu maneno hayo ambayo yalitamkwa na msichana mhudumu wa ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania – ATC. Ndege hiyo ilikuwa ikikaribia kuchukua kasi ili iruke kutoka uwanja wa ndege wa Tanga. Ilikuwa asubuhi, yapata saa nne siku ya Jumatano.

    Belinda aliketi kiti cha dirishani upande wa kushoto sehemu ya kati ya ndege hiyo iliyokuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 42. Karibu naye alikaa mama mmoja chotara wa Kiarabu akiwa amempakata mtoto mchanga.

    Wakati ndege iliponyanyuka na kuingia anga la Tanga kuelekea Bahari ya Hindi, mawazo yake Belinda yalirejea kijijini kwao Sega, na hasa kwa mama yake. Alikumbuka na kuwaza juu ya wasiwasi mkubwa aliomuacha nao mama yake.

    Belinda aliuelewa vyema wasiwasi aliokuwa nao mama yake kuhusu kazi yake na pia kukawia kwake kuolewa. Akiwa mpelelezi wa ngazi ya A-5 katika Kikosi cha BUNDI, Belinda alikuwa mmoja wa wapelelezi waliotumainiwa sana katika kikosi hicho cha Kurugenzi ya Usalama wa Taifa la Tanzania.

    Belinda Bernadoe, ambaye wenzie ndani ya BUNDI walimwita BeBe kwa kufupisha majina yake mawili, alikuwa ndiye mwanamke pekee katika ngazi ya A ndani ya Kikosi hicho. Na kama nambari yake 5 inavyoonyesha, ni kwamba juu yake walikuwepo wapelelezi wengine wanne tu, wote wanaume.

    BeBe alijiunga na Jeshi la Usalama kwa ari ya moyo wake, na wala si kwa sababu nyingine zozote. Umbile lake halikuzidi wala kupungua. Maungo na viungo vya mwili wake vilijitandaza vyema kuunda sura na umbo jamali. Enzi zetu Chuoni wasichana wa umbo la Bebe tuliwapa sifa ya umbo la nambari 8, yaani juu kupana, kati pembamba, na chini kupana. Si unaiona nambari nane (8) ilivyo? Basi bila shaka tupo pamoja.

    Kwa upande wa elimu, BeBe alisoma vya kutosha. Baada ya kumaliza kidato cha sita, angeweza kujiunga na Chuo Kikuu, lakini alikataa, na badala yake akajiunga kwa muda na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kabla ya kujiunga moja kwa moja na Jeshi la Polisi, Idara ya Upelelezi.

    Mwaka mmoja tu baada ya kujiunga na Jeshi hilo la Polisi, ikiwa ni kutokana na juhudi zake, BeBe alipelekwa Uingereza ambako alipata mafunzo ya miaka miwili. Aliporudi, alifanya kazi miaka miwili kisha akapelekwa Cuba ambako alipata tena mafunzo ya miaka miwili.

    Baada ya mafunzo hayo ya nje na ya hapa nyumbani Tanzania, BeBe akatokea kuwa mmoja wa wapelelezi mahiri, akawa sumu ya wahalifu. Alikuwa amefuzu na kupata mkanda mweusi katika fani za kung-fu na judo, na akawa anao uwezo mkubwa wa kujihami katika mapambano ya ana kwa ana akiwa na silaha au kavukavu, bila zana. Viungo vya mwili wake, na hasa mikono na miguu vilikuwa zana tosha katika mapambano.

    Wakiwa angani kuelekea Zanzibar, BeBe alikumbuka jinsi Mama yake alivyougomea uamuzi wake wa kujiunga na Jeshi la Polisi. Laiti kama Mzee Bernadoe asingesimama kidete, bila shaka BeBe asingelikuwa alipo kwenye ulimwengu wa makachero.

    Kwa kiasi fulani BeBe aliuona uhalali wa wasiwasi aliokuwa nao Mama yake. Alizingatia ukweli kuwa yeye ni mtoto wa kwanza katika familia yao. Mdogo wake wa kwanza, Stephano, ndio kwanza alikuwa Chuoni akichukuwa mafunzo ya Ualimu, akiwa amepania kufuata nyayo za baba yao, Mzee Bernadoe. Mdogo wake wa pili na wa mwisho ni yule kijana Mndolwa ambaye alizitimua mbio na wenzie kumfuata kule shambani.

    Pamoja na ukweli kwamba kazi yake ilimwezesha kuisaidia vyema familia yake, na hata kuweza kufungua duka pale kijijini Sega, bado BeBe hakuwa na muda mrefu wa kukaa pamoja na familia yake, na hasa Mama yake ambaye alipenda BeBe awe karibu naye. Lakini kubwa zaidi lililomkera Mama yake ni BeBe kutotaka kuolewa.

    Suala la kuolewa lilimkera sana BeBe mwenyewe pia. Alipenda aolewe na aishi na mume kama walivyo wanawake wengine. Lakini hiyo ingekuwa na maana kuwa ingebidi azipe kisogo kazi halisi za ukachero. Ingebidi asishiriki kikamilifu kwenye uwanja wa mapambano na wahalifu. Kila alipofikiria kazi za kucheza na majalada ofisini, BeBe alitupilia mbali wazo la kuolewa.

    “Mabibi na Mabwana, sasa tunakaribia kutua kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar. Tafadhali, fungeni vyema mikanda na rekebisheni viti vyenu wima tayari kwa kutua.”

    Mawazo yake BeBe yalikatizwa na sauti ya msichana mhudumu wa ndani ya ndege. Aliyafutilia mbali mawazo hayo akayahifadhi katika chumba cha kumbukumbu ndani ya ubongo wake. Alirejesha fikra na fahamu zake kwenye kazi iliyokuwa mbele yake kule Zanzibar, ambayo hadi wakati ule hakujuwa ilihusu nini.

    Kutoka uwanja wa ndege alikodi teksi akaenda hadi Michenzani, eneo ambalo kwa mji wa Zanzibar lina sura na umaarufu wa kipekee. Ni eneo ambalo yapo majumba marefu ya ghorofa, lakini si urefu wa kwenda juu, bali urefu wa mshazari. Ungeunganisha mabogi ya gari moshi, jengo moja la Michenzani lingeweza kuchukua urefu wa mabogi kiasi manane hivi, kama sikosei. Hayo ni majengo ambayo Baba wa Taifa la Zanzibar, hayati Sheikh Abeid Amani Karume aliyajenga enzi za uongozi wake kujaribu kupunguza uhaba wa makazi kwa wakazi wa Zanzibar.

    Teksi ilisimama karibu na ngazi ya Block C, naye BeBe alimlipa dereva nauli yake, akamshukuru wakaagana. Alipanda ngazi hadi ghorofa ya pili, akabonyeza kitufe cha kengele kilichokuwa pembeni mwa mlango wa flati nambari 1202.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa BeBe kufika Zanzibar. Alishawahi kwenda huko mara kadhaa kwa safari za kikazi na za binafsi. Ni katika moja ya safari hizo ndipo alipokutana na msichana aitwaye Zamoradi, wakajenga ushoga uliostawi na kunawiri. Baada ya kufahamiana kwao huko ikawa kila alipokwenda Zanzibar BeBe alifikia kwa Zamoradi, naye Zamoradi akienda Dar es Salaam hufikia kwa BeBe.

    Mara nyingi BeBe alipopata safari kwenda Zanzibar alimfahamisha shoga yake siku kadhaa kabla ya safari. Lakini safari hii kama zilivyokuwa nyingine za ghafla, hakuweza japo kumpigia simu mwenzie. Hata hivyo, hakuwa na wasiwasi maana shoga yake alishazoea kushitukia BeBe keshafika Zanzibar bila taarifa.

    BeBe aliisikia kengele ikilia ndani, akasubiri sekunde mbili tatu lakini hakuona dalili ya mlango kufunguliwa. Alijuwa kuwa wakati ule wa saa tano asubuhi Zamoradi angekuwa kazini kwake, makao makuu ya BIKANGA. Hata hivyo alibahatisha kupiga kengele kwamba labda kungekuwa na mgeni pale nyumbani. Kuna safari moja alifika Zanzibar bila taarifa kama hivi na alimkuta Mama yake Zamoradi akiwa amemtembelea binti yake akitokea kijijini kwao Tumbatu.

    Baada ya kujihakikishia kuwa hamkuwa na mtu mle ndani, BeBe alifungua mkoba wake akatoa kishada cha funguo. Alitumia moja ya funguo hizo kufungulia mlango akaingia ndani. Ufunguo huo alikabidhiwa na Zamoradi siku ya kwanza alipofika pale kwake.

    “Unakaribishwa hapa wakati wowote, ufunguo wako huu,” Zamoradi alimweleza shoga yake siku alipomkabidhi ufunguo ule.

    Naye Zamoradi alipomtembelea BeBe kwa mara ya kwanza Dar es Salaam, mambo yakawa vivyo hivyo. BeBe alimkabidhi shoga yake ufunguo wa nyumba yake ambao Zamoradi aliutumia kila alipokwenda Dar es Salaam.

    Baada ya kuhifadhi begi lake chumbani, BeBe alirudi sebuleni akaketi kwenye sofa na kuchukua simu iliyokuwa juu ya stuli. Alizungusha nambari kadhaa na mara moja kengele ikalia na simu ikapokelewa upande wa pili.

    “Hallo, Ofisi ya Mkurugenzi Masoko, BIKANGA, nikusaidieje tafadhali.” Iliyojibu simu hiyo ilikuwa sauti nyororo ya kike yenye lafudhi halisi ya Kiunguja.

    “Najisaidia mwenyewe nyumbani kwako mpenzi, hujambo?” BeBe alijibu kwa sauti iliyojaa bashasha tele.

    “Haa, Beli, karibu sana. Habari za safari, ndiyo kwanza unafika?” Zamoradi aliuliza kwa shauku kubwa.

    “Ndiyo, nimefika punde tu, lakini tusizungumze mengi sasa, tutazungumza jioni ukirudi. Unatarajia kuwa nyumbani saa ngapi?” BeBe alimuuliza.

    “Maadam upo nitarudi mapema, saa tisaa hivi nitakuwa nyumbani. Utapenda kula nini jioni hii mpenzi?” Zamoradi alimuuliza rafikiye.

    “Usiponikaangia ngisi nitakukaanga wewe mwenyewe nikutoelee!” BeBe alisema katika hali ya kicheko.

    ”Wewe na ngisi! Sawa tutaonana jioni,” Zamoradi alijibu, naye pia akiwa amejawa na kicheko.

    ”Sawa, kazi njema mpenzi,” BeBe alijibu, akarejesha mkono wa simu mahala pake.

    Kabla hajaondoka pale nyumbani kwa Zamoradi, BeBe alichukuwa soda aina ya Heltho ndani ya jokofu, akaifungua akanywa. Aliangaza macho pale sebuleni akaona kulikuwa na mabadiliko makubwa yaliyofanyika tangu alipofika mara ya mwisho, kiasi miezi sita hivi iliyopita.

    Aliona seti mpya ya vyombo ndani ya kabati la vyombo. Aliona pia kuwa pazia zote za milango ya vyumbani na madirisha zilikuwa mpya na za bei mbaya. Kubwa zaidi ni seti ya TV na Video aina ya SONY . TV ilikuwa ya nchi 27. Aliona pia kuwa hata zulia lilikuwa jipya tena la sufu badala ya plastiki ambalo aliliacha alipofika pale mara ya mwisho.

    ”Kwa mshahara wa Katibu Muhtasi, Zamoradi anaishi vizuri mno, kupita uwezo alionao. Labda mwenzangu kapata mshikaji mwenye nazo. Mambo si mabaya,” BeBe alijisemesha, akizingatia kuwa rafiki yake alikuwa Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi Masoko wa BIKANGA, Shirika la umma lililohusika na uuzaji wa zao la karafuu nchi za ng’ambo.

    3 - Magendo

    “Nitaeleza kifupi juu ya kazi uliyoitiwa, maana taarifa nyingine kuhusu suala hili zimo ndani ya majalada ya siri ambayo utakabidhiwa mara tumalizapo kikao hiki,“ Kessi Kussi (KK), Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KKMZ), au kwa jina la siri SIAFU, alisema huku akimwangalia BeBe.

    Walikuwa watu wanne sebuleni mwa chumba alichofikia Mkuu wa Kikosi cha BUNDI, Momaa Bulo (MB). Mkuu huyo ambaye naye alikuwepo akitokea Dar es Salaam, alifikia Hoteli ya Ufukoni, na chumba chake kilikuwa ni vile ambavyo ni maalum kwa wakubwa au wenye nazo (suite), vyenye chumba cha kulala mbali na sebule ya maongezi. Pamoja na wakuu hao wawili na BeBe, alikuwapo pia kijana mmoja mwanamume kwa jina Pei Salem, ambaye alikuwa ni mmoja wa wapelelezi wa daraja la juu katika kikosi cha SIAFU.

    Mara baada ya kunywa soda kule kwa Zamoradi, BeBe alikodi teksi hadi Hoteli ya Ufukoni ambako alijua MB ndiko anakofikia akiwa Zanzibar. Huko aliwakuta wakuu hao wawili wa vyombo vikuu vya Usalama vya Serikali zote mbili, na kijana Pei Salem. Walikuwa wakimsubiri na baada ya kusalimiana mazungumzo yalianza mara moja ambapo Mkuu wa SIAFU, KK, alianza kuelezea kazi iliyowakabili.

    "Kama unavyofahamu, Kikosi cha SIAFU tumekuwa na mapambano makali na waendesha magendo ya karafuu. Tumeweza kuwatia mbaroni baadhi yao, lakini ni wale wadogo. Kama ingekuwa ni uvuvi wa samaki, tungesema tumeambulia dagaa, lakini sangara wametupiga chenga. Ukweli ni kwamba waendesha magendo wakubwa wametuelemea na wanatuambaa kila tunapokaribia kuwatia mbaroni,“ KK alisema hayo akiwa bado anamtazama BeBe ambaye naye alitulia tuli akimsikiliza kwa makini bila kutia neno. MB na Pei nao walikuwa kimya wakisikiliza.

    ”Hivi sasa hali imekuwa mbaya sana, na imefikia kwamba asilimia sabini au zaidi ya karafuu zinazozalishwa nchini zinaishia mikononi mwa waendesha magendo. Sina haja ya kusisitiza ukweli kwamba Taifa linapoteza fedha nyingi za kigeni kutokana na magendo haya ya karafuu. Uzito wa athari ya hali hiyo sote tunaufahamu, tunapozingatia kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea sana zao la karafuu.“

    ”Kwa maneno mengine, anachosema KK ni kwamba uchumi wa Taifa unazidi kudidimia kutokana na pigo hili la magendo ya karafuu. Tunachotakiwa kufanya ni kuutafuta mtandao wa waendesha magendo wakubwa na wadogo, kuzivunjilia mbali nguvu zao ili kunusuru uchumi wa Taifa,“ MB aliongezea.

    ”Ni sawa kabisa, hiyo ndiyo kazi iliyopo mbele yetu, na ni rahisi kuitamka lakini kuitekeleza ni ngumu, ugumu ambao miaka nenda rudi tumekuwa nao,“ KK alisema.

    ”Swali moja Mkuu, tafadhali. Je kuna uhakika kuwa karafuu yote iliyoangukia mikononi mwa hao waendesha magendo imeshavushwa nje ya nchi?“ BeBe aliuliza.

    ”Kwa kweli A-5 kujibu ndio au hapana ni vigumu. Hata hivyo, Serikali inaamini kuwa bado shehena kubwa ya karafuu ipo imefichwa hapahapa nchini na inavushwa kidogo kidogo, hasa baada ya Serikali kuomba msaada wa Serikali za nchi jirani kuwasaka waendesha magendo. Lakini jitihada zetu kufichua maficho ya karafuu hiyo iliyomo mikononi mwa waendesha magendo bado hazijazaa matunda,“ KK alieleza.

    ”Nia ya Serikali ni kuona kuwa kundi la waendesha magendo linakamatwa na njia zao za kuvusha mali zinavunjwa. Serikali ilifikia hatua ya kuomba msaada kutoka nje ili wapelelezi kutoka mataifa rafiki ya Ulaya waje kusaidia, lakini gharama zao ni kubwa mno. Hivyo ikaamuliwa kuwa tuunganishe nguvu na uwezo wa vikundi vyetu, BUNDI kutoka Bara na SIAFU hapa Visiwani, ili kwa pamoja tuifanye wenyewe kazi hii. Ndiyo sababu imebidi niikatize likizo yako, A-5 ili uje ukabidhiwe jukumu hili ambalo lina umuhimu wa kipekee kwa Taifa,“ MB alielekeza maelezo hayo kwa BeBe.

    “Na kwa upande wa SIAFU, Pei ndiye atakayetuwakilisha katika timu yenu ya watu wawili kuchimbua mizizi ya washenzi hawa waendesha magendo. Katika timu yenu hii, BeBe utakuwa kiongozi na Pei atakuwa msaidizi wako,“ KK alitoa maelekezo.

    ”Kama kawaida A-5, mtapata kila msaada utakaohitajika. Nyie mtakuwa msitari wa mbele katika mapambano haya, lakini vikosi vyetu vyote na vyombo vingine vya dola pote Bara na hapa Visiwani, vitakuwa tayari kuwapa msaada wakati wote. Nawapa tahadhari kwamba hawa jamaa waendesha magendo ni hatari. Kwa lugha mnayoifahamu katika kazi zetu hawa ni <extremely dangerous>,“ MB alisema kwa msisitizo mkubwa.

    Kisha akaendelea: “Ingawa haikutangazwa, ilizuiwa, lakini kuna vijana watatu wa SIAFU ambao wamekufa vifo vya kutisha. Wote walikuwa katika kazi ya kuwasaka waendesha magendo ya karafuu na walikufa nyakati na mazingira tofauti. Tunaamini vifo vyao ni matokeo ya unyama wa waendesha magendo. Hivyo, hii ni vita ya kufa au kupona,“ MB aliwatahadharisha BeBe na Pei.

    ”Na ni vyema mkumbuke, pia kwamba muda tuliopewa kupata matokea mazuri ya kazi hii sasa ni mfupi sana. Serikali inataka matokeo mazuri na ya haraka. Je mnalo lolote la kuuliza?“ KK alisema.

    ”Swali moja tu Wakuu. Tukiondoa sisi tuliopo hapa, kuna mwingine yeyote anayefahamu kuwa mimi nipo hapa Unguja kwa kazi hii, hasa katika kikosi cha SIAFU?“ BeBe aliuliza.

    ”Hapana, ni sisi tu ndio tunaofahamu. Vipi unauliza hivyo?“ KK aliuliza.

    “Ni kiasi tu cha kujitoa wasiwasi, na ningeomba ibakie hivyo ilivyo, mwingine asijue kuwa nipo hapa kwa kazi hii,” BeBe alijibu.

    “Vyema, ukiondoa uongozi wa juu kabisa wa taasisi za kitaifa sidhani kama kuna zaidi ya sisi atakayejua. Mkihitaji msaada wasilianeni nami au na MB moja kwa moja, kwa njia zetu za kawaida,” KK aliwaelekeza.

    “Tunawaacha hapa kwa muda A-5, tuna miadi na Waziri wa Usalama wa Taifa. Bila shaka mtapanga kazi zenu. Usiondoke hapa mpaka nirudi A-5, “ MB alimweleza BeBe, kisha yeye na KK wakaondoka.





    “Tunawaacha hapa kwa muda A-5, tuna miadi na Waziri wa Usalama wa Taifa. Bila shaka mtapanga kazi zenu. Usiondoke hapa mpaka nirudi A-5, “ MB alimweleza BeBe, kisha yeye na KK wakaondoka.

    4 - Wasaliti

    ”Jambo moja muhimu ni kwamba nisionekane hadharani mahala popote nikiwa nawe au na afisa mwingine wa SIAFU, au hata afisa wa chombo kingine cha Usalama.

    Sina haja ya kurejea kusisitiza kuwapo kwangu hapa Unguja kwa kazi hii kusifahamike na yoyote zaidi yetu na wale Wakuu wawili,“ BeBe alisema.

    ”Unadhani kuna uwezekano kukawa na ndumilakuwili ndani ya SIAFU?“ Pei aliuliza.

    ”Ndiyo, nahisi hivyo, kwamba yupo afisa mmoja au wapo wengi tena wa ngazi za juu au za kati katika SIAFU ambaye au ambao ni ndumilakuwili, wanavujisha siri. Jiulize Pei, iweje kila mtego uliotegwa huku nyuma ulifyatuka na waendesha magendo wakawazidi maarifa kila mara?“ BeBe alimuuliza mwenzie.

    ”Nafikiri kuna ukweli katika fikara zako. Mimi nimerudi wiki saba hivi zilizopita kutoka mafunzoni Uingereza, na niliacha SIAFU ikiwa katika mapambano na waendesha magendo. Lakini hali nilivyoikuta ndani ya kikosi hiki naona kuna mwanya mkubwa wa siri kuvuja kabla ya utekelezaji wa hatua muhimu,“ Pei alisema.

    Saa nzima hivi ilipita tangu walipoachwa pale sebuleni chumbani kwa MB Hoteli ya Ufukoni. Waliyapitia kwa makini sana yale majalada matatu yaliyokuwa na nembo ya SIAFU, na yaliyoandikwa SIRI KUU kwa wino mzito mwekundu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika muda wote huo, walichoambulia ni taarifa za kufyatuka kwa mitego ya SIAFU iliyotegwa kuwanasa waendesha magendo.

    Vifo vya wale vijana watatu kama alivyoeleza MB vilielezwa kirefu ndani ya taarifa hizo.Mmoja wao alikutwa akielea majini pwani ya Mkokotoni, na uchunguzi ulionyesha kuwa kabla ya kutupwa majini alikuwa amevunjwa shingo. Wa pili aliokotwa karibu na gati bandarini Zanzibar akiwa amefungwa kamba miguu na mikono na ilisadikiwa kuwa alikufa kwa kula au kulishwa sumu kali.

    Kinywa na koo lake vilikuwa na michubuko na malengelenge mfano wa mtu aliyemeza makaa ya moto.

    Kijana wa tatu alikuwa amekatwa vibaya sana tumboni na sehemu zake za siri, naye aliokotwa ufukweni sehemu za Makunduchi, na kabla ya kufa kwao wote hawakuwahi kutoa taarifa yoyote juu ya upelelezi wao.”Hawa jamaa kweli ni washenzi na makatili.

    Umeona jinsi walivyowaua kinyama hawa wenzetu?“ Pei alisema.”Ni kweli, lakini dawa ya moto ni moto, wataipata,“ BeBe alisema huku akifunga na kupanga mezani yale majalada.

    ”Sasa, sikia Pei, kukutana kwetu mara nyingi itakuwa usiku, na hatutakuwa na mahala pamoja pakukutania, itategemea tukio la siku hiyo lilivyo. Lakini, mawasiliano yetu yatakuwa ya simu. Mimi simu nitakayotumia ni Nambari 0748-333300. Wewe nitakuwa nakupata kwa simu nambari ngapi?“

    ”Nipate kwa simu nambari 0744-561000, hapokei mtu yoyote zaidi yangu simu hiyo.“

    ”Vyema, basi kwa shughuli zaidi, na hasa wapi tutaanzia nitakuarifu leo jioni kiasi saa tatu usiku, uwe karibu na simu yako.“

    ”Sawa BeBe, nitasubiri simu yako. Nimewahi kusikia sifa zako juu ya mambo makubwa uliyokwisha kuyafanya katika kazi zetu hizi. Naamini kuwa pamoja nawe tutaifanya kazi hii kwa mafanikio.“

    ”Asante sana Pei. Nami pia naamini kuwa hadi wewe kupewa jukumu hili na Mkuu wangu kukubali ufanye nami kazi, basi nawe ni mahiri. Ndiyo, pamoja tutashinda, tumwombe Mungu atuongoze vizuri.

    “Baada ya Pei kuondoka, BeBe alipekuwa tena yale majalada, akatafakari kwa undani suala lililokuwa mbele yake. Moja lililojirudiarudia akilini mwake ni ile hisia nzito kwamba ndani ya SIAFU alikuwemo au walikuwepo ndumilakuwili, watu waliovujisha siri za Kikosi kwa maadui.

    ”Itakuwaje kila mtego wa SIAFU ufyatuke na hawa waendesha magendo waambae?“ BeBe alijiuliza mwenyewe kwa sauti, na katika kuwaza huko hakumsikia wala kumuona Mkuu wake MB alipoingia pale ndani kupitia mlango wa chumbani kwake.

    BeBe alishtuka kidogo pale aliposikia sauti nzito ya MB aliposema:

    “Hilo ni swali zuri BeBe, je unadhani kuna kasoro gani?”BeBe aligeuza kichwa taratibu kumtazama Mkuu wake, akatuliza macho yake kitambo kifupi katika uso wa MB uliobeba tabasamu, kisha akasema:

    ”Ipo kasoro Mkuu. Viwe viwavyo, yupo au wapo wasaliti ndani ya SIAFU, tena si mtu au watu wa ngazi za chini, bali kiongozi au viongozi wenye kuzijua vyema siri kuu za kazi za kikosi hiki.“

    ”BeBe, nadhani hisia zako zinaweza kuwa na ukweli, mimi pia baada ya kusoma taarifa hizo na kupata maelezo zaidi kutoka kwa huyu mwenzangu KK, fikra ya kwanza iliyonijia ilikuwa ni kuwapo kwa msaliti au wasaliti ndani ya SIAFU.

    Kwa hiyo wewe na mimi hatukutofautiana katika hilo. Nilimuuliza KK juu ya uwezekano huo, naye alisema kuwa inawezekana, lakini hawajafikiria hivyo na hawajachukua hatua zozote za tahadhari,“ MB alisema akiwa sasa ameketi kwenye sofa mkabala na BeBe.

    ”Wajua Mkuu, inashangaza sana. Kwa nini siku zote hizi wasichukue hatua za tahadhari. Huoni kuwa hiyo peke yake ni dosari? Sisemi kuwa KK anahusika kuuficha ukweli, lakini inatia wasiwasi.”

    ”Ipo dosari kubwa, lakini nadhani hawa wenzetu huku wamepitiliza kiwango cha kuaminiana.

    Si rahisi mmoja kumshuku mwingine, hasa kwa vile wote wanaoshughulika na kazi hii ni maafisa walioapishwa wakati wanaingia katika SIAFU.“

    ”Basi kama ni hivyo Mkuu, huyo msaliti au wasaliti zao zimetimia, tutawaumbua.“

    ”Utaanzia wapi?“

    ”Hawa dawa yao ni mtego tu. Mkuu usishangae, lakini mimi safari hii huenda nikaolewa huku Unguja.”

    ”Uolewe? BeBe acha utani.“

    ”Kwani mie na wewe tunataniana Mkuu?“

    ”Sasa kama unajua hatutaniani kwanini unaleta utani?“

    BeBe alicheka kidogo, kisha akasema: ”Mkuu, nitaolewa na waendesha magendo. Ndiyo njia pekee ya kuwa karibu nao!“MB alikaa kimya kwa sekunde kadhaa akitafakari maneno ya BeBe, kisha akamtazama BeBe kwa sekunde kadhaa, akasema: ”Wajua A-5, wewe unastahili nafasi uliyopo katika BUNDI. Mara nyingi sana mimi hushangazwa na unavyoweza kuchambua mambo na kupanga mambo yako haraka haraka.

    Kwa hiyo unaona utaweza kuwafikia kwa urahisi hawa jamaa kwa kuolewa na mmoja wao?“

    ”Ndiyo Mkuu, usishangae kusikia nimeolewa ndoa ya mkeka.

    “Mkuu wake, MB, alicheka akasema: Lakinii, utajuaje kuwa atakayekuoa ni mmoja wao?“

    ”Mkuu, hiyo ni kazi ndogo sana. Si nilikwishakueleza kuhusu yule rafiki yangu aitwaye Zamoradi? Unakumbuka nilishakufahamisha kuwa yeye ni katibu muhtasi wa mkuu wa Shirika la Biashara ya Karafuu Ng’ambo – BIKANG’A.

    Basi yeye ndiye atakayenitafutia mchumba atakayeniweka karibu na waendesha magendo hao.“

    ”Mnhuu, si wazo baya. Nadhani ataweza. Unahisi kuwa kule kwenye Shirika la BIKANG’A kunauwezekano wa kuwepo wanaoshirikiana na waendesha magendo ya karafuu?“

    ”Nina hisia hizo, maana kwa vyovyote vile waendesha magendo ni lazima wawe ni wafanyabiashara wakubwa, na bila shaka wanayo mawasiliano na BIKANGA, hasa katika ngazi za juu za shirika lile. Nitamdodosa Zamoradi na pengine naweza kupata fununu itakayoniwezesha kusonga mbele na upelelezi.“

    ”Sawa BeBe, mimi nakutakia kila la kheri. Mchana huu narejea Dar es Salaam. Ninachotarajia kwako ni mafanikio. Hakikisha kuwa mara hii pia unalijenga vyema jina la Kikosi chetu.

    Usisite kuomba msaada zaidi ikibidi. Nakutakia kila kheri.

    “Wote walinyanyuka wakapeana mikono. Kama ilivyo siku zote Momaa Bulo alipopeana mkono na BeBe mwili mzima ulimsisimka na hisia za kumtamani zilizagaa maungoni.

    Lakini mara hii pia alijizuia, akakumbuka ule mwiko wake mkubwa wa kutoanzisha uhusiano wa kimapenzi na waliopo chini ya uongozi wake kazini.

    BeBe aliutambua sana msimamo huo wa MB na aliuheshimu, ingawa alijuwa kuwa Mkuu wake alimuashiki kama ilivyokuwa kwake yeye.

    Lakini alijua suala la mapenzi na MB lilikuwa ndoto. Alipopeana mkono na MB naye alihisi damu zikimchemka lakini aliuma meno. Walitazamana kwa sekunde kadhaa, kisha wote wakatabasamu.”Kwaheri A-5, jichunge na uwe mwangalifu, maana watu hawa utakaopambana nao ni nyoka.“

    ”Usiwe na wasiwasi Mkuu, dawa ya nyoka ni kukiponda kichwa chake, na tutakiponda.“Waliagana na BeBe akaondoka pale hotelini akimwacha Mkuu wake akijiandaa kwa safiri ya kurudi Dar es Salaam.5 - Nusanusa”Nyama wote wa bahari nawapenda, lakini ngisi ni nambari wahedi, na hasa ngisi aliyekaangwa nawe Zamoradi, ana utamu wa kipekee!“ BeBe alisema huku akichukua kwa umma vipande kadhaa vya ngisi aliyekaangwa.

    ”Usinivishe kilemba cha ukoka, weye wajua mapishi kulikoni mie,“ Zamoradi alimjibu shoga yake huku akiwa na tabasamu.

    Walikuwa wawili tu sebuleni kwake Zamoradi wakila chakula cha jioni kilichojumuisha chapati za maji, mahando, papa mbichi wa mchuzi na ngisi wa kukaanga.

    Alipotoka kule chumbani kwa Mkuu wake Hoteli ya Ufukoni, BeBe alipitia madukani ambako alinunua vifaa vidogovidogo kadhaa vya matashi ya kike. Kisha alikwenda mtaa wa Hodhini kwa wasusi wa nywele, ambako alisuka mtindo wa jakamoyo.

    ”Enhe, Beli safari ya kheri au ni ile misukosuko yenu ya kawaida?“ Zamoradi alimuuliza mwenzie huku wakiendelea kula chakula chao.

    ”Nimekuja kukuchunguza wewe hapo. Kwa mshahara wako ninaoujua miye wa Katibu Muhtasi, hivi vimbwanga ulivyonavyo humu ndani mwako vyatisha atii!“ BeBe alimjibu mwenzie kwa mzaha.

    Zamoradi alicheka, akajibu: ”Huo sasa ni wivu. Usiumie kichwa chako bure, hivi vitu vyote nimenunuliwa na mchumba wangu. Umeniwahi tu kuja hivi ghafla, maana ilikuwa wiki ijayo nikutumie kadi ya kuja kushuhudia kuposwa kwangu.“

    ”Hongera sana, mpenzi, huyo bwana bila shaka ni kizito kwelikweli. Au umempata mzungu wa unga?“ BeBe aliuliza tena kwa namna ya mzaha mzaha hivi, lakini kumbe alikuwa ndiyo keshaanza nusanusa kuhusu ukweli wa mabadiliko aliyoyaona kwa rafiki yake, na huku akijaribu kuona kama atapata fununu juu ya waendesha magendo ya karafuu.

    ”Basi nikupe siri ivyoo. Huyu bwana hata kazi aifanyayo siijui mie. Nami pia hujiuliza kama kweli si mzungu wa unga,“ Zamoradi alijibu.

    ”Kwani ukimuuliza kazi yake hukujibuje?“ BeBe aliuliza.

    ”Hata hanipi jibu lenye kueleweka, tena mara zote hujaribu kunikataza kumdodosa kuhusu jambo hilo. Lakini kila mara huniaga akienda kwenye safari zake, na haniambii anakwenda wapi. Husema tu kuwa hatakuwepo kwa siku kadhaa, na siku hizo kadhaa zinaweza kuwa wiki mbili hadi mwezi na zaidi.“

    ”Mnh, Zamo, mbona unanitisha mwaya. Wajua sipendi watu wa aina hiyo ya mchumba wako. Naogopa asije akakufikisha pabaya, mpenzi. Kwani ulijuana naye vipi mtu huyo, na ni muda gani umepita sasa tangu umfahamu?”

    ”Wala si muda mrefu, ni kama miezi mitatu tu iliyopita, na ilikuwa palepale kazini kwetu. Walifika vijana wane na mzee mmoja wakaomba kumuona bosi wangu. Hawakuwa na miadi naye, lakini wakasema wanashida naye ya muhimu. Basi nikamgongea simu bosi naye akasema niwaulize majina. Yule mzee akasema jina lake ni Mudricki Budji. Nikamtajia jina hilo bosi, naye akaruhusu wakamuone, wakaingia.

    ”Zamoradi alisita kidogo akatafuna na kumeza chakula huku mwenzie BeBe akiwa tuli naye akiendelea kula. Alipoyasikia yale aliyoyasema mwenzie, BeBe aliihisi sehemu fulani ya ubongo wake ikichemka na kuanza kutoa ishara aliyoijuwa sana. Hii ilikuwa ishara ya hatari, ambayo ilimwashiria kuwa hapa kuna jambo.

    ”Basi wajua tena mambo ya vijana. Walipotoka mle ndani ambamo walikaa kiasi lisaa lizima, kijana mmoja akawa amesita kidogo pale mezani kwangu, akatupa ndoana, tena aliitupa bila mimi kutegemea, alinistukiza. “Ndoana huwa na chambo, ulichowekewa wewe kilikuwa nini?”

    “’Zawadi yako hiyo,’ alisema huku akiweka tiketi ya kuingilia kwenye onyesho maalum la kikundi cha taarabu cha Culture ambalo lilikuwa lifanyike kesho yake kule kwenye ukumbi wa Hoteli ya Ufukoni.

    Tamasha lile lilikuwa maalum kwa ugeni wa viongozi wa juu wa Serikali ya Oman ambao ulitembelea Zanzibar. Tiketi ya kuingilia tamasha hilo ilikuwa ikiuzwa kwa Shillingi laki moja, na mie Zamo wala sikuwa hata na ndoto ya kuliona tamasha hilo.”

    “Mnh, makubwa. Kweli ilikuwa ndoana yenye chambo kilichonona. Kwa hiyo ukakipapatikia chambo na ndoana ikakunasa!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wajua mpenzi, mimi si changudoa, kwa hiyo usinifikirie vibaya. Fikiria, ile fikra tu kwamba nami siku ile ningeonekana kwenye tamasha la wazito! Kweli, nilikipapatikia chambo na ndoana ikaninasa barabara. Tena wajua, baada ya kuniachia ile tiketi akasema atanisubiri tuingie wote ukumbini kule Hoteli ya Ufukoni. Waona, ningejinasuaje hapo?”

    “Kwa hiyo baada ya hapo tena, mambo yakaiva, hadi kufikia uchumba. Na hivi ninavyoviona na nisivyoviona ni matokeo ya tiketi ya kuingia kwenye tamasha. Hongera sana.”

    “Nisamehe kama nimekuudhi kwa kujirahisi namna hiyo Beli, najuwa wewe ni mtu wa maadili mema. Hapa nilipo ingawa tumekuwa marafiki kiasi miaka mine sasa simjui hata rafiki yako wa kiume.”

    “Aa-aaa, hujafanya lolote baya. Wewe ni msichana mrembo, na kwa vyovyote vile sikutegemea kama utaishi pekee daima dumu. Hata mimi ninaye nimpendaye, lakini humjui tu, ingawa hajawa mchumba bado. La muhimu ni kuwa hakikisha huyo jamaa ni mkweli na atakufaa katika maisha yako. Sikufichi, mpenzi, kama huyo jamaa ni mzungu wa unga au mwendesha maisha ya ubabaishaji, basi hakufai. Nakuhakikishia nitafanya kila niwezalo uachane naye.”

    “Beli, hata mimi sitakubali kuolewa na mzungu wa unga au mwendesha magendo ya aina yoyote. Hilo nakuhakikishia mpenzi.”

    “Sawa, sasa huyo mchumba wako nitamuonaje?”“Una bahati, kwa sababu yupo, hajasafiri, tena tunamiadi ya kuonana kesho jioni, kuna taarabu ya kikundi cha African Melody pale ukumbi wa Marhubi. Amesema atanifuata, kwa hiyo tutakwenda pamoja nawe.”

    “Mnh, nisingependa kuwavurugia starehe zenu, mimi nitabaki hapahapa.”

    “Usiwe na wasiwasi, nitamwambia aje na rafiki yake ili nawe uwe na mshikaji, unasemaje.”

    “Unataka kuniuza kwa wazungu wa unga siyo?”

    “Kwani kuna ubaya gani, mradi tu usibwie unga.”Basi wakacheka na kuendelea kula chakula chao. Wakati wote huo, BeBe alikuwa anazisikia kwa kishindo zaidi zile ishara za hatari ndani ya ubongo wake.





    “Una bahati, kwa sababu yupo, hajasafiri, tena tunamiadi ya kuonana kesho jioni, kuna taarabu ya kikundi cha African Melody pale ukumbi wa Marhubi. Amesema atanifuata, kwa hiyo tutakwenda pamoja nawe.”

    “Mnh, nisingependa kuwavurugia starehe zenu, mimi nitabaki hapahapa.”

    “Usiwe na wasiwasi, nitamwambia aje na rafiki yake ili nawe uwe na mshikaji, unasemaje.”

    “Unataka kuniuza kwa wazungu wa unga siyo?”

    “Kwani kuna ubaya gani, mradi tu usibwie unga.”

    Basi wakacheka na kuendelea kula chakula chao. Wakati wote huo, BeBe alikuwa anazisikia kwa kishindo zaidi zile ishara za hatari ndani ya ubongo wake.

    ”Kwa hakika, huu ni mwanzo mzuri, nitafuata hisia zangu kwani hazijawahi kunipoteza,“ alijisemesha kimoyomoyo.

    6 - Purukushani

    Ukumbi wa Marhubi ulijaa sana siku hiyo ambapo kikundi maarufu cha taarabu cha African Melody kilikuwa kinatumbuiza. BeBe na rafiki yake Zamoradi walikuwa miongoni mwa wapenzi wa taarabu waliokuwepo kwenye onyesho hilo. Pamoja nao alikuwepo pia mchumba wake Zamoradi, jina lake lilikuwa Burshid. Vilevile, alikuwepo kijana mwingine rafikiye Burshid, ambaye alijulikana kwa jina Osmun.

    Kama ilivyokuwa kwenye maonyesho ya kikundi cha African Melody, viti vilikuwa havikaliki. Mashabiki wa taarabu walijimwayamwaya kila ulipopigwa wimbo. Mambo yalikuwa moto zaidi pale wimbo maalum uliokuwa ukizinduliwa siku hiyo ulipopigwa kwa mara ya kwanza. Wimbo huo: BIBIE KUWAYAWAYA haukubakisha hata mwana dada mmoja kitini. Hata wanaume waliokuwa wameketi walionekana wakiyumbayumba vitini kwa mapigo na mirindimo ya vinanda, tumba na vyombo vingine vilivyoupamba wimbo huo. Lakini kali zaidi ilikuwa ni sauti ya mwimbaji ZUZIA KADRI, ambaye ndiye pia aliyeutunga.

    Ulikuwa ni wimbo uliozungumzia adha ya kumpenda asiyependeka, ambaye macho yake yako juu juu, haridhiki mfano wa kuku. Wajua tena, kuku mwekee mchele ndani ya ungo, hawezi kula bila kuutawanya mchele huo aone chini kuna nini. Matokeo yake anaumwaga chini na kuudonoa pamoja na vumbi. Huu hapa ubeti mmoja na kibwagizo ili upate picha ya ukali wa wimbo huo:

    UBETI: ONENI MAMBO WAGOSI, NA WAVYERE KADHALIKA,

    BIBI HUYU IBILISI, HAWEKWI AKAWEKEKA,

    AKILIZE MUFLISI, NI ZUKO LILILOZUKA,

    KHERI YA MOTO WA GESI, HUZIMWA UKAZIMIKA.

    KIBWAGIZO: BIBIE KUWAYAWAYA, UENDAKO NI KUBAYA,

    HUKAI UKATULIYA, KUTWA KIGUU NA NJIYA,

    KWAKO HUNA RUNGU BAYA, LIJALO WALITUMIYA,

    UTAPOKWAA MIWAYA, NANI UTAMLILIA?

    MPENI POLE MWENZETU........POOOLEEE!!

    MKOMAZENI MWENZETU........KOMAAAAA!!

    Kwa hakika ilikuwa burudani ya kipekee, na hata BeBe ambaye kwake taarabu hakuwa na mapenzi nayo sana, siku hiyo alionekana akiselebuka vilivyo. Lakini muda wote huu alipokuwa akicheza muziki na rafiki yake Zamoradi, wale vijana waliokuwa nao hawakunyanyuka hata mara moja. Kila wimbo ulipokwisha na wakarudi kuketi kwenye viti, BeBe alikuwa akiwaona wale vijana wakiwa katika hali ya kutotulia. Hata maongezi yao yalikuwa ya watu ambao kama vile walikuwa wakisubiri jambo fulani litokee. Na mara kadhaa simu ya yule mchumba wake Zamoradi iliita na akatoka nje kuitikia, na mara zote aliporudi alimnong’oneza rafiki yake bila wao BeBe na Zamoradi kujua nini kiliendelea.

    Wakati wote haya yakitokea, Pei Salem alikuwa upande wa pili wa ukumbi, lakini mahali ambapo aliwaona vyema BeBe na wenzie walipokuwa wameketi. Mchana ule baada ya kukubaliana na Zamoradi kuwa waende kwenye lile onyesho la Melody, BeBe alimpigia simu Pei, na mazungumzo yao yalikuwa:

    "Pei, leo kuna onyesho la African Melody ukumbi wa Marhubi, una habari?“

    “Ndiyo. Vipi ungependa kwenda?”

    “Tayari nina mwaliko. Tafadhali tafuta tiketi, kuna kazi ya kufanya.”

    “Hapana shaka, tiketi itapatikana, nakusikiliza.”

    “Sawa, nisikilize vizuri. Kuna vijana wawili ambao tutakuwa nao mimi na rafiki yangu. Mmoja wao ni mchumba wake huyo rafiki yangu. Huenda ukiwaona utawafahamu. Nitapenda uwe kwenye ukumbi saa zote na uhakikishe unafuatilia kwa karibu kila watakachokifanya. Umenipata?”

    “Nimekupata. Unahisi wanalao jambo? Huyo rafiki yako ni nani, kama hutajali kunieleza?”

    “Sina uhakika, lakini nahisi wale vijana si watu wazuri, na inawezekana wakahusika kwa namna fulani na mambo machafu. Unajua tena katika hii kazi yetu, machale yakikucheza unacheza nayo, au siyo?”

    “Ni kweli kabisa, mara nyingi wingu huashiria mvua.”

    “Swadakta. Na kuhusu huyo rafiki yangu, usiwe na wasiwasi, yawezekana ukimuona utamfahamu. Basi ni hayo tu, mengi yatategemea nini kitatokea leo jioni, jichunge.”

    “Asante, jichunge pia!”

    Pei alifika pale Marhubi nusu saa kabla onyesho halijaanza, akabana mahali hadi alipowaona BeBe na wenzake walipofika wakiwa katika gari moja la bei mbaya. Mara moja aliwatambua wale vijana wawili kwani alikuwa akiwaona mitaani mara kwa mara. Hata hivyo, hakufahamu walikuwa wakifanya kazi au biashara gani. Kwa upande wa msichana aliyekuwa na BeBe, Pei hakumtambua hata kidogo, na wala hakukumbuka kumuona popote kabla ya pale.

    Na kwa ujumla ingekuwa si rahisi sana kwa Pei kuweza kuwafahamu vijana wengi wa mjini Zanzibar, kwani kipindi kirefu cha maisha yake ya masomo ya sekondari na hata vyuo alisomea nje ya visiwani. Kwa hiyo vijana wengi wa rika lake hakuwafahamu, isipokuwa wale tu ambao alisoma nao shule za msingi na wale ambao wanaishi au wametokea maeneo ya kijijini kwao Makunduchi.

    BeBe na wenzake walipoingia tu, naye akaingia, ikawa kama wameongozana. Kundi la BeBe likageukia upande wa kulia mwa ukumbi, wakati Pei aligeukia upande wa kushoto akatafuta mahali pazuri mbele lakini pembeni ambapo angeweza kuwaona vizuri na pia kuweza kutoka kwa haraka kama ingebidi kufanya hivyo.

    Pei pia hakuwa mpenzi wa taarabu, lakini usiku ule hata yeye baadhi ya nyimbo na midundo ya African Melody ilimkuna sana. Alifurahi pia jinsi akina mama walivyojimwayamwaya, ingawa alichukizwa na akina dada wachache ambao mavazi yao yalikuwa ya kihuni na walicheza kihuni vilevile. Hilo halikuwa onyesho lake la kwanza la taarabu kuhudhuria, lakini hili aliona limekuwa na wasichana ambao hawakuwa na heshima, na moyoni akawaza kuwa ilikuwepo haja ya wanaohusika kuingilia kati ili kulinda maadili na utamaduni wa Kizanzibari na Kitanzania kwa ujumla wake.

    Hata hivyo, yote hayo yalipita tu katika fikra zake. Alizingatia sana kubwa lililompeleka pale usiku ule. Kwa hiyo macho yake yote yalikuwa kwa wale vijana waliokuwa na BeBe na shoga yake. Hakuwa mbali sana nao, kwa hiyo hata yeye aliona kama vile wale vijana hawakutulia, na ilikuwa dhahiri kwamba kuwapo kwao pale hakukuwa hasa kwa ajili ya ile taarabu, bali walifika tu kupoteza muda wakisubiri jambo fulani litokee. Na kwa hakika, haukupita muda mrefu hisia zake Pei zilipata majibu.

    Ilikuwa kiasi saa sita na nusu hivi usiku, wakati ambapo muziki ndio ulikuwa umepamba moto. Jukwaani alikuwepo mmoja wa waimbaji mahiri wa African Melody, kwa jina Zaabadi Hamir, na wakati huo alikuwa akiimba wimbo uliokuwa ukijulikana kama HAMU YA TAMU. Kwa wenye kuukumbuka wimbo huo watakubaliana nami kuwa uliwapagawisha wapenda taarabu kila ulipoimbwa, na ndivyo ilivyokuwa majira hayo yaliyopindukia kidogo saa sita za usiku ambapo kila aliyekuwamo mle hakuweza kuvumilia. Ama alinyanyuka kucheza, ama alibakia kitini lakini mwili ulikitikisa kiti.

    Nikukumbushe: HAMU SIO KWA MACHUNGU, BALI KWA VYENYE UTAMU,

    HAMU IKIPIGWA RUNGU, HUGEUKA KUWA SUMU,

    HAMU HATA KWA WAZUNGU, HUFANYA PENZI LIDUMU,

    HAMU KWA WENYE MAPENZI, CHUNGU HUIONA TAMU.

    Lakini kwa wale vijana wa kiume walioingia mle na BeBe na Zamoradi maneno na midundo ya wimbo huo hayakuwa na maana yoyote kwao. Wakati wimbo huo ukiwa katika kibwagizo cha beti ya pili na ukumbi ukiwa umejaa makelele ya raha na furaha, simu ya mkononi ya Burshid ilimkuna kwenye mfuko wa shati ikiashiria kuna mtu anamwita. Akatoka nje haraka akimwacha mwenzake ameketi. Lakini hakuchukuwa hata dakika tano akarudi mbio na kumwashiria mwenzake amfuate, wakatoka wote nje haraka. Wakati wanafanya hivyo hawakujua kuwa kuna mtu mwingine anafuatilia nyendo zao, na huyo alikuwa ni Pei, ambaye naye aliwafuata hadi kule nje.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Aliwaona wakiingia kwenye lile gari lao na wakaondoka kwa kasi kuelekea kutoka kwenye lango kuu la kuingilia Marhubi. Pei hakusita, alikimbilia mahali zinapopaki teksii, akaingia kwenye mojawapo iliyokuwa na nafasi nzuri ya kutoka na akamwambia dereva wa gari hiyo aifuate ile gari ya wale vijana. Kwa bahati nzuri, muda ule magari kadhaa nayo yalikuwa yakitoka, wenyewe bila shaka wakiwa wamechoka na waliamua kuelekea majumbani kupumzika. Kwa hiyo gari la wale vijana lilipoingia barabara kuu iendayo mjini, teksii aliyoikodisha Pei ikawa iko nyuma ya magari mengine mawili kutoka lile la wale vijana.

    “Hakikisha lile gari la mbele kabisa halitupotei, ikibidi yapite haya magari mawili yaliyotutangulia. Tusiwapoteze wale, ni muhimu,” Pei alimwagiza yule dereva.

    “Usiwe na wasiwasi, wale tunao. Vipi, wewe ni askari?” yule dereva alimuuliza Pei.

    “Hujakosea, lakini yatakayotokea yapotelee gizani usijeukaingia kwenye mambo yatakayokuletea matatizo. Nichukulie kama abiria wa kawaida. Ongeza kasi, wamekata kona wale.”

    Wakati Pei anawafuatilia wale vijana, kule ukumbini Marhubi, BeBe alipatwa na mshituko waliporudi kuketi na kukuta wale vijana hawapo. Alitoka nje na Zamoradi akamfuata, lakini hawakuwaona wale vijana wala gari lao. Bebe aliangaza huku na kule kuwa labda angemuona Pei, lakini hakumuona.

    “Unaona Zamo, huyu mchumba wako ni mtu wa ajabu sana. Wataondokaje na kutuacha kwenye mataa. Ni heshima kweli hii?”

    “Samahani sana Beli, kwa kweli hata mimi kitendo hiki kimenifadhaisha sana. Hivi kweli Burshid anaweza kuniai.......,” Zamoradi akaanza kulia.

    “Aa-aa, usilie, hatujui kimetokea nini, labda kuna dharura imewapata,” BeBe alijaribu kumliwaza rafiki yake.

    “Hata kama kuna dhararu, ndio wangeshindwa kutuaga kweli, hii ni dharau tu, tena wananiabisha mbele yako wewe mgeni wangu. Kuanzia leo mimi na Bur......”

    Kabla Zamoradi hajamaliza alichokuwa anataka kusema, simu ya mkononi ya BeBe ililia, akaipokea haraka haraka, lakini akasogea kidogo mbali na Zamoradi.

    “BeBe, tunaweza kuzungumza?”

    “Ndiyo Pei, endelea.”

    “Jamaa waliondoka hapo mkuku, nikawafuatilia. Hivi sasa wapo hapa Hoteli ya Ufukoni. Wamepandisha juu na wameingia chumba namba 406. Nimeulizia nani amepanga chumba hicho, nimeambiwa yupo jamaa mmoja kutoka Visiwa vya Ngazija, jina lake ni Seidati Mohan. Kulingana na vijana wa hapa mapokezi, mgeni wao huyo amefika usiku huu wa leo kwa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania.”

    “Wanasema ameandikisha kitabuni atakaa siku ngapi.”

    “Nimeliuliza hilo, wanasema ataondoka kesho kutwa.”

    “Vyema, endelea kuwafuatilia. Chukua tahadhari sana, hawa jamaa wanaweza kuwa ni hatari kama tunachohisi ndicho.”

    “Sawa, nitakupigia baadaye.”

    Wakati BeBe anaongea na Pei, simu ya Zamoradi nayo ililia, naye akaipokea na akawa anaongea na huyo aliyempigia. Kutokana na mazungumzo yao, BeBe alijua ni Burshid, maana Zamoradi alikuwa analalamika na kuongea kwa hasira wakati huohuo. Hata BeBe alipomaliza kuongea na Pei, bado Zamoradi alikuwa kwenye malumbano na mchumba wake.

    “Sikiliza Bur, huwezi kuniambia kuwa ulishindwa kuniaga. Unadhani huyu shoga yangu atanielewaje. Na watu waliotuona pamoja nanyi pale wataelewaje. Sijaridhishwa na sababu unayonipa ya kuniacha kwenye mataa. Kwaheri.” Akakata simu.

    “Aa-aa, Zamo, hilo ulilolifanya sio sahihi, usingemkatia simu. Kumbuka, huyo ni mchumba wako,” BeBe alimuasa mwenzake.

    “Hajawa mchumba wangu, hajatoa posa kwa wazazi wangu, bado ni urafiki tu uliopo kati yetu. Siwezi kuvumilia madharau ya namna hii. Na hii si mara ya kwanza, alishanifanyia hivi mara mbili, hii ni ya tatu,” Zamoradi alitoboa siri.

    “Hee, kumbe ndiyo tabia yake?”

    “Ndiyo, nimechoka, Beli, kama ni hivyo vitu vyake alivyoninunulia bora avichukue. Hata hilo suala la kuposwa sina hamu tena,” alisema kwa uchungu Zamoradi.

    “Usichukue uamuzi huo, subiri uone kama baada ya mkasa huu wa leo atajirekebisha au la. Kama ni mstaarabu, basi usiku huu itabidi akutafute ili akuombe radhi. Kama hakufanya hivyo basi kweli bwana huyu atakuwa fedhuli.”

    “Sawa, ngoja tuone kama kweli ni mstaarabu. Haya, na wewe hiyo simu kakupigia nani, au alikuwa ni Osmun?”

    “Waala, anipigie kwani mimi kwake yeye ni nani. Ilikuwa simu kutoka kwa kakaangu aliyeko Tanga. Kulikuwa na maagizo nimemwachia, ndio alikuwa ananifahamisha hatua aliyofikia.”

    “Hee, mbona kakupigia usiku wote huu?”

    ”Aah, siunajua tena, mitandao inapunguza gharama usiku.”

    “Sawa, basi tuchukue taksii turudi zetu nyumbani.”

    Wakati haya yakiendelea, kule Hoteli ya Ufukoni Pei alikumbwa na kibarua kipevu. Kumbe pale hotelini inaelekea wale vijana walikuwa na jamaa wahudumu ambao ile uliza uliza ya Pei haikuwafurahisha. Basi mmoja wao akafanya mawasiliano na wale vijana kule walikokuwa chumba namba 406.

    Alitumia simu, na mazungumzo yakawa:

    “Bw. Burshid, hapa kuna jamaa anawaulizia ulizia pamoja na huyo mgeni wenu…Ndiyo, alifika muda mfupi tu nyie mlipofika, nyie mkitumia kipandio yeye kapanda mbio kwa ngazi kuja huko juu…..Ndiyo, bado yupo ameketi hapa, lakini alikuwa na mazungumzo ya simu na mtu fulani…..hapana, sikuweza kusikia alichokuwa akiongea…sawa.”

    Machale yalimcheza Pei. Alimuona yule kijana aliyekuwa akiongea na Burshid kwa simu alipoingia na alipotoka kule ofisini nyuma ya kaunta ya mapokezi. Sura yake yule kijana ilimpa Pei ishara ya hatari na akamwendea.

    “Umefurahi sasa baada ya kuwafahamisha kuwa nilikuwa nikiwaulizia siyo?”

    Yule mhudumu alibabaika akashindwa kujibu, bali alimkodolea macho Pei.

    “Kwa taarifa yako, nipo kwenye utumishi wa umma. Umeisaliti dola, na utalipia kosa hilo. Punde hivi utaona matokeo ya usaliti wako, kwaheri.”

    Pei aliondoka haraka akatoka nje ambako ile taksii ilikuwa ikimngojea. Aliingia na kumwambia dereva waondoke haraka. Dereva aliondoa gari kwa kasi kuelekea mjini, walipofika karibu na ukumbi wa burudani wa hoteli ambako kulikuwa na kivuli kinene cha miti ya maua, ikawa:

    “Punguza mwendo, nitatoka, wewe endelea na safari yako,” Pei akampa pesa yule dereva taksi, akafungua mlango, akatoka na dereva akaondoka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati wanaondoka pale hotelini, tayari wale vijana nao walikuwa wameshashuka na walipoambiwa kuwa Pei alishaondoka punde tu, wakakimbilia kwenye gari lao wakawafuata kwa kasi. Hata hivyo, hawakumuona Pei alipotoka kutoka kwenye ile gari, wakaendelea kuifuata ile teksi ambayo taa zake za nyuma zilikuwa zikionekana kwa mbali.

    Huku nyuma Pei alipoiona ile gari inapita kwa kasi kuifuatia teksi aliyokuwa ameiacha punde, akatabasamu kwa kujuwa kuwa wamemkosa. Hata hivyo, alipatwa na wasiwasi juu ya hatima ya yule dereva wa teksi.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog