Simulizi : Niliua Kwa Kukusudia
Sehemu Ya Tatu (3)
Shangazi alitulia kidogo kisha kukohoa. Akanitazama usoni kwa macho ya mkazo kidogo. Wasiwasi ukazidi kuniingia moyoni. Hata hivyo, nilijikaza na kuwa tayari kupokea jambo lolote nitakaloambiwa na shangazi kwa wakati huo."Sisi tunaoishi eneo hili," Shangazi akaendelea nami nikajiweka sawa mahali nilipokuwa nimejilaza. Nikakaa kitako na kujiegemeza ukutani na kuanza kumsikiliza kwa umakini mkubwa shangazi."Tunaishi kwa kulipia vibanda hivi, sasa kwa kuwa tuko wawili hapa mimi na wewe, na madamu sasa umeshaanza kujipatia riziki, ni vyema sasa kama tutaanza kushirikiana katika ulipaji wa kodi ya pango hili," Shangazi alihitimisha mazungumzo yake na kuniangalia usoni huku akisikilizia kama nilikuwa na chochote cha kuzungumza juu ya hilo."Sawa shangazi, nimekusikia," nilimjibu kwa sauti ya upole na yenye utulivu wa hali ya juu mno.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nashukuru kama utakuwa umenielewa," alijibu shangazi."Nimekuelewa vizuri sana, vipi habari za hapa nyumbani jamani, maana hata hatujasalimiana kwa undani zaidi ya wewe kuleta mada ya kodi ya pango," nilijikuta nikitamka maneno hayo kwa ujasiri mkubwa ambao sikujua ulitokana na nini."Kama nilivyosema hapo awali, hapa nyumbani ni salama kabisa kama ulivyopaacha."
"Kama ni hivyo, ni jambo jema la kumshukukuru Mungu wa Mbinguni."
"Vipi wewe na safari yako, ulifika salama?"
"Nilifika salama kabisa.""Inana anaendeleaje kwa sasa huko kijijini?"
"Anaendelea vizuri tu."
"Inaonekana kwa sasa ni binti mkubwa sana, maana sijamuona kwa muda mrefu sasa."
"Aah, mbona ni mama mkubwa sasa," nilimjibu Shangazi na wote tukaangua kicheko kilichoashiria furaha kubwa baina yetu.Baada ya mazungumzo ya kuchangamshana, shangazi akatoka nje na kuniacha peke yangu kwenye kigodoro changu. Nikaendelea kukaa huku maswali mengi yakipita ubongoni mwangu kwa kasi.Nikawa najiuliza mambo mengi sana kuhusu kauli ya shangazi. Lakini nikajipa moyo kuwa nitaweza kugharamia kodi ya pango kutokana na kipato changu cha kibarua cha hotelini. Nikaendelea kuwaza ndipo katika hali ya kuwaza na kuwazua, nikajikuta nikipata wazo ambalo hakika sikujua lilitoka wapi kwa wakati huo.Nikawaza kuwa hata kama nitasaidizana na shangazi katika kulipia kodi ya pango la kibanda hicho, sitachukua muda mrefu kabla sijapanga chumba changu mwenyewe.Wazo hilo likaendelea kuchukua nafasi kubwa sana kichwani mwangu. Nikakubaliana na wazo hilo kuwa nikusanye pesa kwa juhudi zote, ili niweze kupata kiasi cha kukodisha chumba na kuyaanza maisha yangu pamoja na mdogo wangu Inana.Baadaye, nilitoka nje ambapo tayari ilishafika jioni kabisa. Nikaa kwa nje huku nikiendelea kuwaza.
Usiku ulipotimu, nilikuwa wa kwanza kuingia ndani na kujilaza tena kwenye kigodoro. Shangazi alikuja kuniamsha baada ya kuivisha na kuniomba tujumuike sote kwenye chakula cha pamoja.Sikuwa na hiyana, nikajikokota kwa uvivu hadi mahali alipokuwa ametenga chakula. Tukaanza kula huku tukisimulizana mambo mbalimbali na kuambatanisha mazungumzo hayo kwa vicheko vya furaha.Tulipomaliza kula, niliondoa vyombo vyote na kuvikusanyia kwenye chombo kimoja kikubwa na kuanza kuviosha. Baada ya kumaliza zoezi hilo, nikavipanga mahali pake nami nikaelekea kulala. Nikaanza kuusakama usingizi japo kwa taabu sana. Ukawa unakuja kwa mang'amung'amu tu. Mara nyingi nilikuwa nikishituka na kuketi kitako kutokana na mawazo.Hadi kunapambazuka, sikuwa nimesinzia hata kidogo. Nikaamka na kumsabahi shangazi ambaye hadi wakati huo alikuwa bado akiusindikiza usngizi wa mwisho wenye kibaridi cha asubuhi.Nikajiandaa ili niende kazini kwani siku za kupumzika zilikuwa zimekwisha. Baada ya kumaliza kuoga, nilivaa na kutoka kuelekea kwenye kituo cha mabasi ya kuelekea Mwananyamala. Nilipowasili kituoni, nikiwa naendelea kusubiri basi ghafla nilikumbuka kitu ambacho kiliniondolea kabisa raha ya siku hiyo.
NILIKUMBUKA yale mazungumzo ya shangazi. Nilikosa raha kabisa. Lakini nikajipa moyo na kuamua kupambana na kila hali ya ugumu wa maisha itakayojitokeza mbele yangu. Kwa mbali nilianza kukichukia sana kifo, kwani bila hicho wazazi wangu wangekuwa hai. Mimi na mdogo wangu Inana tungekuwa tunaendelea na masomo.‘Lakini ngoja nijikaze, kwani sina budi kupambana na maisha, imeshakuwa hivyo sasa sina jinsi lakini mwisho wa siku ni lazima nifanikiwe, siko tayari kufa nikiwa maskini', nilijikuta nikiwaza maneno hayo mazito na makali.Niliendelea kungojea usafiri, muda mfupi lilikuja basi la UDA lililokuwa likielekea Mwananyamala. Nikajipakia na kuketi kiti cha nyuma kabisa nikiwa peke yangu. Kama kawaida sikupata muda wa kufurahia jambo lolote, nikaendelea na mawazo yangu.Basi lilifika Mwananyamala-Kwakopa majira ya saa mbili na dakika 45, nikashuka na kumpatia kondakta pesa yake. Nilijikokota hadi hotelini kwenye kibarua changu. Nilikuta baadhi ya wafanyakazi wameshaanza kuwasili. Tulisabahiana kwa furaha kutokana na kukaa muda mrefu bila kuonana. Kila mtu alikuwa mwenye furaha.Nikaenda kujiandaa ili nivalie nguo za kazi. Nikiwa nakaribia kabisa na mlango wa chumba cha kubadilishia nguo, nilisikia sauti ya mtu ikiniita kwa nyuma. Nikageuka na kuangalia kwa haraka. Alikuwa ni mfanyakazi mwenzangu, Sauda."Ah, Sauda habari za asubuhi?"
"Salama Tunu, hujambo?"
"Salama kabisa, sijui wewe?"
"Salama tu," nilimjibu huku nikitaka kuendelea na safari ya kuingia ndani ili nibadilishe nguo.
Nilipopiga hatua ya kwanza, Sauda aliniita tena na kunifanya nirudi na kumsogelea kwa karibu kwani nilihisi alikuwa na jambo alitaka kunieleza."Samahani Tunu."
"Bila samahani Sauda, nakusikiliza."
"Bosi anakuita."
"Bosi yupi, meneja au mkurugenzi?"
"Mkurugenzi."
"Yuko ofisini?"
"Ndiyo," Sauda alinijibu huku akigeuka na kuniacha nikitafakari nilichoitiwa asubuhi ile na yule Mwarabu.Baada ya kuwaza kwa muda, nikajipa moyo na kuamua kwenda ofisini kumsikiliza yule Mwarabu ambaye kwa wakati huo nilikuwa nimeshamjua kwa jina kutokana na kusikia baadhi ya wafanyakazi akiwemo meneja. Alikuwa akiitwa Elihakimu.Nikaingia ofisini kwa heshima na woga kwa mbali. Kule ofisini, nilikuta akivuta sigara huku akiwa amesimama na kushika simu mkononi. Kwenye kiti cha wageni kulikuwa na kijana mmoja ambaye naye alikuwa Mwarabu pia, kwa mbali walifanana japo si kwa sana.
"Ooh, karibu sana Tunu, habari za siku?"
"Salama, shikamoo.""Marahaba, hujambo kabisa Tunu?" alinisabahi kwa uchangamfu wa hali ya juu sana Elihakimu. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kumsalimia, nikamgeukia yule mgeni aliyekuwa kimya kabisa naye akiendelea kuvuta sigara.
"Shikamoo."
"Marahaba binti, hujambo?"
"Salama kabisa.""Kaa hapo Tunu," akaniambia Elihakimu na kunionesha moja ya viti vilivyokuwemo ofisini humo.
Akaendelea kuvuta sigara na kutoa moshi mwingi sana kupitia tundu za pua na mdomoni. Akavuta hadi kilipobaki kipisi alikiminya kwenye kile kifaa kilichokuwa juu ya meza cha kuzimia sigara.
Akaketi na kutuangalia kwa zamu mimi na yule mgeni mwigine Mwarabu.
"Tunu," alininiita na kunikazia macho."Bee."
"Huyu ni mdogo wangu."
"Sawa."
"Anaitwa Ashraf."
"Nimefurahi kumuona," nilimjibu ambapo maneno yangu yalimfanya yule Mwarabu mgeni aniangalie kwa furaha ya wazi.Bosi aliendelea na utambulisho ambapo alieleza hadi jinsi nilivyofahamiana naye.
Mazungumzo yakaendelea. Wakati bosi anaendelea na kuratibu kikao hicho, mlango ulifunguliwa. Akatokeza yule mhudumu wa mapokezi akiwa ameshika sinia lililokuwa na vikombe na birika la kahawa na baadhi ya vitafunwa. Akavitenga mezani kisha kuanza kumnawisha yule mgeni, baadaye bosi. Alikupokuja kwa upande wangu. Nilikataa kwa kisingizio kuwa nilikuwa nimeshiba.Bosi na yule mgeni walinisisitizia kwa hamasa kubwa. Nikajikuta nimekubali na kunawa. Yule mhudumu akatumiminia kahawa na kutuwekea sawa vitafunwa. Akatukaribisha. Alipoondoka tu, bosi Elihakimu alinigeukia.
"Tunu."
"Abee, bosi."
"Huyu mdogo wangu ana shida ambayo naamini utaweza kumsaidia, najua huwezi kuniangusha.
SIKUWA na haraka ya kuitikia. Nikabaki kimya huku nikiwatazama kwa zamu mmoja baada ya mwingine. Mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kwa kuwa sikujua kabisa jambo ambalo walitaka niwasaidie.
"Unasikia Tunu," Bosi alinishitua kutoka kwenye lindi la mawazo ambalo lilikuwa limenivamia ghafla kwa wakati ule."Nakusikia bosi."
"Shida yenyewe ni ndogo sana," bosi akazidi kusisitiza na kunifanya nimuangalie usoni hasa baada ya kusema kuwa shida yenyewe ilikuwa ni ndogo sana.
Alipofika hapo akatulia kidogo, akakohoa kisha kuendelea;
"Shida yenyewe ni kwamba anahitaji mtumishi wa ndani," alisema na kumtazama usoni yule mgeni ambaye alitingisha kichwa kuashiria kukubaliana na alichokisema bosi."Sasa, nakumbuka uliwahi kuniambia kuwa una mdogo wako kule kijijini, naona anaweza kufaa."
"Naomba utusaidie kumshawishi aje kufanya kazi kwa huyu mdogo wangu, naamini ni msichana aliyetulia kama wewe hivyo hawezi kuleta usumbufu," alisema Bosi Elhakimu na kunifanya nitabasamu kwa furaha.Hakika alikuwa amegusa kwenye furaha yangu. Kwa siku nyingi sana nilikuwa nikiwaza ni kwa jinsi gani nitaweza kumtoa mdogo wangu huko kijijini ili aje kuishi nami Dar es Salaam.
"Umenisikia Tunu?" bosi aliuliza baada ya kuona niko kimya kwa muda.
"Nimekusikia bosi, nitafanya hivyo," nilimjibu huku nikionesha furaha ya hali ya juu kabisa."Nimefurahi kusikia hivyo, basi inapaswa uondoke sasa hivi kuelekea Chalinze ili kesho uje naye hapa maana huyu bwana anahitaji mtumishi haraka sana," alisema bosi na kumuangalia tena Ashraf ambaye alitingisha kichwa kama ishara ya kuunga mkono alichokizungumza bosi Elhakimu.
"Sawa, niko tayari."Baada ya kauli yangu, bosi alimgeukia Ashraf.
"Umesikia bwana, yuko tayari kutusaidia."
"Nashukuru sana Tunu kwa hilo, sasa chukua hii kama nauli ya kwenda na kurudi pamoja na huyo mdogo wako," alisema Ashraf huku akinipa noti nyekundu ambazo kwa wakati huo sikujua ni kiasi gani.
"Ahsante.""Sasa utapitia hukuhuku au utaenda hadi Buguruni ukaage nyumbani?"
"Itabidi niende Buguruni nikaage, lakini nitaondoka leo hii," nilimjibu kwa haraka.
Tuliagana, nikatoka nje ambako nilipitiliza hadi kwenye kituo cha mabasi nikarudi Buguruni. Nilipofika nyumbani nilimkuta shangazi akiendelea na shughuli zake. Akashituka na kuacha kila alichokuwa akifanya."Kulikoni tena, mbona umerudi asubuhi yote hii?" aliniuliza kwa hamaki kubwa huku akinitazama usoni.
"Nina safari ya kwenda Chalinze tena."
"Chalinze?"
"Ndiyo."
"Kuna kitu ulisahau?"
"Hapana, namfuata Inana.""Inana! Wa nini?"
"Nimempatia kazi."
"Wapi na kazi gani?" shangazi aliuliza mfululizo.
Ilibidi nikae chini na shangazi ambapo nilianza kumuelewesha kwa kina zaidi. Nashukuru Mungu shangazi alinielewa.
"Kwa hiyo tutakuwa tukiishi naye hapa, siyo?"
"Hapana.""Sasa atakuwa akiishi wapi?"
"Hukohuko nyumbani kwa bosi wake?"
"Wewe unawaamini hao watu?"
"Hawana shida shangazi."
"Sawa, lakini ni vizuri kuwa makini sana maana kwa sasa ulimwengu umeharibika."
"Sawa shangazi, mimi nawaamini.""Mimi sina neno, kwa hiyo unasafiri kesho?"
"Hapana, inabidi niende sasa hivi, kesho nitakuwa hapa."
"Sawa."
Niliingia ndani na kuanza kujiandaa. Nikatoka na kushika njia.
"Haya shangazi, naondoka."
"Safari njema mwanangu."
"Ahsante."Nikaanza safari ya kurudi Chalinze tena. Nikatembea hadi kituoni ambapo nilipanda mabasi ya kwenda Ubungo.
Nilikuta gari la Chalinze likiwa na abiria wachache. Nikakata tiketi na kuingia ndani ambapo nilichagua siti. Nikatulia na kuanza kuyafikiria maisha. Furaha niliyokuwa nayo haikuwa na maelezo, kwani kitendo cha Inana kupata kazi kilinifurahisha mno.Muda mfupi baadaye, safari ikaanza, tuliwasili Chalinze majira ya saa tisa na nusu. Nikakodi baiskeli hadi nyumbani na kumkuta Inana akipepeta mchele.
Kabla sijamfikia, nilishangaa baada ya kumuona akijiinamia na kuanza kulia.
Hali ile ilinishtua sana. Nikatembea kwa haraka kuelekea mahali alipokuwa amekaa. Nikamgusa begani na kumfanya ashtuke na kugeuka kuniangalia kwa hali ya uoga."Hee, dada Tunu umerudi tena?"
"Ndiyo mdogo wangu, mbona unalia kuna nini?"
"Nimekumbuka ndoto mbaya niliyoiota."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ndoto gani iliyokufanya hadi ulie?""Niliota tuko na wazazi, maisha ni mazuri na tunaendelea na masomo, sasa wakati nimekaa hapa, ghafla nikakumbuka ile ndoto ndiyo maana umenikuta nalia."
Kauli hiyo ilinifanya ninyongo'nyee sana. Moyoni nilijisikia uchungu na bila kutarajia nikajikuta nikilengwalengwa na machozi.Sote tukawa katika hali ya maumivu. Kila mtu alilia huku akimbembeleza mwenzake.
"Basi Inana, naomba tuyaache hayo," nilimwambia mdogo wangu huku nikijifuta machozi kwa mkono wa kushoto.
"Sawa dada, lakini inauma sana."
"Achana na habari hizo, sasa tuangalie maisha upya.""Nimekuelewa dada."
Sikuingia ndani kwa wakati huo, Inana alipeleka kifurushi changu ndani. Akarudi na kuungana nami huku akiendelea kupepeta mchele.
"Ehe habari za huko dada?"
"Nzuri za tangu jana?""Nzuri tu, mbona umerudi tena leo, kulikoni?"
"Nina habari njema sana Inana."
"Habari njema?"
"Ndiyo, mbona unashtuka hivyo?"
"Si wewe jamani?""Mimi nimefanyaje?"
"Si unanishtua kwa kusema una habari njema!"
"Usiogope, kuna nafasi ya kazi za ndani imepatikana huko hivyo nimekuja kukuchukua."
"Unasemaje?"
"Kama ulivyosikia Inana, kuna mdogo wake na bosi wangu yule Mwarabu, anahitaji msichana wa kazi za ndani."Inana alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu. Furaha aliyokuwa nayo sina maelezo yake. Alifurahi mno. Nikamueleza kila kitu juu ya mpango huo wa kazi.
"Sasa nitakuwa nikiishi na wewe kwa shangazi?"
"Hapana Inana, utakuwa unaishi mahali unapofanyia kazi."Tulizungumza mambo mengi sana. Inana akaandaa chakula cha usiku. Kilipoiva, tuliingia ndani na kuanza kula. Tulipomaliza nilimwambia Inana ajiandae kwa ajili ya safari kwani nilipanga tuamke mapema ili tuwahi kufika kwa ajili ya maandalizi ya kuonana na bosi.Akafanya kama nilivyomuagiza, akaandaa kila kitu na kukiweka sawa tayari kwa safari. Alipomaliza aliniita na kuniomba tuombe dua kwa ajili ya kulala. Baada ya kuomba dua tulilala huku kila mtu akiwa kimya kwa kuwaza aliyoyaona yanafaa.Kulipopambazuka, Inana alikuwa wa kwanza kudamka. Akaniamsha ambapo niliamka na kumkuta akiwa amekaa kitandani.
"Shikamoo dada."
"Marahaba Inana umeamka salama?"
"Salama kabisa dada, sijui wewe?""Salama kabisa, basi jiandae tuanze safari."
"Kila kitu kipo sawa dada, kuna kitu najiuliza."
"Kipi tena?"
"Hivi vyombo tunaviacha humuhumu?"Tulijadili kwa muda kidogo. Baada ya majadiliano tulifikia uamuzi wa kumuachia vyombo mama mmoja aliyekuwa akiishi jirani yetu.
Tulimuita na kumpa maelekezo yote. Bila hiyana akakubali kuvichukua. Alipomaliza kuvisomba vyombo vyote, tuliingia bafuni na kuoga. Tulipomaliza tukaondoka hadi barabarani ambapo tulikodisha baiskeli hadi stendi ya mabasi.Muda mfupi, lilitokea basi la Kilombero liitwalo Hood ambapo tulipanda na safari ya kuelekea Dar ikaanza.
Tulitumia saa nzima kabla ya kufika stendi ya mabasi ya mikoani ya Ubungo. Tukashuka na mabegi yetu na kuelekea kwenye kituo cha mabasi ya Buguruni. Tukajipakia na kuwasili saa tano na dakika ishirini asubuhi.Wakati tunafika nyumbani, shangazi hakuwepo na nyumba ilikuwa imefungwa hali iliyotulazimu kukaa nje na kumngojea shangazi arudi.Tukaendelea kusubiri hadi alipowasili.
"Jamani kumbe kuna wageni?"
"Kama unavyoona mwenyewe, nimekuletea mgeni."
"Jamani Inana umekuwa hivi!" Shangazi alisema huku akionesha mshangao wa wazi kwa Inana.Baada ya kusalimiana, tukaingiza mizigo ndani. Shangazi aliandaa chakula na kutukaribisha. Wakati wa kula nikamweleza shangazi kuwa napanga kumpeleka Inana kwa yule bosi anayemhitaji.
"Hiyo haina shida, ilimradi tu afajitahidi kuwa na heshima pamoja na bidii katika kazi," shangazi alianza kutoa nasaha zake kwa Inana."Kwa hayo sina shida naye. Kwa hiyo naamini hataniangusha," nikajibu na kumuangalia Inana.
Wakati tunaendelea na mazungumzo, shangazi alisema kitu ambacho kilitufanya mimi na Inana tushtuke.
Ndiyo. Mimi na Inana tulishituka sana hasa kutokana na ukweli kwamba hatukutegemea kusikia maneno kama hayo kutoka kwa mtu kama shangazi.
Alisema: "Maisha hayawezi kutafutwa kwa kuajiriwa na watu hasa weupe." Ni kauli ambayo hakika ilinikata maini. Nikamwangalia Inana kwa macho ya huruma, naye alionesha kuumizwa na kauli hiyo.
"Hata hivyo, siwakatishi tamaa, endeleeni kupambana, huenda mkafikia malengo na ndoto zenu," aliendelea kutuambia shangazi au mama Shufaa kama wengi walivyozoea kumuita licha ya mtoto wake huyo kufariki dunia miaka mingi iliyopita.
Tuliendelea kula japo si kwa hamu ya chakula bali kwa kushiba na kuondoa njaa.
Muda mfupi, niliamua kujitenga pembeni na kisha kunawa.
"Mbona mapema sana?" shangazi aliniuliza kwa sauti ya chini.
"Nimetosheka shangazi," nikamjibu.
Ukimya ukazidi kutawala. Si shangazi, Inana wala mimi aliyefunua mdomo kwa wakati huo. Baadaye Inana naye alishiba na kuungana nami mahali nilipokuwa nimejiegesha.
Shangazi alipomaliza kula, akaingia ndani na kulala bila hata ya kutusemesha tena, hali ambayo ilizidi kutuchanganya mimi na Inana. Lakini hata hivyo, hatukutumia muda mwingi sana kuwaza juu ya kitendo kile.
Mimi na Inana tukalala pamoja na kujifunika shuka moja huku tukitandika jingine. Tukaukaribisha usingizi kwa ukimya wa ajabu. Katika ndoto ya usiku ule, niliota kuwa mimi na mdogo wangu tunaishi maisha ambayo ni ya kifahari sana. Katika ndoto ile, tulikuwa tumepata karibu kila kitu tulichokikosa utotoni.
Kulipopambazuka, nilikuwa wa kwanza kuamka na kumkuta Inana bado akiwa anaufaidi usingizi wa asubuhi uliokuwa ukisindikizwa na sauti za ndege wa asubuhi. Hakika alionekana kukolea kwa usingizi.
Ilipotimu saa moja kamili, nilimuamsha ajiandae ili nimpeleke kazini akakutane na mdogo wake na bosi ili waelewane jinsi gani ataanza kazi.
"Inana," niliendelea kumuita lakini alionekana kuzidiwa kwa usingizi. Lakini kutokana na kumuita kwa nguvu, aliamka na kukaa kitako kwenye kigodoro huku akijifuta usoni kama ishara ya kuyaweka sawa macho kwa ajili ya kukabiliana na hali ya mwanzo wa siku mpya.
"Shikamoo dada," alinisabahi huku akijiandaa kuvaa.
"Marhaba, umeamka salama?"
"Salama kabisa sijui wewe?"
"Salama, basi jiandae nikupeleke ukaonane na huyo bosi anayehitaji mtumishi, sawa?"
"Sawa dada."
Kwa muda huo shangazi alikuwa akiendelea na shughuli yake ya kukaanga chapati kwa ajili ya umama ntilie. Nikaenda kumsalimia kisha nikaingia bafuni.
Baada ya kuoga, Inana naye akaenda kuoga na alipomaliza tulivaa na kumuaga shangazi kwa ajili ya kwenda kazini.
"Haya nawatakia mafanikio mema," alijibu shangazi huku akituangalia mmoja baada ya mwingine.
"Haya, ahsante sana, nawe kazi njema," Inana alijibu kwa uchangamfu, japo si kwa hali ya kujiamini kwa asilimia zote kutokana na maneno ambayo shangazi alikuwa ameyatoa jana yake.
Tukaongozana hadi kwenye kituo cha mabasi ya Mwananyamala ambapo tulipanda na kukaa siti za karibu sehemu ya nyuma kabisa.
Safari ya kuelekea Mwananyamala ikaanza huku Inana akionekana kushangaa kila mahali tulipopita kutokana na ugeni wake ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Kutokana na foleni kubwa iliyokuwepo kwa siku hiyo, tulitumia muda mwingi sana njiani.
Tulitumia mwanya huo wa urefu wa foleni kujadili mambo mengi ikiwemo mustakabali wa maisha yetu. Hatimaye foleni ilipungua na magari yakaanza kwenda japo kwa mwendo wa taratibu sana.
Mara itembee mara isimame, hakika siku hiyo kulikuwa na foleni ndefu sana. Lakini sikushangazwa sana na jambo hilo, kwani ni kawaida kwa Jiji la Dar es Salaam kuwa na foleni ndefu ya magari hasa kwa siku kama hiyo ambayo ni Jumatatu.
"Kwani dada, kwa kuwa mimi nitakuwa naishi mahali nitakapoanza kufanya kazi, wewe utaendelea kuishi na shangazi hadi lini?" Inana aliniuliza huku akiwa amenikazia macho.
"Kwa nini umeniuliza hivyo Inana?" nilimuuliza kwa shauku kubwa.
"Jibu swali dada Tunu, kuna kitu nimekiona kwa shangazi, ndiyo maana nimekuuliza," alisema Inana kwa msisitizo.
ikuwa na haraka ya kuzungumza kitu. Nikabaki nimemtazama Inana kwa umakini wa hali ya juu sana. Alionekana kumaanisha alichokisema. Hapo nikabaki kimya na kuendelea kumtazama.
Mbona huongei kitu na kubaki unanitazama tu dada Tunu jamani? Inana alisema na kunishika begani huku akinitazama machoni kwa ukaribu zaidi.
Nakusikiliza Inana, bado sijajua unamaanisha nini kwa maneno yako.
Hujaelewa nini Tunu?CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Umesema kuna kitu umekiona kwa shangazi?
Ee dada, huamini?
Ni kipi hicho Inana?
Shangazi hataki uendelee kuishi hapo kwake, sasa anatafuta njia ya kukuondoa lakini hajaipata, alisema Inana huku akiniangalia kwa umakini bila kupepesa macho.
Mh! Niliishia kuguna.
Ndiyo hivyo dada, Inana akaendelea kusisitiza zaidi.
Wakati huo foleni ikawa inatembea na muda mfupi baadaye tukawa tumefika kwenye kituo cha daladala cha Peace Mwananyamala. Tukashuka na kuanza kutembea kuelekea mahali ilipokuwa hoteli niliyokuwa nikifanyia kazi.
Tuliwasili na kuwakuta baadhi ya wafanyakazi wenzangu wakiwa wanajiandaa kwa ajili ya kuanza kazi. Tukasabahiana na baadhi yao huku mimi na Inana tukiingia upande wa mapokezi ambapo tulimkuta msichana wa mahali pale akiendelea na shughuli zake za kila siku.
Habari za saa hizi dada? nilimsabahi kwa uso wa uchangamfu wa hali ya juu.
Salama kabisa Tunu, habari za siku nyingi jamani?
Nzuri tu, sijui wewe?
Salama, karibu.
Ahsante sana.
Shikamoo, Inana naye akamsalimia.
Marahaba jamani, mzima?
Salama tu, pole kwa kazi.
Ahsante sana, Tunu huyu ni mdogo wako? Maana mnafanana sana! aliniuliza yule dada wa mapokezi baada ya kujuliana hali na Inana.
Eee, ndiye anayenifuata.
Sawa, mnafanana kama mapacha.
Baada ya kuzungumza na dada huyo, nilimuuliza kama tayari bosi Elhakimu alikwisha wasili ofisini. Alinitaarifu alikuwepo.
Mimi na Inana tuliongozana hadi ofisini na kumkuta bosi akiwa anaandika kitu kwenye tarakishi yake ya mkononi (laptop).
Oooh, karibuni sana Tunu, alitukaribisha yule bosi huku akionesha uchangamfu ambao hapo awali sikuwahi kumuona nao.
Ahsante sana, shikamoo bosi.
Marahaba Tunu, habari za huko nyumbani?
Salama.
Shikamoo, Inana alimsabahi.
Baaada ya kusalimiana na kujuliana hali, nikamtambulisha Inana kwa bosi huku nikichombeza kwa utani jinsi alivyonigonga na gari lake kule Chalinze.
Tukazungumza kwa uchache. Baada ya muda yule bosi akachukua simu yake ya mkononi na kubonyeza namba fulani kisha akaipeleka simu sikioni.
Muda mfupi kidogo akaanza kuzungumza na mtu wa upande wa pili ambaye mimi na Inana hatukumjua.
Eee, tayari wameshafika, sasa uko wapi Ashraf? alisema bosi katika mazungumzo hayo ndipo nikajua kuwa alikuwa akizungumza na yule mdogo wake aliyehitaji mtumishi wa ndani.
Amesema anakuja muda si mrefu, hivyo huyu anaweza kungojea, wewe Tunu unaweza kuendelea na majukumu yako kama kawaida, akija unaweza kuja tena.
Nikaondoka na kwenda nje ambako nilipitiliza hadi kwenye chumba cha kubadilishia nguo. Nikaungana na wafanyakazi wenzangu kufanya usafi ambapo siku hiyo nilipangiwa kukatakata maua na kuyamwagia maji.
Baada ya muda, alikuja msichana mmoja na kuniambia kuwa ninaitwa ofisini kwa bosi. Nikamfuata na kuingia moja kwa moja hadi ofisini kwa bosi ambako nilimkuta yeye, mdogo wake pamoja na Inana.
Nikamsabahi Ashraf kisha nikaketi kwenye moja ya viti.
Utambulisho ukafanyika na Ashraf akaridhika na Inana kuwa anafaa kuwa mtumishi wake wa ndani japokuwa sikujua alitumia kigezo gani kujiridhisha na Inana.
Anaonekana ni mchapakazi sana, nimeridhika naye kwa kila kitu, alisema Ashraf huku akitutazama usoni kwa zamu.
Kweli kabisa, hata mimi naona, alidakia bosi Elhakimu na kumfanya Inana atabasamu na kutazama chini kwa aibu ya kike.
Tukakubalina kuwa waondoke hadi nyumabani kwa Ashraf. Lakini kabla hawajaondoka, yule Mwarabu alilala ubavu na kutoa pochi yake ambapo alichomoa noti nyingi nyekundu na kuanza kuzihesabu mbele yetu. Hakika zilikuwa pesa nyingi.
Akanikabidhi huku akinishukuru kwa kumtafutia msichana wa kazi kwani alikuwa akihangaika sana.
Wakati akinikabidhi zile pesa, Inana aligeuka na kutuangalia lakini walipokutanisha macho na Ashraf, wote wakatabasamu na kunifanya nishtuke.
NIKAWATAZAMA tena usoni kwa zamu. Kila mmoja alijawa na furaha, nikazidi kubaki njia panda. Nilijiuliza maswali mengi ikiwemo inawezekana vipi watu ambao hawajawahi kuonana waweze kuzoeana kwa muda mfupi namna hiyo hadi kufikia hatua ya kuachiana tabasamu murua kama lile.Mshangao wangu uliongezeka kutokana na uchangamfu wa ajabu aliouonesha Inana kwa Ashraf. Nilishangaa kwa kuwa namjua vyema mdogo wangu Inana. Si mtu wa kutabasamu hovyo. Hasa kwa mtu asiyemjua hata kama atamfurahisha vipi."Ahsante sana jamani, Mungu akubariki," nilimshukuru Ashraf.
"Wala usijali Tunu, mimi napaswa nikushukuru kwa msaada wako," alisema Ashraf na kumgeukia tena Inana ambaye awamu hii aliinama chini kwa aibu.Baada ya mazungumzo ya hapa na pale, Bosi Elhakimu aliwaruhusu waondoke nami nikaendelea na majukumu ya kazi za siku hiyo. Inana na Ashraf waliondoka. Nikawa namuangalia mdogo wangu kwa macho ya huzuni ingawa sikujua hasa huzuni ilitokana na nini.Wakatembea hadi nje ambako Ashraf alikuwa ameegesha gari lake la kifahari aina ya Toyota Land Cruiser V8. Lakini kabla hawajapanda, nikamuita Inana na kuzunngumza naye kidogo.
"Inana mdogo wangu," nilimuita kwa sauti ya chini na ya upole mno hali ambayo hata yeye ilimfanya anitazame usoni kwa mshangao."Bee dada."
"Nakutakia kazi njema, lakini kuwa mwangalifu sana."
"Sawa dada, nitafanya hivyo."
"Jitahidi kufanya kazi kwa bidii na juhudi kubwa, si unayaona maisha tunayoishi kwa sasa?"
"Ndiyo dada yangu, nitajitahidi."Baada ya mazungumzo hayo, Inana na Ashraf waliondoka na kuniacha nikiwa nawasindikiza kwa macho hadi walipopotea kabisa kwenye upeo wa mboni zangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Moyo uliniuma sana. Uliniuma kwa mengi lakini kubwa ni kuwa nimewezaje kumruhusu Inana aende mahali ambako hata mimi sikupajua, hata kama nilimuamini sana Bosi Elhakimu.Nilirudi na kuendelea na majukumu yangu kama kawaida. Siku nzima nilishinda bila raha kabisa. Muda mwingi nilikuwa nikimuwaza Inana. Moyoni nikawa namuomba Mungu amtangulie na kumuepusha na mabaya yote.Muda wa chakula ulipowadia, mimi na wafanyakazi wenzangu tuliongozana hadi kwenye bohari la chakula. Nilikula huku nikiwa nimezongwa na mawazo tele kichwani.
"Tunu vipi, mbona kama hauko sawa kulikoni?" alikuwa msichana mmoja ambaye ni mfanyakazi mwenzangu aliyetaka kujua kilichonisibu kutokana na hali yangu."Hapana, niko sawa Misoji," nikamjibu huku nikionesha uchangamfu wa bandia.
"Nimeona kama hauko sawa, unaonekana mwenye mawazo."
"Hapana, ni ukimya wa kawaida tu."
"Sawa, lakini naona kama hauko sawa kabisa."Sikuendelea kumjibu zaidi ya hapo. Ni kweli kabisa sikuwa sawa licha ya kujilazimisha kuchangamka.
Tulipumzika kidogo, lakini kichwa kilianza kuniuma kwa mbali. Nikajilazimisha kufanya kazi. Hatimaye ukawadia muda wa kuondoka. Nikaenda kubadili nguo na kuanza safari ya kurudi Buguruni kwa shangazi.Nikiwa ndani ya basi kuelekea nyumbani, maneno ya Inana kuhusu matendo ya shangazi yakaanza kujirudia. Hakika yalionekana kuwa na ukweli ndani yake.
"Lazima nitafute chumba cha kuishi peke yangu. Tena maeneo haya haya ya karibu na kazini kwangu.Nilipofika nyumbani sikutaka mazungumzo ya aina yoyote na shangazi zaidi ya salamu. Nikajilaza kwenye kile kigodoro changu cha kila siku. Kutokana na wingi wa mawazo na uzito wa kichwa, nilijikuta nikipitiwa na usingizi.Niliamka ikiwa ni saa nne usiku, shangazi alikuwa ameshalala, nikaenda kujisaidia na kurudi kulala. Asubuhi niliamka mapema na kwenda kazini. Jambo la kwanza kufanya ni kuuliza mahali kulipokuwa na chumba cha kupanga maeneo hayo ya Mwananyamala.Nilipata chumba na kuridhika nacho. Nikaamua kuomba kiasi kidogo cha pesa ili niongeze nilipie chumba.Nikaamua kwenda ofisini kwa bosi ili kumuomba pesa hiyo. Moyoni nilipanga kuhamia kabisa siku iliyofuata. Nikapanga kumbembeleza bosi kwa kiwango kikubwa ili aweze kunipa pesa hiyo.
Niliingia ofisini, lakini nilishituka kumkuta bosi akiwa ameshika bunduki aina ya bastola huku akiifuta kwa kitambaa, nikabaki nimetoa macho.Je, nini kiliendelea? Fuatilia leo jioni
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment