Simulizi : Siri Ya Furaha
Sehemu Ya Tano (5)
Mambo aliyokuwa akiyafanya yalimpa jibu Moses kuwa mrembo huyo alikuwa kichaa. Alirudi akikimbia ndani ya nyumba ya Craig akiwaza kufanya jambo.
Alikitafuta kitabu cha mwongozo chenye namba tofauti za mji huo wa Cambridge. Baada ya muda mfupi wa kukipitia kitabu hicho aliipata namba ya Kliniki moja iliyokuwa ikihusika na watu waliokuwa wehu. Hakupoteza muda aliwapigiwa simu watu hao na kuwaelezaa kuwa angelipia gharama yeyote ambayo ingehitajika kwa ajili ya matibabu ya Veronika. Daktari mkuu wa kliniki hiyo alimwahidi Moses kuwa angetuma waguguzi na gari maalumu katika kitongoji hicho cha Croxton ili Veronika achukuliwe mara moja. Moses akiwa na hofu alipata faraja kidogo na alianza kuwasubiria wauguzi hao wa Cambridge Mental Patient Clinic aliokuwa amewapigia simu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati huo aliutumia kuwapigia simu rafiki zake wa karibu na kuwaeleza juu ya jambo hilo. Mtu wa kwanza kufika katika nyumba hiyo alikuwa Craig ambaye alichanganyikiwa na uhalibifu uliokuwa umefanywa na Veronika katika nyumba yake. Moses alimwondoa hofu kwa kumwahidi kumlipa gharama ya kila kitu. Baada ya muda mfupi marafiki wengine wa Moses walifika nyumbani hapo. Walionekana wakimfariji kwa vile kijana huyo alikuwa amekosa amani huku akijihisi kama alikuwa akihusika na tukio hilo. Hatimaye wauguzi wa kliniki ya walemavu wa akili walifika nyumbani hapo kwa Craig na kazi iliyopaswa kufuata ilikuwa moja, kumtafuta Veronika aliyeelekea barabara kuu ya kitongoji cha Girton.
Waliondoka na gari mbili, moja akiwa amepanda Moses na marafiki zake na nyuma walifuatwa na gari maalumu kwa kuwachukua wagonjwa wa akili ambalo walikuwapo wauguzi saba. Waliendesha gari hizo kwa mwendo wa taratibu huku wakiulizia njiani kama Veronika alikuwa amepita na jibu lilikuwa hivyo, mrembo huyo alikuwa ameshapita sehemu tofauti. Baada ya kutembea kwa muda wa saa moja na nusu barabarani wakimtafuta Veronika hatimaye walifanikiwa kumwona akiwa katika kituo cha treni katika kitongoji cha Girton. Wakati huo alikuwa amezungukwa na watu wengi waliokuwa wakimfurahia kwa vile alikuwa akicheza muziki. Nguo zake zilikuwa chafu kupindukia, hakuvutia hata kidogo ingawa sura yake ilikuwa kimwonesha kuwa ni msichana mrembo.
Moses alikuwa mtu wa kwanza kushuka kwenye gari huku akiwa na hasira kuona watu wakimshangilia mwanamke huyo aliyempenda. Aliwasukuma watu waliokuwa wamemzunguka Veronika kabla ya kumfuata na kumshika mkono akiwa na lengo la kuondoka naye. Alipojaribu kumvuta mwanamke huyo hakutikisika hata kidogo zaidi alikuwa akimcheka kwani Moses alitumia uwezo wake wote lakini hakufanikiwa kumwondoa Veronika hata kwa hatua moja. Jambo hilo lilikuwa burudani mpya kwa watu waliokuwa wamewazunguka. Veronika alimkamata Moses na kumnyanyua juu kabla ya kumtupa jambo lililomsababishia maumivu makali. Hakujali juu ya jambo hilo kwani alionekana akicheka kufurahia na watu kadhaa ambao walikuwa wakimshangilia.
Wauguzi alioongozana nao waliokuwa wakitokea katika kliniki ya watu wenye ugonjwa wa akili walianza kazi yao wakiwa na lengo la kumkamata Veronika ili wampeleke latika kituo chao. Kazi yao ilikuwa ngumu isivyo kawaida kwani mgonjwa huyo alikuwa na nguvu zisizo za kawaida. Walifanya majaribio la kumkamata kwa muda saa zima pasipo mafanikio na mwishoe waliamua kukubali kuwa mgonjwa huyo hakuwa wa kawaida. Kushindwa kwa wauguzi katika zoezi hilo kulimchanganya kabisa Moses ambaye alikuwa na maumivu kiunoni baada ya kutupwa na Veronika. Waliondoka eneo hilo wakimwacha Veronika akizunguka katika mitaa ya kitongoji hicho cha Girton.
* * * *
Rashid alilia kwa uchungu baada ya kutekwa kwa Veronika na kuachwa akiwa amefungwa pingu ndani ya nyumba ya mchumba wake huyo. Alilia kwa usiku mzima pasipo kupata msaada wowote, majira ya saa kumi a mbili asubuhi huku akiwa na hofu juu ya jambo lililokuwa linaendelea alisikia harufu ya kitu kinacho ungua nje ya nyumba hiyo. Alijikongoja taratibu huku akiwa amefungwa pingu mikononi na miguuni. Lengo lake lilikuwa kusogea sebuleni ili aangalie nje kupitia dirisha kitu kilichokuwa kinaungua. Baada ya dakika kadhaa alilifikia dirisha la nyumba hiyo kabla ya kupata mshtuko na kuanza kupiga kelele kwa nguvu. Alilishuhudia gari lake aina ya Ferarri pamoja na jingine la Veronika aina ya BMW yakiungua. Magari hayo yalishika moto na kuwaka kwa nguvu kama vile yalikuwa yamechomwa kwa makusudio ya mtu.
Kelele zake hazikusaidia jambo na hakuweza kupiga simu kwa kutumia namba ya maalumu ya kikosi cha zima moto kwa vile simu yake aliiweka juu ya kabali kubwa lililokuwapo sebuleni hapo na hakuweza kuichukua. Baada ya dakika arobaini na tano kikosi cha zima moto kilifika eneo hilo katika wakati aliokuwa amekata tamaa kwani magari hayo yalikuwa yameteketea kwa moto. Aliamini taarifa juu ya tukio hilo zilitolewa na majirani ambao hakuona jambo walilosaidia. Magari hayo yalikuwa yamebadilika ghafla na kubaki mchuma na mabati. Thamani yake haikuonekana hata kidogo, Rashid aliwaomba msaada watu waliofika eneo hilo wamfungue pingu alizofungwa na watu aliodai ni majambazi.
Hofu yake kubwa ilikuwa dhidi ya Veronika huku akiamini gari hizo zilichomwa moto na watu waliokuwa wamemteka. Baada ya dakika kadhaa wakati akifikiria jambo la kufanya alishtushwa na kelele za milio ya simu za Veronika. Simu hizo tatu zilikuwa zikiita mfululizo na kumpa hofu. Alipotazama wapigaji aligundua wote walikuwa wakipiga kutoka Tanzania, mmoja wao alikuwa Alex George tajiri aliyepewa jukumu la kusimamia mali za Veronika akiwa masomoni nchini Uingereza. Mwishoe Rashid aliamua kupokea simu hiyo ya tajiri huyo. “haloo, unaongea na Rashid Kagu, Veronika hayupo wakati huu” alisikika Rashid mara baada ya kupokea simu ya tajiri huyo. “ok! Mwambie huyo binti kuna matatizo makubwa huku mali zake zinateketea kwa moto kwa sababu ambayo hatuifahamu, ukianzia nyumba yake ya Masaki pamoja na maduka zaidi ya ishirini yaliopo sehemu tofauti hapa Tanzania, tunajaribu kuzima moto nitawajulisha baadaye” alimaliza tajiri huyo kabla ya kukata simu yake.
Rashid akiwa amechanganyikiwa aliondoka akikimbia huku akiwa amechukua simu yake na moja ya Veronika. Akili yake haikumpa jibu la jambo lolote, wakati huo alikuwa akiwaza kumtafuta mchumba wake huyo na alifanya hivyo. Alizunguka sehemu tofauti akitumia usafiri wa teksi ya kukodishwa akimtafuta Veronika pasipo mafanikio. Aliamua kutoa taarifa za kutekwa kwa Veronika kituo cha polisi na aliahidiwa kupewa msaada. Aliendelea kumtafuta huku akihisi huenda alitekwa na Moses, alielekea katika kitongoji cha Caxton katika nyumba aliyokuwa akiishi Moses lakini huko hakukuwa na mtu. Majira ya saa nane mchana alipigiwa simu na rafiki yake na kuelezwa Veronika alikuwa mwehu na wakati huo alikuwapo katika kitongoji cha Girton.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati huo Rashid alichanganyikiwa kabisa hata machozi yalikuwa yakimtoka pasipo kujitambua. Alimwamuru dereva aliyekuwa naye ageuze gari waelekee katika kitongoji cha Girton na huko alienda kushuhudia taarifa alizoelezwa. Alilia kwa uchungu akiwa hajui chanzo kilichosababisha jambo hilo kutokea na wakati huo alikuwa amepigiwa simu na Alex George, tajiri kutoka Tanzania ambaye alimweleza kuwa hakuna mali waliyofanikiwa kuokoa. Alielezwa magari kadhaa ya usafirishaji ya Maputo Transpotation Company yaliyokuwa yakimilikiwa na marehemu Lamos Maputo yalikuwa yameshapata ajali katika matukio tofauti. Toka wakati huo Rashid alikuwa mlinzi wa Veronika, alichukua fedha zote katika akaunti yake ya benki na ndizo alikuwa akihakikisha ananunua chakula ili Veronika asile mabaki ya vyakula vibovu. Hakuna mtu ambaye alikuwa akiweza kumsogelea Veronika na kumweleza jambo akamwelewa zaidi ya Rashid. Moses alijaribu kuwafuata sehemu walizokuwa wakizunguka lakini hakufanikiwa hata kumgusa msichana huyo.
Kwa muda mfupi aliokuwa na Veronika, Rashid aliweza kugundua chanzo cha kila kitu kilichohusiana na utajiri wa masharti aliopewa marehemu Lamos Maputo kwa vile Veronika alikuwa akiropoka mambo tofauti kila wakati. Baada ya mwezi mmoja wakati wakiwa katika mazingira ya chuo kikuu cha Cambridge Rashid alianza kuwaza jambo. Alifikiria kurudi Tanzania kutokana na karaha alizokuwa akizipata nchini humo, kila mtu aliyemwona akiwa kando ya Veronika alikuwa akimcheka. Wasichana aliowahi kuwakataa ndio waliongoza kwa dharau tofauti huku wakiamini wangeweza kumpata Rashid lakini haikuwa hivyo. Jambo lililokuwa kituko chuoni hapo Rashid alikuwa akipigana na Moses kwa nyakati tofauti wakimgombania Veronika. Kila mmoja wao alikuwa akihitaji kuwa karibu na mwanamke huyo ambaye alikuwa akimchukia sana Moses.
Rashid alikuwa akimchukia pia Moses, kijana mmarekani ambaye alikuwa hajui chanzo cha tatizo la Veronika kuwa mwehu na alijua lengo lake la kutaka kumpeleka katika kliniki ya wagonjwa wa akili halingesaidia. Ulifika wakati ambao Rashid alikuwa akiwaza kurudi Tanzania kwa kiasi kikubwa kwani alikuwa amechanganyikiwa na mambo mengi. Tumbo la Veronika lilikuwa limeanza kuongezeka kuashiria alikuwa na ujauzito ambao ulimchanganya. Watu walikuwa wakimzomea wakiamini alikuwa akitembea na mwehu huyo. Mbali na maneno hayo ya watu Moses alikuwa akidai ujauzito huo ni wake jambo ambalo Rashid hakuliafiki hata kidogo
Mbali na maneno hayo ya watu Moses alikuwa akidai ujauzito huo ni wake jambo ambalo Rashid hakuliafiki hata kidogo.
Aliamua kwenda kuongea na uongozi wa chuo hicho ili uwasaidie kurudi Tanzania kwani hakuwa na fedha za kutosha wakati huo. Ndoto zake za kuondoka Uingereza zilitimia, tarehe mosi mwezi wa nane alikuwa na Veronika katika chumba maalumu kwenye ndege ya shirika la British Airwaiys wakirudi nchini. Huku wakiwa wameondoka kimya kimya walimwacha Moses akiamini ujauzito wa Veronika ulikuwa wake. Rashid naye alikuwa anaamini hivyo huku akiwa na imani ya kupata ufumbuzi wa tatizo la mchumba wake akiwa nchini Tanzania.
Walifika nchini majira ya saa tatu usiku, Rashid hakupoteza muda alikodi teksi aliyohitaji iwapeleke mkoani Morogoro huko aliamini angeweza kufikia kwa babu yake mzee Kagu. Hakuwa na hofu juu ya malazi kwa vile alimpangia babu yake huyo nyumba mwaka mmoja uliokuwa umepita na mara kadhaa alikuwa akiwasilana naye zaidi alikuwa akimtumia fedha. Hofu yake ilikuwa juu ya waandishi wa vyombo vya habari, alitambua kama wangejua alikuwa amerudi na Veronika wangeanza kuwafuatilia ili kupata habari zao. Walifika mjini Morogoro saa saba na nusu usiku huku Rashid akiwa amechoka kupindukia. Hali ilikuwa tofauti kwa Veronika ambaye bado alikuwa na nguvu tele huku akiwa bado anaongelea mambo tofauti.
Mara baada ya kufika katika nyumba aliyompangia babu yake mwaka mmoja uliokuwa umepita Rashid hakupoteza muda kwani alianza kugonga nyumba hiyo huku akiwa amemshika mkono Veronika akihofia kutorokwa muda wowote. Baada ya muda mrefu wa kugonga mlango huo hatimaye alitoka mama mmoja ambaye aliishia mlangoni pasipo kufungua mlango kabla ya kusikika “mnasemaje jamani usiku huu?” “hapa si nyumbani kwa mzee Kagu? Sisi wajukuu zake” alisikika Rashid akiongea kwa taabu kwani alikuwa amechoka sana. “aah! Poleni, Juma moja limeshapita tangu mzee Kagu afariki na alishazikwa kwao Kidete” alijibu mama huyo ambaye aliondoka mlangoni hapo na kumwacha Rashid akianza kutokwa na machozi juu ya kifo cha babu yake. Mzee huyo ndiye pekee alikuwa amemlea kwa miaka mingi baada ya kifo cha wazazi wake. Hakuwaza jambo jipya usiku huo, aliamua kwenda kulala katika nyumba ya kulala wageni kwa usiku huo uliojaa tabu kutokana na usumbufu wa Veronika.
Siku iliyofuata alifanikiwa kufika katika kijiji cha Kidete ambako alikuwa akiishi na babu yake miaka kadhaa iliyokuwa imepita. Alifikia katika nyumba iliyokuwa imeezekwa kwa majani huku ikiwa imeharibika vibaya. Kwa jinsi nyumba hiyo ilivyokuwa ilionesha dhahiri ilikuwa ikipitisha maji wakati wa mvua. Tayari alikuwa ameliona kaburi la babu yake aliyekuwa amezikwa nje ya nyumba hiyo. Alikuwa akiumia sana kila mara alipoliona kaburi hilo la mtu ambaye alikuwa zaidi ya babu yake. Wakati huo alipata amani kidogo kukaa katika nyumba hiyo iliyokuwa na chumba cha kulala pamoja na jiko. Hakuwaza kuwatafuta na kuwaomba msaada ndugu zake kadhaa ambao siku zote hawakuwa na msaada kwake. Jambo alililofanya aliwatafuta watu waliomsaidia kumfanyia usafi kuzunguka nyumba hiyo iliyojaa majani marefu pamoja na vichaka. Vibarua hao walimsaidia pia kuezeka nyumba hiyo ambayo paa lake lilikuwa limeoza.
Baada ya zoezi hilo Rashid alipata amani moyoni mwake kidogo huku akiamini alikuwa ameepuka mkono wa vyombo vya habari. Aliamini jambo hilo kwa vile nyuma hiyo ilikuwa mbali na makazi ya watu wengine. Alikuwa amebakiwa na kiasi cha laki tatu ambazo aliwaza kuzitumia katika wakati huo ambao alikuwa akitathimini hatma ya maisha yake. Jambo kubwa lililokuwa limemkaa kichwani aliwaza pia kuwatembelea waganga wa jadi ili kupata ufumbuzi wa tatizo la mchumba wake. Alikuwa akiwaza pia juu ya ujauzito wa Veronika ambao kila siku alipokuwa akimtazama alikuwa hapati jibu juu ya ujauzito huo.
Hisia zake hazikutokea hata kidogo siku iliyofuata waandishi wa wa habari walianza kufika kwa wingi nyumbani kwake. Jambo hilo lilimuumiza sana lakini alikosa jibu la kufanya, mahojiano yao siku zote yalimuudhi na kuna wakati aligoma kutoa ushirikiano kwa vile aliamini walikuwa wakimtangaza vibaya. Maisha yaliendelea kwa jinsi hiyo na alianza kuyazoea ilhali ujauzito wa Veronika ukiendelea kuongezeka. Wakati huo alifanikiwa kuwatembelea waganga wa jadi kadhaa na kuwapeleleza juu ya tatizo alilokuwa nalo Veronika. Siku zote alikuwa akielezwa kuwa tatizo la Veronika lilikuwa likiendana na masharti ya kibiashara ya waganga wa bara la Asia. Waganga hao wa jadi walimsisitizia kuwa mtu pekee ambaye angeweza kutengua masharti hayo alikuwa mganga aliyoyatoa.
Alijitahidi kuzunguka sehemu tofauti za mkoa wa Morogoro na Dodoma lakini jibu lilikuwa lile lile. Wakati huo alizunguka peke yake kwani Veronika hakuwa msumbufu kama awali, alikuwa akishinda anacheza kando ya pori walilokuwa wakiishi. Hatimaye Rashid aliamua kurudi na kutulia nyumbani kwake akiwa na mchumba wake katika kijiji hicho cha Kidete. Aliamua kusubiria siku ambayo Veronika angejifungua kwa sababu alikuwa na ujauzito wa miezi saba. Katika kipindi hicho Rashid alikuwa akifanya vibarua tofauti kijijini hapo akikusanya fedha kwa ajili ya kujifungua kwa Veronika.
* * * *
Baada ya miaka minne Rashid bado alikuwa akiishi katika kijiji cha Kidete akiwa na mchumba wake, Veronika ambaye bado alikuwa mwehu. Wakati huo alikuwa amepata faraja kidogo kwani alikuwa na mtoto ambaye alikuwa amefanana kwa kiasi kikubwa na mama yake. Bado kuna jambo lilikuwa likimsumbua kichwani juu ya ukweli wa mtoto huyo ambaye alimpa jina la David. Alikuwa akihisi uwezekano wa mtoto huyo kuwa siyo mtoto wake kwa vile tayari alibaini Moses naye alikuwa akiamini mtoto huyo ni wake. Jambo hilo lilikuwa likimpa utata kichwani kwake kwa vile yeye na kijana huyo mwenzie walilala na Veronika kwa muda tofauti katika usiku mmoja miaka mitano iliyokuwa imepita na kumpa ujauzito. Alijipa faraja kwa vile alitambua ilikuwa vigumu kwa Moses kusafiri kutoka Marekani kuja kuwatafuta na zaidi eneo alilokuwapo katika kijiji hicho aliamini alikuwa katika maficho ya kutosha.
Hakutaka kwenda kuchukua vipimo vya damu ili kubaini kama mtoto huyo alikuwa wake. Alitambua angeumia sana kama angegundua mtoto huyo hakuwa mtoto wake. Wakati huo alikuwa akiendelela na zoezi lake la kumtembeza Veronika kwa waganga wa jadi tofauti ili kumtafutia ufumbuzi. Ni wakati ambao alikuwa akimpeleka pia katika makanisa tofauti kwa ajili ya maombezi. Mbali na jitihada zake alizokuwa akizifanya Veronika hakuweza kupona. Hakukata tamaa na aliamini mwanamke huyo angepona siku moja na wangetimiza ndoto zao za muda mrefu. Maisha aliyokuwa akiishi yalikuwa ya kimaskini huku akiwa ameyazoea, alikuwa akifanya kazi za shamba na kazi ya vibarua iliyokuwa ikimwingizia kipato cha kuendesha familia yake kila siku.
Tarehe mosi mwezi Desemba majira ya mchana wakati akisikiliza redio ya shirika la taifa la utangazaji, Rashid alipata faraja. Alilisikia tangazo moja lililokuwa likimhusu mhubiri wa kimataifa ambaye alikuwapo nchini kwa ziara ya siku kumi na nne. Mhubiri huyo alitajwa kwa jina la Sigismund Leopold aliyekuwa akitokea nchini Ujerumani katika jimbo la Frankfurt. Akiwa na mkewe walikuwa na ziara ya kuzunguka dunia nzima kuwaombea watu waliokuwa na shida mbalimbali ambazo zilipata ufumbuzi. Mhubiri na mchungaji Sigismund Leopold pamoja na mkewe walikuwa viongozi pia wa kanisa lao la `Christianity Way To Lord` lililokuwapo nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania.
Rashid alipanga kutokosa mkutano huo wa injili ambao ulitarajiwa kufanywa kwa siku mbili katika mkoa huo wa Morogoro kuanzia tarehe kumi. Aliamua kuanza kukasanya fedha kwa ajili ya maandalizi ya kushiriki mkutano huo. Alikuwa akiamini wakati huo angepata ufumbuzi juu ya tatizo la mchumba wake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliamua kuanza kukasanya fedha kwa ajili ya maandalizi ya kushiriki mkutano huo. Alikuwa akiamini wakati huo angepata ufumbuzi juu ya tatizo la mchumba wake. Ilipofika tarehe kumi asubuhi alionekana akiondoka nyumbani kwake akiwa na Veronika pamoja na mtoto wao David. Alikuwa amemshika mkono mchumba wake huyo aliyekuwa msumbufu siku zote na wakati huo alikuwa akigoma kusafiri kwa vile alikuwa ameyazoea sana mazingira ya kijiji hicho cha Kidete. Rashid alijitahidi kumshawishi na lengo lake lilifanikiwa, alisafiri na Veronika mpaka Morogoro mjini wakiwa na mwanao. Walifika majira ya saa sita mchana, Rashid aliamua kutafuta chakula kwa ajili ya familia yake hiyo kabla ya kuelekea katika mkutano uliotarajiwa kuanza saa tisa alasiri katika uwanjwa wa michezo wa Jamhuri.
Baada ya kula chakula aliongozana nao mpaka katika uwanja wa Jamhuri, walifika katika uwanja huo na kushuhudia ukiwa umejaa watu wa rika tofauiti waliokuwa wakimsubiri kwa hamu mchungaji Sigismund Leopold na mkewe wafike eneo hilo kwa ajili ya kuhubiri katika mkutano huo. Rashid akiwa amemshika Veronika mkono wake sawasawa alikuwa amekaa eneo la nyuma katika umati huo wa watu huku pembeni yake akiwa na mwanao. Akiwa na mavazi duni na familia yake alikuwa na shauku ya kuona mkutano huo ukianza ili kukata kiu iliyokuwa moyoni mwake. Alikuwa akitaka kushuhudia miujiza siku hiyo, miujiza ambayo aliikosa kwa miaka mingi.
Watu kadhaa walionekana wakiwashangaa jinsi walivyokuwa lakini hakujali jambo hilo alilokuwa amelizoea. Hatimaye majira ya saa tisa kasoro msafara wa magari zaidi ya ishirini ulifika uwanjani hapo. Watu wote akiwapo yeye na familia yake walisimama kuyashuhudia magari hayo. Watu walikuwa wakipiga makofi na kushangilia kuwasili kwa mchungaji Sigismund na mkewe waliokuwa wakisubiriwa kwa hamu. Hatimaye majira ya saa tisa alasiri mkewe Sigismund Leopold alianza kuhubiri baada ya kujitambulisha kuwa alikuwa mzaliwa wa Tanzania.
Rashid alikuwa makini akifuatilia mahubiri hayo yaliyompa faraja, kuna wakati Veronika alikuwa akicheka cheka na kumnyoshea mkono mama huyo. Wakati mahubiri hayo yakiendelela kuna jambo lilimshtua Rashid, mama huyo mkewe Sigismund alikuwa amefanana kwa kiasi kikubwa na Veronika jambo lililomfanya akose jibu juu ya sababu ya kufanana kwao. Aliendelea kuhubiri mpaka alipotimiza saa moja na nusu wakati ambao kwaya zilizokuwapo katika mkutano huo ziliimba kwa nusu saa kabla ya kufuatiwa na muda wa maombezi. “kwa wale wote wenye matatizo mnaombwa mpite mbele katika nafasi ya uwazi tuliyoiweka ili muombewe” ilisikika sauti ya mkewe Sigismund Leopold ambayo ilianza kuwasimamisha watu wenye matatizo walioanza kutembea kuelekea eneo la mbele lililotengwa ajili ya maombezi.
Rashid alikuwa mmoja wa watu walisimama mara baada ya kusikia maelezo hayo. Alimsimamisha Veronika na mwanaye akiwa na lengo kuelekea nao mbele kwa ajili ya kumwombea Veronika. Mara baada ya kusimama alianza kwa kumvuta Veronika ili waelekee eneo husika kwa ajili ya kuombewa lakini hali ilikuwa tofauti. Veronika alianza kugoma kabisa huku akitaka waondoke eneo hilo. Kila Rashid alipojitahidi kumvuta alikuwa hatingishiki hata kidogo kusogea mbele. Aliamua kumwacha mwanao David ambaye alikuwa amemshika mkono na nguvu zake zote alizielekezea kwa Veronika. Alijitahidi kumvuta kwa nguvu zake zote lakini hakufanikiwa kumsogeza mbele hata kidogo. Watu wachache ndio waliokuwa wakishuhudia tukio hilo kwa vile umati mzima ulikuwa umesimama kwa ajili ya maombezi.
Hatimaye maombezi hayo yalianza huku Rashid akiendelea kumvuta Veronika pasipo mafanikio hata alipomshawishi waelekee mbele hakuelewa hata kidogo. Rashid alikuwa akitokwa na jasho mwili mzima huku akiwa hayuko tayari kuondoka eneo hilo pasipo Veronika kuombewa. Wakati huo alianza kuchanganyikiwa zaidi kwani Veronika alianza kumvuta na walikuwa wakiuacha umati huo taratibu. Rashid alilia kwa uchungu akiendelea kumvuta Veronika lakini hakupata msaada kwani watu walikuwa wamefumba macho wakiwa katika maombezi ya watu hao waliokuwa na matatizo mbalimbali. Baada ya dakika kumi na tano, maombezi hayo yalikamilika na kwaya mojawapo iliitwa kabla ya kuanza kuimba ilhali wakisubiria wakati wa watu kutoa ushuhuda juu ya mambo waliyokuwa wamtendewa na mwenyezi Mungu baada ya kuombewa.
Wakati kwaya hiyo ikiwa imeanza kuimba Rashid na Veronika walikuwa umbali wa mita kadhaa kutoka eneo lililokuwa mkutano huyo huku Rashid akiendelea kuvutwa ilhali akilia kwa uchungu. Hata watu waliopita karibu yao hawakuwahusisha na mkutano huo uliokuwa ukiendelea. Mkewe Sigismund Leopold alipata mshtuko wa kiroho moyoni mwake, alisimama kutoka eneo alilokuwa amekaa ilhali kwaya ikiendelea kuimba. Aliangaza macho yake nyuma kabisa ya mkutano huo kabla ya kumshuhudia mtu mmoja akivutwa ilhali akiwa amemng`ang`ania mtu aliyekuwa akimvuta. Aliwakonyeza wahudumu wa mkutano huo ambao walijongea sehemu aliyokuwa amesimama haraka, aliwaonesha watu waliokuwa wakivutana ambao alikuwa akiwashuhudia na alitaka wapelekwe mbele kwa ajili ya maombezi.
Wahudumu wa mkutano huo waliondoka wakikimbia na kuelekea eneo waliloelekezwa walilokuwapo Veronika na Rashid. Baada ya sekunde kadhaa walifika eneo hilo kabla ya kumshuhudia Rashid akilia huku akijitahidi kumvuta Veronika. “mnisaidie hataki kuombewa….” Alikuwa akisikika Rashid akirudia sentensi hiyo pasipo mafanikio huku akiwa amelowa jasho mwili mzima. Alikuwa amechoka kupindukia lakini hakuwa tayari kumwacha Veronika aondoke pasipo kushuhudia muujiza siku hiyo. Wahudumu waliotumwa nao waliungana na kijana huyo kabla ya kuanza kumvuta Veronika ili apelekwe mbele kwa ajili ya maombezi lakini jibu lilibaki lilelile. Veronika alikuwa hatingishiki kusogea mbele hata kidogo.
Wakati huo mchungaji na mhubiri Sigismund Leopold na mkewe walikuwa wamesimama kwenye jukwaa kuu wakishuhudia tukio hilo. Umati wa watu waliokuwapo katika mkutano huo waligeuza vichwa vyao na kuelekeza macho yao kwa watu zaidi ya kumi waliokuwa wakishindwa kumvuta Veronika na kumpeleka mbele kwa maombezi. Mchungaji huyo na mkewe waliamua kushuka jukwaani na kuanza kutembea huku wakikemea mapepo ilhali wakielekea eneo ambalo wahudumu walishindwa kumvuta Veronika. Baada ya dakika moja waliwafikia na walikuwa wamezungukwa na umati huo wa watu waliokuwa wakitaka kujua jambo ambalo lingetokea.
Mchungaji Sigismund alimsogelea Veronika aliyekuwa akiwatukana na kumshika kichwani kabla ya kusikika “muipeleke hii msichana kule mbele…”. Baada ya kauli hiyo hali ilikuwa tofauti, Veronika alipovutwa alianza kusogea mbele ingawaje alikuwa akigoma lakini wakati huo nguvu zake hazikuwa na lolote. Baada ya dakika tano alikuwapo katika jukwaa kuu huku akiombewa na mchungaji Sigismund Leopold na mkewe waliokuwa wamemshika kichwa. Ghafla Veronika alianza kuhangaika jukwaani hapo wakati maombezi juu yake yakiendelea. Kelele zisizoeleweka zilitoka eneo alilokuwapo wakati watu wakiwa wamefumba macho wakimwombea. Rashid naye alikuwa amefumba macho huku akiwa mtulivu ilhali akiamini siku hiyo ilikuwa ya miujiza dhidi yake.
Wakati maombezi hayo yakiendelea mkewe Sigismund Leopold moyoni alikuwa akiumia sana na kukumbuka maisha yake ya awali kabla ya wakati huo. Jinsi alivyokuwa akijisikia moyoni aliamini kulikuwa na jambo ambalo lingetokea siku hiyo katika mkutano huo. Baada ya dakika ishirini maombezi dhidi ya Veronika yalikamilika na wakati huo alikuwa ametulia ilhali akiwa amezimia alibebwa na kupelekwa nyuma ya jukwaa ambako alienda kupewa huduma ya kwanza. Rashid hakuwa nyuma, alikuwa kando akitokwa na machozi kusubiri kwa hamu jambo ambalo lingetokea mara baada ya kuzinduka kwa Veronika. Baada ya dakika tano mwanamke huyo alizinduka na alionekana akiangalia huku na kule kwa sekunde kadhaa, kisha alinyanyuka na kukaa eneo hilo alilokuwa amelazwa.
Baada ya dakika tano mwanamke huyo alizinduka na alionekana akiangalia huku na kule kwa sekunde kadhaa, kisha alinyanyuka na kukaa eneo hilo alilokuwa amelazwa.
Alipoangaza macho yake huku na kule alimwona mtu wa kwanza kumfahamu kabla ya kusikika, “ Rashid, Rashid….” Alisimama na kukimbia kabla ya kwenda kumkumbatia kijana huyo. “tuko wapi hapa?” aliongeza swali ambalo hakujibiwa na Rashid aliyekuwa na furaha kupindukia huku akipiga kelele. “umepona, umepona wewe siyo chizi tena…” alisikika akiongea kauli ambazo zilimshangaza Veronika. Rashid alianza kumvuta kwa nguvu Veronika ambaye alianza kumfuata na alielekea naye katika jukwaa kuu kabla ya kwenda kupiga magoti mbele ya mchungaji Sigismund na mkewe kama ishara ya kushukuru. “Usipige magoti kijana hebu nyanyuka, unapaswa kumshukuru mwenyezi Mungu muweza wa yote” alisikika mkewe Sigismund huku akimnyanyua Rashid. Wakati huo Veronika alikuwa amepigwa na butwaa baada ya kuona umati wa watu waliokuapo eneo hilo wakimshangaa. “kijana unaitwa nani?” “ mimi naitwa Rashid Kagu….” Alijibu,
“ Ok! Na wewe dada uliyekuwa na matatizo unaitwa nani?” alisikika mkewe Sigismund wakati akiendelea kumchunguza kwa makini huku akiwa amemsogezea kipaza sauti “mimi naitwa Veronika Lamos Maputo lakini sikuwa na matatizo” alisikika akiongea na sauti yake kuufikia umati wa watu vizuri.
Mkewe Sigismund alishtuka na hali hiyo ilikuwapo kwa mumewe pia ambaye alisimama kutoka katika kiti alichokuwa amekaa na kwenda kuchukua kipaza sauti kwa mkewe. “umesema iko inaiitwa nani” alisikika kwa sauti iliyoashiria hakujua vizuri Kiswahili. “Naitwa Veronika Lamos Maputo” alijibiwa tena na Veronika. Mchungaji Sigismund Leopold alimsogelea Veronika na kwenda kumshika kichwa kabla ya kuanza kukichunguza katika hali iliyoanza kuushangaza umati uliufika eneo hilo. Baada ya sekunde kadhaa aliliona kovu kichwani kwa Veronika lililomkumbusha miaka zaidi ya ishirini iliyopita aligeuka na kumwangalia mkewe aliyekuwa akitetemeka huku akiwa haamini jambo lililokuwa linaendelea kabla ya kusikika. “she is our daughter…” (ni mtoto wetu).CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mkewe Sigismund aliruka kwa furaha na kumvamia Veronika kwa kumkumbatia kwa furaha kabla ya kuungana na mumewe. Rashid na umati mzima uliofika eneo hilo ulibaki bumbuwazi ukiwa haujui jambo lililokuwa linaendelea.Mchungaji Sigismund alianza kwa kuukumbusha umati juu matukio yaliyotokea kipindi cha nyuma, tangu wakati ambao alimsaidia Veronika kufanyiwa upasuaji wa kichwa. Alieleza pia jinsi Lamos Maputo alivyoitelekeza familia yake na jinsi alivyomteka Veronika na kuacha damu waliyoamini mtoto huyo alikuwa ameuawa. Mchungaji Sigismund alieleza pia jinsi alivyomuoa mkewe baada ya kuamini mwanaye alikuwa amekufa.
Rashid naye aliitwa na alisimulia maisha ya Veronika mwanzo mpaka mwisho kadri alivyotambua mpaka wakati huo ambao alikuwa amepona huku akiwa amefilisika baada ya kukosea masharti ya mganga wa jadi aliyempa utajiri baba yake. Furaha ndiyo iliyotawala eneo hilo, zaidi kwa Veronika ambaye alikuwa haamini kama alikuwa ameishi kama mwehu kwa miaka zaidi ya minne. Tofauti na ilivyotarajiwa mkutano huo uliisha majira ya saa mbili usiku. Mbali na furaha ya ushindi waliyokuwa nayo, waliondoka katika mkutani huo kwa majonzi kwani mtoto wa Veronika hakupatikana. Alitafutwa kila sehemu pasipo mafanikio. Rashid alitambua uwezekano uliosababisha mtoto huyo kupotea kutokana na kumwacha wakati akimvuta Veronika kwa ajili ya kwenda mbele kwa maombezi.
Mpaka inatimia majira ya saa tano usiku mtoto huyo alikuwa hajapatikana. Mchungaji Sigismund na mkewe waliingia katika maombi mazito wakimwombea mtoto huyo na muda wote walikuwa wakiwapa faraja Veronika na Rashid kuwa mtoto huyo angepatikana. Veronika alionekana kukosa amani juu ya jambo hilo kwa vile kumbukummbu zake hazikumkumbusha hata kidogo juu ya mtoto huyo. Mambo aliyokuwa akikumbuka yalikuwa yale tu aliyoyafanya kabla ya kuwa mwehu. Siku mbili zilipita bila mafanikio ya kumpata mtoto jambo lililozidi kuwaongeza hofu zaidi lakini walizidisha maombi wakiamini angepatikana. Wakati huo Mchungaji Sigismund na mkewe walisitisha ziara zao na mkewe na walikuwapo katika hoteli waliyofikia ambako walikuwa wakiendelea na maombi. Walikuwa wakiamini mtoto huyo alikuwapo katika mkoa huo. Tayari walikuwa wametoa taarifa juu ya mtoto huyo katika kiyuo cha polisi pamoja na vituo tofauti vya habari.
* * * *
Moses Malcolm alikuwa akiishi nchini Marekani katika jimbo la Antlanta huku akiwa amerithi utajiri wa familia yake. Wakati huo alikuwa ameoa na kwa kiasi kikubwa alikuwa ameanza kumsahau Veronika, mwanamke aliyempenda sana wakati akiwa katika chuo kikuu cha Cambridge. Jambo ambalo lilikuwa kichwani mwake kwa muda wa miaka minne lilihusiana na ujauzito ambao Veronika alikuwa nao mara baada ya kuwa mwehu miaka kadhaa iliyokuwa imepita. Siku zote alikuwa akiamini ujauzito huo ulikuwa unamhusu. Kwa muda wa miaka minne tangu kuachana na mwanamke huyo aliyerudi Tanzania na Rashid alikuwa akiwaza juu ya jambo hilo. Mwishoe aliamua kupanga safari ya kimya kimya pasipo kumuaga hata mkewe.
Alisafiri kwa ndege katika tarehe za mwisho wa mwaka na alifika nchini tarehe nne mwezi Desemba. Kichwani lengo lake lilikuwa moja, alikuwa na lengo la kumtafuta Veronika ambaye aliamini alikuwa na Rashid ili amwibe mtoto. Mara baada ya kufika jijini Dar es salaam akitumia fedha alizokuwa nazo alitembelea vyombo vya habari tofauti na kufanikiwa kupata taarifa kuwa Veronika bado alikuwa mwehu. Alielezwa kuwa alikuwa akiishi katika kijiji cha Kidete kilichokuwapo mkoani Morogoro. Alipanga ziara yake ya kwenda kumwiba mtoto huyo. Akiwa na msaada wa vijana watatu huku wakitumia gari aina ya Mercedez Benz walisafiri mpaka katika kijiji cha Kidete siku ya tarehe tisa. Walimpeleleza maisha ambayo Rashid alikuwa akiishi na familia yake ambayo hayakuwapa upenyo wa kumteka mtoto wao.
Moses alibahatika kumwona mtoto huyo kwa mbali wakati wakiendelea kuifuatilia familia hiyo na alipata imani kuwa mtoto huyo alikuwa wake kwa jinsi alivyokuwa. Siku iliyofuata waliishuhudia familia hiyo ikisafiri kuelekea Morogoro, nao walisafiri kuelekea katika mkoa huo. Huko waliishuhudia familia hiyo ikiishia katika mkutano wa injili, huko ndiko dhamira ya Moses ilichukua nafasi alifanikiwa kumuiba mtoto huyo wakati Rashid akimvuta Veronika akaombewe ilhali akimsahau mtoto huyo. Mara baada ya tukio hilo safari ilianza wakielekea jijini Dar es salaam ambako Moses aliamini mipango yake yote ingechukua nafasi.
Jijini alifikia katika hoteli ya Movenpick na kwa siku tatu mfululizo alikuwa akicheza ndani ya chumba chake na mtoto huyo waliyezoena ingawaje walikuwa hawaelewani lugha. Tayari alimtafuta mtu ambaye alikuwa akishughurikia taratibu za usafiri za mtoto huyo ambaye alitaka asafiri naye kama mtoto yatima na hatimaye zoezi hilo lilifanikiwa. Siku moja kabla ya safari yake alipata wazo ambalo lilikuwa gumu kufikia maamuzi yake, aliamua kumpeleka mtoto huyo katika hospitali ya Aga Khan ili akachukue vipimo na kubaini kama kweli alikuwa mtoto wake. Jambo hilo ndilo lilimkosesha raha na amani aliyokuwa ameipata kwani vipimo vilionesha mtoto huyo hakuwa wake. Alirudi katika hoteli aliyofikia akiwa hana amani hata kidogo na zaidi alijilaumu kwa nini alikuja Tanzania.
Siku iliyofuata asubuhi na mapema aliondoka katika hoteli hiyo na kumwacha mtoto huyo. Alitoa taarifa juu ya jambo hilo kwa mkuu wa hoteli ambaye alimpa pia fedha akiomba amsaidie kutangaza kwa umma juu ya mtoto huyo zaidi alimpa shilingi milioni ishirini za Kitanzania kwenye mfuko wa kaki pamoja na ujumbe mfupi ndani yake. Alimweleza mkuu wa hoteli hiyo kuwa mfuko huo apewe baba wa mtoto huyo. Hatimaye Moses alisafiri kurudi nchini Marekani. Siku iliyofuata Rashid na Veronika walifika katika hoteli hiyo wakiwa wameongozana na mchungaji Sigismund na mkewe huku wakiwa na shauku ya kumwona mjukuu wao. Walipata taarifa juu ya mtoto huyo David kupitia matangazo yaliyotolewa na vyombo tofauti vya habari. Wakiwa na furaha walimchukua David na kuushukuru uongozi wa hoteli hiyo. Kabla ya hawajaondoka mkuu wa hoteli hiyo alimkabidhi Rashid mfuko wa kaki, alipoufungua aliona fedha pamoja na ujumbe ulioandikwa, “I am Sorry Rashid but I hope this money will help you, Moses Malcolm” (nisamehe Rashid lakini naamini fedha hizi zitakusaidia, Moses Malcolm) alikisoma kikaratasi kidogo Rashid kabla ya kutabasamu kwa furaha. Tayari alitambua vizuri kuwa David alikuwa mwanaye kwa vile alitekwa na Moses ambaye aliamini alishagundua kuwa mtoto huyo hakuwa damu yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya miaka miwili Veronika na mumewe walikuwa wameshafunga ndoa. Walifurahia maisha yao wakiwa na mwanao mpendwa David. Veronika alikuwa mfanyakazi wa wizara ya wanawake, jinsia na watoto huku Rashid akiwa anamiliki kampuni yake mwenyewe iliyokuwa ikichapisha gazeti la Sanatu lililokuwa maalumu kwa katuni. Huko ndiko alikoendeleza kipaji chake cha uchoraji katika gazeti hilo lililokuwa likitoka kila mwisho wa juma. Walikuwa wakiishi Mbezi Beach katika nyumba waliyojengewa na mchungaji na mhubiri Sigismund Leopold akishirikiana na mkewe ambao wakati huo walikuwapo nchini Ujerumani. Waliendelea kufurahia maisha yao huku kila siku wakiheshimu SIRI YA FURAHA waliyokuwa nayo, siri ya uponyaji wa mwenyezi Mungu juu ya familia yao.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment