Search This Blog

Sunday 19 June 2022

ROHO ZA KISHETANI - 2

 







    Simulizi :Roho Za Kishetani
    Sehemu Ya Pili (2)



    Ilikuwa ni siri kubwa. Hakuna chombo chochote cha habari kilichopewa taarifa rasmi na serikali kuhusu tukio hilo . Lakini ilikuwa ni siri iliyodumu kwa siku chache tu na kufichuka taratibu kupitia minong'ono ya hapa na pale kutoka kwa baadhi ya askari wa jeshi.

    Ni minong'ono hiyo iliyogeuka kuwa habari nzito kwa baadhi ya magazeti, redio na televisheni. Baadhi ya taasisi hizo za habari zilitangaza, zikidai kuwa ni habari ambazo hazijathibitishwa rasmi. Kilichofuata ni wakuu wa vyombo hivyo kuitwa kusikojulikana ambako walihojiwa vikali na kupewa vitisho sanjari na onyo kali.

    Gazeti moja lilidai kuwa habari hizo zilipatikana kufuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na waandishi wake na kisha kuthibitishwa na baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa Makao Makuu ya Jeshi, bila kuyataja majina wala vyeo vyao.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mhariri na mwandishi mmoja wa gazeti hilo walichukuliwa kimsobesobe, wakafichwa mahala fulani ambako mahojiano ya kina yalifanyika, mahojiano yaliyoambatana na mateso ya wastani lakini yaliyoacha kumbukumbu ya kudumu miilini mwao.





    *****



    RWEGASIRA, Karumuna na Muganyizi walijificha katika pori la Bunju kwa siku moja tu. Siku ya pili walitokeza hadharani, wakalivamia basi lililokwenda Bagamoyo na kupora pesa kwa abiria na kondakta, pesa ambazo hesabu yake iliwafanya wakenue meno kwa fiuraha.

    Milioni tatu na nusu!

    Hazikuwa ni pesa za kuwafanya wajiamini kupita kiasi, lakini ziliwapa nguvu mpya. Wakiwa bado wanajifichaficha katika eneo hilo , ndipo wazo lilipomjia Kapteni Rwegasira, wazo alilolitoa kwa wenzake bila ya kuchelewa.

    “Hatutakuwa tumefanya lolote la maana kuja kujichimbia humu porini bila ya mpango maalumu,” aliwaambia. “Tunapaswa kuionyesha serikali kosa ililofanya.”

    “Una maana gani?” Karumuna alimwuliza.

    “Kuipa serikali fundisho,” Rwegasira alifafanua. “Lazima serikali ilipe damu za familia zetu zilizoteketezwa na Warundi na Wanyarwanda wanaozidi kuja Tanzania na wengine waliopo wanang'ang'ania kuishi hapa huku wakipewa uraia katika mazingira ya ajabuajabu.”

    Wenzake hawakumwelewa. Muganyizi akamwuliza, “Una maana gani?”

    “Lazima tufanye kitu katika kuwaenzi marehemu wazazi na ndugu zetu waliouawa, na wauaji wakaachiliwa huru!” Rwegasira alisema kwa msisitizo.

    “Kwa hiyo una plani gani?” Muganyizi aliendelea kuhoji.

    “Kuwasiliana na Sengiyumva.”

    “Sengiyumva?!!” Karumuna na Muganyizi walitamka kwa pamoja, mshangao ukiwa dhahiri nyusoni pao. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwao kulisikia jina hilo .

    “Ndio, Sengiyumva,” Rwegasira alijibu. “Ni miongoni mwa watu wenye pesa kama mchanga huko Burundi . Kwa hapa Tanzania ukiwa na pesa kama Sengiyumva wanoko hawachelewi kukupakazia kuwa ni fisadi.”

    “Ni Mrundi?!” Karumuna aliuliza akionekana kutokuwa na imani na huyo mtajwa.

    “Yeah, ni Mrundi.”

    “Mrundi atatusaidia nini?”

    “Atatupa zana za kutimiza azma yetu.”

    Muganyizi aliguna. Kisha akarusha swali: “Unamwamini vipi huyo Mrundi wako?”

    “Ni rafiki yangu wa siku nyingi. Tulikutana Canada . Na sasa anashirikiana na waasi wa serikali ya Rais wa sasa wa Burundi , Pierre Nkurunziza. Kwa jinsi anavyoichukia Tanzania , acha tu.”

    “Chuki ya nini?” Karumuna aliuliza.

    “Anadai kuwa Tanzania inajitia kimbelembele katika kuingilia mambo ya nchi nyingine na kujifanya ina uwezo sana wa kutunza wakimbizi.”

    “Haa! Hilo tu?” Karumuna aliuliza kwa mshangao.

    “Ndio. Na aliwahi kunishauri eti niasi jeshi, na yeye atan'saidia kupindua nchi.”

    Muganyizi na Karumuna waliguna.

    “Ana uwezo kiasi gani kiuchumi?” Muganyizi alihoji.

    “Ana pesa nyingi alizolimbikiza katika benki za Ubelgiji, Ufaransa na Uswisi. Ana mabilioni ya pesa kwa thamani ya pesa za kibongo. Nasikia jumla ya pesa alizolimbikiza katika benki zote huko majuu zinaweza kufikia dola milioni mia nane!”

    “Milioni mia nane!” Muganyizi aliropoka.

    “Yeah, tena ni dola siyo haya madafu yetu,” Rwegasira alikazia.

    “Kwa madafu zinaweza kuwa ni shi'ngapi?” Muganyizi aliuliza.

    Rwegasira alicheka. “Piga hesabu mwenyewe uone. Utaniambia huyo ni milionea au bilionea kwa hapa kwetu?”

    “Kwa Tanzania ni bilionea,” Karumuna alikiri.

    “Na kwa Tanzania ,” Rwegasira aliongeza, “ukiwa na pesa kama hizo, ni rahisi kuinunua serikali. Ni huo uwezo wake wa kiuchumi unaonifanya nimwamini. Nadhani ni muhimu kuwasiliana naye ili azma yetu itimie. Kesho nitarudi mjini ambako nitampa maagizo Makela.”



    *****



    MAKELA alikuwa ni mfanyakazi katika ofisi ya Ubalozi wa Burundi iliyokuwa jijini Dar es Salaam . Kabila lake, Mhutu. Kama Sengiyumva, yeye pia alikuwa hakubaliani na utawala wa Rais Nkurunziza wa Burundi . Na alikuwa na ndoto kuwa siku moja Nkurunziza atatoka madarakani, iwe kwa uchaguzi wa kidemokrasia au kwa mtutu wa bunduki.

    Sengiyumva na Makela sio tu kwamba walifahamiana, bali pia walikuwa ni marafiki wakubwa. Na Sengiyumva aliwahi kumdokeza Rwegasira juu ya uhusiano huo. “ Kama una tatizo lolote kubwa jaribu kuwasiliana na Makela, naye atanitaarifu,” alimwambia.

    Kichwa cha Sengiyumva kilitawaliwa na uchu wa madaraka. Alihitaji madaraka ndani ya serikali ya Tanzania . Alihitaji madaraka makubwa japo siyo urais. Na hakuuhitaji urais. Alitaka kuwa waziri au mkurugenzi wa shirika moja zito ili aendelee kuneemeka kwa mbinu halali na haramu bila ya kubughudhiwa.

    Aliamini kuwa yote hayo yangewezekana kama serikali ingepinduliwa. Na ili hilo lifanikiwe angelazimika kuwatumia askari wa Jeshi la Wananchi, tena askari wa vyeo vya juu. Ndiyo maana alipokuwa Canada alithubutu kumshawishi Kapteni Rwegasira kujenga chuki ya kudumu dhidi ya serikali ya Tanzania.

    Lilikuwa ni pendekezo gumu kichwani mwa Rwegasira. Hakuwa radhi kuliafiki, lakini hakumtamkia bayana Sengiyumva. Jibu alilomwachia ni: “Tutaangalia.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni uchungu wa mauaji ya familia yake ndiyo ulioyafufua mawazo ya 'kuigeuka' serikali yake. Ni mauaji yaliyofanyika takriban mwezi mmoja tu baada ya kuzungumza na Sengiyumva.

    Siku iliyofuata aliingia katikati ya jiji saa tatu asubuhi. Moja kwa moja akaripoti katika ofisi za Ubalozi wa Burundi ambako alikutana na Makela. Wakaongea. Papohapo Makela akawasiliana na Sengiyumva aliyekuwa Bujumbura , Burundi .

    Rwegasira alipoondoka ofisini humo, tayari alikuwa na taarifa kuwa vifaa vilivyohitajika vingesafirishwa kwa siri kubwa hadi jijini Dar es Salaam , siku chache zijazo. Zilikuwa ni chupa tupu tano, chupa ndogo zenye hewa ya sumu kali aina ya PAK. Sumu hiyo ilikuwa na uwezo wa kuua ndani ya sekunde thelathini tu baada ya kunuswa.

    Matumizi ya sumu hiyo, ni kuiweka chupa mahali unapotaka kuangamiza watu au kiumbe chochote, kisha wewe unakuwa umbali wa mita mia moja kutoka hapo huku ukiwa na kifaa maalumu cha kielektroniki. Utakachopaswa kufanya ni kubonyeza kifaa hicho na kifuniko cha chupa kitafunguka hukohuko ilipo.

    Kitendo cha kufunguka kwa chupa hiyo ndicho kitakachosababisha madhara makubwa kwa kiumbe chochote kitakachonusa hewa iliyochanganyika na ile iliyotoka chupani.

    Mfano hai wa matokeo ya matumizi ya PAK ni ule uliotokea mwaka 1992 huko Kuwait . Chupa moja iliyofunguliwa kwenye uwanja mmoja mdogo wa micheazo ulisababisha vifo vya watu mia moja na hamsini ndani ya dakika mbili. Haikujulikana bayana chanzo cha matumizi ya sumu hiyo uwanjani hapo, japo baadhi ya tetesi zilidai kuwa aliyekuwa Rais wa Iraq wakati huo, Saddam Hussein alihusika kwa njia moja au nyingine kufuatia mgogoro uliokuwwepo miaka hiyo baina ya nchi hizo.

    Hazikuwa habari zilizothibitishwa kitaalamu kwa hali hiyo zikafifia taratibu kama zilivyo vuma kwa kishindo. Zaidi, serikali ya Kuwait ilipiga marufuku uingizaji wa sumu hiyo nchini humo huku ikitoa onyo kuwa yeyote atakayekiuka agizo hilo , atakumbana na mkono wa sheria, adhabu ya kifo ikiwa imepewa kipaumbele kwa atakayekumbwa na kadhia hiyo.

    Nchi nyingi duniani, hususan nchi kubwa ziliweka kipaumbele katika upigaji marufuku utengenezwaji, uuzwaji na utumiaji wa PAK. Lakini huenda pia ni hatua hiyo iliyoipa umaarufu sumu hiyo. Hivyo ikawa ikiuzwa kimagendo na kwa bei kubwa.

    Miongoni mwa nchi zilizopiga marufuku na kusimamia kwa dhati agizo hilo ni Tanzania , lakini ikatokea kuwa juhudi hizo hazikuzaa matunda pale alipozuka mwanamke mrembo mwenye shahada ya sheria, Scholastica Temu ambaye alifanikiwa kuipata kule alikoipata na kuwaua watu watatu bila ya kipingamizi.

    Kwamba PAK ni sumu kali sana , na inayotoa matokeo ndani ya dakika moja tu baada ya kuitumia ni sababu iliyowafanya akina Rwegasira waichukulie kama nyenzo madhubuti katika kuifanikisha azma yao .

    Alirudi katika pori la Bunju ambako aliwaeleza wenzake juu ya hatua iliyofikiwa. Akaongeza, “Kuanzia sasa tunaweza kujichimbia ndani ya jiji. Gharama ya kuishi huko ni juu ya Makela. Kazi yetu ni kuchagua hoteli tunayotaka.”

    “Kempiski...” Karumuna alisema.

    “Hapana,” Rwegasira alipinga haraka. “Hatupaswi kufikia hoteli yoyote yenye jina kubwa. Kumbukeni ishu hii ya kambini bado serikali inaitupia macho. Kwa vyovyote vile uchunguzi wa kina unafanyika. Ni aibu kwa serikali. Mataifa wahisani wanaweza kushindwa kuielewa na kuiamini serikali. Tukae tukijua tu kwamba hatupaswi kukaa kwenye hoteli yoyote yenye hadhi kubwa na jina kubwa kibiashara.”

    “Ni kweli,” Muganyizi aliungana naye. “Nadhani tungechagua hoteli isiyo na jina kubwa lakini yenye kila kinachostahili kufanywa angalau iitwe hoteli ya daraja la pili.”

    “Malick,” Karumuna alipendekeza tena.

    “Yes, Malick Hotel inafaa,” Muganyizi alikubaliana naye.

    “Lakini,” Muganyizi alidakia. “Hatutakwenda mjini na hizi silaha.”

    “Kwa hiyo tutaziacha huku?” Muganyizi alimtumbulia macho.

    “Ndio. Ni lazima iwe hivyo.”

    “Lakini bado kuna umuhimu wa kuwa na silaha,” Karumuna alisema.

    “Lakini siyo SMG,” Rwegasira alitikisa kichwa. “SMG ni mzigo. Tutazificha huku huku. Msihofu, kabla ya saa arobaini kila mmoja wetu atakuwa na bastola. Hilo siyo tatizo.”

    Siku hiyohiyo, saa mbili usiku walikuwa wakiteremka katika basi eneo la Morocco, Kinondoni na kukodi teksi iliyowafikisha Malick Hotel, Mtaa wa Jamhuri katikati ya jiji la Dar es Salaam. Hapo walikodi vyumba vinne huku kila mmoja akiwa ameandikisha jina bandia. Vyumba vitatu walivitumia kwa malazi, na vilikuwa ghorofa ya kwanza. Chumba cha nne kilikuwa katika ghorofa ya pili. Hicho kilitumika kwa mikutano yao ya siri. Hawakuongea lolote kuhusu mkakati wao mzito bila ya kuwa ndani ya chumba hicho.



    *****



    TAKRIBAN kila siku jioni wateja humiminika Malick Hotel. Wengi wao huketi katika vibanda vilivyoko nje na kujipatia vinywaji, na wachache huketi katika ukumbi wa baa.

    Siku hii, saa mbili kasorobo usiku, idadi ya wanywaji ilikuwa kubwa zaidi. Labda kwa kuwa zilikuwa ni tarehe za mwisho wa mwezi, siku ambazo wafanyakazi wengi huwa na hali nzuri kiuchumi mifukoni mwao.

    Maongezi yalishamiri katika kila meza, kila mtu akionyesha kufurahi. Hakuna aliyekuwa na muda wa kumchunguza mwingine aliyeketi katika meza nyingine, anayetoka au anayeingia. Kila mtu alikuwa pale kwa mambo yake, kila mmoja alijali yale yanayomhusu tu.

    Wakati gari jeusi, Land Rover Discovery lilipokuwa likiegeshwa katika eneo la hoteli hiyo, hakuna aliyelijali. Kwa ujumla hakuna aliyehisi wala kushuku chochote.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-

    Kijana wa Kirundi, Ndimukanwa Peter aliyetumwa rasmi na Sengiyumva kutoka Bujumbura alizima gari, akateremka na kuvuta hatua ndefu akienda ghorofa ya kwanza. Muda mfupi baadaye aliteremka akifuatana na Kapteni Rwegasira. Kwa dakika mbili, tatu waliketi humo garini wakizungumza. Kisha walitoka huku Rwegasira akiwa na kasha moja dogo ambalo kwa jinsi alivyolibeba ilionesha dhahiri kuwa ni zito.

    Wakapanda hadi ghorofa ya kwanza na kujitoma ndani ya chumba cha Rwegasira. Dakika kama thelathini zilizofuata walikuwa wakizichunguza bidhaa zilizohifadhiwa ndani ya kasha lile.

    Zilikuwa ni chupa tano, chupa zenye ujazo wa lita moja. Kilichokuwemo ndani ya chupa hizo ndicho kilichokuwa kiini cha mkakati wao, na walitegemea kuwa kingetoa matokeo ya kuridhisha.

    Hadi ilipotimu saa sita usiku, walikuwa wamefikia hatua ya mwisho kabla ya utekelezaji. Walikubaliana kuwa, siku ya tatu, saa nne asubuhi, chupa moja iwe imewekwa ndani ya jengo la PPF Tower katikati ya jiji. Katika muda huohuo, chupa nyingine ilipaswa kuwekwa ndani ya jengo la Millennium Tower eneo la Makumbusho na nyingine iwe ndani ya jengo la Ubungo Plaza .

    Kufuatia nguvu ya hewa ya sumu iliyomo ndani ya chupa hizo, haikuhitajika chupa kuwa karibu sana na binadamu. Umbali wa mita hamsini ulitosha kumdhuru binadamu. Hivyo popote itakapowekwa, kisha ikafunguliwa kwa kile kifaa maalumu, sumu hiyo ingeweza kuvutwa na pua ya kila aliye ndani ya jengo husika.

    Katika kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi, kijana Ndimukanwa Peter aliwakabidhi fungu la pesa, kila mmoja dola 50,000. Pia aliwapa bastola tatu kwa ajili ya kujihami kwa kikwazo chochote kinachoweza kutokea.



    *****



    SIKU ya pili ilikuwa ya kuyakagua kwa makini majengo husika. Ndio, ulihitajika umakini wa hali ya juu katika ukaguzi huo na hususan katika kuhakikisha kuwa kila patakapowekwa mtego wao, isitokee ukafyatuka kabla ya malengo yao kutimia. Kwa maana nyingine, ilipaswa kupatikana mahali pazuri ambapo chupa ya PAK itawekwa, na mtu yeyote asiyehusika asibaini kinachoendelea. Kwa ujumla ilitakiwa kuwekwa mahali ambapo jicho lisilohusika halikustahili kuifikia.

    Na baada ya kuhakikisha kuwa chupa hiyo iko kwenye mahali panapofaa kwa malengo yao , mhusika mkuu aliyeiweka chupa hiyo anapaswa kutoka ndani ya jengo na kuhakikisha kuwa yuko katika umbali unaozidi mita mia moja kisha anabonyeza kile kifaa maalumu cha kielektroniki na papohapo chupa hufunguka kule ndani na hewa yenye sumu kali ya PAK husambaa hewani.

    Karumuna, Muganyizi na Rwegasira walifanya zoezi hilo , na hadi ilipotimu saa 9 alasiri kila mmoja alikuwa ametekeleza majukumu yaliyomhusu. Wakakutana tena katika chumba kilekile na kufanya kikao cha mwisho huku kila mmoja akiamini kuwa hatua waliyofikia ni nzuri na hakuna kikwazo chochote, mbele yao .

    Naam, kila mmoja aliamini kuwa siku inayofuata Dar es Salaam itakiona cha moto, Tanzania itatikisika na dunia itaduwaa.

    “Itakuwa ni habari, zaidi ya habari ambazo mapaparazi wamekwishazipata, hususan mapaparazi hawa wa hapa Bongo,” Rwegasira aliwaambia wenzake. “Sasa wataachana na habari za EPA, sijui Richmond , na nyingine zilizokwishageuka sheria badala ya kawaida kutumika katika kurasa za magazeti na kutangazwa redioni na kwenye televisheni.”

    “Yeah, hata BBC wataichukulia kama habari kubwa zaidi ya itakavyokuwa,” Karumuna alisema.

    Ndikumana hakusema kitu, zaidi alitabasamu tu, tabasamu la kifahari huku akikuna kidevu chake chenye ndevu changa.

    “Jambo la muhimu ni kwamba,” Rwegasira alisema, “ Tanzania itaingia katika ramani za dunia ikiwa ni miongoni mwa mataifa yenye mauaji ya ajabu na ya kusikitisha. Hatutatofautiana na Palestina, Iraq, Afghanistan, Sudan na kwingineko.”

    Muganyizi akionekana kujiamini kupita kiasi, yeye hakutamka chochote, alitwaa tambuu kama kawaida yake na kuanza kuzitafuna taratibu, macho yake makali yakiwatazama wenzake kwa zamu.

    “Kilichobaki ni kujiliwaza,” Rwegasira alisema tena. “Kila mtu ana pesa. Tufurahi kwa kazi itakayofanyika kesho. Naamini ni kazi itakayotoa matunda mema, kazi itakayoiliwaza mioyo yetu kutokana na misiba iliyotupata, misiba iliyosababishwa na serikali kwa kujipa mzigo wa kulea wakimbizi, mzigo ambao sasa unamwelemea kila Mtanzania.”

    Hawakuwa na wasiwasi.

    Walijiamini.



    *****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    SAA tatu usiku, Muganyizi akiwa amechota dola 700 katika dola 50,000 alizokabidhiwa kama malipo maalumu kwa kazi iliyowakaabili, alikuwa akimalizia bia yake ndani ya baa ya Zanzibar katikati ya jiji. Baada ya kukabidhiwa kitita chake na Makela mapema mchana, hakutaka kupata usumbufu, baadhi alizibadili katika maduka maalumu ya kubadili fedha na kumiliki kiasi fulani cha pesa za Tanzania. Ndipo alipoagana na wenzake na kuamua kuingia katika baa hii ambayo mara nyingi hufurika watu jioni. Alikaa hapo kwa takriban saa tatu, akinywa bia yake taratibu huku akiwatupia macho baadhi ya akinadada waliokuwa mawindoni na akina kaka waliohangaikia kusaka riziki kwa wanaume wenzao.

    Hakuwa na dhamira yoyote ya kumdaka mwanadada yeyote aliye mawindoni au shoga anayejinadi. Alilijali suala lililompeleka hapo; kunywa bia tu. Lakini sasa alianza kupaona mahali hapo kama pamemkinai. Akaamua kuondoka. Alitoka na kukodi teksi nje ya baa hiyo.

    “Kinondoni,” alimwambia dereva huku akijipweteka kiti cha mbele.

    “Dereva akachangamka. Akakanyaga moto akielekea Kinondoni. Walipofika eneo maarufu la Kwa Manyanya, dereva akamwuliza, “Uelekeo upi, bosi?”

    “ Mango Garden .”

    Gari likashika Barabara ya Kawawa na muda mfupi baadaye likakata kulia na kushika Barabara ya Mwinjuma kabla halijaegeshwa nje ya ukumbi wa Mango.

    Eneo hilo lilikuwa limechangamka sana. Watu wengi walikuwa nje na wengine walikuwa ndani ambako kulisikika mirindimo ya muziki wa taarabu ulioporomoshwa na kikundi kimoja maarufu nchini.

    Muganyizi alikuwa ni mpenda starehe. Alipenda kunywa bia katika kumbi au baa maarufu, alipenda kuchukua wanawake warembo na kustarehe nao. Lakini yote hayo aliyapa kipaumbele pale tu pesa zisizo haba zilipokuwa zikimtembelea mifukoni.

    Kwa siku hii, pesa zikiwa tayari zimefanya ziara katika himaya yake, ndipo alipoamua kuja hapo Mango Garden kusaka kimwana mwenye mvuto mkali. Siyo kwamba asingeweza kujichukulia mwanamke yeyote kule Zanzibar Hotel, la. Kule walikuwepo wanawake wengi, na wengi vilevile walikuwa pale tayari kwa yeyote na tayari kwa lolote. Wao walikuwa wazi zaidi katika kuitangaza biashara yao .

    Kilichomkimbiza kule ni kutomwona mwanamke anayemvutia. Wengi, kama siyo wote walionekana kuwa ni wanawake hadharani lakini hawakuwa na sifa za mvuto. Kingine kilichomkera ni kwa mwanamke kumvaa bila ya soni na kumtamkia bayana kuwa yuko tayari kupanda ghorofani kupewa malipo maalumu.

    Alipenda kumtamkia mwanamke kuwa anamhitaji, siyo mwanamke amtamkie yeye, na tena kumtamkia kuwa 'anafanya biashara.' Hata kama ni biashara, hiyo ingekuwa ni siri ya mwanamke na ingezungumzwa baada ya kustarehe na kwa namna ya kipekee, yenye staha.



    Alikuja hapa Mango akiwa na imani ya kufanikiwa kumpata mwanadada wa kustarehe naye, mwanadada ambaye hata kama yuko tayari kwa lolote na kwa yeyote lakini asiwe na uwazi sana katika kuitangaza biashara hiyo. Mara kadhaa aliwahi kuhudhuria kumbi ambazo vikundi vya taarabu vilikuwa vikitumbuiza. Huko alikuta idadi kubwa ya waliofurika ni wanawake, tena wanawake wazuri, wenye sura za kuvutia na maumbo ya kutamanisha.

    Baadhi yao walikwenda humo kwa minajili ya kujiburudisha tu na muziki lakini wengine walikuwa na dhamira mbili, muziki na kuwanasa wanaume wasiopitwa na vipendezavyo. Mara kadhaa Muganyizi hakukosa kupata wanawake katika kumbi hizo.

    Ndiyo maana, usiku huu, akiwa na kitita cha kutosha mifukoni mwake aliamua kuingia hapo Mango Garden kusaka wa kumliwaza.

    Alikwenda dirishani na kulipa kisha akaingia taratibu, mikono mifukoni huku akiangaza macho huku na kule ukumbini. Wingi wa watu, na watu wenyewe wengi wao wakiwa ni wanawake ilikuwa ni taswira halisi iliyompa matumaini ya kufanikisha azma iliyompeleka hapo.

    Lakini hakuwa na haraka. Alikwenda moja kwa moja kaunta na kuagiza bia. Akanywa akiwa hapohapo kaunta huku akiwatazama waimbaji wa kikundi cha taarabu na mashabiki wa kike waliocheza wakinengua kwa umahiri kama vile hawana mifupa nyongani.

    Saa nzima baada ya kuingia humo hakuwa yule Muganyizi wa awali. Huyu alikuwa ni Muganyizi mwingine, Muganyizi ambaye pindi bia zaidi ya tatu zinapotambaa katika mishipa yake ya damu, uchu wa kujipatia mwanamke humwingia nafsini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog