Search This Blog

Sunday 19 June 2022

ROHO ZA KISHETANI - 5

 





    Simulizi :Roho Za Kishetani
    Sehemu Ya Tano (5) 


    SAA 3:45 iliwakuta Muganyizi na Karumuna wakiwa ndani ya kile chumba cha ghorofa ya pili, chumba maalumu kwa mipango maalumu. Boksi dogo lililohifadhi chupa tano za sumu kali aina ya PAK lilikuwa kando ya kimeza kidogo kilichokuwa nyuma ya mlango. Wakati huo alisubiriwa Rwegasira ambaye tangu jana alipoondoka alikuwa hajarudi. Ni yeye aliyetarajiwa kuja kukamilisha mpango akiwa na usafiri.

    “Tunazidi kuchelewa,” Karumuna alisema. “Kwanini tusingetumia usafiri wa Ndimukanwa?”

    “Haifai kutumia gari lile,” Muganyizi alijibu. “Usafiri wa kukodi ni mzuri, kwa kuwa hata kama mashushushu watakuja kushtuka baadaye, wataishia kuhangaika na madereva teksi pekee. Sisi tutakuwa tukitanua na Discovery bila kelele wala mikwaruzo. Umenielewa?”

    “Nimekuelewa. Lakini muda nd'o unazidi kuyoyoma kwa kasi. Kujali muda ni jambo muhimu sana . Mara nyingi kutojali muda huzaa madhara au hitilafu katika mkakati wowote mzito. Katika kipindi hiki, na tukiwa katika hatua za mwisho sana za utekelezaji wa maazimio, ni vizuri kwenda na wakati na kuwa makini kwa kila tulichokipanga.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni kweli,” Muganyizi alikiri huku akitazama saa ya mkononi. Kisha akaitoa simu mfukoni na kubonyeza tarakimu kadhaa na kuitega sikioni.

    Simu iliita bila ya kupokelewa kisha ikakata. Muganyizi alisonya na kuirejesha kwenye mfuko wa shati.

    “Vipi, yuko hewani?” Karumuna alimwuliza.

    “Yuko hewani lakini hapokei.”

    “Kuna tatizo gani?”

    Hakuna aliyekuwa na jibu. Walitazamana, kila mmoja akiwa na sura yenye maswali mengi yasiyokuwa na majibu.



    *****



    KAMA ilivyokuwa kwa Muganyizi jana, baada ya kila mmoja kukiweka kibindoni kitita kizito cha pesa, Rwegasira naye alitoka ki-vyake hotelini na kwenda Makumbusho. Huko kulikuwa na mtu, mwanamke mzuri ambaye uhusiano mzuri wa mapenzi baina yao ulifufuka na kushamiri pale tu Rwegasira alipokuwa na pesa mifukoni.

    Mariam, mwanamke mrefu, mwenye macho makubwa na umbo kubwa teketeke, hakuwa akijua kitu 'mapenzi’ ni mdudu wa aina gani. Alichojali yeye ni pesa. Kwamba alikuwa akiishi Dar es Salaam kwa mfumo huo haikuwa rahisi kwa kila mtu kubaini.

    Alikuwa ni mtu aliyejiheshimu, na kwa ule utaratibu wake wa kutoka kila siku asubuhi na kwenda maeneo ya katikati ya jiji hususan Posta, kuliwafanya watu wengi wamchukulie kuwa ni mfanyakazi wa serikali au kampuni fulani maarufu. Pia, mavazi na samani zilizorundikana katika vyumba vyake zilitosha kumweka katika daraja la walionazo na kwa hali hiyo baadhi ya watu walifikiria kuwa anapata mshahara mkubwa.

    Naam, alikuwa mzuri, na ni uzuri wake huo wa sura na umbile ndiyo ulioyavuta macho ya Rwegasira siku moja wakiwa ndani ya baa ya Katumba eneo la Mkwajuni Kinondoni na kuulazimisha urafiki kwa mbinu za kistaarabu.

    Urafiki huo ulidumu na kuzaa mapenzi na hivyo usiku wa siku hiyo ukawa wa kwanza kwao kukitumia kitanda kimoja kwa starehe yao . Lakini kama ilivyo kanuni ya Mariam, walifikia hatua ya kuwa pamoja usiku baada ya Mariam kudiriki kutaja ada maalumu ya kutoa huduma hiyo, jambo ambalo kwa Rwegasira 'mtoto wa mjini' halikuwa geni kwake.

    Walikubaliana.

    Huo ukawa mwanzo wa uhusiano wao, uhusiano uliodumu kufuatia utundu wa Mariam pindi kitanda kilipowalaki. Ni mapenzi yake kwa Mariam ndiyo yaliyomfanya hata siku hii aende huko Makumbusho ili aupitishe usiku kwa raha mustarehe.

    Waliachana saa moja asubuhi. Rwegasira akakodi teksi kurudi mjini katika hoteli ya Malick. Teksi hiyo ilipaki nje ya hoteli. Rwegasira alipoteremka alisimama kwanza na kuangaza macho kwa takriban kila aliyekuwa hapo. Macho yake yakampitia huyu na yule kwa wateja hao ambao baadhi yao walikunywa soda, maji ya matunda na wengine, bia.

    Hata teksi ilipoondoka, yeye hakuwa na haraka ya kuingia ndani. Aliisogelea meza moja na kuketi huku akiendelea kuwatazama kwa makini wateja hao. Hakupenda kujipa imani kuwa haiwezi kutokea dosari yoyote inayoweza kutibua mpango huo. Hapana.

    Aliijua Tanzania ilivyo makini katika masuala ya Usalama wa Taifa. Si ajabu wakati wakiwa katika hatua hizo za mwisho kabisa za utekelezaji wa mkakati wao, mambo yakatibuka. Ni hilo alilopaswa kujihadhari nalo.

    Hiyo ndiyo sababu iliyomfanya akae hapo walao kwa dakika moja apate picha ya kila mmoja aliyekuwepo. Hakuwa mjinga wala mbumbumbu, alikuwa na uwezo wa kuyasoma macho ya jambazi sugu, kibaka, mkware, mlevi hata mmbea. Vivyo hivyo alikuwa na uwezo wa kuusoma uso wa askari au mpelelezi yeyote anayeijua vilivyo kazi yake.

    Ni kipawa hicho alichojaaliwa na Mungu ndicho kilichomfanya ahisi jambo zaidi jambo mbele yake, jambo ambalo ni dhahiri lilikuwa katika hatari ya kuuharibu mpango wao.

    Hakushindwa kuzitambua nyuso za watu watatu walioketi katika meza tofauti katika eneo hilo . Mmoja alikuwa akinywa soda, sigara mkononi. Mwingine alikuwa akisoma gazeti, na watatu alikunywa bia.

    'Uwe makini, mambo ni magumu...' alihisi sauti ikimnong'oneza. Akaitii sauti hiyo kwa kuahirisha kwenda vyumbani waliko wenzake. Akataka kuchukua simu na kuwataarifu, lakini hilo nalo akaona kuwa halistahili, ni vizuri wakutane ana kwa ana.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Na katika kuhakikisha kuwa anapata picha sahihi ya hisia zake, na asije akaonekana mtu wa ajabu aliyekaa bila ya kinywaji au kilaji mbele yake, akaagiza toti kadhaa za pombe kali. Wakati huo akawa na kazi moja tu, kuwakagua kwa makini watu hao watatu aliowatilia shaka.

    Mmoja alionekana akiangaza macho huku na kule na kuonyesha dhahiri kuwa ile soda iliyokuwa mbele yake hakuijali. Mwingine, aliyekuwa na gazeti mkononi, asingempa shida mtu yeyote ambaye angekuwa na kazi ya kumchunguza. Kwa ujumla ni kwamba usomaji wake wa gazeti haukuwa usomaji wa msomaji makini. Hilo lilikuwa dhahiri pale alipojikuta akibaki amelishika gazeti hilo huku macho yake makali yakipita huku na kule na kwa huyu na yule kwa chati.

    Yule aliyekuwa na bia mbele yake, macho yake hayakutulia japo angehitajika mtu kama Kapteni Rwegasira kuweza kutambua hivyo.

    Naam, hali ilikuwa tete. Rwegasira aliiona dalili ya nuksi mbele yake. Akajipapasa mifuko na kuigusa bastola yake iliyosheheni risasi. Akashusha pumzi ndefu huku akitwaa glasi ya kinywaji chake na kuipeleka kinywani. Akagugumia kwa mkupuo na kuirejesha glasi mezani ikiwa tupu.

    Akatwaa sigara ndani ya pakiti, akaiwasha na kuvuta mikupuo miwili mikubwa. Akashusha pumzi ndefu na kuupitisha ulimi kwenye papi za midomo yake. Kisha akaendelea na zoezi lake la ukaguzi.

    Kwa sekunde chache alizowatupia macho wale watu aliowatilia shaka, alikuta kila mmojawao akimtupia jicho la siri. Hapo sasa akazidi kuzipa imani ya juu zaidi hisia zake za kuzingirwa na hatari.

    Papohapo akasimama na kujitoma ndani ya hoteli kwa mwendo wa kawaida mithili ya mtu yeyote asiye na wasiwasi wowote kuhusu hatari yoyote dhidi yake. Na safari hii hakusubiri huduma ya lifti, alizikwea ngazi mbili-mbili kwa haraka tofauti na alivyokuwa akitoka kule nje.

    Alipofika ghorofa ya kwanza aliingia chumbani mwake na kusita. Hakujua kilichompeleka humo. Akatoka na kuvivaa vyumba vya Karumuna na Muganyizi ambako alivikuta wazi. Akashangaa.

    Punde akakumbuka. Akatoka tena hima hadi ghorofa ya pili, akikimbilia chumba kile maalumu.



    **********



    KARUMUNA na Muganyizi walishtuka pindi mlango ulipofunguliwa kwa fujo na Rwegasira kuingia. Na siyo kwamba mshtuko huo uliwapata kufuatia namna Rwegasira alivyoingia tu, bali pia hata mwonekano wake ulitangaza jambo zaidi ya kile walichokitegemea kutoka kwake.

    “Vipi?!” Karumuna alimwuliza huku akimtazama kwa makini.

    “Kuna nini?” Muganyizi naye aliuliza.

    Rwegasira hakujibu papohapo. Aliufunga mlango na kuuegemea. Akawatazama wenzake kwa macho makali, jasho likiwa limejiunda katika paji la uso wake. “Kuna kitu,” hatimaye alisema kwa sauti iliyodhihirisha taharuki iliyomkumba.

    “Nini?” Karumuna alisimama na kumtolea macho.

    “Kuna jambo linanitia shaka,” Rwegasira alisema. “Kuna wanoko. Kuna wanoko wa Mwema wako hapo nje.”

    “Hapa hotelini?” Muganyizi alionekana kutomwamini.

    “Wako chini, pale nje,” sauti ya Rwegasira ilikuwa ya msisitizo mkali. “Sibahatishi wala sisemi kwa kuwashuku tu watu ovyoovyo. Nina hakika na ninachokisema. Tuchukue tahadhari. Mzigo uko wapi?” akimaanisha lile boksi lenye chupa tano muhimu kwa kazi iliyowakabili mbele yao .

    Hakuna aliyemjibu, zaidi macho ya wenzake yalitupwa kando ya kimeza kidogo ambako boksi hilo lilikuwepo. Rwegasira naye akalitazama boksi hilo . Kisha akahema kwa nguvu na kusema, “Sasa ni kufa na kupona. Ikibidi kuua, tunaua! Tukikubali kukamatwa na washenzi hao tujue wazi kuwa tutaozea jela.”

    Baada ya kusema hivyo aliitoa nje bastola yake na kuikamata kwa makini, mikono yake mikakamavu ikionesha dhahiri kuwa yuko tayari kuitumia wakati wowote kuanzia dakika hiyo.

    “Tusikubali kushindwa,” Rwegasira aliendelea kusema. “Tuhakikishe tunatimiza walao kiwango fulani cha malengo yetu. Kila mtu hapo alipo ana chuma, sio?”

    Karumuna na Muganyizi waliitika kwa kutikisa kichwa.

    “Zimejaa risasi?”

    “Nd'o maana'ake,” Karumuna alijibu huku Muganyizi akitikisa kichwa kwa mara nyingine, ikiwa ni ishara ya itiko.

    “Okay, tutoke,” Rwegasira alisema. “Na kwa hali ilivyo, tusijitie kuanzia PPF Tower . Hapo tutakuwa tumejiweka kitanzini. Ni rahisi sana kuzingirwa na kukosa pa kutokea. Inatupasa tuwe na hadhari kuwa mambo yakiharibika tunaliacha jiji ama kwa kutumia Morogoro Road au Bagamoyo Road . Kwa hiyo tukiwa maeneo ya katikati humu, hatutaweza kutoka.”

    Akameza mate na kuwasha sigara haraka. Akavuta mikupuo miwili, mitatu hivi ya nguvu na kuendelea: “ Twende Millennium Tower , Makumbusho na Ubungo Plaza . Tukiweza kutekeleza kazi yetu hata kwa jengo moja tu, itakuwa ni faraja kubwa. Bado itabaki kuwa habari kubwa duniani na historia nzuri kama ile ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba mwaka 1996 au kuanguka kwa treni iliyorudi kinyumenyume mwaka 2002 kule Igandu na Msagali, watu takriban alfu moja wakazima! ”

    “Vipi kuhusu usafiri?” Muganyizi aliuliza.

    “ Hilo sio swali,” Rwegasira alisema. “Umesahau kuwa tulishaachiwa Land Cruiser Discovery kwa ajili hiyo? Liko hapo nje. Switch ninayo, na liko full tank!”

    “Lakini si tulikubaliana kuwa tusitumie hiyo Discovery?” Muganyizi alimwuliza.

    “Lakini haikuwa sheria. Tulipanga hivyo, na kupangua hakuwezi kuathiri utendaji wetu.”

    “Lakini...”

    “Punguza maswali, Muganyizi. Twende!”

    Boksi lililokuwa na chupa tano za PAK lilishikwa na Karumuna. Wakatoka huku wakiwa makini, tayari kwa lolote.

    Tayari kuua

    Tayari kufa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    **********



    KILA mmoja alikuwa hapo kivyake. Salum alikuwa mezani, soda mbele yake, akiinywa kwa nadra sana . Kisu, yeye alikuwa na gazeti mkononi, mara chache akivisoma vichwa vya habari na kwa siri akiwatupia macho watu walioingia na waliotoka. Samba alikuwa na bia ambayo aliinywa taratibu katika hali ya kawaida kama mnywaji yeyote mstaarabu.

    Walikuwa hapo kwa kazi maalumu. Na hadi kufikia wakati huo walijua kuwa bado hawajapoteza kitu katika operesheni yao . Walikwishapata uhakika kuwa ndani ya chumba fulani, katika hoteli hiyo kuna watu wawili ambao wanashukiwa kutokuwa raia wema.

    Lakini pia walikuwa na taarifa ya uhakika kuwa kundi kamili la watu hao linatimiza idadi ya watu watatu. Mmoja hakuwepo, na hawakujua yuko wapi, na kama atarudi au hatarudi. Aidha, walikuwa na taarifa sahihi kuwa mmoja wa watu hao ndiye aliyemwambia Tina kuwa asubuhi ya siku hiyo walitarajia kufanya jambo zito litakalowapotezea maisha mamia ya Watanzania kupitia majengo kadhaa makubwa ya jijini Dar es Salaam.

    Wakati Rwegasira alipofika hapo haikuwa rahisi kwa askari hao wa kachero kutambua. Zaidi yake, wakati huohuo magari mengine matatu yaliegeshwa na watu kadhaa wakateremka, baadhi wakijumuika hapo nje na wengine wakiingia ndani. Rwegasira hakuteremka jirani sana na hoteli na hata alipoingia katika eneo hilo alichagua kiti pembezoni na kuketi jambo ambalo makachero hao hawakulitegemea sana kuwa lingeweza kutokea.

    Kitu kimoja ambacho makachero hao walikijua ni kwamba, wanalifuatilia kundi hatari, la watu wanaojua nini cha kufanya pale wanapogundua kuwa kuna hatari mbele yao . Ni makapteni wa jeshi waliohitimu katika fani mbalimbali za kijeshi, matumizi ya silaha na mikono zikiwa ni miongoni mwa nyenzo walizomudu kuzitumia pindi hatari yoyote inapojitokeza. Kwa hali hiyo, umakini ulihitajika.

    Wakiwa bado katika zoezi lao ndipo walipowaona watu watatu wakitoka ndani ya hoteli hiyo kwa mwendo wa asteaste lakini wakionekana kujiamini kwa kiwango kikubwa. Mmoja wa watu hao alikuwa ameshika boksi dogo lililofungwa madhubuti. Ni hapo ndipo walipojua kuwa kazi inaanza.

    Wakawafuatilia Rwegasira na wenzake walipokuwa wakiingia ndani ya gari, Land Cruiser Discovery.

    Makachero hao wakatazamana na mara nao wakalifuata gari lao na kulifuata lile Land Cruiser.



    **********



    MARA tu Rwegasira alipokwishakaa nyuma ya usukani wa Land Cruiser na kulitia moto, aliliondoa kwa mwendo mkali na kushika Mtaa wa Zanaki. Kasi yake hiyo ilimfanya achukue sekunde chache sana kuifikia Barabara ya Bibi Titi Mohammed.

    “Mliwaona wale wanoko?” Rwegasira aliwauliza wenzake.

    “Mi’ sijawaona,” Karumuna alijibu.

    “Hata mimi sikujali kuwatambua, mradi wewe ulishawaona na kujua nini cha kufanya basi akili yangu ilikuwa ni kutoka tu,” Muganyizi naye alijibu.

    “Mimi niliwacheki wakati tumefika nje na kutambua kuwa bado wanatufuatilia,” Rwegasira alisema. “Na, najua wana gari. Watatufuata. Cha muhimu ni kuwatoka tu, tena kwa mwendo wa kupaa.”

    Wakati akisema hayo tayari alikuwa akisubiri taa za Makutano ya Barabara za Bibi Titi na Morogoro. Na taa zilipowaruhusu, Rwegasira akaendeleza ubabe wake kwa kuliingiza gari hilo kwa makeke na kushika Barabara ya Morogoro. Akakanyaga moto kwa nguvu zaidi.

    Naam, mwendo wao ulikuwa wa kupaa.



    **********



    ASKARI maalum aliyekuwa eneo la Barabara ya Morogoro aliliona gari aina ya Land Cruiser Discovery likiendeshwa kwa kasi kama linaloelekea Magomeni. Alikuwa pale kwa lengo maalum. Na lengo hilo likiwa ni kulichunguza gari hilo .

    Papohapo akashika simu na kuwasiliana na Kachero Salum. “Limepita hapa...na wako katika spidi ya kufa mtu...”

    Kachero Salum hakuhitaji kuendelea kupokea taarifa hiyo ya simu. Alikuwa tayari akiwafuatilia akina Rwegasira. Lile Land Cruiser Discovery lilikuwa mbele yao , magari matatu yakiwa kati. Akawa makini akihakikisha gari hilo haliwapotei. Mfukuzano huo ukawafikisha kwenye makutano ya barabara za Morogoro, Mazengo na Msimbazi ambako taa za Usalama Barabarani zilikuwa zikiyaongoza magari.

    Land Cruiser ikalazimika kusimama, gari la makachero nalo likasimama nyuma yao . Foleni ikawa ikiongezeka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tunao!” Kachero Salum aliwaambia wenzake huku akiishika bastola mkononi na kufungua mlango.

    Wenzake nao wakatoka. Wakalifuata gari la akina Rwegasira haraka, bastola zikiwa mkononi mwa kila mmojawao.

    Walikuwa tayari kwa lolote, lakini pia hawakujua kuwa Rwegasira na wenzake wamejiandaa vipi kukabiliana na patashika hiyo.

    Wakitambua fika kuwa askari hao watawafuata baada ya kutoka kule Malick Hotel, Makapteni hao hawakuzilaza akili zao. Walikuwa makini na kuwa tayari kwa lolote.

    Tayari kuua.

    Tayari kufa.

    Hivyo, wakati askari hao walipoteremka kwenye gari lao, makapteni hao waliwaona na hawakutaka kupoteza muda.

    “Mlipue!” Rwegasira alimwamuru Karumuna akimaanisha ampige risasi kachero Salum aliyekuwa mbele.

    Bastola ya Karumuna ikafuka moshi, mlipuko ukatanda hewani. Watu waliokuwa kando ya barabara wakiwa na safari zao, walishtuka, wakagwaya. Kila mtu akakimbilia alikoona kuwa ndipo salama yake ilipo.

    Wakati huo Kachero Salum alikuwa ameshika bega lake lililojeruhiwa na risasi. Bastola ilikuwa imeanguka chini. Wenzake hawakukubali. Wakazitumia bastola zao. Risasi zikaivaa ile Land Cruiser kama mvua.

    Hatimaye kimya kikarejea. Kachero Samba na Kisu wakalisogea gari hilo kwa hadhari, bastola zikiwa zimewatangulia, mmoja akipitia kushoto na mwingine upande wa kulia. Samba ndiye aliyetangulia kulifikia gari hilo na alipochungulia ndani akamwona mtu akiwa ameegemea usukani huku matundu ya risasi yakionekana kisogoni.

    Huyo alikuwa ni Rwegasira, na haikuhitaji uthibitisho wa daktari kuwa tayari ni marehemu. Kushoto kwake aliketi mtu mwingine. Huyo ni Muganyizi na yeye alikuwa ameegemea kiti, katulia kama aliyesinzia lakini hakuonesha dalili yoyote ya uhai. Katika kiti cha nyuma kulikuwa na mwingine, Karumuna. Huyo alikuwa tofauti na wenzake. Risasi kadhaa zilipenya katika kisogo chake na kuufumua uso kiasi cha kuacha sura iliyotisha na kuchefua.

    Kando ya kiti hicho cha nyuma kulikuwa na boksi dogo lililofungwa vizuri, boksi ambalo baada ya kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi, na wataalamu kulifungua, ndipo ilipothibitika kuwa kulikuwa na chupa tano za sumu kali aina ya PAK, sumu iliyodhamiriwa kuwateketeza mamia kama siyo maelfu ya watu wasiokuwa na hatia.

    Naam, zilikuwa ni harakati za waasi, zilizokwama dakika ya mwisho.



    MWISHO 

0 comments:

Post a Comment

Blog