Simulizi : Usinibanie
Sehemu Ya Tano (5)
Muda mfupi baadae tukawa tukiingia barabara ya Bagamoyo
ambako jioni ile hakukuwa na foleni kabisa. Kagiza kalikuwa
kameshamiri.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliingia barabara hiyo kuu nikiendesha huku mpenzi wangu
Tausi kanilalia begani na mkono wake ukiwa pajani kwangu
akinifariji, dunia yote ilikuwa yangu. Muziki laini ulikuwa
ukiunguruma garini huku Lionel Richie akifanya vitu vyake
vya kiutu uzima. Kwa kweli ukijipanga pepo inashuka hapa
hapa bongo!
Ghafla wakati nalipita eneo la Tegeta, nikakutana na lori
lililokuwa likija kwa kasi usawa wa gari nililokuwa
nikiliendesha. Lilikuwa likilikwepa daladala lililokuwa
limeharibika na kusimama njiani.
Nikajaribu kulikwepa kwa kutoka nje ya barabara. Japo
tulikosa kugongwa uso kwa uso, gari langu likaserereka na
kupinduka kisha sikujua ni nini kiliendelea.
*****
Nilipokuja kuzinduka nikajikuta nimelala kitandani
hospitalini nikiwa na maumivu makali ya kichwa. Pembeni
yangu alikuwa amekaa mtu nisiyemfahamu, lakini hakuonekana
kama ni mtu mwenye masihara.
Hakukuwa na dalili yeyote ya kuwepo Tausi mule nilikolazwa,
nikaanza kuvuta kumbukumbu kuhusu kilichotokea lakini
sikuweza kukumbuka chochote cha ziada. Nikatulia pale
kitandani nikimkagua yule mtu ambaye muda wote alikuwa
akiniangalia bila kupepesa macho.
Japo sikuwa nikisikia pilika pilika zozote, mwanga uliokuwa
ukipenya dirishani ulikuwa ukiashiria kuwa ulikuwa ni muda
wa mchana. Akili yangu ilianza kufanya kazi haraka haraka
kujua la kufanya, lakini sikulipata.
Na hata ningelipata nisingeweza kulitekeleza kutokana na hali yangu ya kiafya.
Mtu yule hakuwa hata na utu wa kuniuliza kuwa najisikiaje,
na nilipomkagua vizuri nikaiona bastola imetulia kiunoni
mwake. Ni askari au mtu wa Mzee Nurdin?
Nilikuwa nimefunikwa shuka lakini nikaanza kuhisi ubaridi,
kwa kuwa nilifikiri kuwa hata kama ni askari bado kuna
uwezekano akawa ni mmoja kati ya wale wanaotumiwa na Mzee
Nurdin.
Kidogo akaingia daktari, alionekana ni muungwana sana
machoni na uso wake wa kilevi lakini sikutaka kumuamini
kijinga. Nikatulia kumwangalia ni nini anachotaka kukifanya
au kunifanyia.
"Habari yako bwana Musa Njiwa?" Aliniuliza kwa kulitamka
jina langu kwa ufasaha huku akitabasamu kipombe pombe.
"Najisikia vyema kidogo" nilijibu kwa upole katika sauti ya
utata ambayo isingemfanya ajue hali yangu kwa uhakika.
"Pole sana, ulijigonga tu kichwani lakini bahati nzuri
hukuumia kwa ndani" alinijibu akiniangalia kwa huruma.
Nilitamani kumuuliza kuhusu hali ya Tausi lakini nilisita
kwa sababu ya yule bwege pembeni yangu, sikumjua alikuwa
pale kwa sababu gani. Pia sikutaka kumuuliza daktari kuwa
lile jamaa ni nani na linafanya nini pembeni ya kitanda
changu na ni kwa nini hakumsalimia hata daktari.
Daktari akaondoka bila kunigusa wala kuongea lolote la
maana. Alipofika mlangoni alisimama kidogo, aliingia kiumbe.
Kisha yule daktari akaondoka zake baada ya wawili hao
kusalimiana kwa uchangamfu. Jua tu kuwa kiliingia kiumbe!
Alikuwa ni dada mrefu, mwenye sura nyembamba lakini alikuwa
na figa la kufa mtu, japo hakuwa mnene sana. Yaani kwa wale
wagonjwa wa mifiga ya kuchorwa vitabuni pale wangeweza
kuhonga hadi roho, manake mali tu zisingetosha kuwaridhisha
kama wamehonga. Alikuwa amevaa suti ya sketi fupi,
iliyoonyesha ni kwa namna gani kiumbe huyu amejaaliwa miguu.
Kifupi tu ni kuwa hakuna fundi wa mahesabu kama Mwenyezi
Mungu. Yaani kama binadamu mwili wake unapigwa kwa mahesabu
hapa vifaa vyote vya kupigia mahesabu vilikamilika, vibikari
bikari, rula bila kusahau kikokotozi cha kisayansi!
Alipofika tu yule, jinamizi aliyekaa pembeni yangu aliinuka
na kusimama mbali kidogo na kukipisha kiumbe kikae karibu
yangu. Sijui alikuwa akinifanyia makusudi? Aliingiza mkono
wake kunishika shingoni kwa karibu na kifua, sasa sijui
alikuwa ananipima joto tu au wazimu wake? Labda alitaka
nihisi mikono yake ilivyo laini.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pamoja na yote lakini bado akili yangu ilitaka kujua alipo
Tausi na hali yake. "Yule msichana niliyepata naye ajali ana
hali gani?" Nilimuuliza bila kumsalimia wala kutaka kumjua
kuwa ye ni nani.
"Tausi binti Nurdin?" Aliniuliza swali ambalo lilizidi
kunichanganya. Kwa swali aliloniuliza, na kutokana na uzoefu
wa kazi yangu, pamoja na ujuzi nilionao sikuwa na shaka kuwa
jibu atakalolitoa halingekuwa na ukweli wowote.
Niliamua kutotilia maanani jibu lenyewe, lakini kutokana na
jibu lenyewe ningeweza kuhisi kuwa wale ni kina nani na wana
lengo gani. Baada ya kujishaua shaua pale alipokaa huku
akijifanya kuwa ana huzuni sana, aliniangalia mithili ya
atafutaye namna ya kuongea.
Nilipomwangalia machoni nilijua wazi kuwa anajifanyisha,
aliniwekea ’uso wa plastiki’ huzuni ile haikuwa ya kutoka
moyoni. Akanieleza jibu nililolitarajia, "Tausi tumempoteza,
pole sana"
Japo nilitambua kuwa halikuwa jibu la ukweli, lakini mapigo
ya moyo yaliongezeka na nikajihisi kutetemeka mwili mzima
nikijiuliza, "vipi kama itakuwa ni kweli?"
Nilitaka kuwaridhisha na pia kujua hasa ni nini lengo lao,
hivyo baada ya kuniambia habari hiyo nikapiga ukelele kisha
nikafumba macho kujifanya nimepoteza fahamu.
Nikaanza kuzisikia pilika pilika zao, wakimkimbilia daktari.
Yule kiumbe ambaye nilikuja kulijua jina lake baadae, kuwa
ni Yolanda akawa akijitetea. "Mi nimemwambia tu yale maneno
ndio ikawa hivi" alirudia rudia sentensi hiyo mara nyingi,
hivyo ikanihakikishia kuwa taarifa aliyonipa haikuwa sahihi.
Ina maanisha kuwa alitumwa tu kuniambia maneno na sio kunipa
taarifa ya msiba wa Tausi. Moyoni nilifarijika kugundua kuwa
taarifa zile hazikuwa za kweli. Daktari aliwaambia waniache
kwanza kwa muda, hiyo ilikuwa ni nafasi nzuri ya kutafakari
kuhusu hatua za kuchukua.
Ila nilibaki na wasiwasi mmoja, wale ni akina nani na
wametumwa na nani? Pia nilikuwa na hamu ya kujua alipo
Tausi. Nilimsikia Yolanda akiaga, nikasikia pia miguu
mingine ikitoka. Nilijua wazi kuwa wametoka wawili bado
mmoja yupo na bila shaka ni yule jamaa.
Muda ulipopita sana nikafumbua macho, nikaliona lile jamaa
linazunguka zunguka huku limenipa mgongo. Nilijikohoza kama
nimepaliwa na mate ili ajue kuwa nimezinduka.
Jamaa liliruka ile mbaya likanigeukia, likichomoa bastola
yake kisha likawa limeishika mkononi kwa nguvu. Akabaki
kuniangalia huku akiwa katika taharuki, kwa hesabu za haraka
haraka nikagundua kuwa kuna jambo moja kati ya mawili. Labda
huyu jamaa ni mwoga sana au alipewa sifa zangu.
Nilimaliza kujikohoza nikatulia pale kitandani, akaniangalia
kwa muda kisha akaenda kujiegemeza kwenye kona fulani
akiichezea bastola yake mkononi.
Nikajua alikuwa anamaanisha nini. Ile ni ishara ya kuniambia
kuwa nitulie vile vile kwa kuwa yeye alichoamriwa ni
kuitumia bastola yake kwa lolote litakaloenda tofauti na
mpango uliopangwa.
Nikalihisi jasho jembamba likinichuruzika. Baada ya muda
mchache nililetewa chakula, ulikuwa ni mkate mkavu na soda,
fanta. Nilichekea moyoni kwa kuwa mlo ule ulinikumbusha
wakati nikiwa sekondari.
Ila nilielewa maana ya mlo ule, aliyekileta alikuwa anataka
kunihakikishia kuwa natakiwa bado niendelee kuishi. Alijua
kuwa angeleta kilichopikwa ningesita kula kwa kuhofia sumu.
Ila pia nilijua wazi kuwa kulikuwa na uwezekano wa kuweka
sumu ndani ya soda au kwenye mkate. Kitu ambacho kilinipa
moyo ni kuwa pale niko chini ya himaya yao hivyo hawana
sababu ya kuniwekea sumu kama kweli walikuwa na nia ya
kuniua.
Baadaye waliingia watu watatu walioonekana kuwa wameingia
kishari haswa. Yule jamaa aliyekuwa mule ndani alijiweka
sawasawa na bastola yake mkononi.
Nilikula haswa kwa kuwa njaa ilikuwa ikinitandika ila
sikutaka kuwaeleza watu wale nisiojua lengo lao. Nikabaki
pale kitandani nimejilaza, sikuweza kufanya ujanja wowote
kwa kuwa bado nilihisi maumivu mwilini pia sikujua pale
nilikuwa wapi na kulikuwa na ulinzi wa aina gani.
Nilitumia muda mwingi kujiuliza kuwa wale wametumwa na nani
japo kutokana na taarifa za kuhusu kifo cha Tausi nikahisi
kuwa wana lengo la kuniachanisha na Tausi.
Baadaye waliingia watu watatu walioonekana kuwa wameingia
kishari haswa. Yule jamaa aliyekuwa mule ndani alijiweka
sawasawa na bastola yake mkononi.
Nilipomsoma yule jamaa mwenye bastola nikajua kuwa alikuwa
na taarifa ya ujio ule kwa kuwa hakuonyesha mshtuko wowote
wale jamaa walipoingia. Walinivamia pale kitandani
walinikamata kwa nguvu, mmoja akinibana miguu huku mwingine
akinishindilia sehemu ya kifuani.
Sikutumia nguvu yeyote kuwazuia. Sio kwamba sikuwa na uwezo
wa kushindana nao bali matumizi ya nguvu katika sehemu kama
ile hayakuwa na tija, sana sana ningesababisha waniumize.
Walipoona sishindani nao wakajilegeza, ila ghafla mmojawapo
akatoa sindano na kunichoma.
Nikaona kiza kinene kisha nikapoteza fahamu. Sikukumbuka
tena kilichoendelea baada ya kuchomwa sindano ile.
Nilipokuja kuzinduka nilijikuta katika chumba chenye mwanga
hafifu, na pindi macho yalipozoea nikawa naona kila kitu kwa
ufasaha. Nilikuwa katika sehemu ambayo naifahamu fika na
nimeizoea. Kila ambacho nilikuwa nakiona kilikuwa vile vile
nnavyokijua.
Nilichanganyikiwa na mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi,
sikujua hasa ni nini kilikuwa kikiendelea. Pamoja na uzoefu
wangu katika kazi ya upelelezi hali ile ilikuwa inanitatiza,
na sikuweza kujua haswa ni nani aliyekuwa nyuma ya yale
niliyokuwa nikifanyiwa.
Lakini niliamini kuwa aliyekuwa akinifanyia vile hakuwa na
lengo zuri juu yangu na alikuwa ni mtu aliyenifuatilia kwa
muda mrefu na sasa niko chini ya himaya yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakuna kitu ambacho kinaniudhi kama mtu kuniendesha kwa
rimoti kontroo! Nilikuwa nyumbani kwangu, tena katika chumba
changu cha kulala. Nilikurupuka na kukagua sehemu zote mule
ndani.
Hakukuwa na chochote kilichoguswa kwa maana hiyo ni kwamba
nyumba yangu haikuwa imefanyiwa upekuzi wa aina yeyote.
Kilichofuata ni kwenda kwenye simu na kuangalia rekodi mbali
mbali.
Nikakuta Mkuu amenitafuta sana katika kipindi ambacho
nilikuwa kule nisikokujua bado kama ilikuwa ni hospitali ama
nyumbani kwa mtu.
Mara ya kwanza nilitaka kuamini kuwa Mkuu alinitafuta kweli
lakini kichwani mwangu kuna kitu kilikataa. Kilichonifanya
nisite kuamini ni jambo kuwa, Mkuu alinitafuta tu katika
kipindi ambacho sikuwepo.
Hii iliniashiria kuwa alijua nilipo na pia alijua
kilichokuwa kikiendelea. Nikaanza kukumbuka mambo mbali
mbali, kuhusu mkuu na maswali aliyokuwa akiniuliza hasa
baada ya utekwaji nyara wa Tausi.
Picha ikaja wazi kuwa haya yote yaliyonitokea yana mkono wa
Mkuu, ila ambalo bado lilinitatiza ni kujua sababu hasa ya
Mkuu kunifanyia vile.
Muda ulipita wa takribani saa sita, nikapokea simu toka kwa
Mkuu. Mkuu alinipa pole kwa ajali iliyotokea na akanieleza
wazi kuwa ni yeye aliyetuma watu wanitibie na kunirudisha
nyumbani. Alidai kuwa sababu kubwa ya kufanya hivyo ni
kunilinda.
Eti kwa kuwa kesi ya kumteka Tausi ilikuwa iko polisi
aliniepusha kuhusishwa na hivyo kunifanya nichafue faili
langu. Sikujua kama alikuwa ananiambia ukweli ama alikuwa
akitaka tu kunifariji kwa kuniweka roho juu juu kwa muda
mrefu.
Mwisho aliongea neno ambalo kwa kweli lilinikera. Kama neno
hilo lingetoka kwa mtu nisiyemheshimu, jibu lake lingekuwa
ni tusi la nguoni. Mkuu alinipa pole kwa kufiwa na Tausi,
eti anajua ya kuwa nilimpenda ila Mungu alimpenda zaidi.
Nilijikaza sana kumuitikia, sio tu nilijikaza kwa kuwa
namheshimu bali nilijikaza ili nimfanye aone ya kuwa
nimeamini kuhusu kifo cha Tausi.
Baada ya propaganda za Mkuu, niliamua kwenda ufukweni kukaa.
Sikuweza kuendelea kukaa mule ndani kutokana na kupata hisia
za Tausi kila mara. Niliazimia kumtafuta Tausi kwa udi na
uvumba hadi nimpate, lakini sikutaka kufanya papara.
Nilitaka wote waamini kwanza kama nalia msiba.
Nikaenda kujilaza ufukweni baada ya kutandika kagodoro
kangu, punde nikawa nimepitiwa na usingizi na mawazo
niliyokuwa nayo yakawa yakiendelea kwa njia ya ndoto.
Nilipata picha nzuri za Tausi ndotoni tena alikuwa amelala
kifuani kwangu tukipanga maisha.
Tena tulikuwa tukipanga kuondoka nje ya nchi ili kuondoa
gozi gozi. Nilihisi mipapaso ya Tausi. Lakini kadiri muda
ulivyokuwa ukienda mipapaso hiyo ilikuwa ikihisika
kiuhalisia. Nikashtuka!
Kuangalia pembeni yangu alikuwa mtu, mwanamke mwenye
mipapaso ile niliyodhania kuwa ni ya ndotoni. Lakini hakuwa
Tausi. Na maeneo yake nilikuwa peke yangu, nikajua sasa ni
mambo yale yale ya mpenzi jini! Nikainua uso kumtazama.
Alikuwa Yolanda, yule binti mwenye figa iliyofigika!
Nikakurupuka na kukaa chini, akabaki ananiangalia huku
akitabasamu. "Umeshtuka?" aliuliza swali ambalo jibu lake
aliliona kwa macho yake. Sikumjibu chochote.
Sio tu kwamba sikumjibu chochote kwa sababu jibu analo bali
kuna kingine cha ziada! Sijui alivaaje yule binti! Jamani
wakina dada wengine ni wachokozi, huwezi kuamini.
Si unakumbuka nilikudokeza kuhusu figa yake? Bali alikuwa
amenivalia kiufukweni ufukweni, japo alipendeza sana lakini
zaidi alikuwa anatamanisha.
Nikajikuta nikimuomba baba aliye mbinguni aniepushe na
kikombe kile ila siyo kwa mapenzi yangu bali nilitaka
mapenzi yake yatimizwe. Nikajikuta akili inanizunguka
zunguka kama saa mbovu, mara inatembea, mara inasimama.
"Unanitakia nini mwali wewe?" nilijikuta nikimuuliza kizee
zee.
Alibakia akicheka bila kutoa jibu la uhakika. Nikajikuta
nikimuuliza tena swali ambalo hata mwenyewe nilikuja
kujistukia baadae kuwa lilikuwa ni la kibwege. Eti
nilimuuliza amefikaje pale. Yaani ni kama vile nilikuwa naye
sehemu kisha nikamtoroka!
Mwisho nikaamua kukaa kimya ili akili ikae kwenye mzunguko
wake wa kawaida maana nilijiona kuwa nazidi kuchemka. Baada
ya muda kidogo kupita, akanieleza sababu ya yeye kuwa pale.
Kwa haraka haraka sikuweza kujua Mkuu ananitakia nini?
Eti yule binti ndio kateuliwa ili awe msaidizi wangu na
kaamriwa aje kunisaidia pale nyumbani hadi nitakapopona
vizuri.
Yolanda kumbe ni askari mpya ambaye yuko katika hatua za
mwisho za mafunzo ya upelelezi, na kutokana na alivyo
anaandaliwa kwa ajili ya kupewa kazi maalum.
Najua lengo la Mkuu sio kwamba mimi nianzishe uhusiano wa
kimapenzi na binti huyu bali anafikiri kuwa nimeathirika
kisaikolojia kwa ajili ya Tausi.
Nikatupa tena jicho kumtazama Yolanda, nikajikuta
nikimuamrisha. "Twende kwanza nyumbani."
Yolanda alinitazama kwa jicho la kurembua, kisha akajiinua
taratibu tukaanza kuondoka kuelekea nyumbani kwangu ambapo
ni hatua chache toka pale ufuweni nilipojilaza.
Tukaongozana kimya kimya huku akili yangu ikiwa haijui
inafikiria kitu gani. Tukafika kwangu, nilikuwa mbele ya
Yolanda. Wakati naelekea mlangoni nilishtushwa na jambo.
Kulikuwa na mtu amekaa katikati ya bustani iliyoizunguka
nyumba yangu. Alikuwa ni mgeni machoni pangu lakini
hakuonyesha kama yuko kishari au kiheri, alikuwa yupo yupo
tu haeleweki.
Wakati nikimshangaa, Yolanda alikurupuka na kumkimbilia.
Jamaa akasimama kumpokea, na kilichofuata ni mmiminiko wa
mabusu mithili ya waigizaji wa filamu za wamarekani weusi.
Nikabaki nawashangaa.
Kimsingi nilikereka. Sikukereka kwa sababu wanayafurahia
mapenzi yao, bali ilikuwa kama wananikoga kwa kuwa niko
mpweke bila Tausi.
Yolanda akanigeukia, "bosi huyu anaitwa Jovin, ni boifrendi
wangu. Yeye anakujua". Nikamkenulia meno kumuonyesha
tabasamu feki, ’la kichina’, lakini laiti angujua moyoni
nimekereka namna gani, asingethubutu kunijibu kwa kukenua
meno yake.
"Kwa hiyo bosi mi naomba niende, nitaripoti kesho asubuhi"
aliniaga Yolanda utafikiri mi ndiyo nilimpa kazi ya kuja
pale kwangu kuleta gozi gozi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nadhani usije tena, nahitaji kuwa peke yangu kwa siku mbili
tatu ili nipate muda wa kutafakari mambo yangu" nilimwambia
kikauzu kauzu mbele ya bwana ’ake.
"Samahani bosi, mkuu aliniambia nisiache kuja hata siku moja
hadi pale atakaponipa maagizo mengine." Alitoa maelekezo
utadhani nilitaka kuyajua yote hayo.
Usiku wa siku hiyo sikupata usingizi kabisa kutokana na
panga pangua iliyokuwa ikiendelea kichwani mwangu. Yote
ilikuwa ni katika mpango wa kumrudisha Tausi kwenye himaya
yangu. Ilipofika saa kumi alfajiri, kausingizi katamu kakanipitia.
Saa nne kasoro dakika chache usingizi ulikatika.
Nikakurupuka na kuingia bafuni, kisha nikajiandaa fasta
fasta kwa ajili ya kutoka japo sikujua nataka kuelekea wapi.
Nilipotoka kitu cha kwanza kukiona ni mapaja ya Yolanda.
Alikuwa kajilaza kwenye kochi dogo lililo nje ya nyumba
yangu kainyanyua miguu juu kiasi cha kuifanya sketi yake
ipande.
Kwanza nilidhani amepitiwa na usingizi hadi niliposogea
karibu yake, alikuwa akiniangalia akitapasamu. Kwa tabia
zetu wanaume ningeweza kubadili mawazo pale pale na kuanza
kuchombeza, lakini kutokana na weledi wangu nilijua kuwa
anataka kucheza na akili yangu.
"Natoka, na unisubiri hapa hapa" nilimwambia nikichomoka
haraka haraka kuongozea njia ya kuondokea bila gari. Kabla
hajajiinua pale chini nikawa nimeshatoweka. Nikaenda
kujibanza sehemu.
Baada ya dakika kama mbili tatu, nikamuona Yolanda akipita
kwa kasi. Alipopita tu, nikarudi nyumbani haraka, nikabadili
nguo kisha nikajilaza kitandani nikiendelea kupanga mikakati
ya kumrudisha Tausi wangu.
Yalipita takribani masaa saba ya utulivu. Ghafla nikasikia
pilika pilika za miguu zikiingia nyumbani kwangu, nikafunua
dari nikadandia na kuingia humo. Mara miguu ikaingia
chumbani kwangu.
"Jamani huyu Musa ana nini?" aliuliza mtu mmoja huku wenzake
wakikaa kimya bila kumjibu. Baada ya kuridhika na upekuzi
wao wakaondoka huku wakishauriana kwa kunong’ona.
Nikateremka na kurudi kitandani.
Ilipofika moja kasoro, giza likianza kuingia nikawa nasikia
sauti kwa mbali kama mtu anayelia. Nikatoka nje kwa
tahadhari kubwa, nikamkuta Yolanda kajiinamia akilia.
Nikamuangalia kwa muda.
"We binti!" nilimuita kwa sauti ya upole. Yolanda alishtuka
sana akageuka kuniangalia.
"Pole, nilikuwa nakukuza katika kazi yako" Yolanda
akakurupuka na kunikumbatia kwa muda, akilia.
"Wameniambia kuwa nisingekupata wangenipa adhabu na
ingenichafulia faili langu. Nashukuru umerudi, ulikuwa
wapi?" aliniuliza akiwa kama aliyepagawa.
Nilimruhusu aende baada ya kuongea naye kwa muda nikimueleza
kuhusu masuala ya kazi na namna ya kukabiliana na hali kama
ile. Tuliongea mengi kwa kuwa nilishayakomesha maigizo yake
ya kujifanya kahaba, ’kujikahabisha’.
Zilipita siku kadhaa za kuelewana na Yolanda, sasa tulikuwa
kama mtu na kaka yake. Heshima ilichukua mkondo wake,
nikatumia siku hizo kumuelezea namna Tausi alivyo na nafasi
katika maisha yangu.
Alinionea huruma sana, lakini hakuwa na namna ya kunisaidia
kwa kuwa kumbe hata Tausi mwenyewe hamjui. Alikuwa
akishindiliwa maneno tu ya kuropoka naye akawa anayatoa kama
kasuku.
Kutokana na mazoea yangu na Yolanda na kwa sababu niliamua
kumsaidia katika kumuimarisha katika kazi hii ngeni kwake,
akawa ananisaidia kutafuta taarifa za Tausi. Na hata
nilipokuwa natoka kufuatilia baadhi ya taarifa kuhusu Tausi,
hakuwa akinitilia umbeya.
Baada ya siku kadhaa, nikawa nimepata taarifa kuwa Tausi
alikatiwa tiketi ya kuelekea Ujerumani kupitia Kenya, lakini
nilipofuatilia nikapewa taarifa kuwa alipofika Kenya alirudi
Tanzania kupitia njia ya barabara akitumia jina la bandia.
Hatimaye kwa kuunganisha unganisha taarifa mpya na zile
nilizozipata kwa Mzee Nurdin nikagundua kuwa Tausi atakuwa
kati ya miji ya Kilosa au Iringa. Huko ndiko kuna nyumba za
kisasa zaidi za Mzee Nurdin ambazo hata mwenyewe huzitumia
kwa mapumziko.
"Lazima nifunge safari nikamtafute" nilimwambia Yolanda
jioni moja tukiwa pale nyumbani kwangu. Yolanda aliniambia
ugumu wa mimi kuondoka pale nyumbani kutokana na amri
iliyotolewa na Mkuu.
"Huwezi kwenda popote Musa Njiwa. Ni amri!" alinijibu Mkuu
baada ya kumvaa kuomba ruhusa ili nisafiri kwa mapumziko
mafupi japo moyoni nilijua ninapotaka kwenda.
Kwa mara ya kwanza nikaiona kazi ya upelelezi ni kazi ya
kitumwa, na sikuweza kuvumilia tena kuishi katika hali ile.
Nikafanya uamuzi ambao hakuna aliyeutegemea.
Niliandika barua ya kuacha kazi kwa masaa ishirini na nne,
nikalipa na mshahara wa mwezi mmoja. Toka hapo vikaanza
vikao mfululizo kujadili kuhusu uamuzi wangu huo.
Baada ya kukabidhi kila kitu nikarudi nyumbani kwangu na
kujiandaa kwa safari. Ghafla gari mbili zikawasili nyumbani
kwangu, nikachukuliwa msobe msobe nikaenda kutupwa rumande.
Niliwekwa ndani kwa takribani siku saba nikitolewa kwa
vipindi tofauti kwa mahojiano, lakini haikusaidia kitu.
Katika kipindi chote hicho kwa msaada wa Yolanda, ofisini
walijua kuwa nishaachana na habari za Tausi.
Siku niliyotolewa rumande, niliambiwa na wasaidizi wa Mkuu
kuwa naruhusiwa kusafiri kwa siku zisizozidi saba lakini
niliwajibu kuwa sisafiri kokote na hatanikisafiri sitahitaji
ruhusa ya mtu yeyote kwa kuwa nimeshaacha kazi.
Mkuu alipofikishiwa taarifa, aliwaambia waniache nifanye
ninavyotaka kwa muda fulani ila waangalie mienendo yangu.
Kama kawaida umbeya ukanifikia kupitia kwa Yolanda. Ilikuwa
rahisi kwa Yolanda kupata taarifa kutokana na urembo wake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya siku kama nane za kufanya mazoezi ya nguvu,
nilijifunga kwa safari. Kwanza nilitengeneza utaratibu
fulani ambao uliwarahisishia wanaonifuatilia, niliwataka
wajue naamka saa ngapi naelekea wapi na usiku nalala saa
ngapi.
Siku niliyosafiri niliingia kulala kama kawaida, ilipofika
saa nane za usiku nikafungua dirisha langu ambalo huwa
nalitumia kama mlango wa dharura. Nikatoka na kulifunga.
Nilipita njia ambayo niliibuni kwa ajili ya kuitumia kwa
safari za dharura ambazo sikutaka yeyote ajue. Nikatokea
barabarani na kuianza safari yangu nikianzia na Kilosa.
Usiku mmoja tu ulitosha kujua kuwa Tausi hakuwepo katika mji
ule. Alfajiri nikasafiri hadi Mikumi ambapo nilidandia lori
mpaka njia panda ya kwenda Iringa mjini. Nikakaa pale hadi
usiku, nikakodi taxi hadi mjini.
Ilikuwa yapata saa nne za usiku wakati napita maeneo ya
stendi kuelekea Makanyagio. Taxi likaniacha karibia na geti
la Chuo Kikuu kishiriki cha Ualimu Mkwawa. Lengo lilikuwa ni
kumfanya dereva ahisi kuwa mimi ni mwanachuo.
Ilinichukua takribani masaa kumi na nane kuitambua nyumba ya
Mzee Nurdin sehemu za Kihesa. Kwanza niliihisi nyumba fulani
iliyoko katika mlima wa Wilolese, ikanipotezea karibia masaa
mawili kabla sijagundua kuwa sio yenyewe.
Baada ya kuhakikisha kuwa nyumba niliyoihisi ndiyo ya Mzee
Nurdin nikaanza kupeleleza mambo kadhaa ya msingi. Baada ya
kupata kila nilichokihitaji, niliondoka ili nikajipange.
Nilichukua chumba katika gesti moja ya uchochoroni sana
ambako ni mwenyeji tu anayeweza kupajua. Nikatumia muda
mrefu kulala kisha nikaamka na kuanza maandalizi nikijiweka
tayari kwa lolote.
Niliporidhika na maandalizi, nikaanza safari ya kwenda kwa
Tausi. Baada ya dakika kama kumi na mbili hivi nikawa mbele
ya nyumba ya Mzee Nurdin. Nikawaona walinzi wawili wakiwa
getini.
Nikaizunguka nyumba, nikaruka ukuta kuingia ndani. Nikatulia
kwa muda kisha nikatambaa hadi nikaufikia mlango wa uwani,
nikauchokonoa ukafunguka, nikaingia na kuurudishia.
Nikatulia kimya kwa muda kusoma mizunguko ya mule ndani.
Ilionekana kuwa kuna watu wasiozidi watatu akiwemo Tausi
mwenyewe na wote walikuwa ni wanawake. Nikanyata taratibu na
kuingia chumba kimojawapo nikaacha barua niliyoianda, juu ya
bahasha nikaandika jina la Tausi.
Nikatoka taratibu nikaondoka zangu. Katika barua ile
nilimjuza kuwa nipo katika mji ule kwa ajili ya kumfuata
yeye. Nikamuelekeza nilipofikia, japo nilimdanganya lakini
angekuja angenikuta.
Baada ya masaa kama mawili, lilifika gari moja lenye namba
za serikali. Wakashuka jamaa wawili waliovalia suti nadhifu,
wakaingia ndani kisha wakatoka baada ya dakika kama kumi
hivi wakiongozana na Tausi na mlinzi mmoja.
Wakaingia ndani ya gari kisha gari likaondoka. Nikaanza
kulifuatilia kwa nyumba nikitumia taxi nililokodi.
Mwisho wa safari ya gari la kina Tausi ilikuwa pale
nilipomwelekeza. Walitangulia kuteremka mlinzi na mmojawapo
wa wale jamaa wakaenda kukaa sehemu ya baa ya ile hoteli
niliyomwelekeza, kisha akateremka Tausi.
Nikaliruhusu taxi liondoke, nikaandaa ujumbe mwingine haraka
na kuuweka katika bahasha. Wakati huo Tausi alikuwa
akielekea mapokezi ya hoteli ile, akaulizia akaambiwa kuwa
ni kweli nimechukua chumba pale ila nimetoka.
Tausi akatafuta sehemu ya kunisubiria akaenda kukaa. Nikampa
mtu ampelekee mhudumu mmoja aliyeko mapokezi kisha nikatuli
a sehemu nikiangalia mchezo.
Yule mhudumu alielewa maagizo akampelekea Tausi moja kwa
moja. Nikaondoka baada ya kuona Tausi anakabidhiwa ile
bahasha na anaifungua. Niliandika..
’Mpenzi Tausi, nimefurahi kwa kuwa nimekuona tena ukiwa na
afya njema. Ila nimefurahi zaidi kwa kuwa umeitikia mwito
wangu japo msafara uliokuja nao sikuupenda. Sina na wala
sijawahi kuwa na nia ya kukudhuru, huna sababu ya kuniwekea
mitego. Nakupenda sana’
Sijui alifanyaje lakini baada ya kuupata ule ujumbe.
Nilitoka pale haraka haraka nikarudi nyumbani kwa Tausi,
nikaingia ndani. Nikakagua vyumba vyote wakati huo wale
watumishi walikuwa sebuleni wakiangalia TV.
Kitu ambacho nilikisoma na kikawa kikiniumiza kichwa ni
kuwa, Tausi anaonekana yuko tofauti mno. Yaani muonekano
wake ni kama wa mwanamke aliyekuwa anamuamini mumewe kisha akamfumania, tena na shoga yake.
Nilikigundua chumba cha Tausi mule ndani, nikaingia na
kutulia kimya mule ndani. Harufu ya mule ndani ilirudisha
kumbukumbu zangu mbali mno, nilikumbuka siku za mapenzi
yangu na Tausi. Nikajikuta nasinzia.
Mlio wa gari ulisikika nje, kisha pilika pilika za watu
zikaendelea kwa muda. Baada ya hali kutulia, mlango wa
chumbani kwa Tausi ulifunguliwa.
Niliruka na kujibanza sehemu. Tausi akaingia na kuufunga
mlango kwa ndani. Alionekana kuwa na wasiwasi sana,
akajitupa kitandani kukaa. Nikajitokeza na kuwahi kumziba
mdomo ili asije akapiga kelele kwa woga.
Tulibaki tunaangaliana kwa muda, ila kwa mitazamo tofauti.
Tausi alionekana kuniangalia kwa chuki ya hali ya juu
tofauti na mimi niliyekuwa nikimwangalia kwa mapenzi.
"Kuna nini mpenzi wangu?" niliufunua mdomo wangu na kuuliza kwa sauti ya upole. Tausi alibaki kimya akiniangalia huku machozi yakianza kumtiririka. Nilimsogelea na kukaa karibu yake.
"Kaa mbali na mimi tafadhali. Sipendi kujihusisha chochote
na wewe, nakuchukia Musa," alitamka maneno ambayo yaliuchoma moyo wangu hasa. Nilikaa kimya kwa muda nikiyatafakari maneno yale ambayo kwa
hakika yalionekana kumtoka moyoni.
"Sumu gani umelishwa mpenzi wangu?" niliufungua mdomo hatimaye.
"Sikiliza Musa, najua kama ulikuwa pale kumpeleleza baba
yangu na ulianzisha uhusiano na mimi ili upate urahisi wa
kutimiza kazi yako, bahati mbaya ukanogewa na mimi. Kazi
yako imeisha unanifuatia nini? Ukipata kazi nyingine,
utapata mwanamke mwingine." aliongea huku akitokwa na
machozi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ni kweli nilikuwa nikimpeleleza baba yako. Na ni kwa sababu
anahusika na usafirishaji wa watoto nje ya nchi, watoto
ambao wanaenda kutumikishwa kitumwa na wengine kuuliwa na kuchukuliwa viungo vyao kwa ajili ya matibabu ya matajiri.
Kwa hilo hata ningeamriwa nimpige risasi baba yako
Ningemuua," nilimwambia kwa sauti ya kumaanisha.
Niliendelea kumwambia, "bahati mbaya niliangukia penzini
kwako nikiwa kazini. Nilijitahidi kupuuza hisia zangu lakini
nilishindwa na hadi leo nashindwa kuzipuuza hisia zangu
ndiyo maana niko hapa. Nakupenda sana Tausi na nahitaji
nimalize maisha yangu na wewe."
"Kwa kifupi fanya kama hakijawahi kutokea kitu kati yetu na
nataka uondoke sasa hivi kama ulivyoingia. Neno lolote
utakaloongeza nitapiga kelele, na usidhani kuwa natania"
aliongea kwa sauti ya upole iliyojaa chuki akiwa
haniangalii.
Nilimwangalia binti yule mrembo kwa muda, akageuka
kuniangalia, moyo wangu ulikuwa unalia lakini tabasamu
lilikuwa halijafutika usoni. Nikajiinua taratibu na kuanza
kuondoka bila kusema neno.
Siku hiyo ilikuwa ngumu sana kwangu. Nilirudi nilipofikia
kama nimetoka msibani, tena kwenye msiba wa mtu anayenihusu kwa karibu. Usiku huo huo wa siku hiyo ndipo nilienda kumrushia maneno Tausi.
*********
Nilikaa, nikatafakari kwa muda mrefu. Nikaamua kusafiri
kuelekea sehemu yenye utulivu ili niweze kupata akili mpya,
niweze kujitafuta.
Nilichagua kwenda Kilwa ambako nilikaa kwa takribani wiki
tatu. Iliniwia vigumu kuweza kumsahau Tausi lakini hatimaye
nilimchukulia kama historia.
Nilirudi jijini Dar es Salaam nikiwa mpya kabisa. Sikutaka
tena kuendelea na kazi lakini kichwa changu kilikuwa
kimetulia tayari kwa majadiliano yeyote.
Niliporudi nikaripoti makao makuu ili kujua hatma ya barua
yangu, lakini nilichokikuta pale kilinistaajabisha. Nilikuta
barua ya likizo ya miezi sita, mshahara niliolipia notisi,
na malipo mbalimbali yanayoambatana na likizo.
Kwa kweli sikuweza hata kujaribu kupinga, nilijua kuwa
endapo ningeleta ubishi wowote ningeonekana mkorofi na hatua
zozote za kinidhamu ambazo zingechukuliwa dhidi yangu
zingekuwa sahihi.
Upweke ndugu yangu,upweke! Nilianza kuhisi upweke wa hali ya juu, nikaamua kutafuta binti wa kuniondoa upweke ikiwezekana kuoa kabisa japo kutokana na majukumu ya kazi yangu ilibidi nimpate mke ambaye ni mwelewa hasa.
Yolanda?! Hapana. Pamoja na urembo wake wote lakini Yolanda hakuwa ananivutia kimapenzi, sijui ni kwa nini. Ila nahisi kwamba ana tabia feki, hayuko halisia na mimi na wanawake ‘waigizaji’ ni vitu viwili tofauti.
Nilianza kupanga orodha ya wasichana ambao nimewahi kuwa nan uhusiano nao, nikaanza kuwahakiki mmoja baada ya mwingine.
Nikajikuta kama Marehemu John Mgema na wimbo wake wa
wachumba thelethini.
"Nimeamua kuwa mpya, nataka mahusiano mapya" nilihitimisha na kuanza kujiandaa kutoka. Nilipanga kutembelea sehemu mbalimbali na kujichanganya na watu ili nizidishe fursa za kuanzisha uhusiano mpya.
Baada ya miezi kama miwili hivi ya kutoka na wasichana
mbalimbali nikajionea upuuzi, nikaamua kuachana ma kwenda
mbio. Niliamua kuweka akili yangu yote katika hali kufikiria
masuala ya kiuchumi zaidi.
Jioni moja nilikuwa ufukweni karibu na nyumba yangu,
nilikuwa nimejilaza kwenye kigodoro changu cha ufukweni
nikitafakari mambo yangu. Ilikuwa yapata mwaka mmoja toka
nilipoamua kuachana na habari za kutafuta mwenza.
Simu yangu iliita. Alikuwa ni Omar, moja kwa moja nikajua
kuwa ni kimeo maana urafiki wetu na Omar ni wa kukumbukana
kwenye vimeo tu.
Toka siku ile nilipomhadithia kuhusu Tausi, tulikuja kuonana
siku moja tu makao makuu na hatukupata muda wa kuongea kwa kuwa kila mmoja alikuwa bize na ishu zake. Nikaipokea!
"Njoo haraka Uwanja wa Ndege" alisema Omar na hapo hapo simu ikakatika. Sikuwa na muda tena wa kupoteza, nilijua kuwa
Omar yuko kwenye tatizo kubwa kwa kuwa simu yake haikuwa
ikipatikana tena. Nilikurupuka kujiandaa, baada ya dakika ishirini na tano nilikuwa uwanja wa ndege. Nikaulizia kama kuna tukio lolote lisilo la kawaida, nikaambiwa hakuna.
Nikaanza kumtafuta Omar kwenye sehemu ambazo nilihisi angekuwepo. Baada ya kuchoka nikakaa sehemu ya kusubiria wageni nikifikiria cha kufanya. Mara nikaguswa begani, kuinua uso nikamwona Omar.
"Umenitisha sana Omar, kuna nini?" Nilimuuliza kwa shauku
kubwa.
"Nina tatizo kubwa sana ndugu yangu, nimepokea mgeni lakini
nahitaji ukampe hifadhi kwa usiku huu. Wewe ndiyo
ninaekuamini Musa" alisema Omar akionyesha kweli ni jambo
linalomtatiza.
"Ondoa shaka Omar! Yuko wapi?" nilimuuliza kwa kuwa
sikumuona akiwa na mtu yeyote pembeni.
"Nimemtanguliza kwako, yuko kwenye chumba cha wageni. Ila
ukimkuta amepumzika usimuamshe, ameshakula chakula cha
jioni. Ni mwanamke, na ni ndugu yangu lakini wewe
nakuamini." alisema Omar akitabasamu.
Sikumuuliza kuwa aliingiaje kwa kuwa tunajuana michezo yetu
hivyo hata kama una kitu unataka kukifaya siri unatakiwa
kukifichia nje ya nyumba, sio ndani. Niliagana na Omar na
kurejea nyumbani.
Nilipofika nyumbani, kweli nilikuta dalili za mgeni tena wa
kike kutokana na marashi yanayonukia. Nilimkuta kajifungia
ila sikumtilia maanani, niliamini kuwa Omar hakutaka aende
kwake usiku ule kutokana na vimeo vyake.
Omar huwa anapenda sana wanawake wasio na adabu, mwenyewe anadai ndio anaokuwa nao huru zaidi. Kwa kifupi anapenda wanawake malaya.
Nilimpotezea mgeni wa Omar usiku ule, japo kwa vipindi
fulani nilijihisi mzuka wa kumgongea mlango. Halmashauri ya
kichwa changu ilikuwa makini katika kuidhibiti tamaa yangu
ya mwili.
Ilipofika saa kumi alfajiri niliamka kwa ajili ya mazoezi.
Kwa kawaida mimi hufanya mazoezi kuanzia muda huo na huwa namaliza mara tu mwanga unapoanza, kwa wale watu wa mazoezi yanayohusisha hisia watakuwa wananielewa zaidi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kumaliza na kuoga nikawa chumbani nikisikiliza
muziki kwa mbali huku nikisoma kitabu changu. Nilitoka nje
kwenye saa mbili hivi, nikaona kitu cha kunishangaza.
Mezani kulikuwa kumeandaliwa kifungua kichwa na mgeni wa
Omar. Kabla sijawaza vyema, mgeni alitokea chumbani kwake.
Nilimtambua na sikujua niwaze nini, alikuwa ni Tausi.
"Nimefurahi kuwa una heshima kwa wageni, naomba uendelee
hivyo hivyo" alisema akitabasamu.
Sikuweza kumjibu wala kusema chochote. Nilidhani kuwa
nimemsahau na simpendi tena, lakini nilikuwa ninajidanganya.
Hisia zilirudi ghafla kama mwanzo.
Baada ya muda nikapata swali la kumuuliza, "umefika au
unaendelea na safari?"
"Fungua kwanza kinywa" alinijibu kwa upole ila sikuweza
kutulia nikaendelea kum’bembeleza aniambie. Akanijibu kuwa
atakuwa amefika kama bado nafasi yake ipo.
Nilimnyanyua ghafla na kumuingiza chumbani kwangu ili
nimuonyeshe nafasi yake ilipo, ila yeye alinisisitiza
nifungue kinywa kwanza.
Kumbe operesheni yote ya kunitenganisha na Tausi ilikuwa
inaendeshwa na Omar kwa amri ya Mkuu, lakini alipoona mambo yametulia ilibidi akamueleze kila kitu Tausi. Ndipo
wakakubaliana aje.
Na pia hakukuwa na kikwazo tena kwa kuwa Mzee Nurdin
alihukumiwa kifungo cha maisha baada ya Rais kukataa kusaini
hukumu ya kifo.
Mwisho wa yote nilimkubalia kwa masharti Tausi kuwa
nitafungua kinywa kwanza lakini nikamwambia nikimaliza
kufungua kinywa, USIN’BANIE!
Leo hii yuko mbele yangu, tukijiandaa kufurahia fungate yetu
baada ya kufunga ndoa takatifu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***MWISHO***
0 comments:
Post a Comment