IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)
*********************************************************************************
Simulizi :Roho Za Kishetani
Sehemu Ya Kwanza
(1)KILIKUWA ni kikao kizito, kikao cha siri, kilichoendeshwa kwa umakini wa hali ya juu. Hakuna aliyekuwa na wasiwasi wa kuvuja kwa siri za kikao hicho. Kila mmoja aliamini kuwa yanayojadiliwa humo katu hatayafikia masikio yasiyohusika. Huyu alimwamini yule na yule alimwamini huyu. Waliaminiana.
Zilishakatika saa nne tangu walipoingia ndani ya chumba hiki maalumu, katika hoteli hii ya Malick, mtaa wa Jamhuri, katikati ya jiji la Dar es Salaam. Na haikuwa mara ya kwanza kwao kukutana katika hoteli hii na chumba hiki kwa minajili ya maongezi maalumu, maongezi yaliyohusu mpango wao mzito uliohitaji umakini, gharama ya kutisha sanjari na mioyo ya kijasiri.
Ndio, haikuwa mara ya kwanza. Tayari walishakutana mara kadhaa, siku kadha wa kadha zilizopita na sasa walikichukulia chumba hicho kama ofisi au ukumbi wa mikutano. Katika vikao vilivyopita walipiga hatua kubwa, na hiki kilipaswa kuwa kikao muhimu cha mwisho kabla ya utekelezaji wa maazimio.
Kwa hoteli kubwa kama hii, kushinda chumbani kwa nusu siku, mkivisumbua vichwa kwa kufikiri, kupanga na kuzungumzia suala zito halikuwa tatizo wala kero. Ni hoteli ya kisasa, yenye mvuto nje na ndani. Kwa wanaume hawa watatu, kujichimbia chumbani kwa saa tatu mfululizo, kwao ilikuwa ni sawa na robo saa tu.
Ni chumba kipana. Hutahitaji kutoka ili kwenda msalani au bafuni; mambo ni ndani kwa ndani. Kama koo limekauka utafungua jokofu lililo jirani na kabati kubwa ya nguo ambako utaamua utwae kinywaji ukipendacho; maji, soda na bia zilikuwemo. Pia hakukukosekana chupa mbili, tatu za pombe kali.
Njaa ikikusakama, simu ipo juu ya kimeza kidogo. Ni kwa kutumia chombo hicho ndipo utakapowasiliana na wahudumu ambao dakika chache baadaye watakuletea chakula utakachohitaji.
Msimu wa joto kwa jiji la Dar es Salaam huwa ni wakati wa kero tupu kwa wakazi wake. Lakini ukiwa ndani ya chumba chochote katika hoteli hii, hutajihisi kuwa uko Dar hii ya Tanzania , labda Dar ya Ulaya, kama ipo. Vinginevyo, viyoyozi vilivyotapakaa kila sehemu iliyostahili vitakufanya ujione uko katikati ya jiji la London , Uingereza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni sifa hizo zilizowafanya wanaume hawa waichague hoteli hii na kujichimbia katika chumba hiki, ghorofa ya pili.
Rwegasira aliyekuwa bosi wa kikao, kwa kipindi kirefu alikuwa akivuta sigara huku glasi yake ikiwa haikauki kinywaji kikali.
Karumuna, kama Rwegasira naye alikuwa akivuta sigara lakini tumbo lake likipokea kinywaji laini cha bia.
Muganyizi, yeye alikunywa bia bila ya kuvuta sigara lakini tambuu hazikumwisha kinywani.
Wote hawa walikuwa wakifahamiana kwa muda mrefu. Uhusiano wao ulianzia jeshini, wakiwa waajiriwa wa Jeshi la Wananchi ambako walipata mafunzo mengi, makubwa kwa madogo kabla hawajavikwaa vyeo vilivyowapatia heshima kambini na uraiani.
Vilikuwa ni vyeo vilivyowastahili, kufuatia mafunzo ya kitaalamu waliyopata. Lakini baada ya miaka mitatu waliviona vyeo hivyo ni mizigo mabegani mwao; wakavitua bila ya shinikizo kutoka kwa yeyote. Heshima walizopewa kambini na uraiani hawakuzithamini tena; wakazitapika. Sare za jeshi zilizowaongezea hadhi popote wapitapo, sasa walihisi zikiwaletea muwasho miilini mwao; wakazivua.
Siku chache baada ya kuchukua uamuzi huo, ndipo walipokutana mara kadhaa katika hoteli hii hadi siku hii iliyokuwa muhimu kwa upangaji wa mkakati kabla ya utekelezaji.
Rwegasira aliwatazama wenzake kwa zamu, kisha akasema, “Zimebaki siku mbili tu. Kama hakutatokea mabadiliko yoyote, zana zote zitakuwa chini ya milki yetu kesho kutwa.”
Ukimya mfupi ukatawala. Kisha Rwegasira akaendelea, “Lakini kuna mabadiliko.”
“Mabadiliko?” Karumuna alimwuliza kwa mshangao.
“Yeah,” Rwegasira alijibu kwa msisitizo.
“Mabadiliko gani?” Muganyizi alidakia.
“Taratibu,” Rwegasira alijibu kwa kujiamini, akimnyooeshea kiganja Muganyizi. “Tangu juzi nimekuwa na mawasiliano na wadau, tukakubaliana kufanya mabadiliko kuhusu zana zinazopaswa kutumika. Awali tulipanga kutumia mabomu yenye nguvu kubwa, sio?”
“Nd'o maana'ake,” Karumuna alijibu haraka.
“Sasa siyo hivyo tena.”
Karumuna na Muganyizi waliguna kwa pamoja, huku wakiwa wamemkodolea macho Rwegasira.
“Ndio,” Rwegasira alisisitiza. “Hatutatumia mabomu tena!”
“Kwa nini?” Muganyizi aliuliza na papohapo kuipeleka sigara mdomoni na kuvuta mikupuo miwili ya nguvu.
Kicheko cha dhihaka kikamtoka Rwegasira. Hakujibu mapema. Aliitwaa glasi yake ya kinywaji kikali, akaipeleka kinywani na kugugumia mafunda kadhaa. Mara akakunja uso na kuirejesha glasi hiyo mezani. Sigara ikafuatia. Funda moja lilipopita kinywani na kisha akapuliza moshi juu huku mwingine ukitokea puani, sasa akaonekana kuridhika. Akashusha pumzi ndefu na kuwatazama wenzake kwa zamu.
“Nilijua kuwa kwa vyovyote vile suala la mabadiliko litawashtua na kuwashangaza,” hatimaye alisema. “Lakini tumelazimika kufanya mabadiliko ili kazi ifanyike kwa ufanisi. Na zaidi, naamini kuwa kazi hii itakuwa nyepesi tukilinganisha na mpango wa awali.”
Ukimya ukatanda. Rwegasira akawakodolea macho kwa zamu. Kisha akaendelea, “Hatutatumia tena mabomu makubwa. Kama mnavyojua, tungepaswa kutumia mabomu yenye nguvu kubwa na makubwa. Tumejaribu kutafakari kuhusu hilo tukaona kuwa kuna uwezekano wa kutofanikiwa. Mambo yanaweza kutuharibikia kabla hatujafanya lolote.
“Kutumia mabomu makubwa,” aliendelea, “ingetulazimu pia kutumia mbinu kama ile iliyotumika wakati wa kuzilipua ofisi za Ubalozi wa Marekani. Tungelazimika kuwa na magari makubwa ambayo yangebeba mabomu hayo na labda twende tukayagongeshe kwenye majengo husika. Kwa hali hiyo, Mungu ametusaidia, tumepata zana nyingine nzuri na rahisi kubebeka. Naamini kazi yetu itakuwa nyepesi kuliko ilivyo.”
Kwa mara nyingine ukimya ukapita. Bado Karumuna na Muganyizi walikuwa kizani. Hawakuelewa Rwegasira alikuwa akizungumza nini. Karumuna akaitwaa glasi yake na kuipeleka kinywani. Akanywa funda dogo la bia yake. Akapepesa macho huku na kule kisha akayatuliza kwa Rwegasira. “Hujaeleweka unazungumza nini,” hatimaye alisema. “Jitahidi kuyanyoosha maneno yako ili tukijue kile unachokisema.”
Tabasamu likachanua usoni pa Rwegasira. Kwa mara nyingine akanywa mafunda mawili, matatu ya kinywaji chake kikali. Kisha akashusha pumzi ndefu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tutatumia sumu,” hatimaye alisema. Sauti yake ilikuwa nzito na ya chini, kama vile alitaka hata hao wenzake wasisikie. “Tutatumia sumu ambayo itasambaa katika hewa na kutoa matunda mema.”
Muganyizi na Karumuna walitekwa na kauli hiyo. Wakajiweka sawa vitini huku wakimwangalia Rwegasira kwa makini zaidi.
“Tutakuwa na chupa tano ndogo za ujazo wa lita moja ya maji,” Rwegasira aliendelea kufafanua. “Lakini chupa hizo hazitakuwa na maji. Zitaonekana kuwa ni tupu, lakini pia hazitakuwa tupu. Kila chupa itakuwa imejaa hewa nzito yenye sumu kali sana . Ni chupa ambazo hazifunguliwi kama chupa za soda au bia. No. Zinafunguliwa kwa rimoti. Maelezo mengine hususan jinsi ya kulikamilisha zoezi letu tutapeana baada ya vifaa hivyo kuwasili.”
Kwa mara nyingine ukimya ukalitawala eneo hilo . Kisha tena Rwegasira akauvunja ukimya huo kwa kusema, “Tunataka Dar es Salaam itutambue, Tanzania itikisike na dunia iduwae. Sidhani kama kati yetu kuna asiyeyajua majengo mazuri hapa jijini. Kuna majengo mengi, makubwa kwa madogo yanayostahili kuingizwa kwenye programu hii. Lakini kwa kuwa tutakuwa na chupa tano tu za PAK, tunapaswa kuchagua majengo matano tu.”
Alitaka kuendelea kuongea lakini macho ya Muganyizi yalionyesha kuwa alikuwa na swali au pendekezo. “Vipi, una la kusema?” alimwuliza.
“Ndio. Hiyo sumu inatengenezwa wapi?”
“ Athens , Ugiriki. Ni sumu hatari sana . Kitendo cha kuivuta tu, unaondoka. Zamani iliwahi kuletwa hapa nchini na baadaye ikapigwa marufuku baada ya kiongozi mmoja kubainika kufa kwa sumu hiyo.”
“Poa,” Karumuna alisema na kuongeza, “Suala langu ni kuhusu majengo husika. Ni majengo gani yaliyolengwa?”
“Tuna mpango wa kutumia majengo matano ambayo yako mbalimbali,” Rwegasira alijibu. “ Millennium Tower la Mikocheni lipo katika programu. Jingine ni PPF Tower la Garden Avenue . Tulifikiria pia kulitumia jengo la Benjamin Mkapa la posta mpya lakini tumeachana nalo, badala yake tumehamia mahakamani. Tumeona kuwa siku hizi kuna kesi nyingi zinazowakusanya watu wengi mahakamani. Tunataka tuitumie mahakama ya Kisutu na Mahakama Kuu.”
Kufikia hapo akatulia kidogo akiwatazama wenzake. Karumuna na Muganyizi hawakusema kitu, walionekana kuwa wako makini kupokea maelezo yake.
“Kabla ya kuzitumia mahakama hizo,” aliendelea, “tunapaswa kufuatilia kwa makini siku ambayo kutakuwa na kesi kubwa kama za yale mauaji ya Pande na hizi za ufisadi wa Benki Kuu. Zoezi hili linapaswa kufanyika kwa siku moja na ikibidi kwa dakika moja. Kwa hali hiyo, lazima tujue kuwa ni lini kutakuwa na kesi hizo kuwe na mrundikano wa watu ili tuweze kufanikisha kazi yetu.”
“Itakuwa ngumu,” Karumuna alisema. “ Kesi zile zina watuhumiwa tofauti na mahakimu tofauti. Zina siku tofauti. Usifikiri kuwa kila siku ya kesi ya watuhumiwa wa mauaji ya Pande ndiyo pia siku ya kesi ya watu wa EPA. Ni kesi mbili tofauti. Kwa hilo , kazi itakuwa ngumu kuliko ilivyo.”
Rwegasira alitikisa kichwa akionesha kuafiki. Kisha akasema, “Ni kweli. Au tuache kudili na mahakama?”
“Nadhani hiyo itakuwa safi ,” Karumuna alisema. “Kwanini tusichague hoteli moja au mbili?”
“Hoteli!” Rwegasira alisema kwa mshangao.
“Yeah, mara nyingi viongozi au matajiri wenye vijisenti huwa wanaitisha makongamano kwenye hoteli kubwakubwa. Hapo huwa kuna mkusanyiko wa watu, hususan waandishi wa habari.”
Muganyizi alionekana akitafakari jambo. Akaguna na kusema, “Kwa upande wangu sidhani kuwa itakuwa busara. Hoteli za kitalii zina watu wengi ambao huwa sio Watanzania. Tutakuwa tumeua watu wasiokuwa na hatia hata chembe!”
“Kwani hao wengine wa kwenye majengo mengine wana hatia?” Rwegasira aliuliza.
Muganyizi hakujibu, na sio kwamba alikosa jibu bali alijali kuitwaa glasi yake ya kinywaji na kuipeleka kinywani ambako aligugumia funda zito.
“Hiyo haituhusu,”Rwegasira aliendelea. “Ndugu zetu wameuawa kikatili, ya nini kuwa na uchungu na watalii, matapeli na washenzi wengine waliojipatia pesa kiajabuajabu na kuamua kula raha hotelini?”
Akameza funda zito la mate na kumkazia macho Muganyizi. “Una ndugu zako wanaoishi kwenye hoteli hizo? Una hisa katika hoteli hizo?” hatimaye alimwuliza, sauti yake nzito na yenye mkwaruzo ikionesha ni jinsi gani ana uchungu moyoni.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Safari hii Muganyizi hakuwa na sababu ya kutojibu, lakini kwa kiasi fulani maswali hayo yalikuwa magumu kwake. Akalazimika kuwa kimya.
“Tuendelee na suala letu,” Rwegasira alisema. “Hakuna mwenye ndugu Moven Pick wala Kempiski. Lakini tuseme tu kuwa zana zetu hazitoshelezi kudili kila sehemu. Ni chupa tano tu. Tungekuwa na chupa kumi labda tungefikiria maeneo mengine ya kuyashughulikia.”
Ukimya ukatawala. Huenda kila mmoja alikuwa na mawazo yake kichwani. Ni Rwegasira tena aliyeuvunja ukimya huo. “Kitu kinachonifariji ni picha itakayofuata baada ya kutekeleza suala letu. Piga picha kuwa watu kumi au ishirini hata hamsini ndani ya jengo moja wanaanguka mmoja, mmoja huku wakitapika damu. Na muda mfupi baadaye, wakiwa tayari wamekufa, miili yao inavimba kama iliyotiwa hamira.” Akacheka kwa sauti, kicheko cha dhihaka.
Muganyizi na Karumuna walitazamana, kila mmoja akitabasamu.
“Na pamoja na kuwaambia kuhusu hayo majengo yaliyolengwa, pia nina wazo jingine lililonijia kichwani,” alisema baada ya kukikata kicheko chake. “Ni kuhusu taasisi za kidini. Makanisani na misikitini hufurika waumini wanaojitia kumpenda sana Mungu kama vile wanamjua. Nilifikiri chupa mbili zilistahili kupelekwa katika msikiti mmoja maarufu wenye kufurika watu na katika kanisa moja linalojaa waumini.”
Akatulia tena na kuwatazama wenzake kwa makini. “Kwa wazo hilo nilifikiria kuwa zoezi hilo litalazimika kufanyika kwa siku tofauti,” aliendelea. “Sehemu nyingine zisizokuwa za ibada tufanye Alhamisi, msikitini Ijumaa na kanisani, Jumapili. Mataifa ya Kiislamu yatalaani na Papa pamoja na mataifa mengine yanayoamini sana Ukristo, yatahuzunika. Itakuwa ni habari njema kwao.” Akacheka tena, safari hii kwa sauti ya chini.
“Hebu fikirini, waumini wako msikitini au kanisani, ghafla mmoja, mmoja anaanza kupumua kwa nguvu, halafu anakumbwa na usingizi wa ghafla. Muda mfupi baadaye waumini kama mia hivi wanabaki ni mizoga, damu nzito zikiwatoka masikioni, puani na midomoni. Itabaki picha gani hapo?”
“Itatisha!” Muganyizi alisema.
“Itapendeza,” Karumuna alichangia.
“Ndio, itakuwa ni picha itakayowatisha waoga na kuwasikitisha majasiri pale maiti zitakapokuwa zimezagaa makanisani na misikitini, lakini itakuwa ni habari kubwa ambayo itadakwa na mashirika makubwa ya habari na kuiweka Tanzania katika ulimwengu wa matukio. Siyo kila siku Iraq , kila siku Israel na Palestina. No! Tunataka Tanzania nayo itangazike! Ijulikane kwa fani zote; amani na utulivu hali kadhalika, mauaji ya halaiki, ya kupendeza na kufurahisha!”
Kimya tena.
Nyuso zao zilipogongana tena, ni Karumuna ambaye safari hii aliuvunja ukimya huo. Akauliza, “Ni msikiti gani uliodhani kuwa unastahili kutumiwa?”
“Msikiti wa Manyema wa Kariakoo. Si mnaujua?”
Muganyizi na Karumuna walitikisa vichwa wakionesha kukubali.
“Na nimeona kuwa kanisa la Lutheran la Azania ambako ndiyo makao makuu ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani pia ndilo linalostahili. Naamini hakutakuwa na tatizo wala kikwazo chochote. Kila kitu kitakwenda kama tutakavyotaka.”
*****
KATIKA hali iliyowashangaza na kuwasikitisha wengi, zilipatikana taarifa za mauaji ya kinyama yaliyotokea katika kijiji fulani mkoani Kagera. Watanzania thelathini waliuawa kwa risasi kufuatia uvamizi wa wakimbizi waliotoroka katika kambi ya Lukole wilayani Ngara.
Miongoni mwa Watanzania hao ni familia za Karumuna, Rwegasira na Muganyizi. Rwegasira alipoteza wazazi wake wote pamoja na wadogo zake watatu. Watoto wanne wa Karumuna waliuawa kikatili baada ya mama yao kubakwa kabla ya kuzamishwa risasi ya kichwa. Muganyizi alipoteza mjomba, baba, mama na wadogo zake wanne wa kike ambao nao kabla ya kuuawa walibakwa na wakimbizi hao.
Matukio hayo yalitafsiriwa kwa namna tofauti na Watanzania. Kuna walioishutumu serikali kwa kuendelea 'kuwanyenyekea' Warundi na Wanyarwanda waliozagaa nchini wakiwanyanyasa wazawa na kupora mali zikiwemo fedha taslimu.
Wengine waliilaumu serikali kwa kuendelea kuwa na kambi za wakimbizi nchini, kambi ambazo zimewafuga watu ambao sasa wamegeuka kuwa mzigo wa Taifa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kulikuwa na matukio zaidi, ya kusikitisha, kutisha na kustaajabisha, ambayo yalitoa taswira kwa Watanzania wengi, kuwa wakimbizi ni hatari na mzigo mzito ulioielemea jamii ya Kitanzania.
Mke wa Kamanda wa Polisi wilaya ya Ngara aliuawa kwa risasi na waliosadikiwa kuwa ni wakimbizi waliotoroka kambini.
Siku chache baadaye, mkimbizi mmoja raia wa Burundi alitoroka kambini usiku, akaenda kwa dada yake aliyeolewa na Mtanzania ambako aliwaua watoto wawili na kisha akamkosakosa risasi dada yake. Alifanya hivyo kwa kuamini kuwa, Mtutsi, kuolewa au kuoa Mtanzania ni kujidhalilisha
Pia zilipatikana taarifa kutoka katika vijiji mbalimbali mkoani Kigoma zikisema kuwa, wakimbizi wengi walijihusisha na uhalifu wa kutumia silaha huku wakipewa ushirikiano na Watanzania wazawa wenye roho nyeusi.
Lakini taarifa nyingi ziliwahusu wakazi wa vijiji vilivyo jirani na kambi kadhaa mkoani Kagera, ambao huvamiwa mara kwa mara na watu wenye silaha za moto na kisha kuporwa vitu, fedha na hata kuuawa kikatili.
Japo baadhi ya watu walikamatwa, lakini baadaye waliachiwa huru kutokana na kutopatikana ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani. Hata hivyo tetesi juu ya askari walioasi Rwanda na Burundi na kukimbilia Tanzania , kuwa ndiyo wahusika wakuu wa uhalifu zilizagaa pembe zote za mkoa huo.
Tetesi hizo ziliwahusu wakimbizi watatu ambao waliingia Tanzania na kupewa hifadhi katika kambi moja ya wakimbizi, na siku chache baadaye wakajiingiza katika kazi ya kuwavamia Watanzania na kuwapora fedha na mali nyingine kabla ya kuwaua, zoezi lililofanikishwa kutokana na ushirikiano wa asilimia mia moja uliotolewa na Watanzania wazawa wenye roho nyeusi.
Zilikuwa ni tetesi zilizogeuka kuwa malalamiko makali dhidi ya uongozi wa serikali mkoani humo, malalamiko yaliyosababisha Wahutu watatu asili ya Rwanda waliofikia kambi ya Lukole wakamatwe kwa tuhuma za kuwaua wanakijiji thelathini wakiwemo ndugu na jamaa wa Rwegasira, Karumuna na Muganyizi.
Kuna baadhi wa wananchi waliowafahamu kiundani wahusika hao wakuu wa mauaji hayo ya kikatili. Na hao ndiyo waliosimama kidete kuhakikisha Wanyarwanda hao wanafikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Ndayikengelukiye, Ndikumana na Karikingi, askari walioasi katika jeshi la serikali ya Rwanda ndiyo waliotuhumiwa kushiriki katika mauaji hayo kwa asilimia mia moja. Lakini pamoja na ushahidi ulioongezwa nguvu na watoto kadhaa wenye umri kati ya miaka minane na kumi na miwili, hata hivyo kwa kutumia vigezo hivi na vile vya kitaalamu, vyombo vya sheria havikuwatia hatiani.
Kuachiwa huru kwa Wanyarwanda hao hakukuwaridhisha Rwegasira, Karumuna na Muganyizi. Wakafuatilia katika ngazi za juu serikalini, ambako waliishia kukata tamaa kutokana na kauli kutoka katika taasisi husika kuwa uchunguzi bado unaendelea, uchunguzi ambao hata hivyo ulioonesha kudorora siku hadi siku.
Uchungu uliwatawala askari hao. Hasira zikawapanda. Uvumilivu ukawashinda. Ndipo kwa pamoja walipoamua kutoa taarifa ya kuacha kazi ghafla, taarifa ambayo pindi utawala wa Jeshi la Wananchi ulipohitaji maelezo zaidi, ukawa umeshachelewa. Tayari askari hao walishatoweka kambini na bunduki tatu pamoja na risasi mia tatu.
Jambo jingine lililoyatikisa vilivyo Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi ni kutoweka kwa lori tani kumi katika mazingira ya kutatanisha, muda mfupi tu baada ya kubainika kutoweka kwa Makapteni Karumuna, Rwegasira na Muganyizi.
Kama ni sakasaka basi hii ilitisha. Dar es Salaam ilitikisika kwa msako mkali dhidi ya askari hao wa vyeo vya juu, msako ulioishia kuwachanganya Wakuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na taasisi nyingine nyeti. Karumuna hakuonekana, Rwegasira na Muganyizi hali kadhalika. Hata hivyo, lori lilipatikana likiwa limetelekezwa eneo la Tegeta, pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam siku mbili zilizofuata.
Ilikuwa ni siri kubwa. Hakuna chombo chochote cha habari kilichopewa taarifa rasmi na serikali kuhusu tukio hilo . Lakini ilikuwa ni siri iliyodumu kwa siku chache tu na kufichuka taratibu kupitia minong'ono ya hapa na pale kutoka kwa baadhi ya askari wa jeshi.
Ni minong'ono hiyo iliyogeuka kuwa habari nzito kwa baadhi ya magazeti, redio na televisheni. Baadhi ya taasisi hizo za habari zilitangaza, zikidai kuwa ni habari ambazo hazijathibitishwa rasmi. Kilichofuata ni wakuu wa vyombo hivyo kuitwa kusikojulikana ambako walihojiwa vikali na kupewa vitisho sanjari na onyo kali.
Gazeti moja lilidai kuwa habari hizo zilipatikana kufuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na waandishi wake na kisha kuthibitishwa na baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa Makao Makuu ya Jeshi, bila kuyataja majina wala vyeo vyao.
Mhariri na mwandishi mmoja wa gazeti hilo walichukuliwa kimsobesobe, wakafichwa mahala fulani ambako mahojiano ya kina yalifanyika, mahojiano yaliyoambatana na mateso ya wastani lakini yaliyoacha kumbukumbu ya kudumu miilini mwao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment