Search This Blog

Sunday 19 June 2022

KIVULI (THE CATCHING SHADOW) - 4

 





    Simulizi : Kivuli (The Catching Shadow)

    Sehemu Ya Nne (4)



    Rashad hakuamini macho yake kuwa hatimaye kakutana na yule mwanamke. Moyoni mwake alijikuta akihisi hisia ya ajabu ya furaha iliyochanganyika na huzuni, pengine ya kutokana na kuwa hatimaye kamuona mwanamke aliyekuwa akimuota kwenye njozi zake. Mara hisia kali zilikita kwenye moyo wake na mara chozi lilidondoka toka kwenye macho yake na kulowesha mashavu yake. Kwa muda alibaki kasimama akimuangalia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mara akaona mwanamume mmoja aliyekuwa ndani ya duka akimuendea yule mwanamke pale kwa keshia, akiwa kabeba mfuko wenye bidhaa, kisha akalipia zile bidhaa na akamshika yule mwanamke mkono na wakatoka nje ya supermarket. Kwa haraka sana Rashad alijikuta akitoka haraka nje ya supermarket hiyo hadi nje ili tu kuwawahi. Alipofika nje aliwaona jinsi walivyopanda kwenye gari lao na kuondoka eneo lile la supermarket. Rashad alibaki akisononeka moyoni mwake na kujiuliza wapi atakutana tena na yule mwanamke. Ila pia alielewa akilini mwake kuwa yule mwanamume aliyeongozana nae lazima atakuwa ni mume wake.



    Kitendo cha kumuona tena Johari kilimzidishia mawazo Rashad, sasa kila alipokaa mawazo yake yalikuwa nikumuwazia Johari. Kwanza ieleweke hadi wakati huo, Rashad hakuwa akimfahamu Johari kwa jina zaidi ya kumjua sura tu na kumfahamu kama mwanamke aliyewahi ‘kulala’ nae kipindi yuko chizi.



    Baada ya kilichojiri pale ‘supermarket’, maisha ya Rashad yakawa ndio ya kumuwaza tu Johari, hata watu wengine walianza ‘kunotisi’ jinsi ambavyo Rashad alivyozidi kuwa mtu mwenye mawazo na aliyezidi kuwa mkimya sana. Hali ambayo ilitia watu wa karibu yake hofu kuwa huenda yale matatizo yake ya akili ndiyo yanayomtia ukimya huo, hivyo wote wakawa na wasiwasi na kutaka hali hiyo ikome.



    Basi Imran na Sarha wakawa ndio watu wa mwanzo kumhoji Rashad kulikoni hata amekuwa akipoa sana na kuonekana mwenye mawazo mengi. Ndipo Rashad akawasimulia kuwa alikuwa kakutana na yule mwanamke mzuri, aliyewahi kuwa na mahusiano naye kipindi yuko chizi, mwanamke mzuri kuliko wote aliokuwa akiwafahamu. Na aliwaambia jinsi moyo wake ulivyoumia na kusikitika sana kwasababu alishindwa kuongea naye pale alipomuona supermarket na mbaya zaidi alimuona yule mwanamke akiongozana na mwanaume mwengine, na ilionekana kuwa lazima yule mwanaume atakuwa ni mumewe.



    Hayo masimulizi ya bwana Rashad yalikuwa mazito kwa Sarha na mume wake bwana Imran. Yalikuwa mazito sana. Kwanza walifahamu fika kuwa ndugu yao ‘alikuwaga chizi’ wa zaidi ya miaka kumi, tena chizi mchafu muokota makopo, iwaje ikatokea eti alitembea na mwanamke mwenye akili timamu, suala hilo halikumkinika kabisa akilini mwao. Ila pia walishangazwa na ‘userious’ wa Rashad juu ya kile alichowasimulia. Walimuona akiongea kwa kujiamini.



    Sarha alishindwa kuvumilia na kumwambia kile alichokuwa akifikiria, “sikia Rashad kakaangu, hebu achana na hizi habari zako za kuwa kuna mwanamke ulikuwa na mahusiano nae kipindi uko mwendawazimu. Tafadhali achana nazo hizo habari. Haiyumkiniki hata kidogo kuwa kuna mwanamke mwenye akili timamu ambaye angeweza kuwa na wewe wakati akili zako hazikuwa sawa.”, aliongea Sarha na kumsisitizia Rashad kuwa haina haja ya kumuwaza huyo mwanamke muda wote na kama ana shida sana ya mapenzi atafute mwanamke mwengine, “kaka yangu kama unajiona una hamu sana ya mapenzi tafuta mwanamke mwengine uoe, hizo habari zako za mwanamke anayekujia ndotoni, sijui!, mwanamke ukilala unamuota achana nazo, zinatupa shida kuamini kiwango cha kupona kwako tatizo lako la akili, unatutia wasiwasi kuwa pengine bado kichwani sio mzima”, aliongea Sarha maneno hayo kwa msimamo huku Imran akisapoti alichoongea mkewe.



    Hali yao ya kutomuamini ilimtia hasira Rashad na kuwatamkia kuwa haina haja ya wao kumuamini kile ajuacho kuhusu yeye na maisha yake kipindi yuko chizi ama mahusiano yake na huyo mwanamke aliyekuwa akimpenda. Na kwa hasira akawaahidi kuwa hatozungumzia tena suala la mwanamke ampendaye mbele yao kwa maana alihisi kuwa wanamvunjia heshima kwa kumuona bado kichaa baada ya kuwaeleza kuhusu hisia zake. Basi Rashad akabaki hivyo akijiamini yeye nafsi yake kuwa ipo siku atakutana na yule mwanamke ampendaye na atamueleza jinsi anavyompenda.



    Pamoja na nia yake ya kutaka kuonana tena na Johari, Rashad hakuwa na pa kuanzia kumtafuta. Hakujua lolote juu ya Johari, hakupajua kazini kwake wala hakupajua alipokuwa akiishi.



    Kwa bahati nzuri sana, ikatokea siku moja, Rashad anaangalia taarifa ya habari. Akiwa hana umakini sana na kile kilichokuwa kikiendelea kuoneshwa luningani, ambacho kilikuwa ni habari za uchumi, mara ghafla akaona sura ya Johari kwenye luninga. Ilikuwa ni bahati sana, hatimaye Rashad alimuona tena Johari kwenye taarifa ya habari akihojiwa na mtangazaji juu masuala ya kifedha.



    Basi, kwa utaratibu wa hali ya juu na kwa umakini, Rashad alisoma jina la Johari lililokuwa limewekwa kwenye ‘skrini’. Hatimaye sasa Rashad akafahamu vizuri jina la Johari, alilisoma, tena lilikuwa limeandikwa vizuri kabisa, ‘Johari Chande Munyisi’. Tena kama haikutosha kwa chini ya jina paliandikwa maneno, ‘mchumi, benki ya NIB’. Rashad alifurahi sana. Alifurahi sana na kutoamini kuwa hatimaye alimfahamu Johari kwa jina na hata akawa amefahamu kuwa alikuwa akifanya kazi kwenye benki ya NIB.



    Alijikuta akimuangalia Johari kwa umakini mkubwa. Na ajabu eti kwa muda huo mfupi, chozi lilimteremka tena kwenye macho yake, chozi la furaha, huku likiambatana na tabasamu. Hatimaye haja yake ya kumfahamu Johari ilitimia na alikuwa na pa kuanzia kumfahamu vizuri zaidi.



    Usiku huo kwa mara ya kwanza aliingia mtandaoni kumtafuta Johari kwa kutumia majina yake kamili kuona kama atakuta lolote la zaidi la kumfahamu. Naam, alipoweka tu jina la Johari mitandaoni yalimjia majibu tele, yalioonesha akaunti za Johari za mitandao tofauti tofauti ya kijamii.



    Basi bwana, kama waswahili tujuavyo, kupitia mitandaoni aliweza kufahamu kuwa Johari alikuwa ni mwanamke msomi sana, aliyefanya kazi benki na mwenye cheo kikubwa. Si hivyo tu aliona kuwa Johari alikuwa kaolewa na mtu aliyeitwa Malcom Munyisi ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa wizara ya mambo ya nje. Kupitia picha za mitandaoni Rashad aligundua kuwa Johari alikuwa akimpenda mumewe sana kwa maana alikuwa kamposti kwenye picha nyingi sana za kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii na kuambatanisha na picha nyinginyingi zenye ujumbe wa kumpenda kwa moyo wote.



    Rashad alifurahi kupata taarifa nyingi zilizo mfanya amuelewe vizuri Johari. Ila pia hakufurahia yale mapenzi ambayo Johari alikuwa akimuoneshea mumewe humo mitandaoni. Kwa maana yeye Rashad alikuwa anampenda Johari.



    Basi sasa moyo wake na akili yake akavigeuzia kwenye upande mwengine kuwa lazima afanye namna ya kukutana na Johari na kumkumbushia mahusiano yao ya bomani kipindi yeye Rashad alipokuwa chizi.



    Hadi muda huo lengo hasa la Rashad lilikuwa ni kukutana nae Johari na kumueleza jinsi gani anampenda sana na kuwa hajawahi ona mwanamke mwengine mzuri kama yeye Johari. Lengo lake likamfanya kuunda tabia ya kuendelea kupekuapekua akaunti za mitandao za Johari.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mchana mmoja Rashad alikuwa anatoka zake kwenye masomo yake aliyokuwa akisoma na akiwa anarejea nyumbani alipokuwa akiishi, kwa Sarha. Mara akahisi kuwa simu yake inaita, hivyo akaiangalia na kukuta ‘facebook’ imemtumia ‘notification’ juu ya Johari ambaye yeye Rashad alikuwa ‘keshamfollow’-, ujumbe huo ulimuambia kuwa Johari alikuwa yupo eneo jirani na alikokuwako. Basi naam, kiroho kikamlipuka na kuanza kumuenda mbio. Akaangalia kwa makini kwenye ‘map’ na akaona kuwa kumbe Johari mwenyewe alikuwa amesimama nje ya mgahawa uliokuwa jirani tu kwa mbele yake eneo hilohilo.



    Na kweli alimuona Johari. Basi kijasho chembamba alihisi kinamtoka. Taratibu akamuendea Johari hadi pale alipokuwa amesimama. Alimuendea huku akimuangalia usoni hadi Johari akashtuka kuwa alikuwa anaangaliwa.



    Kwa upande wake Johari, hakumtambua Rashad, hakumuona kabisa kuwa kafanania na yule chizi aliyelala nae kwenye maboma huko zamani. Kwa sababu wakati huo Rashad alikuwa kabadilika kabisa, alikuwa nadhifu, matanashati, msafi aliyevutia na mwili uliojengeka na hakika alionekana kuwa hakuwa chizi.



    “Makubwa, mbona unanitazama sana hadi naogopa?”, aliongea Johari baada ya kumuona Rashad akimkaribia huku akimuangalia kwa makini usoni kama mtu anayetaka kukumbukwa. Johari hakuwa na wazo hata kidogo kuwa chizi wake wa zamani ndio alikuwa akimtazama na kumkaribia.



    Alipomfikia alianza kumwambia kuwa alikuwa anamtafuta kwa muda mrefu sana, kauli hiyo ilimshtua Johari. Na kuhoji chanzo hasa cha kutafutwa kilikuwa ni nini, hasa ikizingatiwa kuwa yeye Johari hadi wakati huo aliona hamfahamu Rashad.



    Mara Rashad akaanza kumwambia Johari amuangalie vizuri uso wake, alimuomba amuangalie kwa makini ili amkumbuke. “Niangalie vizuri Johari, niangalie vizuri utanikumbuka. Nitazame.”, aliongea Rashad huku akimuangalia Johari usoni nae Johari wakati huo alikuwa akimtazama Rashad kwa umakini hasa. Naam! ghafla kumbukumbu zikamrejea Johari na kwa hakika kabisa alimtambua Rashad kuwa alikuwa ni yule mwanaume chizi ambaye alilala nae kwenye boma, miaka ya huko nyuma.



    Johari alishtuka sana na kuanza kujiongelesha moyoni mwake kuwa haiwezekani yule mwanaume chizi kapona na ndiye alikuwa huyo aliyemsimamia mbele yake wakati huo.



    Rashad alihisi kuwa Johari keshamkumbuka, alihisi hivyo kutokana na namna Johari alivyoshtuka, alishtuka katika namna iliyodhihirisha kuwa alimkumbuka vizuri.



    “Johari ni mimi. Mimi yule mwanamume chizi niliyekuwa naishi mabomani na majalalani. Ni mimi ndiye uliyekuwa unamtembelea kule majalalani usiku na kuwa naye ni mimi.”, aliongea Rashad kwa kujiamini na kuamini kuwa Johari alimkumbuka vizuri.



    Hadi hapo Johari alikuwa kachanganyikiwa. Kichwani mwake alijawa na maswali kama alfu ambayo alikosa majibu ya kujipa. Alijiuliza vipi chizi kapona uchizi?, vipi mtu aliyekuwa chizi kaweza kumkumbuka miaka ya baadae jinsi hiyo, hakupata majibu kichwani mwake. Hasira zikampanda kidogo na alijikuta ‘akimkata’ Rashad jicho kali la kiroho mbaya. Kisha akamtolea kauli ya kumuonya. “Samahani sana. Sikufahamu. Samahani sana wewe kaka, tena tafadhali, usiniletee habari za kujuana. Wewe na mimi tumefahamiana watu hadi uniletee habari za kujuana? Mpuzi we”, aliongea Johari kwa kupayuka na hasira, akijifanya hamjui Rashad na hamkumbuki kabisa.



    “Johari mimi ninaitwa Rashad, mimi ni yule chizi uliyekuwa ukilala nae kule bomani. Ndio mimi nimepona. Tena nakupenda sana, nimekutafuta sana”, aliongea Rashad na Johari kuzidi kuchanganyikiwa. “mama yangu nini hiki tena”, alijiuliza Johari moyoni, Rashad alikuwa akiongea kwa akili timamu kabisa. Johari alichanganyikiwa hakutegemea kuwa kuna siku yule chizi angemfuata kwa namna hiyo na kumueleza kuwa anakumbuka yale waliyofanya bomani.



    “Sikufahamu, na naomba kaa mbali na mimi, ‘i am not a rat like you’, mwehu wewe, sikukumbuki. Tena kama unavyojieleza kuwa ulikuwa chizi hakika naamini uchizi wako bado umekujaa kichwani, chizi mwanga wewe”, aliongea Johari kwa hasira.



    Mara mwanadada aliyebeba chakula cha ‘take away’ alitoka toka kwenye mgahawa ambao Johari na Rashad waliusimamia kwa mbele wakati huo, na yule mwanadada akampa Johari mfuko huo na kuondoka. Kumbe Johari alikuwa yuko pale kuchukua ‘take away’ ya chakula toka mgahawani.



    Basi baada ya kupokea chakula chake, kwa sonyo na madharau Johari alimtukana matusi Rashad kisha akaelekea kwenye gari lake na kuondoka eneo hilo na kumuacha Rashad kasimama hapo.



    Akiwa njiani na gari lake anarudi kwake, Johari alifikiria sana juu ya Rashad, alishangaa sana kuwa mtu yule chizi kapona na kurejea. Kilichomkera zaidi Johari ni ile kauli ya Rashad kuwa eti alikuwa akimpenda na kwamba alikuwa anamkumbuka na kuwa alikuwa kamtafuta sana. Hiyo kauli ilimfanya ajiulize sana, hasa alijiuliza, hivi yule chizi alianza kumtafuta kwa muda gani, na ni mangapi aliyokuwa akiyafahamu kumhusu yeye hivi kwamba aliweza kumpata na kumfahamu kwa jina. Hasira zilimpanda Johari na akajikuta akipiga piga usukani wa gari kila mara kwa hasira.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipofika kwake mawazo juu ya jinsi alivyoonana na Rashad yalimjia zaidi. Alikaa kwenye sebule ya nyumbani kwake na wanawe Muujiza, Flora na Florian huku akifikiri jinsi ambavyo walikuwa wakimpa furaha kwenye maisha yake yeye na Malcom na akawaza na kukumbuka kuwa hao watoto wake walikuwa ni watoto wa Rashad. Watoto wa mtu ambaye zamani alikuwa akiugua ugonjwa wa akili. Alifikiria sana Johari juu ya jinsi Rashad alivyomjia na kuongea kuwa alikuwa kawahi kutembea nae kipindi yuko chizi, Johari aliwaza, hivi itakuwa ni watu wangapi Rashad keshawaambia kuwa kawahi kutembea na yeye.



    Aliwaza mengi sana Johari. Jioni ya siku hiyo, ilimkuta kajikunyata chumbani kwake kitandani. Akiwaza yale aliyoyafanya miaka ya nyuma na jinsi alivyopata watoto wake kishirikina. Alikumbuka ile familia ya mfanyabiashara ya vito ambaye aliuwawa na wezake wa kundi la kiharifu na mapanya na kukumbuka ndoto za kutisha alizoota baada ya hapo na kukumbuka ile ndoto aliyooteshwa kuwa hatopata watoto maishani mwake na akakumbuka ile kafala aliyofanyiwa na mganga na kufuata sharti a kukutana kimwili na mtu mwendawazimu, hadi hatimaye akapata watoto aliokuwa nao.



    Alikaa kitandani mwake na kuzitazama picha ya harusi yake na Malcom, pamoja na picha ya watoto wake zilizokuwa karibu na kitandani. Na kwa uchungu alijiambia moyoni “ ’Nimeisoma namba’ katika kuhakikisha najenga familia ya kujivunia kama hii”, na wakati huo hofu na presha juu ya Rashad aliyejitokeza na kudai kuwa anakumbuka kila kitu na kumpenda, ilimpanda hasaa.







    .......................................







    Sasa Rashad alizidi kumfuatilia Johari na maisha yake na akagundua kuwa alikuwa na watoto watatu. Alijua hadi hao watoto walikosoma. Rashad akajua hadi Malcom alikokuwa akifanya kazi na maisha yake ya kusafiri mara kwa mara, kwenda nje ya nchi. Aliweza kufahamu hadi sehemu ambazo Johari alipendelea siku za mapumziko. Hadi Johari mwenyewe alifahamu sasa kuwa Rashad alikuwa anamfuatilia. Maana alianza kuona jina lake likijitokeza kwenye watu waliokuwa ‘wakilaik’ posti zake za mitandaoni. Na hiyo ilimtia hasira sana akamblock kila mahala. Mara nyengine alimuona akimfuatilia akiwa katika mizunguko yake, madukani, migahawani, akiwa anapeleka watoto shule ama hata akiwa anakatiza mitaa fulani mjini.



    Wakati huo, Imran na Sarha walizidi kujawa na hofu na nyendo za Rashad. Hawakutaka kabisa kumsikia anamuongelea Johari. Ikabidi wamwambie na mama yao bi Aisha, ili amkanye mwanae mawazo yake yasiyo yumkinika, kwa kufikiria kuwa aliwahi kuwa na mahusiano na mwanamke kipindi yuko chizi. Kwao waliona madai ya Rashad ni dalili ya uchizi wake kuwa pengine haujapona. Mwenyewe Rashad aliamini akili zake tu. Hakutaka kabisa kuaminiwa na mtu mwengine, alishaona watu wanamdharau hivyo akaamua kuwa hatamshirikisha mtu kwenye kumfuatilia kwake Johari. Na moyoni mwake alijiaminisha kwa asilimia mia kuwa siku moja Johari atamuacha mumewe na kuolewa nae yeye.







    Basi siku moja Johari alikuwa anaondoka toka ofisini mwake, NIB na kuelekea kwenye maegesho ya magari ili aondoke kurejea kwake. Alipofikia gari lake mara akashangaa kumuona Rashad yuko pembeni akimsubiria. Johari alikasirika sana na moyo kwenda mbio na hofu kumjaa hadi akaanza kuongea kwa kulia, “Unataka nini?, unataka nini?”, aliongea Johari, Rashad alimjibu kuwa yupo hapo ili kuonana nae waongee mambo ya muhimu sana. Kwa hasira na kushindwa kutafuta njia ya kumkwepa Johari alimwambia Rashad kuwa apande kwenye gari wakazungumzie mbali na hapo. Basi Rashad akapanda kwenye gari pamoja na Johari na wakaondoka eneo hilo la maegesho la benki ya NIB, na kuelekea maeneo ya ‘Ocean road’, ambako Johari alisimamisha gari na kuanza kumuongelesha Rashad, akimhoji anachokitafuta hasa ni nini.



    Rashad alimuonya Johari asijifanyishe kuwa hamjui na hamkukumbuki. Na kumwambia anafahamu vyema kuwa Johari alimkumbuka ila tu alikuwa akijifanyisha hamjui. Rashad akamuambia Johari sababu ya kumtafuta sana, na kumueleza ilitokana na ukweli kuwa alimpenda sana. Alitaka amwambie jinsi anavyompenda na alitaka kuwa nae, na kwamba hajawahi kuwa na mwanamke mwengine kimapenzi zaidi yake, na aliamini kuwa hakuna mwanamke mwengine mzuri kuliko yeye. Hadi wakati huo machozi yalikuwa wamemjaa Johari, akilia kwa kuchoka mambo aliyokuwa akiambiwa na Rashad. Alibaki akimuangalia huku machozi yakimtoka.



    Johari alilia kwasababu alimuona jinsi Rashad alivyokuwa ‘serious’ kuwa anampenda na anakumbuka kila kitu walichofanya huko numa. Johari alilia kwasababu hakuwaza kuwa siku moja kitu kama hicho kingekuja maishani mwake, na alilia kwasababu alimtazama Rashad na kuona kuwa alikuwa ni mtu aliyekuwa na uwezo wa kufikia hatua kubwa zaidi ya aliyofikia katika kumfuatilifuatilia.



    Safari hiyo, Johari alishindwa kujifanya hamfahamu Rashad na akakiri kuwa ni kweli kumbukumbu za Rashad ziko sahihi kuwa waliwahi kukutana kimwili huko zamani kipindi Rashad akiwa chizi.



    Kukiri kwa Johari kulimfurahisha sana Rashad na kujikuta akitoa machozi ya furaha na kujikuta akianza kumshushia mabusu humo ndani ya gari, kitendo ambacho kilimfanya Johari alie zaidi, na kwa uchungu akaanza kuwaka na kupayuka.



    “Nimeolewa, nina maisha yangu, nina familia yangu, nina watoto wangu. Wewe unanitakia mimi kitu gani hasa”, alilia Johari kwa uchungu mwingi na kushindwa kujizuia. Wakati huo Rashad naye alikuwa akilia.



    “Sijali juu ya mume wako mimi nakupenda wewe”, aliongea Rashad huku akilia, kauli hiyo ilimtia hasira Johari, “Acha upumbavu Rashad, mimi ni mke wa mtu, nakuomba kaa mbali na mimi, chochote kilichotokea baina yetu hakina maana tena, niache na maisha yangu, achana na mimi”, alilia Johari na kuanza kuufungua mlango wa kutokea kwenye gari wa upande wa Rashad na kumuomba ashuke na asimtafute tena. Rashad alishindwa kugoma akashuka toka garini huku akilia, na Johari akimsukuma ashuke haraka huku naye machozi ya hasira yakimtoka basi Johari aliwasha gari na kuliondoa na kuondoka eneo hilo huku nyuma akimuacha Rashad akimuangalia. Ilikuwa ni hali ya kushangaza kabisa, Rashad alikuwa akihisi mapenzi makubwa kwa Johari wakati akijua kabisa Johari ni mke wa mtu, tena mwenye watoto wake kabisa.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Rashad aliumia sana moyo wake siku hiyo Johari aliyomfukuza toka garini. Aliwaza sana na kujiuliza, kwanini Jihari kamtendea vile. Katika hali ya kushangaza Rashad hakutaka kuelewa akilini mwake kuwa Johari alikuwa ni mwanamke aliyekuwa akipenda ndoa yake na familia yake hivyo hakutaka kujihusisha na Rashad.



    Ila sasa kilichompa nguvu zaidi bwana Rashad, ni ukweli kuwa Johari alikiri kuwa kweli wao walikutana kimwili bomani, hivyo Rashad hatimaye akajiamini kabisa kuwa kumbukumbu zake za kutembea na Johari wala haikuwa ni uchizi wake bali ni kumbukumbu sahihi kabisa ambazo muhusika mwenyewe, Johari alikuwa kakiri kuwa kweli hilo suala lilijiri.



    Basi Rashad wala hakukoma aliyokuwa akiyafanya akawa anaendelea kumfuatilia Johari. Mpaka siku ya siku akakutana na ‘article’ ya ‘interview’ aliyowahi kufanyiwa Johari na muandishi mmoja maarufu aliyekuwa akiandika juu ya masuala ya wanawake mitandaoni. Kwenye makala hayo, Johari alizungumzia jinsi ambavyo alikaa kwenye ndoa yake kwa muda mrefu bila ya kupata ujauzito wowote hadi mungu alivyotenda miujiza akapata mtoto wa kwanza kisha akapata watoto wawili mapacha. Hilo lilikuwa ni moja kati ya mengi tu aliyoendelea kuyafahamu juu ya Johari. Johari alikuwa ni mwanamke ambaye habari zake zimezagaa tu mitandaoni, kutokana na cheo chake kikubwa katika benki ya NIB na kazi ya mumewe katika wizara ya mambo ya nje, ilikuwa ni kawaida kuingia ‘youtube’ na kukuta habari zake.



    Rashad aliendelea kumfuatilia Johari, na Johari alitafuta mbinu zote za kumkwepa Rashad, hivi kwamba hata Malcom alianza kunotisi mabadiliko kwa mkewe, kwanza kabisa alimuona mke wake kuwa alikuwa kama mtu mwenye hofu muda wote, na pili aligundua kuwa mke wake alianza tabia ya kuficha ficha shughuli zake za mitandaoni, tena akamuuliza mbona yuko tofauti na Johari akajitetea kuwa kagundua haina haja ya kuposti kila kitu mitandaoni hivyo ndio maana alikuwa akipendelea faragha za kimtandao kadri siku zilivyokwenda.



    Pamoja na kumkwepa Rashad kwa mbinu zote hatimaye Johari aliamua kukutana na Rashad kwenye mgahawa fulani. Katika maongezi hayo, Rashad alimuuliza Johari kwanini, alikuwa akimfuata kule bomani kipindi yuko chizi. Johari alishindwa kujibu jibu hilo, huku hofu ikimjaa.



    Mara Rashad akaachia tabasamu na kukamata mkono wa kuume wa Johari kwa nguvu kumvutia kwake na kumbusu shavuni kwa nguvu bila ya ridhaa ya Johari na kumwambia kuwa, yeye Rashad anafahamu vyema kuwa Johari anampenda hivi kwamba alikuwa yu radhi kulala nae kipindi yuko chizi, na kwa maana hiyo, kama Johari alimpenda yeye kipindi yuko chizi basi kwa hakika lazima atakuwa anavutiwa nae kipindi yuko mzima mwenye akili timamu.



    Kwa hasira Johari alimtamkia Rashad kuwa anampenda mumewe sana tena sana. Na katu hatomuacha Malcom kisa Rashad na kumuonya akae mbali nae na akasimama na kuondoka zake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Eti hadi wakati huo, Rashad alikuwa kajiaminisha kuwa lazima Johari atakuwa anampenda sana hivi kwamba alikuwa radhi kulala nae kipindi yuko chizi. Aliona lazima yatakuwa ni mapenzi ya dhati kwenye kwelikweli ndio yaliyomvutia Johari kujihusisha naye kimapenzi kipindi yuko chizi. Hivyo Rashad alijiaminisha kuwa alichohitaji Johari ilikuwa ni kuachana na Malcom na kuolewa nae yeye ambaye anampenda. Na mawazo hayo yakaanza kumea na kukomaa.

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog