Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

BOMU LA KARAFUU - 5

 







    Simulizi : Bomu La Karafuu

    Sehemu Ya Tano (5)



    Wakati Bwana Seidat akiwa katika hali ya kutaka kupiga magoti, BeBe alimpiga kichwani sehemu ya kichogoni kwa kutumia chuma kifupi lakini kizito, kilichokuwa kimeviringishwa nguo. Bwana Seidat alitoa mguno mdogo wa maumivu akaanguka kama gunia tupu, akawa amepoteza fahamu.

    Haraka haraka, BeBe alitoa donge la tepu lililokuwa ndani ya ule mkoba wake, akamziba mdomo na kisha akatumia tepu hiyo kumfunga mikono na miguu pamoja kwa mgongoni. Hii ilimfanya Bwana Seidat awe katika hali ya kupinda mfano wa upinde pale sakafuni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BeBe alitoa suruali ya kitambaa laini cheusi kaivaa. Akatoa pia fulana laini aina ya T-shirt, nayo nyeusi, akaivaa. Alitoa pia raba nyepesi zilizokuwa na soli ngumu, nazo pia nyeusi akazivaa. Aliweka ile bastola na vitu vingine muhimu ndani ya mifuko ya suruali yake, kisha akavaa tena lile gauni la dira, akajitanda ushungi. Alichukua mkoba wake akashuka hadi pale sebuleni ambapo hakukuta mtu.

    Alichukuwa simu yake ya mkononi kutoka kwenye mkoba wake, akaandika ujumbe mfupi: “Shughuli inaanza, kaa tayari.“

    Kule nje, Dereva Kaku, ambaye wakati wote ule alikuwa ndani ya gari akiwa amekunjua kiti kajilaza, aliupata ule ujumbe, akausoma na kuuelewa. Taratibu alikunja kiti kikawa wima, akaingiza mkono ndani ya koti lake akaigusa bastola iliyokuwemo humo. Hakuitoa. Alishuka kwenye gari akawa kama anajinyoosha.

    Lile jumba lilikuwa kimya, na ilikuwa dhahiri kuwa yale aliyoyasema Bwana Seidat yalikuwa ya kweli, kwamba wale vijana hawakuwepo. BeBe aliangaza pale ukumbini akaona mlango uliokuwa upande wa kulia mwa ukumbi. Aliuendea mango ule akashika kitasa akakizungusha. Mlango ulifunguka na alichokiona mle ndani kilimfurahisha. Kumbe kilikuwa ni chumba cha mitambo ya mawasiliano ya redio, bila shaka ndio mtambo uliokuwa ukiwaunganisha walinzi wa pale kwenye jumba na sehemu nyingine, ikiwa ni pamoja na malango ya kuingia kwenye jumba hilo.

    Haikumchukuwa muda mrefu BeBe kutambua sehemu ya kuwasha na kuuzima mtambo huo. Aliifyatua swichi hiyo na taa zilizokuwa zikiwaka zikazima, hii ikiwa na maana kuwa alikata mawasiliano yaliyokuwepo.

    Wale walinzi wawili waliokuwepo upande ule wa mbele wa lile jengo walimwangalia Dereva Kaku lakini hawakumsemesha. Baada ya kujinyoosha, Dereva Kaku aliegama kwenye gari huku mikono yake yote miwili kaifumbata juu ya tumbo lake. Kwa namna alivyosimama, Dereva Kaku aliweza kuwaona vyema wale walinzi waliposimama, kila pembe ya lile jumba, wote wakiwa wameshikilia silaha aina ya SMG.

    Haukupita muda, alijitokeza mlinzi mwingine kutokea upande wa nyuma ya jumba lile, naye pia akiwa ameshikilia silaha. Alionyesha haraka iliyoashiria kulikuwa na jambo limetokea. Alipomkaribia mlinzi wa kwanza, alimwita:

    “Shaate, nyie seti zenu za radio zinafanya kazi, zetu zimezima.“

    Yule aliyeitwa jina la Shaate alitoa seti yake ya radio akaitazama, naye akasema: “Hee, hata hii yangu imezima. Eti Baita, seti yako ya radio ipo hewani?“

    Baita alikuwa ni yule mlinzi mwingine aliyekuwa pembe ya pili, naye baada ya kuangalia akajibu kuwa haikuwa hewani.

    “Ngojeni niende ndani nikaangalie, labda kuna shoti,“ yule mlinzi aliyetokea upande wa nyuma ya lile jumba alisema kisha akaingia ndani ya lile jumba.

    Kule ndani BeBe alitarajia kuwa kwa vyovyote angeingia mmoja wa walinzi au zaidi kuja kuangalia tatizo ni nini. Alikuwa kajibanza nyuma ya mlango wa kuingilia kwenye kile chumba cha mitambo, mkononi akiwa na kile chuma alichompiga nacho Bwana Seidat.

    Yule mlinzi, ambaye hakuwa na wasiwasi wowote, hakuchukua tahadhari. Bunduki yake akiwa kaitundika begani, alifungua mlango akaingia kwenye kile chumba, mawazo yake yote yakiwa kwenye mitambo. Alipopita tu, BeBe alimshushia kile chuma kichogoni, chini kidogo, pale ambapo kichwa kinaungana na shingo. Mlinzi alitoa mguno kwa mbali, na kabla ya kuanguka akiwa amepoteza fahamu, BeBe alimuwahi na kumlaza chini taratibu.

    Mle ndani ya chumba cha mitambo hamkuwa na nafasi ya kuweza kuuficha ule mwili wa yule mlinzi, kwa hiyo ilibidi BeBe auburuze kwa haraka haraka hadi pale sebuleni akausukumiza nyuma ya moja ya yale masofa. Alitoa kichupa kidogo kilichokuwa na hewa ya usingizi, akampulizia yule mlinzi puani, kisha akarudi tena kwenye kile chumba.

    Tukio hilo lilichukuwa kama dakika tano hivi, na kule nje wale walinzi wengine wakapatwa na wasiwasi.

    “Aisei, Shaate, hebu nenda kamsaidie huko ndani, labda kuna tatizo kubwa,“ yule mlinzi aliyeitwa kwa jina la Baita alimweleza mwenzie, ambaye bila kusita aliweka bunduki yake begani akaingia mle ndani. Naye bila kuchukuwa tahadhari yoyote, alikwenda moja kwa moja hadi kwenye ule mlango wa chumba cha mitambo, akaufungua, lakini hakuingia. Akiwa bado ameushikilia ule mlango kwa mkono wake wa kulia, alipenyeza kichwa na mabega, akasema:

    “Vipi, Ndize, mbona....“

    Hakumalizia alichotaka kuuliza, kwani kile chuma kilichomwangukia mwenzie na yeye kilimmwangukia. Hata hivyo, yeye hakikumpata sawa sawa, na akaweza kujinusuru huku akipiga ukelele mkali ambao ulisikika hadi kule nje. Ingawa alikuwa na maumivu makali akajaribu kuchoropoa bunduki yake ambayo ilikuwa begani, lakini hakuwahi. Kwa wepesi wa kikomandoo, BeBe aliichomoa bastola kutoka kwenye mfuko wa suruali yake akamlenga na kufyatua risasi iliyompata kifuani upande wa kushoto, akaanguka akiwa mfu.

    Bastola yake BeBe ilikuwa na kizuia sauti, kwa hiyo wale waliokuwa nje hawakusikia mlio, lakini tayari walikwisha sikia ule ukemi alioutoa yule mlinzi. Hapo sasa ndipo kazi ilipoanza kwa ukamilifu.

    16 - Mapambano

    Basi ilikuwa patashika nguo kuchanika. Kule nje Dereva Kaku hakulaza damu. Akitumia ujuzi na mafunzo yake ya kiaskari, alingia shughulini. Yeye bastola yake haikuwa na kizuia sauti, kwa hiyo alipofyatua risasi kumpiga yule mlinzi wa tatu, kishindo kikubwa kilisikika. Risasi kutoka bastola ya Dereva Kaku ilimpata yule mlinzi katikati ya mabega upande wa mgongoni na alidondoka chini akiwa katika hali ya kukata roho.

    Milio ile ya risasi iliwashitua walinzi wengine watatu, wawili wale waliokuwa zamu kwenye lango la kuingilia kwenye lile jumba, na mmoja aliyekuwa lindoni upande wa nyuma wa lile jumba, ambako pia ndiko kulikokuwa na maghala.

    Wa kwanza kujitokeza alikuwa yule aliyekuwa kule nyuma. Alikimbilia upande ule wa mbele huku akiwa ameiweka bunduki yake tayari kwa mashambulizi. Hata hivyo, Dereva Kaku naye alikuwa akimsubiri kwa hamu na alipojitokeza tu hakumchelewesha, akiwa amezingatia kanuni moja kuu ya vita, kwamba katika mapambo muwahi adui, usipomuwahi atakuwahi wewe.

    Dereva Kaku alimuwahi yule mlinzi kwa kumfyatulia risasi iliyompata tumboni. Kwa vile yule mlinzi naye alikuwa tayari amekikaza kidole chake kwenye kamsumari kakufyatulia risasi, alipokuwa anaanguka na kukata roho risasi zilifyatuka kutoka kwenye bunduki yake na kusambaa ovyo. Kwa bahati nzuri hata risasi moja haikumpata Dereva Kaku.

    Kule ndani BeBe alisikia shughuli iliyokuwa ikiendelea kule nje, akafahamu kuwa Dereva Kaku alikuwa kesha ingia ulingoni. Kwa vile yeye alishamaliza kazi kule ndani, alisubiri hadi mrindimo wa risasi ulipozima. Hakutoka nje, bali alipanda tena juu ghorofani ambako alipenua moja ya mapazia ya dirisha akaangalia chini. Alimuona Dereva Kaku akikimbia na kujibanza nyuma ya tangi moja la kuhifadhia maji, kwa jina linalojulikana sana ni “Sim Tank.“

    BeBe alitoa simu ya mkononi kutoka mfuko wa suruali yake akapiga namba ya Dereva Kaku. Ilipoita, Dereva Kaku aliipokea.

    “Ndiyo mama, huku nje naona wawili wamezima, lakini nafikiri wale walioko kwenye lango la kuingilia huenda nao wanajipanga kwa mashambulizi. Unasemaje?“

    “Kazi nzuri. Wewe bana papo hapo ulipo, huku juu mimi ninayo fursa nzuri ya kuona kinachoendelea kule kwenye lango. Kwa sasa naona kuko kimya na sioni harakati zozote zikiendelea, bila shaka wanashauriana cha kufanya. Tuwape dakika tatu tu, kisha tutaamua nini la kufanya.“

    “Sawa mama, bila shaka na wao wana simu za mkononi na huenda wakawa wanawasiliana na wenzao, sijui kama huko nyuma ya hili jumba kuna walinzi wengine.“

    “Kwa sasa hapana. Kulingana na yule bwana niliyekuwa naye kule juu, walinzi wengine wameshakwenda lindoni kwenye njia ambayo magari yanayosafirisha karafuu kwenda pwani yanapita. Amesema tayari magari matano yalishaondoka kuelekea huko, hii ikiwa na maana kuwa kule nyuma kwa sasa hakuna walinzi.“

    “Kwa hiyo ina maana kama yule jamaa yetu waliyemteka yupo hapa huenda ikawa wamemfungia huko nyuma au mahala pengine.“

    “Ni kweli, na ndivyo alivyonieleza huyu bwana huku juu. Pei yupo kwenye moja ya maghala huko nyuma, na anasema kuwa mara ya mwisho alipomwona alikuwa bado yu hai lakini katika hali dhaifu sana.“

    “Sawa, naona dakika mbili zimekwisha, je kuna dalili zozote za harakati kwenye lile lango.“

    “Hapana, sioni...subiri, subiri kwanza, naona jamaa wameamu kujitokeza, kumbe walikimbilia kwenye lile rundo la matumbawe upande wa kulia, karibu kidogo na lile lango. Wamesimama, na wanaangalia huku na kule, naona wameamua kuja kuangalia huku kumetokea nini. Wanakuja kwa mtindo wa kulindana, mmoja akikimbia mbele, mwingine anamlinda mwenzie. Kuwa tayari, mimi nitamlenga wa mbele, wewe mlenge wa nyuma.“

    “Sawa mama, nipo tayari...anhaa, na mimi sasa nawaona, wanakaribia, nadhani wakati mzuri wa kuachia risasi ni watakapofika kwenye ule mti wa ua linalofanana na mchikichi.“

    “Sawa kabisa, kumbe bado upo makini, ndio, yule wa kwanza akivuka pale tuziachie.“

    Na ndivyo ilivyokuwa. Yule mlinzi wa kwanza alipovuka tu lile uwa la mchikichi huku akikimbia zigzag, mwenzie alifuatia na kufika pale alipotoka. BeBe alikuwa wa kwanza kuachia risasi ambayo ilimpata yule mlinzi begani upande wa kulia, akaanguka na bunduki yake ikamtoka, lakini hakufa. Yule mlinzi wa pili alijibwaga chini, akainua kichwa juu kuangalia kule mlio wa bunduki ulipotokea, lakini hakuwahi kufanya chochote, kwani risasi zilizoachiwa na Dereva Kaku zilimchanachana mbavu na kummaliza.

    Yule mlinzi wa kwanza alijaribu kujiburuza kutaka aifikie bunduki yake iliyokuwa umbali wa kama futi mbili hivi kutoka pale alipoanguka, lakini hakufaulu maana Dereva Kaku, ambaye wakati huo alikuwa akitumia bunduki aina ya SMG, aliachia raundi nyingine ya risasi ambazo zilimwingia vyema yule mlinzi maeneo ya kiuno na kumviringisha huku akiwa ameachana kabisa na roho yake.

    BeBe alimwendea Bwana Seidat pale alipokuwa amemfunga, akaona bado anapumua. Alimwacha alivyo, alishuka kutoka kule ghorofani akaungana na Dereva Kaku. Walikimbilia kule nyuma ya jengo kwenye maghala ili kumtafuta Pei.

    15 – Sekeseke

    Wakati mapambano yakiendelea kule nyumbani kwa Bwana Mudrick, sekeseke zito lilikuwa likipamba moto pia pwani ya pili ya kisiwa cha Chumbe, ambako kikosi maalum cha wanamaji wa SIAFU kilikuwa kimejiweka tayari kwa mapambano. Kama ilivyokuwa imepangwa, askari wa kikosi hicho walipelekwa pwani ile ya Chumbe kwa mashua maalum, na walishushwa umbali wa kama kilomita mbili hivi kutoka ufukwe ambao maboti ya waendesha magendo yalisubiri kupokea marobota ya karafuu kuyapeleka kwenye meli.

    Kutokea pale waliposhushwa, askari hao ambao idadi yao ilifika 30, walisonga mbele kwa kuambaa ambaa na msitu wa miti ya miombo hadi walipofika umbali wa kama mita mia tano hivi kutoka ufukweni, ambapo waliingia ndani zaidi. Walitokea kwenye barabara ambayo malori yaliyobeba karafuu kuelekea pwani yangepita na wakawa wanasubiri, wakati huo ikiwa tayari ni majira ya saa moja usiku na giza lilishaingia. Hata hivyo, mwezi mpevu nao ulikuwa umeshapanda kutokea upande wa mashariki na hivyo kutoa mwanga wa kutosha.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Taarifa walizokuwa wamepewa ni kwamba kila gari lilikuwa na dereva na mlinzi mmoja aliyekuwa na silaha, na kwamba magari yalikuwa kwenye komvoi yakiongozwa na gari dogo lililokuwa na wale vijana wawili, Barshid na mwenzake. Na kwa upande wa nyuma, lilikuwepo gari jengine lililokuwa na wale vijana wawili waliomteka Pei. Taarifa ambayo BeBe hakuwa nayo ni kwamba kumbe Pei hakuachwa kwenye lile ghala, bali alikuwa ndani ya lile gari la wale vijana waliomteka, na nia yao ilikuwa ni kwenda kummaliza kule pwani kisha wautupe mwili wake baharini kiwe kitoweo cha papa.





    Taarifa walizokuwa wamepewa ni kwamba kila gari lilikuwa na dereva na mlinzi mmoja aliyekuwa na silaha, na kwamba magari yalikuwa kwenye komvoi yakiongozwa na gari dogo lililokuwa na wale vijana wawili, Barshid na mwenzake. Na kwa upande wa nyuma, lilikuwepo gari jengine lililokuwa na wale vijana wawili waliomteka Pei. Taarifa ambayo BeBe hakuwa nayo ni kwamba kumbe Pei hakuachwa kwenye lile ghala, bali alikuwa ndani ya lile gari la wale vijana waliomteka, na nia yao ilikuwa ni kwenda kummaliza kule pwani kisha wautupe mwili wake baharini kiwe kitoweo cha papa.



    Kwa hiyo, BeBe na Dereva Kaku walipofika kule kwenye maghala wakiwa na matumaini ya kumwokoa Pei, waliambulia patupu. Walizunguka kwenye maghala yote, na yalikuwa makubwa yaliyosheheni marobota ya karafuu, lakini hawakufanikiwa kumpata. Walichokiona ilikuwa ni kile kiti alichokuwa amefungwa kamba, ambacho kilikuwa kimetapakaa damu, ambayo pia ilisambaa sakafuni.



    “Duu, hawa jamaa kweli washenzi, bila shaka watakuwa wameondoka naye, au unafikiriaje mama?“



    “Nadhani fikra zako ni sahihi Kaku, itakuwa ama wameondoka naye akiwa hai, au wameshammaliza na wamemfukia mahali. Mimi nadhani hapa hakuna la maana, itabidi tuwafuate hukohuko pwani.“



    “Nakubaliana na wewe, mama, twende zetu, nadhani hawako mbali sana, maana barabara za huku ni mchanga mtupu, na kwa malori yenye shehena ya mzigo mzito hayawezi kuwa na mwendo wa kasi.“



    Wakati wanaongelea hayo, simu ya BeBe iliita, akaipokea.



    “A5, mambo yako vipi huko? Huku kulikuwa na sekeseke kidogo, huyu Bwana Mudrick alikuwa anataka kutoroka. Sijui kumetokea nini huko, lakini alipokea simu na ghafla alikurupuka kutoka alipokuwa ameketi na baadhi ya waheshimiwa akakimbilia kwenye gari lake.“



    “Mkuu, hujakosea, bila shaka alikuwa anajaribu kutoroka, huku kulikuwa na mpambano mkali, bila shaka watu wake walimfikishia taarifa. Je mmemtia mbaroni?“



    “Naam, vijana walikuwa makini kufuatilia nyendo zake tangu alipoingia hapa kwenye uwanja wa sherehe. Hivi sasa yupo pamoja na rafiki yake Swadif mahabusu kituo cha polisi. Vipi, mmesalimika?“



    “Tupo salama Mkuu, na huyu dereva wangu amefanya kazi nzuri sana. Lakini mwenzetu tumemkosa.“



    “Hee, Pei wamemuua?“



    “Hatuna uhakika na hilo, Mkuu. Tunahisi ama wamemuua wakamfukia mahala, au wameondoka naye, maana komvoi yao imeshaondoka hapa kuelekea pwani. Na kama wanaye huko, basi huenda wameshamuua wanakwenda kumtosa baharini, au kama bado yu hai, basi wanampango wa kwenda kumuulia huko huko na kumtosa baharini.“



    “Looh, hiyo sasa kazi. Umepanga nini?“



    “Mkuu, tunawafuata huko huko waliko ili kama wanaye basi tukajaribu kumwokoa Pei, japo tuupate mwili wake kama wameshamuua.“



    “Ni uamuzi mzuri A5, la muhimu ni nyinyi kuwa waangalifu ili nanyi msije mkaangukia mikononi mwao. Bila shaka sasa utaweza kuwasiliana kwa radio na wanamaji wa SIAFU, ambao tayari wapo huko pwani ya mashariki. Ni vyema ukawafahamisha kinachoendelea kwa upande wako. Jina la kiongozi wao ni Hamduni, ana cheo cha Meja.“



    “Asante Mkuu, nitafanya hivyo. Mkuu, naomba waletwe askari hapa kwenye hili jumba pawe na ulinzi, na pia waje wamchukue huyu mwendesha magendo kutoka Ngazija ambaye bado yu hai.“



    “Sawa A5, hilo litafanyika.“



    “Na, Mkuu, wanapokuja huku wachukue tahadhari, kwani hatuna uhakika walinzi wa lango la mwanzo la kuingilia huku bado wapo au wamekimbia.“



    “Vyema, watachukua tahadhari. Kila la kheri A5.“



    “Asante Mkuu.“



    Baada ya mazungumzo hayo, BeBe na Dereva Kaku walipanda kwenye gari walilotoka nalo mjini, lile la Mkurugenzi Swadif. Kabla ya kuondoka, BeBe alimtaka Dereva Kaku aangalie geji ya mafuta ili kuhakikisha kuwa yapo mafuta ya kutosha.



    “Mafuta ni mengi, bado tunatumia tangi kubwa ambalo limepungua lita chache tu, na tangi dogo bado limejaa. Hakuna wasiwasi, tutakwenda na kurudi.“



    “Sawa, twende zetu, lakini kumbuka kuwa huko mbele kuna geti la kuingilia huku. Tuchukuwe tahadhari, kama walinzi wapo, tuwe makini.“



    “Bila shaka, mama. Kitakachotusaidia ni kwamba kama wapo hawatakuwa wakitegemea kuna gari jengine linakwenda huko, yawezekana tukakuta hawajajiandaa.“



    “Ni kweli, lakini hilo la kutotegemea gari lingine linaweza pia kuwa baya kwa upande wetu, na hasa kama wamepata taarifa ya mapambano yaliyotokea huku.“



    “Aaah, kweli, upo sahihi, tunaweza kuwa tunajipeleka wenyewe kwenye mdomo wa mamba.“



    “Usiwe na wasiwasi, tutakabiliana nao.“



    Mwendo wa kutoka kwenye lile jumba hadi kwenye geti la kutokea upande ule wa pili haukuwa mrefu. Baada ya mwendo wa kama kilomita moja hivi, taa za ile gari zilimulika kibanda cha walinzi, kukiwa pia na geti jeusi. Katika umbali wa mita kama mia moja, hawakuweza kuona dalili zozote za kuwepo watu pale kwenye geti, lakini waliposogea zaidi na kukaribia umbali wa mita hamsini, walijitokeza walinzi wawili, wote wakiwa na silaha mikononi.



    Walinzi hao ambao walikuwa wamevaa sare sawa na wale wenzi wao kule kwenye lile jumba la Bwana Mudrick, walisimama mmoja kila upande wa barabara, karibu na geti. Wote walilenga lile gari, wakiwa na bunduki aina ya Rifle - SAR. Mmoja wao alikuwa pia na tochi iliyokuwa na mwanga mkali, ambayo aliichezeshachezesha kuashiria kuwa lile gari lisimame pembeni.



    “Kaku, wako wewe ni yule wa upande wa kulia, wangu ni wa kushoto. Lisogeze gari karibu zaidi, kisha zima taa zote. Ukisimamisha tu gari, tukitoka ni mashambulizi bila kusita, umenipata.“



    “Nimekupata vyema mama.“



    Walipowakaribia wale walinzi, kama mita thelathini hivi kuwafikia, Dereva Kaku alisimamisha gari na kuzima taa zote. Kwa pamoja walifungua milango na kuruka. Wale walinzi hawakuwa wajinga, walikisoma vyema kile kitendo na hawakuzubaa. Walifyatua risasi kwa pamoja. Yule aliyemlenga BeBe alimkosa, lakini yule aliyemlenga Dereva Kaku alibahatisha. Risasi ilimparuza Dereva Kaku sehemu ya chini ya paja lake la mguu wa kushoto, karibu kidogo na goti.



    Bastola ya BeBe ilijibu mapigo, na mmoja wa wale walinzi alitoa ukemi mkali wa maumivu, akaanguka. Risasi ilimpata barabara sehemu ya chini ya tumbo, karibu sana na nyonga ya kulia. BeBe alitumia kanuni moja muhimu sana, kwamba unapolenga mtu akiwa mbali na ukiwa katika hali ya kuviringika, basi lenga sehemu iliyo kubwa ya mwili wake, ambayo ni tumbo.



    Wakati mwenzie akigaagaa kwa maumivu, yule mlinzi wa pili alifanya kosa lililomgharimu. Badala ya kulenga na kufyatua risasi kupiga adui, yeye aligeuka kumwangalia mwenzie. Nukta hizo chache za kitendo hicho zilimwezesha BeBe kufyatua risasi nyingine ambayo nayo alitumia kanuni ileile ya mwanzo, na safari hii risasi ilimpata mlinzi wa pili juu kidogo ya kitovu. Yule mlinzi alianguka, na kama ilivyokuwa kwa mwenzie, naye akawa hajiwezi kwa lolote.



    “Hongera mama, kwa hakika unajua kulenga.“



    “Usijali, vipi wewe, naona damu inavuja pajani.“

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Looh, ile ilikuwa almanusurina kwangu, lakini si jereha kubwa sana, ile risasi imeniparuza tu.“



    Basi kwa pamoja waliwaendea wale walinzi, ambao wote bado walikuwa wakipumua kwa mbali na hawakuweza kusema lolote. Waliwaburuza na kuwaingiza kwenye kile kibanda, kisha wakafungua lile geti wakaendelea na safari yao.



    Wakiwa katika mwendo, BeBe aliwasha radio ya mawasiliano iliyokuwa imefungwa kwenye lile gari. Alibonyeza vitufe viwili-vitatu, na baada ya sekunde kadhaa akapata mawasiliano.



    “Halloo, A5 hapa, naweza kuzungumza na Meja Hamduni, ova.“



    “Ndiyo Afande, dakika moja, tafadhali, ova.“



    Baada ya sekunde kadhaa:



    “Halloo A5, Meja Hamduni hapa, ova.“



    “Oh, Meja, tupo njiani kuelekea huko pwani mliko. Tupo nyuma ya msafara wa magari ya hawa jamaa, ova.“



    “Sawa, poleni, nimepata taarifa kwa ufupi kutoka kwa KK juu ya kilichotokea huko. Sisi huku tumejipanga vyema, tupo tayari, ova.“



    “Vyema, pamoja na kuwatia mbaroni hawa jamaa, vilevile tujitahidi kumwokoa Pei kama wapo naye. Nitashukuru kupata taarifa msafara wao utakapowafikia, ova.“



    “Sawa, tutakupa taarifa.“



    Kama alivyosema Dereva Kaku, ile barabara ilikuwa ni mchanga mtupu, tena mchanga mkavu kabisa. Ilikuwa dhahiri kuwa yale malori ambayo yalikuwa mbele yao hayakuwa katika mwendo wa kasi. Dereva Kaku aliendesha gari kwa ustadi mkubwa, na aliweza kwenda kwa kasi, wakati mwingi akiwa ameweka gia ya matairi manne.



    Baada ya mwendo wa kama nusu saa hivi, BeBe alisikia kama muungurumo wa gari au magari uliokuwa ukitokea mbele yao.



    “Vipi Kaku, ni masikio yangu tu, au huo ninaousikia ni muungurumo wa gari?“



    Kabla hajajibu lolote, Dereva Kaku alipunguza mwendo wa gari, akasikiliza kwa makini.



    “Ni kweli, huo ni muungurumo wa magari, hii inaashiria kuwa hawako mbali sana.“



    “Utaweza kuendesha bila taa kubwa za gari?“



    “Nitajaribu, mwanga wa mbaramwezi utatusaidia, ingawa kasi itapungua.“



    “Basi zima taa, maana naona huo muungurumo wa magari unaongezeka, bila shaka tumewakaribia.“



    Dereva Kaku alizima taa, wakawa wanasonga mbele, lakini kwa mwendo wa taratibu zaidi. Hawakwenda umbali mkubwa, walipokata kona waliyoifikia, kwa mbele waliona taa za nyuma za gari dogo ambalo lilikuwa kama umbali wa mita mia mbili kutoka walipokuwa. Wakati wakitafakari nini la kufanya, radio ya mawasiliano mle ndani ya gari iliita.





    Dereva Kaku alizima taa, wakawa wanasonga mbele, lakini kwa mwendo wa taratibu zaidi. Hawakwenda umbali mkubwa, walipokata kona waliyoifikia, kwa mbele waliona taa za nyuma za gari dogo ambalo lilikuwa kama umbali wa mita mia mbili kutoka walipokuwa. Wakati wakitafakari nini la kufanya, radio ya mawasiliano mle ndani ya gari iliita.



    “Hallo A5, Meja Hamduni, hapa, unanisikia? Ova“



    “Nakupata vyema Meja, kulikoni? Ova.“



    “Msafara wa jamaa tunauona, wamekaribia vizuizi vyetu, ova.“



    “Ahaa, na sisi tupo nyuma ya gari lao la mwisho, kama mita mia mbili hivi, ova.“



    “Vizuri, hiyo itatusaidia sana kuwadhibiti. Wameshakaribia kabisa kwenye vizuizi, sasa ni mapambano, ova na kwa heri.“



    BeBe alizima redio, akachukua moja ya bunduki aina ya SMG walizozichukua kutoka kwa wale walinzi, akaikagua na kuridhika kuwa ipo safi. Akakagua bastola yake, akaridhika pia kuwa ipo safi.



    “Kaku, ongeza mwendo, hili gari lina ngao kubwa, kaligonge kwa nyuma lile gari lao.“



    Na ndivyo ilivyokuwa. Akiwa bado amezima taa, Dereva Kaku aliongeza kasi, wakati huo wakiwa kama mita mia moja kutoka kwenye lile gari liliokuwa mwisho wa ule msafara. Wale vijana waliokuwa mle ndani walishituka pale gari lao lilipogongwa kwa nyuma. Kwa vile kugongwa kule kulikuwa kwa ghafla mno, kijana aliyekuwa akiendesha lile gari, aina ya Toyota Hilux – Double Cabin, alipoteza mshiko wa usukani. Waliyumba vibaya na tairi za gari lao zikachotwa na mchanga, likapinduka na kubiringika mara moja kisha likalala kiubavu, upande wa dereva ukiwa chini.



    Bila kutumia akili na uzoefu wake wa siku nyingi, Dereva Kaku angeyumba na wao gari lao lingepinduka. Lakini alijitahidi sana kutumia breki na kung’ang’ania usukani, huku akinyoosha tairi zibaki barabarani. Alifanikiwa, lakini ilibidi aligonge tena lile gari na kulisukumiza pembeni, na kisha akafanikiwa kulisimamisha gari lao kama mita kumi hivi kutoka lilipopinduka lile lingine.



    Hata kabla gari halijasimama sawasawa, BeBe alikuwa tayari kesha ufungua mlango na kutoka, akakimbilia lilikokuwa lile gari lililopinduka, akajitupa chini kwenye mchanga, huku akiwa amezibwa na manyasi na miti midogo midogo iliyokuwa pembezoni mwa barabara. Dereva Kaku naye alifanya hivyo hivyo, lakini yeye akawa upande wa pili wa barabara. Walitulia tuli wakisubiri kuona kama angetoka mtu yeyote kutoka kwenye lile gari, wakati huohuo silaha walizokuwa nazo zikiwa tayari kutema risasi kuelekea kwa adui ambaye angejitokeza.



    Dakika mbili hivi zilipita na hakukuwa na dalili zozote kwamba kuna ambaye angejitokeza kutoka kwenye lile gari. BeBe hakudanganyika kutokana na hali ile. Alihisi kuwa waliokuwemo ndani ya lile gari nao huenda walikuwa wakisubiri, na pengine na wao pia walikuwa wameshajiandaa kwa mashambulizi.



    BeBe alishawishika sana kulipiga risasi tangi la mafuta ya ile gari, ambalo lilikuwa likionekana waziwazi, na alijua kama angelipiga lingelipuka. Kilichomfanya asite ni fikra ya uwezekano kwamba huenda Pei akiwa hai au mwili wake kama walishamuua ungekuwa mle ndani ya gari, na alihofia ungeteketezwa na moto.



    Hata hivyo, aliamua kuwa asingeweza kusubiri zaidi, hivyo akamwashiria Dereva Kaku abakie palepale alipokuwa, na yeye taratibu akaanza kujivuta kitumbotumbo akilisogelea zaidi lile gari. Kwa vile upande aliotokea ni ule ambao ulikuwa na matairi, hiyo iliweza kumlinda kwa mashambulizi, na alijua kuwa katika hali ile ya kutambaa kama nyoka, wasingeweza kumuona bila wao wenyewe kujiweka katika hatari.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Aliweza kufika hadi lilipokuwa lile gari, akatulia tena kwa sekunde kadhaa, kisha kidogo kidogo alijiinua akiwa upande wa nyuma wa lile gari. Alipofika usawa wa kioo cha mlango wa nyuma, alichungulia ndani. Kwa upande wa mbele hakukuwa na mtu hata mmoja, lakini kwenye kiti cha nyuma aliona mwili wa mtu ukiwa umelala tuli, na alipoangalia vizuri akaona kuwa mwili huo ulikuwa umezingirwa na kamba.



    Alipoangalia tena upande wa mbele kwa makini zaidi, aliona kuwa kioo kikubwa cha kuzuia upepo cha mbele kilikuwa hakipo kabisa, na mara moja akagundua kwamba wale vijana waliokuwa ndani ya ile gari ndipo walipotokea. Alimwashiria Dereva Kaku amfuate pale alipo, lakini akamtahadharisha kuwa asisimame. Akitumia mwendo wa chura, Dereva Kaku aliweza kumfikia BeBe bila kutokea madhara yoyote.



    “Usiinue kichwa Kaku, nadhani hawa jamaa wamejificha upande ule wa pili na tukijitokeza tu watafyatua risasi. Humu ndani ya gari yumo Pei, lakini kwa jinsi alivyotulia, ama amepoteza fahamu au ameshakufa.“



    “Looh, masikini, hata kama walikuwa hawajamuua, ule msukosuko wa kupinduka gari utakuwa umemwongezea maumivu makubwa kutokana na majeraha ambayo tayari alikuwa nayo.“



    “Ni kweli. Sasa basi, hatuwezi kupoteza muda zaidi, itabidi tuharakishe ili tumpe msaada. Mimi nitasimama ili kufungua mlango ni jaribu kumtoa. Wakifyatua risasi, wewe wavurumishie risasi na hiyo SMG.“



    “Hapana mama, wacha mie nifanye hiyo kazi ya kufungua huu mlango na kumfungua, inahitaji nguvu kidogo. Sisemi kuwa hutaweza, lakini kwangu itakuwa rahisi zaidi, na isitoshe, wewe una shabaha zaidi yangu.“



    “Vyema, basi tusipoteze muda, nipe hiyo silaha.“



    BeBe alijivuta kwa tumbo hadi mwisho wa bodi ya lile gari kwa upande wa mbele, akaelekeza macho yake kule alikofikiria kuwa kama ni mashambulizi ndiko yangetokea. Baada ya kupata ishara kutoka kwa BeBe, Dereva Kaku akajiinua taratibu, akasimama wima, kisha haraka akarudi chini. Hiyo ndiyo ilikuwa salama yake, kwani risasi ziliunguruma kutokea kule kichakani, lakini zikamkosa na nyingine zikapiga bodi ya gari.



    Kitendo kile cha wale adui kufyatua risasi kilimpa BeBe wasaa mzuri wa kufahamu ni upande upi walipokuwa. Alilenga chinichini na kuinua juu kidogo, akiwa na imani kuwa walikuwa ama wamelala chini au wamechuchumaa. Alifyatua raundi mbili za risasi kuelekea mahala ambapo aifikiri wangekuwa wamejificha.



    Kutokana na ukemi ulioashiria maumivu kutoka kule kichakani, ilikuwa dhahiri kuwa risasi kadhaa kutoka bunduki ya BeBe zilitua juu ya mwili wa mtu. Ili kusabibisha kashkashi zaidi, BeBe aliachia tena raundi nyingine kuelekea ilikotokea ile sauti, na safari hii pia ukasikika ukemi wa maumivu.



    Mara ukasikika mchakacho wa mtu ambaye ameamua kukimbia, na BeBe aliposimama kuangalia kule kichakani, mwanga mdogo wa mwezi uliokuwa umezibwa na wingu, ulimwezesha kuona mtu akiwa anapangua miti akikimbia kujinusuru. Ilikuwa ni bahati yake mbaya, kwani BeBe aliachia tena raundi nyingine na safari hii akiwa na uhakika wa anachokilenga. Risasi zilimpata yule mtu sehemu kadhaa mwilini akadondoka chini huku akivunja matawi ya miti midogo aliyoiangukia.



    Wakati BeBe akiwa katika mpambano, Dereva Kaku akawa amefanikiwa kuufungua mlango wa nyuma wa lile gari. Aliingia kwa taabu kidogo kwa vile ule mlango ulifunguka kwa juu na haukuwa na kizuizi. Aliweza kuingia kwa kujibanabana. Alitoa kisu kidogo alichokuwa nacho mfukoni mwake akakata kamba ambazo walizitumia wale vijana kumfunga Pei. Shughuli nzito ilikuwa ni jinsi ya kumtoa kwenye gari akiwa hana fahamu.



    Hata hivyo, wawili ni wawili, kwa kushirikiana waliweza kumtoa wakambeba moja kwa moja kumpeleka kwenye gari lao. Walipokwisha kumlaza kwenye kiti cha nyuma, BeBe alitoa kichupa ambacho kilikuwa na dawa ya majimaji, akatoa sindano na bomba lake, akanyonya kiasi kidogo cha ile dawa. Taratibu alimdunga sindano Pei kwenye mshipa wa mkono wake, akaingiza ile dawa polepole hadi ilipoisha yote.



    “Hee, mama, naona hata unesi ungeuweza. Ni dawa gani hiyo uliyomwekea.“



    “Ina kazi nyingi, lakini kubwa ni kumsisimua mishipa ya fahamu na pia kumpunguzia maumivu atakapozinduka.“



    “Sasa mama, kuna haja ya kuendelea mbele, huyu mwenzetu bila shaka anahitaji huduma ya haraka ili kunusuru maisha yake.“



    “Ni kweli, hakuna haja ya kuendelea, tuwaachie wanamaji wa SIAFU watimize wajibu wao. Geuza gari.“



    Wakati Dereva Kaku anageuza gari, BeBe alikwenda kwenye lile gari lililopinduka, akapanda tena mle ndani ambamo hakukuta chochote cha maana. Dereva Kaku alipokwisha kuligeuza gari alilisogeza hadi pale lile gari lingine lilipokuwa, akaweka gari kwenye sailensa akashuka. Kwa pamoja walikwenda hadi kule walikokuwa wamejificha wale vijana. Wote walikuwa wamekufa. Waliiburuza miili yao hadi kwenye lile gari lao, wakiwa tayari wamechukua bastola zao ambazo waliziokota kule walikowatoa.



    “Twende zetu, wanamaji wa SIAFU wataibeba miili yao watakapopita.“







    16 – Pazia



    Wakati BeBe na Dereva Kaku wakiwa kwenye lile sekeseke lao, kikosi cha wanamaji wa SIAFU kilikuwa na kazi nyepesi sana kule pwani. Mashambulizi yao yalipangwa kivita, na ilikuwa ni kama kuvunja chawa kwa nyundo.



    Burshid na mwenzie, wakiwa kwenye gari lao mbele kabisa ya ule msafara wa malori yaliyobeba marobota ya karafuu, walishituka sana walipokiona kizuizi kilichokuwa mbele yao. Ilikuwa ni ghafla mno, maana wanamaji wa SIAFU walitumia ujanja wakawa wamekiweka kizuizi hicho hatua chache tu kutoka kwenye kona ya mwisho kabla ya kufika pwani. Ilikuwa ni kama umbali wa mita mia nne tu kabla ya kufika ufukweni.



    Kwa vile hawakutegemea kukuta kizuizi kwenye msafara wao, wale vijana walichanganyikiwa. Ilikuwa dhahiri kuwa hawakuwa na taarifa ya yaliyotokea kule kwenye jumba lao, kwa mzee wao Mudrick. Hii ilitokana na ile hali kwamba mawasiliano yao ya radio yalikatika na hawakuweza kutumia simu za mikononi kwa vile mitandao ya simu ilikuwa haijafika upande ule wa pwani ya Chumbe.



    Kuwapo kwa vile vizuizi kuliwapapatisha mioyo, na ni mshituko huo ndio uliowafanya watiwe mbaroni kirahisi, kama vile samaki walioleweshwa na utupa. Walisimamisha gari lao ghafla kama mita tano hivi kutoka pale yalipopangwa magogo kuziba barabara. Walibaki ndani ya gari wakisubiri ni nini kingetokea, huku wote wawili wakiwa na bastola mikononi.



    Kwa vile gari lao lilisimama ghafla, yale malori yote yaliyokuwa nyuma nayo ilibidi yasimame. Hali hiyo ndiyo ambayo ilikuwa ikisubiriwa na wanamaji wa SIAFU, ambao walikuwa wamejipanga vyema wakiongozwa na Meja Hamduni.



    “Ninayeongea nanyi ni Mkuu wa Kikosi Maalum cha Wanamaji Zanzibar. Askari wamelenga silaha kuelekea magari yenu pande zote za barabara. Kwa kifupi ni kwamba mmezingirwa na mpo chini ya ulinzi. Jisalimisheni. Tokeni kwenye magari mikono yenu ikiwa imenyooshwa juu. Nitahesabu moja hadi tano, wote muwe mmeshuka kutoka kwenye magari. Yeyote atakayeikaidi amri hii atalipuliwa.“



    Hiyo ilikuwa ni sauti nzito na kali ya Meja Hamduni akitumia kipazaa sauti, naye akiwa bado amejificha pamoja na vijana wake. Wote walikuwa wamelala kwenye manyasi marefu na vichaka vya miti midogo kando ya barabara. Wakati huohuo, taa maalum ambazo walikuwa wamezisimika pembeni mwa barabara ziliwashwa, zikatoa mwanga uliotosha kuyamulika magari yote yaliyokuwa kwenye ule msafara.



    Meja Hamduni alipofika tatu katika kuhesabu kwake, wale madereva wa malori yote matano walishuka mmoja baada ya mwingine. Walijikusanya mahala pamoja, mikono yao ikiwa imenyooshwa juu ya vichwa vyao.



    Meja Hamduni alipofika nne katika kuhesabu, walinzi wote watano waliokuwa kwenye yale malori walikuwa wameshashuka upande wa pili, nao pia walijikusanya pamoja huku mikono yao ikiwa imenyooshwa juu ya vichwa vyao. Kwa hiyo wakabakia wale vijana waliokuwa kwenye lile gari dogo lililokuwa mbele kabisa.



    Meja Hamduni alifikisha tano na hivyo kukamilisha hesabu yake, lakini bado wale vijana hawakushuka kutoka kwenye lile gari, na wala hawakujitokeza. Sekunde kadhaa zilipita, na kilichofuata ilikuwa ni mrindimo wa risasi na milio ya risasi hizo zilipopasua kwenye vioo, kuchana mabati na kugongana na vyuma kwenye lile gari.



    Wakati shambulizi hilo likifanyika, askari kadhaa wa kikosi cha wanamaji wa SIAFU walikuwa wamejitokeza pande zote mbili za barabara na kuwatia mbaroni wale madereva na walinzi ambao walitii amri ya kujisalimisha.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ama ulikuwa mrindimo wa risasi uliodumu kwa takribani dakika moja hivi. Lilikuwa shambulizi la kitaalam lililokuwa na lengo maalum, na lengo hilo lilitimia. Wale vijana hawakuwa na ujarisiri wakuhimili mshindo wa mrindimo ule wa risasi.



    Ingawa hakuna hata risasi moja iliyowapata, mpasuko wa matairi ya gari lao na mlio wa risasi zilipotoboa mabati na kugonga vyuma vya gari, vilitosha kuwajaza hofu wale vijana. Waliamua kujisalimisha baada ya kuona kuwa walikuwa wamezidiwa nguvu na wasingeweza kufurukuta.



    Walitiwa mbaroni wakaunganishwa na wale wenzao. Wakati huohuo, baadhi ya wanamaji ambao walikwenda kule ufukweni nao walifanikiwa kuwatia mbaroni wenye mitubwi iliyokuwa ikisubiri yale malori.



    Kwa hakika ilikuwa ni oparesheni iliyotekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Yale malori na shehena za marobota ya karafuu yalirudishwa hadi kule kwenye jumba la Mudrick. Karafuu yote iliyokuwa kwenye maghala ilirejeshwa mikononi mwa Serikali, na wale wote waliohusishwa na mtandao wa waendesha magendo walitiwa mbaroni.



    Kwenye kikao cha tathmini ya oparesheni ile ya Bomu la Karafuu, kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa SIAFU, Kessi Kusi, a.k.a. KK, BeBe, Pei pamoja na Dereva Kaku walipongezwa kwa kazi nzuri.



    “Mmefanya kazi nzuri sana A5, Pei na Ndugu Kaku. Pongezi hizi si za kwetu tu kama viongozi wenu kwenye vikosi vyetu, bali ni pongezi pia kutoka juu kabisa katika uongozi wa Serikali. Najua Pei bado una mawazo kuwa kukamatwa kwako kumetia doa ufanisi wako, lakini hivyo sivyo hata kidogo. Ukweli ni kwamba kukamatwa kwako ndiko kulikowezesha kuwafikia na kuwatia mbaroni wale waendesha magendo. Kwa hiyo usijisikie vibaya.“



    “Anachosema KK ni sahihi kabisa. Pei, umetoa mchango mkubwa sana, na ni mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye mafanikio makubwa zaidi katika kazi yako. Hongera za kipekee ni kwako Ndugu Kaku. Hii haikuwa shughuli yako, lakini ulijitolea na kuweka maisha yako hatarini. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa na askari wengine wastaafu, na hata raia wa kawaida. Moyo huu wa kujitoa muhanga kwa maslahi ya taifa ni muhimu sana.“



    “Ni sawa kabisa anachosema MB, umeonyesha mfano mzuri na wa kuigwa. Na kwa kujitolea kwako huko na mchango wako mkubwa ulioutoa kwenye oparesheni hii nafurahi kukuarifu kuwa utatunukiwa zawadi ambayo itakuwa siyo ukumbusho kwako, bali pia ni zawadi ambayo bila shaka itabadilisha mwelekeo wa maisha yako na ya familia yako kuwa bora kwa kiasi kikubwa.“



    “Nawashukuru sana Wakuu, na pia namshukuru mama hapa kwa kuniruhusu kuingia kwenye mapambano yale. Imenipa faraja sana kupata fursa ya kuitumikia nchi yangu kwa namna ile. Na kitakuwa tayari wakati wowote kushiriki kwenye oparesheni nyingine endapo mtaona kuwa nitaweza kuwa na mchango wowote.“



    “Je, A5 una lolote la kusema?“



    “Wakuu, nafurahi tu kwamba oparesheni hii ya Bomu la Karafuu imemalizika kwa mafanikio makubwa. Bila shaka pamoja na ushindi tuliopata, imekuwa ni fursa pia ya kujifunza mengi yatakayotuwezesha kufanya vyema zaidi katika operasheni zijazo.“



    “Ni kweli kabisa A5, tumejifunza mengi, na pale tulipoteleza tutarekebisha ipasavyo ili vikosi vyetu viendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.“



    “Naungana nawe KK, kuna mengi tuliyojifunza na yatatuwezesha kuimarisha mbinu na mikakati ya utendaji wa vikosi vyetu kwa siku zijazo. Tutakuwa na vikao maalum vya ngazi za juu kutathmini kwa undani juu yaliyotokea kwenye opareshi hii, na hivyo tutapata fursa ya kulenga kwenye ufanisi bora zaidi.“



    Baada ya maneno hayo yaliyotamkwa na Mkuu wa kikosi cha BUNDI, Momaa Bulo, a.k.a. MB, wote waliokuwepo pale walisimama wakapeana mikono ya kupongezana. KK hakuishia kumpaka mkono BeBe, bali pia alimuuliza:



    “Enhee, A5, lile suala la kuolewa hapa Unguja limeishia wapi?“



    BeBe alicheka kidogo kisha akajibu: “Aaah, usinikumbushe ukiwa Mkuu, mume mtarajiwa yupo rumande, na huenda akaozea jela, nimeanza uchumba na nuksi.“



    “Basi labda kuna mkono wa mtu!“



    Huyo alikuwa ni MB, ambaye alisababisha kicheko huku wakitoka kwenye ule ukumbi wa mikutano.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    **Mwisho**



0 comments:

Post a Comment

Blog