Search This Blog

Sunday 19 June 2022

ROHO ZA KISHETANI - 4

 





    Simulizi :Roho Za Kishetani
    Sehemu Ya Nne (4)



    Kuna ambaye atakuwa ofisini, kompyuta mbele yake akitekeleza majukumu ya kazi yake. Ghafla atainamia meza na kukata roho. Mwingine atakuwa akiifuata lifti ya jengo ili apande. Hataifikia. Ataanguka ghafla sakafuni na kuanza kutokwa damu nzito na povu zito mdomoni, masikioni na puani kabla ya kufa muda mfupi baadaye.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika msikiti fulani waumini watakuwa katika sala, lakini ghafla, mmoja, mmoja wataanguka chini na kufa katika hali itakayoshangaza na kutisha. Kama vile haitoshi, ndani ya kanisa moja napo kutazuka tukio la ajabu. Huenda kwaya itakuwa ikiimba katika kuwasilisha ujumbe wa Neno la Mungu kwa washarika au huenda kasisi atakuwa madhabahuni akihubiri na huenda pia waumini wote watakuwa wamesimama, wakiimba mapambio kwa nguvu na furaha huku wakipiga makofi na vigelegele.

    Chochote kile kitakachokuwa kikiendelea kanisani humo kitasitishwa ghafla, na badala yake, mmoja baada ya mwingine wataanguka huku povu lililochanganyika na damu likiwatoka vinywani, puani na masikioni. Dakika kama tano baadaye ndani ya kanisa hilo hakutakuwa na kiumbe aliye hai! Kila aliyekuwa hai muda mfupi uliopita, akishangilia kwa kuimba nyimbo za kusifu atakuwa sakafuni, maiti!

    Yatakuwa ni maafa makubwa sana , aliwaza. Siyo chini ya watu mia moja au mia mbili watakaopoteza maisha ndani ya siku tatu tu!

    Haiwezekani! alijisemea kimoyomoyo. Ndiyo, hakuwa tayari kuliachia tukio hilo lifanyike, akishuhudia.

    Wakati huo anga ilizidi kutakata. Ilitimu saa 11:30. Kwa mujibu wa Muganyizi, operesheni ingeanza kutekelezwa saa 4 asubuhi ya siku hiyo katika majengo yenye ofisi za taasisi mbalimbali. Kesho yake ambayo ingekuwa ni Ijumaa, msikiti mmoja uliokusudiwa ungefuata, na Jumapili ndipo zoezi lingehitimishwa kwa chupa ya mwisho kufunguka kanisani.

    Sasa kila sekunde ilipopita, chuki dhidi ya Muganyizi ikazidi kujiimarisha moyoni mwa Tina. Lakini hakutaka kuchukulia pupa. Aliamini kuwa pupa ya aina yoyote ingetoa matokeo mabaya, jambo ambalo hakutaka litokee.



    “Natoka,” Muganyizi alimwambia pindi alipomwona ameduwaa, akimtazama. “Tukutane tena saa saba mchana hapahapa. Humuhumu chumbani. Hata kama nitachelewa, tafadhali unisubiri. Naamini utanipokea vizuri na kunilea vizuri kama ilivyonilea usiku huu uliopita.”

    Bado Tina aliduwaa, akimtazama. Alisikia kila alichoambiwa lakini badala ya kupinga au kuafiki, yeye aliendelea kuduwaa. Ni pale alipozinduka na kufumbua mdomo, akitaka kusema lolote alilopanga kulisema, ndipo alipogundua kuwa alikuwa peke yake chumbani humo.

    Muganyizi alishatoweka!

    “Haiwezekani!” aliropoka kwa mnong'ono.

    Papohapo akakurupuka kitandani, akajitanda shuka. Akatoka chumbani humo haraka akimfuata Muganyizi. Alipofika nje hakumwona. Akageuka nyuma na kukutana na mhudumu wa gesti hiyo akitoka ndani ya chumba kimojawapo.

    “Vipi dada kuna tatizo?” mhudumu alimwuliza.

    Tina alifikiri haraka na kuamua kumwongopea mhudumu huyo. “Aaa... hapana, hakuna tatizo lolote,” alimjibu huku akirudi chumbani.

    Mhudumu yule hakuonekana kujali. Tayari kulishapambazuka. Mji ulikwishachangamka. Huko nje ya gesti kulisikika ngurumo za magari na sauti za watu mbalimbali. Hivyo hata kitendo cha Tina kuonekana hapa mapokezi muda huo, saa 12 hakikuwa ni jambo la ajabu wala la kumshangaza yeyote. Na si yeye pekee ndani ya gesti hiyo waliokwishaamka.

    Baadhi ya wapangaji wengine walikwishatoka vyumbani. Kuna waliokwishaondoka, na wengine walikuwa wakioga. Ni hali hiyo ambayo haikumtia mashaka mhudumu huyo. Alibaki akimtazama Tina akirudi chumbani huku akitembea kwa hatua fupifupi za haraka.

    Kwa ujumla Tina hakuwa timamu kifikra wakati huo. Alihisi kichwa kizito. Kabla hajaingia chumbani alishasonya mara mbili na kupiga ngumi kiganjani, uso ukiwa umekunjamana, hali iliyomfanya mmoja wa wapangaji aliyekuwa akitoka bafuni amtazame kwa mshangao kidogo kabla ya kujitoma chumbani mwake.

    Tina alifungua mlango wa chumba kwa nguvu na kuufunga kwa nguvu vilevile nyuma yake. Mambo mengine aliyafanya haraka zaidi na dakika kumi baadaye alikuwa ameshaoga. Saa 12:30 alikuwa mbali sana na gesti hiyo.



    *****



    SAA 3:00 asubuhi, makamanda watatu wa ngazi za juu wa Jeshi la Wananchi, wawili wa Jeshi la Polisi na Maofisa Usalama wa Taifa watatu walikuwa wakikaribia kuhitimisha kikao. Taarifa zilizotolewa na Kanali Thomas ziliweka uhai wa matumaini kwa wajumbe wengine.

    Hakikuwa ni kikao ambacho kilizuka kama mzuka. Hapana. Kulikuwa na chanzo. Ni baada ya mrembo Tina kutoka ndani ya ile gesti ambako usiku uliopita alikuwa na Muganyizi wakiistarehesha miili yao , ndipo alipoamua kumpigia simu mkuu wake wa kazi, kituo cha Oysterbay. Saa moja kamili walikuwa pamoja ofisini ambako Tina alimsimulia kila alichokipata kwa Muganyizi.

    Ikawa ni habari kubwa masikioni na akilini mwa Mkuu wa kituo cha Oysterbay. Nusu saa baadaye habari hiyo ilikuwa imevifikia vichwa vingine vya makamanda wa Jeshi la Polisi ambao nao wakawasiliana na Maofisa Usalama wa Taifa na makamanda wa Jeshi la Wananchi.

    Mkakati mzito ukaandaliwa na wakuu hao katika kuinusuru nchi. Na walipokuja kukutana tena, ni Kanali Thomas aliyetoa taarifa ambayo kwa wengine ilikuwa ni taarifa njema kwa kiasi fulani.

    “Hadi sasa hakuna jengo lolote lililogundulika kutegwa kifaa chochote cha hatari,” alisema kanali huyo. “Tukiachilia mbali majengo ambayo Tina amesema kuwa ndiyo yamepangwa katika programu ya kutegwa vifaa vya kuangamiza wananchi, wataalamu wetu wamehakikisha kuwa majengo yote makubwa na popote penye mkusanyiko mkubwa wa watu panafanyiwa uchunguzi wa kina na habari njema ni kuwa pote huko hakuna tatizo lolote.”

    Ndipo ilipopatikana habari nyingine, na hii ikiwa ni ya kusisimua zaidi. “Wapangaji watatu katika hoteli ya Malick wako katika uchunguzi wa vijana wetu wa doria tangu Koplo Tina alipotupa ripoti kuhusu mpango huo mchafu,” mmoja wa makamanda wa Polisi alisema. “Kwa kweli ni wapangaji ambao kwa namna moja au nyingine wanahusika na mpango huo. Kuna kila sababu ya kuwatia hatiani kwa asilimia mia moja.”

    Nyuso za wajumbe wengine wa kikao hicho zilionesha jinsi walivyochanganywa na taarifa hiyo. Baadhi yao walionekana kuzeeka ghafla. Wengine tayari walishauingia uzee, lakini kwa kipindi hiki kifupi, uzee wao uliongezeka maradufu.

    Kuna ambao walikuwa wanene, lakini kwa kikao hiki cha saa moja na kitu tayari walishakonda. Wale ambao hata wanapochukia nyuso zao huwa zimejaa bashasha, kwa mara ya kwanza asubuhi hii nyuso hizo zilikuwa zimekunjamana, labda ni ujasiri tu uliowafanya wasitokwe na machozi. Kwa ujumla hakukuwa na mjumbe hata mmoja katika kikao hicho aliyelichukulia suala hilo kama masuala mengine ya kutatanisha yaliyowahi kulipata taifa.

    “Hivi hawa watu ni Watanzania?” mmoja aliuliza baadaye.

    “Ni Watanzania halisi,” alijibiwa na mjumbe mwingine.

    “Bangi imewaathiri?”

    “Nani anajua?”

    “Ni wendawazimu?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hakuna mwendawazimu anayeweza kupanga mikakati ya aina hiyo na akafikia hatua hiyo.”

    “Lakini,” Kanali Malingumu alifoka, “hakuna Mtanzania mwenye akili timamu anayeweza kusuka mpango mchafu wa aina hii. Kuna mawili, ama ni Watanzania kwa kutaja ukabila wao lakini kumbe chimbuko la mababu na mababu wa karne iliyopita walitokea nchi jirani ambako kuana mauaji kila kikicha au ni Watanzania halisi ambao mioyo yao imeshakumbwa na ibilisi kiasi cha kutokuwa sawa na binadamu wengine wakamilifu.”

    “Inawezekana,”Ofisa Usalama wa Taifa, Kevin Mpakanjia alisema. “Na hao ni wale binadamu ambao kwa nje wanafanana sana na manabii wa Mungu huku kilichofichika mioyoni mwao...” akaiacha sentensi hiyo ikielea.

    “ Ni roho za kishetani!” mwingine alidakia. “Ndio, wana roho za kishetani, roho nyeusi tii!”

    “Hawastahili kuvumiliwa!” mjumbe mmoja alibwata kwa hasira.

    Kwa ujumla sasa kila mmoja alipandwa na jazba. Ikafikia hatua ya kila mmoja kujikuta akizungumza bila ya kujali kama aliyetangulia amemaliza kusema. Kwa namna moja au nyingine ni kama ulikuwa mzozo. Jazba ilimtawala kila mmoja. Hata hivyo, busara za Mwenyekiti wa kikao zilitumika katika kuurejesha utulivu, na mikakati ikaendelea kupangwa kwa utaratibu mzuri.

    Hatimaye wakatawanyika wakiwa wameshakabidhiana majukumu ya kudhibiti hatari iliyokuwa ikilikabili taifa.



    *****



    SAA 3:45 iliwakuta Muganyizi na Karumuna wakiwa ndani ya kile chumba cha ghorofa ya pili, chumba maalumu kwa mipango maalumu. Boksi dogo lililohifadhi chupa tano za sumu kali aina ya PAK lilikuwa kando ya kimeza kidogo kilichokuwa nyuma ya mlango. Wakati huo alisubiriwa Rwegasira ambaye tangu jana alipoondoka alikuwa hajarudi. Ni yeye aliyetarajiwa kuja kukamilisha mpango akiwa na usafiri.

    “Tunazidi kuchelewa,” Karumuna alisema. “Kwanini tusingetumia usafiri wa Ndimukanwa?”

    “Haifai kutumia gari lile,” Muganyizi alijibu. “Usafiri wa kukodi ni mzuri, kwa kuwa hata kama mashushushu watakuja kushtuka baadaye, wataishia kuhangaika na madereva teksi pekee. Sisi tutakuwa tukitanua na Discovery bila kelele wala mikwaruzo. Umenielewa?”

    “Nimekuelewa. Lakini muda nd'o unazidi kuyoyoma kwa kasi. Kujali muda ni jambo muhimu sana . Mara nyingi kutojali muda huzaa madhara au hitilafu katika mkakati wowote mzito. Katika kipindi hiki, na tukiwa katika hatua za mwisho sana za utekelezaji wa maazimio, ni vizuri kwenda na wakati na kuwa makini kwa kila tulichokipanga.”

    “Ni kweli,” Muganyizi alikiri huku akitazama saa ya mkononi. Kisha akaitoa simu mfukoni na kubonyeza tarakimu kadhaa na kuitega sikioni.

    Simu iliita bila ya kupokelewa kisha ikakata. Muganyizi alisonya na kuirejesha kwenye mfuko wa shati.

    “Vipi, yuko hewani?” Karumuna alimwuliza.

    “Yuko hewani lakini hapokei.”

    “Kuna tatizo gani?”

    Hakuna aliyekuwa na jibu. Walitazamana, kila mmoja akiwa na sura yenye maswali mengi yasiyokuwa na majibu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *****



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog