Simulizi : Macho Ya Bundi
Sehemu Ya Tatu (3)
Baada ya maelezo hayo karamu iliandaliwa ambapo sisi wageni tulitengewa chakula chetu tukala. Hakika wenyeji wa Kijiji cha Nanyindwa walikuwa wakarimu sana.
Nje ya nyumba ya sherehe kulikuwa na ngoma maalum inayoitwa Beni, ilikuwa tofauti na ngoma tunazozijua zinazochezwa na vijana, hiyo asilimia kubwa ya wapigaji na wachezaji ni wazee.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya sherehe tuliingia katika magari yetu na kuondoka kuelekea mjini huku giza likitusindikiza kule tulikokuwa tunakwenda, yaani nyumbani.
Tulipofika hakukuwa na haja ya kupika chakula cha usiku maana kila mmoja alikuwa ameshiba kwenye sherehe.
Mume wangu alinigeukia.
"Salome, leo nimemuoa Pili, hakuna haja ya kusema mengi kwani unajua taratibu. Nitaanza usiku huu kulala kwa bi mdogo, sawa?"
"Sawa." Baada ya mimi kujibu hivyo Mei aliyekataa kubaki kijijini akidai anamsindikiza mwanaye alikunja uso, sikujua kwa nini alifanya hivyo.
Baada ya mazungumzo mafupi wote tulitawanyika pale sebuleni na kwenda kwenye vyumba vya kulala, Mei tulimhamishia chumba cha wageni.
Usiku huo usingizi sikuupata kabisa kwani kwenye dirisha la chumba changu kulikuwa na bundi aliyekuwa akilia.
Nilishituka na kusimama kumuangalia, hakuwa na wasiwasi akawa anaendelea kulia huku akigeukageuka.
Nilijaribu kumfukuza akawa hatoki pale dirishani.
Niliamua kwenda kumgongea mume wangu kwenye chumba alicholala na Pili.
"Ngo, ngo, ngo."
Kabla hajafungua Mei alichomoka chumbani kwake na kuanza kunifokea:
"Tabia gani hiyo ya kuwagongea mtu na mkewe usiku huu, sitaki kabisa umnyime raha mwanangu."
Alinitibua sana Mei kwa kuniambia hivyo. Nilitaka kumjibu hovyo lakini nafsi ikanikataza.
Niliendelea kugonga ndipo mume wangu alifungua mlango.
"Kuna nini mke wangu?"
"Ukiona mtu mzima kama mimi anakugongea usiku kama huu elewa kuna jambo zito."
"Sawa niambie basi."
"Dirishani kwangu kuna bundi na sijui amekuja kufanya nini."
"Mke wangu huyo ni ndege, mfukuze atatoka."
"Nimejaribu kufanya hivyo lakini hatoki badala yake amekuwa akigeukageuka, nimeogopa nikaamua nije kukuita ili na wewe ukajionee."
Mume wangu alijifunika pajama lake na tukaongozana hadi chumbani kwangu.
Tulimkuta bundi akiwa bado dirishani akituangalia bila kuwa na wasiwasi. Mume wangu alijaribu kumrushia boksi, lakini hakutoka.
"Shiiiiii, toka," alisema mume wangu lakini bundi huyo alizidi kutukodolea macho.
Badala ya kuruka na kuondoka akaanza kulia, hali iliyoniongezea hofu. Niliangalia mlango wa chumba chetu nikamuona rafiki yangu Mei akituchungulia. Sikusema chochote ili kumtega nijue atasema nini lakini naye akawa anamuangalia mume wangu akihangaika kumfukuza ndege huyo.
"Lakini mume wangu unafikiri huyu ni bundi wa kawaida?"
"Salome una wasiwasi bure, yule ni bundi wa kawaida kabisa."
"Una hakika?"
"Ndiyo."
"Kivipi?"
"Kama angekuwa bundi mtu' asingeondoka na badala yake angetudhuru."
Sikumjibu kitu.
"Haya mke wangu narudi kwenye chumba cha bi mdogo, usiku mwema."
Sikumjibu chochote akaondoka chumbani kwangu. Nilijiuliza maswali mengi baada ya kuondoka.
Kwanza kwa nini Mei alikuja kutuchungulia? Licha ya kuwa hakustahili kufanya hivyo, hakuona kuwa huyu mume wangu ni mkwewe? Je, ni ustaarabu wa kiafrika kumchungulia mkweo aliye kwenye chumba cha kulala? Je, Pili mbona hakuuliza chochote kuhusu lililonipeleka katika chumba chake? Mwisho, bundi yule ni ndege kweli au ni mauzauza ya Mei?
Nisikufiche, mawazo yangu yalikuwa kwa Mei hasa kwa kuwa nilimshuhudia akitia dawa kwenye kiti alichokuwa anataka kukalia mume wangu. Nilihisi kwamba inawezekana yule bundi ni wakutumwa na amemtuma yeye ili anidhuru.
Usiku huo sikupata usingizi kabisa na nilikuwa najigeuzageuza tu pale kitandani. Niliangalia saa ukutani ikawa inasomeka ni saa tisa usiku.;Pa pa pa papaaa.' Nilisikia sauti kama mbawa za ndege dirishani kwangu.
Nilipoangalia nikamuona bundi yuleyule akitua dirishani kwa mara nyingine kisha kunichungulia kwenye dirisha lilelile.
Safari hii bundi huyo alikuta dirisha nimelifunga lakini kwa kuwa lilikuwa la kioo macho yake ya kung'ara yalikuwa yakionekana wazi pale kitandani nilipokuwa nimelala.
Moyo wa ujasiri uliniingia,nikaamka na kumfuata bundi yule pale dirishani.
Sikuwa na woga kwa kuwa alikuwa nje ya dirisha.Nikienda na kujifanya kumshika, ataruka na kutokomea gizani,' nilijisemea kimoyomoyo.
Taratibu nilimsogelea bundi yule naye akawa ananiangalia bila kuruka.
Mkono wangu niliupeleka na kujifanya kama nataka kumshika lakini ukaishia kwenye kioo ajabu ni kwamba hakuruka na akawa ananikodolea macho.
Nilirudi kitandani huku akiniangalia. Nilijiuliza niende tena kwa mume wangu nikamgongee? Nikasema kimoyomoyo kwamba hapana nisifanye hivyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nililala kitandani na kujifunika shuka gubigubi kwa dakika kama tano hivi. Nikiwa kwenye shuka zaidi ya dakika tano, niliamini kwamba yule bundi atakuwa katimka.
Jambo la kushangaza ni kwamba, nilipofunua shuka nilimuona yule bundi akidonoa kioo kwa mdomo wake kama vile anataka kufungua dirisha. Niliingiwa na woga na kuhisi kama alikuwa amefungua dirisha.
Licha ya kumtishia ili aondoke, hakuonesha dalili za kutoka badala yake alitulia na kuendelea kunitazama huku macho yake yakiwa yanang'aa.
Hapo nikaamini kwamba bundi yule ni wa kishirikina na wala sikuhitaji ramli ya mganga yeyote au kwenda kutabiriwa kwa Maalim Hassan Yahya Hussein.
Niliamka kitandani na nikasimama huku nikimuangalia ndege yule ambaye macho yake yalikuwa na rangi nyekundu na hakuwa na wasiwasi kabisa, kwamba labda naweza kumfanya chochote.
Kilichonishitua ni kitendo cha bundi yule kuendelea kudonoa dirisha, niliamini kwamba alikuwa katika jitihada za kulifungua ili anidhuru. Nilitokwa na jasho jembamba huku nikumuangalia, nilikuwa natetemeka.
Nilitamani niende nikamuamshe mume wangu, lakini nilihofia kama ningetoka yule bundi angenifuata na kunidhuru.
Niliamka kitandani na nikasimama huku nikimuangalia ndege yule ambaye macho yake yalikuwa na rangi nyekundu na hakuwa na wasiwasi kabisa, kwamba labda naweza kumfanya chochote.
Kilichonishitua ni kitendo cha bundi yule kuendelea kudonoa dirisha, niliamini kwamba alikuwa katika jitihada za kufungua dirisha ili anidhuru. Nilitokwa na jasho jembamba huku nikumuangalia.
Sikuvumilia na nikaamua kwenda kumgongea mume wangu kwa mara nyingine tena.
"Ngo ngo ngo."
"Nani?"
"Ni mimi tena mume wangu."
"Kuna bundi tena?"
"Ndiyo."
Hazikupita hata sekunde mbili akawa amefungua mlango wa chumba chake. Tuliongozana hadi chumbani kwangu.
Alichukua bunduki yake aina ya rifle akasema anakwenda kufungua dirisha ili ampige kwa risasi.
"Fungua kabati langu la nguo nipe risasi za ndege."
"Utampigaje pale na kuna kioo?"
"Nitafungua dirisha, kama atakuwa bado yupo dirishani, namtwanga risasi."
"Hapana. Kufungua dirisha mimi sikubaliani. Huyu siyo bundi wa kawaida. Ukifungua anaweza kukudhuru au kunidhuru."
Maneno yangu yalimfanya mume wangu kubadili mawazo na kutoa ushauri mwingine kwamba atampiga risasi dirisha likiwa limefungwa.
Nilimshauri kwamba wazo hilo pia siyo zuri kwa sababu licha ya ukweli kwamba ataharibu dirisha lakini atasababisha matatizo kwa sababu hatujui itakuwaje baada ya kupiga bunduki au kumuua.
"Kwa kuwa mimi naamini kwamba bundi huyu siyo wa kawaida nakushauri usimuue badala yake tufanye kila linalowezekana atoke hapo dirishani, vinginevyo mimi nitashindwa kulala humu chumbani. Unaweza kupiga bunduki usimuue na dirisha litakuwa lina tobo, atatumaliza. "
Maneno hayo yalimfanya mume wangu atafakari kwa kina na kuamua kutoa risasi kwenye bunduki na akanikabidhi.
"Basi irudishie pale ulipoitoa kwenye kabati. Ushauri wako nauzingatia maana hata mimi nimeanza kuingiwa na wasiwasi kwamba huyu siyo bundi wa kawaida, tumemfukuza na amerudi palepale."
Mume wangu alifikiria kwa dakika kama moja hivi huku akiniangalia usoni, akaniambia kwamba ni vyema nikahama chumba na kwenda kulala kwenye chumba cha Pili.
"Wote nyinyi ni wake zangu. Ni vyema tukalale kwenye chumba kimoja maana kama kifo basi tufe sote. Huo ndiyo uamuzi wangu kwa sasa. Unafaa? Nipe ushauri."
Sikuwa na haja ya kufikiri au kutafakari kwa kuwa niliingiwa na woga kwani wakati huo bundi alikuwa bado dirishani akituangalia tukijadiliana.
Nilimkubalia na kuamua kuhama chumba usiku huo. Nilichukua shuka na mto na tukawa katika msafara wa pamoja na mume wangu kuelekea kwenye chumba alichokuwa Pili.
Ile kufungua tu chumba chetu ili tutoke, tulikutana uso kwa uso na Mei akiwa amesimama.
"Nimesikia yote mliyokuwa mkizungumza, wewe mkwe nimesikia kila kitu ulichosema kwamba ni vyema mlale chumba kimoja na mwanangu. Utamaduni wa wapi huo. Huyu Salome badala ya kukupa ushauri anachekelea kwenda kumvurugia mwanangu ndoa yake?."
"Lakini rafiki yangu"
"Rafiki yako nani? Huoni jinsi unavyomvurugia mwanangu. Siku ya kwanza tu katika ndoa yake unaanza kumletea vurugu?"
Mume wangu alimuambia Salome arudi chumbani kwake kwa kuwa haya yanayotokea hayamhusu.
Tuliingia kwenye chumba cha Pili. Mke mwenzangu huyo hakuwa na furaha baada ya kuniona mimi lakini alipoelezwa sababu za mimi kuja chumbani kwake, alitulia.
***
Mimba ya Pili ilikuwa na akawa anakaribia kujifungua. Mume wangu alihamisha mahaba kwangu akawa anashinda chumbani kwa Pili.
Hali hiyo ilinitisha kwa kuwa tabia ya Pili na mama yake, yaani Mei zilianza kuingilia himaya ya nyumba yangu.
Mei alianza kuwa mwamuzi wa mambo katika nyumba yangu. Mume wangu akienda kazini alikuwa akiwaachia wao fedha za matumizi na walikuwa wakiamua siku nyingine kutopika na kwenda kula hotelini na kuniacha mimi nikishinda na njaa.
Siku moja mume wangu nilimuambia kwamba anachokifanya siyo kitu kizuri lakini badala ya kusikiliza ushauri wangu akafoka.
"Hujui kwa nini mimi nawaachia wale fedha za matumizi, kwani wewe una ujauzito? Wewe si kila kitu unakula, Pili anachagua ndiyo maana nimeamua kuwachia wao fedha za matumizi," alisema mume wangu Chinchi akiwa amekunja uso.
Sikukubaliana na maelezo yake kwa sababu hata nilipomuambia kuwa huwa hawapiki mchana siku mojamoja, hakujali au kuchukua hatua.
Baada ya hapo kila siku tukawa tunagombana na Mei akadai kuwa mwanaye ni lazima atunzwe kwa kuwa ameshika ujauzito tofauti na mimi ambaye najaza choo.
"Nimeambiwa na Pili kwamba eti unamkataza mumewe asimuachie fedha za matumizi akuachie wewe."
"Siyo kwamba namkataza. Nimemshauri kwamba matumizi aniachie mimi kwa kuwa ndiye mkubwa kwenye nyumba hii."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Una ukubwa gani? Pili angekuwa mdogo angepata mimba?"
"Mei nakuambia acha ujinga, elewa kwamba mimi ndiye niliyewakaribisha hapa nyumbani."
"Usinitishe, acha hizo. Wewe kwa kuwa huzai ndiyo maana mumeo kakuweka kando."
"Unasemaje?"
"Umesikia halafu unajifanya hukusikia."
"Kweli nimeamini methali ya wahenga waliosema tenda wema nenda zako, usingoje shukurani."
"Nakuambia wazi, mtoto wangu Pili ana mimba, akipatwa na matatizo wakati wa kujifungua nitajua ni wewe."
Niliumia sana kuona Mei ambaye ni rafiki yangu wa siku nyingi akiniambia maneno hayo. Mume wangu aliporudi nilimwambia lakini akawa hatilii maanani kabisa kila nilipokuwa nikimshitakia hali iliyonipa imani kuwa ametengenezwa.
***
Pili siku zake za kujifungua zilifika ikawa yupo hospitali kwenye chumba cha kujifungulia, yaani leba. Mimi, mume wangu Chinchi na Mei tulikuwa nje ya chumba hicho huku nikiwa kama nasikia maneno ya Mei, ";Pili ana mimba, akipatwa na matatizo wakati wa kujifungua nitajua ni wewe,"
Tulikaa nje ya hospitali hiyo kwa saa kadhaa kila mmoja akiwa na mawazo yake kichwani. Mume wangu Chinchi alionekana kuwa na wasiwasi kama Pili atajifungua salama au la.
Wakati tukiwa katika mawazo tuliona mlango wa leba ukifunguliwa, akatokea daktari mmoja ambaye alikuwa na karatasi mkononi.
Kila mmoja moyo wake ulienda mbio. Daktari akasimama mbele yetu huku akiangalia zile karatasi alizokuwa amezishika mkononi.
"Jamani nawaona mna nyuso za mashaka, poleni sana;"
"Unasema nini? Sijakuelewa." Alidakia mume wangu.
"Daktari usizunguke. Tuambie nini kimetokea, kama si riziki tueleze," Mei alisema. Ni mimi tu ndiye sikuonesha wasiwasi.
"Jamani mbona mna wasiwasi hivyo, hata kabla sijasema mnanikatisha. Nani kasema kuna matatizo huko leba? Ni kwamba mtoto wenu kajifungua kichanga cha kiume na wote wako salama."
Mume wangu, Chinchi aliruka kama mwendawazimu. Alitaka kwenda kwenye chumba alichokuwa Pili lakini akazuiliwa na yule daktari.
"Muda wa kumuona mzazi bado. Kwa sasa anaendelea kufanyiwa tiba za uzazi. Nimetoka mara moja ili kuwaondoa hofu maana nilikuwa nakuona mzee kupitia dirisha lile la kioo hutulii," alisema daktari huyo.
"Mzazi ni nani wako?"aliuliza.
"Ni mke wangu mdogo, mkubwa ni huyu," alimjibu huku akinishika bega, Mei hakufurahia kitendo hicho kwani alikunja uso.
Baada ya jibu hilo daktari aliingia ndani ya chumba cha kujifungulia bila hata kutuaga.
Nilihisi kwamba alichukizwa na mume wangu kumuoa mtoto mdogo saizi ya mtoto wake.
***
Maisha ya Pili na mtoto wake pamoja na mama yake Mei ndani ya nyumba yangu yalikuwa na maudhi sana kwangu.
Pili alijiona sasa yeye yupo juu yangu na akawa anadiriki eti kunituma mimi kazi za nyumbani.
Siku moja tulipigana na kugalagazana sebuleni kwa sababu alinitukana na kuniambia maneno yakuudhi sana. Ugomvi huo uliingiliwa na mama yake ambaye aliamua kunichangia kunipiga.
Hawakuniweza kutokana na ukweli kwamba mimi nilikuwa na nguvu kwa kuwa niliwahi kupitia Jeshi la Kujenga Taifa miaka ya zamani.
Ghafla wakati tunapigana mume wangu aliingia na kukuta vita ikiendelea.
"Jamani kwa nini mnafanya hivi? Mnataka kuniua kwa presha?," alifoka mume wangu.
Baada ya kutuachanisha wote tulikaa kwenye kochi huku kila mtu akitweta.
"Mume wangu nakuomba, hawa watu watafutie nyumba wahame hapa nyumbani, watanitoa roho bure," nilimuambia.
"Nani ahame? Mwanangu hawezi kuhama labda uhame wewe," alidakia Mei.
"Wewe unaingilia yanakuhusu?... Yanakuhusu? Badala ya kurudi nyumbani kwako, unang'ang'ania katika nyumba za watu na kuziharibu. Umechangia sana kutugombanisha wewe," nilimjibu.
Mume wangu alikuwa amesimama katikati ya sebule huku akitokwa na jasho jingi usoni kana kwamba alikuwa anafanya mazoezi ya judo.
BADALA ya kusikiliza upuuzi aliokuwa akiusema Pili na mama yake, nilikwenda chumbani kwangu na kumuacha mume wangu akiwa amesimama akiwaangalia.
Lakini mara tu baada ya mimi kufika chumbani nilimuona mume wangu akinifuata na kuja kuingia chumbani nilipokuwa mimi.
"Mume wangu, hawa watu wahamishe. Niliwakaribisha kwa kuamini kuwa tutaishi kama ndugu lakini kwa kuwa wananiona mimi sizai wananinyanyasa na kujifanya wao ndiyo wenye nyumba hii," nilinyamaza kidogo kupisha neno litoke kwa mume wangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sikiliza Salome. Kuwahamisha siwahamishi isipokuwa cha kufanya ni kumtimua Mei kwani ndiye anayemharibu Pili."
Tulijadiliana mambo mengi sana kuhusu Pili na mama yake Mei na kuafikiana kwamba mama wa Pili ahame kwa kuwa yeye ndiye chanzo cha ugomvi unaoibuka mara kwa mara katika nyumba yetu.
Mume wangu aliamua kutoka chumbani na kumuita Pili sebuleni kwani sisi tulipoingia chumbani yeye na mama yake wakaingia kwenye chumba wanacholala.
"Pili sikiliza. Wewe ndiye mke wangu na ndiye unastahili kukaa hapa kwangu. Mama yako alikuja kwa ajili ya kukusaidia wakati una ujauzito. Sasa umejifungua tena salama nitaomba umuambie mama yako kuwa arudi kwake.Sawa?"
Pili badala ya kujibu swali hilo alinyanyuka na kwenda chumbani kwa mama yake. Alikaa huko ndani kwa dakika kumi na tano au ishirini hivi kisha.
"Huyo atakuwa anamuambia mama yake haya maagizo niliyompa. Hafai yule mama kukaa hapa, kwanza mshirikina," alisema mume wangu.
"Umeonaee. Nafurahi umeliona hilo wewe mwenyewe."
Wakati tunaendelea kuzungumza na mume wangu tulishitukia Pili na mama yake pamoja na mtoto mchanga wakitoka chumbani kwao huku wakiwa na mabegi ya nguo.
Moyoni nilidhani ni nguo za mama yake Pili, yaani rafiki yangu Mei kwamba sasa anakwenda kwake.
"Wewe umesemaje?" lilikuwa swali la Mei akilielekeza kwa mume wangu.
"Lazima uwe na adabu, huwezi kuniuliza hivyo. Mimi mkweo lakini pia nimekuzidi umri," alifoka mume wangu.
"Nakuambia nikiondoka hapa naondoka na mwanangu Pili na mjukuu wangu, siwezi kuwaacha hapa."
"Huwezi kuondoka na mke wangu pamoja na mwanangu. Nimemuambia Pili uondoke wewe haraka sana. Huwezi kunivunjia heshima mimi na mke wangu."
"Nitafutie gari niondoke. Usinitishe mimi mtoto wa mjini babu wee!"
"Nikutafutie gari? Ingiza mizigo yako kwenye gari langu, nitakupeleka mimi huko kwako."
"Unipeleke wewe wakati umenifukuza kwako? Sikubali. Niletee gari hapa niondoke."
Mume wangu alimuagiza mlinzi akatafute taksi na punde si punde ikawa imefika.
"Dereva kutoka hapa mpaka Mkuti bei gani? Nataka umpeleke huyu mama."
"Shilingi elfu tano na mia tano."
"Nakuambia simuachi mwanangu ng'o, mwanamke wako asiyezaa asije kumuua mjukuu wangu."
"Unasemaje?" nilisema nikamvamia na kumkaba koo akawa anahema kwa shida. Mume wangu alijitahidi kutuachanisha lakini mikono yangu ilikuwa kama ina sumaku.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment