IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS
*********************************************************************************
Simulizi : Macho Ya Bundi
Sehemu Ya Kwanza (1)
NAITWA Salome Katonaga, ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia yetu ya watoto watano. Nimeamua kuwasimulia simulizi hii ili mfahamu kwa nini wahenga walisema dunia ni tambara bovu. Nitaeleza machache lakini ya kuhuzunisha sana ambayo nilifanyiwa na watu wenye roho mbaya.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku moja nikiwa katika pitapita yangu nilikutana na kijana mmoja ambaye aliniuliza ilipo Hoteli ya Wapiwapi mjini Masasi.
Nilikuwa naifahamu hoteli hiyo, hivyo nilimuelekeza lakini akadai kwamba hajaelewa na kuniomba nimpeleke.
Kaka huelewi nini, kutoka hapa stendi ya mabasi, ongoza moja kwa moja barabara ya Newala utaikuta hoteli hiyo, ipo barabarani kabisa, nilimuambia.
Hapana, pamoja na kunielekeza vizuri itakuwa vizuri kama utanisindikiza, alisema kijana huyo.
Nilimuangalia na kuona kuwa alikuwa mtanashati na hakuwa mtu mbaya na kwa kuwa ilikuwa jioni ya saa kumi, sikuwa na
hofu ya kufanywa chochote na yule kijana.
Niliamua kumpeleka huku naye akiniomba nimsaidie kubeba mzigo wake wa begi dogo ambalo halikuwa zito baada ya
kumkubalia kumsaidia.
Njiani tulikuwa tukizungumza hili na lile na alitaka kujua jina langu, nikamuambia naitwa Salome.
Jina zuri sana kwa sababu hata mama yangu anaitwa jina hilo, alisema.
Kwani mama yako anaishi wapi?
Anaishi wilaya hiihii.
Wilaya ni kubwa taja sehemu.
Kijiji cha Nanyindwa.
Nakifahamu sana kijiji hicho.
Unakifahamu?
Ndiyo.
Ulifika pale kufanya nini?
Nilikuwa na rafiki yangu lakini siku hizi yupo Dar es Salaam. Nilikwenda kumtembelea wakati huo kabla hajahamishia makazi yake Dar.
Ahaa, anaitwa nani maana pale kijijini watu wote tunajuana.
Huwezi kumjua, kahamia Dar miaka mingi sana.
Nimekuambia kijiji kile kina watu wachache sana tunajuana nitajie jina nitamjua tu.
Anaitwa Roja Mchopa.
Namjua tena sana lakini mbona siku hizi karudi kijijini anajishughulisha na kilimo na biashara ndogondogo?
Usiniambie! Yupo kijijini Mchopa? Nilijua yupo Dar.
Kwa hiyo alipokuwa Dar uliwahi kumtembelea?
Nilimtembelea ndiyo, alikuwa akikaa Magomeni Mikumi na aliwahi kupiga muziki.
Kama ni muziki bado anaendelea nao, maana ana vyombo vya disco pale kijijini.
Mazungumzo kati yangu na kijana huyo yalikuwa marefu sana. Ni kweli alikuwa akijuana na baba huyo wa kijijini kwetu lakini kama alivyosema mwenyewe walionana muda mrefu mrefu, mwaka 1977.
Ahhh, nilipokuwa kijijini kwenu nilikuwa mdogo, mwaka 1977 nilikuwa na miaka kumi tu.
Unaitwa nani?
Ihopa Chinchi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ihopa Chinchi? Jina gumu, wewe mwenyeji wa wapi?
Kwetu ni Ndanda lakini babu zetu walihamia kutoka Msumbiji miaka mingi sana iliyopita. Kwani wewe una miaka mingapi?
Nina miaka 26.
Mwendo wa kutoka stendi ya mabasi Masasi mpaka Hoteli ya Wapiwapi ulikuwa mfupi maana hatukukodi Bajaj, badala yake tuliamua kutembea kwa miguu.
Baada ya kumfikisha katika hoteli hiyo aliulizia chumba lakini akaambiwa vyumba vilijaa. Ilibidi tugeuze na kwenda Masasi
Hoteli ambapo tulikutana na mzee David aliyekuwa akifanya kazi hotelini hapo.
Mzee huyu unamfahamu?
Mzee Daudi alimuangalia yule kijana akatikisa kichwa kuashiria hakumfahamu.
Anasema amewahi kukaa Kijiji cha Nanyindwa nikadhani utakuwa unamfahamu kwa kuwa umeishi sana kule.
Hapana, simfahamu.
Anasema alifikia kwa mzee Mchopa.
Mzee Mchopa nilikuwa namfahamu.
Kwa nini unasema ulikuwa unamfahamu kwani amehama huko kijijini? aliuliza.
Nimesema hivyo kwa sababu ameshafariki, miaka mingi.
Ooh jamani, kumbe huyo mzee hayupo duniani?
Ndiyo hivyo, katangulia nasi tupo nyuma yake, alisema David.
Mzee David alitufikisha katika chumba cha hoteli hiyo, ghorofa ya kwanza chumba namba saba. Tuliingia chumbani na kuweka mizigo yake. Mimi nilikuwa nimeketi kwenye kiti wakati yule mgeni anafikiri sanduku lake aliweke wapi. Baadaye akaamua kuliweka kwenye kabati.
Alisema nimsubiri kwani alikuwa anakwenda kujimwagia maji. Nilimuitikia kwa kichwa. Alichukua taulo na kuingia bafuni kwani katika chumba hicho choo na bafu vilikuwa humohumo.
Akiwa anaoga nilipenda kutafiti, nilikwenda kwenye sanduku lake nikaona kuna kifurushi kinatutumuka na kusinyaa kama vile kulikuwa na kitu ndani kinapumua.
Nilirudi haraka kwenye kiti changu huku moyo ukinidunda na kujiuliza mle ndani mlikuwa na kitu gani? Nilianza kutokwa na jasho jembamba.
IHOPA Chinchi alitoka bafuni akiwa amejikausha. Alichukua suruali yake na kuingia tena bafuni ambako alivaa na kutoka akiwa nadhifu.
"Basi mimi naomba niondoke," nilimuambia.
"Ngoja basi tukapate chochote kitu hotelini."
"Hapana. Mimi nimeshiba."
"Ngoja basi nikutoe."
Bwana Chinchi alinitoa nje ya hoteni na akaniambia kuwa atanitafuta kwa simu kwa kuwa kuna jambo anataka kuniambia.
"Kwani ee ee" Nilisita.
Nilitamani kumuuliza kile ambacho kilikuwa kikipumua ndani ya sanduku lake lakini nilikuwa nilishindwa kwa kuwa angejua kuwa alipokuwa anaoga nilipekenyua mizigo yake.
"Inaonekana kama una jambo unataka kuniambia lakini unasita, uwe huru sema tu, usiwe na wasiwasi."
"Hapana, nitakuambia siku nyingine."
"Salome Ni nini? Mbona unanipa wasiwasi."
"Hapana nitakuambia siku nyingine," nilizidi kusisitiza.
Baadaye tuliagana name nikaenda kwetu Mtandi, nje kidogo ya mji wa Masasi.
Usiku ule sikulala kufikiria kile kilichokuwa kinapumua kwenye sanduku. Maswali yalikuwa mengi kuliko majibu. Nilijiuliza ama kuna kitoto kichanga? Lakini kama ni kitoto kichanga kwa nini muda wote huu hakikulia? Au ni kitu gani hasa?
Kwa kweli sikupata jibu sahihi na badala yake baada ya mawazo mengi nilijishitukia nikiwa nimepitiwa usingizi.
Asubuhi nilipigiwa simu na nilipoangalia kwenye skriini, sikujua ni nani aliyekuwa akipiga.
"Haloo."
"Haloo, hujambo salome Katonaga."
"Sijambo, nani mwenzangu?" nilihoji.
"Aaahh wewe Salome umenisahau? Jana hukumbuki kuwa ulinipeleka wapiwapi kisha Masasi Hoteli?"
"Nimekukumbuka." Nilitamani kuikata hiyo simu kwa kuwa sikutaka kuzungumza na yule mtu, hasa nilipokuwa nikifikiria kitu kilichokuwa kikipumua kwenye sanduku lake.
"Sasa naomba leo nikuone nikueleze kile ambacho nilitaka kukueleza jana." Akaniambia.
"Leo sina nafasi."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hapana, chukua Bajaj utarudi sasa hivi, nikueleze jambo halafu ukalifanyie kazi."
"Nipigie baada ya dakika ishirini au nusu saa nione kama kazi zangu zitakuwa zimeisha."
Akakata simu baada ya kunishukuru.
Nilikwenda moja kwa moja kwa rafiki yangu mpenzi Mei ili akanipe ushauri.
"Mei rafiki yangu, naomba unishauri jambo."
"Jambo gani tena?"
"Ni hadidhi ndefu kidogo, itabidi univumilie."
"Heee makubwaa; nipe habari,"
Nilimsimulia mkasa wote wa jana kuhusu yule bwana na kisanduku chake chenye kitu kinachopumua.
"Sasa shoga itafaa nikuzindikize, maana watu wengine siyo wazuri, isije ikawa ni wachawi, wasije wakakutoa kafara bure."
"Sawa, tutaenda wote."
"Mtakuja kufa hivihivi shoga. Kwa nini ulikuwa laini na kukubali kuingia naye hadi chumbani? Kama ni hotelini si mlishafika?"
"Mtu mwenyewe nilimuamini baada ya kuniambia kuwa aliwahi kuishi kijijini kwetu na watu kadhaa anawafahamu kwa hiyo sikuwa na wasiwasi naye."
Simu inalia.
"Huyo mtu anapiga, nilimuambia apige baada ya nusu sasa,"
"Pokea muambie tunakuja."
"Haloo."
"Nimekaa zaidi ya nusu saa nimepiga sasa, utakuja?"
"Nakuja sasa hivi."
Kutoka Mtandi hadi hotelini kwake siyo mbali hasa kwa Bajaj. Nilifika nikiwa na rafiki yangu Mei.
"Karibuni." Alitukaribisha kwani tulimkuta akiwa nje ya mlango mkuu wa kuingilia hotelini.
Wakati tunaingia katika hoteli hiyo, tulikutana na mzee David, yule ambaye alitupokea jana na akatupatia chumba.
"Binti habari tangu jana."
"Nzuri sana mzee David, shikamoo."
"Marahaba, leo umekuja na kimwana, mtoto mzuri, lainiii," alisema na wote tukacheka.
"Mzee acha utani."
"Mgeni, naongopa?"
"Huongopi," alidakia Chinchi.
Tulikwenda kwenye meza moja na kukaa wote watatu. Chinchi alituambia tuagize tunachokitaka, tukafanya hivyo.
"Bwana Chinchi huyu ni rafiki yangu wa kufa na kuzikana, anaitwa Mei,"
"Mei, nafurahi kukufahamu."
"Huyu ni Bwana Chinchi, mgeni niliyekutananaye jana. Sasa mwaga habari."
"Hapana Salome. Nina jambo la siri nataka kukuambia. Tukiwa wawili tu. Jana uliniudhi sana, nisubirini napanda juu nakuja sasa hivi."
Salome alishangaa, "Au jana aligundua nimeona kitu kinachopumua sandukuni mwake?" alimuuliza mwenzake.
Mei hakunijibu haraka swali hilo. Alinitazama kwa sekunde chache, tukaendelea kupata kifungua kinywa.
Baada ya kumeza funda moja la chai alinijibu:
Siyo kwamba aligundua jambo, anasema ulimuudhi, inawezekana kuna kitu alikuambia nawe ukakataa.
Kama ulikuwepo. Aliniambia ana jambo anataka kuniambia akataka turudi chumbani mimi nilimkatalia.
Basi kama ni hivyo ni bora tungoje nini atashuka nacho kutoka huko ghorofani.
Hakuchukua muda mrefu Chinchi alishuka akiwa na kifurushi mkononi. Nilihisi kile kifurushi kile ndicho kilichokuwa kwenye sanduku kikipumua.
Chinchi baada ya kufika kwenye meza yetu alikiweka juu kikawa kinaendelea kuonekana kana kwamba ndani kuna kitu kinapumua.
Salome hii ni zawadi yako, alisema Chinchi.
Sikutabasamu wala kuifurahia zawadi hiyo kwa kuwa sikuwa najua nini kilichowekwa, tena basi kinachopumua.
Niliogopa hata kukishika kifurushi hicho.
Mbona unaonekana kutofurahia hii zawadi.
Sijui ni zawadi gani, naiogopa, mbona kuna kitu kama vile kinapumua humu ndani na kwa nini unizawadie.
Sikiliza Salome. Usiwe na wasiwasi, kwani kitu kibaya naweza kukupa tena mbele ya watu namna hii?
Alichukua kile kifurushi na kukifungua. Mimi na rafiki yangu Mei tukiwa tunatumbua macho kukiangalia.
Mimi na rafiki yangu tuliangua kicheko baada ya kukiona kilichokuwemo ndani ya kifurushi.
Mbona mmecheka sana, au zawadi hii ziyo nzuri?
Niliishuhudia saa nzuri sana ambayo ilikuwa ina umaridadi wa hali ya juu. Ilikuwa imetengenezwa mfano wa tumbo na kila dakika zinapogonga, tumbo lilikuwa likifutuka kana kwamba inapumua.
Baada ya kumshukuru aliniambia ameniita kwa nia moja tu, kwamba anataka kunioa. Hujawahi kuwa na mke katika maisha yako?
Sijawahi.
* * *CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulioana na Chinchi. Ndoa ilikuwa ya kifahari kutokana na uwezo mkubwa wa kifedha aliokuwa nao.
Baada ya ndoa nilimshauri mume wangu twende tukamtembelee Mei nyumbani kwake, akakubaliana nami. Alinisindikiza hadi nyumbani kwa rafiki yangu huyo.
Kiumri Mei alikuwa mkubwa kuliko mimi japokuwa tulikuwa marafiki sana. Mwenzangu tayari alikuwa na binti wa kike aliyekuwa anasoma kidato cha pili anayeitwa Pili, mimi nilikuwa bado sijazaa.
Karibu na nyumbani kwangu kulikuwa na jirani yetu ambaye alikuwa anaitwa mama Koki, siku moja alipofika kwangu nikasikia mtu anagonga mlango kwa nguvu.
Karibu, mama Koki.
Sijui utanielewaje, nimeona nikuambie ujue la kufanya.Una kifua shoga?
Niambie tu mama Koki.
Mama Koki alinyamaza kwa muda akaniambia kuwa jambo analotaka kuniambia ni zito.
Sikiliza Salome. Kuna msichana ulinifahamisha siku moja kuwa anaitwa Pili na ni mtoto wa rafiki yako Mei. Huwa anakuja hapa kwako mara kwa mara kila unapokuwa umeenda kazini. Anamkuta mumeo tu, mama Koki alinyamaza akaniangalia.
Huyu binti nina wasiwasi naye, atakuvunjia ndoa yako. Fanya uchunguzi.
Machozi yalinitoka na kujiuliza kweli mtoto wa Mei anaweza kuniingilia katika ndoa yangu? Nilichanganyikiwa.
Mama Koki hakukaa sana baada ya kutoa taarifa aliyokuwa ameniletea lakini aliniachia mawazo tele kichwani mwangu nikawa najiuliza hili na lile bila kupata jibu.
Haya aliyoniambia huyu mama ni kweli au anataka kunigombanisha na rafiki yangu?
Wakati naendelea kuwaza hayo nilisikia mngurumo wa gari nikajua kwamba ni mume wangu Chinchi anarudi.
Alipoingia sebuleni alinikuta nikiwa nimelala kwenye sofa la watu watatu. Sikuinuka kumpokea.
Leo unaumwa? aliniuliza. Nilijishitukia machozi yakitiririka kwa hasira na niliendelea kuwa kimya.
Nakuuliza Salome, una nini leo?
Najisikia naumwa sana kichwa, nilimdanganya.
Umeanza kuumwa saa ngapi?
Siyo muda mrefu. Mchana.
Twende hospitali.
Hapana, nimekunywa dawa ya kutuliza maumivu na tangu ninywe naona kuna nafuu, nilimdanganya.
Umekula chakula chochote?
Baada ya kula ndipo nilianza kusikia kichwa kikinigonga.
Ni vyema kama tutakwenda hospitali wakaangalie vipimo mke wangu.
Nilimsisitizia kuwa tusubiri kwa kuwa nimemeza vidonge na kama nitaona hali inazidi kuwa mbaya nitamuambia.
Aliniaga kwamba anakwenda kumuona rafiki yake mmoja ambaye alikuwa na ahadi naye kuhusiana na shughuli za kibiashara.
Nilimruhusu kuondoka lakini moyoni mwangu nikiwa na wasiwasi mkubwa kwamba inawezekana anakwenda kukutana na Pili, mtoto wa rafiki yangu Mei.
Saa mbili usiku mume wangu alirudi nyumbani akiwa hana raha kabisa.
Nilijiuliza maswali mengi lakini nikaamini inawezekana hali ile amekuwa nayo kutokana na mimi kuumwa mchana kutwa.
Wakati anaingia nilikuwa nipo chumbani kwetu. Nilitoka kwenda kumuandalia chakula.
Alikaa kama dakika kumi bila kunyanyuka kitini na kwenda kwenye meza ya chakula. Alionekana wazi kwamba ana jambo rohoni.
Vipi dia, kwani nawe unaumwa kama mimi? Nilimtupia swali la mtego.
Na mimi najisikia kama vile nina homa.
Niliinuka na kwenda kugusa shavu lake kupima kama ana joto au la. Nililikuta shavu baridi kabisa wala dalili za homa hazikuwepo.
Lakini unaonyesha huna homa kabisa, sijui unajisikiaje? nilimuuliza.
Najisikia mapigo ya moyo kuongezeka sana.
Kwa nini au umepoteza fedha nyingi huko ulikokwenda?
Hapana.
Sasa nini kinakuumiza mume wangu.
Basi nadhani mwili tu umekataa leo.
Basi inuka tukapate chakula. Nilimuinua na kwenda naye moja kwa moja kwenye meza ya chakula.
Nilikuwa nimeandaa ugali na nyama ya kuku wa kuchoma. Nikaandaa mezani.
Tulianza kula huku kila mmoja akiwaza lake kichwani. Mimi nilikuwa namuwaza Pili mtoto wa rafiki yangu Mei. Nilikuwa siamini kama anaweza kunifanyia unyama wa aina ile.
Haukupita muda mrefu alikuja rafiki yake mume wangu ambaye sikutarajia kama angefika wakati ule. Lakini ajabu ni kwamba badala ya kuzungumza pale sebuleni, walitoka nje kabisa ya nyumba na wakawa wanazungumza kwa kunongona.
Baada ya dakika kumi na tano akawa amefika. Salome alimsimulia yote aliyoyaona wakati anataka kwenda kazini na kupishana na gari lililowabeba Mei na mwanaye Pili.
"Nilishangaa kwa sababu siyo kawaida ya Mei kuja nyumbani kwangu asubuhi tena bila kuniarifu."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ina maana shemeji una wasiwasi na mumeo?"
"Tena sana. Kwa nini waje asubuhi nami sina taarifa? Hata ndugu yako hajaniambia kwamba kuna ugeni unakuja."
"Basi tuingie ndani tuone. Kama ni kufumania ukafumanie."
Wakati mlango wa geti nikiufungua, askari ambaye alikuwa akiangalia jengo hakuwa na habari kuwa kuna watu wanaingia ndani.
Nilitamani nimtandike kofi yule askari lakini nikajiambia moyoni kwamba hata kama nitampiga hahusiki na chochote kilichokuwa kikiendelea ndani.
"Karibu mama, nimeshangaa rafiki yako Mei na mtoto wake Pili wameingia kwa shari."
"Wameingia kwa shari? Kwa nini unasema hivyo?"
"Nimeona Mei amekasirika sana, nilichelewa kidogo kumfungulia akanifokea sana mpaka, nikamshangaa."
"Ngoja tuingie ndani tuone kuna nini," alisema shemeji yangu Kalikalanje.
Tukiwa tunakaribia getini tulisikia maneno makali ambayo alikuwa akiyasema rafiki yangu Mei lakini nilikuwa sijajua bado ni nini hasa kimemfanya awe akifoka kwani nilikuwa nikisikia sauti yake tu.
"Kwa nini urafiki wangu na Salome ndiyo uniponze?" maneno ya mume wangu Chinchi yalikuwa hayasikiki, alikuwa akisema polepole mno.
Nilifungua mlango mkubwa kwa nguvu na kuingia ndani nikiwa na shemeji yangu.
Wote waliokuwa mle ndani wakatulia na hakuna hata mmoja aliyefungua mdomo wake kusema chochote. Waligeuza shingo zao na kutuangalia.
"Hamjambo?" nilisalimia lakini hakuna aliyejibu.
Nilisogea mbele zaidi na kufika alipokuwa mume wangu. Niliketi na yeye kwa kuwa alikaa kwenye kochi la watu watatu.
Mei na mwanaye waliketi kila mmoja kwenye kiti chake.
Tuliowakuta waliangaliana bila shaka walikuwa wakitupiana mpira kwamba nani ataanza kusimulia kisa cha wao kukusanyika mle ndani.
"Rafiki yangu Salome. Nakuheshimu sana lakini mume wako amenivunjia heshima na amekuvunjia heshima na wewe pia. Huyu Chinchi ametuvuruga. Amemtia mimba mtoto wangu Pili!"
Baada ya Mei kusema hayo nilihisi jasho jembamba likinitoka kwapani na nguvu kuniishia.
"Unajua kumbe alikuwa akija nyumbani na kumchukua au siku nyingine Pili alikuwa akija hapa wakati wewe umekwenda kazini. Alikuwa akimpa fedha za kukodi teksi na wakishafanya mambo yao hapa, anamsindikiza mpaka nyumbani. Umeonaee?"
Nilitamani nimvamie mtoto wa Pili kwa kuniingilia katika ndoa yangu.
Hata hivyo, shemeji yangu Kalikalanje ndiye aliyelikoroga baraza kwani alifungua mdomo.
"Sasa Mei sikiliza ni kweli mwanao amepewa mimba kama unavyodai? una hakika ni ya bwana Chinchi?"
"Usianze kunitibua, kwa nini hatukuja kwako na tukaamua kuja hapa. Sisi ni wendawazimu? nakuuliza ni mazuri hayo mpaka nisingizie?"
Pale ukumbini hakuna mtu aliyekuwa akimuangalia mwenzake kwa dakika moja, Chinchi alikuwa akipepesa macho kuniangalia kwa wasiwasi.
"Basi tumpe nafasi Salome mwenye mume, unasemaje shemeji?" aliuliza Kalikalanje.
"Unaniuliza miye kwani mimba nimetia mimi?" Nilimjibu huku nikimtupia jicho baya Pili nikiwa na hasira huku nikitamani kumrukia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment