Simulizi : Niliua Kwa Kukusudia
Sehemu Ya Pili (2)
Hakuna shida," nilijibu kwa haraka sana.
"Sasa ngoja nimuite meneja nimpe maelekezo sahihi," akasema kisha akanyanyua simu ya mezani.
"Haloo Robert!" Akaanza kuzungumza kupitia simu hiyo ya mezani huku nikiwa namtumbulia macho na kuendelea kushangaa uzuri wa ofisi ile.
"Haya, basi njoo mara moja hapa ofisini kwangu," alisema na kisha kukata simu.Japokuwa sikujua walichokizungumza kwa kina, lakini nikajua ni lazima atakuwa amemwagiza huyo meneja aje kwa ajili ya kunitambulisha kwake.
Baada ya dakika tatu au nne, akaja kijana mmoja mweupe kidogo akiwa amevalia suti nyeusi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Naam bosi.""Unamuona huyu binti," alisema huyo Mwarabu huku akininyooshea kalamu aliyokuwa nayo mkononi.
"Nimemuona bosi," akaitikia huyo meneja na kuniangalia tena.
"Kuanzia leo atakuwa pamoja nasi hapa, nimempangia sehemu ya mazingira kwa maana ya usafi," alisema na kisha kutulia kidogo."Sasa nataka umchukue kwa ajili ya kumtambulisha na kumwelekeza baadhi ya taratibu nyingine za kazi."
"Sawa," akajibu meneja na kunionesha ishara ya kumfuata.
Tukatoka nje, nikiwa nyuma yake lakini mkimya sana.
"Twende huku," akaniambia lakini sikujibu chochote zaidi ya kumfuata kwa nyuma.Tukazunguka upande mwingine wa pili wa hoteli hiyo. Kulikuwa na bustani nzuri ya kupendeza sana. Kulikuwa na watu wengine wakiendelea na kazi mbalimbali za usafi. Kulikuwa na waliokuwa wakikata maua kwa kutumia mikasi mikubwa.
Wengine walikuwa wakimwagilia maji na kuchimbua udongo kabla ya kuusawazisha kwenye mashina ya baadhi ya maua."Hawa ni wenzako, utakuwa nao kwenye kazi mbalimbali za usafi ila kwa leo ni heri uungane nao ili kesho tukupangie sehemu zingine za usafi," alisema meneja.
"Sawa, niko tayari."
"Sasa ngoja nikupe sare za usafi."
"Sawa."Meneja alitoka na kuniacha nikiwa naendelea kuwaangalia wenzangu waliokuwa bize na kazi. Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu.
Muda mfupi baadaye, meneja alirejea akiwa na sare mkononi.
Akanipa na kunionesha sehemu ya kubadilishia nguo. Nikaingia chumba hicho na kuvaa zile sare.
Nilifanana kabisa na wenzangu. Nikapangiwa sehemu moja na mvulana mmoja aliyeonekana kuwa mpole na mkimya sana.
Tukasalimiana. Kazi zikaendelea kama kawaida."Karibu sana dada," alinikaribisha huyo kijana nami nikamjibu kwa sauti ya chini kabisa.
Jua lilikuwa kali sana siku hiyo. Ilipowadia saa nane, tukapumzika kidogo ambapo wenzangu walianza kuzungumza na kusimuliana habari mbalimbali.Nilikuwa kimya sana. Sikuwa na mtu wa kuzungumza naye kutokana na hali ya ugeni. Lakini pia hata ukimya wa yule mvulana niliyepangwa naye sehemu moja, ulichangia kunifanya mpole na mkimya mno.
Wakati tumepumzika, nikapata wasaa wa kumuwazia mdogo wangu Inana. Nikawaza jinsi nilivyomuacha huko kijijini na kujikuta nikitamani sana kujua anaendeleaje na maisha ya Chalinze. Kichwa changu kikajawa na kughubikwa na mawazo.
Nikaona wenzangu wakifuata chakula upande wa pili kulikokuwa na jiko la hoteli hiyo.Kila mmoja akawa anatoka na sahani ya wali na kabeji. Sikuwa na hamu ya kula kabisa, sijui ni kwa sababu gani!
Tukaendelea kupumzika, lakini mawazo yaliendelea kunisumbua sana kichwani hasa nikimfikiria mdogo wangu.
"Mungu yupo," nikajikuta nikitamka maneno hayo kwa sauti na kumfanya yule mvulana niliyekuwa nimekaa naye karibu ageuke na kuniangalia kwa umakini kidogo.Akanikazia sana macho na kuonesha dalili zote za kutaka kunisemesha jambo japo hakuthubutu kufunua kinywa.
Tukiwa tumejipumzisha, ghafla yule meneja akatokea na kutufanya sote tuendelee na kazi.
Ilipohitimu saa kumi jioni, meneja alikuja na kutuambia kuwa tukabadilishe nguo ili tuwapishe wenzetu waliotakiwa kuingia jioni na kuendelea na kazi."Wewe njoo huku," alisema meneja kwa ishara ya kunitaka nimfuate.
"Vipi, najua hutakuwa na nauli ya kurejea nyumbani Buguruni kama nilivyoelekezwa na bosi, chukua hii itakusaidia, lakini kesho ukifika unione kabla ya kufanya chochote," akaniambia yule meneja huku akinikabidhi shilingi elfu kumi.
"Sawa, ahsante," nikaitika na kumshukuru.
"Haya, basi tutaonana kesho.""Haya," nikamjibu na kuelekea kwenye chumba cha kubadilishia nguo.
Baada ya kubadili nguo, nilitoka pamoja na baadhi ya wafanyakazi wengine.
"Dada," nilisikia sauti kutoka nyuma yangu ikiniita.
Nikageuka bila kuitikia.
Kumbe alikuwa ni yule kijana niliyekuwa nimepangwa naye sehemu moja ya kazi."Unasemaje kaka?"
"Samahani."
"Nakusikia."
"Naomba kuzungumza na wewe kidogo."
"Endelea.""Unaitwa nani vile?"
"Tunu, kwani vipi?"
"Nilitaka tufahamiane, mimi naitwa Hemed.""Nashukuru kukufahamu," nilimjibu huku nikianza kupiga hatua kuendelea na safari yangu.
"Kuna jambo moja nataka nikuulize."
"Jambo gani tena?" Nikamuuliza kwa sauti ya juu na ukali kidogo kutokana na uchovu pamoja na mawazo niliyokuwa nayo.
Ukali wangu ulimfanya yule kijana kunyamaza kidogo. Akakosa neno la kuongeza, nami nikaendelea na safari yangu.
Nikatembea hatua chache kabla ya kufika eneo la kupandia mabasi ya Ubungo ambapo baadaye nilitakiwa nikapande tena mabasi ya Buguruni.
Nilipofika kwenye kituo hicho, nikaungana na abiria wenzangu waliokuwa wakisubiri mabasi. Nikajitenga pembeni kidogo.
Muda mfupi baadaye, yalifika mabasi mawili ya kuelekea Ubungo. Nikapanda mojawapo na kuketi kiti cha nyuma kabisa ambapo niliendelea kuwa mkimya sana.
Mawazo yaliendelea kuisumbua akili yangu. Nikaendelea kumkumbuka sana mdogo wangu. Inana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliendelea kuzama kwenye lindi la mawazo hadi niliposhtuliwa na sauti ya kondakta aliyekuwa akiomba nauli yake baada ya basi hilo kuwasili kituo cha Ubungo.
"Oyaa wewe sista, nipe changu bwana."
"Sawa jamani," nilimjibu yule kondakta huku nikimkabidhi nauli yake.
"Hayo ndiyo mambo," alisema yule kondakta lakini sikumjali zaidi ya kushuka na kuelekea kwenye kituo cha kusubiria mabasi ya kuelekea Buguruni.
Kutokana na wingi wa watu kituoni hapo, abiria wengi walikuwa wakigombania mabasi. Nami nikaungana nao nikiwa na mkoba wangu begani. Niliuangalia kwa uangalifu wa hali ya juu mno.
Baada ya pilikapilika ya kugombania mabasi, nilibahatika kupata basi moja na kukaa kwenye kiti ambapo niliendelea kuwa kimya huku msongo wa mawazo ukizidi kuniandama.
Nilifika nyumbani jioni sana kutokana na foleni ndefu iliyokuwepo kwa siku hiyo. Nilikuwa nimechoka kweli.
"Naona mwenzangu sasa mambo yameanza kukuendea sawa," shangazi aliniuliza baada ya kusalimiana na kujuliana hali tangu tuachane nyakati za asubuhi.
"Afadhali kidogo, Mungu ameanza kuonesha mwanga," nilimjibu lakini kwa sauti iliyoashira uchovu mno.
"Umeanza kazi?"
"Ndiyo shangazi."
Baada ya kubadilishana mawazo na shangazi, niliingia chumbani ambapo nilitandika jamvi langu la kulalia lililokuwa limechakaa kupindukia.
Sijui ni saa ngapi nilipitiwa na usingizi, nilishituka ikiwa tayari ni asubuhi.
Nilimsabahi shangazi aliyekuwa tayari anajiandaa kwa biashara zake za mama ntilie.
Haraka sana nikaingia bafuni. Nikaoga pamoja na kusukutua mswaki kabla ya kujiandaa kwa safari ya kurejea kazini ili niwahi majukumu ya usafi nitakayopangiwa kwa siku hiyo.
"Haya kwaheri shangazi."
"Haya basi, baadaye," shangazi alinijibu lakini kwa sauti iliyojaa utulivu mno.
Nikawahi hadi kituo cha mabasi ya Ubungo. Nikawasili na kuunganisha hadi Mwananyamala, eneo langu jipya la kazi.
Niliendelea na kazi za usafi hotelini hapo kwa siku kadhaa bila kuona dalili yoyote ya kubadilishiwa nafasi nyingine ya kazi. Hata hivyo sikukata tamaa hata kidogo. Nikaendelea kujipa matumaini huku Mungu akiendelea kuwa nguzo na tegemeo langu kuu.
Kawaida wafanyakazi wote wa hotelini hapo walikuwa na desturi ya kubadilishana siku ya kupumzika kwa siku nne mfululizo baada ya kuingia kazini kwa muda wa majuma mawili mfululizo.
Siku moja nilipokuwa naingia kazini asubuhi, nilimkuta yule Mwarabu amesimama pembeni mwa lango kuu la kuingilia hotelini hapo.
Tofauti na siku nyingine nilizokuwa nimemzoea kwa ukarimu wake, siku hiyo hakuwa mwenye furaha kabisa. Wajihi wake ulionekana kugubikwa kwa mawazo tele.
"Salama, za kwako," aliniitikia kwa sauti ya chini baada ya kumsabahi.
Nilipompita nikiwa naelekea eneo la kubadilishia nguo kabla ya kuanza kazi, nilisikia akiniita.
"Naamu," niliitikia kwa uoga kidogo.
"Njoo. Unaendeleaje na kazi," aliniuliza akiwa amenikazia sana macho.
"Vizuri tu bosi," nilimjibu kwa utulivu.
"Mbona kama…"
"Hebu njoo ofisini kwangu," aliniambia huku akipiga hatua kuelekea ofisini ambapo nami nilimfuata.
Baada ya kufika ofisini, alivua koti lake na kulitundika juu ya kiti chake kirefu kilichokuwa nyuma ya meza nzuri ya kifahari sana.
Akashika mkebe uliokuwa na sigara mezani hapo. Akachomoa moja na kuiwasha kabla ya kuanza kuivuta.
Moshi ulitapakaa chumba kizima cha ofisi hiyo. Ulipita ukimya kwa muda.
"Nimekuita asubuhi hii kwa lengo la kuzungumza na wewe," yule Mwarabu alifungua uwanja wa mazungumzo huku akiinua uso na kupumua moshi mwingi wa sigara kupitia matundu ya pua na mdomoni.
Alikohoa kabla ya kuendelea.
"Nilikuuliza unaendeleaje na kazi," alirudia swali lake la awali huku akimalizia kukaa.
"Naendelea vizuri bosi," nilimjibu na kumwangalia usoni ambapo tulikutanisha macho kwani naye alikuwa amenikazia ya kwake.
Akatulia na kuendeleza mazungumzo yake.
"Nimeambiwa na meneja kuwa unaendelea vizuri sana, lakini mara nyingi sana unaonekana mkimya na mnyonge kuliko kawaida, una tatizo gani kwani," aliniuliza kwa kuonesha hali na wajihi wa ukarimu sana.
"Niko sawa," nikajibu japo ukweli ni kwamba muda wote nilionekana kuwa mwenye msongo wa mawazo kutokana na magumu tunayoyapitia mimi na mdogo wangu Inana.
"Sikiliza."
"Ndiyo bosi."
"Hapa tuna utaratibu wa watu kupata muda wa kupumzisha akili baada ya kuhudhuria kazi kwa wiki mbili mfululizo."
Alipofika hapo akatulia tena.
"Miongoni mwa wafanyakazi tuliowateua kuwapa mapumziko ya muda wa wiki mbili ni pamoja na wewe," alisema kisha kufungua droo ambapo alichomoa bahasha fulani yenye rangi ya kaki.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akanikabidhi bahasha hiyo na kuniambia ndani mlikuwa na kiasi fulani cha pesa ambacho kingenisaidia kwa kipindi chote cha likizo kabla ya kurudi kazini ambapo mshahara ungekuwa tayari.
Tulizungumza mengi sana ofisni kwake, lakini akanitakia mapumziko mema na kuniambia kuwa naweza kurudi nyumbani kuanzia wakati ule.
"Ahsante sana bosi," nilimjibu na kuinuka.
Nilipofika nje, nilikutana na meneja. Nikamueleza yote tuliyozungumza na bosi ambapo aliridhia vyema na kuniruhusu.
Nilipanda basi nikiwa mwenye furaha kubwa sana. Nikawa nawaza jambo moja tu, kwenda kumjulia hali mdogo wangu Inana kule kijijini.
Japo sikujua ni kiasi gani hasa kilikuwa ndani ya bahasha hiyo, moyoni nilijipa matumaini makubwa kuwa nitaweza kujikimu vyema.
"Sijui Inana atakuwa anaendeleaje na vibarua vyake kwa sasa," nilijikuta nikiwaza nikiwa nimekaa kwenye siti ya basi kuelekea Ubungo kabla ya kuunganisha hadi Buguruni yaliko makazi yangu.
"Hee, kulikoni tena mapema hii yote kurudi nyumbani mwanangu," shangazi aliniuliza kwa shauku baada ya kuwasili nyumbani nikiwa sina raha kabisa.
"Hapana shangazi, nimepewa mapumziko kwa muda wa wiki mbili ambapo ni utaratibu wa hoteli ile kwa watumishi wake."
"Haya, sasa unawaza nini?" Shangazi aliniuliza akiwa amejishika kiunoni.
"Kwa sasa nawaza kwenda kumjulia hali mdogo wangu huko kijijini, nikajue ana hali gani na anaendelea vipi na mihangaiko yake," nikamjibu kwa sauti iliyoashiria uchungu mwingi kwa ndani.
Roho ilikuwa ikiniuma sana siku hiyo. Kichwani niliitabiri vyema hali ya mihangaiko anayokabiliana nayo Inana kwa kuhangaikia vibarua ili kujikimu na maisha magumu.
Nikiwa naendelea kuwaza na kuwazua, ghafla mawazo yalinirejesha kipindi kirefu cha nyuma. Nikakumbuka jinsi tulivyoishi maisha ya furaha na wazazi wetu. Machozi yakaanza kunilengalenga. Niliumia mno moyoni.
Nikazidi kuwaza jinsi tulivyositisha masomo baada ya kufiwa na wazazi wetu, nikafikiri namna nilivyokuwa na ndoto za maisha mazuri baada ya kumaliza masomo. Machozi yakazidi kunibubujika kwa wingi.
"Wewe mbona unalia tena?" Shangazi aliniuliza baada ya kunitazama kwa umakini.
"Hapana shangazi."
"Hapana wakati naona machozi yakikumwagika?"
"Kichwa kinaniuma shangazi," nilimdanganya japo ukweli ni kwamba siku hiyo mawazo juu ya maisha yetu na mdogo wangu yaliutesa sana ubongo wangu.
"Umeshameza dawa?"
"Ndiyo shangazi."
"Basi kalale ili upate wasaa wa kupumzika."
"Sawa," nikamjibu na kunyanyuka kuelekea ndani.
Nilipofika ndani, jambo la kwanza kulifanya ilikuwa ni kufungua ile bahasha nikiwa na hamu kubwa sana ya kujua ni kiasi gani cha pesa kilikuwemo.
"Mungu wangu!" nilijikuta nikitamka kwa sauti baada ya kufunua ile bahasha na kuona kilichokuwemo.
Noti nyekundu zilikuwa zimejipanga kwa wingi. Haraka sana nikazichomoa na kuanza kuzihesabu.
"Nne, tano, siiita," nilitamka kwa sauti nikimalizia kuihesabu noti ya mwisho na kugundua kuwa zilikuwa ni shilingi elfu sitini. Nilipiga magoti chini na kuanza kumshukuru Mungu kwa riziki aliyokuwa amenijalia kwa siku hiyo.
"Ahsante muumba wa mbingu nchi, jina lako lihimidiwe baba," nilitamka maneno hayo huku machozi yakinitiririka kwa wingi. Ilikuwa ni kama muujiza kupata kiasi kikubwa namna hiyo cha pesa.
Nikajizoazoa na kujilaza kwenye kigodoro changu. Kichwani nilijawa na mawazo tele. Kutokana na wingi wa mawazo, nilipitiwa na usingizi hadi saa nane mchana nilipoamshwa na shangazi kwa ajili ya chakula.
"Unaendeleaje na hali kwa sasa?" Shangazi aliniuliza huku akinisogelea.
"Najisikia nafuu ila mwili hauna nguvu tu."
"Kula upate nguvu, halafu umeze dawa zako, sawa eeh."
"Sawa."
Nilienda kunawa na kujumuika mkekani na shangazi kwa ajili ya kupata chakula.
Wakati wa kula, nilitumia mwanya huo kumjuza shangazi juu ya mipango yangu ya safari ya kwenda kumjulia hali mdogo wangu Inana kule kijijini.
"Ulisema umepanga kwenda lini?"
"Kesho asubuhi."
"Utarudi lini?"
"Nitakaa kwa juma moja."
"Sawa, sina kipingamizi juu ya hilo mwanangu," shangazi aliniambia huku akiniangalia kwa macho ya huruma.
Baada ya mazungumzo hayo, sikuendelea kula. Nikanawa na kurudi ndani ambako nilijiandaa kwenda kuoga.
Nilimaliza kuoga na kubadili nguo. Nikaanza kupanga baadhi ya nguo zangu ndani ya furushi ikiwa ni maandalazi ya safari.
Niliendelea kujipumzisha hadi saa kumi ambapo shangazi aliniagiza sokoni kwenda kumnunulia mchele na baadhi ya vitu vingine vya kwenye mgahawa wake wa mama ntilie.
Nikiwa sokoni, nilimnunulia mdogo wangu nguo kadhaa zikiwemo za ndani. Nikafanya na manunuzi madogomadogo kama dawa ya meno, sabuni, mafuta ya kupaka na vitu mbalimbali vya kawaida.
Nilirejea nyumbani nikiwa mchovu sana. Nilimkabidhi shangazi vitu vyake kisha nikaingia ndani. Baadaye nilitoka na kujiegesha kwenye ukuta wa kijumba chetu kibovu. Mawazo juu ya maisha yetu na hatma yetu yaliendelea kunisumbua sana akilini mwangu. Nikiwa nawaza, sauti ya mama yangu iliyojaa upendo ilinijia akilini. Nikajikuta nikiingiwa na uchungu mkubwa mno moyoni.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Machozi yakaendelea kutuama kwenye mboni. Macho yangu yakadhoofu kwa machozi. Ulikuwa ni uchungu wa hali ya juu.
Niliendelea kukaa ukutani hapo hadi ilipojiri saa moja na nusu nilipoingia ndani. Nilala mapema huku nikiendelea kuwaza mambo mengi sana juu ya maisha. Niliendelea kumuomba Mungu atende miujiza yake.
Asubuhi nilidamka mapema na kumkuta shangazi akiwa anaendelea na shughuli zake. Nikamjulia hali.
"Mbona umeamka mapema sana."
"Nataka nijiandae kwa safari shangazi."
"Mapema yote hii jamani!"
"Ningependa nifike mapema."
Niliingia ndani na kutoka na kifurushi changu.
"Haya shangazi, ngoja nijikongoje," nilimuaga huku nikiwa nimepiga magoti kwa ishara ya heshima.
"Sawa mwanangu, nakutakia safari njema."
"Ahsante sana shangazi."
"Bahati mbaya hali yangu siyo nzuri ningekupa walau chochote kwa ajili ya Inana," alisema shangazi akiwa ameshika tama kwa masikitiko.
"Usijali shangazi," nikamtia matumaini.
Nikaelekea kwenye kituo cha kupanda mabasi hadi Ubungo ambako nilichukua gari la kwenda Chalinze. Niliwasili Chalinze saa tatu na nusu asubuhi. Nikapanda baiskeli hadi nyumbani.
"Iiiii, jamani dada," Inana alisema baada ya kuniona na kunikimbilia kwa furaha kubwa.
Habari za huko jamani dada?
Nzuri, sijui wewe?
Salama jamani.
Za hapa nyumbani vipi?Mm! Nipo nahangaika hivyohivyo, Mungu anasaidia sana.
Nilimlipa yule mwendesha baiskeli ya kukodisha ujira wake. Akaondoka na kutuacha na Inana.
Nilikukumbuka sana mdogo wangu.
Hata mimi dada, unaendeleaje huko Dar es Salaam?Vizuri, ngoja nikikaa nitakusimulia yote. Kwa sasa ngoja nipumzike kidogo.
Hali niliyoikuta nyumbani ilinitia simanzi. Kijumba kibovu kilikuwa kimezidi kujiinamia. Nikamuangalia Inana. Moyo uliniuma mno. Hakika niliumia kupita kiasi.
Nikashindwa kuingia ndani kwanza, nikawa nakikagua kile kijumba chetu kwa macho.Dada, Inana aliniita huku akinisogelea baada ya kupeleka ndani kifurushi nilichokuwa nimebeba.
Bee, niliitika huku nikijifuta machozi kwa kiganja cha mkono wa kushoto.
Kuna jambo nataka nikuambie, alisema Inana na kunifanya nimuangalie kwa umakini ili nisikie alichokusudia kunieleza.Ha! Sasa mbona unalia tena dada?
Maisha mdogo wangu, maisha Inana.
Kwani hujafanikiwa kupata kazi ?
Siyo hivyo.
Sasa kumbe nini tena?Hii hali Inana, inaniuma sana kuona tuko katika hali hii.
Mmh! Inana aliishia kuguna.
Hee, wewe Inana wewe.
Vipi dada.
Yaani siku hizi una simu? nilimuuliza Inana kwa taharuki kubwa baada ya kuona ameshikilia simu kwa mkono wa kushoto.Mmh!, ina maana dada ndiyo umeiona sasa hivi?
Eee, nilikuwa sijaona kabisa umenunua simu! nilisema huku nikikaa kwenye mfuko wa foronya uliokuwa karibu na mahali tulipokuwa.
Mshangao na maswali yangu mengi, yakamfanya Inana asahau alichotaka kuniambia baada ya kuniita.
Inana alikuwa amenunua simu aina ya sumsung. Ilikuwa ni fupi yenye mwanga wa njano kila ikiwaka.
Nimebangaiza polepole kwa kujinyima dada, maisha ni magumu sana, alinieleza Inana akiwa anaishika simu yake.Sasa inakusaidia nini kwa sasa, nilimuuliza huku nikimkazia macho ya udadisi mkubwa.
Inanisaidia kwa mambo mengi mno dada.
Kama yapi?
Kuna wakati vibarua huwa vya shida sana, ninalazimika kukaa nyumbani, lakini vikipatikana, watu mbalimbali wenye namba zangu hunipigia na kunitaarifu kuwa sasa vinapatikana, Inana alinijibu kwa kirefu na kunifanya nimuelewe.Haya bwana, nimekuelewa.
Vipi huko mjini, maisha yanaendeleaje?
Mungu anasadia sana.
Aisee.
Unamkumbuka yule mwarabu aliyenigonga kwa gari wakati ule?
Ee dada.Basi nilikutana naye.
Ha! Ikawaje sasa, Inana aliniuliza kwa shauku ya kutaka kujua kilichojiri.
Nikamweleza jinsi nilivyokutana na yule mwarabu.
Hadi jinsi alivyonisaidia kupata kazi hotelini kwake. Inana alishangaa sana kusikia nafanya kazi kwenye hoteli ya yule mwarabu.Aisee Mungu ni wa ajabu sana, alijikuta akitamka maneno hayo na kunifanya nimwangalie tena usoni.
Moyoni nikajikuta nikipata hamu ya kununua simu.
Niliingia ndani na kukuta mazingira kama niliyoyaacha, japokuwa kuna baadhi ya vitu vichache ambavyo Inana alikuwa amevinunua kwa kuibangaiza na vibarua.
Niliendelea kuishi huko kijijini kwa muda wa juma moja, ndipo nikaamua kurejea tena Dar es Salaam.
Kwa hiyo mimi naondoka kesho.Sawa dada, lakini mimi niko mpweke sana hapa nyumbani, alisema Inana na kunifanya nijisikie uchungu mkubwa sana moyoni. Maneno yake yalinichoma kwa hisia kali mno. Nikanyanyuka mahali nilipokuwa nimekaa na kumfuata Inana. Nikamkumbatia kwa upendo.
Tulibaki tumekumbatiana kwa muda, huku kila mmoja akisikiliza mapigo ya moyo ya mwenzake. Ulikuwa ni usiku wa maumivu mno kwetu. Kwa muda wa juma moja tulilokaa pamoja, tulizoeana sana.
Lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kurejea kwenye kazi yangu.Siku hiyo tukafanya agano kubwa na la ajabu mno maishani.
Inana, nilimuita mdogo wangu huku nikibubujikwa machozi yaliyolowanisha mgongo wake. Hali kadhalika kwa upande wake, naye alikuwa analia huku akinilowanisha kwa machozi mgongoni mwangu.
Na...aaamu dada, aliitika kwa sauti iliyojaa kwikwi na kigugumizi cha machungu na maumivu makali sana.Acha niende, nakwenda kukuandalia mazingira ya kupata kazi, baadaye nitarejea kukuchukua ili tuwe pamoja Dar es Salaam kupambana na maisha, nilisema maneno hayo kabla ya kutulia kidogo.
Nitashukuru sana dada, alisema Inana kwa sauti ya utulivu.
Kitu kimoja nataka nikuambie.
Nakusikiliza dada.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Katika maisha yetu hatutakufa masikini, nilisema huku nikijinasua mikononi mwake na kubaki tumetazamana.Nikamwambia ni lazima tufikie vilele mbalimbali vya mafanikio maishani mwetu. Kwa pamoja tukaapa kupambana na maisha kwa kiwango cha juu mno. Umasikini uliokuwa umetuzunguka ulitutia uchungu mkubwa.
Kwa muda wa saa moja na dakika kadhaa, tulibaki tumeshikana mikono na kupeana faraja ya matumaini.Sawa dada, nimekuelewa lakini tutatumia njia gani kufanikiwa? Inana aliniuliza huku akinitazama kwa umakini mkubwa.
Ipo njia, nitakuambia kesho asubuhi, nilimjibu kwa ujasiri hali iliyomfanya ashituke.
Mm!," Inana aliishia kuguna na kuendelea kunitazama.
"Basi tujiandae kulala mdogo wangu," nilimsemesha kwa sauti ya juu kidogo iliyompelekea kushituka kutokana na kuzama kwenye lindi kubwa la mawazo.
Inana alinielewa, sote tukaachaana na kuongozana hadi kulipokuwa na kijitanda chetu kilichochakaa na kutandikwa kwa matambara mabovu.
Tulipiga magozti na kumshukuru Mungu kwa kutujaalia afya njema kwa siku hiyo, pia tulimuomba atulinde kwa usiku huo, tuweze kuamka tukiwa wazima wa buheri wa afya.
Baada ya maombi, tulijitupa na kuanza kuusaka usingizi kwenye kitanda hicho cha kuchosha.
Tukiwa kitandani, tulisimulizana simulizi mbalimbali kuhusu maisha, pia tulijikumbusha mambo ya nyuma ikiwemo nyakati za shule. Ni hapo ndipo kila mmoja wetu alipatwa na majonzi mazito moyoni.
Tulijikuta tukipitiwa na usingizi hadi asubuhi. Nilikuwa wa kwanza kudamka, nikakaa kitako na kumuangalia Inana aliyekuwa bado anaufaidi usingizi wa asubuhi ulioambatana na kibaridi cha kisurisuri.
Nikawa nawaza ni kwa jinsi gani nitamtafutia Inana kazi huko mjini, angalau tuanze kusaidizana majukumu mbalimbali.
Tulikuwa na vita kubwa iliyokuwa mbele yetu, vita ya kupambana na umasikini uliokuwa umezonga na kutuzunguka kila mahali penye uwepo wetu.
Hakika tulikuwa tumezama na kutitia kwenye tope la ufukara. Hii ilitokana na kuondokewa na wazazi wetu ili hali akili zetu zilikuwa bado nyembamba.
Baada ya kuwaza na kuwazua mengi kuhusu maisha, hatimaye kulizidi kupambazuka. Mwanga wa jua ukaimulika nchi na kulifukuzia mbali giza lote. Kulikuwa na utulivu wa hali ya juu mno.
Nikatoka nje na kuchuchumaa mlangoni. Milio ya ndege waliokuwa wakiruka kutoka tawi moja kwenda jingine wakifurahia mapambazuko na mwanzo wa siku mpya ilikuwa ikisikika kwa ustadi mkubwa.
Nikiwa naendelea kusikilizia milio hiyo mitamu ya ndege wa aina mbalimbali, nilisikia Inana akiniita. Bila kuitikia niliingia ndani haraka na kumkuta akiwa amekaa huku akiwa ameshika simu yake.
"Vipi?," nilimuuliza huku nikimsikiliza kwa umakini.
"Umeamka saa ngapi jamani?."
"Sasa ndiyo salamu hiyo Inana?," nilimuuliza na kumkazia macho.
"Samahani dada, shikamoo," Inana alinisabahi kwa heshima na hali ya uoga kidogo iliyoashiria kujutia kosa lake la kuanzisha mazungumzo bila ya kujuliana hali.
"Marhaba, umeamkaje?"
"Sijambo tu, sijui wewe?"
"Salama, najiandaa kuondoka mapema hii."
Tulizungumza mengi, lakini Inana akanikumbusha juu ya vipi tutaweza kutokana na hali yetu ya umasikini iliyokuwa ikitukabili kwa kiasi kikubwa, kama nilivyomuahidi jana yake usiku wakati wa mazungumzo yetu maalumu.
"Na wewe husahau tu jamani?"
"Siwezi kusahau dada, si unajua ninavyouchukia umasikini huu."
"Sikiliza Inana, njia pekee bora ya kutusaidia sisi kuondokana na umasikini tulionao, ni kufanya kazi kwa nguvu na bidii zote, kuwa na nidhamu katika matumizi ya pesa pamoja na na kumtanguliza Mungu katika kila tulifanyalo.
"maana yeye ndiye nguzo muhimu sana maishani mwetu, na bila yeye hakuna linazoweza kufanyika chini ya jua, tupendane sisi kwa sisi, tuwaheshimu watu na kuwatendea yaliyo mema kama jinsi ambavyo tungependa kutendewa na watu," yalikuwa ni maneno mazito mno yalivyoonekana kumuingia vilivyo Inana.
Inana aliangalia juu, akashusha macho chini na kuvuta pumzi kwa nguvu na kuishusha taratibu.
"Dada Tunu," Inana aliniita kwa sauti ya uchungu huku machozi yakianza kutengeneza mifereji kwenye mboni za macho yake.
Huo ndiyo ukweli Inana, inabidi tukabiliane na maisha kwa kutumia silaha hii," niliendelea kumwambia mdogo wangu huku nikijiandaa kwa safari ya kurejea Dar.
Ilipofika saa moja na nusu asubuhi, niliagana rasmi na Inana nikimuahidi kumtafutia kazi maalum ya kujipatia kipato angalau kama kile cha kwangu kuliko kuendelea kuhangaika na vibarua kama alivyokuwa akifanya kwa wakati huo.
"Sawa dada, nitafurahi kama utafanya hivyo maana nimechoka kubangaiza na vibarua vya leo vipo kesho hamna," alisema Inana wakati akinitoa nyumbani kuelekea kwenye stendi ya Chalinze.
Alinisindikiza hadi nilipopata baiskeli ya kukodi kuelekea stendi ya mabasi ya Chalinze. Inana akarudi nami nikapanda. Wakati baiskeli ikianza safari, niligeuka na kumuangalia Inana ambaye naye alikuwa akigeuka nyuma kuniangalia kila mara. Tulikutanaisha macho na kujikuta tukiachiana tabasamu.
Kwangu halikuwa tabasamu la furaha, bali lilimaanisha huzuni na maumivu makali ya ugumu wa maisha uliokuwa ukitukabili mimi na mdogo wangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sikuacha kugeuka nyuma na kumuangalia hadi alipopotea kabisa kwenye upeo wa mboni za macho yangu ndipo nikaamua kuendelea na safari yangu. Nusu saa baadaye, tukawasili kwenye stendi ya mabasi ya Chalinze ambapo nilimlipa mwendesha baiskeli ujira wake nami kuendelea na ratiba zangu za safari.
Nilisimama kwa muda nikingojea basi la kuelekea Dar na muda mfupi baadaye lilifika basi la Morogoro liitwalo Hood. Nikapanda na kukaa kwenye siti iliyokuwa imebaki kwa nyuma kabisa. Safari ikaanza. Njia nzima nilikuwa nikitafakari ni jinsi gani nitaweza kutimiza ahadi ya kumtafutia kazi Inana. Nikawa namuomba Mungu kimoyomoyo. Nikamwambia hakuna wakati niliokuwa namhitaji kama kipindi hicho cha magumu nilichokuwa nakipitia. Niliendelea kusali moyoni kwa imani kubwa.
Safari ikaendelea, tulipofika Kibaha nilianza kuhisi usingizi mzito ukininyemelea, nikawa najikaza lakini sikuweza, hatimaye nililala. Katikati ya usingizi huo mtamu, nilijiwa na ndoto ambayo hakika ilinijaza nguvu na matumaini makubwa mno maishani mwangu.
Katika ile ndoto, mimi na mdogo wangu tulikuwa tunaishi maisha ya kitajiri na kifahari kupita kiasi. Kila kitu kilikuwa kimebadilika na kubaki historia tu. Tulikuwa na ukwasi wa hali ya juu uliotokana na kufanya kazi kwa bidii. Katika utajiri wetu, asilimia ishirini tuliitoa kwa watoto yatima ambao kila tukiwaangalia walitukumbusha maisha yetu ya zamani.
Ndoto yangu ikazidi kukolea, lakini nikiwa naendelea kuifaidi, ghafla niliamshwa na sauti nzito ya mwanaume akiniambia tumefika hivyo niamke. Nilifumbua macho. Niliangaza huku na kule ndipo kupitia dirisha la basi hilo nikakutana na maandishi yaliyosomeka Ubungo Bus Terminal'. Tayari tulikuwa tumewasili Dar. Haraka nikajiandaa na basi liliposimama vyema nikashuka na kimzigo changu.
Nikaanza kutoka ndani ya stendi na kuelekea kwenye kituo cha mabasi ya kwenda Buguruni nilikokuwa nikiishi. Nikajikokota kwa uvivu uliotokana na usingizi hadi nikavuka upande wa pili wa barabara na kunyoosha hadi karibu na eneo la daraja ambapo nilisimama na kungojea mabasi ya Ubungo Posta ili nikashukie Buguruni-Malapa.
Basi lilifika nami nikapanda. Nilipokaa kwenye siti sikuwa na mazungumzo na mtu yeyote zaidi ya kuwa kimya na kuanza kutafakari kwa kina ile ndoto. Baada ya kuzama ndani ya mawazo nilijikuta nikifurahia moyoni. Lakini nilipoyafikiria maisha niliyomuacha nayo mdogo wangu Inana pamoja na ninavyoishi kwa tabu na shida kule Buguruni kwa shangazi, furaha yote iliyeyuka.
Yalikuwa ni maisha yaliyoumiza mno. Basi likaanza safari na baada ya dakika chache tukawasili Buguruni-Malapa. Nikapiga hatua hadi nyumbani. Sikumkuta shangazi lakini kwa kuwa mlango ulikuwa ni wa kuegesha tu, sikupata tabu sana. Nilifungua na kuingia.
Kutokana na uchovu niliokuwa nao, nilijilaza kwenye kile kigodoro changu kichafu ambapo nilijikuta nikipitiwa na usingizi tena. Nilipoanza kusinzia tu, shangazi aliingia na kuniamsha.
"Habari za siku?"
"Nzuri," niliitikia huku nikifikicha macho yaliyokuwa na usingizi mzito.
"Bora umerudi, kuna kitu nataka nikujulishe kuhusu makazi tunayoishi hapa," shangazi aliniambia kwa uso wa huzuni na kunifanya nihisi kitu kisicho cha kawaida.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment