Search This Blog

Sunday 19 June 2022

KISU CHENYE MPINI MWEKUNDU - 3

 





    Simulizi : Kisu Chenye Mpini Mwekundu

    Sehemu Ya Tatu (3)



     Aliondoka pale nyumbani huku akikabiliwa na mtihani mgumu kwa mke wa Gervas. Atampata vipi ili amweleze ukweli wa mambo. Iwapo atamueleza kweli haitamletea matatizo. Aliona wazi kuwa kuna hatari ya kushtakiwa kwa kueneza maradhi wakati anajua wazi kuwa yeye ni muathirika. Lakini kama angeweka wazi kweli angepata ule msaada? Angeupata vipi wakati Gervas alikataahata fedha. Kwanini Gervas ambaye kafunga ndoa kanisani atake liwazo lingine nje ya ndoa? Labda haya ni malipo mazuri ya usaliti. Hapana lazima nimuokoe mkewe, nitajibu nini mbele ya Mungu kama yule mwanamke atakufa kwa ajili yangu? Alijiuliza maswali mengi bila kupata njia sahihi ya kumnusuru mwanamke mwenzake.

    Maandishi makubwa ya shule ya Sekondari Mbagala yalimzindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Akatembea moja kwa moja kuelekea ofisi ya mkuu wa shule. Alikuwa hajui kama afurahi au ahuzunike. Kitendo cha kupata nafasi ile baada ya kuudhalilisha utu wake kilimuumiza sana. Alitamani amfanye jambo baya Gervas ambaye alimfanyia mambo yale bila hiyari yake upande mwingine ukamwambia kuwa hakuwa na sababu ya kufanya yote yale adhabu aliyoipata ilitosha.

    Akaingia moja kwa moja kwenye ofisi ya walimu. Hakukuwa na mwalimu yeyote, akafuata kidirisha kidogo kilichoandikwa MAPOKEZI.

    “Habari yako dada.”

    “Nzuri nikusaidie nini?”

    “Naomba kuonana na mkuu wa shule.”

    “Una tatizo gani?”

    “kuna barua inabidi nimfikishie imetoka kwa Afsa elimu taaluma.”

    “Ni barua ya kikazi au binafsi?”

    “Ni barua ya kikazi.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naomba hiyo barua.” Akampa. Yule dada akaisoma kisha akagonga muhuri.

    “Nifuate.” Akafungua mlango na kuja kule nje aliko mama Beda. Akamfuata.

    “kaa hapo.” Akakaa sehemu iliyoandikwa wageni.

    Akaingia kwenye ofisi iliyoandikwa MKUU WA SHULE . Baada ya dakika kama kumi na tano yule dada akatoka. Akampa karatasi nyingine zipatazo nne. “Mwanafunzi amekubaliwa kujiunga lakini inabidi ujitahidi ndani ya wiki mbili awe amesharipoti.” Aliongea yule dada.

    “Ahsante.”Alisikika mama Beda huku akipiga hatua kuiacha ofisi ile.



    * * *



    Muda wa masomo ulikuwa umeisha wanafunzi wa Zanaki walianza kuondoka madarasani. “Vick nisubiri nina maongezi kidogo na wewe.” Alisikika kijana mmoja wa kidato cha nne akimsimamisha Vick. “Shikamoo.” Aliamkia Vick

    “Aah. Noma hiyo hakuna mzee wa kuamkiwa hapa mambo.”

    “Poa.” Alijibu Vick huku moyo ukienda mbio.

    “Unajua Vick natafuta nafasi ya kuongea na wewe siku nyingi lakini siipati.”

    “kwanza nani kakutajia jina langu?”

    “Mtu ukimpenda tu lazima utajua jina lake.”

    “unasema unatafuta nafasi ya kuongea na mimi, haya umeipata ongea basi?” alisikika Vick huku akianza kushikwa na hasira.

    “Neno langu ni fupi sana nakupenda Vick.” Vick hakujibu badala yake alitoka mbio.

    “Vipi alikuwa anakuambia nini yule kaka mbona umetoka mbio?” Aliuliza Zuwena mwanafunzi aliyekuwa anasoma nae darasa moja.

    “Eti anasema ananipenda.”

    “Mh. Mwenzangu kweli yule kaka ni fataki Ziada, Pili na mimi sote katutongoza anataka amalize form one wote bora tumsemee kwa mkuu wa shule”

    “Achana nae atatupotezea muda bure.”

    Wakafika getini kila mmoja akaelekea upande wake. “Mbagalaa… Mbagalaa…” Konda alimshitua vick ambaye alikuwa kwenye dimbwi la fikra. Akakimbilia lile gari.

    Ilikuwa ni safari ya dakika arobaini na tano kufika rangi tatu. Aliteremka pale kituoni na kupanda kwenye daladala lililokuwa linaelekea kongowe. Mawazo yake yote yalikuwa kwa Beda. Alitaka kujua kama mpango wa kupata shule umefanikiwa. Hivyo alipofika nyumbani tu alibadili nguo haraka na kuondoka. Hakukumbuka hata kula.

    Ulikuwa ni umbali wa dakika kama Thelathini kwa miguu lakini alijikuta akitumia dakika ishirini tu.

    “Karibu Vick, ulikuwa unatamani kumuona mama yangu leo umemkuta.” Alisikika Beda akimkaribisha.

    “Oooh mwanangu huyo.” mama Beda akamkumbatia Vick kwa furaha.

    “Karibu sana mwanangu.’

    “Ahsante mama shikamoo.”

    “Marahaba mwanangu hamjambo huko nyumbani?”

    “hatujambo mama .” Alijibu Vick huku akiminyaminya vidole vyake kwa haya.

    Akatembea taratibu hadi pale alipokaa Beda wakapeana mikono.

    “Vipi umepata shule?”

    “Nimepata Vick, Mungu atakulipa kwa wema ulionifanyia.” aliongea kwa sauti ya kunong’ona lakini ilifika kwenye masikio ya mama yake.

    “wapi?”

    “Mbagala sekondari.”

    “Hongera.”

    “Ahsante.”

    “Nilitaka kujua kama umepata shule, nashukuru kama umepata kwa heri.”

    “Mbona mapema?”

    “Hata chakula sijala nisije nikazusha maswali.”

    “ Ahsante kwa moyo wako mwema” Akamuaga mama Beda, akaondoka



    ****



    Alipanda ngazi taratibu kuelekea katika ofisi ya afisa elimu taaluma. Moyo wake ulikuwa unapiga kwa kasi. Alijua wazi kuwa anayemwendea hayupo ofisini. Alikaa nje ya ofisi muda mrefu akisubiri aondoke. Ni fursa hiyo ndiyo aliyoisubiri sana. Bahati Ilikuwa upande wake kwani yule mtu aliondoka nusu saa kabla ya muda wa kazi kumalizika. Hakutamani kabisa kuonana naye. Licha ya msaada aliompa bado alimchukia kuliko mtu yeyote. Bila ridhaa yangu. Aliwaza kwa huku akisaga meno kwa hasira.

    Alikumbuka kuwa jana yake alikuwa hapa. Hakuwa na bahati kwani mlengwa alikuwa miongoni mwa watu wa mwisho kutoka pale ofisini. Akafika hadi pale mapokezi alipofikia siku ya kwanza. Ilikuwa ofisi ya mapokezi. Alimkumbuka vema yule dada aliyempokea siku ya kwanza ingawa yule dada alimsahau mama Beda. “Habari dada.” Alisalimia mama Beda.

    “Nzuri nikusaidie nini?”

    “Naweza kumuona Mr. Gervas?”

    “Hapana ameondoka, mpaka kesho.”

    “Unaweza kunielekeza nyumbani kwake?”

    “Anaishi Kimara baruti, si mbali sana kutoka kituoni. Kama unatoka kariakoo ukishuka kituoni nenda upande wa kushoto, fuata mtaa wenye maduka mwisho kabisa utakuta saluni imeandikwa Mama K uliza hapo au nenda mbele kuna kanisa la mabati pia unaweza kuuliza hapo kanisani kwani mkewe ni mwekahazina hapo kanisani.”

    Sina swali amemaliza kazi. Aliwaza mama Beda huku moyoni akiwa na furaha kubwa.

    Huyu dada kanisaidia sana sasa nina uhakika wa kumnusuru Mrs. Gervas. Aliendelea kuwaza mama Beda. Akaondoka akiwa mwenye furaha kubwa sana.

    Kimara baruti, kituo cha kwanza mtaa wenye maduka uliza Mama K saluni au kanisani, kanisani ni kuzuri zaidi. Aliwaza huku akichukua beseni lake la matunda ambalo aliliacha getini kwa mlinzi. Huyo, akaendelea kukata mitaa mbalimbali ya jiji hili lenye kila aina ya raha na karaha. Akauza, akauza…. Alipofika Mtongani Beseni lilikuwa tupu.

    Akapanda daladala ambalo lilimfikisha mbagala rangi tatu.



    * * *

    Hakuhitaji daladala kumfikisha shuleni. Wiki hii ya kwanza haikuwa ngumu sana kwake. Alifurahia masomo ingawa shule aliyosoma ilikuwa na uhaba wa walimu. Kwa kushirikiana na Vick aliweza kupata vitu vingi zaidi. Ni kipindi hiki ambacho uhusiano wake na Vick ulikua zaidi. Sasa walitambuana rasmi kuwa ni wapenzi. Mapenzi yao yalitambulika kwa mama Beda.

    Kwa ujumla masomo yaliendelea vizuri. Siku moja jioni akiwa chini ya mti pale nyumbani kwao Beda alimuona Vick akimjia mbio.

    “Vipi Vick mbona unanitisha?

    “Usitishike Beda nimekuja kukufuata twende twisheni.”

    “Mbona sina hela ya kulipia hiyo twisheni?”

    “Usijali nitakupa.” Aliongea kwa sauti ya kunong’ona.

    “wapi?”

    “Rangi tatu kuna kituo kipya cha masomo ya jioni kinachoendeshwa na wanafunzi wa chuo kikuu.”

    Kisha wakaondoka kuelekea huko



    * * *

    Alianzisha tabia mpya kwenda kuuza matunda maeneo ya Kimara baruti. Ni mitaa ambayo hakuwa na mazoea nayo kabisa. Alilazimika. La sivyo asingefanikiwa mpango wake. Ilikuwa siku ya kumi sasa toka aanze kufanya biashara mitaa hii. Ingawa alikuja maeneo haya kwa sababu tofauti na biashara lakini alijikuta akipata wateja wengi na faida kubwa. Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wateja alilazimika kurudia mara mbili. Alileta matunda asubuhi na jioni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kama zilivyo siku nyingine pia siku hii alipeleka matunda pale saluni kwa Mama K. akiwa pale saluni mara nyingi alipiga jicho nyumbani kwa Gervas yule afisa elimu. Alifanya hivyo kwa siku zote tisa. Alishaanza kukata tamaa ya kufanikiwa mpango wake kitu kilichomfanya aanze kuzingatia zaidi biashara. Wakati anaondoka pale saluni akakutana na dada ambaye alikuwa amebeba begi huku akiwa na mtoto mgongoni. Alikuwa ameongozana na msukuma mkokoteni ambaye alipakiza baadhi ya vitu kwenye mkokoteni wake. Alitaka kumpuuza lakini mapokezi ya pale saluni yakamshitua.

    “Karibu Mama Gervas.” Alisikia sauti ya Mama

    ‘K’ yule mama mwenye saluni akimkaribisha yule mgeni.

    Mungu wangu ndiye yeye yule? Alijiuliza huku moyo ukianza kupiga kwa nguvu. Ingawa dhamira yake ilikuwa thabiti kwenye moyo wake hapa alianza kuyumba. Alijiuliza kama amwambie au aendelee kumficha. Msimamo wake ulianza kuyumba. Akapiga moyo konde.

    Ngoja amalize kuongea na wambeya wa pale saluni kisha nitamfuata. Aliwaza mama Beda.

    Baada ya kusalimiana na kina dada wa saluni akaendelea na safari. Hakutaka kujiuliza akaanza kumfuata nyuma taratibu. Alipofika pale nyumbani kwake akasimama upande wa hatua kama kumi kutoka nyumba ile akajifanya kuhesabu matunda yake. Mtu mmoja aliyekuwa nyumba ya jirani akamwita. “Matundaa.” akaenda kumuuzia. “Haya maparachichi shilingi ngapi?” Aliuliza yule mteja. Akamtajia bei kisha akamuuzia.

    Baada ya hapo akajikuta ujasiri ukimwingia zaidi. Akapiga hatua za haraka kuelekea kule nyumbani kwa mke wa Gervas. Alishaamua kumwambia ukweli wote.

    Liwalo na liwe. Aliwaza kwenye nafsi yake huku akilisogelea geti la nyumba ile. Kijasho chembamba kilikuwa kinamtoka. Alihisi joto kuliko kawaida. Pumzi zake aliona kama hazitoki vizuri. Alikuwa anatetemeka lakini maji alishayavulia nguo. Aliona utakuwa wehu kwenda bafuni na kurudi bila kuoga.

    Huruma imewaponza wengi lakini sina jinsi. Aliendelea kujifariji mwenyewe. Maadamu nimeamua basi nifanye hayo mengine nimwachie Mungu. Aliendelea kuupunguzia hofu moyo wake.

    “Ngo.ngo.ngo.” aliendelea kubisha hodi kwa nguvu ambayo ilisababishwa na hofu. Kama kungekuwa na daktari ambaye angempima mapigo yake ya moyo basi yalikuwa juu sana muda huu. Hofu hiyo ilitokana na dhima iliyokuwa mbele yake. Alikuwa na mambo mawili tu ya kuchagua: Anyamaze amuue mwanamke asiye na hatia tena alishasikia ni mlokole au atoboe ukweli avunje ndoa ya watu.

    Uwezekano wa kuendelea kwa ndoa ya Gervas

    na mkewe kama angetoa siri ile ulikuwa ni asilimia kumi tu. Wapo wanawake wenye mioyo ya ajabu ambao hukubali yote lakini sidhani kama ni hawa wanawake wa kipindi hiki. Hata hao wa kipindi hicho wengi wao ilikuwa ni simulizi ambazo hazina uhakika kama ile simulizi ya wafalme wa nchi fulani ambao ilikuwa ni sheria katika nchi yao mfalme akifa kuzikwa na mkewe akiwa hai.

    Nani yuko tayari kuyatoa sadaka maisha yake kwa ajili ya mtu anayempenda? Watu huhatarisha maisha yao kwa ajili ya fedha na si mapenzi. Hizi ndizo zama tulizo nazo.



     Uwezekano wa kuendelea kwa ndoa ya Gervas

    na mkewe kama angetoa siri ile ulikuwa ni asilimia kumi tu. Wapo wanawake wenye mioyo ya ajabu ambao hukubali yote lakini sidhani kama ni hawa wanawake wa kipindi hiki. Hata hao wa kipindi hicho wengi wao ilikuwa ni simulizi ambazo hazina uhakika kama ile simulizi ya wafalme wa nchi fulani ambao ilikuwa ni sheria katika nchi yao mfalme akifa kuzikwa na mkewe akiwa hai.

    Nani yuko tayari kuyatoa sadaka maisha yake kwa ajili ya mtu anayempenda? Watu huhatarisha maisha yao kwa ajili ya fedha na si mapenzi. Hizi ndizo zama tulizo nazo.



    “Karibu pita.” Sauti kutoka ndani ilimshitua. Ni kana kwamba hakuitarajia hii sauti. Kwake ilitisha kuliko simba. Alisahau kabisa kuwa ni yeye ndie aliyebisha hodi. Upande mwingine akajilaumu kwanini alikuja kutoa taarifa hii. Alikuwa hana chaguo zaidi ya kuingia ndani. Kivumbi kilikuwa hapo. Akakumbuka jinsi mtu anavyopewa taarifa ya msiba wa kipenzi chake. Huanza kwa kufichwa na kuliwazwa. Aanze vipi? Lilikuwa swali gumu kwake. Kilichomtisha zaidi ni jinsi mke wa Gervas atakavyolipokea.

    “Ingiaaa.” sauti iliendelea kusisitiza huku mama Beda akiwa ameganda pale getini. Kwa moyo uliokosa ujasiri akasukuma lile geti na kuingia ndani.

    “Karibu dada, muda mrefu ulikuwa unabisha hodi nakuambia ingia ulikuwa husikii?”

    “Nilisikia. Kuna mtu nilikuwa namuuzia matunda.” Alijitetea.

    “Hapa ndani pako shaghalabaghala nyumba ukimwacha mwanaume lazima ibadilike tu.”

    “Sio wote dada unatuonea.” Msukuma mkokotena alijitetea na kumfanya mke wa Gervas acheke. Mama Beda alijaribu kulazimisha kucheka lakini hakuweza. Asingeweza abadani. Kwani kucheka sehemu kama ile ni sawa na kucheka mbele ya jaji wakati una kesi ya mauaji.

    “Ongea dada nataka kwenda kuoga.” Aliongea mke wa Gervas.

    “Nitaongea kwanza malizana na huyo mtu wa mkokoteni nina maongezi muhimu sana.” Aliongea kwa sauti ya msisitizo ambayo kidogo ilimtisha Mrs Gervas ambaye alikuwa na mtoto mdogo mgongoni.

    “Karibu ukae ndani basi.” mama Beda akapita na kukaa sebuleni. Hali ya sebuleni haikumpendeza mke wa Gervas. Chupa za bia zilitawanywa hovyo, baadhi ya glasi zilikuwa na mabaki ya bia. Aliichukia sana tabia hii ya mumewe. Hakupenda kabisa tabia ya ulevi. Kilichomshinda ni kuwa walifunga ndoa kabla hajaokoka, hata yeye muda huo alikuwa mnywaji. Hivyo alikosa mbinu nzuri ya kumshawishi mumewe aache pombe wakati anakumbuka wazi kuwa walikutana baa.

    “Umesema shilingi elfu moja eeh.” Aliuliza mke wa Gervas

    “Ndiyo shangazi.” Alijibu kijana wa mkokoteni. Akafungua zipu ya mkoba wake uliokuwa kwapani akatoa noti ya shilingi elfu moja akampa.

    Akaanza kupanga vitu kabla ya kwenda kuoga.

    “Ni maongezi marefu?” aliuliza huku akiendelea kupanga vitu pale sebuleni.

    “Sana. Tena nitapenda tuongee baba mchungaji akiwepo.”

    “Mchungaji!” Diana mke wa Gervas akashituka huku akiwa na mshangao wa wazi.

    “Ni muhimu sana tena kwa faida yako.” Aliendelea kuongea huku akihisi kupungukiwa na woga alikokuwa nao hapo awali.

    “Ngoja nimtume mtu aniitie.” Akatoka nje na kumwacha mama Beda akijipongeza kwa mbinu alizotumia. Alisikia kiu kikali lakini alishindwa kunywa maji kwani mwenyeji wake alikuwa nje.

    “Haya dada mi naenda kuoga wakati tunamsubiri huyo mchungaji.” Aliongea Mrs Gervas.

    “Hodi.” Sauti kali yenye mikwaruzo kiasi ilimthibitishia mama Beda kuwa aliyeko nje ni mchungaji.

    “Karibu.” Alilazimika kukaribisha mama Beda kwani mwenyeji wake alikuwa anaoga.

    “Habari mama.” Alisalimia mchungaji.

    “Nzuri baba shikamoo.”

    “Marhaba.”

    “Anakuja nafikiri anabadili nguo maana katoka safari.”

    Mchungaji akaitikia kwa kichwa huku na yeye akijiuliza maswali mbalimbali maana alishazoea waamini kwenda nyumbani kwake. Inapotokea muamini akamuhitaji basi mara nyingi huwa ni tatizo kubwa. Kuna tatizo gani kwa mtu huyu ambaye ndio kwanza anatoka safari? Ni miongoni mwa maswali ambayo yalipita kwenye kichwa cha mchungaji.

    Pangaboi lilikuwa linazunguka lakini mama Beda hakuweza kuhisi kama kuna upepo ulikuwa unamfikia pale alipokaa. Joto kwake lilikuwa kali ingawa mchungaji alitamani ile swichi ya pangaboi inayoruhusu kasi ya mzunguko ingepunguzwa.

    “Karibu baba mchungaji.”

    “Ahsante, Bwana asifiwe.”

    “Ameen.” Wakapeana mikono kwa furaha.

    Bado tu saa yenu ya kukatisha furaha. Aliwaza mama Beda huku ujasiri wa kutimiza azma yake ukianza kujirudia.

    “Hongera sana, umepata mtoto gani?” Aliendele kuuliza mchungaji.

    “Wa kike amepewa jina la Merina na bibi yake.”

    “Ooh Bwana ambariki sana na aibariki ndoa yenu.”

    Hakuna ndoa na yule maluuni. Aliendelea kuwaza mama Beda.

    “Enhe nimesikia unaniita kuna maongezi muhimu.”

    “Ni kweli nimekuita kwani kuna huyo mgeni hapo anasema ana maongezi muhimu lakini kaweka sharti la kuwepo mchungaji.”

    “Enhe mama tunakusikiliza.” Alisikika mchungaji huku akimgeukia mama Beda.

    “Ni kweli nilikuwa nahitaji kuongea na Mrs Gervas lakini nikaona si busara kutokana na uzito wa mazungumzo niongee naye peke yake, ni mazungumzo mazito mazito sana.” Alisisitiza na kutulia kidogo jambo lililowatia hamu zaidi ya kumsikiliza mchungaji na Mrs Gervas.

    “Enhe.” Alisisitiza mchungaji huku akionyesha wazi hamu ya kutaka kusikia hicho kilichosisitizwa kuwa ni kizito.

    “Nafikiri hatufahamiani, mimi naitwa Sakina Msangi au mama Beda, mimi si mwenyeji mtaa huu. Hii ni kama siku ya kumi toka nianze kujenga mazoea ya huu mtaa lengo kuu ikiwa ni kuonana na Mrs Gervas ili niongee jambo hili nililolikusudia.” Akatulia na kusababisha hamasa ya kumsikiliza izidi.

    “Kama nilivyoeleza jambo lenyewe ni zito linahitaji ujasiri kulieleza na kupokelewa kwake vile vile unatakiwa ujasiri.”

    Huyu mtu mbona hasemi maneno mengi tu kama mshairi. Aliwaza mchungaji huku shauku yake ikiongezeka maradufu.

    “Kabla ya yot…………” hakuweza kumaliza alilokusudia kuongea. Mlango ukagongwa kwa nguvu huku sauti ya furaha ikifuatia. Sauti haikuwa ngeni masikioni mwa mama Beda. Ni miongoni mwa sauti zilizomkera sana, alimchukia sana mwenye sauti hiyo. Alimkumbuka vema mtu huyo ambaye ameuingiza utu wake kwenye idhilali kubwa. Alikuwa ni mtu wa mwisho aliyehitaji kumuona hapo. Afanyeje? Lilikuwa swali gumu lililopita kwenye akili yake.

    “Ooh karibu mke wangu.” Alifurahi Gervas huku akimkumbatia mkewe.

    Pale alipokaa mama Beda alikuwa amechanganyikiwa, alijiuliza kama ataambiwa aendelee na ile hadithi itakuwaje?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Eee Mungu ninusuru Sakina mimi. Aliomba moyoni mwake.

    “Twende chumbani mara moja nina maongezi muhimu kidogo.” Aliongea kwa furaha Gervas huku akisahau kuwasalimia wageni. Mchungaji aliwasindikiza kwa macho mtu na mkewe wakati wanaingia chumbani. Akaamua kurudisha macho kwa mama Beda.

    Hakuna mtu. Akapigwa na butwaa. Mama Beda alikuwa ameshaondoka eneo lile. Yaani muda huu huu? Alijiuliza mchungaji huku akishangazwa na kitendo kile cha haraka.



    * * *



    Alirudi nyumbani saa kumi na nusu. Siku hiyo hakumuona kabisa Vick. Kuna mambo walikuwa wanasimulia wanafunzi wenzake. Walisimulia mambo mengi ambayo alikuwa hayajui. Alisimuliwa raha ya kuwa na mpenzi. Siku ile alitamani sana kujaribu kwa Vick yale mambo aliyosikia. Upande mwingine nafsi yake ilisita. Lakini masimulizi yale yalimhamasisha. Aah. Nisije kumuudhi Vick bure nikakaosa msaada. aliwazaBeda. Akaendelea na kazi ndogo ndogo za nyumbani.

    Wakati akiendelea na kazi hizo mara akamuona vick anakuja. Hakuwa Vick aliyemzoea. Vick aliyemzoea alikuwa mtu mchangamfu tena mwenye furaha. Leo Vick kaja mnyonge mwenye huzuni. Kidogo hili lilimtatanisha Beda.

    “Vipi vick mbona unanitisha?” alisikika Beda. Vick hakujibu akaenda pale kwenye gogo la mnazi alipokaa Beda. Akaanza kulia. Wakati analia mama Beda naye akawasili. Akashangaa kumkuta Vick analia.

    “Enhe Beda, umemfanya nini mtoto wa watu.” Aliuliza mama Beda huku akionyesha wazi kutaharuki.

    “Kaja sasa hivi tu mama sijui nini kinamliza.”

    Mama Beda akambembeleza Vick ili aeleze kinachomliza.

    “Kuna mtu katoka hapa mtaani kaenda kumwambia mama kuwa mimi nimejenga mahusiano na familia ya wachawi eti ninyi ni wachawi mama kanigombeza sana.” Mama Beda hakupata tabu kumjua nani kapeleka taarifa hizo. Alijua kuwa lazima atakuwa mke wa mzee Uwesu kwani ndiye mwenye tabia za umbea kama huo.

    “Pole sana mwanangu hiyo ndiyo dunia sisi tumeishi hapa miaka mingi hatuna ugomvi na yeyote lakini umaskini wetu ndio unaotutesa, labda tungekuwa matajiri kama wao.” Mama Beda aliongea kisha naye akaanza kulia.

    “Usilie mama.” Kilio cha Vick kilikwisha akajikuta akimhurumia zaidi mama Beda.

    “Mama mimi nitakuwa nanyi muda wote wa maisha yangu kwani nafahamu fika kwanini unazushiwa hayo yote kama ni wekundu wa macho mara nyingi naona jinsi unavyoshinda jikoni ambako kuna moshi unaotokana na kuni za miti mbalimbali usiwe na wasiwasi hata kama nitafukuzwa nyumbani bado nitakuwa nanyi.” Aliongea Vick kwa hisia kali jambo lililomfanya mama Beda kutokwa na machozi zaidi.



    * * *



    Gervas alipata taarifa kutoka kwa mfanyakazi mwenzake kuwa amemuona mkewe kituo cha daladala cha ubungo. Wakati huohuo alikuwa amepata barua inayomtaka kwenda kwenye semina ya uongozi chuo cha ADEM Bagamoyo. Semina hiyo ilipangwa kufanyika siku inayofuata. Ilikuwa ni semina ya siku saba. Akiwa mwenye furaha kwa vyote viwili akaamua kupitia nyumbani ili amsalimie na kumuaga mkewe kwanza.

    “Nipeleke fasta si unajua tutaondoka jioni hii kwenda Bagamoyo?” Alihimiza Gervas akiwa na dereva wa gari lile la idara ya elimu katika manispaa ya wilaya ya Temeke. Dereva akafanya kama alivyoamrishwa na mkuu wake wa kazi.

    Baada ya kuingia chumbani na mkewe akambusu na kumshikashika mtoto huku akimbusu kwa furaha.

    “Vipi mume wangu mbona hujawasalimia wageni pale sebuleni?”

    “Ah. Samahani mke wangu furaha ilinizidia nikashindwa hata kuwasalimia”

    “Ina maana hata mchungaji hujamfahamu?”

    “Yaishe mke wangu nimeshindwa kumfahamu yeyote pale.”

    “Eh. Nataka uniambie mbona unaonekana mwenye haraka?” Aliuliza mke wa Gervas.

    “Nimepata safari ya kikazi mke wangu, naenda kwenye semina ya wiki moja bagamoyo.”

    “Haya nakutakia safari njema.”

    Wakatoka mle chumbani. Alipofika sebuleni hakumuona mgeni mwingine wakapeana mikono na baba mchungaji. Baada ya kusalimiana hakuuliza kuhusu mgeni mwingine badala yake akaaga na kuondoka.

    Mchungaji alikuwa ametulia pale kwenye kiti.

    “Mgeni yuko wapi?” Aliuliza Mrs Gervas.

    “Ametoweka.”

    “Ametoweka?”

    “Ndiyo ni dakika chache za kufumba na kufumbua sikumuona tena.”

    “Mh. Makubwa tujaribu kumsubiri labda hajaenda mbali”

    Wakamsubiri mgeni hakutokea. Wakakata tamaa kisha wakaagana.



    Zilikuwa zimepita siku tatu toka mgeni yule atoweke. Mchungaji na Mrs Gervas walishaanza kumsahau. Walijua ni mwehu au mtu aliyekuwa na jambo fulani ambalo lilihusu pesa akashindwa kuongea. Hawakulitilia maanani tena.

    Siku hiyo mchungaji alikuwa kwenye mafundisho ya kawaida ndani ya kanisa ndipo akatokea mtoto mdogo ambaye alienda mbele moja kwa moja akampa karatasi ambayo ilikuwa na ujumbe fulani. Akaufungua na kuusoma.

    Samahani mchungaji, niliondoka bila kukuaga ile siku tuliyokutana nyumbani kwa Gervas kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika. Naomba tukutane tena mahali palepale. Ulisomeka ujumbe huo na kumfanya mchungaji akatishe somo. Akakumbuka jinsi alivyovutiwa na mazungumzo ya yule dada siku waliyokutana. Kutokana na shauku aliyokuwa nayo hakutaka kupoteza muda akaingia kwenye gari lake Prado nyeusi akaondoka kuelekea kwa Mrs Gervas. Ulikuwa ni mwendo wa dakika tano kwa gari kutoka kanisani hadi nyumbani kwa Mrs Gervas.

    Alipofika akashangaa kumkuta yule dada akiwa amesimama mlangoni. Akasimamisha gari wakasalimiana.

    “Leo usitutoroke mama.” Alitania mchungaji huku akicheka. Mama Beda hakucheka alikuwa ‘siriasi’. Mchungaji akapiga honi mara tatu. Mrs Gervas akaja kufungua geti. Akashituka baada ya kumuona tena mama Beda akiwa pale getini. “Yesu wangu.” Alishituka Mrs Gervas. Bado utashituka sana. Aliwaza mama Beda huku akijikohoza kuliandaa koo lake kwenda kulipua bomu zito.

    Katika sebule ileile, tofauti ilikuwa ni mpangilio na usafi wa ndani tu. Mama Beda alikaa akiwa mwenye fikra nyingi hasa akihofia kutokea tena mumewe yule dada mlokole.

    “Haya nadhani tumekutana sasa.” Alianza mchungaji mara tu baada ya kuhakikisha kuwa wote wamesalimiana.

    “Siri ya mkutano wetu unayo wewe bi Sakina au mama Beda kama ulivyojitambulisha mwanzo lakini kabla ya yote tunaomba maelezo kwanini ulitutoroka.”

    “Jambo nililotaka kuzungumza ndilo lililonifanya nitoroke sikutaka Gervas awe hapa wakati tunazungumza ni jambo zito ajabu.” akatulia kidogo na kuwaangalia washiriki wenzake wa mkutano ule ambao haukuwa na ajenda zilizo wazi kwa wajumbe. “kabla ya kuendelea naomba nipate uhakika kama Gervas yuko mbali na eneo hili.”

    “Hilo usihofu kwani siku ileile Gervas alisafiri kwenda Bagamoyo ambako wana semina ya siku saba.”

    “Ina maana hukuwahi kupata faragha na mumeo?” Swali hili kidogo lilimkera Mrs Gervas.

    “Faragha ipi unakusudia?” Aliuliza huku akionyesha hasira kidogo.

    “binti mbona unauliza maswali mazito?”

    “Naomba nijibiwe kila ninachouliza na nafikiri mutakubaliana na mimi kuanza na maswali ambayo pengine munayaona ya kijinga nakusudia faragha ya tendo la ndoa.”

    “Hatujawahi kuipata hiyo faragha nafikiri mpaka arudi.” Hakuwa na jinsi alilazimika kujibu.

    “Sawa, sasa naona nieleze mkasa wote uliosababisha tuwe hapa, awali ya yote naomba uvumilivu mkubwa toka kwa Mrs Gervas.”

    Akaanza kusimulia matatizo yake ya kimaisha akianzia na la kufiwa na mumewe mpaka kuhangaika juu ya ada ya mwanawe. Mrs Gervas alikuwa analia kutokana na maelezo ya mama Beda wakati mchungajia alilazimika kufuta machozi kutokana na simulizi ile ya kusikitisha. Alitulia kidogo na kuvuta pumzi kwani alikuwa anaelekea kwenye kiini au ajenda kuu. Kisha akaanza kueleza alivyohangaika kutafuta shule mpaka akakutana na Gervas. Akatulia kidogo kwani mapigo ya moyo yalishaanza kubadilika na kwenda kasi.



    Kisha akaanza kusimulia jinsi alivyolazimishwa kufanya mapenzi na Gervas. Mchungaji akamkazia macho Mrs Gervas ambaye alitulia lakini akionekana wazi kuhema kwa hasira. Alitaka kuangua kilio lakini mchumgaji akawahi kumtuliza.

    “kwa hiyo dada umetoka huko kuja kunitia uchungu kwa kunisimulia uchafu wa mume wangu?” Aliuliza Mrs Gervas kwa hasira akitamani kumrukia mama Beda kwani alishasimama. “Umemsumbua mchungaji kuja kusikia huo upuuzi ili nidhalilike?”

    “Tulia dada utanifanya chochote baada ya kumaliza maneno yangu na sasa ninaelekea ukingoni kwani nataka kueleza kile ambacho sikupenda kukueleza ukiwa peke yako.” Akatulia na kumkazia macho mwanamke yule ambaye alijirudisha tena pale alipoketi na kuendelea kumsikiliza mgeni yule.

    “Mchungaji na Mrs Gervas, naomba niweke wazi kuwa mimi ni muathirika wa virusi vya ukimwi na mumeo alinilazimisha kukutana kimwili bila kinga haikuwa hiyari yangu kama nilivyoeleza kuwa ni kama alinibaka.” Hakuwa na haja ya kumaliza maneno ya mwisho, neno lile lile kuwa yeye ni muathirika liikuwa kama mkuki wa sumu uliopita kwenye moyo wa Mrs Gervas. Alimkazia macho mama Beda. Alikuwa mwenye bumbuwazi ya aina yake. Hakujua kama alitakiwa kuhuzunika au kufurahi.

    Mchungaji naye pale alipokaa alikuwa amepigwa na butwaa. Kwa dakika kadhaa hakuna aliyeongea, hakuna aliyecheka na hata kulia pia. Hapo mchungajia akaelewa kwanini yule mgeni aliuliza kama Mrs Gervas na mumewe walishakutana faragha. Moyoni alimsifu mwanamke yule kwa ujasiri wa aina yake pia alipanga kulifanya tukio lile kuwa moja ya masomo yake.

    Akamgeukia mgeni na kumuuliza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sina nia mbaya mama isipokuwa nataka kujua lengo la kufanya yote haya ninini?”

    “Nasikia huruma kwenye nafsi yangu sikutaka mwanamke mwenzangu aingie kwenye matatizo kama yangu. Nilihisi wazi nafsi ikinisuta ndio maana nikaamua kufanya uchunguzi ili niweze kujua aliko mke wa Gervas kwa bahati nikaelezwa na mwenyewe Gervas kuwa mkewe amesafiri hivyo nikaamua kufanya biashara maeneo haya ili kuvizia isipatikane faragha ya ndoa kabla ya kupata vipimo kutoka hospitali.” Mchungaji akatikisa kichwa baada ya kusikia maelezo ya mama Beda. Ingawa alikuwa kwenye taharuki bado Mrs Gervas aliendelea kuwa mtulivu na kumsikiliza mama Beda.

    “Mama tunashukuru kwa maelezo yako; kimsingi umefanya jambo la busara sana kulifikisha katika namna nzuri kama hiyo. Pia napenda nikupe pole kwa yote yaliyokukuta tena si vibaya nikikupongeza kwa uamuzi wa kijasiri wa kukubali kuja kuyapigania maisha ya mwenzako ingawa hapo mwanzo tulianza kuchukizwa na maelezo yako tukidhani kuwa wewe ni mshari lakini sasa tunakubali kuwa Mungu ndiye aliyekuongoza kufanya yote haya.”

    Kabla hajaendelea kuongea Mrs Gevas akataka kuanguka lakini mchungaji akawahi kumdaka. Akamlaza vizuri pale kwenye kiti. Alikuwa amepoteza fahamu. Mchungaji akaanza kumpepea. Kama siku ya kwanza Mama Beda akatumia mwanya huo kuondoka mle ndani.

    Alikuwa amemaliza kazi, hakuwa na sababu ya kuendelea kubaki pale. Akiwa na beseni lake la matunda alitembea haraka kulekea kituo cha daladala.



    * * *

    Jumamosi hii ilimkuta Beda akikusanya kokoto kwa ajili ya kwenda kuuza. Kazi hii ilikuwa ngumu lakini hakuwa na namna kwani kuna mahitaji mengine madogo madogo aliona hakuna ulazima wa kumwambia mama yake. Alikuwa na huzuni kidogo kwani ni juma la pili alikuwa hajamuona rafiki yake Vick. Hakujua nini kimemsibu. Yeye ndiye aliyekuwa anampa fedha za matumizi. Kukosekana kwake kwa hizo wiki mbili kulimfanya atafute vibarua ambavyo vingemsaidia mahitaji madogomadogo. Ndani ya wiki mbili alikuwa amepasua mawe, amekusanya mchanga na vibarua vingine ambavyo havikuendana na umri wake.

    Akiwa amebeba kiroba cha kokoto akakutana na Happy mwanafunzi wanayesoma naye darasa moja.

    “Vipi Beda mambo.”

    “Poa Happy unaenda wapi?”

    “Nawahi twisheni vipi mbona wiki ya pili hii hujaonekana twisheni?”

    “Mambo ya fedha ndugu yangu, hapa naenda kuuza hizi kokoto nipate chochote.” Alijibu.

    “Haya wacha niwahi.” Alisema Happy huku akiongeza mwendo.

    “Ah. Samahani nilitaka kusahau.” Alirudi nyuma Happy.

    “Unajua Ijumaa umeondoka mapema sana kuna mtu alikuja kukutafuta pale shuleni.”

    “Yukoje?”

    “Mbaba mmoja hivi mrefu wa wastani nasikia ni afisa elimu.”

    “Afisa elimu alikuwa ananitafuta mimi?”

    “Ndiyo tena kauliza hadi nyumbani kwako lakini wote tuliobaki hakuna aliyepafahamu.”

    “Afisa Elimu?”

    “Eeeh. Mbona unashangaa sana tena nimekumbuka alijitambulisha kwa jina la Gervas Msangi.”

    “Hakueleza shida yake?”

    “Hakuna aliyemuuliza kwani alionekana mtu mwenye hasira huku macho yake yakiwa yameiva kwa wekundu, nfikiri hata angekuwepo mtu anayekufahamu asingethubutu kumuelekeza huko kwako kutokana na hasira alizoonyesha.’

    Beda akashituka baada ya maelezo hayo. Mtu mwenye hasira ananitafuta nimekosa nini? Alijiuliza Beda huku akianza kutawaliwa na hofu.

    Hapy alikuwa ameshaondoka wakati Beda akiwa ameishiwa nguvu za kubeba kile kiroba kutokana na taarifa ile iliyomtatanisha. Likamjia wazo la haraka, mapigo ya moyo yakaongeza kasi yake. Alijua jinsi mama yake anavyoandamwa na mikosi.

    Akarudi haraka nyumbani huku akikiacha kile kiroba pale kilipo. Alipofika nyumbani akashituka sana baada ya kukuta chanjo za gari pale nyumbani kwao. Hofu ikazidi kuutawala moyo wake. Alijua wazi kuwa mama yake yuko hatarini, kwa kosa lipi? Alijiuliza.

    Akakaa pale kwenye gogo akitafakari. Alikaa pale kama masaa mawili ndipo akamuona mama yake akirejea na beseni tupu.

    “Vipi mwanangu mbona unaonekana huna raha?” Aliuliza.

    “Mama nahisi kuna matatizo yanatuandama tena.”

    “Kwanini?”

    “Nasikia kuna mtu mwenye hasira ambaye alikuja kwa shari pale shuleni alikuwa ananitafuta, wanasema ni afisa elimu alijitambulisha kwa jina la Gervas Msangi.”

    Akatulia na kumshangaa mama yake ambaye aliyeonyesha kushitushwa na taarifa hiyo kuliko alivyotarajia. Mama Beda alikaa chini akionyesha kukosa nguvu kwa hofu.

    “naomba unieleze ukweli mama umefanya nini?”

    Mama Beda akainuka bila kusema lolote akamshika mkono mwanawe kisha akaanza kumsimulia kila kitu kuhusu Gervas mpaka siku aliyoenda nyumbani kwake. Simulizi ile ilimfedhehesha sana Beda. Alijisikia kudhalilika kwa mambo aliyofanyiwa mama yake. Upande mwingine alijihisi uchungu mkubwa baada ya kugundua kuwa mama yake ni muathirika. Alishindwa kujua kama ampongeze au amlaumu mama yake kwa hatua alizochukua.

    “Mama nakushauri uishi maisha ya kujificha mpaka mambo yatakapopoa vinginevyo anaweza kukuua huyu.”

    “Mwanangu nimechoka haya maisha bora nife siwezi kuendelea kuishi maisha ya mateso namna hii.” Alisikika mama Beda huku akilia.



     Semina ilikuwa imeisha. Gervas alirejea nyumbani akiwa mwenye furaha kubwa. Alijua kuwa sasa atapata muda wa kucheza na mtoto wake. Pia alikuwa amemkosa mkewe kwa siku nyingi toka alipoondoka akiwa mja mzito baada ya kujifungua akaongeza miezi sita hukohuko. Gari lilisimama mbele ya nyumba yake akaagana na dereva na wanasemina wenzake ambao nao walikuwa na hamu ya kufika majumbani kwao.

    Akashangaa kuona akilakiwa na ukimya. Akafungua mlango na kuingia ndani. Mkewe alikuwa amekaa kwenye kiti bila kuonyesha hisia zozote za kuwa aliyeingia ni nani kwake.”

    “Vipi mke wangu mbona hivyo?” Mkewe hakujibu akamkazia macho kama anaeyemuona mtu mgeni. Gervas akashitushwa na hali ile. Akamsogelea mkewe ili amshike.

    “Usinishike.” Alifoka mkewe. “Eh. Una nini mke wangu?” Aliuliza Gervas kwa mshangao.

    “Sikiliza wewe baradhuli kuanzia leo, mimi sio mkeo mpaka pale utakapopima na kuthibitishwa kuwa ni mzima na huna maambukizi ya virusi vya ukimwi.” Kauli hiyo ikamshitua na kumshangaza Gervas.

    “Umechanganyikiwa mke wangu?”

    “Nani amechanganyikiwa mimi au wewe ambaye husaidii watu mpaka uwadhalilishe.’

    Hakugundua mapema nini maana ya kauli ile. Akashika kichwa kisha akakaa.

    “Mke wangu naomba unieleweshe vizuri maana naona unazidi kunichanganya.”

    “Kama kuchanganyikiwa basi mimi ni zaidi yako kwani tunakoelekea ni kama kusema ndoa yetu imefika mwisho.”

    “Kwanini mke wangu mbona unaongea mambo mazito?”

    “hukumbuki wewe kama kuna mwanamke alikuja kukuomba msaada kwa ajili ya mwanae aliyefaulu ukaena nae gesti?” Gervas akatahayari baada ya kusikia kauli ile.

    “Mke wangu kwa nini unapenda kusikiliza umbeya?”

    “Sawa ni umbeya lakini siko tayari kuendelea na wewe mpaka pale utakapopima.”

    “Kwanini umeweka sharti la kupima.”

    “Kwa sababu yule dada ni muathirika anaishi na virusi vya ukimwi.”

    Ikawa zamu ya Gervas kuchanganyikiwa. Akainuka pale alipokaa. Akaanza kutembea tembea mle ndani bila uelekeo. Kweli Gervas alikuwa amechanganyikiwa kwani aliliona kaburi likiwa mbele yake.

    “Suala la msingi ni kwenda kupima huko kuzunguka zunguka hakutasaidia kitu.” Aliendelea kuongea Mrs Gervas. Akaingia chumbani kwake akajitupa kitandani. Akaanza kulia. Hakuwepo wa kumbembeleza kwani kutokana na kilio kile mkewe alithibitisha kuwa ni kweli mumewe kafanya kitendo hicho ambacho kinahatarisha ndoa yao.

    “Muda umeenda mke wangu nitaenda kesho kupima.” Sauti ya mumewe ilisikika kutoka chumbani huku akilia.

    Alijaribu kulala lakini usingizi haukuja. Akabaki kukodoa macho huku akiwa na huzuni kubwa kabisa. Hasira ilimjia kuhusu mama Beda. Alisahau kabisa jinsi mama Beda alivyombembeleza kuhusu kutumia kinga bila kukubali. Alijiuliza kwanini hakuelezwa ukweli juu ya afya ya yule mama ingawa kimsingi alijijua wazi kuwa asingeweza kutoa msaada wowote bila malipo. Majuto ni mjukuu na wakati wa kujuta ulikuwa umefika. Upande mwingine alijilaumu kwanini alishindwa kukubaliana na yule mama? Akaanza kulia tena huku akikumbuka safari ya kwenda kupima siku inayofuata.

    Wakati yuko kwenye lindi la mawazo hakujua kama mkewe alikuwa anapiga hatua kuiacha nyumba ile akiwa na mtoto wake mchanga mgongoni. Begi alishaliaandaa hivyo mumewe alipoingia chumbai akaondoka na begi lake kuelekea nyumbani kwa baba mchungaji. Hakutaka kulala pale mpaka apate majibu ya mumewe.

    Ingawa mumewe alikuwa kwenye wakati mgumu hakukubali kubaki na kumliwaza kwani alijitia kitanzi mwenyewe kwa kuisaliti ndoa yao. Kama alitaka suluhu kwanza apime pili amfuate kwa baba Mchungaji.



    * * *

    “Gervas Msangi.” Daktari wa hospitali ya wilaya ya Temeke aliita. Akanyanyuka na kufuatiwa na mkewe. Wote wakaingia kwenye chumba kile.

    “Vipi mbona mmeingia wote wawili.” Alihoji daktari

    “Huyu ni mume wangu.” Alijitetea mkewe.

    “Bwana Gervas uko tayari kupokea matokeo mbele ya mkeo?”

    “Niko tayari alijibu.” huku akianza kubanwa pumzi kutokana na hofuCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Vipimo vinaonyesha kuwa una maambukizi ya virusi vya ukimwi hivyo….” Kuli ya dokta haikufika mwisho Mrs Gervas aliinuka kwenye kiti na kutoka nje haraka.

    “Binti subiri….” Aliita dokta baada ya kumuona akitoka mle ndani.

    “Mke wangu nisubiri.” Alilalamika Gervas wakati mkewe anakatisha kwenye kundi la watu mbio. Msongamno wa watu pale hospitali ulimfanya Gervas ashindwe kujua mkewe alikuwa amekimbilia wapi. Akamtafuta pale hospitali hakumuona. Baada ya kutafakari kwa muda akaamua kuchukua teksi hadi nyumbani kwa baba Mchungaji.

    “Ongeza mwendo dereva.” Alihimiza Gervas huku akionekana wazi kuchanganyikiwa.

    Gari ilikuwa kwenye kasi kikubwa kitendo kilichowashawishi trafiki wa tazara kuwasimamisha na kuanza kuwahoji. Kitendo hicho kilikuwa karaha kubwa kwa Gervas ambaye alikuwa anajaribu kuokoa ndoa yake. Moyoni alimchukia sana mama Beda. Alimuona kuwa shetani mkubwa katika maisha yake akiusahau ushetani alioufanya yeye.

    “Naomba uturuhusu afande mke wangu anataka kujifungua inabidi nimuwahi tumpeleke hospitali.’ Alibembeleza Gervas. Kwa jinsi alivyochanganyikiwa yule askari akamruhusu huku akiwahimiza kuwa waangalifu.



    Gari ikaongeza tena kasi yake hadi maeneo ya kimara Baruti.

    “Kata kushoto kisha nyoosha mpaka utakapoona kanisa la mabati.” Alielekeza Gervas huku akitamani kushika usukani. Gari ikafunga breki mbele ya kanisa lile. Gervas akashangaa kuwakuta waamini wa kanisa lile wakiwa nje makundimakundi. Hakutaka kuuliza akatembea hadi pale aliposimama baba mchungaji.

    “Samahani mchungaji mke wangu amefika hapa?”

    “Mke wako alikuwa hapa kama dakika kumi zilizopita amechukua begi lake ameelekea huko nyumbani kwako.”

    “Akarudi tena kwenye teksi.”

    “Anko utanilipa kweli?” Aliuliza dereva teksi.

    “Kijana endesha gari tunachelewa.” Alifoka Gervas huku akitoa noti kwa hasira. Dereva hakusema kitu zaidi ya kupokea zile noti bila kuhesabu kwani kwa macho tu zilikuwa nyingi kuliko malipo yoyote ambayo angehitaji siku hiyo.

    “Wapi?”

    “Nyumba ile yenye geti jeusi.” Alielekeza Gervas.

    Waliposimama gervas akakimbia kuelekea ndani. Hakukuta mtu zaidi ya kuona wazi upungufu wa baadhi ya vitu mle ndani. Alijua nini kimefanywa na mkewe. Akaanza kulia kwani alijua wazi kuwa hawezi tena kumpata mkewe. Akatoka nje huku machozi yakimtoka. “Twende Ubungo bus terminal.” Alihimiza Gervas huku akiingia kwenye teksi.

    Teksi iliondoka kwa kasi hadi ubungo. Wakati wanataka kuingia wakakutana na basi lililokuwa linatoka. Siti ya nyuma kabisa Mrs Gervas alikutanisha macho na mumewe aliyekuwa kwenye teksi. Akampungia mkono. Pingu ya maisha ilikuwa imefunguka. Hakuna shaka huo ulikuwa ni mwisho wa maisha matamu ya ndoa ambayo tamaa ya Gervas ilimfanya ayatie sumu na kuyaharibu mwenyewe. Alitikisa kichwa huku akitazamana na mkewe ambaye naye alikuwa anatokwa na machozi. Ulikuwa mwisho mchungu kama shubiri. Akachungulia tena dirishani huku akilitazama kwa uchungu jinsi basi lile lilivyokuwa linauacha mji wa Dar es salaam. Kwa jinsi alivyochanganyikiwa dereva hakutaka kuuliza akaamua kumpeleka nyumbani kwake.



    * * *

    Miezi ikakatika mwaka ukaisha yule afisa elimu hakuonekana tena. Hofu ya mama Beda ikaisha. Tayari Beda alikuwa kidato cha pili. Hakukuwa na mabadiliko katika maisha yao. Vick alikuwa anakuja mara moja moja na kumpa msaada Beda. Hakuwa na nafasi nzuri ya kupata fedha kama alipokuwa kidato cha kwanza. Upotevu wa fedha wa mara kwa mara ulimfanya baba yake ashindwe kujua ni nani anahusika hivyo akaamua kubadilisha namna ya utunzaji wa fedha. Beda alilazimika kuingia mtaani siku za jumamosi na Jumapili na kufanya vibarua mbalimbali.

    Jumamosi moja Beda alikuwa amejipumzisha nyumbani. Siku hiyo hakwenda kwenye vibarua vyake. Akiwa kwenye lile gogo la mnazi alilozoea kukaa akamwona Vick akimjia. “Karibu dear.” Alikaribisha Beda kwa utani.

    “Ahsante, mama nimemkuta?”

    “Ameshaondoka kwenda kwenye biashara zake.”

    “Leo baba na mama wamesafiri tena, nataka kutoroka kama siku ile nije kulala kwako.”

    “Poa tu unakaribishwa sana.”

    “Leo sichelewi inabidi niwahi kuwawekea maji kuku.”

    “Kumbe munafuga kuku?”

    “Ndio tuna kuku wa kisasa kama mia nne.”

    Wakaagana na Vick.

    Muda mfupi baada ya kuondoka Vick mama Beda akawasili.

    “Shikamoo mama.”

    “Marahaba mwanangu habari za shule.”

    “Mama leo jumamosi mara hii umesahau.’

    “ah. Mwanangu mi naishi tu sijui hata siku” Kauli hiyo ikamchekesha Beda.



    * * *

    “Beda, Beda……..” Sauti iliita kutoka Dirishani. Sauti hiyo haikuwa ngeni katika masikio ya Beda. Asingeweza kuishangaa sauti ya vick hata kidogo. Akatembea kwa kunyata ili mama yake asisikie. Akafungua mlango. Vick akiwa na kandambili zake mkononi akazama ndani. Mlango ukafungwa wakaingia chumbani kwa Beda. Kibatari kikazimwa.

    Saa kumi kamili wote walishitushwa na adhana.

    “kumekucha Vick twende nikusindikize.” Wakaondoka. Ulikuwa ni mwendo wa dakika ishirini. Walipofika Beda akamwacha Vick pale getini. Akamuona Vick akivuta geti ambalo alilitegesha ili atakaporudi apate urahisi wa kuingia. Akageuka na kurudi nymbani akiwa na furaha ya kufungua ukurasa mpya na Vick. Ilikuwa ni siku yao ya kwanza.

    Baada ya miezi minne Vick alianza kusumbuliwa na kichwa mara kwa mara. Si hivyo tu mara nyingi alisinzia darasani na kulalamika kizunguzungu. Hali hiyo ilimtia wasiwasi mwalimu wa darasa ambaye aliamua kufuatilia afya ya mwanafunzi wake. Akamchukua hadi zahanati ya shule.

    “Vick, nimekuleta huku ili nipate uthibitisho wa afya yako.” Aliongea mwalimu wake wa darasa.

    “Muda wa vipimo ukafika.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog