Simulizi : Bomu La Karafuu
Sehemu Ya Pili (2)
Pei aliondoka haraka akatoka nje ambako ile taksii ilikuwa ikimngojea. Aliingia na kumwambia dereva waondoke haraka. Dereva aliondoa gari kwa kasi kuelekea mjini, walipofika karibu na ukumbi wa burudani wa hoteli ambako kulikuwa na kivuli kinene cha miti ya maua, ikawa:
“Punguza mwendo, nitatoka, wewe endelea na safari yako,” Pei akampa pesa yule dereva taksi, akafungua mlango, akatoka na dereva akaondoka.
Wakati wanaondoka pale hotelini, tayari wale vijana nao walikuwa wameshashuka na walipoambiwa kuwa Pei alishaondoka punde tu, wakakimbilia kwenye gari lao wakawafuata kwa kasi. Hata hivyo, hawakumuona Pei alipotoka kutoka kwenye ile gari, wakaendelea kuifuata ile teksi ambayo taa zake za nyuma zilikuwa zikionekana kwa mbali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Huku nyuma Pei alipoiona ile gari inapita kwa kasi kuifuatia teksi aliyokuwa ameiacha punde, akatabasamu kwa kujuwa kuwa wamemkosa. Hata hivyo, alipatwa na wasiwasi juu ya hatima ya yule dereva wa teksi.
“Sijui watamfanyaje watu hawa watakapogundua kuwa simo kwenye ile teksi wanayoifukuzia!“ aliwaza.
Wale vijana waliifukuzia ile teksi kwa mwendo wa kasi sana, na walipofika karibu na makutano ya barabara za Darajani na Mtendeni wakaipita na kuizuia kwa mbele, ikabidi yule dereva wa teksi asimame.
Wale vijana walishuka kutoka kwenye gari lao na kumwendea dereva taksi ambaye naye alikuwa ametoka kwenye gari. Kwa namna wale vijana walivyomjia, yule dereva taksi ambaye alikuwa ni mtu wa makamo alijua walikusudia shari, kwa hiyo naye akajiandaa kujinusuru kwa namna yoyote ile.
Walipomfikia pale alipokuwa walifungua milango ya gari na kuchungulia ndani, na walipoona hakukuwa na mtu wakaibamiza na kumkabili yule dereva.
“Tuambie haraka na ukweli. Abiria uliyeondoka naye pale hotelini umemwacha wapi?“
“Abiria niliyemleta hotelini nimemwacha palepale, sikuondoka naye,“ yule dereva taksi alijibu.
“Unatuongopea siyo? Usitupotezee muda, na usitukasirishe tukakuumiza bure. Tuambie ukweli, umemshusha wapi?”
“Mbona hamnielewi vijana. Abiria niliyemleta pale sikuondoka naye, nilimwacha palepale hotelini.”
Wale vijana wakatazamana, kisha Burshid akasema, “OK, unamfahamu kwa jina au kwa namna yoyote huyo abiria uliyemwacha pale hoteleni?”
“Hapana, simfahamu. Yeye alikodi gari akaniambia nimpeleke hoteli ya Ufukoni, nami ndicho nilichofanya,” yule dereva taksi alisema.
“Alikukodi kutokea wapi?” Burshid aliuliza.
“Sioni sababu ya kujibu swali hilo,” dereva taksi alijibu.
“Ahaa, kwa hiyo wewe na yeye lenu ni moja siyo? Mlitufuatilia nyuma wakati tunakuja, si ndiyo?” Burshid alisema huku akimsogelea yule dereva wa teksi.
Dereva teksi naye pamoja na utu uzima wake hakutikisika, aliamua kumkabili.
“Suala la kuwafuata nyuma mimi silijui. Yeye kwangu alikuwa abiria kama abiria mwingine yoyote.”
“Sasa mbona ulimsubiri hadi alipotoka ukaondoka naye?”
“Vijana, mbona hamnielewi? Kama nimeondoka naye mbona hayupo ndani ya gari yangu?”
“Yeye kutokuwa ndani ya gari haimaanishi kuwa hukuondoka naye. Umemshusha wapi?”
“Sikuondoka naye kwa hiyo suala la kumshusha...”
Hata kabla hajamaliza alichotaka kusema dereva teksi alishtukia amechukua konde lililompata usoni na kumbwaga chini. Lilifuatia teke la mbavuni ambalo lilimfanya atoe ukelele mkali na hiyo ndiyo ikawa salama yake. Jirani na purukushani hiyo ilipokuwa ikiendelea kulikuwa na ofisi za Umoja wa Vijana na kulikuwa na walinzi.
Ule ukemi aliotoa dereva teksi uliwashtua walinzi na wakatoka mbio kuangalia kuna nini. Wale vijana walipoona walinzi wanakimbilia pale walipokuwa, wakatoka mbio kuelekea kwenye gari lao na wakaondoka wakimwacha dereva teksi akigaragara kwa maumivu.
Wale walinzi walifika alipokuwa amelala dereva teksi akiugulia kwa kile kipigo alichopata. Walimuinua naye akajikaza akasimama huku bado akigugumia maana mateke aliyopigwa mbavuni yalimuumiza.
“Vipi ndugu, mbona wamekupiga wale?” walinzi walimuuliza teksi dereva.
“Aaah, hii dunia imeharibika. Hata sijui walikuwa wanataka nini? Niliona tu ghafla wamenizuia mbele, wakashuka wakaanza kunifokea na kisha kunipiga. Msingejitokeza wangeniua wale!”
“Na wala huwafahamu?” mmoja wa wale walinzi aliuliza.
“Hata, siwafahamu,” dereva teksi alijibu.
“Sawa, kama unatuficha lolote ni juu yako. Utaweza kuendesha gari?”
“Nitaweza. Nitakwenda kituo cha polisi pale mlimani nikatoe taarifa ya tukio hili.”
“Bora ufanye hivyo. Kama watahitaji uthibitisho wa kilichotokea tupo tayari kuja kutoa ushahidi wa kile tulichokiona,” wale walinzi walisema huku wakimsaidia yule dereva kuinuka na akaingia ndani ya gari lake.
7 - Mtego
Wakati dereva taksi akipata kichapo kutoka kwa wale vijana, Pei alikuwa amerudi tena kule Hoteli ya Ufukoni, na safari hii hakupita mlango uliopitia deski la mapokezi, bali alipitia mlango wa nyuma ambao hutumiwa sana na wapangaji wa hotelini hapo wanapotaka kwenda sehemu ya chakula au vinywaji, ambayo ilikuwa kwenye jengo tofauti. Kwa kupitia mlango huo, Pei hakuonwa na wale vijana waliokuwa pale kwenye meza ya mapokezi.
Alipanda hadi ghorofa ya pili ambako alikwenda moja kwa moja hadi chumba namba 406 Aligundua kuwa chumba hicho kilikuwa na milango miwili ambayo ilikuwa na alama za namba 406A na 406B, akafahamu kuwa kilikuwa ni chumba ambacho kilikuwa na sehemu ya kulala na sehemu ya maongezi, yaani “suite” kwa lugha ya Kiingereza.
Pei aliangalia upande wa kulia na kushoto wa korida ndefu ya ghorofa hiyo ya pili akaona kuwa hakukuwa na yeyote zaidi yake. Aliusogelea mlango uliokuwa na namba 406A, akabandika sikio lake kwenye tundu ya funguo, hakusikia mlio wowote ukitokea kule ndani. Akahamia kwenye mlango uliokuwa na namba 406B, akafanya vilevile, na huko akasikia sauti ya mchakacho, kama vile mtu anapangapanga vitu kabatini. Kwa uzoefu wake akafahamu kuwa kile ndio kilikuwa chumba cha kulala, akahisi kuwa labda huyo mgeni aliyekuwa katembelewa na wale vijana alikuwa ndio anataka kulala.
Wakati Pei anafikiria nini la kufanya, simu yake ikaita, na kwa bahati ilikuwa ipo kwenye mlio mdogo sana tena katika hali ya mtetemeko, kwa hiyo isingemshtua yoyote asiyestahili. Kabla hajaipokea simu hiyo alitembea haraka haraka hadi kwenye ngazi za kutokea nje, ambako alikitofya kitufe cha kupokelea na maongezi yakawa:
“Uko wapi Pei, mbona kimya?”
“Aaah, BeBe, bado nipo hoteli ya Ufukoni. Nimeweza kuwapiga chenga wale vijana, na nikarudi kukagua chumba alichofikia mshikaji wao ambaye ametoka Comoro. Yaelekea anajiandaa kulala. Mawazo yangu ilikuwa niingie kisha nimbane anieleze wana dili gani, lakini naona ni mapema mno, au unasemaje?”
“Uko sahihi, ni mapema mno. Bali jambo moja tu la kufanya, hakuna ubaya wa kupekuwa chumba chake na kujua yeye ni nani, na mengineyo. Tukiweza pia tutaweka vifaa vyetu vya kunasa maongezi yoyote yatakayofanyika kama hao vijana au yeyote mwingine atawatembelea kesho, sawa?”
“Sawa, ni wazo zuri, nikusubiri?”
“Ndiyo, nipe robo saa tu, kwaheri.”
Bebe alikuwa anaongea akiwa nyumbani kwa rafiki yake Zamoradi. Baada ya kutelekezwa na wale vijana kule Marhubi, walikodi taksi na kurudi nyumbani kwao Michenzani. Ulikuwa usiku mnene, yapata saa saba na nusu. Wakati Bebe akiongea na Pei, Zamoradi alikuwa bafuni, na alishangaa alipotoka na kumkuta rafiki yake akiwa amevaa suruali ya jinzi nyeusi na fulana ya mikono mirefu nayo pia jeusi, kichwani kafunga kitambaa cheusi na miguuni kavaa raba nyeusi.
“Hee, haya ni vipi tena? Ndio kumekucha eenh?” Zamoradi alimuuliza Bebe.
“Ndiyo Zamo, kazi imeanza. Usiulize maswali mengi kwa sababu hupaswi kujua mengi, bali niombee salama tu,” alimjibu shogake.
“Nimekoma kushangaa muda mrefu. Lakini hii kazi yako, mnh, mimi kamwe siitaki. Haya, uwe mwangalifu, na ujue kuwa sintolala mpaka utakaporudi.”
“Inshallah, nitarudi. Lala, wala sitakugongea, ufunguo ninao, kwaheri.”
Bebe alitoka akashuka ngazi hadi chini. Barabara ya Michenzani ilikuwa kubwa na kwa usiku ule magari yaliyokuwa yakitokea kwenye majumba ya starehe yalikuwa mengi. Haikuchukua muda akapata taksi ambayo haikuwa na abiria.
“Tafadhali nipeleke hoteli ya Ufukoni,” Bebe alimwagiza dereva taksi ambaye alikuwa mtu wa umri wa kati.
“Sawa mama,” dereva taksi alijibu.
“Naomba twende haraka kidogo,” Bebe alisema.
“Bila shaka mama,” naye dereva taksi alijibu.
Na kweli, yule dereva alijitahidi kwenda mwendo wa kasi, ikawachukuwa takriban dakika tano tu kutoka Michenzani hadi hoteli ya Ufukoni. Walipofika walikuta yalikuwepo bado magari kadhaa upande ule uliokuwa na sehemu ya chakula na vinywaji, na mlango wa kuingilia ndani kwa upande ule ulikuwa bado uko wazi.
“Nisubiri, sitachukuwa muda mrefu,” BeBe alimwambia yule dereva taksi.
“Sawa mama,” dereva taksi alimjibu huku akifyatua kiti ili aweze kujilaza.
BeBe alitazama huku na kule hakuona mtu, lakini mara Pei ambaye kumbe wakati wote huo alikuwa amejibanza nyuma ya mnazi, alijitokeza.
“Nipo hapa BeBe, umekuja kamili?”
“Ndiyo. Hapa ni salama?”
“Hakuna tatizo, itakuwa kama kumsukuma mlevi.”
“OK, twenzetu.”
Walipanda ngazi haraka haraka lakini bila kelele ambazo zingewashtua wapangaji wengine au hata wahudumu wa pale hotelini. Walipofika mlango wa chumba namba 406B Pei aliweka tena sikio lake kwenye tundu ya kuingizia funguo, na baada ya sekunde kadhaa akasema kwa kunong’ona:
“Naona hali ni kimya, yaelekea jamaa kalala.”
“Yawezekana yupo macho au ndio ana utia kasi, inabidi tumsafirishe. Chukua hii, lenga kwenye tundu ya kuingiza funguo kisha puliza. Usihofu, haina harufu.”
Pei alichukua kile kichupa alichopewa na BeBe ambacho kilikuwa na mrija mwembamba ambao aliupenyeza kwenye tundu la kuingizia funguo akapuliza, wakati akifanya hivyo, BeBe alikuwa macho akiangalia usalama.
Walisubiri kama dakika tano hivi kisha BeBe alitoa kishada cha funguo kutoka kwenye kijimkoba kidogo alichokuwa nacho. Alichagua funguo moja akaitumbukiza kwenye tundu la kitasa cha mlango wa chumba namba 406A, akazungusha taratibu. Huo haukufungua, lakini alipojaribu mwingine ulifungua kwa urahisi wakaingia.
Kule ndani kulikuwa kimya na baridi maana kiyoyozi kilikuwa kinafanya kazi. Hawakuwasha taa bali waliingia hadi kwenye chumba cha kulala ambako walimkuta mgeni aliyekuwemo amelala fofofo. Bila shaka ile dawa ya usingizi waliyompulizia ilimwongezea kasi ya uzito wa usingizi, maana hata walipomsukasuka hakushituka, aliendelea kukoroma. Waliwasha taa.
Aliyekuwa amelala kitandani alikuwa mtu wa umri wa kati, kiasi miaka 45 hivi na alikuwa ni chotara, labda wa kiarabu. Hakufuga ndevu, lakini alikuwa na sharafa nyingi kifuani, na alikuwa na sharubu ambazo alizitunza vizuri. Hakuwa na umbo kubwa. Alikuwa mfupi na mnene kiasi.
BeBe na Pei walianza pekuapekua yao mle ndani kwa ustadi mkubwa, na ni dhahiri hata baada ya upekuzi wao yule bwana asingeweza kung’amua kuwa chumba chake kilikuwa kimepekuliwa. Walianzia kwenye kabati la nguo ambapo hamkuwa na vitu vingi. Kulikuwa na shati moja la maumaua na suruali ya rangi ya kahawia na fulana kata makono, ambazo zote zilitundikwa kwenye heng’a.
Mifukoni mwa suruali na shati hamkuwa na chochote cha maana isipokuwa ndani ya pochi ambamo mlikuwa na noti 15 dola za Marekeni za thamani ya 100, zikifanya jumla ya dola 1,500. Kwa wakati ule ambapo dola moja ilikuwa na thamani ya Shillingi za Tanzania 965/=, ilimaanisha kuwa yule bwana angebadilisha dola zake angepata Shillingi za Tanzania 1,447,500/=. Hilo halikuwa jambo la kustusha.
Kilichostusha ni pale ambapo walipopekuwa kwenye begi lake ambalo alikuwa kalificha nyuma ya kabati la nguo, walikuta ndani kuna suruali nyingine mbili na mashati mawili, yote ya maua maua, lakini ya rangi tofauti. Mlikuwa pia na chupi tatu na fulana za kata makono tatu. Lakini kikubwa zaidi ni mabunda ya noti za dola za marekani ambayo yalifutikwa kwenye begi hilo chini ya nguo na katika mfuko maalum. Walipozitoa noti hizo ambazo zilikuwa na thamani ya 100, walikuta jumla dola 88,000 ambapo kwa fedha ya Tanzania wakati huo zingekuwa Shillingi 84,920,000/=.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mifukoni mwa suruali na shati hamkuwa na chochote cha maana isipokuwa ndani ya pochi ambamo mlikuwa na noti 15 dola za Marekeni za thamani ya 100, zikifanya jumla ya dola 1,500. Kwa wakati ule ambapo dola moja ilikuwa na thamani ya Shillingi za Tanzania 965/=, ilimaanisha kuwa yule bwana angebadilisha dola zake angepata Shillingi za Tanzania 1,447,500/=. Hilo halikuwa jambo la kustusha.
Kilichostusha ni pale ambapo walipopekuwa kwenye begi lake ambalo alikuwa kalificha nyuma ya kabati la nguo, walikuta ndani kuna suruali nyingine mbili na mashati mawili, yote ya maua maua, lakini ya rangi tofauti. Mlikuwa pia na chupi tatu na fulana za kata makono tatu. Lakini kikubwa zaidi ni mabunda ya noti za dola za marekani ambayo yalifutikwa kwenye begi hilo chini ya nguo na katika mfuko maalum. Walipozitoa noti hizo ambazo zilikuwa na thamani ya 100, walikuta jumla dola 88,000 ambapo kwa fedha ya Tanzania wakati huo zingekuwa Shillingi 84,920,000/=.
BeBe na Pei walitazamana kwa mshangao. Kisha walipanga vizuri vitu vilivyokuwemo kwenye lile begi wakalirudisha kama walivyolikuta. Hawakuona chochote kingine zaidi ya hati za kusafiria za yule bwana ambazo zilionyesha kuwa jina lake lilikuwa Seidati Mohanei na kwamba alikuwa raia wa Visiwa vya Ngazija.
Wakati walipomaliza pekuapekua yao ilikuwa tayari ni saa 9 za usiku. Walitoka mle chumbani wakahamia chumba cha pili ambako kwa haraka haraka waliweka vinasa sauti chini ya masofa na sehemu nyingine ambazo isingekuwa rahisi kwa mtu mwingine asiye mtaalam wa mambo hayo kugundua vilipo. Kisha walihakikisha wamepanga vitu kama walivyovikuta, wakaondoka wakimwacha yule bwana akiwa bado anakoroma.
8 - Harakati
“Mnhu, vipi njendo zako za leo, au ndiyo yaleyale ya harakati za usiku?” Zamoradi alimuuliza shogake ambaye bado alikuwa kajifunika shuka kitandani.
“Aaah, nitapumzika kidogo hadi majira ya jioni nina miadi na jamaa mmoja. Wewe nenda kazini nikiwa na lolote nitakupigia,” BeBe alimjibu mwenzie.
“Sawa, sina haja ya kukuagiza chochote kwani nyumba ni yako, fanya upendavyo kula utakacho. Nitasubiri unipigie.”
“Sawa Zamo, kazi njema.”
Ilikuwa ni asubuhi, kiasi saa moja na nusu ambapo Zamoradi alikuwa tayari kuondoka kwenda kibaruani. Mwenzie BeBe alikuwa bado kitandani akiwa yungali na usingizi kwani usiku ule alikuwa na muda mfupi sana wa kulala.
Kwa hiyo Zamoradi aliondoka kuelekea kibaruani kwake, naye BeBe akavuta shuka kuutafuta usingizi. Hata hivyo, wakati akijaribu kuuvuta usingizi, fikra za yaliyotokea usiku ule zilimjia, akatabasamu alipokumbuka maneno ya Pei wakati walipokuwa wakiondoka pale hoteli ya Ufukoni.
“Unajua BeBe, hii kazi inahitaji kufanywa na wenda wazimu kama sisi. Mtu mwenye akili zake timamu haiwezi.”
“Kwa nini Pei?”
“Unadhani mtu mwenye akili timamu ataacha dola za marekani elfu kumi na mbili zimpite hivihivi? Kama si wenda wazimu ni nini?”
BeBe alicheka, kisha akasema: “Wajua Pei, unalo sema ni kweli kabisa, lakini dunia inahitaji wawepo wenda wazimu kama sisi ili baadhi ya mambo yaende. Usizifikirie sana zile dola, zitakuchanganya. Lakinii, hebu nambie, baada ya kuziona umepata wazo gani?”
“Wazo moja tu. Nalo ni kwamba yule bwana na washirika wake wana lao jambo, na kwa vyovyote si jambo zuri. Nahisi ni biashara mbaya. Ni ipi hiyo? Magendo ya karafuu, madawa ya kulevya, vipusa, madini au nini? Hicho ndicho kitendawili cha kukitegua.”
“Ni kweli Pei. Kama hii ingekuwa ni biashara ya kawaida au ya halali, kwa nini mtu atembee na mipesa yote ile? Si wangepitisha biashara yao benki? Wanajambo, tena jambo baya na arobaini yao imefika. Mimi hisia zangu zipo kwenye karafuu, na hasa tukizingatia kuwa kuna kila sababu ya kuamini kwamba wale vijana wanao uhusiano wa karibu sana na Meneja mkuu wa BIKANGA.”
“Ni kweli, na pia ukiondoa madawa ya kulevya, ambayo hapa Zanzibar ni biashara iliyoshamiri sana, hayo mengine ya madini, vipusa nakadhalika bado hapa visiwani si makubwa kihivyo. Nadhani hisia zako juu ya karafuu zinaweza kuwa za kweli.”
“Tutafahamu kukicha salama kesho. Mwendelezo wa harakati zetu uanze mapema sana asubuhi. Wewe tayari wamekushitukia pale hotelini, kwa hiyo si vyema uonekaneonekane maeneo yale. Mimi wale vijana wananifahamu lakini hawajui nipo hapa Zanzibar kwa shughuli gani. Yule rafiki yangu alinifahamisha kwao akisema tu kuwa ni mgeni wake kutoka Dar. Kwa hivyo hata wakiniona pale kwa sasa haitakuwa mbaya, nitajua jinsi ya kuwavunga. Kesho asubuhi kazi ya kuutegua ule mtego utaniachia mimi, sawa.”
“Sawa BeBe, nami nitaingia mitaani, yawezekana nikagongana nao na hivyo kuweza kufuatilia nyendo zao bila kufika kule hotelini.”
“Ni wazo zuri, lakini uwe mwangalifu sana. Kama hawa wapo kwenye uhalifu tunaouhisi, basi ni watu hatari.”
“Usiwe na wasiwasi, nitakuwa mwangalifu. Nawe pia uwe macho.”
“Bila shaka. Tutawasiliana kadri mambo yatakavyokwenda.”
Wakati wanaongea yote hayo walikuwa wamejibanza pembezoni mwa mlango wa kuingilia hotelini. Baada ya mazungumzo yao walikwenda kwenye ile taksi aliyokwenda nayo BeBe pale hotelini na walimkuta dereva akiwa anauchapa usingizi. Walimwamsha, wakaondoka. BeBe alifikishwa kwanza Michenzani na kisha Pei akapelekwa kwake.
BeBe alitumia ufunguo wake akafungua mlango na kuingia ndani ambako alimkuta rafiki yake Zamo akiwa amelala. Hata hivyo sauti ya mchakacho wa kuchojoa nguo ulimwamsha.
“Mnh, wee BeBe una hatari kweli. Wala sina haja ya kuuliza umetoka wapi maana najua umeshatunga uongo wa kuniambia. Haya panda ulale.”
“Nitakuja kulala, lakini kwanza naenda kujimwagia maji, nasikia uchovu sana.”
“Sawa, kwanza kumeshakucha. Looh, saa kumi na moja! Ama kweli nyie ndio mnaolitumikia taifa. Mimi na uvivu nilionao kamwe nisingeiweza kazi uliyonayo.”
“Ungeweza tu Zamo, kila kitu ni kujituma na kuwa na mapenzi nacho. Muda wako wa kuswali sala ya asubuhi umewadia, je wendaoga kwanza au nikaoge?”
“Tangulia wewe unayetoka kwenye harakati kisha nitafuatia mimi.”
“Sawa.”
BeBe alikwenda kuoga na baadaye Zamo naye akafuatia. Wakati Zamo akijiandaa kwenda kibaruani baada ya kuswali, BeBe alikuwa tayari keshapitiwa na usingizi.
Ilipofika saa tatu na nusu hivi asubuhi BeBe alishtuka kutoka usingizini. Kilichomshtua ilikuwa ni njozi yenye matukio mabaya. Aliota akiwa kwenye mtumbwi amefungwa kamba miguu na mikono na amekalishwa chini ambapo kulikuwa na majimaji. Ndani ya mtumbwi kulikuwa na mijibaba miwili ambayo ilikuwa na sura zilizoonyesha ukatili wa waziwazi. Boti lilikuwa likienda kwa kasi, bila shaka likisaidiwa na mashine. BeBe aliangaza huku na kule, lakini macho yake yaliona maji tu kukiwa na mawimbi mazito, hakuona hata chembe ya nchi kavu.
Wakati anatafakari nini cha kufanya, ile mijibaba ilimwendea, mmoja akasimama mbele yake na mwingine nyuma.
“Tumfungue kamba,” mmoja alisema.
“Hapana, tumrushe hivihivi na kamba zake,” mwenzie alijibu.
“Mnh, mie nadhani ni vyema tuwe na huruma kidogo. Huyu ni mwanamke, hata bila kamba hawezi kufurukuta.”
“Nani kakwambia? Huyu ni hatari. Tusipoteze muda bwana, shika miguuni tumalize kazi tuliyotumwa turudi zetu.”
Ni wakati ile mijibaba ilipokuwa imembeba mzegamzega na kuvuta kasi ya kumvurumushia baharini ndipo BeBe aliposhituka kutoka usingizini.
Aliketi kitandani akitafakari juu ya ile ndoto. Hali kama ile ya kuota ndoto za kutisha huwa ikimtokea mara kwa mara, hasa anapokuwa katika kazi yenye hatari kama ile iliyompeleka Zanzibar. Mara zote, BeBe alizichukulia ndoto za aina hiyo kama ni onyo kwake kwamba shughuli aliyonayo ni pevu na kwamba alitakiwa awe macho sana.
Alikumbuka zile taarifa alizosoma kwenye majalada aliyopewa na wakuu wake siku walipokutana pale hoteli ya Ufukoni, akakumbuka vifo walivyokutana navyo wale vijana wa Siafu.
“Mnh, kwa hakika hawa jamaa tusipokuwa makini nao tutaishia pabaya,” BeBe alijisemesha.
Alinyanyuka kutoka kitandani akanyoosha maungo yake kwa muda kama wa robo saa hivi, kisha akatandika kitanda na kufanya usafi pale chumbani ndipo akaingia bafuni kuoga. Ni wakati alipokuwa mezani akikoroga chai ndipo simu yake ilipoita, akaipokea. Alikuwa ni Pei.
“BeBe, habari za asubuhi. Upo wapi?”
“Bado nipo hapa Michenzani, vipi wewe uko wapi?”
“Nipo hapa BIKANGA, jamaa zetu wameingia sasa hivi na yule mgeni wao.”
BeBe alishtuka, akasimama.
“Ni wao watatu tu au wako pamoja na mtu mwingine?”
“Umejuaje? Wanae mtu mwingine, ni mtu wa makamo, au tuseme ni mzee. Vipi una habari zake?”
“Nadhani huyo ndiye yule mzee ambaye huyu rafiki yangu Zamo alinieleza kwamba hao vijana walikuwa naye siku walipokwenda kwa mara ya kwanza hapo BIKANGA.”
“Sawa, basi mimi nipo nao, nitakupa taarifa ya kitakachoendelea.”
“OK, mimi ninakwenda kule hotelini nikaangalie kama ule mtego wetu umenasa chochote. Inawezekana kabla ya kuja huko walifanya mazungumzo kule chumbani kwa yule bwana.”
“Ni kweli, bora ukaangalie. Wakitoka huku nitakuarifu.”
“Sawa, lakini uwe mwangalifu, kwaheri.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
BeBe alikunywa juisi glasi moja haraka haraka, kisha akatoka kuelekea hoteli ya Ufukoni. Asubuhi ile alivaa gauni refu la moja kwa moja, ni yale ambayo ni maarufu kama dira. Kichwani alijifunga ushungi ambao ulifunika kabisa kichwa chake, na usoni alivaa miwani mieusi. Miguuni alivaa viatu vya kutumbukiza ambavyo havikuwa na kisigino. Mkono wake wa kushoto alikuwa ameshika mkoba mkubwa kiasi, ambao aliweka vifaa vyake vya kawaida vya kike na pia vifaa kadhaa vya kazi ikiwemo bastola ndogo aina ya rivolva, kiasi cha ukubwa wa pakti ya sigara.
Alipofika hoteli ya Ufukoni hakupita sehemu ya mapokezi bali alizunguka hadi upande wa kuingilia kutokea kwenye sehemu ya chakula na vinywaji.
“Usiondoke, nisubiri,” alimwagiza dereva wa taksi aliyoikodi kutokea Michenzani.
“Sawa mama, nitakusubiri,” dereva taksi alijibu.
BeBe alipandisha ngazi hadi ghorofa ya pili. Kwa bahati nzuri korido ya ghorofa hiyo ilikuwa nyeupe, hakukuwa na mtu, na hata wafanyakazi wa hoteli hawakuwepo. Kulikuwa kimya kabisa. Haraka haraka alikwenda hadi mlango namba 406A akaingiza funguo malaya aliyoitumia usiku, mlango ukafunguka akaingia na kuufunga.
Hakupoteza muda, moja kwa moja akaanza kuondoa vile vinasa sauti alivyoweka usiku na kuweka vingine. Vyote alivikuta sehemu zilezile walipoviweka. Aliingia chumba 406B ambako mara moja aligundua kuwa ule mkoba wa pesa waliouona jana haukuwapo, akajua bila shaka yule bwana aliondoka nao. Aliporidhika kuwa hamkuwa na chochote cha maana mle ndani alirudi tena chumba 406A akafungua mlango akatoka. Safari hii ile korida haikuwa tupu, kwa upande wa pili bwana mmoja alikuwa anatembea kuelekea kule alikokuwa akitokea BeBe na walipopishana yule bwana akamsalimu:
“Asalaam Aleikum bibie.”
“Wa aleikum salaam,” BeBe alijibu huku akipiga hatua kwenda mbele.
Hata hivyo yule bwana hakuishia hapo, akasema:
“Samahani, nawe ni mkazi hapa hotelini?”
BeBe alisitisha hatua kidogo akamgeukia na kusema: “La hasha, mimi si mkazi wa hapa, nilikuja kumtembelea jamaa yangu.”
Yule bwana bado aliendelea kudadisi: “Niwie radhi kama nakusumbua, lakini mimi ni mgeni hapa na kidogo niko mpweke, kuna uwezekano wa kunitembelea baadaye?”
BeBe alitabasamu, kisha akasema: “Nasikitika, hilo haliwezekani, mimi si hao unaowafikiria wewe. Kuja hapa hotelini haina maana kuwa nimefata kutongozwa.”
Yule bwana hakuwa na la ziada, aliishia kumwangalia BeBe akipiga hatua kuelekea kwenye ngazi za kutokea nje. Na kama ulivyokwisha kusoma pale mwanzoni, BeBe alikuwa ni mwanamke aliyeumbika, basi na ile dira aliyovaa, mnh, kama u mwanamume uliyekamili hata ingekuwa wewe ungesuuzika.
Yule bwana bado aliendelea kudadisi: “Niwie radhi kama nakusumbua, lakini mimi ni mgeni hapa na kidogo niko mpweke, kuna uwezekano wa kunitembelea baadaye?”
BeBe alitabasamu, kisha akasema: “Nasikitika, hilo haliwezekani, mimi si hao unaowafikiria wewe. Kuja hapa hotelini haina maana kuwa nimefata kutongozwa.”
Yule bwana hakuwa na la ziada, aliishia kumwangalia BeBe akipiga hatua kuelekea kwenye ngazi za kutokea nje. Na kama ulivyokwisha kusoma pale mwanzoni, BeBe alikuwa ni mwanamke aliyeumbika, basi na ile dira aliyovaa, mnh, kama u mwanamume uliyekamili hata ingekuwa wewe ungesuuzika.
Alipofika kule nje BeBe aliikuta ile taksi aliyokuja nayo ipo lakini dereva hakuwemo. Alijaribu kufungua mlango lakini alikuta umefungwa. Akahisi kuwa yule dereva alikuwa kule kwenye sehemu ya vinjwaji, hivyo akamfuata, na kweli alimkuta anakunywa soda. Yule dereva alipomuona tu alinyanyuka haraka haraka, lakini BeBe alimwambia amalize soda yake na kwamba angemkuta nje.
Wakati hayo yakiendelea kule hoteli ya Ufukoni, Pei naye alikuwa na yake kule ofisi ya BIKANGA. Kwa bahati nzuri ofisi hiyo ilikuwa maeneo ambayo ni ya shughuli nyingi, watu wakipita kwa wingi kwa vipandio na kwa miguu huku wakiwa katika shughuli zao. Katika hali hiyo haikuwa rahisi mtu kuhisi kuwa kulikuwa na lolote la ajabu kwa mtu mwingine kuwa sehemu moja akionekana hana lolote la kufanya ila kusoma gazeti kama ilivyokuwa kwa Pei.
Alikuwa amesimama upande wa pili wa barabara karibu na duka la vifaa vya ujenzi. Pale alipokuwa kasimama alikuwa na fursa nzuri ya kuona kila aliyeingia na kutoka ofisi za BIKANGA, ndio maana walipoingia wale vijana na mgeni wao kutoka Visiwa vya Ngazija aliwaona.
Masaa mawili ya usiku kuelekea alfajiri yalikuwa ya usingizi wa mang’amng’am kwa Pei. Hisia zake zilimrejesha kwa BeBe na ile taarifa kwamba mmoja wa wale vijana ni rafiki wa yule shoga yake Zamoradi na kwamba walishawahi kwenda ofisi za BIKANGA. Pei aliheshimu sana hisia zake na zimekuwa zikimsaidia sana katika kazi zake. Kwa hiyo alipoona anapata msukumo wa fikra kwamba aamkie ofisi za BIKANGA hakupuuza.
Basi asubuhi ile kiasi saa moja na nusu hivi, Pei alikuwa tayari kesha fika maeneo zilipo ofisi za BIKANGA. Na kweli hisia zake zikawa zenye utambuzi mzuri, kwani majira ya saa mbili na nusu aliliona gari la wale vijana likisimama kwenye eneo la kuegeshea magari la ofisi hizo. Kutoka ndani ya gari hilo walishuka watu wanne, wakiwemo wale vijana wawili, yule mgeni kutoka Visiwa vya Ngazija na mtu mwingine wa makamo hivi ambaye Pei hakupata kumwona kabla ya hapo.
Macho yake Pei mara moja yaliuona na akili yake ikautambua ule mkoba walioupekua chumbani kwa yule mgeni kule hoteli ya Ufukoni usiku. Kumbukumbuku za minoti ya dola za Marekani walizoziona ndani ya ule mkoba ilimjia Pei, akatabasamu na huku akitikisa kichwa. Pamoja na ujarisiri na moyo wa kulitumikia taifa, lakini pia udhaifu wa kibinadamu upo. Pei aliumia alipofikiria kuwa zile pesa zilikuwa zinapelekwa mahala ambapo harufu ya uvundo wa rushwa na hujuma ilinuka.
“Kwa hakika hawa jamaa ni washenzi,” Pei alijisemesha kimoyomoyo.
Ndipo alipoamua kumpigia simu BeBe kumfahamisha alipokuwa na alichokiona.
Jambo ambalo Pei hakulijua ni kwamba wakati yeye akiwa katika harakati za kufuatilia nyendo za wale jamaa na yeye zake zilikuwa zikifuatiliwa. Baada ya tukio la usiku uliopita ambapo wale vijana waligundua kuwa kuna mtu au watu waliokuwa wakiwafuatilia, nao wakaamua kuweka mtego ili kujuwa kama wataendelea kufuatiliwa siku iliyofuata. Kwa hiyo walipokwenda ofisi za BIKANGA waliweka vijana wawili wachunguze kama kulikuwa na dalili zozote za wao kufuatiliwa.
Pei hakuwaona vijana wawili ambao walifika maeneo ya ofisi za BIKANGA muda mfupi tu baada ya wale vijana kufika. Wale vijana waliokuwa wakifuatilia nyendo za Pei hawakuwa pamoja lakini walikuwa katika hali ambayo walikuwa wakionana na kuwasiliana. Mmoja alikuwa kama umbali wa mita kumi hivi kutoka alipokuwa kasimama Pei, akiwa ameketi kwenye benchi la msafisha viatu. Mwenzie alikuwa mbali kidogo akiwa amejibanza nyuma ya mlango wa duka moja la vifaa vya umeme.
Haikuwa vigumu kwao kugundua kuwa kuwapo kwa Pei pale kulikuwa kwa mashaka na hasa kitendo chake cha kupiga simu mara tu msafara wa wale vijana na mgeni wao kuingia ofisi za BIKANGA. Basi ikawa nao wapo makini kuona Pei angefanya nini kadri muda ulivyokuwa ukienda. Mmoja wao, yule aliyekuwa mbali kidogo alipiga simu kwa mmoja wa wale vijana na kumwambia:
“Boss, kuna jamaa tumemshtukia huku nje, tuna wasiwasi naye. Yaelekea anawafuatilia.”
“Kweli? Ok, kuweni makini wala msimshtue, tukitoka angalieni muwe naye beneti. Akitufuata nanyi mfuateni, sawa?”
“Sawa Boss.”
Wakati hayo yakiendelea, Pei alikuwa kaamua kuitisha teksi ili kama wale jamaa wakitoka awafuatilie nyuma. Kwa upande mwingine BeBe naye machale yalimcheza. Alipata wasiwasi kwamba isijekuwa wale vijana wakawa wamechukuwa tahadhari na kuweka mtego na hivyo kumfanya Pei anaswe. Naye pia akiwa kachero aliyebobea hakupuuza msukumo wa hisia hizo, akaamua aende moja kwa moja kule kwenye eneo la ofisi za BIKANGA ili akaone mambo yalivyo.
Na ulikuwa ni uamuzi mzuri, kwani alipofika tu eneo la ofisi hizo, na akiwa hata hajashuka kwenye gari aliyokuwa amekodi aliwaona wale vijana, yule mgeni na mtu mwingine wakitoka kwenye mlango mkubwa ofisi za BIKANGA. Walielekea eneo la kuegeshea magari na wakaingia kwenye gari moja aina ya Toyota Landcruiser. Wakati huo huo, macho yake yalimwona pia Pei akitembea haraka kuelekea kwenye teksi ambayo ilikuwa imeegeshwa si mbali sana na gari ambao yeye BeBe alikuwemo.
“Babu unaiona ile gari, ile Toyota ya kijivu, tuifuate. Hakikisha haitupotei, lakini uwe mwangalifu, na ni vyema uwe mbali nayo kidogo,” BeBe alimwelekeza dereva.
Alikuwa amekodi gari kutoka kwenye moja ya makampuni yanayokodisha magari, hasa kwa watalii, ambapo gari hizo zilikuwa na namba za kawaida na siyo namba za teksi.
“Sawa mama. Vipi wewe ni mwana usalama?” yule dereva aliuliza.
“Unaweza kuichukulia hivyo na ikaishia hapo. Lolote litakalotokea, nichukulie kama abiria wa kawaida, nina maana isiwe ni simulizi kwa yeyote maana haya ni mambo hatari,” BeBe alimtahadharisha yule dereva.
“Ondoa wasiwasi mama, mimi si mgeni sana wa mambo haya, niliwahi kuwa askari miaka ya ujana wangu,” yule dereva ambaye kwa kukisia umri wake ulikaribia au kuvuka kidogo miaka 50 alimtoa shaka BeBe.
“Mnhuu, kumbe wewe ni askari mstaafu? Basi kumbuka kiapo ulichokula kuhusu siri katika kazi zetu hizi. Au umesahau?” BeBe alimuuliza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana, siwezi kusahau, si unakumbuka ule msemo –“once a soldier, always a soldier!” Usiwe na wasiwasi, twende kazini,” yule dereva alisema huku akiwa na tabasamu pana usoni kwake.
Na kweli waliingia kazini. Ile Toyota ya wale vijana ilipoingia barabarani, gari aliyokuwa kapanda Pei iliacha magari mawili yatangulie kisha na wao wakaingia.
“Hakikisha ile Toyota haitupotei, ni muhimu sana,” Pei alimweleza dereva wa teksi.
“Haina shaka bosi, naiona na tutakula nao sahani moja,” yule dereva ambaye alikuwa ni kijana wa umri wa kadri miaka 28 hivi alisema.
“Nikutahadharishe ndugu, tunaowafuata si watu wazuri, kwa hiyo usiichukulie hali hii kimzahamzaha. Wakijua tunawafuatilia inaweza kuwa hatari,” Pei alimtahadharisha dereva.
“Sawa, nitasikiliza amri yako, lakini naomba usiniingize matatani,” yule kijana alisema, sasa akawa kidogo ameingiwa na woga baada ya Pei kugusia suala la wale wanaowafuatilia kuwa watu hatari.
“Ndiyo, fuata nitakachokuelekeza,” Pei alisema.
Wakati hayo yakiendelea, Pei hakuwa na habari kuwa naye alikuwa akifuatiliwa. Wale vijana waliokuwa wakimfuatilia nao walijiunga na ule msururu wa magari, wakawa nyuma ya gari alilokuwamo Pei. Wakati huo ilikuwa tayari inakaribia kuwa saa tano za asubuhi, ambapo harakati za mjini zilikuwa ndio zinapamba moto na magari barabarani yalikuwa mengi.
Msafara ule ulifuata barabara ya Uwanja wa Ndege ambapo tayari wale vijana waliokuwa wakimfuatilia Pei walishawasiliana na wale vijana waliokuwa kwenye ile Toyota.
“Bosi, jamaa anawafuata, yupo ndani ya taksi, magari mawili nyuma ya gari lenu, na sisi tupo nyuma ya gari alilopanda,” mmoja wa wale vijana alimweleza Burshid.
“Vyema, chukueni tahadhari asigundue kama mnamfuatilia, tunaelekea Chumbe,” Burshid alimjibu.
“Sawa Bosi,” yule kijana naye alijibu.
Kwa upande mwingine mawasiliano yalikuwa yakifanyika kati ya BeBe na Pei.
“BeBe, uko wapi?” Pei aliuliza.
“Nipo magari matatu hivi kutoka gari yako,” BeBe alimjibu.
“Hee, sikujua kama tupo pamoja, afadhali maana huko tuendako sijui kutatokea nini,” Pei alisema.
“Sikiliza, ni vyema tusianzishe valangati, nia iwe ni kufahamu wanadili gani, na hasa kufahamu wanaendesha shughuli zao kutokea wapi. Nadhani huku wanakokwenda ni sehemu wanayofanyia shughuli zao, kama hivyo ndivyo basi tutapanga kuwatembelea baadaye tukiwa kamili, hivi sasa hatujajiandaa, mimi hapa sina zana muhimu,” BeBe alitahadharisha.
“Ni kweli unalosema BeBe. Basi ngoja tuone kitakachotokea,” Pei alijibu.
Mazungumzo yale yalimpa hamasa dereva wa gari alimokuwa BeBe ambaye kama alivyokuwa amejitambulisha alikuwa askari mstaafu.
“Vipi mama, hao jamaa mnaowafuatilia ni majambazi?” yule dereva aliuliza.
“Unaweza kuwaita hivyo, lakini tunahisi ni waendesha magendo ya karafuu,” BeBe alimfahamisha.
“Mnh, mama, kama ni hao basi kweli inabidi muwe makini sana maana hawa jamaa wanamtandao mkali mno na ni wauaji,” dereva alisema.
“Vipi ulishawahi kupambana nao?” BeBe aliuliza.
“La hasha. Wakati nipo kikosini sikuwahi kupangiwa kazi ya kusaka watu wa aina hiyo, sana nafahamu jamaa zetu wa KKMZ ndio wanalo jukumu hilo. Lakini habari za mapambano yao na watu hawa tunazipata, na kwa kweli vijana kadhaa wamepoteza maisha na bado magendo yameshamiri,” dereva alielezea.
“Ni kweli, hali si nzuri ndio maana tupo kazini, tutawapata tu, na hasa tunatafuta mizizi yao na sio matawi, maana ukipurura matawi, bado shina litakuwepo na mti utaendelea kunawiri,” BeBe alisema.
“Ni sawa, kabisa. Wewe umetokea Bara?” dereva aliuliza.
“Hujakosea lakini kama nilivyokwishasema mambo haya ni siri, ujue kuwa kadri unavyoelewa mengi ndivyo ambavyo likitokea lakutokea utakuwa hatarini. Ndiyo, natokea Bara, tumeunganisha nguvu na wenzetu wa hapa Visiwani,” alimfahamisha.
“Usiwe na wasiwasi, mimi bado ni askari na sihofii lolote, ikibidi kupambana nitapambana, na kusema kweli ningepata nafasi japo kidogo tu ya kuwaadabisha hawa waendesha magendo ningefurahi sana maana wanatuingizia hasara kubwa sana,” yule dereva alisema huku akionyesha wazi kukerwa kwake.
BeBe alicheka kidogo kisha akasema, “Huwezi kujua ya mbele, labda nafasi hiyo utaipata.”
9 - Kashikashi
BeBe na yule dereva wa teksi, ambaye baadaye alijitambulisha kama Kaku Hassan, walipokuwa katika mazungumzo yao, mara waliona kwa mbele yao gari alilokuwamo Pei likipinda kuelekea kushoto. Magari mawili yaliyokuwa mbele yao yaliendelea mbele, lakini gari la tatu nalo likapinda kushoto.
“Je, mama nasi tuingie kushoto?” Dereva Kaku alimuuliza BeBe.
“Hapana, nenda mbele kidogo kisha simama. Kwa uzoefu wako wa eneo hili kuna njia yoyote ambyo itatuwezesha kuzunguka ili tutokee pale yale magari yalipoingilia?” BeBe aliuliza.
“Ndiyo, ipo. Wajua huku walikoelekea hawa jamaa barabara inatokea pwani, na huko kuna harakati nyingi za uvuvi na safari za maboti madogo yaendayo visiwani nje ya Unguja,” Dereva Kaku alisema.
“Vyema, basi fanya haraka, tuzunguke tukatokee huko mbele,” BeBe alitoa maelekezo.
“Sawa, mama,” Dereva Kaku alijibu akaenda mbele kidogo ambako alipinda kushoto akaongeza kasi ya mwendo wa gari.
Kwa upande wa pili hali ilikuwa tete kwa Pei. Walipopinda kushoto kuifuata ile gari ambayo walikuwemo yule kijana Barshid na wenzake, hawakwenda umbali mrefu, ile gari nyingine iliyokuwa nyuma yao ikawapita kwa vurugu kubwa, almanusura ingewagonga. Dereva wa ile teksi alifanya jitihada kubwa kuepusha ajali, lakini katika kufanya hivyo alitoka nje ya barabara na gari ikaingia kwenye mtaro.
Ile gari iliyotaka kuwagonga ilipofika mbele kidogo ikasimama na ikarudi nyuma hadi pale ambapo Pei na yule dereva teksi walikuwa wametoka na wakawa wanaangalia jinsi ya kujikwamua.
Wale vijana wawili walitoka na kwenda hadi walipokuwapo Pei na yule dereva wake.
“Poleni jamani, naona mmetoka nje ya njia. Tungeweza kuwapa msaada zaidi lakini tuna haraka. Kama upo tayari kwenda nasi tunaweza kukupa lifti wakati huyu dereva taksi akishughulikia kuitoa gari,” kijana mmoja alimwambia Pei.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa vile alikuwa na shauku ya kuifuata ile gari waliyokuwemo Barshid na wenzake, na bila kujua kuwa ule ulikuwa mtego, Pei alikubali, akatoa pesa kumlipa yule dereva teksi.
“Pole sana bwana, bila shaka utapata msaada, ngoja nichukuwe lifti ya hawa jamaa,” Pei alimweleza yule dereva.
“Haina shida bro, nitatoka tu, kila la kheri,” Dereva alijibu, akiwa amepokea zile pesa.
Pei, ambaye hakuwa na mzigo wowote, aliingia kwenye ile gari akakaa siti ya nyuma pamoja na mmoja wa wale vijana.
“Vipi, unakwenda pwani, Bro?” yule kijana aliyekaa siti ya mbele alimsemesha Pei.
“Ndiyo, kuna wenzangu wametangulia na gari nyingine,” Pei alijibu.
“Anhaa, ni ile Toyota iliyokuwa mbele, au siyo?” yule kijana alimuuliza.
“Ndiyo,” hawako mbali sana.
Yule kijana aliyekuwa amekaa nyumba na Pei akaangua kicheko cha dharau sana kisha akanyamaza ghafla na mkononi mwake akawa ameshika bastola ambyo mtutu wake ulielekezwa kichwani kwa Pei.
Pei, ambaye hakuwa na mzigo wowote, aliingia kwenye ile gari akakaa siti ya nyuma pamoja na mmoja wa wale vijana.
“Vipi, unakwenda pwani, Bro?” yule kijana aliyekaa siti ya mbele alimsemesha Pei.
“Ndiyo, kuna wenzangu wametangulia na gari nyingine,” Pei alijibu.
“Anhaa, ni ile Toyota iliyokuwa mbele, au siyo?” yule kijana alimuuliza.
“Ndiyo,” hawako mbali sana.
Yule kijana aliyekuwa amekaa nyumba na Pei akaangua kicheko cha dharau sana kisha akanyamaza ghafla na mkononi mwake akawa ameshika bastola ambyo mtutu wake ulielekezwa kichwani kwa Pei.
“Bwege mkubwa wewe, na leo utakiona cha moto. Ukitikisika tu na ubwaga ubongo wako humuhumu ndani ya gari. Tulia kama unanyolewa,” yule kijana alisema, wakati huo akiwa amesogea pembeni kabisa mwa ile siti ya nyuma mbali na Pei.
“Pole sana Bro, safari hii huna ujanja. Jana usiku ulichoropoka, lakini leo utajinyea. Ile gari ya mbele ni ya mabosi wetu na wewe ni mateka wetu, unaelewa?” yule kijana aliyekaa mbele alimweleza Pei.
“Mbona siwaelewi, nadhani mmepotea. Mimi siye mnayemdhania,” Pei alijaribu kujitetea, lakini moyoni alijua kuwa alikwisha nasa kwenye mtego ambao hatma yake ilikuwa mbaya.
Pei aligeuka nyuma kuangalia kama kuna gari yoyote iliyokuwa ikiwafuata, akidhani kuwa labda BeBe naye alipinda kona kuelekea kule, lakini hakuona gari yoyote.
“Usijisumbue, Bro, huku huna msaada wowote, tulia. Gugu, mchome hiyo sindano,” yule kijana aliyekuwa siti ya nyuma alimweleza mwenziye ambaye alitoa sindano iliyokuwa na dawa ya maji ya rangi nyeupe.
“Nyoosha mkono wako,” yule kijana aliyekuwa siti ya mbele alimwamrisha Pei.
“Lakini jamani..”
Pei alijaribu kujitetea na hakumaliza alichotaka kusema kwani alishitukia amepigwa ngumi moja nzito ya taya, na kabla hajafurukuta zaidi alipigwa nyuma ya shingo na kitao cha bastola akawa kimya, kapoteza fahamu. Bila kujali hali aliyokuwa nayo Pei, yule kijana aliyekuwa siti ya mbelea alimchoma sindano ya mkono na kuhakikisha dawa yote iliyokuwemo imeingia mwilini mwake.
BeBe na Dereva Kaku walifika pwani kabla ya ile gari iliyokuwa na wale vijana waliomteka Pei. Hata hivyo, walifika wakati mzuri ambapo waliona Barshid na wenzie wakiingiza gari kwenye kivuko kilichokuwa kimeegeshwa ufukoni kikipakia abiria na magari.
“Vipi mama, na sisi tuingie?” Dereva Kaku alimuuliza BeBe.
“Hapana, kuna mwenzangu ambaye alikuwa akiwafuata hawa kwa karibu, simuoni wala silioni gari alilokuwemo. Nina wasiwasi, isije ikawa kaangukia kwenye mtego. Paki gari pale pembeni nijaribu kumpigia simu,” BeBe alitoa maelekezo.
Hata hivyo simu ya Pei iliita mara moja tu kisha ikakata bila kupokelewa. Akajaribu kupiga tena, lakini mara hii haikuita, bali alipata mlio wa sauti iliyomwashiria kuwa namba aliyokuwa akipiga haipatikani.
“Mnh, hii siyo kawaida, Mzee kuna tatizo. Nahisi mwenzangu kaangukia mtegoni. Inaelekea hawa walikuwa na magari mawili, moja ni hili na lingine lilikuwa nyuma ya lile alilokuwemo mwenzangu, nahisi wamemteka,” BeBe alisema, huku akijilaumu moyoni kwa nini hakuwa amechukuwa tahadhari zaidi.
“Huyo mwenzio naye ni mama kama wewe?” Dereva Kaku aliuliza.
“Hapana, ni mwanaume, tena ni mtu wa hukuhuku visiwani, ametokea kwenye kikosi maalum cha kuzuia magendo,” BeBe alisema.
“Looh, kama ni kweli wamemteka, basi atakuwa katika hali ngumu sana. Au ameona arudi mjini?” Dereva Kaku alitafakari.
“Hapana, sidhani kama ni hivyo. Jukumu lake lilikuwa ni kuwafuatilia ili tujue nyendo zao. Watakuwa wamemteka. Ona ile si ile gari iliyokuwa nyuma ya gari aliyokuwamo Pei? Bila shaka atakuwa mle,” BeBe alisema huku akijaribu kuangalia kwa makini kama angemuona Pei, lakini vioo vya ile gari vilikuwa ni vile vyenye rangi nyeusi, hakuona ndani.
“Kweli, ile gari ni ile iliyopinda kona pamoja na ile Toyota. Inawezekana unalohisi likawa kweli. Bora na sisi tuingie, tuvuke nao,” Dereva Kaku alishauri.
“Hapana, tusifanye hivyo. Hapa tulipo hatujajiandaa kwa lolote. Kwani hiki kivuko si kinakwenda kwenye kisiwa kimoja tu?” BeBe aliuliza.
“Ndiyo, kinakwenda kisiwa cha Chumbe,” Dereva Kaku alisema.
“Sawa, ni vyema turudi mjini tukajiandae, wajua hii ni kashkashi nzito, tukijipeleka kichwa kichwa tutaangukia pabaya. Je, utakuwa tayari kwa mapambano?” BeBe alimuuliza Dereva Kaku.
“Bila shaka mama, na hata kama utataka tuongeze nguvu, wapo vijana ninaowaamini,” Dereva Kaku alisema.
“Hapa, ni mapema mno kuhusisha watu zaidi, na hata hivyo hii ni kazi ya Serikali, tukihitaji msaada zaidi tutapata kutoka vikosi vinavyohusika. Lakini kwa sasa nitataka wewe uwe pamoja nami mpaka pale tutakapoona kama tunahitaji msaada, na ni msaada wa aina gani,” BeBe alisema.
“Sawa mama, mimi nakusikiliza wewe,” Dereva Kaku alisema, huku akigeuza gari na kuondoka pale ufukweni kuelekea mjini.
“Tufanye haraka kidogo, nitapenda kurudi mapema huku ili tuwahi kuvuka kabla jua halijatua,” BeBe alimweleza Dereva Kaku.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimekuelewa. Bado kuna kama masaa manne hivi kabla kivuko hakijafungwa kwa leo, naamini tutawahi,” Dereva Kaku alisema.
Kwa upande mwingine kivuko nacho kilikuwa kiking’oa nanga kuelekea Kisiwa cha Chumbe. Wakati wote ule Pei alikuwa katika usingizi mzito kutokana na kipigo na ile sindano ya usingizi aliyodungwa na wale vijana. Ndani ya kile kivuko hakuna aliyejali la mwenzie, labda kama safari ilikuwa ya pamoja.
Wakati kivuko kiking’oa nanga, yule kijana aliyekuwa ameketi siti ya mbele kwenye lile gari alilokuwamo Pei alitoka akaenda kwenye gari walilokuwamo Barshid na wenzie.
“Bosi, kama nilivyokufahamisha, jamaa tunaye, tumemtuliza na hajazinduka,” yule kijana alimweleza Barshid.
“Vyema, una hakika yu hai bado,” Barshid aliuliza.
“Ndiyo, yu hai, anapumua,” yule kijana alisema.
“Ok, tutamalizana naye tukifika kambini,” Barshid alimweleza yule kijana ambaye alirejea kule kwenye lile gari alilokuwamo Pei.
Upande wa pili BeBe na Dereva Kaku walikuwa wameshika kasi kurejea mjini, lakini walipokaribia kuingia barabara kuu walikuta pembeni mwa barabara kuna hekaheka ya kulikwamua gari dogo ambalo lilionekana kuwa limekwama mtaroni. Walikuwapo watu wawili tu wakijaribu kulisukuma na ndani akiwemo mtu mwingine ambaye alikuwa ni dereva wa gari lile.
Macho ya Dereva Kaku yalipoliona tu lile gari akakumbuka kuwa ndilo lililokuwa mbele yao walipokuwa katika zile harakati za kuwafuatilia wale waliokuwa kwenye Toyota.
“Mama, lile gari lililokuwa mbele yetu ni lile, ambalo alikuwamo huyo mwenziyo ambaye unadhani ametekwa na wale jamaa,” Dereva Kaku alimweleza BeBe.
Baada ya kuiangalia vizuri BeBe naye alikubali kuwa ndiyo.
“Ni kweli, ndilo lenyewe, hebu simama pembeni tumuone yule dereva,” BeBe alisema.
Dereva Kaku aliegesha gari pembeni, kisha wote wakashuka wakakatiza barabara hadi lilipokuwepo lile gari lililokwama.
“Poleni jamani, tumekuja kuwapa msaada,” Dereva Kaku alisema huku yeye na BeBe wakijiunga kusukuma lile gari.
Baada ya nguvu kuongezeka, lile gari liliweza kutoka pale lilipokwama na dereva wake akaliegesha vizuri kisha akashuka kuwashukuru wale waliomsaidia.
“Asanteni sana jamani, bila nyie leo ningeshinda na pengine hata kulala hapa,” alisema huku akiwapa mkono wale jamaa wawili waliokuwapo mwanzo na kisha Dereva Kaku na BeBe.
Alipofika kwa BeBe yule dereva alikuwa na shukurani maalum. “Looh, mama asante sana. Ni akina mama wachache ambao wanaweza kufanya ulichofanya, wengi huwa hawatoi msaada kama huu uliotoa wewe, wangesimama pembeni kuangalia, hata kama gari iliyopata matatizo inawahusu,” alisema.
“Aaah, ni kweli hilo linatokea, lakini ni upuuzi kwa sababu sote tunapaswa kusaidiana. Mwanamke anaweza kuwa hana nguvu kama mwanamume, lakini hizo nguvu kidogo alizonazo zinaweza kuchangia kufanikisha jambo kama hivi nilivyofanya,” BeBe alisema.
“Ni kweli kabisa unachosema. Nawashukuru sana jamani, naona sasa bora nigeuze nirudi mjini maana abiria niliyekuwa naye alipata lifti ya gari nyingine,” yule dereva alisema.
“Hee, kumbe ulikuwa na abiria akakuacha uhangaike peke yako?” Dereva Kaku alimuuliza.
“Aaah kaka, siunajua tena watu na harakati zao. Alisema alikuwa na haraka, basi wale vijana waliotaka kutugonga wakampa lifti akaondoka nao,” dereva alieleza.
“Mnhuu, walitaka kuwagonga? Ilikuwaje, mbona hapa ni peupe kabisa?” BeBe aliuliza.
“Mamangu wee, siunajua tena haraka zetu vijana. Sisi tumepinda kona, ghafla bin vuu tukaona gari yao ikija kasi tena kutuelekea. Katika jitihada za kuepusha kugongwa ndio nikatumbukia kwenye huu mtaro,” yule dereva alieleza.
BeBe na Dereva Kaku walitupiana macho yakiashiria kuelewa jambo.
“Kwani hiyo gari ya hao vijana mlikuwa mmeongozana nayo?” BeBe aliuliza.
“Naam, tena baada ya wewe kuuliza swali napata wasiwasi kidogo, isije ikawa walikuwa wakitufuatilia! Maana tangu mjini tulikotoka walikuwa nyuma yetu na hawakuonyesha dalili za kutupita. Mnh, yawezekana walikuwa wakitufuatilia wale,” yule dereva akajisemesha.
“Kwani huyo abiria uliyekuwa nae naye alikuwa anaelekea wapi?” BeBe aliuliza.
“Wajua, mnhuu, hii dunia ina mambo. Yule bwana niliyekuwa naye alikuwa akiifuatilia gari moja ya mbele, ni aina ya Toyota na akaniagiza nihakikishe haitupotei. Ilipokatiza kuja huku nasi tukakatiza. Sasa napata picha kamili ya hili jambo, nafikiri wale vijana waliotaka kutugonga lao moja na wale waliokuwa kwenye ile Toyota. Sisi tulikuwa tunawafuatilia, kumbe na sisi tulikuwa tukifuatiliwa!” yule dereva alisema.
BeBe na Dereva Kaku wakatupiana tena macho ya kuashiria kuelewa jambo.
“Kwa hiyo inawezekana huyo abiria wako akawa ametekwa na hao jamaa,” Dereva Kaku akauliza.
“Sio inawezekana tu, nadhani ndivyo ilivyo, maana baada ya kutukosakosa kwa makusudi, wale vijana walirudi hadi hapa wakatupa pole ya uongo na kweli, kisha wakasema wana haraka na kwamba kama abiria wangu angependa wangempa lifti. Basi, yule bwana akakubali, wakaondoka naye. Looh, masikini, nafikiri atakuwa katika wakati mgumu maana wale vijana hawakuonekana kuwa ni watu wazuri,” yule dereva akalalama.
BeBe na Dereva Kaku wakatizamana na kukawa na ukimya kidogo ambao ulivunjwa na yule dereva.
“Wajua kaka, pengine ni bahati yangu wameniacha, maana hata yule jamaa alinionya kuwa wale watu tunaowafuatilia sio watu wazuri. Looh, jamani, hebu tuondoke mahala hapa. Asanteni kwa msaada wenu,” yule dereva akaingia kwenye gari lake akaondoka.
BeBe na Dereva Kaku nao wakavuka barabara kuelekea kwenye gari lao.
“Subiri, Kaku, usiondoe gari, nahitaji kupiga simu,” BeBe alimwambia Dereva Kaku kisha akatoa simu yake ya mkononi akabonyeza vitufe kadhaa na kisha simu ilipoita na kupokelewa upande wa pili akaongea.
“Hallo Zamo, upo kazini?“
“Ndiyo Beli, vipi uko wapi?“
“Na mimi pia nipo kazini. Vipi bosi wako yupo“
“Ndiyo, yupo. Mbona unamuulizia?“
“Aaah, usijali. Nafahamu alipata wageni asubuhi, wale jamaa zetu, mchumba wako na wenzie, au siyo?“
“Ni kweli Beli, ulijuaje, mbona unanitisha?“
“Usitishike, ni mambo ya kazi tu. Je tangu wageni wake walipoondoka alikwishatoka hapo ofisini?“
“Hapana, hajatoka. Beli, maswali yako yananitatiza. Kuna nini?“
“Mnnh, usiwe na wasiwasi Zamo, tutaongea zaidi tutakapokutana nyumbani jioni.“
“Sawa Beli, lakini umeshaniweka kwenye wasiwasi mkubwa. Haya, tutaonana baadaye.“
Baada ya kuongea na Zamoradi, BeBe alimpigia simu Mkuu wake wa kazi, na maongezi yakawa:
“MB, mambo huku yameiva na ninahitaji ushiriki wako wa haraka,” BeBe alimweleza mkuu wake, Momaa Bulo (MB).
“Nakupata vizuri A-5, mnhuu nini kinaendelea na unahitaji ushiriki wa aina gani kutoka kwangu?” MB alijibu.
“La kwanza muhimu na ambalo ni la haraka sana naomba uzungumze na KK. Nahitaji ufanyike upekuzi haraka ofisini kwa Mkurugenzi Mkuu wa BIKANGA. Uwezekano mkubwa ni kwamba anayo mamilioni ya pesa za magendo alizopokea kama saa moja iliyopita pale ofisini kwake. Akikutwa nazo akamatwe mara moja,“ BeBe alieleza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“A-5 hilo unalotaka lifanyike ni jambo kubwa. Una uhakika na hisia zako?“ MB aliuliza.
“Kwa asilimia 90 mkuu. Hivi tunavyoongea, Pei ametekwa na waendesha magendo na wamekwenda naye nisikokujua. Kukamatwa kwa Mkurugenzi wa BIKANGA kunaweza kutupa mwanga juu ya hilo, ingawa nami nipo mbioni kuwafuatilia,“ BeBe alisema.
“Pei ametekwa? KK ana habari hiyo? Ametekwaje?“ MB aliuliza.
“Mkuu, namna alivyotekwa ni hadithi ndefu, KK hana habari, naomba umfahamishe. Twende kwa haraka, naomba suala la upekuzi ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji BIKANGA lifanyike haraka asije akahamisha pesa ninazohisi bado zipo ofisini kwake na ambazo ni kidhibiti kikubwa,“ BeBe alisisitiza.
“Sawa A-5, mimi nipo Arusha kikazi, lakini nitaongea na KK. Nashauri kuwa kesho tukutane hapo Zanzibar ili nipate taarifa kamili ya hali inavyoendelea huko,“ MB aliagiza.
“Sawa Mkuu, nadhani mpaka hiyo kesho mengi zaidi kuhusu kashkashi hii yataeleweka vizuri,“ BeBe alisema.
“Ok A-5, ningependa tuongee zaidi lakini naona hali hairuhusu. Kwa sasa fanya unachoweza, na tafadhali uwe mwangalifu zaidi. Kutekwa kwa Pei ni pigo kwetu,“ MB alisema.
“Nakuelewa Mkuu, nitafanya ninachoweza kujaribu kumuokoa,“ BeBe alijibu.
Baada ya mazungumzo hayo, BeBe aliingia ndani ya gari na akamwambia dereva Kaku waelekee mjini.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment