Search This Blog

Sunday 19 June 2022

SIRI YA FURAHA - 3

 





    Simulizi : Siri Ya Furaha

    Sehemu Ya Tatu (3)



    "Samahani, jina langu ni Craig na nina huu mzigo wako….. kumbuka upendo wa kweli haufi, anaweza kuwa mpenzi wako wa kweli" Alimaliza kijana huyo kuongea huku akiwa amemkabithi Veronika bahasha iliyokuwa ya rangi nyeupe na alianza kuondoka. “Hey guy! Tell me, who gave you this parcel?” ( niambie, ni nani amekupa mzigo huu?”) alisikika Veronika akimuuliza kijana huyo “worry not miss just go and check it….” ( usijali, nenda kauangalie…”) alimjibu huku akiendelea kutembea kurudi katika eneo la chuo na hatimaye alizamia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Veronika alitulia kidogo na kuvuta pumzi, alianza kutembea akielekea katika kituo cha treni. Baada ya dakika kadhaa alikuwa katika kituo hicho na alikaa kituoni hapo kwa dakika tano kabla ya kupanda treni. Robo saa baadaye alikuwa katika eneo la Horningsea huku akitembea taratibu akielekea katika hosteli za chuo chao. Alikuwa akiiwazia bahasha aliyokuwa amepewa kwani ilikuwa nyepesi na hakujua kitu kilichokuwapo katika bahasha hiyo. Tayari alishatambua uwezekano wa mwanafunzi kumfuatilia, hilo lilifuata kutokana na maneno aliyoambiwa na kijana aliyempa bahasha hiyo. Hatimaye alifika katika chumba alichokuwa akikaa katika hosteli hizo zilizokuwa za mtu mmoja mmoja. Alijilaza katika kitanda chake kwa sekunde kadhaa kwa vile alikuwa amechoka sana. Baada ya dakika tano alijisikia vizuri kidogo alichukua bahasha aliyopewa na kuifungua. Mara baada ya kuifungua bahasha hiyo aliiona picha ya kijana mtanashati ambayo ilimfanya mapigo yake ya moyo yaende kwa kasi kidogo.

    Kijana huyo aligundua alikuwa amezaliwa kutoka kwa mzazi mwenye asili ya kizungu na mwingine ya kiafrika. Alipoigeuza picha hiyo aliliona jina la kijana huyo lililoandikwa Moses Malcolm na kwenye mabano liliandikwa Mos Q. Veronika alivuta pumzi ndefu kabla ya kuelekeza macho yake kwenye bahasha aliyotoa picha hiyo na alikiona kipande kidogo cha karatasi kilichokuwa kimeandikwa. Alikitoa haraka kipande hicho na kuanza kukisoma. `Dear The One I love, I Have Nothing To Prove How Much I Love You But Don’t Miss This Month`s Cambridge Music Concept Because I Will Tell The World About This…” ( kwako ninayekupenda, sina kitu cha kukuhakikishia kwamba nakupenda ila usikose tamasha la muziki la mwezi huu kwa sababu nitaueleza ulimwengu juu ya jambo hili….) alimaliza kukisoma kipande hicho cha karatasi huku akitabasamu kidogo. Alipata maswali mengi kichwani juu ya kijana huyo mtanashati ambaye alimtaka ahudhurie katika tamasha la muziki la mwezi huo wa nne. Hakutambua jambo ambalo kijana huyo alitaka kulifanya katika tamasha hilo lilolokuwa mfululizo wa matamasha ya muziki yaliyokuwa yakifanyika kila mwisho wa mwezi katika chuo chao.

    Hakufikiria kuhudhuria tamasha hilo lililokuwa limebakiwa na wiki moja, aliwaza kufanya jambo hilo kwa vile alikuwa hafahamu nia ya kijana huyo aliyemwandikia ujumbe huo. Siku zilijongea na Jumamosi ya tamasha hilo ilizidi kusogea, siku ya Ijumaa Veronika aliwaza juu ya uamuzi wake wa kutoenda kujumuika katika tamasha la muziki la mwezi huo wa nne na alihisi angeweza kukosa jambo. Hatua hiyo ilifuata baada ya kuiangalia mara nyingi picha ya Moses ambayo ilimvutia kumwona na kumfahamu zaidi.

    Siku iliyofuata alijiandaa mapema kwa ajili ya kujumuika katika tamasha hilo. Siku hiyo alivaa jinzi pamoja na fulana iliyokuwa na rangi nyekundu pamoja na raba zilizokuwa za rangi hiyo.

    Majira ya saa sita mchana alikuwa akiondoka katika chumba cha hosteli yake akiwa tayari kwa safari ya kuelekea katika tamasha la muziki la mwezi huo. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuhudhuria tamasha la muziki hata jinsi alivyovaa ilitokana na kuwashuhudia watu wengi wakivaa hivyo katika matamasha ya muziki. Kwa mwonekano alikuwa akivutia na ilikuwa rahisi kwa mwanamume yeyote kumtamani kutokana alivyokuwa amependeza. Rangi yake halisi ya weupe wa asili, sura nzuri ya kuvutia pamoja na umbile la kirembo ndivyo vilivyoonekana kwa Veronika. Vitu hivyo ndivyo mara kadhaa viliwafanya watu wapinge ukweli kuwa Veronika alikuwa akitokea Tanzania. Wanafunzi wengi wa chuo walikuwa wakihisi alikuwa Mmarekani mweusi aliyekuwa akitokea katika familia ya kitajiri.

    Majira ya saa nane na nusu alikuwa akiingia katika ukumbi wa chuo hicho cha Cambridge na tayari tamasha la muziki lilikuwa limeshaanza. Akiwa mtulivu alitembea taratibu kabla ya kwenda kukaa katika eneo lililokuwa karibu na jukwaa ambalo lilikuwa limepangwa viti kwa ajili ya watu ambao walikuwa hawachezi muziki zaidi ya kutazama wasanii tofauti wa chuo waliokuwa wakitumbuiza. Akiwa hana amani sawasawa kutokana na ugeni wake katika tamasha hilo alinunua soda ya kopo ya Pepsi ambayo alikuwa akiendelea kunywa taratibu. Aliwashuhudia wanafunzi kadhaa wa chuo waliokuwa wakiendelea kucheza wimbo pamoja na kumshangilia msanii mmoja ambaye alikuwa jukwaani wakati huo.

    Ndani ya robo saa za kuwapo katika ukumbi huo wa chuo kuna jambo lilianza kumkera, tayari wanaume zaidi ya watano walikuwa wamemfuata wakitaka asimame ili akacheze nao. Hakukubaliana na jambo hilo hata kidogo zaidi ya kubaki mtulivu katika eneo alilokaa sambamba na watu kadhaa. Baada ya nusu saa, hatimaye alimfuata mwanafunzi mmoja wa kiume ambaye tayari alikuwa amelewa na alikuwa akimn`gan`ganiza waende wakacheze muziki. Mbali na kumkatalia kijana huyo alikuwa mbishi na alianza kumvuta akimlazimisha wakacheze muziki. Jambo hilo lilimuudhi sana Veronika na aliwaza kuondoka ukumbini hapo. Alianza kuweka vizuri vitu vyake kwenye begi dogo alilokuwa nalo akiwa na nia ya kuondoka huku akiwa na jazba. Wakati huo kijana aliyekuwa akimtaka wakacheze bado alikuwa kando yake akimsisitiza, alikuwa akinuka pombe kali na Veronika hakujisikia vizuri hata kidogo kuwa karibu na mwanamume huyo. Baada ya kuweka sawa vitu vyake alisimama akiwa na lengo la kuondoka, akiwa ametembea hatua kadhaa huku akifuatwa na kijana huyo alisimama baada ya kusikia tangazo kutoka kwa mshereheshaji wa tamasha hilo. “ Yeah! Wharap guys in the building, again your host Fwizkaz introducing to you The One and Only, Mos Q, To day he is going to perform his new hit which is known as I love You Veronika, Please Guys make some noise for Mossss QQQ” ( mnaendeleje ndani ya ukumbi huu, kwa mara nyingine mshereheshaji wenu Fwizkaz namleta kwenu mmoja na pekee, Mos Q, leo ataimba wimbo wake mpya unaoitwa nakupenda Veronika, piga kelele kwa Mos Q) alisikika mshehereshaji wa tamasha hilo na sauti yake ilipenya vizuri kwenye masikio ya Veronika aliyejikuta akisimama na kuelekeza macho kwenye jukwaa.

    Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio na kelele za watu wakimshangilia Mos Q zilimchanganya zaidi akabaki ametoa macho akiangalia jukwaa kuu. Tayari kulikuwa na sauti za muziki uliokuwa ukisikika lakini Moses alikuwa hajafika jukwaani. Baada ya sekunde kadhaa mapigo yake ya moyo yaliongezeka zaidi baada ya kuiona sura ya kijana ambaye mara ya mwisho aliiona picha yake aliyoituma ikiwa sambamba na ujumbe mfupi. Alikuwa kijana mtanashati ambaye alikuwa jukwani huku akiwa ameshika kipaza sauti mkononi mwake tayari kwa kuanza kuimba. Kelele za juu zilizosikika kutoka kwa kwa warembo wa chuo hicho pamoja na wanaume kadhaa, zilimwacha Veronika katika hofu. “ hey! Beautiful lady Veronika, can you come on the Stage?” (msichana mzuri Veronika unaweza kuja jukwaani) yalikuwa maneno ya kwanza kabisa kutoka kwa Moses ambaye aliwafanya watu waliohudhuria tamasha hilo waanze kuangaliwa huku na huko wakiwa na lengo la kumwona msichana huyo, Veronika.

    Sauti hiyo ilimfikia vizuri Veronika aliyejihisi kuchanganyikiwa zaidi aliona jambo hilo lilikuwa gumu kwake kulifanya. Alitulia huku akiwa ameinamisha kichwa chake akiwa hayuko tayari kuenda jukwaani. “Ooh! Don’t hurt me like this Girl because I have seen you five minutes ago….” ( Usiniumize kama hivi, kwa sababu nimekuona dakika tano zilizopita ) alisikika tena Moses kwa sauti ya kumubembeleza. Wakati akiendelea kutafakari, ghafla Veronika alishtuka baada ya kuona akishikwa mkono wake. Alipogeuka alimwona Craig, kijana aliyemkabidhi bahasha ya Moses juma moja lililokuwa limepita. Taratibu Craig alianza kumvuta Veronika ili aende jukwaani, wakati huo alishindwa kugoma na alianza kutembea kuelekea jukwaani na watu kadhaa walioshuhudia jambo hilo walianza kupiga makofi wakishangilia tukuo hilo. Hatimaye walipofika katika ngazi za kupandia jukwaa kuu, Craig alichukua kibegi alichokuwa nacho Veronika na hatimaye mrembo huyo alipanda jukwaani. Kelele ndizo zilitawala ukumbini hapo wakati Veronika akikumbatiana na Moses aliyempokea jukwaani.

    Alijihisi amechanganyikiwa na akili yake ilikuwa haijatulia vizuri. Mambo mengi yalikuwa yametokea kwa muda mfupi sana na tayari aliamini alikuwa ndani ya mtego wa kijana huyo mtanashati. Moses au Mos Q alihurusu muziki na jambo hilo lilichukua nafasi kabla ya kuanza kusikika akiimba wimbo wake mpya aliokuwa amemtungia mrembo huyo, Veronika. Wimbo huo mzuri uliowavutiwa watu wengi alikuwa akiuimba huku akimzunguka Veronika, watu walipiga kelele wakishangilia juu ya wimbo huo na taswira nzima iliyokuwa jukwaani. Baada ya sekunde kadhaa Veronika alishtuka na hakutaka kuonekana mshamba katika tukio hilo. Alionekana akitembea sambamba na Moses huku akiishika tai ya suti nadhifu aliyovaa kijana huo. Mara kadhaa Moses alionekana akimshika Veronika katika paji lake la uso huku akiimba kumwelezea uzuri wake ambao alisisitiza kuwa hakuwahi kuuona katika maisha yake.

    Jambo hilo lilikuwa kivutio na kusababisha watu wawapigie kelele za furaha. Warembo wengi pia walipiga kelele juu ya shoo hiyo lakini katika mioyo yao walikuwa wakiumia kumshuhudia msanii waliyekuwa wakimpenda akiwa anampenda mrembo kutoka Tanzania.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya dakika tano Moses alimaliza kuimba wimbo huo uliojaa hisia za mahusiano, alionekana akikumbatiana na Veronika kwa muda mrefu huku wakipigiwa kelele za kila aina na watu waliofika katika tamasha hilo. Mwishoe waliondoka jukwaani hapo wakitumia mlango aliopandia Moses jukwaani. Walitembea huku Moses akiwa amemshika vizuri Veronika mkono wake wa kushoto. Waliongoza mpaka nje ya ukumbi huo, huko walimkuta Craig akiwasubiri huku akiwa na kibegi cha Veronika. Wakati huo Moses alikuwa hajaongea jambo huku Veronika naye akiwa mtulivu , Craig alimpa Moses ufunguo wa gari lake kabla ya kumkabidhi Veronika kibegi chake pia. Moses na Veronika walipanda katika gari aina ya Ferarri lililokuwa limeegeshwa eneo hilo na Moses aliliondoa kwa kasi.

    Huo ulikuwa mwanzo wa ukurasa ambao Veronika hakuupanga kabisa kwani mara kadhaa alikuwa akimwaza Rashid kijana aliyekuwa na uhusiano naye miaka kadhaa iliyokuwa imepita wakati akiwa Tanzania.



    Huo ulikuwa mwanzo wa ukurasa ambao Veronika hakuupanga kabisa kwani mara kadhaa alikuwa akimwaza Rashid kijana aliyekuwa na uhusiano naye miaka kadhaa iliyokuwa imepita wakati akiwa Tanzania. Siku hiyo alienda kulala katika nyumba aliyopanga Moses iliyokuwa katika kitongoji cha Caxton. Aligundua mambo mengi kutoka kwa kijana huyo aliyekuwa raia wa Marekani akitokea katika jimbo la Illinois. Familia ya kijana huyo ilikuwa ikimiliki kampuni kubwa ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya meli. Uwezo wa kifedha wa familia hiyo ndio uliodhihirisha hata tabia ya Moses ambaye alikuwa akipenda sana muziki na mambo mengine ya starehe. Uthibitisho wa jambo hilo ulitokana pia na shahada ya muziki na filamu ambayo alikuwa akiichukua katika chuo kikuu hicho cha Cambridge.

    Mambo yalibadilika chuoni na Veronika hakutaka kuwa mbali kabisa na Moses Malcolm ambaye ghafla alikuwa akimpenda kupindukia. Mara nyingi walikuwa wakitembea pamoja chuoni hapo huku kila mmoja akiwa na lengo la kumlinda mwenzake. Moses alikuwa akihofia uwezekano wa mpenzi wake huyo kuanza uhususiano na mtu mwingine kwa vile wanaume wengi walikuwa wakimfuatilia chuoni hapo. Veronika naye alikuwa akihofia jambo hilo pia kwani toka aanze uhusiano na Moses hata marafiki aliokuwa nao walipungua huku wakionesha dhahiri kuumia juu ya uhusiano wa wawili hao.

    Siku moja kama ilivyokuwa kawaida ya Moses, majira ya mchana alimpitia Veronika katika idara yao ya masomo ya biashara. Waliondoka wote wakielekea katika mgahawa wa chuo huku wakitumia gari la Moses aina ya Ferarri. Baada ya dakika kumi walionekana wakiendelea kula chakula katika mgahawa mmoja wa chuo. Walikuwa wamekaa katika meza moja ndogo huku wakitazamana katika nyuso zao. Mara kadhaa walionekana wakionegea mambo yao. Hatimaye walimaliza zoezi hilo la kula chakula na walionekana wakiendelea kunywa vinywaji laini vilivyobakia katika meza zao. Ni wakati ambao Moses alimsogelea vizuri Veronika usoni kabla ya kumuuliza swali.

    “you know I love you aah!, please my dear I beg your promise… will you marry me?”

    ( Unajua nakupenda, tafadhari naomba uniahidi utaolewa na mimi). Veronika alitulia kidogo bila kujibu swali hilo huku akionesha mshtuko. Alikuwa ametoa macho akimwangalia mwanamke mmoja ambaye alikuwa na kamera umbali wa mita kadhaa toka eneo walilokuwa wamekaa. Mwanamke huyo tayari alikuwa amewapiga picha moja akiwa na Moses eneo hilo na zaidi wakati huo alikuwa ameficha sura yake. Akiwa katika wimbi la mawazo na shauku za ghafla juu ya mwanamke huyo mwafrika alikuwa ameanza kuhisi jambo. Mwanamke huyo aliyemwona alimfananisha na mwalimu wake aliyewahi kumfundisha kwa miaka yote ya shule ya msingi wakati akisomea nyumbani kwao. Baada ya kumwona akijificha, Veronika alirudisha haraka kichwa chake katika paji la uso la Moses huku akijifanya hamwoni mwanamke huyo aliyewapiga picha. Wakati huo Moses ambaye alikuwa haelewi jambo lililokuwa likiendelea alimuuliza tena swali lake Veronika ambaye wakati huo alimjibu “Don’t worry Moses I will marry you because I adore you” (usijali Moses nitaolewa na wewe kwa sababu nakupenda na kukuheshimu) Veronika aliongea hayo huku akiwa makini kumchunguza mwanamke ambaye alihisi alikuwa akimfahamu.

    Moses alifurahi kusikia jibu hilo ambalo alilihitaji, alimsogelea zaidi Veronika na kumbusu katika paji lake la uso. Wakati akifanya jambo hilo Veronika alimshuhudia mwanamke aliyekuwa akimhofia akinyanyuka na kuwapiga picha haraka kabla ya kuanza kuondoka katika mgahawa huo. Mwanga uliotoka kwenye kamera ya mwanamke huyo ulimshtua hata Moses ambaye aliungana na Veronika kumwangalia mwanamke aliyewapiga picha ambaye alikuwa akizamia nje ya mgahawa huo. “ she is following us” ( anatufuatilia ) alisikika Veronika kabla ya kusiamama haraka na kuanza kutembea akielekea nje ambako mwanamke huyo alizamia. Nyuma yake alifuatwa na Moses ambaye pia alitembea haraka.

    Mara baada ya kutoka nje waliishuhudia tesksi moja ya kukodishwa ikiondolewa kwa kasi eneo hilo. Veronika alikuwa na shauku ya kuwafuata watu hao lakini Moses alimtuliza akimwambia jambo hilo ni la kawaida na alihisi mtu aliyewapiga picha alikuwa mwandishi wa jarida la chuo hicho. Veronika alitulia lakini alianza kujenga hisia zake juu ya jambo jipya. Alihisi uwezekano wa baba yake kuendelea kumfuatilia akiwa chuoni hapo. Alimini jambo hilo kwa vile mwanamke aliyekuwa akimpiga picha alitambua aliwahi kumfundisha nyumbani kwao miaka mingi iliyokuwa imepita. Moses alimrudisha Veronika katika kitivo chake cha masomo ya biashara ambako wanafunzi wa shahada yake ya biashara na masoko walikuwa wakisomea. Majira ya jioni kama ilivyokuwa kawaida yake Moses tena alienda kumchukua Veronika na kumpeleka katika hosteli alizokuwa akiishi zilizokuwapo kitongoji cha Harningsea.

    Maisha yao ya mahusiano yaliendelea huku Veronika akiwa hajali kumbukumbu zake juu ya mwanamke aliyekuwa akiwafuatilia. Wakati huo alikuwa tayari kwa lolote ambalo baba yake angeweza kuamua mara baada ya kusikia alikuwa katika mahusiano. Jambo alilolitambua aliamini tayari alikuwa mwanamke mkubwa wa kuweza kuwa na maamuzi sahihi juu ya maisha yake. Wakati huo pia akiwa katika uhusiano wake huo hakuacha kumkumbuka Rashid kijana aliyekuwa moyoni mwake kwa miaka mingi kabla ya kukutana na Moses. Mara kadhaa alikuwa akiangalia picha za kijana huyo alizomchorwa miaka ya nyuma ambazo zilikuwa zimechakaa sana. Moyoni alikuwa akiumia kila alipomfikiria kijana huyo lakini alikosa njia yeyote ya kutambua kama alikuwa hai au la! Jambo hilo ndilo lilimfanya aanze kufikiria kuwatafuta wanafunzi waliokuwa wakisoma sanaa ya uchoraji chuoni hapo ili wamchore. Aliwaza jambo hilo kwa vile aliipenda sana sanaa hiyo toka akiwa kidato cha tatu baada ya kuchorwa na Rashid katika shule ya sekondari ya St. Mary.

    Siku moja ya Ijumaa ikiwa ni mwisho wa masomo ya wiki nzima, Veronika alionekana akimsubiri Moses nje ya geti kuu la chuo hicho. Siku hiyo alipanga kwenda kulala nyumbani kwa mpenzi wake huyo katika kitongoji cha Caxton. Alikuwa amechoka sana kutokana na mitihani kadhaa aliyokuwa ameifanya katika juma hilo na aliamini sehemu pekee ya kupumzika na kusahau karaha zote za juma zima ilikuwa nyumbani kwa Moses ambaye alikuwa ameshamwambia juu ya jambo hilo.

    Wakati akiwa amekaa katika viti kadhaa nje ya geti hilo alikuwa ameinama huku akiwa anawaza mambo tofauti. Baada ya dakika kadhaa alisikia mngurumo wa gari likitoka katika geti kuu la chuo hicho, alibaki ametulia na hakuinuka. Ghafla alisikia kelele za mtu akionekana kuwaita watu waliokuwa katika gari hilo lililokuwa limetoka katika geti hilo huku likielekea barabara kuu.” Hey! Joe Joe Please wait….. wait for me Joe ( tafadhari Joe nisubiri…. Nisubiri Joe ). Kelele hizo zilimshtua Veronika ambaye alinyanyua kichwa chake na kumshuhudia kijana mmoja upande wa mgongoni kwake akilikimbilia gari aina ya Land Cruiser ambalo liliegeshwa kando kidogo ya barabara kuu. Kijana huyo aliyekuwa amebeba faili mkononi alimfanya Veronika atabasamu kabla ya kuishia kucheka. Alikuwa amefurahishwa na jinsi ambavyo kijana huyo alikuwa akikimbia kama vile alikuwa mchekeshaji. Ghafla Veronika alishtuka kidogo, jambo hilo lilifuata baada ya kuona karatasi moja likiruka kabla ya kuanza kupeperuka kuelekea eneo alilokuwao.

    Kijana huyo aliyekuwa akikimbia hakugundua jambo hilo na aliishia kuingia kwenye gari hilo aina ya Land Cruiser ihali karatasi yake ikiishia kugota miguuni mwa Veronika huku likipulizwa na upepo kiasi uliokuwapo. Veronika alichukua haraka karatasi hilo kabla ya kuanza kuwaita watu waliokuwa kwenye gari hilo ili kijana aliyeangusha karatasi hiyo arudi kuichukua. Aliita mara kadhaa kwa uvivu kutokana na njaa aliyokuwa nayo na mwishoe aliamua kutulia na kukaa tena chini baada ya kulishuhudia gari hilo likiondolewa kwa kasi katika eneo hilo. Alitulia kidogo kabla ya kuhitaji kuona karatasi hiyo ilikuwa na nini? Aliinyanyua na kuielekeza kwenye paji lake la uso ili aione vizuri. Mara baada ya kufanya hivyo alipata mshtuko ambao hakuwahi kuupata kwa muda mrefu katika maisha yake. Karatasi hiyo ilikuwa na picha yake iliyochorwa vizuri sana kwa mkono, picha hiyo ilimkumbusha kijana ambaye alikuwa akimwazia kila siku, Rashid ambaye ndiye pekee aliwahi kumchora kama alivyo katika maisha yake. Wakati akiwa na shauku ya kuichunguza vizuri picha hiyo aliyaona maandishi yaliyoandikwa chini katika picha hiyo ambayo alihitaji kuyasoma. `My Lost Face` (Uso Wangu Uliopotea) yalikuwa maandishi yaliyoandikwa chini ya picha hiyo na alipoichunguza vizuri alimalizia furaha aliyoipoteza kwa muda mrefu katika maisha yake. Picha hiyo iliandikwa jina la mchoraji kwa maandishi madogo yaliyoandikwa Rashid Kagu. Veronika alipiga kelele katika eneo hilo alilokuwapo huku akilitaja jina la Rashid kama mchumba wake. Wakati akiendelea kuwa katika furaha hiyo alilishuhudia gari la Moses kwa mbali likijongea eneo hilo la chuo. Akili yake ilifanya kazi haraka na moyoni aliamua kuvunja uhusiano wake na Moses rasmi, hakuwa tayari kuwa naye wakati alishagundua kuwa Rashid alikuwapo chuoni hapo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikimbia haraka na kwenda kujificha katika maua marefu yaliyokuwapo eneo hilo huku akiwa hana mpango na Moses tena. Wakati akifanya jambo hilo kuna wanafunzi kadhaa walikuwa wakitoka katika geti kuu, walioneka na wakicheka kuona Veronika akikimbia na walisimama nje ya geti hilo kabla ya kuanza kutoa maneno ya kejeli. Baada ya sekunde kadhaa Moses aliegesha gari lake nje ya geti hilo lakini hakumwona Veronika eneo hilo zaidi ya vijana ambao hakuelewa wakikuwa wakimkejeli nani. “hey! beautiful lady, why are you hiding, are you affraiding us?” ( wewe mrembo, kwa nini unafichama, unatuogopa?) alisikika kijana mmoja kati ya watatu waliokuwa wakimsema Veronika kwa kumkejeli. Moses hakujali juu ya jambo hilo alisogea kando kidogo akiwa na lengo la kumpgigia simu Veronika. Alifanya jambo hilo na baada ya muda mfupi simu ya Veronika ilianza kuita kutoka kwenye maua yaliyokuwa karibu na eneo hilo. Moses alishtuka na aliamua kuyasogelea maua hayo kabla ya kumwona mpenzi wake akihangaika kuitoa simu kutoka katika kibegi chake. Alimnyanyua na kumtoa eneo hilo.

    Wakati huo kelele za kejeli kutoka kwa vijana waliokuwepo eneo hilo zilizidi huku wakidai Veronika alikuwa akimfichama asionane na mchumba wake. “whats the matter here” ( kuna nini hapa ) aliuliza Moses huku akielekeza mkono wake kulichukua karatasi ambalo Veronika alikuwa amelishika mkononi. Wakati hayo yakiendelea Veronika alikuwa akitetemeka kuhofia jambo. Moses aliliinua karatasi hilo kabla ya kuishuhudia sura ya mpenzi wake ikiwa imchorwa vizuri. “ ok!.... My Lost Face…. Rashid Kagu…. He loves you aah he is your boyfriend…. Is that true?” (“sawa…. Uso wangu uliopotea….. Rashid Kagu….. anakupenda aah ni mpenzi wako…. Si ndiyo”) Moses aliuliza kwa hasira akiwa amemkazia macho Veronika ambaye hakujibu zaidi ya kuendelea kutetemeka. Hatimaye kwa kasi ya ajabu Moses aliichana picha hiyo katika vipande viwili tofauti kabla ya kuitupa. Wakati huo aliibua hasira za Veronika aliyeudhika na jambo hilo, haraka aliviokota vipande hivyo vya karatasi hiyo ililokuwa na picha yake kabla ya kuanza kurudi nyuma akiwa na lengo la kuondoka. “ I don’t love you any more its over….you don’t know even the value of this picture aah… leave me alone” (“sikupendi tena tuishie hapo…. Hujui hata thamani ya hii picha aah… niache peke yangu”)

    Alianza kutembea haraka akielekea barabarani, Moses akiwa amechanganyikiwa alianza kumfuata nyuma huku akijaribu kumtuliza Veronika ambaye hakumsikiliza. Alisimama barabarani kwa sekunde kadhaa akiwa na Moses aliyekuwa akimbembeleza kabla ya kuishia kupanda teksi aliyoisimamisha.

    Hakuwa na huruma hata kidogo juu ya kijana huyo zaidi ya hasira kutokana na kuchanwa kwa picha yake. Siku zote alikuwa akiziheshimu picha za Rashid na hakupendelea mtu awe anaziangalia. Yeye peke yake ndiye alikuwa akiziangalia kwa muda wa miaka kadhaa na tayari zilikuwa zimechakaa sana. Kitendo cha Moses kuichana picha hiyo aliyoiokota siku hiyo kilimuudhi sana. Alimweleza dereva wa gari hilo aelekee katika kitongoji cha Harningsea ambako kulikuwa na hosteli alizokuwa akiishi Veronika. Baada ya dakika arobaini na tano Veronika alionekana akitembea taratibu kuelekea katika chumba chake huku akiwa ameiunganisha picha yake iliyokuwa katika vipande viwili ilhali akiiangalia kwa makini.

    Hakumwazia tena Moses na akilini alikuwa akiwaza jinsi ambavyo angeweza kumpata Rashid. Hata mara baada ya kuingia katika chumba chake alijipumzisha kitandani na kuendelea kuiangalia picha hiyo huku akikumbuka mambo mengi juu ya Rashid. Baada ya muda mfupi wa kuwapo chumbani kwake alisikia mlango wa chumba hicho ukigongwa. Alishuka taratibu kitandani na kutembea mpaka katika mlango huo ambao hakuufungua zaidi ya kumwangalia mtu aliyekuwa akiugonga kwa kutumia lensi iliyokuwa kwenye mlango huo. Haikuchukua muda kumgundua mtu aliyekuwa nje ya chumba hicho, kwani hakuwa mwingine zaidi ya Moses aliyeonekana kukosa amani. Veronika hakutishika juu ya jambo hilo na taratibu alirudi katika kitanda chake na kujipumzisha. Hakuwa tayari kuendeleza uhusiano na kijana huyo na zaidi aliamini kwa kufanya hivyo angekuwa anamdanganya kwani upendo wake alishaurudisha kwa Rashid kijana aliyekuwa akimpenda kwa muda mrefu. Moses aligonga kwa nguvu mlango wa chumba hicho cha Veronika lakini mrembo huyo hakuongea jambo na wala hakuthubutu kuufungua mlango huo. Mara kadhaa alisikika akimwomba msamaha Veronika lakini hakusikilizwa. Baada ya dakika kadhaa aliamua kumpigia simu, zilipita sekunde kadhaa kabla ya simu ya Veronika kuanza kuita kwa mlio ambao alikuwa akiutumia katika simu yake.

    Simu ya Veronika iliita ilhali Moses akiisikia kuwa ilikuwa inaita lakini mrembo huyo hakuthubutu kufungua mlango wa chumba chake wala kuipokea simu hiyo. Wakati huo alikuwa kitandani kwake akiendelea kuangalia picha za Rashid ambazo nyingine alipewa miaka kadhaa wakati akiwa Tanzania. Moses alikaa nje ya mlango wa chumba hicho kwa muda wa saa sita na mwishoe aliamua kuondoka huku akiwa ameudhika kupindukia. Kichwani alikuwa ametawaliwa na jina la Rashid Kagu ambaye aliamini alikuwa amechangia kuvunjika kwa uhusiano wake na Veronika.

    Akiwa na furaha siku iliyofuata Veronika aliamka mapema na kuanza kufikiri jinsi ambavyo angeweza kukutana na Rashid, hakumhofia Moses kwa fedha zake na umaarufu aliokuwa nao hata kidogo. Alijiamini pia kutokana na fedha nyingi alizokuwa nazo katika akaunti ya benki ambazo hakuwahi kuzitumia kwa jambo lolote na hakuna mtu aliyekuwa akijua kama alikuwa akitokea katika familia ya Lamos Maputo, tajiri mkubwa nchini Tanzania ambaye jina lake halikuwa geni katika nchi nyingi za Afrika. Majira ya saa tano asubuhi aliondoka katika chumba chake huku akiwa na lengo la kwenda chuoni ili kumpeleza Rashid. Alitambua sehemu ya kwenda kuanzia jambo hilo. Alipanga kwenda kukutana na wakuu wa idara ya sanaa ya chuo hicho kwa vile aliamini Rashid lazima alikuwa akisomea sanaa ya uchoraji chuoni hapo.





    Alitambua sehemu ya kwenda kuanzia jambo hilo. Alipanga kwenda kukutana na wakuu wa idara ya sanaa ya chuo hicho kwa vile aliamini Rashid lazima alikuwa akisomea sanaa ya uchoraji chuoni hapo.

    Hakupata shida katika jambo hilo kwani alipofika chuoni hapo alipewa ushirikiano wa kutosha na wakuu wa idara ya sanaa ambao walihisi Veronika alikuwa ndugu yake Rashid kwa vile aliwaeleza kuwa alikuwa akitokea Tanzania. Uwezo wake kitaaluma katika shahada aliyokuwa akiichukua ndio uliosaidia wakuu wa idara hiyo waweze kupata taarifa za kutosha kuhusu Rashid. Alikuwa akiishi katika hosteli za chuo zilizokuwapo katika kitongoji cha Dullingham. Wakuu wa idara hiyo walimpatia pia namba ya chumba cha kijana huyo na mwishoe Veronika aliondoka akiwa na lengo la kwenda katika kitongoji cha Dullingham kilichopo mashariki mwa mji wa Cambridge. Alitumia usafiri wa treni na baada ya nusu saa alikuwapo katika kitongoji hicho lakini alikumbana na tatizo moja dogo.

    Rashid hakuwepo katika chumba chake katika hosteli zilizokuwepo katika kitongoji hicho. Alikuwa amebandika kikaratasi chenye ujumbe mfupi akiwaeleza wageni wake kuwa mapumziko ya mwisho wa juma hilo alisafiri kuelekea katika jimbo la Liverpool na alidai angerudi siku ya Jumapili. Tangazo hilo lilimuumiza sana Veronika lakini alipata faraja kwa kiasi kikubwa kutokana na kuhakikisha uwepo wa Rashid katika chuo hicho. Aliamua kurudi katika hosteli za Harningsea alikokuwa akiishi huku akiamini angekutana na Rashid chuoni siku ya Jumatatu. Majira ya saa moja na nusu jioni wakati akifika katika chumba chake aliiona kadi kubwa iliyokuwa imepitishwa chini ya mlango. Alipoichunguza tu kwa haraka aligundua kadi hiyo ilikuwa imetoka kwa Moses. Aligundua jambo hilo kwa vile alikuwa akiutambua vizuri mwandiko wa kijana huyo.

    Jambo alilo lifanya aliitupa kadi hiyo katika ndoo maalumu kwa ajili ya taka bila kuisoma. Hakuwa tayari kurudi nyuma na kumfikiria Moses. Aliamini kwa kufanya hivyo angemwekea mazingira magumu sana kijana huyo kwa sababu hakufikiria kuolewa tena na Moses. Mara kadhaa alipofikiria sababu iliyomfanya aanzishe uhusiano na Moses aligundua jambo moja. Alifanya jambo hilo kwa sababu alijihisi yuko tofauti na wanawake wengine na zaidi hakuwahi kuwa karibu na wanaume katika maisha yake.

    Siku ya Jumatatu ikiwa ni mwanzo wa juma, katika chuo kikuu cha Cambridge kulikuwa na pilikapilika za watu chuoni hapo kama ilivyokuwa kawaida katika siku hiyo ya kwanza ya juma. Majira hayo ya saa saba mchana, ukiwa ni wakati wa chakula cha mchana, Veronika alionekana akitembea taratibu akielekea eneo lililokuwa na majengo ya wanafunzi waliosoma sanaa. Akilini alikuwa ametawaliwa na jina la Rashid pamoja na sura ya kijana huyo aliyoiona miaka mingi iliyokuwa imepita. Huku akitembea akiwa na mawazo hayo tele hakuangalia hata nyuma ambako Moses akiwa na rafiki yake Craig walionekana wakimfuatilia huku wakijificha mara kadhaa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Veronika alitembea haraka mpaka katika madarasa ambayo wakuu wa idara hiyo walimweleza siku mbili zilizopita kuwa yalikuwa yakitumiwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza. Aliyapitia madara hayo kadhaa pasipo kufanikiwa kumwona Rashid na mwishoe alianza kukata tamaa kwa vile njaa ilimuuma huku akiwa amechoka baada ya kuwepo darasani kwa muda mrefu. Hatimaye alionekana akifungua mlango wa darasa ambalo lilikuwa la mwisho kati ya madarasa aliyoelezwa kuwa yalitumika na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo. Aliufungua mlango huo taratibu kabla ya kushtuka kuona taswira ya chumba hicho. Kulikuwa na wanafunzi wakike kadhaa pamoja na wengine wachache wa kiume. Mshtuko wake uliongezeka alipomwona kijana mmoja ambaye alionekana akiendelea na sanaa yake ya uchoraji.

    Kijana huyo alikuwa akimwona mgongoni na alikuwa ameinamia meza yake huku akimchora mrembo mmoja aliyekuwa amekaa mbele yake. Watu wengine walionekana wakindelea kumsifiwa kijana huyo ambaye alikuwa akichora na mara kadhaa wasichana waliokuwapo katika chumba hicho walimshika mabega mchoraji huyo huku wakimsifia. Baada ya kutulia kwa sekunde kadhaa akiangalia taswira ya chumba hicho Veronika alianza kutembea taratibu akilisogelea eneo hilo na sauti ya viatu vyake ndiyo iliyokuwa ikisikika. Watu waliokuwapo katika chumba hicho walionekana wakimwangalia lakini hakujali na akilia yake ilikuwa mbali huku akiamini sekunde chache ndizo zilibakia ili atimize ndoto zake za muda mrefu.

    Hatimaye aliwafikia na kusimama nyuma ya Rashid aliyekuwa anaendelea kumchora msichana aliyekuwa mbele yake. Alitulia kidogo bila kufanya jambo lolote, watu waliokuwa katika chumba hicho walikuwa wakimshangaa huku wakiwa kimya na zaidi hawakutambua jambo lililokuwa linaendelea. “ Rashid nimekuja kwa ajili yako……” alisikika Veronika na kuwafanya watu waliokuwa katika chumba hicho wamshangae zaidi kwani hawakufahamu lugha aliyokuwa akiongea. Rashid alitulia kidogo na kuacha kuchora kabla ya kusikika “who is that?,,,,” ( “ni nani huyo” ).

    Hakuna mtu aliyemjibu swali hilo zaidi ya vicheko vilivyotoka kwa wenzake na mwishoe aliamua kusimama kabla ya kuanza kugeuka taratibu. Kelele ndizo zilichukua nafasi baada ya Rashid kugeuka na kumwona Veronika, walikumbatiana kwa nguvu na kwa muda mrefu huku kila mmoja wao akilia. Jambo hilo liliwashangaza wanafunzi waliokuwa katika chumba hicho ambao hawakuelewa lolote.

    Wakati huo Moses na Craig walikuwa wameingia katika chumba hicho na walishuhudia tukio hilo ambalo lilimuuma sana Moses aliyeamua kutoka katika chumba hicho na baada ya sekunde kadhaa Craig naye alitoka akihofia kuonwa na Veronika. “naamini ndoto zangu zimekamilika, siku zote nilikuwa nikiishi mpweke kwa sababu nilikuwa na imani ya kukutana tena na wewe Veronika, nakupenda sana” alisikika Rashid ambaye alikuwa amemshika Veronika mashavu yake yaliyolowa machozi kwa furaha. “nakupeda pia Rashid sijawahi kukusahau katika maisha yangu…. Nakupenda sana” alisikika Veronika akijibu huku akiwa na furaha. “Jamani kuna jambo moja mnapaswa kujua huyu ndiye mchumba wangu”. Rashid aliwafahamisha wenzake kwa kimombo. Kauli hiyo ilipokelewa vizuri na wanafunzi wa kiume ambao mara nyingi walikuwa hawaelewi kwa nini rafiki yao hakuwa karibu na wasichana chuoni hapo. Jambo hilo liliwafanya wanafunzi hao wa kiume washangilie juu ya kauli hiyo. Haikuwa hivyo kwa wasichana ambao waliichukia kauli hiyo kwa vile walikuwa na imani kuweza kumpata kijana huyo siku moja.

    Huku nyuso zao zikiwa hazina furaha walimpongeza Rashid kwa shingo upande. Msichana aliyekuwa anachorwa alipandwa na hasira kuondoka akitembea kwa haraka katika chumba hicho. Aliumia kuona Rashid, kijana mtanashati akiwa na uhusiano na msichana mwingine ambaye pia alikuwa mrembo haswa. Rashid hakujali jambo hilo zaidi aliwaaga rafiki zake kabla ya kuondoka na Veronika wakiwa na furaha. Hawakuwaza kuendelea na masomo tena kwa siku hiyo. Waliongozana huku wakiwa wameshikana mikono mpaka katika kituo cha treni, walikuwa wakiwaza kuelekea katika kitongoji cha Dullingham ambako kulikuwa na hosteli za chuo kikuu cha Cambridge. Hosteli hizo ndizo alizokuwa akiishi Rashid, baada ya nusu saa walionekana wakitoka katika kituo cha treni cha kitongoji cha Dullingham ikiwa ni baada ya kusafiri kwa dakika ishirini.

    Waliongoza mpaka katika chumba cha Rashid ambako Veronika alivutiwa na mandhari ya chumba hicho ambacho kilikuwa kimepambwa na picha za kuchorwa za watu wanne, moja ilikuwa picha yake na nyingine ilikuwa ya mzee mmoja ambaye kwa jinsi alivyomwona alikuwa akifanana na Rashid. Kulikuwa na picha nyingine ya mwanamke na mwanaume ambao kwa kuziangalia aligundua picha hizo zilikuwa za wazazi wa Rashid. Mara baada ya kutulia kwa muda mfupi Veronika alitaka kujua sababu iliyofanya wakapotezana miaka mingi iliyokuwa imepita. Jambo hilo lilimuumiza sana Rashid ambaye alijikaza na kuanza kumsimulia mchumba wake huyo.

    Alimweleza sababu ya kuacha shule ghafla wakati akiwa katika shule ya kimataifa ya St. Mary iliyopo jijini Dar es salaam. Sababu hiyo ilimuumiza Veronika pia kwa vile alimweleza wazazi wake walipata ajali mbaya na kufariki wakati wakiwa safarini kuelekea mkoani Morogoro. Ajali hiyo iliyotokea maeneo ya Kibaha ilikuwa ya gari dogo la kutembelea lililokuwa la kikazi ambalo baba yake alipewa na wizara ya nishati na madini ambayo alikuwa akifanya kazi. Ajali hiyo ilitokea wakati baba yake akiwa na siku chache toka aanze kufanya kazi. Hivyo wazazi wake walifariki huku wakiwa hawajaacha kitu chochote cha kumsaidia Rashid kimaisha hata malipo ya ada lilikuwa jambo ambalo alikosa ndugu wa kuweza kumsaidia.

    Rashid alirudishwa wizara hiyo kwao mkoani Morogoro na vitu kadhaa ambavyo vilikuwa nyumba ya wizara waliyokuwa wakiishi awali. Akiwa na majonzi alienda kuungana na babu yake mzee Kagu aliyekuwa akiishi mkoani humo ambaye pia alikuwa akiumia juu ya kifo cha mwanaye kila siku. Rashid alifanikiwa kujiunga na shule ya sekondari ya Morogoro na kumaliza kidato cha nne. Vitu vyote walivyoviacha wazazi wake ziliuzwa na ndivyo vilimsaidia katika malipo ya ada. Rashid alirudi tena katika shule hiyo na kumalizia kidato cha tano na cha sita. Wakati akiwa kidato cha sita alishiriki katika shindano la uchoraji lililokuwa limeandaliwa na shirika la kimataifa la wanawake na watoto, shindano hilo lilihitaji wachoraji kutoka nchi tofauti duniani kuchora maisha ambayo watoto na wanawake walikuwa wakiishi katika kambi za wakimbizi. Rashid alishiriki vyema katika shindano hilo huku akitumia michoro ya picha kuelezea jinsi ambavyo wanawake hubakwa na askari katika kambi za wakimbizi zaidi michoro yake ilitoa taswira nzima ya maisha ya wakimbizi ambao mara kadhaa walikuwa wakifa kwa njaa.

    Rashid alifanikiwa kuwa mshindi kati ya washindi wa tatu wa shindano hilo na zawadi aliyoichagua alihitaji kusomeshwa chuo kikuu na shirika hilo. Alisikilizwa ombi lake kabla ya kutafutiwa chuo hicho cha Cambridge. Veronika akiwa na huzuni juu ya maisha aliyopitia Rashid alimpa pole wakati ambao alikuwa amekaa pembeni yake huku akiwa amemwegamia kijana huyo. Walibaki kimya katika wakati ambao Rashid bado alikuwa akitafakari juu ya maisha yake aliyopitia kwa vile mambo mengi alimficha Veronika akihofia kumuumiza. Kwa miaka mingi akiwa Tanzania jambo la kulala njaa lilikuwa la kawaida kwake kutokana na ugumu wa maisha aliyokuwa akiishi. Wakiwa bado wamekaa pamoja ilisikika sauti ya mtu akigonga mlango wa chumba cha Rashid. Jambo hilo lilimfanya ajitoe kwa Veronika aliyekuwa amemwegamia kabla ya kuanza kutembea taratibu kuelekea mlangoni.

    Mara baada ya kuufungua mlango huo alishtushwa na taswira aliyoiona nje ya chumba chake. Kulikuwa na vijana kadhaa wakiwa na wamevaa vinyago katika nyuso zao. Alipojaribu kuufunga mlango huo alishindwa kwa vile vijana hao waliusukuma kwa pamoja kabla ya kufanikiwa kuingia ndani. Rashid alirudi haraka na kwenda kusimama mbele ya Veronika huku akionekana kama alitaka kumzuia na hatari iliyokuwa ikifuata. Wakati huo Veronika alikuwa amesimama huku akitetemeka baada ya kuwaona vijana hao waliokuwa watano wakiwa katika harakati za kufanya jambo.

    “Hey! Rafiki nakuona, unapendeza na mwanamke wetu” Mmoja wa wale jamaa alimwambia kwa kimombo. Rashid akaja juu.

    “Mwanamke wenu? Ni upumbavu gani unaoongea…. Huyu ni wangu na sikufahamu”.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "mwanamke wenu? Ni upumbavu gani unaoongea…. Huyu ni wangu na sikufahamu”.

    Kijana aliyekuwa akiongea na Rashid alimsogelea kwa kasi kabla ya kumpiga ngumi usoni iliyompeka mpaka chini. Veronika alipiga kelele juu ya jambo hilo kabla ya kumfuata Rashid eneo alilokuwa ameangukia huku akiwa anatokwa damu mdomoni. Akiwa na hasira alisimama na kumfuata kijana aliyempiga Rashid akiwa na lengo la kumgipa. Aliporusha mkono wake huku akilia alidakwa kirahisi na kijana huyo ambaye alimkamata mikono miwili kabla ya kumkonyeza kijana mwingine aliyekuwa kando yake.

    Kijana aliyekonyezwa alimsogelea na kumkamata Veronika sawasawa. Baada ya jambo hilo kuchukua nafasi vijana hao wengine walimsogelea Rashid ambaye alikuwa ameanza kusimama katika eneo alilokuwapo. Walianza kumpiga kwa zamu kila eneo la mwili wake huku wakimtukana na kumkejeli kwamba hakufaa kuwa na Veronika. Wakati jambo hilo lilo likiendendelea Veronika alikuwa akipiga kelele kuwasihi wamwache Rashid lakini hawakufanya hivyo. Alipojaribu kujitoa kwa kijana aliyemshika alishidwa kwa vile alikuwa amemshika sawasawa.

    Baada ya dakika tano walimwacha Rashid akiwa amelala chini katika eneo walilokuwa wakimpiga huku kukiwa na kiasi kikubwa cha damu iliyotapakaa eneo hilo. Wakati vijana hao wakiondoka kwa kasi eneo hilo Veronika alimkimbilia Rashid na kumkumbatia huku akilia. Alikuwa akilitaja jina la Moses ambaye aliamini alikuwa akihusika na jambo hilo.

    Mara baada kumkumbatia Rashid kwa sekunde kadhaa alitoka akikimbia katika chumba hicho akiwa na lengo la kuomba msaada. Aliongoza mpaka katika chumba cha pili kilichofuatana na cha Rashid ambako aligonga. Alifunguliwa mlango na kijana mmoja ambaye alipoelezwa juu ya tukio hilo la kuvamiwa kwa Rashid alishtuka kwa vile alikuwa rafiki yake. Aliwaita wenzie kadhaa na walishilikiana kwa pamoja kumwahisha Rashid katika hospitali iliyokuwepo katika hosteli hizo. Muda wote wakati zoezi hilo likiendelea Veronika alikuwa akilia huku akielewa jambo hilo lilikuwa limeafanywa na Moses. Mara baada ya kupokelewa Rashid, walikaa nje ya chumba maalumu ambacho alikuwa akifanyiwa matibabu na daktari waliyemkuta.

    Baada ya saa moja zoezi hilo lilikamilika huku akiwa ameshonwa sehemu tatu tofauti ikiwa ni pamoja na jeraha alilolipata usoni. Wakati akitoka katika chumba alichokuwa akifanyiwa matibabu hayo alipokelewa kwa kukumbatiwa na Veronika. Rashid alionekana kuudhika na zoezi la kupigwa lililokuwa limetokea, “pole Rashid, sijapenda juu ya jambo hili lililotokea ila nitakueleza kila kitu” “ usijali…” alijibiwa na mchumba wake huyo. Daktari wa hospitali ya hosteli hizo alimwambia Rashid aendelee kuwepo hospitalini hapo lakini hakukubaliana na jambo hilo, hakutaka kukaa hospitali hapo kwa wakati huo ingawaje alikuwa na maumivu sehemu tofauti za mwili wake.

    Mara baada ya kutoka hosptitalini hapo Rashid hakutaka kulala katika hosteli hizo pia, alikuwa amekosa amani kabisa. Alimweleza Veronika waongozane kuelekea kwa mtanzania mmoja ambaye Rashid alimchukulia kama ndugu yake. Mtanzania huyo alikuwa akiishi katika kitongoji hicho cha Dullingham, kilometa kadhaa kutoka katika hosteli hizo za chuo. Veronika aliamua kukodi teksi na safari ilianza kuelekea kwa mtanzania huyo ambaye Rashid aliongea naye kuwa angekuwa mgeni wake siku hiyo. Wakati wakiwa njiani, Veronika alimweleza Rashid juu ya uhusiano wake wa awali ambao alikuwa nao na Moses. Alimweleza pia hisia zake za kuamini kijana huyo ndiye aliyekuwa akihusika na jambo hilo lililokuwa limetokea.

    Baada ya nusu saa walifika katika eneo alilokuwa akiishi mtanzania huyo. Mara baada ya teski waliyokuwa wamekodi kuegeshwa mbele ya nyumba hiyo, Rashid alishuka taratibu huku akisaidiwa na Veronika, dereva wa teksi hiyo alilipwa malipo yake kabla ya kuondoka. Walianza kutembea taratibu kuelekea katika nyumba hiyo huku wakiwa watulivu. Mara baada ya kuufikia mlango wa nyumba hiyo waliugonga na baada ya sekunde kadhaa mwenyeji wao alisikika akitembea kwenda kuufungua, hatimaye alitekeleza jambo hilo. “mwalimu… mwalimu Jane haa..!” alisikika akipiga kelele Veronika kwa mshangao mara baada ya mlango huo kufunguliwa. “haa wewe umefikaje hapa, mh! Umekuja kunipeleleza nini? Eeh!” alisikika mwanamke huyo ambaye kwa wastani alikuwa na umri wa miaka therathini na tano. “Vero, kwani mnafahamiana na huyu mama” aliuliza Rashid “ndiyo Rashid amewahi kuwa mwalimu wangu”

    Wakati akiendelea kuwakaribisha alionesha ishara za dharau dhidi ya Veronika ambaye aliwahi kumfundisha miaka kadhaa iliyopita wakati wakiwa Tanzania. Mwanamke huyo aliwakaribisha ndani ya nyumba yake huku akionesha kuhoji maswali mengi juu ya jambo lililokuwa limetokea mpaka Rashid akawa na majeraha mengi mwilini. “tutakueleza jambo lililotokea lakini kabla ya yote naomba uniambie sababu ya kunipiga picha na kukimbia wakati nikiwa chuo” aliongea hayo Veronika mara baada ya kukaa katika kochi lililokuwapo kwenye nyumba hiyo. Aliuliza swali hilo kwa vile alikumbuka siku kadhaa zilizokuwa zimepita alipigwa picha na mtu aliyemfananisha na mwanamke huyo wakati akiwa katika mgahawa wa chuo na Moses. Mwanamke huyo alicheka kidogo kabla ya kusikika “ haa! We unafikiri upuuzi unaoufanya na Moses, baba yako anaupenda?”. Rashid na Veronika walitazamana baada ya kusikika maneno hayo.

    Veronika alionekana kuudhiuka juu ya jambo hilo na alichukua simu yake akiwa na lengo la kumpigia simu baba yake. Wakati akiendelea na zoezi hilo Rashid alimzuia akiwa na lengo la kufanya jambo. Tayari wakati huo simu ya bwana Lamos Maputo, aliyekuwa baba yake Veronika ilikuwa inaita. Huku akiwa ameelekeza simu yake katika sikio lake la kulia alionekana akipumua kwa taabu huku akiwa na jazba. Rashid aliendelea kumwoneshea ishara Veronika atulie na asimweleze jambo baba yake. Baada ya sekunde kadhaa wakati simu hiyo ikiendelea kuita, Veronika alielewa jambo hilo. Mara baada ya kupokelewa simu na baba yake, Veronika aliongea naye kawaida kama alivyokuwa akifanya siku nyingine.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-

    Alipomaliza maongezi hayo na baba yake, Rashid alimgeukia Bi. Jane kabla ya kuanza kumsisitizia mwanamke huyo kuwa asijaribu kuzituma picha hizo kwa Bwana Lamos Maputo. Walimshawishi mwanamke huyo kwa dakika kadhaa pasipo kuelewa, baada ya muda mrefu wa zoezi hilo alikubaliana na ombi hilo kabla ya kuwaahidi kuwa asingetuma picha hizo kwa baba yake Veronika ambaye alimtuma nchini humo, Uingereza ili kumfuatilia mwanaye. Jambo ambalo lilikuwa likiwakosesha jibu ni jinsi ambavyo bwana Maputo alikuwa akimfuatilia mwanaye. Rashid alikumbuka kipigo alichowahi kupata kutoka kwa tajiri huyo miaka kadhaa iliyokuwa imepita wakati akiwa katika sekondari ya St. Mary jijini Dar es salaam, jambo hilo lilimfanya amwogope sana tajiri huyo. Aliamini kama picha alizopigwa Veronika na Moses zingetumwa kwa bwana Maputo basi angeweza kumkosa pia mchumba wake huyo aliyekuwa akimpenda kwa miaka mingi.

    Mbali na makubaliano ya kutoa fedha ambazo Veronika alimwahidi bi. Jane kumpa iwapo asingetoa taarifa yeyote kwa baba yake au kumtumia picha zinazohusu mahusiano yake, kuna jambo lilikuwa mawazoni mwa mwanamke huyo. Alikubali kutomtumia picha bwana Lamos Maputo kutokana na ukweli kwamba alimsikiliza Rashid. Alikuwa akimpenda sana kijana huyo ambaye hakubahatika kumweleza hisia zake hata siku moja. Wakati huo alikuwa na mtoto mmoja ambaye alimwacha Tanzania na awali aliwahi kuolewa na mwanamume mmoja ambaye waliachana miaka kadhaa iliyokuwa imepita huku wakiwa na huyo mtoto mmoja. Toka wakati huo Bi. Jane aliyependa maisha ya ujana sana alikuwa akitembea na watu tofauti akiwa nchini Tanzania. Hakubahatika kuendeleza tabia yake hiyo akiwa nchini Uingereza na alipanga kuhakikisha kumpata Rashid akiwa nchini humo. Jambo hilo ndilo lilichangia akubali kutotuma picha za Veronika kwa vile alikuwa akimpenda sana kijana huyo na alikuwa hajatambua kuwa Rashid alikuwa na uhusiano na Veronika kwa wakati huo.

    Rashid alihisi jambo toka kwa Bi. Jane na aliamua kumweleza pia Veronika juu ya hisia zake kuwa mwanamke huyo alikuwa anampenda. Alimweleza ukweli huo kwa vile alikataa kuzituma picha baada ya kubembelezwa sana na Rashid na zaidi alionesha ishara tofauti machoni mwake zilizo ashiria jambo. Waliamua kuishi kama marafiki mbele ya Bi. Jane kwani waliamini kama mwanamke huyo angegundua kuwa walikuwa na uhusiano jambo hilo lingempa hasira na angezituma picha hizo kwa bwana. Lamos Maputo, nchini Tanzania.

    Wakati huo Veronika alihama hosteli alizokuwa akiishi za Harningsea na kwenda kupanga nyumba kubwa katika kitongoji cha Yelling. Rashid naye alihama katika hosteli zake za Dullingham na kwenda kuungana na Veronika katika nyumba aliyopanga. Maisha waliyokuwa wakiishi huko yalikuwa kama mke na mume huku kila mmoja wao akimfurahia mwenzie. Ni wakati ambao walihisi ndoto zao za muda mrefu zilikuwa zimekamilika wakiwa nchini humo. Veronika ambaye alikuwa akiishi kama vile hakuwa mtoto wa tajiri mkubwa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, wakati huo alionesha uwezo wake kifedha. Alikuwa amepanga katika nyumba iliyokuwa ya ghari sana huku ikiwa na ulinzi wa kutosha, zaidi wakati huo alinunua gari aina ya Ferrari ambalo walikuwa wakilitumia na Rashid kwenda chuo kila siku.

    Alikuwa ametumia kiasi kidogo cha fedha zake kati ya nyingi ambazo siku zote baba yake alikuwa akimtumia kwenye akaunti yake ya benki. Wakati huo Moses ambaye alikuwa katika jaribio la kuvunja uhusiano wa Veronika na Rashid alipata maswali mengi juu ya mabadiliko ya ghafla waliyokuwa nayo watu hao. Jambo hilo lilimfanya ampeleleze zaidi Veronika kabla ya kuja kugundua kuwa alikuwa ni mtoto wa tajiri mkubwa bwana. Lamos Maputo ambaye alikuwa akitokea Afrika. Jambo hilo lilimfanya Moses aanze kufikiria zoezi jingine la kufanya ili kuhakikisha anampata Veronika ambaye siku zote alijiapiza kuwa hangekubali kuona mwanamke huyo anaolewa na mtu mwingine.

    Siku zilisogea hatimaye ulifika ambao chuo kilikuwa kikifungwa ikiwa ni mwisho wa masomo ya mwaka wa kwanza kwa Veronika. Wakati huo ilikuwa mwezi wa kumi na mbili na Veronika aliwaza kurudi nchini Tanzania ili kusherekea sikukuu za mwisho wa mwaka akiwa na baba yake kabla ya kurudi tena shule kwa ajili ya masomo ya mwaka wa pili. Rashid hakuwaza kurudi Tanzania kwa wakati huo kwa vile alikuwa amebahatika kupata nafasi ya kuchora katuni katika gazeti la The Sun lichapishwalo kila siku nchini humo.

    Hakuwaza kurudi nchini ambako alimwacha babu yake pekee aliyekuwa akiishi mkoani Morogoro ambaye siku zote alikuwa akimtumia fedha za kujikimu kimaisha. Veronika alionesha kuikumbuka sana Tanzania na alikata tiketi yake ya ndege mapema katika shirika la Ethiopian Airlines. Tahehe nane ya mwezi huo wa kumi na mbili majira ya kumi na mbili jioni, Rashid alionekana akiendesha gari lao aina ya Ferrari huku akiingia katika geti kuu la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Heathrow uliopo jijini London. Mara baada ya kuingia katika uwanja huo, Rashid alionekana akimsaidia Veronika kubeba mabegi yake na alimsindikiza mpaka sehemu ambayo mizigo ilikuwa ikipokelewa, hatimaye waliagana kwa kukumbatiana kwa muda mrefu kabla ya Veronika kuanza kufuata taratibu za uwanjani hapo. Baada ya nusu Veronika alikuwa katika siti yake aliyokuwa ameilipia katika ndege hiyo, eneo hilo alilopaswa kukaa alimwona kijana mmoja katika siti iliyofuatana naye ambaye alikuwa ameshakaa. Kijana huyo aliyekuwa amevaa kofia, alijifunika koti lake kichwani na Veronika aliamini alikuwa amelala. Hakujali juu ya jambo hilo na alibaki mtulivu katika siti yake huku akisubiria safari hiyo iianze.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA





0 comments:

Post a Comment

Blog