Simulizi : Hatia
Sehemu Ya Pili (2)
“Shiit!!! Nimeacha mguu wangu ndani ya gari!!!” John alijisonya baada ya kugundua amesahau bunduki yake garini, haukuwa utaratibu wake kutembea bila silaha. Lakini hakujisumbua kusimama na kuifuata. Kauli hiyo ilizidi kumtetemesha Michael.
Ina maana ndio amekuja kunifichulia maovu yangu na kuniua hapahapa!!!! Mungu wangu, lakini nilimwambia Matha kila siku kuwa ananitia matatani ona sasa!!! Aah!! Ona sasa Matha!! Aliwaza Michael kwa uchungu na kuzitupa lawama kwa Matha kabla John hajaendelea kuzungumza
“Eeeh!! Umeuliza kuwa nina maana gani, ujue Michael kuna wakati unafika lazima kila ukweli uwe wazi na uamuzi ufanyike mara moja, na uamuzi mgumu ni ule unaomuumiza aliyeuamua!!!” John aliendelea Michael akawa kimya, alikuwa amekodoa macho funda la mate alilotaka kumeza ni kama lilikuwa linataka kumshinda, koromeo lilionekana kuwa dogo lakini akajilazimisha likapita.
“Michael nakupenda sana lakini………” hakuweza kuendelea John muhudumu akawa amefika na vinywaji, akawafungulia , Michael akapiga mafunda mawili kulainisha koo lake, John hakupiga funda lolote bali alitia kiasi fulani kwenye glasi yake, wakati muhudumu huyu anaondoka kupisha faragha ya Michael na John, muhudumu wa kiume kutoka jikoni naye akafika kuwasikiliza.
Paja la mbuzi, weka pilipili, tenganisha sahani, ndizi nne zikaushe vizuri, mwambie huyu aongeze bia. Ni baadhi ya maneno mengi waliyozungumza na hatimaye mada ikawa imesahaulika!!! John hakuendelea na maelezo. Simu aliyopigiwa na Bruno ikawa imeingilia kati.
Michael akapata ahueni!!
*******
Joyce Keto alionekana kuwa kikwazo pekee kwa John Mapulu katika mipango yake ya kujipanga upya katika shughuli zake. Alitambua ni kiasi gani wasichana ni dhaifu. Hivyo kuwa mikononi mwake lilikuwa jambo salama sana.
Iwapo Joyce angetiwa mikononi mwa polisi, lazima angesema lolote analojua kuhusu Michael hali ambayo ingemuweka matatani Michael, kijana ambaye ametokea kushibana naye.
Sasa Joyce alikuwa mikononi mwake katika nyumba ya mafichoni nje kidogo ya mji wa Mwanza. Kama ilivyokuwa kwa Michael. Joyce naye alijazwa chuki na kujihisi yupo hatiani. Hasahasa baada ya kuelezwa kuwa Michael anakabiliwa na kesi ya mauaji.
“Kuonekana kwako tu pale kituoni..unatafutwa sasa ukasaidie upelelezi. Maana Michael alitoroka.” John alimwogopesha Joyce. Kisha akamalizia kwa kumueleza juu ya Michael kumkimbia.
“Kwa hiyo mlivyotoroka, amekutoroka na wewe.”
John akakubali kwa kutikisa kichwa juu na chini.
Sumu pandikizi ikapenya katika akili ya Joyce. Akawa mtumwa wa kifikra.,
Uhusiano wa kimapenzi ambao Joyce alimueleza John kati yake na Michael haswa ndio ulimfanya John asipendezwe na kitendo cha wawili hao kukutana mapema. Alihofia kusalitiwa. Hivyo alijionya kuwa muangalifu sana.
Akaamua kumuweka Joyce mbali na Michael hadi wakati stahili utakapowadia.
KILICHOJIRI BAADA YA WATUHUMIWA KUTOROKA
Askari wa zamu usiku wa tukio la mauaji na kutoroka mahabusu wa kituo kikuu cha polisi wapatao kumi kwa kulinda maisha yao waliificha siri ya kutoroka kwa mahabusu wanne katika mazingira tatanishi. Pia mauaji ya askari usiku huo huo. Kwa uzembe huo kama wangethubutu kubaki, kifungo cha maisha ilikuwa halali yao kwani watuhumiwa wote wanne waliofanikiwa kutoroka walikuwa wanahusika na mauaji, John akiwa mkongwe anayefahamika kwa kesi hizo, Michael akiwa amesingiziwa lakini ushahidi ukimuhitaji sana kwa upelelezi na wengine wawili wakiwa na kesi ya kuiba na kuua kwa kutumia bunduki.
Kwa watuhumiwa wa kesi nzito kama hizo ni nani angepona kwa kusema kuwa hajui wanne wametoroka toroka vipi??? Bila kushirikishana lakini kila mmoja akijua lake moyoni, wanne kati yao wakaamua kutoroka wawili wakajiua na wanne waliojisalimisha wakaanza kusota rumande na baadaye gerezani Butimba kwa kesi ya kuwasaidia mahabusu kutoroka pia kuhusika katika kuua askari mmoja. Wema waliodhani ni silaha ukawa umewaponza, upelelezi unaendelea ndio kauli pekee iliyosalia wakati wanazidi kuteketea mahabusu. Mmoja baada ya mwingine wakaanza kupoteza maisha kutokana na mateso makali na msongo wa mawazo huku wengine wakigeuzwa wake za watu angali walikuwa mahabusu.
Akabakia askari mmoja huyo alikuja kutoka kwa msamaha wa raisi miezi miwili baadaye baada ya kesi yake kukosa ushahidi wa kutosha, huyu aliweza kuona na kutembea kama aliyekamilika lakini hakuwa na uwezo tena wa kuzaa, mateso aliyopitia tayari yalikuwa yamemvuruga uzazi lakini kubwa zaidi ni kuingiliwa kimwili mara kadhaa na wafungwa wazoefu wakati yupo gerezani akisubiri hukumu yake. Hakurudishwa kazini baada ya msamaha hakuwa na vigezo tena. Uaskari wake ukawa umeishia katika simulizi mbaya na ya kuumiza kama hiyo. Huyu aliyepona aliyebahatika kurejea uraiani alikuwa ni Sajenti Kindo Malugu, hakuwa sajenti tena alibakia kuwa mzee Malugu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku chache kabla ya kukamatwa kwake alipokea taarifa ya mwanae mpendwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, ni baada ya kukumbana na unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa baba yake mdogo aliyekuwa amechukua jukumu la kumlea baada ya mzee Kindo kuhamishwa kikazi kutoka Singida na kuhamishiwa Mwanza.
Baada ya mwanae huyo wa pekee wa kike aliyezungukwa na wenzake wawili wa kiume ambao walikuwa wameathirika na matumizi ya madawa ya kulevya ndio kwanza alikuwa amejitahidi na kumaliza kidato cha sita.
Hakuwa tayari kuolewa bali alitaka kundelea na masomo yake ya chuo kikuu. Mateso, kejeli na dharau kubwa kutoka kwa baba yake mdogo pamoja na mkewe zilikuwa zimemsukuma kutoroka katika mji huo na kwenda mahali alipopajua mwenyewe. Baada ya kupata taarifa hiyo mzee Kindo alinuia kuchukua ruhusa na kurejea nyumbani kushughulikia suala hilo, halikuwa suala dogo hata kidogo ile ilikuwa ni damu yake inatangatanga. Lakini akiwa katika kusubiri ruhusa yake ipitishwe ndipo linatokea tukio la mauaji katika nyumba ya kulala wageni jijini Mwanza.
Hakuwa mmoja kati ya askari walioenda kwenye tukio kwani alikuwa anahangaikia ruhusa lakini alikuwa ni yeye aliyeandika maelezo mafupi ya awali kuhusu mali alizonazo mtuhumiwa kwa wakati ule yaani PPR baada ya Michael kukamatwa. Ruhusa ilizidi kumchelewesha hadi linapotokea tatizo jingine kubwa la kuuwawa kwa askari aliyekuwa lindoni na kutoroka kwa watuhumiwa wanne wa kesi za mauaji, hata siku hii pia alichelewa sana kuingia kazini kwani suala la ruhusa yake lilikuwa bado gumu. Siku hiyo alikuwa zamu, hivyo alikuwa anahusika katika kujibu kitakachoulizwa.
Mwanzoni alikubaliana na wenzake kuhusu kutoroka lakini alipompigia mkewe simu na kumuomba ushauri alipinga vikali na kumsihi asijaribu kutoroka kwani alikuwa na mtihani mwingine wa kumtafuta mwanae je angeuweza vipi huu mtihani wakati asingekuwa huru tena??? Maneno hayo makali yaliyosindikizwa na kilio kisha meseji kadhaa za kumsisitiza asifanye alichokusudia zilibadili mawazo ya Sajenti Kindo, yeye pamoja na askari wengine watatu wakajisalimisha, siku hiyo ndiyo ilikuwa ya mwisho kwake kuwa huru hadi alipotoka kwa msamaha wa raisi.
“Vua gwanda, vua mkanda, saa na hiyo kofia” haya yalikuwa maneno yaliyowaamrisha siku wanaingia mahabusu, ilikuwa kama utani lakini miaka miwili ikathibitisha si utani ule.
“Mwanangu Joyce, sijui alipatikana???” ni swali la kwanza alilojiuliza mzee huyu, punde tu baada ya kuambiwa yuko huru.
“Poti!! Poti!!....” Kindo alisikia sauti ikimuita wakati akiondoka katika mahakama hiyo ambapo alikuwa amemaliza hatua zote za kuachiwa huru kutokana na msamaha wa Raisi, hakugeuka mara moja kwani aliamini kuwa si yeye aliyekuwa anaitwa. Sauti ile ilipoendelea kusisitiza alisimama na kugeuka. Sura haikuwa ngeni sana machoni mwake lakini hakutaka kuonyesha dalili zozote za kuikumbuka sura hiyo.
“Poti!! Pole sana kaka….nafurahi kukuona mtaani tena dah!! Ya Mungu mengi” mtu huyo mfupi mnene aliyekuwa ananyemelewa na kitambi alizungumza kwa furaha.
“Sijakukumbuka ujue!!!” Kindo alinyanyua mdomo wake na kuzungumza. Bwana yule alifuta tabasamu lake usoni na kuvaa huzuni alimsikitikia Kindo kwani aliamini ni maisha ya kukosa uhuru yalikuwa yamemsababishia hali hiyo ya kukosa kumbukumbu.
“Kura tumekura pakurara je!!!!” badala ya kujibu alitoa kauli hiyo, Sajenti Kindo akashtuka sana kisha akamkumbatia kwa nguvu zake zote mzee huyo, machozi yakawa urembo katika nyuso za wawili hawa.
“Poti Magembe ni wewe kaka???” aliuliza Kindo pasipo kuamini macho yake.
“Ni mimi poti!!! Pole sana kaka, tuliumia sana kukupoteza uraiani” alizungumza kwa huzuni huku akimkagua Kindo kwa macho jinsi alivyozeeka ghafla ndani ya miezi ishirini na nne (24). Walizungumza mengi wakiwa wamesimama wima, Kindo bado alikuwa mkakamavu kiasi licha ya masumbufu ya maisha ya mahabusu bado alikuwa imara. Walikumbushana mengi sana yakiwemo maisha yao ya uaskari tangu wakutane Singida na baadaye Kindo akahamishwa kwenda Mwanza.
“Vipi na wewe ulihamishwa nini??” aliuliza Kindo.
“Ndio hivyo kaka, yaani baada ya wewe kutupwa huko ndani wiki mbili baadaye nikahamishiwa hapa, hivyo niliipata stori yako punde tu baada ya kuhamia hapa. Mazungumzo yalikuwa mengi sana lakini hasahasa kumbukumbu ndio zilitawala.
“Poti hapa nilipo ni kama nashuhudia muujiza nimeachiwa, sina kazi nimefukuzwa tayari, hapa nilikuwa natembea kwenda nisipopajua nashukuru nimekuona, huu mji ninauchukia sana nahitaji sana kurudi nyumbani kwangu huko Singida hapa Mwanza hapana, ngoja nirudi nyumbani…lakini poti!! Mi hapa sina hata nauli, tusizungumzie njaa ninayoisikia hapa hii nitaivumilia…suala ni nauli” alijieleza Kindo kwa sauti ya chini. Magembe akawa amemuelewa.
Kitu cha kwanza walipata chakula ambacho Kindo hakikukifurahia sana, baada ya hapo wakaelekea nyumbani kwa Magembe maeneo ya National housing. Alipumzika kwa siku mbili pale wakati Magembe akihangaika huku na huko hatimaye akapata kiasi cha pesa akampatia Surgent Kindo, akashukuru akaaga na kuondoka.
Siku iliyofuata akaiacha ardhi ya Mwanza.
*****
Maongezi kati ya Michael na John yaliendelea baada ya John kumaliza mazungumzo yake kwenye simu na Bruno mazungumzo yaliyochukua takribani nusu saa huku John akizungumza kwa makini na utulivu asiweze kusikiwa na mtu yeyote. Hali hiyo ilizidi kumtia Michael katika jitimai la nafsi. John aliporejea mezani tayari huduma kutoka jikoni ilikuwa tayari, wakaanza kula na kunywa baada ya hamu kuanza kuwaisha ndipo maongezi yakaendelea.
“Michael naamini una ukaribu flani na Matha!!!” John alisema, lilikuwa shambulizi kubwa sana lililomzidi ujanja Michael akayumba kimawazo lakini hakuanguka, wasiwasi wake ulikuwa wazi sana lakini bahati ilikuwa kwake kwani John alikuwa ameinama akichezea vipande vya mifupa vilivyosalia katika sahani.
“Ndio kwa sasa nipo naye karibu tofauti na mwanzo wakati sijamzoea” alijaribu kujibu mashambulizi Michael.
“Unamchukuliaje kwa jinsi alivyo sasa na kipindi cha nyuma”
Mimba!! Mimba!! Mimba!! Kengere za hatari zililia kichwani mwake.
“Sijaona mabadiliko sana” alijibu huku akiwaza juu ya uwezekano wa swali hilo kuhusisha mimba.
“Michael natamani sana ungejua ni kiasi gani mimi nampenda Matha na nilivyohangaika naye hadi hapa tulipo, ungelijua hilo nadhani ungenionea huruma” aliongea kwa huzuni sana John. Michael akaanza kutetemeka miguu alitamani amtumie ujumbe Matha lakini alihofia huenda tayari simu yake ipo mikononi mwa John hivyo kwa kitendo cha kutuma ujumbe angeongeza maradufu hasira za John.
“Michael Msombe!!!! Nisaidie kitu kimoja tu!! Naamini unakiweza”
“Ni kipi hicho??”
“Unapafahamu kwa Matha??”
Mtego!!!! Alishtuka Michael
“Hapana sipafahamu, sijawahi kwenda” alidanganya Michael kwani aliwahi kukitumia kitanda cha Matha kwa masaa kadhaa kufanya mapenzi na binti huyu mpenzi wa John Mapulu. John alimtazama Michael usoni kwa muda huku akiwa kama anasoma kitu fulani.
“Ok!! Nitakuelekeza….au nitakupeleka…nahitaji msaada wako, wewe ni mwanaume kama mimi” alizungumza John, pombe ilikuwa kidogo imemchangamsha.
“Nimekuelewa kaka” alijibu huku akimeza funda la bia na kukunja sura yake ili kuupokea ukali wake tumboni.
Kimya kikuu kilitawala kwa muda kila mtu alikuwa anawaza na kutenda la kwake hadi walipomaliza na kulipia huduma walizofanyiwa kisha wakaondoka baada ya kuwa wamechukua makopo kadhaa yaliyojazwa bia.
“Endesha!!!!” John alimwomba Michael.
“Sina uzoefu na hizi left hand kaka” alijitetea Michael.
“Ah!! Madereva wa VETA na nyie mna matatizo kweli” alitania John huku akiingia katika kiti cha dereva, safari nyingine ikaanza. Muziki wa hip hop ndio ulitawala ndani ya gari, John aliweza kuimba mistari aliyoifahamu na Michael akijiumauma pale anapoweza hadi gari iliposimama maeneo ya Buzuruga jirani na stendi ya mabasi yaendayo mikoani, ni ya pili kwa ukubwa baada ya ile ya Nyegezi.
“Unaona lile ghorofa pale, acha hilo linalomeremeta hiyo ni bar, hili la pembeni yake, chumba cha tatu juu, hapo ndipo anakaa Matha, fanya kama surprise sawa” alielekeza John.
“Sasa naenda kufanya nini???” aliuliza Michael. John alijigongesha kichwa chake katika usukani na kusababisha gari ipige honi isiyo na maana, John alikuwa anajishangaa kwani alikuwa hajampa maelekezo yoyote yale Michael.
“Dah!! Mapenzi haya, ok!! Michael kwa maneno yako yote yaliyo kichwani naomba ukamweleze Matha kuwa ninammpenda sana” John alisema kisha akatulia kidogo.
“Najua hakuna rafiki yangu mwingine ambaye ataeleweka kwa Matha lakini wewe naamini atakuelewa, naamini hivyo Michael” John akatulia akamwangalia Michael, macho yake yalikuwa mekundu sana dalili zote za kutaka kulia.
“Ni kitu gani simpi mimi?? Najua amepata kimwanaume kinamzuzua lakini mwambie akumbuke tulipotoka!!!!” alishindwa kuendelea akaanza kulia, Michael akashuka garini akaupunga mkono ishara ya kuaga na kutokomea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Michael aliamini yupo katika mtego mkubwa kuliko yote maishani mwake, suala la kuagizwa usiku wa saa tano kwenda nyumbani kwa Matha aliamini kuwa ni mpango wa kumtia katika hatia yenye ushahidi wa kutosha ili kuhalalisha hukumu yake. Alitamani sana kumpigia simu Matha lakini bado nafsi yake ilikuwa na mashaka.
“Hapana sipigi simu yoyote ile…nitawapa uhakika mapema sana” alizungumza peke yake. Akiwa na simu yake mkononi badala ya kumpigia Matha alimpigia John, simu yake ikawa inatumika. Akakata baada ya dakika tano John akapiga.
“Vipi mdogo wangu umepotea nini??”
“Umejuaje?? Umesema chumba namba??” alizuga Michael
“Namba tatu upande wa kulia, pembeni yake kuna jiko” alielekeza John baada ya kujilazimisha kucheka kidogo.
“Poa kaka nimeuona mlango, haya baadae” aliaga.
Kwa tahadhari kubwa sana aliufikia mlango, palikuwa kimya sana lakini hilo halikumtisha haikuwa mara ya kwanza kwenda mahali usiku, mara nyingi akiwasindikiza akina John huwa ni usiku. Mlango ulikuwa umerudishiwa kidogo bila shaka muhusika alikuwa hajalala bado. Michael aligonga mlango kwa utaratibu sana. Sauti kutoka usingizini ilimuuliza yeye ni nani hakujibu akausukuma mlango na kuingia ndani.
“Matha!!! U hali gani??”
“Michael!!!!” aliita kwa mshangao mkubwa Matha huku miguu yake tayari ikiwa sakafuni, mikono ikiyapikicha macho yake yaweze kupambana na giza lililokuwa limetanda.
“Upo na nani??”
“Peke yangu kwani vipi???” alihoji Matha kwa sauti ya chini sana huku akiuendea mshumaa na kuuwasha, chumba kikapata mwanga.
“Matha umemfanya nini John”
“Hamna kitu kwani vipi??”
“Una uhakika upo peke yako??”
“Nipo peke yangu jamani sasa haka kachumba na wewe huoni au??” alisema kwa ghadhabu kidogo.
“John ameanza kutushtukia” Michael alisema kisha akaelezea stori yote ya siku hiyo wakiwa na John, Matha alionekana msikivu sana na ambaye huenda angeuliza maswali mengi sana baada ya hiyo simulizi lakini haikuwa hivyo.
“Ujue Michael, huyu John huyu anataka kuchanganyikiwa yule John yule niachie mimi, wewe haumuwezi hata kidogo, yaani yule John….” Matha akiwa anayazungumza hayo alikuwa mbele ya Michael, akiyabinyabinya mabega yake, punde akawa amemkumbatia kabisa, joto kali kutoka kwa Matha, pombe alizokunywa Michael zikaungana kwa pamoja kumshabikia shetani, mapepo yakaruhusiwa kuamka Michael akawa ameagizwa na John kwenda kuzini na Matha, Michael akakisahau kilio cha mwanaume jasiri kama John. Michael akatumia masaa manne kumbembeleza Matha, wakaoga pamoja kwa mara ya kwanza. Walisahau hata mimba iliyokuwa inakua taratibu katika nyumba ya uzazi ya Matha.
“Mwambie John asante sana kwa zawadi eeh!!..mwambie awe anakuagiza kila siku tena usiku ndo inapendeza” Matha alimtania Michael wakati anaondoka. Michael akatikisa kichwa akatabasamu akaondoka. Tayari ilikuwa saa kumi adhuhuri. Kutoka Buzuruga kwenda Mecco ni mbali kiasi lakini Michael aliamua kutembea kwa miguu. Wakati akiwa kwa Matha hofu haikuwepo lakini alipokaribia Mecco, hofu ikamtwaa upya akaanza kumuogopa John, kitendo alichotoka kufanya na Matha kikamtia hatiani tena, hatia ikainyanyasa nafsi yake akaukosa uhuru wa nafsi.
“Hujalala mpaka sasa hivi kaka??” aliuliza Michael baada ya kumkuta John sebuleni akiwa macho anaangalia luninga.
“aaah!! Nilale wakati askari wangu hujarejea bwana!!!” alijibu kwa furaha John .
“Dah!! Nimekuja kwa miguu, si unajua tena daladala hazijaamka bado” alisema kwa utulivu huku naye akichukua nafasi.
“Mh!! Una mambo kaka, nadhani shughuli ilikuwa nzito sana”
“Aah!! Kiasi chake lakini kawaida”
“Si kawaida yaani hadi kufikia suala la kuoga si mchezo ati!!!” alisema John, kauli iliyovunjavunja ujasiri wa Michael, almanusura apige goti kuomba msamaha kwa aliyoyafanya muda mfupi uliopita lakini alisita akabaaki kushangaa.
“Mh!! Aaah!!! Umejuaje kaka” alijipa ujasiri wa bandia na kuuliza.
“Marashi gani ya Matha nisiyoyajua mimi???? Sabuni uliyotumia ni Candy na marashi ni Halloween uongo uongo!!!” alisema kwa utani John ili kumdhihirishia Michael kuwa anamfahamu Matha nje ndani.
“Dah!! Na Matha kanambia hivyo hivyo nikakataa kumuamini mh!! Mnajuana nyie watu si kitoto” alipata uongo wa kujibu Michael.
“Hah!! Matha kakwambia ehee ilikuwaje??” John alikaa vizuri aweze kumsikia Michael vyema.
“Siwawezi nyie…hamuwezi kuibiana kama mnajuana hivyo” alijibu pasipo imani hata kidogo kwani alijua kila kitu tayari John anajua. Michael hakuelewa kuwa kuendelea kusema uwongo ndio yupo sahihi ama auseme ukweli aujue mwisho wa mchezo.
“Nimezungumza na Matha, kwanza amestushwa na imani yako ndogo na amesema kesho niende anipe kitu nikuletee na amesema asante sana kwa Surprise!!!!!” alijilazimisha kufurahi Michael lakini hatia yake iliimeza furaha yote.
“Hata mimi kanitumia meseji!!! Kashtuka sana najua kukuona usiku huu??” aliongezea John. Michael bado hakuelewa kama John alikuwa hajashtukia kinachoendelea ama la!!!
“Vipi kesho muibukie basi au vipi, mi ntakutoa za viroba na nyama choma” kwa sauti iliyojaa ubembelezi John alimsihi Michael.
“Ngoja nikalale maana nimechoka mie, shem kanidekeza hadi nimeoga dah!! Sijui alijuaje kuwa sikuoga wakati natoka” Michael alisema, John akamuunga mkono kwa kicheko kikali cha furaha. Siku ikaisha hivyo tena walakini ukiwa bado umetawala.
Michael aliingia chumbani kwake, hakuamini kama siku hiyo inakatika bila John Mapulu kuusema ukweli wote juu ya uovu aliougundua dhidi yake. Usingizi ulimchukua mapema sana kutokana na uchovu na ulevi wa siku hiyo. Alijilazimisha kuwa na amani ilhali moyoni haikuwepo hata chembe. Michael aliamini kuwa alikuwa mtegoni.
“Mh!! Sijui kama patakucha salama!!” ni wazo la mwisho kichwani mwa Michael kabla hajapitiwa na usingizi mzito.
Majira ya saa nne asubuhi ndipo alishtuka kutoka usingizini lakini alitumia nusu saa nyingine kuuruhusu mwili wake ubanduke kitandani. Njaa ilikuwa inamuuma lakini hakuwa na hamu na kitu kingine zaidi ya supu. Hang over zilikuwa zimemtawala!!
“Oyo!! Huoni au mbwembwe tu!!!” sauti ya John ilimsimamisha Michael aliyekuwa anataka kutoka nje huku akipiga mluzi bila hata kutoa salamu. Michael alisimama na kumwangalia John kwa hofu.
“Ah! Sijakuona wala nini, nawaza tumbo tu hapa nataka nikarekebishe kiaina si unajua tena!!!” alijibu Michael huku akijiegemeza kwenye mlango ambao ulikuwa nusu wazi nusu umefungwa.
“Nilikuchukulia supu na chapati nenda ukacheki jikoni!!” John alimwambia Michael kwa sauti ya upole sana. Kengele za hatari zikalia kichwani mwa Michael. Sumu!!! Aliwaza mara moja kabla ya kushukuru na kujongea jikoni kwa ajili ya hicho alichohifadhiwa.
“Ukimaliza kula uniambie kuna jambo nahitaji tuzungumze!!” John alimwambia Michael ambaye aliupokea ujumbe huu akiwa anakaribia kulifikia jiko. Uoga ulikuwa umeitwaa nafsi yake, kila jambo alilofanyiwa na John alitia walakini ndani yake Hatia iliyokuwa inamkabili ndiyo ilimhangaisha. Kwa mwendo wa kunyata kama mwizi wa njiwa Michael alichukua kipande kidogo cha nyama iliyokuwa katika supu na kurushia paka aliyekuwa akifugwa hapo kwao. Paka alikitafuna kipande kile kwa shangwe zote hata kabla hakijatua chini vizuri kisha akajilambalamba ulimi na kutoa mlio wa nyauuu!!! Huku jicho lake likimtazama Michael kwa matamanio ya kupewa tena kipande cha nyama. Michael alisubiri kwa dakika kadhaa na yule paka naye akisubiri kuongezwa kipande kingine. Paka hakukumbwa na mushkeli yoyote ile. Chakula kilikuwa salama!! Michael alikuwa katika maisha ya mashaka sana!!
“Ah!! Kama ameniwekea sumu juu kwa juu bwana maisha gani haya ya wasiwasi? Bora nife!” alijisemea kwa sauti ya chini Michael huku akiivamia supu ile ambayo ilikuwa ya moto bado, hakujiandalia chakula mezani alimaliza kila kitu pale pale jikoni.
“Asante sana braza maana mh!!!” Michael akiwa na glasi ya maji ya kunywa baridi kabisa alimshukuru John.
“Hapo sasa safiiiiiii!!!!” alizungumza John kwa furaha.
“Ah!! Hapa hata nisipouona mchana poa tu” Michael alijibu huku akichukua nafasi yake katika sofa iliyokuwa ikiangaliana na sofa aliyokalia John.
“Michael nina zawadi yako nahitaji nikupe leo nadhani utafurahia”
“Zawadi kwa lipi kaka nililofanya”
“Jana umetumia muda wako mwingi sana kuzungumza na Matha nimeyaona mabadiliko leo mabadiliko makubwa nilikuwa na Matha asubuhi ya leo hapa!!” John alizungumza huku tabasamu likichanua katika mdomo wake.
“Aaah!! Amakweli leo nimelala sana”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa suala hilo nahitaji kukupongeza!!!”
“Usijali wewe ni kaka yangu” Michael alisema huku hasira zikiwa zimemtawala ndani ya nafsi yake pepo wa wivu akaanza kumtafuna taratibu, akaanza kuhisi Matha ni mali yake peke yake.
“Hata kama lakini unastahili zawadi” alisisitiza John. Michael hakupinga zaidi ya kukubali kwa shingo upande hiyo zawadi.
“Matha amekuja??? Muda gani na saa ngapi ameondoka?? Au mtego huu?? Eeh!! Mungu nisaidie” baada ya muda mrefu sana kupita Michael alikumbuka kupiga dua.
Au wananichora hawa kasha wanitoe kafara! Alijiuliza.
****
Hali ya utulivu ilitawala eneo hili la Nyegezi jirani kabisa na chuo kikuu cha mtakatifu Augustino maarufu kama SAUT. Pumzi na mapigo ya moyo ya wawili hawa yalisikika, mmoja akiwa anajiamini na mwingine akiwa ametekwa na uoga. Ilikuwa saa sita na nusu usiku, sauti za ndege wasiojua ubora wa nyimbo zao zilisikika kwa mbali na mara chache kuingiliwa na sauti mbaya za popo. Maumbo yao yalikuwa yanaendana walikuwa wamesimama kama vile kuna jambo flani walikuwa wanazungumza kwa siri kutokana na ukaribu wao.
Majira ya saa saba usiku mmoja alisogea na kujificha mahali na kumwacha mwenzake akivuta sigara na kupuliza moshi hewani. Michael alikuwa ameachwa na John eneo lile, uoga ulipitiliza kipimo hadi akaizoea hali ile kwa kuamini kuwa kama John angekuwa ameamua kumuua angeweza kufanya hivyo mapema na si lazima kutumia mbinu zote hizo. Lakini licha ya kujiaminisha sana, suala la kupewa zawadi eneo kama hili halikuwa la kawaida. Zawadi yangu ni kifo!!! Alijiuliza. Alitamani kumpigia simu Matha lakini akakumbuka alikuwa amepewa onyo kali juu ya kuwasha simu.
“Shika huu waya, nitakuamuru uuvute!!!!” John alimuelekeza Michael kwa sauti ya chini. Michael akatii. John akawasha sigara na kuanza kuvuta. Mara ghafla akamuamuru Michael kuuvuta ule waya hadi kwenye ki-mti kidogo kilichokuwa jirani kabisa na njia hiyo ya uchochoroni baada ya kuufunga waya huo Michael alisikia muziki kwa mbali ukizidi kusogea karibu. Kufumba na kufumbua Michael aliuzuia mdomo wake usiweze kupiga kelele. Pikipiki ilikuwa imeachana na dereva aliyekuwa anaiongoza kama hiyo haitoshi kichwa kilikuwa kinakaribia kuachana na kiwiliwili. John alikuwa ameua kwa kumtegea waya dereva wa pikipiki.
“Panda twende…” John alimwambia Michael ambaye bado alikuwa amezubaa asijue la kufanya. Kwa sauti kali ya John akawa amerejewa na ufahamu akapanda katika pikipiki.
“Bila shaka itakufaa kwa safari za hapa na pale, kifo hiki kinanikumbusha enzi hizo naanza maisha ya ujambazi!!” John alizungumza kwa sauti ya juu ili Michael aweze kumsikia, hakuwa na wasiwasi hata kidogo. Michael hakujibu kitu.
Mnamo saa nane na nusu kila mmoja alikuwa amejichukulia nafasi katika sebule kubwa kabisa. Michael hakuwa na amani lakini John alikuwa mzoefu sana.
“Zawadi yangu!!!!!! Oooops!!! Nilikuwa nimesahau” John alikumbuka zawadi aliyoahidiwa na Matha kupitia Michael.
“Mh!! Hiyo mpaka pakuche tena” alijibu Michael.
“Hapana twende hiyo pikipiki ina mafuta ya kutosha” alitoa hoja John, Michael kwa kumuhofia John akakubali.
Mwendo wa dakika kumi tayari walikuwa Buzuluga. Kama kawaida John akamwacha Michael aende mwenyewe. Siku hii hakukaa sana alirejea na bahasha na kumpatia John kisha wakaondoka kurudi nyumbani. Ilikuwa ni nguo ya ndani ya kiume!!
Asubuhi sana aliwasili mtu asiyefahamika machoni pa Michael alikuwa maalum kwa ajili ya kubadilisha namba za pikipiki ile. Zoezi lilifanyika kwa umakini na kufikia jioni John kwa uhuru wote alitoka na pikipiki ile nje akiyapita kama hayaoni magazeti yanayozungumzia kifo cha muendesha bodaboda mitaa ya Nyegezi.
John alifika nyumbani kwa Matha majira ya saa tatu usiku baada ya mizunguko mingi ya kujaribu ubora wa pikipiki ile.
Matha alitegemea ujio huo hivyo chumba kilikuwa kinanukia sana kutokana na maandalizi ya uhakika. John alipokelewa kwa upendo wa hali ya juu sana, mabusu kadhaa ya hapa na pale yalikonga sana nyoyo zao lakini hasahasa John aliyekuwa hana la kusema mbele ya Matha.
“Nakupenda Jo!!”
“Sina la kusema nadhani unajua kuwa nakupenda”
“Asante sana” alisema Matha kinafiki, huku akijua fika ana hatia ya kumsaliti John tena kwa mtu wake wa karibu Michael. Matha alimkaribisha mezani John ili wapate kwa pamoja chakula alichokuwa amekiandaa. Walijumuika kwa pamoja na baada ya hapo wakahamishia mashambulizi kitandani. John alikuwa anampenda sana Matha!!.
Vurugu hizo zilitwaliwa na usingizi baadaye hadi John alipokuja kushtuka alfajiri. Alikuwa na miadi mida ya saa nne hivyo alivaa nguo zake bila hata kuoga kwani hapakuwa na choo wala bafu la ndani kwa ndani katika chumba cha Matha.
“Mh!! Kuoga usioge yaani na Suruali unavaa hiyo hiyo??”
“He! Sasa nitavaa ipi nyingine?? Unaota nini!!”
“Subiri” Matha alisema huku akiinuka kizembezembe, umbo lake zuri lilijihifadhi katika nguo hii ya kulalia John alipatwa na matamanio wakati Matha amegeukia upande wa kabati, John hakujua ni nini anatafuta mawazo yake yote yalikuwa katika maungo ya Matha.
“Mh!! Na wewe kunichungulia tu loh!! Mwanaume huna haya wewe, usiku mzima hujaridhika tu!!” alitania Matha na kumkurupua John aliyezuga kwa kucheka. Matha alimshangaza John kwa kumpatia suruali ambayo ilimkaa na kumpendeza vyema.
“Asante mke wangu!!!” alishukuru John na kisha akahamishia vitu kadhaa kutoka katika suruali aliyoivua na kuvitia katika hii aliyokua ameivaa.
“Umenipatia hadi kiuno” alisifu John huku akijitazama. Matha akajibu kwa tabasamu. Baada ya kujitathmini akambusu Matha katika papi za midomo yake na kuondoka. Pikipiki bado ilikuwa na mafuta ya kutosha. John alipofika nyumbani aliingia moja kwa moja bafuni akaoga kisha akavaa suruali aliyopewa na Matha na juu akaweka shati jingine halafu akachomekea, uchaguzi wa kiatu ukamshinda akaamua kuvaa viatu vya wazi. Tayari ilikuwa saa mbili na nusu asubuhi. Michael alikuwa hajaamka bado, Bruno ndiye aliamka kumfungulia geti John kisha akalala tena hivyo hata wakati (John) alipokuwa anatoka hakuweza kumsikia tena. Wakati huu alitoka na gari ndogo Toyota Corolla. John alikuwa anawahi miadi ya kwenda kuzungumza na wenzake juu ya ‘dili’ la kuvamia mahali.
****
Kituo cha mafuta kilichopo maeneo ya Miti mirefu karibu na shule ya sekondari ya Pamba ndipo John alijijengea mazoea ya kwenda kujaza mafuta hivyo alikuwa anafahamiana na wafanyakazi wengi wa pale. Siku hii pia alikwenda na gari yake hadi katika kituo hicho. Alichangamkiwa na muhudumu ambaye pia alikuwa anamfahamu japo hawakuwa karibu sana.
“Weka ya elfu thelathini” aliamuru John huku akimkabidhi pesa kijana huyo aliyeonekana kutamani sana mazoea na John lakini ikawa inashindikana, John alikuwa bize sana na simu yake. Baada ya kuhudumiwa John alimpatia kijana huyo shilingi elfu tano kama malipo ya uchangamfu wake (bakhishishi) tangu John anafika hapo.
“Akhsante sana bosi”
“Kwa heri” aliaga John.
John alikuwa wa mwisho kuingia katika mkutano huo wa siri, ulikuwa ni mkutano wa watu sita wakiwa na lengo la kuvamia na kupora katika Supermarket ya Imalaseko jijini Mwanza, mpango ulikuwa umewekwa tayari kabisa kilichokuwa kimebakia ni kutekeleza. Kikao kiliendeshwa kwa sauti za chini sana katika hotel ya Mwanza (New Mwanza Hotel). Wakati kikao kinaendelea simu ya John iliyokuwa katika mlio wa kimya (silent mode) iliita, ilikuwa namba mpya John akapuuzia. Ikaita tena kwa mara ya pili na ya tatu hadi ya nne.
“Naingia uwani dakika sifuri” aliomba ruhusa John.
“Uwahi kurudi” mwenyekiti wa kikao alijibu.
Alipofika chooni simu iliita tena.
“We nani??” aliuliza kwa jazba John
“Samahani bosi….”
“Nimeuliza wewe nani??” aliendelea kusihi
“Bosi ni mimi Minja, wa hapa sheli”
“Tatizo!!”
“Bosi kuna kikadi cha hospitali hapa nadhani kilikuwa katika pesa zako ulizolipia hapa”
“Kikadi gani, sidhani kama ni mimi” alipinga John
“Aaah!! Bosi ni cha kwako, angalia bwana kikipotea hiki itakulazimu kupima upya..??” upande wa pili ulilazimisha uchangamfu ambao haukupokelewa na John. Sauti ilikuwa imemkumbusha John kuwa anayezungumza ni kijana aliyemjazia mafuta kwenye gari asubuhi hiyo
“Mbona sikuelewi”
“Matha Mwakipesile ndio mkeo!!!”
“Ndio kwani nini mbona husomeki jombaa” John alizungumza kwa jazba hakupenda jinsi alivyozungushwa zungushwa.
“Basi kuna kikadi chake hapa cha hospitali….”
“Haya nitakupigia baadaye nipo kwenye kikao” alisema John na kukata simu, alihofia kuwaudhi wenzake waliokuwa wanamsubiri.
Laiti kama angeendeleza mazungumzo japo kidogo tu yangekuwa mengine.
****
Mapigo ya moyo ya Matha yalikuwa yakienda kasi tofauti na siku zote maishani mwake. Kabati la nguo halikuwa na kitu chochote ndani yake, kila kitu kilikuwa shaghalabaghala. Matha alikuwa anatokwa na jasho jingi. Kwa mara ya kwanza tangu aingie katika suala zima la ujambazi alijihisi kutingishika na kushikwa na uoga wa hali ya juu. Kadi iliyokuwa na majibu kwamba yeye ni mjamzito ilikuwa haionekani, kila kona alipojaribu kugusa hapakuwa na chochote, tegemeo la mwisho na aliloliamini zaidi ilikuwa ni katika suruali aliyomzawadia John asubuhi hiyo. Matha alitamani kurudisha muda nyuma lakini muda ulizidi kwenda mbele. Amani ikatoweka, giza likatanda, kizunguzungu kikamtwaa akakaa kitandani, alilazimisha kilio ili kuondoa donge la wasiwasi na karaha kooni, kilio hakikutoka akawa kama anakoroma, akaligundua hilo akanyamaza kimya. Akatamani aizime simu yake bado hakuona tija. Hatia ikaanza kumtafuna, hatia ikaanza kuipasha joto damu ya mlimbwende huyu. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Matha alichukua simu yake na kutaka kumpigia Michael lakini kabla ya kupiga alisita. Hofu ikamkumba Matha, Michael angeweza kukimbia. Nguvu za Hatia ziliendelea kumtafuna kwa kasi Matha aliamua kumpigia simu John japo hakuwa amejiandaa nini cha kumuuliza. Mikono yake ilikuwa inatetemeka wakati simu inaanza kuita, simu iliita bila kupokelewa.
"Tayari amekiona!!" alitahayari Matha, wakati akizipiga tena namba za John. Wakati huu iliita mara mbili kabla ya kukatwa. Wasiwasi ukatanda. Nimelikoroga!! kwa mara ya kwanza Matha alijikuta anamuogopa John. Huku akijitazama kwenye kioo, mikono yake ikiwa imekishika kiuno chake chembamba.
*****
Akiwa amewakera wenzake katika kikao hicho cha watu wachache japo chenye mpango wa kuumiza wengi John Mapulu hakuumizwa sana na hilo ila ile hali ya kupigiwa simu na Matha kisha hakuzipokea ndio ilimtia mawazo. Kengere za tahadhari zilipiga masikioni mwake, huenda Matha yupo matatani, ama ana shida ya msingi sana. Akafikiria kuomba ruhusa tena lakini nyuso zilizojaa chuki zilikuwa zikimtazama yeye, akahairisha! lakini kwa kujificha akatuma ujumbe.
'Nipo kwenye kikao honey! kuna nini?' baada ya kutuma ujumbe ule akahifadhi simu yake, punde wakati akijiweka sawa kuendelea na kikao akaisikia simu yake inatoa mlio, akaichomoa tena.
"Message sending failed" alijilaumu John kwani alikuwa hana salio kwenye simu yake hivyo ujumbe haukufika, kwa ujasiri akaomba ruhusa.
"Dakika moja ni 'waifu' sijui kuna nini" alijieleza John. Hakuna aliyemjibu. Alijua wamekasirika lakini hakujali, alimpenda sana Matha. Alipofika chooni akambip Matha. Punde akapigiwa.
"Yes sweet heart nambie"
"Kwani vipi?...kwema huko, nimekukumbuka wewe" alijiumauma Matha.
"Huku poa tu sijui hapo nyumbani"
"Poa tu upo kwenye kikao eeh!...nimekusumbua" alijishaua huku sauti yake ikitawaliwa na mawimbi mawimbi ya hofu
"Hujanisumbua hata kidogo" alijibu John
"Haya endelea na kikao mume wangu" Matha alitoa neno hilo ambalo lilimlegeza John akauhisi upendo wa Matha ulioanza kupotea ukirejea kwa kasi.
"Asante 'waifu' ehe! unatoka saa ngapi leo ulisema?"
“N’taenda baadaye mjini mpenzi wangu kuna mahitaji nitafuata supermarket"
Suala la Matha kuelekea mjini likaifungua akili ya John akakumbuka kitu, ilikuwa ni simu aliyopigiwa kutoka sheli. Upuuzi wa kimaamuzi alioufanya haustahili kusamehewa. John Mapulu akamgusia suala hilo Matha 'mkewe'
"Tena afadhali pitia hapo sheli hapo kuna jamaa mmoja mchaga hivi anafanya hapo kazi amesema sijui kuna kidude gani nimempa kimakosa hebu kaanga.. . . . ." kabla hajamalizia kuongea simu ilikatwa na kuzimwa, mwenyekiti wa kikao alikuwa amemfuata John huko huko chooni, kwa hasira akaitwaa simu na kuizimisha, John akasonya kwa ghadhabu lakini hakufanya lolote zaidi ya kurejea kwenye kikao.
Matha alikuwa anatetemeka tangu anaongea na John neno la kwanza kwenye simu, alikuwa anajaribu kuzichanga karata zake aweze kufahamu kama John alikuwa anafahamu juu ya uwepo wa kikaratasi kinachoonyesha majibu yake siku alipoenda kupima ujauzito. Hofu ilikuwa imetanda lakini aliamua kujaribu. John hajui lolote! ndio mshangao alioupata Matha baada ya kuisikia sauti ya John ikiwa tulivu na iliyojaa mahaba.
"Sheli...kidude. . . Mchaga hivi vitu vinahusiana kweli na hicho kikaratasi" alijiuliza Matha baada ya mawasiliano kukatika. Alikodolea macho simu yake huwenda John atampigia, hakupigiwa, akaamua kupiga tena, simu ikawa haipatikani. Sentensi isiyonyooka na isiyomaliziwa kutoka kwa John ilimuacha Matha katika jitimai la nafsi. Hakuelewa John alimaanisha nini.
Matha hakuelewa kama John alimaanisha hicho kikadi alichokuwa akikiwaza yeye ama la! . Akili ya Matha ilikumbwa na zizimo, muda ulikuwa unasogea bila maamuzi sahihi kupita katika halmashauri ya ubongo wake.
Aliingia bafuni akaoga akavaa nguo zake alizokuwa amevaa siku iliyopita. Kama vile mtu anavyoitwa na wachawi usiku wa manane kutokea usingizini ndivyo Matha alivyotoka chumbani kwake na kuanza kutelemsha ngazi hadi akafika chini.
Sheli!! lilimjia hilo wazo ghafla baada ya kugundua hakuwa na mahali rasmi pa kwenda.
"Sheli gani sasa??" lilikuwa swali lililofuata. Hakika lilikuwa swali gumu sana kwa maana sheli zilikuwa nyingi mno. Matha aliweka kituo kisichokuwa rasmi katika banda linalouza magazeti, akawa kama anasoma vichwa vya magazeti mbalimbali kwa umakini mkubwa sana lakini hakuna alichokielewa, mawazo yake hayakuwa hapo.
"Naomba KIU" Matha alitoa pesa na kumlipa muuzaji akapewa gazeti alilohitaji. Macho yake yakakutana na sheli upande wake wa kushoto alipogeuka. Bila kujiuliza mara mbilimbili akawa ameamua kuifuata baada ya kuhakikisha upande wa kushoto na kulia mwa barabara usalama ulikuwepo. Pale sheli palikuwa na mgahawa, Matha akapenyeza hadi karibu na huo mgahawa, walipita watu kadhaa akaishia kubadilishana nao salamu, mara aanze yeye ama wao, hakuongeza neno.
Niulize mchaga au? huu ni upuuzi!! Matha akajifanyia mahojiano mafupi na kugundua alikuwa anajidanganya. Alipiga hatua kadhaa kuuacha mgahawa kwa ghadhabu lakini mara upepo ukavumia usawa wa pua yake, harufu nzuri ya chai ya maziwa, donati, sambusa, chapati na mayai ya kukaangwa mchanganyiko na eggchop vyote vikaungana na kupenya katika pua yake. Minyoo ikashtuka usingizini, tumbo likaunguruma Njaa!! Matha akabadili uelekeo akaurejea mlango wa mgahawa, akachukua nafasi yake.
"Maziwa ya moto, donati na egg chop" aliagiza kwa utulivu Matha huku macho yake yakizipitia kurasa za gazeti alilonunua, simulizi ya Beka Mfaume ya WIVU ambayo siku zote ilikuwa inateka akili yake leo hii alikuwa anaiona kama makala mbovu ya siasa za ughaibuni tena iliyoandikwa katika lugha ya kigeni.
Chai ilipoletwa ukawa mwisho wa kusoma gazeti. Tumbo lake ambalo halikuwa na chochote tangu kupambazuke lilikuwa linafurahia maziwa ya moto yaliyopenya katika kinywa kisichopatwa na ladha yoyote. Mfululizo wa matukio yasiyokuwa katika mtiririko maalum uliisumbua akili yake hatimaye akaiona sura ya Michael, akajutia kukutana naye lakini akajilaumu kwani yeye ndiye alimwendesha hadi akafikia kuwa mpenzi wake wa siri. Hakujua alitumia muda gani kufikiri lakini alipokumbuka tena kupeleka kikombe cha maziwa mdomoni yalikuwa yamepoa hakuendelea kunywa.
Akalipa akaondoka!!
Kelele za mpiga debe zilimvuta akapanda daladala inayoelekea Nyegezi ikitokea Igoma. Matha alipanda kwa msukumo wa mpiga debe hakuwa amenuia rasmi kwenda huko Nyegezi.
Muziki mkubwa ndani ya gari hiyo ulimtia ghadhabu, alitamani kushuka lakini alikuwa siti ya nyuma akahofia kufanya usumbufu.
"Tuache hapo Natta!" abiria mmoja aliyekuwa jirani na Matha alimkumbusha kondakta ambaye naye aligonga bodi dereva akasimamisha. Aliposimama kuanza kushuka Matha naye akaamua kushuka, baada ya kulipa nauli alishangaa hapa na pale na kujiangalia amepungukiwa nini ndipo alipogundua ameacha gazeti ndani ya gari, bila uelekeo maalum Matha alianza kukaza Mwendo.
"Mh! au ile sheli ya Mitimirefu??" swali la ghafla likanasa katika ubongo wake likisubiri jawabu.
****
Minja Meri alikuwa mmoja kati ya wachaga wachache waliokimbia maduka ya wazazi wao na kuamua kupambana kivyao jijini Mwanza, kabla ya kuingia jijini Mwanza Minja aliwahi kuwa dalali mjini Morogoro, muosha magari jijini Mbeya na sasa alikuwa jijini Mwanza akifanya kazi sheli. Kipato cha masaa alichokuwa akiingiza Minja kwa muda anaokuwa kazini hakikumtosheleza kujikimu maisha yake mwenyewe katika chumba chake cha kupanga maeneo ya Mabatini jijini Mwanza. Kwa kulitambua hilo kijana huyu mrefu wa kimo, ngozi yake maji ya kunde na kichwa chake kisichokuwa na nywele huku rangi ya meno na lafudhi ikiuweka hadharani uasilia wake. Minja akawa amebuni mbinu ya kuwa anawachangamkia sana wateja wake, hasahasa wenye magari binafsi na yale ya serikali na wale wenye kawaida ya kuweka lita nyingi za mafuta, tabia yake hiyo iliyojawa na ucheshi akafanikiwa kuwateka matajiri wengi hivyo kwa siku alikuwa hakosi shilingi ya ziada (Bakhshishi) tofauti na malipo yake. Kwa muda mrefu alikuwa amejaribu kwa hali zote kumtia John Mapulu katika himaya yake lakini tabia zake za ajabu ajabu zilimshangaza, mara leo anacheka mara kesho hazungumzi neno. Hata siku hii alipomjazia mafuta katika gari yake bado John hakuzoeleka, kitendo cha kuchanganya pesa za malipo na kikaratasi kidogo japo muhimu cha hospitali kwa Minja ilikuwa kama nafasi yake kubwa kumthibitishia John uaminifu wake hivyo kwa kikaratasi hicho aliamini siku hiyo lazima angepata shilingi kadhaa bila jasho.
Minja hakutaka kumshirikisha mtu yeyote aliamini ilikuwa bahati yake na wala hakulichukulia uzito jambo lililoandikwa na daktari alichoangalia yeye ni maslahi atakayopata. Kwa mbinu hafifu aliweza kuinasa namba ya John Mapulu kutoka kwa mmoja wa mabosi wake, ni baada ya kuomba aazimwe simu ili apige namba yake kwani alikuwa haioni simu yake, bosi akaingia mkenge akampatia. Kitendo cha dakika mbili dalali huyu mstaafu alikuwa ameinakiri namba ya John kichwani mwake. Ilikuwa bahati yake kuwa namba ya John ilikuwa imehifadhiwa kwa jina halisi la ‘John Mapulu’
"We boya kweli, ona simu ipo kwenye soksi unatafuta mfukoni" Minja alishtuliwa na mwenzake wakati anaendelea kuipiga namba yake.
Danganya toto!! aliwaza Minja huku akizuga kujicheka. Kwake ulikuwa ushindi, wakati kwa wenzake ukageuka utani. Muda wake wa mapumziko ulipowadia Minja Meri alibonyeza namba za John Mapulu ambapo walizungumza, Minja alijaribu kuweka ukaribu na heshima za hapa na pale lakini John bado hakuchangamka.
Hawakufikia mustakabali John akatoa ahadi ya kupiga simu baadaye. Minja hakukata tamaa aliendelea kubaki maeneo ya karibu na sheli alikuwa akisubiria simu ya John, alikuwa akihitaji pesa bila jasho. Muda ulisogea bila kupokea simu yoyote, hakutaka kumsumbua John kwa kumpigia simu alisubiri apigiwe kama alivyoahidiwa. Usingizi ulimpitia mara kadhaa alizokuwa amejiegesha katika kiti cha plastiki kilichokuwa mbele ya duka la spea za pikipiki jirani na Sheli. Mara hii alipogutuka kutoka usingizini alikumbana kwa mbali na hisia za kumfahamu mtu aliyekuwa anakuja mbele yake, sura haikuwa ngeni. Hakupata kumbukumbu ni wapi aliwahi kumuona lakini kama kawaida akainuka kwenda kumlaki.
Tabia za kidalali zilikuwa zinamtafuna!
Minja alipandisha juu suruali yake na kuficha kitundu kidogo kilichokuwa kimeishambulia suruali hiyo iliyokuwa mpya miezi mitano iliyopita, bila shaka kitundu hicho kilikuja kuhitimisha uchakavu wa suruali ile. Baada ya kujiweka sawa kabisa kwa ujasiri wa hali ya juu alichanganya miguu yake hadi akawa ameiziba njia aliyotaka kupita mwanadada huyu mrefu wa haja, mweupe wa rangi' uzuri wake haukukamilika kutokana na kukosa tabasamu, japo simanzi iliyomtawala usoni haikuficha uzuri wake.
"Sista....sista..nakusalimia" Minja alinyanyua mkono wake na kutaka kumsalimia Matha. Matha hakutoa mkono wake, akamkazia jicho lililojaa chuki bwana Minja.
"Shimboni..." alisalimia kikwao katika hali ya utani, bado Matha aliyekuwa amesimama akimshangaa hakujibu lolote. Wala hakuruhusu tabasamu!!
"Yesu na Maria naumbuliwa mie leo" alijaribu karata ya mwisho ya utani! akafanikiwa Matha akajenga tabasamu hafifu, Minja akaviona vishimo vilivyozama katika mashavu ya Matha. Akausikia moyo wake unadunda, akaelewa alikuwa ameanza kumtamani yule binti.
"We mkorofi wewe mwone meno yake..." Matha aliongea huku akijizuia kucheka.
"Meno yangu ya dhahabu, usimwambie mtu yeyote wataniteka" Minja alimnong'oneza Matha huku akitazama kushoto na kulia kama vile kuna watu wanafatilia mazungumzo yao. Safari hii Matha akalipuka na kicheko kikubwa lakini cha kistaarabu meno yake meupe yakammulika Minja. Ile kujizuia kucheka mabega yakawa yanatikisika, na maungo mengine yakaiga mfano wa mabega. Akapendeza!!!
Minja akawa amefanikiwa kuujenga urafiki.
"Ehe! unajua ni kama nimewahi kukuona vile mahali fulani...kwema utokeapo lakini?"
"Kwema sana aisee!!...naingia hapa sheli mara moja" Matha alijibu huku akianza kuondoka.
"Sheli ndio mimi, kwani una tatizo gani…gari ipo wapi tujaze mafuta upesi" Minja aliwahi kumzuia Matha kwa kumdaka mkono asiondoke! wakati huo akiendelea kuvuta kumbukumbu ni wapi amewahi kumuona
"Ehee! tena we nimewahi kukuona hapahapa sheli nimekumbuka tayari, ni dada nani vile waitwa" Minja alimweleza Matha. Matha akavutiwa na uchangamfu wa Minja akamuona ni mtu sahihi wa kuweza kumuuliza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hivi nanii? hapa kuna....." Matha akakatishwa na mlio mkubwa wa simu ya kichina ya Minja. Minja akataka kusogea pembeni aweze kuipokea simu, ikawa zamu ya Matha kuingiza utani akamdaka Minja mkono.
"Hauondoki na wewe!! chagua simu au mimi" Minja akainama chini kama aliyekuwa anafikiria jambo kwa sekunde kadhaa akapata maamuzi
"Fimbo ya mbali haiui nyoka! huenda huyu ndo riziki yangu" alijifikiria na kisha akakata simu na kuizima. Ikapiga kelele wakati inazima, akatumia viganja vyake kuiziba spika.
"Nimekuchagua wewe mama naniii" Matha akalipokea jibu hilo kwa kicheko hafifu.
"Naitwa Matha"
"Matha MWAKIPESILE yeah!" alimalizia Minja kwa sauti yenye mshangao. Matha macho yakamtoka alishindwa kupiga kelele, hakuweza kucheka wala kulia, sura yake ikawa kama aliyeshtuka kutoka usingizini.
"Umenijuaje?" aliuliza
"Nilikwambia nakufahamu..sasa nimekumbuka vizuri" alijibu Minja.
"Ndio umenijuaje kwani?" alihoji tena Matha wakiwa bado wamesimama
"Nikikwambia jingine ...we mke wa mzee John Mapulu" alisema Minja kisha akacheka huku akimkimbia Matha kiutani, Matha naye akamkimbilia. Minja akasimama. Hofu kubwa ikamzunguka Matha hakumfahamu mtu huyu lakini yeye alimtambua. Wapita njia wakawa wanaosha macho yao kufurahia mchezo huu wa Matha na Minja.
"Mungu mkubwa sana nilikuwa nakusubiri wewe, na niliyemzimia simu ni mumeo..nina bahati mie" alizungumza Minja, Matha akahisi nguvu zikipungua mwilini, ujasiri ukaaga mwili wake Hatia ikachukua nafasi yake.
Mambo yameharibika??? akajiuliza
"Hebu tukae basi!!" Matha alizungumza huku akitupia macho yake huku na huko kuangalia wapi pa kukaa. Minja alitambua msako huo, akamshika Matha mkono hadi kwenye kimgahawa fulani wakakaa, Minja alikuwa ametawaliwa na tamaa na ujivuni alitamani kila mtu amwone jinsi alivyokuwa anatembea huku amemshika Matha mkono. Alitamani sana kuwa na uwezo wa kumiliki mtoto mzuri kama yule lakini hakujua upande wa pili wa Matha kuwa ni mtu hatari sana.
"Ujue mzee wetu asubuhi amesahau kitu cha msingi sana, nilimpigia simu lakini hatukuelewana.
"Kitu gani"
"Kwanza naitwa Minja wa Meri" alijitambulisha bila kuwa ameulizwa na yeyote. Alifanya hivyo baada ya kugundua kuwa hakuna atakayemuuliza hapo baadaye.
"Haya!! haya ehee!!" alikubali harakaharaka Matha, hakulitilia maanani jina la Minja kwa wakati ule.
Muhudumu akafika na kuwasikiliza, wote wakaagiza maji ya matunda, wote walichagua mchanganyiko wa embe na parachichi.
Mlipaji alikuwa ni Matha!!!!
"Hongereni sana maana dah!! ujue mtu akikuangalia hawezi kuamini mh!! watu mmeumbwa mkakubali kuumbika" Minja alizungumza huku akiupima urembo wa Matha kwa macho yake. Tabia za kidalali zikaendelea kumtafuna Minja. Maneno mengi!!!. Akili ya Matha ikagutuka hakika alikuwa akimuhitaji sana Minja, hapakuwa na kingine cha kupewa hongera zaidi ya huo ujauzito, tena kwa mtu kama yule wasiyefahamiana.
Noti nyekundu nne tayari zilikuwa halali ya Minja baada ya mazungumzo hayo na kumkabidhi Matha kile alichokuwa anakitafuta.
"Sitaki John ajue sawa!!! nilikuwa nimemfanyia kama 'surprise' hivyo usimwambie kitu chochote kile" Matha alidanganya, Minja akauingia mkenge.
"Usiwe na shaka bosi wangu!!!" alitii.
*****
Michael alishindia nyumbani akitathmini juu ya mauaji aliyoyafanya John, lakini mauaji hayo hayakuwa ya kumuweka kitandani kubwa zaidi ilikuwa juu ya Matha na mimba aliyonayo. Maswali na hofu kuu ilikuwa dhidi ya John iwapo akigundua itakuwaje. Je ataniua kikatili zaidi ya yule bodaboda?? au atanipiga risasi?? Alijiuliza Michael bila kupata majibu sahihi. Simu yake ya mkononi ndio ilimkatisha kupata jibu sahihi, alikuwa ni Matha, Michael aliitazama sana simu ile kabla ya kuamua kuipokea, aliamini ilikuwa ni kero nyingine tena.
"Michael nahitaji kuonana na wewe kuna jambo hapa haliendi sawa!" aliongea huku akitweta Matha
"Nini tena??" aliuliza kwa utulivu
"Nahitaji kukuona" sauti hii sasa iliamrisha, Michael akashtuka
"Sawa muda gani??"
"Saa mbili usiku we utajua jinsi ya kufika nitakuwa SHETHEMBAA SHETHEMBA BAR Mecco"
"Haya nitakuja" alijibu na kukata simu.
Hakuwa na hamu ya kuwa karibu na Matha tena kutokana na hatari iliyopo lakini hakuwa na ujanja aliitii amri, tayari ilikuwa saa kumi na mbili jioni. Michael akajikokota hadi sebuleni akaliendea jokofu na kujitwalia maji ya kunywa yaliyokuwa kwenye kopo dogo, wakati anayafungua akasikia injini za gari zikiunguruma nje, alikuwa ni John amerejea, akahairisha kunywa maji akaliendea geti na kufungua.
"Usifungue nahitaji kutoka na wewe, vaa viatu twende maeneo kidogo" sauti ya amri ya John ilimzuia Michael. Kama vile roboti akatii amri akaingia ndani na kuvaa viatu kisha akarejea baada ya kuwa amemuaga Bruno aliyebaki ndani.
Mwendo haukuwa mrefu sana, injini ikazimwa mbele ya maandishi 'WELCOME CHEERS PUB" wakatafuta mahali tulivu wakakaa, muhudumu akawasikiliza haja zao na kuwapatia huduma.
"Michael nimepata safari ya dharula, nadhani nitaondoka kwa wiki kama mbili hivi" alianza kuzungumza John kisha akaendelea, "Ishi vizuri na Matha na Bruno sawa, wasikilize wanachokueleza na wala usilete ubishi" Michael akakubali kwa kichwa.
"Nakuachia jukumu kubwa moja, chunguza sana mienendo ya Matha halafu nikirejea utanipa taarifa rasmi japo naamini hakuna baya analofanya nyuma yangu, zawadi nitakayokuletea itakufanya utabasamu maisha yako yote!!!"
Michael akawa msikilizaji hadi mambo ya msingi yalipoisha, pombe alizokunywa zikamsahaulisha kuwa alikuwa na ahadi na Matha, majira ya saa tatu kasoro alijongea kwenda haja ndogo, mezani akimwacha John akiendelea kupata mvinyo wake. Baada ya dakika kadhaa alirejea.
"We dogo hapa kwa wasukuma utarogwa!!!!"
"Nirogwe na nani na kwa nini??"
"Wake za watu ni sumu" alisema John huku akimpa Michael simu yake. Upande wa ujumbe ulikuwa wazi yaani kuna ujumbe umesomwa.
"Nimekwambia tuonane umepuuzia ngoja sasa bwege akigundua kuwa una mahusiano na mimi utakoma, usinipigie simu" Michael alitetemeka dhahiri, pombe ikayeyuka, aliogopa kumtazama John aliyekuwa hoi kwa kicheko.
"Cheki unavyokodoa macho!!!! ndo unaachwa hivyo" alitania John
Michael hakusema lolote, licha ya kwamba jina lilikuwa halijahifadhiwa kama Matha lakini bado aliogopa. Akajichekesha kidogo na kujidai hakuna anachoogopa. John naye akaacha kucheka.
Wakaendelea kunywa hadi usiku wa manane ndipo wakarudi nyumbani, wakalala sebuleni, siku iliyofuata John akasafiri, alimtaarifu Matha kwa njia ya simu.
*******
Mazingira yalikuwa yamebadilika sana japo ni miezi mitano tu tangu afike pale kwa mara ya mwisho, mabadiliko yalikuwa makubwa mno, ni yeye alituma pesa kwa ajili ya marekebisho hayo lakini hakutegemea kama ingekuwa kiasi hicho. Geti lilikuwa kubwa jeusi la kisasa, katika mitaa yote ya Lincon, Maree, Maruku na Uhasibu palikuwa na nyumba mbalimbali lakini hii ilikuwa na ulinzi mkubwa zaidi pia ilikuwa nzuri sana.
Barabara ya Ginery iliyokuwa lami tupu hadi maeneo ya uhasibu ilimpa raha sana John kuliendesha gari aina ya Landcruiser Prado alilotokanalo Mwanza, ulikuwa ni mwendo mkali sana lakini alifika Singida bila wasiwasi wowote.
Honi mbili alizopiga zilimsukuma mlinzi hadi nje, akalifanyia usahili wa macho gari lile, likawa geni machoni mwake.
"Shida!!!" aliuliza kwa amri yule mlinzi, sauti yake ilikuwa ya kujiamini sana.
"Mgeni wa mzee Bushir!!!" alijibu John huku akijiamini
"Mna 'pointment' " aliuliza tena kwa kiingereza cha kubahatisha lakini bado alizungumza kwa amri kama vile askari polisi.
"Mwambie John Mapulu"
"Nani??"
"John Mapulu!!!!" alirudia kwa utulivu. Simu ikanyanyuliwa na kubonyezwa namba kadhaa. Baada ya maelezo mafupi akairudisha mahali pake na kufungua geti, John akaingiza gari. Jumba lile lilikuwa limependeza sana na lilimvutia John akaridhika na kiasi cha pesa walichotoa kulikarabati.
"Comrade John Mapulu!!!! Mapulu ze great" akiwa bado nje analitathmini jengo hilo, mzee Bushir akawa amefika na kumlaki John. Wakakumbatiana kwa sekunde kadhaa; lakini Bushir mzee huyu wa kiarabu hakuwa na furaha sana.
"Vipi malaria au?? mbona hivyo??"
"Hapana ni unyonge tu, si unajua tena mama yako ameenda kwao kusalimia" alidanganya, John akaridhika.
"Vipi mgeni wangu naye mzima?? au naye malaria" aliuliza John.
"Mzima yule" alijibu kana kwamba hakulitaka swali hilo. Wakaongozana hadi ndani ambako hawakukaa sana , jokofu halikuwa na vilevi hivyo wakaamua kuhamishia maongezi yao Bar ya uhasibu iliyokuwa maeneo ya jirani.
"Sam Mayuni bado yupo??" John alimuuliza Bushir wakati wakikatiza maeneo jirani na chuo cha uhasibu Singida T.I.A.
"Yupo, aende wapi yule??" alijibu.
Pale bar, nyama choma na bia zilitawala maongezi yao lakini kuna mada ambayo mara kwa mara mzee Bushir alikuwa anaikwepa ni mada kuhusu mgeni wa John. Yote walizungumza lakini walipofikia mada juu ya Joyce Keto mzee Bushir alilegea sana.
"Kwani vipi mbona kila unavyomzungumzia unaguna???" John aliuliza akiwa na mashaka kidogo
"Aah!! hapana hapana kitu" alijitahidi kujibu Mzee Bushir bila kujua kwamba alikuwa akijiumauma. John akapandisha mabega juu, akabetua midomo kisha akakata pande la nyama akalitupia mdomoni na kushushia na Kilimanjaro baridi.
Waliendelea kupiga pombe huku wakisimuliana mikasa mbalimbali iliyowahi kuwasibu katika shughuli zao hizo haramu, kwa jinsi walivyokuwa wakisimuliana ni kama vile suala la kwenda jela kwao kilikuwa kitu cha kawaida.
"Hivi Dulla yupo???" John alimuuliza Bushir
"Ah!! Dullah alipigwa condemn" alijibu Bushir. Ndugu msomaji 'Condemn" maana yake ni kuhukumiwa kunyongwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
John alisikitika kidogo kisha akaendelea kula nyama.
"Ulisikia kuhusu Soja.....dah!!! msela wetu yule wamemuua vibaya sana, wamemvisha tairi wakamtia moto....halafu nilikuwa naye kwenye ule msala pale Kariakoo sokoni...unadhani napatamani Dar tena???" John alisimulia ikawa zamu ya mzee Bushir kusikitika.
Majira ya saa nane usiku wakaanza kujikongoja kurejea nyumbani, kwa kuwa hawakuja na gari lao walijikokota kilevilevi hadi wakafika nyumbani, kila mmoja akalala hoi. Asubuhi wote waliamka mapema 'hangover' haikuwa kikwazo kwa wawili hawa kupanga mipango yao. Kilichokuwa kimemleta John katika mji huo ni silaha na funguo kwa ajili ya tukio walilotegemea kulifanya la kuiba katika supermarket
"Bushir jana usiku nimeota mambo ya kiajabu ajabu lakini nimekumbuka asubuhi kuwa haikuwa ndoto bali ukweli mtupu"
"Nini tena" aliuliza kwa hamu ya kujua jambo
"Joyce Keto na Minja"
"Minja??? ndo nani huyo"
"Lofa mmoja anauza mafuta huko mwanza"
"Mafuta ya kusafishia bunduki!!! kafanyaje" aliendelea kuwa gizani mzee Bushir
"Petroli...nimekumbuka niliwahi kuzungumza naye kwenye simu aliniambia mambo ya ajabu ajabu hata hayana msingi ila nashangaa eti namkumbuka"
"Ushaanza ule ujuaji wako wa kuhisihisi wewe..machale yalikuaga zamani ushachoka wewe!!" alisema Bushir wakati huo walikuwa chumba cha silaha wakisafisha Bunduki. John hakuendelea kuzungumza.
"Anaweza kuwa 'Informer' yule" alijisemea John, mzee Bushir akasikia. Msomaji, INFORMER ni askari aliyestaafu ambaye anajichanganya na watu waovu huku akijidai ni mwenzao kumbe anatoa taarifa kwa polisi walio kazini.
"Unamuacha anaishi hadi leo???" alishangaa Bushir.
“Nikirudi Mwanza namchukua mateka, kama ni informer namuua kwa mkono wangu!!!” aliapa John, kwa kusema hivyo na Bushir naye akasita kuendelea na zoezi lile.
"Hata mimi kuna mjinga namsaka, yaani zingekuwa enzi zangu kabla ya huu uzee ningekuwa nimemkamata tayari na kumtoa uhai"
“Nani tena huyo”
“Fala mmoja alikuwa mlinzi hapa!!!”
“Akaiba???”aliuliza John
"Bora angeiba, ame......" alisita kuzungumza akamtazama John machoni, John akasita kuendelea na zoezi la kusafisha bunduki. Bushir akaendelea, "Alimbaka Joy!!!" alimalizia kwa sauti ya chini. John akajikuta yuko wima, laiti kama angekuwa mchina nywele zake zingesimama.
"Joyce Keto alibakwa?????" alihoji John, ni kama hakuelewa nini Bushir anazungumza. Bushir akaanza kusumbuliwa na hatia, hatia ya kubakwa kwa Joyce. Aliamini itamuwia ngumu sana John.
"Joyce yupo wapi sasa????" aliuliza John baada ya kufanikiwa kuituliza hasira yake. Bushir hakujibu kitu akawa anatetemeka midomo. John aliliona hilo, mapigo ya moyo yakaamua kuongeza mwendo kumaanisha kwamba John alikuwa anaogopa kusikia jibu kutoka kwa Bushir.
John alijaribu kujizuia asihamakinike lakini alishindwa kujizuia kwa hilo, Bushir akaliona hilo. Hofu ikamtanda akamuogopa John kama kiumbe cha ajabu kisichofaa kuishi na mwanadamu. John alikuwa ameiva kwa hofu kuu iliyochanganyika na hasira.
"Kwa hiyo Joyce ametoroka ama ame.."
"Hapana hajatoroka wala hajafa.....tatizo ni kwamba baada ya miezi minne atajifungua" alijikakamua na kujibu Mzee Bushir.
"Joyce ni mjamzito!!!!!"
"Ana mimba" alijibu Bushir, John akalegea akakaa chini, hakupenda kabisa kuisikia taarifa hiyo. Hiyo ndio zawadi alikuwa ameiandaa kwa ajili ya kumpelekea Michael kwa ukarimu wake na kumrejesha Matha katika himaya yake, zawadi ya pikipiki pekee ilikuwa haijatosheleza. John akajikuta katika dimbwi kubwa la mawazo, moyo wake ulijutia kitendo cha kumficha Joyce kwa muda wote huo. Michael hatanielewa kabisa!!!! alisema John, Bushir hakuelewa lolote hakuwa akimjua Michael.
Hakuwa na jinsi aliamua kuendelea na zoezi la kusafisha bunduki huku wote wakiwa kimya sana, kitendo cha Joyce kuwa mjamzito kilimtia uchungu sana na kuikaribisha shubiri ya hatia kuanza kumshambulia, hakuwa akimuogopa Michael hata kidogo lakini pia hakutaka kuweka udikteta mbele ati kisa yeye ni mbabe mbele ya Michael.
*****
Tumbo lake lilikuwa halijachomoza bado, kipande cha limao kilikuwa pembeni ya kitanda chake. Alikuwa amejilaza huku akilitazama panga boi lililokuwa linapambana na joto lililokuwa linataka kuingia humo ndani, bila shaka katika mpambano huo panga boi lilishindwa ndio maana akatumia leso aliyokuwanayo kujifuta jasho lililopenya katika vinyweleo vyake. Mawazo yake makuu yalikuwa juu ya kiumbe aliyekuwa amejihifadhi katika tumbo lake, wazo la pili lilikuwa juu ya utata uliopo katika kiumbe huyo asiyekuwa na hatia kwa upande wake lakini mama yake alifikiria kwamba kiumbe huyo naye pia ana hatia kwanini aingie sehemu isiyokuwa salama.
Mwanamama huyu mtarajiwa alisita kumuwazia kiumbe aliyebebwa na tumbo lake baada ya kusikia hodi mlangoni. Aliuvuta mdomo wake na kumlaani huyo aliyekuwa anaugonga mlango wake, hakutaka usumbufu wowote ule siku hiyo alikuwa ameamua kupumzika na kujichukulia maamuzi ya kipekee.
"Ulikuwa umelala nini??" aliulizwa bila hata kusalimiwa
"Wala kwani vipi??"
"Niazime elfu mbili, baba Rozi akija nitakurudishia" ilikuwa sauti ya upole kabisa ya mama Rozi sauti ile ilielezea waziwazi shida. Matha Mwakipesile hakujibu kitu aliingia ndani na kurejea na noti ya shilingi elfu mbili akamkabidhi mama Rozi, akashukuru na kuaga. Wakati anataka kurejea ndani alimuona mtu kwa mbali chini kabisa, alidhani mwanzoni kuwa amemfananisha lakini hakuwa amemfananisha.
Mbiombio akashuka akiwa na kanga moja hakujalisha ni wangapi watamuangalia japo alijijua kabisa ni kiasi gani ana makalio makubwa na mitikisiko yake ni kanga hiyo pekee ingeweza kuijibu kuwa ni kiasi gani inaipa shida. Mwendo wa harakaharaka akaona kama haumsaidii akaamua kukimbia kumuwahi mtu yule, vijana wavuta bangi na wasiokuwa na kazi walianza kupiga miluzi, Matha hakujali lolote. Alishawazoea!!!
Alilipita hilo kundi kama vile upepo na kuendelea mbele, akiwa hajategemea tukio kama hilo kumtokea Matha alihisi kuguswa na mkono wa mtu, kuna bwana alikuwa amemshika Matha makalio. Miluzi ikazidi kwa sababu ya tukio hilo, hasira ikamkumba Matha. Yule mwanaume akaleweshwa sifa na ile miluzi akaanza kukimbia kumfuata Matha ili amshike tena na kujizolea sifa zisizokuwa na tija.
Macho makali na maangavu yakamtoka Matha akahisi kudhalilishwa na mtu dhaifu sana, akauvua urembo wake akauvaa umafia aliofunzwa na John Mapulu, Matha akauvaa ukichaa wake akaudaka ule mkono kwa kutumia mkono wake wa kushoto. Mkono wa kuume ukatamani nao kufanya walau kazi kidogo, Matha akauruhusu, ngumi moja imara ilitosha kuuchana chana mdomo wa mtumiaji huyu wa madawa ya kulevya ambaye shibe kwake ni hadimu sana, damu ilibakia katika mkono wa Matha wala haikumshtua alishayazoea matukio hayo. Mzuka wa mapambano tayari ulikuwa umempanda. Akamuona yule kiumbe alifaa sana kwa kushushia mzuka huo. Mwanamke huyu jasiri alifanya kitendocha ghafla lakini cha maajabu. Alijitupa hewani kwa mzunguko wa teke la Vandame, teke la kwanza likamkosa lakini like la pili likatua sawia shingoni. Akatua chini kama mzigo. Tendo alilolifanya Matha mwanamke wa kawaida hawezi kulifanya lakini MATHA si mwanamke wa kawaida!!!
Alipomaliza kumuadabisha kelele hazikuwa kwake tena bali alikuwa akizomewa yule aliyeadhibiwa, Matha alikuwa amempoteza machoni mtu aliyekuwa anamfuatilia lakini alijipa moyo kuwa atakuwa ameingia stendi.
Akaamua kuingia hapo ndani, kwa macho makali kabisa ya kijambazi aliangaza haraka haraka ndani ya dakika tatu tayari alikuwa amemtia machoni.
"Michael!!!!" aliita Matha, bado alikuwa na ari ya kijambazi. Michael aligeuka na kukutanisha macho yake na Matha, alitaka kukimbia pasipo sababu Matha akaligundua hilo akamdaka mkono, Michael hakutegemea Matha huyu ambaye huwa anamsukuma anavyotaka wakiwa kitandani anaweza kuwa imara kiasi hiki, hakuweza kuutoa mkono wake katika mkono mmoja wa Matha.
"Unaenda wapi Michael"
Michael hakujibu, Matha akamkokota hadi pembeni kidogo ambapo waliweza kusikiana wao wawili tu. Matha akamtazama Michael machoni kisha akamwachia
"Naomba unipe dakika mbili tu nizungumze ukimaliza endelea na safari yako, safari ya kumkimbia mwanao, safari kafiri ya kuyakimbia majukumu!!! Michael samahani kama nakulazimisha, kuwa huru wewe ondoka lakini kamwe sitakiua kiumbe ndani ya tumbo langu, nipo radhi John aniue lakini si mimi kuua, nilitegemea muunganiko huu wa damu ndio ungetupa akili ya kutanua penzi letu lakini kwako haikuwa hivyo, ni wapi sasa waelekea??? sitaki kujua jibu la swali lako, kwani najua ni wapi unaelekea, unatokea katika uanaume wako kamili na kuukimbilia ushoga kwa ufahari mkubwa.
Nenda Michael, nadhani umenichoka na unatamani kuolewa gerezani, nenda Michael nenda!!!" alishindwa kuendelea kuzungumza Matha donge la hasira lililokuwa limemkaba kooni likapasuka na kuleta sayansi ya ajabu kuliko zote duniani, uchungu wa moyoni unaosikika kooni na kifuani kisha kutokea machoni kama machozi na kujihifadhi tena mwilini kama majonzi makubwa. Kwa haraka haraka akaanza kuondoka, mkono wake ukawa unamsaidia kuyafuta machozi kwa nguvu zote, machozi yakakaribisha kamasi nyepesi hasira kali ikamfumba macho Matha barabara mbovu ikamkaribisha kipofu huyu wa muda akajikwaa na kuisalimia ardhi kwa heshima zote, kichwa, kidevu, mikono, miguu na tumbo vyote vikaibusu barabara!!!! Matha hakupata hata nafasi ya kupiga kelele akatulia tuli.
Michael akaliona tukio lile, begi lake dogo likamponyoka lakini hakujua kama limeanguka akaanza kutimua mbio, Matha alikuwa ametulia tuli
*******
Joyce Keto alikuwa amejikita katika kucheza game katika kompyuta ndogo iliyokuwa chumbani kwake, tayari alikuwa ameyazoea maisha ya kufugwa, miezi kadhaa aliyokuwa amekaa hapo bila kuwasiliana na upande wa pili wa dunia ulikuwa umetosha kumbadilisha, alipata kila alichokitaka katika nyumba ile aliishi na familia ile kama yupo nyumbani kwao, japo alipata tabu sana siku za mwanzo kuzoea lakini baada ya kipindi hicho kirefu alizoea.
"Da Joy baba anakuita!!!" aliitwa na mtoto wa bwana Bushir aliyeitwa Davda alikuwa na asili ya kihindi.
Joyce Keto hakujibu kitu aliendelea kucheza game kisha baada ya dakika kadhaa aliinuka na kuelekea katika wito.
"We!! Davda yupo wapi mheshimiwa" aliuliza Joyce. Davda akamweleza akatoweka kuelekea katika wito.
"Neh neh papa!!!" Joyce alizungumza akimwambia Bushir, Bushir akajilazimisha kucheka. John akajua kuwa Bushir alikuwa na utani na Joyce.
"Shkamoo bosi!!!" alimsalimia mgeni aliyekuwa na Bushir. John Mapulu naye hakujibu bali alicheka japo si kicheko halisi, Joyce akachukua nafasi katika kiti kilichokuwa wazi, akaiunganisha miguu yake katika staili ya kukunja nne, kinguo kifupi alichokuwa amevaa kikayaweka mapaja yake wazi, kwa Bushir lilikuwa jambo la kawaida lakini kwa John moyo ulighafirika akahisi anaingizwa majaribuni.
"Mambo vipi Joy....unanikumbuka???"
"Hapana tangu nizaliwe ndo nakuona mara ya kwanza hata ndotoni sijawahi kukutana nawe" alijibu Joy, John akacheka. Hakika Joy asingeweza kumkumbuka John kwani kwa sasa alikuwa ana afya tele tofauti na awali alipokuwa ametoroka rumande.
"Naomba niwaache kidogo!!" aliaga Bushir
"Naitwa John.......John Mapulu" alijitambulisha
"Mara ya mwisho nilikuona ukiwa unamtesa bwana mmoja kule Mwanza ni nani yule??" aliuliza Joyce huku akilamba kipande cha limao. John hakuwa na la kujibu.
"Mimi!!!!!"
"Ndio wewe John, japo umebadilika, nilikuwa nimekusahau lakini sio jina lako kamwe sijalisahau"
John alijaribu kupambana na wasiwasi uliomkumba kwa kupiga funda kubwa la juisi iliyokuwa mezani, akafanikiwa.
"Utajua siku nyingine" akajibu kwa amri, Joyce Keto akanywea.
"Unamfahamu aliyenibaka" aliuliza Joyce
John akashindwa tena kujibu, Bushir alikuwa amesahau kumwambia John kuwa tukio la kubakwa alilofanyiwa Joyce liliathiri akili yake na kumfanya kuonekana kama kiumbe wa ajabu asiyeogopa kitu.
"Nitampata!!!!" alijibu John swali ambalo hakuwa ameulizwa
"Ukimpata utanipa na mimi nimtese kama mlivyomfanya yule wa Mwanza" alizungumza Joyce akikumbuka tukio la kumuona John akimuadabisha mateka wake jijini Mwanza.
"Usijali!!!!"
“Yule mjomba wetu mzima…”
“Mjomba? Yupi?”
“Yule ambaye mlikuja naye siku zile kunichukua ….” Joyce alikuwa akimaanisha Bruno. John akaishia kucheka bila kujibu. Joyce naye akafanya tabasamu!!!
Hawakuzungumza zaidi!!
*****
Hofu aliyokuwa ameipata Michael ingeweza kumletea uwendawazimu kichwani kama tu asingekuwa jasiri wa kukubaliana na hali, jambo zuri ni kwamba walikuwa jirani sana na kituo kikubwa cha mabasi hivyo usafiri wa kukodi halikuwa jambo lenye usumbufu sana.
Ndani ya dakika mbili Michael alikuwa amepata wasaidizi wa kutosha wengine walikuwa kazi yao ni kulia wengine walimgusagusa Matha Mwakipesile kama vile walikuwa wanampima homa kwa njia ya hisia za mkono. Matha hakutikisika, baada ya ushirikiano mkubwa Matha alikuwa ndani ya 'Taksi' safari ya kuelekea hospitali ya mkoa ya Bugando!!! Hakuwa akijitambua kwa lolote, fahamu zilikuwa zimeuacha mwili kwa muda.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wazo la Michael kutoroka likawa limeishia pale.
******
Umati wa watu katika jumba la kifahari alilokuwa anaishi John na Bruno kabla ya ujio wa Michael ulimshangaza kila mtu, ulikuwa ni msiba wa aina yake, watu wote walikuwa wamevaa sare sare, wanaume walikuwa wamevaa suti nyeusi huku akina mama wakiwa na mavazi yao ya vitambaa vyeupe, kila mmoja alipendeza. Katika kundi la wanawake wale ni mwanamke mmoja tu aliyemshtua Michael, huyu kwa kila kitu alifanana na Joyce Keto, msichana ambaye kwa namna kubwa sana alikuwa amechangia yeye kuwa katika janga hili lililotawaliwa na Hatia.
"Ametoka wapi??? au nimemfananisha" alijiuliza Michael wakati huo akijipenyeza katika kundi la wanaume na kuingia katika kundi la akina mama, lengo likiwa kuhakikisha kuwa aidha yule ni Joyce ama la!!.
"Mambo vipi dada!!" alimsalimia, yule mwanamke aligeuka na kuanza kumshangaa, wakati wakiwa bado wanashangaana Michael alihisi kuguswa begani, mwanzo alipuuzia hadi pale Joyce alipomwambia kuwa anaitwa. Alipogeuka alikutana na sura ya Matha ikiwa inatabasamu kinafiki.
"Mamaaaaaaaaaaaaaaaa!!!!!!" alilipuka kwa kelele kubwa Michael.
"Vipi kaka nini???" Michael aliulizwa na mtu aliyekuwa pembeni yake.
"Ah!! ni ndoto kaka dah!!!" Michael alijibu huku akiyapikichapikicha macho yake ili aweze kuipata nuru mbele yake, nuru iliyokuwa imemezwa na usingizi, usingizi ulioambatana na ndoto, ndoto ya ajabu, ndoto ya kifo cha Matha na marejeo ya Joyce Keto. Ah!! ni ndoto tu Matha hawezi kufa!! aliwaza Michael na kupuuzia alichokiota. Pia alijenga tabasamu baada ya kuyakumbuka maneno ya mama yake aliwahi kumwambia ukimwota mtu amekufa, huyo hafi.
"Lakini Joyce hivi atakuwa wapi yule binti!!!" alijiuliza, hakuwepo wa kujibu. Majira ya saa kumi na moja jioni majibu kutoka chumba cha uangalizi alichokuwa Matha yalitolewa. Hakuwepo mtu mwingine wa kuyapokea zaidi ya Michael ambaye ndiye alimleta.
Majibu hayakuwa ya kufurahisha sana, kwani maombi ya Michael yalikuwa juu ya mimba alitamani sana itoke lakini wala jambo hilo hakulisikia kutoka kwa daktari.
"Jitahidi sana, hakikisha anapata pumziko la kutosha na matunda ale mara kwa mara."
"Hamna shaka dokta" alikubali Michael. Saa moja usiku Michael aliruhusiwa kumchukua mgonjwa wake, pesa ya ziada aliyobaki nayo mfukoni alilipia matibabu na usafiri wa kurudi nyumbani, safari nzima walikuwa kimya hadi wakafika nyumbani kwa Matha, Michael akamsaidia Matha kupanda ngazi taratibu hadi wakafika chumbani. Siku mbili mfululizo Michael alikuwa anashindia nyumbani kwa Matha akimuuguza, Bruno hakuwa akifahamu ni wapi huwa anaenda na wala hakujali sana kwani ni mtoto wa kiume. Furaha ya Matha ilirejea tena kutokana na upendo wa Michael.
Maisha yakaendelea!!!
Haikuwa kawaida ya Michael kulala nyumbani kwa Matha, nafsi haikumvusha hadi kuufikia ujasiri huo. Lakini siku hii ya ijumaa tulivu kabisa Michael alijikuta akifanya mambo kinyume na matakwa yake.
Ilianzia kwenye sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Matha, Michael pamoja na Bruno walikuwa wamealikwa.
Bruno aliaga mapema na kuondoka kwani haukuwa utaratibu wake kukaa maeneo ya watu wengi kwa muda mrefu, kwa kuwa Michael alikuja na pikipiki yake hakuwa na wasiwasi wowote muda wowote angeweza kurejea.
Kadri muda ulivyokuwa unaenda ndivyo Matha alizidi kunywa pombe hadi akawa hoi kabisa. Michael alikuwa amelewa kiasi cha kawaida sana, kwa pamoja waliondoka majira ya saa tano usiku kurejea nyumbani. Michael alitegemea kumfikisha Matha na kuondoka zake kuelekea nyumbani lakini haikuwa hivyo. Matha alimletea vurugu za kilevilevi hadi wakaoga wote, kama hiyo haitoshi wakaingia kitandani wote. Michael hakuweza kujizuia zaidi akakiri kuzidiwa maarifa akasalimu amri. Saa saba usiku simu ya Michael iliita, hawakuwa wamelala wawili hawa.
"Ni John!!!!" alihamaki Michael, Matha hakusema neno. Zilikuwa ni siku nne tangu aondoke na kuahidi kurejea baada ya wiki mbili.
"Niambie kaka mkubwa!!" alianza kuzungumza baada ya kupokea simu.
"Poa dogo, nishakukataza mambo ya wake za watu shauri zako hapo najua upo na mke wa mtu!!!" sauti ya John ilijibu.
"Hamna nipo kwa mwanangu mmoja hivi kanipiga pombe hatari"
"Haya bwana mi naenda kwa shemeji yako hivyo, si nilikuwa nimesahau kama leo ndo 'birthday' yake!!...yaani najua atakuwa amenuna huyo"
"Nani Matha au....eeh!! upo Mwanza" alizungumza bila kujiamini, wakati huo yule Matha aliyekuwa anajidai amelewa chakari alikuwa amekaa kitako macho yamemtoka pima.
"Ndio nipo hapa maeneo jirani na nyumba yake dakika sifuri tu nafika ndani, we endelea kulewa si ushalijua jiji mi ntafanyaje??"
Tumekwisha Matha, tumekwisha!!!! alisema Michael huku akitapatapa pale ndani. Matha naye alikuwa wima, kanga ilikuwa imedondoka na alikuwa amesalia uchi lakini hata hakulitambua hilo.
Hatia ikaunda hofu katika mioyo yao!!!
******
Matha hakuonyesha kufurahia ujio wa John pale ndani, alijifanya kuwa amelewa sana ilimradi tu John aweze kuondoka mapema, ujanja wake ukafanikiwa John aliaga na kuondoka huku akiahidi kufika pale asubuhi.
"Na hiyo pikipiki ya nani hapo nje??." John alimuuliza Matha, hakujibiwa lolote Matha akajifanya amesinzia tayari. John akajikongoja akatoka nje, alijaribu kupiga simu ya Michael haikupatikana.
"Hili toto hili na wake za watu, shauri zake!!!" alijisemea John huku akiufungua mlango na kutoka nje.
Michael hakuwa na hali kabisa, mchezo uliokuwa unaendelea ni hatari sana kwa upande wake, hali ya kuwa katika chumba kimoja na John Mapulu ilimchanganya sana, japo alikuwa katika uvungu wa kitanda na John akiwa kitandani huo haukuwa umbali mkubwa sana kati yao, alisikia kila alilozungumza John, hisia alizomueleza Matha.
Hatia ikampa shambulizi kali akajikuta anatokwa machozi kimya kimya ni dhambi aliyokuwa akiifanya na Matha ni usaliti mkubwa sana ni zaidi ya hatia.
John alipotoka na kuhakikisha kweli ametoweka Michael alitoka uvunguni na kuvaa nguo zake vizuri kabla ya kuaga, safari hii hakukubali kutawaliwa kimawazo na Matha. Aliondoka!!!
"Naomba uiache pikipiki!!!" Matha alimwambia Michael, kidogo apinge lakini kwa shingo upande akakubaliana naye.
******
Asubuhi John aliamka akiwa amechelewa kiasi, majira ya saa nne. Simu yake ilikuwa inawakawaka kuonyesha kuwa kuna ujumbe ama simu imepigwa haijapokelewa. Ulikuwa ujumbe wa Matha. Ujumbe uliozidisha hofu ya John juu ya Michael. Matha alikuwa ameuelezea ukarimu wa Michael kwake.
"Tazama ameenda kwenye sherehe, tazama amemrudisha nyumbani na pikipiki, amehakikisha usalama wake upo kabisa, ni mashemeji wachache wanaweza kuwa kama Michael!!!" aliwaza John huku akirudia kuisoma meseji ile.
John alizidi kumchukia kijana aliyempa ujauzito Joyce Keto. "Isingekuwa mimba basi hiyo ndio ilikuwa zawadi ya kipekee kwake" alisema John peke yake.
Mawazo ya John dhidi ya Michael yaliipunguza furaha yake. Siku hiyohiyo jioni baada ya kumtembelea Matha alimtafuta Michael ambaye walikuwa hawajaonana ili waweze kuzungumza.
Kituo cha mafuta maeneo ya mitimirefu ndicho kilimkumbusha kuhusu kijana Minja. Alikumbuka simu yake ya mwisho na mazungumzo kati yao.
"Oyo niaje"
"Poa kaka karibu!!"
"Namuulizia Minja sijui yupo?" aliuliza John
"Yupo kaka yule pale anakuja" alijielezea bwana huyu aliyekuwa na sare za wafanyakazi wa pale sheli huku akielekeza mkono wake kwa Minja, kama vile tayari alikuwa ameitwa Minja alifika pale, mara moja alimtambua John Mapulu.
"Heshima yako mkurugenzi, heshima yako kaka" Minja alianza porojo zake. John hakujibu kitu
"Kulikuwa na nini siku ile kwani, uliponipigia simu" swali lile Minja hakulitegemea ghafla kiasi kile akajiweka sawa kwa kukohoa kidogo kisha akamtazama John, alikuwa amemkazia macho, sura ya Matha akiwa anamsisitiza asimwambie John ikatokeza na kumwambia tena.
"Aaah!! siku zile bosi wangu!! kilikuwa kikaratasi cha mtu mwingine tu nikadhani chako" alijaribu kudanganya.
"Matha Mwakipesile unamfahamu??" aliuliza John kama vile alikuwa akimtuhumu Minja.
"Matha.....Matha......" alijaribu kukumbuka
"Ni wewe uliniambia hilo jina kivipi leo humkumbuki???" aliuliza tena. Kijasho chembamba kikamkumba Minja, mzigo wa kuchukua pesa za Matha ili asiseme lolote ukawa unamzidia na sasa ulikuwa unamwangusha chini.
"Matha ni yule mkeo eeeh!!!" alijifanya kukumbuka Minja. Honi za magari yaliyokuwa yakihitaji kupita ndio ilikatisha maongezi yao, John aliondoa gari, alijaribu kutafuta wapi aweze kupaki lakini hakupata nafasi yoyote.
"Nitakupigia simu!!" alisema kwa sauti ya juu iliyomfikia Minja ambaye alikuwa anatetemeka hovyo. Alikuwa anawaogopa sana watu wenye pesa zao kama John Mapulu.
Njia nzima John alikuwa anamuwaza Minja Meri, alianza kuhisi kuna kitu anafahamu na ameamua kumuingiza mkenge, John alianza kuhisi kuna jambo la maana sana kama sio kitu cha thamani ambacho bwana Minja alikuwa anataka kumtapeli.
Haiwezekani siku ile amesema kuna kitu, leo hii anasema hakuna kitu!!! hapana!!! alisema kwa ghadhabu huku akiupiga kwa ngumi usukani wa gari lake mlio wa honi ukatoka, aliyekuwa na baiskeli mbele yake akapisha njia. John bado hakuwa na uhakika kama aweke kituo kwa Matha au aonane na Michael kwanza. Akaamua aanzie na Michael.
******
Watu hawakuwa wengi sana katika ukumbi wa 'If not why not' Igoma jijini Mwanza, Michael na John walikuwa na masaa mawili tangu wafike pale, baada ya maongezi ya kawaida ya hapa na pale ndipo John alipoleta mezani mada ambayo kwa upande wake ilikuwa ni sawa na kucheza bahati nasibu wakati kwa upande wa Michael ilikuwa ni kama kaa la moto katika kichwa cha mwanadamu.
"Michael mdogo wangu hivi hata wewe si huwa unapenda kwa dhati!" alianza John
"Ndio tena sana tu!!!"CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sasa kwa mfano, namaanisha ni kwa mfano sawa!!!" alisita John akapiga funda moja la bia yake kisha akaendelea
"Mtu unayempenda unasikia kuwa.....kuwa ni...ni mjamzito" alizungumza kwa kusitasita John, Michael akahisi nguvu zote hakuna mwilini, pombe yake aliyokuwa anaifurahia ikageuka kuwa na ladha ya pilipili, na nyama choma ile iliyopendezesha meza yao ikawa inamzomea, HATIA ikaendelea kumuadhibu na sasa ilikuwa imefikia pabaya zaidi.
Michael sasa kila kitu aliamini kuwa kipo hadharani, sasa afanye nini hilo ndio likawa swali kuu.
"Mbona umeshtuka sana?? au swali limekuja wakati mbaya???" John alimuuliza Michael aliiyekuwa anajaribu kuushinda uoga uliokuwa umemtawala.
"Swali gumu sana kaka, kwani unamaanisha nini hapo???" na yeye Michael akauliza, John akacheka bila kusema lolote akachana pande la nyama akaanza kutafuna na kushushia na bia.
"Wewe ni mwanaume na mimi ni mwanaume, kwa sasa nawahi sehemu, hebu kaa ufikiri halafu unipe ushauri kuwa kwa mtu unayempenda ukigundua kuwa ana mimba unafanya nini???" aliuliza tena kwa sauti tulivu John, Michael akakubali kwa kutikisa kichwa.
John alimpatia nauli Michael kisha akamwacha pale na kuelekea nyumbani kwa Matha, tayari ilikuwa saa tatu usiku.
“Kumbuka kuwa hiyo mimba si ya kwako….” Alisisitiza John. Michael akabaki kumtazama.
John akatoweka!!! Safari ya kwenda kwav mpenzi wake. MATHA!!
Michael akabaki kimya huku akiona kifo chake kikimtongoza!!!
*****
Matha aliufungua mlango taratibu, John akaingia ndani bila kuvua viatu, Matha alivyoufunga mlango John akamkumbatia ishara ya kumjulia hali.
"Vipi unaumwa??" aliuliza Matha. John hakujibu, akamtazama Matha usoni.
"He!! vipi wewe??"
"Hata siumwi ila kuna tatizo nadhani"
"Usinambie kuwa umechezwa machale kuwa tukienda kuiba tutakamatwa? maana na wewe kwa hayo machale" alidakia Matha huku akimfungua John vishikizo vya shati lake.
"Matha hakuna kitu chako chochote kimepotea humu ndani??"
"Mbona wauliza hivyo kuna nini??"
"Kuna kitu umepoteza??" alirudia swali lake.
"Hapana sidhani!!!"
"Mimi nadhani na kuna mjinga mmoja anataka kutuchezea!!"
"Nani huyo??? na ni kitu gani??" Matha aliuliza kwa umakini mkubwa, sura ya kikatili ilikuwa imemuingia tayari.
"Anajiita sijui Minja sijui nani ni wa pale sheli Mitimirefu" Alijieleza awezavyo John, Matha moyo ukamshtuka kwa hofu kuu baada ya kusikia hilo jina Minja, kwa kuwa alizijua mbinu za John, hakutaka kukutanisha macho naye hivyo akainama chini. Alimfahamu fika Minja Meri, ni huyuhuyu aliyekuwa anaijua siri ya ujauzito wake, lakini haikuwa siri kiasi cha hatari iliyopo, aliamini kuwa Minja alichukulia kama kamchezo flani tu kati ya mtu na mpenzi wake. Hofu ikazidi kumtanda Matha alipomfikiria John, aliijua fika ghadhabu yake ikipanda juu ya mtu hatua ya chini kabisa ni kutesa hadi kuua kama si kuua mara moja.
"Vipi unamfahamu huyo jamaa"
"Jina sio geni sana!!" alijibu Matha akiwa bado na ameinama
"Utakuwa unamfahamu, ni bwege mmoja hivi, kesho nitakupitia ukamuone, anadhani mimi bwege, yaani asiposema kitu kesho namuua!!!" aliapiza John huku akiuma meno yake, Matha akatambua John yupo katika hasira kali juu ya Minja.
Taratibu akamsogelea na kuanza kumpepea kwa kutumia shati alilokuwa amemvua, jasho lilikuwa linamtoka. Matha alifanikiwa kuishusha jazba ya John, tatizo likabaki kwake ni nani wa kuishusha presha iliyokuwa inazidi kumpanda, hofu iliyokuwa ikimtawala. Ni nani wa kumsaidia kuibeba hatia hii, kama Minja atakutana na John katika faragha lazima atausema ukweli, na hata akisema bado atauwawa je itakuwaje kwa yeye Matha atakayesalia duniani kumkabili John, na vipi juu ya kijana Michael. Hayo yote yalimuumiza na kumkera Matha.
"Hata nikiitoa kwa sasa haina maana tena!!!" aliwaza Matha. John aliaga akaondoka na kuahidi kufika siku inayofuata muda wowote kwa ajili ya kwenda kwa Minja. Kuondoka kwa John kidogo kulimpa nafuu Matha, akaondoa nguo zake zote ili kukabiliana na joto, Matha alitamani sana iwe ndoto lakini hii ilikuwa hali halisi.
John atatuua!!!!
Wazo la kuuliwa na John, Matha hakutaka kulilazia damu kwani alimjua nje ndani. Baada ya kufikiria sana alipata wazo, wazo la kuonana na Michael ili waweke mipango sawa.
Wazo hilo likapitishwa na asubuhi ya siku iliyofuata Matha akafanya ugeni wa ghafla nyumbani kwa John. John hakuutegemea.
"Mambo vipi Michael....darasani tafadhali" aliamuru Matha, John na Bruno wakavutiwa na amri ile wakamchukulia Matha kuwa ni mwanamke wa shoka. Michael alighairi kuendelea kunywa chai akamfuata Matha katika chumba cha mafunzo.
"Nakupenda sana Mic" Matha aliyeonekana mwanamke wa shoka mwenye amri sasa alikuwa amelegeza macho na kumwangukia Michael begani.
"Matha hali sio nzuri huyu jamaa amegundua kitu"
"Kitu gani???" aliuliza Matha huku akisimama imara na kumkazia macho Michael. Michael alimueleza swali zito alilopewa na John ili alifanyie tafakari.
"Kwa hiyo nani atakuwa amemwambia??" aliuliza Matha japo hakutegemea jibu lolote kutoka kwa Michael
"Au Minja amemwambia kilichopo katika kile kikaratasi"
"Minja ndo nani???" aliuliza Michael, ikawa zamu ya Matha kuelezea juu ya huyo Minja na wasiwasi wake juu yake.
"Atakuwa ni huyo hakuna mwingine!!!" alisema Michael huku akikaa kitako.
"Tukamtafute baadae" alitoa wazo Matha likakubaliwa na Michael. Hakuna mazoezi yoyote waliyofanya wawili hawa, Matha alikuwa anakwanguliwa na makali ya Hatia wakati Michael alikuwa kama mfu tayari. Matha alijaribu kumtia moyo Michael lakini ilikuwa sawa na bure hata yeye alilitambua hilo.
"Sasa tukishamuona tunamwambia nini?"
"Mbele kwa mbele itafahamika" alijibu Matha kisha akaendelea, "Akileta upuuzi atanijua mimi ni nani" Michael akawa kimya hakujazia neno.
Baada ya masaa mawili walitoka katika chumba cha mazoezi, Matha aliaga akaondoka Michael akaingia chumbani kwake. Hakuna ambaye aliwagundua kuwa walikuwa katika matatizo makubwa.
****
Minja Meri akiwa bado hajausahau ujio wa John Mapulu siku iliyopita. Siku iliyofuata akiwa kazini amehudumia magari mengi, lilikuja gari dogo aina ya Toyota Vitara, vioo vyake vilikuwa vimewekewa utando mweusi 'tinted' hivyo ilikuwa ni vigumu kuwaona walioko ndani.
"Ya shilingi ngapi bosi wangu???" Minja alimuuliza dereva ambaye alikuwa ameshusha kioo.
"Elfu ishirini....chukua pesa dirisha lile pale" alielekeza dereva, Minja kwa nidhamu akaelekea alipoelekezwa.
"Mambo vipi Minja??....sikia pesa hii hapa...unatoka kazini saa ngapi??" Minja alikutana na sura yenye uchangamfu ya Matha. Kwa kuwa walionekana kuwa na haraka naye Minja alijibu upesi.
"Ndio natoka sasa hivi hapa namalizia tu hizi gari mbili tatu, kuna ishu halafu nataka..."
"Poa nakuja muda si mrefu" Matha alimkatisha.
Baada ya kujizungusha kwa dakika kadhaa Matha alimpitia Minja wakaondoka eneo lile wakati huu alikuwa alikuwa anaendesha mwenyewe hivyo kwenye gari walikuwa wawili tu.
"Jana akaja mume wako bwana lakini hatukuweza kuzungumza vizuri....mh!!" Minja akaanza simulizi zake, Matha akawa kimya akijitwalia pointi mbili tatu.
"Minja unaipenda sana kazi ya sheli?" Matha alituliza swali hilo kwa Minja, walikuwa maeneo ya Mkuyuni tayari mezani pakiwa na vinywaji baridi.
Nitafanyaje sasa dadangu!!!" Minja hakuwa amejibu swali, lakini Matha alielewa.
"Nahitaji kukusaidia" alizungumza akasita kisha akaendelea, "nataka ufanye kazi nyingine tofauti na hii"
"Nitafurahi sana dadangu" alidakia.
"Unalipwa au unapata shilingi ngapi kwa siku??"
"Inategemea kuna siku napata elfu kumi siku nyingine hadi kumi na tano"
"Na una familia??"
"Naishi peke yangu maisha magumu sana!" alivutia kwake Minja.
"Pole sana!!" alisema Matha huku akimkazia jicho Minja.
Hisia za Minja zikaangukia katika mapenzi akaanza kuhisi kuwa Matha alikuwa amempenda tayari. Walipomaliza maongezi Matha alimkabidhi Minja shilingi laki moja na kumsihi asirejee tena kufanya kazi eneo lile. Minja alikuwa dhaifu katika pesa alipozipokea na amri aliifuata kama alivyotakiwa. Hakujua kuwa alikuwa kipofu anayepelekwa njia yenye miiba mikali, Minja akajihesabia kuwa ametoka kimaisha kwa kupendwa na mtoto mrembo sana tena mke wa tajiri.
Siku iliyofuata hakwenda kazini!!!
Na hata John alivyomchukua Matha jioni kwa ajili ya kwenda kumtambua na kumuadabisha Minja hawakumkuta. Matha akatabasamu ndani ya nafsi, kwake yeye ulikuwa ushindi wa chee!!! John akazikuza hasira zake juu ya Minja.
"Boya amekimbia ngoja!!!"
"Achana naye mjinga tu!!!" alidakia Matha
"Simuachi kirahisi hivyo......." alijibu John kisha akapiga kite cha hasira na kuondoa gari. Matha akazishusha pumzi zake na kumbusu John katika papi za midomo yake. Akawa amempumbaza!!!. ikabaki kazi ya kumtafutia kazi Minja Meri ambaye amebeba siri nzito bila kujijua kuwa ushahidi wake unahitajika ili dunia ipokee damu itakayomwagika.
*****
Usiku mzima Minja alikuwa akitafakari juu ya ukarimu aliotendewa na Matha, fikra zake bado zilikuwa bado katika mapenzi.
"Hivi nini kimemvutia kwangu mtoto mzuri kama yule jamani halafu kesho ananiletea jibu kama nimepata kazi ama la!!" Minja alijiuliza kwa sauti ya chini kama vile pembeni yake kuna mtu atampa jibu.
"Nikishakuwanaye najua hata haka kajumba nitahama...mbona akina Mussa watakoma" aliwakumbuka rafiki zake waliokuwa wanaishi maisha ya kufanana.
"Lakini kuhudumiwa na mwanamke mh!!!" aliendelea kuwaza. Usingizi ukampitia hatimaye. Asubuhi nayo ikachukua nafasi tena, Minja alikuwa amedamka mapema sana, tabasamu lilimtawala muda wote. Mara kwa mara alimfikiria Juma, huyu alikuwa ni jirani yake aliyekuwa anaishi nyumba ya vyumba viwili tena umeme na maji vilikuwepo, pia alimkumbuka mkewe Juma alivyokuwa mrembo aliyemtamanisha kila siku alipomtia machoni, dharau za mwanadada huyu aliyeitwa Husna zilikuwa zinamkera sana Minja lakini hakuwa na la kufanya. Minja aliamini kuwa karibu na Matha ndio kutawafunga mdomo wavimba macho wote mtaani, hisia za mapenzi zikamezwa na hisia za majivuno Minja akawa na ndoto ya kupata jina upesi upesi mtaani. Subira ikashindwa kutulia katika moyo wake, mguu na njia Minja akitembea mwondoko tofauti kabisa akaamua kwenda kumtangazia rafiki yake jambo hilo. Kwa kawaida huwa anatembea kwa miguu na kupita mikato ya hapa na pale hadi kufika nyumbani kwa Rashid, lakini siku hiyo aliamua kupanda gari la kukodi aina ya 'taksi'. Alifanya hivyo ili akajitwalie sifa mbele ya familia hiyo ya kimaskini maeneo ya Mbugani.
"Elfu tatu!!!"
"Twende!!!" alijibu kwa sauti iliyojaa ujivuni, Minja. Dereva akawasha injini gari likaondoka kwa mwendo wa kawaida hadi nyumbani kwa bwana Rashid, kabla ya kushuka kwa mbali kabisa aliwaona watoto wawili wa mzee Rashid wakikimbizana aliyetangulia alikuwa na hindi la kuchemshwa huku wa nyuma akiwa uchi na kilio kikimtawala. Rashid alikuwa akiwaangalia hakuwa na la kufanya bila shaka alikwishazoea maisha hayo.
"Hebu twende pale mara moja!!!, nitakuongezea malipo" Minja alimwamrisha dereva naye akatii bila kutia neno. Alisimamisha gari mahali ambapo palikuwa na duka kubwa kwa kiasi chake, Minja akatelemka na kuingia pale alitoa noti ya shilingi elfu kumi akanunua mikate na soda za kopo kisha akarejea garini.
"Simama mlangoni kabisa!!!" alielekeza Minja.
Kadri gari lilivyokuwa linasogea ndivyo watoto na mzee Rashid akishirikiana na mkewe walilikaribisha kwa macho yenye mshangao sana, haikuwa kawaida kabisa kupokea ugeni wa namna hiyo kwenye kibanda hicho cha mlinzi asiyekuwa na vyeti aliyeajiriwa kulinda duka la mtu binafsi.
Minja alishuka kwa madaha yote, akamwita yule dereva nje na kumlipa pesa yake umati wote umtazame, kisha akashusha mifuko ya mikate na vinywaji alivyokuja navyo. Heshima yake kwa siku hiyo ikawa juu sana, alifanikiwa kuwateka maskini wenzake.
Mtoto wa mwisho wa Rashid akamlilia Minja waondoke naye. Minja akambeba juu juu akampatia noti ya shilingi elfu tano. Kilio kikaishia pale.
Minja na Rashid wakatoka!!!! Rashid hakuisha kujichekesha kila mara mbele ya bosi wake wa siku hiyo. Kwa mwendo uleule wa kuchukua teksi Minja na Rashid walipotea mbele ya eneo hilo la kimaskini na kutua maeneo ya Nyegezi wakatafuta mgahawa mzuri wakakaa na kuanza kunywa taratibu. Kisha maongezi yakaingilia kati, Minja akamueleza kila kitu Rashid juu ya zali/bahati iliyomwangukia kupendwa na mke wa tajiri.
Maelezo ya Minja si tu kwamba yalimpa wivu uliokithiri Rashid lakini pia yalimuweka katika kizungumkuti, hakuelewa kama alikuwa sahihi ama la!!
"Umesema John Mapulu ndio mume wa huyo binti!!!!"
"Ndio lakini huwezi kumjua" alijibu Minja huku akipiga funda kubwa la bia.
"John Mapulu!!!" Rashid alifanya tafakari ya miaka miwili nyuma katika kazi yake ya ulinzi aliamini kuwa huyu mtu anayezungumziwa na swahiba wake aliwahi kuwa bosi wake tena si mara moja kwani aliwahi kupumzishwa na kurejeshwa tena, na baadaye bosi wake alitoweka katika mazingira ya ajabu hivyo akapewa chake na kuachishwa kazi. Hawezi kuwa amesahau zama hizo kwani alikuwa analipwa vizuri sana na familia yake ilikuwa inaneemeka na kazi ya baba yao, lakini baada ya kuachishwa kazi mambo yakawa magumu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Namfahamu lakini mbona...."
"Wewe humjui nakwambia cha msingi nipe ushauri!!!" aliingilia kati Minja. Rashid akakaa kimya kwa sekunde kadhaa akiikodolea macho sahani iliyokuwa imesheheni nyama ambazo ni kama zilikuwa zimekosa mlaji.
"Minja hapa kuna namna!!!"
"Namna gani, unadhani nimetumia juju" aliuliza Minja.
"Hapana sivyo!!! ila huyo John huyo John Mapulu namfahamu hana uwezo wa kuzaa iweje useme mkewe ana ujauzito?" aliuliza kwa sauti ya chini Rashid, macho yakamtoka Minja akabakia na pande la nyama mdomoni bila kutafuna, kauli ile ilikuwa imefungua akili yake kwa kiasi kikubwa.
Akatulia hivyo kwa sekunde kadhaa bila kusema lolote. Kisha akatikisa kichwa kumaanisha kuwa ametambua jambo. Akili yake ilifanya kazi harakaharaka tamaa ya pesa ya kichaga ikamwingia, ikamtuma kumchenga Rashid ili aweze kula peke yake.
"Ah!! wanawake wa mjini hao, hebu achana naye" alisema Minja. Rashid akaafiki, baada ya nusu saa wakaagana. Safari hii kila mmoja aliondoka kivyake.
****
Matha baada ya kumhadaa Minja na kumsimamisha kazi aliamua kutokuwa mbinafsi na kumshirikisha suala hilo Michael ambaye mara nyingi alikuwa msikilizaji. Lakini katika maongezi ya siku hiyo hakuwa ameridhia maamuzi hayo yaliyotaka kufanywa na Matha, yaani kumtafutia kazi nyingine Minja ili kumuweka mbali na John.
"Na vipi siku akikutana na John, au akimpigia simu???" aliuliza Michael, Matha akakiri kuwa hali bado ni tete.
"Minja sio mropokaji ni muelewa sana" alijaribu kutetea Matha, Michael akakubali kwa shingo upande.
"Akithubutu kunichezea nitamuua!!!" alijisemea kwa sauti ya chini lakini Michael aliweza kumsikia.
"Kuliko kuua ni heri tutoroke Matha!!" alishauri Michael, Matha akamkazia macho, Michael akawahi kukwepesha macho yake. Matha akaaga na kuondoka, John na Bruno hawakuwa nyumbani.
Huo ni uoga wa kunguru!!! Akawaza Matha juu ya kauli ya Michael kuhusu kutoroka.
****
Ukaidi wa Minja mbele ya John ilikuwa dharau kubwa sana, John alijua lazima kuna kitu, hisia za kwamba Minja anaweza kuwa 'informer' na huenda ameishtukia dili yao ya kwenda kuiba Supermarket. John akawaeleza wasiwasi huo wenzake, hisia za John zikawashtua wenzake, mara moja msako Minja ukaanza. Sehemu ya kwanza kabisa ilikuwa kazini kwa Minja yaani sheli ambapo hakuwepo. Msako haukuishia hapo lilikuwa jeshi la watu wanne wenye mioyo ya kuua.
Minja alikuwa katika hatia asiyoitambua.
John alikuwa amekerwa sana na dharau aliyofanyiwa. Msako huu kwa upande wa John ulikuwa kwa faida ya Matha, alitaka kujua kuwa ni kwa jinsi gani Minja amemfahamu Matha tena kwa majina yote mawili kiufasaha.
"Au Matha ana uhusiano naye jamaa ananifanyia jeuri!!!" alihisi John, wivu ukachukua nafasi yake ukaanza kuikwaruza nafsi ya John, hasira ikajikaribisha katika kiti kilichokuwa wazi katika moyo wake.
"Nitamuua kwa mkono wangu!!!" aliapiza baada ya kumkosa pale sheli kwa mara ya tatu.
Wenzake na John walichukulia kuwa hizo ni hasira za kawaida ambazo John alikuwanazo lakini haikuwa hivyo ni wivu wa mapenzi ulikuwa unamshambulia tena shambulio la nguvu na la ghafla.
Msako ukatoka pale sheli na kuhamia nyumbani kwake, ramani ilikuwa tayari mkononi mwa kundi hili.
Wakashauriana waende usiku!!!!
*****
Kitanda kilikuwa hakilaliki, si kwa sababu ya godoro lililokuwa limechakaa sana bali kutokana na mgogoro wa nafsi, mke wa Rashid aliigundua hali hiyo kwa mumewe ambaye siku hiyo alipendezesha chumba kwa harufu ya bia tofauti na siku nyingine ambazo hunuka pombe za kienyeji.
"Baba Karim!!!....vipi mbona hulali"
"Sina tu usingizi mke wangu" alijibu kwa sauti ya kukwaruza.
Rashid alikuwa katika dimbwi kubwa la mawazo baada ya kupata taarifa kutoka kwa Minja. Umasikini ulikuwa unamtia katika fedheha kubwa, alidharauliwa na wala hakupendwa na mtu yeyote maana hakuwa na msaada wowote kwao. Wazo la utajiri kupitia kuusema ukweli unaomuhusu mke wa John lilimwingia lakini kisu kilikuwa kimeshikiliwa na Minja. Tamaa ikamwingia Rashid akatamani akishike yeye kisu hicho.
"Nitamweleza Minja na kama akikataa je?" alijiuliza.
"Akikataa nitaenda mwenyewe kwa John Mapulu" alijipatia jibu.
Mgogoro mkubwa wa nafsi ukautwaa usingizi wake, maumivu ya kichwa yakayeyusha usingizi wake. Rashid akaamua kuamka na kukaa kitandani, wakati huo mke wake alikuwa amelala tayari.
Nimeuchoka umasikini!!! alisema kwa nguvu kisha akajaribu tena kuutafuta usingizi.
Safari hii usingizi ulimchukua.
Siku iliyofuata akaamua iwe siku ya vitendo hakutaka kuchelewa zaidi. Kwa kuwa alipajua nyumbani kwa Minja aliamua kwenda usiku baada ya kuwa ametoka lindoni majira ya saa kumi na mbili jioni.
Siku nzima lindoni Rashid alikuwa anatazama vitu vya thamani huku akiamini kuwa iwapo Minja atakubaliana naye basi baada ya muda mfupi atakuwa na uwezo wa kuvinunua.
Ujio wa Minja nyumbani kwake siku moja iliyopita ulimzidishia tamaa zaidi ya kuipata pesa, miaka yake 40 aliyokuwanayo bado ilimruhusu kuwa na tamaa za kimwili, Rashid aliwatamani wanawake waliokuwa wakipishana katika maduka mbalimbali kununua vitu vya gharama.
"Nikizipata hawa watakuwa wananiheshimu na pia watakuwa wakinisalimia, hebu tazama wanavyonipita kama hawanioni vile!!!" Aliwaza Rashid, donge la hasira likamkaa kooni akajilazimisha kumeza mate lakini hayakupita. Akasonya!!
Alitamani jioni iweze kufika aijaribu bahati yake ya kupata pesa.
Jioni ilifika akaaga na kurejea nyumbani, hapo pia hakukaa sana alimuaga mkewe kuwa anatoka kisha akatoweka!! Hakusema anakwenda wapi.
*****
Chumba cha Minja kilikuwa kimya sana wakati anaingia, alijaribu kuita lakini hakupewa jibu lolote, lile giza lilimlazimu kutumia simu yake ya tochi kuweza kuona vyema ndani.
Chumba kilikuwa na harufu nzuri za manukato jambo ambalo halikuwa kawaida hata kidogo.
Jeuri ya pesa!!! aliwaza Rashid huku akichukua nafasi na kukaa.
Baada ya dakika kadhaa pakiwa na giza hivyo hivyo alisikia vishindo vya watu vikiingia ndani. Miale mikali ya tochi ilitua katika macho yake, alitumia viganja vyake kujikinga.
Maumivu makali katika paji la uso wake aliyasikilizia huku mwili wake ukiwa ardhini.
"Kwa nini leo hujaingia kazini??, kwa nini umeacha kazi tangu tufike siku zile??" Alisikia maswali yakimuelekea.
"Ni juzi tu ndio sijaenda jamani!!! sijaacha kazi, hata leo mchana nilikuwepo" alijitetea.
John alipatwa na ghadhabu akiwa nje ya chumba kile akiangalia hali ya usalama.huku akipuliza sigara yake.
"Fala huyo anawadanganya!!!" alikoroma kwa sauti ya hasira tena yenye kisilani, wivu juu ya mpenzi wake ulimtwaa kwa kiasi kikubwa. Aliamini kuwa yule ndani ya chumba kile alikuwa ni Minja.
Waliokuwa wameingia ndani waliposikia kauli inayoitwa kudanganywa moja kwa moja wakajua kuwa aliyekuwa mbele yao ni adui.
Dakika tano pekee zilitosha kumbadilisha Rashid na kuwa tayari kwa kuhamia kaburini. Ilikuwa ni kabali baabkubwa iliyomzidi nguvu mlinzi huyu ambaye hata chakula cha usiku alikuwa hajapata.
Timu nzima ya John ikajua kuwa imemuangamiza Minja.
Tamaa zikawa zimemponza Rashid, utajiri alioutaka ukawa umeingia shubiri. Mchezo asioujua mwanzo wake ukawa umetwaa uhai wake.
Rashid akatokomea na tamaa yake!!
******
Minja akiwa na jeuri ya pesa ambayo sasa ilikuwa imebaki kama shilingi elfu sitini. Aliichukia sana hali ya chumba chake kutokuwa na umeme, siku hiyo hakutaka kuuvuta moshi mkali wa kibatari, giza lilivyoanza kuwa totoro akaamua kutoka, kwa kuwa hakuwa na chochote cha thamani kinachoweza kuwavutia wezi aliurudishia mlango wa chumba chake na kutoweka, alikuwa amevalia nguo mpya alizokuwa amenunua siku hiyo, aliamini kuwa alikuwa amependeza sana. Pesa zile kidogo zilikuwa zinamuwasha, taratibu huku akiepuka kuchafua kiatu chake kilichokuwa kimeng'arishwa haswa alizipiga hatua hadi akafika katika 'bar' maarufu pande za Mabatini iliyokwenda kwa jina la 'Corner bar', akachagua meza ambayo ilikuwa tupu ikiwa imepambwa na viti vinne visivyokuwa na watu.
"We mwanamke!!!" alikoroma Minja, muhudumu akajikimbiza mara moja akasimama mbele ya Minja.
"Kasto laga (Castle lagger)" alibwatuka.
Muhudumu akachukua pesa na kuondoka kisha akarejea na kinywaji, Minja alianza kunywa taratibu kama mwanaume asiyekuwa na hofu ya pesa kumuishia. Baada ya pombe kumkaa sawa kichwani alipata ujasiri wa kwenda kumhadaa muhudumu ambaye alikuwa anashangaa shangaa huku na kule kutazama kama kuna mteja atamuita kwa ajili ya kutoa huduma.
"Njoo saa nne!!" yule muhudumu alimpa ahadi hiyo Minja. Minja hakutaka kurejea katika kijumba chake alichokuwa anakichukia kwa siku hiyo kutokana na giza lililokuwepo. Alichofanya ni kuhamia 'bar' nyingine huku akienda sawa na muda.
Saa nne kamili alikuwa amerejea 'Corner bar', muhudumu alikuwa tayari amevua sare zake. Akatokomea na Minja kama mpenzi wake wa siku nyingi sana.
Safari yao ikaishia nyumba ya kulala wageni.
"Mi silali lakini mwisho saa saba"
"Usijali" alijibu Minja huku akizivua nguo zake haraka haraka.
"Kwanza nipe pesa yangu kabisa!!"
"Shilingi ngapi??"
"Elfu tano"
Minja akatoa elfu kumi akampatia.
"Sihitaji chenji baki nayo" alisema kwa ujivuni Minja baada ya yule binti kuulizia kama Minja anayo 5000 iliyoshikana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Binti akatabasamu na yeye akaanza kuzipunguza nguo zake mwilini. Tayari kwa kutoa huduma.
Hakuna aliyekumbuka suala la kutumia kinga, na hakuna aliyejutia baada ya tendo.
Saa sita usiku Minja alikuwa anarejea nyumbani kwake, alijihisi mwepesi na aliyechangamka sana baada ya tendo hilo alilokuwa amelikosa kwa siku nyingi sana.
Alipokikaribia kibanda chake furaha yake ilianza kupungua kwa kasi, alilitambua joto lililokuwa linamnyanyasa katika kijumba chake ambacho hakikuwa na 'sealingboard'. Alitamani kurejea katika nyumba ya kulala wageni ila akakumbuka kuwa alilipia kwa masaa kadhaa tu na wala si kulala hadi asubuhi.
Akapiga kite cha hasira kisha akaingia katika kijumba chake cha kupanga kama amelazimishwa hivi. Giza lilimpokea, lakini kwa kutumia uzoefu wa eneo hilo alipapasa hadi akakifikia kitanda chake akajibwaga bila kushusha neti. Usingizi haukumpitia kwa wepesi alipanga mipango kabambe ya siku inayofuata.
"Hivi nianzie na John ama nile pesa za Matha!!!" Alijiuliza huku akijipiga bega lake kupambana na mbu waliokuwa wanamzengea. Minja alikuwa katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi, kauli aliyokuwa amepewa na rafiki yake Rashid juu ya tatizo la John la kutozaa na kijitambulisho cha ujauzito wa Matha vitu hivi vilimtia kizunguzungu, akajiuliza ni nini cha kufanya. Hakika alikuwa masikini na hii kwake aliiona kama bahati ya walau kuukwaa huu ugonjwa unaotawala Tanzania, ugonjwa wa umasikini, ugonjwa uliokosa tiba ya kudumu.
Tamaa za kuwa na mahusiano na Matha zilimtawala, roho mpenda sifa alimkaa mwilini akashindwa kubanduka.
"Matha atake asitake atakuwa mpenzi wangu wa siri....na kama akikataa namueleza John ukweli" Alijisemea Minja huku akizikumbuka raha alizozipata na yule muhudumu wa 'bar' katika nyumba ya kulala wageni. Aliamini kuwa sasa atakuwa akizipata raha hizo bila kulipia bali kulipwa.
Hali ya hewa ilibadilika taratibu, ulianza kuvuma upepo ambao ulipunguza joto kidogo pale ndani, kisha ikafuata miungurumo. Bila shaka ilikuwa dalili ya mvua.
Minja alikereka kutokana na hali hiyo kwani dari la chumba chake lilikuwa linavuja. Kwa mara nyingine alipiga tena kite cha hasira.
Miale ya radi za hapa na pale ilileta mwanga pale ndani, Minja akaona kitu ambacho hakukitilia maanani sana kwani aliamini yalikuwa mawazo tu.
Alikuwa ameiona sura ya Rashid mbele yake.
Rashi cha ulevi!! Huyu jamaa anakunywa pombe huyu!! Alisema kwa sauti ya juu kidogo kisha akacheka.
Akapuuzia akiamini ni mawazo tu, akaendelea kuwaza na kuwazua, mwanga wa radi ulipopiga tena, Minja akaamini hapakuwa na mawazo ya namna hiyo, kulikuwa na kitu chini ya kimeza chake.
Mara moja akaiwasha simu yake akapapasa kidogo akapata kiberiti akakiwasha kimshumaa kilichokuwa kinakaribia kuisha. Kama vile amesukumwa kwa mitambo maalum alijikuta anajibamiza kitandani akasimama tuli akiwa ameyakodoa macho yake.
Alikuwa ni Rashid akiwa amekodoa macho na kutoa ulimi nje!!! Hakuwa Rashid tena alikuwa hayati Rashid.
Minja alitamani kumeza mate kulainisha koo ili aweze kupiga kelele lakini kinywa kilikuwa kimekauka sana ikashindikana. Upepo ukavuma tena. Mshumaa ukazimika!!! Hofu ikaongezeka, haikuwa ndoto tena Minja alikuwa chumba kimoja na maiti. Alitamani kukimbia lakini akajivika ujasiri alikuwa anatetemeka akapapasa tena akakipata kiberiti akawasha tena mshumaa, ukawaka. Akapiga hatua, akafika mahali ulipokuwa mwili wa Rashid.
"Minja! Minja! usimguse!!! utaacha ushahidi" Sauti ya ndani (Conciousness) ikamwambia Minja, akashtuka akasimama wima akaanza kurudi nyuma, joto katika suruali yake mpya lilitoa jawabu la mkojo uliopita bila idhini maalumu kutoka kwa muhusika.
Upepo ulivuma tena, mshumaa ukazima Minja hakuuwasha tena.
Wazo la kukimbia likavamia ubongo wake, wazo hilo likaambatana na milango ya jela. Minja akatetereka kidogo aanguke akahimili kuendelea kusimama. Harufu ya kwenda jela ikamtuma kukimbia, hakuna kitu alichokiogopa kama polisi bila kuchukua chochote zaidi ya pesa alizokuwa amezihifadhi chini ya godoro lake Minja alitoka usiku uleule bila kumwambia yeyote.
Hatia ya mauaji ikatembea naye kila hatua aliyokuwa akinyanyua. Ladha tamu ya pesa yake ikapotea, mawazo ya utajiri yakayeyuka.
Minja akawa mfuasi wa Hatia, kila mara Hatia ilivyochachamaa ndivyo ndugu yake aitwae hofu alikurupuka na kumtetemesha Minja. Jasho likawa linamvuja 'Singlend' yake ikazidiwa ikaruhusu na shati lake kuubeba mzigo wa jasho. Minja hakujua ni wapi anaelekea. Alichowaza wakati huo ni kutoroka!!! Hatia ikawa inampa suluba takatifu!!
*****
John Mapulu baada ya tukio hilo la mauaji alitaka kurejea nyumbani kwake lakini akakumbuka kuwa zilikuwa zimepita siku mbili hajaenda kumjulia hali Joyce Keto katika kasri lao jingine walilolipata kwa shughuli za kijambazi. Aliagana na wenzake akaelekea Nyasaka, jirani na shule ya mwanzo na upili ya Jerry's.
Ulikuwa ni usiku sana lakini John aliamua kuwa kwa usiku huo azungumze na Joyce kuhusu Michael Msombe. Hatia iliyokuwa inamkabili kuhusu ujauzito wa Joyce ilikuwa imemzidi uzito akaamua kuigawa kwa Joyce ili aone kama nafsi yake itakuwa huru, kwa kiasi kikubwa kifo cha Minja kilikuwa kimempa ahueni, aliamini kuwa mwanaume huyo kuna jambo la siri alikuwa anafanya na Matha, hivyo hata kabla hajalifahamu ni vyema alikuwa amemwondoa duniani.
John hakuwa tayari kumshuhudia Matha na mwanaume mwingine. Alikuwa anampenda sana, japo hakuwa na uwezo wa kumzalisha. Hiyo pia ilimsumbua kichwa kwani Matha hakuwa akijua lolote juu ya tatizo hilo..
Bahati nzuri Joyce alikuwa hajalala hadi muda huo kuna mfululizo wa sinema ya 'Nikita' alikuwa anaitazama. Ni yeye aliyekwenda kumfungulia John mlango.
Sura ya Joyce Keto ilimsababisha John kukosa ujasiri wa kuzungumza naye juu ya suala la Michael, ujasiri wote ukawa umeyeyuka!!!
"Mambo bro!!"
"Poa Joy, hulali wewe"
"Nimelala sana mchana, hata sina usingizi kwa sasa"
"Aaah!! ok!!" alijibu John huku akichukua nafasi katika moja ya sofa pale sebuleni.
John alikaa bila kusema lolote kwa dakika mbili, Joyce alikuwa bize anatazama mtiririko ule wa 'Nikita'.
"Rajab yupo!!" aliuliza.
"Yeah!! watakuwepo lakini walilala mapema"
"Basi utamwambia nilikuja" alisema John kisha akasimama na kuaga.
Ujasiri wa John ulikuwa umeyeyuka, alikuwa amepata wazo la kwenda kwa Matha aliamini huenda ndiye mtu sahihi wa kugawana naye ile hatia, japo Matha alikuwa hajui kama Michael alikuwa na uhusiano na Joyce ama la. John alikanyaga mafuta ya gari kwa kujitawala hadi akafika Buzuluga. Akazima injini ya gari yake katika moja ya sehemu za kuhifadhi magari akatembea kwa mwendo wa miguu kuanza kuzipanda ngazi ambazo zingemfikisha katika chumba cha Matha ghorofani.
"Kesho saa kumi jioni nitakutafuta"
"Uwe na namba hiyo hiyo usiweke ile ya zamani"
"Usijali usijali"
"Hakitaharibika kitu!!"
Ilisikika sauti ya Matha ikijibishana katika simu na mtu ambaye sauti yake haikusikika bali ilikoroma kumaanisha kwamba alikuwa ni mwanaume, John alisikia kila neno alilosema Matha kwa sababu ilikuwa ni usiku sana na kila mtu alikuwa amelala.
Wivu ukamvamia!! ukampiga mtama akaanguka, akajikongoja akainuka. Wivu aliodhani ameuzika kwa kumuua Minja ulikuwa umefufuka tena. Hasira zilipanda zikapita kipimo, John akauma meno kupambana na ghadhabu yake. Kinyumenyume akarejea hatua kadhaa, akataka kuondoka mara anataka kuendelea agonge hodi akawa anaenda mbele na kurudi nyuma.
Akawa kama kichaa hivi!! hatimaye akaamua kuondoka. Alikuwa amechukia sana japo hakuwa na uhakika huyo mwanaume ni nani kwa Matha.
"Matha kwanini ananifanyia hivi??" alijiuliza John wakati anaitoa gari sehemu alipokuwa ameihifadhi.
"Unasemaje bosi!!" aliulizwa na aliyehusika na kuingia na kutoka kwa magari. Kumbe alivyoongea alisikika. John hakujibu kitu akaondoka zake. Akaamua kuelekea nyumbani, mawazo tele yakamtawala, alimfikiria mwanaume aliyetaka kuingia katika anga zake kwa kumchukua Matha wake.
Kesho nitamjua lazima, saa kumi jioni!!!! alifikiria John huku akizidi kuiendesha gari yake kwa umakini.
*****
Kelele za simu yake alizifananisha na ule mlio wa 'alarm' akajiuliza aliitegesha kwa sababu zipi za maana. Akabonyeza kitufe bila kufumbua macho ikaacha kutoa mlio, baada ya dakika moja mlio ukaanza tena akaamka akiwa ametaharuki, aliamini simu ile haikuwa ikimtendea haki, macho makubwa yaliyokuwa yamekodoa yalitua katika simu yake.
Haikuwa alarm kama alivyodhani, ilikuwa namba mpya inampigia. Kidogo Matha aipuuzie lakini pia aliamua apokee ili ampe vidonge vyake mpigaji ambaye hajui kuwa ule ni usiku.
Matha alipopokea alikutana na sauti ya kiume iliyokuwa katika uoga.
"Mi Minja..nahitaji sana kuonana nawe" Sauti hiyo ikampasua donge la usingizi likayeyuka, akakaa kitako, na hakujua kama amekaa uchi. Minja hakuielezea shida yake katika simu alihitaji kumuona Matha, ndipo Matha akampa ahadi wakutane siku inayofuata majira ya saa kumi jioni. Kumbe wakati wote wa mazungumzo sikio la John lilikuwa makini kunasa kila kitu.
Hofu kuu ilimtanda Matha hakujua ni nini kimeharibika ghafla kiasi hicho, alitaka kumpigia Michael lakini akasita alihofia huenda angeweza kuwa karibu na John.
Hatia kuu ikamkaba kooni, akainuka akachukua maji yasiyochemshwa katika moja ya ndoo zilizokuwa ndani akajaribu kunywa, yalikuwa ya moto tena yenye chumvi akajilazimisha kumeza funda moja.
Hakuongeza tena!!! akakaa kitandani, kichwa kikaanza kumuuma. Alijutia mengi sana lakini, kubwa lililomnyanyasa ni mimba aliyokuwa nayo.
Matha akatanabai kwamba yupo katika vita kubwa sana, halafu yeye hana silaha wala hajaamua kujihami.
Akaisogelea kabati yake akatoa bunduki yake akaitazama kwa jicho la upendo kisha akaibusu. Akachukua na kisu chake akakibusu pia.
Nitamuua Minja nipunguze mateso haya!!!! alijiapiza Matha kisha akazirudisha silaha zake pahala pake.
Baada ya hapo alirejea kitandani akafanya sala fupi kumuomba Mungu amuepushe na balaa lililopo mbele yake, sala ilikuwa katika mtindo wa kubahatisha kwani alikuwa na siku nyingi sana hajaenda kanisani. Aliulazimisha usingizi kwa kujigeuza hapa na pale hatimaye kifo hicho cha muda kikampitia.
Asubuhi na mapema tayari Matha alikuwa amedamka, alifanya usafi wa hapa na pale kisha akajitosa bafuni akapambana na maji ya baridi, tayari ilikuwa saa mbili asubuhi akajipamba kidogo, akavaa suruali yake na blauzi chini akaweka viatu vya wazi akaufunga mlango akaondoka na kuingia katika mizunguko isiyokuwa rasmi ilimradi tu muda usogee na kuifikia saa kumi.
Hapa na pale hatimaye ilitimu saa nane na nusu, funguo zilikuwa zinatekenya kitasa cha mlango wake, mlango ukafunguka akaingia ndani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Upo wapi muda huu??” aliuliza kwenye simu.
“Nipo huku Makoroboi”
“Tukutane hapo kwenye maduka ya nguo karibu na geti la kuingia chuoni” alitoa maelekezo Matha, Minja upande wa pili akawa ameelewa tayari, simu ikakatwa.
Matha akaingia kuoga tena kwa mara ya pili, akajipamba tena akatia kisu pamoja na bastola yake katika mkoba wake, akauweka kwapani akajiangalia kwenye kioo kisha akatoka.
*****
John alifika na kujitupia katika kitanda chake bila kuvua viatu, alikuwa anashambuliwa na wivu mkali, alikuwa na hasira kali juu ya mwizi wa mpenzi wake. John Mapulu alikuwa anajiuliza ni nani huyo alikuwa na ujasiri wa kumgusa sharubu, midomo ikawa inatetemeka usingizi ukakataa kukaribia pale alipokuwa. Akasimama akajongea hadi sebuleni akaliendea jokofu akafungua akakutana na chupa ya kilevi, akaitwaa akaimimina katika glasi akainywa kwa vurugu, akawasha luninga akakutana na mechi ya mpira wa miguu akazimisha. Akaendelea kuubugia kwa fujo. Katika mawazo ya hapa na pale akapitiwa na usingizi hadi saa moja asubuhi aliposhtuka.
Alikodoa macho hapa na pale hakuna aliyekuwa ameamka hapo ndani, akaitwaa ile chupa ya mvinyo akaiweka juu ya jokofu akarejea chumbani kwake.
Akili yake ilikuwa katika mvutano mkubwa sana, siku hiyo ilikuwa ndio siku ya tukio la kwenda kuiba Supermarket kwa kutumia silaha lakini siku hiyo pia lilikuwepo tukio kubwa sana la kwenda kumfumania Matha. John akachekecha mawazo hapa na pale akaamua kuchagua moja. Kwenda kufumania!!!
Akanyanyua simu yake akabonyeza namba za mkuu wa kitengo cha maandalizi ya tukio la wizi.
“Mambo vipi kaka” alisalimia John kwa unyonge.
“Shwari kaka, vipi kwema”
“Ebwana si shwari sana, nitachelewa kuja huko, kichwa kinanisumbua sana” alidanganya John. Upande wa pili haukupinga akakubaliwa. Akakata simu.
Usingizi ulimchukua tena hadi saa nane mchana alivyoamka, akafanya maandalizi yake bila kumshirikisha mtu yeyote.
Saa tisa kasorobo tayari alikuwa maeneo yaliyomruhusu kuitazama vyema nyumba aliyokuwa akiishi Matha, ilimchukua dakika arobaini kumshuhudia Matha akitoka katika chumba chake. Laiti kama asingekuwa amelikariri umbo la Matha asingeweza kumtambua na angesubiri kwa muda mrefu bila kumuona. Matha alikuwa amevalia baibui la staili ya kininja alikuwa anaonekana macho peke yake. Hali hiyo ilimtikisa John, akazidi kuamini kuwa Matha alikuwa anaenda kufanya jambo baya.
Matha bila kujua kuwa anafatiliwa alielekea barabarani akaangaza hapa na pale akanyanyua mkono wake wa kuume akaita taksi, haraka haraka dereva aliyekuwa amemuona Matha aliifikisha gari yake Matha akaingia ndani.
John akasubiri ile teksi ilivyoanza kuondoka naye akaingia katika teksi aliyokuwa amekodi.
“Fuata gari hiyo!!” alitoa maelekezo hayo John, dereva akafuata maelekezo. Gari mbili zikawa zinafuatana bila gari ya mbele kuwa na habari juu ya hilo, John alikuwa amevaa miwani nyekundu kuziba macho yake yaliyokuwa mekundu sana, hakutaka kumtisha dereva.
*****
***WIVU umempelekea JOHN kuamua kumuua MINJA lakini bahati mbaya inamuangukia RASHID nakufa na umasikini wake.
***MINJA anajikuta katika HATIA ya mauaji...harufu ya jela inampa wazo kuu la kukimbia.......
***MATHA anapigiwa simu na mwanaume usiku...JOHN anasikia mazungumzo haya...WIVU unamkumba tena anaamua kufuatilia ni nani mwizi wake.
***MATHA ametembea na kisu na bastola...je? anaenda kuua ama???
HATIA INASUMBUA WAHUSIKA WOTE WA RIWAYA HII.
NAWE MSOMAJI UNA HATIA YAKO.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment