Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

KIVULI (THE CATCHING SHADOW) - 3

 





    Simulizi : Kivuli (The Catching Shadow)

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Hivyo Kama kawaida kwa maraya pili mambo yalitiki tena kwa Johari. N kweli akapata ujauzito na kuzidi kumfurahisha Malcom na ndugu zake.

    Na miezi tisa baadae akajifungua, safari hiyo alijifungua watoto mapacha wawili, wasiofanana, wa kike na wa kiume, na kuzidisha furaha maradufu kwenye familia hiyo ya Malcom na ndugu zake ya akina Munyisi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Johari alifurahia sana mafanikio ya mchezo wake mchafu. Na akafurahi pia kuwa hana haja ya kuuendeleza kwasababu watoto watatu walimtosha sana yeye na Malcom. Hivyo Johari alijiona ni shujaa aliyeweza pambana na lana ya uovu aliowahi kuufanya na kuushinda. Na nyodo zake kwa ndugu wa Malcom zikazidi maradufu hadi wakajutia madhira waliyomfanyia. Kwanza Johari watoto zake hakutaka mtu awaguse, aliwalea kama kitu gani sijui!, aliwalea kama ‘maprince’ na ‘princess’. Ndugu wote kimdomomdomo ‘kikawakatika’ wakabaki kuangalia malezi ya kiulaya ulaya.

    ...................................



    Basi miaka ikaenda na kichwani mwake Johari alimsahau kabisa yule chizi, utadhani haikuwahi kutokea kwenye maisha yake kutembea na mtu chizi, yeye aliwaza furaha yake na Malcom na watoto wao watatu, Miujiza, Flora na Florian. Kwake watoto walikuwa ni wa Malcom sio mtu chizi. Hakuwa hata na haja ya kujua yule mtu chizi aliishia vipi maisha yake, kwake yule mtu hakuwa na umuhimu wowote. Kwake kilichokuwa na umuhimu kilikuwa ni furaha ya familia yake na mumewe. Na kweli hakuna kilichowabughudhi tena familia yao. Waliishi kwa raha mustarehe.



    Ila sasa mikasa ikawa upande wa yule chizi. Wakati Johari, alisahau juu ya yule chizi, kwa upande wa yule chizi haikuwa hivyo. Kwa upande wake alimuwaza Johari kwa mapenzi makubwa.



    Pamoja na uchizi wake, alimkumbuka vizuri Johari, kwa sura na hasa alikumbuka uzuri wake. Na alimuwaza sana na ‘kummiss’ sana. Alipokuwa akilala alimuota, tena mara nyengine alihisi Johari kamsimamia pembeni na kuamka kwa furaha ili kumkumbatia na kumkaribisha bomani ilihali hakukuwa na Johari bali mawazo yake tu ya kichizi. Na alipogundua kuwa Johari hakuwa akija tena bomani yule chizi alikuwa akilia.



    Katika hali isiyo ya kawaida, ilitokea siku moja, yule chizi kakatiza mitaa fulani na kusikia wimbo wa mapenzi ukipigwa toka kwenye redio ya duka la mtaani huko. Wimbo huo ulikuwa na mashairi ya mtu aliyemkosa mpenzi wake, na ulikuwa na ‘tyun’ ya kusikitisha iliyogusa moyo na kuwasilisha huzuni ya kimapenzi. Basi katika hali ya kushangaza kabisa yule chizi alijikuta akitoa machozi na kulia. Kwa uchungu na maumivu ya moyo alijikuta akikosa nguvu kabisa ya kuendelea na kuzurura kwake na akabaki mbele ya duka hilo kusikiliza wimbo wa hisia uliokuwa ukipigwa hadi akashindwa kuendela na safari zake za kichizi na akabaki chini kulia kwa uchungu hivi kwamba watu waliomuona walishangazwa sana na kumjaalilia, na kumuwazia iwaje mtu taahira kama yeye, ashikwe na hisia kali za wimbo wa kimapenzi toka redioni hadi afikie hatua ya kutoa machozi. Hivyo ndivyo maisha ya ya yule chizi yalivyoendelea mitaani.



    Basi siku moja, jambo la ajabu lilitokea kwenye maisha ya yule chizi. Siku hiyo akiwa katika kuzurura kwake na kuokoteza alikutana na mwanamama mmoja na bintiye. Katika hali isiyokuwa kawaida yule mwanamama alishtuka sana kumuona yule mwanamume chizi kisha ghafla akaanza ku,piga ukelele mkali na kulia kwa nguvu sana na kushtua wapita njia wengine ikiwamo yule chizi, huku binti wa mama huyo akiwa haelewi mama yake kapatwa na kitu gani.



    Yule mama katika kulia kwake alitoa kauli, akisema, “nimekwisha, nimekwisha, hakika leo hii nimekwisha”, alilia yule mama na mara akaanza kukimbia hovyo huku mwanae akimfukuzia na kumkamata. Ndipo yule mama akamgeukia yule chizi na kumnyooshea kidole na kusema kwa uchungu, “wewe Rashad wewe, ulipaswa utokomee wewe, usiwepo tena, kijana mbaya kabisa. Nyota yako niliyo ipotezea mbali naona sikuipoteza vya kutosha”, alilia huyo mwanamama, huku bintiye akiwa kamshikilia huku kachanganyikiwa na kutoamini kilichokuwa kinaendelea, na wapita njia wengine walikuwa wakiwamshangaa huyo mama na bintiye.



    Wakati huo yule chizi, alikuwa katulia ghafla. Alitulia visivyo kawaida kwa mtu mwenye uchizi kama yeye, huku akiwa kawatolea macho yule mama na bintiye. Mara akaanza kutetemeka, na kupepesuka, hivi kwamba akawa akijaribu kusimama vizuri ili asianguke. Na mara, kwa hali ya kustaajabisha alihisi kama kitu kkikimtoka mwilini mwake ghafla. Huku yule mwanamama aliyekuwa na binti yake alianza kupiga mayowe zaidi kama mtu aliyeingiwa na ukichaa.



    Kumbe ule uchizi ulikuwa umehamia kwa yule mama na kumhama yule chizi. Na watu wote waliokuwapo eneo hilo walibaki wakishangaa walichokuwa wakishuhudia kwa macho yao mawili, walistaajabu kuona jinsi yule mama alivyowehuka kwa ukichaa huku yule chizi akiwa katulia na aliyeonekana kama kupona ukichaa.



    Basi yule mama aliyeingiwa na ukichaa alizidi kuchanganyikiwa na kisha akajinasua toka kwenye mikono ya binti yake na kuanza kutokomea mitaani huku bintiye akimlilia na kumfuatia na kumkamata. Na mara umati mkubwa wa watu ukawa umezunguka eneo hilo kujionea hekaheka.



    Basi yule mwanamume ambaye uchizi ulimtoka, alikuwa kapigwa bumbuwazi, na kujishangaa na kujiuliza, amepatwa na nini na kuwauliza watu hapo ni wapi, na aliwauliza kwanini yeye alikuwa mchafu namna ile. Watu walimzunguka na kumjaalilia wakimshangaa kwa kuona jinsi mtu chizi alivyopona na kuwa na akili timamu katika namna ya kushangaza kabisa na huku wengine wakimuonea huruma yule mama aliyegeuka chizi.



    Wingi wa watu walizunguka eneo lile na kushangaa ulifanya polisi kufika eneo lile, kufuatilia nini kilikuwa kinaendelea. Na kisha wakambeba yule mama aliyegeuka chizi na binti yake pamoja na yule jamaa aliyepona uchizi na kwenda nao kituoni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walipofika kituoni, binti wa yule mama alijitambulisha kuwa alikuwa anaitwa Zena, na kueleza kuwa mama yake alipatwa na ukichaa ghafla baada ya kumuona Rashad ambaye ni mpwa wa mama ke huyo, yani Rashad alikuwa ni mtoto wa kaka yake yule mama aliyegeuka chizi. Kumbe yule mwanamume chizi aliyepona, jina lake halisi lilikuwa ni Rashad. Na yule mama aliyeingiwa na uchizi kisha yeye akapona alikuwa ni shangazi yake na hivyo yule binti wa yule mama alikuwa ni binti wa amu yake ama shangazi. Askari walistaajabu hata zaidi kujua uchizi ulimuhama yule jamaa na kumhamia shangazi yake ulikuwa ni mkasa ulioshangaza kweli mapolisi hasa ikizingatiwa dola haimini katika kutokea mambo yanadhanika kuwa ya kichawichawi.



    Basi huo ukawa mwisho wa Rashad kuishi maisha ya kusikitisha ya uchizi na kuzurura na kulala majalalani, maisha ambayo aliyaishi kwa zaidi ya miaka kumi.



    Ukweli hasa wa maisha ya Rashad ulikuwa ni mkasa mrefu na wa aina yako nao ulikuwa kama ufuatao;



    Rashad alikuwa kazaliwa kwa baba yake na mama yake waliokuwa wakimpenda sana. Yeye alikuwa ndiyo mtoto wao wa kwanza, tena wa kiume na mwenye akili sana toka utotoni hivi kwamba kila mtu alimpenda. Pia alikuwa na mdogo wake wa kike aliyeitwa Sarha. Yeye Rashad na Sarha waliishi kwa furaha sana na upendo wakiwa pamoja na wazazi wao, walipata kila kitu na walikuwa na akili hasa. Baba yao alikuwa ni mfanyabiashara mwenye mali kubwa. Na alikuwa na moyo wa kutoa sana kwa ndugu zake. Na alikuwa kaizoesha familia yake kuchangamana na ndugu zake kwa furaha na kusaidia ndugu zake kila walipohitaji msaada.



    Maisha yao yaliendela hivyo mpaka siku moja ya bahati mbaya, baba yao alipokuwa akitoka safari ya mbali na kupata ajali ya gari na kupoteza maisha. Lilikuwa ni pigo kubwa, kwa familia na kwa ndugu wote. Na msiba ulikuwa mkubwa na ndugu wote walionesha kuguswa saana na msiba. Ila mambo yakaanza kubadilika baada ya msiba kuisha.



    Kwanza kabisa kaka wa marehemu wakaanza kudai kuwa nyumba ambayo ndugu yao kaacha ilikuwa imejengwa kwenye kiwanja cha marehemu baba yao. Hivyo nyumba hiyo ni mali ya familia nzima na si ya mke na watoto wa marehemu kaka yao peke yao. Mzozo ukawa mkubwa hivi kwamba nyumba hiyo ikauzwa ili wagawane fedha eti kila mtu apate chake, na hilo lilifanyika haraka bila hata ya kujali hali ya familia iliyoachwa na marehemu.



    Kama haikutosha mama yao akina Rashad akataka aende kuishi kwa ndugu zake, mara familia ya mumewe ikang’ang’ania kuwa kwa mila za kwao watoto wa marehemu hawapaswi kuishi ujombani bali kwa mashangazi zao. Hivyo kama mama huyo ataondoka basi aondoke yeye na aache watoto kwa shangazi na baba zao wakubwa na wadogo. Mama yao akina Rashad, bi Aisha alishindwa kukubali kuacha wanae peke yao kwa shangazi zao, kwa maana alifahamu aina ya maisha waliyoishi, maisha yaliyokosa muamko na kuishi kizamani na kienyeji sana na alijua watoto wake wasingeweza kuishi kwa furaha bila yeye.



    Hicho kilikuwa ni kipindi cha majonzi sana kwa Aisha na wanawe, Rashad na Sarha. Yale maisha ya kula na kusaza, ‘family picnics’ na kupata kila walichokuwa wakikitaka yalitoweka. Sasa walikuwa wakiishi kwa watu, shangazi zao kina Rashad, huko mikoani tena kijijini, maisha magumu tena yale ya kilimo tu na hakkukuwa na kipato chochote cha maana na watu waliokuwa huko walikuwa na roho mbaya mtindo mmoja.



    Ila maisha yaliendelea vivyo hivyo na Rashad na mdogo wake walijiunga na shule ya jirani na huko kijijini. Kwa kuwa walitoka shule za ‘international’, walijikuta wakiwa wanafahamu vitu vingi kuliko wanafunzi wezao wa kijijini, tena walikuwa wakiijua lugha ya kiingereza vizuri, na kuwafanya wafanye vizuri sana darasani.



    Walimu wao waliwapenda sana na kuwatumia kama mifano ya kuelekezea wanafunzi wengine namna uvaaji wa sare ya shule, utulivu darasani na bidii katika masomo.



    Hatimaye mama yao alianza kupata matumaini kuwa ipo siku ya inakuja ambayo watoto wake wangemtoa kimasomaso kwa kuondokana na umaskini na majanga yaliyowapata na kuishi tena yale maisha ya furaha waliyoishi awali.



    Wakati huo, walikuwa wakiishi nyumba moja na shangazi yao akina Rashad aliyeitwa mama Zena. Shangazi huyo alikuwa na roho mbaya tena ya waziwazi. Hakupenda familia ya marehemu kaka yake hata kidogo. Aliwaona kuwa ni watu waliokuwa wakiringa sana enzi baba yao yu hai na chuki zake zilimfanya awazie sana jinsi familia ya kaka yake ‘itakavyosoma joto ya jiwe’.



    Wakati huo Aisha, alikuwa mwema kwa wifi yake, kwa kumtabasamia na kumtabasamia na kumuongelesha maongezi ya kufurahisha, kumbe wifi yake huyo alikuwa akimchukia vibaya sana.



    Sasa, Zena binti wa huyo mama Zena, alikuwa akisoma darasa moja na Rashad. Ila sasa yeye alikuwa ni ‘kilaza’, darasani hajiwezi kabisa, alikuwa mtu wakushika nafasi za mwisho darasani. Tofauti kabisa na Rashad ambaye alijulikana kama mwenye akili sana darasani. Kumbe kitu hicho kilimuuma sana mama Zena. Hakupenda kabisa kuona akina Rashad na mdogo wake wanakuwa watoto wa kutolewa mfano. Ilimuuma kuwa watototo zake yeye ndio walikuwa wakitolewa mifano ya kijinga kijinga.



    Maisha yaliendelea, na Rashad aliendelea na elimu yake hadi akafika kidato cha nne na kufanya mtihani wa taifa. Matokeo yalipotoka, Rashad alifaulu kwa alama za juu sana na kupongezwa na kila mtu. Kijiji kizima kilimsifu kwa kufanya vizuri darasani. Zena kwa upande mwengine naye alikuwa kafaulu vizuri tu na alipongezwa na watu, na alijiunga kufurahia matokeo ya mtihani pamoja na Rashad.



    Katika hali ya roho mbaya ya waziwazi, mama Zena hakufurahia jinsi mwanae alivyofurahia matokeo ya mtihani pamoja na Rashad. Yeye hakufurahia kuwa mwanae hakupata alama za juu kumzidi Rashad. Yeye hakupenda hilo hata kidogo alitaka binti yake ndio awe amefaulu zaidi na Rashad awe aliyefeli kabisakabisa. Sasa roho yake ilimuuma zaidi pale nafasi za shule zilipotoka na Rashad akawa kapangiwa kwenda kusoma shule moja iliyokuwa ikisifika sana kuwa ni shule ambayo wanafunzi wanaoenda ni wale waliofaulu vizuri kupitiliza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kwa jinsi alivyojawa na roho mbaya, mama Zena akaamua kuwa Rashad ni kijana wa kupotezwa kwa namna yeyote ile. Akaamua kuwa lazima amkomeshe kijana huyo na mama yake kwa ujumla kwa kumpoteza kabisa na kumfuta toka kwenye maisha na kufupisha kabisa safari yake ya kimasomo. Hivyo akaamua kumuendea kijana huyo kwa mganga wa kichawi, ili kumroga na kumtokomeza kabisa. Hakuna mtu aliyefikiria mama Zena alikuwa na uwezo wa kufikiria kufanya jambo baya kama hilo pamoja na kuwa walifahamu roho mbaya yake.



    Basi usiku mmoja wa kuamkia asubuhi ambayo Rashad ilikuwa anapaswa aondoke kwenda shule aliyopangiwa, Bi Aisha alikaa na wanawe mkekani kwenye baraza ya nyumba waliyokuwa wakikaa ili kuzungumza nao na kuwaambia jinsi alivyokuwa na matumaini kuwa siku moja shida zao zote zitaisha na wataishi kwa furaha kama zamani. Aisha alizungumza na wanawe kwa kujivunia, maana alijua kuwa walikuwa ni watoto wenye akili nyingi na vile Rashad alikuwa akienda kusoma katika shule bora kabisa ya serikali nchini, Aisha aliuhisi kabisa kuwa mkono wa mungu ulikuwa unaanza kuinua tena familia yake. Kwenye maongezi hayo Rashad alimuambia mama yake ni jinsi gani anavyompenda na kumuahidi kuwa atafanya jitihada huko shuleni anakokwenda na kuja kuwa mtu mwenye mafanikio sana na kurudisha yale maisha ya furaha mama yake aliyokuwa akiombea yarudi tena.



    Kumbe, maongezi ya usiku ule kati ya Aisha na watoto zake akiwamo Rashad, yalikuwa ndio maongezi ya mwisho kufanyika kati ya Aisha na mwanae Rashad. Kwa maana usiku wa manane wa usiku huo Rashad aliamka kwa mayowe na makelele, na kupiga kelele nyingi na kuwaamsha mama yake na mdogo wake na ndugu zao waliokuwa wakiishi nyumba moja na majirani wa hapo kijijini.



    Aisha, Sarha na ndugu wengine walipokimbilia chumbani kwa Rashad walimkuta akiruka ruka juu ya kitanda kama mtu aliyewehuka. Walishtuka sana kwa maana haikuwa hali ya kawaida kwa mtu mzima aliyetimamu kufanya kitu kama kile usiku wa manane. Basi wakajaribu kumuongelesha na kumtuliza bila mafanikio, na wao wakazidi kuchanganyikiwa na kujiuliza nini kilikuwa kimempata Rashad. Majirani walipoingia ndani humo walishangaa sana kuona kilichokuwa kikiendelea. Na wote wakabaini kuwa Rashad alikuwa kapandwa na wendawazimu. Na ukweli ulikuwa ndio huo kuwa Rashad alikuwa kaingiwa na uwendawazimu.



    Kumbe wakati huo Rashad anaingiwa na ukichaa, shangazi yake, mama Zena alikuwa yuko kwa mganga ‘akimkoroga akili’ ili awe mwendawazimu. Kwa mganga kwenyewe kulikuwa porini kwelikweli na kunakotisha na giza lililokuwepo kulifanya kutishe hata zaidi, ila shangazi huyo kutokana na jinsi alivyodhamiria hasa kumfanyia Rashad ubaya, alikuwa na ari yote iliyomuwezesha kuwepo huko mizimuni. Akiwa huko mama Zena alipewa ‘kizizi’ na mganga kisha mganga akamwambia kuwa anuie kumtokomeza Rashad na kisha atupe hicho kizizi kama ishara ya kumpoteza Rashad atokomee kusikojulikana. Basi mama Zena alishika kizizi cha mganga na kuanza kunuia. “ninataka, Rashad aingiwe na ukichaa, na ukichaa wake umpande hivi kwamba apotee na atokomee mbali, mbali sana na asirudi tena na asipatikane tena” baada ya kusema maneno hayo alikitupa kile kizizi mbali kwenye vichaka.



    Naam! wakati mama Zena akinuia maovu yale, basi Rashad uchizi wake ukamkolea kichwani na akajinasua toka mikononi mwa watu waliomshikilia kumtuliza, na akatoka ndani mwao mbio na kuanza kukimbia hovyo kwenye njia za kijiji huku mama yake na watu wengine wakijaribu kumfukuzia bila mafanikio. Hadi jua lilipochomoza asubuhi, wanakijiji walikuwa hawajampata Rashad na hakuna aliyejua kakimbilia wapi. Basi hivyo ndivyo Rashad alipata ukichaa na kutokomea asipatikane tena na ndugu zake.



    Lilikuwa ni pigo kubwa kwa mama yake. Alichanganyikiwa na kushindwa kuelewa ni janga la namna gani lilimpata mwanae. Hakuna polisi wala mtu aliyeweza kumpata Rashad miaka na miaka ikapita. Bi Aisha aliumia sana, kwa kilio na kufanya sala, akiamini kupitia dua zake mungu angemsaidia mwanae kuonekana tena, ila wala halikutokea. Alimuwaza sana mwanae na kumkumbuka jinsi alivyomlea, hasa hakusahau ule usiku wa mwisho kabla hajapatwa na ukichaa. Alikumbuka ule usiku jinsi Rashad alivyomwambia kuwa anampenda sana, alikumbuka jinsi Rashad alivyoahidi kufanya vizuri ili kumtoa kimasomaso siku moja na kuagana na dhiki zilizokuwa zimetamalaki kwenye maisha yao, aliwaza sana bi Aisha hadi akafika hatua ya kukufuru na kumuuluza mungu, “ina maana zile dua na sala za kumuombea afanye vizuri na kule kufaulu kwake, kote kulitokea ili tu kunipa tumaini kabla ya janga la kupatwa kwake na uchizi ili nije kulia zaidi kama niliavyo sasa”, aliuliza swali hilo bi Aisha huku akiangalia kwenye mbingu kwenye anga la bluu huku kapiga magoti, kavalia khanga zake kuukuu na mashavu yake yalikuwa yamejaa machozi.



    Bila ya kujificha moyo wake, mama Zena alifurahia hasa yaliyompata Rashad. Mwanzoni kiunafiki nafiki alijitia akionea huruma, baadae akaanza kumsimanga wifi yake. “unajua hata misiba watu hulia halafu wananyamaza” alikuwa akitoa kauli za hivyo, “na mtu kama haonekani mnalia kisha mnanyama na kuendelea na maisha. ila sio watu wa nyumba hii toka huyo Rashad apotee mnatujazia vilio na simanzi. Imekuwa kama mnatuchuchuria sasa, mana watu mmekuwa tena ninyi ni kujiliza mtindo mmmoja, utafikiri nyie ndo wa kwanza kupata matatizo duniani wakati wapo watu wana matatizo, hayo yenu hayaingizi mguu ”, aliongea hiyo kauli mama Zena huku bi. Aisha, Sarha na ndugu wengine wakimsikia. Kauli hiyo ilizua utata sana kwenye familia hivi kwamba Sarha alipigana na shangazi yake na kusababisha ugomvi mkubwa zaidi kuwahi kutokea hapo kijijini. Hayo ndiyo yakabaki kuwa maisha yao baada ya Rashad kuwa chizi na kutokomea kusikojulikana.



    Ila sasa, kumbe kule kwa mganga, mama Zena alipewa sharti kuwa, isitokee hata siku moja kukutana na Rashad, kwa maana kuwa siku ambayo Rashad atakutana tena ana kwa ana na mama Zena basi uchizi utahama toka kwa kwake na kumuhamia mama Zena.





    Naam baada ya usiku ule miaka mingi ilipita. Na hakuna aliyekuwa na tumaini la kumuona tena Rashad, hata mama yake mwenyewe alikuwa kakata tamaa kumuona tena. Na Mama Zena alijiona kuwa kafanikiwa mpango wake wa kiovu na kamwe hakufikiri kuwa uovu wake ulikuwa una mwisho na alisahau ule usemi wa ‘milima haikutani, binadamu hukutana’.



    Basi ikatokea siku moja Mama Zena na binti yake walikuwa kwenye matembezi mjini. Na kwa bahati mbaya sana, wakakutana na Rashad na hapo ndipo uchizi ukamtoka Rashad na kuhamia kwa mama Zena, na mama huyo akageuka kuwa kichaa kabisa na huku Rashad akipona na kurudi kwenye akili zake timamu kabisa.





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Basi huo ndio ulikuwa mkasa wa maisha ya Rashad jinsi alivyopata uchizi na kisha akapona kurudia akili zake timamu. Na hatimaye bi Aisha na Sarha walimpata tena Rashad. Kwao ilikuwa ni zaidi ya muujiza. Kwa maana walikuwa washakata tamaa ya kumuona tena. Na waliumia sna kugundua kuwa uchizi wa Rashad ulisababishwa na mama Zena ambaye sasa uchizi ulimuingia mwenyewe. Hatimaye bi. Aisha na Sarha waliona kabisa kuwa mungu kajibu dua zao.



    Mambo mengi yalikuwa yamebadilika toka Rashad apotee, Sarha alikuwa tayari kashamaliza elimu yake na alikuwa tayari kashakuwa daktari mkubwa. Hivyo maisha ya Sarha na bi Aisha yalikuwa mazuri kwa wakati huo sio ya kimaskini tena na walikuwa washahama kijijini siku nyingi na waliishi Dar es Salaam. Tena Sarha alikuwa tayari kashaolewa. Kwa kifupi maisha ya mama na dadake Rashad yalikuwa yamerejea kwenye ile hali nzuri ambayo walikuwa wakiiombea hapo zamani, na kurudi kwa Rashad kwenye maisha yao kuliongeza furaha kwao hata zaidi.



    Mambo mengi sana ya kimaisha yalikuwa wamempita Rashad kutokana na unyama aliotendewa na shangazi huko miaka ya nyuma. Na kamwe hakukuwa na njia ya kufidia hasara yote aliyoipata kwa kushindwa kuendelea na ndoto zake za kimaisha na hasa kumalizia elimu yake. Hivyo alikuwa na kazi ya kujifunza mambo mengi ili aje kuweza kuishi maisha yake kama watu wengine wenye maisha ya kawaida. Ila pia alimshukuru mungu kuwa walau alikuwa mwenye bahati vya kutosha hata akabahatika kurejea kwenye akili zake timamu.







    Rashad alitokea kuunda urafiki mkubwa na wa karibu sana na shemeji yake, mume wa Sarha. Kwa haraka sana walijikuta wameshibana. Shemeji yake huyo aliitwa Imran, na alimfundisha Rashad vitu vingi sana kwa haraka, ikiwamo kuendesha gari, kumtembeza mitaa mbalimbali ya mji na kumkutanisha na watu wengi aliofahamiana nao na ndiye aliyemtafutia mwalimu wa kumsaidia kusoma tena, ili siku moja Rashad aendelee na elimu yake aliyokuwa kakatizwa. Walikuwa ni zaidi ya mashemeji wakawa kama mtu na kaka yake ama mtu na rafiki yake wa karibu.



    Rashad mwenyewe tangu apone uchizi wake alikuwa keshabadilika sana, hata haikuwa rahisi kwa mtu asiyemfahamu kujua kuwa yeye alikuwa ni mwanaume aliyewahi kuwa chizi, kichaa na taahira kabisa. Kwanza alikuwa yuko nadhifu sana, aliyejipenda, msafi na mtanashati. Muda wote alivalia vizuri na kunukia marashi. Hayo yote, ukiongezea na urefu wake na mwili wake ulioanza kujijenga vizuri ulifanya wanawake wengi kuanza kuvutiwa naye. Ila mwenyewe alikuwa yuko ‘serious’ sana na maisha yake, alikuwa yuko bize na kusoma kwake na mambo yake mengine hivi kwamba hakuwa akijiweka karibu na mwanamke yeyote yule.



    Kumbe kwake yeye Rashad sio kwamba alikuwa hawatamani ama hawaoni wanawake waliokuwa ‘wakimshobokea’, aliwaona sana, ila tatizo lilikuwa ni moyo wake na akili yake. Yani katika hali ya kushangaza sana. Rashad alikuwa akimkumbuka sana Johari. Sura ya Johari ilikuwa bado haijamtoka kichwani mwake.



    Katika hali isiyokuwa ya kawaida, hakuona mwanamke yeyote ambaye alifikia uzuri wa Johari. Kichwani mwake alimuwaza, na alipolala alimuota. Aliposikia nyimbo za mahaba redioni, kichwani mwake ilimjia sura ya Johari. Rashad katu, hakuona wanawake wenye sifa ya uzuri na kuvutia kiasi cha kumshinda Johari. Na moyo wake ulisononeka sana kwa maana hakujua wapi angekutana naye tena.



    Basi bwana, jioni moja, Rashad, na Imran walikuwa wamemaliza kufanya mazoezi ya kucheza mpira wa kikapu na walikuwa wamekaa pembezoni mwa uwanja wa michezo wakiangalia wachezaji wengine wakiendelea na mazoezi yao. Ndipo mara Imran akamuona mwanamke aliyeitwa Sandra akikatiza kwa mbali kidogo nje ya uwanja huo wa mazoezi, huyo Sandra alikuwa ni jirani yao.



    Imran akamuonesha Rashad amuone Sandra na kumsifia huyo mwanamke kuwa ni mzuri sana, na akamkumbushia Rashad kuwa Sandra alikuwa akimkubali sana. Kwamba kila mara Sandra alipomuona Rashad mtaani basi alikuwa akimchangamkia sana na kuleta mazungumzo mengi. Imran akamwambia Rashad kuwa siku atakayo mtaka Sandra basi mwanamke huyo ‘hatochomoa’ atakubali moja kwa moja.



    Rashad alicheka maongezi ya Imran na kumwambia Imran kuwa kuna mwanamke anayempenda sana, na si Sandra, tena mzuri kumzidi Sandra hata kwa mara alfu. Mwanamke aliyevutia kwa kila kitu na mwanamke ambaye yeye Rashad aliwahi kuwa kwenye mahusiano nae kipindi anaumwa ugonjwa wa akili.



    Mwanzoni Imran alichukulia Rashad anamletea masihara, kwa maana haikuingia akilini hata kidogo, kuwa Rashad aliyekuwa akiugua ukichaa aliweza kuwa na mahusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote yule. Haikuingia akilini kuwa kuna mwanamke aliyeweza kuwa na mahusiano na mtu chizi.



    Lakini Rashad akaendelea kumsimulia Imran kuwa kipindi yuko chizi na kuishi mabomani, mitaani na majalalani. Kulikuwa na mwanamke ambaye alikuwa akimfuata usiku kwa lengo la ‘kulala’ nae. Na kwamba yeye Rashad kichwani mwake sura ya yule mwanamke bado ilibakia. Na kwamba kila usiku alimuota yule mwanamke na kwamba hakuna mwanamke yeyote atakayeweza kumfanya amsahau yule mwanamke.



    Imran akazidi kuona maajabu, hakuamini kabisa kuwa Rashad aliamini kwamba aliwahi kuwa na mahusiano na mwanamke kipindi yuko chizi. Imran aliona pengine Rashad uchizi wake haujapona vizuri kwa kuongea mambo kama hayo. Ila Rashad mwenyewe alijiamini hisia zake kuwa ni kweli aliwahi kuwa na mahusiano kipindi yuko chizi na kwamba pamoja na uchizi wake aliokuwa nao kumbukumbu zake zilikuwa sahihi kabisa bila wasi.



    Jambo hilo lilimshangaza sana Imran, na akajikuta akimwambia Sarha, mke eake. Na kumwambia kuwa pengine Rashad bado hajapona vizuri uwendazimu kwa kuongea mambo aliyokuwa kaanza kuongea.





    ................







    Kwa upande wa Johari maisha yalizidi ‘kunoga’. Alifurahia jinsi Malcom alivyowafurahia watoto watatu aliompatia. Alijiona kila kitu kimekamilika. Kamwe hakudhania kuwa ipo siku yule chizi aliezaa nae watoto wake watatu atarejea kwenye maisha yake, tena akiwa si chizi tena bali mwanaume mwenye akili zake timamu.



    Basi kama wasemavyo waswahili kuwa ‘milima haikutani, binadamu hukutana’, siku ya siku ikafika ambayo Rashad alikutana na Johari. Siku ambayo kibao kilipoanza kumgeukia johari.



    Siku hiyo, Rashad alikuwa kaingia kwenye ‘super market’ kununua kinywaji fulani hivi alichoagizwa na Sarha. Akiwa yumo dukani, kwenye kabati za vinywaji mara kwa mbali alimuona mwanamke aliyependeza, aliyekuwa kasimama pembeni ya ‘keshia’ wa ‘supermarket’ na aliyeonekana kama vile kuna mtu anamsubiri, na wanamke huyo alikuwa anaangalia saa yake ya mkononi mara kwa mara. Alikuwa kavaa gauni refu la rangi nyekundu, na nywele ndefu zilizovutia. Kwa haraka Rashad alimfikiria kuwa yule mwanamke ni mrembo sana na akajikuta akimuangalia vizuri.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndipo mara akagundua kuwa yule mwanamke hakuwa mtu mwenye sura ngeni kwake. Na akamtazama vizuri sana na moja kwa moja akili yake ikatambua kuwa yule alikuwa ni yule mwanamke ambaye alikuwa akimjia kwenye boma lake alilokuwa akilala kipindi yuko chizi, alimuangalia vizuri na kukubaliana na akili yake kwa asilimia mia kuwa yule mwanamke ni yuleyule ambaye alikuwa akimjia usiku wa manane kipindi yuko chizi na kukutana nae kimwili bomani. Yani yule mwanamke alikuwa ni Johari.

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog