Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

SIONDOKI MPAKA NIFE - 5

 





    Simulizi : Siondoki Mpaka Nife

    Sehemu Ya Tano (5)



    Jambo la kumuingiza Titus katika chumba ambacho Agape amehifadhiwa lilikuwa ni kosa kubwa sana. Kosa kwa kuvunja miiko ya kazi yake na kosa kubwa kwa Maliki endapo angefahamu jambo hilo. Labda angemkata kichwa? Au abda angemfanya unyama wa kutisha na kuandikwa katika magazeti njaa na waandishi njaa labda wangetajirika kwa kuuza stori iliyosheheni kisa cha kusisimua. Huenda kutokana na kutokujua wangeandika mwanaume mmoja amuua mpenzi wake kinyama. Nani asingenunua gazeti lililopambwa na picha ya kutisha ukurasa wa mbele kisu kikubwa kilicholowa damu kwa kutenganisha kichwa cha msichana mrembo kama Suleya na kiwiliwili chake? Basi ndivyo ambavyo mawazo hayo hupita kichwani kwa mtu mwerevu anayeuelewa fika ukatili wa Maliki na kitendo ambacho anakifanya Suleya akiwa na Titus. Kufungua tu mlango, Titus akiwa ameshika kiuno cha Suleya huku akiwa anamkokota kilevi, alimuona msichana alitejiinami sakafuni amefungwa kamba akiwa amezivaa nguo kama za Agape wake. Hapana si kama bali ndiye Agape aliyezivaa nguo zake mwenyewe. Moyo wa Titus ulimlipuka kiasi cha kuhisi anaishiwa na nguvu za kusimama. Alijaribu kuita kwa sauti ambayo haikusikika vyema.

    "Aga.. Agape.. ee!"CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Iikuwa ni yenye utetemeshi kiasi. Sauti ile ikapenya katika masikio ya Suleya na kuongea kilevi.

    "Wewe nawe ushaanza kumtamani yule mahabusu wa bosi wangu? Ndio maana sikutaka kukueta humu ndani"

    Sauti ile ya kilevi kutoka kwa Suleya ndiyo iliinua uso wa Agape na kukutana uso kwa uso na Titus.



    Kutokana na pupa za kukimbia ovyo bila kutazama alipokuwa akienda, akadondoka baada ya kumpiga kikumbo yule muhudumu; basi pupa zile hazikuishia pale. Aliwasha gari kwa fujo, injini ikawaka kisha ikazima. Hakuwa makini kabisa Twaha. Gari ya Suleya na Titus ikampotea kabisa machoni mwake na kujilaumu kwa kufanya kosa la kutokuwa makini. Alipiga piga usukani wa gari yake na kupiga kelele kwa fujo ndani ya gari mule akiwa peke yake. Kutokana na aibu aliyoisababisha pale katika mgahawa hakuona kama ingekuwa vyema angerudi tena pale kwenye meza aliyokuwa amekaa. Akaiwasha gari yake injini ikaitika akaondoka taratibu kuelekea masaki alipokuwa akiishi huku machozi yakiwa karibu kumtoka. Machozi ya hasira ya kumkosa hasimu wake anayemkosesha usingizi kila siku



    ...



    Akiwa bado amelala akaota ndoto mbaya. Ndoto ambayo hakuwahi kuiota kabla. Ndoto ya Titus kupafahamu anapoishi na kaingia ndani ya chumba alichomuhifadhi Agape.

    "Mungu wangu"

    Jasho jingi lilikuwa likimtoka. Akaitafuta simu yake ya mkononi kumpigia Suleya. Simu haikuwa na salio la kutosha. Akanyanyuka kwa ghadhabu kuelekea katika nyumba yake. Nyumbani kwake alipo Suleya Titus na Agape. Pombe bado zikiwa kichwani lakini alielewa kila hatua aliyokuwa akiifanya. Mwendo ulikuwa wa wastani na kuliingiza gari lake ndani ya jumba hilo la kifahari.





    Macho ya Agape yalipokutana na ya Titus, kilitokea kitu cha tofauti. Moyo wa Agape ulilipuka na kutoamini alichokuwa akikiona mbele yake. Vivyo hivyo ikawa sanjari kwa Titus. Aliendelea kushangaa kwa kitambo kiasi huku akiwa amekiacha kiuno cha Suleya. Hazikupita dakika nyingi fahamu zikamrudia Titus baada ya kusikia sauti dhaifu iliyomtoka Agape.

    "Titus mpenzi!"

    Huku machozi yakimtoka. Wakati huo Suleya alikuwa hajitambui. Alikuwa akitapika sana. Pombe ilikuwa nyingi kichwani iliyoibua kichefu chefu kinywani mwake. Hivyo alikuwa hajui chochote kilichokuwa kikiendelea baina ya Titus na Agape. Titus alimsogelea Agape pale alipo na kuanza kulia pamoja naye

    "Usilie mpenzi nimekuja kukuchukua tuondoke"

    "Hapana Titus niache nife" Agape alikuwa akilia kwa uchungu na sauti iliyojaa kwikwi

    "Siondoki hapa mpaka nife Titus"

    Akiwa yupo katika hali ya kuchanganyikiwa, Titus hakuelewa sababu ya Agape kusema yale yote. Akamuuliza kwa ghadhabu kiasi

    "Una maana gani Agape? Sikuelewi una nini?"

    "Nimesema siondoki mpaka nife"

    Ikabidi Titus kuwa mpole kujua maana ya Agape kusema maneno mazito kiasi hicho

    "Titus siamini kama wewe umeamua kunifanyia kitu kama hiki. Huyu aliyeniteka ni mtu wako wa karibu na wewe ndiye uliyesababisha mimi nikakaa ndani ya chumba hiki kwa muda mrefu bila kujua hatima ya maisha yangu wala baba yangu anaendeleaje. Haiwezekani mimi nibakwe kinyam...aaa"

    Kilio kikaanza upya tena kile cha sauti ya juu kabisa. Titus akamkumbatia katikati ya mikono yake na kumbembeleza kwa huba zito.

    "Naahidi ntakueleza yote. Nitakueleza yote kuhusu mimi, tafadhali tutoke hapa kwanza"

    Akiwa anongea zaidi, bila kujua maana ya maneno aliyokuwa akiongea; alikuwa akimfungulia alizofungwa Agape. Agape alikuwa amelegea kupitiliza na kumfanya Titus kuamua kumbeba. Mngurumo wa geti likifunguliwa ukawashitua wote kwa pamoja. Agape hakuwa na uwezo wa kukataa tena kupatiwa msaada na Titus, hivyo alijilegeza mikononi mwake na kufuata kile alichoambiwa na Titus. Ni wakati huo ndipo wakasikia sauti ya injini ya gari ikizimwa na milango ikifungwa. Walikuwa wamesimama katikati ya sebule wasijue wapi wataelekea. Ndani ya chumba kile cha siri wakiwa wamemuacha Suleya akiwa anatapika.



    Aliifunga milango ya gari yake na kushuka kwa umakini mkubwa akilitazama gari la Titus bila kuelewa kinachoendelea. Ngozi yake ikamsisimuka na vinyweleo vikamsimama kwa kuchanganyikiwa. Aliitoa bastola yake ndogo nyuma ya kiuno chake na kuikamata kiukakamavu katika mikono yake. Aliuma meno kwa hasira huku pumzi zikipishana kwa kasi katika tundu ndogo za pua yake. Akaufungua taratibu mlango wa sebuleni kwake na kwa mwendo wa kunyata taratibu akawa anaipita sebule na kuingia katika moja ya kila chumba taratibu masikio yakiwa wazi maradufu. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakienda kasi zaidi ya kawaida. Haijulikani kama ilikuwa ni uwoga ama ni hasira juu ya kufahamu kama Titus ameshaifahamu nyumba aliyopo Agape? Aliendelea kukagua taratibu kila chumba na cha mwisho kilikuwa kile cha siri alichomuweka Agape.

    "Titus mpenzi" ilikuwa ni sauti iliyopwaya iliyomtoka Suleya.

    Tusi zito likamtoka Maliki na kumpiga teke la mbavu Suleya.

    "Yuko wapi"

    "Agrrrr!! Nani?"

    "Malaya mkubwa wewe nakuahidi kifo ni haki yako"

    Akampiga teke lingine na mguno wa maumivu ukamtoka tena Suleya.

    "Nakuuliza yuko yule msichana?"

    Kamba alizofungwa Agape, zilikuwa chini zimetapakaa. Pombe ikawa ikimtoka taratibu Suleya kutokana na kipigo cha mbwa mwizi. Hayo yote Titus na Agape walikuwa wakiyasikia mahali pale walipokuwa wamejificha.



    ...



    Kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya na wahusika kutopatikana, jeshi la polisi likazidi kupakwa doa na waandishi mbalimbali wa habari. Kutopatikana kwa majambazi walioiba kiasi kikubwa cha pesa katika benki kuu ya kenya, likawachafua sana maafisa wote wa polisi walioheshimika sana katika nchi ya Tanzania. Twaha alizidi kuchanganyikiwa baada ya kuitwa ndani ya chumba cha mikutano na wakuu wake wa kazi kumwambia jambo lililomkaba koo kwa hasira.

    "Haiwezekani!"

    Alimaka kwa hasira akiwa na Rashid FungaFunga.

    "Haiwezekani mkuu. Hii sio kesi yenye utata kama ya jadu mfaume. Wahusika wa kesi hii nimeshakutana nao lakini waliniponyoka tu kwa bahati mbaya. Naomba mkuu unipe nafasi ya kuitetea roho ya mwanangu na kuwatia nguvuni wabaya hawa"

    Alikuwa akizungumza kwa hisia sana. Kiasi cha kutaka kumdondosha chozi la masikitiko Rashid Fungafunga.

    "Naamini utendaji wako wa kazi Twaha ndugu yangu lakini kesi hii imechukua muda mrefu sana ndio maana wakuu wameisitisha kesi hii na kukuhamisha wewe katika kesi nyingine juu ya maharamia wanaoiba madini na pembe za tembo"

    "Lakini vipi kuhusu binti yangu? Mna uchungu ninyi? Sipo tayari, sipo tayari"

    "Lakini..."CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sauti hiyo ahaikumfikia vyema Twaha. Alikuwa ameshatoka na kuelekea nyumbani kwake akiwa na barua mkononi iliyompiga 'stop' kuendelea kuifuatilia kesi hiyo kwa kile kilichoonekana kuwa ameishindwa.



    Alirudi nyumbani akiwa na mawazo lukuki kichwani mwake. Machozi mepesi yakilowesha taratibu mashavu yake. Aliona serikali pamoja na wakuu wake wa kazi, hawajamtendea haki hata kidogo. Hawakuwa na huruma hata chembe juu ya roho na maisha ya binti yake, Agape.



    "Nimeitumikia kazi hii kwa muda mrefu kwanini inataka kuingia dosari kwa kipindi hiki cha mwisho cha kustaafu kwangu? Sitakubali kuiacha kesi hii apewe mtu mwingine nitapambana kufa kupona kuitetea haki ya nchi yangu na roho ya mwanangu. Nipo tayari kuonekana nimekaidi agizo la wakuu wangu lakini si kuiachia roho ya binti yangu. Nitapambana. Nitapamb..."



    Chozi la uchungu likamtoka akabaki akisikilizia donge lake lililomkaba kooni. Alinyanyuka asijue wapi anaelekea na kuiingiza gari yake barabarani kwa mwendo wa hatari. Mwendo ulikuwa ni mrefu kiasi cha kuwashangaza wengi aliowapita barabarani na kuwatimulia vumbi.

    "Jamaa jambazi nini?"

    Wengine walinong'onezana kwa hofu na wengine wakimtusi kimoyomoyo na wale wasio na adabu wakayaropoka moja kwa moja. Breki ya mwisho aliipiga katika kituo cha diplomasia na kumtafuta Gunga rafikiye Agape.

    "Tunaenda wapi mzee"

    Twaha hakujibu chochote baada ya kumchukua Gunga bila kumjuza walipokuwa wakielekea. Mwendo ulikuwa ni ule ule kama aliotoka nao nyumbani kwake. Walielekea mpaka katika chuo cha uhadhili wa fedha na kumpata Nadia. Naye vivyo hivyo kama alivyofanyiwa Gunga. Aliingizwa kwenye gari na gia kupachikwa mwendo ukawa wa fujo kama awali. Sasa alikuwa akilipeleka gari lake moja kwa moja eneo la baharini. Aliipita benki kuu ya Tanzani kwa kasi ya ajabu na moja kwa moja akaiacha mita chache ile hoteli ya kitalii Kilimanjaro hiyat kempinsiki hotel. Nadia na Gunga walikuwa hawafahamiani lakini kila mmoja aliwahi kusikia jina la mwenzake katika stori mbali mbali walizokuwa wakisimuliwa na Agape. Nadia alijitahidi kuuliza nini kinachoendelea hakuna aliyekuwa na jibu la kumpa. Gunga alikuwa ameinamisha kichwa chini na kukikumbatia na viganja vya mikono yake yote miwili. Nadia alipopata wazo la kufungua mlango na kuchomoka ndani ya gari hilo, akaona lingekuwa kosa ambalo lingepaswa kumgharimu maisha yake. Mwendo wa gari hilo ulikuwa ni wa kasi san. Uzuri ilikuwa ni siku ya jumapili, saa 11 jioni. Hivyo hakukuwa na magari yaliyokuwa yakirandaranda katika barabara hiyo. Zikiwa zimebaki mita chache gari kuyalamba maji ya bahari, kikafanyika kitu ambacho hakukitegemea Nadia aliyetumbua macho yake akitazama uelekeo ambao gari lile lilikuwa likielekea. Gunga akiwa bado amejiinamia naye aliinuka ghafla na kupiga ukelele wa kutisha na uoga wa ajabu.

    "Mamaaaaa!!!"

    Twaha akacheka kwa kebehi.



    ...



    Maliki aliendelea kumpiga Suleya bila kupata mafanikio yoyote kuhusu alipo mateka wake Agape. Kwa hasira akamuoneshea bastola na kumuuliza kwa ghadhabu

    "Wewe mbwa utanieleza alipo Agape la sivyo na kuto ubongo wako"

    Titus akiwa nyuma ya friji pamoja Agape aliyemuweka pembozoni na kiti kilichoegemea friji hilo, akamshitua kuwa anyanyuke taratibu na atoke nje. Kuna kosa dogo ambalo alilifanya Maliki wakati anaingia ndani ya nyumba hiyo. Wakati anaingiza gari yake ndani na kuliona gari ya Titus, alisahau kufunga geti. Aliposhuka kwenye gari kwa mwendo wa kunyata huku akiwa na wasiwasi juu ya pigano atakalolipata kutoka kwa hasimu wake akaingia ndani ya nyumba yake kama mwizi na kusahau hata kuufubga mlango wa kutokea nje. Hivyo Agape alitoka kiurahisi na kuingia mpaka kwenye gari ya Titus. Titus naye alikuwa akisikilizia kipigo alichokuwa akikipata Suleya, kipigo ambacho kwa hakika kilikuwa ni cha kusikitisha kupigwa kwa kiumbe kizuri kama yeye. Maliki hakuwa hata na chembe ya huruma juu ya Suleya. Hakukisikia kilio chake, hakutaka kujua ni vipi anaumia; alizidi kumpiga kwa hasira. Suleya alitema madonge mazito mazito ya damu na kuchafua sakafu ya maru maru. Gari ya Titus ikawa imekaa uelekeo mzuri wa kulitazama geti, hivyo Titus naye alitoka kwa mwendo wa kunyata na kufanikiwa kutoka mpaka nje akaingia kwenye gari na kupachika gia baada ya kuwasha injini kilichofuata hapo, zilionekana vumbi pekee katika uwanja wa Maliki mbele ya macho yake alipotoka mkuku baada ya kusikia sauti za mngurumo wa injini. Kutokana na usiku na hali ya kuhamanika, Maliki akafanya pupa. Akaingia ndani ya gari lake bila ufunguo aliouacha juu ya kochi la sebuleni. Akatoka mbio mpaka sebuleni na kuuchukua ufunguo na kurudi ndani ya gari huku akijaribu kuliwasha gari, injini ikakataa kuitika. Titus akawa amefanya jambo. Kwa wakati huo pia Titus alikuwa amefika mbali kiasi cha kutopatwa hata na nini endapo Maliki angefanikiwa kumkimbiza kama alivyotaka. Titus alichomoa baadhi ya nyaya katika betri ya gari ya Maliki. Titus akazipachika gia kwa fujo na kuitafuta barabara ielekeayo posta.



    Maliki alirudi ndani akiwa na hasira sana kwa Suleya. Suleya alikuwa akitapika madonge mazito ya damu yaliyotoka katika mbavu zake zilizopasuka kutokana na kipigo cha mateke mazito ya Maliki.

    "Leo nakuua Suleya"

    Aliikoki bastola yake karibu na kichwa cha Suleya, Suleya hakujibu kitu. Maliki alikuwa akimuangalia kwa hasira na kuuma uma papi zake. Uchungu wake ukaleta uhusiano na hisia za kumdondosha machozi.

    "N'nisa...Mmee..he"

    Suleya alisema kwa shida huku akiishikilia sehemu ya mbavu zake zilizovunjika. Uso haukutamanika pale alipomgeukia Maliki na kumtazama.

    "Mwanahramu mkubwa wewe nikusamehe nini?"

    Maliki akampiga Suleya teke lingine la uso lililomuangusha mpaka sakafuni na damu nzito kumtoka kama maji ya bomba.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Yuko wapi Agape? Yuko wapi Titus?"

    Alifoka kwa hasira huku akimpiga piga kwa kitako cha bastola yake juu ya paji la uso. Suleya alikuwa akilia kwa uchungu wa maumivu na kuzidi kumuomba Maliki amsemehe.

    "Sikusamehi malaya wewe, huwezi kumrudisha Titus wala Agape humu ndani hivyo pongezi yako ya kukaa na mimi muda wote, unastahili kifo"

    Maliki akasimama na kuitengeneza vyema kiwambo chake cha kuzuia risasi katika bastola yake. Suleya akiwa ameilalia sakafu huku akiwa kama amekaa au amelala mkono mmoja ukiwa sakafuni hapo mwingine tumboni kwake, risasi moja ikafumua kichwa chake hazikupita sekunde nyingine ikafumua kinywa sehemu za taya. Hiyo iliingia mara baada ya kugeuza uso wake kutokana na maumivu aliyoyapata mara baada ya kupigwa risasi ile ya kichwa. Maliki akamtemea mate na kumuacha Suleya akiyafumba macho yake na kukikaribisha kifo chake kwa uchungu.



    Maliki alitoka ndani ya chumba hicho cha siri na kwenda katika chumba chake. Chumba alichokuwa akikifungua kwa nadra sana. Ni huko ndipo alipohifadhi vitu vyake vingi vya siri. Kulikuwako na pasport bandia kadha wa kadha na viti mbali mbali vya kiharamia. Hata kiasi fulani kikubwa cha pesa walivhoiba kutoka katika benki kuu ya kenya, alikihifadhi humo. Titus, Jonathan na fredy walikuwa wanafahamu kuwa, fedha hizo ameziweka benki. Aliziweka ndani ya begi dogo jeusi, hilo pia alilichukua na kulipachika begani mwake. Alichukua silaha zake zote na kila kilichomuhusu na kuondoka ndani ya chumba hicho. Aliporudi kwenye chumba kile cha siri, alimkuta Suleya alikwisha kata roho.

    "Shenzi taipu"

    Kisha akasonya na kurud tena sebuleni kuchukua ufunguo wa gari yake. Alitoka mpaka nje na kuondoka na gari yake kusikojulikana. Huo ukawa mwisho wa Suleya aliyekuja kujulikana kuwa maiti yake yamo umo ndani baada ya siku tatu baadaye kupita. Maliki naye alirudi nchini kwao baada ya usiku ule kumtafuta sana Agape na Titus bila mafanikio.

    "Yuko wapi Suleya?" Baba yake akamuuliza kwa ukali kiasi

    "Amekufa baba"

    "Unasema nini? Ilikuwaje?"

    "Nimemuua"

    "Ume..? Umefanya nini!?"

    Baba yake Maliki aliuliza kwa hasira na mshangao zaidi na kwa hali ya kuchanganyikiwa.

    "Ina maana mimi nilikuletea mke ili umuue?"

    "Mke?"

    "Ndiyo, Suleya alikuwa ni mke wako ina maana hakukueleza?"

    "Sifahamu kitu kama hicho na alikiuka masharti ya kazi zetu baba"



    Baada ya miezi kadhaa kupita Maliki aliuwawa na baba yake, kwa bastola yake mwenyewe. Baba yake Maliki hakupendezwa kabisa na kitendo cha Maliki kumuua Suleya. Hivyo baada ya kilevi kilichomkoea kichwani siku hiyo aipoamka, kikaibua wazo alilolikataa mara kwa mara lilipokuwa likimpitia kichwani mwake.

    "Nisamehe mwanangu. Nisamehe Maliki baba. Sikuwa na budi ni hasira tu mwanangu"

    Jinamizi lile lile lililomtuma kumtandika Maliki risasi, ndiyo lililomsukuma yeye kuinyanyua bastola yake na kujitandika kwenye kichwa chake. Huo ukawa mwisho wa Maliki na Baba yake.



    ...



    Gari aliyokuwa akiiendesha Twaha ilikata kona kali na kumfanya Nadia kupiga ukunga wa kuogopa. Gunga naye kudhani gari ilikuwa ikienda kutupwa baharini na wao wakiwa ndani.

    "Tunakufaaa!!!"

    Zikawa kelele za Nadia zilizomfanya Twaha kucheka kwa kebehi na kuikunja kona kali na kuelekea upande wa Masaki. Huko alielekea moja kwa moja mpaka katika hoteli ya golden tulip. Aliiegesha gari yake kwenye maegesho ya hoteli hiyo na kuwageukia Nadia na Gunga kule nyuma walipokaa. Wote kwa pamoja walikuwa wakitumbua macho kwa hali ya uwoga uliokithiri na kumuangalia Twaha kwa maswali mengi.

    "Msiogope, sina nia mbaya nanyi ila nimewaleta hapa kwa ajili ya mazungumzo"

    "Mazungumzo? Mazungumzo gani unataka kutuua kwa kuendesha ovyo?"

    Nadia ndiye aliuliza kwa ghadhabu na kutaka kufungua mlango wa gari hiyo.

    "Unaenda wapi Nadia" Twaha alikuwa akicheka kwa kebehi na kuufungua wa kwake. Alitoka na kuanza kumfungulia Gunga.

    "Toka nje"

    Gunga alitoka akiwa bado na hali ya uoga.

    "Usithubutu kunikimbia au kufanya kitu kinachoweza kukuletea matatizo"

    Twaha alijaribu kumtisha na kuuendea mlango wa Nadia ambaye tayari alikuwa ameshatoka nje.

    "Tafadhali nahitaji kuongea nanyi juu ya..."

    Ghafla ukasikika mlio mkubwa wa kitu kilichogongwa ama kugongana na kitu kingine. Zilikuwa ni mita chache kutoka pale walipo Twaha Nadia na Gunga. Ilikuwa ni gari ndogo ambayo Twaha alikuwa anaifahamu fika. Kwa mara ya kwanza alikutana nayo pale Courtyard na kumuona binti yake Agape akiingia ndani yake akiwa pamoja na Titus muhalifu aliyekuwa akimkosesha usingizi. Alikimbia ovyo barabarani kulifuata gari lile. Gari hilo liligonga nguzo ya taa ya barabarani na kuumia vibaya sehemu ya mbele, waliokuwemo ndani walikuwa wazima wa afya. Titus alitoka na kumtoa Agape.

    "Mikono juu"

    Twaha alisema ikiwa mikono yake imeongozwa na bastola mbele. Agape akamuona baba yake kwa mara ya kwanza. Macho yakamtoka pima na kupiga ukunga wa furaha

    "Babaaa!"

    Lakini Titus akawa shapu kufanya jambo lililomshangaza Agape. Alimkamata mkono wake na kuikaba shingo yake na kumuwekea bastola kichwani mwake.

    "Ukijaribu kufanya kosa nafyatua risasi"

    Ilikuwa ni sauti isiyo na mzaha iliyomtoka Titus. Agape alikuwa akitetemeka kwa uoga na uso wake ulimitiririsha machozi ya uchungu Twaha. Twaha aliona alama za vidole na damu zilizomvilia Agape. Akafanya kosa. Kosa lililogharimu maisha ya binti yake. Kosa lililomfanya Titus pia kutenda kosa bila kukusudia. Twaha alimpiga Titus risasi ya mguu, risasi ambayo ilimshitua Titus naye bila kutarajia akafyatua bastola yake na risasi iliyotoka ikapenya katika bega lake.

    "Na..kufaaa" kilio cha uchungu kikamtoka Agape baada ya kudondoka chini kama gunia.

    "Agapeee" Titus akiwa anavuja damu kwa risasi iliyotenganisha mifupa yake alijikokota mpaka pale alipodondokea Agape na kumlilia.

    "Nisamehe mpenzi wangu nisamehe Agape. Nakupenda mpenzi ni bahati mbaya agape wangu. Nisameheeee"

    Huku Nadia na Gunga wakiwa wanatazama tukio hilo kwa hali ya kutoelewa kitu, Agape akazungumza kauli ya mwisho.

    "..umeniua nikiwa bado nakupenda. Furaha yangu ni kukuona ukifurahi kutokana na kifo changu"

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Twaha naye alikuwa akilia sana mpaka akaishiwa nguvu. Umati mkubwa wa watu ukawa umekusanyika eneo hilo kutokana na milipuko ya sauti ya risasi hizo. Agape akawa amekata roho mikononi mwa Titus aliyekuwa anavuja damu katika jeraha lake. Askari kutoka katika bar ya jeshi iiyopo jirani hapo officers mercy walikuwa wameshakuja na kumkamata Titus na Nadia pamoja na Gunga walichukuliwa na kupelekwa kituoni. Twaha akapatiwa huduma ya kwanza na Mwili wa Agape ukachukuliwa na kuhifadhiwa katika chumba ca kuhifadhi maiti.



    ...Mwisho...

0 comments:

Post a Comment

Blog