Simulizi : Mcheza Filamu Za Ngono
Sehemu Ya Tano
(5)Mhudumu wa mghahawa wa Casannova ambao ulikuwa katika hoteli ile ile ya Cassanova bado alikuwa akiwahudumia wateja wake, Reuben, Filbert na Andrew
kama kawaida yake. Kila wakati alikuwa akiitwa na kurudi huku akiwa na vinywaji mbalimbali mikononi mwake.
Hamadi hakuonekana kuwa na wasiwasi na wateja wale, alikuwa akiendelea kuwahudumia kama kawaida yake. Hakutaka kuongea nao hata kidogo japokuwa
moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kutamani kuongea na wazungu.
Wazungu wale kwake walionekana kuwa tofauti kidogo, walionekana kuwa haraka huku muda mwingi macho yao wakiwa hawayatulizi sehemu moja. Hamadi
hakuonekana kujali sana hali ambayo walikuwa nao, kitu ambacho alikuwa akiendelea kukifanya ni kuendelea kuwahudumia kama kawaida tu.
Wateja wote zaidi ya ishirini ambao walikuwa kwenye mghahawa ule walikuwa wamekwishahudumiwa na wakati huo walikuwa wakiendelea kula kitendo
ambacho kilimfanya Hamadi na wahudumu wengine wa mghahawa ule kutulia pembeni huku nao wakiangalia televisheni.
Habari ya utekaji ikaanza kutolewa, kila mhudumu alionekana kuwa na utulivu mkubwa kuangalia televisheni ambayo ilikuwa imewekwa kituo cha televisheni
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ya Taifa. Taarifa ile ikaonekana kumshtua kila mmoja, mtangazaji alikuwa akitangaza kwamba kulikuwa na wazungu watatu ambao walikuwa wamehusika na
utekaji wa mwanamke mmoja na mtoto mmoja ambaye alikuwa na umri wa takribani mwaka mmoja.
“Watekaji hao wanakisiwa kukimbilia mkoani Kilimanjaro, Tanga, Arusha au Manyara” Mtangazaji alisema huku akionekana kutokuwa na uhakika.
Hapo ndipo ambapo Hamadi alipoanza kuwaangalia wazungu wale ambao walikuwa mezani. Kwanza akaanza kuwahesabu kwamba walikuwa watatu kama
ambavyo mtangazaji alikuwa ametangaza kwenye televisheni, akawaangalia tena, wawili nywele zao zilikuwa nyeupe na mmoja nywele zake zikuwa nyeusi, nao
wale wazungu walikuwa vile vile.
Kila kitu ambacho kilikuwa kikitangazwa kuhusiana na watekaji nyara wale, kilikuwa kikifanana sana na wazungu wale ambao walikuwa wamekaa katika
mghahawa ule. Hamadi akashindwa kuvumilia, tayari alikuwa na uhakika kwamba wale watekaji ambao walikuwa wakizungumziwa kwenye televisheni
walikuwa wale wazungu ambao walikuwa katika mghahawa ule.
Alichokifanya Hamadi ni kutoka na kuanza kuelekea jikoni. Alipofika huko, akachomoa simu yake na kuanza kupiga namba za polisi ambazo zilikuwa
zikijulikana sana 911. Simu ikaanza kuita, wala haikuita muda mrefu, ikapokelewa na sauti nzito ya mwanaume kusikika.
“Karibu katika kitengo cha usalama wa Taifa” Sauti ile ilisikika.
“Hallow. Naitwa Hamadi hapa, nipo Tanga Mjini barabara ya kumi na tatu” Hamadi alisema huku akionekana kuwa na haraka.
“Kuna tukio lolote lile limetokea huko?”
“Ndio. Hapa kwenye mghahawa nawaona watu watatu ambao taarifa zinasema kwamba wanatafutwa na jeshi la polisi kwa tukio walilolifanya la utekaji”
Hamadi alisema.
“Sawasawa. Wapo vipi hao watu?”
“Ni wazungu watatu. Wana kila sifa ambazo mtangazaji wa televisheni alivyotangaza” Hamadi alisema.
“Upo Tanga sehemu gani?”
“Barabara ya kumi na tatu katika hoteli ya Cassanova hapa. Fanyeni haraka, naona kama wanataka kuondoka” Hamadi alisema na kisha kukata simu.
Hamadi akarudi tena ndani ya mghahawa. Reuben na wenzake bado walikuwa wakiendelea kunywa kama kawaida yao, walichukua dakika mbili tu baada ya
Hamadi kutoka jikoni wakasimama, wakalipia na kuondoka mahali hapo.
Hamadi aliwaona polisi wakichelewa kufika mahali hapo, alionekana kuwa na shauku ya kuwaona polisi wakifika hapo, wakiwakamata na kisha kupewa zawadi
nono ambayo ilikuwa imeandaliwa kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwa watu wale.
Wala hazikupita dakika nyingi, defender ya polisi ikasimama nje ya mghahawa ule na kisha polisi kuruka chini kikomandoo na kuelekea ndani ya mghahawa ule
ambapo moja kwa moja wakamhitaji Hamadi.
“Wapo wapi?” Polisi mmoja alimuuliza huku akiwa ameshika bunduki.
“Wameondoka muda mchache uliopita”
“Unajua wameelekea wapi?”
“Wameelekea kule upande wa kaskazini”
“Wamekwenda na gari gani?”
“Starlet nyeusi”
“Sawa. Twende garini tuwafuate” Polisi yule alisema.
Hamadi hakuwa na wasiwasi, alichokifanya ni kupanda ndani ya defender ile ambayo ilikuwa na polisi zaidi ya kumi ambao walikuwa na bunduki na kisha
kuanza kuelekea kule gari lile la watekaji lilipoelekea.
Mpaka kufikia kipindi hicho polisi wakawa na uhakika kwamba watekaji wale walikuwa njiani kuelekea mpakani mwa nchi ya Tanzania na Kenya, kuingilia
ndani yamji wa Mombasa. Dereva wa defender lile alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi sana, mpaka kufika ndani ya dakika ishirini, walikuwa wakiliona
gari lile kwa mbele umbali wa nusu kilometa.
“Watakuwa ndio wenyewe wale. Ongeza kasi dereva” Polisi ambaye alionekana kuwa kiongozi alimwambia dereva.
Gari likaongezwa kasi, kila polisi ambaye alikuwa na bunduki akaanza kuikoki bunduki yake. Tayari muda wa vita ukaonekana kufikia, walitakiwa kupambana
kiume mpaka kuona kwamba wanawaokoa mateka ambao walikuwa wameshikiliwa.
Gari lile la watekaji likaenda kwa umbali fulani, wakaliona likikata kona upande wa kushoto na kuingia porini, nao walipofikia eneo lile, wakakata kona na
kuingia porini. Tayari mpaka kufikia kipindi hicho walikuwa na uhakika kwamba watu wale walikuwa watekaji na kulikuwa na uhakika wa asilimia mia moja
kwamba mateka wale bado walikuwa nao.
Wakaendelea kuelekea kule porini mpaka kufika sehemu ambayo kulikuwa na gari lile tu. Walipoanza kulisogelea na kulifikia, hakukuwa na mtu yeyote yule
zaidi ya khanga moja tu ambayo alikuwa ameivaa Prisca.
Wakaanza kusogea mbele zaidi mpaka kufika sehemu ambayo wakaanza kusikika minong’ono ya watu. Wakajificha na kuanza kuchungulia kule minong’ono
ilipokuwa ikitokea, macho yao yakatua kwa watekaji wale huku Reuben akiwa amemkaba Prisca ambaye alikuwa akijitahidi kujitoa katika roba ile.
Kila mmoja alijua kwamba ule ndio ulikuwa mwisho wa Prisca, polisi mmoja ambaye alikuwa akisifika kwa shabaha akaandaa bunduki yake tayari kwa
kuwalenga. Mapolisi walionekana kutokuwa na wasiwasi hata kidogo, tayari walikwishagundua kwamba watekaji wale wala hawakuwa na bunduki yoyote ile.
“Mlenge yule aliyemkaba mwanamke yule” Polisi kiongozi alimwambia.
“Kichwani au wapi?”
“Usimuue. Mlenge kwenye ule mkono uliomkaba mwanamke”
“Nimekuelewa”
Mlio wa risasi ukasikika mahali hapo, Reuben akaanza kupiga uyowe mkubwa sana, damu zilikuwa zikimtoka mkononi ambao ulikuwa umepigwa na risasi.
Filbert na Andrew wakaona kwamba tayari kila kitu kilikuwa kimeharibika, walichokifanya ni kuanza kukimbia.
Polisi yule wa shabaha wala hakuwa na haraka, alichokifanya ni kuilenga miguu yao, wote wakajikuta wakianguka chini kama mizigo huku wakilia kama
watoto. Hawakutaka kumuacha Reuben vile vile, nae akapigwa risasi nyingine ya mguu, hawakutaka mtu yeyote yule atoroke kutoka katika mikono yao.
“Kweli una shabaha”
“Hii ndio kazi yangu bwana. Hata ungeniambia nilenge jicho, ningelilenga tu”
Polisi wale wakawasogelea na kisha kuwachukua. Wote walikuwa wakilia kwa maumivu makali, risasi zile zilikuwa zimepenya miguuni mwao. Baadhi ya polisi
wakaanza kumsogelea Prisca, walipogusa mapigo yake ya moyo, alikuwa akihema kwa mbali sana.
“Tuondokeni” Kiongozi alisema na kisha wote kuingia ndani ya gari huku mapolisi watatu wakiingia ndani ya ile Starlet pamoja na Prisca ambaye alikuwa kimya
na safari kuelekea Tanga mjini kuanza.
****
Manase alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kasi huku Gibson akiwa pembeni yake. Mawazo ya Gibson kwa wakati huo hayakuweza kutulia hata kidogo,
muda wote alikuwa akiiwaza familia yake, mke wake, Prisca pamoja na mtoto wake, Genuine.
Akili yake wala haikutulia hata kidogo, kama kuhuzunika tayari alikuwa amehuzunika sana kiasi ambacho wakati mwingine alikuwa akishikwa na hasira hata
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
zaidi ya simba aliyejeruhiwa. Maswali kibao yalikuwa yakijazana kichwani kwake kuhusiana na watekaji ambao alikuwa na uhakika kwamba walikuwa
wametumwa na msichana Katie, msichana ambaye alikuwa amemuoa na kuachana nae kwa sababu kulikuwa na mtu mwingine ambaye alikuwa akimhitaji zaidi.
Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akiongea kitu chochote ndani ya gari, kila mtu alikuwa kimya huku wakionekana kuifuatilia kwa ukaribu safari hiyo ambayo
kwao waliiona kwamba ingezaa matunda kwa kile kitu ambacho walikuwa wakikifuata.
“Wanasemaje? Wamewakamata?” Gibson alimuuliza Manase ambaye alikuwa amemaliza kuongea na simu.
“Bado wanaendelea na upekuzi wa kila gari. Nadhani tunaweza kukutana nao njiani pia” Manase alimjibu Gibson.
Safari bado ilikuwa ikiendelea kama kawaida tena gari likiendeshwa kwa mwendo wa kasi sana. Baada ya umbali fulani, wakafika katika eneo ambalo lilikuwa
na watu kadhaa wasiozidi ishirini ambao walikuwa wamezunguka kitu karibu na kichaka huku mikono yao ikiwa kichwani.
Hawakutaka kusimama wala kushuhudia ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea mahali pale, walichokifanya ni kuendelea na safari yao huku wakionekana
kuwa na haraka kupita kawaida bila kujua kwamba watu walewalikuwa wameizunguka maiti ya genuine ambaye alikuwa ametupwa wakati gari likiwa katika
mwendo wa kasi. Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka kufika Segera, hakukuwa na mtekaji yeyote ambaye alikuwa amekamatwa na polisi wale.
Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa, hawakuonekana kuelewa mahali ambapo watekaji wale walikuwa wamepitia. Kila mmoja alionekana kutokuelewa,
mpaka kufikia muda huo hawakuwa na uhakika kama watekaji wale walikuwa wamekwishavuka mahali hapo au bado.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo walionekana kuchanganyikiwa zaidi, kwanza hawakutaka kuendelea na safari yao, walichokifanya ni
kupaki gari pembeni hapo Segera na kuanza kuongea kuona nini kilitakiwa kufuata.
“Kwa hiyo tufanye nini?” Dokta Phillip aliuliza.
“Bado sijajua. Yaani hapa nimekwishachanganyikiwa kabisa. Sijui hawa watekaji watakuwa wamepita njia gani na wakati watu kule Chalinze waliwaona
wakichukua njia hii” Manase alisema huku akiitoa simu yake.
Muda wote huo Gibson alikuwa amebaki kimya, kichwa chake kilikuwa kikiifikiria familia yake tu. Hakujua mahali ambapo watekaji wale walipokuwa
wameichukua familia yake. Muda wote moyo wake ulikuwa ukifahamu kwamba ni msichana Katie ndiye ambaye alikuwa ameucheza mchezo mzima mpaka
kufikia muda huo.
“Huku hawajafika” Manase aliongea simuni.
“Hawajafika? Hawajafika vipi na wakati watu wamekamatwa Tanga?” Sauti ya pili ilisikika.
“Wamekamatwa Tanga?” Manase aliuliza huku akionekana kushtuka.
Swali lile likamfanya Gibson pamoja na dokta Phillip kumsogelea Manase ambaye bado alikuwa akiongea na simu kutoka makao makuu ya kituo cha polisi
kilichokuwa jijini Dar es Salaam. Aliongea kwa sekunde kadhaa na kisha kukata simu.
“Wamekamatwa mkoani Tanga” Manase aliwaambia huku akionekana kutabasamu.
“Asante Yesu! Na vipi kuhusu familia yangu?” Gibson aliuliza.
“Hilo sijauliza. Cha msingi twendeni Tanga” Manase aliwaambia.
Hakukuwa na kitu kingine cha zaidi cha kufanya zaidi ya kuingia ndani ya gari na safari ya kuelekea Tanga kuanza mara moja. Muda mwingi Gibson alikuwa
akiuliza swali lakini maswali yake hayakuwa na majibu zaidi ya kutakiwa kusubiria mpaka pale ambapo wangeingia Tanga na kuangalia kama familia yake
ilikuwa salama.
Safari iliendelea kwa muda wa dakika arobaini na tano, wakawa wamekwishafika Tanga ambako wakaelekea mpaka katika kituo kikubwa cha polisi cha mkoa
huo. Kutokana na kujulikana na mapolisi wenzake, Manase akaingia mpaka ndani.
“Wapo wapi?” Manase alimuuliza polisi mmoja.
“Wapo ndani”
“Mateka nao wamepatikana?”
“Kwani walikuwa wangapi?”
“Wawili” Manase alijibu.
“Ndio. Ila sisi tumefanikiwa kumpata mmoja tu”
“Yupi?”
“Mwanamke”
“Mliangalia vizuri garini na kuona kwamba hakukuwa na mtoto?”
“Ndio. Tena gari lao lenyewe tumekuja nalo. Nadhani tukiwabana watatueleza mtoto yupo wapi” Polisi huyo alimwambia Manase.
“Kwa hiyo huyo mwanamke yupo wapi?”
“Hospitalini. Kijana mmoja alikuwa akitaka kumuua kwa kumnyonga shingo. Bahati nzuri shabaha za Shabani zilitusaidia” Polisi yule alijibu.
“Mmempeleka hospitali gani?”
“Hospitali ya mkoa”
“Hali yake ilikuwaje?”
“Mbaya. Yaani mbaya sana”
Manase hakutaka kuendelea kukaa ndani ya chumba kile, alichokifanya kwa wakati huo ni kutoka nje na kisha kumfuata Gibson ambaye akaanza kumuelezea kile
ambacho alikuwa ameelezewa na polisi aliyekuwa ndani ya chumba kile.
Gibson alionekana kuchanganyikiwa zaidi, hasira kali dhidi ya watekaji wae ikaonekana kumkaba, walichokifanya kwa wakati huo ni kuingia ndani ya gari na
kisha kuanza kuelekea hospitalini ambako wala hapakuwa mbali kutoka mahali hapo.
Ndani ya gari bado Gibson alionekana kuwa na hasira kupita kawaida, chuki juu ya Katie ikaanza kumuingia moyoni mwake na kuzidi kuongezeka kadri muda
ulivyozidi kwenda mbele. Alimchukia sana Katie, kwake, tayari aliona kwamba kila kitu kilikuwa kimekwisha, hakuona sababu iiyompelekea Katie kuamua
kuwatuma watu kuja nchini Tanzania kwa ajili ya kuiteka familia yake.
“Nitamuua huyu mwanamke” Gibson aliwaambia huku akionekana kuwa na hasira za waziwazi.
“Achana nae. Kwanza tuangalie hali ya mke wako” Manase alimwambia Gibson.
“Sawa! Ila haijalishi kama atapona au atakufa. Nitamuua tu” Gibson alimwambia.
“Nakushauri uiachie sheria ili ichukue mkondo wake. Unaweza kujuta hapo baadae kwa kujichukulia sheria mkononi” Manase alimwambia Gibson ambaye
alionekana kutokuelewa kabisa.
Baada ya dakika chache wakawa wamekwishafika katika hospitali ya mkoa wa Tanga na kisha kuteremka. Moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kuelekea
sehemu ya mapokezi ambako wakajitambulisha na kisha kuelekezwa sehemu ambayo walitakiwa kuelekea.
“Twendeni kwa dokta mkuu kwanza” Manase aliwaambia.
“Kwa nini tusielekee kwenye chumba alicholazwa mke wangu na mtoto wangu?” Gibson aliuliza bila kujua kwamba mtoto wake hakuwepo mahali hapo
“Muda wa kuona wagonjwa umekwishapita na ndio maana nawaambia twendeni huko ili tuongee nae na kuturuhusu” Manase aliwaambia.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kupinga, walichokifanya ni kuanza kuelekea katika ofisi ya dokta mkuu na kukaribishwa. Uso wa Gibson
haukuonekana kuwa na furaha kabisa, muda wote alikuwa akionekana kuwa na majonzi makubwa.
Wakaanza kujitambulisha kwa dokta Mnyuzu na kisha kutaka kupatiwa maelezo yanayotosheleza kuhusiana na mgonjwa wao ambaye alikuwa ameletwa ndani ya
hospitali ile ya mkoa. Hata kabla ya kuongea kitu chochote kile, dokta Mnyuzu akakaa kimya kwa muda huku akiwaangali kwa zamu, aliporidhika,
akayagandisha macho yake usoni mwa Gibson.
“Mwanamke yule ni mke wako?” Dokta Mnyuzu alimuuliza Gibson.
“Ndio” Gibson alijibu.
“Pole sana. Ni habari mbaya lakini haina budi kukupa. Wewe ni mwanaume, nakuomba ujikaze kiume” Dokta Mnyuzu alimwambia Gibson ambaye hapo hapo
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
akaonekana kuishiwa nguvu, akakiegemeza kichwa chake huku akimwangalia Dokta Mnyuzu.
“Mkeo amefariki” Ilikuwa ni sauti ambayo ilikuwa ikisikika mara kwa mara kichwani mwa Gibson.
Msichana Katie alikuwa akiendelea kufanyakazi zake kama kawaida huku akionekana kutokuwa na wasiwasi hata kidogo. Muda wote alikuwa bize akifanya kazi
zake lakini huku mawazo yake yakiwa yanamfikiria Gibson. Mapenzi ambayo alikuwa nayo kwa Gibson yalikuwa makubwa, pengo kubwa ambalo alikuwa nalo
moyoni mwake wala halikuweza kuzibika hata mara moja.
Gibson alikuwa ameuumiza moyo wake kupita kawaida, muda mwingi alikuwa akionekana mpweke, muda wote alikuwa akiomba Mungu vijana ambao alikuwa
amewatuma nchini Tanzania wafanye kazi kama ambavyo aliitaka ifanyike. Muda mwingi alikuwa akiwasiliana nao kwa kutumia mtandao wa simu wa Kimataifa
wa Tricom ambao ulikuwa ukitumiwa sana na wazungu kutoka Marekani na barani Ulaya.
Kila alipokuwa akiwasiliana nao, aliambiwa kuwa mvumilivu kwa sababu kila kitu kilikuwa kikiendelea kama kilivyotakiwa kiwe. Katie hakuwa na jinsi, kitu
ambacho alikuwa akikifanya kwa wakati huo ni kuendelea kuwa mvumilivu kama kawaida.
Katie aliendelea kuwa kwenye lindi la mawazo mpaka kipindi kile ambacho akaanza kupokea maua mbalimbali ya kimapenzi pamoja na zawadi nyingi
zilizokuwa zikihusu mapenzi. Katie alionekana kushangaa, hakujua ni mtu gani ambaye alikuwa akimtumia zawadi hizo ambazo zilikuwa zikija mfululizo, yaani
asubuhi, mchana na jioni.
Kutokana na hali ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho wala hakutaka kujali sana kuhusiana na maua hayo na wala hakutaka kumjua mtu ambaye alikuwa
akimtumia vitu hivyo vyote. Mawazo yake kwa wakati huo yalikuwa yametulia kwa mtu mmoja tu, mtu ambaye alikuwa amemuachia tundu kubwa moyoni
mwake, tundu ambalo lilikuwa likiendelea kuuma kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Zawadi ziliendelea kumiminika nyumbani kwake zaidi na zaidi mpaka kufikia kipindi ambacho akatamani kumuona mtu huyo ambaye alikuwa akitumia muda
mwingi kumtumia zawadi mbalimbali. Alichokifanya ni kumpigia simu kupitia namba zake ambazo alikuwa akiziambatisha katika zawadi mbalimbali alizokuwa
akimletea.
Siku iliyofuata, mwanaume huyo, Daniel akafika nyumbani kwa Katie na moja kwa moja kukaribishwa ndani. Katie hakuonekana kuamini, mwanaume ambaye
alikuwa ameingia ndani ya nyumba yake alikuwa akimfahamu vilivyo, alikuwa Daniel, mtu ambaye alikuwa mpenzi wake na ndiye alikuwa mtu ambaye aliutoa
usichana wake katika miaka ya nyuma, kipindi ambacho walikuwa wakiishi mitaani.
Kwa mbali, uso wake ukaanza kuonyesha tabasamu, akaanza kumsogelea Daniel na kisha kumkumbatia. Hiyo ikaonekana kuwa faraja kwake, kumbatio ambalo
alikuwa amelipata kutoka kwa Daniel likaonekana kumfariji na kumsahaulisha na Gibson kwa sekunde chache.
Baada ya hapo wakaanza kuongea mambo mengi ya nyuma ambayo yalikuwa yametokea katika maisha yao katika kipindi ambacho walikuwa wakiishi mitaani
hata kabla ya Katie kujiingiza katika uchezaji wa filamu za ngono, hatua ambayo ilionekana kumuumiza sana Daniel ambaye alikuwa kwenye mapenzi mazito na
Katie.
Daniel hakutaka kuwa nyuma, nae akaanza kumuelezea Katie kuhusu maisha yake toka siku ambayo walikuwa wametengana. Alimuelezea mambo mengi mpaka
alivyokwenda nchini Uingereza na kutafuta fedha kwa nguvu mpaka kufikia hatua ya kuwa tajiri mkubwa. Historia zao zilionekana kufanana, walianzia maisha
ya mitaani, maisha ambayo hayakuwa na ubora kabisa ila katika muda huo, wote walikuwa matajiri wakubwa.
Daniel hakutaka kukaa kimya, kwa wakati huo bado alikuwa akiona kwamba kulikuwa na uhitaji mkubwa wa kuzielezea hisia zake kwa msichana huyo, Katie na
kwa jinsi moyo wake ulivyokuwa umeumia hasa mara baada ya kuona kwamba alikuwa ameolewa na mtu mwingine. Uso wa Daniel ulionyesha dhahiri kwamba
alikuwa ameumizwa sana na tukio lile la ndoa na hivyo alikuwa akiomba Mungu kila siku kwamba awe tena na Katie kama ilivyokuwa zamani.
“Unafikiri Mungu amejibu maombi yako?” Katie aliuliza huku akimwangalia Daniel usoni.
“Yeah! Asilimia mia moja” Daniel alijibu huku akionekana kujiamini.
“Bado Daniel Itakubidi uombe sana. Unakumbuka kwamba nilikuacha ingawa ulikuwa kwenye mapenzi nami?” Katie alimuuliza Daniel.
“Ndio! Nakumbuka”
“Nilikuacha kwa sababu nilitaka kuwa huru zaidi ya jinsi nilivyokuwa. Sikuwa na fedha, nilikuwa nikishinda hata masaa kumi bila chakua. Nilitaka kuwa tajiri
kama nilivyo kwa sasa. Nitazame sasa, ninaweza kula chochote ninachotaka, ninaweza kwenda popote ninapotaka kwenda. Nina kila kitu kwa sasa Daniel” Katie
alimwambia Daniel.
“Ninafahamu. Lakini una maana gani kuniambia hayo yote?” Daniel aliuliza.
“macho yangu” Katie alimwambia Daniel.
“Ninakupenda Katie” Daniel alimwambia Katie.
“Macho yangu yanakwambia kila kitu” Katie alimwambia Daniel.
Daniel akasimama pale alipokuwa amekaa na kisha kuanza kumfuata Katie katika kochi alilokuwa amekaa na kisha kupiga magoti mbele yake. Tayari macho ya
Daniel yalikuwa yamekwishabadilika, yakaanza kuwa mekundu kwa wakati huo.
Tayari macho ya Katie yalikuwa yamekwishamueleza kila kitu kwamba kwa wakati huo hakutaka kuwa nae. Kwa kiasi fulani Daniel akaonekana
kuchanganyikiwa, alikuwa ametumia kiasi kikubwa cha fedha kwa kumtenganisha Katie na Gibson, sasa ingeleta maana gani kama nae pia asingekuwa na
msichana huyo na wakati alikuwa ametoa zaidi ya dola milioni kumi.
Daniel aliona kwamba kulikuwa na kila sababu ya kulipigania penzi lake, aliona kwamba kulikuwa na kila sababu ya kumrudisha Katie katika mikono yake.
Hakujali ni kiasi gani cha fedha ambacho angetumia kwa wakati huo, kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kumuona Katie akirudi tena katika mikono yake kama
ilivyokuwa zamani, nyakati zile walizokuwa wakiishi mitaani kama watoto wa mitaani.
Daniel akamshika Katie mkono huku akimwangalia usoni mwake. Macho ya Daniel yalikuwa yakionyesha kila dalili kwamba kwa wakati huo alikuwa akimhitaji
sana Katie zaidi ya kitu chochote kile. Alipoona kwamba mguso wake mkono mwa Katie haukubalisha kitu chochote kile, akaupandisha na kuishika shingo ya
Katie kwa mikono yake miwili.
“Ninakupenda”Daniel alimwambia Katie kwa mara nyingine tena.
Mawazo ya Katie yakaanza kurudi nyuma, tayari hali ya huruma ikaonekana kumuingia. Katika maisha yake, hakuwahi kumuona mwanaume akitoa machozi kwa
ajili yake kama ilivyokuwa kwa Daniel katika kipindi hicho. Mawazo yake ya nyuma ndio ambayo yalikuwa yakiongeza chachu ya kuona kwamba kulikuwa na
kila sababu ya kuwa na mwanaume huyo ambaye kwake alionekana kuwa mvumilivu kupita kawaida.
“Halikuwa chaguo langu sahihi” Katie alimwambia Daniel.
“Ninafahamu. Muache aende zake. Sahau kila kitu kuhusu yeye” Daniel alimwambia Katie.
“Vipi kuhusu kisasi?” Katie aliuliza huku akianza kulia.
“Hakuna uhitaji wa kufanya hivyo” Daniel alimwambia Katie.
Wote wakajikuta wakisimama na kisha kukumbatiana. Japokuwa kwa wakati huo lilikuwa jambo gumu sana kwa Katie kumsahau Gibson lakini akaona
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
kulikuwa na kila sababu za kumsahau mwanaume huyo na kumuacha Daniel achukue nafasi ndani ya moyo wake. Mpaka kufikia hatua hiyo, tayari Daniel
alikuwa akijiona kuwa mshindi, kiasi kikubwa cha fedha ambacho alikuwa amekitumia kilionekana kufanya kazi ile ambayo aliikusudia kufanyika.
Huo ndio ukawa mwanzo wa mahusiano yao ya kimapenzi kwa mara ya pili tena. Kila mmoja akaanza kumuahidi mwenzake kwamba angempenda mpaka pale
ambapo kifo kingewatenganisha. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifikiria maisha ya baade yangekuwaje baada ya hapo, kitu walichokuwa wakikifikiria ni
kufunga ndoa na kuishi pamoja hapo baadae.
****
“Unamaanisha mke wangu na mtoto wangu wamekufa” Gibson aliuliza huku akionekana kutokuamini.
Kila mmoja ndani ya ofisi ile akaonekana kumshangaa Gibson. Dokta hakuwa ameongea kitu chochote kuhusiana na mgonjwa wake lakini tayari Gibson
akaonekana kufikiria jambo jingine zaidi. Hata kabla ya kuongea kitu chochote kile, dokta akaanza kuyafikiria maneno ya Gibson. Alijua na uhakika kwamba
mgonjwa ambaye alikuwa ameletwa hospitalini pale ambaye alitekwa alikuwa mmoja, sasa huyo mtoto alitokea wapi?
Ingawa swali hilo lilianza kumtatiza kichwani mwake lakini dokta Mnyuzu hakutaka kuuliza kitu chochote kile zaidi ya kulifungua faili ambalo lilikuwa mezani
mwake na kisha kuanza kuandika vitu fulani ambavyo hakukuwa na mtu yeyote ambaye alivifahamu.
“Mke wako ni mzima japokuwa hali yake ni mbaya sana” Dokta Myuzu alimwambia Gibson.
“Imekuwaje tena?”
“Hali inaonyesha kwamba alikuwa amekabwa kwa kipindi kirefu hali ambayo ilimfanya kutovuta pumzi kwa kiasi kikubwa, mbaya zaidi, kila alipokuwa
akijaribu kuvuta pumzi, hiyo hivyo pumzi ndogo ambayo ilikuwa ikiingia, ilikuwa ikiingia na vumbi jingi” Dokta Mnyuzu alimwambia Gibson maneno ambayo
yalionekana kumchanganya.
“Kwa hiyo hatopona?”
“Simaanishi hivyo. Kupona anaweza kupona japokuwa inaweza kuchukua muda mrefu kwani tumemuwekea mashine ya hewa ya oksijeni ili tuweze kuona
maendeleo yake yatakuwaje?” Dokta Mnyuzu alimwambia Gibson.
“Nakuomba mponyeni mke wangu. Ninampenda sana, sitaki kumpoteza” Gibson alimwambia dokta Mnyuzu.
“Hata sisi hatutaki kumpoteza na ndio maana tunajitahidi kufanya kila tuwezacho kufanya kwa ajili ya kuirudisha afya yake kama ilivyokuwa kabla” Dokta
Mnyuzu alimwambia Gibson.
“Na vipi kuhusu mtoto wangu?” Gibson aliuliza.
“Mtoto yupi?” Dokta Mnyuzu aliuliza huku akionekana kushangaa.
“Mtoto wangu, Genuine”
“Sijui kama kuna mtoto aliletwa hapa. Alikuwa na mkeo?”
“Ndio”
“Hapana. Mwanamke aliletwa peke yake” Dokta Mnyuzu alimwambia Gibson.
“Sasa mtoto wangu yupo wapi?” Gibson aliuliza.
“Mmmh! Sijui” Dokta alijibu.
“Kuna kitu nadhani kitakuwa kimeendelea. Maelezo yote juu ya mtoto tutayapata kutoka kwa wale watekaji” Manase aliwaambia.
Hawakutaka kuendelea kusubiri ndani ya ofisi ile, walichokifanya ni kuondoka na kuelekea katika chumba alicholazwa Prisca na kisha kumuangalia. Prisca
alikuwa kimya kitandani, kwa kifupi alikuwa akionekana kama mtu ambaye tayari alikuwa amekwishakata roho. Gibson akasimama pembeni yake, tayari macho
yake yalikuwa yamekwishaanza kutoa machozi, picha iliyoonekana kwa mkewe ikaonekana kumuumiza sana.
“Prisca mke wangu! Genuine yupo wapi?” Gibson alimuuliza Prisca huku machozi yakimtoka japokuwa alikuwa akifahamu kwamba Prisca asingeweza kujibu
kitu chochote kile.
*****
Reuben, Filbert na Edward walikuwa chini ya ulinzi katika chumba kimoja kidogo huku tayari mawasiliano yakiwa yamekwishafanyika na makao makuu ya
polisi ya jijini Dar es Salaam na hivyo watu hao walitakiwa kusafirshwa mpaka ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Taratibu zote zilikuwa zimekamilika lakini mpaka muda huo ni kamanda Manase ndiye alikuwa akisubiriwa kutokana na kuwa na maswali machache na watu
hao. Ilipofika saa kumi na mbili jioni, Manase akaingia katika kituo hicho na moja kwa moja kuelekea katika chumba kile na kuonana na watekaji wote watatu
ambao walikuwa chini ya ulinzi wa polisi.
Kamanda Manase akaanza kuwaangalia kwa zamu, alipoona ameridhika, akakiweka chini kiti ambacho alikuwa ameingia nacho ndani ya chumba kile na kisha
kutulia. Kwa wakati huo alikuwa akihitaji kufahamu kitu kimoja tu, sehemu alipokuwa mtoto Genuine ambaye hadi katika kipidi hicho hawakuwa wamemuona.
Reuben hakutaka kuficha, akaanza kuelezea kila kitu kilichokuwa kikihusiana na mtoto Genuine. Ilikuwa ni taarifa ambayo ilimhuzunisha sana Manase, hakujua
namna ambavyo alitakiwa kuifikisha taarifa ile kwa Gibson ambaye alikuwa akitamani sana kusikia taarifa kuhusu mtoto wake wa pekee.
Manase hakutaka kukaa sana ndani ya chumba kile, alichokifanya ni kuanza kuelekea hospitalini ambako akamkuta Gibson akiwa ndani ya chumba kile huku
akiendelea kuongea maneno mengi mbele ya uso wa mke wake japokuwa Prisca hakuwa amefumbua macho.
“Kuna taarifa nimepewa kuhusu mtoto wako” Manase alimwambia Gibson ambaye akamsogelea karibu huku akiwa na shauku ya kutaka kujua zaidi.
“Inasemaje?”
“Njoo nje kwanza” Manase alimwambia Gibson na kisha wote kuelekea nje.
Manase hakutaka kuficha kitu chochote kwa wakati huo, akamwambia Gibson kila kitu ambacho aliambiwa na Reuben ndani ya chumba kile. Gibson akauhisi
mwili wake ukifa ganzi, akaanza kutetemeka huku hasira zikianza kumpanda.
“Unasemaje?”
“Hivyo ndivyo ilivyotokea. Kwa kweli imenihuzunisha sana. Huu ni unyama mkubwa sana kuwahi kutokea” Manase alimwambia Gibson.
Hiyo ilikuwa ni taarifa mbaya ambayo iliuumiza moyo wa Gibson kupita kawaida. Machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwa Gibson, kile ambacho alikuwa
amekisikia kiliuchoma sana moyo wake. Akalifuata benchi na kisha kulikalia huku akikiinamisha kichwa chake chini.
Taswira ya mtoto wake ikaanza kumjia kichwani, alikumbuka mambo mengi kuhusiana na mtoto wake, akalikumbuka tabasamu lake, akaanza kukikumbuka
kicheko chake hasa pale ambapo alikuwa akimfanyia vitu ambavyo vilikuwa vikimfanya kucheka.
Katika kila kitu ambacho alikuwa akikifikiria kwa wakati huo kilikuwa kikizidi kumuumiza moyo wake kupita kawaida. Mtoto wake ambaye alikuwa
akimpenda sana, kwa wakati huo hakuwa pamoja nae tena, alikuwa ameuawa katika kifo kibaya ambacho kila mtu ambaye angesikia, angeumia moyoni.
Wakati mwingine, alihisi kuisikia sauti moyoni mwake, sauti ambayo ilikuwa ikisisitiza kwamba kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea yalikuwa ni matunda ya
vitu ambavyo alikuwa amevipanda kabla. Kwa wakati huo ulikuwa muda wa mavuno wa yale ambayo alikuwa amepanda siku za nyuma.
Usaliti ambao alikuwa ameufanya kwa mke wake, Prisca ndio ambao ulikuwa umeleta matatizo yale yote. Alijua fika kwamba kama asingekuwa amemsaliti mke
wake, Prisca basi kwa wakati huo asingekuwa katika wakati mgumu kama ambavyo alivyokuwa kwa wakati huo.
“Ila mimi ndiye niliyesababisha haya yote” Gibson alimwambia Manase.
“Najua. Ila kwa sasa hautakiwi kujilaumu. Kila kilichotokea, kimetokea” Manase alimwambia Gibson.
“Nafahamu. Ila naamini kama nisingekuwa nimemsaliti Prisca kipindi cha nyuma, nina uhakika hata jambo hili lisingetokea kwa sasa. Usaliti wangu
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
umenigharimu sana katika maisha yangu. Usaliti ambao niliufanya kipindi kile, hizi ndizo athari zake. Ninajuta kumsaliti mke wangu” Gibson alimwambia
Manase ambaye alikuwa kimya kumsikiliza.
“Fedha zilinifanya nimsaliti mke wangu. Hizi hizi fedha haziwezi kunirudishia mtoto wangu. Huu umekuwa ni kama msumali wa moto ndani ya moyo wangu,
tukio hili limeniachia kidonda kikubwa moyoni, kidonda ambacho sidhani kama kuna siku kitakuja kupona” Gibson alimwambia Manase.
“Usijali Gibson. Kila kitu ni mipango ya Mungu”
“Hapana. Vitu vingine si mipango ya Mungu. Mungu hakupanga nimsaliti mke wangu, Mungu hakupanga nisafiri kwenda nchini Marekani na kufunga ndoa na
msichana Katie. Hii ilikuwa mipango yangu, tamaa zangu za kutaka fedha ndizo ambazo zimenifanya niwe katika hali hii kwa sasa” Gibson alimwambia Manase
huku akitokwa na machozi.
“Usilie Gibson. Jikaze. Wewe ni mwanaume” Manase aliendelea kumbembeleza Gibson.
“Kujikaza ni vigumu sana. Inaniuma sana kumpoteza mtoto wangu ambaye nilikuwa nikifanya mambo mengi kwa ajili yake. Inawezekana mtoto wangu
angekuwa rais, inawezekana mtoto wangu angekuwa waziri mkuu. Ndoto zake za kufikia mafanikio zimefutika kwa sababu ya tamaa zangu za kutamani sana
fedha. Nilichokuwa nikikifikiria ni fedha tu, sikutaka kufikiria ni kitu gani kingetokea baada ya hapo. Moyo wangu unajuta, sijui ni kwa namna gani nitakuwa
nikiishi na mke wangu bila ya kuwa na mtoto wetu. Nadhani yatakuwa maisha yatakayoniumiza sana, nadhani yatakuwa ni aina ya maisha ambayo yatanifanya
kukosa amani na furaha ndani ya moyo wangu” Gibson alimwambia Manase ambaye alibaki kimya huku nae akianza kuyafikiria maneno ya Gibson.
Gibson aliongea maneno mengi tena kwa sauti ya unyonge. Ingawa maneno yalikuwa mengi lakini hayakuweza kubadilisha kitu chochote kile, ukweli ulibaki
vile vile kwamba Genuine alikuwa ameuawa kinyama.
Kila kitu kikapangwa na kisha baada ya siku moja safari ya kurudi jijini Dar es Salaam kuanza. Gibson hakutaka kumuacha mke wake ahudumiwe mkoani Tanga
jambo lililompelekea kumsafirisha kuelekea jijini Dar es Salaam kwa kutumia usafiri wa ndege.
Watanzania bado walikuwa wakiendelea kulaani kitendo kile cha utekaji ambacho kilikuwa kimefanyika. Muda mwingi watu walikuwa wakitembea na mabango
kuelekea katika ubalozi wa Marekani. Maandamano yalikuwa yamefanyika kwa takribani siku tatu mfululizo jambo lililompelekea balozi wa Marekani nchini
Tanzania kuwasiliana na serikali ya Marekani ili kuanza kufuatilia kuhusu vijana wao, ikiwezekana harakati zote zifanyike mpaka hukumu ya watekaji wale
kufanyika.
Waandishi wengi wa habari walikuwa wakifika katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuanza kuongea na Gibson ambaye muda mwingi alikuwa akionekana
kuwa mnyonge kupita kawaida. Mtu ambaye alikuwa akisubiriwa apate fahamu ni Prisca tu ambaye angeeleza kila kitu na hata mahali ambapo mtoto Genuine
alikuwa ametupwa.
Siku zikaendelea kukatika, wazazi wote wa pande mbili pamoja na ndugu na marafiki wa karibu walikuwa wakifika hospitalini pale kwa ajili ya kumjulia hali
Prisca ambaye mpaka wiki imekatika lakini bado hakuwa amerudiwa na fahamu.
“Kipindi kirefu kimepita. Hii inaonekana kuwa si kawaida kabisa” Gibson alimwambia dokta Marwa ambaye alikuwa akimshughulikia Prisca kila siku.
“Mshipa wake wa fahamu umeshtuka sana. Mara nyingi watu ambao wanapatwa na tatizo hili huwa wanatumia muda mrefu kitandani. Mshipa wa fahamu
unaposhtuka kwa nguvu, huwa wakati mwingine unaweza kuufanya hata uti wa mgongo kupata matatizo. Na ikitokea uti wa mgongo kupata tatizo, mgonjwa
anaweza akapooza sehemu moja ya mwili” Dokta Marwa alimwambia Gibson maneno ambayo yalionekana kumshtua.
“Kwa hiyo mke wangu atapooza?”
“Sikuwa na maana hiyo. Hapo nimejaribu kukwambia kitu ambacho mara nyingi hutokea. Mkeo anaweza kurudiwa na fahamu na wala asipate tatizo lolote lile”
Dokta Marwa alimwambia Gibson.
Yalikuwa ni maneno makali ambayo yaliuumiza sana moyo wa Gibson, muda mwingi alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi kupita kawaida, meneno yale
ambayo aliambiwa kwamba mke wake angeweza kupooza yalikuwa yamemtiwa wasiwasi kupita kawaida. Upweke ukaongezeka maishani mwake, kwa wakati
huo wala hakutaka kusimamia biashara zake ambazo zilikuwa zikiendelea kumuingizia mamilioni, muda mwingi alikuwa akiutumia kuwa karibu na kitanda
alicholazwa mke wake.
“Utarudi katika fahamu zako mpenzi na kuniambia mtoto wangu walimtupa sehemu gani. Hata kama atakuwa amekufa, nitahitaji kuliona hata kaburi lake tu”
Gibson alikuwa akimwambia mkewe ambaye bado alikuwa kwenye usingizi wa kifo.
Maisha ya kutokwa na machozi yakawa sehemu ya maisha yake, kila siku alikuwa mtu wa kulia sana jambo ambalo lilikuwa likimpelekea kudhoofika mwili
wake kupita kawaida. Watu mbalimbali walikuwa wakimtembelea na kumfariji lakini wala hawakuweza kubadilisha kitu chochote kile, kila siku Gibson alikuwa
mtu wa kulia tu.
Wiki ya pili ikakatika, wiki ya tatu ikaingia lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yale. Bado Prisca alikuwa kwenye usingizi wa kifo jambo ambalo lilionekana
kuwachanganya hata madaktari wenyewe. Mirija ambayo ilikuwa ikipitishwa katika sehemu yake ya tumbo ndio ambayo ilikuwa ikitumika kumlisha chakula
pamoja na kumywesha maji.
“Au amekwishakufa?” Gibson alimuuliza dokta Marwa.
“Hapana. Bado ni mzima. Hata moyo wake unadunda. Tuvumilie hadi mshipa wa fahamu utakapokuwa sawa” Dokta Marwa alimwambia Gibson.
Hakukuwa na cha kufanya kwa wakati huo, waliendelea kusubiri zaidi na zaidi. Mwezi ukakatika, hakukuwa na mabadiliko yoyote ya maendeleo, bado Prisca
alikuwa amelala kitandani huku moyo wake ukidunda kwa mbali sana.
****
Katie alikuwa akijiandaa kutoka mtoko wa usiku pamoja na Daniel ambaye alipanga waonane katika mghahawa wa Mc Donald kwa ajili ya kupata chakula cha
usiku pamoja na kununua Ice Cream ambazo zilikuwa zikipendwa sana. Huo ulikuwa ni mtoko ambao ulikuwa ukiwahusisha watu wawili ambao walikuwa
wameishi sana katika maisha ya mitaani kipindi cha nyuma na wakati huo walikuwa matajiri wakubwa.
Kila vazi ambalo alikuwa akilivaa Katie lilionekana kutokumpendeza jambo ambalo lilimfanya kubadilisha kila aina ya vazi ambalo alikuwa ameliweka katika
kabati lake kubwa la nguo. Alianza na gauni jekundu ambalo lilikuwa na maua mawili kiunoni, hilo hakuliona kumfaa kwa siku hiyo, akaamua kuliweka
pembeni.
Hapo ndipo alipoamua kuchukua gauni jingine ambalo lilikuwa na rangi mbalimbali zilizopangwa kimpangilio huku likiwa na vitu vilivyokuwa vikinga’aa sana,
hilo nalo akaliona kutokufaa kwa usiku huo. Mtoko huo kwake ulionekana kuwa mtoko mmoja mkubwa sana ambao ungewafanya kuongea mambo mengi,
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
kupeana mapenzi na Daniel na hata kufanya mapenzi kama siku ile ya kwanza ambayo walifanya.
Alibadilishabadilisha mavazi zaidi ya kumi na mbili usiku huo na ndipo alipolipata vazi moja ambalo kwake lilionekana kuwa zuri katika usiku huo wa siku
hiyo. Baada ya kumaliza kujiandaa, akajipulizia manukato mazuri ambayo yalikuwa na gharama na kisha kulifuata gari lake na kuanza kuelekea katika mghahawa
huo.
Ndani ya gari, mawazo yake kwa kipindi hicho yalikuwa yaimfikiria Daniel tu, Gibson kwa wakati huo wala hakutaka kumpa sana nafasi kichwani mwake.
Aliona kwamba kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea kati yake na Gibson kilitakiwa kusahaulika katika maisha yake na kujipanga upya na Daniel.
Kwa wakati mwingine alikuwa akiwafikiria vijana wake ambao alikuwa amewatuma kwa kufanya kazi moja ya kumuua mwanamke ambaye alikuwa akiishi na
Gibson kwa wakati huo. Mpaka kufikia kipindi hicho wala hakuwa amepata taarifa zozote kutoka kwa vijana wake tangu siku mbili zilizopita ambazo zilikuwa
siku za mwisho kuongea nao.
Wala Katie hakuchukua muda mrefu akawa amekwishafika katika mghahawa huo ambao mara nyingi sana ulikuwa ukitembelewa na masupastaa nyakati za usiku
na kisha kuanza kupiga hatua kuelekea katika meza ambayo Daniel alikuwepo. Mara tu Daniel alipomuona Katie, akainuka na kuanza kumsogelea, alipomfikia,
akamkumbatia na kumshushia mabusu kadhaa ya mdomoni.
Wakaifuata meza na kukaa huku mhudumu akija na wote kuagiza chakula ambacho walikiona kufaa sana kula siku hiyo. Wakabaki wakiongea mengi, katika
kipindi hicho ndio ulikuwa muda muafaka wa kukumbushiana mambo mengi ya nyuma yaliyopita, hasa katika kipindi kile ambacho walikuwa watoto wa
mitaani.
Kipindi kile kilionekana kuwa kipindi kizuri kwao wote, walikula na kinywa huku wote wakionekana kuwa na furaha. Furaha ambazo walikuwa nazo katika
kipindi hicho ndizo ambazo ziliwafanya kupeana ahadi ya kuishi pamoja kama mume na mke mara kila kitu kitakapokaa sawa.
Baada ya hapo, moja kwa moja wakaanza safari ya kuelekea katika hoteli ya Pasiphian ambayo ilikuwa kando ya jiji hilo la New York na kisha kulala huko.
Usiku wa siku hiyo kwao ukaonekana kuwa usiku wa kukumbuka, walipeana mapenzi ya dhati mpaka kufikia kipindi ambacho kila mtu alikuwa hoi kitandani.
Asubuhi ya siku iliyofuata, wakaongozana wote na kuelekea nyumbani kwa Katie. Hali ambayo waliikuta nyumbani hapo ilionekana kumshtua kila mmoja. Nje,
kulikuwa na magari mawili ya polisi huku mapolisi wawili wakiwa nje ya eneo la nyumba ile na huku wengine wakiwa wamekwishaingia ndani ya eneo la
nyumba ile.
Katie akaonekana kushtuka, akateremka kutoka garini na moja kwa moja kuwafuata mapolisi ambao walikuwa nje ya nyumba yake. Kitu cha kwanza
walichokifanya mapolisi wale mara baada ya kumuona ni kuanza kumsogelea.
“What the hell is going on here? (Kitu gani kinaendelea mahali hapa?)” Katie aliuliza huku akionekana kushangaa.
“We are looking for you mom (Tunakutafuta wewe)” Polisi mmoja alimwambia.
Hapo hapo mapolisi wale wakamwambia dhumuni la wao kufika mahali pale na kisha kumwambia kupanda ndani ya gari huku wale mapolisi ambao walikuwa
ndani ya eneo la nyumba yake wakiwa wamekwishafika mahali pale.
Daniel ambaye alikuwa amekwishateremka garini akaanza kuwafuata na kisha kuanza kuwauliza maswali kadhaa ambayo hakukuwa na polisi yeyote ambaye
aliyajibu maswali yale. Moja kwa moja safari ya kuelekea katika kituo kikuu cha polisi katika jiji hilo la New York kuanza huku tayari Katie akionekana kuanza
kuhisi kitu.
Walipofika kituoni, akateremshwa na kisha kuanza kupelekwa ndani ya jengo hilo ambako akaingizwa ndani ya chumba kimoja kwa ajili ya kuulizwa maswali
kadhaa. Polisi mmoja ambaye alivalia suti akaingia ndani ya chumba kile na kisha kuanza kumuuliza maswali kadhaa huku akimtolea picha ambazo walipigwa
Reuben, Filbert na Edward nchini Tanzania jambo ambalo lilimfanya kuona kwamba hisia zake zilikuwa zimehusika moja kwa moja na kile ambacho alikuwa
akikihisi.
“I want to talk to my lawyer (Nataka kuongea na Mwanasheria wangu)” Katie alimwambia polisi yule kila alipoona maswali yakizidi kuulizwa.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kesi hiyo ulipoanza huku Reuben na wenzake wakiwa wamepelekwa nchini Marekani. Kwa kuwa Prisca bado alikuwa amepoteza
fahamu, Gibson na dokta Philip ndio ambao walikuwa mashahidi wa kwanza katika kesi hiyo ambayo ilikuwa ikivuma sana katika vyombo mbalimbali vya
habari duniani.
Kesi ilivuma zaidi ya miezi mitatu, Katie akakutwa na hatia ambayo ikampelekea kufungwa miaka ishirini jela huku vijana wake ambao alikuwa amewatuma
kufanya mauaji wakifungwa miaka ishirini na tano jela.
Hiyo ilionekana kuwa hukumu kubwa kwa Katie, muda wote mahakamani alikuwa akilia huku akijaribu kumuomba msamaha Gibson ambaye alishindwa
kuvumilia na machozi kumtoka. Hilo halikuweza kubadilisha kitu chochote kile, siku hiyo ndio ambayo Katie alikwenda kuanza kukitumikia kifungo chake
katika gereza la South Greeen, gereza lililokuwa kusini mwa jiji la New York nchini Marekani.
Japokuwa Katie alikuwa amefungwa lakini Daniel hakutaka kuachana nae, bado mapenzi ambayo alikuwa nayo kwa Katie yalikuwa makubwa. Mara kwa mara
alikuwa akimtembelea gerezani na baada ya mwaka mmoja kufunga ndoa pamoja katika kanisa la gereza lililokuwa hapo hapo gerezani.
Japokuwa maisha yalionekana kuwa magumu, lakini katika kipindi ambacho alikuwa akionana na mke wake Katie yalikuwa yakionekana kuwa rahisi sana.
Furaha ikaonekana kutawala katika mahusiano yao japokuwa walikuwa wakiishi tofauti sana. Kwa kuwa walikuwa mume na mke, kila walipokuwa wakikutana
walikuwa wakipewa uhuru wa kufanya kila kitu mpaka pale Katie alipojifungua mtoto wa kiume na kumuita jina la Hope kwa kutumaini kwamba kuna siku
angetoka gerezani na kuishi pamoja na familia hiyo.
“I love you Katie.....I love you Katie (nakupenda Katie....Nakupenda Katie)” Daniel alimwambia Katie muda mchache mara baada ya kujifungua huku wakiwa
wamekumbatiana na mtoto Hope akiwa mikononi mwa Katie.
“I love you too (Nakupenda pia)” Katie alimwambia Daniel.
****
Miezi sita ilikuwa imekatika lakini Prisca hakuweza kurudiwa na fahamu zake. Kila siku Gibson alikuwa akiomba Mungu lakini sala zake zilionekana
kutokujibiwa kabisa. Hali ya mke wake, Katie ilikuwa ikimuumiza kila siku, kila alipokuwa akimuona pale kitandani alikuwa akiumia kupita kawaida.
Moyo wake bado ulikuwa na mapenzi ya dhati kwa mke wake huyo ambaye kwake alionekana kuwa kama mfu kitandani pale. Kila siku marafiki zake pamoja na
ndugu zake walikuwa wakifika hospitalini pale kwa ajili ya kumuona Prisca ambaye alikuwa hajafumbua macho yake.
Siku ziliendelea kukatika mpaka pale Gibson alipokwenda nchini Marekani kusimamia kesi ya mauaji ambayo ilikuwa ikiwakabiri watu wanne. Kwa jinsi
alivyokwenda na kurudi baada ya miezi mitatu wala hakukuwa na mabadiliko yoyote yale, Prisca hakuwa amefumbua macho yake, alikuwa kama jinsi
alivyomuacha kabla ya kuondoka.
Siku ziliendelea kukatika. Ilipofika tare 5 mwezi wa 7, siku hiyo ilionekana kuwa kama muujiza kwa Prisca, kwa mara ya kwanza baada ya miezi mingi, akaweza
kufumbua macho yake tena. Tukio lile likaonekana kumshtua kila mtu, manesi wote waliona jambo lile kuwa kama muujiza ambao wala hawakuwa
wakiutegemea. Kitu walichokifanya ni kumpigia simu dokta Marwa ambaye akafika mahali hapo na kushuhudi kwa macho yake. PRISCA ALIKUWA
AMERUDIWA NA FAHAMU.
****
Dokta Marwa hakuweza kuvumilia, kitu alichokifanya kwa wakati huo ni kuchukua simu yake na kisha kumpigia Gibson ambaye baada ya dakika thelathini
akawa amekwishafika ndani ya eneo la hospitali hiyo na moja kwa moja kuelekea katika chumba kile. Gibson hakuweza kuyaamini macho yake, machozi ya
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
furaha yakaanza kumtoka, akaanza kumfuata Prisca pale kitandani na kisha kumkumbatia. Muda wote Prisca alikuwa akimshangaa Gibson, kwake alikuwa
akionekana kuwa kama mtu mpya.
“Umeamka. Umeamka hatimae” Gibson alimwambia Prisca ambaye bado alikuwa akimshangaa.
Kwa haraka sana Gibson akaichukua simu yake na kisha kuwapigia wazazi wake na kisha kuanza kuwaambia kuhusu muujiza ambao ulikuwa umetokea
hospitalini. Wazazi wa pande zote mbili wakafika mahali hapo. Mara Prisca alipowaona wazazi wake, tabasamu pana likatawala uso wake.
Huo ndio ulionekana kuwa muujiza mkubwa. Prisca hakuwa na nguvu za kuongea japokuwa alikuwa amefumbua macho. Baada ya mwezi mmoja kupita, Prisca
akaruhusiwa kurudi nyumbani huku kila kitu ambacho alikuwa akikiona kilionekana kuwa kipya machoni mwake.
“Nimewakumbuka sana. Mdogo wangu Dorice yupo wapi?” Prisca aliuliza huku akionekana kuwa mwenye furaha.
“Amekwenda chuoni” Mama yake, Bi Magreth alijibu.
“Mnanitania. Lini ameanza chuo? Si yupo kidato cha pili?” Prisca aliuliza swali ambalo lilimshangaza kila mtu.
“Unasemaje?”
“Toka lini mwanafunzi wa kidato cha pili akaanza chuo?” Prisca aliuliza.
Kila mmoja alionekana kushtuka, si wazazi tu ambao walionekana kushtuka bali hata Gibson mwenyewe alikuwa ameshtuka kupita kawaida. Hakujua ni kitu
gani ambacho kilikuwa kimetokea, kila wakati alikuwa akijiuliza kama tukio la kupoteza kumbukumbu lilianza kumfanya kuwa chizi au la.
“Prisca! Unamjua huyu?” Baba yake, mzee Steven alimuuliza huku akimnyooshea Gibson kidole.
“Hapana” Prisca alijibu.
“Haumjui?”
“Ndio. Ni mgeni amekuja leo au?” Prisca aliuliza swali ambalo lilionekana kumshtua kila mtu.
“Ila sisi unatujua?”
“Ndio. Ninyi ni wazazi wangu”
“Ila huyu haumjui?”
“Simjui kabisa. Sidhani kama nilikwishawahi kumuona mtu huyu. Mara ya kwanza kumuona ilikuwa pale hospitalini, nilishangaa kumuona akinikumbatia. Siku
nyingine alikuwa akiniletea zawadi pale hospitalini. Kitu cha ajabu, ninyi hamkuonekana kujali, yaani mimi kutembelewa na kuletewa zawadi na mtu
nisiyemfahamu mlikuwa mkiona kuwa ni jambo la kawaida sana na wakati nilikuwa nikifikiria sana” Prisca aliwaambia wazazi wake.
“Ok! Kuna mtu yeyote unamkumbuka?” Mzee Steven alimuuliza.
“Namkumbuka rafiki yangu, Pamela, Happy, Everlyn. Hivi Vonso amekwisharudi kutoka Uganda?” Prisca aliuliza maswali ambayo yaliendelea kumshangaza
kila mtu.
Hiyo ndio hali ambayo ilikuwa imemtokea Prisca. Mshipa wake wa kumbukumbu ulikuwa umeharibika sana, katika kipindi hicho alikuwa akiwakumbuka watu
ambao alikuwa akiishi nao katika kipindi ambacho alikuwa kidato cha tatu. Hakumkumbuka tena mume wake Gibson, kila alipokuwa akimwangalia, kwake
alionekana kuwa mtu mgeni.
Prisca hakukumbuka kitu chochote kile, alikuwa akiwakumbuka wazazi wake pamoja na marafiki zake kwa sababu tu alikuwa ameishi nao katika kipindi kirefu.
Hakukumbuka kama alikuwa ameolewa, hakukumbuka kama alikuwa amezaa mtoto ambaye alikuwa ameuawa zaidi ya kujishangaa kila alipokuwa akiyaminya
matiti yake na kuona yakitoa maziwa.
“Nini kimenitokea mama?” Prisca alimuuliza mama yake.
“Kuna nini?”
“Matiti yangu. Nashangaa yanatoa maziwa kama mwanamke aliyejifungua” Prisca alimwambia mama yake.
“Mmmh! Hebu kesho twende hospitalini, linaweza kuwa tatizo la kiafya” Mama yake alimjibu.
Hayo ndio maisha yake yalivyokuwa. Prisca huyu alikuwa tofauti na Prisca yule ambaye alikuwa akikumbuka kila kitu. Hapo ndipo ambapo Gibson alipoanza
kazi ya kuuteka moyo wa Prisca kwa mara nyingine tena. Mara kwa mara alikuwa akienda nyumbani kwao ambako huko alikuwa akikaa nae sana na kuongea
pamoja.
Kila walipokuwa wakiongea, Gibson alikuwa akijisikia uchungu moyoni, hakuamini kama mke wake alikuwa amemsahau. Kazi ya kuuteka moyo wa Prisca kwa
mara nyingine haikuwa rahisi ingawa alikuwa akijitahidi kadri ya uwezo wake. Mara kwa mara alikuwa akitoka nae na kuelekea ufukweni, katika mighahawa
mbalimbali ili mladi kumfanya Prisca kuangukia katika mapenzi yake kwa mara nyingine.
“Unaonekana kama unaniogopa Prisca” Gibson alimwambia Prisca.
“Hapana Gibson. Unajua nahitaji muda zaidi wa kukuzoea. Unaponiona hivi, usijali. Tutaendelea kuzoeana tu” Prisca alimwambia Gibson.
Gibson hakutaka kukata tamaa, kila siku alikuwa akiangaika kumfanya Prisca amzoee na hatimae atamke neno ‘Nakupenda’ mbele ya macho yake. Hali hiyo
iliendelea zaidi na zaidi, ukaribu wao ukaendelea kadri siku zilivyozidi kwenda mbele. Mwezi wa kwanza ukapita, mwezi wa pili ukaingia huku bado Gibson
akiendelea kumfanya Prisca kujisikia kuwa huru nae.
“Lini utamwambia kwamba unampenda?” Mzee Steven alimuuliza Gibson.
“Muda bado. Ukifika, nitamwambia. Akikubali, nitamuoa kwa mara ya pili tena na kuzaa nae mtoto mwingine” Gibson alimjibu mzee Steven
Hiyo ndio hali ilivyokuwa, kila siku Gibson alikuwa akijitahidi kumfanya Prisca amzoee zaidi na zaidi. Kwa sababu yeye ndiye alikuwa amesababisha hayo yote
basi hakuwa na budi kuangaika kumfanya Prisca ampende kwa mara ya pili hasa mara baada ya kupoteza kumbukumbu yake ya miaka saba iliyopita.
“Nitaendelea hivi hivi mpaka nitakapokuja kumuoa kwa mara nyingine tena” Gibson alikuwa akijisemea katika kipindi ambacho alikuwa akielekea Zanzibar
pamoja na Prisca kwa ajili ya kuangalia mambo mbalimbali yaliyoachwa na wakoloni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHO
0 comments:
Post a Comment