Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

MACHO YA BUNDI - 2

 





    Simulizi : Macho Ya Bundi

    Sehemu Ya Pili (2)



    “BASI tumpe nafasi Salome mwenye mume, unasemaje shemeji?” aliuliza Kalikalanje.

    “Unaniuliza miye kwani mimba nimetia mimi?” Nilimjibu huku nikimtupia jicho baya Pili nikiwa na hasira huku nikitamani kumrukia kwa kula vyangu.





    Shemeji yangu Kalikalanje alimuuliza mzee Chinchi kama anahusika na ujauzito wa binti huyo, mtoto wa rafiki wa mkewe.

    “Sina haja ya kukataa, ujauzito huu ni wangu,” alisema huku akifikicha macho kwa kitambaa.

    “Nini?” Niliuliza.

    “Shemeji Salome acha hasira.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unataka niache hasira nishangilie siyo.”

    “Siyo hivyo shemeji.”

    “Sasa nakusihi Mei. Kwa kuwa jambo hili ni la ghafla na bwana Chinchi hajapinga, amekubali kuwa anahusika na mzigo huu, nendeni nyumbani na sisi tubaki tukijadili, tuone nini cha kufanya.”

    “Tuondoke mjadili, mtajadili na nani kama siyo sisi? Mimi ndiye mzazi wa huyu binti ambaye kwanza amemkatisha masomo yake, pili anaweza kuwa ni mbakaji kwa sababu binti yangu ana miaka kumi na sita tu, nadhani mnajua sheria za siku hizi,” alisema Mei huku akiniangalia.

    Hakika dakika kadhaa tulikuwa tumeshakuwa maadui kati yangu na rafiki yangu Mei. Nilishangaa kabisa kuona amebadilika kana kwamba tulikuwa hatujuani.

    “Sawa, wewe ni mzazi wa Pili binti anayetajwa hapa kuwa amepewa mimba na mume wa rafiki yako Salome. Nakuomba chonde, nenda nyumbani nijadili na hawa wenyeji wako.”

    “Nakushangaa. Kwa nini sisi tusishirikishwe huo mjadala?” aliuliza Mei.

    “Utashirikishwa baada ya kujadiliana hawa wahusika wawili si unajua kuwa hawa ni wana ndoa?”

    “Unaona begi lile pale. Mimi Pili aliponiambia kuwa ana mimba ya bwana Chinchi nilikasirika sana na nikaamua akusanye nguo zake tuje huku kwake tena nilimpa taarifa hizi jana.”

    Baada ya Mei kusema hivyo nikakumbuka kuwa kumbe ndiyo maana jana Chinchi aliporudi kutoka huko alikokuwa amekwenda alishindwa kula chakula na kusingizia alikuwa anaumwa.

    Nakumbuka nilimgusa shavu lake na kuona likiwa baridi kuonyesha kuwa hakuwa na homa yoyote. Shaka ilinijaa.

    “Sasa Mei, wewe unasemaje? Maana nimekuomba sana muende kwenu kisha kesho nitakuita tujadili haya mwenzangu unaonekana hauko tayari, hutaki kabisa.”

    “Kweli sitaki mzungumze peke yenu, mimi na mwanangu ni lazima tuwepo.”

    “Lakini mimi nimekuambia kuwa tuwaache wana ndoa hawa wajadiliane kuhusu hili kwa sababu siyo kitu kidogo hiki,” shemeji yangu Kalikalanje alizidi kumuomba.

    “Najua sana kwamba hiki siyo kitu kidogo lakini napenda kukuhakikishia kwamba sisi pia tumeona kuwa hili ni jambo zito ndiyo maana tukaja hapa, tena na nguo zetu.”

    “Ni sawa, lakini kwa nini unaupuuza ushauri wangu? Tuambie tutazungumzaje bila wana ndoa kukaa na kukubaliana?”

    “Mhusika amekubali kuwa mimba hii ni yake, wajadili nini tena?”

    “Sawa amekubali kuwa hii mimba ni yake, je ungekuwa wewe ni Salome, usingependa kuafikiana na mumeo na kuona nini cha kufanya?”

    “Maswali yako ni mengi sana na unanihoji kana kwamba mimi ndiye mkosaji. Mimi sijakosea kumzaa mtoto wa kike. Alikuwa na tabia njema sana najua mia kwa mia kuwa mwenye makosa ni huyu bwana.”

    “Kwa nini unasema hivyo?”

    “Nasema hivyo kwa sababu nina uhakika kuwa alitumia uwezo wake wa kifedha kumshawishi mwanangu kufanyanaye mapenzi.”

    Mei alitulia kidogo akameza mate kisha akaendelea.

    “Ushahidi wote mimi ninao na kuna hata baadhi ya akina mama majirani wa huyu mzee walikuja nyumbani kwangu juzi kuniambia, wakati najiandaa nimuulize binti akanifahamisha kuwa yeye ni mjamzito.”

    USITAKE kunitibua, Salome ni rafiki yangu, ina maana mtoto wako akipewa mimba siyo tatizo isipokuwa tatizo mume wa mtu akimpa mimba mtu mwingine? Acha wendawazimu, umetumwa eh?”

    Mei alikuwa akiyasema hayo huku akiwa amesimama na mikono yake ilikuwa kiunoni.

    Nilimuangalia Mei kwa jicho la chuki. Ni kutokana na madai yake kuwa kupewa mimba mtoto inauma zaidi kuliko mume wangu kumpa mimba mwanaye.

    Sikutaka kujibu lolote hapo kwa kuwa nilijua kuwa nikisema chochote zogo litazuka.

    Nilimtupia jicho mume wangu Chinchi na macho yetu yalipokutana akakwepesha na kumuangalia Mei aliyekuwa bado amesimama na mikono yake ikiwa kiunoni.

    Kwa mara ya kwanza Chinchi akapanua mdomo.

    “Shemeji Mei…”

    “Shemeji yako nani? Mwanaume mbaya wewe? Huna haya hata kidogo, huyu si ni kama mtoto wako tu!”

    “Sawa. Nisikilize basi shemeji. Mimi nakuomba urudi kwako na nitabaki hapa na mke wangu kisha tutajua nini cha kufanya kuhusu huyo binti yako.”

    “Labda nikuambie kwa herufu moja moja kwamba si-to-ki- ha-pa ng’o.”

    “Hutoki hapa una maana gani?”

    “Huelewi, kwani nimezungumza Kifaransa? Maana yake tuonyeshe chumba chetu, suala la kutoka hapa halipo na msahau.”

    Maneno hayo yalitufanya sisi watatu, yaani mume wangu Chinchi na shemeji Kalikalanje tuangaliane.

    “Hakuna haja ya kutupiana macho, semeni sasa sisi tutakuwa tunalala chumba gani?” alisisitiza Mei huku akiketi kwenye kiti chake.

    Mume wangu alisimama akanishika mkono na akampa ishara shemeji Kalikalanje kuwa atufuate.

    Tulitoka nje na kwenda kuketi kwenye viti vilivyokuwa kwenye kivaranda na kuanza kujadiliana kuhusu tatizo lililokuwa mbele yetu.

    “Sasa bwana Chinchi, umelikoroga, unafanya maamuzi gani?” alihoji Kalikalanje.

    “Nimechanganyikiwa, sijui cha kufanya, naomba sana ndugu yangu nipe ushauri!”

    “Lazima ujue na utoe maamuzi, shemeji Salome siwezi kumuuliza swali kama hilo, wewe ndiye mtoa maamuzi.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitaamua nini?”

    “Sasa bwana Chinchi badala ya mimi kukuuliza wewe, unageuka na kuniuliza mimi, tutakusaidiaje?”

    “Mke wangu kwanza naomba sana unisamehe. Nimekosa sana na nimekukosea.”

    Baada ya kusema hayo huruma ilinijia, nikataka kuwaambia kwamba nimemsamehe lakini nikaona ni vyema nikamchemshe kidogo kutokana na upumbavu alionifanyia.

    “Sikiliza shemeji yangu Salome. Mumeo amekuomba msamaha ni kweli kabisa kuwa amefanya kosa kubwa, ambalo hakika anajuta sasa kwa kuwa, kwanza aliyempa mimba ni mtoto wa rafiki yako tena basi ni sawa na mtoto wake. Pili ameletewa huyo mtoto hapa nyumbani. Ni vyema sasa wewe ukatoa tamko la ama umpokee yule mtoto mwenye mimba au umruhusu ampangie nyumba. Huo ni ushauri wangu.”

    Nilifikiri kwa sekunde kama kumi hivi maneno ambayo aliyasema shemeji yangu. Nilijikuta nikitokwa na machozi. Nilichukua upande wa kitenge changu na kuyafuta machozi yaliyokuwa yakinitiririka.

    Nilimuangalia mume wangu ambaye alionyesha wazi kunyong’onyea. Naye alikuwa na kitambaa na alikuwa mara kwa mara akifuta uso wake. Siyo kwamba alikuwa akifuta machozi, hapana alikuwa akifuta jasho. Hakukuwa na baridi lakini naamini kuwa lile tukio lilikuwa limemtia presha sana katika mwili wake.

    Nikajikuta nikiongea.

    “Sikiliza shemeji, ndugu yako Chinchi ni kama mwiba umemkwama kooni. Mimi nasema tuwaache tu hapa nyumbani. Mei ni rafiki yangu. Tuache wakae tuone mwisho wake utakuwa nini.”





    “Sijaelewa shemeji Salome, wakaekaeje? Au mpaka ajifungue?”

    “Ndiyo maana yake na nadhani ni moja ya sababu iliyomfanya rafiki yangu Mei kuja na mwanaye, sasa sijui watakaa wote au abaki Pili tu?”

    “Hayo nadhani wataamua wenyewe, shemeji utawauliza wewe.”

    “Sijui bwana Chinchi una la kuongeza au kupunguza?”

    “Sina. Kama mke wangu ameona hivyo nami naungana naye na sina la kufanya, nakubaliana naye.”

    Kikao hicho tulikivunja na kurejea ndani ambako Mei na mwanaye Pili walikuwa wameketi kusubiri uamuzi wetu.

    Wakati wote wakiwa peke yao, hakuna aliyekuwa akizungumza isipokuwa Pili alikuwa ameshika mikono yake na akawa anavunja vidole vyake kwa kuvivutavuta.

    Shemeji Kalikalanje aliwatazama wageni hao na akawaambia:

    “Tumekubaliana kwamba Pili akae hapa hadi atakapojifungua.”

    Jibu hilo lilimfanya Mei asonye na kutuangalia kuanzia miguuni hadi kichwani.

    “Msitufanye wajinga. Akae hadi ajifungue baada ya hapo mumbwage siyo?”

    “Hapana shemeji, akishajifungua tutaona tufanye nini.”

    “Hakuna cha kusubiri, uamuzi utoke leoleo.”

    “Shemeji Mei wewe unataka tutoe uamuzi gani?” alihoji Chinchi.

    “Wewe nyamaza. Utaniudhi, haya mambo tunakurekebishia wewe. Umempa mimba mtoto wangu ambaye ana miaka 16. Unajua unaingia katika kundi la wabakaji?”

    “Shemeji tusifike huko…”

    “Tusifike huko wewe unataka tufike wapi? Huko kwa kumtelekeza mwanangu? Acha hizo, naweza kuamua vinginevyo ukataabika na dunia hii.”

    “Tuliza hasira shemeji, hakuna kitakachoharibika.”

    “Haya semeni mnataka tufanye nini?”

    Kilipita kimya cha kama dakika mbili hivi kisha Chinchi akafuta jasho usoni na kusema;

    “Ushauri wangu,tupumzishe akili, acha wageni walale hapa na kesho tukiwa na mawazo mapya tutaona nini cha kufanya.”

    “Uamuzi huo ni sahihi, shemeji yangu Salome sidhani kama ana pingamizi, au unalo la kuongeza?”

    “Sina. Ngoja nikawaonyeshe chumba chao waweke mizigo yao na kupumzika kama watataka kufanya hivyo.”

    Nilipanda nao ghorofani na kuwaonyesha chumba ambacho watakuwa wanalala.

    “Usishangae shoga, ukisikia ukware ndiyo huu, umeonaee!”

    “Nimeona. Sasa wekeni masanduku yenu kisha tushuke chini maana naamini hamjala chochote maana mmeamkia hapa kwangu.”

    “Sawa. Twende tushuke.”



    ***

    Asubuhi na mapema Chinchi aliamshwa na mlinzi wao ambaye alimwambia kuwa kuna wageni wamekuja na wapo getini.

    “Wageni gani asubuhi yote hii na wametoka wapi?”

    “Mimi siwajui mzee, wanataka kukuona.”

    “Wako wangapi?”

    “Wako wanne na wote ni wazee, nadhani wana matatizo maana wote hawaoneshi sura za furaha.”

    “Hawakukudokeza kuwa wanataka nini asubuhi yote hii?”

    “Sijawauliza.”

    “Hebu wapeleleze kisha nijulishe,” Chinchi alisema huku akiniangalia.

    “Hao wageni ulikuwa na ahadi nao?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Salome umesikia nilipokuwa nazungumza na mlinzi nami nashangaa kupata ugeni asubuhi hii.”



    Baada ya dakika tano simu ililia kutoka getini, haraka sana Chinchi akainyakua.

    "Niambie, ni akina nani?"

    "Wanasema ni wakwe zako."

    "Umesema wako wangapi vile?"

    "Wanne."

    "Hawakusema kama kuna tatizo huko nyumbani wanakotoka."

    "Sikuwauliza maswali hasa baada ya kuniambia kuwa ni wakwe zako, niliona itakuwa ni ukosefu wa adabu."

    "Umefanya vizuri."

    "Niwaambiaje?"

    "Tunakuja kuwapokea, wafungulie geti."

    Chinchi alinigeukia na kuniuliza kama nimewaambia wazazi wangu habari ya jana kuhusu Mei na mwanaye Pili.

    "Aka, sijawaambia chochote, nitawaambiaje wakati hatujajadili la maana, nashangaa kusikia kuwa wamekuja hapa."

    "Sasa nini kimewaleta hapa asubuhi yote hii? Watanichanganya sana kama wamekuja kwa ajili ya hili. Au kuna tatizo kijijini? Lakini kwa nini wasituambie kabla hawajaja?"

    "Maswali yako ni mengi na hayana majibu. Ngoja nikawalaki, labda wana jambo, ni kweli siyo kawaida yao kuja asubuhi hivi tena basi wanne."

    Nilishuka ngazi kwa kuwa vyumba vyetu vya kulala vilikuwa ghorofa ya kwanza. Havikuwa mbali na chumba ambacho nimewapa kulala Mei na mwanaye Pili.

    Niliteremka ngazi taratibu huku nikiwaza kwamba inawezekana wambeya wamepeleka habari nyumbani na wazee wakaona waje wasawazishe mambo.

    Nilipofika mlango mkubwa nilisikia ukigongwa. Nikajua kuwa yule mlinzi amewafungulia geti na kuwaleta pale mlangoni.

    Haraka sana nikafungua mlango. Niliokutananao mlangoni ni watu wanne, wote wanaume na wala siyo wazazi wangu! Nilikuwa siwafahamu.

    Moyo ulipiga paa, hata kuwaamkia nilishindwa mpaka baada ya sekunde kama kumi hivi ndipo mmoja wa wazee wale akafunua kinywa chake na kusema:

    "Hujambo binti yetu?"

    "Sijambo, shikamooni,"

    "Mbona umeshangaa," alisema mmoja wa wazee hao.

    "Nimeshangaa kwa kuwa niliambiwa kuwa wazazi wangu wamekuja."

    "Nani aliyesema hivyo?"

    "Mlinzi aliyewafungulia geti."

    "Hapana, sisi tulimuambia kuwa sisi ni wakwe wa Bwana Chinchi na wala hatukusema ni wazazi wako wewe. Alikosea kusema."

    "Sasa kama ni wakwe wa mume wangu si ni moja kwa moja kwamba ni wazazi wangu?"

    "Hapana mama, kwani jana hamkupata ugeni hapa nyumbani?"

    "Tumepata."

    "Basi sisi ni wazazi wa hao waliokuja jana."

    Nilinyong'onyea baada ya kupata jibu hilo. Nilitamani nisiwakaribishe sebuleni.

    Lakini wakati natafakari, mzee mmoja akawa tayari ameingia ndani na kuketi kwenye kochi.

    Ilibidi niwaache waingie wenyewe sebuleni bila kuwakaribisha nami kwenda moja kwa moja kwa mume wangu juu ghorofani.

    "Vipi, wanasemaje?"

    Aliniuliza mume wangu lakini sikumjibu. Kichwa kilianza kuniuma na mawazo yakaja kwamba wale wageni ni watu wa shari.

    "Mke wangu nimekuuliza hao wazee wako wanasemaje? Ili nitakapokwenda kuwaona nijue nini cha kufanya hata kabla ya wao kunieleza tatizo."

    "Wala siyo wazazi wangu."

    "Ina maana mlinzi katuongopea? Ameanza lini kutudanganya kijana huyu?"

    Nilimsimulia mume wangu kilichotokea naye akawa anatafakari cha kufanya.



    Mume wangu aliamua kutoka kwenda kwa wageni baada ya mdogo wake, Kalikalanje kufika nami nilimfuata. Mei, Pili na wale wazee wakawa wanatuangalia.



    Mume wangu ni kama alipigwa na butwaa maana baada ya kufika pale walipoketi wale wazee wala hakukumbuka kuwasalimia na badala yake alijibwaga kwenye kiti na kuwakodolea macho.

    Mdogo wake, bwana Kalikalanje ndiye aliyeanza kuzungumza.

    "Kaka hili jambo naona limekuchanganya maana hujanisalimia na hata wageni hujawataka hali."

    Mume wangu aligutuka na kuwasalimia wageni.

    "Shemeji Salome mbona na wewe huwasalimii?"

    "Mimi ndiye niliyewafungulia mlango."

    Wageni wale walisema kwa nyakati tofauti kwamba hawakuja kwa shari katika nyumba yetu na wamepata habari kwamba mtoto wao amepewa mimba na mzee wa nyumba yetu.

    "Ni kweli kwamba binti yetu amekatisha masomo na hilo limetuuma sana lakini tumekuja kukuarifu bwana kwamba busara nyingi imetumika kutatua hili."

    Alinyamaza kidogo na kumeza mate kisha akaendelea.

    "Mjadala wa jana baada ya kupata taarifa hii ya mimba ilikuwa tukushitaki mahakamani kwa kumbaka binti yetu kwa kuwa ana miaka 15 lakini Mei ambaye ni rafiki wa mkeo akasema mmekubaliana kuwa utamuoa, je ni kweli?"CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mume wangu alipata kigugumizi kidogo kujibu swali hilo, bila shaka alitegemea mdogo wake, Kalikalanje angemjibia.

    Lakini alipoona mdogo wake naye ;amemezea' kutoa jibu mume wangu akasema ni kweli aliyoyasema akatakiwa kwenda kijijini.

    "Je, nije na mahari kabisa?"

    "Ingefaa maana haya mambo yamalizwe kabisa kusiwe na longolongo."

    Hawakuchukua muda wakaaga bila hata kunywa chai.



    ***

    Bwana Chinchi, Kinjeketile na wazee wengine wawili waliondoka kwenda kijijini kupeleka posa.

    Walikaribishwa na mzee wa Kijiji cha Nanyindwa anaitwa Atu Woopiha, ni mzee anayeaminika kwa kuwa na busara kijijini pale na ni mkuu wa familia.

    Baada ya majadiliano mume wangu alitoa barua ya posa kisha wale wazee wakakaa kikao.

    Mume wangu aliambiwa mahari na akapigwa faini kwa kumharibu' mtoto. Alilipa zote na baada ya kulipa alipangiwa siku ya kwenda tena akiwa na Pili ili wafungishwe ndoa ya kimila.

    Mume wangu aliporudi mjini alituita wote yaani mimi mkewe, Mei na Pili akatuambia kuwa mahari amelipa na Jumamosi ijayo wote tutakwenda kwenye ndoa ya kimila.

    "Mzee Woopiha na wenzake nimewaachia fedha kwa ajili ya kufanya maandalizi ya harusi."

    Taarifa hiyo niliona wazi kabisa kuwa ilimfurahisha sana rafiki yangu Mei kwani aliinuka na kwenda kumkumbatia mume wangu.

    "Sasa umekuwa mkwe wangu rasmi. Ni marufuku kuanzia sasa kuniita shemeji."

    Baada ya mazungumzo hayo Mei aliniomba ruhusa ili siku hiyo aandae yeye chakula.

    Nilimpa mchele na mazagazaga ya pilau, akawa jikoni akiandaa chakula.

    Jioni aliandaa meza kwa ajili ya chakula. Ilikuwa ni mara ya kwanza sisi sote kula pamoja.

    Wakati anandaa meza mimi nilikuwa juu kwenye mlango wa kuingilia chumbani kwetu. Ukiwa kule unaona pale penye meza ya chakula.

    Nilishangaa kumuona Mei akipaka kitu kama unga mweusi kwenye kiti ambacho hupendelea kukaa mume wangu.

    Unga huo alikuwa ameufunga kwenye kona ya kanga yake aliyoivaa. Alikuwa akiangalia huku na huko kwa wasiwasi na alisahahu kuangalia juu nilipokuwa nimesimama.

    ;Huyu ni mchawi?" nilijiuliza bila kupata jibu.



    Baadaye aliniita kwa sauti kwamba chakula tayari. Nilishuka ghorofani na mume wangu na kwenda moja kwa moja kwenye meza ya chakula.

    "Kaa hapo," alinielekeza.

    Nilijifanya nimejikwaa na juisi iliyokuwa imo kwenye glasi ilimwagikia kwenye kiti ambacho ilikuwa akalie mume wangu.

    Nilikiinua na kukitoa pale na mume wangu akakalia kiti ambacho nilitaka kukikalia mimi.

    Mei nilimuona akikunja uso japokuwa sikuwa namuangalia moja kwa moja au uso kwa uso. Ni wazi kwamba hakuwa amefurahishwa na aliamini kuwa juisi ilimwagika kwa bahati mbaya.

    Asubuhi tulikuwa kwenye gari tukisafiri kuelekea Kijiji cha Nanyindwa.

    Mimi nilikuwa nimeketi kiti cha mbele, nyuma aliketi Pili na mama yake na mzee mmoja ambaye ni ndugu na mume wangu.

    Nyuma ya gari letu lilikuwepo gari ambalo alikuwa akiliendesha shemeji Kinjeketile na ndani yake kulikuwa na abiria wengine watano.

    Hatukupenda kualika watu wengi kwa kuwa tukio lenyewe lilikuwa ni la aibu kwani mume wangu ni mtu mzima na kumtia mimba mtoto mdogo kama yule lilikuwa ni jambo la kusikitisha.

    Ndani ya gari letu kulitawala ukimya kila mtu akifikiria lake kichwani. Mume wangu alivunja ukimya.

    "Hatutachukua muda mrefu kwenye sherehe hii," alisema huku akiniangalia.

    "Kwa nini unatabiri hayo?"

    "Siyo kwamba natabiri, sitapenda tukae sana,sina furaha kabisa."

    Tulifika kijijini na kupokelewa na mzee Atu Woopiha, mzee Mpupua na wazee wengine kama vile Noel Sinyaapi na mabibi kadhaa wakiongozwa na Mama Mponda.

    Kwanza kabisa mume wangu alikalishwa kwenye kigoda na akapakwa unga kisha ikachukuliwa pombe isiyokomaa Nrushu' ambayo ilikuwa ndani ya chombo maalum wanayoiita ichinumba na akaambiwa akamnyweshe Pili.

    Pili naye akamfanyia hivyo hivyo mume wangu. Baada ya hapo ilichukuliwa mikia miwili ya nyumbu, mmoja alishika mzee Atu Wopiha na mwingine mama Mponda kisha wote wawili wakaambiwa wainame, migongo yao ikafagiliwa kwa kutumia mikia hiyo.

    Baadaye ikatangazwa kwamba tayari ndoa ya kimila imepita. Vigelegele vilipigwa na ikatangazwa kwamba wanandoa waingie katika chumba maalum.

    Waliingia humo lakini mimi pia nilikaribishwa. Wenyeji walisema katika chumba hicho kutakuwa na kitu walichokiita ;chitaamo'.

    Chitaamo ni kikao maalum cha wazee kwa ajili ya kuwafunda wanandoa huko waendako kuanzisha maisha mapya.

    Mume akaambiwa asiache kumtunza mkewe na mke naye akaambiwa asiache kumtunza mumewe na kumheshimu mke mkubwa, yaani mimi.

    Baada ya maelezo hayo karamu iliandaliwa ambapo sisi wageni tulitengewa chakula chetu tukala. Hakika watu wa Nanyindwa walikuwa wakarimu sana.

    Nje ya nyumba ya sherehe kulikuwa na ngoma maalum inayoitwa Beni, ilikuwa tofauti na ngoma tunazozijua zinazochezwa na vijana, hiyo asilimia kubwa ilichezwa na wazee.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog