Simulizi : Ahadi Ya Ndotoni
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya mwezi mmoja, siku moja akiwa anatoka kuswali swala ya alasiri, alipigiwa simu kutoka kwa baba zake wadogo.
“Haloo ba’ mdogo.”
“Haloo mama.”
“Shikamoo.”
“Marahaba.”
“Ndiyo baba.”
“Tunashukuru sana mama.”
“Kwa kipi?”
“Kweli wewe ni kiumbe cha ajabu.”
“Kivipi?”
“Pamoja na kukufanyia mambo mabaya bado umeonesha moyo wa kibinadamu, mumeo ametusamehe na wewe kutuwezesha tuishi maisha ya raha.”
Lakashina alishtuka na kutulia kwa muda kujiuliza amewezaje kuwawezesha kuishi maisha ya raha, lakini alikumbuka kauli ya mumewe kwenye njozi kuwa ataisaidia familia yake.
“Ndiyo hivyo baba, siku zote ubaya ukilipwa wema, hukosa nafasi.”
“Ni kweli mwanangu, kwa ulichotutendea tumejifunza kuwa ubaya haufai.”
“Ni kweli wazazi wangu, mimi niliwasamehe japo niliapa sitawasamehe.”
“Asante mama, sasa tumekaa kikao cha familia zote tumepanga kuja kukutembelea tujue unapoishi na kuja kukushukuru kwa kuyanyanyua tena maisha yetu.”
Lakashina kabla ya kuzungumza alihisi simu ya moto iliyomuunguza sikioni, kitu kilichomfanya aitoe haraka. Alipoiangalia alikuta imezima, alishtuka na kujiuliza kuna kitu gani kilichofanya simu iwe ya moto kiasi kile. Alipotaka kuiwasha iligoma kuwaka, alizidi kushangaa. Kama kuichaji muda si mrefu alikuwa ameitoa kwenye chaji na ilionesha imejaa.
Haikuwahi kutokea hata siku moja simu izimike muda mfupi toka alipoitoa kwenye chaji. Wakati akijaribu kuiwasha ilimuunguza tena mikononi kitu kilichofanya aitupe chini. Ilipogusa chini ilijiwasha yenyewe na kuanza kutoa mlio wa simu kuingia.
Aliitazama kwa muda akiiogopa kuipokea, mlio uliongezeka kila dakika na mwisho wake kuwa kero, aliinama aichukue.
Kwa kuhofia kuungua aliigusa kwa mbali ili kuona kama moto wake unashikika, lakini ajabu simu ilikuwa ya kawaida haikuwa na moto wowote.
Aliiokota na kushangaa kutoonekana namba ya mpigaji. Simu iliita ikiwa kama imezimika, akaipeleka sikioni na kuzungumza.
“Ha..a..loo.”
“Haloo,” sauti ya upande wa pili iliitika, ilikuwa nzito kama ya awali iliyokuwa ikimtisha, mapigo ya moyo yalimwenda kwa kasi lakini iliyadhibiti.
“Ndiyo unasemaje?”
“Nakuomba usiwaruhusu ndugu zako wakusogelee, ulichowafanyia kinatosha.”
“Kwa nini wasinisogelee?”
“Ni viumbe wabaya.”
”Lakini wameshagundua kosa lao, hivyo wanakuja kunishukuru pia kurudisha uhusiano uliopotea.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Lakashina nisikilize mimi tusibishane,” sauti ya upande wa pili iliongeza ukali.
“Sibishani na wewe, siku zote kiumbe anayegundua makosa yake na kuyakubali kisha kuomba msamaha anatakiwa kusamehewa.”
“Nakuomba uniamini nikwambiayo, familia yako ni viumbe wabaya kuliko kifo, nakuomba achana nao kabisa.
Ni kweli kwa sasa hawana nia mbaya, lakini nakuhakikishia maisha unayoishi wakiyaona, lazima watabadilika na kupanga mipango ya kukudhuru.”
“Wee umejuaje?”
“Sitaki malumbano, wee wakaribishe litakalotokea utalimaliza mwenyewe. Wewe si mwepesi wa kujiua sasa hivi kifo kitakukimbia ili ufaidi jeuri ya kiburi chako.”
“Sasa niwajibu nini?”
“Wajibu kwamba haupo nchini.”
“Nikikutana nao je?”
“Hautakutana nao milele.”
“Sawa nimekuelewa.”
“Umenifurahisha Lakashina, unaonekana muelewa.”
Baada ya kusema vile, sauti ile iliendelea kushukuru kwa kusema maneno ya kujirudia:
Asante Lakashina...Asante Lakashina sauti ile ikizidi kufifia na kutoweka kabisa.
Baada ya sauti ile kutoweka, Lakashina alibakia akiwaza juu ya ujumbe ule na tabia za baba zake wadogo.
Aliamini kabisa kama baba zake kweli watayaona maisha anayoishi ni mazuri kiasi kile, lazima roho zitawauma na kuanzisha mpango mwingine wa kumuangamiza ili wazipate zile mali.
Alijiuliza hali ile inatokana na nini? Na kwa nini sauti zile kuna moja ilitaka atiwe adabu na nyingine ilikataa. Alikumbuka dua aliyofundishwa na ustaadh mmoja aliyekuwa akimfundisha mafunzo ya dini ya Kiislamu ya kufukuza vitu vibaya.
Aliisoma komoyomoyo huku mbavu zikimbana, alipoimaliza ile dua viungo vya mwili aliviona vinafanya kazi. Lakini hali ya hewa bado ilikuwa nzito na harufu mbaya iliendelea kutawala chumba kizima. Alipapasa mkono kuitafuta swichi ya taa. Alipoipata aliwasha, baada ya taa kuwaka alishangaa kujikuta yupo kitandani mwake na ndani ya chumba kulikuwa kama siku zote.
Kingine hali ya hewa ilikuwa ya kawaida ya harufu nzuri ya manukato, wala hakukuwa na sauti tena za watu kubishana. Aliketi kitandani jasho likimvuja na kifua kikiwa kizito, alikohoa mfululizo mpaka machozi yakamtoka.
Alijiuliza mbona chumbani kuna hali ya kawaida lakini kifua chake bado kizito? Kilichotokea ilikuwa ni ndoto au nini? Alinyanyuka kwenda kutawadha kwa vile alfajiri ilikuwa inaingia. Alikwenda kuswali, alipomaliza kuswali hakunyanyuka haraka kwenye msala wake. Aliyafikiria yaliyomtokea muda mfupi kabla ya kuamka yalikuwa na maana gani.
Alinyayuka na kwenda kulala kutokana na kusumbuliwa na kifua, akiwa amejilaza kitandani simu yake iliita. Aliipokea na kuanza kuzungumza.
“Haloo.”
“Lakashina kwa nini umepinga amri yangu?” Sauti nzito ya upande wa pili iliuliza, kwa vile alikuwa ameizoea hakushtuka.
“Ndiyo maana unataka kuniua?” Aliiuliza ile sauti ambayo hakujua ni ya nani.
“Hujanijibu kwa nini unapinga amri yangu?”
“Nipinge! Wewe nani?”
“Siyo lazima kunijua.”
“Kama hutaki nikujue basi achana na mimi.”
“Mbona unaonekana una kiburi?”
“Kiburi gani, jitokeze ili nijue nazungumza na nani na unieleze kwa nini unanikataza.”
“Lakashina kumbuka hukuwa mtu mbele ya watu, leo unajisahau?”
“Sijajisahau, kosa langu nini?”
“Sasa kwa nini unapinga kila ninachokueleza, umevunja amri kwa kuwaleta wazazi wako, bado hukuona kuwa hiyo imetosha, umeamua kukaa na adui ndani.”
“Adui?”
“Eeh, adui.”
“Adui nani?”
“Kwani unakaa na nani?”
“Na wafanyakazi wangu wawili na mdogo wangu.”
“Basi huyo mdogo wako ndiye atakayekumaliza.”
“Mbona sikuelewi, animalize vipi mtoto mdogo?”
“Lakashina unasahau matatizo haraka sana lakini utanitafuta na hautanipata.”
“Lakini wewe ni nani?”
“Kama hutaki kunisikiliza kwa lile la ukweli hata ukinijua haitasaidia kitu.”
“Basi kama hutaki nikujue, niache na maisha yangu.”
“Eeh, leo unasema hivyo wakati ulikuwa ukitembea barabarani ukizungumza peke yako?”
“Hata nikizungumza, wewe inakuhusu nini?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Asante mama yangu, yameishia hapa ila utanitafuta na hautaniona kamwe.”
“Nikutafute vipi mtu sikujui?”
Baada ya mabishano yale simu ilikata. Ilikuwa ni jambo la kushangaza kwa Lakashina, hasira alizokuwa nazo zilisababisha kifua chake kujaa. Zilipopoa maumivu yote kifuani yalipotea na sauti yake ilirudi katika hali ya kawaida.
Alishangaa kujiona hajambo kabisa, kila dakika matukio yalizidi kumchanganya, alijikuta akitamani mumewe Lakashi awepo ili amsaidie matukio yale ya kutisha ambayo aliamini yeye ndiye mhusika mkuu. Akiwa katika mawazo mazito ya kumuwaza mumewe, usingizi ulimpitia na kuota yupo na mumewe kitandani.
“Vipi mke wangu mbona unalia?” Lakashi alimuuliza mkewe aliyekuwa akitokwa na machozi baada ya kumuona mumewe.
“Hali hii mpaka lini?”
“Kwani tatizo nini?”
“Kwa nini niishi maisha ya mashaka?”
“Mashaka unayataka wewe mke wangu.”
“Kivipi?”
“Umesahau ulipotoka na upo wapi na kwa nini umetoka huko.”
“Lakini mume wangu kosa langu nini, kuna kosa kuwasamehe ndugu zangu?”
“Hakuna kosa lakini kumbuka umeshaumwa na nyoka, kwa nini huogopi unapoguswa na nyasi?”
“Mume wangu kama wewe umeweza kuwasamehe na kukubali kuyabadili maisha yao kuna ubaya gani wa kuwa karibu nao?”
“Unayakumbuka maswali ya baba zako wadogo?”
“Ndiyo.”
“Kwa nini ulikasirika?”
“Maswali yao yalikuwa hayana msingi.”
“Sasa mpaka iwe vipi ndiyo ujue kuwa hao siyo watu wema?”
“Mmh!” Lakashina alikosa jibu na kuguna tu.
“Sikiliza mpenzi, mimi kukuonya nimeona mbali sana.”
“Ina maana wewe ndiye unayenipigia simu?”
“Lakashina siku zote nakufundisha kitu kimoja, unapoonywa usitake kuangalia nani anakuonya la muhimu kumuelewa.”
“Sasa kama ni wewe mbona unakuja kwa lugha ya kunitisha?”
“Lakashina mimi si unaniona, kwa nini nije kwa sauti?”
“Sasa yule ni nani?”
“Kwani kipi amekueleza kibaya?”
“Hakuna, ila hunitisha sana.”
“Nakuomba umsikilize, ni mwema kwako acha kumjibu maneno ya kiburi.”
“Sawa nimekuelewa mume wangu.”
“Niambie tatizo nini?”
“Nataka niwe na wewe siku zote.”
“Hata mimi najua jinsi gani ninavyotaka kuwa na wewe karibu, vumilia muda bado.”
“Muda bado mpaka lini?”
“Sijajua, nimekueleza nasafiri.”
“Mbona upo?”
“Lakashina mke wangu, nipo nawe ndotoni lakini si kimwili. Nilikueleza nitakuwa nawe muda wote wa majonzi yako.”
“Kumbuka nateseka, nahitaji kuwa karibu yako muda wote, Lakashina nakupenda mume wangu.”
“Hata mimi nakupenda ndiyo maana kila kukicha nayaimarisha maisha yako.”
“Ni kweli mume wangu, kwa hilo nashukuru.”
“Basi nakuomba umsikilize rafiki yangu.”
“Mume wangu siwezi kupanda farasi wawili.”
“Una maana gani?”
“Ulinieleza nikusikilize wewe tu.”
“Ni kweli lakini kwenye matatizo hata kama sipo msikilize, ni mtu mwema sana kwako.”
“Sawa lakini naomba niwe na mdogo wangu.”
“Kwani yeye alikueleza nini?”
“Eti ni mtu mbaya.”
“Yaweza kuwa kweli.”
“Kwa hiyo nimrudishe?”
“Ikiwezekana.”
“Kwa hili mume wangu sikubaliani nalo, toka amekuwa hapa furaha yangu imeongezeka mara dufu.”
“Mmh! Haya.”
“Umekasirika?”
“Ili iweje.”
“Kwa hiyo umenikubalia?”
“Nimekukubalia.”
“Asante mume wangu,” Lakashina alimkumbatia mume wake kwa furaha, alishtuka usingizini na kujikuta ameukumbatia mto. Lakini chumba chote kilikuwa na manukato ya mumewe Lakashina.
****
Tokea siku ile Lakashina aliamini kuipata haki yake lazima afanye kiburi, kwa kauli ya mumewe japo ilikuwa na mashaka, hakuwa tayari kuitii amri ya sauti ya kiumbe asichokijua na kusimamia uamuzi wake ambao aliuona kila siku upo sawa japo ni mwanamke.
Shughuli zake nazo zilikwenda kama alivyopanga na mapato kila kukicha yaliongezeka. Ilifika hatua hata muda wa kuswali akawa anakosa zaidi ya kushughulika na biashara zake na aliporudi nyumbani alikuwa amechoka sana. Ndotoni alijiwa na mumewe aliyemkumbusha kuswali lakini alipuuza na kuendelea na kazi zake ambazo kila muda ziliongezeka na kupanuka.
Akiwa katika kazi zake, alikutana na watu wengi akiwemo kijana mmoja ambaye alionesha ushirikiano mkubwa kiasi cha kumteka akili. Lakashina akiwa chumbani kwake kitandani alijikuta akimjaza akilini kijana yule ambaye alionesha ni mstaarabu sana.
Alikumbuka siku moja katika kazi zake Lakashina aliposahau mkoba wake uliokuwa na pesa nyingi lakini kijana yule alimpelekea tofauti na vijana wengine ambao walikuwa wanamuibia hata pesa kidogo. Pia swali la kijana yule liliupasua moyo wake na kumuweka kwenye wakati mgumu pale alipomuuliza:
“Lakashina umeolewa?”
“Mbona umeniuliza hivyo?”
“Katika maisha yangu sikuwahi kuwaza kumuona mwanamke kama wewe.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Lakashina una kila sifa za mwanamke mwenye kuifahamu thamani yake.”
“Kivipi?”
“Kwanza muumba kakujalia umbile na sura, pili kakujalia heshima busara na ustaarabu pia huruma na mwisho pamoja na utajiri wako bado huridhiki.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni hayo tu,” Lakashina alimwambia kijana yule kwa sauti ya chini huku akiwa ameangalia chini kwa aibu.
“Ni mengi sana ambayo kama mbingu ingekuwa karatasi na bahari ni wino vingejaa na wino kukauka lakini sifa zako zisingeisha.”
“Unanipamba tu Sadat.”
“Ni kweli, huwezi kujiona bila kuonwa.”
“Kama ndiyo hivyo nashukuru.”
“Basi nijibu, umeolewa?”
“Nitakupa jibu tukionana, naomba uniache kwa leo.”
Lakashina alirudisha mawazo yake na kutabasamu huku akijiuliza ampe Sadat jibu gani ili asimuudhi moyoni mwake.
Akiwa kwenye mawazo mazito juu ya uamuzi wake mzito wa kutoa jibu kwa Sadat, simu yake iliita. Aliichukua simu na kuipokea.
“Haloo.”
“Haloo.” Sauti nzito ya upande wa pili ilipokea.
“Unasemaje?” aliuliza kwa hasira.
“Lakashina nakupa onyo la mwisho.”
“Kuhusu nini?”
“Kwa yote niliyokueleza na hili unalowaza.”
“Nawaza nini?”
“Unalijua lakini ukifanya unachowaza tusilaumiane.”
“Nimeishakueleza maisha yangu hayakutegemei wewe ila Mungu.”
“Hicho ndicho kitakachokuponza.”
“Nimekueleza usinitishe na sitakuogopa.”
“Narudia tena japo masikio yako yamejaa kutu mpaka yatoke damu, zingatia yote ninayokueleza. Nakuonea huruma kwa kuingia kwenye matatizo makubwa.”
“Hata yakinikuta wewe yanakuhusu nini?”
“Eeh, leo unasema hivyo?”
“Ndiyo.”
“Kwa heri.”
Simu ile ilikatika ghafla, Lakashina alitulia kwa muda akiwaza sauti ile ni ya nani na kwa nini kila anapotaka kufanya jambo lake hutokea na kumpa onyo. Lakini aliamini uamuzi aishi maisha gani anao yeye mwenyewe, hata kuwa karibu na ndugu zake sauti ile ilikataa. Kwa uamuzi wake mwenyewe aliweza kuungana na familia yake. Hata vitisho alipopewa kuhusu mdogo wake kila kukicha hakuviona.
Alitupia simu pembeni aliyokuwa bado ameshikilia mkononi, aliamua kujilaza akiwa na hasira ya kusumbuliwa na sauti iliyokuwa ikimnyima raha kila alipokuwa na furaha moyoni mwake. Kuendelea kulala alikuwa akitaka mumewe aje ndotoni ili amueleze ukweli kuchoshwa kuendelea kutishwa na sauti ya mtu asiyeonekana na ikiwezekana waachane kabisa na yupo tayari kurudia maisha yake ya zamani.
Aliamini maisha ya masharti hayana uhuru, pia alijua kama ataachana na Lakashi lazima ataolewa na Sadat kijana mwenye pesa tena mwenye mapenzi ya dhati kwake kuliko kuendelea kuishi na kiumbe wa ajabu kama Lakashi.
Alipojilaza usingizi haukuchelewa kumchukua lakini mpaka anashtuka mumewe Lakashi hakuonekana ndotoni.
Ajabu ilionesha alilala sana na kuamka muda umekwenda sana ilikuwa inakimbilia mchana. Alipoamka alijawa na maswali mengi juu kulala bila kujiwa ndotoni mumewe, alikumbuka njia nyingine ya kumwita kwa kuchoma manukato aliyoelekezwa na mumewe.
Akiwa mtu mwenye hasira aliingia chumbani na kuchoma manukato lakini alisahau kufuata maelekezo ya kuchukua udhu kabla ya kufanya vile. Alichoma manukato yale na kutulia kwa muda lakini mpaka moshi unapotea hakukuwa na dalili zozote za kuonekana Lakashi. Baada ya kumkosa mumewe kwa hasira alisema:
“Na huyu mtu anayenijia kwa sauti akinitokea nitampa vipande vyake na tena anikome.”
Baada ya kusema vile, vilizuka vicheko mfululizo vilivyoonesha kumcheka yeye, aligeuka kumtafuta anayemcheka hakumuona kwa hasira alisema:
“Kama wanaume kweli mbona mnajificha, nakuhakikishieni kufanya mambo ninayoyataka mimi na siyo nyie.”
Alikwenda kuoga kujiandaa kwenda kwenye biashara zake ambazo kila kukicha zilizidi kupanuka, akiwa anajifuta simu yake iliita tena. Hakutaka kuichukua aliiacha iite mpaka ikate. Baada ya kumaliza kujipamba aliichukua simu na kuangalia nani aliyepiga, alishtuka kuona ni Sadat.
Kwa haraka alimpigia simu, baada ya kuita ilipokelewa.
“Haloo.”
“Haloo, Sadat.”
“Lakashina.”
“Ndiyo mimi, Samahani kwa kutopokea simu yako, kuna mjinga mmoja alikuwa akinisumbua.”
“Bila samahani, nilidhani labda ombi langu ndilo lililokuudhi.”
“Hapana Sadat, wewe ni mtu muhimu sana kwangu siwezi kukufanyia hivyo.”
“Nani kakuudhi tena malkia wa moyo wangu?”
“Achana naye tuzungumze yetu.”
“Upo wapi?”
“Nyumbani.”
“Mbona leo umechelewa sana, au huji mjini?”
“Aah, uchovu tu, nakuja sasa hivi.”
“Bado hujatoka nyumbani?”
“Nipo njiani.”
“Basi nakusubiri.”
“Shaka ondoa.”
Lakashina alikwenda kwenye gari lake na kuelekea kwenye biashara zake, njiani alijikuta akimchukua Lakashi na kumpa nafasi Sadat, alijua mapenzi na jini yana masharti makubwa na ukikosea lazima upate matatizo. Lakini Sadat ni mwanadamu ambaye mapenzi na maisha yake hayana masharti yoyote.
Alipanga kumueleza ukweli juu ya uamuzi wake wa kuvunja ndoa yao ya ndotoni na kuolewa na mwanadamu mwenzake. Japo alijua itakuwa si rahisi Lakashi kukubali lakini aliamini penzi la kweli halilazimishwi.
Lakashina alijikuta akihamisha mawazo yake yote kwa Sadat mwanaume ambaye aliugusa moyo wake na kutamani siku moja awe mumewe. Alipofika dukani kwake bila kutulia alimpigia simu Sadat amfuate wakapate chakula cha mchana.
Sadat alifika dukani baada ya muda mfupi, waliongozana wote hadi kwenye hoteli iliyokuwa karibu kupata chakula cha mchana. Baada ya mhudumu kuchukua mahitaji yao aliondoka na kuwaacha wakizungumza.
“Mh, Lakashina lete habari.”
“Aah, kawaida tu.”
“Mbona leo umechelewa?”
“Si muhimu kuyajua tuzungumze yetu.”
“Basi jana usiku nilipokupigia simu nilikuwa nimeshtuka usingizini baada ya kuota tupo ufukweni tukipunga upepo na niliposhtuka nikajikuta nipo kitandani peke yangu.”
“Ooh, po...,” Lakashina alishtuka kumuona mtu kama mumewe Lakashi akipita mbele ya meza yao, harufu ya manukato apendayo kujipaka ilikatisha kwenye pua zake.
“Vipi?” Sadat alishtuka baada ya kumuona Lakashina akishangaa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hebu ngoja,” Lakashina alinyanyuka kumfuata mtu aliyemfananisha na mumewe aliyekuwa amesimama amempa mgongo akizungumza na mtu ili kupata uhakika.
Alikwenda mpaka sehemu ile na kumpita, alipomuangalia usoni hakuwa yeye, alishusha pumzi na kurudi kwenye meza yake. Alipoketi Sadat alimuuliza.
“Vipi Lakashina?”
“Hapana.”
“Kuna kitu gani, naona umenyamaza ghafla na kunyanyuka, umeona nini?”
“Achana nayo tuendelee na yetu.”
“Mh, umefikia wapi?”
“Kuhusu nini?”
“Jibu langu.”
“Sadat lazima nikwambie ukweli toka moyoni mwangu hata mimi nakupenda.”
“Sasa basi nipe jibu langu.”
“Naomba unipe muda.”
“Kuna kipingamizi gani cha kuchelewesha jibu?”
“Hakuna kipingamizi si unajua jambo zuri halihitaji haraka.”
“Lakashina, kumbuka moyo wangu wote nimekuachia wewe, kwa nini usiniruhusu kuwa sehemu ya pili ya mwili wako?”
“Unajua Sadat mi...,” Lakashina alinyamaza tena kimya baada ya kumuona mumewe Lakashi akiwa amekaa meza ya jirani akiwa amemkazia macho, kitu kile kilimshtua tena Sadat.
“Lakashina vipi tena?”
Hakumjibu kitu, aliendelea kumkazia macho mtu aliye mbele yake ambaye aliamini kabisa ni mumewe Lakashi.
Mtu yule aliendelea kutulia akiwa amemuangalia huku machozi yakimtoka, ilikuwa ajabu ya mumewe Lakashi kunywa pombe, kitu kilichokuwa haramu kwake na kumzuia hata yeye mwenyewe asinywe pombe.
“Lakashina vipi?” Sadat aliuliza huku akigeuka kumuangalia mtu aliyekuwa meza ya mbele yao.
Lakashina ambaye moyo ulikuwa umemlipuka na kwenda mbio, bado aliendelea kukaza macho yake kama kaona kitu cha ajabu ambacho hajawahi kukiona maishani mwake.
Sadat baada ya kuchanganywa na hali ile alinyanyuka na kuwafuata meza ya pili kutaka kujua wamemfanya nini Lakashina.
“Samahani ndugu.”
“Bila samahani.”
“Eti mmemfanya nini huyu mwanamke?”
“Sisi?”
“Ndiyo.”
”Kwani amekwambia tumemfanya nini?”
“Hata mimi nashangaa, tulikuwa tunazungumza mara aliwatazama na kushindwa kuendelea kuzungumza.”
“Muulize vizuri, sisi hapa tuna mazungumzo yetu wala hatuna habari na meza yenu.”
“Eti wamekufanya nini?” Sadat alimuuliza Lakashina.
Swali la Sadat kwa Lakashina lilikuwa kama kumzindua
Sister sisi tupo hapa muda mrefu umekuja mmetukuta, sasa nani kaondoka?”
“Mbona sasa siyo wenyewe.””Kina nani?”
“Sadat tuondoke hapa hapatufai.”
“Samahani brother,” jamaa aliyekuwa amekaa meza ya pili alisema.
“Bila samahani.”
“Huyu ni mpenzi wako?”
“Ni dada yangu.”
“Hajawahi kupatwa na ugonjwa wa akili?”
“Bado.”
“Muwahishe hospitali huenda malaria imeanza kumpanda.”
Kauli ile ilimuumiza moyo Lakashina, hakutaka kusema kitu, alijikuta akidondokwa na machozi.
“Sadat unasubiri nini? Kama hutaki kuondoka nakuacha,” Lakashina alitoka eneo la hoteli na kwenda kwenye gari la Sadat, alifungua mlango wa gari na kuingia ndani. Wakati huo Sadat alikuwa bado anazungumza na jamaa ambao walikuwa wakimshangaa Lakashina.
Lakashina alimuona Sadat anachelewa aliteremka kwenye gari na kwenda kukodi gari lililokuwa likishusha mtu njiani. Alipoingia ndani ya gari hakuwa na hamu ya kurudi dukani, alimwambia dereva ampeleke moja kwa moja kwake.
“Nipeleke Mbezi.”
“Ipi?”
“Beach.”
“Elfu thelathini.”
“Nani kakwambia siwezi kukulipa?” Lakashina alijibu kwa hasira.
“Siyo hivyo dada, wapo ambao ukiwaambia mwisho wa safari wanalalamika.”
“Nimekueleza sitaki maelezo zaidi niwahishe nyumbani.”
Dereva aliondoa gari kuelekea Mbezi akiwa na mawazo mengi juu ya hali ya yule dada aliyeonesha kuchanganyikiwa.
Alipofika kwake alilipa fedha na kwenda moja kwa moja chumbani kwake, alijilaza kitandani akiwa mwingi wa mawazo juu ya yote yaliyomtokea muda mfupi baada ya kumuona mwanaume aliyefanana na mumewe Lakashi zaidi ya mara mbili.
Alijiuliza ni wasiwasi wa kuonesha anatoka nje ya ndoa yake na Lakashi kufikia hatua ya kumuona kila sehemu aliyokwenda. Aliamua kujilaza ili Lakashi aje ndotoni na kuzungumza naye lakini alilala mpaka jioni hakukuwa na sura wala kivuli cha Lakashi.
Baada ya kuamka alikwenda kwenye kabati kuangalia mafusho ya kumwita Lakashi lakini cha ajabu hayakuwemo. Alijiuliza yamekwenda wapi au aliyamaliza, alijikuta akipandwa na hasira na kusema kwa sauti.
“Nasema siogopi chochote kama na wewe umeamua kuondoka sawa, njoo uchukue kila kilicho chako na uniache peke yangu. Nahitaji maisha ya kujitawala.”
Lakini hapakuwa na jibu lolote zaidi ya kimya cha ajabu kutokea ndani, hali ile ilimtisha na kujiuliza ilitokana na kitu gani au Lakashi amekasirika na kuja kumtia adabu? Wasiwasi ulimjaa na kutoka nje, kama kuna tatizo basi apate msaada.
Alitoka nje lakini alikuta hali ya kawaida, alizidi kushangaa mauzauza yakimuandama. Aliamua kurudi ndani, akiwa ndani alipigiwa simu kuwa anatakiwa dukani. Aliingia kwenye gari na kwenda mjini, alipofika dukani alishangaa kukuta duka limepungua sana, kitu kilichomshtua.
“Vipi kuna usalama?” Aliuliza huku akitweta.
“Kwema tu vipi ulikwenda wapi, kuna mteja mmoja alikuwa akitaka mali nyingi hivyo tulikupigia ili mzungumze naye lakini alionesha ana haraka ameacha karatasi na kuondoka.”
“Na vitu vya dukani vimekwenda wapi?”
“Amenunua yeye.”
“He! Alikuja na gari kubwa?”
“Eeh dada.”
“Ningempata mtu kama huyo ningefanya naye biashara nzuri.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kweli dada hatujawahi kuuza mali nyingi toka tufungue duka, mali ya kuuza miezi mitatu tumeuza kwa siku moja. Ukipata wanne kama yule kaka ungekuwa milionea.”
Habari zile zilirudisha furaha moyoni mwake na kusahau yaliyomsibu muda mfupi. Akiwa na furaha alizungumza na wafanyakazi wake:
“Jamani leo mmefanya kazi nzuri naombeni mfanye usafi kisha niwape mapumziko ya wiki, kesho kutwa lazima nisafiri kufuata biashara nyingine. Pia mtapata ahsante ya mshahara wa mwezi mmoja.”
“Asante dada, inaonesha yule kaka alikuwa na fedha nyingi, roho iliniuma pale alipotuonesha fedha na kutueleza alitaka zote ziishie dukani, alisikitika na kusema fedha alizokuja nazo hata robo haikufika.”
“Jamani, hakusema atarudi lini?”
“Hakusema zaidi ya kuacha mawasiliano kwenye karatasi.”
“Haya endeleeni kufanya usafi mimi nipo hapa nje.”
Lakashina alikaa kwenye kiti chake na kufungua kile kikaratasi ili apate mawasiliano na mteja ambaye alionesha kutaka kuyabadili maisha yake. Alifungua na kukutana na neno lililomfanya arudie kusoma zaidi ya mara tano lilikuwa lile lile, hakuyaamini macho yake ilibidi amwite mfanyakazi wake mmoja amsomee aliamini kabisa alichokisoma sicho kilichoandikwa, kingine kilichomshtua na manukato ya karatasi ambayo hayakuwa mageni puani mwake.
“Zubeda njoo unisaidie kusoma kikaratasi hiki.”
Alipofika alimpa na kukisoma kisha alimgeukia Lakashina na kumuuliza:
“Kwani dada kuna nini?”
“Hilo karatasi limeandikwa nini?”
“Sijui ni jina au nini?”
“Zubeda kumeandikwa nini? Sitaki maswali,” Lakashina alisema kwa sauti ya ukali kidogo.
“Limeandikwa Lakashi.”
“Eeh!” Alishtuka.
“Lakashi.”
“Mmh! Upo sahihi?”
“Sahihi kabisa kwani vipi?”
“Huyo kaka unamfahamu?”
“Ndiyo leo tumemuona.”
“Hakuniulizia?”
“Mmh, sidhani kwani alipofika mimi ndiye wa kwanza kuonana naye kisha aliniuliza tunauza vitu gani. Nilimueleza tunavyouza, akafungua begi lake na kutoa pesa kununua vitu alivyotaka. Nilishangaa duka lilipungua kabisa kutokana na vitu vingi alivyonunua na baada ya manunuzi aliondoka. Kwani vipi?”
“Mtu huyo yuko vipi?”
“Kama Mpemba hivi.”
“Amenyoa o?”
“Ndiyo.”
“Ana kionja mchuzi?”(ndevu za chini ya mdomo).
“Ndiyo.”
“Hana nywele nyingi kichwani?”
“Ndiyo.”
“Si mtu wa kukasirika, ni mtu wa kutabasamu muda wote?”
“Tena lazima niseme ukweli, nimeshaona wanaume wazuri lakini yule kaka ni mzuri sana. Pamoja na uzuri wake ni mwenye huruma na mpole sana.”
“Siyo mume wangu huyo?”
“Mumeo! Dada umeolewa?”
“Ooh, samahani achaneni na hayo, alivaa nguo gani?”
“Alivaa kama Wahindi, suruali na shati kama kanzu lakini vilikuwa vimedariziwa kwa nyuzi kama za hariri, pia chini alivaa makubazi ya bei mbaya.”
“Jamaniii.”
“Kwani vipi?”
Wakati huo Sadat alikuwa akiingia dukani na kumshangaa Lakashina.
“Mbona umeniacha?”
“Sadat naomba leo uwe mbali nami nina mambo mengi sana yanahitaji niwe peke yangu.”
“Kwa nini nisikupe msaada wa kimawazo?”
“Sadat kuwa mwelewa, sitaki chochote kwako nakuomba uondoke mbele yangu mara moja.”
Lakashina alikuwa mkali kitu kilichowashangaza hata wafanyakazi wa dukani kwake. Waliamini kabisa Lakashina na Sadat ni wapenzi. Sadat aliondoka bila kuongeza neno, akizidi kuamini maneno ya jamaa waliowaacha hotelini kuwa Lakashina lazima atakuwa amechanganyikiwa.
Baada ya Sadat kuondoka, Lakashina alichukua karatasi na kuisoma upya, jina lilikuwa lile lile Lakashi, manukato yaliyokuwa yakinukia ni yale yale ya Lakashi mume wake ambayo hakuwahi kuyasikia sehemu yoyote duniani.
“Eti baada ya kununua alisema nini?”
“Dada alisema shida yake akuone wewe, kwa vile hatukujua upo wapi nawe ulitueleza unapokuwa umepumzika hutaki simu hatukuwa na jinsi.”
“Mkononi hana pete ya rangi ya zambarau?”
“Mmh! Dada kwa kweli hatukumchunguza.”
“Sasa fanyeni hivi, kila mmoja atachukua kiasi chake cha pesa, zitakazobaki mtaziacha kisha fungeni duka, funguo mtaniletea nyumbani.”
Kauli ya Lakashina iliwachanganya sana wafanyakazi wake kuonesha taarifa walizompa zimemchanganya sana. Walijiuliza mteja na tajiri yao wana uhusiano gani kiasi cha kumchanganya kiasi kile?
Kabla hawajapata jibu, Lakashina alikuwa tayari kwenye gari lake na kuondoka bila kuongeza neno. Lakashina alionekana kama kuchanganyikiwa na habari zile. Alijiuliza kile kinachomtokea ni nini? Muda mfupi amemwona mtu kama mumewe akipita lakini hakuwa yeye, wakati amekaa amemwona mtu mwingine kama yeye lakini hakuwa yeye. Anakwenda dukani anakutana na taarifa za mtu anayeitwa Lakashi, jina ambalo alijua ni mumewe, hata manukato ya karatasi iliyoachwa ujumbe yalinukia harufu ile ile.
Alijiuliza maswali yasiyo na majibu kuhusu mtu anayejiita Lakashi, bado akili yake haikukubali kwa kuamini Lakashi anayemfahamu yeye asingefika kununua vitu kwenye duka lake akijua kabisa yeye ndiye mmiliki mkuu wa duka lile.
Alipofika nyumbani alikwenda kuchukua udhu japo alikuwa ameshaasi kuswali, baada ya kuchukua udhu alilala usingizi. Pamoja na kuchukua udhu bado Lakashi hakuonekana usingizini. Alishtuka alfajiri ya siku ya pili bila kumwona Lakashi alijikuta akizidi kuchanganyikiwa.
Wazo lingine lilikuwa huenda ni wasiwasi wake Lakashi ameamua kuachana naye, alijikuta akijilaumu kwa kumkaripia Sadat, alichukua simu yake na kumpigia Sadat ili kumuomba msamaha.
Alipopiga simu ilipokelewa upande wa pili na sauti ya kilio ya Sadat akiomba msamaha.
“Basi nimekoma... sirudii tena... simfuati tena... mama nakufa.”
Kelele za Sadat kuonesha anapata kipigo kizito zilimshtua Lakashina.
Aliyenunua vitu dukani ni Lakashi gani? Na Sadat anapigwa na nani?
LakasHina alijiuliza kauli ya Sadat ilikuwa inamaanisha nini, amekoma, amekoma nini? Harudii tena, harudii tena nini? Hamfuati tena, hamfuati tena nani?
Lakashina alipiga tena simu kwa Sadat kupata uhakika wa kile alichokisikia.
Simu upande wa pili iliita na kupokelewa.
“Haloo Lakashina.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Haloo Sadat, upo sawa?”
“Nipo sawa kwani vipi?”
“Hapana.”
“Mbona simu usiku?”
“Sadat kabla ya yote hebu nieleze ukweli upo sawa?”
“Lakashina mbona tangu tulipoachana mi nipo sawa, nilijua kuna kitu kimekuchanganya ndiyo maana niliondoka bila kukusumbua,” Sadat alimjibu Lakashina bila kulielewa swali lake lilikuwa likimaanisha kelele za muda mfupi alizosikia kwenye simu na si mambo yaliyotokea mchana.
“Sadat si mambo ya mchana, ya usiku huu.”
“Mi nipo sawa.”
“Kama upo sawa vizuri.”
“Vipi ulikuwa unasemaje?”
“Kuhusiana na mambo ya mchana, najua nimekukosea naomba unisamehe.”
“Lakashina mbona nilikusamehe tokea hiyo jana, na pia suala hili hata ungenipigia asubuhi tungezungumza bila tatizo.”
“Sadat basi nilikuwa naomba kesho nije kwako usitoke.”
“Hakuna tatizo.”
Lakashina aliagana na Sadat na kujilaza kitandani akiwa bado hajapata jibu la lile alilolisikia kwenye simu. Alijiuliza sauti aliyoisikia kwenye simu kama ya Sadat akiomba msamaha ni ya nani? Lakini akili yake iliamini ni ya Sadat, kilichomshangaza baada ya kumpigia simu Sadat amemkuta kwenye hali ya kawaida.
Hakutaka kujisumbua sana kuwaza, alivuta shuka na kujilaza.
Siku ya pili Lakashina aliamka na kwenda moja kwa moja kwa Sadat, alipofika alimkuta ndiyo anaamka. Sadat alipomuona Lakashina ambaye siku ile hakuvaa mavazi ya kuuficha mwili, alichanganyikiwa. Alivaa nguo za kidunia za kuiacha sehemu kubwa ya mwili wake wazi.
“Karibu mpenz....,” Sadat hakumalizia neno lake.
“Sadat hofu yako, niite tu mpenzi.”
“Haya mpenzi karibu.”
“Asante, ndiyo unaamka?”
“Ndiyo, huwezi kuamini leo mwili umekuwa mchovu kuliko kawaida, yaani jana baada ya kuzungumza na wewe kuna njozi moja niliota na nilipoamka asubuhi bado mwili ulikuwa umechoka kama nimepigwa.”
“Sadat hiyo njozi umeota kabla ya kukupigia au baada ya kukupigia?”
“Baada ya kunipigia.”
“Uliota nini?”
“Ni mmh, we acha, ngoja nitoke kuoga nitakueleza.”
“Mmh! Sawa.”
Sadat alimuacha Lakashina sebuleni na yeye kuelekea bafuni kuoga, kwa upande wa Lakashina ile ndiyo ilikuwa siku yake ya kwanza kuingia ndani kwa Sadat. Aliliangalia jumba zuri la Sadat ambalo halikuwa na mwanamke ambaye angeongeza uzuri wake.
Moyoni alilisifia huku akitamani siku moja awe mama wa jumba lile. Akiwa katikati ya dimbwi la mawazo, sauti ya kilio cha kuomba msaada ya Sadat ilisikika kutoka bafuni.
“Samahani... utaniua bure, sijamwita... kaja mwenyewe, nisamehe...nisamehe nimekoma...nakuapia sitarudia tena, kama ukiniona hata namsalimia nifanye lolote, nipo chini ya miguu yako tafadhali usiniue.”
Sauti ile ilimshtua, haikuwa na tofauti na aliyoisikia usiku wakati alipompigia simu Sadat kwa mara ya kwanza. Alijiuliza sauti ile ni ya Sadat lakini mhusika alikuwa amekwenda kuoga, alijiuliza ni nani mwenye sauti kama ya Sadat anayemchezea akili.
Sauti ya kulalamika maumivu iliendelea huku sauti ya mtu kupigizwa ukutani ikizidi ndani ya nyumba ile. Mwanzo aliidharau, baada ya sauti ile kuzidi kulalamika huku ikionesha wazi malalamiko yale yanamhusu yeye, alishtuka. Wasiwasi ulimjaa lakini kwa ujasiri mkubwa alielekea bafuni akaone kuna kitu gani kimempata Sadat au ni hali ile ile sauti ya ndotoni.
Mlango wa bafu ulikuwa umerudishwa kidogo, Lakashina alisimama mlangoni na kumwita Sadat, wakati huo hakukuwa na sauti ya mtu kulalamika.
“Sadat... Sadat,” hakukuwa na jibu zaidi ya ukimya wa ajabu kutawala sehemu ile.
Akiwa anajifikiria kufungua mlango alishtushwa na michirizi ya damu, alitaka kukimbia lakini alijipa moyo ili ajue mwisho wa damu ile. Alipaza sauti yake tena kumwita Sadat kwa sauti ya kitetemeshi.
“Sadat upo sawa?”
Vile vile hakupata jibu lolote, kitu kilichozidisha wasiwasi. Wakati huo damu zilizokuwa zikitoka bafuni zilianza kuongezeka. Kabla ya kuusukuma mlango alijiuliza damu ile ni ya nani na Sadat alikuwa wapi?
Lakashina kwa ujasiri mkubwa aliusukuma mlango wa bafuni kuangalia kuna nini. Picha aliyoiona ndani kidogo mapigo ya moyo yasimame kwa mshtuko. Sadat alikuwa amekufa kifo kibaya sana, sehemu zake tumboni zilikuwa zimepasuka na utumbo ulining’inia nje. Macho yake na ulimi vilimtoka pima, alijikuta akipiga kelele za woga, akaanguka chini na kupoteza fahamu.
Aliposhtuka alijikuta amelala katikati ya dimbwi la damu, nguo zake zote zililoa. Alijinyanyua chini huku akitetemeka, kilichomshangaza ni muda alioanguka na aliozinduka. Alikumbuka tukio lililotokea asubuhi lakini alizinduka usiku tena wa manane.
Bafuni bado alikuwepo Sadat akiendelea kuvuja damu iliyokuwa ikiongeza dimbwi la damu sehemu aliyokuwa amelala. Alijiuliza Sadat ana damu nyingi kiasi gani ya kumtoka tangu asubuhi mpaka jioni bila kukatika? Akiwa anatetemeka alitoka mbio hadi kwenye gari lake.
Aliliondoa gari kama mwendawazimu hadi nyumbani kwake, alipofika alikimbilia bafuni kuoga. Baada ya kuoga alijiuliza kilichomtokea kama ni kweli au alikuwa akiota. Baada ya muda alipitiwa na usingizi mpaka asubuhi ya siku ya pili.
Siku hiyo ndiyo ya kusafiri kufuata biashara, aliamini kuondoka kule kungemsaidia kupunguza mawazo. Akiwa njiani kwenda uwanja wa ndege alinunua gazeti ambalo lilionesha kifo cha kutisha cha Sadat. Taarifa zilisema kifo kile kimegunduliwa na jamaa wa karibu majira ya saa tano asubuhi na mwili wake umehifadhiwa chumba cha maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikisubiri uchunguzi baada ya kifo chake kuonekana si cha kawaida.
Taarifa zile zilimchanganya sana Lakashina, alijiuliza kama mwili uligundulika saa tano asubuhi yeye alikuwa wapi, na watu waliokuja kumchukua yeye hawakumwona? Kingine kilichozidi kumchanganya ni taarifa za kuchukuliwa mwili wa marehemu na kupelekwa chumba cha maiti.
Alijiuliza kama mwili ulichukuliwa saa tano asubuhi na kupelekwa kuhifadhiwa chumba cha maiti, ule uliokuwa bafuni ukiendelea kuvuja damu ni wa nani? Muda wa kuingia ndani ya ndege ulipofika alikaa kwenye siti yake kusubiri iondoke.
Mtu mmoja aliingia ndani ya ndege akiwa amechelewa kidogo kabla mlango haujafungwa alimshtua Lakashina. Mtu yule alikuwa akifanana na Lakashi mumewe, hata harufu ndani ya ndege ilibadilika na manukato ya yule mwanaume yalitawala.
Kwake Lakashina hayakuwa mageni kutokana na kutumiwa na mumewe Lakashi, hakuwahi kuyasikia kwa kiumbe yeyote zaidi yake. Hata marashi aliyokuwa akijipaka yeye hakuwahi kuyasikia kwa mtu yeyote, hata rafiki zake walimwomba awatafutie kwa gharama yoyote.
Alimsindikiza kwa macho yule mwanaume ambaye aliamini kabisa ni Lakashi, lakini alikaa siti ya mbele yake. Aliachana na yule mtu kwa kuamini ni kiini macho kinachomtokea, lakini hakuwa na uhakika wowote kwa kile anachokiona. Aliendelea kulisoma lile gazeti kwa kupitia tena maelezo ya kifo cha Sadat, jina lilikuwa lile lile na sura ya marehemu ilikuwa ile ile. Lakini maelezo yake yalikuwa tofauti na yeye alivyoshuhudia mwili wa marehemu mpaka anatoka ndani kwa Sadat.
Taratibu sauti ya Sadat ya kuomba msamaha ilijirudia akilini mwake.
“Samahani... utaniua bure, sijamwita... kaja mwenyewe, nisamehe... nisamehe nimekoma...nakuapia sitarudia tena, kama ukiniona hata namsalimia nifanye lolote, nipo chini ya miguu yako tafadhali usiniue, aaaaaaah!”
Lakashina alijikuta akijiuliza aliyemuua ni nani na kwa nini alipomuuliza Sadat kuhusiana na sauti ya kuomba msamaha alimficha. Bado hakuamini kama kweli Sadat amekufa, aliona kama ni kiini macho cha kumtisha. Alijiuliza anayefanya vile ni nani? Kama ni mumewe anafanya ili iweje? Hakupata jibu.
Alijikuta akiapa kuwa siku akikutana na Lakashi atamweleza ukweli kuwa hataki tena kuolewa naye na alikuwa tayari kuishi maisha ya taabu kuliko maisha ya kutishana. Safari iliendelea, Lakashina akiwa katika kipindi kizito cha mambo ya ajabu yaliyokuwa yakimtokea.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mpaka mwisho wa safari, ilikuwa tofauti. Yule mwanaume anayefanana na mumewe aliteremka akiwa katika sura ile ile. Lakashina alikuwa na hamu ya kumsogelea ili athibitishe kama kweli ni yeye. Ajabu yule mtu alipotea katika mazingira ya kutatanisha kwani alijichanganya katikati ya watu. Lakashina alikwenda hoteli aliyozoea kufikia kabla ya kuingia kwenye maduka kukusanya mali.
Alipofika kwenye hoteli, alipotaka kulipa pesa alishangaa kuambiwa na mhudumu:
“Samahani dada umelipiwa.”
“Nimelipiwa! Na nani?”
“Kuna kaka mmoja amekuja hapa na kusema utafika na kukulipia kabisa ukifika wee kaa utakavyo hata chakula cha siku utakazokaa.”
“Amejuaje mimi nafikia hoteli hii?”
“Mmh! Kwa kweli dada swali gumu.”
“Anaitwa nani?”
“Amesema anaitwa Lakashi.”
“Lakashi?” Lakashina alishtuka.
“Mbona umeshtuka, kwani humjui?”
“Sijui kama ni yeye.”
“Dada kwani jina hilo hulijui?”
“Nalijua ni la mume wangu.”
“Sasa kipi kilichokushangaza?”
“Sikutegemea kumkuta huku.”
“Kwani yeye ulimwacha wapi?”
“Dada mengine hayakuhusu nioneshe hicho chumba nikapumzike.”
“Kile kile cha siku zote.”
Lakashina alipitia mizigo yake kuelekea chumbani kwake akiwa njia panda asijue nini kipo mbele yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment