Simulizi : Muuaji Aliyebakia
Sehemu Ya Pili (2)
Kila familia ilipewa vyumba vyake na kila hitaji lilikuwa likitimizwa na wahudumu wa hoteli hiyo.
Jackson ndiye aliyefanya mipango yote na wakati huo aliona ulikuwa ni muda muafaka wa kuuawa kwa James na mkewe. Alikuwa ameongea na kundi la majambazi lililopaswa kuwasaidia kukamilisha mauaji hayo, majira ya saa tatu usiku watu hao walifika hotelini hapo wakiwa na gari zao tatu. Mara baada ya kufika walimpigia simu Jackson ambaye aliwaahidi kutoka nje baada ya muda mfupi. Baada ya kupigiwa simu Jackson alimuaga mkewe na watoto wake akiwaambia kuwa alikuwa na kikao kifupi na wamiliki wenzie wa kampuni yao. Alipotoka nje aliwapigia simu Amos, Hamis halikadhalika Onesmo akiwaeleza watoke nje. Walitekeleza jambo hilo kwani walielewa zoezi ambalo lilifuata, nao waliaga familia zao wakieleza kuwa walikuwa na kikao.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walipofika nje walipanda katika gari moja lililokuwa la mwisho kati ya hayo matatu ya majambazi yaliyokuwa yamefuatana, Jackson alimpigia simu kiongozi wa kundi hilo aliyekuwa gari la mbele na kumweleza jambo walilotakiwa kufanya. Mara baada ya zoezi hilo Jackson alichukua tena simu yake na kumpigia James na punde ilipopokelewa alianza kwa kusikika “haloo James, njoo nje hapa na mkeo ikibidi kuna tatizo limetokea”
“tatizo? tatizo gani tena!” aliuliza James kwa mshangao. “njooni tu jamani mtaliona tusipoteze muda”
“sawa tunakuja” alimaliza James akiwa ameahidi kutoka na mkewe. Baada ya dakika tano James alitoka na mkewe wakiwa na nguo za kulalia, walisimama katika mlango wa kuingilia katika hoteli hiyo. Jackson na wenzie walishuhudia vizuri tukio hilo, alichukua tena simu yake na kumweleza James aende katika Range Rover iliyokuwa ya kwanza kati ya tatu zilizokuwa zimeegeshwa zikiwa zimeongozana. James alifanya hivyo na alianza kutembea akielekea katika gari hilo na hakuonyesha hofu yeyote. Alikuwa amemwacha mkewe akimwangalia hatimaye James aliingia katika gari hiyo aina ya Range Rover.
Baada ya dakika tano Jackson alielewa mpango alioufanya ulikuwa umefanikiwa alichukua tena simu yake na kumpigia mkewe James ambaye walimwona vizuri akiwa katika mlango wa hoteli hiyo. Hatimaye walimshuhudia akipokea simu “shemeji vipi? mbona unakaa nje, kuna mgonjwa hapa tunashauriana cha kufanya njoo” alisikika Jackson akimweleza mkewe James. “hee! kumbe mgonjwa nakuja” alijibu kabla ya kuanza kutembea akielekea kwenye Range Rover aliyoelekea mumewe. Hatimaye naye alipanda gari hilo, Jackson na wenzie walipiga kelele za kupongezana wakiamini kazi ilikuwa imeisha. Ziliwashwa gari zote tatu huku lao likiendeshwa na jambazi aliyekuwapo toka awali, mara baada ya kufunguliwa geti la hoteli walianza safari kwa mwendo wa kasi wakiwa na lengo la kuelekea eneo la Garrissa lilokuwa kando ya mto Tana walikopanga mauaji ya James na mkewe yaende kufanyika.
Mr. Tyoso kama alivyofahamika kutokana na matukio yake tofauti haramu ndiye aliyehusika katika mpango huo wa kutekwa kwa James na mkewe huku safari ikiendelea kuelekea eneo walilopanga kumfanyia mauaji. Mara baada ya James kupigiwa simu aelekee kwenye gari aina ya Range Rover, Walijiandaa na kijana wake mmoja wa kazi aliyekuwa kwenye gari hilo na punde alipoingia walimpiga na kitako cha bunduki na kumfanya azimie walimfanyia hivyohivyo mkewe ambaye pia alikuwa amezimia. Wakati huo mr. Tyoso alipanga kufanikisha mauaji hayo ili kutimiza matakwa ya wateja wake na mwishoe alihitaji kuendelea na shughuli zake akiwa na kundi lake hilo.
Walikimbiza gari zao na masaa mawili baadaye walikuwa katika eneo la Garrissa lililokuwa na giza nene kando ya mto Tana, wakati huo ilikuwa yapata saa tano na nusu. Waliegesha gari zao katika eneo hilo ambalo pia halikuwa na njia ila vichaka na mti kadhaa iliyokuwapo. Lilikuwa ni eneo lenye giza nene ambalo mtu mwoga asingevumilia kukaa. Gari moja kati ya hizo tatu walizokuwa nazo liliwashwa taa zake na kufanya eneo hilo liwe na mwanga kama ilikuwa mchana. James na mkewe walishushwa na kuwekwa eneo la mbele ambalo taa hizo za gari zilielekezwa, kwa umbali James alianza kurudiwa na fahamu ila kichwa kilimuuma sana. Hali haikuwa hivyo kwa mkewe ambaye bado alikuwa amezimia, mr. Tyoso aliwaamuru vijana wake wakachote maji katika mto Tana ambao ulikuwa umbali mfupi toka hapo, lengo lao likiwa ni kuwamwagia maji. Walitaka kufanya hivyo ili kurudisha kumbukubu za James na mkewe.
Baada ya dakika tano vijana wake hao watatu ambao walikuwa na bunduki mabegani mwao walirudi na madumu matatu ya maji ambayo walianza kwa kuwamwagia James na mkewe. Wakati hayo yote yakiendelea Jackson alikuwapo eneo la tukio na wenzie, alikuwa na hasira akihitaji kuuwa lakini alitulizwa na mr Tyoso aliyemtaka asiwe na haraka. Dakika kadhaa baada ya kumwagiwa maji ambayo yalikuwa ya baridi sana James na mkewe walishtuka na kukutana na picha mbili zilizonekana vizuri. Mkewe James hakuzitambua picha hizo ila mumewe alionyesha kushtuka, wakati huo walikuwa wako chini eneo walilokuwa wamemwagiwa maji. Waliponyanyua vichwa vyao walikutana na sura waliyoifahamua ya mtu aliyekuwa ameshika picha hizo ambaye alikuwa Jackson.
James na mkewe walishtushwa na hali halisi iliyokuwapo eneo hilo, watu zaidi ya watano walikuwa na bunduki, aliwashuhudia wamiliki wenzie wa kampuni wakiwa eneo hilo mbali na Jackson aliyekuwa ameshika picha. Tayari alijua kulikuwa na shari kwani aliiona picha ya mzee Samola na mwanaye Frank ambao wote kwa pamoja walihukumiwa kunyogwa kwa kosa la mauaji ya familia yake. Muda huo wote hakuna mtu aliyekuwa akiongea zaidi ya Jackson aliyeshika picha huku akitetemeka.
“ulizani ungepona kwa kusababisha kunyonga kwa baba na kaka yangu?” alisikika Jackson baada ya kimya cha muda mrefu, kabla hajajibiwa kitu wakati huo James na mkewe wakitetemeka alikurupuka na kuchukua moja ya bunduki ya kijana wa mr. Tyoso na kimumiminia kifuani mkewe James risasi zaidi ya saba.
James alipiga kelele juu ya tukio hilo, na kwa kasi ya ajabu alikurupuka kumvamia Jackson aliyekuwa na bunduki akiwa na lengo la kumpiga, kabla hajafanikisha lengo hilo alikamatwa na Amos aliyesaidiana na Hamis kabla ya kususkumwa tena chini.
“wewe ni kama muuaji unadhani utatuweza” Aliongea Onesmo aliyekuwa ameshika nondo mkononi na alianza kumpiga nayo, Amos na wenzie nao walijumuika naye kumpiga James ambaye alilia kwa uchungu akiwa haelewi kosa alilowafanyia wenzie hao waliomiliki kampuni moja.
Baada ya dakika tano James alikuwa ameumizwa sana na damu nyingi ilikuwa imemtoka nguo zote alizokuwa amevaa zilikuwa zimelowa damu.
“ mfungeni kamba huyu kinyago..” alisikika Jackson baada ya kuwasitisha wenzie wasiendelee kumpiga. Baada ya agizo hilo vijana wa mr. Tyoso walitekeleza jambo hilo na kuanza kumfunga kamba, muda wote matukio hayo yakiendelea hawakuingilia kitu kazi yao ilikuwa ni kuhakikisha usalama wa wateja wao. Mara baada ya kufungwa kamba kwa James aliyekuwa akilia kwa sauti ya chini Jackson na wamiliki wa kampuni wenzie waliopanga mauaji hayo walichukua bunduki kila mmoja. Walianza kuzikoki tayari kwa kufyatua risasi wakiwa wamezielekeza eneo alilokuwa amelala James akiwa hatazamiki mara baada ya kipigo. Jackson aliwaeleza wenzie wakae tayari kwa kufyatua risasi akihesabu mpaka tatu “ moja….! mbili….! ta…”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
* * * * *
George Johnson alikuwa ni kijana ambaye alizaliwa nchini Kenya na baada ya masomo yake ya shule ya msingi na sekondari alianza kujishughulisha utengenezaji filamu. Mara kadhaa alifanya kazi hiyo katika sherehe mbalimbali jijini Nairobi zikiwamo harusi na mahafali. Aliishi akitegemea kazi hiyo na mara nyingine alikuwa akiwafanyia kazi ya kuwapiga picha watalii kadhaa waliokuwa wakitembelea nchini Kenya. Alikuwa akiwaandalia filamu za ziara zao watalii nchini humo na hatimaye walikuwa wakimlipa pindi walipokuwa wakirudi katika nchi zao.
Mwezi wa kumi na mbili wakati sikukuu zikiwa zimekaribia alipigiwa simu na shirika moja lililohusika na watalii. Alielezwa kuwa kuna watalii walikuwa wakimhitaji awapigie picha za filamu kwa ajili utafiti wa viumbe vilivyoishi kando ya mto Tana. George alitaka kupuuza ombi hilo kutokana na sikukuu zilizokuwa zimekaribia lakini aligundua baadaye kazi hiyo ilikuwa muhimu zaidi. Aliwajibu watu hao kuwa alikuwa tayari kwa kazi hiyo, na hatimaye utafiti huo ulienda kuanzia eneo la Kipini ambalo ndipo Mto Tana ulikuwa ukiishia kuingia bahari ya Hindi.
Aliwajibu watu hao kuwa alikuwa tayari kwa kazi hiyo, na hatimaye utafiti huo ulienda kuanzia eneo la Kipini ambalo ndipo Mto Tana ulikuwa ukiishia kuingia bahari ya Hindi.
Watalii hao wanne waliokuwa wazungu wakitokea Norway walianza utafiti wao huo wakiwa na George aliyechukua picha kila jambo aliloambiwa kuchukua.
Alikuwa akipiga picha vyura wa aina tofauti waliokuwa kando ya mto huo na hilo lilikuwa ndilo lengo kubwa la watalii hao walitaka kujua aina za vyura waliopatikana kando ya mto huo. Walikuwa wakitumia gari aina ya Land Cruiser na kila ilipofika jioni walikuwa wakiweka mahema na kulala. Maisha hayo yalimchukiza George lakini jambo hilo lilikuwa la kawaida kwa wazungu hao waliozoea kazi hizo za utafiti. Siku iliyofuata walikuwa eneo la Burra wakiendelea na utafiti huo, hali kadahalika George alikuwa akipiga picha kwa ajili ya kuandaa filamu ya watafiti hao waliokuwa wakitokea Norway.
Siku ya tatu walikuwa eneo la Garrissa na mara baada ya utafiti wao huo liliwekwa hema na walilala tena eneo hilo wakiwa na gari lao katika sehemu hiyo iliyokuwa na miti pamoja na vichaka, walikuwa wakiweza kupita kutokana na uwezo mkubwa wa gari walilokuwa nalo. Muda wote waliokuwa wakilala George hakuwa na mazoea ya kufanya hivyo kutokana na uoga aliokuwa nao, lakini haikuwa hivyo kwa watafiti aliokuwa ameongozana nao ambao walikuwa wakilala pasipo hofu. Alikuwa na kamera yake kifuani ambayo kamba ya kibegi chake ilikuwa imemkaa shingoni, alitamani kazi hiyo ikamilike ili waondoke maeneo hayo ya mto Tana.
Majira ya saa tano na nusu usiku alishtushwa na kelele za magari yaliyonguruma upande wa magharibi wa eneo walilokuwapo. Jambo hilo lilimshtusha kwani hakufikiria kama kuna gari lingeweza kufika eneo hilo aliamua kutoka nje na alishuhudia mwanga uliotokana na taa za gari na kufanya eneo hilo lililokuwa na giza nene liwe kama mchana. Dakika kadhaa akiwa hajagungua jambo la kufanya alishuhudia taa kadhaa za gari hizo zikizimwa na mwanga wa kawaida ulibaki katika eneo hilo.
Alipata ujasiri wa ghafla uliomtuma aende eneo hilo bila kijiuliza mara mbili alianza kutembea eneo la pembeni na mwanga huo akiwa anausogelea. Lengo lake lilikuwa asionwe na watu hao waliokuwa wamefika eneo hilo nyakati hizo za usiku, mara baada ya kukaribia eneo hilo na kuanza kuyaona magari hayo vizuri alilala chini na kuanza kujiburuza kwa tumbo akisogea zaidi eneo hilo.Hatimaye alikuwa umbali wa kama mita nane na alishuhudia kila kitu kilichokuwa kikiendelea eneo hilo lililokuwa na mwanga kama wakati huo ilikuwa mchana.
Aliwashuhudia watu kadhaa wakiwa na bunduki mabegani mwao na wengine wawili mwanamke na mwanamume walikuwa chini kama vile walikuwa wamepotelewa na fahamu. Baada ya dakika chache aliwashuhudia watu wengine watatu wenye dunduki zao wakiwa na madumu aliyohisi yalikuwa maji kwani walikuwa wametokea eneo la mto Tana. Walianza kuwamwagia watu hao maji ambao walishtuka baada ya muda mfupi, George alihisi kuna jambo lilitaka kutokea juu ya watu hao na aliamua kuwasha kamera yake ya filamu ili ajumuike nayo katika kushuhudia tukio hilo. Taratibu aliiegesha na ilianza kuchukua picha za kila kitu kilichoendelea eneo hilo, alimshudia mtu mmoja akiwa anawaonyesha watu hao waliomwagiwa maji picha.Baada kimya cha muda mrefu mtu huyo aliongea kidogo kabla ya kukurupuka na kuchukua bunduki kisha kumumiminia mwanamke aliyekuwapo chini na mwanamume kwa risasi zaidi ya saba.
George alishtushwa na unyama huo uliokuwa ukiendelea hata hali ya hofu juu yake ilianza kumwingia lakini alijikaza akiamini alikuwa mwanamme kamili. Aliigeukia kamera yake na kushuhudia ikiendelea kuchukua kila tukio lililoendelea. Alimwona mwanamme aliyekuwa chini na mwanamke huyo aliyepigwa risasi akijaribu kumvamia mtu aliyekuwa amefanya tukio hilo. Hakufanikiwa zoezi hilo kwani alisukumwa chini na alianza kupigwa na watu hao ambapo mmoja wao alionekana alichukua kitu kizito kama chuma.
Dakika chache baadaye mtu huyo alikuwa ameumizwa vibaya na aliamriwa afungwe kamba, baada ya kufungwa kamba aliwashuhudia wanaume wanne wakizikoki bunduki zao wakiwa tayari kwa kumuua mtu huyo aliyefungwa kamba. Mmoja wao alianza kuhesabu akisikika “moja….! Mbili…! tatu…!” mara baada ya kuhesabu mara tatu watu hao walianza kummiminia risasi mtu huyo kama vile walikuwa vitani walikuwa hawana huruma hata kidogo. Wakati tukio hilo likiendelea George aligeuza kichwa chache asishuhudie tukio hilo, aliiacha kamera yake ikipiga picha kila kilichoendelea. Katika maisha yake alikuwa akidhani matukio kama hayo yalikuwa ya filamu za kuigiza lakini alishuhudia kwa macho yake na kubaini kuwa yalikuwa yakitokea.
Baada ya zoezi hilo watu hao waliwasha gari zao na kuondoa kwa kasi eneo hilo la tukio, George alijikuta akilia peke yake juu ya mauaji hayo yaliyokuwa yametokea. Aliikumbuka tochi aliyokuwa nayo baada ya giza nene kutanda eneo hilo ikiwa ni baada ya kuondoka kwa magari hayo, alichukua kamera yake na kuanza kusogea taratibu eneo la tukio. Mara baada ya kufika eneo hilo alitumia tochi akiendelea kuwapiga picha watu hao waliokuwa wameuawa, moyo ulimuuma sana na hakuelewa kosa walililokuwa wamefanya.
Akiwa anaendelea kizichukua vizuri picha za sura za watu hao waliouawa alishtushwa na mngurumo wa gari lililokuwa likirudi kwa kasi eneo la tukio. Alitoka mbio na kwenda kufichama katika kichaka cha karibu, aliwashuhudia watu sita wakishuka katika gari hilo na mmoja wao aliwaamuru wenzie wakaitupe miili hiyo katika maji ya mto Tana. Walitii maagizo hayo na kuibeba miili hiyo, walianza kuelekea upande uliokuwa na mto huo. Baada muda mfupi walikuwa wametimiza zoezi hilo waliwasha tena gari zao na kuondoka kwa kasi. George alikuwa amechanganyikiwa na katika maisha yake hakuwahi kushuhudia mauaji kama hayo, aliingiwa hofu juu ya uhai wake kuhusiana na picha hizo alizozipiga.
Siku iliyofuta ambayo ilikuwa ya mwisho aliendelea kuchukua picha zilizohusiana na utafiti uliofanywa na raia wa Norway. Hakujaribu kumwambia mtu juu ya tukio alilokuwa amelishuhudia usiku wa siku iliyopita, hakuwa na furaha sana jambo lililofanya watafiti hao wamwulize mara kadhaa kama alikuwa na tatizo. Hakuthubutu kutoa siri hiyo aliyokuwa ameishuhudia, mara baada ya utafiti huo aliandaa filamu ya watalii hao na hatimaye aliikabidhi na kupewa malipo yake. Tayari pia alikuwa ameandaa filamu ya dakika ishirini na tano iliyohusiana na mauaji aliyoyashuhudia, alikuwa akisubiri asikie tukio lolote lililohusiana na mauaji hayo ili aipeleke filamu hiyo kituo cha polisi. Matukio ambayo yalikuwamo katika filamu hiyo ilikuwa na vigumu kwa mtu kuamini kama yalikuwa ni mauaji ya kweli, alifanikiwa kuzipata picha za watu ambao walionekana vizuri mwanzo mpaka mwisho.
Siku kadhaa zilipita pasipo kusikia jambo lolote lililohusiana na mauaji hayo, alipata wazo la kupeleka kituo cha polisi filamu hiyo lakini kabla hajafanya hivyo aliamua kuomba ushauri kwa mjomba yake aliyekuwa mwanajeshi mstaafu. Alisimulia tukio lililoendana na lake na kujifanya akiomba ushauri wa tukio kama hilo, mjomba yake huyo alimtisha akimwambia matukio kama hayo ni hatari. Aliongezea kuwa angefanikisha kukamatwa kwa watu hao lakini mwisho wake lazima ungekuwa kifo. George jambo hilo halikumwingia akilini hata kidogo, moyoni aliumia juu ya mauaji aliyokuwa ameyashuhudia na alipanga kuifikisha filamu hiyo kituo cha polisi endapo angesikia mauaji yeyote yaliyohusina na tukio alilolishudia. Suala la kutafutwa na wauaji hakuliogopa lakini mawazo yake yalimtuma kuhakikisha haki inatendeka juu ya wauaji.
* * * *CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mara baada ya kukamilisha mauaji ya James na mkewe, Jackson na wenzake pamoja na kundi la vijana wa mr. Tyoso waliondoka eneo la tukio na gari zao kwa kasi kubwa. Wakiwa wametembea kilomita moja Tyoso aliamua kutoa wazo la kutupwa miili ya watu hao waliokuwa wameuawa katika maji ya mto Tana na waliamua kutekeleza zoezi hilo. Gari moja liligeuzwa kurudi eneo la tukio likiwa na Jackson pamoja na vijana watano wa mr Tyoso, mara baada ya kufika eneo la tukio walifanikisha kutupwa kwa miili ya James na mkewe katika maji ya mto Tana na hatimaye safari ilianza wakirudi eneo walilowaacha wenzao.
Mara baada ya kufika eneo la tukio walifanikisha kutupwa kwa miili ya James na mkewe katika maji ya mto Tana na hatimaye safari ilianza wakirudi eneo walilowaacha wenzao.
Walipofika walianza safari ya kuelekea Machakos eneo waliloziacha familia zao, majira ya saa nane usiku walifika eneo hilo na Jackson alichukuwa jukumu la kumlipa mr. Tyoso alyesaidia kufanikisha mauaji hayo akiwa na kundi lake. Mara baada ya tukio hilo mr Tyoso aliondoka akiwa na kundi lake katika hoteli hiyo waliokuwa wamefikia.
“sasa mmeona watu wangu kazi imeisha na utajiri ule ni wetu” alisikika Jackson mara baada Tyoso kuondoka na kundi lake.
“mwache aende kuzimu mtu gani anamikiki nusu ya hisa za kampuni” aliongezea Hamis jambo hilo, wote walikumbatiana na kupongezana na walirudi katika vyumba vya familia zao kama vile walitoka kwenye kikako kirefu cha kampuni.
Siku iliyofuata kama ilivyopangwa ilikuwa na siku ya kuanza safari ya kurudi nchini Tanzania, asubuhi kilifanyika kikao cha safari hiyo. Jackson aliwaeleza wanafamilia hao kuwa James na mkewe walikuwa na mambo ya ziada ya kufanya nchini humo Kenya hivyo wangerudi Tanzania wiki moja baadaye. Jambo hilo lilieleweka na safari hiyo ilianza, siku tatu baadaye walikuwapo nchini Tanzania.
* * * *
Robert ambaye alikuwa mtoto wa pili wa James hakufurahishwa na safari iliyokuwa imeandaliwa dhidi ya kaka yake Geofrey aliyetakiwa kurudi nchini Tanzania kutokana na homa za mara kwa mara alizokuwa nazo. Baada ya maandalizi ya safari ilikuwa ikisubiriwa siku hiyo wakati Robert akiwa hayuko tayari kuachana na kaka yake huyo ambaye pia hakupenda tukio hilo. Siku ya safari ilipofika Robert akiwa na mwalimu wake waliondoka shuleni hapo kuelekea uwanja wa ndege wa Chicago kwa lengo la kumsindikiza Geofrey. Walikuwa wakilia wakiwa hawaamini kuwa wangetengana kwa miezi kadhaa iliyokuwa imebakia kabla ya likizo.
Hatimaye walifika katika uwanja huo wa ndege na Robert aliagana na kaka yake na kuishia kupanda ndege akiwa na mwalimu wao. Walikuwa wakielekea jimbo la Washington ambako safari ilitarajiwa kwenda kuanzia. Robert alirudi shule akiwa na dereva wa gari hilo la shule ila hakujisikia vizuri muda wote kutokana na tukio hilo la kuagana na kaka yake. Alijipa matumaini akiamini angerudi Tanzania wakati wa likizo yake ndefu jambo lililomfanya ajipe moyo wa kubaki shuleni hapo kuendelea na masomo yake.
Hatimaye majira ya saa moja jioni Geofrey alikuwa akiagana na mwalimu wake tayari kwa safari ya kurudi Tanzania. Ndege aliyopanda ilikuwa ikitarajiwa kupita katika bara la Amerika ya kusini katika jimbo la Rio de Jeneiro nchini Brazil kabla ya kupita Uingereza na mwishoe Afrika. Geofrey alielezwa kuwa taratibu zote za mapokezi yake zilikuwa zimeshakamilika na angepokelewa mara baada ya kufika Tanzania. Safari ya ndege hiyo ilianza mara baada ya muda uliopangwa kutimia, Geofrey mtoto wa miaka kumi alikuwa akiona mwisho wa kuyaona maghorofa ya kifahari ya nchi hiyo ulifika.
Aliamini angeikumbuka sana Marekani hususani jimbo la Illinois ambalo alikuwa akisoma, hiyo yote ilitokana na kuumwa kwake mara kadhaa akaamua kukubaliana na kila lililokuwa limetokea.
Mbali na mabegi yake ya nguo yaliyokuwa yamehifadhiwa eneo la mizigo alikuwa amebeba begi lake dogo alilokuwa akihifadhi vitu vyake muhimu. Moja ya vitu alivyohifadhi humo zilikuwa picha za familia yake ambayo aliipenda sana, alikuwa na picha zidi ya ishirini zikiwamo ambazo alikuwapo mdogo wake Robert.Safari iliendelea kukiwa na kila raha ambazo siku zote alitambua kuwa zilikuwa za kawaida katika usafiri huo wa ndege. Baada ya masaa kadhaa ya safari hiyo alishtushwa na hali ya mtikisiko ambayo ndege hiyo ilianza kukumbana nayo. Jambo hilo pia liliwashtua hata abiria wenzie waliohofia hali hiyo ya mtikisiko, hakuna taarifa zozote zilizotolewa na dakika kadhaa baada ya mtikisiko huo kuzidi. Walitoka wahudumu wa ndege ambao pia walikuwa na hofu na walianza kutoa maelezo ya hatari ambayo ndege yao ilielekea kukumbana nayo.
Walieleza kuwa kila mtu asali kwa imani yake kwani ndege ilikuwa imepoteza mwelekeo kutokana na ukungu mzito uliokuwa umetanda angani. Taarifa hizo ziliwashtua abiria hao ambao kila mmoja alianza kufanya jambo lake, wengine walikuwa wakilia, wapo waliokuwa wakiomba pasipo kumaliza sala zao kutokana na hofu iliyokuwa imetanda. Kuna wengine walianza kuzunguka zunguka katika ndege hiyo ambayo haikuwa na raha tena kutokana na mtikisiko uliongezeka na kuwafanya watu wengine washikilie vizuri viti walivyokuwa wamekalia.
Marubani wa ndege hiyo walikuwa wamechanganyikiwa baada ya ndege yao kupoteza mwelekeo walikuwa hawaelewi walichokuwa wakikifanya kutokana na ukungu uliokuwa umetanda angani. Katika harakati zao hizo za kujiokoa walishtushwa na mlima uliokuwapo umbali mfupi toka eneo walilokuwapo. Jambo hilo liliwaogopesha na waliishia kufumba macho baada ya kuamini haikuwezekana kuukwepa mlima huo wakiwa tayari kwa lolote ambalo lingetokea.
* * * *
Hali haikuwa shwari katika milima iliyokuwa eneo la jimbo la New Amsterdam nchini Guyana bara la Amerika ya kusini kwani kulikuwa na ajali mbaya ya ndege iliyokuwa imetokea katika eneo hilo. Askari wa jimbo hilo walitumia usafiri tofauti kufika katika eneo hilo lililozungukwa na misitu ambalo lilitumiwa zaidi na wawindaji. Hali iliyokuwapo eneo hilo ndiyo iliyowakatisha tamaa askari hao kwani kulikuwa na miili ya watu saba tu ambao walikuwa wameokolewa wakiwa wamejeruhiwa vibaya. Watu wengi walikuwa wamepoteza maisha katika ajali hiyo ya ndege iliyokuwa inabeba abiria zaidi ya mia moja ishirini.
Askari waliwakimbiza hospitali watu walikuwa wamejeruhiwa vibaya na walikuwa wakiendelea kuwatafuta watu wengine na tayari miili ya watu zaidi ya sabini ilikuwa imepatikana. Ndege hiyo ilikuwa imesambalatika katika vipande vidogo vidogo na sehemu yake kubwa ilikuwa imelipuka kwa kuwaka moto. Mpaka jioni ya siku iliyofuata zoezi hilo liliendelea kuleta matuamaini japo kuwa watu wengi walikuwa wamepoteza maisha. Eneo ambalo ajali hiyo ilitokea lilikuwa halipitiki kirahisi kutokana na miti iliyokuwa imebanana sana jambo lililowachosha sana askari na kuamini huenda watu waliokuwa katika ndege hiyo tayari walikuwa wameisha. Ndipo walipohitaji orodha ya abiria waliokuwapo kwenye ndege hiyo iliyoonyesha zaidi ya watu saba walikuwa hawajapatikana. Taarifa za awali zilizofanywa zilieleza ndege hiyo ilipata ajali kutokana na ukungu ulikokuwa umetanda angani siku ya tukio.
Siku tatu baadaye bado miili ya watu wawili ilikuwa haijapatikana na askari baada ya kuitafuta kwa muda mrefu walitoa tamko lao la kuamini miili hiyo ilikuwa imelipuka na sehemu kubwa ya ndege hiyo. Hatimaye zoezi hilo lilisitishwa na ndugu wa marehemu hao walianza kuwasili nchini Guyana ili kuitambua miili ya ndugu zao waliopata ajali katika tukio hilo lililojawa majonzi. Viongozi mbalimbali wa nchini Guyana walitembelea eneo la tukio lakini pia walikuwapo waliotembelea mochuari ya hospitali ya mji mkuu wa nchi hiyo wa Georgetown ambako miili yote ilihifadhiwa.
Siku iliyofuata aliwasili mwanamke mmoja mzungu ambaye mara baada ya kujitambulisha aliongoza eneo ambalo kulikuwa na watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo.Mara baada ya kumkosa mtu aliyemtafuta kati ya hao waliokuwa wamejeruhiwa alianza kutembea kwa haraka akielekea mochuari huku akilia, alionekana akiamini mtu huyo alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wamefariki. Mkononi alikuwa na picha ya ndugu yake huyo aliyekuwa akimtafuta, mara baada ya kufika mochuari alianza kuzunguka kila sehemu ambayo miili ya watu hao ilikuwa imehifadhiwa. Alizunguka kwa mara tatu lakini hakufanikiwa kumwona ndugu yake huyo jambo lililopelekea aanze kuonyesha picha ya ndugu yake aliyemtafuta lakini hakuna aliyemwona mtu huyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kuona jitihada zake zikigonga ukuta aliamua kuelekea katika kituo cha polisi ili kukutana na mkuu wa kikosi kilichotumika kutafuta miili ya watu hao waliopatwa na janga hilo la ajali ya ndege. Huko alijitambulisha kama Lashay na alieleza kuwa alikuwa akitokea Marekani, alidai alikuwa akimtafuta mwanafunzi wake aliyeitwa Geofrey James ambaye alikuwa safarini kuelekea Tanzania. Mara baada ya maelezo hayo askari aliyeongoza kikosi cha kuitafuta miili ya wahanga hao alitoa masikitiko yake akidai mtu huyo ni mmoja kati ya wawili ambao miili yao haikupatikana eneo la tukio.
Mara baada ya maelezo hayo askari aliyeongoza kikosi cha kuitafuta miili ya wahanga hao alitoa masikitiko yake akidai mtu huyo ni mmoja kati ya wawili ambao miili yao haikupatikana eneo la tukio.
Hiyo ilitokana na taarifa ya majina waliyopewa na shirika la ndege iliyopata ajali na baada ya kufanya utambuzi wa miili waligundua Geofrey ni mmoja ya watu hao ambao hawakupatikana. Zaidi alitoa maelezo ya imani yao kuwa Geofrey alikuwa amepoteza maisha katika ajali hiyo ya ndege.
Baada ya taarifa hiyo Lashay aliyeeleza kuwa alitokea shule ya American Academic School aliondoka katika kituo hicho cha polisi na kurudi katika hoteli aliyofikia katika jimbo hilo la Georgetown. Alikuwa na majonzi juu ya tukio zima la mwanafunzi wake Geofrey James aliyesoma katika shule yao ambaye alikuwa akirudishwa Tanzania kutokana na homa za mara kwa mara. Alikaa jimboni hapo kwa siku tatu akiamini huenda angepata taarifa za kupatikana kwa Geofrey lakini haikuwa hivyo, baada ya kuona hakuna dalili zozote za mafanikio aliamua kuanza safari ya kurudi Marekani.
Mra baada ya kufika alitoa taarifa za kila kitu kilichokuwa kimetokea katika uongozi wa shule yao na taarifa za kuaminika alizozitoa zilieleza Geofrey alikuwa amefariki katika ajali hiyo ya ndege.
Robert James pia alielezwa taarifa hizo alizozipokea kwa majonzi hali iliyopelekea aanze kulia muda wote akiwa shuleni hapo. Mwalimu wao Lashay ambaye awali James aliwahi kumkabidhi watoto wake ndiye aliyechukuwa jukumu la kumpeleka Robert nyumbani kwake akimfariji juu ya tukio hilo. Uongozi wa shule ulikuwa ukijaribu kufanya mawasiliano na James ambaye hakupatikana muda wote katika namba yake ya simu hali kadharika mkewe alikuwa hapatikani. Hatimaye waliamua Lashay aongozane na Robert kurudi Tanzania ili kutoa taarifa zilizohusiana na kifo cha Geofrey, mikakati yote ilifanyika na safari hiyo iliandaliwa. Siku husika ilipofika walianza safari ingawaje Robert kwa kiasi kikubwa alikuwa ametawaliwa na mawazo juu ya kifo cha kaka yake.
Siku ya Jumatatu majira ya saa kumi na moja jioni Lashay alikuwa ameongozana na Robert wakitembea kutoka katika eneo la uwanja wa ndege wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Lashay alikuwa na mabegi kadhaa wakati Robert aliyeonekana mchovu na alikuwa hajabeba kitu, waliongoza hadi eneo la lililokuwa na teksi za kukodishwa na kupata moja wapo. Safari ilianza kuelekea nyumbani kwao maeneo ya Masaki ambako Robert aliyekuwa na miaka saba alikuwa akikukumbuka vizuri, wakati huo Lashay alikuwa akitizama mandhari ya Tanzania aliyokuwa akiisikia tu kupitia vyombo vya habari juu ya utajiri wake wa maliasili.
Baada ya saa moja walikuwa nje ya geti la nyumba ya James ambalo lilifunguliwa baada ya kupigwa honi ya gari hilo walilokuwa nalo. Mara baada ya kuingia walishtushwa na kundi la watu waliokuwapo eneo hilo ambao walionekana walikuwa wakijadiliana jambo. Robert alishtushwa na kelele za vilio zilizompokea kutoka kwa majirani kadhaa na ndugu zake wachache aliowatambua ambao awali walikuwa wakiwatembelea nyumabni kwao.
“jikaze mwanangu baba na mama wamepotea na hivi zimepita wiki mbili” aliongea mama mmoja aliyemtambua kama shangazi yake. Taarifa hizo zilimshtusha zaidi Robert ambaye alianza kulia kwa sauti na mwishoe aliishia kupoteza fahamu walimchukua na kumpeleka katika miti ya kupumzika iliyokuwa na kivuli na kuanza kumpepea. Mwalimu wake Lashay ambaye alikuwa ameongozana naye hakutambua chanzo cha kupoteza fahamu kwa Robert kwani hakuelewa kitu. Alikaribishwa na mwanamme wa makamo aliyejitambulisha kwa jina la Jackson ambaye alidai awali walimiliki pamoja na James kampuni ya JAJHO Company Limited. Alimweleza Lashay kila kitu kilichohusiana na mazingira ya kupotea kwa James akiwa na mkewe nchini Kenya. Zaidi alidai mchakato wa kutafutwa kwao ulikuwa ukiendelea, Lashay naye alieleza kuhusiana na kifo cha Geofrey aliyekuwa mtoto wa James. Jackson aliwatangazia watu wote waliokuwapo nyumabni hapo kuwa James aliyeaminika kuwa huenda alikuwa ameuawa na mkewe, pia mwanaye alikuwa amefariki katika ajali ya ndege iliyotokea nchini Guyana. Taarifa hizo ziliangua vilio vya watu waliokuwapo eneo hilo zaidi majirani ambao walimtambua vizuri mwanae huyo wa James.
Siku tatu baadaye wakiwa wanaendelea kusubiri jitihada za vyombo vya habari na polisi ambao walikuwa na taarifa za kupotea kwa James, ndugu zake waligundua jambo lililowafanya waondoke nyumbani hapo kimyakimya. Waligundua Jackson aliyesimamia zoezi hilo la kutafutwa kwa James na mkewe ambaye pia alikuwa mmoja wa wamilikiwa JAJHO Company Limited alikuwa ni mtoto wa marehemu Mzee Samola aliyekufa kwa kunyongwa. Hisia za kulipizwa kisasi ziliwajia na hofu zaidi ilitanda juu ya uhai wao walimwacha Lashay aliyedai alihitajika kurudi Marekani na Robert ambaye ada aliyolipiwa ilikuwa ni ya miaka mitatu na zaidi msimu wa masomo ulikuwa haujaisha. Lashay alihisi jambo juu ya tukio hilo la ndugu zake na James kuondoka wakati taratibu za kumtafuta ndugu yao zikiwa bado zinaendelea.
Siku iliyofuata hata majirani wachache ambao walikuwapo nyumbani kwa James kwa muda siku kadhaa wakisubiria taarifa zozote zilizomhusu na mkewe waliamua kuondoka. Jambo hilo lilimshangaza Lashay ambaye alibaki na Robert sambamba na wafanyakazi wawili waliokuwapo nyumbami hapo. Majira ya saa saba mchana Jackson alifika na watu kadhaa na kumwita Lashay kando na kumweleza kuwa jambo lililokuwa likifuata wakati huo ni uuzaji wa nyumba ya James. Alimweleza kuwa James alikuwa akidaiwa na kampuni yake ya JAJHO na kulikuwa hakuna njia nyingine ya kulipa deni hilo zaidi ya kuuza nyumba yake iliyokuwapo baada ya kupotea kwake. Zaidi alidai kuwa hata hati ya nyumba hiyo ilikuwa mikononi mwao kama dhamana ya deni alilokuwa nalo. Mnada wa nusu saa ulifanyika na nyumba hiyo iliuzwa, waliamriwa wahakikishe wametoka katika nyumba hiyo ndani ya masaa matano.
Lashay alizidi kuchanganyikiwa na zaidi ni Robert aliyemshangaa mr Jackson kwa maamuzi yake, alikuwa akimtambua kama mjomba kutokana na biashara aliyofanya na baba yake lakini aligundua ukosefu wa utu wa mjomba huyo. Hilo lilitokana na kutowajalia kwani hakuzingatia ni wapi wangelala siku hiyo zaidi aliondoka na watu waliokuwa wamenunua nyumba hiyo wakiwa wamepewa agizo la kuondoka kwao. Lashay hakuwa na la kufanya zaidi ya kuchukuwa mizigo yake hali kadharika Robert alichukuwa mizigo yake. Aliamua kuwalipa wafanyakazi ambao walikuwa wakifanya kazi nyumbani hapo kwa James kwa vile walionekana kutokuwa na mwelekeo na jambo lililofuata hakujua kwani hakuwa na mawasiliano yeyote na ndugu zake James.
Aliamua kupanga katika nyumba ya kulala wageni akiwa na Robert aliyekuwa amechanganyikiwa juu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika familia yake. Lengo kubwa la Lashay lilikuwa ni kuvuta subira akiamini huenda James na mkewe wangepatikana. Baada ya kutopatikana mafanikio yeyote ndani ya siku tatu aliamua kuanza safari ya kurudi Marekani akiwa na Robert, hisia za mauaji dhidi ya James na mkewe zilianza kumwingia. Nafsi yake ilikuwa ikimtuma kuwa mtu ambaye huenda alihusika na mauaji hayo ni Jackson hiyo ilitokana na kukosa utu na kuonyesha ukatili wake waziwazi. Tayari aliingiwa na hisia akiamini alikuwa na kazi juu ya Robert ambaye hakuwa na msaada kwa wakati huo.
* * * *CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jeshi la polisi nchini Kenya lilikuwa na taarifa juu ya kupotea kwa watanzania wawili mtu na mkewe wakati wakiwa katika ziara yao binafsi. Taarifa hizo ndizo zilizowafanya polisi kadhaa waanze upelelezi juu ya tukio zima la kupotea kwa watu hao, wiki moja baadaye kulikuwa hakuna dalili zozote za kupatikana kwa watu hao jambo lililopelekea askari hao waachane na upelelezi wao. Wiki ya nne tangu kupotea kwa watu hao polisi walipata taarifa za kupatikana miili ya watu wawili kando ya mto Tana katika eneo la Burra ikiwa imeharibika vibaya. Taarifa za awali zilidai watu hao walikuwa ni mwanamke na mwanamme ambao walibakiwa na mifupa kwa kiasi kikubwa kutokana na muda mrefu waliokuwapo majini.
Miili hiyo ilichukuliwa mpaka jijini Nairobi kwa uchunguzi zaidi, askari hao walituma taarifa kwa askari wa Tanzania wakihitaji vielelezo zaidi juu ya James na mkewe ambao walikuwa wakitafutwa hadi muda huo. Hiyo yote ilitokana na kutokuwa na taarifa zozote za kupotea au kuuawa kwa raia wa nchi hiyo, siku mbili baadaye walipokea vielelezo zaidi vilivyomuhusu James na mkewe na mwishoni uchunguzi ulibainisha kuwa watu waliouawa walikuwa ni wenyewe.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment