Search This Blog

Sunday 19 June 2022

DEMU WA FACEBOOK - 1

 





    IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA





    *********************************************************************************





    Simulizi : Demu Wa Facebook

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Kituo cha mabasi yaendayo Tegeta kilikuwa kimesheheni watu kama ilivyo kawaida. Magari yanayoishia Magomeni hayakuwa katika kashkashi yoyote ile na wala yale yaendayo Kariakoo pia hayakuwa katika suluba ya kugombewa kama yalivyokuwa yale ya Tegeta.

    Katika kituo hicho cha Kinondoni Biafra umati wote uligeuka kuwa na hulka ya aina moja. Gari likija wote wanageuka kuwa wanariadha. Na wanapoufikia mlango wa gari wanageuka kuwa mabondia kwa jinsi wanavyougombea mlango mmoja wa gari aina ya DCM.

    Mchezo huu wa kugombea magari haukuchagua jinsia wala umri. Na pia hata kadhia ya urembo haikutazamwa. Wapo wasichana warembo ambao walikuwa na hadhi ya juu kumpita hata yule mrembo anayeshikilia taji la urembo wa taifa lakini hata hawa walikuwa wameipakata vyema mikoba yako makwapani, macho mbelembele tayari kwa kuwania basi litakalosimama na kutaja kuwa linaelekea Tegeta.

    Huu ndio ubaya wa Dar es salaam na usiombe kuumbwa ukiwa na aibu maana kila siku utakuwa mtu wa kurudi nyumbani usiku sana. Ama ukubali kuwa unalipia bei kubwa kupanda teksi zinazogeuzwa matumizi jioni na kuwa ‘matatu’.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni kweli wasichana wameumbwa wakiwa na aibu sana lakini sio wote, wapo wengine hawatazami kabisa ni macho mangapi yanawatazama, hufanya wanavyojisikia kulingana na nafsi zinavyowatuma.

    Mmoja kati ya wasichana wa namna hii naye alikuwa pale kituoni, akiwa amejiweka sawa kabisa kuvamia gari lolote litakaloidhinishwa kuwa linaelekea Tegeta. Kwa jinsi alivyoonekana ni kama mwanariadha anayesubiri amri aweze kuanza kufukuza upepeo.

    Ilipendeza kumtazama!! Iwapo tu wewe sio mmoja kati ya wale wanaowania usafiri!!!



    ********

    “We bwege nini…yaani sijui likoje tu hili, unikome we kinyamkera hujui nilipotoka na mimi sikujui tumekutana hapahapa kwenye daladala tuachane hapahapa umenielewa wewe mpuuzi" sauti kali ya msichana umri kati ya miaka 22 hadi 26 ilikuwa ikishusha matusi makali kwa kondakta wa gari la kwenda Tegeta ambaye huenda ni bahati mbaya au maksudi alimshika makalio wakati anapanda ndani ya gari. Konda hakuthubutu hata kujibu kitu na abiria wote walikuwa kimya wakishuhudia timbwili timbwili hilo. Wengine walikuwa wakijaribu kujiweka katika nafasi zao kwani ndio kwanza lile basi lilikuwa limefika. Bahati nzuri lilikuwa wazi kabisa. Abiria wote wakajitosheleza. Na nafasi zikabaki. Dada akachukua nafasi huku akiendelea kumbwatukia kondakta.

    "Samahani basi dada yaishe" alijikakamua kondakta na kuomba radhi. Ni nadra sana kwa makondakta.

    "Nyooo! Nani dada yako hapa,una hadhi ya kuwa na dada kama mimi hebu niangalie mara mbili we katuni" alijibu kwa fujo yule dada huku akimwonyesha yule konda uso wake uliopakwa poda iliyozidi kipimo na midomo yenye lipstick ya kizamani sana iliyokolea mdomoni. Alikuwa anavutia kumchekesha mtoto aliyenuna.

    "Mh! Watu wana mambo duniani!..sijui angekuwa mrembo tungesemaje…" Kijana mmoja aliyekuwa siti ya mbele kabisa alijikuta akisema baada ya kuona yule dada amezidi kumtusi yule kondakta. Kama mwanamme akajaribu kumtetea mwenzake. Laiti kama angemjua vyema msichana huyu….

    "Na we hebu nipishe huko na para lako hilo, kijana mdogo para kubwaa kha! Na utakayemuoa ana kazi huo mbichwa mbona hatapumua…shenzi mkubwa kazi kuingilia yasiyokuhusu" mvua ya matusi ikifuatiwa na vicheko ndani ya gari ilifuata,uso ulimshuka kaka huyu kwa aibu tele vicheko vilizidi kuongezeka pale abiria walipozidi kuhadithiana bango alilopewa yule kijana ambaye bila shaka alijutia kuingilia kesi isiyomuhusu hata kidogo. Yule binti alipomaliza akabetua midomo yake. Alizidi kufurahisha. Na akama angebetua zaidi basi angetisha kwani alifanania na kinyago kilichokosewa kuchongwa!!!

    Yeye hakujali hayo!!!



    Hakuwa binti mzuri wa kutisha hata kwa mbali, licha ya kujaribu kujiremba lakini ukweli ulibaki kuwa isingekuwa jeuri ya mdomo wake basi asingethubutu kumjibu kondakta hata kama angempapasa kifua chake bahati mbaya. Alikuwa ameuvuta mdomo wake na kuzidi kuufanya ubaya wake kuwa wazi zaidi. Kondakta hakumwangalia machoni, jeuri ya makondakta dada huyu alikuwa ameikata sasa. Kimyaa!!!



    ****



    Ilikuwa kawaida yake kupitia katika 'status' za rafiki zake katika mtandao wa kijamii wa facebook na kwa anaokuta wameweka coments zao aliwaongeza kuwa marafiki, alifanya hivyo kuondoa kama sio kupunguza tatizo la kuwa na marafiki wengi halafu hawana mchango wowote ule, aidha kuandika status, notes ,au kwenye wall ,kucoment na hata ku-like kwao inakuwa shida. Hawa aliwahesabu kama mizigo isiyostahili kubebwa!!!

    "Mapenzi kwa sasa basi,nimetendwa imetosha" ilisomeka hivyo status ya binti bingwa wa kuandika status za mapenzi aliyeitwa Sarafina Mgalagoso. Alianza kusoma kwa umakini coment moja baada ya nyingine, hadi akaifikia coment ambayo ilimvutia zaidi

    "Usiseme hivyo Sarafina, mapenzi ni maamuzi ya Mungu, tulia na wala usiyalaani ipo siku utapendwa na hautakumbuka tena machungu yote uliyopitia mwenzio pi nilitendwa yaani basi tu!!" alianza kwa ku-like ile coment kisha akamwongeza kama rafiki Husna Ali binti aliyeandika coment hiyo. Baada ya dakika tano ombi likakubaliwa.Kama kawaida yake Peter akaamua kutuma shukrani zake kwa njia ya wall. Hakuna kitu alikuwa akipenda kama kuunda urafiki na msichana!!

    "He! Mpaka kila mtu ajue mi na wewe tumekuwa marafiki au?" ndio jibu alilopokea baada ya kutuma shukrani.Peter alichukulia lile jibu kama utani.

    "Aah! Mrembo kwani vibaya sana jamani wananchi wengine kujua kwamba mimi na we ndo hivyo tayari marafiki?" alijibu Peter palepale kwenye Wall.

    "Haya yameisha" alipokea ujumbe huo katika inbox. Peter akaachia tabasamu huku akimwonea huruma yule binti kwa kujileta mwenyewe inbox. Huo ndio ulikuwa uwanja wa Peter. Mchezo huu ukaanzia hapa.



    PETER: Unaishi wapi?

    HUSNA: Tanzania, na wewe?

    PETER: Dah! We Husna mkorofi sana, namaanisha mkoa, mi nipo jijini Dar

    HUSNA:Jamani kwani kwenye profile yangu hauoni nilichoandika? Anyway!! nipo Dar pia, najua utauliza tena naishi wapi..,mi nipo Kinondoni kwa wazazi wangu. Alijibu kwa kirefu Husna.

    PETER: Aaah! Okay! Unasoma au unafanya kazi?"

    HUSNA: Nafanya kazi vipi kwani??

    PETER: Hapana napenda tu kukufahamu.

    HUSNA: Ah! Sio vibaya hata kidogo,

    Peter: Nimeipenda picha yako.

    HUSNA: Oya badae nalog out mimi. Alijibu tofauti na sifa alizopewa na Peter. Ikiwa ni dalili za kumpotezea Peter.



    Kwa muda wa dakika tano nzima Peter alikuwa bize akiipitia picha pekee katika album ya Husna, ilikuwa ni picha nzuri sana, nguo fupi aliyoivaa iliruhusu mapaja yachungulie nje kidogo na pozi lake liliupa fursa mguu wake mnene kuonekana vizuri kabisa. Sura ilikuwa ya kuvutia sana..na alitabasamu kuonyesha kwamba alifurahia kupigwa picha ile. Mtindo aliokuwa amekaa uliyaruhusu vyema maungo yote kuonesha kuwa yana rangi inayoshabihiana. Rangi ya chocolate!!!

    "Kuna watu wameumbwa na wakaumbika haswaaa" Alizungumza Peter huku akiihifadhi ile picha katika memory kadi yake ya simu.

    "Lazima aingie kwenye orodha huyu, hawa madem wa facebook simple (rahisi) sana kuwapata" alijipa uhakika Peter huku akiamini kuwa historia yake ya kukubaliwa na wasichana kirahisi itaendelea kumbeba kila pande hadi hapa kwa Husna.

    "Amekwisha huyu!!” alimalizia Peter na kuendelea na mambo mengine. Husna akasahaulika kwa muda!!



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ****



    Heriety Charly alikuwa ni binti mrembo wa wastani tu, alijiheshimu sana mbele za watu na hakuwa na skendo wala makuu yoyote pale mtaani kwao, mtaa wa Kigogo,mtaa ambao Peter pia alikuwa anaishi. Rafiki yake kipenzi na Heriety alikuwa ni binti mwenye matatizo sana na katika mtaa wao wa kinondoni aliitwa 'Mwajuma ndala ndefu' jina ambalo laiti angekusikia ukilitamka utaiona dunia chungu na hautatamani kuendelea kuishi. Binti huyu hakuwa mwingine bali Husna wa Ali. Ilipopita siku bila kukwaruzana na mtu basi mtaani ilikuwa sherehe kubwa sana, si wanaume wala wanawake, wazee kwa vijana hadi watoto Husna alikuwa anaingia nao katika migogoro na wakati mwingine wanafikia hatua ya kupigana.

    Inaamika kwa wanasayansi kuwa binadamu mwenye kasoro kubwa inayoonekana basi huwa mwingi wa hasira, hasira ambayo huitumia kujilinda na watakaothubutu kumsema vibaya. Sasa kwa Husna ilizidi, ni kweli umbo lake lilikuwa halielewekieleweki lakini tabia zake za kujisikia kama yeye ni malaika ziliwafanya wenye timamu zao waamini kuwa ana matatizo ya akili.

    Lazima usalimu amri mbele ya Husna binti wa kiislam aliyekulia uswahilini na kutimiza lile neno kwamba watoto wa kike wa uswahilini ndio wanaoongoza kwa kuwa micharuko, lakini kwa Husna ilikuwa zaidi, mcharuko si mcharuko, chizi na uwendawazimu vyote vyake. Mara chache sana akili yake ilikuwa sawa na kufanya vitu vya maana,ngao yake ya wingi wa maneno ilimlinda sana. Na lilipokuja suala la ubabe na penyewe pia alikuwa vyema. Mchokoze ujilaani mwenyewe!!

    "Yaani muda si mrefu huyu Heriety ataiga tabia ya Husna maskini mtoto wa watu alikuwa na tabia nzuri kweli lakini Husna atampoteza" yalisikika maneno ya waswahili pale Kinondoni Shamba, kila mara ambapo Heriety alikuja kumtembelea Husna. Lakini hata hao waliotamka walifanya kwa tahadhari kubwa sana ili Husna asiweze aidha kuwasikia ama kuwahisi kuwa wanamteta maana kivumbi cha binti huyu walikitambua mbele nyuma na kati.

    Husna hakuwa na mfano!!!



    "Hivi Husna facebook ndio nini" siku moja Heriety alimuuliza Husna.

    "Kwa nini unauliza?" badala ya kujibu na yeye alijazia swali. Watanzania sisi!!!

    "Aaah!! Kuna rafiki yangu ananiambia nijiunge kila siku hata simwelewi, anadai sijui ni kuchat sijui nini ah! Mi simwelewi bwana" alijikanganya Heriety. Husna alikuwa makini kusikiliza kama daktari anavyomtilia maanani mgonjwa akiwa anajieleza.

    "Aah! Nadhani itakuwa promosheni ya hawa tigo ya kupiga simu" alijibu Husna jambo asilolijua.

    "Aah! Mi simwezi huyo shoga angu..mi kwanza simu yangu betri mbovu halafu nianze tena kujiongelesha hovyohovyo..atajijua na hao facebook wake na tigo wake sijui." alimalizia Heriety huku akionekana kukerwa na hiyo promosheni ya facebook. Hakujua kuwa Husna naye hajui lolote!!!



    ****

    Ni kama jambo hili lilikuja wakati muafaka kabisa. Husna alikuwa anapenda sana kujishaua na ili ujishaue lazima kiwepo cha kukufanya uwe na mashauzi. Kama alifanya sala sasa haya yalikuwa majibu.

    Nokia 6030, zawadi aliyoletewa Husna na kaka yake aitwaye Musa aliyekuwa amehitimu masomo ya stashahada ya ualimu katika chuo cha Butimba jijini Mwanza ndiyo ilifanya ongezeko la mashauzi ya Husna kuzidi kipimo hasa hasa baada ya kugundua maana halisi ya facebook sio hizo promosheni za tigo alizomdanganya Heriety bali ni mtandao wa kijamii wa kuchat na marafiki,kubadilishana mawazo na kufanya matangazo dunia nzima. Alikuwa ni kaka yake aliyemweleza kuhusu facebook. Husna alipuuzia lakini hatimaye akajiunga. Awali hakufurahia lakini baadaye kaka mtu alijuta kumnunulia ile simu na kumweleza juu ya mtandao huo wa kijamii wa facebook. Husna akawa kama kichaa katika mtandao huu. Akiwa amejikita katika kuchat ni heri umwache alivyo, kuliko kumsumbua kwa namna yoyote ile na uambulie kubwatukiwa katika namna usiyoitegemea.

    Marehemu baba yake Husna aliwahi kugombana na mkewe katika ugomvi huo akamtusi mkewe kuwa siku anabeba mimba ya Husna alikuwa amekasirika sana ndo maana akazaliwa Husna!!! Neno hili lilimkwaza mama Husna lakini lilimuumiza kwani ni kama lilikuwa na ukweli hivi. Husna hakuwa msichana wa kawaida. Na baada ya kifo cha baba yake. Mama alikiri kuwa ikitokea binti yake akaolewa basi ataolewa katika sayari nyingine lakini si duniani. Nafsini alikiri kuwa Husna hakuwa na mvuto kwa mwanaume.

    Nani aliyekudanganya kuwa msichana akikutana na mwanaume ndio maziwa yanakuwa kwa kasi?? Nani anajua huenda Husna bado alikuwa bikra lakini kile kifua chake!!! Ni kama alikuwa amewasaidia na wasichana wengine wawili kubeba mzigo ule. Cha kukufanya utoe tabasamu ni mguu wake. Eti wenyewe ukawa mwembamba. Maajabu!!



    " Da Husna sufuria limechemka! Njoo usonge ugali" Mdogo mtu kistaarabu alimwambia dadaye usiku mmoja.

    "Mtoto huna adabu eeh! Huoni kama nachati" ndio jibu alilompa mdogo wake alipothubutu kumuingilia katika starehe yake. Maskini aliyeambiwa hata maana ya kuchati hajui.

    "Nikome mtoto na upotee hapa unaniharibia mood yangu" alisisitiza Husna na kisha akasonya na kuvuta charger ya simu yake akaichomeka panapo tundu husika. Bila kuaga wala kukohoa akajiondokea mtoto huyu. Alikuwa amefadhaika. Hata aliposhtaki kwa mama yao. Mama hakuchukua maamuzi yoyote. Na yeye alikuwa anamuhofia Husna.

    "Husna twende tukale mdogo wangu chakula kinapoa" kaka yake alimkumbusha Husna baada ya mama mtu kuwa ameingia jikoni na kusonga ugali yeye mwenyewe!!

    "Halafu hizi status utacoment wewe au!" kaka mtu alipewa jibu ambalo liliongeza kasi ya usagaji wa chakula tumboni na kisha njaa ikafuatia kama vile hajala.

    "Umelaaniwa we mtoto"

    "Asante,na usiku mwema" alijibu Husna huku akibetua midomo yake. Akafanana na sanamu baya la kuchonga!!!





    * * *





    "Mh! Huyu Husna angejua nilivyo mlevi linapokuja suala zima la makalio kwa msichana na kifua kipana haki ya Mama asingeweka hiyo picha kwani mizuka imepanda na wa kuishusha ni yeye dah!" Peter alikuwa anajisemea alipokuwa anaiangalia picha ambayo tayari alikuwa ameifanya wallpaper katika simu yake. Picha aliyoamini kuwa ni ya Husna. Tamaa za kimwili zikamwongoza tayari akawa anamtaka Husna kingono.

    "Na hapa kumpata ni lazima, naazima gari ya David, natia mafuta namuibukia siku akikubali kuonana na mimi we ngoja lazima kieleweke." alijiapiza Peter kana kwamba asingempata Husna angekufa. Kiapo kikamkaa nafsini!!! Tendo likasubiriwa!!!



    Zilipita siku kadhaa Peter akaamini sasa alikuwa amejipanga sawa sawa na sasa alikuwa tayari kuweka mitego yake ambayo alitegemea kwa namna yoyote ile lazima ingenasa na Husna angekuwa wake, imani yake katika picha ilimpa kiburi.

    Akatamani kufanya kwa vitendo.

    “Mh!! Peter naona kakitu kaukweli kwenye screen yako vipi tena umedownload au ndio….” Rafiki yake Peter aitwaye Dany alimuhoji Peter baada ya kuiona picha iliyokuwa katika kioo cha simu ya Peter.

    “Ah!! We we we chezea mbali hiyo mambo ndugu yangu huyo ndio shemeji yako ambaye naoa kabisa hivi karibuni” alijibu Peter huku akiwa anajiamini kabisa

    “Mh!! Umempatia wapi tena huyu ina maana umeachana na Maria??” aliuliza Danny.

    “Ah!! Zamani sana yani huyu ninae hata kabla ya Maria, halafu huwezi amini alinitongoza mwenyewe” alidanganya Peter ili azidi kupata sifa huku akijua kabisa hata sauti ya huyo Husna alikuwa haijui.

    “Dah!! Kaka we ni mkali tenasana tu mh! Unakismati mwenzetu!!!” alipewa sifa ambazo si za kwake naye akazipokea kwa mikono miwili. Laiti kama sifa zingekuwa zinamnenepesha mtu basi Peter angekuwa kijana mnene kupita wote duniani.

    “Naomba simu yangu wabongo hamchelewi kuwataka hata shemeji zenu” alisema Peter huku akichukua simu yake na kuondoka nyuma akiacha gumzo kwa kuonekana yeye ana maujanja sana katika fani hiyo ya mapenzi.

    Laiti kama wangejua kuwa hajawahi kumwona huyo binti!!!!!



    * * *CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Husna kwa muda aliokuwa amejitolea kwa ajili ya mtandao wa kijamii wa facebook na tangu aweke picha aliyodai ni ya kwake katika mtandao ilimchukua muda mfupi sana kuwa maarufu, kwa ulimbukeni aliokuwa nao haikupita status aache kutoa comments, asione watu wanapiga stori kwenye wall huyo nae anaingilia, ujumbe wowote uliotumwa alijibu haraka haraka.

    “Hiyo ni picha yako?”

    “Yeah!! Ni ya kwangu kwani vipi?”

    “We mkali aisee na unavutia sana”

    Ni baadhi ya maoni katika picha ya Husna ambayo ilivutia macho ya wengi.

    “Aah!! Mbona kawaida tu.” Naye alikuwa anawajibu bila wasiwasi. Huku akitambua fika kuwa picha ile sio yake.

    “Siku wakigundua sio mimi mh!! Aibu kweli jamani” alijiwazia Husna wakati anaitazama picha iliyokuwa kwenye profile lake kwa jicho kwa namna ya kuishangaa kama sio yeye aliyeiweka.



    Siku zilipita Husna halisi akiendelea kutesa mtaa wa Kinondoni shamba huku yule feki naye akizuzua akina Peter katika mtandao wa kijamii wa facebook. Maisha yakasonga mbele!!

    Abiria walikuwa wametulia, kila mtu akiwaza la kwake. Waliokuwa wanafahamia walikuwa wakipiga stori za hapa na pale, waliokuwa na magazeti walikuwa bize wakisoma, na wengine baadhi walibadili gari lile kuwa nyumba za kulala. Waliuchapa usingizi haswaa!!

    Kelele pekee zilizosikika mara kwa mara ni za kondakta aliyekuwa anataja vituo. Baada ya kutambua kuwa abiria wanashukia vituo vya mbele sana sasa zoezi la kudai nauli lilianza. Kila abiria alilipa kile lichotakiwa kulipa. Hapakuwa na utata wowote.

    Sasa alimfikia msichana aliyekuwa ametulia tuli!! Mwanzoni walisikika wakizozana kwa sauti za chini, kondakta akifanya kama kukaripia huku binti akijaribu kujitetea kadri alivyoweza!! Baada ya maelewano kuonekana kukosekana sasa kila mmoja alipaza sauti yake. Matusi nayo hayakukosekana!!!

    “Nasema hivi hiyo hamsini sikupi kama unataka tukabane poa tukabane mimi hiyo pesa sina!!! Isitoshe mimi ni mwanafunzi” zilikuwa vurumai kati ya kondakta wa daladala na binti aliyeonakana kuwa shupavu hasahasa . sasa walikuwa wameshuka chini. Gari lilikuwa limefika mwisho wa kituo. Yule dada alikuwa amesimamia msimamo kuwa yeye ni mwanafunzi japo hakuwa na kitambulisho.

    “Yaani umepandia gari mwanzo kabisa halafu umeshuka mwisho unanilipa 200 nasema nauli yangu utatoa mwanafunzi gani wewe kifua kipana hivyo ka mama mjamzito” kondakta alimbwatukia yule binti huku akimpa dereva amshikie nauli alizokuwa amekusanya kutoka kwa abiria wengine wastarabu.

    “Kwa hiyo unataka unipige au!!!” aliuliza yule binti baada ya yule kondakta kumfuata kwa kasi pale alipokuwa. Maajabu msichana kasimama imara akimngojea kondakta aliyekuwa na macho mekundiu. Bila shaka alikuwa ni mtumiaji mzuri tu wa madawa ya kulevya aina ya bangi.

    “We we we we!! Unajua thamani ya kifua unachokishika, tafadhali niachie,…yaani ukinichania blauzi yangu leo utajuta kuwa kondakta wa hili basi” alipaza sauti ya vitisho yule binti baada ya kondakta kumshika kifuani ili aikamate vizuri blauzi aliyokuwa amevaa. Watazamaji walikuwa makini kufuatilia tukio lile. Cha kushangaza na kukera hakuna raia mwema aliyesogea kuamua ugomvi ule. Hali ile haikumfanya yule binti ashikwe na uoga !!

    Peter alikuwa mmoja kati ya wananchi wengi waliokuwa wanashuhudia tukio hili la kustaajabisha. Alikuwa makini kabisa katika kuukusanya umbea huu ili aweze kujizolea sifa katika umati utakaomzunguka ukiwa umetega masikio kwa makini ukimsikiliza anachosimulia, nyongeza ya chumvi za hapa na pale ni moja kati ya silaha aliyoitegemea kumuongezea pointi za sifa zisizokuwa na msingi.

    Sifa za kijinga !!!!

    “Dah!! Kuliko kuwa na demu kama huyu ni bora uwe padri au usioe kabisa!! Dah !! eti huyu naye demu aisee” Peter alikuwa anawaambia watu waliokuwa pembeni yake huku akiwa hoi kwa vicheko vilivyopelekea atokwe na machozi. Umati haukumtegea sikio sana kila mtu alikuwa akiwaza la kwake.wakati wakishuhudia haya mara !!!!

    “Paaaaaa!!!” bila kutegemea kondakta alishtukizwa na mkono wa yule binti ulipotua katika paji la uso wake na kumfanya apepesuke hadi chini. Huenda sio uzito wa kibao hicho alichopokea bali kelele nyingi za wananchi za kumzomea zilipelekea kondakta yule kushindwa kunyanyuka pale chini huku yule binti akiondoka pale huku akishangiliwa kama mshindi wa vita kuu. Ndio alistahili kushangiliwa maana alikuwa ni mshindi wa kweli tena kumbukumbu ya kwamba yeye alikuwa ni msichana na yule aliyepigwa alikuwa mwanaume ilizidisha shangwe hizo. Kubwa zaidi hata ile nauli hakulipa. Alikuwa mshindi haswaa!!!

    Wananchi wasiokuwa na kazi za kufanya walimfuata kwa nyuma bila sababu za msingi hadi alipotokomea katika mihangaiko yake.

    Siku hii nayo ikamalizika!!!

    Husna akiendeleza rekodi ya kutikisa makondakta!!!



    * * *



    Peter aliyekuwa bado akiamini kuwa safari ya kumpata Husna ni fupi tu. Siku hii aliingia tena mtandaoni kujaribu kujitengenezea mazingira!!!



    PETER.helow!! Mambo vipi Husna,unafanya nini muda huu

    HUSNA: Poa…nipo tu kitandani bado

    PETER:We mvivu kweli hadi saa tatu hii hujaamka

    HUSNA:Hapana sio uvivu sina kazi ya kufanya mie wafanyakazi wamefanya zote tayari

    PETER:Jamani si uwasaidie kidogo

    HUSNA:Mh!! Mom hapendi nifanye kazi za hapa nyumbani ninaumwa mafua.

    PETER:Maskini pole jamani umetumia Pilton tayari au!!

    HUSNA:Ndio nini hicho?..i mean Pilton ni nini ??

    PETER:Ni dawa za mafua hizo

    HUSNA:Sizifahamu mie kama ni za hapa kwenu bongo. Sorry lakini

    PETER:Kwani we unatumia za wapi mpendwa

    HUSNA:Mara nyingi nikiugua natibiwa Uganda na kwa ugonjwa wangu wa kifua huwa dady ananipeleka India.

    PETER:Mh!! Jamani mi ninatamani kweli huko India sijawahi kufika mwisho wangu kwenda nje ni hapo Kenya.

    HUSNA:Ni pa kawaida sana hata sio pa kushangaa, may be Paris ndio kidogo unaweza kushangaa. One day utafika usijali Peter. Ok!!

    HUSNA:Ok!! Boy simu yangu inakata charge nitafute baadaye have a good time.



    “Mh! Hapa kuna umuhimu wa kujipanga sawasawa kwa huyu binti maana mh!! Kama ndio mtu wa nchi za watu mimi nitamuanzaje sasa” alijiuliza Peter baada ya mawasiliano hayo aliyokuwa amefanya na Husna.

    Usiku ulikuwa umeenda sana na kihoma kilikuwa kinamsumbua Husna!! Akalala mapema baada ya kumchachafya Peter.



    Usingizi ule uliotokana na kusumbuliwa na kihoma ukamzoa katika namna ya kushangaza na kisha kumfumbua macho lakini katika filamu ya ajabu, filamu ya kutatanisha



    “Karibuni sana sauti ya mama yake Husna iliwakaribisha wageni wale pale nyumbani.

    “Asante mama tumekaribia”alijibu kijana mmoja aliyeongozana na mwenzake.

    “Hapana msivue viatu jamani na hili vumbi humu ndani hata nyumba haina sakafu ingieni tu” mama Husna aliwaambia waggeni wake walipotaka kuvua viatu vyao,ni kweli nyumba ile haikuwa na hadhi ya kuvua viatu kwani ilikuwa haina tofauti kubwa sana na ardhi ya nje ya nyumba.

    “Mama yenu mzima?

    “Mama mzima anakusalimia sana” walijibu kwa pamoja wawili hawa.

    “Mama tusaidie maji ya kunywa” aliomba kijana mmoja akimuwakilisha mwenzake

    “Nanii!!! Husna!! Husna!!”

    “Bee!! Mama” aliitikia Husna kutokea ndani kwa sauti iliyotangaza kukerwa kwake na wito huo. Hakuwa na jinsi yoyote aliyemuita alikuwa mama yake.

    “Hebu leta maji ya kunywa hapo ndani haraka” alijibu mama kwa sauti ya kuamrisha

    Macho yalimtoka Husna ni ujasiri tu uliomsaidia asiweze kuangusha jagi la maji alilokuwa amebeba, katika kitundu kidogo cha pazia iliyochakaa aliweza kumwona mtu ambaye hakuwa na uhakika sana lakini alimfananisha na Peter, yule mvulana wa facebook aliyemwambia kuwa nyumba yao ni self contained ina geti kubwa na zaidi ya hapo kuna bustani ambayo yeye (Husna) hupendelea kukaa mara kwa mara mida ya jioni na mchana.Vipo wapi vyote hivi?? Ndio swali lililomuumiza kichwa.

    “Leta hayo maji we mtoto” alisisitiza mama yake.

    “Nitalivunja hilo lisimu lako siku moja umetuchosha humu ndani” aliendelea mama Husna kusisitiza.

    Hali ikawa tete, dalili za kuumbuka hadharani.

    Ghafla filamu ile ikakoma.

    Ilikuwa NDOTO. Ndoto ya maajabu.



    “Mh!! Ni nini hiki tena kinaingia katika akili yangu jamani yaani namwota yule kaka wa facebook sijui Peter kulikoni tena jamani” alijiuliza Husna huku akiwa anatetemeka na jasho likitiririka alipoamka na kukumbuka kuwa alikuwa ameota kuwa amemwona Peter ndotoni tena akiwa ndani ya nyumba yao.

    “Mh!! Ipo siku nitafahamika mie au hii ndoto ina maana gani kwangu??......ila mh! Ataanzaje kunifahamu na lini ataniona??” alijipa ujasiri Husna akiwa kitandani na hofu ikitoweka baada ya kugundua hakuna ukweli wowote uliokuwepo.

    “Vipi tena dada mbona usiku huu umekaa hapa, unaongea mwenyewe”

    “Hebu lala ukue mambo ya wakubwa hayakuhusu hata kwa mbali…sura bayaa kama bibi yako nyooo. Sijui likoje tu hili?” Husna alimjibu mdogo wake aliyetoka usingizini na kumkuta amekaa anaongea mwenyewe.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Mdogo mtu hakuongeza neno, akajilaza.



    Hadi saa kumi na mbili Husna ulikuwa hajaupata usingizi tena.

    Ile ndoto ilikuwa imemchanganya. Na ilikuwa lazima imchanganye. Maana alikuwa anasema uongo hivyo kwa namna yoyote ile lazima nafsi imsute.



    Majira ya saa kumi na mbili na nusu alichomeka simu yake katika ‘charge’ na kuingia katika kazi yake ya facebook, kitu cha kwanza aliingia katika profile la member mmoja wa facebook ambaye ni rafiki yake pia moja kwa moja katika notes zake ambapo alikuwa na kawaida ya kuandika hadithi fupi fupi na usomaji wa hadithi hasahasa za mapenzi ndio ulikuwa ulevi mwingine wa Husna.

    “CHINI KIDOGO” Ndio hadithi aliyokutana nayo siku hiyo, hadithi hiyo ya kimahaba iliyokuwa inaelezea jinsi mwanamama alivyomnasa kijana mdogo daktari wa magonjwa ya kinamama katika himaya yake ya mapenzi kwa ujumbe wa simu uliokuwa unasema

    “naumwa chini kidogo”. Alianzia kichwani akasema chini kidogo ya kichwa halafu ikawa sio shingo lakini ni chini kidogo pia hakikuwa kifua mwanamama alidai ni chini kidogo, kijana akadhani ni tumbo lakini mwanamama akapinga na kusema ni chini kidogo, hakikuwa kiuno pia lakini chini kidogo……



    Simulizi hiyo sio tu kuwa ilimvunja mbavu bali kikubwa zaidi alijikuta akijiamini kuwa na yeye licha ya kuwa na umbo lisilokuwa na mvuto sana lakini angeweza siku moja kumteka mwanaume kimapenzi. Aliamini kuwa wanaume wanategeka tu bila kujalisha muonekano wa msichana.

    Akiwa bado anafanya tafakari ya jinsi mwandishi wa chombeza hiyo alivyopanga maneno hadi yakawa tendo linalosisimua uliingia ujumbe katika inbox yake.



    PETER: Hellow!! Umeamka my dear au ndio kama kawaida yako kulala masaa mia

    HUSNA: Hi! Mi nimeamka mapema leo kila weekend ninawahi kuamka ujue!!

    PETER: Wenzako Weekend ndo tunalala wewe unawahi kufanya nini?

    HUSNA: Hamna siwahi sana sema huwa naamka na kufuta vioo vya madirisha hapa nyumbani, mom anapenda niwe nafuta mimi. Hawa wasichana wa kazi naona hawajui vizuri kufuta.

    PETER: Ok! Nimekuelewa..vipi weekend hii unaenda wapi??

    HUSNA: Mi ntakuwepo tu bustanini najisomea vitabu vya hadithi, za mbele lakini maana waandishi wa bongo magumashi tu.

    PETER:Kwa nini hautoki? Au hayupo wa kukutoa mrembo!!

    HUSNA: Wapo wengi lakini mimi bila laki na nusu hujanitoa ujue! Sasa mi mtu na ki elfu hamsini chake ananipeleka wapi au ndio kuaibishana tu na kunichosha mtoto wa watu. Sipendi mie!!. Hao wengi ninaokwambia nd’o hao wa kielfu hamsini sijui kilaki khaa. Uchafu.



    Peter alibaki ameduwaa mambo yalikuwa kama yanaanza kumuwia magumu vile. Laki na nusu anaitoa wapi!!!

    “Mh!! Hivi kweli huyu Husna ni Level zangu au nimekurupuka??” alijiuliza Peter akiwa amehamaki.

    Alisahau kwa muda kama alikuwa anachat na Husna.



    HUSNA:Hellow! Mbona kimya au umelala

    PETER: Ah!! Hapana simu ilikata charge. Ngoja basi ipate moto tutaendelea baadaye!!!



    ****



    Umaarufu wa Peter Isuti katika redio mbalimbali za burudani ulimfanya asiamini kama anamkosa Husna hivi hivi.

    Ule umaarufu wake wa kwenye redio ulimpatia unafuu wa kuwanasa wasichana wengi sana kirahisi.

    Lakini kwa Husna akaona mambo yanakuwa magumu.



    “Hivi ina maana Husna hajui kama mimi ni Mkali wa Media? Kina Dj Fetty wananitaja kila siku hanisikii ama anazuga?” Peter akajiuliza huku akijitazama.

    “Au hamuoni Adam Mnchomvu na Dj Fetty nimepiga nao picha katika profile langu…” Peter aliendelea kushangaa kama vile ilikuwa lazima kila mtu amjue.



    Peter alikuwa amekata tamaa kabisa juu ya kumpata Husna, gharama zake zilikuwa juu sana naye Peter alikuwa na maisha ya kawaida sana ya 'chipsi kuku' mara moja moja.

    Lakini Husna huyu alikuwa ni matawi mengine kabisa ambayo Peter aliamini hawezi kuyagusa lakini aliendeleza ubishi wake bado.



    "Yeah! Nimepata jibu na hiyo pekee ndio njia" aliwaza Peter huku akichukua simu yake ya mkononi na kubonyeza namba kadhaa kisha akaanza kusikiliza inavyoita.

    "Ng’wadila mayo" alisalimia Peter kwa kabila ya kisukuma salamu maalum kwa mama mzazi.

    "Ng’wadila bhabha za Dar huko mwanangu!" alijibu mwanamke ambaye alikuwa mama yake Peter.

    Lafudhi yake ilikuwa inatangaza vyema kabila la kisukuma.

    "Mama mi sina pesa huku halafu hapa nilipopanga wanadai mara umeme, maji na bado hata nauli mi zinaniishia. Nyie mko kimya tu kama hamjui mi nipo shule huku" alianza kulalamika Peter, dhahiri alionekana kudeka sana mbele ya mama yake.

    "Pole mwanangu pole sana baba yangu, nimemwambia kaka yako yale mahindi tuliyouza atoe laki mbili akutumie, na utumie pesa vizuri mwanangu yaani pesa hakuna, we ukitumia hovyo hovyo shauri zako, unajua baba yako ni wa kushindia kilabuni analewa kila siku magongo yake na mimi nauza wanzuki na siku hizi tunauza kwa siri hawa sungusungu wanatuzuia kwa hiyo ukae ukijua huku Bariadi mama yako hana biashara usome Peter usomee umenisikia" alijieleza kwa kirefu mama Peter, maneno ambayo kiuhalisia yalikuwa mazito sana lakini kwa Peter yaliingia sikio hili na kutokea kule.

    Ni maneno ambayo kwa mwanadamu wa kawaida yangemaanisha kitu fulani lakini Peter hakuwa mwanadamu wa kawaida.

    Hakuwa na huruma kwa mama yake!!

    "Nimekuelewa mama, sasa mnanitumia lini hiyo pesa mi nateseka huku" aliongea kwa madeko Peter bila kujalisha ndevu alizokuwa nazo zilimaanisha kuwa amekuwa mkubwa na si mtoto tena. (amakweli mtoto kwa mama hakui).



    …"Una M-pesa si ndio hivyo"

    …"Ndio ninayo"

    …"Basi kesho atakutumia sawa"

    …"Haya mama asiache mi nateseka"

    …"Hataacha baba yangu vumilia kidogo sawa mzee" alijibu mama yake Peter kisha wakaagana na kukata simu.

    …"Yes! Kilo mbili hizo zinajileta nikijumlisha na ile fote inafika kilo mbili na arobaini" alijisemea Peter kwa furaha huku akitabasamu.

    Husna kitu gani!!! Huyu wangu tu. We ngoja!! Alijisemesha.





    * * *





    Husna hakuamini kilichokuwa kinamtokea.

    Hakuwahi kuwa katika hisia za namna hii tangu azaliwe, hakuweza kujieleza vyema katika nafsi yake juu ya kile anachohisi lakini baadaye akahisi kuwa ameanza kuzama katika dimbwi fulani la ajabu.

    Lilikuwa dimbwi la Mapenzi!! hisia za mapenzi zikaanza kumtawala, hali hiyo ilikuwa haijawahi kumpata katika miaka ya karibuni kwani aliamini hakuna mwanaume wa kuweza kumpenda kimapenzi alitambua ni kiasi gani hapendwi mtaani kwao kutokana na ubabe wake lakini baya zaidi ni mdomo wake mchafu. Nani wa kuzipooza hisia hizi sasa!!

    …"Husna mpendwa wangu leo haupo sawa kabisa kulikoni?" Heriety alimuuliza Husna siku alipoenda kumsalimia na kumkuta katika hali isiyokuwa ya kawaida. Husna jasiri alionekana kuwa dhaifu.

    …"Acha shoga yangu ni makubwa sijui madogo lakini ni ya kushangaza sana" Husna alianza kujieleza huku dhahiri akiwa hayuko sawia.

    …"Mh! Niambie jamani ni nini tena cha kukufanya hivi shoga yangu wewe??" alihoji Heriety kwa shauku.

    …"Mapenzi shoga mapenzi yananitesa mwenzio" alijibu Husna kidhaifu huku akijirekebisha nguo yake iliyotaka kumwanguka mwilini.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    …Heriety aliangua kicheko kikali na cha muda mrefu kilichozitesa mbavu zake katika mtindo wa raha na baadaye karaha hadi machozi yakamtoka aliamini kuwa hata siku moja Husna hakuwaza mapenzi hivyo aliamini Husna ameamua kumchekesha. Na kama alikuwa ameamua hivyo basi alikuwa amefanikiwa sana!!! Lakini mbaya zaidi Husna hakuonekana kuchekesha.

    …"Una utani wewe Husna ndio nini sasa kunivunja mbavu mtoto wa watu mie,we na mapenzi wapi na wapi?" alihoji Heriety huku akiwa anajifuta machozi kwa kutumia leso yake.

    …"Heriety najua itakuwia ngumu sana kuniamini lakini mh! Niamini mwenzio hata sijui imekuwaje lakini ndio hivyo nimeangukiamo lakini sijui nimepotea njia?" alijieleza Husna katika hali ya upole sana jambo lililomfanya Heriety aanze kuhisi kweli kuna jambo limemkumba Husna.

    …Heriety alianza kugundua kuna ukweli kutoka kwa Husna na kweli ilikuwa hivyo na alipata jibu baada ya maelezo marefu kutoka kwa Husna.



    …"Sasa shogangu mtu hata kumtia machoni bado unakurupuka tu eti umempenda na anavyoonekana mashauzi sana huyo,hapa shoga kazi unayo tena si kazi ndogo ni kubwa sana" Alianza kuzungumza Heriety baada ya kumsikiliza vyema Husna.

    …"Hilo sio tatizo shoga tatizo ni vile ambavyo nimejieleza kwake" alijibu Husna

    …"Kwani umejielezaje?"

    …"Aah! Kawaida tu,embu achana na hiyo mada lakini nikihitaji msaada nitakwambia tena" alikatisha maongezi hayo Husna na kuingia katika mazungumzo mengine lakini hakuwa na raha hata kidogo siku hiyo.





    * * *



    Mama Peter hakumwangusha mwanaye anayempenda siku iliyofuata asubuhi na mapema Peter alipokea pesa aliyoahidiwa na mama yake, furaha aliyoipata haielezeki hata kwa mbali,furaha hiyo ilikuwa imepambwa kwa picha ya Husna, Peter aliamini tayari anammiliki Husna kimapenzi kwani laiti kama angekubali ofa ya kutoka naye basi alikuwa amekwisha na angekubali kuingia chumbani basi ujanja wake ungeishia hapo.



    …"Hawezi kuchomoka mbele yangu, nimekutana na wangapi kwani? Pesa ndo kila kitu bhana" alijipa moyo Peter.

    Akiwa bado ana furaha kubwa na macho yake yakiwa bado yanaisoma meseji ya M-pesa iliyokuwa inamjulisha kuwa amepokea pesa mara simu yake iliyokuwa katika mtindo wa 'mtetemo' (vibration) ilianza kutememeka pale ishara ya kuwa kuna mtu anampigia. Ilikuwa ni namba mpya 07677790* iliyoonekana pale, Peter alisubiri kwa muda kabla ya kupokea ili ahakikishe yule anayepiga ni kweli amekusudia kupiga na wala 'habip'

    …"Huyu atakuwa bi mkubwa anataka aniulize kama nimepata pesa ah! Maza naye kwani anahisi kompyuta inakosea?" alilalamika peke yake Peter huku akiichukua simu ili apokee.



    …"Hallo!" alisikia sauti ya kike upande wapili

    …"Hallo mayo ng’wadila asante nimeipata" alikandamiza kabila la kisukuma harakaharaka akiamini yule ni mama yake. Kwani alimtegemea sana kuwa atampigia muda wowote kumjulisha juu ya pesa hiyo kutumwa.

    …"Oooh! Sory kama nimekosea namba I thought kwamba wewe ni Peter" badala ya kusikia jibu kutoka kwa mama yake Peter alipokea sauti nyororo ya kike ambayo ilipenya vyema katika tundu za sikio lake na ubongo kushindwa kutambua huyo alikuwa nani anaongea.

    Akiwa bado anatafakari anayeongea ni nani sauti ile iliendelea, "Mh! Usiogope kuniuliza mimi ni nani najua hunifahamu kwa sababu wewe sio Peter"

    …"Ah! Hapana mimi ni Peter jamani mimi ni huyo Peter kwani nani anaongea" alijikaza na kuongea Peter baada ya kuwa kimya muda mrefu. Sauti ya kike kwa Peter ilikuwa ni tatizo yaani ni kama alikuwa mtumwa wa wanawake wenyewe wazungu wanawaita 'womanizer' huyo ndio alikuwa Peter.

    …"Waweza kubahatisha unaongea na nani? Kama kweli wewe ni Peter" ilihoji kwa shauku sauti ile ya kupendeza. Peter akabaki katika zizimo!!!

    …"Dah! Sauti zinabadilika sana kwenye simu ujue naogopa kubahatisha si umesikia pale mwanzo nimedhani mama yangu" alijitetea Peter huku sauti yake ikitangaza heshima ya uoga kwa wanawake.

    …"Ok mimi naitwa naniii wa naniii bwana otea basi" kwa sauti iliyozidi kumuuma Peter uliongea upande wa pili.

    …"Ah! Jamani niambie basi mwenzio roho inadunda sana" alijibu Peter katika njia ya kujenga urafiki.

    …"Naitwa Husna, unanifahamu?" hatimaye alijitambulisha

    …"Nani? Husna? Yule Husna wa facebook ninayekufahamu au? Hebu ngoja ngoja nikupigie usikate Husna ah! yaani usizime simu sawa jamani mrembo" alipagawa Peter kusikia jina hilo lililotajwa haraka haraka akaikata simu ili yeye aweze kupiga.

    …"Mh! Sina salio" alishtuka Peter lakini upesi akili yake ikafanya kazi akabonyeza menyu ya M-pesa na kufuata maelekezo ya kuongeza salio kwenye simu yake

    …"Buku tano haitoshi ngoja niweke elfu kumi kabisa" alijiongelea Peter huku akiwa na haraka kana kwamba ile simu alikuwa anapiga polisi kuwataarifu kuwa amevamiwa. Ama labda nyumba inaanza kuungua na anataka kuwataarifu zimamoto.

    Peter alipomaliza kuijaza simu yake salio la shilingi elfu kumi haraka haraka akaipiga ile namba ambayo hata alikuwa hajai-save kwenye simu yake.

    …“Yeah! Peter mbona umenikatia simu yangu ulimaanisha nini labda” ilihoji sauti ya Husna ikionyesha kukereka.

    …“Samahani Husna ilikuwa bahati mbaya lakini eeh...mmh! Nisamehe” alikosa la kujitetea Peter.

    …“Sio bahati mbaya nimekusikia unasema eti unipigie kwani mimi mpuuzi kukupigia? Sio vizuri ulivyofanya, lakini yameisha, ndio mie ni Husna wa facebook” Alilalama kisha akayamaliza na kushusha pumzi ambazo Peter alizisikia vyema. Mhemko wa kimwili ukamwandama akajikuta akijengea picha uzuri wa Husna. Akajikuta katika matamanio ya hali ya juu.



    …“ Asante Husna,ehe! Habari yako lakini”

    …“Ni shwari tu sijui wewe mwenzangu”

    …“ Mi mzima pia lakini sio sana”

    …“ Ooh! Vipi unaumwa au nini tatizo”

    …“ Nimekumiss sana Husna unajua”

    …“He! Makubwa haya yaani unammis mtu hujawahi kumuona we kaka are you serious lakini au watania”

    (alijibu kwa nyodo za hali ya juu lakini alisema ukweli)

    …“Ah! Nimekumis kule facebook” Peter alijirekebisha lakini alijulikana waziwazi kuwa hakuwa na uwezo wa kujitetea.

    …“Usijali nilikuwa na mambo mengi ya kufanya ofisini kwa dady na kompyuta yangu amechukua mom kuna kazi anafanyia so nakuwa sipati nafasi ya kuingia mara kwa mara ndio maana nikachukua namba yako ili nikupe taarifa” Maneno hayo yakampumbaza Peter, kwa mara ya kwanza akajisikia faraja sana kuwa mdau wa mtandao huu wa kijamii, pia aliufurahia uamuzi wake wa kuweka namba yake halisi kuliko wengi ambao huwa hawaweki namba zao wazi katika profiles zao.

    …“Pole sana Husna pole, asante kwa kunikumbuka na je hii ni namba yako?”

    …“Yeah! Ni namba yangu ila mara kwa mara natumia airtel au simu ya ofisini kwa dady, sipendi usumbufu ujue.”

    …“ We mrembo Husna lazima usumbuliwe kubaliana na hali yenyewe, mimi pia nakaribia kukusumbua kwani nimeteseka imetosha sasa.

    …“ Ok. Naingia ofisini nakutakia siku njema young boy.”

    aliaga Husna na kukata simu)

    …"Mh! Amemaindi nilivyoanza kumuingia au vipi,ah! Petr umekuwa na haraka Peter vipi papaa Peter eeeh!! Umeharakisha sana..papara hazitakiwi Peter.” Alijilaumu Peter lakini akakosa adhabu yoyote ya kujitwika.

    …"Dah! Halafu ameniita young boy ndio anamaanisha dogo au niaje...ina maana Husna ananizidi umri au hizo pesa zake zinampa kiburi? We ngoja nikimuweka kwenye kumi na nane zangu atajuta kuniita dogo..kisa mrembo ndo ndo anishushe hivi?"aliendelea kujikaripia na kujiapia mwenyewe Peter mtoto wa Isuti huku akimtukania Husna mama yake pasipo hatia yoyote.

    …Peter alikuwa amepania!! Alihitaji kumwonyesha Husna kuwa yeye sio tu kuwa ni mkali wa media bali ni zaidi ya hapo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Husna mtoto wa uswahilini huyu mwingi wa mashauzi na asiyekuwa na mvuto mbele ya wanaume lakini aliyeyaishi maisha yake kama malkia sasa alikuwa amenasa katika penzi la Peter. Uongo aliokuwa amemwambia ndio ulimkosesha raha kabisa, alishindwa ni kwa jinsi gani angerekebisha kauli zake ili hatimaye aweze kumpata Peter. Na siku wakikutana pasiwepo na mshangao.

    Hamu yake kwa Peter ilimpelekea kuchukua namba ya simu ya Peter kutoka katika mtandao na kuamua kumpigia. Maongezi yake na Peter kwa njia ya simu yalimpa picha kwamba Peter naye tayari alikuwa amempenda lakini alimpenda kwa sababu ya picha nzuri iliyokuwa facebook. Pabaya hapo!!

    "Mh! Hivi akikutana ma Husna mimi wa kiukweli ukweli wakati ana mategemeo ya kukutana na mrembo hasahasa hivi hatazimia au kufa kabisa mtoto wa watu mie nipate kesi ya mauaji ya maksudi....hivi sisi ambao hatuna mvuto ndio hatuna haki ya kupendwa au? Hapana nasema hapana lazima nifanye mapinduzi nasema hivi Peter utake usitake utanipenda tu hivyohivyo..kwani kitu gani sina ambacho wanawake wenzangu wanacho!!!...mh! Lakini mi naye kiukweli mvuto sina" alijiongelea kwa ghadhabu Husna huku akimalizia kwa upole baada ya kuwa amekata simu ya Peter. Mambo yalianza kumuwia magumu sasa!!!

    Husna alichekecha mawazo yake huku akifikiria ni mbinu gani atakazotumia kumtia Peter katika himaya yake tayari kwa kufaidi penzi lake. Kwa lengo la kukidhi haja zake.

    "Cha msingi hapa ni mimi nimuone kabla yeye hajaniona, huenda naye wenzangu na mimi tu hohehahe naogopa bure" aliamua Husna huku akifungua simu yake na kufungua mtandao wa facebook na kama kawaida yake akafungua sehemu ya notes za rafiki yake ambaye huwa anaandika simulizi za mapenzi, na macho yake yakakutana na hadithi ya "MAHABATI YA KIKURYA"

    "Mh! Ndo yakoje tena haya dah! Huyu mwandishi huyu ana mambo hebu ngoja nijisomee na nijifunze pia" aliongea hayo huku akijiweka vizuri kichwa chake katika mto uliokuwa pale kitandani.

    Baada ya kujiliwaza na hadithi ile, Husna akajikongoja mpaka katika sebule yao ndogo akawasha luninga na kisha deki ya VCD akatumbukiza CD aliyokuwa ameazimishwa na rafiki yake, ilikuwa ni filamu ya kimarekani inayoitwa COLLEGE ni katika filamu hiyo Husna alikuwa anajifunzia mashauzi ya mtoto wa kike huku pia akiiba vijimaneno vya kiingereza alivyowazugia rafiki zake wa facebook 'damn, amazing, awesome, pit, duces..LOL!, suck, hell, haters!' yalikuwa baadhi ya maneno ambayo aliyanyaka katika filamu na kuyaleta facebook. Wasiojua maana na wanaojua maana wote akawa amewateka. Peter naye akiwa mateka!!!

    Husna alizikuta meseji zaidi ya tano kutoka kwa Peter akiomba msamaha kama alimkera lakini alijifanya hazioni huku akiwa na kiburi kuwa mtandao wa facebook sio kama simu eti itoe 'delivery report' kwamba ujumbe uliotumwa umefunguliwa na kusomwa.

    "Ngoja nimzungushe kwanza kama alivyosema Fid q kwamba usimkubali haraka, lakini laiti kama ningekuwa mrembo kamwe nisingejichelewesha kwa Peter..yaani nahisi kabisa kuwa nampenda huyuuu!!" alijisemea baada ya kumaliza kusoma meseji za Peter zilizompagawisha zaidi.



    * * *



    …"Huyu Husna yani tangu akate simu siku ile hadi leo siku ya nane kauchuna dah aibu kweli sasa washkaji wakikomaa wamuone itakuwa vipi?" alijiuliza Peter baada ya kuona kimya cha Husna kimezidi.

    …"Huwa nawaponda wasanii wa bongo fleva wanavyoimba eti kusoma sitamani kwa sababu ya mawazo, sasa haya ndio yananikuta mimi siku ya tano sijatia maguu shuleni, halafu maza anadhani ninasoma mwanae" aliendelea kuwaza Peter kabla mawazo yake hayajaingiliwa kati na mlio wa simu, ilikuwa namba ngeni tena lakini sio ile ya Husna.

    "Halow!" alianza kuongea Peter.

    …"Ebwana Peter mambo vipi mkali, ishu niaje lakini Asha hapa naongea mpango mzima vipi katika kitaa chako?" ilijibu sauti ya upande wa pili kwa mbwembwe nyingi sana kama vile Peter na yeye walikuwa wanafahamiana sana.

    …"Najua hujanisoma lakini mi ni Asha wa facebook nipo pande za Kigogo upo wapi?" ilendelea kuchangamka sauti ile.

    …"Ok! Mambo vipi Asha nimekusoma sasa kumbe ndo mchangamfu hivyo kwenye simu mh! Mi sijaingia shuleni leo najiandaa kwenda ilala boma hapo kama vipi twaweza kuonana upajue kwangu aisee..halafu ile status yako ya jana…."

    …"Dah! Hata mimi naingia huku Boma naenda kwa mshkaji mmoja hivi kupiga stori tu, we waenda kufanya ishu gani?"

    …"Naenda kisaluni kimoja hivi kinaitwa Obama ni hapo karibu na stendi tu ya Boma naenda kupunguza nywele" alijibu Peter.

    Peter hakuwa na ratiba ya kuondoka kwake lakini simu iliyopigwa na mtoto wa kike ilimkurupua akaingia kuoga haraka, akachagua nguo nzuri anazoamini zinampendeza kisha akaweka poda kidogo usoni na baadaye akajaza lip bam mdomoni kabla ya kujimwagia unyunyu na kuangusha mzigo wa kofia kichwani pake. Mh! Alikuwa kama mtoto wa familia ya kitajiri na sio mtoto wa mama muuza wanzuki na baba mnywa gongo. Mjini hapa!!!



    * * *



    …Husna alijipanga sawa sawa na hatimaye akawa ameamua rasmi kuanza kumfuatilia Peter, kwa makini kabisa alipitia majina ya rafiki zake Peter katika mtandao ni humo alivutiwa na jina Asha Scooby kwani alikuwa ni rafiki wa Peter lakini mara kwa mara alikuwa haingii katika mtandao na picha yake ilikuwa ina mvuto kuitazama.

    …"Huyu anafaa sana" alisema Husna huku akiweka line mpya ya simu aliyoinunua na kupiga namba za Peter.

    …Kwa kutumia sauti tofauti kabisa tena ya kuigiza Husna alianza kumlegeza Peter hadi akajieleza alipo.

    Safari ya kuelekea kumwona Peter ikafuata. Husna akiwa anajiamini kabisa kwa mbinu mahususi aliyoitumia.



    Kelele za wananchi waliokuwa wameshtukia mchezo unaoendelea kwenye basi litokalo Mwenge kwenda Mbagala zilisikika kwa wingi watu waliokuwa katika mitumba ya eneo la Karume waliacha shughuli zao na kwenda kushuhudia sakata lililokuwa linaendelea ndani ya gari hilo. Foleni ndefu iliyokuwepo iliwapa fursa ya kujionea video ya bure.

    Ulikuwa mpambano mkali sana kati ya wanawake wawili mmoja alikuwa ni mnene sana huku mwingine akiwa wa kawaida kiasi chake japo mzigo aliokuwa ameubeba kifuani ulimfanya aonekane mbabe..

    Kwa tofauti ya maumbo yao ungeweza kudhani ni mtu na mama yake lakini katika mpambano ule hazikuwepo hizo sera ulikuwa ni ubabe ubabe kila mmoja alikuwa amemkaba mwenzake huku yule mnene akiwa amechubuliwa usoni vibaya mno, alitamani watu waachanishe lakini hakuna aliyekuwa na wazo hilo kila mmoja alifurahia burudani hiyo kasoro abiria wenye watoto kwani hali hiyo ilikuwa hatari sana kwa watoto wao.

    Muda ukazidi kusonga na mashabiki wakazidi kuongezeka. Ugomvi wa wanawake ni burudani tosha!! Lakini kwa hapa kuna mmoja alikuwa anaugulia maumivu

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    * * *



    Husna alipoambiwa na Peter kuwa atakuwa maeneo ya Ilala Boma saluni ya kiume iitwayo Obama alijiandaa upesi na kisha kuchukua gari liendalo Mbagala likitokea Mwenge, bahati nzuri alipoingia tu akapata siti kwani katika kituo alichopandia alishuka abiria mwingine.

    Safari yote mawazo yake yalikuwa ni kwa Peter, muonekano wake na je baada ya hatua hiyo nini kingefuata. Akiwa katika dimbwi la mawazo alihisi maumivu makali usoni.

    "We dada makucha yako hayo umenikwangua" alilalamika Husna akimwambia dada huyo ambaye alikuwa amekosa siti akawa amesimama. Mawazo aliyokuwa nayo Husna hata hakuwa amesikia wakati dada huyo alipokuwa anatukanana na kondakta alipokuwa analazimishwa kusogea nyuma, akili yake ilirudi garini baada ya kuwa amekwanguliwa.

    "Hebu na wewe nipishe huko, nimekukwangua nimekukwangua wapi sasa au mashauzi tu unaleta hapa. Ilimradi tu usikie naongea eeh!! Nitue bibie nitue kabisa ohooo. Teeena." Alibwatuka yule mdada mweupe.

    "Rekebisha kauli zako we mwanamke yaani unaniumiza halafu unakuwa mkali.we vipi?" alijibu kwa hasira kidogo Husna.

    "Ha! Nikurekebishie kauli wewe, kwa lipi, au gari la babako, hata kama mi hayanihusu" alijibu tena yule dada kwa mashauzi zaidi, garini pale hakuna aliyemchekea wote walimshangaa kwa kauli yake hiyo isiyokuwa na upole wala ustaarabu.

    Wengi waliamini kuwa atakuwa amelewa.

    "Haya pita ukae wewe mwenye hadhi" Husna alipisha kitini ili yule dada akae, watu wote wakabaki midomo wazi kwa hatua aliyofikia Husna.

    Bila kujua janja ya Husna yule mdada bila aibu akasogea ili akae.

    "Sijagombana siku nyingi hebu ngoja nimfunze adabu yake huyu mjinga akawasimulie wenzake popote ." Aliwaza Husna wakati anasubiri yule dada asogee.

    Kofi moja la nguvu lilisababisha gari zima wanyamaze kwa sekunde kadhaa, ni Husna kiujasiri alikuwa amemzabua yule dada, watu wakiwa bado hawajui nini kitaendelea Husna alituliza mikono yake miwili yenye kucha ndefu na kuanza kumkwangua kwa fujo. Kilio alichotoa hakikusaidia kitu, abiria wote walifurahia kichapo hicho.

    Alijaribu kujihami yule dada lakini Husna alikuwa mjanja tayari akaendelea kumtwanga kwa hasira. Ikwa kama filamu Fulani ya jitu kubwa kudundwa na mtoto mdogo.

    Fujo hizo zilipelekea wawili hawa kushushwa hapa eneo la Ilala Boma tofauti na Keko alipokuwa anaenda yule binti mwingine, ugomvi uliendelea hapa walipokuwa wameshushwa chini. Husna alikuwa hajaridhika bado.

    "Dah! Yule dada kama namfahamu vile" sauti ya kiume ilisikika ikielekea walipokua Husna na mgomvi wake.

    Husna aliponyanyua kichwa chake kuangalia mbele alikutana na neno "OBAMA BARBER SHOP" Kimya kikubwa kikamtawala akahisi nguvu zinamwishia mwilini.

    Akili ya Husna ilipata kumbukumbu kuwa ni sehemu hiyo hiyo ambayo Peter alisema atakuwa hapo kwa ajili ya kupunguza nywele zake.

    Hofu ilimwingia akawa mkimya hakutaka kuendeleza ugomvi ule. Hiyo ndio ikawa pona pona yake.

    "Mara ya kwanza nimemwona Kariakoo huyu demu kagombana na kondakta kisha akamzabua kofi akaangukia huko mbali watu tukacheka ile mbaya, dah! Ama hakika ana timbwilitimbwili huyu mwanamke" aliendelea kuongea kwa sauti ya juu yule kijana aliyedai anamjua Husna. Kwa jicho la kiwiziwizi Husna alimchungulia huyo aliyekuwa anaongea maneno hayo, hakuwa na haja ya kuendelea kumuangalia alimtambua mara moja!! Ndio alikuwa ni yeye.

    "Mungu wangu ni Peter tena ile cheni inaonekana katika picha yake facebook" alijiwazia Husna huku akizidi kutetemeka, na taratibu akitoweka eneo lile na umati ukimpigia kelele. Wengi wakimpa sifa za kijinga na majina mengimengi kuibuka. Mara Komando Suzi, steringi na mengineyo.

    "Jamani kumbe na wavulana ni wazuri hivi mh! Peter ni mzuri jamani" mawazo juu ya Peter yaliziba masikio yake na wala hakusikia hizo kelele za watu.

    "Peter lazima unioe kwa kweli we ni wangu hata kama mi mbaya vipi nasema" aliapa Husna huku akibadilisha line na kuweka ile ambayo ni ya kwake kabisa. Safari yake ilikuwa ya mafanikio lengo lake la kumuona Peter lilikuwa limetimia na sasa aliamini anaweza kuanza zoezi zima upesi.

    Husna alipanda gari za kurejea kinondoni akiwa na furaha moyoni. Kama kawaida yake hakuchukua muda mrefu akaingia facebook.

    "Dume jike kazini usiombe likukumbe" ndiyo status aliyokutana nayo, akaachia tabasamu huku akiifungua ajue kulikoni.

    "Mamaaa" alipiga kelele Husna na kushtua abiria ndani ya gari. Ilikuwa ni picha yake akiwa anatwangana na yule kibonge. Status hiyo ilikuwa imeandikwa na Peter mwenyewe. Status ilikuwa imeambatanishwa na picha. Picha ya Husna halisi. Alinipiga muda gani hii picha mama weee!!!

    "Vipi binti unaumwa?"

    "Hapana nimesahau kitu cha msingi sana" alidanganya Husna huku akijidai hana hofu kubwa.

    "Lazima zoezi lianze upesi kabla hajanifahamu" aliwaza Husna huku akifungua jina la Peter ili aweze kuchat nae. Haku like wala kucoment ile status. Alijifanya hajaiona.



    HUSNA. Mambo vipi mfalme?

    PETER: Aah! Malkia wangu mi mzima za kunigaya

    HUSNA:Hapana usiseme hivyo Peter sijakugaya, ni mambo mengi lakini kila siku Nakuwaza na hata usiku mmoja hivi nilikuota.

    PETER:Mh! Husna unasema ukweli dear wangu.

    HUSNA:Sina haja ya kukudanganya, hivi Peter we unafanya kazi au unasoma.

    PETER: Mi nafanya kazi na pia nasoma

    HUSNA: Aah! Unasoma wapi kwani??

    PETER: Nipo chuo cha biashara kinaitwa CBE kipo hapa hapa Dar.

    HUSNA: Hongera mpendwa mambo mengine vipi

    PETER: shwari tu nimekukumbuka sana nikawa naogopa kupiga simu yako

    HUSNA: mh! Sawa nikwambie kitu kimoja

    PETER: Niambie Husna.

    HUSNA: Jumamosi nataka tuonane mimi na wewe

    PETER: Husna unamaanisha kweli nitafurahi sana kwa kweli

    HUSNA: Yeah namaanisha kutoka moyoni nitakwambia muda sawa

    PETER:Sawa sawa Husna nina furaha hata kabla sijakuona

    HUSNA.Mh! Hata mimi nitafurahi sana na tutazungumza mengi

    PETER:Mh! Nadhani itabidi tuwe pamoja kuanzia asubuhi ndio tutalizika

    HUSNA:ni wewe tu Peter lakini usiwe na haraka nitakwambia sawa

    Peter hakuamini macho yake kama kweli amepewa ahadi hiyo na Husna. Jumamosi alipaona mbali kama vile ni mwezi mmoja mbele wakati zilikuwa siku tatu tu zimebakia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ratiba ya Peter ikabadilika akawa anakula milo miwili tu kwa siku ili pesa iendelee kuwa nyingi kwa ajili ya kumridhisha Husna, wakati mwingine alikuwa anadandia milo ya wenzake wakipika katika vyumba vyao ilimradi tu asije kuabika siku akikutana na Husna. Yale maneno ya Husna kuwa bila laki na nusu hatoki nyumbani yalimsumbua sana.

    Bila laki na nusu hujatoka na mimi!!! Peter aliyakariri maneno ya Husna siku chache nyuma walipokuwa wamewasiliana!!!! Kazi ninayo!!! Alikiri Peter mtoto wa Isuti mjukuu wa Mioyo mkali wa media, Peter hakuionea uchungu pesa iliyotokana na jasho la mama yake huko kijijini, wazimu wa mapenzi ukamsahaulisha yote, huruma kwa mama ikatoweka na sasa alikuwa anafanya analojua yeye na akili zake finyu. Ubongo ulikuwa umelala!!!

    Huku kwa upande wa Peter siku zikionekana kwenda taratibu sana kwa jinsi alivyokuwa na hamu ya kuonana na kimwana Husna aliyeaminika katika ubongo wake kuwa ni binti mrembo sana na anayetoka katika familia ya kitajiri sana, kwa upande wake yeye Husna binti fukara wa kutupwa aliyedanganya kuwa ni mtoto wa kitajiri aliona siku zikiwa zinakimbia kwa kasi kubwa sana na alikuwa hajajua bado atatumia uongo gani kumlaghai Peter ili awe nae katika mapenzi kwani aliamini kwa umbo lake na sura yake mbovu kamwe kijana mtanashati Peter asingeweza kusimama naye hata dakika moja kwa ajili ya mazungumzo kwani kwa dakika chache alizopata nafasi ya kumuona siku ile ya ugomvi alimuona kuwa ni mtu wa mashauzi ambaye vijana wa mjini wanamuita ‘sharobalo’ ni hapo moyo wake (Husna) ulikuwa umependa kwa dhati na kwa mara ya kwanza. Mara ya kwanza katika maisha yake

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog