Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

ROHO MKONONI - 1

 







    IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA





    *********************************************************************************



    Simulizi : Roho Mkononi

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Malumbano yaliendelea, ilikuwa kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya usichana kujikuta katika mkwaruzano na wazazi wake wote wawili,tena wote wakiwa wanayapinga maamuzi yake aliyokuwa amefikia. Ni kweli alikuwa na umri mdogo na hakudanganywa na mzigo wa matiti ulioanza kujaa kifuani pasina kumtia kero. Bado aliamini ana hadhi ya kuitwa ‘mtoto’ maana aliwategemea wazazi wake kwa kila kitu. Lakini katika jambo hili aliamua kusimama kidete kujitetea.

    Mama alikuwa haamini anachokisikia na mzee Kisanga n’do alikuwa akihisi yu ndotoni.

    “Mama…” aliita kisha akageuka na upande wa pili akiwa wima, “Baba….nawaheshimu sana na hilo wote mnalijua….lakini naomba katika hili muielewe azma yangu…muwe na utu katika hili baba…hivi leo Betty akifikia hatua ya kuwa yatima tutakuwa na furaha gani? Ndio undugu huu tunaojisifia kila kukicha. Undugu wa kushindwa kufanya jitihada kidogo tu kuokoa uhai….” Aliongea kwa huzuni kuu, sauti yake ikipambana na mikwaruzo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Mama Joyce….mwanao huyo.” Mzee Kisanga alimwambia mkewe katika namna ya kushutumu. Kisha akasimama ili aweze kuondoka.

    “Baba Joyce mume wangu, yaani leo hii amekuwa mwanangu na si mtoto wetu heee! Makubwa mbona haya.” Mama Joyce aliduwaa.

    Mzee Kisanga hakujibu lolote, akaingia chumbani kwake.

    Baada ya dakika kadhaa ulisikika mchakato wa baiskeli ikiegeshwa nje ya nyumba yam zee Kisanga.

    “Kaka yake huyo labda aongee naye vizuri, mimi sitaki kuamshwa na upuuzi wenu.” Mzee Kisanga kutokea chumbani alizungumza. Joyce na mama yake wakasikia. Walikuwa wanatazamana tu kama majogoo yaliyopigana na kukosekana mshindi sasa yamekosa la kuamua mshindi.

    “Ehee! Joy Joy mdogo wangu nini tena? Umekuwaje kwani eeh …mama Shkamoo.” James kwa papara na kiherehere alianza kuzungumza huku akitumia kiganja cha mkono wake kujifuta jasho. Alikuwa amevaa mavazi yaliyotangaza dhiki kuu.

    Joyce hakujibu kitu, mama yake akaamua kuzungumza.

    “Ameng’ang’ania sasa hatujui tumfanyeje tena.” Alisema kwa upole. James akaketi jirani na Joyce ambaye ni mdogo wake toka nitoke.

    “Joyce mimi sina elimu hakika, hata hilo darasa la saba sikumaliza mdogo wangu, lakjni hilo jambo unalotaka kufanya dadangu litakugharimu maisha Joy, hivi unataka mama na baba waanze kupalilia mashamba wenyewe ama shida yako umuue baba kwa presha. Joy kama chumvi inakosekana humu ndani, tutaitoa wapi pesa ya kukupeleka hospitali kwa ajili ya tiba.

    Hakuna serikali hapa Ukala nadhani unajua ni sisi kama sisi. Joy utatutia wazimu, mtoto wangu huko anaumwa nimeshindwa hata kupata shilingi ya kumnunulia Panado. Joy katazame nimenyonga baiskeli isiyokuwa na upepo ili nije huku mdogo wangu, tuhurumie basi. Eeh! Mambo mengine tumwachie Mungu….unanielewa kadadaa” James alimaliza kwa kumuita jina lake la utotoni. Jina ambalo humfanya Joyce atabasamu lakini siku hiyo hakutabasamu, hakika hali ilikuwa tete.

    “Mama!” Joyce aliita. Mama yake akanyanyua kichwa na kumtazama, Joyce akawahi kukwepesha macho hakupenda kumtazama mama yake akiwa anatokwa machozi. Kisha akaendelea, “Unakumbuka siku ile shambani……ulipojikata na jembe tukiwa tunalima?”

    “Nakumbuka mwanangu.”

    ”Mimi sikuwepo…..ni nani aliyefanikisha wewe kufika hospitali.” “Ni Betty lakini…”

    “Hakuna lakini mama niache niendelee kuongea…..” Joy aligeuka mbogo.

    “Ni Betty na la kuongezea ni kwamba alitumia ile pesa yake ya ada kulipia huduma hospitali.

    Nani anajua kama wazazi wake walimtukana, nani anajua kama pesa ile ndo ilikuwa akiba pekee ya wazazi wake?” alihoji. Hakuna aliyemjibu, wote walikuwa katika hamaniko.

    “Mtumbwi wa baba ulipovunjika ziwani, wavuvi waliozama kumtafuta ni ndugu zake…ina…” kabla hajaendelea sauti nzito ya kukaripia kutoka chumbani ilichukua hatamu.

    “Joyce nitakupiga bakora…nitakuharibu sura yako malaya wewe…nasema sitaki uniunganishe katika upumbavu wako huo..tena Joy ukome nasema…” Kimya kikatanda mzee Kisanga alikuwa ametetemesha.

    “Baba Joy usimuite mtoto Malaya lakini nini baba….”

    “Na wewe kimya pumbavu kabisa wewe na mtoto wako tena unganikeni basi tuone kama mtanipunguzia chochote, kwa hiyo mnafichiana tabia zenu sivyo….”

    Wakati mama na kaka yake Joyce wakiwa wameinama bila kujua nini cha kufanya, mzee Kisanga akiendelea kupiga makelele. Joyce alisimama kwa unyonge kama asiyekuwa na mipango yoyote kichwani, kwa kumtazama alikuwa ameathirika na kauli za baba yake.

    Mama yake akanyanyua kichwa akamtazama. Kilichofuata hapo hakuna ambaye alitarajia kingeweza kutokea. Ulisikika mchakato wa mara moja. Walipochelewa kwa sekunde kadhaa walikuwa wamempa nafasi Joyce. Nafasi hadimu kabisa. “We Joy wewe….njoo hapa nikikukamata Joy njooo!!” James, kaka yake Joyce alipiga kelele za hamaniko wakati Joy akionekana kwa mbali akiinyonga baskeli huku akiwa amesimamia. Mwendokasi alioondoka nao ni wanawake wachache wanaweza kuumudu.

    “Nini? Amekuwaje eeh!” sauti ya mzee Kisanga ikaingilia mshangao wa mama na mwana. Wakageuka na kumtazama bila kumjibu kitu chochote.

    Akatukana kikerewe huku akiingia ndani na laana zake zisizokuwa na mlengwa. Joyce alikuwa ametoweka.

    “Wewe na wewe…..nawapa masaa matatu aaah manne..namtaka mwanangu hapa….” Maajabu sio huyu alisema yule Malaya ni mtoto wa mama yake!!

    Mama Joyce na mtoto wake wa kiume wakastaajabu, lakini hawakusema lolote kwani tabia ya mzee Kisanga waliijua fika.

    Wakatoweka bila kuwa na uelekeo maalum. Huku kila mmoja akijitahidi kulaani kitendo hicho kuliko mwenzake.

    ****

    Ugumu wa maisha katika kisiwa cha Ukala wilaya ukerewe haikuwa simulizi mpya. Sema ilikuwa haizoeleki, si kwa wageni wala wazawa. Wapiga kura walitegemea kushibisha matumbo yao kwa uvuvi mdogomdogo ambao viongozi waliuita haramu, kilimo nacho hakikuwa uti wa mgongo wa maendeleo na badala yake mavuno yaliyopatikana yalitumika kama chakula tu baada ya mahindi kusagwa na jiwe la mkono na kuwa unga wa kupikia ugali na uji kwa watoto wadogo.

    Huduma za kiafya zilikuwa mbali sana huku wakazi wengi wa kisiwa hicho wakitegemea hospitali ya Murutunguru ambayo ilikuwa maalumu kwa ajili ya wanachuo na wanafunzi wa shule za sekondari Murutunguru.

    Licha ya huduma hizi mbovu ambazo zilionekana ubovu wake katika kipindi cha kampeni na mikutano ya kisiasa, bado wananchi walitembelewa na wageni waliojiita wataalamu na kuwahusia kuhusu kutoa damu kwa lengo la kusaidia ndugu zao na pia kwa akiba ya siku za usoni iwapo watakumbwa na jambo lolote litakalohitaji damu.

    “Changia damu sasa kwa uhai wako na wa jamaa zako” hiyo ilikuwa kauli mbiu iliyokaririwa hassahasa na watoto wa shule za msingi ambao viatu kwao vilikuwa anasa.

    Wazawa wakajipanga foleni na kutolewa damu hasahasa baada ya kupimwa uzito. Betty na Joyce walikuwa kati ya wasichana wachache waliohamasika na tungo hizo za kuburudisha kutoka kwa wataalamu. Walihamasika kwa sababu walikuwa na kumbukumbu ya baba yake Betty kupoteza uhai kwa kupungukiwa damu mwili, ikakosekana damu ya ziada ya kuongezewa. Baba yake Betty akaaga dunia huku akilalamika kuwa anakufa kwa sababu ya umaskini.

    Laiti angekuwa na pesa angekimbizwa mkoani Mwanza, huko angepata tiba madhubuti na hakika asingepoteza uhai.

    Kwa hiari yao huku wakitabasamu wakajitolea damu kwa ajili ‘yao na ndugu zao’. Lile tabasamu likatoweka zilipoanza kusikika tetesi kuwa wagonjwa wanauziwa damu kila wanapohitaji huduma hii. Ina maana hawa si ndugu zetu!! Betty na Joyce walijiuliza.

    Nani angewajibu…… Lisilokufika huwezi kulijua uchungu wake hadi likukumbe moja kwa moja. Zile tetesi kuwa damu ianuzwa tena kwa bei ghali; hazikuwa tetesi tena, mama yake Betty alikuwa matatani. Upungufu wa damu ulikuwa umemuweka katika kitanda cha zahanati ya kijiji.

    Lilikuwa tukio la kushangaza ambalo lilianzia shambani mfanowe tamthilia ya kufikirika.

    "Uuuuuuwiii" kilio kikali kilisikika kutokea shambani walipokuwa wanalima ilikuwa sauti ya mamake Betty akitoa kilio cha uchungu tena uchungu mkali..

    "Mamaaaa weeeee nakufaaaa" alipiga kelele huku akiliachia jembe lake, Betty alisikia kilio kile cha mtu mzima mbio mbio kuelekea alipokuwa mama yake huku Joyce naye akifuatilia nyuma kwa kasi lakini ajabu yeye (Joyce) ndiye aliyewahi kufika kabla ya Betty.

    Mama Betty alikuwa chini akilia kwa maumivu makali, damu ilikuwa inaruka juu kama mkojo wa mtoto mdogo aliyekuwa amebanwa muda mrefu na sasa uvumilivu umemshinda akawa ameuachia, jembe lilikuwa limejeruhi mguu wa mama Betty, bila kupoteza muda huku Betty akishangaa Joyce alivua blauzi yake ambayo zamani lilikuwa jeupe kwa ajili ya shule lakini sasa lilikuwa na rangi ya vumbi kutokana na shughuli za kilimo huku likiwa limechanika makwapani, alipolivua akabakiwa na sidiria ya njano iliyofubaa aakaizungusha kwenye mguu wa mama Betty kwa ustadi mkubwa kisha akashauri wajikongoje kwenda nyumbani kwa msaada zaidi.

    "Hapana Joyce, najiskia vizuri naweza kuendelea kulima." mama Betty alisema kwa sauti ya chini huku akiukunja uso wake kukabiliana na maumivu ya jeraha lile.

    “Hapana mama hapana hiyo damu haijakatika hata kidogo inaendelea kuvuja, twende walau tukaweke chumvi kidogo itasaidia japo kukausha" Joyce alipinga vikali akisaidiwa na Betty, wote hawa walitumia taaluma yao ndogo waliyopata katika somo la sayansi walipokuwa shuleni, mama hakuwa na la kupinga walielekea nyumbani huku ile shati aliyofungwa mama Betty ikizidi kuwa nyekundu. Wekundu wa damu!!

    Walipokelewa na wazazi wa Joyce kwa huzuni huku kila dakika mama Betty akitoa shukrani kwa Joyce kwa ukarimu na huruma aliyoonyesha kwake. Mguu wa mama Betty ulipofunguliwa hali haikuwa shwari bado damu ilikuwa inavuja kudhihirisha jembe lilikata mshipa mkubwa wa damu, hata chumvi aliyowekewa haikusaidia kitu zaidi ya kupotelea kwenye dimbwi la damu kimaajabu. Ilistaajabisha hakika!!

    "Nahisi nachoka na ninaishiwa nguvu….nahisi kizunguzungu jamani" alitoa kauli hiyo ya kushtua mama Betty ambaye alikuwa amejikaza kwa muda mrefu, hali iliyozusha hofu kwa kila mtu. Ilikuwa lazima wahofie kwa sababu vifo mfululizo vilitokea katika namna hiyo ya kustaajabisha.

    Bila kuaga Joyce alichomoka mbio na kurejea baada ya dakika 20 akiwa na baskeli, alikuwa anahema juu juu, jasho likiwa linamtiririka. "Twende hospitali" aliomba Joyce na wote wakatii amri mama Betty akapandishwa kwenye baskeli "Sidhani kama nitafika" alianza kulalamika jambo ambalo lilimrejesha Betty kwenye kumbukumbu ya kifo baba yake alijisikia upweke sana kwa mara nyingine alikuwa anataka kukubali mama yake afe kizembe, Joyce hakuacha kumfariji na kumtia moyo.

    ****

    Ilikuwa kama bahati usafiri wa mtumbwi kuvuka visiwa vya Ukara kuelekea Ukerewe ambao zamani ulikuwa wa tabu sana kutokana na wavuvi kuwa bize na zoezi la kuvua samaki na dagaa muda wote lakini tangu serikali ipandikize kampuni ya kigeni ya "Fisheries" kutoka Uswisi ambayo ilitawala maeneo yote yaliyosifika kwa kuwa na wingi wa samaki wavuvi wazaliwa wa hapo hawakuwa na shughuli za kufanya tena, hali ilikuwa ngumu sana. Hivyo mitumbwi yao wakaigeuza matumizi na kuwa ya kuvushia maskini wenzao. Kisiwa kimoja kwenda kingine.

    Ujio wa akina Betty na mgonjwa wao ilikuwa kama bahati ya mtende walipokelewa kama wafalme na kugombaniwa kama mpira wa kona tena katika dakika za majeruhi, gharama za mtumbwi uendao kasi kwa sababu ya kuwa na injini, shilingi 5000 iliwashnda hivyo iliwalazimu kuchukua mtumbwi wa kawaida wa makasia ambao kulingana na hali ya mama Betty ilikuwa ni kama kucheza bahati nasibu. Bahati na sibu na roho ya mwanadamu!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/"Mungu atakuwa nasi" baba Joyce aliwaambia wenzake wakati wakiijiandaa kupanda ndani ya usafiri huo.

    "Mama Joyce wewe rejea nyumbani ukatazame watoto na mji mimi na Joyce tutaongozana na Betty huko Hospital. Alianza kupakiwa mgonjwa, baadaye baiskel na kisha wakapanda watatu hawa kwenye mtumbwi ambapo wapiga makasia wawili walikuwa wametangulia.

    Mtumbwi wa kubeba watu wanne ulikuwa na idadi ya watu sita sasa.

    Utata!!

    "Ee Mungu weka mkono wako katika safari hii" Lilikuwa ombi la Joyce wakati mtumbwi ukiachia nanga yake.na makasia kuanza kupigwa kwa kasi sana. Alijua kuwa walikuwa katika hali ya hatari lakini wangefanya nini kama serikali haikuwa ikijali lolote kuhusu wao.

    * * * *

    Baba yake Joyce alinyonga baiskeli kwa kasi, mgonjwa akiwa ameshikilia kiti cha mbele kwa nguvu sana. Joyce na Betty walifuata kwa nyuma mbiombio kwa miguu huku wakiwa peku wote hawa dhumuni lao kufika mapema katika kituo cha afya cha Murutunguru.

    Pancha katika matairi yote haikuzuia safari kuendelea. Ilikuwa ni bora kuacha kuziba pancha lakini wawahi kufika hospitali. Nguvu zilikuwa zinazidi kumwishia Mama Betty japo damu zilikuwa zimekatika sasa kama ni kweli zilikuwa zimekatika. Huenda zilikuwa hazijakatika bali zilikuwa zinaelekea kuisha mwilini.

    Saa tisa alasiri walikuwa tayari chumba cha daktari, Joyce na Betty wakiwa hoi kwa kukimbia mwendo mrefu sana bila kupumzika wakati mama Betty alikuwa amepewa dawa aina ya PPF kwa ajili ya kukausha damu na Panadol kwa ajili ya kupunguza maumivu, hizo ndio dawa zilizopatikana hapo pamoja na Asprin, pilton na dawa mseto za malaria kwa uchache. Kwa waliotoka mjini wangejiuliza kama eneo hilo lina mwakilishi bungeni.

    "Mgonjwa wenu anaupungufu mkubwa wa damu na ni hatari kwa maisha yake" aliongea daktari huyu ambae vazi lake jeupe lilikuwa limechakaa sana huku likiwa na matundumatundu kama limeliwa na Panya. "Na kituo chetu hakina akiba ya damu mpaka Bugando Mwanza" "Kwa hyo tunatakiwa kufanya nini?" alihoji.

    "Kama hamwezi kwenda Mwanza kuchukua au kama yupo wa kujitolea atoe kuokoa maisha yake" "Nitajitolea mimi" alijibu haraka Baba Joyce. "Damu yako ni kundi gani??" aliuliza daktari. "Mh! sifahamu kwa kweli" alijibu

    "Haya nifate huku ukapime kwanza" palepale alisimama daktari akifuatiwa kwa nyuma na Baba. Joyce hadi chumba chakavu kilichoandikwa kwa kutumia mkaa "MAABARA"

    "Mgonjwa wenu kundi 'O' na wewe ni kundi 'B' haiwezekani hata siku moja" alitoa majibu daktari baada ya kuipima damu ya mgonjwa na baba Joyce. "Tunafanya nini sasa tena Daktari?" alirudia kuuliza lile swali tena baba Joyce "Ni kama nilivyokwambia agiza kutoka Mwanza" alijibu kwa ukali wakati huu. Kijasho chembamba kikamtiririka babake Joyce, wakati huo Betty na Joyce walikuwa mlangoni wakisikia maongezi yanavyoendelea. "Sasa....aah! Mwanza mh!" "Ndio ni shilingi elfu thelathini tu chupa moja…." daktari alimwambia huku akikunakuna kichwa chake chenye mvi. Kisha akamalizia, “Nadhani hiyo itamwongezea siku za kuishi.”

    "Kama shilingi 5000 ya imetushnda itakuwa 30000?" alijiuliza baba Joyce huku akisimama na kutoka nje ambapo aliwakuta Betty na Joyce. Hakuwa hata na la kusema zaidi ya kuwakodolea macho yaliyokata tamaa kabisa.

    "Basi mimi nina dadu ya kundi 'O' niruhusu nitoe" alisema Joyce kwaq kiherehere akikumbuka majibu aliyopewa juu ya kundi la damu yake siku alipojitolea damu, jambo ambalo mzazi wake alipinga vikali kwa kuhofia usalama wa mwanae huyo mkubwa kutokana na umri wake kuwa mdogo..

    Mgogoro ukaanzia hapa na kusafiri hadi nyumbani, wazazi wakipingana na Joyce. Joyce akisimamia msimamo kuwa anaweza kutoa damu na kumwokoa mama yake Betty…. Huu ukawa utata ulioishia katika mtafaruku, Joyce akakimbia na baiskeli akiwaacha mama na kaka yake wakitukanwa…… Akakimbilia alikotambua yeye na akili yake………

    *****



    BETTY ni kama alikuwa amekata tamaa tayari, hakuna aliyemtegemea zaidi ya sala zake zisizokuwa na imani ndani yake. Anakumbuka aliwahi kumwombea baba yake aliyekuwa mahututi lakini bado alikufa. Sasa ni mama yake. Betty akajitayarisha kuwa yatima na bado huo utayari hakuuona kama unawezekana. Ataishi vipi sasa? Bila mama na baba….. Ulikuwa mtihani mkubwa kuliko…..daktari alingojea mama Betty avute pumzi ya mwisho, mwili ukabidhiwe kwa ndugu zake kisha ukafukiwe ama kuzikwa kama ingekuwa hivyo.. Baridi lililovuma kutoka usawa wa ziwa Victoria lilichangia zaidi Betty kutetemeka huku meno yakigongana kinywani, nguo yake nyepesi iliruhusu kila aina ya karaha, wakiwemo mbu. Kanga yake alikuwa amefunikwa mama yake mzazi ambaye alikuwa akiishi kwa chembechembe masalia za damu katika mwili wake. Maskini mama yule kabla ya kuwa kimya hakupata hata nafasi ya kusema neno la mwisho kwa mwanae. Labda neno moja lingejenga tumaini kuu la siku nyingi. Neno kutoka kwa mama mzazi. Umasikini ulichelewesha hata teknolojia kupenya katika kijiji hiki, simu zilikuwa anasa. Alimiliki daktari na matajiri kadhaa kutoka mkoa wa Mwanza waliojihusisha na uvuvi wa samaki. Hii ilisababisha hata jamaa wa karibu wa familia ya Betty wasiweze kupata taarifa. “Binti……” ilisikika sauti kutokea gizani, tayari ilikuwa saa moja na dakika kadhaa usiku. Betty akageuka na kukutana na kivuli kirefu, alipotazama kwa makini alikuwa ni daktari. Akapiga hatua kumsogelea. “Kuna mbu wakali sana hapa, unaweza kupatwa hata na Malaria….” Alisema kisha akamsogelea zaidi na kuendelea .. “…nadhani ukajiunge na watoto wangu wa kike ujibane hivyo hivyo walau asubuhi tupate jibu kuhusu mama.” Sauti tulivu ya daktari ilimsemesha Betty.

    Badala ya kujibu, Betty akaanza kusina kisha kwikwi. Maskini Betty alikuwa analia. Daktari akamsogelea na kukikumbatia kiganja chake cha baridi kilichopoteza uvuguvugu wa kike. Haikuwa mara ya kwanza daktari huyu kukipakata kiganja hiki. Mara ya kwanza alikuwa akimpa pole Betty baada ya baba yake kupoteza maisha katika vitanda vibovu vya zahanati hiyo pekee katika kisiwa cha Ukala. Kule kuguswa na daktari kisha kupigwa pigwa begani, Betty akaikumbuka taarifa ya kifo cha baba yake. Kwikwi zikazidi, kadri alivyokuwa anazibana na kujaribu kupambana nazo mabega na kichwa chake vilikuwa vinapanda juu na kushuka huku akitetemeka.

    “Pole sana binti…” daktari akatamka na hapo akawa amekifungulia kilio kikubwa kutoka kwa Betty. Daktari alitaka kumtuliza lakini akasita ili asije akamliza zaidi. Badala yake akamsogelea na kumnong’oneza.

    “Mama atapona usihofu..” neno hili kwa kiasi fulani likamrudisha Betty katika hali ya kawaida. Daktari akamkokota hadi nyumbani kwake, nyumba isiyokuwa na umeme lakini walau taa za kandili zilileta Nuru.

    “Mama Kezirahabi…..” aliiita daltari, sauti ya mwanamke kutoka jikoni ikaitikia kwa heshima kabisa.

    “Kuna mgeni wako huku..” alimalizia daktari na tayari mama kutoka jikoni alikuwa amefika. Daktari Kezirahabi akamweleza mkewe juu ya uwepo wa Betty kwa usiku ule, mama mkarimu akampokea kama mwanaye wa kumzaa, akampatia chakula kilichokuwa kimesalia. Betty akajilazimisha kula, mama yule akamtia moyo sana. Majira ya saa tatu akamwongoza katika chumba cha wasichana aweze kupumzika.

    Wawili hawa walipokelewa na mikikimikiki ya Panya waliokuwa wameutawala ukumbi baada ya wahusika kuwa wamesinzia. Jambo hilo halikumshtua Betty. Ile ilikuwa hali halisi ya maisha katika kijiji chao.

    “Lala na wenzako mwanangu….we Jeni, Jenii….” Mama alimtikisa msichana mmoja akainuka na kisha kumpa maelekezo. Wakajibanabana Betty akalala huku akikiri kuwa mama yule hakika alikuwa na upendo wa dhati. Upendo wa mama. Baada ya kandili kutoweka, vita dhidi ya mbu wakali ikafuata. Japo palikuwa nyumbani kwa daktari hali ya kimazingira ilikuwa utata. Cha kushangaza hao mbu alijikuta akipambana nao peke yake, wenzake watatu walikuwa wanakoroma.

    ****

    Jane ndiye aliyegundua utofauti asubuhi katika mwili wa mgeni waliyelala naye. Wadogo zake wawili hawakujua lolote juu ya afya ya mwanadamu. Alipomaliza kuwaandaa ili waende shule hakuweza tena kumezea suala la yule mgeni. Alikuwa anatetemeka sana wakati hapakuwa na baridi kali la kutisha. Jane mtoto wa kwanza wa daktari Kezirahabi akaifikisha taarifa kwa mama yake mzazi.

    Mama yule mwenye upendo akawahi upesi kule chumbani. Mama mkongwe aliyeolewa na daktari hakuhitaji vipimo kutambua kuwa binti yule yu katika mahangaiko mwilini akiibeba Malaria. Aliwaza hili, sit u kwa kuwa amewahi kuwashuhudia wagonjwa wa Malaria, bali kwa sababu usiku ule binti mgeni hakujipakaa mafuta yenye dawa ya kupambana na mbu waenezao malaria. Upesi Betty akanyanyuliwa, mama akautega mgongo wake Betty akapanda akazungusha mikono yake na kumkumbatia.

    Upesi akamkimbiza katika zahanati ya mume wake. Betty aliona kila kitu kilichokuwa kinaendelea lakini hakuweza kusema lolote. Kwa macho yake walipokaribia zahanati aliiona baiskeli ya kaka yake Jane. Aliitambua kutokana na bango lililokuwa likining’inia kwa nyuma. “MASIKINI HAPENDWI”…..Joyce akajaribu kutabasamu lakini hakuweza. Akaingizwa katika wodi, humo akakutwa mgonjwa mwingine akiwa amelazwa na ndugu zake wamekizunguka kitanda. Wodi pekee iliyokuwa wazi ni ya wanaume, mama akafanya maamuzi akamuhifadhi upesi kitandani na kukimbilia chumba cha daktari kwenda kumpa taarifa. Daktari alikuwa ametingwa na jambo lililohitaji uangalifu mkubwa. Bila kuvaa mavazi yoyote ya kazi yule muuguzi mstaafu akatwaa dawa na maji akakimbilia katika chumba alichokuwa amemlaza Betty. Betty akameza zile dawa bila kuchukuliwa vipimo. Dawa maalum kwa ajili ya kutibu Malaria ambazo ni daktari na mkewe walitambua mahali zinahifadhiwa. Baada ya masaa kadhaa hali ya Betty ikapata ahueni kiasi. Kisha kuweza kusimama kabisa baada ya kuambiwa kuwa mama yake mzazi alikuwa anamuita. Akakurupuka kutoka katika chumba kile akiwa na kiherehere cha kutaka kujua kama anaota ama ni kweli mama aliyedhaniwa kuwa atakufa amemuita. Hakika haikuwa ndoto lakini ulikuwa zaidi ya muujiza. Alitegemea kukutana na uso wa mama yake pekee lakini sasa haikuwa hivyo tena, alikutana na nyuso mbili zilikuwa zinatangaza uchovu waziwazi lakini bado zilitabasamu, lile tabasamu kutoka moyoni.

    “Betty!!!”

    “Joy!!!” Walisogeleana kwa kutoamini kisha wakakumbatiana….mama Betty naye akaungana nao katika kumbatizi hilo. Joyce alikuwa amempunguzia damu mama yake Betty kwa kulazimisha akipingana na fikra za mama na baba yake. Mama Betty alikuwa hai tena…..jeraha likiwa limefungwa kitaalamu na yeye akiwa wima tena. Alikuwa anaongea kama awali. Miguu ya Joyce ilikuwa imevimba sana, alikuwa amenyonga baiskeli kwa kilometa nyingi sana hadi kuifikia zahanati. Mikono nayo ilikuwa imeumuka…..lakini haya yote hakujali, alichojali ni uhai. Uhai wa mama Joyce. Na hakika alikuwa amefanikiwa kumuokoa.

    “Joyce mwanangu….Mungu akubariki mwanangu….Joyce umeniokoa mimi nilikuwa nimekufa Joy..Joy ulikuwa umeishika roho yangu….umeiponya roho hii…Mungu akubariki sina jingine la kusema mama!!” mama Betty alianza kusema. Maneno yake yakaamsha kilio upya. Mama Kezirahabi naye alianza kulia kwa sauti. Lakini kilikuwa kilio cha furaha japo furaha ambayo haikukamilika bado.

    Mshawasha wa kuonana na mama yake akiwa hai ulikuwa umemsahaulisha kabisa juu ya ile Malaria mwilini mwake, lakini baada ya damu kupoa na akili kurejea sawasawa kile kizunguzungu kikarejea upya tena, kichefuchefu na kichwa kikaanza kugonga. Malaria hii ya sasa ilicharuka na kumpelekesha haswaa. Mama Betty akaazima simu kwa daktari akapiga simu kwa ndugu zake mkoani Mwanza. Akamueleza juu ya hali ile ya hatari. Walau huyu ndugu alikuwa na uwezo kifedha. Hatua za upesi zikachukuliwa. Siku iliyofuata Betty akasafirishwa kuelekea Mwanza akiongozana na mama yake mzazi ambaye bado alikuwa na jeraha bichi mguuni. Walitamani sana kumuaga Joyce lakini haikuwezekana kwa sababu mzee Kisanga alikuwa amemfungia ndani baada ya kumshushia kipigo cha uhakika kwa kosa aliloliita utovu wa nidhamu. Mama Joyce alipojaribu kumtetea naye alibamizwa kofi moja tu lililompopeza uelekeo kabisa na kukomesha kiherehere chake. Joyce alikuwa matatani kwa kujaribu kuokoa maisha ya mama wa rafiki yake mpenzi….. Urafiki uliotukuka!!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Juma moja baadaye Betty mwenye afya kamili alirejea kijijini lakini si kwa lengo la kuendelea na maisha yale magumu. Mjomba wake kutoka Mwanza alikuwa ameamua kumchukua na kuishi naye. Marafiki wawili wakakumbatiana, wakalia kama kwamba kuna msiba wa mzazi mmoja wao.

    Ilikuwa ngumu kuamini kuwa wanatenganishwa wakati urafiki wao ukiwa umefikia pomoni. Hali hii ilimsikitisha hata mzee Kisanga, baba mzazi wa Joyce lakini aliendelea kuikunja sura yake kama kwamba hakuna lolote linalotokea pale. Hatimaye Betty akatoweka kama anayerejea baada ya masaa kadhaa lakini ikakatika miaka bila wawili hawa kuonana, hadi Joyce akakiri kuwa wasingeweza kuonana tena, hasahasa baada ya mama yake Betty naye kutoweka kijijini kuelekea mjini Bukoba kuwasabahi ndugu zake kisha akaipanda meli ya Mv Bukoba aende Mwanza kumsalimia Joyce. Ile ajali mbaya isiyosahaulika nchini Tanzania, ajali ya meli ya MV Bukoba: na yeye ilimkumba akiwa ndani. Mwili wake haukuweza kupatikana, labda uliliwa na samaki ma vinginevyo…..

    Kizazi cha Betty kikatoweka rasmi Ukala. Katika namna ya kufadhaisha na kuumiza mioyo.

    Hii ilikuwa mnamo mwaka elfu tisa mia tisini na tano (1995)



    Kifo cha mama Betty kilipokelewa kwa simanzi kuu, lakini kwa kuwa hakikuwa kifo cha kwanza kuwahi kutokea. Nacho kilisahaulika kama vingine kisha maisha yakaendelea. Joyce akabaki mpweke kwa miezi kadhaa kisha akaizoea hali, akapata marafiki wapya. Alipobalehe na kuingia darasa la sita tayari alikuwa amemsahau Betty. Akabakia katika simulizi tu hasahasa wanafunzi walipokuwa wakikumbushana umahiri wake katika michezo ya riadha.

    “Angekuwepo Betty, tungeshinda….” N’do kauli zilizosikika. Kisha kupotea kama upepo maana huyo Betty hakuwapo tena.

    Ilikuwa siku ya mtihani wa kumaliza muhula wa kwanza na kwenda likizo ya mwezi wa sita. Likizo ndefu ya mwezi mzima. Joyce alikuwa ametoka katika mtihani akiwa na furaha sana. Licha ya usichana wake kuanzia utoto na sasa akiwa amebalehe hakuwahi kutoka katika kisiwa cha Ukerewe na kusafiri hadi mkoa ama wilaya nyingine. Sasa likizo hii alikuwa ana safari ya kwenda mkoani Mwanza. Mama yake mdogo aliahidi kumchukua kwa ajili ya kwenda kumsaidia kulea mtoto wake ambaye alikuwa na miezi minne tangu azaliwe. Joyce hakujali kuhusu ugumu wa kulea mtoto, alichotazama ni kupanda meli na kuufikia mkoa wa Mwanza, mkoa ambao alikuwa akiusoma tu katika masomo ya Jiografia na Historia. Safari hii ilikuwa iwe siku inayofuata asubuhi sana, kwani mama yake mdogo alitarajiwa kujiunga nao nyumbani siku hiyo ya kumaliza mtihani kisha kufunga safari siku inayofuata. Tofauti na siku nyingine za kufunga shule ambapo Joyce huungana na wanafunzi wengine kufanya lolote lile ambalo litaitangaza furaha yao ya kumaliza ngwe moja na kuhamia nyingine, siku hii alikuwa tofauti sana, hakuwa na hamu kabisa na vikundi vikundi, na hata makamu mkuu wa shule alivyotangaza rasmi kuwa shule inafungwa Joyce alitimua mbio kuelekea nyumbani ili aweze kujiandaa na safari siku inayofuata. Alihisi akitembea atachelewa kufika, basi akawa anaimba huku akiruka rukia huku na kule. Hatimaye akaikaribia nyumba.

    Tabasamu likachanua usoni alipoona begi jipya nje ya nyumba yao ndogo.

    “Mwee!! Mam’dogo kafika huyo.” Joyce alijisemea, kisha kabla ya kupiga hatua zaidi akaikung’uta sketi aliyokuwa amevaa na kisha kuichomekea vyema blauzi yake. Halafu akasita kujirusha rusha akawa anatembea kwa ustaarabu. Akafika mlangoni akajikoholesha, maana kuna wakati mama na baba yake huwa na faragha hivyo anahofia kuwaingilia. Kimya!! Hakuna aliyesema neno lolote. Akaanza kujiimbisha nyimbo zisizokuwa na mantiki yoyote ili kutambulisha marejeo yako kutoka shuleni, waliomo ndani waweze kumsikia na kumlaki kama itafaa. Nyimbo hazikumshtua yeyote.

    “Au wameenda kisimani….” Alijiuliza tena. Lakini akajikuta kama kuna sauti inamsihi kuwa kisimani hawawezi kwenda na kuacha begin je. Joyce akajikongoja akaufungua mlango huku akisindikizwa na neno ‘hodi’ neno lisilojibiwa na mtu yeyote hadi pale jicho la Joyce liliposhuhudia dimbwi la damu katika sebule yao isiyokuwa na marumaru wala sakafu. Aliyelizunguka dimbwi lile alikuwa ni mwanamke wa makamo. Alikuwa ameuma meno yake kwa maumivu makali sana, mikono yake ililikumbatia tumbo lake na uso wake ulifanywa wa kutisha na yale macho ambayo yalikuwa yamekodolewa. Joyce alidondosha bila kutambua kalamu zake pamoja na rula chini. Hivyo hivyo bila kujua nini anafanya akajikuta anapiga yowe moja kubwa sana huku mikono yake ikiwa imekipakata kichwa chake. Kisha historia ikabadilika……

    *****

    Kifanya NJOMBE, 1998.

    Mwanafunzi mwembamba, si kwa kuzaliwa bali lolote lile linalohusiana na hitilafu kiafya alikuwa akitetemeka. Meno yakigongana kinywani, wanafunzi wenzake hawakupoteza muda wao kumtazama, kila mmoja alikuwa na mambo yake anayofahamu mwenyewe. Nguo zake mpya zilizolizidi umbo lake zilimfanya asikitishe zaidi kumtazama, kichwa chake kisichokuwa na nywele nd’o walau kingeweza kuushawishi umati wa wanafunzi kumtazama kwa jicho la kuibia kutoka mbali. Maana wasichana walikuwa katika harakati za kushindana mitindo ya nywele lakini mwenzao hata hakuonekana kuhangaika na mambo hayo. Alishangaza.

    Msichana mmoja aliyetembea kijivuni alijikwatua huku macho yake yakipepesa huku na kule. Na kila alipoangaza huku na kule wanafunzi walizidi kujikita katika majukumu yao nje ya darasa. Macho yale yanayopepesa kwa shari na midundiko ya kijivuni hatimaye kituo kikawa mita hamsini kutoka mahali alipokuwa ameketi msichana mwembamba akisota na baridi.

    “Yaani wewe wenzako wanadeki madarasa, wengine wanafyeka nyasi wewe ambaye hii shule ni ya baba’ko unaota jua sivyo bosi!!” ilisikika sauti ile kali kwa uzuri kabisa. Macho ya wanafunzi yakahamia tena katika kuwatazama wawili hawa, bila shaka lilionekana kama jambo la kushangaza sana kwa sauti hii kukoroma kisha yeyote yule anayeambiwa asiruke upesi na kujitetea ama la kukimbilia mahali anapoelekezwa. Lakini leo ilikuwa tofauti.

    Sauti ililazimika kurudia mara ya pili.

    “We mtoto una kiburi eeh!! Yaani mimi naongea……..” akaikata kauli yake ile kwa muda kisha akapiga hatua kubwa kubwa akamfikia yule msichana mwembaba, “…halafu wewe mjinga umekaa umeridhika” akaimalizia kauli yake kwa kofi zito lililotoa mlio mkubwa sana na kuwaduwaza wachache kwani wengi kati yao walikuwa wakiitambua vyema shughuli ya dada yule.

    “Mi mge…ge…ni dada!!” hatimaye yule msichana mwembaba ambaye hakujishughulisha kupambana na dada yule alijitetea kwa sauti ya kulalamika huku kwa mbali akiugulia maumivu.

    “Mgeni?..mgeni hapa kwa mama yako nimekuuliza, shule alijenga baba yako hii pumbavu wewe…..ujinga ujinga mwingine uwe unamfanyia mama’ko nyumbani sio hapa…..hili ni jeshi. Bastard!!!” alizidi kupayuka yule dada, sasa alikuwa anaiweka sawa fimbo yake ambayo ilikuwa imehifadhiwa kiunoni. Hapa sasa wengi walimuonea huruma msichana mwembamba kwani kilichokuwa kinaenda kufanywa na dada mwenye mikogo kingemuharibia siku kabisa na huenda kumtia makovu kadhaa ya muda mrefu.

    Msichana mwembamba aliunyanyua uso wake vyema na kumtazama yule dada mkubwa kiumbo na mwenye madhari yote ya ujivuni wa maksudi, na uso wake ulitangaza mamlaka. Macho yalinata katika uso wake, hiyo sura aliwahi kuiona mahali lakini hakumbuki ni wapi. Alijaribu kumkazia macho huenda na yule mtazamwaji atamkumbuka lakini haikuwa hivyo. Akashtukia ghafla fimbo ikipenya katika shingo yake, mauymivu yakatambaa kuanzia shingoni kisha kuutawala mwili mzima, hakumbuki kama alipiga yowe kubwa kwani alikuwa ameendelea kumkodolea macho msichana yule ambaye midomo yake ilikuwa inachezacheza kama anayesema kitu. Hatimaye akamkumbuka……

    “We mshenzi ninarudia tena, ujinga ujinga kafanye kwa mama yako nyumbani sawa!!!” neno kutoka kwa dada mjivuni likamwingia msichana mwembamba masikioni vyema. Na hapo akili yake ikiwa imemkumbuka vyema yule dada, pigo lililofuatia msichana mwembamba akafanya jitihada za kupangua. Kama alipanga vile akafanikiwa kuikamata ile fimbo. Na hakuiachia, hapa macho ya wanafunzi yakazidi kuweka umakini, walikuwa kimya bila kushabikia lolote maana halikuwa tukio la kwanza shuleni hapo. Wengi walisikitika maana kuikamata fimbo ya dada yule akiwa anakuchapa ni kujihalalishia kung’atwa meno na kupigwa mateke.

    Mama!! Anamtukana mama yangu….mama yangu hakuzaa mtoto mjinga kama anavyodai, mama yangu aliwahi kusema kuwa nina akili sana…..mama hakuwahi kunipiga namna hii…hakuwahi hakuwahi……ANAMTUKANA MAMA!!!!! Msichana alifunguka akili na wakati huo yule dada mweupe alikuwa anajiweka sawa kwa shambulizi jipya.

    Ni hapa alipokutana na upinzani wa kwanza katika maisha yake ya uonevu, msichana mwembamba ambaye baridi lilikuwa limeukimbia mwili kwa kashkashi zile alimrukia na kumtia kucha za usoni kisha hakutuliza mikono akaanza kumkwangua. Puuu! Dada mweupe akaanguka chini.

    “Wewe mjinga unamtukana mama yangu…” alisema haya huku sasa akipiga bila kuangalia wapi anapiga, “hujui wapi alipo mama yangu unamtukana tu….umenichokoza pumbavu wewe!!” aliendelea kumdhibiti. Kwa kuwatazama ilishangaza sana ni sawasawa na ule ugomvi wa ‘Zena na Betina’ katika majarida ya Sani enzi hizo. Hapa sasa wanafunzi wakasogea kuangalia tukio hilo la kuuanza mwaka. Dada mjivuni alijaribu kufurukuta lakini hakufua dafu, sasa wanafunzi walipata nafasi ya kutangaza chuki zao, kelele za kuzomea zikachukua hatamu. Waalimu ofisini wakashtuka na kukimbilia eneo la tukio wajue nini kinawasibu wanafunzi.

    Lahaula!! Dada mkuu shule ya msingi Kifanya alikuwa amewekwa katika wakati mgumu na msichana mgeni shuleni pale, upesi waalimu wakaingilia, wakajaribu kumwondoa yule binti lakini alikuwa ameung’ang’ania uso wa dada mkuu, hata waliposaidiana ndipo walifanikisha. Dada mkuu alikuwa hatamaniki, waungwana wakawahi kumstiri, matiti yake makubwa yalikuwa nje..msichana mwembamba alikuwa amemrarua haswaa. Wakati wakijishughulisha na matiti mara sketi nayo ikaanguka, kumbe zipu ilishavurugwa na mikono ya dada mwembamba. Wanafunzi wa kiume wakashangilia kwa nguvu zote. Sio kwa kukifurahia kile kitendo bali kwa kufurahia ni nani kimemtokea. Msichana mwembamba akiwa bado na hasira kali alibebwa mzegamzega na kufikishwa ofisini. Ofisi ya mkuu wa shule.

    Akafungiwa humo.

    Ni huku macho yake yakakutana na picha ya yule dada aliyetoka kumjeruhi vibaya pale nje. Kumbe ile sura aliyodhani aliwahi kuiona mahali, mahali penyewe ni katika ofisi ya mkuu wa shule juma moja lililopita alipokuja kuandikishwa kama mwanafunzi mgeni.

    SIKU HIYO hapakuwa na jingine la kutetemesha kijiji zaidi ya jina la Keto. Keto alitajwa kila mahali kwa kitu alichomfanyia dada mkuu wa shule hiyo. Hata ulipojili wakati wa kuipokea shule ya msingi Namvura kutoka Makambako iliyokuja kwa ajili ya michezo, bado stori ilikuwa ileile, wageni walijikita zaidi katika kusimuliwa simulizi ile kwani hata wao walimfahamu vyema Jackline Mageta yule dada mkuu na ubabe wake. Jackline alikuwa amefunzwa adabu na msichana ambaye kila mmoja alitamani kumjua kwa ukaribu zaidi. Kwa wakati huu walimtambua kwa jina moja tu la Keto.

    “Bado wewe shoga…..na wewe watakudunda siku moja mwee!” msicha mmoja kutokea shule ya Namvura ya Makambako alimtania dada mkuu wao ambaye alikuwa mpole sana tofauti na Jack Mageta.

    “Wee mi sigusi mtoto wa mtu, kwanza nataka nimwone huyo Keto sijui ili awe rafiki yangu anifundishe mbinu.” Naye alijibu kimasihara, mambo mengine yakaendelea. Majira ya jioni mzee mmoja akiwa anaikokota baiskeli yake alikuwa akimlaumu msicha mwembamba huku wakiongozana kuelekea nyumbani.

    “Sawa amekutukania mama yako, lakini ulipompiga hayo matusi yamemrudia eeh!!” mzee alilalamika kwa sauti iliyoonyesha upendo. Msichana hakujibu zaidi ya kuendelea kulia kwa kwikwi. Msichana mwembamba alikuwa amefukuzwa shule rasmi bila mjadala wowote. Aliondoka akiwa ameukomesha ubabe wa Jack Mageta.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ****

    MAKAMBAKO

    Wanafunzi wakiwa kimya darasani, kilikuwa kipindi cha somo la Baiolojia na mwalimu alikuwa mkali sana. Hodi ikasikika kutokea mlangoni.

    “Nani wewe unayekuja darasani muda unaotaka….” Ilihoji kwa fujo sauti ile.

    “Mi mgeni…”

    “Mgeni? Mgeni nd’o hajui kama kuna kuwahi. Piga magoti hapo nje.” Alikoroma, wanafunzi kadhaa wakaguna. Mwalimu Simba akawageukia. Ndani ya dakika saba darasa zima kasoro msichana mmoja tu aliyepona, wengine wote walikuwa wameoga fimbo za mgongoni.

    “Na wewe nenda ukaniletee uthibitisho wa ugeni wako, mtafute dada mkuu akupe maelezo upesii.” Wanafunzi wakacheka, safari hii hakujali yule mwalimu kwani alijua kwanini wanacheka. Yule msichana aliyekuwa amepiga magoti nje akasimama upesi na kuanza kurandaranda, tayari aliiona hatari ya mwalimu yule. Ilikuwa kama bahati, akakutana na mwanafuzi aliyeagizwa chaki ofisini. Akamsimamisha na kuulizia darasa analosoma dada mkuu. Akaelekezwa!!

    Akastaajabu kuwa ni darasa lile lile alilokuwa ameomba ruhusa ya kuingia mwanzo. Hata alipokutana na mwanafuzi mwingine na kuelekezwa darasa lile lile alirejea na msimamo wa liwalo na liwe. Akaugonga tena mlango.

    “Dada mkuu yupo wapi?” ilihoji sauti ile.

    “Nimeambiwa anasoma humu mwalimu….” Darasa likacheka tena.

    “Dada mkuu!!” sauti ile ikaita. Yule msichana aliyenusurika kuchapwa fimbo za mgongoni akasimama, akatembea kwa maringo kama ilivyo kawaida yake. Blauzi yake safi na sketi iliyonyooshwa na soksi zinazowaka. Nywele ndefu zilizopakwa mafuta vizuri. Hakika alipendeza kumtazama. Akaruka miguu ya wanafunzi wanyonge walioketi chini na kwenye matofali. Akamuaga mwalimu kisha akatoka nje kwenda kuonana na huyo aliyedai ni mwanafunzi mgeni.

    “Wewe…ndi…..” hakuweza kuendelea na kauli yake, macho yake yakanata katika uso wa yule mwanafunzi mgeni, mwembamba na asiyekuwa nadhifu. Wakazidi kutazamana kwa mshangao wa aina yake. Hawakuwa wakifananishana tena, japo dada mkuu alikuwa anasita kubashiri kama ni kweli ama la!

    Lakini msichana mwembamba tayari moyoni alikuwa amekiri kuwa huyu ndiye.

    “Joy….Joyce……” aliita kwa kusitasita.

    “Betty!!!!!” msichana mwembamba hatimaye alitokwa na neno hilo. Wakakaribiana, Joyce akamezwa na mikono ya Betty ambaye alikuwa na mwili mkubwa kiasi. Lile joto la miaka kadhaa nyuma wakiwa wanafunzi wa shule ya msingi visiwa vya Ukala wilaya ya Ukerewe. Joto likatambaa katika miili yao. Lilikuwa joto la upendo, tena ule upendo wa dhati isiyofichika.

    Kilichofuata baada ya joto la upendo ni kilio ambacho kwa kila mmoja kilianza kama machozi pekee kisha kwikwi na hatimaye wakaharibu utulivu wa darasa. Wakaugulia kwa sauti za juu na hakutakiwa mtu kuwanyamazisha maana hakuna aliyeijua sababu. Yule Joyce aliyempigania marehemu mama yake Betty kwa kujitolea damu ili aweze kupona sasa alikuwa mbele ya Betty. Rafiki wa dhati ambaye alionekana kuwa katika muonekano ambao kidogo ulitia matumaini. Lakini yule Joyce, masikini kutoka Ukala alizidi kukondeana na kuonekana mdogo sana.

    Darasa halikuendelea, wanafunzi wakaanza kuchungulia madirishani, waalimu wakatoka nje. Wakabaki kuwatazama jinsi walivyolia huku wakiwa wamekumbatiana. Dada mkuu Betty, alimwongoza Joyce hadi chini ya mti.

    Hatimaye wakasimuliana yote yaliyotokea, Betty hakuwa na jipya sana maana kifo cha mama yake kwa ajali ya meli kilikuwa kinafahamika. Lakini upande wa Joy ilikuwa zaidi ya simulizi nzito sana hadi kufika hapo alipo kwa dakika ile.

    ”Joy inaniuma sana sikuweza kumuona mama kwa mara ya mwisho…. Ziwa Viktoria liliamua kunipa uchungu wa milele…lilimmeza mama yangu, na halikutaka kumtapika tena.” Aliongea huku akibubujikwa na machozi. Ni heri yeye alijua ni jinsi gani mama yake alipoteza uhai. Ama anajitambua kwa nini ni yatima…….

    Laiti angejua kuhusu upande wa Joyce!!!!..... Simulizi ya Joyce Kisanga ilianzia siku ambayo alikuwa amemaliza mitihani na anatarajia kusafiri kwenda Mwanza siku inayofuata. Akafumba macho na kuanza kusimulia kama kwamba vile anavyosimulia vipo katika giza lipatikanalo macho yakiwa yamefumbwa. Ilikuwa simulizi inayotisha sana na kwa yeyote mwenye moyo wa nyama angeguswa.



    Wakabaki kuwatazama jinsi walivyolia huku wakiwa wamekumbatiana. Dada mkuu Betty, alimwongoza Joyce hadi chini ya mti. Hatimaye wakasimuliana yote yaliyotokea, Betty hakuwa na jipya sana maana kifo cha mama yake kwa ajali ya meli kilikuwa kinafahamika.

    ”Betty inaniuma sana sikuweza kumuona mama kwa mara ya mwisho…. Ziwa Viktoria liliamua kunipa uchungu wa milele…lilimmeza mama yangu, na halikutaka kumtapika tena.” Aliongea huku akibubujikwa na machozi.

    Ni heri yeye alijua ni jinsi gani mama yake alipoteza uhai.

    Simulizi ya Joyce Kisanga ilianzia siku ambayo anatarajia kusafiri kwenda Mwanza.

    Akafumba macho alipomueleza Betty alichokikuta sebuleni. Mwili wa mama yake mdogo ukiwa umetapakaa chini huku damu zikimvuja. Baada ya hapo akapoteza fahamu na kuzinduka tena akiwa hospitali ya Murutunguru. Huko alipewa huduma zilezile za kawaida. Kisha akarejeshwa nyumbani.

    “Betty nilikuta umati wa watu pale nyumbani nikajiuliza kulikoni, nini kimetokea. Wazo langu la kwanza na kuu likawa huenda ma’mdogo atakuwa amekufa. Betty ni bora uwaze jambo fulani maishani na kisha lisiwepo kuliko kutoliwaza halafu unalikuta…Joy uchungu huu hautaisha kamwe rafiki yangu. Eti nakuta taarifa kuwa mama yangu………” Joy akaanza kulia Betty akambembeleza, akatulia na kuendelea, “mama alikuwa ameuwawa Betty….na bora basi angekuwa mama mwenyewe..na ma’mdogo ambaye nd’o ilikuwa mara ya kwanza kuja kijijini na alikuja kwa ajili yangu tu jamanii…ma’mdogo naye alifia sebuleni kwetu alifia eneo lile ambalo nilikuwa natandika mkeka usiku nalala.” Akakoma akajifuta machozi na kupenga kamasi nyepesi.

    “Sasa baba yupo wapi, hakika hilo ni pigo mpenzi” Betty alisema bila kumtazama Joy machoni.

    “Halafu ikamalizikia nyundo ya mwisho Betty wangu…na mzee Kisanga huyo unayeulizia yuko wapi alikutwa kichakani amejinyonga kwa kutumia kanga ya mama yangu….” Hapa sasa kilio kikawa kikubwa sana. Betty akafanya kazi ya ziada kumtuliza rafiki yake.

    Mwalimu mkuu akafika eneo lile lakini kwa uchungu wa waziwazi aliouona hakutaka kuuliza chochote naye akawaacha kwa muda.

    Joyce akajielezea juu ya mume wa mama yake mdogo alivyomchukua kwa ajili ya kumsomesha lakini chuki kutoka kwa ndugu walioweka imani za kishirikina mbele kuwa mkewe aliuliwa maksudi kwa ajili ya kafara zikasababisha amani kutoweka na baada ya mwaka miaka miwili akaamua kumleta Njombe kwa aliyetakiwa kumuita mjomba.

    Hapa akaelezea juu ya shule ya msingi Kifanya na balaa alilomfanyia dada mkuu.

    “He! Joy kumbe ni wewe uliyemuadabisha” hapa sasa Betty akatabasamu.

    “Aliniletea ujinga wakati nina uchungu. Hakika nilimwadabisha sikufichi…nilimsulubu, na wangenipa walau dakika kumi nyingine za nyongeza angewafuata akina mzee Kisanga huko mbinguni mi sijui.” Alijibu kwa jazba kuu.

    “Sasa mbona walisema ni Keto nd’o kafanya hivyo.”

    “Yeah kwa sasa naitwa jina hilo na hata baada ya kufukuzwa nimeondoka na jina hilo hilo kuja hapa. Hilo jina nimelikuta pale shuleni kuna mwanafunzi aliacha shule anaitwa hivyo. Joyce Keto.” Alimaliza maelezo.

    Sasa kidogo walikuwa wanatabasamu. Marafiki wa kufa na kuzikana. Kutoka Ukala Ukerewe sasa wanakutana, Makambako Iringa (sasa Njombe).

    “Nilidhani shule nimerudia mimi peke yangu kumbe na wewe mwenzangu umerudia, sa’hivi si tulitakiwa kuwa Kidato cha kwanza sijui cha pili” alisema Joyce, kwa pamoja wakacheka.

    Dada mkuu Betty akamuongoza rafiki yake wa dhati hadi mgahawani. Wakaagiza chai.

    Wakati wanakunywa chai, Betty alitumia fursa hiyo kumweleza maisha yake ya huko Makambako. Alikuwa akiishi kwa mjomba wake pia ambaye alimchukua baada ya mama yake kukumbwa na umauti. Alimchukua akiwa darasa la sita lakini walipofika Makambako alilazimika kurudia darasa la nne ili aweze kusajiliwa kwa jina lake la kuzaliwa.

    Alijieleza mengi sana juu ya maisha ya kawaida anayoishi na mjomba wake. Lakini walau alikuwa ana furaha na ukiwa ulikuwa umepungua.

    “Heri yako Betty, yaani mimi huku ni ilimradi, hebu nitazame…” alikata kauli kisha akamwonyesha Betty mwili wake jinsi ulivyopauka. Halafu akaendelea “maisha ni magumu pale yaani magumu sana, bora nilipokuwa Kifanya huko maisha yalikuwa yana unafuu. Sema namshukuru Mungu bora uzima.”

    Betty akaguna huku akibetua mabega yake. Akaimalizia chai yake wakasimama na kuondoka baada ya kulipia huduma.,

    Baada ya muda mrefu ule wa utengano, umoja ukaunganika huku wote wakiwa YATIMA!!

    Kubwa zaidi walikuwa wanafunzi wa shule moja. Shule ya msingi Namvura. Maisha yakaendelea, wawili hawa wakiwa darasa moja, darasa la sita katika shule hiyo.

    Joyce akiwa na miaka kumi na saba huku Betty akiwa anamzidi kwa miezi mitatu tu….

    Licha ya umri wao miili yao iliwabeba, si kwamba ilikuwa miili midogo sana la! Palikuwa na wanafunzi wakubwa zaidi yao.

    Miaka ile hapakuwa na utaratibu wa kumpeleka mtoto wa miaka minne darasa la kwanza kisa tu ana uwezo mkubwa wa kuelewa.

    Umri mkubwa ulipewa kipaumbele kwanza.

    Sina imani kama dhana hii ilimaanisha ukubwa wa mwili na umri nd’o wepesi wa kuelewa!!!

    Lakini ilikuwa hivyo kwa miaka ile.

    Miaka ambayo shule za awali ziliheshimika sana. Ilikuwa nadra kwa mtoto kutokea nyumbani moja kwa moja na kujiunga na darasa la kwanza bila kupitia shule ya awali.

    ****

    MAKAMBAKO IRINGA (Sasa Njombe), 2000.

    Redio iliyosikika kwa kukwaruza kiasi fulani kutokana na mawimbi kutokamatika barabara katika kijiji chao ilitangaza jambo lililomshtua mzee Kamese. Kama kawaida yake hakuwa mtu wa kukurupuka, akatulia aweze kusikiliza vyema taarifa ile kiundani. Hakika ilikuwa kama alivyoisikia awali.

    Hapo sasa aliweza kunyanyuka katika kiti chake cha kamba, akajinyoosha kidogo huku akiiweka vyema suruali yake kiunoni.

    “Mke wangu weeee!! ….mama watoooo” sauti yake ya kukoroma ambayo ilifanania na mtu ambaye amebanwa na kikohozi sasa anataka kukohoa lakini kabla ya kukohoa anajikuta kuna jambo la msingi la kuongea kabla hajakohoa.

    Lakini kwa huyu haikuwa hivyo, umri wake ulikuwa mkubwa sana. Na sauti nayo ikawa imefikia kikomo. Kwa jinsi alivyoita ungeweza kutarajia mkewe huyo anayemuita angeweza kuwa kikongwe asiyeweza kusimama wima tena na uso wake hautabasamu vizuri na meno yaliyotoka kichwani ni mengi zaidi ya yale yaliyosalia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilianza kusikika sauti ikiitika. “Bee mume wangu!” ilikuwa sauti nyororo na kama ingekuwa inatoka kwa kikongwe basi angekuwa kikongwe wa maajabu. Mzee Kamese akatabasamu mapengo yakaonekana, hiyo ni baada ya kusikia sauti ile.

    Macho yake yakawa makini, mlango ukafunguliwa, ukatangulia uso kuchungulia. Wakakutana ana kwa na mapengo yakawa yanatazamana na mwanya maridadi.

    “Mke wangu huyooo….mwanyaaa.” mzee Kamese akasema kwa sauti yake ileile ya kukwaruza. Mwanamke aliyekuwa mlango akajiziba uso kisha akaanza kulalamika, “Babu mi s’takiii, unanicheka na mwanya wangu”

    Mzee Kamese akacheka kwa sauti ya juu kidogo kisha akaketi tena na yule binti akaketi karibu yake.

    “Hapo unataka ugolo wako au mapombe yako, mi n’takuwa sikubusu tena shauri zako.” Kwa sauti inayoshawishi kuendelea kusikiliza hata kama anazungumza ujinga binti alilalamika kiutani.

    “Mh!! Hayo nilishaacha mke wangu, leo nina habari njema sana.”

    “Mwee! We nawe babu cha uongo ka’ nini habari gani?” aliuliza kwa kiherehere.

    “Nipe mji kwanza….” Babu akazuga, binti akajifanya kununa. Babu akamwita kisha akamnong’oneza.

    Binti akaruka juu kwa shangwe.

    “Babu usije kuwa unanitania babu…” alilalamika.

    “Betty mjukuu wangu, mimi nakuombea Baraka tele ufanikiwe kujiunga na kidato cha kwanza, naombea matokeo yako wewe na yule rafiki yako nani yulee…..”

    “Joyce!” Betty akamalizia, “Ehee huyohuyo, kati ya marafiki zako yule nd’o rafiki sasa mjukuu wangu achana na wale wengine sijui wana tabia za wapi wale….”

    “Babu kwa hiyo yapo wapi hayo matokeo.”

    “Wilayani pale kesho alfajiri kimbia mapema ukajionee kama umechaguliwa. Nakuombea heri mwanangu….haya nenda kaoshe vyombo maana najua nimekukurupusha huko…mtazame na masabuni yake mikononi huyooo” Akamalizia babu, mjukuu akatimua mbio huku akilalamika.

    Hakika ilifurahisha kuwatazama!!

    Saa kumi na moja alfajiri Betty akiwa ameuhifadhi mwili wake katika jaketi kubwa na zito kabisa, alikuwa akitembea upesi upesi, hakuwa akielekea wilayani la! Alikuwa anaelekea mahali pengine kabisa.

    Kiza bado kilikuwa kimeitawala anga lakini hilo halikumpa hofu. Alipoifikia nyumba aligonga mlango kwa sauti ya chini kidogo. Akamsikia mtu akijigeuza pale kitandani.

    “Nani?” sauti ya kukoroma iliuliza.

    Alikuwa ni Joyce

    “We Joyce wewe amka…amka Joy!” sauti ya Betty ilisihi. Mchakato ukasikika tena, kisha hatua zikafuata, mlango ukafunguliwa. Joyce alikuwa katika dimbwi la usingizi bado, usiku uliopita alichelewa sana kulala.

    “Joyce matokeo yametoka mwenzangu.” Betty alimweleza hatimaye, taarifa hii ikauondosha usingizi wake.

    Baada ya dakika kumi wawili hawa walikuwa barabarani wakitimka mchakamchaka kuelekea wilayani. Licha ya unene aliokuwa ameupata, bado Betty alikuwa na spidi katika kukimbia, Joyce alikuwa akimshangaa ni kwa jinsi gani Betty aliweza kukimbia kiasi kile wakati alikuwa amenenepa tofauti na alivyokuwa wakati wapo Ukala.

    Hatimaye wakafika wilayani, matokeo yakiwa na takribani nusu saa tangu yabandikwe. Macho yakisaidiwa na vidole yakaanza kutafuta majina yaliyokuwa ukutani.

    Wa kwanza kushangilia alikuwa Betty, na dakika chache baadaye furaha ikawa kubwa zaidi. Joyce Keto naye alikuwa amechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza. Furaha ikazidi kipimo, wote walikuwa wamechaguliwa kujiunga na shule moja ya upili. Kwa maana hiyo wataendekea tena kuwa pamoja.

    Ilikuwa siku ya kipekee, walijipongeza kwa kila neno waliloweza kusema kwa vinywa vyao. Siku hii ikaisha huku kila mmoja akiiona kuwa ya kipekee sana. Huenda siku ya kipekee kupita zote.

    Haikuwa kama wanavyodhani kuwa furaha yao itadumu kwa muda mrefu huku wakitimiza ndoto zao bila vikwazo vyovyote. Asubuhi iliyofuata Betty mwenye furaha akafunga safari tena kwenda nyumbani kwao Joyce. Nia ikiwa kumkaribisha nyumbani kwao ambapo alikuwa amechinjiwa kuku kama namna ya kumpongeza.

    Aliyefanya yote haya alikuwa mzee Kamese yule babu yake Betty aliyekuwa wa kwanza kusikia katika redio kuwa matokeo yametoka na sasa mjukuu wake alikuwa ameyaona tayari na alikuwa amechaguliwa kuendelea mbele. Kuku mkubwa wa kienyeji akaandaliwa, ubwabwa ukatiwa nakshi kadha wa kadha ili uwe na utofauti.

    Betty akafanywa mtu maalum siku hiyo, akaambiwa awaalike marafiki zake wasiozidi wanne. Sasa anaanza na Joyce yule rafiki yake wa dhati.

    Haikuwa mpaka afike nyumbani kwa akina Joyce la! Alikutana naye njiani, Betty alikuwa wa kwanza kumuona akajificha mahali ili aweze kumshtukiza. Lakini kabla hajafanya hivyo alisikia kilio. Joyce alikuwa analia.

    Betty akaghairisha mpango wake, akajongea taratibu. Macho yake yakagongana na yale ya Joyce. Wakatazamana kwa muda kisha Joyce akaangua kilio kikubwa baada ya Betty kumkumbatia. Kilikuwa kilio kikubwa haswaa.

    Betty akatumia busara na kumwongoza hadi chini ya mti. Joyce akasina kwa muda kisha akamsimulia Betty chanzo cha kilio chake.

    “Eti hawana pesa ya kunilipia ada, na kukaa nyumbani haiwezekani…eti Betty wanataka niolewe….” Hapa akashindwa kuendelea zaidi akaangua kilio upya. Betty akajikaza asiweze kutokwa machozi kwani angekosekana wa kumbembeleza mwenzake.

    Ilikuwa taarifa ya kushtua sana ambayo Betty hakuitegemea kabisa. Lakini Joy alimuhakikishia kuwa hiyo aliyoambiwa ni amri na wala si ombi.

    “Eti cha muhimu nimejua kusoma na kuandika hivyo niolewe eti huyo mume wangu ataniendeleza kielimu hapo baadaye…sasa bora hata huyo mume angekuwa mume kweli, yaani anao wake wawili na watoto ni mkubwa umri wa marehemu baba yangu. Betty mi sitakiiii, sitaki kuolewa Betty!!!” aligalagala chini Joyce huku akilia kwa uchungu. Betty ambaye naye alikuwa anatiririkwa machozi kimya kimya alifanya bidii ya kumtuliza. Lakini alikosa neno lolote la kumtuliza na kumpa matumaini. Maana yeye binafsi pia alikuwa ni yatima. Betty alikuwa akizilaani ndoa za mitaara, sasa rafiki yake anataka kuolewa huko!!! Atafanya nini sasa? Hili likawa swali gumu katika mtihani wa muhimu.

    Ghafla katika kujigalagaza huku na kule kitu kikachomoka kutoka katika nguo za Joyce, Betty akakikwapua mara moja na kukitazama vyema. Joyce akakoma kulia naye akawa anamtazama Betty.

    “Joy mpenzi……hii sio sumu ya panya hii? Ni yenyewe Joy unaipeleka wapi hii….” Betty akiwa ameduwqa alimuuliza Joy.

    “Bora nife Betty. Bora nife tu, kuishi na yule mwanaume kama mume wangu ni nusu ya kifo tu….alikuja nyumbani akiwa amelewa mapombe ya kienyeji, mbele ya watu wazima akaanza kunishika shika huku….sio kifo kile.” Alilalamika huku machozi yakimtiririka.

    “Joy….kama kweli una mpango wa kujiua na hukunishirikisha, kamwe nisingekusamehe katika maisha yangu, nisingekusamehe kwa ubinafsi huo uliotaka kuufanya. Kwa nini hukunishirikisha, kumbe mimi si rafiki yako Joy…kumbe sina maana kwako mimi si ndiyo…Joy unataka kujiua unikimbie mimi si nd’o hivyo….nasema na wewe Joy. Yaani kukuthamini kote huku, kila mmoja anatambua mimi na wewe ni kama mapacha. Leo hii unataka kujiua …haya jiue Joy nenda ukajiue na dakika moja baada ya kifo chako tutakutana mbinguni ili nikwambie kuwa sitakusamehe kamwe kwa jambo hilo. Kufa name nakuja huko.” Betty aling’aka kisha akaanza kupiga hatua aweze kutoweka. Ikawa zamu ya Joy kubembeleza huku akiomba msamaha.

    Hakika nguvu ya upendo inashinda nguvu zote, wakakumbatiana tena na kusameheana.

    *****

    SHEREHE hiyo ndogo ilipooza sana, Betty alijilazimisha kufurahi lakini kila alipogundua kluwa Joy hana furaha na yeye alifadhaika. Chakula kikalika na sherehe ikaishia hapo. Joyce akarejea nyumbani kwao, Betty akabaki nyumbani.

    Usiku huu ulikuwa wa aina yake, Betty ambaye sasa alikuwa binti mkubwa tu. Miaka kumi na saba si haba alikuwa akijaribu kuwaza kiutu uzima ni kipi afanye aweze kumsaidia rafiki yake walau kupata tumaini jipya.

    Aliamini kuwa familia aliyokuwa anaishi kamwe isingeweza kumsaidia kwa hili. Akamfikiria babu yake na kuwaza kuwa laiti kama angelikuwa na pesa angeweza kumsaidia, lakini hakuwa na pesa naye alikuwa anatunzwa tu pale.

    Akafikiria ni wapi pengine anaweza kupata pesa, hakupata jibu. Na hapakuwa na njia yoyote ya kufanya haya bila pesa. Kwani ukiweka ada pembeni, yalihitajika madaftari, vitabu na sare za shule. Mara akamfikiria Dulla, hapa hakuumiza kichwa chake, kijana yule asingeweza kumsaidia kwa lolote.

    Hatimaye akapitiwa na usingizi mzito bila kuwa na jibu sahihi. Cha ajabu asubuhi aliamka akiamini kuwa usiku alipata jibu. Na hili jibu alitakiwa kulifanyia kazi ili aone kama inawezekana kumpa furaha Joy.

    Lilikuwa jibu la maajabu sana, yeye binafsi alishangaa kwa nini lile liwe jibu!! Lakini likabakia kuwa jibu sahihi.



    Akafikiria ni wapi pengine anaweza kupata pesa, hakupata jibu. Na hapakuwa na njia yoyote ya kufanya haya bila pesa. Kwani ukiweka ada pembeni, yalihitajika madaftari, vitabu na sare za shule. Mara akamfikiria Dulla, hapa hakuumiza kichwa chake, kijana yule asingeweza kumsaidia kwa lolote.

    Hatimaye akapitiwa na usingizi mzito bila kuwa na jibu sahihi. Cha ajabu asubuhi aliamka akiamini kuwa usiku alipata jibu. Na hili jibu alitakiwa kulifanyia kazi ili aone kama inawezekana kumpa furaha Joy.

    “Aunt naenda kwa Joy…” aliaga baada ya kuwa amemaliza kazi zote za ndani.

    “Mh haya na huyo Joy wako sijui siku akihama itakuwaje…mnavyopendana mwee!” shangazi yake Betty alimwambia huku akitabasamu. Maneno yale yakampa hulka zaidi Betty. Kumbe jamii inatambua kuwa wanapendana!!! Hadi shangazi yake……..

    Betty akatoweka.

    ****

    ZOEZI la ufuaji lilikuwa linaendelea huku redio ikiwa inapiga kelele ndani bila mtu yeyote kufanya jitihada za kuizimisha, licha ya redio kupiga na mfuaji mwenyewe alikuwa anapiga mluzi usioendana na wimbo wowote ule.

    Mara mfuaji akahisi kuguswa sikio la kushoto akageukia upande wa kushoto, hola! Hakuna mtu. Akageukia upande wa kulia akakutana na muujiza. Muujiza wa aina yake.

    “Shkamoo mwalimu!” alisalimiwa na kiumbe yule ambaye alionekana kama muujiza mbele yake.

    “Marahaba…we mtoto wewe…hee karibu…karibu mpaka ndani.” Akakaribishwa huku yule mfuaji akiishia pale pale katika zoezi lake la ufuaji.

    Wakaongozana na kuingia katika chumba kile kimoja kilichotenganishwa na pazia katikati na kufanya mfano wa vyumba viwili. Mgeni akaketi katika kiti cha mbao kilichokuwa katika kona ya nyumba. Akaangaza huku na kule katika nyumba ile, mara akaona hereni, akaguna kidogo.

    “Ehe utatumia soda gani mrembo wewe.”

    “Hapana sitatumia chochote kile. Ninahitaji kukaa kidogo tu kisha niondoke.” Alijibu. Mwenyeji akalazimisha hatimaye akaomba aletewe Fanta.

    Baada ya muda walikuwa katika maongezi mazito na soda ikiwa mezani, bila kunyweka.

    “Kwa hiyo ni hivyo nina shida sana na sijaona msaada mwingine zaidi ya kuja kwako, walau unaweza kunishauri ama kunisaidia kama unaweza.” Alimalizia yule msichana.

    “Umesema unataka elfu hamsini…..lakini kwa nini umenifuata mimi eeh.”

    “Kwa sababu naamini kama unaweza kunisaidia utanisaidia.” Alijibu kwa ufupi.

    “Vipi kwanza Dula mzima.” Aliuliza lile swali kinafiki.

    “Yupo tu anakusalimia.” Binti naye alijibu kinafiki. Kwani alijua kuwa yule mwalimu alikuwa akimchukia sana Dula kutokana na kijana yule kumpumbaza kimapenzi Betty, wakati na yeye alikuwa akimuhitaji sana. Mada juu ya Dula ikazua ukimya wa sekunde kadhaa kisha mwalimu akatupia chambo, “Nitakusaidia lakini iwapo nawe utanisaidia Betty.”

    “Una maana gani?” aliuliza huku kichwani akitambua yule mwalimu ana maanisha nini.

    “Hali ya hewa leo Makambako baridi kali. Nilikuwa najiuliza sana nitaishi vipi leo kwani we husikii baridi?.” Swali hili lilimalizika Mwalimu akiwa mbele ya Betty.

    Alipoona Betty hana amani, akafunua lile pazia akakiendea kitanda akabenjua godoro akapekua kidogo akatoka na noti kadhaa. Macho ya Betty yakaona pesa kisha hapo hapo akaona chupi mbili za kike, akaguna tena kidogo. Mara yule mwalimu akamkabidhi ile pesa.

    “Mimi nimemaliza msaada wangu, bado wewe.”

    “Ticha ila…ila ni kwa leo tu na Dulla asijue tafadhali mwalimu.” Betty alisihi, kwa maana hiyo alikuwa amempa nafasi mwalimu kufanya lolote lakini kwa siku hiyo moja tu.

    Mwalimu yule ambaye hana ugeni kwa wasichana na mapenzi kwa ujumla. Alimvamia Betty na kumrusha kitandani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Betty alikuwa akiogopa sana kile kilichokuwa kinaenda kutokea, lakini ilikuwa lazima akipokee.

    Yote haya kwa sababu ya kutii ndoto yake juu ya kipi afanye kumsaidia rafiki yake kipenzi.

    ****

    JOYCE alikuwa anapalilia shamba la nyanya lililokuwa mbali kidogo na nyumba yao, alikuwa na masaa matatu tangu alipoanza shughuli hiyo. Kwa mbali aliwaona watu wakiwa wanaonyeshea vidole mahali alipokuwa, mmoja alikuwa ni msichana ambaye walikuwa wanaishi naye hapo nyumbani na mwingine alikuwa mgeni machoni pake. Hakujishughulisha kuwatazama akaendelea na kilimo hadi pale alipomuona yule mtu aliyekuwa mgeni machoni akijongea pale shambani.

    “Hee kumbe wewe Jesca, ulivyojitanda leo hata nikakusahau.” Joy alisema huku akitabasamu. Akaegemea mpini wa jembe lile huku akimtazama Jesca.

    “Shkamoo da’ Joy.”

    “Marahaba Jesca ehee wazima huko nyumbani.” Aliuliza

    “Wazima tu nimeagizwa hii..” alionyeshea bahasha ndogo ya kaki. Joy akatoka pale shambani na kumsogelea Jesca.

    “Nani kakuagiza?”

    “Da Betty.” Alijibu huku akimkabidhi kisha akaaga na kutoweka.

    Wakati Jesca anatoweka Joy alimuona kwa mbali mama mwenye mji akiwa anasogea kule shambani, upesi akaipachika ile bahasha katika nguo yake ya ndani kisha akaendelea na kilimo.



    SAA TATU USIKU.

    Joy akiwa amemaliza kuosha vyombo baada ya kuwa wamekula, tayari alikuwa ameoga. Sasa aliikumbuka ile bahasha ambayo kwa muda ule ilikuwa chini ya kitanda, akaifunua upesi upesi huku akijiuliza Betty kamwandikia nini maana haikuwa kawaida yao kutumiana barua.

    Akauendea mlango wa chumba chake akaufunga vyema, akaifungua bahasha ile kwa uangalifu mkubwa huku akishindwa kubashiri ndani ya bahasha ile kuna kitu gani.

    Alhamdulilah! Noti saba rangi ya bluu zikamwagika sakafuni, Joyce akatokwa na yowe dogo la hofu. Hakuwa amewahi kukutana na kiasi kikubwa cha pesa, noti za bluu, kwa malipo ya shilingi elfu kumi. Akazikamata vyema kabla hajakutana na karatasi jingine, hili lilikuwa limeandikwa maneno kadhaa.

    Akazificha zile pesa kisha akaketi kitandani, akaisogeza taa ya kandili ikamulika vizuri naye akaweza kusoma vyema.



    Dear, Joyce

    Naamini hapo ulipo hauna furaha hata kidogo na hakuna chochote cha kukuletea furaha. Naamini hauna ndugu wa karibu hapa Makambako zaidi ya rafiki ambaye ni mimi Joy.

    Sitaki kusema kuwa nalipa wema lakini ni heri iwe hivyo. Naikumbuka sura yako siku uliyojaribu kumtolea mama yangu damu. Ukaokoa maisha yake, ulipigwa kwa sababu yangu. Kamwe wema wako haufanani na chochote ninachoweza kujaribu kusema.

    Ningefanya nini Joyce walau ufurahi kidogo rafiki yangu mpenzi, kamwe nisingeweza kufurahi tena iwapo ungetoweka duniani bila mimi kujaribu kukupigania.

    Joy mpenzi wangu. Tatizo lako ni tatizo langu na limeniumiza kichwa sana. Unadhani ningefanya nini kama si kujaribu kukupigania. Ni kweli sina biashara na unajua kuwa nyumbani kwetu si matajiri na mbaya zaidi ninaishi kwa ndugu tu.

    Neno hili nakwambia wewe kwa maandishi haya kwa sababu sitaweza kusema kwa maneno na wala sitamweleza mtu yeyote tena. Nakwambia haya wewe ukiwa shahidi yangu kuwa sijawahi kuwa na mwanaume mwingine zaidi ya Dulla, nipo wazi kwako kwa kila kitu kama ndugu yangu wa dhati. Na unajua kuwa nampenda Dull asana. Lakini leo nakuandikia neno hili kuwa Dulla hana nafasi linapotokea tatizo linalokukabili wewe Joyce….” Joyce akachukua kanga yake akajifuta machozi, machozi ya furaha, nenohili kutoka kwa rafiki yake lilikuwa limemgusa sana.

    Kisha akaendelea….

    “Kama wewe ulivyompigania mama yangu na kuwanyima baba na mama yako nafasi basi name nipo hivyo.

    Naamini kuwa kuna kitu niliwahi kukwambia, kuwa mwalimu Japhari alikuwa akinisumbua na alikuwa anamchukia Dulla. Mimi na wewe tukaungana kumchukia pia.

    Lakini niseme tena hili, adui yeyote awezaye kumsaidia mwanadamu ninayempenda basi adui huyo huwa rafiki kwa muda. Joy ni wewe ninayekupenda, basi niliamua Japhari awe rafiki yangu, rafiki wa muda ilimradi tu wewe ambaye ni wa muhimu upate furaha walau kidogo. Hakika yule adui amenisaidia….amenipa hizo pesa.” Joyce akakoma kidogo kisha akajisemea “Jamani Betty, Mungu sijui umpe nini rafiki huyu….”

    Akarejesha macho yake katika barua.

    “Lakini alinipa kwa masharti, Joy yalikuwa masharti magumu, lakini kwa mema yote uliyowahi kunitendea sharti pekee ambalo linaweza kunishinda iwapo natakiwa kukusaidia ni kwenda kwa mganga tu nadhani unakumbuka kuwa nilikwambia siamini mambo hayo.

    Joy mpenzi, Mwalimu alinitaka kimapenzi. Nilijaribu kujitetea lakini nikajikuta katika maamuzi mawili tu, niondoke bila pesa wewe Joyce ukose furaha, ama niondoke na pesa baada ya kumpa penzi.

    Wewe ni rafiki na zaidi ya ndugu kwangu, sijisikii vibaya kukwambia kuwa Dulla akigundua yeye aniache tu Mungu atakuwa hajapanga lakini nafsi yangu ina furaha sana. Hiyo pesa Joy mbona shule tunaenda wote. Ifiche sana wala usishawishike kuitumia hata kidogo. Wewe acha tukazane tusome mpenzi si unajua huku Makambako sio kwetu tuna mtihani mkubwa sana wa kukikwamua kisiwa chetu cha Ukala.

    Nina ombi moja kwako. Sihitaji tukikutana uniulize jambo lolote juu ya kilichotokea.

    Uwe na amani Joy.

    Akupendaye kwa dhati, Betty.

    Joyce alikuwa analia kwa kwikwi. Kuna ladha ya upendo ilikuwa inawakilishwa na machozi yale. Alijizuia asilie kwa sauti kubwa, akafanikiwa. Akaikunja ile barua, akaihifadhi mahali ambapo ni yeye tu angeweza kuijua.

    ****

    KWELI, ilibaki kama walivyokubaliana. Mara moja!! Mara moja kweli!! Mwalimu Japhari alijaribu kwa kila namna kumshawishi Betty waweze kushiriki tena tendo lakini haikuwezekana, Betty alilichukulia jambo lile kana kwamba halikuwahi kutokea katika maisha yake. Joyce naye akaendelea kudumu na ile siri aliyoitunza kwa muda mrefu.

    Suala la ndoa likasahaulika baada ya Joyce kufanikiwa kuwashawishi walezi wake kuwa amepata mtu wa kumlipia ada, hivyo atasoma hadi kifato cha nne ndipo ataolewa na huyo bwana, ukatokea mvutano lakini hatimaye mshindi akawa Joyce.

    Muda ukafika Joyce na Betty wakaanza maisha mapywa katika shule ya upili Makambako. Ilikuwa furaha ya aina yake kwa wawili hawa kuwa pamoja tena.

    Maisha yakaendelea katika namna ya kutia moyo hadi ilipofika tarehe 19 mwezi wa tatu mwaka 2002. Siku isiyosahaulika kamwe katika vichwa vya watu wengi lakini iliwaumiza zaidi Betty na Joyce.

    ILIKUWA taarifa mbaya sana, Joyce alijiuliza anaanza vipi kumweleza Betty lakini hata kama asingemweleza bado tu angeipata kwa namna yoyote ile.

    Muda wa mapumziko, Joyce alimsaka Betty na kumvuta kando kisha kwa masikitiko makubwa na wasiwasi hadharani akamweleza jambo.

    “Mwalimu Japhari amefariki.” Alisema kwa masikitiko makubwa.

    “Wacha wee!! Amejifia bora kero zipungue maana alitaka kunigombanisha na Dulla yule” Betty alisema kwa shangwe kubwa. Joyce hakuungana naye…bali akaendelea kuongea. “amekufa kwa UKIMWI Betty…..”

    Hapa sasa Betty akatulia kidogo akapepesa macho huku na kule. Kisha akamtazama Joyce.

    Kwa mara ya kwanza tangu ampe onyo katika ile barua kuwa asimuulize chochote Joyce akavunbja masharti.

    “Betty….mlitumia kinga….” Akamuuliza..

    “Mhh Mhh” akakataa Betty huku akizidi kutingwa na hofu. Kisha akatia neno, “Hivi anaweza kuwa kaniambukiza na mimi eti!!” aliuliza swali la kipumbavu Betty. Joyce hakulijibu.

    “Kesho twende tukapime Betty wangu.” Joyce akashauri, shauri likapita.

    Siku ikaisha katika namna ya kipekee, Joyce na Betty wakiwa hawana furaha.

    Siku iliyofuata ilihitimisha kiza kinene, kiza kisichofahamika hatma yake. Kiza cha kutisha sana.

    Machozi hayakuwa tiba ya matokeo aliyotoa daktari. Betty alikuwa mwathirika wa ‘homa ya Makambako’, lile gonjwa hatari la Ukimwi lilikuwa limemkumba mwanafunzi huyu wa kidato cha pili.

    ‘CD4’ zake zilikuwa imara sana, hakutetereka kwa muda wote tangu afanye mapenzi na Marehemu mwalimu Japhary.

    Lakini mwezi wa sita mwaka huo huo 2002, ile siri haikuwa siri tena. Betty akajikuta yu katika kuugua ‘Ukimwi wa kishamba’ ule Ukimwi wa kuhara, kutapika na mkanda wa jeshi wa ajabu.

    Ilisikitisha kumtazama, ikiwa tu ulikuwa umemwona miezi kadhaa nyuma.

    Kila mtu alitambua kuwa siku za Betty zilikuwa zinahesabika. Hata Joyce alikiri kuwa rafiki yake kipenzi angekufa muda wowote.

    Kila siku alimtembelea nyumbani kwao alipokuwa anauguzwa. Siku ambayo hakumkuta Betty katika kitanda kile.

    Yakajirudia yaleyale ya Ukala. Betty alitoweka na hakuna hata mmoja aliyejua wapi amekwenda. Wapo waliosema kuwa Betty alikuwa marehemu tayari na wapo waliodai ameenda kutupwa katika mapori ya Malawi afie huko.

    Hakuna aliyekuwa na jibu sahihi, hata Joyce alibaki katika sintofahamu na nyumbani kwao hawakutaka kuulizwa lolote juu ya wapi alipo Betty.

    Maisha ya upweke yakarejea tena!! Shule nzima ikazizima. Yule mtaalamu wa somo la Kiswahili na hesabu katika shule yao alikuwa ametoweka. Kila mmoja alilalamika na kuweka hisia alizozifahamu yeye.

    Wengi walidhani kuwa Joyce anafahamu lolote kuhusu Betty lakini hakuna alilofahamu zaidi ya kutambua kuwa marehemu mwalimu Japhari ndiye aliyemuambukiza.



    MAWAZO na mtazamo wa Joyce kuwa marehemu mwalimu Japhari ndiye aliyemwambukiza Betty Ukimwi yaliingia doa baada ya kukumbuka kuwa yawezekana kabisa ni Betty aliyemwambukiza mwalimu. Aidha kwa kuambukizwa na Dulla, ama vyovyote vile.

    Joyce hakutaka kuendelea kuishi na kinyongo ndani yake, akaamua kumtafuta Dulla ili aweze kuzungumza naye kwa kina huku akiamini kuwa kwa kupitia majibu ya Dulla lazima ataujua ukweli tu. Alitambua fika kuwa Dulla hakuwa akitambua mahusiano yaliyowahi kutokea kati ya (Betty) na mwalimu Japhari hivyo ilikuwa kazi nyepesi tu kumvaa kwa nia ya kumshutumu kisha majibu yake yatauweka ukweli wazi. Shida kubwa ya Joy ni kuujua ukweli tu, ama ni Dulla ama mwalimu Japhari aliyemwambukiza Betty.

    Akiwa amefura kwa hasira kali za kukusudia ili kumtikisa Dulla na asiweze kudanganya chochote kitu. Joyce alifika nyumba ambayo alikuwa anaishi Dulla, kijana aliyekuwa akijishughulisha na shughuli unyoaji nywele (Kinyozi). Alikuta makundi makundi ya watu. Haikuwa kawaida kwa makundi yale kujijenga katika mazingira yale ya kuwakosesha uhuru wapangaji. Hata Joy hakuweza kukatiza. Kwa kutaka kujua nini kinajiri akalazimika kuuliza.

    Taarifa aliyopewa ililainisha zile hasira zake kisha ikamvika uoga na hofu kuu!!.

    Dulla alikuwa amejinyonga. Mbaya zaidi hakuacha ujumbe wowote ule. Ilifadhaisha na kushtua sana, mwili ukaota vipele vya baridi ghafla jambo hilo likamkumbusha taarifa aliyopewa siku anazinduka kutoka usingizi mzito na kuambiwa mzee Kisanga ambaye ni baba yake alikuwa amejinyonga.

    Joyce akajifanya hajui lolote kuhusu Dulla akatoweka bila kuaga. Huku kichwani maswali yakiongezeka badala ya kupungua.

    Na maisha yakaendelea huku sintofahamu ikiwa imetanda kuhusu Betty, je na yeye amejiua ama. Jambo hili Joyce hakutaka kukubaliana nalo kabisa, naye alijikuta akimlaumu sana Betty iwapo amechukua uamuzi huo. Maana ni huyo huyo Betty alimkataza katakata asifikie hatua ya kujiua kwa sababu ya matatizo. Leo hii yeye anajiua!!! Hapana. Aliongea peke yake Betty njia nzima bila kufahamu kuwa kuna watu walikuwa wakimtazama njiani kwa jinsi alivyofanania na mwendawazimu.

    Joyce licha ya mawazo yote yaliyomkatisha tamaa bado alijipa imani kuwa Betty atarejea tena machoni pake katika namna ya muujiza kama ambavyo alirejea baada ya kuwa ametoweka kijijini Ukala.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    DAR ES SALAAM TANZANIA, 2008.

    ALIZIWEKA nywele zake sawa huku akijitazama katika kioo kikubwa kilichokuwa mbele yake. Unywele ulikuwa mweusi haswaa!! Ukiongezea na mafuta aliyopakaa kiustadi zilizidi kuyavutia macho kutazama. Kisha akachukua mafuta ya kupaka midomoni akafanya hivyo kisha akaziminyaminya papi za midomo yake, vishimo kwa mbali vikaonekana katika mashavu yake, hakuwa mweupe na pia hakuwa akifanania na mkaa, lakini alikuwa na mchanganyiko wa rangi hizo mbili. Macho yake wakati akipakaa wanja yalifanya mfano wa kurembuka hivi kimahaba bila kusudio lake mrembuaji. Atafanyaje wakati amebarikiwa kuwa hivyo?

    Kisha akapiga hatua moja nyuma akajitazama vizuri, akafanya mfano wa tabasamu dogo. Vishimo vikachokoza tena, macho nayo yakarembuka. Alicheka kisha akajiwazia ‘Vimatiti vyenyewe vidogo halafu navaa sidiria mwee!’..hapa akacheka kicheko kikubwa kiasi. Nyama za mabegani zikavutika juu kidogo, nyonga zake zikatikisika.

    Ewalaa!! Ule mzigo alioubeba nyuma yake nao ukatikisika kistaarabu. Alivutia kimahaba lakini hakuwa na nia hiyo. Atafanyaje lakini?....akajitazama mara ya pili tena, kisha akachukua utuli na marasharasha akapakaza mwilini. Harufu mwanana ikatoka. Sasa alikuwa tayari.

    “Kidoti umependeza jamani….yaani wewe kila nguo inakukaa duh!” msichana mwenzake alimsifia. Ni nadra sana hii kutokea na ukiona hivyo kama huyo msifiaji hana unafiki basi umependeza kweli.

    Kidoti alikuwa amependeza.

    “Asante jamani..” alishukuru kwa sauti ya chini huku akipiga hatua, mkoba wake begani simu moja mkononi. Akaurudishia mlango vyema. Akaendelea kunyata. Alipokaribia mahali fulani akalazimika kulitua begi lake kisha akatoa kitambulisho chake akamwonyesha yule aliyekihitaji. Kisha akaendelea kupiga hatua zaidi akalifikia eneo tulivu kabisa mfanowe hakuna mtu ndani.

    Akatazama huku na kule akaketi mahali. Akafanya sala fupi kisha kwenye mkoba akaitoa kompyuta mpakato yake akaiwasha na kuendelea na kilichomfikisha hapo.

    Alitumia takribani masaa mawili, kisha akaamua kutoka. Njaa ilishaanza kumuuma na alipanga kuwa atakula baada ya masaa mawili.

    Akakusanya vifaa vyake, akatoka.

    Alipofika nje akaitazama anga, akajitazama kidogo jinsi alivyovaa kisha akafumba na kufumbua macho tena.

    Kidoti mimi jamani, amakweli Mungu mkubwa. Kisha akatazama kushoto kwake, akakutana na picha yake chakavu kiasi. Picha iliyomkumbusha alipokuwa mwaka wa kwanza wa chuo. Picha iliyomkumbusha mbali sana.

    Duh! Hadi leo ipo tu! Hawa nao jamani. Alilalamika na nafsi yake. Lakini hakufanya jitihada za ziada kuibandua.

    Pembeni ya ile picha akaona tangazo la mwanafunzi akilalamika kuwa amepoteza kompyuta yake ndogo akaweka aina na imepotea katika mazingira gani.

    Akalipuuzia tangazo lile maana yalikuwa matangazo mengi sana pale yanalalamika kuhusu kuibiwa. Hatua kwa hatua akazishuka ngazi za maktaba kuu ya chuo kikuu cha Dar es salaam. Alitambua fika kuwa kila mtu alikuwa akimtazama, wasichana kwa wivu na wanaume kwa matamanio. Hakujilazimisha kuwa vile lakini! Alivaa kiheshima sana na alipendeza.

    Wakati anapata Chipsi mayai, alikuwa akimwangalia kwa jicho la kuibia mkaanga chipsi ambaye alikuwa akijishughulisha kukaanga sahani nne za chipsi kwa wakati mmoja, mpishi huyu alimfanya Kidoti atabasamu kila akimtazama na hivyo kufanya mlo wake kushuka taratibu kabisa.

    Alikuwa katika mgahawa uliofahamika kwa jina maarufu la Daruso lakini kwa wenyeji tu, wale wageni walipaita Kontena.

    Haya yote yalikuwa yanatokea katika chuo kikuu cha Dar esa salaam.

    Baada ya Kidoti kuridhika aliukwapua tena mkoba wake akaelekea bomba lilipo aweze kunawa mikono yake, wakati ananawa akakumbana tena na tangazo. Sasa alijikuta akilisoma vyema.

    “Nipo chini ya miguu yenu jamani, hiyo laptop haikuwa ya kwangu aliyenipa ndiyo shule yake yote ipo humo ndani, irudishe basi mimi nitakupatia pesa za kununua laptop kama hiyo ama yenye uwezo zaidi ya hiyo. Nawaombeni muwe na huruma wanafunzi wenzangu, na roho wa Mungu awatawale.” Haya yalikuwa baadhi ya maneno katika tangazo lile.

    Kidoti akajikuta akilisoma mara mbili mbili, kisha akaichukua namba ya simu kwa ajili ya mawasiliano. Bila shaka kuna jambo alikuwa anafahamu.

    Alijikuta akiumizwa sana na maelezo yale, mwaka 2008 ‘laptop’ zilikuwa anasa. Na ilikuwa kwamba mmiliki lazima awe mwenye pesa zake haswa. Haikuwa tofauti sana na simu mnamo mwaka 2000. Aliyeweka tangazo kama alikuwa tayari kulipa gharama zote zile bila shaka alikuwa ana maanisha kweli kuwa shule yake yote ilikuwa ndani ya ile laptop.

    Kidoti akaamua kumsaidia kadri ya uwezo. Kwa lolote lile ambalo alikuwa anafahamu.

    Majira ya jioni akampigia simu. Mpokeaji akaanza kuzungumza na kuuliza ni nani alikuwa anazungumza. Kidoti hakutaka mazungumzo ya kwenye simu, akamwomba wakutane.

    Kidoti alikuwa anaishi hosteli za ‘HALL 3’ akajikongoja wakakutana katika vimbweta (sehemu zilizojengwa kwa ajili ya wanafunzi kujisomea) vilivyokuwa katika chuo cha Injinia (COET). Kidoti aliwahi kufika kabla ya mlengwa, jambo ambalo lilimkera sana kwani alitarajia kumkuta pale wazungumze kisha atoweke, hakupenda kukaa mahali bila shughuli ya msingi.

    Alingoja kwa dakika kadhaa akaagiza soda na kuanza kunywa taratibu, hatimaye simu yake iliita. Alipoipokea, mara akaliona kundi la wanaume wane waliovaa kisasa zaidi huku wakitembea kimagharibi wakimfuata mahali alipokuwa, hii ilikuwa kinyume na matarajio, lile tangazo lilimtanabaisha kuwa mtangazaji alikuwa mpole na mtaratibu sana. Lakini kabla hajawaza zaidi kundi lile likamfikia.

    Ni katika mgahawa huu ndipo alikutana na ISAYA mtoto wa AKUNAAY.

    Yalikuwa majira ya saa kumi na mbili jioni!!

    ****

    Wakati Kidoti anayeaminika kuwa mrembo haswaa ana anayependeza katika kila vazi akichukua nafasi pale katika mgahawa na vijana wane watanashati na wajivuni wanaoutukuza umagharibi.

    Upande mwingine wa chuo kulikuwa na mabishano, wasichana wawili wapashkuna na mwingine wa tatu mshakunaku walikuwa wakinong’ona katika namna ya kung’ong’a. mmoja alisimamia msimamo kuwa Kidoti alikuwa mrembo zaidi ya yule msichana aliyekuwa mbele yao akipata juisi, wengine wawili walikataa katakata na kusema yule binti wasiyemjua jina alikuwa anamwacha Kidoti mbali sana.

    “Angalia mguu…Kidoti ni mrembo lakini hana mguu, tazama nyonga…..mwanamke nyonga babu wee..Kidoti mbona wa kawaida tu kwa huyu…jicho lile bibi jicho tazama anavyomwangalia yule muhudumu..haya utaona lazima huyo muhudumu atageuka yaani lazima ngoja….” Mpashkuna aliwaambia wenzake, mara kweli akageuka nabii..muhudumu akageuka kumtazama msichana asiyekuwa na jina.

    Wakacheka kwa sauti za juu kisha wakagonga mikono.

    Wapashkuna na mshakunaku wakakubaliana kuwa yule msichana wasiyemjua jina alikuwa mrembo kuliko Kidoti.

    “Sema ujue anachokosa huyu dada ni kitu kimoja tu…..”

    “Kitu gani we nawe..”

    “Hana tabasamu….”

    Wote kwa wakati wao wakamtazama, hakika hakuwa akitabasamu hata kidogo, alikuwa kama amekasirika muda wote.

    Mshakunaku na wapashkuna wakakubaliana tena katika hili.

    “Chezea chuo wewe…utakuta amepata ‘Supp’ huyo….hiki nd’o chuo hakiangalii cha wewe ni mzuri wala babu yake nani..ukileta urembo tu kinakukanyaga.” Mpashkuna mmoja alitoa bango.

    Wakasimama wakimpita dada asiyekuwa na jina. Walivyompita naye ikawa zamu yake kuwatazama. Walisimama katika mwanga hivyo aliwaona vyema.

    “Mh! Sasa hawa nao wamevaa suruali ili iweje dah….vimiili hawana, vimiguu vyembamba, ona yule naye amevaa kimini na makovu yote yale.” Kwa mara ya kwanza tangu akanyage jiji la Dar es salaam, akafanya kicheko kidogo.

    Juisi nayo ilikuwa imemalizika, akanyanyuka bila kuwa na uelekeo maalumu. Akajiuliza aanzie wapi baada ya kupata hiyo juisi.

    Ilikuwa kama kuna nguvu inazidi kumvuta na kumtembeza huku na kule lakini hakupata kile alichokuwa anakitaka.

    Ni kweli alitambua kuwa anayemtafuta ni mwanafunzi katika chuo kile, lakini hakutegemea kama ni kikubwa kiasi kile. Chuo kilikuwa kikubwa haswaa na wakati mwingine alihitaji kupanda gari ili kuhama kutoka kituo kimoja hadi kingine.

    Alijipa moyo kuwa ikitimu saa mbili usiku akiwa hana hili wala lile basi atalazimika kufanya kama alivyofanya kabla ya kufika jijini Dar es salaam na aliamini kuwa atafanikiwa tu.

    Akiwa katika barabara pweke akihangaika huku na kule mara aliona kundi la wanaume wapatao wanne, alitambua mihemko yao wakiwa kama kundi, aliamini watamsimamisha na kuanza kumuuliza maswali ya hapa na pale lengo kuu likiwa kumtongoza.

    Ili kuwakwepa akakunja kushoto, huku akiwa hana uhakika na njia anayoifuata akakutana na bango la matangazo, akajitia kutingwa na shughuli ya kusoma kilichoandikwa pale.

    Bango lile lilikuwa limezuiwa kwa kioo chepesi. Katika kupepesa huku na kule mara akajikuta kweli amevutiwa na kilichobandikwa. Zilikuwa picha kadha wa kadha. Picha moja ikamvutia sana. Msichana mmoja akiwa amevikwa kikofia cha ushindi wa mashindano nguo yake ikizungukwa na ufito ulioandikwa ‘MISS UNIVERSITY’…huyu hakumaanisha lolote kwake, bali aliyekenua meno upande wa kuume. Alifanana na yule anayemuhitaji…..au duniani wawili wawili…..akatazama kama kuna majina yao, akaambulia kapa.

    Akiwa katika kujiuliza mara msichana mwingine naye akalifikia bango hilo la matangazo. Msichana asiyekuwa na jina hakutaka kulaza damu.

    “Samahani anti…..mambo”

    “Poa tu niaje?”

    “Shwari samahani…unaweza kuwa unafahamu jina la huyu dada….” Aliuliza huku akiishika ile picha.

    “Sio Kidoti huyo…”

    “Kidoti?”

    “Ndiye Kidoti huyu kwani vipi?”

    “Hilo ndo jina lake kabisa..”

    “Mi first year dada hata simjui zaidi ya hapo lakini ndo anajulikana hivyo….Hall 3 ndo anapoishi, ukifika humkosi. Sema mashosti wake sasa, wanamringia kama walimzaa vile.” Akajibu huku akiongezea na manung’uniko.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Msichana asiye na jina akakariri hilo jina la Kidoti na pia akakariri jingo la HALL 3.

    Hakutaka kulaza damu, akaendelea na shughuli yake usiku ule ule. Kweli akaipata HALL 3, na kweli akasikia kuna mtu anaitwa Kidoti lakini hakuwepo na alipouliza anarudi muda gani aliambiwa akmaulizie ‘utawala’ watamjibu. Akayakumbuka maneno ya yule dada kuwa marafiki wanamringia Kidoti.

    “Jamani…au sio yeye….mh! kweli abadilike hivi, hapana …lakini labda.” Alikata shauri kujiondokea pale kabla hayajawa mengine wakati alitahadharishwa mapema kabisa.

    Wakati anaanza kutoka akasikia sauti za kufoka huko nje, akatabasamu huku akimjengea picha huyo mfokaji kama aina ya mropokaji tena mshamba.

    Ýaani mamtu mengine sijui yakoje tu….yanadhani kila msichana wa ku..(akatamka lugha chafu)..hovyoo kweli, yaani ningekuwepo ningewachamba hao, pumbavu zao mianaume suruali!! Aliendelea kuwaka.

    “Kidoti huyooo.” Msicha mmoja akasema huku akiendelea na mambo yake. Msichana mgeni akasikia. Mapigo ya moyo yakaongeza mwendo wake.

    Sauti ikazidi kuyafikia masikio ya msichana asiyekuwa na jina. Mara macho yakawaona waliokuwa wakipayuka. Kumbe walikuwa wengi. Macho yakatembea kwa mmoja baada ya mwingine.

    Mwisho yakatua katika mashavu ya msichana aliyekuwa amefura kwa hasira. Shavu lile lilikuwa na kidoti cha kupendeza. Kundi lile likampita hivihivi huku akiona, akajipa ujasiri akalivaa kundi lile na kumshika mkono msichana aliyekuwa na kidoti.

    Wapambe wakamrukia.

    “Na wewe hebu tutokee hapa….shenzi zako..” akasukumwa chini akapepesuka huku na kule lakini hakuanguka.

    Yule mwenye kidoti akageuka, macho yao yakagongana. Waliachana umbali wa mita kadhaa.

    “Betiiiiiiiiiii!!!!” Kidoti akapiga kelele ya nguvu na kubwa kupita zote alizowahi kupiga hapo kabla.

    “Joyceeeee jamaniiiiiiii” mrembo mwingine aliyekaribia kuanguka baada ya kusukumwa akajibu kwa kupaza sauti iliyosindikizwa na mikwaruzo ya kutaka kulia…..

    Kimya kikatanda kila aliyekuwa na shughulia akaiacha na kuwatazama wawili wale. Wakakimbilia na kukumbatiana kwa nguvu.

    Ilistaajabisha, Kidoti akawa wa kwanza kupoteza fahamu kwa mshtuko kisha msichana asiyekuwa na jina naye akaanguka chini na kupoteza fahamu, naye pia kwa mshtuko na mengine yoyote yale ambayo atayasema yeye akizinduka. Mimi kama wewe tu sijui nini kilitokea.

    Lakini kwa kuwa wewe haukuwepo basi tulia nitakuhadithia!!!!

    Lakini wale mapacha wasitoka tumbo moja.

    BETTY (Msichana asiye na jina) na JOYCE (Kidoti) walikuwq wamekutana tena……wote wakiwa hai….

    Lakini kwa mara nyingine tena ni katika wajihi tofauti.



    Wawili hawa hawakuhitaji kukimbizwa hospitali ili waweze kurejewa na fahamu. Baada tu ya kupungiwa upepo wa haja na marafiki pamoja na kumwagiwa maji kiasi fahamu ziliwarudia. Wakaachwa watulie kidogo na kumbukumbu zao zikawakaa sawasawa. Hapa sasa hawakuhitaji kujibu swali lolote kutoka kwa mtu yeyote yule, walihitaji kupumzika. Lakini sio katika chumba cha hapo chuoni, Joyce Keto Kidoti alichukua taksi akamuamuru dereva akawapeleka maeneo ya River Side Ubungo, huko wakachukua chumba katika hoteli ya kisasa. Usiku huu ukawa wa aina yake!! Ulikuwa usiku ambao kila sentensi kutoka kwa aidha Joyce ama Betty ilichangamsha ubongo na kuulazimisha kufikiri kwa uyakinifu.

    Zilikuwa ni kumbukumbu za miaka sita iliyopita. Kumbukumbu za Makambako, kumbukumbu zilizotatanisha haswa. Na kisha ukazuka mtihani wa aina yake!! Mtihani ulioufanya usiku huu kuwa wa kukumbukwa tena!!! Mazungumzo ya awali kabisa Betty alimuuliza Joyce Keto, kisa cha kuwa amekasirika vile usiku ule na inakuwa vipi anakuwa na wapambe wengi vile.

    ******

    WANAUME wanaume wanaume aaargh!!! Alianza kulalamika Joyce. Betty akawa msikilizaji. Joyce alielezea juu ya kushiriki kwake mashindano ya urembo chuoni na kisha kuzua kizaazaa baada ya mshindi kutajwa mwingine wakati kila mmoja akitegemea kuwa Joyce Keto ama maarufu kama Kidoti atanyakua taji hilo. Mtafaruku huo ukampa jina kubwa pale chuoni, na akapata marafiki wengi japo sitakosea nikiwaita wapambe.

    Ni hawa waliokuwa kama walinzi wake, wakimfuata hovyo kila mahali. Huku wakijisahau kuwa wote ni wanafunzi tu wa pale chuoni. Joyce akamaliza kwa ufupi kisha akahamia tukio la jioni ile. Hili alilielezea kwa ghadhabu. Kama ambavyo hakutegemea kuwa mpotezaji wa vitu vile kuwa katika hali ya majivuno na ulimbukeni ulo’kubuhu kiasi kile, basi nd’o ambavyo hakutegemea kuwa yatazuka mambo ya ziada. Joyce alituliza akili yake wakati wale vijana wanne wanajongea katika kimbweta alichokuwa ameketi, aliwatazama kwa jicho la kuibiaibia akawaona jinsi walivyokusudia kuvuta macho ya watu kuwatazama.

    “Karibuni.” Aliwakaribisha. Wakaketi wote baada ya kumpa salamu kwa kumshika mkono. Joyce alitamani kuwaomba watoke abaki na mmoja lakini aliona hilo kama haliwezekani, halafu mbaya zaidi walipofika na kumtambua ni yeye wakaongeza majisifu. Kijana aliyekuwa mbele yake kwa kudhamiria kabisa akalegeza vishikizo vya shati lake.

    Ewalaa!! Mkufu wa dhahabu ukaonekana, laiti kama angekuwa msichana mwingine angeanza kuuvaa mkenge lakini Joyce Keto hakuwa msichana wa kawaida, huo aliuona ni ushamba. Akataka kusonya lakini akajikuta akiguna, akataka kuangalia kwa jicho baya lakini badala yake akajikuta akirembua jicho lake.

    Joyce hakujua kuuvaa uhusika wa kukasirika, suluhu yake ni kuvimbisha mashavu kisha anatokwa machozi. Mwisho wa mchezo. Joyce akapuuzia yote yaliyokuwa anaendelea. Akataka kuanza kujieleza jambo alilolifahamu, mara mmoja kati yao akatoa simu aina ya Nokia yenye kamera, ambayo kwa wakati ule ilikuwa katika chati. Hapa Joyce akashusha pumzi kwa nguvu bila kusema lolote. ‘Hivi wanadhani mimi wa bei rahisi hivyo!...pole yao maskini dah!’ aliwaza haya huku akijitahidi asizungumze kwa hasira. Hatimaye walianza maongezi, Joyce akaanza kujieleza lakini akakatwa kauli na mmoja wao.

    “Aaah! Sorry sister, yo know hatujafahamia bado walau majina something which is not good at all.” Mtumwa mmoja wa maisha ya kighaibuni akasema.

    “Naitwa Joyce” akawahi kujitambulisha kwa karaha.

    “Ben”

    “Simon”

    “George”

    “Isaya” alimalizia mwanaume wa mwisho ambaye kama ni mashindano ya ujivuni alikuwa anaongoza, ni kweli alikuwa amependeza lakini ujivuni ulimfanya aonekane mpuuzi tena.

    “Nafurahi kuwafahamu.” Alisema kwa kujilazimisha Joyce, kisha akaendelea na alichokusudia kuwaeleza, akawaelezea kwa pamoja ni kitu gani anafahamu kuhusu kompyuta iliyopotea, alishangazwa sana na umakini wao. Hawakuwa makini kabisa kumsikiliza alichokuwa akiwaeleza, labda kidogo Isaya alikuwa anasikiliza kitu japo naye kila mara alikwenda kupokea simu bila kuomba radhi.

    “Basi ni hivyo nijuavyo, kama bado haijatoka nje ya chuo basi ni mtu huyo niliyemshuhudia akitoweka nayo maktaba.”

    Alimaliza. Baada ya maswali mawili matatu yasiyokuwa na uzito ndipo wanaume hawa walipohamisha mada na kuibua mada iliyomkera waziwazi Joyce. Haikuwa mada mbaya, ilikuwa mada ya kuhusu mapenzi….na hapakuwa na ubaya mtu kuzungumza mapenzi, lakini walichofanya wanaume hawa ni kumtongoza kwa pamoja. Walimfanya kama changudoa mzoefu.

    Mara huyu amwambie hivi mara yule aseme hiki. Kwa akili zao waliamini kuwa Joyce atazenguka na ufajari wao. Kitendo cha kutongozwa na wanaume wanne ilikuwa ni dharau iliyopitiliza kabisa.

    Dharau iso’kuwa stahiki yake. Ni hapa Joyce alipoamua kuwatumia ujumbe marafiki zake wa kike ambao ni mcharuko haswaa. Wakati anawatumia ujumbe walimjibu kuwa walikuwa mahali wanapata juisi, akawasihi waende alipo wakamweleza kuwa wanaenda huku wakimtumia ujumbe wa ziada kuwa wamekutana na pacha wake kwa urembo. Walipofika wakatumia mbinu zao kumtoa Joyce katikati ya kundi lile, hapa ukazuka mtafaruku mwingine baada ya wanaume wale kudai kuwa kwa sababu rafiki zake Joy wametimia wanne na wao wapo wanne basi wagawane.

    Hapa ukazuka mcharuko wa ajabu kutoka kwa rafiki zake Joy. Mcharuko ambao uliwafanya wafike hosteli huku wakitukana matusi yote wayajuayo na Joyce akiwa kimya tu.

    Marafiki/wapambe hawa ni walewale wapashkuna na washakunaku waliokuwa wameketi jirani na Betty wakiujadili urembo wake huku wakiulinganisha na wa Kidoti Joyce Keto.

    Ni huku walipokutana tena mapacha hawa na kubadilisha simulizi ya usiku ule!!!! Joyce kidoti alimaliza ngwe ya kwanza ya simulizi. Betty alikuwa anatabasamu tu…

    “Ila umekuwa mrembo sana Betty jamani…” alimsogelea rafiki yake na kuanza kujidekeza katika mapaja yake kama mtoto mdogo. Kisha akaanza kulia akimlalamikia kwa nini aliondoka bila kuaga.

    “Yaani Betty jamani….nd’o ukaniacha pekee ukaniacha vile kweli Betty mimi mwenyewe huko….mi s’taki…..s’taki….” akazidi kudeka huku machozi mepesi yakimtoka. Betty akambembeleza huku akimfuta machozi, walikuwa wamekuwa wadada watu wazima lakini ule urafiki wao wa tangu utotoni uliwafanya waendelee kuwa watoto.

    Betty aliifahamu tiba ya kumfanya Joyce atabasamu tena, baada ya kuonekana kuzidiwa na majonzi, na aliihitaji sana furaha yake ili na yeye aweze kumhadithia jambo zito. Akasimama akimwacha Joy kitandani. Akasogea hadi katikati ya chumba. Joy alidhani anaenda uani, akajilaza kifudi fudi. Mara…………………

    “Ukutiii ukutiiiii……wa mnaziii…..wa mnaziiiiiiiiii……..mwenzetu….mw enzetu……..kagongwa ……kagongwa……na nini na nini…. Na gaaari na gaari……..”

    Joyce akakurupuka kutoka kule kitandani, alikuwa na kanga iliyofunika kiguo kifupi cha kulalia, kanga ikaanguka hakujihangaisha kuiokota……akafika kwa fujo mahali alipokuwa Betty akiimba kipweke kabisa, akaunganisha mikono yao upesi kisha akendelea kwa sauti kuu yenye furaha..huku wakirukaruka.

    “…Tumpeleke hosibitali asije kusema kwa mama yake….yesayesayesa yaaah…..bado kidogo….yeasayesayesa yaah!! Baaado kidogo ….yesayesayesa yaah!!”

    Hakika Betty alikuwa amemkamata Joyce haswaa, waliruka ruka wakabadili kila aina ya nyimbo za utotoni na zile ambazo waliimba wakiwa wanakua. Furaha ikakipamba kile chumba. Kisha kwa furaha wakakumbatiana huku wakilia, zile nyimbo ziliwakumbusha mbali. Enzi hizo Joyce ni mwembamba na kidoti chake kikiwa sio biashara hadimu.

    Betty naye akiwa ‘kimbaumbau’.

    WAKATI wawili hawa wakikumbushia enzi zao kwa nyimbo za kitoto, upande mwingine wa maisha wanaume wanne ambao waliita kile kitendo cha Joyce kuondoka kinguvu na wale wasichana ambao ni rafiki zake kilikuwa ni utovu wa nidhamu.

    Wanaume wale waliamini hapakuwa na msichana hata mmoja ambaye ana uwezo wa kuwakatalia kimapenzi, walikuwa na kila kitu ambacho msichana wa wakati ule alikuwa anatamani kukifahamu aghalabu kama si kukipata kabisa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mara ya mwisho mi kukataliwa na demu ilikuwa mwaka juzi, tena tulikuwa ikulu nd’o kitoto cha prezidaa kikanitolea nje, tena ni vile sikukaza uzi tu na alishajua kuwa nilikuwa natoka na mtoto wa waziri, hiki kishamba kutoka wapi nd’o kinisumbue. Sasa hapa naweka kando mambo yangu kwa muda. Lakini tupinge nawapa wiki mbili tu huyo Kidoti sijui nakuja kumtambulisha mbele yenu” alijigamba Isaya.

    Wale wanaume wengine wakapiga kelele za shangwe kumpamba Isaya. Walizungumza mengi huku yule mtoto wa mbunge wa wilaya ya Geita (kwa sasa mkoa wa Geita) ambaye alionekana kudhamiria waziwazi kuhusiana na Joyce akiweka kiapo. Safari zake za kwenda Marekani na uingereza mara mbili tatu akiambatana na mzee Akunaay Zingo ambaye ni baba yake mzazi na pia mbunge, zilikuwa zimempagawisha sana na kujikuta akitamani kuishi maisha ya kimagharibi katika nchi ya Tanzania. Alijipa kiburi kuwa kwa safari zake hizo na pesa aliyokuwa nayo basi angeweza kufanya kila kitu na kila mtu akakubali. Ni heri asingeweka kiapo kile maana alikuwa anajiingiza katika safari asiyoijua mwisho wake wala mwanzo wake!!! Ni basi tu wanadamu hatukupewa jicho la kujua yatakayojiri wakati ujaoo…….

    ***

    Kabla ya kulala Betty naye alisema machache kuhusu yeye.

    “Joyce Kidoti.” Aliita kwa utani, Joyce akacheka. “Najua una maswali mengi ya kutaka kuniuliza, lakini baadhi nayajibu katika maelezo yangu, kwanza unajiuliza Dar nipo tangu lini na nimekuja kwa nani….Joy mpendwa mguu huu kutoka huko nitokapo ni mguu wa kuja kwako wewe.” Akasita na kumtazama machoni rafiki yake.

    “Nimekuja kwako wewe ukiwa ndugu yangu wa karibu sana na mwandani wa kuzifahamu siri zangu na matatizo yangu hata kama ni makubwa vipi. Nimekuja hapa nikihitaji msaada wa vitu viwili kwako, yaani vitu viwili tu! Na kama vikiongezeka nitakueleza…” Joy akamkatisha, “Betty hutakiwi kuhesabu kitu chochote kwangu Joy ni yuleyule na nitafanya kila kitu kwa ajili yako hata kama ni vitu elfu moja.” Alisema kwa hisia, Betty akaipokea kwa kutikisa kichwa juu na chini. Kisha akaendelea. “Kitu cha kwanza ni hifadhi, sina hifadhi katika jiji hili na kubwa zaidi ni mara yangu ya kwanza kufika jijini hapa. Kitu kingine ambacho nahitaji unisaidie ni kunitunzia siri yangu, Joyce Ukimwi ….ukimwi hauponi hata asikudanganye mtu, mimi na afya yangu yote hii bado unaishi nami ugonjwa huo mbaya.” Hapa Joyce akatikisa kichwa kwa masikitiko.

    “Usiumie Joyce hiyo ilibidi itokee iuli wewe ufike hapa kisha urejee Ukala kama shujaa wangu, shujaa wa kijiji chetu. Na katika huo ushujaa ukilitaja jina langu kichwani mwako nitafarijika sana. Maana kitu ninachokiamini mimi katika vita hata wale ambao huteteketea na kupoteza uhai wao wakiligombania taifa na wao huitwa mashujaa pia. Hivyo mimi nimekufa katika harakati, ningeweza vipi kukuacha Joy uolewe…nigekuacha vipi uolewe na wale watu wazima ambao huenda wana Ukimwi wakakuambukize. Joy imekuwa heri punda afe mzigo ufike na sasa imekuwa heri Betty afe JHoyce akikomboe kisiwa cha Ukala, kisiwa kilichowameza wazazi wetu, kikawatafuna waalimu wetu kwa sababu ya kukosa huduma za kiafya.

    Kisiwa kilichosahaulika kabisa. Ni furaha yangu nimekukuta ukiwa hapa na utanieleza ulifikafika vipi hapo baadaye maana tupo pamoja tena…..Joy msaada huo wa kuitunza siri hiyo kwa upendo ni kwa manufaa yetu pia, najua mzigo wa kuipigania Ukala ni mkubwa sana, nilitamani tushirikiane kimasomo hadi huku lakini haikuwezekana, lakini nikaipata njia mbadala huko Lilongwe Malawi nilipokuwa naishi kwa kipindi kirefu. Nimekuja nikiwa na nia moja tu, nahitaji pesa. Pesa kwa ajili ya kijiji chetu, pesa kwa ajili ya maisha yetu. Mara ya kwanza nilivua nguo nikapata pesa, sasa ni mawili KISASI na PESA…wataumia hao walio na tamaa watambuao kuwa sisi ni vyombo vya starehe, na wataumizwa na tamaa zao, sitajiuza Joy sitamtega mwanaume kwa maksudi ili aninase lakini nasema OLE WAO wajilengeshe na kujifanya wanajua kupenda na wanayo pesa……moyo wangu umebakiza nafasi ndogo sana ya upendo, na huu ni kwa ajili yako tu Joy, sihitaji kumpenda mtu mwingine kabisa. Namaanisha ninayoyasema. Nd’o maana nikahitaji hifadhi za aina mbili, kwanza mimi kama mimi kisha hifadhi na siri yangu hiyo nzito. Huku ukijua wazi ndugu yako sina upendo zaidi ya kwako wewe na nd’o maana ninakupa siri na mipango yangu ya sasa” alimaliza na kuweka kituo Betty kisha akamtazama tena Joyce. Joyce alikuwa ana wasiwasi mkubwa sana. Alishangaza sana kumtazama.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA!!!

0 comments:

Post a Comment

Blog