Simulizi : Roho Mkononi
Sehemu Ya Pili (2)
JOYCE alikosa cha kujibu kwa usiku ule, akatamani kumshauri Betty walale kwanza huku akifikiria nini cha kujibu lakini akajikanya kuwa huyu Betty hakufikiria mara mbilimbili wakati anaamua kufanya mapenzi na mwalimu Japhari ili aweze kupata pesa kwa ajili yake. Kumbukumbu hii ikampa ujasiri..akakifungua kinywa chake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Betty, nadhani unafahamu kuwa sina uwezo wa kusema hapana kwako, nadhani unajua kuwa wewe ni zaidi ya mwandani wangu, sina kipingamizi, kama ambavyo sikunyanyua kinywa changu kumshirikisha mtu yeyote juu ya mahusiano yako na mwalimu, basi hivyo hivyo sitapoteza hata sekunde moja kumshirikisha mtu yeyote juu yako. Kwa hili NAAPA!!” Alisema Joyce kwa ujasiri huku akimtazama Betty machoni moja kwa moja akimaanisha kuwa kile ambacho anakiongea anamaanisha na wala hatanii. Betty akavutiwa na jibu hilo, alitegemea elimu ya Joyce itakuwa imeanza kumbadili lakini la haikuwa hivyo.
Joyce alikuwa yuleyule. “Ehe na wewe nambie uliunga unga vipi hadi kufika huku maana sikuamini siku nilipoona jiba lako katika mtandao kuwa unajiunga na chuo hiki, hakika nilistaajabu. Sikuwa tu na mtu yeyote kule Lilongwe ambaye alikuwa anakufahamu hivyo sikuwa na wa kumweleza kuwa pacha wangu amefikia elimu ya chuo kikuu.” Aliuliza kwa shauku, Betty.
“Mhhh! Kwanza nimalizie wewe ulipoteaje pale Makambako jamani watu wakaanza kusema umekufa, wee nililia sana, mara Dulla naye akajinyonga yaani nd’o nikachanganyikiwa mimi.” Hapa Betty alitabasamu kidogo kisha akajisemea mwenyewe,
“Mwanaume pekee niliyemuua kimakosa ni Dulla waliosalia wote ni haki yao, watajuta kuzaliwa wanaume na tamaa zao” Baada ya kujisemea akaendelea kuzungumza tena na Joyce, akaipandisha sauti juu kidogo.
“Hofu, aibu, mawazo, na uoga wa kifo humfanya mgonjwa wa Ukimwi kujihisi anakufa kesho yake, hapa sasa hujikuta akiteswa na hivyo vitu vitatu hasahasa mawazo na uoga wa kifo. Hapa sasa mgonjwa huonekana kama aliyezidiwa tayari na anakufa muda wowote.” Ni hivyo daktari aliwaeleza ndugu zangu wa kule Makambako. Kisha wakawasihi wanipeleke mbali kabisa na Makambako ambapo nitapotelewa na ‘aibu’ kwa sababu hatakuwepo mtu anayenitambua, pia mawazo yatapungua kutokana na mazingira mapya.
Betty alisimulia jinsi alivyosafirishwa hadi Malawi kwa mganga wa tiba za asili. Akapewa tiba za kiasili kwa juma moja akinyweshwa madawa makali makali asiyoyajua majina yake. Madawa ambayo yalimsaidia haswa. Kisha akasafirishwa hadi Lilongwe mji mkuu wa Malawi, huku ndipo akaanza huduma za kisasa. Ushauri wa daktari ulipozingatiwa Betty akanawiri tena.
Alitamani sana kusoma lakini ilimlazimu kuanza upya tena jambo ambalo hakuwa tayari kulifanya, basi akabaki kuwa msaidizi tu nyumbani kwa huyo aliyeambiwa kuwa ni ndugu yake. Maisha yalikuwa ya wastani na familia ilikuwa na furaha tele, lakini Betty hakuridhika kabisa kuishi na kufia utumwani, hapo likamjia wazo la kutoroka. Alikutana na mwanaume kutoka Tukuyu Mbeya, katika orodha huyu ndiye wa kwanza. Akampamba Betty kwa maneno matamu.
Betty akaomba kitu kimoja tu, awezeshwe kufika Tukuyu ama Mbeya mjini iwapo itawezekana. Mnyakyusa akaingia mtegoni. Betty akatoroka nyumbani, akiwa na fikra moja tu kichwani mwake, fikra ya kufia nyumbani na si ugenini kiasi kile hata kama alikuwa akipendwa vipi, bado aliamini kuwa yeye ni marehemu wa wakati wowote. Basi kwa kitendo cha mwalimu Japhari kumpa pesa baada ya kumwambukiza Ukimwi basi alihitaji ‘ka-mchezo’ kaendelee. Ule Ukimwi aliopewa na mwalimu yeye akaamua kuufanya kitega uchumi.
Betty akaamua kuuza Ukimwi kwa manufaa ya kisiwa cha Ukala. Kutokea Tukuyu, baada ya mnyakyusa kulipia pesa nyingi ule Ukimwi ambao alipewa katika nyumba za kulala wageni mjini Mbeya. Betty akaamua kusafiri kwenda Dar. Alifanya hivi akiamini kuwa pesa na kila wanaume punguani waliovurugwa na pesa wapo jijini Dar es salaam. Sasa yupo Dar, yupo na Joy na amemweleza kila kitu na amekubaliwa.
Joyce akashusha pumzi baada ya Betty kusimulia. Kwa upande wake hapaukuwa na longolongo nyingi, alifaulu kwa kiwango cha juu kidato cha nne, mkuu wa shule akaitisha mkutano wa wazazi na wanakijiji wengine, harambee ikapitishwa kwa Joyce na wanafunzi wengine wawili waliofaulu kujiunga na kidato cha tano. Pesa ikapatikana ya kutosha wakaingia shuleni bila mashaka yoyote. Hata safari ya kwenda chuo kikuu haikuwa ngumu, serikali ilikuwa inatoa mikopo. Na bado mkuu wa shule aliendelea kuhitisha mikutano mara kwa mara hadi Joyce pekee akiwa kati ya wanafunzi watatu kutoka Makambako waliofaulu kidato cha sita na kuingia ngazi ya chuo kikuu. Wakati Joyce anamaliza kusimulia Betty alikuwa amesinzia tayari, bila shaka hakusisimuliwa na maelezo yale ama la! Alichoka. Hivyo Betty hakupata nafasi ya kusikia juu ya Joy kugombea ‘urembo’ wa chuo, jinsi wanafunzi walivyomtunuku pesa kuonyesha kuwa wanapingana na matokeo yaliyotajwa, akajitokeza mdau mwingine na kuahidi kisha kumnunulia Joyce Kidoti ‘laptop’…..
****
MACHO ya wasichana walimbwende haswa kutoka chuoni yalikuwa yakistaajabishwa na hali ya sintofahamu iliyokuwa inaendelea kati ya mwanafunzi aliyekuwa na pesa na pia majivuno huenda kuliko wanafunzi wote wa chuo hicho kikuu na msichana aliyesadikika kuwa ni mrembo aliyeshinda taji lakini akachakachuliwa na wajanja. Kwa ufupi ilikuwa ni sintofahamu kati ya watu maarufu chuoni hapo. Walikuwa waeneo ya Mabibo Hostel, eneo maarufu kabisa kwa wapendanao ‘Block G’. Kwa mtazamo wa macho ilionyesha kabisa kuwa msichana alikuwa akipingana na yule mvulana, mtoto wa mbunge wa Geita.
Isaya Akunaay, hali ile iliwatia hasira wasichana ambao walitamani sana kuwa katika mahusiano na watu maarufu na wenye pesa zao. Kila msichana wa kisasa angeweza kutamani kuwa na Isaya Akunaay, si tu kwa sababu alikuwa na pesa la! Alikuwa mtanashati pia, jamari wa sura ana umbo. Vipi kuhusu Joyce? Mbona kama hana dalili za kushawishika!!! Hiyo ikawa sintofahamu kuu.
“Isaya…unanirudisha hostel ama nikapande daladala.” Alihoji Joyce huku akirusha mikono huku na kule. “Nisikilize kwanza nd’o nitakurudisha kama hunisiki…”
“Kaka, sitapanda gari yako nimeghairi, nitapanda daladala. Naomba niende tafadhali.” Sauti ya Joy ilishuka chini sana, hii hutokea akiwa amekasirika sana. Isaya alidhani Joyce alikuwa anatania, mara yule msichana akasimama wima….
“We Kidoti…Kido….” Hakumalizia kauli yake, binti akarusha mikono hewani kumaanisha kuwa hataki kusikia lolote kisha kwa mwendo wake uleule wa kilimbwende akatoweka machoni. Isaya akabaki ameduwaa, hakika aliduwaa na ilikuwa mara yake ya kwanza. Mara ya kwanza kudhalilishwa kama ambavyo angeweza kusema yeye iwapo angeulizwa.
Wapambe wake waliokuwa ndani ya gari la Isaya walilitazama tukio lile katika hali ya mshtuko pia, hawakutarajia kuona walichokiona. Wakapigwa na bumbuwazi na hata Isaya alipoingia ndani ya gari hakuna aliyemuuliza kitu. Mpambe akawasha gari. “Nipeleke room.” Aliamrisha. Gari ikatoweka. Kichwa kilimuuma Isaya.
HAIKUISHIA hapo, mara ya pili walikuwa maktaba wakijisomea, wapambe wakamtonya Isaya kuwa Kidoti alikuwa humo. Isaya akajibebesha mkoba wake wenye laptop akaingia maktaba. Huko akamfuata tena Joyce katika namna ya kutaka kuendeleza na ombi lake la kumtaka kimapenzi. Pasipo kutarajia baada ya kuongea maneno mengi sana kwa sauti ya kunong’ona, sasa ulikuwa wakati wa Joyce kujibu. Likatokea jingine ambalo lilimlaza Isaya hoi kitandani siku hiyo bila ugonjwa wowote kichwani. Joyce akaandika katika kikaratasi na kukisukuma kwa Isaya Akunaay. Mtoto wa mbunge anayejihisi kuwa nay eye ni mbunge.
“DON’T MAKE NOISE IN THE LIBRARY…..haukusoma pale mlangoni??” maandishi yalisomeka hivyo. Isaya akabaki na kile kikaratasi huku akitazama kama kuna mtu yeyote ameona wakati akisukumiwa, akakikunja kunja. Akataka kusema neno lakini Joyce hakuonekana kuwa tayari kusikiliza chochote kile. Karata hii nayo ikagonga mwamba!!
Isaya akazidi kuchanganyikiwa, mapema akalala fofofo mchana, kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya chuo.
Jaribio la tatu lilikuwa shukrani alizopeleka kwa Joyce kwa kumsaidia kuipata ‘laptop’ iliyokuwa imepotea maktaba. Isaya aliamini shukrani pekee ni pesa, akamtumia Joyce kiasi cha shilingi laki mbili kama shukrani. Hapa napo mambo yakawa yaleyale na akili yake ikazidi kuduwaa. Pesa ilirudishwa bila kupungua hata noti moja.
“Amesema haukutangaza dau lolote kwa atakayefanikisha kupatikana kwa laptop nd’o maana aliamua kwa moyo wake tu!!” kauli hii ikamchanganya Isaya japo alikiri kuwa Joyce alisema ukweli kabisa. Akazipokea pesa zake kinyonge.
Kuanzia hapa hakufanya papara tena, akajifanya hana haja na Joyce tena. Lakini moyoni akikiri kuwa wale wasichana wote aliowapata zamani kwa kutumia jeuri ya pesa zake hawakuwa na ladha na hawakumkaa akilini kabisa, alifanya nao mapenzi na kuwaacha mara moja.
Wengine walimlilia lakini hakujali, lakini sasa akakitambua kilio chao kilivyokuwa na maana kubwa na kikiwaachia jeraha la aina yake. Jeraha la hisia!! Sasa jeraha hili likaanza kumtambaa nay eye pia, akajikuta akimuhitaji sana Joyce kuliko yule mtoto wa raisi wan chi ambaye alimkataa kimapenzi.
“Kumbe pesa sio kila kitu eeeh!!” aliwaza Isaya kisha akamalizia, “Kipi sasa ni kitu zaidi ya pesa jamani.” Hakuwepo wa kumjibu. Tabia ya Isaya ikabadilika, akawa mtu wakulala tu, kila alilolifanya aliona haliendi sawa iwapo kuna msichana alimuhitaji na hakumpata.
Mara akaanza kudhoofika. Hili likawashtua rafiki zake nay eye mwenyewe pia. Alidhoofika kwa sababu ya kuwaza juu ya jeuri ya Joyce , alijiuliza nani anayempa kiburi. Msako ukaanza ili amjue mwanaume ambaye anampa kiburi Joyce, akishampata ndipo atajua nini cha kumfanya ama uamuzi gani wa kuchukua.
*****
WAKATI huu Joyce alikuwa amehamia chumba chake mwenyewe nje na chuo, huku alikuwa akiendelea kuishi na Betty ambaye alikuwa kazini katika namna ya kipekee, kama alivyosema awali. Hataki mwanaume njaa anayetegemea mkopo wa serikalini utoke ndipo aanze mbwembwe zake chuoni, ama mwanaume shida anayetegemea wazazi wapate mishahara yao midogo wamtumie pesa za matumizi.
Betty alikuwa anahitaji wale wanaojiita watoto wa ‘misheni tauni’. Wenye pesaa zao bila kujalisha ni wapi walipozitoa. Cha msingi wasiwe na mikono ya birika, wajue kuhonga. Na kwake yeye ilikuwa lazima wahonge, hakuwa msichana wa kutongozeka kikawaida kawaida. Alikuwa kikazi zaidi, na katika kazi yake hiyo alikuwa makini mno.
“Vipi jamaa keshaacha kukusumbua siku hizi…maana kimyaa au ndo tayari na wewe…ushadata.” Betty alimchokoza Joy wakiwa kitandani.
“Aaargh asingeweza kunipata kirahisi, ameuchuna siku hizi aibu kwake…ananitishia mimi pesa ananitishia majivuno.” Alijibu Joy kwa jeuri huku akiibetua midomo yake. “Na hicho kidoti wanakomaje!!!” Wakacheka kwa pamoja!!! Mara simu ya Betty ikaita akaipokewa, alikuwa bwana mmoja mfanyakazi wa benki.
“Mi natoka shoga!!.” Alimuaga Joyce wakati anajiandaa kwenda kwa bwana mwingine.
“Huyu ananipa laki tano leo, nakaribia kufikisha milioni nne dah safi sana. Na roho saba zipo rehani tayari pumbavu zao.” Alibwabwaja huku akitangaza chuki ya waziwazi. Akaondoka zake!!!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
HAKIKA Isaya mtoto wa Akunaay alikuwa amepatikana kwa mara ya kwanza katika uwanja wa mapenzi, alijaribu kufikiria na kuweka picha za wasichana lukuki ambao aliwahi kuwanao katika mapenzi na kisha kuwaacha solemba.
Alijiuliza kama kuna msichana walau mmoja ambaye amewahi kumuumiza kichwa aidha katika kumpata kimapenzi ama la kumwacha. Jibu lilikuja upesi tu, jibu la HAPANA. Hapa Isaya akatabasamu kidogo na kisha kujiona yeye ni wa pekee sana na hana hadhi ya kukataliwa na msichana yeyote aidha ndani ya chuo ama nje ya chuo hicho. Lakini sasa mbona anaumia kichwa iwapo yeye ni wa pekee?? Swali hili lilimvamia katika namna ya kumfadhaisha katika namna ya pekee. Alitambua nini maana ya swali lile, akajaribu kulikwepa jibu lakini haikuwezekana akaamua kukiri kuwa, Joyce alikuwa pekee zaidi yake.
Maana yeye na upekee wake anaouamini amejikuta akiumia kichwa kwa sababu ya msichana huyo.
“Kama ni wa kipekee zaidi lazima atulizwe kipekee huyu.” Alipata wazo hilo, lakini wazo hili likajijenga na swali jingine. Nini maana ya kumtuliza mtu kipekee…..
Ghafla akamkumbuka, Joseph Matanuru, huyu alikuwa ni rafiki yake ambaye walikuwa hawachangamani sana kwa sababu ya kutofautiana mitazamo yao. Isaya akiwa mtu wa starehe na Matanuru akiwa hapendi kujirusha.
Kilichoendelea kuwaunganisha ni ule uenyeji wao wa Geita, walikutana huko kipindi cha likizo hivyo wakawa kama ndugu. Matanuru alikuwa na maadui wengi kuliko marafiki kutokana na kupendq kusema ukweli.
Ukweli unaoumiza lakini kila aliyeambiwa alikiri moyoni kuwa Matanuru alikuwa sahihi, hali ikamfanya Matanuru kuwa na maadui lakini wasioonyesha chuki waziwazi. Isaya alikuwa mmoja kati ya waathirika wa maneno ya Matanuru.
Kila mara alipozungumza naye alikuwa akimshauri mambo mengi. Yalikuwa na ukweli lakini starehe zilikuwa zimemtawala Isaya na kamwe asingeweza kubadilika.
SASA kwa mara ya kwanza Isaya kwa hiari yake mwenyewe anaenda kwa Matanuru kwa ajili ya ushauri, aliyafanya haya baada ya kumaliza kuoga na kubadili nguo zake.
Isaya alijieleza kinagaubaga juu ya tatizo lake. Na kisha akajieleza pia njia anayodhani kuwa ni sahihi kwa ajili ya kumpata Joyce kimapenzi. Matanuru akatabasamu kisha akasimama na kuanza kutembea kwenda mbele kisha kurudi nyuma katika namna ya kujitamba.
“Isaya….hivi huju kuwa msichana anapenda kunyenyekewa, pia anapenda ufanye yale anayoyataka yeye?? Angalia huyo Kidoti anapenda nini na wewe kipende, hana shida na utajiri wako, hana shida na pesa zako Yule. Kama ni hoteli za kifahari walipokuwa kambi ya kuwania u-miss chuo walienda huko, kama ni magari ya kifahari nadhani kwa urembo wake ameshapewa na kuzikataa ofa nyingi tu….si ndo huyu walienda kupiga picha na Raisi ikulu, sasa unahisia kuwa bado ni mshamba….huyu anakuona wewe mshamba na hizo mbinu unazozitumia. Badili mbinu Isaya halafu……usimchezee yule mtoto bwana kama kweli unampenda…..” alimaliza mtaalamu wa saikolojia Matanuru. Maneno ya ukweli kama kawaida yakauchoma moyo wa Isaya lakini atafanya nini wakati alihitaji kushauriwa. Akaondoka kichwa chini mikono nyuma, kichwani akiwa ametingwa na mawazo mazito zaidi… Isaya alikuwa anaionja ladha ya kupenda kwa mara ya kwanza baada ya kuwachezea wasichana lukuki kwa misingi ya kufurahisha mwili wake. Hakuwahi kujua kupenda ni nini lakini alifahamu ladha ya kutamani na kisha kukipata akitakacho, sasa hali ilikuwa tofauti kabisa. Isaya akajikuta akikubaliana na maneno ya Matanuru japo kimoyomoyo.
*****
JOYCE KIDOTI alikuwa amejifunika shuka gubigubi kutokana na hali ya hewa kuwa ya ubaridi kiasi, lakini licha ya kujifunika haikumaanisha kuwa alikuwa amelala la! Bali alikuwa anatabasamu peke yake huku akirejea kumbukumbu kadhaa. Joyce alikuwa akijilazimisha kuamini alichokiona na anachoendelea kukiona, japo hakumshirikisha mtu yeyote furaha hiyo ya aina yake, mastaajabu yakabaki katika akili yake.
Isaya amekuwa mchangiaji katika tamasha la Ukimwi na jinsia? Anavyojivuna yule, duh! Watu wanabadilika sana aisee!! Alijisemea kwa sauti ya juu kidogo. Hakika si yeye tu aliyejiuliza kuhusu mabadiliko ya Isaya bali hata wanachuo wengine waliokuwa wakimfahamu fika kijana yule walistaajabu, lakini shukrani zote zilienda kwa Matanuru ambaye kwa sasa alikuwa rafiki yake mpendwa na wa karibu kabisa. Isaya alikuwa ameacha matumizi mabaya ya pesa, alikula katika migahawa ya chuo, alikuwa akivaa kistaarabu na alipunguza kabisa starehe na dharau. Katika mikutano ihusuyo mambo ya kijamii alishiriki ipasavyo, na kwenye mambo ya kijamii kama kutembelea wagonjwa na kusaidia yatima alitumia vyema ile kofia yake ya kuwa mtoto wa mbunge kusimamia vyema.
Tabia hii ikapenya na kumfikia Joyce ambaye alikuwa na muda mrefu tangu akate mawasiliano na Isaya. Taarifa hizi zilimshtua Joyce hivyo akaamua kuhudhuria kongamano la Ukimwi na jinsia ambalo alisikia kuwa Isaya atakuwa meza kuu kwa ajili ya kutoa mada. Hakika Joyce akamshuhudia Isaya mpya akiwa ndani ya suti nyeusi iliyomkaa vyema, maneno yenye busara yaliyomtoka yaliendana na muonekano wake. Baada ya kongamano alimshuhudia akisalimia na watu wenye heshima zao na wsalionekana kumsikiliza sana huku wakiona fahari kuwa naye katika kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi mashuhuri wa Nkurumah uliopo ndani ya chuo kikuu cha Dar es salaam.
Joyce naye akavutika kusalimiana na Isaya, hakika aliipata nafasi hiyo hadimu ambayo wengi walionekana kuitafuta kwani kusalimiana na Isaya ilikuwa pia nafasi ya kusalimiana na mtu ambaye Joyce alihisi kumfananisha na kama aliwahi kumwona mahali, alikuwa amechelewa utambulisho wa wahusika wa meza kuu na wageni waalikwa hivyo hakuweza kumtambua mara moja mtu yule lakini akili yake ilimsisitiza kuwa aliwahi kumwona mahali. Wakati Joyce akizidi kupenya kundi la wanafunzi na wanaharakati wengine ili aweze kumfikia Isaya, alishangaa alipoguswa begani, alipogeuka alionana ana kwa ana na Isaya. Kumbe na yeye alikuwa katika jitihada za kumtafuta.
“Za siku Joyce Kidoti….umenitenga wewe.”
“Njema tu bro…masomo si unajua tena halafu tupo kozi tofauti tofauti nd’o maana.” Alijibu Joyce huku akionekana dhahiri kustaajabu kabisa na muonekano huu mpya wa Isaya.
Kumbe mtanashati eeh!! Alijisemea Joyce. Wakati akipitiwa na wazo hili Isaya alikuwa amekidaka kiganja cha mkono wake na kumwongoza katika kundi la watu huku akiendelea na salamu za hapa na pale zikiongozwa na malalamiko ya kupotezana.
Mara Joyce akapigwa na butwaa, wakasimama mbele ya mwanaume ambaye Joyce alikuwa anamfananisha kama aliwahi kumwona sehemu. Joyce akazidi kuduwaa pale Isaya alipomgonga begani kisha naye akageuka.
“Yes Son!” aliitika yule mwanaume mtu mzima.
“Joyce huyu jamaa anaitwa Akunaay Zingo…”
“Aaaah niite muheshimiwa bwana Isaya..” aliingilia kati katika namna ya utani. Isaya akacheka kisha akampa cheo chake, “Anaitwa mheshimiwa Akunaay Zingo…..mzee wangu huyu. Mbunge wa Geita” alitoa utambulisho huo kwa Joyce kisha akamgeukia mzee wake.
“Mheshimiwa, huyu anaitwa Joyce kidoti, nd’o mlimbwende wa chuo chetu, pia mwanaharakati mwenzangu, mkishaachia ngazi nyie wazee sisi nd’o tunaingia bungeni sasa. Ana nia nami nina nia…” alitoa utambulisho ule bila kumpa nafasi Joyce ya kusema chochote.
“Ohh safi sana, mimi nawabariki sana na ninafurahi iwapo vijana kama ninyi mnapata changamoto na kuwa na akili ya kuthubutu…Joy asante sana kwa kunibadilishia huyu mtu maana alikuwa hashikiki kabisa, usimwache apotee tena.” Mzee Akunaay alisema kauli ambayo ilimfurahisha Isaya huku ikimshtua sana Joy, lakini alitabasamu tu bila kuleta ubishi. Huyu ndiye alikuwa Isaya mpya na Joyce alikuwa akiduwaa peke yake kitandani wakati huo Betty alikuwa katika hekaheka zake za kutafuta pesa.
MWEZI WA TATU TATA.
Isaya alikuwa ameanza kukata tamaa juu ya lengo lake la kummiliki Joyce kama mpenzi wake. Alikuwa amebadilika haswa lakini bado Joyce alikuwa katika msimamo wake kuwa hakuwa tayari kujiingiza katika mapenzi.
“Isaya kiuhakika kabisa sijawahi kukupenda nisikudanganye.” Jibu hili lilikuwa pigo la mwisho kwa Isaya. Joyce alimwambia waziwazi bila kificho chochote, jibu ambalo lilimkasirisha Isaya na kuhisi hata kujishusha kwake hakukuwa na maana yoyote ile, kujiingiza katika mambo ya kijamii pia hapakusaidia kitu. Wapambe hawakuwahi kung’amua Joyce yupo katika mapenzi na nani jambo ambalo lilikuwa likimghafirisha sana. Akajiuliza ana tatizo gani binti yule, urafiki wa kawaida alikubali bila kinyongo na walikuwa karibu mara kwa mara mithili ya wapendanao lakini siri ilibaki mioyoni mwao. Hawakuwa katika mapenzi. Hali hii ilimchukiza sana Isaya lakini angefanya nini wakati alikuwa akimuhitaji sana Joyce. Akaamua kuendelea kuvumilia. Lakini siku aliyopewa jibu lile alijipanga upya kiakili na kujivua ubwege akaona ngoja ngoja inaumiza matumbo na ile subira haikuvuta heri ya aina yoyote.
Isaya akaamua kufanya jambo jingine, maamuzi ya hasira yakapita kichwani mwake. Maamuzi ambayo yanazua kizaazaa!!
****
WAKATI Isaya akijikatia tamaa na kuamua kufanya maamuzi mengine, Joyce alikuwa katika mateso ya nafsi. Kuna jambo lilikuwa linamkereketa haswa, alitambua wazi kuwa Isaya ndiye mwanaume pekee anayeweza kujiingiza naye katika mapenzi. Moyo wake ulimwambia kuwa ni huyo pekee anayeweza kutii kiu yake na wakadumu kwa muda mrefu.
Joyce hakutaka kukumbuka jinsi Isaya wa zamani alivyokuwa na dharau na maisha ya kujikweza. Huyu wa sasa alikuwa mwanaume kamili ambaye aliamini ana vigezo vyote vya kuwa mume. Lakini kitu ambacho Joyce hakutaka kukurupuka ni kumtamkia wazi kuwa yu tayari kuwa naye kwani alikuwa katika kumpima imani Isaya iwapo ni mvumilivu ama la! Hakika Joyce hakuwa akiweza kudumu siku nzima bila kumjulia hali Isaya na mara alipomuona na msichana mwingine moyo wake ulilipuka kwa kwa wivu.
Hapo ndipo alipogundua kuwa yu penzini. Tena penzi haswaa. Kufikia hapo Joyce alipoigundua hali ile kuwa yeye si chochote bila Isaya akajiapiza kuwa baada ya kufanya mtihani wa kumaliza mwaka wa pili wa chuo atamfanyia shtukizo la aiana yake Isaya kwa kumweleza kuwa yu tayari kuwa naye katika uchumba na kisha ndoa iwapo itawezekana. Ahadi hii ikaendelea kuishi na Joyce bila kumshirikisha mtu mwingine. Angeweza kumshirikisha Betty lakini Betty huyu wa sasa anayewachukia wanaume angemshauri kitu gani?? Maisha yakaendelea!!! Hadi ilipokuja ile siku ya utata katika mwezi wa tatu.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Isaya alikuwa amepata majibu juu ya uwepo wa msichana mwingine jirani na Joyce ambaye ni rafiki kipenzi kabisa. Taarifa hii ilimfanya Isaya ajikute katika maamuzi yenye utata, maamuzi ya kulipiza kisasi. Kisasi cha kukataliwa na msichana maskini anayeringia urembo wake, msichana aitwaye Joyce. Isaya akaamua kubadili uelekeo wake akaamua kuhamishia nguvu zote kwa huyo msichana anayesemekana nkuwa yupo jirani sana na Joyce japo haijulikani kama ni mwanafunzi ama la!
Isaya akaipanga siku, akawaagiza wale wapambe wake wa zamani wakamweka sawa yule binti bila Joyce kujua, binti akachukuliwa na kisha kukutanishwa na Isaya maeneo ya Mlimani City.
Moyo wa Isaya ukasukuma damu kwa kasi, kisha akashusha pumzi kwa nguvu yule binti alivyopiga hatua akiongozana na wapambe wawili kuelekea alipokuwa ameketi. Dhahabu kutoka Geita!! Isaya alijisemea huku picha ya Joyce iukifutika upesi kama maandishi katika karatasi inayoungua.
“Naitwa Betty….” Alijitambulisha yule binti.
“Naitwa Joram…” alidanganya Isaya huku macho yake yakiushuhudia mwanya katika mpangilio wa meno yake. Ama kwa hakika Joyce alikuwa wa pili kwa urembo, Isaya akakiri. Hapakuwa na utambulisho zaidi, Isaya ambaye alionekana dhahiri kuwa hana shida ndogondogo alikuwa kivutio mbele ya Betty.
Ni aina hii ya wanaume alikuwa akihitaji. Aliwahitaji kwa ajili ya kuwachuna. Wapambe nao walikuwa wamemjaza maneno Betty wakimsimulia juu ya bwana huyo kuwa ni mtoto wa waziri. Betty akavutika, wapambe weakajua ameshoboka na bwana huyo. Lakini kichwani mwake hawakujua ana nini cha ziada.
Na laiti kama Isaya na kamati yake wangepewa walau ndoto ya kumjua vyema Betty, wasingethubutu hata kidogo kukaa naye na kujidanganya wamemteka.
Betty alikuwa mwanamke mwingine kabisa.
Betty alikuwa kazini!!!
*****
ZILIKUWA zimepita siku tatu bila Joyce kuonana na Isaya. Jambo hili lilimuumiza sana Joyce lakini alijipa imani nkuwa huenda ametingwa na mambo yake binafsi. Ulikuwa usiku wa saa moja, simu ya Joyce ilivyopokea ujumbe. Akaufungua na kufanya tabasamu hafifu, alikuwa ni Isaya.
“Mambo J.K, naomba unielewe kwa hili na ninajua utanielewa, sitaki mazoea yoyote yale ya karibu na wewe. Mpenzi wangu anahisi kuwa mimi na wewe ni wapenzi kumbe ni marafiki tu, hata mpenzi wako sidhani kama anaufurahia ukaribu huu kati yetu. Naomba tuwe tunakutana nna kuwasiliana kwa mambo ya msingi tu KAMA YATAKUWEPO. Tafadhali nisaidie kwa hili, na hizi meseji za hapa na pale tuachane nazo maana simu yangu mara kwa mara anakuwa nayo yeye. Maisha mema mdada.”
Ujumbe ule ulimalizika huku Joyce akitetemeka. Macho yalikuwa yamemtoka mithili ya Panya aliyenasa mtegoni. Aliirudia mara mbilimbili na ujumbe ulimaanisha hapakuwa na utani hata kidogo. Joyce alitaka kumpigia simu Isaya lakini akakumbuka kuwa aliwahi kumwambia ‘Hakuwahi kumpenda hata kidogo’ sasa watazungumza nini kigeni. Joyce akahaha, akatafuta wa kumshirikisha na hakupatikana kwa wakati huo. Hofu ikatanda, moyo ukaulaumu mdomo kwa kujificha kusema ukweli juu ya hisia alizokuwa nazo. Joyce akashuka pale kitandani na kuvaa viatu, akakimbia dukani na kujikuta akinunu vocha wakati simu yake ilikuwa na salio la kutosha. Akahaha huku na kule na bado hali ikiwa ileile. Isaya amemtamkia rasmi kuwa yupo na mpenzi mpya.
Mshikemshike!!!
WIVU….huwezi kutambua kama una ugonjwa huo mpaka pale utakapoanza kukushambulia, wivu hushambulia katika namna ya kipekee, wivu ambao ni kidonda na wahenga walisema ukiushiriki utakonda, haswaa!! Ilikuwa hivyo maradhi ya wivu huishambulia akili vyema, huifanya isifanye kazi ya kufikiri mambo mengine na badala yake kufikiria juu ya kitu kimoja tu. Wivu ukishaimaliza akili huuvamia mwili na kuupunguza kilo katika namna ya kustaajabisha isiyosimulika kwa namna yoyote ile, kisha wivu humfanya mgonjwa kuwa mwewndawazimu wa jambo Fulani, kwa mtazamo wa haraka haraka mtu mwenye wivu na mwendawazimu hawana tofauti kubwa. Maana mwenye wivu yupo tayari kukimbizana na magari barabarani akiamini anaweza kuyafikia, mwenye wivu yupo tayari kujifanya yeye ni mpelelezi japokuwa hajasomea. Na mara nyingine mgonjwa wa wivu huwa bingwa wa kutukana na kupigana. Ubaya wa gonjwa hili, hukomaa kimya kimya bila mtu kujua kama tayari limejipandikiza katika mwili wake.
Wivu hauchagui jinsia wala umri, wivu huja wakati usiotegemea ilimradi tu kukuonyesha kuwa una jambo katika mwili wako. Gonjwa hili huchukiwa na wengi, lakini afadhali basi wanaoyatambua madhara ya wivu wanaweza kujiongoza wanapougua lakini vipi kwa Joyce Kidoti ambaye hakuwahi kujua vyema wivu ni ugonjwa wa aina gani. Ile hali ya kujisikkia vibaya Isaya asipompigia simu nd’o alitafsiri kama wivu. Hakika! Alikuwa sawa lakini huo ulikuwa ni wivu mdogo usokuwa na madhara.
Siku alipoupokea ujumbe matata kutoka kwa Isaya ndipo lile gonjwa rasmi la wivu likajitangaza kuwa limo katika damu yake. Limekaa katika akili na muda si mrefu litatapakaa na kuanza kuutafuna mwili wake. Joyce aliketi kitandani vyema na kujiuliza ni msichana gani huyu ambaye Isaya anamuita mpenzi wake. Shida ya kwanza kabisa akataka amjue ni wa aina gani ili kabla hajamsikitikia Isaya ajisikitikie mwenyewe.
Sifa za kwamba yu mrembo wa kutisha zilimfanya awe na kiburi bila kujijua, aliamini hata Isaya alidatishwa na urembo wake. Sasa kwa huyo mwingine amedata na nini? Alijiuliza….. Mawazo lukuki na ndoto kufifia vyote vilimuandama. Wakati alikuwa akitarajia kwa kupitia Isaya anaweza kujipenyeza na kuingia rasmi katika siasa ambayo inaweza kumfanya awe kiongozi siku moja katika kisiwa cha Ukala na kuleta mabadiliko, sasa huyu Isaya hataki kutumiwa ujumbe hovyo.
Kunani??? Alijiuliza. Nani angempa jibu….
Hakuna!! Alitakiwa kulitafuta jibu. Jibu ambalo litampa mwongozo wa nini kinafuata iwapo mwanaume ambaye ametokea kumpenda anajihusisha na mwanamke mwingine. Akajilazimisha kulala bila mafanikio ya upesi hadi majira ya saa nane alipofanikiwa kupotea katika lindi la usingizi. Asubuhi akamka akiamini kuwa ile ilikuwa ndoto, akaichukua simu yake akafungua na kukutana na ujumbe wa Isaya.
Akafadhaika!! Siku hiyo mapema wivu ukamdanganya kuwa yeye ni mpelelezi wa kimataifa na mpiganaji mzuri sana iwapo itabidi. Akaingia chuo akiwa na lengo moja tu kumjua mpinzani wake. Huku akijilaghai kuwa huenda Isaya alikuwa anampima imani…. “Yaani kama ananipima imani itakuwa nafuu maana dah….” Alijipa moyo wa imani.
ALIPOKIFIKIA chuo akitokea maeneo anayoishi katika chumba cha kupanga, macho baadhi ya watu waliokuwa wakimfahamu yalimtazama kwa mashaka na huruma kiasi Fulani. Hakufanikiwa kuona matukio hayo maana alikuwa akiwaza mengi sana. Usiombe kukwazwa na jambo ewe mtu mzima kisha mtu akwambie neno pole. Hili neno huonekana kuwa la kistaarabu lakini kwa mpokeaji huhisi linamaanisha hakuna kinachowezekana tena, ni sawasawa na mfiwa kupewa pole. Marehemu hataamka kamwe. Joyce alikutana na maneno haya kutoka kwa marafiki zake. Baada ya kumweleza mengi kuhusiana na Isaya.
“Yaani yule ni kawaida yake, tulijua tu maskini ona hata nywele umesahau kuziweka vyema.” Rafiki yake mmoja alimweleza huku akimweka sawa nywele zake kichwani.
“Ujue Isaya atajuta sidhani kama atadumu na yule msichana, au ule urembo nd’o umemvutia labda…” rafiki mwingine alisema. Neno ‘urembo’ likamvuruga akili Joyce. Akastaajabu kuwa kumbe Isaya amepata msichana mrembo zaidi. Maneno yakaendelea na pole zikifululiza.
Hapo sasa Joyce Keto akakosa uvumilivu, chozi likajiviringisha katika jicho lake la kuume na kisha kuchuruzika katika mashavu yake. Wivu ulikuwa unamsulubu!! Hakuweza kusema neno lolote lile. Marafiki zake walimwondoa katika mgahawa na kumpeleka chini ya mti huku wakiendelea kumfariji.
ILIBAKI kidogo tu Joyce aridhike na matokeo na kukubali kuwa Isaya hakuwa chaguo sahihi kwake, nafsi ilipingana naye lakini hakuwa na jingine la kujifariji. Lakini siku hiyohiyo kwa maksudi ya kila namna Isaya na weapambe wake wakaitafuta namna ya kumwonyesha Joyce kuwa hawamnyenyekei. Ni siku hii iligeuza kila kitu katika historia ya maisha yake ya chuo kikuu. Ni siku hii alipogundua kuwa kuna tofauti kati ya mapenzi na urafiki. Ni siku hii alipobaini kuwa Betty yule rafiki yake wa dhati ndiye alikuwa katika mahusiano na Isaya Akunaay. Betty yule muathirika wa gonjwa hatari la Ukimwi ambaye anausambaza maksudi kwa nia moja tu ya kupata pesa. Joyce alitamani kusema neno lakini akasita akakumbuka kuwa aliweka kiapo cha moja kwa moja kuwa kamwe hatafungua kinywa chake kusema juu ya tatizo la Betty.
Lakini alipokuwa amegusa Betty ni pabaya sasa, alikuwa amegusa mahali ambapo Joyce amekufa na kuoza kimahaba. Akili ya Joyce isingeweza kulala zaidi, akamtafuta rafiki na mpambe halisi wa Isaya, akamchimba maswali mawili matatu. Akapata jibu kuu alilokuwa akilihitaji. Isaya hakuwahi kufanya mapenzi na Betty katika hizo siku tatu.
Hakika! Joyce akafumba macho na kukumbuka kuwa Betty alikuwa katika siku zake kwa kipindi hicho. Joy akafanya ishara ya msalaba kama ishara ya kushukuru kuwa Isaya bado anayo nafasi ya kuishi. Shughuli ikawa kile kiapo alichoweka mbele ya Betty siku ya kwanza kiapo cha milele.
Alitaka kukipuuzia kisa Isaya ni hapo alipokumbuka jinsi Betty alivyoukwaa Ukimwi kwa sababu yake yeye Joy aweze kusoma. Kwa maana hiyo bila Joy hata hapo alipo asingekuwepo na bila yeye kuhitaji elimu bila shaka Betty asingeukwaa Ukimwi. Mbaya zaidfi akakumbuka kuwa bila Betty huenda angeibwia sumu ya panya baada ya kulazimishwa kuolewa.
Betty akamzuia na kumwahidi kumpigania……hakika alimpigania haswaa. Mapenzi kitu gani? Alijiuliza baada ya kugundua mapenzi yanataka kuyumbisha msimamo wake kimaamuzi.
Joyce Keto Kidoti alipogundua kuwa hawezi kumsaliti Betty na kuitoa siri yake ili kumwokoa Isaya ni hapo pia alipogundua kuwa hawezi kushiriki dhambi ya kumtazama kijana ambaye anampenda kwa dhati ateketee kwa kuukwaa Ukimwi kisa tu analipiza kisasi cha kutopendwa na Joyce.
Ni hapa ndipo Joyce alipoinama na kuitazama mikono yake miwili akakutana na maajabu, alikuwa amebeba roho za watu wawili, roho moja kila upande, huku ya Isaya na huku ya Betty. Ni roho ipi ina thamani kwa wakati ule, ni roho ipi aikamate imara ili asijedhurika na usemi wa mshika mbili moja humponyoka.
Ama!! Hazikuwa mbili tena, Joy akakumbuka pia kuwa ana masomo kichwani mwake, hiyo ilikuwa roho nyingine, kwani kwa kufeli masomo yake basi kila kitu kingeharibika. Je aitunze siri ya Betty ili Isaya afe, ama amwokoe Isaya kwa kuitaja siri ya Betty ili Betty aabike na uwe mwisho wa urafiki wao, ama ashikilie masomo huku yatakayoendelea yatajulikana mbele kwa mbele.
Hili la kuendelea kusoma bila kujihusisha na wawili hawa likawa mbinde sana, asingeweza kusoma katika hali ile. Maamuzi yakawa magumu sana kufikiwa.
Roho tatu katika mikono miwili. Kila roho na thamani yake ya kipekee. Kichwa kikamuuma haswa. Akajikongoja akachukua taksi ikamrudisha nyumbani kwake. Huku akakutana na uso wa Betty ukiwa umechanua kwa furaha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Shosti…mtoto wa mbunge kiganjani kwangu pumbavu zake…atanikomaje?” Betty alimweleza Joy huku akirusha mikono yake juu. Kichwa ni kama kilitaka kupasuka na kujiondokea kabisa, Joy alihitimisha kile alichokiona na kukisikia. Macho yalikuwa mekundu sana, akasingizia kuwa anaumwa kichwa, Betty akamtafutia dawa na kumpatia anywe, Joy akazipokea na kuzimeza. Kisha akakirukia kitandani, kizunguzungu kikiwa kimemwandama. Kitanda kikaonekana kama kinazunguka kwa kasi katika namna yua kukera, joto likaizidi maarifa feni iliyokuwa inapuliza pale ndani, Joy akaondoa nguo zake na kujifunika na kanga pekee. Akajilazimisha kulia machozi hayakutoka lakini kuna donge lilikuwa limemkaba kooni. Ama kwa hakika Joyce alikuwa amefikwa.
Uzito wa roho kadhaa mkononi mapema kabisa ulionekana kumzidia. Ili apate ahueni alitakiwa kuchagua nini cha kutupa na kipi cha kubaki nacho. Joyce alitakiwa kufanya maamuzi ya kuokoa roho mojawapo. Ili asishindane na ule usemi ambao mchumia janga hula na wakwao. Joy akabaki kuwa mfa maji asiyeisha kutapatapa….
USINGIZI ukiwa umegoma kabisa kumtembelea Joy na kumtenganisha na dunia kwa muda na kuyasimamisha mawazo. Mara alisikia mivumo ya sauti ikinena lugha ambayo hakutaka kuisikia kabisa, lugha ya kumzungumzia Isaya. Na mnenaji alikuwa ni Betty.
“Yaani huyo ameingia pabaya lakini ujue nini, mimi shida yangu ni huyo baba yake anayejiita mbunge. Nikimpata huyo sikosi milioni kama thelathini hapa. Wanajua kuhonga hao wajinga. Sasa milioni thelathini hapa hatujarekebisha walau ki’zahanati chetu cha Ukala, hatujaweka madawati kadhaa katika ile shule tuliyosoma pale Ukala. Ujue nilikuwa nachukia kukaa chini yaani we acha tu, nd’o maana nakwambia Joy mi sitaki kuondoka hivi hivi acha tu nizichume dhambi lakini hata Mungu anajua kuwa sizichumi kwa sababu ya starehe Joy wangu. Ingekuwa ni kwa ajili ya starehe nadhani hata hapa kwako ningekuwa n’shahama…mi nataka pesa kwa ajili ya maendeleo. Sijui mtoto wa mbunge sijui mtoto wa diwani mimi sijali cha msingi ni mwanaume mwenye tamaa basi ile OLE inamuhusu…..” mara Betty akasita kisha akasema kwa sauti ya chini kidogo, “Sijui Joy mwenyewe keshalala najipigisha makelele peke yangu!!” kisha akaanza kujiimbia nyimbo alizokuwa amezikariri.
Joy hakuwa amelala alisikia kila kitu, maumivu makali kabisa yakapenya katika moyo wake, akajikaza asisike kama analia lakini machozi yalimwagika kwa wingi.
Akiwa hapo kitandani akakumbwa na wazo la kutatua tatizo hili, akafikiria kumweleza Isaya kuwa anampenda sana na yupo tayari kuwa katika mahusiano naye. Lakini akakumbuka mambo mawili makuu, jibu la mwisho alilowahi kumpa Isaya, “SIJAWAHI KUKUPENDA ISAYA”….hili lilimuumiza hata yeye maana lilikuwa jibu kavu linalochoma kwelikweli. Kisha akakumbuka na ujumbe alioupokea kutoka kwa Isaya siku moja iliyopita, “SITAKI MAZOEA YA KARIBU NA WEWE.”
Joy alipoukumbuka ujumbe huu akazidi kutiririkwa machozi na kuona kuwa hakutendewa haki hata kidogo kupewa jibu lile.
Ama hakika mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu.
Kwa majibu haya mawili katika siku tofauti Joyce aliuona utata waziwazi, Isaya asingekuwa mwanaume mjinga akubali kirahisi kuwa katika mahusiano na mtu ambaye alimtamkia kuwa hana hisia naye.
Hapa sasa Joy akaamini kumwendea Isaya na kumweleza kuna uwezekano wa kukutana na mambo mengine yenye utata zaidi, ama kupuuzwa na kutukanwa hadharani kuwa anamtaka Isaya kwa ajili ya pesa zake, ama la kuwa katika mapenzi ya foleni. Jambo ambalo binti huyu hakuwa tayari.
Mawazo haya yakazidi kumpasua kichwa Joy.
Mara akafikiria pakipambazuka amweke Betty kitako na kumweleza kila kitu kilivyo juu ya huyo Isaya ambaye anajiita Joram. Wazo hili akaliona ni jema sana, lakini ghafla akakumbuka kitu. Ni kwamba Betty atamkubalia hoja yake mara moja na ataachana na Isaya.
Ehe! Baada ya hapo!!
Hakuna jipya jingine Isaya ataendelea na maisha yake na atakuwa na msichana mwingine ambaye Joy hana mazoea wala ukaribu naye, hivyo Joy atazidi kuumia akimuona Isaya na msichana mwingine.
Joy akatambua kuwa alichokitaka yeye ni kuwa katika mahusiano na Isaya na wala si kwamba Isaya asiwe katika mahusiano na Betty.
Silaha kubwa na pekee ambayo ingeweza kuirejesha imani ya Isaya kwa Joy ni kiasi cha Joy kumtafuta na kumweka kitako kisha kumweleza kuwa msichana ambaye wapo naye katika mahusino ni mwathirika. Hivyo amemweleza hayo kwa sababu anampenda sana. Kwa kauli hiyo mwanaume yeyote duniani hawezi kuchomoka tena, na hatahitaji uthibitisho mwingine kujiaminisha kuwa anapendwa.
Lakini kumweleza Isaya hayo ni sawasawa na kumsaliti, tena usaliti mkubwa kwa Betty.
Kizungumkuti kikuu!!!
Joy akakosa maamuzi.
****
ISAYA AKUNAAY. Mtoto wa mbunge wa Geita mjini, alikuwa ameamua kumuumiza Joyce haswaa kwa akitendo chake cha kuingia katika mahusiano mengine na msichana mwingine ambaye ni mtu wa karibu wa Joyce.
Alijua kuwa taarifa zimemfikia tayari, lakini hiyo ilikuwa haitoshi bado alihitaji kufanya jambo kwa ajili ya kupigilia msumari wa mwisho.
Pesa huzungumza, hii ni kweli. Akiwa kitandani kwake akapata wazo la kumtambulisha Betty kwa marafiki zake na wanachuo wengine. Hakuwa na wasiwasi katika hili kwa sababu kwa kitendo chake cha kubadilika ili ampate Joyce hakuwa na wasichana wengine tena, hivyo hakutegemea mtafaruku wa aina yoyote ile. Na isitoshe alikuwa amepigiwa chapuo agombee nafasi ya uraisi wa chuo basi alihitaji kuwa mfano kwa wanafunzi wengine. Mfano katika namna ya kuishi na pia uwazi katika mahusiano.
“Yes! Ndege wawili kwa jiwe moja tu. Hapa namkomoa Kidoti na upande huu najijengea mazingira mazuri ya kuuchukua uraisi wa chuo.” Alishangilia Isaya huku akijirusha rusha kitandani kwake.
Wazo hilo halikuhitaji mshauri bali lilihitaji utekelezaji.
Siku iliyofuata akiwa na Betty ufukweni na wapambe lukuki kama kawaida alimweleza nia yake ya kufanya ‘engagement’ na kumvika pete rasmi kabla ya uchumba.
Kwanza Betty hakuamini kama Isaya alikuwa amezama kiasi kile, alidhani ni wale wanaume wa kuhitaji mapenzi tu na kisha kuendelea na mambo yao. Tangu atue jijini Dar es salaam hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mwanaume kumtamkia juu ya kumtambulisha kisha uchumba na ndoa.
Mapigo ya moyo yakaongezeka kasi yake, hakika hili lilikuwa shambulizi la ghafla sana. Shambulizi lisilotegemewa kabisa.
Betty akashikwa na kigugumizi akakosa cha kusema, wakati huo tayari Isaya alikuwa amemvuta na kumlaza kifuani mwake.
Zile busara alizorithi kutoka kwa mtaalamu wa saikolojia na mapenzi bwana Matanuru sasa zikaanza kufanya kazi, akamshawishi Betty kwa maneno makali ya kimapenzi, sauti maridhawa kabisa ya kiume ikapenya katika masikio ya Betty na kisha kwa mara ya kwanza ikatua katika mtima wake.
Betty alikuwa amekutana na mwanaume ambaye ana hisia za hali ya juu kwake. Akajisikia vibaya kwa sababu hana msamaha kwa ajili ya mwanaume yeyote akajijutia kuupata Ukimwi akiwa bado mdogo.
Laiti ningekuwa salama ningenyanyua kinywa change na kukiri kuwa hatimaye nimempata mwanaume anifaaye!! Aliwaza Betty.
“Mbona kimya mamii.” Sauti ya Isaya ilimrejesha tena mahali pale.
“Hapana mpenzi basi tu nilikuwa nafikiria juu yako. Elewa kwamba wewe ni kila kitu kwangu, nilikueleza siku ya kwanza kuwa umenikuta mimi kama Betty na sasani Betty wa Isaya. Nakusikiliza wewe.” Betty alinong’ona kimahaba. Akamkosha Isaya. Kijana akambeba na kumrusha juu juu. Kisha wakakimbilia ndani ya maji wakikimbizana huku na kule.
Siku hii ikamalizika kwa furaha ya aina yake. Lile lengo la Isaya likapiga hatua moja mbele.
****
JOYCE alikuwa akingojea wakati ambao Betty atarejea aweze kuzungumza naye na kumweleza kitu ambacho kinaisumbua nafsi yake. Aliamini kuwa ni Joyce pekee awezaye kumshauri ama walau kumtia moyo juu ya kitu ambacho kinaendelea kusafiri katika moyo wake. Aliamini fika kuwa bila kulitatua tatizo hilo basi ajiandae kuanguka vibaya katika masomo yake jambo ambalo hakuwa tayari kulishuhudia kwa macho yake likitokea.
Masaa yakasogea hatimaye mlango ukagongwa, alikuwa ni Betty. Betty mwenye furaha tele.
Ni heri Betty angemwacha Joy azungumze kwanza, lakini ilikuwa bahati mbaya kwake maana Betty alianza kuzungumza kabla.
“Mwenzangu…..kuna wanaume wanapenda jamani. Eti katangaza uchumba mwenzangu duuh. Sema ni mtanashati ila ndo hivyo mi siangalii nyuma, hiyo sherehe nahudhuria, pete navikwa halafu usiku huo wa pete nampa na zawadi yake ya tamaa za kijinga jinga. Maskini Joram wangu. Pole yake.” Alizungumza Betty kwa papara huku akihesabu noti kadhaa alizopewa na Isaya aitwaye Joram kwa ajili ya kununua vazi maalum kwa sherehe ile na pia kwa ajili ya matumizi yake.
He! Wamefikia mambo ya uchumba tena? Mungu wangu Isaya anakufa jamani. Isaya wangu!! Alilalamika Joyce katika nafsi yake. Lakini kufikia pale hakuwa na kauli tena dhidi ya Betty.
“Sasa hapo najua atataka kunipeleka kwa mzee wake, huyo mbunge. Hapo ndo napataka sasa, si ifike hiyo siku ya kuvikwa pete mtoto wa watu mie. Duh sipati picha, shosti wewe usihudhurie maana nitaona aibu si unajua nipo kazini mimi.” Alizidi kubwatuka Betty bila kumpa nafasi Joy kusema lolote.
Joy alilazimisha tabasamu huku akijiona akiisindikiza safari ya Isaya kuelekea kaburini.
WAKATI Joyce akiwa aamsikiliza Betty, wafuasi wa Isaya akiwemo Matanuru ambaye alikuwa mshauri mkuu walikuwa wakipanga bajeti kuhusiana na sherehe hiyo.
Ukumbi, vinywaji, muziki, mapambo na mengineyo mengi vilikuwa katika orodha kuu.
Isaya alingojea tu kupewa jumla ya pesa inayohitajika.
Kubwa zaidi Isaya aliwahakikishia wajumbe wake kuwa patakuwepo na wabunge wasiopungua wanne pamoja na baba yake mzazi. Ilisisimua sana kuisikiliza habari hii.
Baada ya siku mbili habari hii ikatapakaa chuo kizima. Isaya anamvisha mtu pete. Kila mpenda sherehe aliingoja sherehe hii.
Sherehe ya mtoto wa mbunge.
****
UKUMBI ulikuwa umetapika haswaa, wenye nazo wachache walichanga pesa, mtoto wa mbunge akajazia za kwake na baba yake.
Waalikwa hawakutakiwa kuchangia chochote zaidi ya zawadi ambazo pia zilikuwa hiari. Isaya aliutazama ukumbi na kukiri kuwa hili ni pigo kwa Joyce Kidoti na pia ni nafasi ya yeye kujitangaza kisiasa hapo chuoni. Mzee wake alihimiza uhudhuriaji wa watu wengi ili kuzidi kumkita mtoto wake katika siasa ili ikiwezekana aweze kumrithi kiti chake cha ubunge wakati atakapostaafu.
Sherehe ikafana haswa!!
Kila jicho la mwsanaume lilimtazama Betty katika namna ya matamanio, wasichana wenye wivu walitafuta cha kukosoa wakakikosa, wakabaki kusema neno moja tu ambalo huenda lilikuwa na ukweli ndani yake.
Betty alikuwa akijilazimisha kutabasamu!! Japo alipendeza lakini lile tabasamu….lile tabasamu lilikuwa na utata…..
Lakini nani angejali kuhusu tabasamu wakati alikuwa ameng’ara?
Akavikwa pete Betty, akakumbatiana na mbunge wa Geita, na wabunge wengine watatu wa majimbo tofauti tofauti. Picha zikapigwa kwa wingi.
Wale wenye wivu nao wakajisemesha kuwa wanawatakia maisha mema wawili hao.
Isaya alitabasamu kutoka moyoni, alitabasamu kwa sababu alikuwa ni mshindi katika vita mbili. Vita ya mapenzi na siasa.
Lakini angetambua kuwa palikuwa na vita kubwa inamsubiri, vita yenye kuogofya na kufedhehesha basi asingeruhusu jino lake hata moja kutazamwa na watu.
Ama kwa hakika liishalo ni heri kuliko lijalo.
Hakulijua hili Isaya.
Majira ya saa sita usiku wale wapendanao walipanda katika gari la kifahari kuelekea katika hoteli ya kifahari katikati ya mji.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jicho kali liliitazama ile gari, mwanaume akiwa amekumbatiana na mwanamke.
“Isaya….Isaya usife Isaya….nakuhitaji bado pliiz!!” mwenye lile jicho alisema kwa sauti ya juu kidogo kisha akajikurupua na kujiapiza kuwa alikuwa muuaji kuruhusu Isaya afanye zinaa na Betty muuaji wa kukusudia.
Lakini akiwa anawaza haya magari yalikuwa yametoweka tayari.
Joyce akataharuki, akahaha huku na kule. Alitamani kupiga mayowe kila mtu ajue kuhusu hatari iliyopo mbele yake.
Lakini mara akakumbuka kile kiapo cha kuitunza siri ya Betty, siri ya kuua maksudi kwa kuambukiza Ukimwi.
Nafsi ikamsuta akajiona mjinga sana anayeenda kujichumia dhambi ambayo anaweza kuiepuka.
Joy akaikumbuka ahadi ya Betty kuwa usiku huo ndio usiku wa kumpa zawadi Isaya. Zawadi ya kifo.
Kauli hii ikamsisimua na kumtoa katika pumbazo Joyce. Nguvu ya mapenzi ikamtekenya, ni kweli alikuwa anampenda sana Isaya, na sasa alikuwa anabariki mauaji haya ya maksudi.
Upendo gani wa kushindwa kutetea ukipendacho…
UTATA….
JOYCE akaamua kufanya jambo. Jambo ambalo badala ya kuwa utatuzi wa tatizo, jambo likazua jambo. Roho mkononi zikamzidia uzito, tamaa ya kuzishikilia zote tatu kwa pamoja ikamvuruga akili.
HEKAHEKA
CHUMBA kikubwa chenye hadhi ya kuitwa cha ‘kisasa’ kiliwapokea kwa manukato ya aina yake. Isaya alitabasamu huku akiuzungusha mkono wake katika kiuno cha Betty ambaye sasa alikuwa akimfahamu kwa majina yote mawili, Isaya kama jina la ubatizo na Joram jina maarufu alilopewa na babu yake kipindi cha utoto. Betty naye aliuchanua uso wake kujibu tabasamu la Isaya.
Mlango ukafungwa na Isaya, kisha wakakumbatiana na kupeana mabusu mashavuni na kisha katika papi za mdomo. Wakaketi kitandani, kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita na kisha kuanza kupongezana huku wakipeana michapo ya hapa na pale iliyokuwa inatokea ukumbini wakati wa sherehe.
Mvinyo waliokuwa wamekunywa ulikuwa umewachangamsha haswaa. Na kila mmoja alikuwa muongeaji. Mvinyo huu ukawafikisha hatua ya kutamaniana, kwa Isaya hii ilikuwa nafasi hadimu aliyokuwa anaisubiri. Lakini kwa Betty ilikuwa hadimu zaidi maana alikuwa anaendeleza safari yake ya kuwakomesha wanaume na kisha kujinufaisha yeye kwa ajili ya kisiwa alichozaliwa.
“Tukaoge kwanza…” Betty alimwambia Isaya ambaye alikuwa ameanza kumzongazonga akimvuta kitandani. Isaya akacheka kidogo baada ya kugundua kuwa Betty ametambua nini kinachotaka kuendelea.
Isaya akaondosha baadhi ya nguo zake kisha akamsaidia Betty pia, kisha wakajongea katika bafu kubwa lililozungukwa na marumaru inayovutia machoni. Waliingia bafuni bila kuufunga mlango, hii iliwasaidia kuweza kuisikia simu ya Isaya ilivyokuwa inaita. Kwa jinsi Isaya alivyoweka milio yake kwa ajili ya watu maalum basi hakuhangaika kujua kuwa ni mzee wake anapiga.
“Mzee huyo, hapa hatachelewa kuanza kutoa semina zake za mara tuwe makini sijui nini dah! Wazee wa zamani oooh!!” alilalama Isaya wakiwa hawajaanza kuoga.
“Kapokee simu mpenzi.” Betty alimchombeza. Isaya akaondoka huku Betty akimtazama mwanaume yule ambaye yupo njia ya kuzimu akisubiri usafiri wa kwenda huko.
“Eeeh unasema….nini?......Haiwezek…. .sasa kwa hiyooo!!” alisikika Isaya akibwatuka katika simu bila utulivu, Betty akajisogeza hadi mlangoni na kumtazama mpenzi wake yule ambaye walikuwa wamevishana pete muda mchache uliopita. Isaya hakurejea bafuni tena, alimsisitiza Betty naye avae waondoke eneo lile.
Hakuweza kujieleza zaidi nini kinatokea lakini alionyesha kupagawa sana. Betty akatii alichoambiwa, akasimama na kuvaa nguo zake upesiupesi kisha wakatoka huku wakitoa taarifa kuwa watarejea. Walivyoondoka hawakurejea tena katiuka hoteli ile. Huu ukawa mwanzo wa hekaheka!
****
MPANGO wa ujambazi kisha mauaji ya kutisha hii ndiyo ilikuwa habari iliyozungumzwa katika simu ya bwana Akunaay Zingo kwenda kwa watu wake wa karibu.
Wakati huo akiwa ameanza na yule wa karibu zaidi. Usingizi uligoma kabisa kushirikiana naye kitandani. Alijiuliza ni nani hawa wa kutaka kumvuruga akili yake kwa kushiriki katika kumvamia mwanaye.
Kitu cha kwanza alichojiuliza na kuhisi ni usahihi mtupu ni juu ya zawadi ambazo Isaya na mwenzake walipewa na wageni waalikwa. Aliamini kuwa hili liliwavuta sana vibaka ama majambazi na kutaka kugawana na mwanaye zawadi hizo. Jambo ambalo hakuwa tayari kuona likitokea. Haraka akachukua simu yake na kubonyeza namba za maaskari fulani ambao walikuwa wanamuheshimu sana. Akataka kupiga namba zao lakini akajiona mpuuzi wa kwanza kabisa kupata kutokea.
Yaani awaelekeze polisi kwenda kuulinda uhai wa mtoto wake mkubwa? Wakati na wao wanalinda uhai wao…. Hapana! Akapingana na shauri hili, akajikita katika mtazamo wa mzazi ndiye awezaye kumlinda mtoto wake kwa moyo wote na si askari ambaye ataleta habari ya tulirushiana risasi wakatushinda tumeua mmoja lakini mtoto wako alipigwa risasi. Hii itakuwa na maana gani kwake sasa. Isaya atakuwa marehemu wakati taarifa hii ikitolewa.
Ghafla akabadili maamuzi na kuamua kumpigia Isaya moja kwa moja na kuzungumza naye kama mtoto mdogo anayehitaji uangalizi wa karibu. Isaya alipokea simu yake akianza na utani kwenda kwa baba yake.
Bahati mbaya hakujibiwa chochote badala yake mzee Zingo alikuwa ametaharuki na alitoa taarifa ya mapema sana na iliyotakiwa kufanyiwa kazi mara moja.
“Ondoka katika hoteli hiyo, sasa hivi, unajua maana ya sasa hivi…nasema toka hapo upesi kijana wangu, kuna mambo ya hatari yamepangwa juu yako. Fanya hima mtoto. Usiwaeleze chochote hao wahudumu wa hapo, ondoka Isaya ondoka sasa hivi” Mzee alisihi sana huku akijisahau kuwa Isaya hayuko peke yake bali yupo pamoja na msichana wake ambaye ametoka kumvalisha pete. Ni simu hii iliyozua hekaheka katika chumba alichokuwa ametegemea kulala Isaya pamoja na Betty.
Wakatoweka upesi wawili hawa bila kuwaeleza wale wahudumu wa hoteli ile juu ya taarifa ya hatari waliyopewa.
****
KADRI muda ulivyozidi kwenda ndivyo Joy alizidi kuumia, aliamini kuwa hakuna alichofanya kwa ajili ya kumsaidia Isaya wake. Akajigalagaza kitandani huku akiugulia maumivu makali ya nafsi, machozi yakaunda unyevuunyevu katika shuka lake huku yakiacha michirizi mashavuni lakini kubwa zaidi yakiweka maumivu moyoni.
Maumivu yasiyostahimilika katu! Alipoitazama saa yake ulikuwa ni usiku mnene haswaa. Mara akashtuliwa na simu yake. Nani wa kumpigia simu usiku huo. Alipoitazama aliona namba mpya!!
Mtego!!
Akahisi lakini akajikosoa baada ya kukumbuka kuwa namba yake hiyo hakuitumia hapo kabla katika kufanya jaribio. Akaipokea simu bila kusema chochote.
“Joy mama mbona makubwa huku, yaani ni hatari roho zetu mkononi kuna watu wanazisaka jamani mwee! Nakuja nyumbani kwa kweli mi s’taki mjadala hapa.”
“Kuna nini lakini?” aliuliza Joyce katika namna yua mshangao.
“Nakuja Joy mamangu nakuja nitakusimulia bora nifie mikononi mwako mwenzangu.” Alijibu Betty kisha akakata simu. Joyce akajikuta akiunda tabasamu hafifu kidogo, ujio wa Betty kidogo ungeweza kumrejeshea faraja na pia kujikuta yu katika mapambano hai.
Aliamini fika kuwa iwapo Betty hakufanikiwa siku hiyo basi amempatia muda wa kujipanga upya. Na kupambana naye kwa kila hatua.
Baada ya saa zima Betty alifika akiwa amepagawa. Hata kabla ya salamu akamsimulia
Joyce juu ya simu ambayo alipigiwa Isaya. Simu iliyotoa ujumbe hatari unaokaribia kumaanisha kifo. Joyce alifanya igizo la kusikitika, kisha akamliwaza rafiki yake huyo apumzike watazungumza asubuhi. Baada ya Betty kusinzia, Joy alifanya tabasamu jingine.
Kisha akajipongeza kwa uamuzi wake aliofikia dakika za mwisho kabisa kumpigia simu baba yake Isaya kwa namba tofauti kabisa na ile ambayo walibadilishana siku ambayo alionana naye mara ya kwanza nje ya ukumbi wa Nkrumah. Simu hii ilibeba ujumbe mfupi lakini ulionyooka, ulikuwa ni uongo uliotungwa ukatungika na mzee Akunaay Zingo akauvaa mkenge.
Karata aliyocheza Joyce ikawa karata sahihi kabisa ya kumwokoa Isaya.
Mpambano huu wa kwanza Joyce akaibuka kidedea, japo alizua hofu baina ya nafsi kadha wa kadha lakini ni heri hofu kuliko uhai kupotea kirahisi. Uhai wa mwanaume ambaye anampenda kwa dhati. Kuanzia usiku huu Joyce akajiapia kwamba ameanzisha vita ya kimya kimya dhidi ya mahusiano ya Betty na Isaya.
Joyce alikuwa na nia moja tu katika mapambano haya, alihitaji kumlinda Isaya asiukwae Ukimwi na kisha baada ya miezi mitatu akiwa amemaliza mitihani yake aweze kumtamkia bayana kuwa alikuwa akimpenda nab ado anampenda haswa. Kwa wakati uliokuwepo alihofia kuchanganya mambo, iwapo tu Isaya atamjibu vibaya basi atavurugika kiakili na kuyumba kimasomo. Joy hakuwa tayari kwa anguko hili. Hivyo akapendekeza kuwa akimaliza mitihani yake ya mwisho utakuwa wakati muafaka wa kumweleza Isaya jambo kuu kama lile.
Usiku huu ukamalizika huku nafsi ikiwa katika amani.
ASUBUHI ambayo ilianzisha siku nyingine, Joyce alianza kujiweka karibu sana na Betty huku akitaka kujua mambo yake mengi kuhusiana na Isaya. Alifanya hivi ili aweze kuzijua vyema ratiba za wawili hawa kila zinapotokea. Joyce alifurahia sana ile hali ya Betty kutojichanganya na wanafunzi wa chuo, hii ilimsaidia kumweka mbali juu ya ufahamu wa Joyce kujihusisha na Isaya kabla hajaamia kwa Betty.
Wanachuo wengi walilijua hili lakini wangeanza vipi kumweleza Betty iwapo hana mazoea nao na ilikuwa nadra sana kuonana naye?
****
ZILIPITA siku tano bila Betty kuonana na Isaya japo waliwasiliana mara kwa mara kwa njia ya simu. Betty hakuwa akilala nyumbani na kupumzika kama alivyodhani Isaya na badala yake alikuwa akiongeza mtaji wake kwa vibopa wengine wenye pesa zao. Siku ikawadia ya Betty kuonana tena na Isaya.
Bila kujua Joy ni adui yake ndani ya nafsi kwa sababu ya Isaya alimweleza kila jambo lilivyo, muda na mahali ambapo watakutana na Isaya.
“Yaani huyu mkaka anaulilia ujira wake hadi namwonea huruma ati.” Alisema Betty huku akifanya maandalizi ya mwishomwisho kwa ajili ya kwenda kukutana na Isaya. Joy alijilazimisha kutabasamu bila kusema neno lolote lile.
Mapigo ya moyo yalianza kwenda kasi tena. Alikuwa anaingia tena katika vita ya aina yake, safari hii alikuwa hajajipanga kabisa japo awali pia hakuwa amejipanga kwa shambulizi lile. Betty akaaga huku akimweleza Joy kuwa atakuwa akiwasiliana naye mara kwa mara kwa kila hatua atakayokuwa amefikia. Joy alibaki nyuma akiumiza akili yake ni kitu gani anaweza kufanya ili aweze kumwokoa tena Isaya na janga hilo lililokuwa likielekea kumkabili.
Akili ilizunguka sana bila kupata suluhisho, hofu nayo ikazidi kumwandama. Joy akatamani kumweleza Betty hata kwa njia ya simu juu ya utaabani wake juu ya penzi la Isaya, alitamani na angeweza kufanya hivyo lakini alijionya mengi sana ambayo yakakifanya kichwa chake kiume haswa. Alikosa maamuzi!! Mara akaamua jambo moja ambalo lilikuwa zito kukubaliana nalo kama litaweza kufanya kazi lakini aliamua kujiaminisha
Mara akaamua jambo moja ambalo lilikuwa zito kukubaliana nalo kama litaweza kufanya kazi lakini aliamua kujiaminisha Alitambua kuwa alikuwa na kipindi darasani muda huo ambao aliamua kuutumia katika kutimiza azma yake na kujiepusha na hatia ya nafsi kumsuta. Kama alivyotarajia Betty alikuwa akimpa maelekezo kadha wa kadha juu ya wapi walipo na nini kinaendelea, hivyo hakuhangaika sana kutambua wapi pa kuanzia, lakini kigumu kilikuwa ni nani atamsaidia katika hili jambo.
Akiwa amekitoa muhanga kipindi cha darasani kwa ajili ya kumfuatilia Betty na Isaya, Joy aliamini kuwa kuna mtu alikuwa akimuhitaji ili aweze kumsaidia zaidi katika hili. Akakumbuka kuwa katika akaunti yake kuna pesa, ni lazima na yenyewe itumike ili jambo hilo liweze kwenda sawa. Wakati akiumiza kichwa na huku dakika zikizidi kusogea mbele, mara akamkubuka Fonga, tabasamu likajisogeza kidogo katika himaya ya uso wake na kisha likatoweka upesi kama halikuwepo hapo kabla. Hakika Fonga angeweza kumfaa zaidi kwa kipindi kile. Huyu alikuwa ni kijana ambaye alikuwa shushushu wakati wa kinyang’anyiro cha taji la urembo hapo chuoni, huyu alikuwa kambi ya Kidoti. Alikuwa akizipata siri za wapinzani na kuzifujisha katika kambi anayoishabikia ili waweze kujipanga vizuri.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Fonga alikuwa mwingi wa maneno na kuna watu walikiri kuwa alikuwa na akili ya ziada nd’o maana aliwafaa sana. Wagombea mbalimbali wa vyeo kadhaa hapo chuoni walipenda sana kumtumia katika kuzing’amua siri za wapinzani. Kwa mtaji huu Fonga akawa anachuma pesa za wanaotaka kumtumia kujua mambo, kilichokuwa kizuri kwa Fonga alikuwa na timu yake ambayo watu wengi hawakuijua, ni jambo hili lilimpa wepesi katika kufanya ushushushu wake. Wakati kambi pinzani inategemea kumwona Fonga akianza kujisogeza, wanashangaa yupo amejikita na mambo yake lakini siri inapovuja ndipo hupagawa na kukiri kuwa Fonga ni kiboko.
Joyce, akaichukua simu yake na kuwapigia watu kadhaa baada ya dakika mbili akawa na namba ya Fonga kwenye simu yake. Upesi akaipiga namba ile. Hakika alikuwa Fonga, Joyce akamsihi kuwa anahitaji mno kuonana naye. Fonga aliposikia kuwa anayemuhitaji ni Kidoti hakuwa na nafasi ya kukataa. Mwanaume kwa mwanamke!!!!
Bahati ikawa upande wa Joyce, Fonga akafika upesi. Baada ya salamu mbili tatu, Joyce alimwelezea Fonga hali halisi juu ya kitu anachokihitaji kwa wakati huo. Aliufahamu vyema wivu wa wanaume hivyo hakutaka kumtajia Fonga moja kwa moja kuwa anamwokoa Isaya kutoka mikononi mwa Betty, bali alizuga kuwa anamuokoa Betty ambaye ni ndugu yake kutoka katika mikono ya Isaya.
“Yaani shida yangu ni kwa leo tu yaani. Tena leo yenyewe nd’o muda huu Fonga.” Alisihi Joyce, kisha akaendelea… “yaani huyo binti ni machachari sana….” Joyce alianza kuelezea kuhusu Betty na tabia zake, lakini hakuthubutu kusema kama ni muathirika wa gonjwa la Ukimwi, alieleza mengi ambayo Fonga aliyahitaji katika kutimiza shughuli yake. Kwa mara ya kwanza akausikia moyo wake ukimshtaki kwa kumsema rafiki yake kipenzi mbele za watu baki wasiotambua historia iliyopo kati yao. Akaunganisha meno yake kwa uchungu lakini akakiri kuwa penzi lashinda nguvu ya kiapo.
Lakini hakutaka wazo hili lifikie jibu baya la kutoboa siri!!
Fonga akashusha pumzi kisha akamweleza Joyce kuwa hakika hakuwa amewahi kujihusisha katika ushushushu wa mapenzi kama alivyotaka yeye Joyce, lakini hili halikuwa jibu pekee aliloishia. Akampa moyo Joyce kuwa kwa sababu amesema ni kwa siku hiyo tu basi atamsaidia kwa kadri ya uwezo.
“Shilingi ngapi nikuandalie sasa.” Alihoji tena Joyce. Hapa Fonga akawa mzito kiasi, kisha akamwambia ampatie pesa ya nauli tu ya taksi. Mengineyo watazungumza baadaye.
“Ujue nahofia kuchukua pesa yako kwa jambo la kushtukiza kama hili. Ngoja tupate matokeo kwanza.” Fonga alimwambia Kidoti. Kisha akamfanyia konyezo maridhawa.
Kidoti akajilazimisha kutabasamu. Akafungua pochi na kumpatia Fonga kiasi cha pesa, halafu akamkumbusha mahali ambapo walikuwepo wawili wale. Fonga akatokomea. Joyce akamtazama kijana yule kisha akakiri kwa imani nyake ya dini ambayo aliijulia ukubwani alikuwa anafanya makosa makubwa sana kumtegemea mwanadamu mwenzake, hiyo haikuwa na tofauti ya kumfanya Fonga kuwa Mungu wake. Dhambi!!
Akainama kwa aibu tele. Amemsaliti rafiki japo kwa siri chache, kisha ameisaliti na imani yake!! Pabaya hapo….. Mapenzi ni kitu gani??
*****
MAENEO ya Kinondoni Morocco, katika mgahawa wa Best Bite. Mgahawa maarufu jijini Dar es salaam. Betty na Isaya walikuwa wakipata kitu roho inapenda. Isaya aliamua wapate chakula eneo lile kwa sababu tayari alikuwa amechukua chumba katika hoteli ya Chichi ambayo haikuwa mbali sana na maeneo yale.
Wote walikuwa wanafurahia ‘chicken chips’ iliyokuwa mezani. Betty aliwasifu kutokana na kuku wao wa kienyeji kuandaliwa katika namna ya kipekee inayovutia.
Isaya naye alisifia kile alichoweza ilimradi kuusindikiza mlo wao. Walimaliza kwa kunywa juisi kushushia kile chakula. Lakini Betty hakunywa sana ile juisi akaagizia mvinyo maridadi kabisa uliotengenezwa kwa zao la ‘rozela’. Mvinyo maalum kwa ajili ya kuchangamsha mwili. Hakika ulikuwa unachangamsha!!
Taratibu huku mvinyo huku maji ya matunda, hatimaye walikuwa wameimaliza shughuli ya kukipata chakula. Kilichofuata hapo ni kulipa bili kisha kuondoka, Betty akiwa nyuma ya Isaya ambaye alikuwa amekikamata kiganja cha Betty. Haukuhitaji elimu ya chuo kikuu kutambua kuwa wale ni wapenzi.
Tena wa siku nyingi tu. Walipotoka waliangaza huku na kule kwa muda kisha wakaanza kujongea katika gari lao.
“Samahani bro…” Isaya aliitwa akageuka.
“Nani…mimi?” aliuliza kizembe huku akijiona ni yeye pekee ndiye yupo na jinsia ya kiume pale. Kijana nadhifu aliyemuita akamsogelea kisha akamsalimia na kisha kumvuta kando kidogo, biula shaka Betty asiweze kusikia kitu chochote.
“Kaka samahani, nadhani huyu uliyenaye ni mpenzi wako.” Alielezea yule kijana. Isaya kwanza hakujibu swali lile, akamtazama vyema muulizaji.
“Aaah! Samahani kama nimeuliza vibaya lakini sisi tuna shida naye.” Aligandamiza tena kijana yule. Shida gani na mpenzi wangu!!
Alijiuliza Isaya. Lakini ni kama yule kijana alikuwa katika akili ya Isaya.
“Demu wako ni tapeli!!” alijibu kijana yule. Hapa sasa Isaya akataka kugeuka mbogo, akajaribu kuidhibiti hasira yake. Akamtazama Betty aliyekuwa ametangulia ndani ya gari huku akiwa ameuacha mlango wazi. Isaya alitamani kuwatukana vijana wale lakini ghafla akaonyeshwa kithibitisho cha kumkamata Joyce, yaani ‘RB’. Hapa sasa Isaya akapagawa, jazba aliyokuwa nayo ikashuka.
“Afande Meku! Mchukue huyo.” Aliongea kiaskari sasa akiamrisha na sio kuomba, upesi mwanaume mwingine akaruka ndani ya gari kwa mbwembwe na machachari yote akamkwapua Betty. Akamshika mkono vyema kisha akmwingiza katika taksi waliyokuja nayo.
“Joraam…Joraam….sijaiba cha mtu mimi Joram, wazuie Joraaam…..” alilia huku akitapatapa Betty, kilio chake kikaufikia moyo wa Isaya. Akazidi kuhaha nini afanye lakini akapewa onyo kuwa akithubutu kufanya vurugu basi amelizuia jeshi la polisi lisiifanye kazi yake ipasavyo.
“Utakuja kumtoa kituoni na milioni tatu na laki sita za watu.” Yule bwana aliyekuwa anazungumza na Isaya aliruka garini upesi huku akimweleza Isaya maneno yale. Hakuna aliyejua nini kinaendelea, Isaya alibaki katika hamaniko akijiuliza jambo kama hilo linatokeaje. Kilio cha Betty kikamfanya azidi kuumia nafsi. Ghafla akajiona mpumbavu, akaikumbuka simu kutoka kwa baba yake kuwa kuna watu wabaya wanawafuatilia. Maskini Isaya hakukumbuka hata kuomba vitambulisho vya watu wale!!!
Sasa Betty ametokomea na hajulikani alipo!! Hajui hata ni kituo gani cha polisi aende kumuulizia. Isaya akabaki mpweke eneo lile. Akaamua kupiga simu kwa marafiki wa baba zake ambao ni maafisa wa juu wa polisi. Akawaeleza kilichotokea. Taarifa zikasambazwa katika vituo kadhaa wakingojea Betty afikishwe kituoni ili Isaya aweze kupewa taarifa.
Lakini kadri muda ulivyokwenda ndivyo hali ilizidi kuwa tata.
Jioni Joyce anapewa taarifa na baadhi ya watu kuwa mchumba wa Isaya, Betty ametekwa na hajulikani alipo. Joyce akapagawa huku akiwa amesahau kabisa kuwa aliwahi kuzungumza na Fonga juu ya mpango wa kumchoropoa Betty kutoka katika mikono ya Isaya. Hofu ikamtawala, akajitoa katika kundi la watu wengi akajiweka mahali na kumpigia simu Fonga.
Wapi!! Haipatikani. Hapa akazidi kujikuta katika sintofahamu ya aina yake. Akajaribu kumpigia Betty, na yeye hakuna kitu hapatikani. Jasho likaanza kumtoka, na akajikuta akatika msimu mbaya wa majuto.
Akahisi huyu majuto amekuja kabla hajawa mjukuu. Ilikuwa mapema sana kujutia maamuzi yaliyotoka ndani ya dakika kadhaa nyuma. Lakini atafanya nini wakati hali ilikuwa namna ile. Usiku ukafika!! Betty hajulikani alipo bado!!!
Joyce akiwa kitandani aliikosa amani kabisa. Alishindwa kulala bila kuwa anafahamu hatma ya Betty. Alihaha huku na kule. Akajikuta akitamani kurudisha muda nyuma asiweze kufanya jaribio alilofanya la kumdhibiti Betty asimwambukize Isaya Ukimwi lakini sasa anajikuta ile roho mkononi ambayo ni halali ya Betty ikikaribia kumponyoka, hakujua nini kimetokea kiuhakika lakini alisikia kuwa ni wateka nyara wamemkwapua Betty mikononi mwa Isaya kwa kujifanya kuwa wao ni polisi na wamekuja kumkamata Betty kwa shutuma za kufanya udhulumaji wa pesa taslimu shilingi milioni tatu na ushee. Taarifa hii ikamfanya Joyce aamini kuwa huenda Betty alikuwa amekamatwa na wale vibopa ambao aliwaambukiza Ukimwi huku akifanikiwa kuzitwaa pesa zaona kisha kutokomea bila kuaga. Lakini akiwaanapitiwa na mawazo haya mara simu yake iliita. Hii ilikuwa ni namba mpya akapokea upesi kabisa.
“Kidoti…..Fonga naongea hapa!!” alijitambulisha kisha akaacha nafasi kidogo ya jina lake kumuingia msikilizaji.
“Fonga,nini kimetokea kwani eeh!! Fonga amefanya nini Betty kwani..”
“Punguza papara Joy. Hili jambo ni zito kiasi fulani na hata mimi linanichanganya sana, sijui tu hata nikuelezeeje lakini naomba uelewe kuwa vijana wangu hawakufanikiwa kumpata Betty.wamefika eneola tukio lakini hawakumkuta na baadaye nasikia kuwa ametekwa.” Alijibu Fonga kwa sauti tulivu. Acha wee! Hapa sasa Joyce akaruka kutoka kitandani akaanza kupiga mayowe huku akijisahau kuwa simu yake bado ipo hewani. Akalia akimuita mama yake ambaye ni marehemu tayari.
Simu kutoka upande wa pili ikakatwa!! Joyce akauhisi ule upendo ambao alidhani unatoweka kwa Betty ukirejea maradufu na kujikuta akijutia kila kitu, hakutaka kuamini kuwa Fonga hajui lolote. Akajutia kumuamini na kumvujishia baadhi ya siri kuhusu Betty. Alipokuja kutulia na kujaribu kupiga simu tena Betty hakuwa akipatikana. HEKAHEKA!!!!
Hali aliyoikuta kwa Fonga ilimfanya afikirie upya juu ya Isaya!!
Akafikiria kumwendea bwana huyo ili amlilie katika shida yake, nafsi ilimwingia baridi sana kwa jaribio alilotaka kulifanya lakini angefanya nini iwapo mambo yanamuwia magumu kiasi hicho!! Akaishika simu yake aweze kumpigia Isaya!!
Alisita mara kadhaa, akaghairi na kuamua tena zaidi ya mara tatu. Kisha akabofya na kuanza kusikiliza upande wa pili. Simu ikaita lakini haikupokelewa!! Alipojaribu kupiga tena mara simu yake ikaanza kuita akajikuta anapokea upesi akidhani ni Isaya.
“Mambo bro Isaya!!” alisabahi..
“Kituo cha polisi Magomeni Usalama….Joyce Keto. Unahitaji kituoni haraka iwezekanavyo!! Fika upesi bila kukosa, Asante. Ukifika mapokezi utakuta maelezo.” Simu ikakatwa!!
Ebwana eee!! Joyce alitamani kukimbia, akatamani apae juu na apotee kabisa. Miguu ilikuwa inatetemeka kupita kawaida, mara mkoba mdogo aliokuwanao ukaanguka chini. Akahaha huku na kule katika kuuokota mara pikipiki zikapiga honi. Hofu hii ilikuwa kubwa zaidi, yaani anaitwa polisi? Kwa jinsi alivyokuwa anayaogopa mambo ya polisi leo hii anaitwa polisi haraka iwezekanavyo!!
Weeee! MSHIKEMSHIKE!!!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Joyce baada ya kutuliza akili kwa muda akaamua kuondoka muda huo huo kuelekea kituo cha polisi Magomeni. Njia nzima alikuwa analikumbuka onyo alilopewa la kutowashirikisha polisi juu ya taarifa na masharti aliyopewa, kwani kwa kufanya hivyo angeupoteza uhai wa Betty na yeye pia kujiweka katika mashaka ya hali ya juu. Joyce akitokea maeneo ya chuo kikuu, aliwasili Ubungo baada ya robo saa kisha akachukua basi lililompelekahadi Magomeni Usalama.
Ndani ya dakika ishirini alikuwa akitazamana na kituo cha polisi. Kwa mara ya kwanza jijini Dar es salaam. Mawazo yake kila alivyotazama kituo cha polisi yalikuwa juu ya kufungwa jela, alivyofikiri kuhusu hili akaanza kutetemeka miguu na mikono huku moyoni akifanya majuto asijue anajutia nini. Macho ya askari wa kike yakatazamana naye mbele ya mzunguko wa mapokezi.
“Nini shida!” aliulizwa Akajieleza juu ya kupokea simu ya kuhitajika kituoni pale. Alipojieleza zaidi na zaidi akaombwa ile namba ambayo ilimpigia. Wakati anataka kuitoa ile namba mara akaganda kama sanamu la kuchongwa. Macho yake yalikuwa yanatazamana na Isaya, alikuwa pamoja na polisi aliyevaa sare zake rasmi. Isaya alipomuona Joyce akanyoosha kidole kama anamwonyesha kitu yule afande.
Hapa Joyce alitamani kukimbia lakini miguu ikawa mizito!! Yule askari akamkaribia Joyce na kumuuliza iwapo ni yeye aliyepokea ile simu, Joyce akakubali kuwa ni yeye. Akashikwa mkono na kuongozwa kuelekea mahali. Wakakifikia chumba fulani hivi, huko yakaendelea mahojiano juu ya wapi asili ya Betty na ni nani yake, na kuhusu namna alivyotekwa iwapo kuna taarifa yoyote anaweza kuwanayo.
“Joyce, inavyoonekana kuna dalili kuwa unajualolote kuhusiana na jambo hili, maana kwa maelezo ya Isaya ni kwamba mlikuwanaye karibu lakini ghaflaakamvisha pete Betty ambaye ni rafiki yako, hivyo wivu wa kimapenzi ukakusababisha uchukue uamuzi wa kumteka Betty na kumfanya lolote ujualo.
Na baada ya muda mrefu kupita leo Isaya akiwa chumba cha mahojiano ulimpigia simu, bila shaka ulitaka kumweleza kuwa Betty ametoweka wewe uchukue nafasi binti” alijieleza yule askari huku akimkazia macho Joyce. Joyce ambaye hakuna hata dakikamoja aliyojaribu kuizoea hali yam le ndani alifanya jitihada za kujitetea lakini kwa sababu ilikuwa mara yake ya kwanza kuhusisishwa katika kesi ya aina hii alijikuta akijiumauma tu!
“Naapa afande, Betty ni rafiki yangu sana mimi, hakuna ubaya kati yangu mimi na yeye. Sijawahi kufikiri na sikuwahi kumfanyia hivyo!!
Naapa kabisa afande.” Alijibu huku akitetemeka. “Lakini umewahi kuwa na wivu juu yake alipovishwa pete na Isaya.”
“Hapana sijawahi afande, sijawahi hata siku moja.”
“Mbona hukuhudhuria sherehe yake kama kweli hauna wivu, tena wivu mkubwa?” aliulizwa swali ambalo lilimchanganya sana. Alikosa cha kujibu akaanza kujiuma uma kucha zake. “Na inavyoonyesha wakati sherehe zikiendelea wewe hapo na ndugu zako mlikuwa katika mpango kabambe wa kumteka Betty na Isaya, mbinu yenu chafu ikatibuliwa ndipo mkajipanga tena.
Ndo maana haukuwa katika sherehe wewe Joy. Unaona sasa ulivyokuwa muongo?” askari mpelelezi wa ile kesi akazidi kumbana maswali yenye ushahidi Joyce. Hapa sasa Joy akaona amekamatika, kweli hakuhudhuria sherehe na ni kweli muda ule aliutumia kufanya mtego wa kumzuia Isaya asifanye mapenzi na Betty ilimradi tu asiukwae Ukimwi. Mambo mengi kwa pamoja yakakizingira kichwa cha Joy. Akatamani sana kusema juu ya tukio la usiku ule, lakini bilakusema kuwa Betty ni muathirika basi hataaminika na atajiweka katika kitanzi mwenyewe, akatamani pia kusema juu ya ujumbe alioletewa usiku katika bahasha ya kaki, lakini akahofia kuwa Betty atauawa na yeye kujikuta matatani. Mkanganyiko huu wa aina yake ukamweka katika fumbo. Akakosa cha kujibu, jasho likaanza kumtoka.
“Mtoto mzuri kama wewe unajihusisha katika utekaji nyara, kwani wanaume mbona wapo wengi tu akina sisi hapa hatujaoa mbona umng’ang’anie huyo Isaya. Tatizo lenu watoto wa chuo mnapagawa sana kusikia mtoto wa mbunge…haya nd’o hautoki tena hapa.” Alisema kwa kebehi yule askari.
“Jamani afande mimi sijahusika na chochote, siwezi kumfanyia hivyo swahiba wangu siwezi mimi hata yeye akiletwa hapa sekunde hii hapa atausema ukweli lakini mimi sijui lolote afande, jamani afande mimi bado mwanafunzi nionee huruma mimi nakuomba.” Joyce alisihi, safari hii huku akibubujikwa na machozi.
Afande yule hakujali, badala yake akachukua karatasi na kalamu.
“Haya binti nyamaza, huu ni wakati wa kutoa maelezo yaliyonyooka sasa kuhusiana na utekwaji nyara wa rafiki yako.” Afande alimsihi, kisha akaanza kumuuliza maswali ya kawaida tofauti na yale ya awali ambayo yalikuwa maalum kwa ajili ya kumtetemesha.
Na hakika alitetemeka kweli!! Baada ya mahojiano Joyce pasi na kutarajia alishangaa akiingizwa katika karandinga ya polisi. Alitakiwa kuongoza njia kwenda mahali alipokuwa anaishi ili aweze kupekuliwa iwapo kuna ushahidi wowote wa kumuweka matatani.
Moyo wa Joyce ukapasuka kwa hofu kuu! Akaduwaa kama vile anaangalia filamu ya kutisha ambapo anangoja tukio moja limalizike kisha lifuate jingine. Alikuwa amekumbuka juu ya ujumbe aliotumiwa katika bahasha ya kaki. Alitamani kumwagiza mtu yeyote yule akautoe kabla hawajafika pale lakini bahati mbaya simu yake ilikuwa imekamatwa na kuzimwa tayari ili asije kuharibu upelelezi wa kesi ile. Karandinga lilifunga breki kwa fujo katika maeneo ya Ubungo Kibangu ambapo ndipo aliishi Joyce na Betty katika nyumba ya chumba kimoja na sebule, huku sebule ikigeuzwa kuwa jiko.
Askari takribani wanne walishuka kisha akatelemka Joyce, mrundikano wa watu kundi kwa kundi ukaanza kufuatilia tukio hili huku wengine wakijifanya wanajua tayari kinachoendelea. Joyce alikuwa katika fedheha kubwa ambayo hakuwahi kuitegemea hata siku moja, hakikalilikuwa jaribu ambalo alihisi lilikosea njia na kumkumba yeye. Mapenzi haya!!
Alijisemea huku akimfikiria Isaya. Laiti kama asingekuwa yeye basi asingekuwa hapo alipo. Akatamani kumchukia lakini akakosa sababu ya kumchukia maana alimpenda mtu aisyejua kama anapendwa kwa dhati!! Chumba kikafunguliwa, baada ya mwenyekiti wa mtaa kutoa Baraka za ukaguzi huo. Joyce akaingia pamoja nao ndani iwapo watahitaji upekuzi zaidi aweze kuwasaidia. Hii haikuwa kesi ya kawaida!! Polisi walikuwa wamejikita vilivyo, wakapekua kila kona, lakini waliishia kupata picha za Joyce na Betty wakiwa katika furaha. Mara maua na kadi walizotumiana kama ishara ya upendo.
Simu ya Joyce nayo ikapekuliwa lakini hapakuwa na ujumbe wowote hatarishi. Hatimaye wakafikia madaftari ya Joyce, daftari moja bada ya jingine. Sasa walikuwa wamelifikia daftari lililokuwa na ile bahasha, lilivyonyanyuliwa tu bahasha ikadondoka chini, askari akainamana kuikota.
Joyce alitamani kufanya muujiza bahasha ile isifunguliwe lakini haikuwa hivyo bahasha iukafunguliwa. Karatasi ikatolewa.
Nimekwisha!! alijisemea Joyce huku akiinama chini kungojea aibu ya mwaka ya kupigwa pingu na kisha kubambikiziwa kesi ya utekaji nyara. Karatasi ile ilikuwa imeandikwa maneno machache tofauti na awali. Polisi akasonya na kuitupa mbali, Joyce bado alikuwa ameinama akingoja maswali lakini hapakuwa na swali lolote. Polisi wakakiri kuwa hapakuwa na lolote la kuwasaidia kutoka kwa Joyce.
“Tukikuhitaji wakati wowote tutakuita kituoni na ufike mara moja kwa wakati.” Askri mmoja alitoa amri hiyo, kisha akaongozanana wenzake wakatoka nje na kuliendea karandinga.
Joyce akaketi huku akiwa haamini kabisa kama alikuwa ameachwa huru siku hiyo. Machozi yalikuwa yanamtoka na jasho jingi. Alikuwa akijiuliza ina maana hawakuelewa ujumbe katika ile bahasha, hapo akainuka ghafla na kuisaka tena ile bahasha. Huku akakutana na ile bahasha, ujumbe ukiwa pembeni lakini safari hii ulikuwa tofauti kabisa na ule wa awali.
“MAMBO SHOSTI” ujumbe uliandikwa hivyo kwa herufi kubwa!! Joyce akachoka!!
Majirani walikuwa mlangoni wakitaka kumuuliza nini kimetokea, akasimama kama anayetaka kuwasikiliza, akaufikia mlango akaufunga kisha akaingia chumbani kwake akajirusha kitandani. Tayari ilikuwa saa kumina moja jioni!!
*****
FONGA alishtushwa sana na habari za Joyce kuwa kituo cha polisi. Habari hizi alizipata mapema sana kupitia kwa Isaya ambaye alikuwa amemaliza kuhojiwa. Kwa uzoefu wake kidogo Fonga alitambua kuwa Joyce atatetemeshwa sana na kutishwa sana ili aseme hata asilolijua. Huruma ikamwingia na akawa kama anayemuona Joyce jinsi anavyohangaishwa na maswali ya polisi watukutu. Fonga akaamua kutumia nafasi hii!! Aliiona ya kipekee sana.
Majira ya saa tatu usiku alikuwa katika nyumba ya kulala wageni maeneo ya Sinza, alikuwa ametulia tuli akijitahidi kuondoa uoga aliokuwanao. Baada ya nusu saa mlango ukagongwa. Akaufungua, Joyce akaingia ndani!!
Akaketi katika mojawapo ya viti vilivyokuwa katika nyumba ile. Fonga alikuwa mwingi wa mawazo na aliyetazamika kama mtu mwenye uchungu sana. Macho yake yalipepesa huku na kule kabla hayajatua katika uso wa Joyce. Akainama chini na kuanza kutiririka maneno mfululizo ambayo yalikuwa mageni sana kwa Joyce.
“Unajua Kidoti, huwa inafikia mahali kama mwanadamu inabidi useme tu inapobidi. Ni muda mrefu sana mimi nimefahamiana na wewe japo sio kwa ukaribu kama huu wa sasa. Joyce nimeguswa sana na tatizo lako, na nimesikitika zaidi na kufadhaika niliposikia umepelekwa polisi na kisha kuondoka na karandinga, mrembo kama wewe hakika haustahili hata kidogo.
Ni kweli mimi ni maskini lakini hii haijalishi linapotokea tatizo kwa mtu ambaye unampenda. Nipo radhi kufanya jambo lolote jema hata kama linanigharimu kwa mtu nimpendaye, Joyce Kidoti mimi sina elimu labda nd’o maana nikajikuta nikishindwa kuwa imara na kukabiliana nawe wakati ukiwania mashindano ya urembo hapo chuoni, lakini sasa najihisi kama nakosa kabisa amani nikiendelea kujinyima haki hiyo.
Huenda Mungu ametuunganisha tena kwa namna ya kipekee ili niweze kujieleza kuwa nakupenda sana. Na ninakuhitaji hakika, ulipokuwa jirani na Isaya sio siri nilikuwa naumia sana. Niliumia sana kwa sababu moja tu Isaya hana mapenzi ya kweli. Na hapo alipo anafanya kuwachezea tu wasichana na kuwaacha, wewe hukustahili kuchezewa hata kidogo, mimi ni jasiri na huwa sina mpango wowote na watoto wa kike zaidi ya kujikita katika kazi zangu uzijuazo lakini kwako Joy naweza kusema nimeshindwa kabisa. Sitaki niseme mengi katika hili tatizo huenda unaweza usinielewe kutokana na wakati tunaopitia kwa sasa ambapo Betty ametoweka. Basi nakuomba tu kwa muda huu utambue kuwa ile milioni tatu, imepatikana na kama kweli hao watekaji wana shida hiyo tu basi Betty watamuacha huru!!
Haijalishi imenigharimu ama itanigharimu katika siku za usoni lakini nimeyafanya haya kwa msichana ambaye ninampenda kwa dhati” hapa akamaliza akamtazama Joy machoni. Akakutana na macho yanayong’ara kwa furaha kuu, Fonga akatambua kuwa amezipanga karata zake vizuri kabisa na sasa alitakiwa kufunga goli na mchezo uishie hapo. Joy akamrukia Fonga na kumkumbatia, alimkukumbatia kwa mambo mawili makuu kwa wakati huo, kwanza alikuwa ameongea maneno ambayo Joy aliwahi kuyasema wakati akijitoa kwa marehemu mwalimu Japhary na kisha kuukwaa Ukimwi, ‘Nipo tayari kufanya lolote kwa mtu ninayempenda’……pili alimkumbatia kwa sababu alikuwa kama malaika wa ukombozi. Hapa angeweza kumwonyesha Betty ni jinsi gani anamjali kwa kumwokoa kutoka katika mikono ya watu wabaya. Furaha ikizidi sana hupunguza uwezo wa kufikiri!!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Uchungu ukizidi vilevile huleta tatizo hilo hilo. Joyce akalala na Fonga hadi asubuhi. Alipotoka pale ndani alikuwa na milioni tatu kibindoni huku nyuma akimwacha Fonga akijiuliza ile ladha ya penzi alilolingoja kwa muda mrefu hatimaye ameipata. Watu wawili walikuwa wanaota kwa pamoja lakini ndoto mbili tofauti. Joyce akiota kumuokoa Joy kwa sababu pesa aliyoipata akiongezea na ile ya kwenye akaunti ya Betty basi jumla inafika milioni sita!! Fonga akaota ndoto ndogo tu lakini nzito, akaamua kuweka tena kichwani suala la kuoa. Kumuoa Kidoti. Baada ya muda mrefu wa kuachana na mapenzi baada ya tukio la mwenye pesa mmoja kumnyang’anya mpenzi wake aliyempenda hadharani kisha kumweka rumande kwa kesi asiyoijua, kesi iliyomfanya atumikie kifungo cha miezi tisa jela. Kitendo ambacho kilimfadhaisha Fonga na kukoma kabisa kujihusisha na mapenzi, sasa alikuwa amefika tena kwa Joyce Kidoti.
Na kisha akatangaza ndoa katika nafsi yake. Hakika ilikuwa ndoto ndogo, lakini nzito sana!! Ilikuwa nzito kwa sababu hakujua kama kuna mambo mengine mazito yalikuwa yakiendelea chini ya pazia!!
ITAENDELEA!!!
0 comments:
Post a Comment