Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

DEMU WA FACEBOOK - 5

 





    Simulizi : Demu Wa Facebook

    Sehemu Ya Tano (5)



    “Unanipenda?? Kwa misingi ipi sasa?? Yaaani ungekuwa unanipenda kweli ungeniacha niteseke hivi kweli dada!!!” aliuliza Peter

    “Ndio maana nipo hapa leo, Peter mimi ni Husna, msichana niliyekupenda na bado nakupenda sana na hadi kufikia sasa nimebeba mzigo wako katika tumbo langu…..” alizungumza huku kigugumizi kikiingilia kati.

    “Nani Husna….Husna kwa nini wanitenda hivi mpenzi wangu….kwa nini??” aliuliza Peter

    “Unaniuliza au unanisanifu, Peter ulifurahi kuuchezea mwili wangu na kuudhalilisha utu wangu….baada ya kukupa penzi langu ukaona tayari umeridhika ukanikimbia, ulitaka huyu kiumbe alelewe na nani?? Eeeh!!! Nakuuliza wewe Peter, ulitaka nyumbani wanieleweje….kwa nini unakosa ubinadamu kwanini unakuwa mnyama hivyo??.....” alishindwa kuendelea kuongea kilio cha kwikwi kikafuata

    “Nisamehe Husna….nisamehe tafadhali mimi bado mwanafunzi nilihofia kufukuzwa shule lakini kusema ukweli bado nakupenda sana Husna” Alijitetea Peter. Alikuwa anadanganya!!

    “Mwanafunzi!!!...wewe si ulisema unafanya kazi ….haya tuachane na hayo na kwa nini nilipokueleza kuwa nina ujauzito ukaamuas kuacha kupokea simu zangu” aliuliza kwa ghadhabu Husna.

    “Mhhh!!!...aaaah!!!….eeeeh!!” alijiumauma Peter

    “Sasa utakula jeuri yako” alisema Husna na kuondoka mahali pale na kuufunga tena mlango, hakujali kilio cha Peter kwani tayari hasira zilikuwa zimemkamata

    * * *CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa kama ratiba sasa katika chumba alichokuwa amehifadhiwa Peter, ni katika kijumba hicho kidogo alichokuwa anaishi askari mgambo (Omary) ambaye Peter aliamini kuwa ni askari polisi. Tangu Husna aingie ndani ya chumba kile wakati wa usiku kwenda kuonana na Peter hisia kali za kimapenzi ambazo awali zilikuwa zimeibuka tayari zilirejea kwa kasi kubwa sana, haikupita siku bila ya Husna kumtembelea Peter katika kile chumba, alimtekelezea huduma zote za muhimu ambazo Peter alikuwa akitakiwa kuzipata kama mwanadamu, aliandaliwa chakula, aliwekewa maji ya kuoga alichokosa kwa wakati ule ni hali nzuri ya hewa na fursa ya kuuona uso wa huyo anayemuhudumia, kwa imani alibaki akiamini ni Husna kama alivyojitambulisha Peter hakujua ni kitu gani kilimkumba katika nafsi yake taratibu uoga ukaanza kumwisha, akawa anayazoea mazingira yale ya pale ndani na hasahasa ukarimu uliokuwa ukionyeshwa na Husna ulizidi kumfanya ajisikie huru zaidi.

    “Husna nakupenda sana mpenzi wangu nisamehe kwa yote niliyokutendea hapo kabla” siku moja Peter alimweleza Husna wakati akipata chakula cha usiku pamoja na Husna katika giza nene wakitenganishwa na mlango wenye ‘drill’ kama ilivyo milango ya mahabusu. Alikipata wapi chumba hiki, Omary anajua mwenyewe!!! Lakini kilifaa sana kwa matumizi yake ya sasa!!! Kumwadhibu Peter.

    “Asante sana Peter hata mimi nakupenda sana, na nimesamehe yote yaliyotokea kabla” alijibu Husna kwa upole sana. Penzi la dhati likaanza kujijenga tena katika moyo wa Peter msukosuko aliokuwa amepewa na Husna lilikuwa fundisho tosha na aliamini kuwa huyo Husna ndiye alikuwa amepangwa kwa ajili yake, kiunganishi cha mtoto ambaye alikuwa amehifadhiwa katika tumbo la Husna kilizidisha upendo kati yao.

    Upande wa Husna mimba yake ilikuwa wazi sasa mama yake mzazi alikuwa amehoji mara kadhaa lakini Husna alimwambia amsubili mkwelima wake atakuja hivi karibuni.

    “Mama nimekaribia kuondoka hapa kwako” siku moja Husna alimwambia mama yake walipokuwa wameketi pamoja wakipata chai ya asubuhi.

    “Ndio huko kwa huyo mume wako ambaye huwa hutaki tumuone huwa unaenda kila siku unataka uhamie kabisa sasa” mama yake alimwambia.

    “Ndio nataka kuhamia huko ndio huko ninapoolewa cha msingi michango yenu tu na vikao vianze kukaa” kwa ujasiri alijieleza Husna.

    “Husna mwanangu unayoyasema unamaanisha kweli au ndio unataka uniaibishe mama yako mimi”

    “Nikuaibishe kwa lipi mama yangu au na wewe unadhani hii mimba nimeipata ndotoni” alijibu kwa shari kiasi fulani Husna

    “Sio hivyo mwanangu namaanisha huyo bwana amekubaliana na hii ndoa au hata hamjazungumza??”

    “Tumezungumza kila kitu na kilichobaki ni utendaji tu….nyie kama kunichangia hamtaki sawa nitajuamwenyewe cha kufanya” alijibu Husna huku akiondoka pale kwa hasira na kiburi.

    Mama Husna aliyefahamika hasa kwa jina la Kidawa hakupenda kumkera mwanaye huyo ambaye licha ya ukorofi wake bado alikuwa akitoa heshima zote kwa mama yake. Alianzia kumueleza rafiki yake wa karibu kuhusu maneno aliyoambiwa na mwanaye

    “Wewe mama Husna mwanao ana kichaa cha mimba muwaishe hospitali….we unaamini kabisa kuwa anamaanisha anachokiongea???” alihoji rafiki yake na mama Husna aliyeitwa Bi.Mwarami.

    “Ndio yeye amesema tena akirudia mara tatu tatu,sasa mimi ningemfanyaje na hapo tayari ana hiyo mimba anayodai kuwa ni ya mume wake anaitwa Peter sijui” alijibu kwa unyonge mama Husna

    “Heee!!! Makubwa hayo tena makubwa sana yaani Husna huyu mwanao leo anakuwa mke wa mtu dah!! Haya mie nakuungeni mkono na nitashiriki mwanzo mwisho maana itakuwa harusi ya kipekee kuwahi kutokea” alimalizia Bi. Mwarami na wakaagana.

    Bi. Mwarami hakuwa na kifua cha kutunza siri hata kidogo siku hiyo hiyo habari zilitapakaa kila mahari kuwa hatimaye Husna anaolewa,watu waliipokea taarifa hiyo kwa msisimko sana na kwa ari kubwa kila mtu alitaka kuona ni mwanaume yupi aliyeamua kumuoa Husna. Tetesi zilizidi kusambaa kwa kasi ya ajabu na baada ya wiki moja kila mahali alipopita Husna alinyooshewa vidole na watu mbalimbali, si watoto,kina mama, kina baba wazee kwa vijana wote walikuwa na lao la kusema

    Mke mtarajiwa!!!

    *****

    Peter alikuwa hajui mipango kabambe iliyokuwa inaendelea mtaani kwa akina Husna hakujua ni jinsi gani jina lake lilikuwa midomoni mwa watu wengi ndani ya muda mfupi sana. japo hawakumtambua kama Peter lakini alisemwa sana kama mume wa Husna!!!

    Kila mtu alitamani kumuona. Wengi waliamini kuwa nasaba za huyo mume na za Husna zinaendana!!!

    “Peter kuna jambo nimelifikiria sana na ni la busara sana katika uhusiano wetu” Husna alimwambia Peter siku moja wakiwa bado katika giza lile lile. Husna akiwa upande wa pili wakitenganishwa na kijipazia.

    “Jambo gani hilo kwani mke wangu!!!”

    “Nataka tuoane halafu wewe utaendelea na masomo yako kama kawaida wakati mimi nitakuwa mtaani nakusubiri tuanzishe maisha yetu sisi wawili” alijieleza Husna, jambo ambalo lilimshtua sana Peter, hakutegemea kabisa kulisikia katika maisha yake kwa miaka aliyonayo!!

    “Jamani Husna mbona mapema sana lakini kwa nini nisimalize shule kwanza halafu ndio tuoane??” alihoji Peter kw wasiwasi.

    “Hapana Peter haitawezekana kamwe sitaki kuzaa mtoto nje ya ndoa ni heri azaliwe wakati tayari sisi tupo katika ndoa” aliongea maneno hayo Husna yaliyokuwa na ukweli mwingi ndani yake. Mtihani!!!

    “Peter samahani mume wangu lakini nakuachia muda ufikiri na uamue” alisema Husna kisha akatoka nje na kumwacha Peter pale ndani peke yake hadi mida ya saa kumi alivyorejea kwa ajili ya kumpa Peter maji ya kuoga pamoja na chakula kama ilivyokuwa ada.

    “Husna nimekubaliana na wewe lakini tafadhali naomba shuleni wasijue kwani nitafukuzwa sheria za shule haziruhusu kuoa wakati bado mtu upo masomoni, nitafukuzwa mie ujue” Peter alijieleza punde tu baada ya Husna kuwa ameingia pale ndani.

    “Kamwe sitaingilia wala kukuharibia masomo yako kama nilivyokwambia awali mimi nakupenda na nia yangu ni kukuona ukifurahi kuliko kusikitika…na kwa misingi hiyo basi utatoka humu na hautarudi kamwe katika karaha hizi” alijibu Husna kwa upole sana.

    “Lakini Husna kwa nini hutaki mimi nikuone uso wako unajua tayari nimekusahau!!!!!” Peter alimweleza Husna aliyekuwa kimya baada ya kuwa ametoa jibu lile.

    “Mara ya kwanza uliponiona ndio kilikuwa chanzo cha hii mimba sasa sihitaji tuingie majaribuni tena maana mimi mwenyewe navutiwa na wewe na nikiiona sura yako tu nitataka huduma…..” alidanganya Husna na kueleweka vyema mbele ya Peter.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Peter aliendelea kudumu pale ndani kwa siku nne zaidi ndipo siku hii ya nne Peter akiwa katika chumba alichohifadhiwa mlango ulifunguliwa aliyeingia alikuwa ni yule mwanamgambo ambaye yeye Peter aliamini kwamba ni askari ambaye ni kaka yake Peter.

    “Shkamoo afande!!!” alisalimia Peter kwa uoga mkubwa

    “Marahaba Peter habari za siku!!!”

    “Ni nzuri sana afande” alijibu Peter huku akitetemeka mwili wake.

    “Haya nifate” aliamrisha yule mgambo na Peter akafuata,ilikuwa mara ya kwanza kutoka nje tangu aingizwe pale ndani,moja kwa moja akaingizwa katika teksi iliyokuwa imepaki pale nje, macho yake hatimaye yaliuona mwanga wa jua Peter hakuleta usumbufu wowote ule kwani alikuwa amegundua kuwa Husna alikuwa ni kiboko yake katika masuala ya mjini hivyo alitulia tuli ili asije kuzua mengine makubwa zaidi, yule mgambo akiwa na dereva wa teksi walifika hadi mbele ya eneo tulivu maeneo ya Magomeni lililosomeka ‘Mikumi Inn’ bila shaka ile ilikuwa ni nyumba ya kulala wageni Peter aliingizwa humo na kukabidhiwa chumba, alipoingia pale chumbani akiongozana na yule mgambo alionyeshwa bafu lilipo akaoga kisha baadaye akaingia mwanaume mwingine aliyekuja na mavazi ambayo Peter aliamuliwa kuyavaa hakika alipendeza sana hata yeye alijiona amependeza lakini wasiwasi wake ulikuwa ni harusi inayomsubiri, harusi ambayo katu hakujiandaa nayo. Kwa mara ya kwanza Peter akavikwa suti

    “Nitafanya nini sasa hapo!!!” alijiuliza Peter na kugundua kuwa hakuwa na cha kujitetea.Baada ya kuhakikisha kuwa alikuwa amependeza katika hadhi ya kuwa bwana harusi yule mpambaji alijiondokea na kuwaacha Peter na yule mgambo pale ndani.

    Omary kazini !! Peter matatizoni !!!

    Kapu la michango likapitishwa, hata wale waliokuwa wabahili walichanga visenti vyao. Kisa? Husna anaolewa!!! Nani asiyemjua Husna!! Kila mtu alikuwa anamfahamu mitaa ya Kinondoni shamba na mitaa ya jirani. Na hata mbali pia alijulikana Kigogo, Kurasini, Kariakoo, Tegeta, Posta, Ilala..pote huku aliwahi kuzusha matafrani. Kwanini wasimjue?? Michango ikawa michango!!.

    “Mimi nitatoa turubai!!”

    “Mimi nitaleta kreti nne za bia”

    “Kuhusu Muziki niachieni mimi”

    “Nina kikundi changu cha mnanda nitakileta bure.”

    “Picha zote za mnato (still picture) nitapiga mimi”

    “Ukumbi nitapamba mimi.”

    Haya yote yalikuwa maneno ya baadhi ya wadau waliojitolea kuidhami harusi hii!!

    Maajabu!! Kumbe Husna alikuwa anapendwa kiasi hiki!! Alishangaa mama yake.

    Sasa shughuli ilibarikiwa kufanyika. Husna akapewa kitchen party!! Makubwa haya jamani!!!

    Haya ile siku iliyokuwa inangojewa ikawadia!!! Ni wewe tu na macho yako!! Nani wa kukudai kiingilio?? Kama hukupata muda wa kwenda kushuhudia basi usinisumbue mimi niliyeenda!!

    Siku hii maeneo ya Kinondoni jambo la kuvutia na kushangaza lilikuwa linasubiriwa, watu wengi walikuwa wamemiminika chini ya turubai, ilikuwa ni harusi ambayo iliteka hisia za wengi, binti ambaye hawakutegemea kama atakuja kuolewa sasa ilikuwa siku yake ya kuitwa mke. Nyimbo za taarabu zilitawala eneo lile huku wanawake wakiwa wametingiana kanga zao zilizojaa vijembe, mara ‘utajiju’, ’umefulia mama’, ’sanamu la michelini’, ‘Choo cha kike’ na mengineyo ilimradi burudani. Macho na masikio ya watu yalikuwa kwa watoto waliokuwa wanacheza kiduku na wengine walioimba kaswida, mwenye kikundi cha mnanda aliendelea kuwatumbuiza wageni wasiokuwa rasmi na wale waliodhani kuwa wao ni rasmi katika shughuli hiyo.

    Katika kundi hilo kati ya watu wote ni mama mmoja tu aliyekuwa amenyong’onyea sana licha ya kwamba mtoto wake ndio alikuwa anaolewa lakini alijilazimisha kutabasamu,mama yake na Husna alikosa raha kwani hata siku moja hakuwahi kumuona mkwelima wake (Peter) mara zote aliishia kuonyeshwa picha hivyo hakuamini kama mtu huyo yupo duniani au ndio aibu za watu kudai michango yao waliyotoa kwa hali na mali kufanikisha sherehe hii.

    Alikuwa amejikunyata ndani ya vitenge vyake vya kupendeza akisubiri aibu itakayomkumba. Alikuwa kama aliyemwagiwa maji ya baridi!!!

    “Mama Husna mwanao amempata wapi yule kaka dah!! Pale kweli kala dume, ni mume wa ukweli ameng’ara kweli……” mama Husna aliambiwa na mwanaume aliyetoka kumpamba Peter.

    “Mh!! Wanajuana wenyewe mwanangu utawaweza vijana wa sasa????” Alijibu mama Husna kwa upole sana.

    Harufu kali ya pilau na mazagazaga mengine ilitawala eneo lote lile kwa uzuri kabisa, mchango ulikuwa ni mkubwa sana uliotolewa hivyo harusi ilifana sana, suala la chakula halikuwa tatizo hata kidogo, ratiba ilisomwa na bibi harusi alitakiwa kuingia ukumbini saa kumi adhuhuri akiongozana na bwana harusi kutokana na ratiba punde tu baada ya kufika wao ndipo chakula kingeanza kuliwa.

    Hadi kufikia saa tisa na nusu bado walikuwa hawajatokea wawili hawa wala wasindikizaji wao, ukumbi uliokuwa umejengwa kwa mabanzi imara ulikuwa umefurika, watu walikuwa bize kila mtu na lake kutokana na sekta waliyopangiw a na kamati husika. Hakika ilikuwa vyema na kupendeza kuitazama harusi hii. Kama uliikosa!!! Basi tusiulizane!! Au ngoja niendelee kukusimulia!!

    Muda ulizidi kusogea mbele na shamra shamra za kumsubiri bibi harusi na bwana harusi zilizidi kuongezeka, vigelegele miluzi na mbinja zilizidi kuvuma kwa fujo kila gari yoyote iliyoingia pale watu walidhani ndio wahusika wenyewe. Dakika zilizidi kusogea na hatimaye saa kumi ikawadia, watu walianza kulalamika chinichini kuwa walikuwa na njaa. Vile viduku vikaanza kufifia, mnanda ukalala, miduara ya taarabu ikapungua urefu. Kina mama wasema sasa makoo yakawakauka. Kila mmoja analalamika njaa. Tena wale wasiochanga ndio walilalamika sana!!

    Vituko!!

    Malalamiko haya yaligeuka maana yake baada ya nusu saa kila jicho liligeuka kujionea nini kinatokea meza ya wageni rasmi ilisimama pia lilikuwa jambo la kushangaza sana na kila mmoja hakulitegemea aina hiyo ya maharusi kuingia ukumbini hawakuwahi kuiona kamwe na ndio ilikuwa mara ya kwanza, ulikuwa msikemshike wa hali ya juu.

    Hali tete!! Nani hakutaka kuona mbele, kila mmoja kumsukuma mwenzake.

    Njaa zikasahaulika!! Ngoma za mnanda nazo zikaachwa katika upweke. Wale wacheza viduku wakasimama wima!!!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Fahari ya macho!!!

    * * *



    Kilikuwa kikao cha dharula. Tena dharula kubwa.

    Wanajeshi wawili wenye vyeo tofauti vinavyotambuliwa na serikali za vichwa vyao walikuwa katika majadiliano ya dharula sana.

    Wanajeshi hawa walikuwa ni wa jinsia ya kike mmoja akiwa Bregedia Mwamvua na Luteni Husna. Nyota nyingi zilitawala mabega yao!!

    Walikuwa wanajadili juu ya vita iliyokuwa inaelekea mwishoni. Maadui wote walikuwa wameangamizwa. Adui moja ambae katika mazungumzo haya alitambuliwa kwa jina la uficho ‘Raisi”.

    Maajabu kumbe hawa wanajeshi walikuwa wanataka kumpindua Raisi. Na hatua waliyokuwa wamefikia ni kumteka. Tayari walikuwa wamefanikiwa!! Sasa hatua iliyofuata ni kuichukua nchi!!!

    Raisi huyu alikuwa wa nchi ya Kigogo. Raisi wa Kigogo!!! Peter Isuti mjukuu wa Mioyo.

    Brigedia Mwamvua aliongoza maongezi!!

    “Sikiliza Husna, huyu mtoto tukisema tu tumpeleke kwenye ndoa za serikali atatuzidi ujanja. Na atapata upenyo wa kutupiga bao.”

    “Kwa hiyo tunafanyaje sasa…” alihoji Husna.

    “Kule serikalini, mara wataomba vyeti vya kuzaliwa..we unacho sawa je Peter..”

    “Hata mimi sina shosti..” Aliingilia Husna. Mwamvua akaduwaa.

    “OK!! Sio mbaya sana….kwa namna yoyote serikali watataka kila mmoja aape kuwa hajalazimishwa katika ndoa hii..hapa napo tutaumbuka. Peter atakukana. Ubabe wake huwezi kuwaletea polisi watakuvunja miguu wewe.”

    Husna kimya!!!

    “Lakini bado hakijashindikana kitu!!!.”

    “Mh!! Shoga ujue kule nyumbani sherehe zimeanza..”

    “Najua ndio..sasa unataka twende kwenye sherehe ama…we vipi.” Aliwaka Mwamvua.

    Husna kimya!!!

    “Twende huku nishapata wazo!!!” alimaliza maongezi Mwamvua.

    ****

    Peter alibakia pale chumbani kwa muda mrefu kidogo hadi baadaye alipoingia msichana ambaye alimfahamu vizuri sana kwani ni mara nyingi sana aliweza kubambana naye kwenye matukio mbalimbali, alikuwa amelembwa sana lakini urembo haukuonekana kubadili hali yake. binti yule alikuwa hajapendeza lakini kidogo alikuwa tofauti na aliyezoea kumuona. Aliingia pale ndani akiwa ameongozana na kundi la wasichana wawili waliokuwa na uzuri wa wastani, baada ya kumsalimia pale walimpiga maswali machache huku wakimuita shem yaani shemeji, alijua kwanini wanamuita shem ni kwa ajili ya uhusiano wake na Husna lakini ambacho hakujua ni kuwa Husna ni yupi kati ya wale wasichana. Labda Husna yupo nje?? Ama labda Husna ni rafiki yake huyu binti…..Mariam!! alikumbuka jina hilo liliwahi kutambulishwa mstarini siku binti huyo akiambatana na mama yake walileta malalamiko juu ya mimba.

    Ni siku hiyo walipomwachia namba ya Husna. Inamaana inamaana!!!...aliduwaa Peter.

    Baada ya kama nusu saa wasichana wawili waliaga na kumwacha mmoja ambaye tangu waingie pale ndani hakuwa ameongea neno lolote, Peter hakutaka jambo linaloitwa kwamba yule ndio Husna litokee hapana hakuwa tayari kuwa katika mahusiano na binti yule hata kuwa naye chumba kimoja aliona sio sawa. Kashkashi zake alizifahamu fika na kitendo cha kuthubutu kukwaruzana naye kingeweza kuleta matatizo.

    “Peter……” alijikakamua yule msichana na kuzungumza, sauti yake haikuwa ngeni masikioni mwa Peter, hakika yule alikuwa ni Husna, lakini Peter alidhani amefananisha.

    “Umenijuaje” aliuliza Peter kwa uoga.

    “Mimi ni mkeo Husna kwa nini nisikujue!!!!!” alijibu Husna kwa jeuri. Peter alibaki anamshangaa binti yule alidhani anatania lakini hapakuwa na utani yule ndio alikuwa Husna halisi. Peter alitamani kupitia ukutani lakini hizo zilikuwa ni ndoto tu isingewezekana.

    Peter aliamua kupambana aweze kutoka pale ndani lakini alitua katika mikono kakamavu ya Husna akiwa katika kukuru kakara za kujiondoa pale ndani mara ghafla, nguo ya Husna kanga nyepesi kabisa ikaagana na mwili ikajiunga na sakafu. Paja jesi tii!! Likachungulia nje. Peter akatoa yowe la la hofu!! Kibao kimoja kikamfanya awe kimya. Mrusho mmoja wawili hawa wakawa kitandani. Usiniulize suruali ya Peter ilitoka vipi katika kiuno chake!!!

    Mara ghafla mlango ulianza kugongwa. Peter akakumbuka tukio la kufumaniwa kule Kigogo. Afadhali kule alikuwa na binti mrembo. Sasa leo yupo na Husna!!! Akiwa hajajinasua bado katika mikono ya Husna ulifunguliwa mlago likaingia kundi la watu kama watano, pale pale Husna akaanza kulia kilio cha kwikwi kisichokuwa na machozi.

    Ile sauti ikawa inakoroma!!

    “Eheee!!! Huyu hapa ndio anatembea na mwanangu….na wewe unalia nini si bwana yako huyu…” mama mmoja aliyekuja siku moja pale shuleni kulalamika kwamba mtoto wake amepewa mimba na mwanafunzi wa Jitegemee alianza kugomba, Peter alibaki anajiumauma asijue la kufanya. Peter tunduni!! Wapi achomokee!!!

    sasa leo unamuoa huyu binti nasema….huwezi kumjaza mwanangu mimba halafu umuache haiwezekani nasema siwezi kulea watoto wawili kwa pamoja..nilikupa onyo siku zile ujilete mwenyewe ukajiona mjanja sasa leo.” alizidi kugomba yule mama huku wenzake wakimzuia asimkaribie Peter kwani kwa hasira aliyokuwanayo angeweza hata kumuua, mara akawaponyoka akamnasa Peter kibao kikali shingoni. Peter akatowa yowe la uchungu!! Wanawake wenzake waamkamata imara. Alikuwa anatetemeka kama anapandisha mashetani. Hofu!! Uoga!! .

    Peter hakunyanyua mdomo wake alikuwa anaogopa sana. Punde Peter alishuhudia mkeka ukitandikwa pale pale chumbani na kuamriwa kukaa yeye pamoja na Husna, kwa Husna hata halikuwa tatizo sana alikaa pale huku akijifanya kulialia akafuatiwa na Peter baadaye akafika mbele yao shehe, kosa kubwa alilolifanya Peter ni kugusa kitambaa cheupe alichokuja nacho shehe, palepale akahesabiwa kuwa amesilim yaani ameukana ukristo na kuuvaa uislamu.

    “Ataitwa Hemed huyu” shehe alimpa jina la kiislamu Peter na baadaye ndoa ikachukua nafasi yake, ndoa ya mkeka. Uzuri wa ndoa hii hakuna cha kuulizwa kama unamkubali ama la!! Hapa ni mwendo wa kijeshi. Utake usitake utaoa!!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kilichofuata baada ya hapo Peter (Hemed) alipandishwa ndani ya gari pamoja na Husna safari ya kwenda katika eneo la tukio ikafuata, Peter aliwekewa ulinzi madhubuti na mgambo watatu akiwepo Omary asije kukimbia na kuharibu shughuli, aliposhuka kwenye gari Hemed alitaka kutimua mbio lakini ulinzi uliowekwa aligonga mwamba ndio hapo aliposhikiliwa mkono wake na wale mgambo ambapo alimwongoza hadi ukumbini, jambo hilo lilikuwa tofauti sana na harusi nyingine ambapo maharusi huingia kwa mwendo wa kunyata au kwa mdundo wenye utaratibu maalum, Peter hakuamini alivyoshabikiwa na umati mkubwa kiasi kile, lakini sauti zilipanda juu zaidi baada ya Husna kuonekana, licha kwamba alikuwa hana umbo zuri lakini alionekana kuwa ‘super star’ eneo lile watu walishabikia sana na kwa wakati huu mama yake mzazi aliamini kweli mwanaye anaolewa furaha ikarejea na akawa shabiki namba moja eneo lile. Shamra shamra ziliendelea kwa fujo eneo lile huku Husna akiwa amejituliza pembeni ya Peter ambaye sasa alikuwa anaizoea ile hali ngumu kabisa.

    Ilikuwa burudani tosha, watu walishangaa hadi wakaridhika na hatimaye wakazoea ile hali waliyoisubiria kwa hamu.

    Burudani iliisha kwa maharusi kufungua muziki na wageni kujimwaga ukumbini kufurahia disco vumbi hadi wageni walipoaga na kuondoka zao kuelekea katika hoteli ya Lamada ambapo mimba ilitungwa, tofauti ni kwamba sasa kilikuwa chumba namba 18 tofauti na awali. Peter hakuwa na ujanja sasa!! Maji ameyamwaga kamwe hayazoleki.

    Onyo alilopewa na Husna kuwa iwapo ataleta ujanja ujanja atafukuzishwa shule, lilimkaa vyema kichwani. Hakuwa tayari kupoteza shule.

    Peter taratibu alimzoea Husna na hatimaye kumchukulia kama mabinti wengine, upendo wa dhati aliokuwa ameuonyesha Husna ulimteka Peter na kujikuta ameamua kutulia palepale. Kwa Husna ulikuwa ushindi mkubwa sana kwani ndoto yake ya kuolewa na Peter ilikuwa imetimia sasa. Kijana mtanashati ambaye wasichana wengi wangetamani kuolewa naye.

    Penzi lake la dhati alilokuwa amekihifadhi kwa ajili ya Peter sasa alikuwa analitenda kwa vitendo bila uoga wowote ule, Peter aliendelea na masomo akitoa taarifa kwa waalimu kuwa ametokea msibani huku Husna akitulia nyumbani kwao akilea mimba yake changa. Kagenge kadogo alikofungua kalimpatia kipato!! Walau akaweza kuilea mimba.

    “Hakika nimegundua jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza!!!” Peter alimwambia Husna siku moja alipomtembelea

    “Kwa nini wasema hivyo mpenzi”

    “Sikutegemea kama una mapenzi ya dhati kiasi hichi,nakupenda sana” Peter alimwambia Husna alipokuwa amekuja ‘geto’ kwake kumsalimia. Lakini kichwani alihifadhi maneno kadhaa!! Nikimaliza shule mi namkimbia huyu!!!

    “Asante kwa upendo wako nakupenda sana, sikutegemea kama siku moja nitakuja kupendwa kama hivi” alijibu Husna na safari yao kimapenzi ikaendelea kama kawaida kwa furaha tele.

    *****

    Husna alikuwa anabanwa hasa na kigenge chake. Asubuhi alipika chai, mchana chakula n usiku uji, makongoro na makorokocho mengine.

    Safari za Kigogo zikahamia kwa Mwamvua. Ni huyu alikuwa anaagizwa kila Husna anapohitaji kumpelekeakitu Peter.

    Peter akanenepa!!! Mapenzi ya Husna!! Geto lake likapendeza kutokana na zawadi zilizotolewa siku ya harusi!!! Peter akawa Peter kweli.

    Hadi wakati huo alikuwa akijidharau kwa mchezo aliochezewa na mabinti hawa na kuingizwa mkenge akazini na mtu asiyemtegemea!!!

    Hawa makamanda. Ni kiboko!! Alikiri Peter.

    VITA BARIDI (Demu wa fabook 2)

    Mwamvua naye ni mwanamke tena kamili. Na Peter alikuwa muhuni, hii tabia bado ilikuwa damuni japo ilikuwa imejificha. Kwa kumuogopa Husna, Peter alishindwa kumtaka Mwamvua kimapenzi.

    Mwamvua anazisoma nyendo za Peter na kugundua hali hiyo!! Na yeye taratibu anaanza kuvutiwa na mwisho wa siku anajiahidi kuwa lazima alionje penzi la Peter wakati huu ambao Husna ametingwa na pia yu mjamzito. Wazo hilo analipigia msumari. Linaanza kukomaa kichwani!!

    Mwamvua anajikuta anakabiliwa na pepo la usaliti!!

    Wawili hawa wanaanza kutamaniana. Changudoa mzoefu anaigundua hali hii. Sasa anaamua kabisa kumsaliti Husna. Kumbuka Husna amempigania sana Peter na bado anaendelea kumpigania kwa kumpa visenti kadhaa vinavyotokana na genge lake. Peter alikuwa mumewe wa ndoa!!

    Dalili za vita zinanukia. Ni vita kati ya wanawake wawili ambao wana historia za ajabu ajabu. Vita ambayo hayupo wa kuiamua. Vita isiyohitaji bunduki

    Ni VITA YA MAPENZI!!!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog