Simulizi : Ripoti Kamili : Mkasa Wa Mapenzi
Sehemu Ya Nne (4)
JIJINI Dar es salaam ni biashara iliyozoeleka kabisa ya vijana kuokota makopo tupu ambayo awali yalikuwa yametumika kuhifadhi maji ama vinywaji vingine baridi. Makopo haya tupu huuzwa kwa wanunuzi wa jumla ambao nao huyauza viwandani.
Hivyo shughuli za misiba, harusi na sherehe nyingine jijini Dar es salaam huzungukwa na vijana ama yeyote yule ambaye anafanya biashara hii. Wahudhuriaji mkinywa maji na kutupa makopo wao wanaokota.
Hata katika msiba huu walikuwepo pia watu wa biashara hii ya makopo tupu!
Ubaya wa jiji la dare s salaam, mtoto ni yule ambaye asubuhi akiamka anamsalimia mama yake na baba yake, anakula walichoamua wazazi na mchana hivyohivyo na usiku analala nyumbani. Lakini ikiwa kinyume na hapo umri wako haumaanishi wewe ni mtoto katika jiji hilo. Unaweza kuwa na miaka kumi na sita lakini kitendo cha kujitafutia kula yako basi wewe si mtoto tena, na hivi ndivyo nilivyoshuhudia katika hili pia.
Watoto wadogo walikuwa wanagombania yale makopo tupu ya maji, ilikuwa inastaajabisha sana walivyokuwa wakipeana matusi ya nguoni na ikibidi kupigana kabisa.
Ajabu sasa ni watu wazima wachache sana waliojali magomvi haya na kuwakanya lakini wengi walikuwa kama waliokuwa wamezoea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kuna wakati nilitupa kopo la maji kwa madhumuni liokotwe na mtoto mmoja ambaye alikuwa na umbile dogo kuliko wenzake na alionekana mpole sana kwa tabia, ile anataka kuliokota lile kopo akawahi mtoto mwenzake na kumkwapua. Ile anajaribu kujitetea nikashuhudia jinsi mwenzake alivyomtwanga ngumi ya mgongo bila kujali.
Yule mtoto akaanza kulia huku akilaani kitendo kile.
Nilijisikia vibaya sana na ninahisi nilipewa damu ya kupenda watoto japokuwa hadi wakati huyo sikujaliwa kabisa kupata wangu mwenyewe.
Nilimsogelea yule mtoto na kumuita akasogea huku akifuta machozi yake, nguo yaqike chakavu iliyaruhusu macho yangu kuona idadi ya mbavu zake kwa jinsi alivyokuwa amekondeana.
Nilimuuliza jina lake akanieleza kuwa anaitwa Bahati. Nikamuuliza maswali ya hapa na pale, akawa ananijibu kiufasaha nikamuuliza ni kwanini na utoto wake wote ule yupo mtaani anaokota makopo. Akanieleza kuwa anamsaidia mama yake ambaye hajiwezi kwa sababu ni mlemavu.
Nilijiskia vibaya sana, nikakipa maji ili kinawe uso wake uliojichora michirizi ya machozi.
Baada ya kunawa ndipo nikaanza kuona kitu ambacho kilikuwa kinanikumbusha mbali sana,niliiona kwa mbali sana sura ya Tina katika uso wa mtoto yuole ambaye alinieleza kuwa anayo miaka tisa.
Nilimuuliza iwapo mama yake anaitwa Christina akasema hapana mama yake anaitwa Zawadi.
Nilijiuliza je yawezekana nimemsahau Christina hadi naifananisha sura ya mtoto huyu na yake ama ni vipi? Nikakosa jibu....
Lakini ndugu msikilizaji napenda kukusihi kitu kimoja, jifunze kuziheshimu sana hisia zako ziheshimu kwa sababu kuna wakati unaweza kuzipuuzia na kujikuta umepoteza mambo mengi sana.
Hisia zangu zisizokuwa na ushahidi zilinituma kwenda kumjua mama yake kile kitoto.
Na hii ilikuwa sababu ya mimi kushindwa kwenda makaburini kwa sababu ningeweza kwenda na kisha kumpoteza mtoto huyu aliyenikumbusha kuhusu mtu aliyewahi kuwa wa muhimu sana katika maisha yangu.
Nilimuuliza mtoto yule kama akipata mtu wa kumsomesha atakuwa tayari kwenda shule akasema hata kama ni dakika hiyohiyo yupo tayari.
Nilivutiwa sana na mtazamo wake juu ya elimu, na hapo nikakumbuka kumuuliza jina lake akaniambia jina lake ni Sarafina.
Niliongozana naye kuelekea nyumbani kwao, palikuwa mbali sana lakini yeye alikuja kwa miguu kwa sababu hakuwa na namna nyingine.
Majira ya saa kumi na mbili tulifika nyumbani kwao na kile kitoto, na kweli ile kufika tukamuona kwa mbali kabisa mwanamke akiwa ameketi chini.
“Mama yuleee!” kikanieleza huku kikinyoosha mkono wake kuelekea alipokuwa yule mama.
Nilifika na kumsalimia mama yule na kumpa pole, akaniuliza majina yangu nikajitambulisha naye akanieleza kuwa anaitwa zawadi.
Nilizungumza naye juu ya maisha na nikamueleza kuwa nimempenda sana mtoto wake na sijapendezwa kumuona akihyangaika mitaani, Zawadi akanieleza kuwa hana namna kwa sababu yeye ni mlemavu na hana msaada zaidi hivyo ameshindwa kumpeleka shule sarafina.
Baada ya kuzungumza mengi nikamuulizia baba wa yule mtoto ikiwa bado yupo hai.
Zawadi akanijibu kuwa baba wa mtoto yupo hai lakini ndo hivyo hujitokeza mara moja moja sana siku akijisikia kuleta unga analeta na siku akiamua kukaa kimya anakaa hata miezi mitatu bila kusema lolote.
Zawadi alinieleza kuwa ana mengi sana yanamsibu lakini mtoto yule ni mzigo zaidi kwake kwa sababu anamuumiza sana anapolala njaa ama anapomuulizia babayake.
“Zawadi unadhani kwa nini mzazi mwenzako hamjali mtoto wake, kwanini usilipeleke hili suala ustawi wa jamii...” nilimuuliza kiutulivu.
Akashusha pumzi kwqa nguvu sana na kisha akaniambia.
“Ndugu yangu, ni heri basi angekuwa mtoto wangu ningeshikia bango mambo kama hayo, mama yake mwenyewe ni kama aliyeridhika na hali hii...” alinijibu huku akijilazimisha kutabasamu.
“Unamaanisha kuwa Sarafina sio mtoto wako au?” nilihoji.
Akatabasamu kisha akatikisa kichwa kuashiria kukubali lakini akanisihi sana yule mtoto asijue kwa sababu anajua yeye ndiye mama yake.
Nikaulizia ni wapi alipo mama yake, akanieleza kuwa mama yake si mkaaji sana ni mrukaji rukaji, leo anaruka huko mara leo hapa. Akanieleza kuwa mamam yake Sarafina ni mdogo wake wa damu.
“Leo alisema atakuja kumletea Sarafina nguo....sijui kama atakuja maana yeye na baba mtoto hawana tofauti linapokuja suala la kuahidi na kutotimiza ahadi..” alinijibu kinyonge.
Nilimuonea huruma sana mama yule, ulemavu wake na mzigo huu nao wake. Wamiliki halali hawajali kitu!!
Majira ya saa tatu usiku na dakika kadhaa hivi nilimuaga mama yule na kumsihi atamuaga Sarafina ambaye alikuwa amelala tayari.
Nikajipekua mfukoni na kutoka na notimbili za shilingi elfu kumi na kumkabidhi, alinishukuru sana nikamwambia asijali sana na nitakuwa namkuja mara kwa mara kumtazama yeye na Christina.
Neno moja nililomwambia ni kwamba, sikujaliwa kuwa tajiri sana lakini nayafanya yote hayo kwa sababu moyo wangu unanituma kufanya hivyo!!
Nikamsihi sana asimruhusu Sarafina kwenda kuokota makopo kwani ni hatari sanakwa mtoto wa kike hasahasa wa makamo yale.
Akanikubalia!!
Nikaanza kupiga hatua kutoka eneo lile nikaisikia sauti kwa mbali ikiita jina la sarafina kwa fujo.
Nilipogeuka yule mama akanieleza kuwa mama yake sarafina huyo amerudi!!!
“Sasa mbona anamuamsha mtoto!” nilihoji huku nikipiga hatua kadhaa nyuma.
“Kawaida yake huyo hapo amelewa atamuamsha atamsumbua wee hadi pombe zitakaposema imetosha!!” alinijibu huku akitabasamu.
Na mara alianza kumuita mama yake sarafina.
“Wewe mwanamke, hebu muache mtoto wangu amelala mbona unakuwa hivyo lakini Tina??” aliita kwa sauti ya juu katika namna ya kulalamika.
Ile kuita jina hilo nilipatwa na shoti kali katika mwili wangu, mapigo ya moyo yalienda kasi sana huku nikijiuliza nitazoea lini jina lile.
“Zaa wako ndo unipangie sheria...” sauti ya kilevi ya mwanamke ilijibu kutoka ndani... kisha matusi mazito yakaanza kuporomoshwa huku mtukanaji akizidi kusogea nje.
Hatimaye akafika nje alipokuwa ameketi Zawadi.
Looh! Macho yakanitoka gizani, licha ya mabadiliko yote makubwa katika mwili wa mtukanaji yule bado sura yake haikuweza kuyapotea macho yangu.
Alikuwa ni Tina!
Tina mke wangu, aliyepotea katika uso wangu miezi mingi sana iliyopita tena katika mazingira ya kutatanisha.......
Midomo ilijifumba kila nilipojaribu kuifunua, miguu iligoma kupiga hatua yoyote ile mbele.
Nilikuwa nimepagawa!!!
WATU hujiaminisha kuwa siku hizi hakuna mapenzi ya kweli na hata ukiwauliza mapenzi ya kweli yalikuwepo lini hawana jibu!! Zaidi watasema enzi za wazee wetu... kana kwamba waliishi enzi hizo na kushuhudia haya!!
Tafadhali usiwasikilize hawa, kwa sababu maneno yao ni yale maneno ya wakosaji... penzi la kweli chanzo chake ni wewe.. amua sasa kuzalisha penzi la kweli... usiishi kwa kufuata maneno ya watu.
NA HII NI SEHEMU YA KUMI NA SITA.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Looh! Macho yakanitoka gizani, licha ya mabadiliko yote makubwa katika mwili wa mtukanaji yule bado sura yake haikuweza kuyapotea macho yangu.
Alikuwa ni Tina!
Tina mke wangu, aliyepotea katika uso wangu miezi mingi sana iliyopita tena katika mazingira ya kutatanisha.......
Midomo ilijifumba kila nilipojaribu kuifunua, miguu iligoma kupiga hatua yoyote ile mbele.
Nilikuwa nimepagawa!!!
Nilidhani akifika na kunibaini sura yangu labda naye atapagawa na kuzizima kama mimi lakini ajabu aliniona na ni kama ambaye hakukumbuka lolote, hapo kweli nikakiri kuwa pombe si rafiki mzuri sana hasahasa kama utamuendekeza, Tina niliyekuwa namjua mimi ni yule Tina aliyenikanya juu ya matumizi ya vitu visivyokuwa vya msingi... akaniachisha sigara niliyoizoea, akaniweka katika mstari ulionyooka. Akaapa kuwa kamwe hatakuja kuwa na urafiki na pombe kwa sababu ilimsababishia umaskini mkubwa ulioambatana na fedheha baba yake!! Nami akanisihi nisije nikaingia katika mkumbo huo.
Leo hii namshuhudia Tina yuleyule akiwa amelewa chakari, afya yake imezorota sana.
“Tina!” nilijaribu kumuita.
“Nd’o jina langu unasemaje na wewe hanisi!!” alinibwatukia huku akikishika kiuno chake kana kwamba hapo awali tulikuwa tumegombana.
Alipomaliza kunibwatukia akamgeukia dada yake.
“sasa wewe nawe ushapewa huo ulemavu bado tu unataka wanaume.. hivi ungekuwa mzima si ungetembea na kila rika wewe..... dada uwe unaona aibu wakati mwingine”
Zawadi aliinama chini kwa aibu huku akitikisa kichwa, bila shaka aliamini kuwa Tina anazungumza jambo asilolijua hata kidogo.
Baada ya hapo akanyanyua kichwa.
“Kaka Mjuni, mzoee tu huyu mdogo wangu.... hajui alitendalo.” Alinieleza kwa sauti ya kinyonge kabisa.
Tina akaingilia kati akawa kama mbogo mwenye ghadhabu anatokwa na matusi makali ya nguoni ajabu hakuna aliyejali, bila shaka walikuwa wamemzoea tayari. Majirani walipita na kuendelea na shughuli zao bila kushangaa.
Nilimsogelea Tina huku nikishindwa kuamini eti kwa miezi hiyo michache alikuwa amenisahau... au ni mimi nilikuwa nimemfananisha!! Nilijiuliza huku nikizidi kumkaribia.
“Vipi kaka, unahamia kwangu ushamalizana na huyo mwenzako au? Naona unataka kula kuku na mayai yake!!” alinihoji.
“Tina mimi ni Mujuni... Mujuni Kalisti.....” nilijitambulisha huku nikimkazia macho yangu.
“Namfahamu Mjuni mmoja tu.... kuna Mjuni mmoja katika duniani nzima.. wewe labda fotokopi... ehee sawa Mjuni fotokopi nieleze unataka nini?” alinihoji kilevilevi.....
“Ni mimi huyo Mjuni unayemfahamu........” nilimsihi na sasa nilimfikia na kumshika mkono wake.
Nikautazama ule mkono huku akijaribu kuutoa kwa nguvu, hapo sasa akaanza kulalamika kuwa mimi ni polisi nimekuja kumpeleleza..... sikumuachia badala yake nilikifikia kile kidole ambacho nilimvisha pete siku ya harusi yetu ya kimila.
La!haula... ile pete ilikuwa palepale katika kidole kile. Ile kuigusa ile pete nikapatwa na mguso wa aina yake katika moyo wangu!!
“Ni mimi niliyekuvalisha pete hii... hakuna mwingine zaidi yangu...” nilimsihi... sasa Zawadi dadake alikuwa amepigwa na butwaa hakudhani hata kidogo kuwa tunaweza kuwa tunafahamiana.
“Niache wewe mwanaume, niache wewe ni mzimu.... mzimu jamanii mzimuuu nisaidieni..” alipiga mayowe huku akilazimisha nimuachie. Sasa majirani walianza kututazama kwa makini wakijongea eneo lile.
Hapo nikakumbuka jambo moja la mwisho ambalo nilihisi linaweza kusaidia kwa kiasi fulani. Niliukumbuka wimbo fulani wa kizazi kipya ulioimbwa na msanii aitwaye Dito unaoitwa Tushukuru kwa yote. Wimbo huu Tina aliyekuwa kama mimi tu ambao hatukuwa wapenzi wa nyimbo hizo lakini huu alikuwa akiupenda sana na ni yeye pia alinishawishi mimi kuupenda wimbo ule. Niliupenda sio tu kwa sababu Tina aliupenda bali niliupenda kwa sababu kila mstari ulikuwa na maana kubwa katika penzi letu... ni wimbo uliokuwa unatia moyo, unaimarisha penzi na pia kuamsha hisia thabiti......
Nilijikohoza kidogo na kisha nikayafumba macho yangu na kuhamia duniani yangu pekee dunia ambayo nilijiona ninaishi mimi na Tina tu hakuna aliyekuwa anatutazama. Na hapo nikaanza kuimba kama nilivyozoea kumuimbia.
“Kwa pamoja tutazame hapa tulipo
Anatuonyesha picha ya mbali huko tuendapo
Mengi utasikia yakisemwa usiweke moyoni
Kuteleza inatokea mambo ya ndani usiyalete hadharani
Kama ndege njoo turuke angani woote
Nikushike unishike ili tuwe woote!
Mvua ikinyesha iwe Baraka ya penzi letu
LOLOTE LIKITOKEA BASI TUANGUKE NA TUFE WOTE”
Nilimuimbia kipande hicho ambacho na yeye alikuwa akiniimbia mara kwa mara hasahasa nikiwa nimekwazika.....
Naam! Hakuna kitu kinaleta kumbukumbu na hisia kali kama nyimbo, msisimko uliompata Tina ulionekana dhahiri baada ya kuwa nimefumbua macho.
Tina sasa hakuwa na papara tena bali alilegea na kisha akaangukia magoti, na hapo alianza kuangua kilio kikubwa, sio kilio kwa sababu ya kuongozwa na pombe bali alikuwa akiumizwa na uwepo wangu pale. Alikuwa amekumbuka mbali Tina wangu!!
Alinisihi sana niondoke na akiamka pale aichukulie kama ndoto tu, alizungumza mengi sana ya kujutia hakika alisikitisha sana, hata kama una moyo mgumu lazima huruma ingechukua nafasi.
Nilibaki kimya nikimsikiliza tu.... huu ulikuwa usiku wa aina yake... sasa watu walianza kujaa na hakuona aibu yoyote ile kuendelea kuzungumza......
Alinieleza kuwa Mungu aliye hai anamuadhibu, sasa hana mbele wala nyuma yupoyupo tu... na alikiri kuwa anaamini kwa zaidi ya asilimia sabini atakuwa ameathirika.
“Ni heri nife kwa UKIMWI ili adhabu ikamilike, mimi si mwenye haki hata kidogo Mjuni, mimi ni wa kufa tu na ninastahili yote haya ninayopitia...” alizungumza Tina kwa uchungu mkubwa. Na hapo dada mtu hakuwa na swali, alikuwa ameanza kuupata mwanga.
Nilimsihi Tina asiendelee kuzungumza mbele ya watu na nikamuomba niondoke naye.
“Hapana Mjuni... hapana utaniua mjuni.....” alikataa. Nikamsihi kuwa mimi ni yuleyule na kamwe sijawahi kubadilika hivyo aniamini.
“Maneno yako yataniua mjuni..... yataniua.... niache tu nife kwa UKIMWI!!” alizidi kusihi.
Niliona nizungumze naye tena kidogo huenda atanielewa.
“Tina, hata mimi nimewahi kufanya makosa mengi sana na nikasamehewa.. hakuna mwanadamu ambaye hajawahi kufanya kosa... wewe ni nani hadi ujipe adhabu kubwa hivi....” nilimuhoji.
“Mjuni.... mimi ni mchafu, changudoa, mlevi, sina utu hata kidogo... yule Tina uliyemuoa akakuonyesha mapenzi si huyu wa sasa huyu ni shetani. Niache Mjuni na uende zako.... niliyokufanyia yanatosha....” alinijibu huku akilia......
Kilio cha Tina kiliniumiza sana kwa sababu alikuwa analia akimaanisha na ni kama alikuwa anayeombea nyakati zirejee nyuma. Na haikuwezekana......CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ndugu msikilizaji, ni kweli sikuwa na hisia za kimapenzi na Tina lakini kwa mwanamke niliyeanza naye maisha kuanzia chini, tukapanda hadi juu upendo ule wa kawaida tu usingeweza kufutika. Na hasahasa nilivyomtazama katika hali aliyokuwanayo basi ulikuwa wakati ambao alikuwa ananihitaji zaidi.
Nikaendelea kumsihi aongozane nami na hatimaye akakubali, nikachukua ruhusa kwa dada yake na kumuahidi kuwa siku inayofuata nitarejea nikiwa pamoja na Tina.
Wakati huo swali kuu lililokuwa linanisumbua ni juu ya Sonia... yupo wapi mtoto yule niliyempenda na swali jingine lilikuwa juu ya sarafina nilitaka kujua ni lini alimzaa mtoto yule na ni nani baba yake!!!
***Naam! Ndugu msikilizaji je? Ndo Ripoti inafikia ukingoni au ndo kwanza inanoga...ni nini hatma ya wawili hawa......
UKWELI HUMWEKA MTU HURU WAHENGA WALISEMA, lakini yapo mazingira ambayo ukiutanguliza ukweli basi unakuwa mwanzo wa kuwa mtumwa...... na ukiuficha huo ukweli unakuangamiza kabisa. Je kipi bora kuwa mtumwa ama kuangamia......
Nikaendelea kumsihi aongozane nami na hatimaye akakubali, nikachukua ruhusa kwa dada yake na kumuahidi kuwa siku inayofuata nitarejea nikiwa pamoja na Tina.
Wakati huo swali kuu lililokuwa linanisumbua ni juu ya Sonia... yupo wapi mtoto yule niliyempenda na swali jingine lilikuwa juu ya sarafina nilitaka kujua ni lini alimzaa mtoto yule na ni nani baba yake!!!
Sikuona kama ni jambo la busara sana kumpeleka Tina nyumbani kwangu, kwanza mchana ule sikuwa nimeenda makaburini kumsindikiza Freddy aliyekuwa ametutoka baada ya kujinyonga hivyo kuonekana na mwanamke pale ningeweza kuleta tafsiri nyingi sana mbayambaya machoni kwa wapangaji wenzake, na jambo la pili ambalo nililihofia lilikuwa juu ya kukosa uhuru sana. Kama marehemu Freddy na mkewe walipokuwa wanagombana kila mtu aliweza kusikia vipi kuhusu mimi kuzungumza na Tina. Sikutaka jambo hili liwe matangazo kwa kila mtu...
Nikaamua kumchukua Tina hadi katika nyumba ya kulala wageni yenye hadhi ya wastani.
Ndani ya kile chumba baada ya Tina kurejea katika hali yake ya kawaida alianza kuzungumza na kunisihi sana nisimuulize maswali na badala yake nimsikilize tu huenda mazungumzo yake yanaweza kutatua maswali yangu.
Na kweli Tina alianzia pale palipokuwa pananitatiza...
Akanikumbusha mara kadhaa alivyokuwa anaweweseka usiku enzi za raha katika ndo yetu, akanikumbusha pia jina alilokuwa akilitaja mara kwa mara hadi nikafikia hatua ya kumuuliza hilo jina ni la nani...
Aliposema hivi nikakumbuka kuwa alikuwa akiota sana jina la Sarafina!!
Hapa sasa nikaanza kuupata mwanga huku nikipata pia cha kuongeza katika Ripoti yangu.
Kumbe nilimuoa Tina akiwa tayari yu na mtoto mkubwa tu. Na kuhusu huyo mtoto ambaye ni Sarafina alijazwa mimba na mwanaume tapeli wa mapenzi aliyemdanganya kuwa akimzalia atamuoa. Ile kubeba mimba na mambo yakabadilika, mwanaume akawa haeleweki mara leo aseme hivi na kesho anabadilika kama kinyonge. Hadi unafika wakati wa kwenda hospitali kujifungua bado alikuwa hana msimamo, baada ya kujifungua maisha yakawa magumu sana na mwanaume akiwa haonekani mara kwa mara.
Tina akawahi sana kumwachisha titi sarafina ili aweze kuingia mtaani kupambana kumtafutia chakula, na hapo ndipo akaanza kumuacha mikononi mwa dada yake ambaye ni mlemavu.
Tina alifuta machozi kidogo kisha akaendelea kusema kuwa kutendwa vile na yule mzazi mwenzake haikuwa sababu kubwa sana ya kuwachukia wanaume na hata hapo anapozungumza hajawahi kuwa na chuki na wanaume wote kwa sababu anaamini wazi kuwa wapo wanaume wanao upendo wa dhati kabisa.
Maisha yalivyozidi kumpiga ndipo kama bahati akakutana na mwanaume wake wa kwanza kabisa aliyemtoa usichana wake. Alikuwa amechakaa vibaya sanaalipokutana na mwanaume huyu... na hapa akajikuta akiingia penzini angali mwanaye alikuwa mdogo sana.
Tina anakiri wazi kuwa alifahamu kuwa anafanya makosa lakini tatizo ni kwamba alikuwa muhitaji zaidi.
Hapo nikamuingilia kati na kumuuliza wazazi wake walilichukuliaje jambo hili na kwa nini hakuwaomba msaada.
Tina akatabasamu na kisha akaanza kujitukana yeye kisha akawatukana na wasichana wote wanaofanana na yeye katika jambo hilo la kudanganyika. Akaelezea kuwa aliibeba ile mimba nje ya matakwa ya wazazi wake ambao walimuapia kuwa iwapo atabeba mimba nje ya ndoa basi watampa laana, hivyo alipoibeba mimba hii alijidanganya kuwa wataoana upesi na yule mwanaume hivyo hata wazazi hawatajua kama alikuwa na mimba kabla ya ndoa. Na hata wakijua atakuwa ameolewa tayari haitakuwa na uzito...
Baada ya bwana yulekuikataa mimba ile basi ikabidi hata wazazi wasijue. Dada yake mlemavu wa miguu akamsaidia kuitunza siri....
Akashusha pumzi zake kishaakaendelea......
“Huyo mwanaume kweli alinifaa sana katika kipindi kile kigumu, na kwa sababu alikuwa mwanaume wangu wa kwanza sikuwa na mashaka naye na ninakiri kweli nilimpenda na nilitamani sana anioe.... hata yeye sikumueleza iwapo nibna mtoto tayari,nilikuwa najisikia vibaya sana kumkana Sarafina wangu kwa wanaume lakini nililazimika kufanya vile kwa sababu baadhi ya wanaume wakisikia una mtoto hata mpango waliopanga juu yako unaisha...” akasita Tina akanitazama na kuniita jina langu nikaitika.
“Bila shaka umemjua tayari baba yake Sarafina... nikikueleza kuwa mimi ni mchafu sana kwa maneno matupu hauwezi kunielewa lakini jaribu kufikiri mtoto wa kwanza haya huyo sawa utasema nilimpata kabla sijaolewa na wewe haya na huyu wa pili naye nikampata kwa ujinga ujinga tu.....” alisonya kisha akavuta pumzi na kuzishusha kwa nguvu.
Tina aliendelea kusimulia hadi akafikia kwenye lile tukio ambalo nilikuwa nalihitaji sana, nilitaka kufahamu baada ya kutoroka nyumbani akiwa pamoja na Sonia ni wapi alielekea na ni wapi yupo Sonia.
“Niliyopitia ni mengi sana Mjuni nakusihi usiklize tu kwa sababu hata nisipoyasema ndo tayari yametokea na hayawezi kubadilishwa!!” alitoa kauli ile na kunifanya nibaki njia panda nikijiuliza ni kitu gani kilitokea huko nyuma. Wakati najiuliza haya nilikuwa pia najiuliza nitahimili vipi kupokea taarifa eti kuna namnanamna zilijitokeza Sonia akaaga dunia.
Nilikuwa nampenda sana mtoto yule.
“Sonia yupo wapi Tina?” uvumilivu ulinishinda nikajikuta nauliza....
Sonia badala ya kujibu alinitazama sana machoni moja kwa moja, kisha akainama na kuinuka tena......
“Mjuni Kalisti...” akaniita jina langu kikamilifu.....
Nikajikakamua na kuitika....
“Wewe ni mwanaume wa kipekee...” alisema huku akilazimisha kutabasamu.
“Tina tafadhali nieleze kuhusuSonia kwanza tafadhali nieleze.....” nilimsihi na hapo wasiwasi ukizidi kuchukua nafasi katika moyo wangu.....
“Nitaeleza kila kitu bila kuacha neno lolote Mjuni ninachoomba ni usikivu wako tu......”
Kauli hizi za Tina ziliendelea kunitafuta vibaya mno.........
**ehee! Ni kitu gani kilimtokea Tina na Sonia kuanzia alipotoroka hadi alipo hivi sasa?
Usiikose sehemu inayofuata... itakupa baadhi ya majibu......
MAISHA ni darasa lenye somo jipya kila siku. Wewe ni mwanafunzi katika darasa hili, ombea sana kila kukicha kuwa usije kuwa mfano kwa wanafunzi wenzako kujifunzia..... na inapotokea moja kati yenu anakuwa mfano jitahidi sana kuufanyia kazi mfano huo.
Kuna mengi sana huwatokea wanadamu wenzetu ambayo ni sawasawa na darasa la bure kabisa kwetu lakini wanadamu hufunga macho yao ili wasione na masikio yao ili wasisikie kisha kesho yake wanafanya kosa alilofanya fulani na kuambulia majuto....
Baada ya mimi kuamua kutulia na kumweleza Tina kuwa sitaingilia akizungumza ni hapo alianza kuelezea lile tukio la usiku ule mnene.
Haikuwa mpango wake lakini majuto yalimuongoza kufanya kile alichokifanya, kunyata usiku mnene wakati mimi nimelala hoi nikiwa nakoroma akamchukua mtoto wake nanguo chache za mtoto pamoja na zake, akaichukua pochi yake iliyokuwa na akiba kiasi ya pesa na hapo akanitazama nikiwa nimelala usingizi akanipungia mkono huku akinitupia busu la hewani kisha akaondoka zake dhamira ikiwa inamsuta kabisa kuwa halitakuwa jambo la heri hata kidogo kuendelea kuishi na kunitazama usoni wakati amenitendea mambo mengio mabaya,.
Safari yake hii haikumuhusisha mtu mwingine zaidi ya yeye kuwa mratibu wa kila kitu, alipoutoa mguu wake nje alijenga chuki rasmi dhidi ya wanaume wengi. Historia yake ilimuonyesha jinsi wanaume walivyosaidia kuyaharibu maisha yake, huku wawili kati yao wakimuachia kumbukumbu ya maisha yote. Walimzalisha watoto.....
Mtoto wa kwanza akitelekezwa huku huyu wa pili akiiharibu ndo kati yake na mtu aliyempenda yaani mimi Mjuni.
Tina akajiondokea kinyongea hadi kituo cha mabasi akapanda basi linaloelekea wilaya ya Kilindi huko Tanga.
Huko alikuwa anaishi rafiki yake wa kibiashara waliyefahamiana wakati ule anafanya biashara ya kuuza nguo.... ni huyu ambaye alimweleza kuwa anahitaji ampokee huko, japokuwa hakumueleza ni jambo gani linampeleka huko.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa safari ndefu sana iliyogubikwa na wimbi kubwa la mawazo kichwani mwa Tina, yote yaliyotokea alikuwa hajayasahau na yalikuwa yanamsulubu.
Alifika Kilindi na kupokelewa na huyo rafiki yake, hakumueleza kiundani sana yaliyojiri lakini alimueleza kuwa anaomba apumzike walau kwa siku kumi kisha atapata uelekeo mwingine.
Rafiki yule hakuwa na hiyana akamuhifadhi Tina, lakini siku mbili tu zilitosha kufahamu fika kuwa baridi kali kupitiliza katika wilaya ya Kilindi lilikuwa ni tatizo kwa mtoto Sonia.
Kifua kilianza kumbana mara ikawa kikohozi na akawa anashindwa kupumua vyema.
Wataalamu wa afya wakamshauri Tina amwondoa mtoto upesi katika wilaya hiyo kwani hali ile ya hewa ni hatari kabisa kwa usalama wake.
Wakati huo Tina hana pesa na rafiki yake yule alikuwa amesafiri kibiashara. Alijaribu kuwasiliana naye kwa njia ya simu na kumuo9mba msaada wa upesi lakini rafiki hakuwa akipatikana kwenye simu na pale nyumbani alikuwa amebaki na msichana wa kazi tu.
Tina angefanya nini angali alikuwa mgeni katika mji huo??
Alilazimika kuendelea kusubiri, lakini ukaja usiku ule ambao Sonia alizidiwa sana. Alikuwa anatetemeka sana na alionekana dhahiri kuwa hawezi kupumua vyema... haya yalitokea majira ya saa nne usiku.
Tina hana pesa, hana mtu amjuaye pale na rafiki hapatikani kwenye simu... msaidizi wa kazi hakuachiwa pesa ya kutosha zaidi ya shilingi elfu tano tu ya dharula kwa sababu ndani kila kitu cha kupika kilikuwepo.
Elfu tano ingesaidia kitu gani......
Hakiuweza kufaa kitu...
Mzazi hawezi kukubali kumtazama mtoto wake akiteseka atajaribu kufanya kila kitu ili kuweza kuitafuta nafuu ya mtoto....
Tuina akaona suluhu ni kuwasha jiko la mkaa ilimradi tu kulitafuta joto kiasi...
Unaweza ukawa umeishi mikoa na wilaya nyingi zenye kusifika kwa baridi... lakini kama haujaishi Kilindi.. huko kuna baridi haswa!!!
Kweli jiko likawashwa, na joto likapatikana walau. Na kitoto kikapunguza kutetemeka... sasa hata kutabasamu kilitabasamu...
Tina akapata tumaini jipya akaendelea kumbembeleza mtoto hadi akalala.
Tina akaingia katika dimbwi la mawazo, aliwaza siku za usoni za mtoto yule zitakuwaje na yeye pia akajiuliza baada ya siku kumi alizoomba ni wapi ataipeleka aibu yake??
Mawazo haya yakamtesa sana Tina hata akajikuta anasinzia bila kujua alisinzia saa ngapi......
Majira ya saa sita usiku alikuja kugutuka kutoka usingizini huku akipigania pumzi zake, alihema juu juu sana......na hakujua ni kitu gani kilisababisha hali hii.
Alipoipata nafuu akarejea kukinyanyua kitoto chake....
Naam! Hapa ikatokea taswira inayoumiza isiyofaa kusimuliwa mara kwa mara, Sonia alikuwa amekauka kau kama kipande cha mti mkavu.... alikuwa wa baridi kabisa....
Sonia hakuwa na uhai!!
Lile jiko waliloliacha linawaka liliendelea kuitumia hewa ya oksijeni ambayo Sonia na mama yake pia walikuwa wanaivuta usiku ule.
Tafadhali mpenzi msikilizaji wa mkasa huu, kamwe usije kuthubutu kulala na jiko la mkaa ndani na likiwa limewashwa... mkaa unatumia hewa ya oksijeni kuendelea kuwaka na wewe unatumia hewa ya oksijeni ili uendelee kuishi.....
Vita kati ya jiko la mkaa na mwili wa mwanadamu siku zote jiko la mkaa hushinda na mwanadamu huambulia mauti!!!
Asalaale! Tina akawa ameuchoma na kuupondaponda moyo wangu, kwani kati ya kila kitu nilichotaka kusikia kutoka kwake basi kimojawapo ni juu ya Sonia kupoteza uhai... sikuwa tayari kabisa kwa jambo hili hata kidogo. Lakini sasa Tina alikuwa amenieleza kuwa Sonia hakuwa anaishi tena alikuwa mfu!!!
Nilitaka kusema neno lakini ningesema neno gani la kubadili ukweli huu... sikuwa na neno lolote lile la kusema.
Nikabaki kulia kama mtoto mdogo, Tina akafika na kunikumbatia mabega yangu na kisha akaniomba sana msamaha...
“Kwa hiyo Sonia mlimzika wapi? “ nilimuuliza Tina kwa utulivu huku nikiyafuta machozi yangu.
Tinaakazishusha pumzi zake kwa nguvu na kisha akaendelea kunisimulia....
USIKU ule ulikuwa mrefu sana kwake aliomboleza sana kifo cha mtoto wake, msaidizi wa kazi aliamka na kusaidia kuomboleza na hatimaye majirani kadhaa walifika katika tukio hili lakini hawakuwa wakaaji sana walipita kutoa pole kisha wakamuacha Tina na maiti yake.
Hali hii ilimuonyesha Tina waziwazikuwa huu mzigo wote ulikuwa wake...
Alipoteza fahamu na kuja kustuka alfajiri akiwa bado yu na mwili wa mtoto wake alianza upya kumuita Sonia ili aamke na kumkumbatia lakini haikuwa kama alivyotaka iwe...
Majira ya saa nne rafiki yake alifika kutoka katika safari yake ya kibiashara.... alimweleza Tina kuwa akiwa safarini alipoteza simu hivyo hakuweza kufanya mawasiliano ya aina yoyote ile.
Akamtia sana moyo na kishaakashauri kuwa siku hiyohiyo Sonia apumzishwe kaburini!!
Tina alikataa kata kata na bila shaka alikataa kwa sababu aliamini labda Sonia ataamka baadaye.....
Katika purukushani za hapa na pale Tina alipoteza fahamu na zilipokuja kurejea Sonia alikuwa amezikwa tayari...
Kilio cha Tina kiliendelea kudumu zaidi na zaidi hadi siku alipomuomba rafiki yake nauli ili aende mbali na ardhi ya Kilindi kwa sababu kamwe hatakoma kulia....
Na hakutaka kuliona kaburi la mtoto wake kabisa, alipoulizwa sababu hakuwa na sababu alichoomba ni kuondoka tu!!!
Ikawa kama alivyohitaji... rafiki yule akamsaidia nauli na kumtakia mema popote atakapokuwa.
**Ni nini kilifuata baada ya kuingia jijini Dar es salaam??
Na nini hatma ya Ripoti hii kamili...
Usikose sehemu inayofuata
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mamlaka ya kuhukumu si yetu wanadamu... na kama yangekuwa yetu basi dunia isingekuwa sehemu salama ya kuishi. Hakuna mwanadamu mwenye utashi kiasi cha kufahamu huyu ni mwema na huyu si salama.
Wanadamu tunaongozwa na hulka, kama utamuhukumu mwenzako kwa hulka na mitazamo yako binafsi kumbuka na wewe wapo watakaokuhukumu hivyohivyo...
Ukihitaji kuhukumu hakikisha kwanza umeiandaa ripoti kamili.
Na je utajuaje kuwa ripoti yako ni kamili????
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment