Simulizi : Ripoti Kamili : Mkasa Wa Mapenzi
Sehemu Ya Tano (5)
Tina alikataa kata kata na bila shaka alikataa kwa sababu aliamini labda Sonia ataamka baadaye.....
Katika purukushani za hapa na pale Tina alipoteza fahamu na zilipokuja kurejea Sonia alikuwa amezikwa tayari...
Kilio cha Tina kiliendelea kudumu zaidi na zaidi hadi siku alipomuomba rafiki yake nauli ili aende mbali na ardhi ya Kilindi kwa sababu kamwe hatakoma kulia....
Na hakutaka kuliona kaburi la mtoto wake kabisa, alipoulizwa sababu hakuwa na sababu alichoomba ni kuondoka tu!!!
Ikawa kama alivyohitaji... rafiki yule akamsaidia nauli na kumtakia mema popote atakapokuwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tina aliondoka na kufanya safari hadi jijini Dar es salaam. Ilikuwa ni safari ambayo hakuelewa hata ina maana gani hasa na ilibaki kidogo tu wazo la kujiua limpitie kichwani mwake kwa sababu alijiona ni mtu asiyekuwa na thamani yoyote ile katika dunia.
Lakini wazo hili likaingiliwa na wazo jingine akamkumbuka sarafina mtoto wake. Akaona kuna namna fulani ya kutomtendea haki yule mtoto iwapo ataamua kumuacha duniani akiteseka pamoja na dada yake mlemavu.
Alipofikiria jinsi maisha yalivyo magumu na baba wa mtoto bado anaishi akajiapiza kuwa atafika jijini Dar Es salaam na kumshurutisha yule mwanaume aanze kumuhudumia mtoto wake. Tina akajikuta kwa mara ya kwanza akiwa na roho mbaya kabisa dhidi ya yule mwanaume.
“Mjuni.. nilikuwa nipo tayari hata kuua kama ingebidi... ni huyo aliyeanzisha njia mbaya katika maisha yangu na kisha kunitelekeza pasi na msaada madhubuti...” alizungumza Tina kwa hasira sana. Mimi nilikuwa mtulivu nikichukua neno kwa neno huku nikiendelea kuichambua ripoti yangu kichwani. Hasahasa vile vipande vya ripoti ambavyo nilikuwa sijamsomea Tina..... lakini sikutaka kumuingilia kwa sababu alikuwa yu katika morali nyingine kabisa.
Tina aliendelea kusimulia juu ya safari yake na hapa akafikia kuelezea jambo ambalo lilinifanya nimuonee huruma na kuyasahau kwa muda mengi aliyonikosea.
Tina alinieleza kuwa kweli alifika jijini Dar es salaam na kwa sababu hakuwa mgeni wa jiji hilo alifanikiwa kuwapata marafiki kadhaa wa mzazi mwenzake. Wakamuelekeza anapopatikana na kweli akafika kwa mwanaume huyo.
Mapenzi acha yaitwe mapenzi, hasahasa mtu ambaye mmechangia naye damu tayari na kuwa na kiunganishi cha mtoto, Tina alimkuta yule bwana akiwa anaishi na mwanamke mwingine. Hakutaka kuleta vurugu zozote zile kwa sababu hata yeye alikuwa ameolewa tayari, tatizo lilikuwa ile hali ya yule mwanaume kumkana Tina na kusema kamwe hajawahi kuzaa naye.
Hapo Tina akavumilia akaondoka, lakini ajabu yule mwanamke ambaye alikuwa ni halali kwa wakatio ule kwa yule mzazi mwenzake Tina akaropoka jambo la kidhalilishaji kwa Tina.
Tina aliyevurugwa na maisha tena aliyetoka kumpoteza mtoto wake mdogo akaona isiwe tabu ni heri amnyooshe kidogo yule dada. Na kweli akafanya vile akifanikiwa kumnasa vibao vitatu vikali kabla yule mwanaume hajaingilia kati kisha kumpeleka Tina hadi kituo cha polisi kuwa amekuja kumfanyia vurugu nyumbani kwake.
Tina akaingizwa rumande alipokaa kwa siku tatu kabla ya kuachiwa baada ya mashemeji zake wa zamani kufanya mpango hilo jambo likapita.
Kwa sababu hakuwa na pa kwenda akalazimika kwenda kuishi kwa siku hizo kwa hao waliomtoa rumande.
Walikuwa ni vijana waliokuwa wanaishi maisha ya kibachela al maarufu kama ‘maisha ya geto’. Angefanya nini Tina na hakuwa na pa kuelekea, ikawa siku ya kwanza ikawa ya pili na hatimaye siku saba zikapita akiwa anahudumiwa na mashemeji hao wawili ambao usiku walikuwa wanalala chumbani huku yeye Tina akilala sebuleni. Moyoni alitambua wazi kuwa ni hatari sana kwa sababu kuwa shemeji haibadilishi mihemko ya kiume.
Akili yake haikuwa imepata njia mbadala ya kufanya hadi usiku ule wa manane ambapo mashemeji wale waligeuka kuwa viumbe hatarishi kwake.
Walikuja wakiwa wamelewa na bila shaka walikunywa kwa ajili yake.....
“Mjuni mume wangu.... nilitetemeka sana na kuwasihi sana wasifanye wanachotaka kufanya lakini hawakuwa wakinielewa... japokuwa walikuwa wamelewa lakini walikuwa na nguvu sana. Na tatizo kubwa ni kwamba nilikuwa nimelala nikiwa na nguo nyepesi tu, kwa sababu nguo zangu nilikuwa nimezifua.
Nilijaribu kupiga kelele lakini haikusaidia kitu... mashemeji zangu zamu kwa zamu walisaidiana kunibaka... niliumia sana Mjuni niliumia moyo wangu.....” alishindwa kuendelea kusimulia Tina na kuanza kububujikwa na machozi huku akitokwa na kilio.
Nikaingia katika jukumu la kumbembeleza Tina aliyekuwa anaugulia katika hali inayogusa moyo sana.
Nilipomkumbatia Tina niligusana na mbavu zake, alikuwa amekonda sana... sio Tina yule niliyekuwa namkumbatia enzi zile!!
Tina baada ya kutulia aliendelea kunisimulia kuwa alipoteza fahamu na zilipokuja kurejea alijikuta yupo jalala asilolifahamu na watu wachache wakiwa wanamshangaa.
“Mjuni kama uliniombea mikosi naomba sana msamaha wako, nimelaaniwa Mjuni.... nimelaaniwa.....” alilalamika Tina huku akiendelea kulia.
Nilimueleza kuwa hakuna baya lolote nililowahi kumuombea.
Tina akatabasamu na kisha akaelezea kuwa kwa aliyoyapitia haiwezekani hata kidogo kuwa yametokea bila sababu.
Kuna jambo moja ambalo nilitamani sana Tina anielezee ili niweze kuufunga ukurasa wa Ripoti yangu lakini niliona hajanieleza. Nikamueleza kama ananiruhusu na mimi nizungumze, akasema nimwachie kwanza amalize yote kisha ataniachia nafasi.....
Na hapo akaelezea juu ya safari yake ya kutoka Dar kuelekea jijini Mwanza...... akaniambia kuwa anajisikia vibaya sana kunieleza alipata vipi nauli lakini nielewe tu kuwa alifika jijini Mwanza na kumkuta mtoto wake akiwa salama katika uangalizi wa mama yake mkubwa yaani Zawadi dada yake.
Chuki yake kwa yule mtoto ilikuwa inakuja pale alipokuwa akiiona sura ya baba yake katika uso wake... lakini anakiri kuwa hakuwahi kuacha kumpenda mtoto wake kamwe kwa sababu ilikuwa ni damu yake.
Lakini chuki dhidi ya wanaume ndiyo iliyomfanya awe kama nilivyomkuta.....
“Tina.. ni nini hasa kilikusibu ulipokuwa Mwanza hadi ukaanza kunywa pombe na yote haya mapya ninayoyaona kwako....” nilimuuliza kiutulivu.
Tina akaniuliza swali.
“Mjuni una moyo mgumu sana natambua lakini sidhani kama upo tayari kulisikia na hili nqa kulipokea!! alijibu huku akinitazama.
Nikamsihi sana kuwa nipo tayari kusikia jambo lolote lile... Tina akaniuliza mara mbilimbili kama nitaweza kuvumilia!!
Swali hili la kujirudiarudia lilinitia mashaka kidogo japokuwa nilijiaminisha kwake kuwa nipo tayari kusikia na kupokea lakini kiukweli nilikuwa naogopa.
Na tena tusichoke katika kutenda mema na katu tusihesabu maovuya wenzetui ili kuukadiria wema wa kuwatendea..... malipo ya wema ni makubwa kuliko wema wenyewe!!!!
Na hii ni sehemu ya ishirini!!
“Tina.. ni nini hasa kilikusibu ulipokuwa Mwanza hadi ukaanza kunywa pombe na yote haya mapya ninayoyaona kwako....” nilimuuliza kiutulivu.
Tina akaniuliza swali.
“Mjuni una moyo mgumu sana natambua lakini sidhani kama upo tayari kulisikia na hili nqa kulipokea!! alijibu huku akinitazama.
Nikamsihi sana kuwa nipo tayari kusikia jambo lolote lile... Tina akaniuliza mara mbilimbili kama nitaweza kuvumilia!!
Swali hili la kujirudiarudia lilinitia mashaka kidogo japokuwa nilijiaminisha kwake kuwa nipo tayari kusikia na kupokea lakini kiukweli nilikuwa naogopa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tina aliniomba niende nje kumchukulia maji anywe kisha tutazungumza vizuri. Nikaitazama saa yangu na kugundua kuwa ilikuwa yapata saa tano na nusu usiku tulikuwa tumezungumza kwa masaa mengi sana na bado yalikuwa hayajaisha mazungumzo yenyewe.
Nilijipekua na nilipohakikisha kuwa ninayo pesa mfukoni nilimuaga Tina kwa kumbusu shavuni huku nikitoa tabasamu ambalo niliamini kuwa litamuongezea tumaini ambalo hakuwa nalo tena.....
Njia nzima nilikuwa namfikiria Tina na kitu ambacho alikuwa anahitaji kunieleza, sikupata duka lililokuwa wazi nikawqauliza watu wachache niliokutana nao wakanieleza kuwa nizidi kwenda mbele kuna duka moja huwa linafungwa ikiwa tu mwenye duka ameamua lakini kwa masaa zaidi ya ishirini na mbili huwa lipo wazi.
Huo mwendo niliuona mrefu sana kwa sababu nilitamani tu kukaa pamoja na Tina ili anieleze ni jambo gani hilo zito ambalo alihitaji kunieleza na hapohapo akiwa amejawa na hofu tele kuwa sitaweza kulipokea.
Hatimaye nililifikia lile duka nikanunua maji na kisha upesi nikaanza kutembea kurejea kule nilipomuacha Tina.
Nikiwa nimetembea mwendo mrefu kiasi nikakumbuka kuwa nimempa muuzaji noti ya shilingi elfu tano na katu hakunirudishia mabaki baada ya huduma ile.
Nikasimama kidogo nikiwa katika kujiuliza maswali iwapo niiache tu ile chenchi ama niiruduie.
Nikachekecha kichwa kidogo na hatimaye maamuzi yangu yakawa kurejea dukani kuitwaa iliyo halali yangu nikijisemea kuwa Tina yupo na ameamua kuwa na mimi usiku huo hivyo hakuna cha kuwahi!!
Nikarejea dukani na kudai haki yangu nikapatiwa na kuondoka, lakini sikufika mbali tena nikaona banda la chipsi nikajisemea kuwa Tina wangu hakuwa amekula chochote zaidi ya zile pombe alizokuwa amekunywa hivyo lingekuwa jambo la hekima kumpelekea chakula pia.
Naam! Nikaagizia chipsi mayai na mishkaki mitano kwa ajili yangu na Tina!!
Huduma ilichukua muda kidogo kwa sababu moto ulikuwa umeanza kufifia lakini baada ya nusu saa hivi nilipata kuhudumiwa.
Naam! Nikaondoka huku nikiwa na imani tele nafsini kwangu.
Hatua moja ikifuatiwa na hatua nyingine nikakifikia kile chumba nilichomuacha Tina. Kilikuiwa tulivu kabisa kama nilivyokiacha tu, nami nikaingia kwa kunyata ili ule ukimya ubaki vilevile na kama Tina amesinzia basi nikamshtukize anikute nipo ndani ya chumba.
Nikapiga hatua na kuingia ndani... kweli Tina alikuwa amwelala lakini hakuwa ametulia alikuwa akijirusha huku na kule mapovu yakimtoka mdomoni na macho yake yakigeuka huku na kule.
Palepale nikauachia mfuko ule wa chipsi na kopo la maji, miguu na mikono ikiwa imekosa ushirikiano nilianza kutetemeka.
Nikamfikia Tina na kuanza kumtikisa lakini mara nikaacha baada ya kugundua kuwa nilikuwa namwongezea mtikiso wakati alikuwa anatikisuika tayari.
Hapo sasa nikajikuta natokwa na yowe kubwa sana la kuomba msaada.
Yowe lile la kujirudia mara kwa mara linkawaamsha wateja na wahudumu wa nyumba ile ya kulala wageni.
Hapo hekaheka zikaanza nikiwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa kila kitu kinakuwa sawa, Tina alikuwa amekunywa sumu!!
Nilikuwa nahaha huku nikishangaa ni kwa nini Tina amekuwa na nafsi iliyojawa na ubinafsi kiasi hiki! Yaani licha ya kumsihi kuwa sina tatizo wala kinyongo naye bado ameenda kunywa sumu!!
Nikakumbuka kuwa aliniambia kuwa jambo analotaka kunieleza ni zito sana na haoni kama naweza kuhimili kulipokea na kulihifadhi katika moyo wangu.
Dah! Kumbe jambo lenyewe ndo hili, kujiua!!
Hakika sikuwa tayari kulishuhudia na kulihifadhi moyoni jambo lile. Tina aondoke wakati Sonia naye ameondoka tayari...
Hapana haikuwa sawa hata kidogo kwangu.
Nilikuwa nalia kama mtoto wanaume wachache niliokuwanao katika hekaheka hizi walinitia moyo na kunieleza kuwa machozi hayasaidii kitu chochote badala yake nijikaze tu.
Ndugu msikilizaji, waweza kuwa mmoja kati ya watu ambao huwatia moyo watu wengine lakini hakuna kitu kigumu kama kutiwa moyo katika mazingira kama haya, wale wanaokutia moyo unawaona kama wasioelewa hata kidogo jambo wanalokueleza.
Na ndivyo ilivyokuwa hata kwangu. Ilikuwa ngumu kuwasikiliza watu hawa........
Tulipofanikiwa kumtoa nje kitu cha kwanza tulimlazimisha Tina kunywa maziwa akiwa hana fahamu sawia hivyohivyo kweli jitihada kiasi fulani zikazaa matunda akaanza kutapika na wakati huo teksi ikafika tukampakia hadi hospitali.
Ni huko Tina alipoupata uhai tena na uhai huu ulikuja nikiwa pembeni yake.
*****
Punde baada ya kurejewa na fahamu Tina mtulivu kabisa alipepesa macho huku na kule....... kisha akakohoa kidogo na kunieleza.
“Kwanini hamkuniacha nife... ni kitu gani unataka kwangu Mjuni. Niache Mjuni. Niache nife tu....” alizungumza kwa utulivu huku akipepesa macho huku na kule.
Sikujali maneno aliyokuwa anasema Tina badala yake nilifurahia tena ule uhai wake na sauti kutoka katika kinywa chake.
Hakika moyo wangu haukuwa tayari kushuhudia Tina akimfuata Sonia.
Baada ya kimya cha muda kupita Tina alianza kuzungumza kana kwamba eneo lile yupo peke yake na hakuna anayemsikiliza. Ilikuwa sauti ya chinichini lakini niliweza kumsikia na kumuelewa kwa sababu chumba kilikuwa kimya sana.
Alielezea juu ya safari yake ya Mwanza kisha akatajka majina kama ya wanaume sita tofauti na hapo akatikisa kichwa na kutabasamu peke yake. Akanieleza kuwa kamwe hakuwahi kujua eti ipo siku atapitia njia ya uchangudoa kwa hiari yake mwenyewe lakini akiwa jijini Mwanza huku akiwa na jeraha la kubakwa na kudhalilishwa alijikuta akiiona thamani yake haiishi tena katika ulimwengu huu na hapo lolote akawa anafanya.
Akajiingiza katika ulevi uliokithiri, uvutaji wa sigara na hatimaye uchangudoa. Na hapo akauelezea kuwa huu ulikuwa mwanzo wa mwisho wa safari ya maisha yake...
Akanigeukia akiamini kuwa sijaelewa lile neno lake
“Mjuni mimi ni wa kufa tu... nimeathirika Mjuni na sio jana wala leo.... nina miezi mingi tu na muda wowote ule nitakufa.” Tina alinieleza huku akitabasamu kwa kujilazimisha na macho yake yakilengwa lengwa na machozi.
Nilidata ghafla na mwili wangu ukapooza sabna, nilihisi kiubaridi kikali sana kikipenya katika mwili wangu.
Tina akaendelea kuniomba sana msamaha na kisha akaniambia kuwa kama yawezekana nimpe tu sumu anywe kisha nimpe msaada wa kumzika....
Maneno haya ya Tina sikutaka kuyasikia hata kidogo hasahasa alipokuwa anazungumzia jambo la kujitoa uhai.
Ni kweli alikuwa ameathirika labda lakini bado hiyo haikuwa sababu kuu ya kujitoa uhai......
Bila shaka alikuwa hajapata mshauri mzuri.
Nilipiga goti chini kisha kimoyomoyo nikamuomba Mungu wangu kuwa iwapo nimekutana na Tina ili niwe nafasi ya pili katika maisha yake basi na anijaze nguvu lakini kama Tina ni shetani na nimekutana naye bahati mbaya nikamuomba Mungu aniepushie mbali huku nikikumbuka pia kumueleza Mungu ninayemuamini kuwa mitihani ya mateso niliyopitia inatosha aniepushe kama huu nao ni mtihani.
Mungu ninayemuamini mimi anaishi, hilo ndilo ninaloliamini hadi wakati huu ninapokusimulia mkasa huu wa mapenzi.
Niliamini pia katika ombi langu hili atanipa jibu stahiki kabisa ambalo litanifanya nisirejee nilipotoka.
Naam! Asubuhi nikajisikia amani kabisa kuondoka pamoja na Tina na hapa tulienda moja kwa moja nyumbani kwangu......
Sikujua ni kipi nitafanya kwake angali amevikwaa virusi tayari lakini niliamini kuwa kadri ninavyopiga hatua moja mbele na ndivyo majibu yatakavyojileta yenyewe.
Hatimaye hadi tukafika nyumbani kwangu......
Tina akawa mgeni wangu mgeni niliyeishi naye kwa tahadhari kubwa sana ili asije akajaribu kujiua ama kujifanyia lolote baya.
Kwa juma moja niliishi naye huku nikijitahidi kumfikisha vituo vya ushauri nasaha, alipoimarika nikampangishia chumba chake mwenyewe eneo lisilokuwa mbali sana na nilipokuwa naishi. Nikampatia mtaji kidogo ili afanye biashara yake ya kumuingizia kipato, sikuwa na mashaka na uwezowake katika kupambana......
Naam! Maisha yakaanza upya yakiwa na tumaini tele upande wa Tina na tabasamu la kutosha kwangu mimi...CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Katika tumaini na tabasamu hili akaingiolia kati bwana mmoja aliyeitwa Abduli.........
Huyu akauleta mwisho wa ajabu wa mkasa huu........
MAPENZI upofu wahenga walisema.....
Unaweza penda usipopendwa , ama unaweza kuangukia sehemu ambayo unahisi kwako ni sahihi lakini mwishowe inakuwa kinyume na hapo.......
NA Hii ni sehemu ya ishirini na moja.
Washauri wa kisaikolojia wanayo nafasi kubwa katika maisha yetu. Watu wengi hujikuta wakifanya maamuzi mabovu kwa sababu ya kuathirika kisaikolojia na kuikosa tiba walau ya kiushauri tu.
Hata kwa Tina ingeweza kuwa hivi iwapo tusingekutana lakini ya Mungu mengi...
Tina alipata washauri wazuri waliomjengea kujiamini na kisha kumpa tumaini jipya la kuishi!!
Tina aliendelea na biashara zake huku mimi peke yangu nikiwa na utambuzi kuwa yu muathirika wa virusi vya Ukimwi!! Alichoniomba sana ni kwamba nisimvujishie sirio yake kwa watu wengine....
Wakati huo hata mapenzi kwa Sarafina yule mtoto wake aliyekuwa amebakia yalikuwa yamerejea kwa hali ya juu...
Kiafya Tina alibadilika na taratibu ule mvuto wake wa zama zile ukarejea. Hakuwa akifanania na changudoa ama aina yoyote ya msichana ambaye ananunulika kwa bei nyepesi...
Na kama ilivyo kawaida ya wanaume bila kujua mwili wa mwanamke umependezeshwa na nani huishia kuziruhusu tamaa zao ziwatawale na kisha kurusha ndoano.
Wengine waliopewa jibu la hapana walijiondokea zao, lakini tatizo lilikuja kwa kijana mtanashati aliyeitwa Abduli. Huyu alienda kwa gia ya kumuoa Tina kabisa...... Tina akajitetea kuwa dini ni kikwazo yule bwana akatangaza ndoa ya bomani, lakini Tina akazidi kuweka ngumu.
Huyu hakwenda kama wenzake wa awali walivyojaribu kumshawishi Tina huyu alitumia njia ndefu sana......
Kwanza alijiingiza kama mteja wa Tina, baadaye akaketi naye na kumuomba wafanye biashara ile pamoja, Tina akakubaliana naye kwa sababu alionyesha nia.. kweli wakafanya biashara ile kwa mafanikio, hatua kwa hatua ukaribu ukazidi kuongezeka na hatimaye yakafikia hapo yalipokuwa yamefikia.
Nakiri kuwa kuna muda Tina alipokuwa akinieleza juu ya Abduli nilikuwa naguswa na pepo la wivu lakini kwa usalama wa afya yangu nilikuwa napuuzia wivu ule......
Nilimsihi sana Tina afuate kile alichotueleza daktari kuwa ajitahidi sana kuwa na imani na asivisambaze virusi maksudi kwa kushiriki ngono zembe.
Sasa Tina alikuwa anakabiliana na kijana Abduli ambaye alikiri kuwa alikuwa mmoja kati ya watu waliomfanya akue kibiashara na pia alikuwa rafiki yake wa karibu sana ukiniondoa mimi.
Maisha yakaendelea kwenda mbele na ukaribu kati ya Tina na Abduli ukaendelea kuongezeka, Tina hakuacha kunishirikisha kuwa mara kwa mara Abduli ameendelea kumsihi juu ya kuwa naye katika mahusiano.
Siku hii alikuja na wazo moja ambalo liliyazua mengine mengi......
Tina akashauri kuwa niigize kana kwamba mimi ni mpenzi wake ilimradi tu Abduli aache kumsumbua. Sikuona kama ni wazo bay asana kwa hapo awali kwa sababu yule tayari aliwahi kuwa mke wangu na hatukuwahi kutalikiana......
Kweli ikawa siku ambayo Abduli alikumbushia juu ya jibu lake kwa Tina, akaelezwa kuwa mimi ndiye mpenzi wake.
Kitu ambacho tulikosea ni kwamba hatukujua kuwa moyo wa mwanadamu ni kichaka hujui ameficha nini humo.
Abduli alikuwa anamaanisha aliposema anampenda Tina hivyo kitendo cha Tina kumueleza kuwa anaye mpenzi tayari lazima tu kingemvuruga kwa kiasi kikubwa sana.
Kweli alivurugika!!
Japokuwa hakuonyesha mbele ya Tina wakati uleule lakini ni dhahiri shahiri kuwa alichanganyikiwa......
Na maamuzi ya mtu aliyechanganyikiwa mara nyingi huwa ni maamuzi mabaya.
Hata alichoamua Abduli hakikuwa kitu kizuri kabisa.
Kwanza alivunja mawasilino na Tina kwa muda na kisha akajenga chuki ya waziwazi kwangu.
Awali kila alipokuwa akienda nyumbani kwa Tina walipita nyumbani kwangu kunisalimia.... hili likaishia pale. Hata tulipokuwa tunakutana barabarani hakuwa tayari kusalimiana na mimi.
Mapenzi jama mapenzi! Yanaweza kukufanya ukafanya mambo ya kipuuzi bila kujua kama ni wewe unayafanya.
Nilikuwa namsikitikia sana Abduli......
Kitu kimoja ambacho mimi na Tina tulikisahau ni kujiuliza je nini kinafuata baada ya kumfanyia vile Abduli?
Tuliposahau kuwaza hilo yeye Abduli aliwaza nini kinafuata baada ya kumkosa Tina?
Alichokiwaza nd’o kilichokuja kuleta mshtuko!!
*****
Siku hiyo ilikuwa ni jumamosi tulivu kabisa jijini Mwanza, siku hii jioni baada ya shughuli zangu za hapa na pale nilijisogeza katika mgahawa mmoja wenye hadhi ya kati kwa ajili ya kupata kinywaji huku nikitazama mechi ya soka nakumbuka ilikuwa ni Manchester united na Liverpool zote za uingereza, mimi ni shabiki wa klabu ya Arsenal lakini mtanange huu kamwe huwa sipo tayari kuukosa.
Nilikuta shamra shamra katika mgahawa ule, mashabiki wakipeana vijembe hapa na pale, nikafika na kuchukua nafasi nikaagiza kinywaji...
Baada ya dakika tano mechi ikaanza.
Ilikuwa mechi kali sana kiasi kwamba ilizichota akili zangu kwa dakika zotwe arobaini na tano hadi ukafika ule muda wa mapumziko ndipo nikakumbuka kuitazama simu yangu.
Nilikuta kuna jumbe nne mpya.. nilipozifungua zote zilikuwa zinatoka kwa Tina. Nadhani sikuzisikia kutokana na yale makelele ya mashabiki lukuki
Ujumbe wa kwanza uliuliza nipo wapi, ujumbe wa pili ulisema njoo, ujumbe wa tatu ulisema tafadhali njoo kwangu nimelewa, ujumbe wan ne ukasema tafadhali Mjuni nakuomba.
Nilibanduka upesi kutoka kwenye kiti nilichokuwa nimekaa na kutoka nje. Nikazisoma tena zile meseji na kugundua kuwa zilikuwa zimetumwa dakika thelathini zilizopita.....
Swali nililojiuliza ni kwamba imekuwaje Tina akaanza tena kunywa pombe wakati alikuwa ameacha kabisa hata ile ya kuonja....
Pili nikaikumbuka vyema ile tarehe huku nikijisemea isijekuwa ni sikukuu ya wajinga tarehe mosi Aprili!!
Hapana haikuwa!
Hapo nikajionya kuwa chelewa chelewa utakuta mwana si wako, nikachukua pikipiki upesi na kumpa maelekezo ya wapi anatakiwa kunipeleka.
Akaondoa chombo chake kwa kasi ya kawaida ambayo niliridhika nayo,moja kwa moja hadi nyumbani kwa Tina.
Alinifika nikashuka upesi maana pesa yake nilimlipa mapema kabisa.
Nikaufikia mlango wa chumba cha Tina na kuugonga mara moja ile naugonga nikaona unafunguka kumaanisha kuwa haukuwa umefungwa kwa ndani.
Kwa sababu nilikuwa mwenyeji sana pale niliingia tu bila kusita.
Kweli harufu ya pombe ikanipokea.....
Na Tina alikuwa amelala kitandani dhahiri akionyesha kutotambua lolote linaloendelea duniani. Nilimtikisa kama mara mbili na hapo nikatambua jambo jingine, alikuwa amejifunika ama amefunikwa shuka tu na ndani hakuwa amevaa kitu chochote......
Haikuwa kawaida ya Tina kulala kizembe namna hii..... labda baada ya kukaa mbali nami ndo alianza tabia hii.....
Nilimtikisa sana lakini bado hakuonyesha kurejewa na fahamu zake vyema, uzuri ni kwamba mapigo yake ya moyo yalikuwa yapo sawa na alikuwa anapumua vyema.
Kwa sababu alikuwa amelala bila kushusha chandarua chake niliamua kukishusha chandarua asiendelee kuwapa mbu faida.
Wakati nashsha chandarua nikakutana na pochi ya kiume pale kitandani..... mshtuko ukanikumba. Ni nani alikuwa yu pamoja na Tina pale kitandani....
JIFUNZE kuwa mtu wa kusamehe, baba yetu wa mbinguni anatusamehe kila siku... kama yeye anatusamehe sisi kwa nini sisi kwa sisi tusipeane msamaha??
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Na hii ni sehemu ya ishirini na mbili
Nilibaki katika butwaa kwa muda nilipoifungua pochi ile, nilikutana na picha ya Abduli.
Moyo wangu ulikufa ganzi, kijana muhangaikaji ambaye alikuwa mchapakazi kabisa alikuwa amefanya kitendo cha kizembe kabisa, kitendo cha kumnyewesha pombe Tibnaili ashiriki naye mapenzi.
Tina ambaye alikuwa ni muathirika........
Nilibaki katika utulivu uleule nikimtazama Abduli katika picha iliyokuwa katika pochi ile.
Nikatazama huku na kule kuwa huenda hata alitumia kinga.. sikuona dalili yoyote ya ganda lililotumika.
Ndugu msikilizaji, sikuumizwa bna kitendo alichomfanyia Tina kijana huyu, nilisikitishwa na ukungu ulotanda katika macho yake na hata asijue kile anachokifanya kuwa ni kosa kubwa ama la!
Niliichukua simu ya Tina kisha nikazitafuta namba za Abduli nilijua tu kuwa lazima waliwasiliana kabla Abduli hajaenda nyumbani kwake. Kweli ilikuwa hivyo.... lakini nilipotaka kupiga simu ile nilipata mashaka nitamueleza nini aweze kunielewa.
Kwa jinsi ninavyoyajua mapenzi, kwa lolote nitakalomweleza lazima atadhani ni wivu wa mapenzi unaonituma sema nisemalo.
Nikaachana na namba ile nikabaki kungoja Tina apatwe na fahamu.
Nilingoja hadi saa sita usiku ndipo Tina alizinduka kutoka kitandani.
Aliniitakwa jina la sabduli na kisha akaniuliza ni kwa nini nipo pale hadi giza lile.....
Baada ya kuona kimya akayapekecha macho yake na kutambua kuwa si Abduli bali ni Mjuni.
Tina akabigwa na butwaa akanbiuliza nilifika pale muda gani nikamueleza kuwa aliponitumia ujumbe niende kwake ndo muda niliokwenda.
Akatulia kwa muda akijiuliza kwa sauti ya chini ni ujumbe upi alikuwa amwenitumia.....
Na mara akakurupuka na kuketi kitako.... akaanza kuongea hovyohovyo kama mtu aliyepandisha mashetani.
Akaelezea kana kwamba tukio lile ndo kwanza linataka kutokea akasema kuwa Abduli alimchanganyia kilevi asichokijua katika juisi aliyomletea na anakumbuka alimuona akimpapasa kabla fahamu hazijamtoka.......
Wakati anamalizia kusema hayo nilimwona akijitazama katika maungo yake.
“Mjuni... Abduli ame... amenibaka jamani...” alisema Tina na kisha akaniangukia mapajani na kuanza kulia akiomboleza kwa hilo lililotokea. Nilimtia sana moyo na kumweleza kuwa yeye si chanzo cha jambo hilo hata kidogo hivyo asilie sana badal;a yake ni vyema tu ampe taarifa Abduli ili akapime afya yake.
“Noo! Mjuni sipo tayari mtu mwingine aijue afya yangu zaidi yako wewe....” alikataa Tina katakata. Na mimi nikamuunga mkono wazo lake hilo lakini huruma yangui ikiwa kwa Abduli kijana mchapakazi aliyeponzwa na tamaa zake za kimwili.”Nilikuahidi siku ya kwanza kabisa nitakuwa nawe kwa shida na raha... basi hata sasa sitakuwa upande wa mtu mwingine zaidi yako Tina..” nilimwambia huku nikimkumbatia kwa nguvu sana.
Ndugu msikilizaji wa mkasa huu wa mapenzi. Niliwahi kukuelezeni kuwa unaweza kulisubiri jambo fulani kwa muda mrefu na kamwe lisitokee na kukufanya ukate tamaa lakini kuna jambo linaweza kuja kwako kwa ghafla bila wewe kutarajia na kukufanya upigwe na bumbuwazi.
Ilikuwa hivi kwangu Mjuni mimi niliyepitia mengi huku nikitaraji kuwa na siku njema za usoni lakini majanga yakawa upande wangu kila kukicha.
Hatimaye ikafika siku ambayo walau nilipata kutasamu, siku hiyo Tina mwenye furaha aliomba kukutana na mimi. Akanieleza kuwa ameenda kwa madaktari bingwa na kisha kuomba ushauri juu ya jambo fulani na ameambiwa kuwa yawezekana kabisa japokuwa kuna gharama kiasi.
Nilimuuliza ni jambo gani akanieleza kuwa kuhusu gharama wala nisiwe na wasiwasi kwa sababu gharama zote zimelipwa tayari na kilichobaki ni kutelekeza tu jambo lenyewe.
Nilikuwa sijaelewa alikuwa ana maana gani Tina, nikabaki katika kusubiri atakalosema.
Kati ya siku ambazo Tina alizungumza mafumbo ya kunichanganya sana basi ni siku hii.. kila alichokuwa akisema kwangu ilikuwa ni msamiati mkubwa na mzito sana.
Na muda wote alikuwa ni mtu wa kutabasamu ama kucheka cheka bila mimi kuijua sababu bali yeye na nafsi yake!!!
Mwishowe akanieleza kuwa anahitaji kunizalia mtoto!
Nilishtushwa na kauli ya Tina na kuzidi kuvurugika zaidi... Tina ni muathirika na bado anasema anataka kunizalia mtoto hii inamaanisha nini hasa?
Nilijiuliza huku nikimtazama alivyokuwa akinisoma uso wangu!!!
Tina aliniambia nisimame kisha akaniambia nimsogelee, nikamsogelea na kumkumbatia kwa nguvu sana.
“Mjuni Kalisti, umekuwa nguzo kuu katika maisha yangu kulikoni hata wazazi wangu ambaowalikata tamaa juu yangu... umekuwa nuru mpya katika njia yangu mbovu. Na zaidi umekuwa mwanaume kati ya wanaume ninaowajua.....” akasita na kunitazama usoni. Bado alikuwa anatabasamu.
Akaendelea kunimwagia sifa kemkem mimi nikawa najibu asante.
Baadaye akaiendea pochi yake na kutoka na karatasi kama nne.
“Hizi ni nini” nilimuuliza. Akacheka kisha akaniambia nizisome.....
Nilichokuwa naambulia ni kuona herufi tatu tu ‘H.I.V’ lakini mengine sikujua yana maana gani.
“hiyo ya bluu ni Bugando hiyo nyingine Angaza, na hiyo nyekundu ni Seketulee” akanijibu Tina akiwa bado mwenye furaha.
“Najua huwezi kuelewa upesi kwa nini basi nahitaji kukupa zawadi ya mtoto.....” akasita na kuelezea mlolongo wote wa maisha yake kama anielezavyo mara kwa mara.
kisha akanieleza jambo ambalo lilinifanya niupate ukurasa wa mwisho kabisa wa ripoti hii kamili.
Tina akanieleza kuwa hajawahi kuathirika na virusi vya Ukimwi bali alihitaji niwe mbali na maisha yake tu kwqa sababu alikuwa amejikatia tamaa, lakini kwa namna nilivyomjali na kumjali mtoto wake mwingine ambaye hata baba yake sikuwa namjua kwa sura, Tina alijikuta akinipenda upya na kujionayu mwanamke kati ya wanawake.
Hii ilikuwa taarifa ambayo niliiona kama ndoto ya mchana kweupe.
“Mjuni... nahitaji kukuzalia tu si mengineyo.....” alinisihi Tina.
Naam! Ili kuhakikisha tulienda kupima afya zetu upya, Tina alikuwa safi na mimi vilevile.
Kugundua kuwa Tuina yupo safi nikajikuta si tu kuhitaji mtoto na Tina bali kuyaendeleza mahusiano yale na kurejea kule tulipokuwa zamani.
Na hii ilikuwa rahisi kumshawishi Tina hasa baada ya kubeba mimba kweli......
Ule ukaribu ukazifanya zile pete zirejee katika matumizi yake, pete ambazo hakuna hata mmojawetu aliwahi kuivua.
Yule mtoto aliyekuja kuzaliwa miezi kadhaa baadaye akatuunganisha upya na kutufanya wamoja.
Yaliyopita yalipita sikujali nani atasema nini kuhusu mimi.....
Mtoto aliyezaliwa alikuwa wa kike, sikuwa na haja ya kuzunguka huku na kule kutafuta jina litakaloyafurahisha masikio yangu na Tina...... sote kwa pamoja tukakiita kitoto kile SONIA!! Hiyo ni Kwa heshima ya yule mtoto asiyekuwa damu yangu niliyekuwa nampenda kupita maelezo. Mtoto aliyepoteza maisha katika harakati za Tina kuikimbia aibu yake.
Nilijua kuwa wa kusema watasema mengi na wa kusengenya watasengenya sana, hata wewe unayeisomaripoti hii waweza kuwa mmoja wapo lakini amini kitu kimoja nilisema mwanzoni kabisa mwa ripoti hii kuwa.
Nimejifunza mengi katika maisha yangu, nimejifunza kuliweka wazi sikio langu kumsikiliza kila mtu iwe anazungumza upuuzi ama anajenga hoja chanya na madhubuti!!
Lakini yote juu ya yote, nafanya hivi lakini naweka maanani kitu kimoja tu. Ninakuruhusuni kunieleza lolote mnaloweza, ninakuruhusuni kunishauri lolote mnaloona linafaa kunishauri lakini aidha kuchukua ushauri wenu na kuufanyia kazi hii inabaki juu yangu mimi na akili zangu!!!
Sio kila mtakalosema nitalifanyia kazi...CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakuna gharama yoyote katika kusikiliza ila kuna gharama katika kufanyia kazi hayo uliyoyasikiliza.
Naam!! niliufungua ukurasa wa ripoti hii nikiwa na Tina kama mke wangu ninayempenda sana na ninaufunga tena nikiwa na Tina lakini sasa akiwa mama Sonia na ndiye mwanamke ninayempenda zaidi...... sijui kuhusu hatma ya Anita yule mke wa marehemu Freddy na nijue ili iweje tena, nadhani wakati mwingine tunatakiwa kupuuzia yale yasiyotuhusu kiukaribu.
**Asanteni kwa kuufuatilia mkasa huu mwanzo hadi mwisho wake ikiwa kwa namna yoyote ile mkasa huu umeleta taswira hasi kwako natumia fursa hii kukutaka radhi......
MWISHO!!!
0 comments:
Post a Comment