Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

RIPOTI KAMILI - 3

 





    Simulizi : Ripoti Kamili : Mkasa Wa Mapenzi

    Sehemu Ya Tatu (3)



    MUNGU na akutie nguvu ewe uliyempoteza mama yako, ama wewe usiyemjua mama yako kabisa.

    Mungu ni kimbilio la yote lakini mama ni kimbilio la mengi sana..... ukipatwa na jambo ambalo unahisi kwa kiasi fulani linaizidi akili yako tafadhali mkimbilie mama mueleze pasi na kumficha chochote!!

    Niamini mimi, hautaondoka kama ulivyoenda..... hautakosa chembe za matumaini. Kama ulikuwa umeanguka utasimama tena........

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    NA HII NI SEHEMU YA KUMI NA MOJA.



    BAADA ya kutafakari kwa kina ni ni kitu gani ambacho naweza kufanya kwa wakati ule nikiwa katika nyumba ile nikaona hapo la kufanya ni kuondoka bila kuamua chochote. Nikamuaga yule mama nikamueleza kuwa nitarejea tena, akaniuliza mimi ni naniili mumewe akirejea amueleze nikamueleza kuwa naitwa Steven lakini mumewe hanifahamu kabisa mpaka nijieleze zaidi.

    Akaniaga nikaondoka!!!

    Nilipofika nje ya uzio ule nikaichukua simu yangu nikatafuta sehemu imetulia nikaingiza namba za mama yangu na kumueleza kuwa iwapo anayo nafasi ninahitaji sana kuzungumza naye. Akaniambia nimpigie bada ya nusu saa, tukaagana hivyo. Nikaondoka hadi nyumbani nikajirusha kiotandani, ile nusu saa ilikuwa imemalizika tayari na sasa ulikuwa wakati wa kumueleza mama kile ambacho kilikuwa kinanisibu kwa wakati hu.

    Nilimueleza mama hatua kwa hatua niliyopitia hadi hapo nilipokuwa, nilimwambia kuwa nilitamani sana nizungumze naye ana kwa ana maneno haya lakini wakati unanitupa mkono nahitaji ushauri wake ni kitu gani nifanye ambacho ni sahihi kwa wakati huo. Mama alishusha pumzi zake kwa nguvu sana, kisha akaniita jina langu la utotoni jina la Nshomile.

    Nikaitika kwa utulivu akanieleza kuwa na yeye ana mengi ya kuzungumza lakini akasema tumweke kando Tina na sasa tuzungumze kuhusu mtoto.

    Akaongezea kuwa yupo tayari kuniunga mkono kwa lolote jema ambalo litanifanya mimi nifurahi, na kwa hili pia akanieleza kuwa ni jema kwa sababu mtoto nimemlea na ninampenda basi huyo ndiyo furaha yangu, isitoshe hata kliniki jina aliloandikwa ni jina langu.... hivyo cheti chake cha kuzaliwa kinamtambulisha kama mtoto wangu.

    Mama akanieleza kuwa. Yeyote aingiaye katika vita kwa pupa huishia kuangukia pua lakini yule aingiaye kwa tahadhari kubwa anazo asilimia nyingi sana za ushindi. Akaendelea kunieleza kuwa hii ni vita na sehemu kubwa tayari nilikuwa nimeipigana tena kwa ushindi mnono sana, hivyo kuimaliza si kazi ngumu, mama akanishauri niende kuonana na mgoni wangu, huyo aliyekuwa akimfanya Tina vile alivyokuwa anapenda kumfanya. Akanieleza kuwa nikishakutana naye nisiwe na papara bali mpole na niliyekubali kujishusha kabisa.



    Dah! Ushauri wa mama niliuona mzito lakini akanieleza kuwa kama nilijishusha mbele ya Tina huku najua kila alichofanya, nashindwa vipi kumalizia kwa huyo mwanaume ili nijue kipi kinaendelea. Nikamuelewa mama na nikajipanga jioni ya siku hiyo kwenda kuonana na huyo bwana wa kuitwa Eric. Maneno ya mama yalikuwa yamenitia nguvu sana....

    Na sikutaka siku hiyo ipite kabla ya kuonana naye, nikahairisha mpango wangu wa kulala na badala yake nikaamua nifunge safari kwenda nyumbani kwake tena lakini safari hii sifiki ndani ila nitajiweka nje na kutazama kila anayeingia na kutoka, akiingia tu na mimi naingia ama akitoka tu na mimi namfuata......

    Wazo hili nikaliona ni wazo stahiki, nikavaa viatu vyangu kisha nikaufikia mlango wangu nikaufungua.

    Moyo wangu ulipiga kwa nguvu sana yaani ilikuwa kama filamu fulani hivi isiyokuwa na ukweli ndani yake.

    Filamu ambayo mwandishi wake ameunda tukio la mimi kufungua mlango na wakati huohuo mtu ambaye naondoka kwa ajili yake akiwa amesimama mlangoni kwangu akijiandaa kubisha hodi.

    Alikuwa ni Eric akiwa amesimama huku mikono yake ikiwa inatetemeka, sijui kama na yeye aliuona mshtuko wangu lakini mimi niliuona mshtuko wake vyema kabisa.

    “Karibu bwana!” nikamkaribisha.....

    “Tafadhali bwana Mjuni nakuomba sana unipe nafasi ya kunisikiliza nakuomba Mjuni!!” alinisihi nikabaki kushangaa... lakini hapohapo hofu ikaanza kuniingia kutokana na wasiwasi wake yule bwana.

    Na wasiwasi wa kwanza kabisa ulikuwa ule wa kupokea taarifa za msiba wa Tina na mtoto wake, nilikuwa tayari kupokea taarifa yoyote ile lakini sio taarifa hii. Niliamini kuwa nitakatishwa tamaa mno klulisikia jambo kama hili kwa masikio yangu.

    “Karibu ndani bwana Eric... karibu tafadhali...” nilimsihi akaingia ndani nikafunga mlango.

    Akaketi katika kochi mojawapo sebuleni na mimi nikaketi mkabala naye, nikawa namtazama kwa nukta jinsia livyokuwa akijiumauma kuzungumza... alikuwa anarudia rudia maneno sabna na hadi dakika tano zinapita nilikuwa sijaelewa lolote alilokuwa akisema zaidi ya kusisitiza kuwa anahitaji sana msamaha wangu.

    “Tina yupo wapi?” hatimaye nilimuuliza, na kabla hajanijibu nikaliboresha swali, “Tina na mtoto wapo wapi kwanza kabla ya yote?” nikasita na kumpa nafasi azungumze.

    “Kaka, ni mimi niliyetaka kukuuliza hilo swali.... nipo tayari umuite Tina na mtoto niwaombe radhi wote kwa pamoja....”

    “Hah! ina maana hujaonana na Tina ama?” nilimuhoji.

    “Nina zaidi ya wiki moja sijawahi kuwaona....” alinijibu, sasa alikuwa anatulia kiasi fulani....

    “Na ni kipi hasa chanzo cha wewe kuja hapa?” nilimuuliza. Akanieleza kuwa nilipoenda nyumbani kwake alikuwa ndani na aliweza kufuatilia baadhi ya maongezi kati yangu na mkewe na kwa sababu alikuwa ananitambua alijua pia nini dhumuni langu la kwenda kwake.

    Akaendelea kunisihi kuwa mkewe ana matatizo ya moyo na laiti kama akigundua jambo hili la mimi kwenda kushtaki kuwa yeye ana mahusiano na mke wangu basi anaweza kufa palepale.

    Nilimsikiliza na kuuona udhaifu wa hoja yake ya kujitetea, alinikasirisha sana, yaani alikuwa anamuonea huruma mkewe lakini katu hakuwahi kufikiria ni uchungu kiasi gani ninapitia mimi kwa kutambua kuwa anahusiana na mke wangu tena mara kwa mara wanakutana na kisha kunisema watakavyo. Niliidhibiti hasira yangu lakini ikashindikana.

    “Eric unasema kwamba..... yaani unamuonea mkeo huruma lakini mimi haujali uchungu wangu si ndo hivyo....” nikaenda mlangoni na kuufunga mlango vyema na kutoa funguo.

    “Sasa Eric nahitaji tufahamiane vizuri kuwa nani ni mwanaume... umenitesa sana mwanaharamu mkubwa wewe....”

    Sasa ni hasira ilikuwa inaniongoza, nilimvamia Eric na kumkaba shingo yake, kilichosababisha hasira ipungue makali kidogo nmi kile kitendo chake cha kutopambana na mimi bali kuniacha nifanye nifanyavyo.......

    Mwishowe nilimuachia na kuruhusu machozi yanitoke..... na hapo nikaendelea kuzungumza.

    “Eric, nimeumia sana... umeniumiza sana... na bado unataka kuendelea kuniumiza. Yuko wapi Tina na mtoto....” nilikuwa nasita kila mara kumalizia mtoto wangu kwa sababu nilitambua kuwa aliyekuwa mbele yangu alikuwa baba halali.

    “Mjuni.. nielewe tafadhali... sijui na sina taarifa yoyote juu ya hili....” alizungumza huku akisihi haswa na nikaamini kabisa kuwa alikuwa haongopi.....

    “Sasa atakuwa wapi labda, ok! Tuachane na haya ya kale kwanza tuyaweke kiporo... tafadhali sana Eric nadhani waweza kuwa na mawazo walau mawili matatu ni wapi Tina anaweza kuwa.” Nikamueleza Eric huku nikimueleza pia kwa ufupi juu ya kilichotokea kabla Tina hajaondoka.

    Akafikiria kwa muda na kisha akanieleza kuwa huenda ameenda kwa shoga yake fulani hivi, akanielekeza mahali anapoishi, tukakubaliana kwenda wote. Tukafanya hivyo.....



    MAAMUZI ni jambo ambalo huamua kesho yetu wanadamu.

    Kuna maamuzi ambayo huwa tunafanya huku tukiamini fika kuwa ni sahihi lakini kesho yake tunajikuta katika wakati mgumu wa kujutia maamuzi......CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    NA HII NI SEHEMU YA KUMI NA MBILI.



    Kweli tulienda hadi huko aliposema ni kwa rafiki yake mkubwa Tina lakini bado hatukufanikiwa kuambulia jambo lolote lile rafiki alikuwepo lakini hakuwa na taarifa zozote juu ya Tina.

    Kufikia hapo nikaamini kuwa Eric hakuwa akifahamu lolote juu ya wapi Tina yupo....

    Sikuwa na haja ya kuyaendeleza mambo haya, niliachana nayo baada ya kuzungumza na mama yake Tina juu ya kilichotokea niliwaeleza mangapi niliyovumilia, walinishangaa sana nilivyowasimulia mkasa huu wa aina yake lakini hakika nilikuwa sijaongeza hata chembe ya uongo. Ulikuwa ni ukweli mtupu......

    Baba yake Tina alinikumbatia kwa nguvu sana na kunieleza kuwa mimi ni mwanaume wa aina yake, laiti kama angekuwa ni yeye huenda angekuwa jela zamani na angekuwa amezoea hukumu ya kifungo cha maisha ambayo angekuwa amepewa.

    Niliwaeleza wakwe zangu wale kuwa nilimpenda sana mtoto wao na hata siku wakipata kuwasiliana naye wamueleze kuwa sina kinyongo naye na ninamkaribisha ikiwa yu tayari kuuvunja moyo wake na kuujenga upya!!

    Niliondoka nikaenda kwa wazazi wangu na wenyewe nikawaeleza yote yaliyonisibu.... na baada ya hapo nikaanza maisha mapya pasipo uwepo wa Tina wala mtoto. Na ili nisiwakumbuke wawili hawa nikaamua kuhamia jijini Mwanza......

    Vitu vyote vilivyokuwa katika kile chumba cha awali niliviuza sikutaka kubaki na kumbukumbu yoyote ile zaidi ya picha ambazo nilizihifadhi mbali kabisa na nilikuwa nazitazama mara chache sana.







    Jijini Mwanza niliendelea na shughuli zangu, moyo wangu ukiwa umepoa kabisa. Nikisema umepoa namaanisha kuwa wanawake niliitambua tofauti yao kwa sababu ya sauti zao na mavazi lakini vinginevyo hakuna hisia yoyote iliyoamka katika mwili wangu nilipokutana na viumbe hawa.....

    Nikiwa Mwanza nilijitahidi kadri nilivyoweza kuhakikisha kuwa nawasahau kabisa Tina na mtoto wake.... nililazimisha hili kwa sababu kuna aina fulani ya chuki iliyoanza kujijenga katika nafsi yangu dhidi ya wanawake, nikisikia kuna mwanamke analalamika kuwa ananyanyaswa kimapenzi nilihisi kuwa hana haki na anastahili kunyanyaswa tu.. hii ni kwa sababu ya Tina!! Aliyonifanyia yalikuwa yameacha doa kubwa sana......

    Naam! Naukumbuka usiku ambao kwa mara ya kwanza niliingiwa na huruma juu ya wanawake....

    Haikuwa mara yangu ya kwanza kumsikia jirani yangu mmoja mwanaume akimwadhibu mwanamke ambaye nilikuja kufahamu baadaye kuwa hakuwa mkewe wa ndoa bali walikuwa tu wanaishi kimazoea.

    Kama kumwadhibu yule bwana alikuwa amezidi, lakini kamwe sikuwahi kujishughulisha na ugomvi wao, nilikuwa nawasikia majirani wengine wakimsihi aache kumwadhibu mkewe kiasi hicho cha kumvimbisha kila siku.

    Jambo moja ambalo nilijifunza katika maisha yangu ya kupanga pale Mwanza ni kwamba yule mwanamke alikuwa jasiri haswa, hakuwa na mvuto wa kufaa kuitwa mrembo wa dunia lakini alikuwa ana hadhi ya kuvuta macho ya wanaume wawili kati ya watatu watakaopishana naye......

    Mvuto wake huu angeweza kujinmilikisha kwa mwanaume mwingine lakini ajabu ni kwamba alikuwa mvumilivu... na mara kadhaa nilizowahi kushiriki maongezi ya hapa na pale na majirani nilikuwa namsikia akimtetea sana mwanaume wake... licha ya majirani kumkosoa sana mwanaume yule yeye alimtetea.

    Nilishangaa sana lakini sikuwahi kutia neno.....



    Siku moja usiku wa saa sita na madakika kadhaa nikiwa natoka katika mihangaiko yangu ya siku zote nilipita kona za hapa na pale, huku nikiwa nimetawaliwa na uoga kutokana na vitendo vya kihuni vilivyokuwa vikitendeka usiku hasahasa wizi, nilisikia sauti ya kike ikijikaza kulia. Nilishtuka lakini nikajikaza na kuendelea mbele.... uelekeo niliokuwa naenda uliifanya sauti ile ianze kufifia na kupotelea mbali.... nikajisemea kuwa huenda nimejishtukia tu hamna kitu kama hicho.

    Nikiwa bado natafakari hiyo sauti mara nikasikia nikiitwa jina langu. Hapo hofu ikazidi lakini sikuwa mwepesi wa kukimbia, na hapo nikaona mfano wa kivuli kikinyooka kutoka katika mkunjo na kuwa katika umbo la mwanamke. Alikuwa ni Anita.

    Yule mwanamke anayenyanyaswa na mwanaume wake.....

    Nilisogea huku nikitetemeka lakini sio sana kama nisingekuwa nafahamu anavyofanywa na bwana wake yule.

    Nilimfikia na kumuona akiwa antetemeka, akiwa na upande mmoja tu wa kanga.

    “Kaka Mjuni nakuomba kama unayo shilingi elfu tano nisaidie nitumie kama nauli niende kwa dadsa yangu huko Nyamanoro...” alizungumza kwa shida akiidhibiti midomo yake iliyopasuka huku ikivuja damu isipasuke zaidi.

    Nilishusha macho yangu hadi chini na kushuhudia miguuni akiwa peku huku akiwqa anavuja damu gotini.

    “Kwanini usilale nyumbani kwako?” nilimuuliza huku nikitambua kuwa si rahisi jibu kuwa eti ameamua tu.

    “Kaka Mjuni, sio nyumbani kwangu tena leo amekuja na mwanamke mwingine amesema niwapishe!!!” alizungumza kwa shida meno yake yakigongana kinywani mwake.

    Jibu lake na hali aliyokuwanayo nilinifanya kwa mara ya kwanza kabisa nipatwe na chembe ya huruma kwa wanawake.

    Nilijiona nina mengi ya kusema lakini nikajikuta linatoka moja tu.

    “Pole sana Anita... pole sana!!” nilimwambia huku nikijaribu kumgusa walau bega lake. Nilijipekua na kutoka na shilingi elfu kumi na tano nikampatia, na kisha nikamuuliza usiku huo itakuwaje.

    “Siwezi kurudi ataniua yule!! Acha tu niende hukohuko mbele....” alinijibu kisha akanishukuru huku akiondoka mguu wake ukiwa unachechemea.

    Nilisikitika sana lakini sikutaka kujihusisha zaidi na maisha ya wawili hawa!!!

    Lakini huu haukuwa mwisho bali mwanzo kabisa, tena mwanzo wenye mengi|!!!!



    KUNA mambo yanakera sana duniani, kila mmoja anayo kero ambayo kwake anaiona kubwa kupita zote.

    Fikiria kuhusu kusingiziwa, tena bora usingiziwe katika jambo ambalo halina madhara. Tatizo linakuja pale unaposingiziwa jambo ambalo linaharibu kabisa munekano wako katika jamii...

    Unaweza kujikuta unatenda dhambi kwa sababu ya kusingiziwa!!

    NA HII NI SEHEMU YA KUMI NA TATU.....



    Niliingia ndani nikaoga uzuri ni kwamba kila chumba kilikuwa kinajitegemea upande wa choo na bafu. Baada ya hapo nikajilaza kitandani na kuikumbuka sauti ya kusikitisha ya Anita na ule mwendo wake wa kuchechemea.

    Usiku ule mnene msichana kama yule anatembea peke yake gizani!!!

    Niliyasikia maumivu waziwazi moyoni mwangu yakifukuta, napenda kukukumbusha mpenzi msikilizaji kuwa baada ya siku nyingi sana kupita hatimaye nilikuwa nimeumia moyo wangu kwa sababu ya mwanamke.

    Lakini niliapa kuwa pakipambazuka siwezi kujihusisha zaidi na jambo lile ili nisije kujizulia maumivu yanayoepukika.

    Kweli palivyokucha sikutaka kujihangaisha na jambo lile niliendelea na shughuli zangu, hadi zilipopita siku takribani nane ndipo nikakutana na kizaazaa kingine.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Usiku huu nilikuwa nimewahi sana kurejea nyumbani, kichwa changu kilikuwa kinauma kiasi fulani hivyo nikaona si vibaya nikimeza dawa na kisha kutulia nyumbani.

    Hivyo majira ya saa mbili usiku nilikuwa tayari nimelala!!

    Ilikuwa saa tano na nusu usiku kwa mujibu wa saa yangu ya mkononi niliposikia mlango wangu ukigongwa.

    “Aaargh! Rose huyu naye...” nilijisemea nikiamini kuwa ni jirani mmoja aliyeitwa Rose. Dada mmoja ambaye tangu alipogundua kuwa ninaishi mwenyewe alikuwa analazimisha maozea, kila akirejea usiku lazima aniite kwa sauti na kisha kunisalimia. Sikuwa napendezwa na hali hii lakini ningefanyaje sasa??

    Lakini hii ya siku hii ilikuwa tofauti hii ilikuwa hodi ya kimyakimya. Nilisikilizia kabla ya kujipachika taulo yangukiunoni na kwenda mlangoni nikauliza anayegonga ni nani.... sauti ya kike ikajitambulisha. Alikuwa ni Anita.

    Mapigo yangu ya moyo yalipiga kwa kasi sana, mke wa mtu mlangoni kwangu usiku ule kufanya nini. Niliachana na saa yangu ya mkononi kwa kuamini kuwa huenda inaniongopea nikaitazama saa katika simu yangu, mambo yalikuwa yaleyale.....

    Ilikuwa usiku sana, huku nikiwa natetemeka kiasi fulani mikono yangu niliufungua mlango.... nikatangulia kutoa kichwa ni hapo nilipozidiwa na hofu zaidi alikuwa amesimama pamoja na mwanaume wake akiwa amevalia pensi akiwa kifua wazi, Anita alikuwa analia na kama kawaida alikuwa amejeruhiwa.

    “Haya sasa si huyu hapa aliyekurudisha kwa wazazi wako, naomba uingie ndani kwake mjadiliane ili kesho akakutambulishe kwa wazazi wake na akuoe kabisa, si mnajifanya wajanja.” Alizungumza yule mwanaume kwa sauti isiyokuwa na masihara ndani yake.

    “Lakini Fred huyu kaka alinipa nauli tu! Hakunielekeza wapi pa kwenda!!” Anita mnyonge kabisa alimweleza yule mwanaume, hapohapo nikashuhudia anavyonaswa kibao kikali sana usoni. Damu ilinisisimka sana, nikatamani kusema neno lakini nikajizuia.

    “Anita nitakucharanga viwembe huo uso wako we mwanamke..... naomba tusijibishane ingia humu na nguo zako zitafuata!!” alimwambia kana kwamba pale mlangoni hapakuwa na mtu amesimama.

    Na mara akamshika ili amsukume aingie chumbani kwangu...... hapo nikauweka ukimya wangu kando.

    “Bro vipi mbona sielewi ni kipi unataka kufanya hapa!” nilimuuliza kwa sauti ya kushangaa kiasifulani..

    Badala ya kunijibu swali nililouliza eti akanitukana tena tusi zito tu!! Nilishtuka mno.. huyu bwana tangu nianze kuishi pale sijawahi hata kutukanana naye zaidi ya kusalimiana mara moja moja leo hii badala anieleze kinachojiri ananitusi tena tusi zito kabisa.

    “Anita... sielewi kinachoendelea....” nilimgeukia Anita.

    “Waone Malaya wakubwa nyie, ujue mimi sio mjinga mnajifanya eti hamjuani si ndo hivyo, na siku ulipompa nauli anede kwao saa nane za usiku mlikuwa hamjuani si ndo hivyo!!” alihoji kisharishyari.. ile sauti yake ya juu ikasababisha majirani waamke mmoja baada ya mwingine. Sikuamini kitu kile kilikuwa kinatokea lakini haikuwa ndoto bali uhalisia.

    Mimi si muongeaji sana na sikutaka eti siku hiyo ndiyo nianze kuwa muongeaji, na wala si mpenzi wa kutukana hasahasa matusi mazito ya nguoni... na sikupenda kutukanwa vilevile.....

    Ili kuepusha lolote ambalo lingeweza kujiri nikaamua kuingia ndani, ile nataka kufunga mlango yule bwana akafika na kuuzuia. Nikatumia nguvu kidogo nikafanikiwa kuufunga......

    “Aaah umemkimbia mwenzako eeh sasa utaukuta mwili wake hapa ukitoka....” niliisikia sauti yake ikionya.

    Na kweli haikuwa utani kilio cha Anita kilianza kusikika na milio ya mikanda ikiambatana na kilio hicho.

    Niliwasikia majirani wakimsihi huyo bwana aache kumpiga mkewe lakini alichojibu ni hiki.

    “hadi huyo Malaya mwenzake amfungulie mlango ndo ntamuacha!”

    Majibu ya huyu bwana yalinikera sana, nini cha kufanya usiku ule??

    Nikaishughulisha akili yangu upesi na kumkumbuka rafiki yangu aitwaye Tito ambaye ni askari, nilichukua simu yangu na kumpigia nikamueleza kuwa aje nyumbanikwangu usiku ule kuna tatizo la kiusalama nikamuomba sana. Kwa sababu na yeye hakuwa ameoa kama mimi alilalamika lakini mwisho wa yote alikubali kuja, nikamsihi achukue pikipiki.

    Akakubali!!

    Ukimya wangu uliendelea, na bila shaka ukimya huu ulimkera yule bwana wa Anita, alinitukana sana na alipoona matusi yamemuisha na amechoka kumpiga Anitha alianza kugonga mlango wangu na kisha akasemamkuwa kama sitoki anauvunja mlango ule!!

    Kama masihara vile akaanza kugonga kwa nguvu, majirani wengi wakiwa kinamama walimsihi asifanye hivyo, lakini kiburi kikampanda na mara akageuza usiku ule kuwa usiku wa fumanizi akasema mimi natembea na mkewe!!

    Ebwana eeh! Nilikuwa si mwepesi sana wa hasira nd’o maana niliweza kumuandalia Tina ripoti lakini kitendo alichofanya huyo bwana kudai mi natoka na mkewe na amenifumania nilijikuta nachemka vibaya sana.....

    Nikaitoa taulo ile na kisha nikavaa suruali ambayo nilitokanayo katika mihangaiko yangu ya siku hiyo......

    Baada ya hapo nikiwa kifua wazi niliufungua mlango!

    Wacaha wee! Majirani walikuwa wengi na kila mmoja akingoja kuona nini kitatokea.

    “Nakuomba sana bwana kaka, kuwa mbali na chumba changu. Simjui mkeo zaidi ya usiku ule aliomba nauli nikampatia na sijawahi hata kuzungumza naye nakuonba sana sitaki matatizo na mtu...” nilimweleza kiukarimu sana, majirani wengi sana walikuwa wananiheshimu hata Rose alikuwa ananiambia mara kwa mara kuwa majirani huwa wananizungumza kwa mema na wanapenda jinsi ninavyoishi!!

    Hata nilipoongea pale wengi walitikisa vichwa kuniunga mkono.

    Lakini yule bwana ambaye hakuwa amelewa alikuwa an akili timamu akajifanya hana cha kunielewa, hapo sasa aanitukania mama yangu tena mara mbili!!!

    Akili yangu ikatulia kwa muda, sekunde mbili nikamtazama Anita akiwa anavuja damu akiwa ameketi chini akiugulia, sekunde iliyofuata nikamkumbuka Anita usiku ule wa giza akiwa hana msaada wowote na sekunde iliyofuata nikamkumbuka Tina na maasi yote aliyowahi kunifanyia hadi alipokuja kupotea akiwa na mtoto ninayempenda sana!

    Yote yalinipandisha mori lakini hili la Tina lilinipandisha hasira kuu...

    Nilikwambieni awali kuwa mimi si muongeaji sana.. hivyo sikuweza kuzungumza neno la ziada. Badala yake nilimvamia kwa kasi kubwa sana nikiwa nimeikunja ngumi yangu lakini sikuitumia badala yake nilimtandika teke kali sana mbavuni, akaanguka chini na hakuweza kuamka upesi kabla sijafika na kumkalia tumboni, na hapo kilichofuata ilikuwa ni kama filamu, nilikuwa naulenga uso wake na kupiga ngumi kalikali.

    Ndugu zangu, sikuwahi kuwa mgomvi mimi.., sikuwahi kumchokoza mtu ili tupigane tangu udogo wangu sijui hata hizi ngumi nilizitolea wapi.

    Ninachokumbuka kuwa nilikuwa napiga ngumi huku nikitukana, kila ngumi ilivyokuwa inatua ilisindikizwa na tusi. Baadhi ya matusi ninayoyakumbuka ni, mbwa kasoro mkia, mjinga mkubwa, mpuuzi, mnyanyasaji mkubwa.... lakini katu sikumtuykania mama yake wala tusi lolote la nguoni.

    Hakika nilimnyoosha sio siri!

    Sauti za majirani wakinisihi nimuache nilizisikia lakini zilikuja kama kichina sikuelewa wanamaanisha nini.



    “Sasa leo nakuua mbwa koko wewe!!” hili lilikuwa neno la mwisho kabisa kumweleza yule bwana kisha nikamtandika kichwa kimoja hadi mimi mwenyewe nikakumbwa na kizunguzungu!!!



    Jifunze kuwa mwisho wa jambo moja ndio mwanzo wa jambo jingine.



    Na hii ni sehemu ya kumi na nne



    Ninachokumbuka kuwa nilikuwa napiga ngumi huku nikitukana, kila ngumi ilivyokuwa inatua ilisindikizwa na tusi. Baadhi ya matusi ninayoyakumbuka ni, mbwa kasoro mkia, mjinga mkubwa, mpuuzi, mnyanyasaji mkubwa.... lakini katu sikumtuykania mama yake wala tusi lolote la nguoni.

    Hakika nilimnyoosha sio siri!

    Sauti za majirani wakinisihi nimuache nilizisikia lakini zilikuja kama kichina sikuelewa wanamaanisha nini.



    “Sasa leo nakuua mbwa koko wewe!!” hili lilikuwa neno la mwisho kabisa kumweleza yule bwana kisha nikamtandika kichwa kimoja hadi mimi mwenyewe nikakumbwa na kizunguzungu!!!



    Nikiwa bado katika hali ile mara ghafla nilisikia nikivutwa kwa nguvu sana nikaondolewa juu ya tumbo la yule bwana mnyanyasaji, nilipofanikiwa kugeuka kutazama ni nani aliyenitoa pale nikakutana na yule rafiki yangu askari.

    “Mujuni, nini hiki rafiki yangu... we sio wa kufanya hivi kaka!!” alinisemesha huku akiniongoza kuelekea katika chumba changu.

    Nilitamani kuongea lakini sikuweza, kooni bado donge la hasira lilikuwa limenikaba...

    Wakati naingia ndani ndipo walau masikio yangu yaliwasikia majirani wakimzomea yule bwana kuwa kwa kipigo kile nilikuwa nimemuweza.

    Tulifika ndani na yule rafiki yangu askari nikamueleza kila kitu kama kilivyokuwa, alitoka nje akamkuta Anita akiwa pale chini akiwa bado yu katika hali mbaya na hapo hakupoteza muda sheria ilichukua mkondo wake, kwanza akamtia pingu yule mwanaume. Kisha akanieleza kuwa kuwa yule Anita lazima awahishwe hospitali usiku uleule....CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ikawa kama alivyoshauri, kwa sababu Anita hakuwa na ndugu pale yule askari akanisihi niongozane naye, tukafanya vile.

    Nilikumbuka kumuuliza kwanini alikuwa amewahi kumfunga pingu yule jamaa, akaniambia kuwa akibaki salama anaweza kuwahi kutoa taarifa kuwa nimempiga hivyo atanipotezea muda kuanza kuifuatilia kesi ile.

    Nilikubaliana na hatua ile na kuamini kuwa ni ya msingi sana.

    Tulichukua taksi hadi kituo cha polisi ambapo Anita alichukuliwa PF3 na kisha tukampeleka hospitali walipompokea.

    “Mujuni eeh! Ujue leo geto kwangu shemeji yako amenitembelea sasa we kama vipi baki na huyu dada asubuhi nitafika hapa!” alinieleza askari yule na sikuwa na la kumpinga zaidi ya kucheka tu.

    Nilibaki kumtazama Anita kwa ukaribu wakati akipata matibabu katika zahanati ile, uzuri ni kwamba hapakuwa na wagonjwa wengi hivyo japokuwa ilikuwa wodi ya akina mama bado niliruhusiwa kuendelea kuwemo lakini nikipewa tahadhari kuwa ikitokea akaingizwa mgonjwa mwingine nitatakiwa kutoka kwa sababu sio utaratibu.

    Kufikia asubuhi Anita alikuwa mwenye nafuu kubwa alinishukuru sana kwa moyo wangu, nikamwambia kuwa asijali!! Na sikutaka kuendelea kuzungumza naye juu ya jambo hili maana natambua wazi kuwa ukaribu ukizidi yataibuka mazoea ya juu zaidi ambayo kwa lugha moja yanaitwa mapenzi. Kitu ambacho sikuwa tayari kabisa kukipokea kwa wakati ule.





    *****







    Baada ya majuma mawili kupita nikiwa sijajua ni kitu gani kiliendelea katika kesi ya unyanyasaji iliyokuwa inamkabili yule bwana, niliamua kumpigia simu Tito yule afande ambaye ni rafiki yangu, baada ya salamu za hapa na pale nilimuulizia juu ya maendeleo ya ile kesi akanieleza kuwa yule bwana aliachiwa huru baada ya mkewe yaani Anita kugomea mambo yale kupelekwa mahakamani na badala yake akiomba waachiwe jambo lile wakalizungumze kifamilia.

    Tito alicheka sana kisha akaniambia ya wapenzi niwaachie wapenzi wenyewe.....

    Nilimaliza kuzungumza naye huku nikijisemea tena kwa kurudia.

    “Amakweli ya wapenzi ni kuwaachia wapenzi wenyewe”



    Nikiwa bado na mshangao, niliusikia mlango wangu ukigongwa!

    Nikatazama saa ilikuwa saa mbili usiku.....

    Nikakumbuka kuwa nilikuwa sijalipia pesa ya umeme na maji kwa mwezi huo. Nikapatwa na mfedheheko sana, hakuna kitu nilichokuwa nachukia kama kuja kugongewa mlango na mwenye nyumba kisa kuna kitu natakiwa kulipia na sijalipia ndo maana nilikuwa nalipa mapema kabisa kodi zangu!!

    Upesi nilijipekua na kutoka na shilingi elfu ishirini na tano nikaziweka mfukoni na kisha nikauendea mlango. Kweli alikuwa ni mama mwenye nyumba, nikamsalimia na kisha kumsikiliza ili akianza tu kudai chake nimpatie na kumuomba radhi kwa kuchelewesha pasipo kukusudia.

    “Haujambo mwanangu Mujuni....” alinisalimia.

    “Sijambo mama shkamoo..... karibu” nilimjibu....

    “Mwanangu Mujuni nilikuwa nimelala si unajua tena uzee huu nawahi kulala, lakini kuna mwenzako mmoja amekujakunigongea mlango na amenieleza jambo la msingi na nikaona nikiache kitanda nije hapa kwako...” al;isita na kunitazama vyema usoni kisha akaendelea.

    “Mwanangu Mjuni ukiona mtu mzima anaamua kumfata mzee kama mimi kwa ajili ya kuja kumuombea kwako ili mzungumze basi analo la msingi la kukueleza Mjuni nakuomba umsikilize mwenzako....” alimaliza kisha akageuka na kuita jina fulani ambalo sikulisikia vizuri. Na hapo nikakiona kivuli cha mwanaume kikitokea mbali kiasi. Akajongea hadi akafika tulipokuwa, na hapo nikatambua kuwa alikuwa ni Fred mume wa Anita. Alikuwa mtulivu haswa, mama mwenye nyumba akanisihi nimsikilize. Sikumpinga mama, na ningeanzaje kumpinga wakati bado nilikuwa katika mshangao.....

    Nikamkaribisha ndani, akaingia taratibu akataka kuvua viatu mlangoni nikamzuia.

    Akaingia na kuketi katika mojawapo ya kochi kati ya yale yaliyokuwa pale sebuleni. Alihangaika sana kuanza kuzungumza lakini alipoanza aliniomba msamaha kwa jinsia livyonivunjia heshima yangu usiku ule wa ugomvi. Nikamwambia kuwa yale yameisha....

    Akatulia kwa muda kisha akaniita jina langu.

    “Mujuni kaka yangu, mimi sio kijana mbaya kama ambavyo wewe na majirani wengine wanavyoweza kunifikiria Mjuni..... sipo hivyo kabisa. Hata mama yangu akifufuka leo na kuelezwa kuwa ninampiga mke wangu ama ninatukana matusi ya nguoni anaweza kufa tena tukamzika upya..... na kitakachomuua ni mshangao na mshtuko mkubwa..... hakuniacha nikiwa hivyo na aliwahi kusema wazi kuwa kati ya watu kumi wapole aliowahi kukutana nao basi na mimi ni mmouja wao. Mimi Fred ninywe pombe? Mimi niende disko? Ah wapi hicho kitu hakikuwahi kuwepo...... ila mapenzi kaka Mujuni... mapenzi kaka.” Alisita akaonekana kuzidiwa na hisia. Hakusema kitu akaufungua mlango na kutoka nje nikashindwa kumzuia, nikabaki kujiuliza tu ni kitu gani kinamkabili bwana huyu.

    Nikalala nikitaraji kuwa huenda siku inayofuata atazungumza na mimi. Lakini alfajiri vilio vilisikika, na vilipozidi nikalazimika kuamka.

    Fredy alikuwa amejinyonga!!!

    Alijinyongea chumbani kwake huku akiacha ujumbe mfupi sana ambao hakuna aliyeweza kuuelezea maana yake, ni kama mtu aliyekuwa akiandika kwa kujilazimisha tu.

    Nilichoka haswa!!!

    Fredy alikuwa amekufa bila hata kunieleza ni kitu gani kilikuwa kinamsibu, mama mwenye nyumba alinihoji sana kuwa ni kitu gani marehemu alikuwa anahitaji kunishirikisha, nilimueleza mama kile kilichotokea!

    Kila mmoja akabaki na jibu lake.

    Ajabu, Anita hakuonekana katika tukio lile!!

    Na hakuna aliyekuwa anajua nduguze Fred, hapa ndipo huwa pagumu linapokuja suala la msiba katika nyumba za kupanga.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Marafiki kadhaa wa Freddy waliokuwa wakifahamiana naye walijiunga na kukubaliana kumzika Freddy... msiba uliwekwa palepale nyumbani. Majirani tulishiriki kikamilifu katika michango ili kufanikisha kumpumzisha yule mwenzetu katika nyumba yake ya milele.

    Niliendelea kuwa katika upande wa kustaajabu.... Anita hakuja msibani kabisa hadi siku ya kuzika ilipofika hakuwa ameonekana. Nilitamani kuuliza lakini ningemuuliza nani.



    Wakati hili likisumbua kichwa changu, ile siku ya kuzika watu wote walioshiriki nasi waliandaliwa chakula.

    Hapa nikajikuta napatwa na jambo jingine zito zaidi ambalo lilinifanya nishindwe kwenda hata makaburini pamoja na wenzangu......



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog