Search This Blog

Sunday 19 June 2022

MUUAJI ALIYEBAKIA - 4

 





    Simulizi : Muuaji Aliyebakia

    Sehemu Ya Nne (4)



    Siku iliyofuata waliamka majira ya saa tatu asubuhi na walikuwa na hofu wakihisi muda wowote askari waliotumwa na rais wangerudi tena eneo hilo.

    Walianza kujiandaa kama walivyokuwa wamepanga kuondoka eneo hilo, kulikuwa na shati moja ambalo lilikuwa la mzee Rogart lililokuwa limechakaa sana ndilo alimpa alivae Geofrey. Shati hilo lilikuwa nje ya nyumba hiyo hivyo halikuungua katika janga la moto, alimpa kwa vile hakuwa na mazoea ya kuvaa shati akiwa porini hapo. Wote walikuwa katika mavazi duni kwani hata mzee Rogart alikuwa amevaa shati lililokuwa limechakaa sana na suruali iliyojaa viraka zaidi walikuwa hawavijui viatu. Mtu wa kawaida angewachukulia kama watu waliokuwa masikini wa kupindukia, walianza kutembea kwa tahadhari kubwa wakielekea eneo la kusini mwa eneo hilo walilokuwapo ambapo walipanga kuelekea jimbo la Linden.

    Mzee Rogart alikuwa amebeba bunduki tatu zilizokuwa na risasi, wakati Geofrey alikuwa amebeba upinde na mishale mingi iliyokuwa kwenye mfuko wake lakini pia hakuacha dawa aliyoitumia ambayo ilisababisha usingizi. Moyoni kwa kiasi alikuwa na furaha kwani alikuwa amelichoka eneo hilo alilokuwa ameishi kwa miaka kadhaa. Walikuwa wakiongea mambo tofauti ya hapa na pale wakati wakiendelea kutembea kwa kasi lengo likiwa ni kupunguza umbali wa msitu huo uliokuwa mkubwa. Majira ya saa kumi na mbili jioni walikuwa wametembea umbali wa kilometa nyingi wakiwa wamekutana na wawindaji wachache pasipo kuwaona askari. Bunduki moja kati ya tatu walizokuwa nazo walibadilisha na chakula kwa wawindaji waliokutana nao ambao walikuwa wakitokea makwao. Kubadilisha vitu wakiwa porini hapo lilikuwa jambo la kawaida kwani wawindaji wachache waliokuwa wakitokea vijiji vya karibu walikuwa na mazoea ya kuweka kambi porini kwa muda na baada ya kuwanasa wanyama walikuwa wakirudi katika vijiji vyao. Njiani walikuwa wanakutana na wanyama ambao wengine walikuwa wakali ili kutokana na uzoefu wao walikuwa wakiwafukuza wasiwadhuru.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hatimaye wakati wa nyakati za jioni walifika katika eneo waliloamua kulala lilikuwa pembezoni kidogo na mto mdogo wa maji, walikuwa wamechoka sana na malengo yao yalikuwa ni kuhakikisha siku iliyofuata wanatoka katika msitu huo. Waliamua kukata miti na kuikusanya sehemu moja lengo lao likiwa ni kuzuia upepo na baridi vilivyokuwapo eneo hilo. Mara baada ya zoezi hilo walianza kula chakula walichokuwa wamepata kwa wawindaji, walipokamilisha zoezi hilo walilala wakisubiri safari yao iendelee siku iliyofuata.

    Muda wote wakati mzee Rogart akiwa amelala Geofrey alikuwa hapati usingizi, mara kadhaa alisinzia lakini alirudi katika hali yake. Mkononi alikuwa na upinde na mshale alivyoviweka sawa kwa shari muda wowote, hakuwa na amani ya kulala na hakumshangaa mzee Rogart kwani aliamini mzee huyo alikuwa amezeeka baada ya harakati kama hizo wakati wa ujana wake. Majira ya saa sita usiku akiwa amesinzia kwa muda mfupi alishtushwa na miale ya tochi aliyoiona kwa mbali upande wa mbele walikoelekea baada ya kuvuka mto mdogo uliokuwapo. Jambo hilo lilimpa shauku ya kutaka kujua mwanga huo ulikuwa ukitolewa na nani. Wawindaji wachache aliwafahamu hawakuwa na mazoea ya kutumia tochi pasipo kumwamsha mzee Rogart alitoka mbio akiwa na upinde sambamba na mishale yake akielekea eneo alilouona mwanga huo.

    Hatimaye aliukaribia mwanga huo na taratibu alianza kusogea akijificha kwenye miti akiwa na lengo la kuwona wau ambao walikuwapo eneo hilo. Aliziona tochi kadhaa zikiwa zimeegeshwa maeneo tofauti ya eneo hilo lililokuwa na mahema lakini pia aliwaona askari wakizunguka zunguka eneo hilo wakiwa na bunduki zao. Hisia za msako uliokuwa ukiendelea zilimjia kichwani na aliamini askari hao walikuwa wengi. Akili yake iliona huo ulikuwa muda muafaka wa yeye na mzee Rogart kuondoka eneo hilo ili kuokoa uhai wao, taratibu alianza kuondoka eneo hilo na alipofiaka umbali mrefu alikimbia kwa kasi akirudi eneo walilokuwa wamelala.

    Alipofika eneo hilo alishtuka baada ya kuona sehemu aliyokuwa amelala mzee Rogart ikiwa wazi hata bunduki zake hazikuwapo, hofu ilimwingia akiamini tayari mzee huyo alikuwa amekamatwa. Alibaki ametulia akiwa hana jambo la kufanya, baada ya dakika kadhaa alishtushwa na sauti ya mzee Rogart akimwita ambaye naye alionekana alitokea sehemu ambayo ilikuwa na askari hai. Alifurahi kumwona mzee huyo na walikubaliana safari iendelee usiku huo kwani eneo hilo lilikuwa tayari na matatizo. Walibeba vitu vyao vichache na waliendelea na safari yao wakiwa wamechoka lakini waliamini kupona kwao kulikuwa bora zaidi kuliko kitu kingine.

    Siku iliyofuata majira ya saa sita mchana waliweza kutoka katika barabara kuu iliyoelekea jiji la New Amsterdam na mwishoe jimbo la Georgetown. Walificha silaha zao pembeni kidogo na barabara na walianza kusimamisha magari tofauti yaliyopita eneo hilo yaliyoelekea Linden walikopanga kuelekea. Magari mengi yalisimama ila baada ya kuwaona watu hao na hali zao kiujumla madereva walikuwa wakiingiwa hofu na kukataa kuwapa msaada. Hata magari ya abiria yaliposimama yalikataa kuwachukuwa wakiamini huenda walikuwa majambazi, watu wengi walimshangaa zaidi Geofrey kwa vile alikuwa mwafrika na zaidi katika mavazi machafu. Hofu yao pia ilikuwa kwa mzungu mwenzao mzee Rogart aliyekuwa na ndevu pamoja na nywele nyingi vyote vikiwa na mvi lakini pia sura yake ilikuwa haionekani vizuri kutokana na nywele hizo.

    Baada ya kukaa barabarani hapo pasipo kupata msaada kwa zaidi ya saa zima huku wakiwa na hofu ya kukamatwa wakiwa eneo hilo, mzee Rogart alitoa ushauri wa kufanya unyan`ganyi wa gari ili waweze kuondoka eneo hilo. Alielekea katika kichaka kilichokuwa pembeni kidogo ya barabara na kutulia na bunduki yake akiwa amemwacha Geofrey ajaribui kuendelea kusimamisha magari ambayo yangepita eneo hilo. Magari mengine yalikuwa hayasimami na baada ya muda mfupi gari moja lilisimama lilokuwa la kutembelea, teski aina ya Toyota. Alikuwamo kijana mmoja ambaye baada ya kuelezwa kuwa walihitaji msaada alipuuza akiimhofia kwani hata kioo alishusha kidogo alianza kulisogeza gari lake barabarani tayari kwa kuendelea na safari. Geofrey alibweka kama mbwa ishara iliyomtoa mzee Rogart kwa kasi kichakani na kuelekezea bunduki yake eneo la mbele la uskani ambapo dareva huyo alikuwapo.

    Alimuamru ashuke haraka jambo ambalo alitekeleza, wakati huo Geofrey alianza kupakia upinde na mishale yake na bunduki nyingine aliyokuwa nayo mzee Rogart kwenye gari hilo ambavyo walikuwa wamevificha pembezoni mwa barabara. Mara baada ya zoezi hilo mzee Rogart alimweleza kijana aliyekuwa na gari hilo aanze kukimbia bila kugeuka kurudi na barabara sehemu aliyokuwa ametoka. Alitekeleza jambo hilo akiwa na hofu huku akiamini watu hao aliowachukulia kama majambazi wangemuua, alitoka mbio akitekeleza masharti hayo.

    Mzee Rogart aliamini kazi ilikuwa imeisha aliingia kwenye gari na kulitoa kwa kasi eneo hilo akielekea upande wa jimbo la Linden, alikuwa na uzoefu mkubwa wa kuendesha magari hiyo ilitokana na enzi za ujana wake akiwa jambazi mkubwa. Geofrey alikuwa haamini kilichoendelea zaidi alifurahishwa na gari hilo, alikumbuka mara ya mwisho kupanda gari ilikuwa wakati ambao alisindikizwa na mwalimu wake wa American Academic School katika uwanja wa ndege wa Washington. Hakuwahi kupanda tena gari kwa zaidi ya miaka sita aliyokuwepo porini na mzee Rogart. Alikimbiza gari lao huku wakiwa na imani ya kufika jimbo la Linden baada ya masaa machache.

    Muda wote wakiwa kwenye gari walikuwa wakizungumza mambo tofauti zaidi walijisifia kwa kuukwepa mkono wa askari waliowafuata porini. Wakiwa wamebakiwa na kilomita kadhaa ili wafike katika jimbo hilo, walishtushwa na gari la askari lililokuwa likija nyuma yao kwa kasi na hisia zote za kukamatwa kwao zikawaingia. Furaha waliyokuwa nayo iliwaishia ghafla na mzee Rogart aliongeza kasi ya gari lao akiwa na hofu. Dalili zote za kukamatwa kwao zilianza kuonekana na tayari kulikuwa na vipaza sauti vilivyotumiwa na askari hao waliowataka wasimamishe gari lao.

    Baada ya muda mfupi huku wakiwa hawatii amri hiyo ya askari walifika aktika eneo la mpaka lililotenganisha jimbo la Linden na lile la New Amsterdam eneo ambalo lilikuwa na askari wengi na geti lake lilifungwa kutoruhusu gari lolote kupita kwa wakati huo.



    Baada ya muda mfupi huku wakiwa hawatii amri hiyo ya askari walifika aktika eneo la mpaka lililotenganisha jimbo la Linden na lile la New Amsterdam eneo ambalo lilikuwa na askari wengi na geti lake lilifungwa kutoruhusu gari lolote kupita kwa wakati huo.

    Mzee Rogart alisikika akiongea kwa machungu akimweleza Geofrey kuwa wakati wake wa kuishi ulikuwa umeisha. Jambo hilo lilimfanya Geofrey aanze kulia kwa uchungu akiwa hayuko tayari kutenganishwa na mzee huyo. Mwishoe aliamua kusimamisha gari hilo wakiwa umbali mfupi na geti hilo, alianza kwa kumshukuru Geofrey akiamini asingepewa adhabu kama ambayo angepewa yeye ambayo aliamini ilikuwa ni kifo.

    Baada ya muda mfupi mzee Rogart akiwa hajaongea mambo aliyotaka kumweleza Geofrey, tayari kundi la askari walikuwa wamelizunguka gari lao wakiwa wamewaelekezea bunduki zao wakiwaambia watoke. Mzee Rogart na Geofrey walitekeleza amri hiyo na wote kwa pamoja walitoka wakiwa wamenyoosha mikoni juu, askari waliwafunga pingu kila mmoja na walipakizwa katika gari tofauti kabla ya kuanza kuondoka gari hizo za polisi eneo hilo.

    Siku iliyofuata vyombo vya habari nchini Guyana vilitawaliwa na habari za kukamatwa kwa jambazi sugu aliyetafutwa kwa zaidi ya miaka kumi na tano pasipo kupatikana. Zaidi vilielezea kuwa mtu huyo ndiye aliyesababisha ajali iliyopelekea kifo cha mke wa rais bwana Zakheem Pirjah. Magazeti tofauti yalichapisha picha ya mzee Rogart akiwa na kijana aliyeishi naye porini aliyekuwa mwafrika. Mwonekano wa mavazi yao na jinsi walivyokuwa vilikuwa kivutio kwa raia wa nchi hiyo walionunua magazeti wakihitaji kujua habari zao zaidi. Tayari kesi dhidi yao ilifunguliwa wakati Geofrey akiwa na kosa la kufanya unyan`ganyi wa gari pamoja na kuishi na mtuhumiwa huyo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Geofrey hakuwa na shaka sana juu ya hukumu ambayo ingeenda kutolewa ila alimwonea huruma mzee Rogart akiamini kesi yake ilikuwa kubwa ambayo usalama wake ulikuwa mdogo. Kilichompa shaka zaidi ni vile muda akiwa anashikiliwa na askari katika kituo cha New Amsterdam hakuelewa kituo ambacho mzee Rogart alikuwapo. Siku yake ya kesi alipelekwa mahakamani na baada ya kukubali makosa yake alihukumiwa kwenda jela kwa miaka mitatu. Geofrey aliumia kufuatia adhabu hiyo na aliona mpango wa kurudi Tanzania kuiona familia yake ulikuwa unapotea kabisa. Kichwani aliingiwa na imani ya kuwapo nchini Guyana kwa miaka mingine zaidi ya mitano, kwani alielewa mara baada ya kutoka jela alipaswa atafute fedha kwa ajili ya nauli kurudi Tanzania.

    Askari walimchukuwa tayari kwa safari akiwa na wafungwa wenzie kuelekea katika gereza kubwa lililokuwapo kusini mwa nchi hiyo katika jimbo la Biloku. Safari ilianza wakiondoka mahakamani hapo akiwa pia haelewi mahali ambapo mzee Rogart alikuwapo zaidi alikuwa hajui kesi yake ilikuwa ikisomwa siku gani. Ndani ya gari hilo la magereza alikuwa mwafrika peke yake na alitulia pasipo kuongea na mtu ingawaje wenzie wachache walikuwa katika maongezi. Mawazo yake alikuwa ameyarudisha nchini Tanzania akiwa anaikumbuka familia yake. Siku zote alikuwa akiamini familia yake ilimtambua kuwa alikufa katika ajali ya ndege na hilo ndilo lililokuwa likimpa hamasa ya kutaka kurudi nchini Tanzania.

    Hatimaye walifika gerezani na aliweza kukutana na wafungwa weusi kama yeye kadhaa ambao walikuwa rafiki zake. Gereza hilo lililokuwa na taabu nyingi lakini kwake aliona kila kitu kilikuwa sawa kwa vile maisha aliyokuwa akiishi porini yalikuwa magumu zaidi. Baada ya wiki moja alipata taarifa kutoka kwa wafungwa kadhaa waliokuwa wakiingia gerezani hapo baada ya hukumu zao ambao walimweleza kuwa mzee Rogart alifariki kwa maradhi siku moja kabla ya hukumu yake. Geofrey alilia kwa uchungu juu ya taarifa hizo lakini pia hakuamini kama ni maradhi yalipelekea kifo chake, kichwani mwake aliaminii kifo hicho kilipangwa na rais wa nchi hiyo bwana Zakheem Pirjah. Wafungwa gereza hilo walikuwa wanamwogopa sana Geofrey, kwani kwa muda mfupi alifahamika kutokana na jitihada zake za kuwasaidia wafungwa waliokuwa wanaonewa. Alikuwa na mwili wa kawaida lakini alikuwa tayari kupigana na mfungwa yeyote aliyekuwa mkorofi na kumpiga.

    Baada ya miezi sita Geofey alizoea zaidi mazingira ya jela na hakuwa na imani kama angemaliza muda wake na kuondoka eneo hilo. Alijifunza kusahau kurudi Tanzania na zaidi juu ya kifo cha mzee Rogart, siku moja akiwa anaendelea na kazi za shambani gerezani hapo alishtushwa na kauli ya askari aliyemweleza kuwa alikuwa na mgeni.

    Geofrey alimkabidhi mfungwa mwenzie jembe alilokuwa akilitumia na aliongozana na askari magereza kuelekea chumba cha wageni. Hakupata picha juu ya mtu aliyefika gerezani hapo akiwa na nia ya kutaka kumwona, hiyo yote ilitokana na vile alivyokuwa akiamini jambo hilo lilikuwa gumu akiwa gerezani hapo.

    Mara baada ya kufika katika chumba hicho cha wageni alimwona msichana mmoja mrembo aliyeonekana alikuwa na mchanganyiko wa damu ya kiafrika na ya kizungu akiwa amekaa katika mojawapo ya kiti kilichokuwapo. Akili yake kwa haraka ilimtuma akiamini mtu huyo hakumfuata yeye, hata siku moja hakuwahi kuingiwa na fikra juu ya ujio wa mtu kama huyo aliyevutia kwa mwonekano. Alibaki kimya akimsikiliza askari amwekekeze kuhusu mgeni wake na wakati huo alihisi mgeni huyo alikuwa nje. Askari huyo alimweleza Geofrey akimwonyesha kwa kidole msichana aliyekuwa ameshangazwa naye kuwa ndiye mgeni wake, alimpa dakika kumi za maongezi.

    Alianza kutembea kuelekea katika meza ambayo msichana huyo alikuwa amekaa, hatimaye alifika na kuketi katika kiti cha upande wa pili akitazamana uso kwa uso na msichana huyo huku wakitenganishwa na meza ndogo.Kabla hajaongea kitu alishangazwa kuona msichana huyo akimsalimia kwa lugha ya kiswahili ambayo hata askari aliyekuwapo pembeni kidogo hakuielewa.

    “Geofrey mambo, mzima?” alisikika msichana huyo mara baada ya kuketi kwake “mimi mzima sijui wewe” alijibu Geofrey akiwa hajiamini na zaidi alikuwa hajaitumia lugha hiyo toka aingie nchini hapo Guyana.

    Msichana huyo alianza kwa kujitambulisha kuwa aliitwa Magreth na alikuwa raia wa nchini Tanzania, alimweleza kuwa alikuwapo nchini humo Guyana kwa vile baba yake alikuwa balozi wa Tanzania nchini humo. Aliendelea kumweleza jinsi alivyomfahamu Geofrey kupitia vyombo vya habari baada ya kukamatwa kwake jambo lililomfanya apange siku moja kumtembelea gerezani hapo. Alihitaji kufahamu juu ya mkasa uliomfika Geofrey mpaka alikuwa gerezani hapo akidai kuwa aliwajali waafrika wote waliokuwapo nchini humo. Muda wote wakati Magreth akisimulia hayo kuna jambo alilokuwa ameligundua ambalo tayari lilianza kuwa kikwazo moyoni mwake.

    Baada ya maelezo hayo mafupi ambayo Geofrey aliyaelewa alianza kumsimulia mkasa wa mambo yote aliyokutana nayo hadi wakati huo akiielezea pia familia yake. Muda wote akimsimulia, Magreth alipatwa na uchungu akionyesha dalili zote za kutokwa na machozi. Akiwa anaendelea kumwelezea, askari magereza aliyekuwa kando ambaye pia hakuelewa walichoongea alimweleza Geofrey kuwa muda uliisha, alisimama tayari kwa kurudi tena kwa wafungwa wenzie. “ahsante dada Magreth kwa kunijali..” alisikika Geofrey akiwa na anavutwa na askari huyo.

    “usijali kuna chakula nimekuletea watakupatia, lakini pia nitarudi siku nyingine uumalizie mkasa wako” alisikika Magreth akiwa na huzuni akimweleza Geofrey aliyeanza kuondoaka eneo hilo na hakujibiwa. Kichwani alipata hisia za ugumu wa maisha ya Geofrey ingawaje alimsimulia mpaka wakati anaokotwa kwenye ajali ya ndege na kwenda kuishi na mzee Rogart.

    Mbali na huzuni aliyokuwa nayo Magreth alishtushwa na hisia zake za ghafla juu ya Geofrey, alimhitaji awe mwanamme wake wa ndoto. Alikuwa ameishi kwa miaka mingi nchini humo Guyana lakini hakuwahi kuwapo katika mahusiano, jambo hilo lilimshangaza kuona alivutiwa na mtanzania mwenzake aliyekuwa gerezani. Geofrey alikuwa tofauti na yule aliyemwona kwenye vyombo vya habari siku anakamatwa, kwa vile alikuwa mwanamme aliyevutia. Baada ya kuelezwa kuwa chakula alicho mpelekea angekipata aliondoka gerezani hapo na kuelekea uwanja wa ndege kwa safari ya kurudi jimbo la Georgetown ambalo alikuwa akiishi na familia yake. Mara baada ya kufika nyumbani kwao hakumweleza mtu juu ya zoezi alilolifanya la kumtembelea mfungwa wa kitanzania. Jambo lililomkaa kichwani mwake na kutawala mawazo yake lilikuwa juu ya mfungwa huyo, hakuelewa sababu iliyopelekea jambo hilo. Siku tatu baadaye aliondoka nyumbani kwao na kusafiri tena kurudi jimbo la Biloku lengo kuu likiwa kwenda kukutana na Geofrey ili amumalizie mkasa wake lakini zaidi alikuwa amemkumbuka kupita kiasi.

    Kama ilivyokuwa awali alifanikiwa kupata nafasi ya kuongea naye ingawaje Geofrey alishtushwa na bahati aliyoipata ya kutembelewa tena zaidi alishukuru juu ya chakula alichokipata. Hatimaye alimumalizia mkasa wake na kumfanya Magreth akose raha akiwa hana njia ya kumsaidia lakini alimweleza kuwa angejaribu kwenda kufanya jitihada za kuwatafuta wazazi wake Geofrey. Alimweleza kuwa angempa mtu jukumu kutoka Tanzania ili awatafute jambo ambalo alifurahi kulisikia. Hatimaye Magreth aliondoka na kuanza kurudi nyumbani kwao, akiwa na furaha ya kumwona Geofrey wakati lengo lake likizidi kujengeka zaidi moyoni.

    Wakati huo alikuwa akisoma chuo kikuu cha Guyana akisomea udaktari na alikuwa katika likizo fupi. Tayari alikuwapo nchini humo na wazazi wake kwa zaidi ya miaka saba, mama yake alikuwa na asili ya Uingereza wakati baba yake alikuwa mtanzania akiwa balozi nchini humo kutoka Tanzania. Mara baada ya kufika nyumbani kwao alimpigia simu rafiki yake wa karibu aliyekuwapo nchini Tanzania na kumwomba aulizie mtu aliyeitwa James Kibudo kama Geofrey alivyolitaja jina la baba yake.Baada ya kumpa rafiki yake huyo kazi hiyo alianza kusubiri taarifa zozote kutoka kwa mtu huyo ambaye mwishoni alidai kulikuwa hakuna mtu aliyeitwa jina hilo. Bila kuchelewa alimpa taarifa hizo Geofrey ambaye alichukulia jambo hilo kama la kawaida na aliamini siku ambayo angerudi Tanzania mambo yote yangekuwa sawa.





    Bila kuchelewa alimpa taarifa hizo Geofrey ambaye alichukulia jambo hilo kama la kawaida na aliamini siku ambayo angerudi Tanzania mambo yote yangekuwa sawa.

    Magreth alikuwa amejiwekea utaratibu wa kumtembele gerezani kila mwisho wa wiki jambo lililompa sana faraja. Geofrey naye tayari alianza kuingiwa na mshtuko wa moyo juu ya Magreth kutokana na ishara za wazi alizozipata lakini aliona jambo hilo haliku wezekana kwa yeye kuwa na uhusiano na mrembo huyo. Siku zote alimchukulia kama msichana mwenye huruma na aliamini hakuna jambo ambalo lingeweza kutokea kuhusiana na hisia zake. Muda ulikwenda na hatimaye Geofrey alibakiwa na wiki mbili za kutumikia adhabu yake, hakuamini hata kidogo kuwa angeliacha gereza hilo na kuwa huru. Furaha yake iliongezeka zaidi kutokana na ahadi ambayo Magreth alishampa ya kufanikisha safari yake kurudi Tanzania.

    Zilibaki siku mbili, hatimaye moja na mwishoe siku ya Jumapili majira ya saa nane alipewa nguo za kuvaa alizoelezwa aliletewa na mtu aliyefika gerezani hapo kumchukua. Geofrey hakujiuliza maswali mengi akiamini nguo hizo zilitoka kwa Magreth aliingia katika chumba cha kubadilishia nguo na kuanza kuvaa nguo hizo. Lilikuwapo shati moja rangi nyekundu pia viatu na soksi vilikuwa vya rangi hiyo pamoja na jinzi moja iliyovutia kwa muonekano. Geofrey alivivaa na kuanza kutembea akitoka katika chumba hicho askari magereza walishtuka na kuanza kumshangilia kwa mwonekano mzuri aliokuwa nao. Mkuu wa gereza alimsifia kwa tabia yake nzuri aliyokuwa nayo kipindi akiwa gerezani hapo zaidi kitendo chake cha kuwatetea wanyonge. Alimaliza akimwambia aliamini toka wakati huo angekuwa raia mwema na mwishoe alimhurusu aondoke. Geofrey alianza kutembea kuelekea geti kuu la gereza hilo kwa haraka akiwa hajiamini kwani alihisi angeitwa tena kurudi kifungoni. Mara baada ya kutoka katika geti hilo kidogo moyo wake ulitulia lakini alihitaji kuondoka kabisa eneo hilo. Alikuwa akimwangalia Magreth kama alikuwapo eneo hilo kumchukua kama alivyoelezwa na askari magereza. Alizungusha kichwa kila upande eneo hilo pasipo kumuona zaidi ya gari lililokuwa na rangi nyekundu ambalo lilikuwa kando yake kidogo ambalo vioo vyake havikuhurusu mtu wa nje kuona ndani. Akiwa anatafakari juu ya jambo la kufanya alishtushwa mlango wa gari hilo uliokuwa ukifunguliwa, alielekeza macho yake ili aone mtu ambaye angeshuka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alishuhudia mguu wa mwanamke ukiwa na kiatu rangi nyekundu ukitoka kabla ya mtu huyo kutoka kabisa. Mshtuko wake uliongezeka zaidi baada ya kuona mtu huyo alikuwa Magreth, alikuwa amevaa vitu vyenye rangi nyekundu toka chini hadi juu. Alikuwa na gauni la kuvutia na zaidi mkononi pia alikuwa na maua ya rangi hiyo, alianza kutembea akielekea eneo ambalo Geofrey alikuwa amesimama. Mara baada ya kumfikia alimkubatia kabla ya kusikika “ pole sana Geoffur…..” “ahsante lakini zaidi nashukuru kwa kunijali muda wote nikiwa jela” Alijibu Geofrey ambaye mapigo yake ya moyo yalimwenda mbio hakuelewa jambo lililoendelea siku hiyo lakini rangi nyekundu ndiyo ilimpa shaka zaidi. Aliongozwa mpaka kwenye gari hilo lililokuwa Range Rover, kabla ya kuondoka kwao Geofrey aliamua kuuliza jambo lililomtatiza ingawaje lilimpa hisia za ushindi moyoni mwake.

    “kwa nini kila kitu kina rangi hii..” aliuliza Geofrey baada ya kushindwa kujizuia, Magreth alicheka kidogo kabla ya kumgeukia akimtizama usoni “Geoffur leo ni tarehe kumi na nne mwezi wa pili siku ya wapendanao duniani, naamini tunapendana” alimjibu jambo lililomfanya Geofrey acheke kwa furaha ingawaje hakujibu kitu ila aliona kama vile alikuwa amelala masikini na kuamka mfalme. Tayari alijipa aslimia mia za kuwa na Magreth mpaka mwisho wa maisha yake. Waliongoza mpaka hoteli ya kifahari iliyokuwapo katika jimbo hilo la Biloku na huko ndipo uhusiano wao ulianza rasmi baada ya ahadi nyingi walizowekeana. Siku iliyofuata Magreth alianza kumtafutia Geofrey hati ya kusafiria kurudi Tanzania.

    Mara baada ya taratibu zote kukamilika alimsindikiza Geofrey uwanja wa ndege tayari kwa safari kurudi Tanzania, alimweleza angerudi pia mara baada ya masomo yake ya mwaka mmoja uliobakia. Magreth alikuwa akilia kwani alihisi huo ndiyo ulikuwa kama mwisho wa yeye kuonana na Geofrey, mara baada ya kuagana alikuwa amempa namba ya simu na fedha za kutosha akiwa amemweleza mara baada ya kufika Tanzania amjulishe. Safari hiyo ilianza na mwishoe walifika Tanzania wakiwa wamepita Uingereza, Ethiopia na nchi nyingine. Geofrey bila kupoteza muda alikodi teski na alimweleza dereva ampeleke eneo lililokuwa na kampuni ya JAJHO, halikuwa jambo gumu kwa dereva huyo kwani alidai kampuni hiyo ilikuwa kubwa sana wakati huo. Alihitaji kufikia katika kampuni hiyo kwani bado Geofrey kumbukumbu alikuwa nazo juu ya kampuni hiyo aliyoiacha akiwa anaelekea Marekani na ilikuwa chini ya umiliki wa baba yake na wenzie wanne.

    Hatimaye walifika katika foleni ya magari iliyokuwapo maeneo ya posta akiwa ameelezwa walikaribia kufika katika eneo lililokuwa na ofisi hizo za kampuni ya JAJHO. Alikumbuka kumtaarifu Magreth kuwa tayari alikuwa amefika Tanzania, wakati huo alikuwa amekaa upande wa mbele wa teski hiyo akiwa na dereva na kioo cha gari kilikuwa wazi. Alichukua simu yake na kumpigia mara baada ya kuita mara moja ilipokelewa “nimeshafiaka Tanzania na niko nae…..” kabla hajamalizia sentesi hiyo mara baada ya kusalimiana kwao kibaka mmoja aliinyan`ganya simu hiyo kwa nguvu na kuondoka kwa kasi eneo hilo la foleni na tayari magari yalikuwa yamehurusiwa. Geofrey alichanganyikiwa ghafla juu ya tukio hilo zaidi hakuwa na namba ya mawasiliano ya Magreth ambayo ilihifadhiwa kwenye simu hiyo. Baada ya jitihada za haraka za kuipata simu hiyo kushindikana aliamua kukubaliana na tukio hilo na alimhurusu dereva waendelee na safari akiwa na imani kuwa angeitafuta namba hiyo. Mara baada ya kufika eneo hilo aliongozwa mpaka kwenye ofisi ya mmiliki mkuu wa kampuni hiyo aliyekuwa na hisa nyingi, aliamini alikuwa anaenda kuonana na baba yake.

    Mara baada ya kuingia katika ofisi hiyo alikutana na sura tofauti na baba yake ila kumbukumbu zake zilimjia kwa mbali juu ya mtu huyo.

    “ samahani namuulizia James Kibudo” Alisikika Geofrey mara baada ya kuketi, mtu huyo alishtuka kidogo kabla ya kumuuliza “unamuulizia kama nani katika kampuni hii” alijibu mtu huyo “kama mmoja wa wamiliki wa kampuni hii” alijibu “sikiliza kijana James Kibudo alifilisika miaka mingi iliyopita na hayupo kwenye orodha ya wamiliki wa wa kampuni hii, alituuzia hata jina lake ndiyo maana hatujabadili jina la kampuni hii ya JAJHO tukihofia soko letu mtaani, zaidi alikutwa ameuuawa nch…” kabla hajamalizia kuongea Geofrey alikurupuka na kumvamia akitaka kujua vizuri sentesi ya mwisho iliyohusu mauaji.

    Walinzi kadhaa waliitwa ofisini hapo na kumkamata zaidi mtu huyo aliyekuwa bosi aliyejitambulisha kama Jackson aliwaita wamiliki wenzie Amos, Hamis na Onesmo ili wamhoji mtu huyo. Geofrey baada ya kutulia kidogo alijieleza vizuri na mwishoe watu hao walimpa taarifa za kuuawa kwa baba na mama yake miaka kumi iliyopita na mdogo wake Robert walidai hawakujua eneo alilokuwapo na imani yao ilikuwa alikuwapo Marekani.

    Walimweleza juu ya taarifa walizokuwa nazo juu ya kifo chake baada ya ajali ya ndege iliyotokea nchini Guyana. Baada ya maelezo hayo Geofrey akiwa na majonzi aliaga na kuondoka eneo hilo la ofisi za JAJHO, mawazo yake yalikuwa ni kuhakikisha anaenda Kenya na kushuhudia kabuli la baba na mama yake.Jackson na wamiliki wenzie waliitana na kushangilia juu ya tukio hilo la maelezo ya kifo cha James na mkewe waliyoyatoa kwa mwanaye na waliamini siri yao isingevuja.

    Alielekea katika nyumba moja ya kulala wageni maeneo hayo ya Posta na muda wote alikuwa akilia juu ya tukio hilo alillolisikia, siku iliyofuata alianza safari akielekea Kenya kwa lengo la kwenda kuliona kabuli la baba na mama yake. Mara baada ya kufika jijini Nairobi aliongoza katika kituo kikuu cha polisi cha jiji hilo na kuomba kuonyeshwa makabuli hayo. Tayari alishaelezwa awali na mr. Jackson kuwa askari wa kituo hicho wangemsaidia kwani walihusika kwa kiasi kikubwa na mazishi ya wazazi wake.



    Tayari alishaelezwa awali na mr. Jackson kuwa askari wa kituo hicho wangemsaidia kwani walihusika kwa kiasi kikubwa na mazishi ya wazazi wake.

    Askari hao walimwelewa na mara baada ya kurejea kumbukumbu zao aliongozwa na askari mmoja hadi eneo la makabuli hayo. Geofrey alilia kwa uchungu mara baada ya kuona vibao ambavyo rangi yake ilikuwa ikikwajuka vikiwa na majina ya wazazi wake na aliamini aliloelezwa kuwa waliuawa. Siku iliyofuata aliwatafuta mafundi ujenzi kadhaa na kuwataka wamjengee makabuli hayo yaliyokuwa katika hali mbaya ya kuweza kupoteza kumbukumbu yake. Mara baada ya zoezi hilo aliweka mataji kama ishara ya kushiriki kwake katika msiba huo na kwa wakati huo aliamini hata mdogo wake Robert angeweza kwenda kuiona kumbukumbu hiyo ya kifo cha wazazi wao.

    Tayari alikuwa ameishiwa fedha zote alizopewa na Magreth kabla ya kuondoka kwake nchini Guyana na wakati huo aliona hana njia ya kuweza kumuokoa. Aliamua kumpigia simu mr. Jackson wa kampuni ya JAJHO akiomba uwezekano wa kupatiwa kazi lakini alijibiwa kwamba hawakuwa na nafasi hiyo. Aliumia juu ya jibu hilo lakini alijipa moyo ingawaje kuna wakati aliwahisi vibaya wamiliki wa kampuni hiyo. Jambo lililomkaa kichwani aliwaza kuwa ni lazima atafute fedha kwa ajili ya kufuatilia watu waliofanya mauaji dhidi ya familia yake. Akili yake ilimtuma kuua kama akiwagundua watu waliohusika na mauaji hayo kwani aliamini jeshi la polisi la nchi zote mbili za Tanzania na Kenya lilishindwa kazi yake.

    Baada ya kujibiwa vibaya na mr. Jackson alijichanganya katika mitaa ya jiji la Nairobi ili kutafuta maisha akianza kwa kuuza vitu tofauti barabarani. Wiki moja baadaye aligundua kuwa alijichelewesha kufanya malipo ya vifo kwa watu ambao walihusika na kifo cha wazazi wake. Kwani aliamini ilimbidi apate fedha ili afanye upelelezi na mwishoe apange malipizi hayo, aliamua kuanza kutafuta kundi la majambazi nchini humo akiamini aliweza kazi hiyo kwani alipata mafunzo mengi toka kwa mzee Rogart akiwa nchini Guyana. Baada ya wiki moja alikutana na mtu aliyejulikana kama mr. Tyoso ambaye alikuwa na kundi lake la majambazi, hivyo alianza kazi na watu hao.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndani ya mwezi mmoja kundi la mr. Tyoso lilipata mafanikio kupindukia kupitia uwezo mkubwa aliokuwa nao Geofrey. Kikubwa ni utumiaji wake wa bunduki na zaidi upinde na mishale walivyofanyia unyan`ganyi sehemu tofauti nchini Kenya. Alikuwa akiishi na mr. Tyoso mwenyewe kwa vile hakuwa na nyumba katika jiji hilo. Baada ya miezi mitano ya mafanikio tayari Geofrey pia alikuwa ni mtaalamu wa kuendesha magari hata pikipiki. Siku moja Geofrey alipatwa na homa ya malaria na hivyo alibakia nyumbani kwa mr. Tyoso wakati kundi hilo likiendelea na ujambazi. Muda wote akiwa nyumbani hapo alikuwa akisikiliza redio na mwishoe nyakati za jioni aliamua kuigeukia luninga ya mr. Tyoso. Alianza kuchagua filamu mbalimbali ambazo angeweza kuangalia lakini alivutiwa na moja iliyoonekana ilikuwa ya wanyama kwani iliianza kwa kuonyesha vyura. Ilimvutia zaidi kutokana na maisha ya porini aliyokuwa ameishi kwa muda mrefu nchini Guyana, ilionyesha ilikuwa imeandaliwa na George Johnson raia wa Kenya miaka kumi iliyokuwa imepita.

    Aliendelea kuangalia filamu hiyo huku akifurahia aina ya vyura walioonyeshwa, ghafla filamu hiyo ilikatishwa katikati na maneno yaliyoandikwa ‘MAUAJI YA KUTISHA’ yalitokea. Geofrey alikaa vizuri ili aone kilichokuwa kikifuata, alishtushwa na filamu hiyo iliyoendelea na baada ya sekunde chache aliwaona wazazi wake wakiwa porini kama wametekwa. Alikaa vizuri zaidi na kutoa macho, alimwona Jackson,Hamis,Amos na Onesmo wote wakiwa wamilikiwa kampuni ya JAJHO wakiwa katika eneo hilo la tukio na zaidi bosi wake mr. Tyoso alikuwapo. Jasho lilimtoka kama maji mara baada ya kuanza kushuhudia mauaji ya wazazi wake, aliwashuhudia jinsi wamiliki wa JAJHO walivyommiminia risasi baba yake wakati mama yake akiuawa na mr. Jackson. Zaidi aliona kila kitu katika tukio hilo kwani mpiga picha aliwachukua wazazi wake kwa karibu sana na kamera yake kabla ya wauaji hao kurudi na kuwatupa wazazi wake katika mto Tana.

    Geofrey hakuamini vizuri na wakati huo alichukua upinde na mishale yake tayari kwa shari aliwaza kuanza mauaji na mr. Tyoso aliyeonakana kuhusika. Tayari ilikuwa yapata saa moja jioni, alikuwa ameirudisha kwa mara ya pili filamu hiyo akiiangalia tena. Ghafla wakati akiendelea kuangalia filamu hiyo mr. Tyoso aliingia lakini Geofrey hakusikia chochote kutokana na hali ya kuchanganyikiwa aliyokuwa nayo juu ya filamu hiyo. Shati lake lilikuwa limelowa jasho kama vile alikuwa amenyeshewa na mvua, mr Tyoso alishtushwa na filamu hiyo iliyompa hisia za mauaji waliyoyafanya miaka mingi iliyokuwa imepita. Alikurupuka na kwenda kuitoa filamu hiyo kabla ya kuivunja akikanyaga na buti lake lililokuwa kama la jeshi, jambo hilo lilipelekea filamu hiyo kugawanyika katika vipande.

    Geofrey akili yake kidogo ilianza kumrudia sawasawa akiwa amegundua kuwa mtu aliyepaswa kuanza naye kumuua alikuwa amefika. Mr. Tyoso akilini hakuwahi kuhisi wala kuambiwa kuwa watu waliouawa katika filamu hiyo walikuwa ni wazazi wa Geofrey. Hata baada ya kuivunja filamu hiyo alielewa lilikuwa jambo la kawaida kwani walikuwa wamefanya mauaji kadhaa na Geofrey hivyo aliamini alikuwa mtu muuaji kama yeye. Wakati huo Geofrey mishipa ya hasira ilikuwa imemtoka shingoni na usoni na alikuwa kimya bila kusema kitu akiwa ameshika upinde na mshale alioupachika sawasawa lakini pembeni na eneo alilokaa akiweka mishale mingine mingi.

    “ebwana hili dili kuna mzushi alituona tulivyokuwa tunawasaidia watanzania fulani wa kampuni ya JAJHO kumuua mwenzao, kwa hiyo huwa siipendi hiyo filamu kwanza sikujua kama bado ipo” aliongea mr Tyoso baada ya ukimya kwa muda mrefu. Geofrey alisimama akiwa na mshale wake na upinde akiwa amemwelekezea mr. Tyoso usoni , “piga magoti haraka sana” aliongea kauli ambayo mr. Tyoso hakuitekeleza akijua ni utani. “vipi tena tunataniana toka…..”alisikika akijibu kauli ya Geofrey lakini kabla ya kumalizia sentensi yake alipigwa teke la uso lililompeleka mpaka chini. Hapo mr Tyoso aligundua kulikuwa na shari hivyo alitekeleza amri ya kupiga magoti, Geofrey aliivuta kamba ya upinde wake ambao alipachika mshale akiwa ameuelekeza kifuani kwa mr Tyoso. “jina langu ni Geofrey James Kibudo kwa hiyo wewe ulishiriki kuwaua wazazi wangu sina zawadi ya kukupa zaidi ya hii….” Aliongea Geofrey kauli iliyomshangaza mr Tyoso na mara baada ya kuimaliza kauli hiyo aliachia kamba ya upinde na mshale wake kwa kasi ya ajabu ulielekea kifuani mwa mr Tyoso na kupenya sawasawa ukiwa umeingia zaidi ya nusu.

    Mr. Tyoso alianza kupiga kelele za maumivu aliyoyapata wakati damu ilianza kumtoka, Geofrey aliingia kwenye chumba chake na kuchukua fedha zake zote. Mara baada ya kufanya hivyo alielekea katika chumba cha mr. Tyoso na kuchukua bunduki mbili walizozitumia kwa ujambazi lakini pia alichukua fedha ambazo aliziona. Alirudi na kuchukua funguo za gari katika suruali aliyokuwa ameivaa mr. Tyoso ambaye bado alikuwa akilalamika kwa maumivu makali. Alifanikisha mambo hayo ndani ya dakika saba na alitoka mbio nje akiwa pia amebeba upinde na mishale, mara baada ya kupakia vitu vyote kwenye gari alilitoa kwa kasi eneo hilo la nyumba ya mr Tyoso. Alikuwa amebeba bunduki, upinde na mishale sambamba na fedha za kutosha kwani alielewa jambo lililofuata lilikuwa malipizi ya vifo vya wazazi wake.

    Alikimbiza gari hilo aina ya ‘Land Cruiser’ akiwa na mpango wa kuvuka mipaka kuelekea Tanzania na hatimaye kuingia Dar es salaam kwa ajili ya kufanya malipo ya mauaji. Wakati akiwa anaendelea kuliacha jiji la Nairobi kuna jambo aligundua lilikuwa la muhimu kulitekeleza, alichukua simu yake na kumpigia mr Jackson ambaye baada ya simu kuita kwa muda mfupi aliipokea “baada ya kumuua mr. Tyoso nakuja kuwaangamiza na nyinyi wote nawapa siku saba za uhai wenu” alisikika Geofrey mara baada ya simu kupokelewa kabla ya kukata na kuizima. Aliendeleza kasi ya kuendesha gari lake, hakuwa na mpango wa kuwashirikisha polisi jambo hilo kwani aliamini walishindwa kufanya kazi yao kwa zaidi ya miaka kumi, alipanga kuwauwa wamiliki wa kampuni ya JAJHO wote kwa mkono wake.

    Mr. Jackson alishtushwa na kauli aliyoipokea toka kwa mtu ambaye namba yake aliihifadhi kama Geofrey akiwa mtoto wa marehemu James. Hisia za kugundulika kwa siri yao zilimjia jambo lililopelekea ampigie simu tena Geofrey ili ajue kama alikuwa ameigundua siri hiyo lakini simu ya kijana huyo haikupatikana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog