Search This Blog

Sunday 19 June 2022

MUUAJI ALIYEBAKIA - 5

 





    Simulizi : Muuaji Aliyebakia

    Sehemu Ya Tano (5)



    Hisia za kugundulika kwa siri yao zilimjia jambo lililopelekea ampigie simu tena Geofrey ili ajue kama alikuwa ameigundua siri hiyo lakini simu ya kijana huyo haikupatikana.

    Aliamua kumpigia simu mr Tyoso ili ahakikishe kama kweli alikuwa ameuawa, simu yake ilipokelewa na mtu mwingine aliyemthibitishia kifo cha mr. Tyoso. Upelelezi wa haraka alioufanya mr Jackson aligundua Geofrey alikuwa akifanya kazi kama jambazi chini ya usimamizi wa mr Tyoso.

    Uthibitisho wa siri hiyo kuvuja ulikamilika na aliwaita wenzie na kuwaeleza juu ya jambo hilo lakini zaidi aliwataka wajiweke katika tahadhari ili wafanikishe kumuua Geofrey kabla ya kuuawa kwao. Walitafuta vijana wakakamavu zaidi ya ishirini na kugawana watano kila mmoja na zaidi waliwatafuta wengine zaidi ya thelathini waliopewa jukumu la kufuatilia nyendo za Geofrey waliyeamini bado alikuwa hajaingia Dar es salaam. Jackson na wenzie walijipa matumaini wakiamini kuwa ni lazima Geofrey angeuawa kabla yao kutokana na mikakati waliyoiweka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya siku tatu Geofrey alikuwapo nchini Tanzania, alikuwa amefikia wilaya ya Bagamoyo katika kijiji cha Fukayosi akiwa amejitambulisha kama mpangaji katika nyumba yenye vyumba vitatu aliyoishi mzee mmoja. Alikuwa amepewa chumba kimoja kati ya hiyo vitatu wakati vingine vilitumiwa na mzee huyo, alimtoa hofu mzee huyo akidai kuwa alikuwa akifanya utafiti katika maeneo hayo na angeishi kwa muda wa wiki mbili. Mzee huyo hakuwa na ubishi kwani alipea fedha za kutosha, tayari Geofrey alikuwa na pikipiki aliyoinunua njiani wakati akitokea Kenya. Siku iliyofuata aliondoka na pikipiki akielekea jijini Dar es salaam ambako alifanya zoezi la kuzitambua nyumba za wamiliki wa kampuni ya JAJHO ambalo halikuwa gumu kutokana na umaarufu na utajiri waliokuwa nao. Tayari aliamua kuanza mauaji na Onesmo baada ya kuona uwezekano wote wa kufanikisha zoezi hilo, alikuwa amepanga kuwauwa wamiliki hao ndani ya usiku mmoja siku iliyofuata.

    Siku iliyofuata majira ya saa tatu usiku aliondoka Bagamoyo na pikipiki akielekea jijini Dar es salaam akwa na lengo moja la kwenda kuwauwa wamiliki wa kampuni ya JAJHO. Alikuwa amebeba upinde na mishale sambamba na na bunduki moja iliyokuwa na risasi za kutosha, vyote alikuwa ameviweka kwenye begi kubwa alilokuwa amelibeba mgongoni lakini pia alikuwa na tochi pamoja visu kadhaa vilivyozunguka kiunoni mwake. Alikuwa hajatumia dawa zozote za kulevya lakini akili yake kwa ujumla ilimtuma kuua, alikuwa mtu aliyeathirika kisaikolojia ambaye ilikuwa vigumu kuubadili msimamo wake.

    Saa tano usiku alikuwa nje ya geti la mr. Onesmo akiwa ameshaiegesha pikipiki yake na bila kuchelewa aligonga akiwa amejitega kwa shari pembeni na mlango mdogo wa geti hilo. Alisikia vishindo mlinzi akijongea getini na kuanza kufungua mlango mdogo wa geti hilo, alijiweka tayari akiamini alipaswa kuanza na mlinzi huyo akiwa ameshika moja ya kisu kilichon`gaa kutokana na ukali wake. Mara baada ya kutoka mlinzi huyo aliyekuwa na bunduki yake alipokelewa na teke zito la usoni lililomrudisha ndani ya geti hilo akiwa ameanguka. Kabla hajafanya jambo lolote alinyan`ganywa bunduki aliyokuwa nayo, Geofrey alimwelekezea bunduki hiyo mlinzi huyo kabla ya kuambiwa aongoze kwenye chumba chake cha ulinzi kilichokuwa getini hapo. Alitekeleza jambo hilo na kwa haraka aliingia kwenye chumba hicho akifuatwa na Geofrey ambaye alimuhoji maswali kadhaa na aligundua Onesmo alikuwa hajarudi nyumbani kwake. Alieleza lengo lake la kumuhitaji Onesmo na si mlinzi huyo hivyo alitumia kamba zilizokuwapo katika chumba hicho na kumfunga mikono na miguu. Baada ya kufanikisha zoezi hilo alimpiga mlinzi huyo na kitako cha bunduki yake katika mishipa yake ya fahamu ya shingoni iliyopelekea mlinzi huyo aanguke chini akiwa amepoteza fahamu.

    Alitoka nje kwa kasi na kuchukua pikipiki yake na kuiingiza ndani katika chumba hicho cha cha mlinzi alibadilisha shati lake na kuvaa la mlinzi huyo sambamba na kofia yake hakubadili suruali kwa vile iliendana na ya mlinzi huyo.Wakati akitafakari jambo la kufanya alishtuhwa na honi za gari zilizopigwa nje ya geti hilo. Bila kujiuliza mara mbili aligundua mtu huyo alikuwa Onesmo akirudi nyumbani kwake, alielekea katika geti hilo na kulifungua kwa kasi la kwanza na hatimaye la pili ambalo alijificha nyuma yake. Alishuhudia gari mbili zikiingia na kwenda kuegesha eneo la mbele la nyumba ya hiyo alishuka Mr Onesmo na watu zaidi ya kumi walioonekana walikuwa wakimlinda.

    Tayari alikuwa amefunga geti hilo na kurejea katika kibanda chake, kwa sauti ya chini alisikia maongezi yaliyoendelea “bosi leo tunaomba tukapumzike ili turudi kwa kasi mpya ya kesho lakini pia huna haja ya kumuogopa Geofrey huyo ni mtu mdogo sana hatuwezi” alisikika mmoja wa watu hao aliyeonekana alikuwa kiongozi wao. “sawa kwa leo tu ila saa kumi na moja muwe mmefika hapa” Aliwajibu Onesmo ambaye alianza kutembea akielekea katika nyumba yake kabla ya kufunguliwa na kuingia. Watu hao walioonekana kama walinzi wa Onesmo waliingia kwenye gari hizo Mercedez Benz mbili walizofika nazo na walianza kuziendesha wakiziondoa eneo hilo. Geofrey alijua jukumu lake kwa kasi alifungua geti na watu hao waliondoka.

    Hapo aliamini mchezo ulikuwa umeisha bila kupoteza muda alichukua visu vitatu na bunduki moja iliyokuwa na risasi za kutosha aliongoza hadi kwenye mlango wa kuingilia wa nyumba hiyo na kuanza kugonga. Aliamini mtu aliyekuwa amemfungulia Onesmo lazima angerudi kumfungulia baada ya muda mfupi akisikia vishindo vya mtu huku akiongea “jamani mlinzi nini tena….” Aliongea dada huyo ambaye mara baada ya kufungua mlango alipokelewa na bomba la mbele la bunduki. “kwa usalama wako tulia naomba unionyeshe chumba anacholala mr Onesmo” Aliongea Geofrey akiwa amemkazia macho dada huyo ambaye alinyosha mkono akionyesha ghorofa ya kwanza ya nyumba hiyo. Baada ya maelezo hayo Geofrey akitumia nguvu alimpiga msichana huyo na kitako cha bunduki na kupelekea kuanguka kwake kabla ya kupoteza fahamu.

    Bila kupoteza muda Geofrey alikimbia akielekea ghorofani mwa nyumba hiyo alipofika aliuona mlango mmoja ambao ulikuwa haujafungwa vizuri huku taa yake ikiwaka aliingia na kumshuhudia mr. Onesmo akibadilisha nguo za kulalia huku mkewe akiwa amelala “mamaaa weeee nafwaa huwiiiii” alipiga kelele mr Onesmo ambazo zilimwamsha hata mkewe. “tulia mbwa wewe nisije nikakuua kabla ya wakati” aliongea Geofrey akiwa amemwelekezea bunduki yake jambo lililoleta utulivu hata kwa mkewe Onesmo ambaye hakujua jambo lililoendelea. “ nipe simu yako haraka iwezekanavyo” alitoa agizo hilo ambalo Onesmo alilitekeleza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “ulidhani mlivyowauwa wazazi wangu nisinge wagundua” aliongea Geofrey wakati akikipitisha kisu chake tumboni katika hali iliyoonyesha alikisafisha na bado alikuwa amemwelekezea bunduki mr Onesmo. Alikuwa ameshika kisu kirefu mithili ya panga kilichon`gaa kupindukia, ghafla alikurupuka na kumvamia Onesmo akiwa amelekezea kisu hicho tumboni kilichompata sawasawa. Wote alianguka chini huku Geofrey akiwa bado amekishikilia kisu, alikitoa kwa kasi na bila huruma alishindilia mara tatu zaidi akichoma na kuchomoa. Damu iliyotoka na kuruka ilikuwa ni zaidi ya machinjio, jambo hilo ndilo lililopelekea mkewe Onesmo kuzimia. Geofrey akiwa amebeba bunduki yake alitoka mbio chumbani hapo na kuongoza moja kwa moja hadi kwenye kibanda cha mlinzi ambaye alikuwa hajarudiwa na fahamu. Aliwasha pikipiki na kuchukua vitu vyake vyote kabla ya kuiondoa pikipiki hiyo kwa kasi eneo hilo la nyumba ya Onesmo.

    Baada ya saa moja alikuwa maeneo ya Kimara katika hoteli iliyotambulika kwa jina la `Mwalon West` ambako bila kupoteza muda alilipia chumba kimoja.Tayari ilikuwa yapata saa saba na nusu usiku bado lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha anakamilisha mauaji kwa wamiliki wa kampuni ya JAJHO katika usiku huo. Aliamini simu ya Onesmo aliyoichukua kabla ya kumuua ndiyo ingekamilisha zoezi hilo, aliandaa visu, bunduki yake sambamba na upinde na mishale ambavyo aliviweka chini ya uvungu. Alikuwa amechanganyikiwa na hakuwaza jambo lolote zaidi ya kuua, alichukua simu ya Onesmo na kufanikiwa kuziona namba za simu za Jackson, Hamis na Amos. Baada ya kuziona namba hizo alifungua sehemu ya ujumbe mfupi wa maandishi na kuanza kuandika.





    Baada ya kuziona namba hizo alifungua sehemu ya ujumbe mfupi wa maandishi na kuanza kuandika.

    Alipanga kuwatumia wamiliki hao ujumbe wa maandishi ili wafike hotelini hapo akiamini wangeshawishika.

    Baada ya dakika tatu alikamilisha ujumbe huo uliokuwa hivi ‘Mkubwa Nimefanikiwa Kumkamata Mshenzi Geofrey James Kibudo, Fanya Haraka Uje Katika Hoteli Ya Mwalon West Chumba Namba 25 . Njoo Peke Yako Kama Unavyojua Inatubidi Tuue Na siri Hii Asiijue Mtu…..! Nakusubiri!’ Alikamilisha Geofrey ujumbe huo wa simu na kuutuma kwa namba za watu hao kwa pamoja. Ujumbe huo ulionyesha kupokelewa na Hamis pamoja na Amos lakini haikuwa hivyo kwa Jackson. Geofrey alijaribu kumpigia namba yake ilikuwa haipatikani. Baada ya dakika tatu akiwa anatafakari jambo la kufanya alishtushwa na mlio wa simu hiyo kabla ya kushuhudia ujumbe wa maandishi toka kwa Hamis ulioandikwa ‘Msimuue Huyo Mshenzi Nakuja Sasa Hivi…’ dakika moja baadaye Amos naye alithibitisha kufika hotelini hapo.

    Geofrey alijua kazi ilielekea kuisha aliandaa upinde na mshale tayari kwa mauaji, alikuwa akiwasubiri kwa hamu ili aendelee kukamilisha ndoto yake ya kuwaua wote usiku huo. Baada ya nusu saa alisikia mlango ukigongwa, jambo lililompa hisia kuwa mmoja wa watu hao alikuwa amefika, kwa kasi alienda kusimama kando ya mlango huo akiwa na upinde na mshale uliotegeshwa tayari kwa shari. “tafadhari ingia…” alisikika Geofrey na kumfanya mtu aliyekuwa angonga kufungua mlango na kuanza kuingia. Mara baada ya kuingia alianza kuangalia huku na huku akionekana kama alitafuta kitu, Geofrey alikuwa ametulia huku akiwa amegundua mtu huyo alikuwa Hamis.

    Akiwa bado hajatulia vizuri alishtushwa na sauti ya mtu aliyekohoa alipogeuka alitoa macho kabla kuanza kupiga kelele “siniue usiniue tafadhari..” alipiga kelele Hamis baada ya kumshuhudia Geofrey akiwa tayari kwa kumuua “tulia we mbwa huna muda wa kupoteza inakupasa uuangane na mwenzio Onesmo…” alisikika Geofrey kabla kuachia mshale ulioenda kumpata sawasawa Hamis tumboni, akiwa hajatulia vizuri alisindikizwa na teke la uso lililompeleka mpaka chini, alianza kulalamika kutokana na maumivu aliyoyapata. Geofrey alichukua bunduki chini ya uvungu wa kitanda akiwa anahofia usalama wake baada ya kelele zilizotolewa na Hamis, aliiweka vizuri baada ya ya kusikia vishindo vya mtu akija kwa kasi eneo la chumba hicho. Punde alishtushwa na sura mtu huyo aliyeingia bila kugonga baada ya kuona alikuwa ni Amos “mikono juu kunguru mkubwa na taratibu sogea kwa mwenzio…” alisikika Geofrey kwa jazba na kumchanganya Amos aliyetetemeka kupindukia baada ya kumwona Hamis akiwa ametokwa na damu nyingi na bado alikuwa akihangaika. Jambo hilo lilimfanya Amos achanganyikiwe ghafla na kushindwa kutimiza amri aliyopewa, hasira za Geofrey ziliongezeka na kuamua kuanza kumiminia risasi Amosi ambaye alianguka baada ya muda mfupi.

    Alimgeukia Hamis na kumpiga naye risasi ya kichwa na kumfanya atulie kabisa. Kulikuwa na kelele za watu waliohofia uhai wao baada ya kusikia milio hiyo ya risasi. Bila kuchelewa Geofrey alichukuwa funguo za pikipiki yake pamoja na bundu ki hiyo aliyokuwa bado kaishika alianza kukimbia akitoka katika hoteli hiyo. Aligongana na watu waliokuwa wamechanganyikiwa wakizunguka katika hoteli hiyo, alipiga risasi nyingine mbili sakafuni ambazo ziliwafanya hata walinzi wakimbie. Geofrey alifanikiwa kuichukua pikipiki yake na kuondoka kwa kasi eneo hilo la hoteli ya Mwalon West. Alikimbiza pikipiki yake akielekea Bagamoyo alikokuwa amepanga chumba, tayari aliona ndoto zake zilikuwa zimeingia dosari kwa vile hakufanikisha mauaji ya watu wanne. Alikuwa anawaza kuhakikisha anaenda kujiandaa kwa ajili ya kurudi kumalizia mauaji na Jackson.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    * * * *

    Magreth alikuwa ameshtushwa na kukatika kwa mawasiliano ghafla kati yake na mwanamme wa ndoto zake, Geofrey. Muda wote alikuwa akilia akiwa hajui jambo lililokuwa limemtokea, kuna wakati alikuwa akihisi mwanamme huyo alikuwa amemsaliti. Alikuwapo katika chuo cha Guyana akiwa amebakiza muda mfupi ili amalize elimu ya chuo, wakati huo maendeleo yake kitaaluma yalikuwa mabovu kutokana na mawazo aliyokuwa nayo juu ya Geofrey muda wote. Baada ya miezi kadhaa alishindwa kuvumilia na aliamua kuondoka chuoni hapo pasipo kuaga na kuandaa safari yake ya kurudi Tanzania. Hatimaye siku hiyo ilifika na safari ilianza akiwa hajatoa taarifa ya safari hiyo hata kwa wazazi wake.

    Baada ya wiki moja alikuwapo nchini Tanzania akimtafuta Geofrey kila kona ya jiji la Dar es salaam pasipo mafanikio yeyote, jambo lililomkatisha tamaa kwa kiasi kikubwa.Alikuwa amefikia katika nyumba yao na kila siku alitumia gari lake kumtafuta Geofrey akiwa anatembea na picha yake lakini hakuna mtu aliyemfahamu. Hapo ndipo Magreth alipozidi kuchanganyikiwa zaidi akiamini alikuwa amepoteza mwelekeo wa kumpata. Siku moja akiwa Kariakoo katika mizunguko yake hiyo ya kumtafuta, alishtuka baada ya kumuona kwa umbali mtu aliyeamini alikuwa ni Geofrey. Alishuka kwenye gari na kuanza kumkimbilia mtu huyo huku akimwita. “Geoffur!, Geoffur……..” alimwita mtu huyo ambaye hakuitika na baada ya sekunde kadhaa kelele za kuita zikiwa zimeongezeka mtu huyo alisimama.

    Magreth akiwa anakimbia alimrukia na kumkumbatia na wote waliaanguka chini, watu waliokuwa katika pilikapilika zao walianza kushawashangaa. “ wewe dada vipi? mbona unanirukia inakuwaje?” Alisikika mwanamme huyo mara baada ya kusimama. “samahani kaka unafanana sana na mchumba wangu” aliongea Magreth huku akiwa na anajisikia aibu ikiwa ni baada ya kugundua mtu huyo hakuwa Geofrey ila walifanana sana. “samahani naomba tuondoke wote maana watu wanatushangaa nitakueleza vizuri niko na gari” Alisikika Magreth na walianza kutembea na mwanamme huyo hadi kwenye gari na kuondoka eneo hilo. Baada ya muda mfupi wa maongezi Magreth aligundua jambo lililompa matumaini, mwanamme huyo alikuwa mdogo wake Geofrey aliyeitwa Robert. Alikuwapo Tanzania kwa miezi zaidi ya sita akiwa na mchumba wake wakitokea Marekani na kazi aliyoifanya alikuwa akipeleleza juu ya tukio la mauaji ya wazazi wake zaidi alikuwa anaamini kaka yake Geofrey alikufa katika tukio la ajali ya ndege nchini Guyana. Robert alikuwa ameacha biashara zake nchini Marekani na jambo lililopelekea hayo yote lilihusiana na upelelezi juu ya kifo cha wazazi wake. Magreth pia aligundua juu ya kifo cha wazazi wa Geofrey na zaidi alimweleza Robert kuwa kaka yake bado alikuwa hai na alimsimulia kisa kizima cha maisha ya kaka yake huyo na zaidi alimwonyesha picha zake. Jambo hilo lilimfurahisha kwa kiasi kikubwa Robert, alijiona kama hakuwa mpweke kutokana na uhai wa kaka yake.

    Siku iliyofuata waliendeleza zoezi la kumtafuta Geofrey wakati Robert alikuwa na mchumba wake aliyeitwa Annie ambaye alitoka naye Marekani. Ni siku ambayo ilikuwa ngumu na iliwachanganya zaidi kwani vyombo vingi vya habari vilitawaliwa na kisa cha kuuawa matajiri wakubwa watatu wakitanzania. Muuaji alitajwa kwa jina la Geofrey James Kibudo, ingawaje picha zake hazikupatikana lakini polisi walikuwa wakiendelea na msako mkali ili kumnasa. Magreth alichanganyikiwa hata hamu ya kumtafuta Geofrey ilianza kupungua lakini Robert naye hakuwa ametulia kwani alishtushwa juu ya taarifa hizo. Annie aliwapa moyo akiwaeleza huenda Geofrey hakuhusika na waliendelea na zoezi lao hilo la kumtafuta Geofrey. Muda wote Magreth alikuwa akilia na kuonekana kujuta kukutana na Geofrey lakini bado alithibitisha kuwa Geofrey alikuwa mwanamme wa ndoto zake.

    Siku tano zilikatika na kulikuwa hakuna taarifa zozote kutoka jeshi la polisi juu ya kupatikana kwa muuaji lakini bado Magreth na wenzie walikuwa wakiendelea na zoezi la kumtafuta Geofrey. Walikuwa wakilala kwenye gari na walitembelea kila sehemu waliyohisi wangempata, siku hiyo majira ya saa mbili usiku walikuwa maeneo ya Bagamoyo katika kituo cha kuuza mafuta ya gari.Walikuwa wakiongeza mafuta katika gari lao baada ya mizunguko mingi, wakati zoezi hilo liliendelea kuna mtu alifika na pikipiki na kuegesha eneo la mbele yao akiwa na nia ya kuongeza mafuta. “Geoffur, Geoffur…..” alipiga kelele Magreth huku akishuka kwenye gari walilokuwa nalo na kumfuata mtu aliyekuwa kwenye pikipiki ambaye pia alishtuka kabla ya kushuka katika pikipiki. Magreth alimkimbilia na kumkumbatia Geofrey aliyeanza kulia baada ya kumwona.



    Magreth alimkimbilia na kumkumbatia Geofrey aliyeanza kulia baada ya kumwona.

    Hatimaye Robert na Annie walijongea eneo hilo, Robert alikurupuka kwa kasi na kumkumbatia Geofrey na wote walianguka chini. Geofrey ambaye alikuwa mnyonge huku akiwa amebeba begi kubwa, hakuuliza na alionekana kumkumbuka mdogo wake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Magreth nisamehe nadhani nimeharibu ahadi yetu kwa vile sidhani kama ndoto zetu zitatimia kama tulivyopanga, bado nahitajika kuua mtu wa mwisho aliyewaua wazazi wangu” alisikika Geofrey huku akiweka begi lake vizuri alilolibeba mgongoni kabla ya kuisogelea pikipiki na kupanda. “ nakupenda sana Magreth lakini yanipasa niondoke, Magreth, Roby aamh! Annie naenda, lakini muwe waangalifu” Alisikika Geofrey kabla ya kuwasha pikipiki yake na kuiondoa kwa kasi eneo hilo.

    Wote walibaki wamepigwa na butwaa na zaidi Magreth aliyeonekana akilia, ghafla aliacha kulia akasikika akisema “hapana, hapana Geoffur nampenda…,haiwezekani..! kama kufa tufe wote” alitoka akikimbia na kwenda kuingia kwenye gari kabla ya kuliwasha na kuliondoa kwa kasi eneo hilo akiwa amemwacha Robert na Annie wakiwa hawaelewi jambo la kufanya. Annie alimtuliza Robert aliyechanganyikiwa kwa kiasi kikubwa na alimtaka waende wakatulie ili watafakari jambo la kufanya na ikawa hivyo. Walipata chumba katika hoteli moja na walikuwa wakitathimini juu ya matatizo hayo waliyokumbana nayo.

    Siku iliyofuata majira ya saa moja asubuhi walipata taarifa za kifo cha Magreth aliyepata ajali mbaya mara baada ya kuondoka akiwa na lengo la kumfukuzia mchumba wake Geofrey. Baada ya dakika tano walipata taarifa nyingine iliyoeleza Geofrey James Kibudo alikuwa katika hali mbaya akiwa amelazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili baada ya kushambuliwa na askari wakati akijaribu kumuua tajiri Jackson. Ilielezwa alikuwa amepigwa risasi zaidi ya nane, bila kupoteza muda Robert na Annie walikodi teksi na kuondoka maeneo ya Bagamoyo wakiwa na lengo la kwenda kumuona. Robert alikuwa na hasira na mpaka wakati huo alikuwa hajui juu ya jambo lililoendelea juu ya mkasa huo.

    “waliowaua wazazi wetu ni wamiliki wa kampuni ya JAJHO na amebaki Jackson John Samola hakikisha unamumaliza mwenyewe kwa vile naamini jeshi la polisi lilishindwa kazi hiyo” ilikuwa ni kauli ya Geofrey aliyeongea kwa taabu sana mara baada ya Robert na Annie kufika hospitali. Alikuwa hajazungumza kitu kwa askari waliokuwa wanamlinda zaidi ya kauli hiyo aliyoitoa kwa Robert.Hata hivyo hakuna askari aliyesikia maelezo hayo, na Geofrey alionekana hakuwa na imani na jeshi la polisi. Baada ya dakika chache alifariki na Robert alilia kwa uchungu juu ya tukio hilo lililomuuma na aliamini kuuawa kwa Jackson ilikuwa ni kazi iliyokuwa mikononi mwake. Alitoka mbio eneo hilo la hospitali kabla ya kwenda kukodi teksi akihitaji apelekwe Masaki katika nyumba aliyoishi Jackson. Alikuwa hana silaha ya aina yeyote lakini imani yake ilikuwa ni kufanikisha mauaji hayo. Annie aliamua kuwaeleza askari juu ya kila kitu alichokisikia na askari waliondoka naye wakiwa na lengo la kwenda kumkamata Jackson kwa kuhusika na mauaji.

    Teski aliyokodi Robert ilienda kusimama nje ya geti la nyumba ya Jackson, kulikuwa na kundi kubwa la watu maeneo hayo. Mara baada ya kumlipa dereva wa gari hilo alishuka na kujichanganya na watu hao “du! yani jamaa amejiua… aah! hii kali kaka…” alisikika mmoja wa watu waliokuwapo eneo hilo na kumfanya Robert aliyekuwa na hasira kuuliza swali “nani kajiua na kwa nini….” “Aah.. Mr Jackson Samola amejipiga risasi kichwani…” alijibu mmoja wa watu hao. Robert alianza kulia kwa sauti kama na yeye alikuwa mfiwa wa tukio hilo, lakini hiyo yote ilitokana na hasira alizokuwa nazo. Baada ya dakika kadhaa askari walifika eneo hilo na kukamilisha taratibu zote zilizohitajika.

    Hatimaye Geofrey na Magreth walizikwa mjini Moshi eneo ambalo baba yake Magreth alizaliwa. Hiyo yote ilitokana na ombi la Robert aliyependa watu hao wawekwe karibu ingawaje hawakuwa katika ndoa. Jambo hilo lilikuwa la kusikitishwa hasa kwa watu waliopata kisa cha Magreth na Geofrey.Baada ya maombolezo ya msiba huo Robert alipanga safari tayari kwa kurudi na mchumba wake Marekani kuendeleza biashara zake. Siku moja kabla ya safari alipigiwa simu na askari waliomhitaji, alitii agizo hilo na mara baada ya kufika kituo cha polisi alipewa ujumbe mfupi ulioandikwa kwenye karatasi ambao Mr Jackson aliandika kabla ya kujiua alianza kwa kuusoma

    “…nilikuwa mpumbavu kwa kupingana na mkono wa sheria ya nchi yangu, kwani sheria ikiamua inapaswa itekelezwe lakini nilipinga adhabu ya kunyongwa aliyopewa kaka na baba yangu mzee Samola…, mwishoe walinyongwa. Niliamua kulipa kisasi cha vifo hivyo kwa James Kibudo na mkewe wasio na hatia lakini nimesababisha madhara makubwa kwani watoto wake nao wananitafuta waniue. Nimeamua kujiua kwa vile mimi pekee ndiye ‘MUUAJI ALIYEBAKIA’, hata nikisubiri mkono wa sheria lazima nitanyongwa na siri zangu zimeshagundulika.Naomba nusu ya utajiri wa kampuni ya JAJHO wapewe wanawe James Kibudo…….” Alimaliza Robert kusoma ujumbe huo ulioandikwa na Mr Jackson kabla ya kujiua. “du! sichukui kitu kutoka kampuni ya JAJHO, sihitaji kuona damu ikimwagika zaidi, nawaachia kila kitu” alisikika Robert mara baada ya kutoka kituoni hapo.

    Hakuwa tayari kuchukua mali ya kampuni hiyo iliyokuwa na historia ndefu ya mauaji, aliona jambo la msingi ni kutochukua kitu na zaidi biashara zake aliamini zilimtosha.

    Baada ya miaka kumi Robert alikuwa tajiri mkubwa katika jimbo la Illinois, Marekani na tayari alishaanza kusahau matatizo yaliyoikumba familia yake miaka kadhaa iliyokuwa imepita. Tayari alikuwa na watoto wawili na alikuwa akifurahia maisha ya ndoa na Annie, kumbukumbu zake zilikuwa hazimtoki kichwani juu ya kifo cha familia yake na mchumba wa kaka yake Magreth. Siku zote katika maisha yake sala zake alimaliza kwa kusema ‘Mungu Azilaze Roho Zao Mahali Pema

     Peponi’.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    MWISHO.



0 comments:

Post a Comment

Blog