Search This Blog

Sunday 19 June 2022

ROHO MKONONI - 4

 





    Simulizi : Roho Mkononi

    Sehemu Ya Nne (4)



    Kundi dogo la akina Fonga ambalo halikuwa limejipanga ki-silaha, likajikuta limecheza makosa mawili ambayo yaliubadili usiku huu kuwa usiku wa machozi na damu!!

    Huku nyuma Rasi alirejewa na fahamu, huku nje Malle na Rambo walikuwa moto wa kuotea mbali katika kitu kinachoitwa ulinzi wa nje. Rambo mtaalamu katika mashambulizi ya kutumia silaha. Huku upande mwingine Malle akiwa bingwa wa machale. Na kwa sababu alishachezwa machale mapema juu ya watu wale waliojitambulisha kama askari. Aliwangoja wakitoka aweze kuthibitisha utambulisho wao.

    HEKAHEKA USIKU MNENE, SINZACHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    HALI ya hewa ya jiji ilikuwa kama iwavyo siku nyingine. Joto kali kwa wageni lakini kwa wazawa hali hii ikionekana kuwa kawaida na wengine wakiona kuwa ile hali ya joto la kawaida ni baridi kutokana na vimanyunyu vilivyokuwa vimedondoka jioni ya siku hiyo. Baa na kumbi nyingine za starehe ndio kwanza kama zilikuwa zimefunguliwa na zikiwa hazina dalili ya kupooza bali shangwe kuongezeka kila nukta ya saa ilivyosogea mbele. Baa hii ikipiga muziki huu basi nyingine itapiga wimbo mwingine, huku ikiwekwa bendi kuwaburudisha wateja upande wa pili wataweka wasakata dansi wakate mayenu ili wateja wafurahi. Mambo yalikuwa mpweto mpweto!! Na hapa ule usemi wa kila baada ya nyumba baa ukaonekana maana yake. Haya yalitokea maeneo ya Sinza. Kuanzia Legho na kuendelea!!

    MSICHANA mmoja alikuwa amejichanganya na kundi la watu waliokuwa wakisukumana waweze kutazama burudani ya wacheza sebene katika jukwaa dogo lililokuwa katika baa mojawapo jirani na Rombo Green View. Hakushawishika hata kidogo kugeuka kuwa shabiki wa kweli lakini badala yake alikuwa akiangaza kwa makini kabisa matukio mbali mbali yaliyokuwa yanaendelea kulizunguka eneo lile. Akilini alikuwa akiwaza juu ya milioni zaidi ya tano alizokuwa ameahidiwa iwapo watafanikisha mpango wao kabambe wa usiku huo. Mpango ulionekana kukamilika bila kuleta mushkeri wowote ule, sasa alikuwa akitabasamu katika nafsi yake kuwa baada ya muda atakuwa anamiliki pesa ambayo hakuwahi kuishikahapo kabla. Kuanzia maisha yake ya uyatima, ubaamedi na ufungwa hakuwahi kufikiria juu ya kiasi kile cha pesa. Sasa alikuwa anakaribia kukipata kwa kufanikisha mbunge kuwekwa chini ya ulinzi wao. Husna Ngumi jiwe alikuwa makini na kila kitu!! Jicho lake jepesi kuona, lilivutiwa kumtazama kiumbe aliyeuhifadhi mwili wake katika fulana iliyombana vyema na chini akiwa na suruali ya kitambaa na moka. Kijana huyu alikuwa akilitazama kwa wiziwizi, gari ambalo wao walikuja nalo kwa nia ya kumuadabisha mheshimiwa Beka na kisha kujua yu wapi Betty!! Hii ilikuwa shida kuu ya Fonga. Lakini Mark akajiongezea jukumu, alimuhitaji Beka ili aweze kupata pesa ambazo hatakuwa amezitolea jasho sana. Na sasa alikuwa yu pamoja na Beka na walitaka kumwingiza ndani ya gari. Lakini kwa jinsi gari lilivyokuwa limeegeshwa iliwawia ngumu sana kutoka eneo lile. Mark alikuwa ameelewana na Husna juu ya mahali ambapo atamkuta baada ya kutoka na gari. Husna hakuongozana nao, akapitia njia alizozifahamu yeye bila kuonekana na watu. Sasa Husna kutokea mahali alipokuwa amejichanganya anamuona mwanaume akiwa anafuatilia jambo fulani, na mbaya zaidi hakuwa mwenzao. Husna akaona dalili ya kuzipoteza zile pesa imenukia, iwapo tu yule mtu atakuwa upande wa Beka, ama akiwa ni kutoka jeshi la polisi. Upesi Husna akaruka hatua mbili tatu akazidi kumkaribia mwanaume yule!! Akiwa anamvizia aweze kufanya lolote lile naye aweze kutambua nini cha kufanya mara, kwa pamoja yeye na yule mwanaume wakajikuta wakigeuka nyuma kutazama kelele kubwa ilipotokea. “Rasi!! Alijikuta akisema kwa hofu yule mwanaume baada ya kumuona kijana akitoka katika mlango wa hoteli ya Rombo Green view. Hakuwa peke yake bali alikuwa amemkamata vyema msichana ambaye alikuwa na mavazi maalum ya wasichana wa mapokezi. Ni yuleyule msichana ambaye awali aliwapokea wakajitambulisha kuwa wao ni askari na walikuwa pale kwa madhumuni ya upelelezi juu ya tukio la mauaji na kisha wakamkamata bwana Beka. Ambaye alikuwa lengo haswa! Macho ya Husna yakageukia upande walipokuwa akina Fonga, akatamani kuwapa tahadhari watoweke upesi lakini walikuwa mbali kiasi kwamba asingeweza kuwahi. Tayari akili ya Husna ilikuwa imepata majibu kuwa yule kijana mwenye fulana alikuwa ni mmojawapo wa walinzi wa bwana Beka. Kwa macho yake yalivyomtambua Rasi yule kijana ambaye Husna alimtwanga kichwa kimoja kizito kisogoni. Husna akabaki kumtegea yule kijana ili uelekeo atakaokwenda naye aelekee huko huko. Kijana akanyanyua simu yake akiwa mita kadhaa kutoka alipokuwa Husna. “Rambo, wahi maeneo ya Parking wanaondoka na muheshimiwa!!” alisema kwa sauti ya kusisitiza. Kisha akakata simu. Husna akatabasamu kisha akajisikia akifurahia tukio lile linaloendelea.

    Walinzi wa hoteli ile walijaribu kumtetea yule msichana aliyekuwa amekamatwa na Rasi bila mafanikio. Walijaribu kumsihi Rasi lakini hakuonekana kuelewa lolote. Husna alipofanikiwa kuyatazama macho ya Rasi akatambua kuwa Rasi hakuwa katika uwezo wake wa kawaida wa kufikiri,na punde akaipigia mstari kauli yake baada ya Rasi kuwavaa wale walinzi waliokuwa na gobore kisha kuanza kutoa kichapo tena, hapa sasa ukawa mshike mshike wa hali ya juu. Wateja waliokuwa katika utulivu wakaikosa amani. Rasi alikuwa amepandwa na wazimu uliosababishwa na kutetemeka kwa ubongo wake wa nyuma kutokana na pigo maridadi kutoka kwa Husna. Husna ambaye alitarajia kuwa Rasi hataweza kuamka tena sasa alikiri kuwa mafunzo ya ubondia aliyokuwa anahudhuria yalikuwa yamemjenga zaidi kimapigano na alizitambua vyema sehemu hatari katikamwili wa binadamu ambazo zikiguswa huzua tafrani.

    Wakati mwendawazimu Rasi akifanya yale anayoyajua yeye na akili yake ya muda ule. Gari ya akina Fonga ilikuwa imepata upenyo wa kutoka, wakati inaanza kuingia barabara ya Shekilango kuelekea maeneo ya Sinza Kamanyola, Husna alimuona tena yule bwana aliyevaa fulana akijipekua katika kiuno chake. Bunduki!! Alitahayari Husna, lakini hakupoteza zaidi ya sekunde tatu akachukua maamuzi. Tamaa ya kuzipata pesa na kuukimbia umasikini zilikuwa zinamuongoza. Husna akiwa amefahamu fika lengo la kijana yule ni kuachia risasi ambayo itafanya madhara katika gari ambayo Beka alikuwa ndani yake, akatimua mbio akiwa pekupeku akipishana na watu ambao walikuwa wamechanganywa na vurugu za Rasi. Kwa mwendo uleule akamfikia kijana yule aliyekuwa amejikita katika kulingojea lile gari lifikie upande ambao alikuwa ametega. Bila kijana yule kuelewa azma ya Husna aligutuka bunduki ikiwa imepigwa na kuruka mbali naye. Na mara mbele yake akasimama Husna, suruali yake aina ya traksuti na jezi ya timu ya mpira vikimeremeta katika mwili wake. Malle alikuwa anatazama na Husna, mwanamke ambaye aliingia katika hoteli ile kama askari. Malle alikuwa mwepesi, akarusha teke kali. Husna akalipangua kama awezavyo kupangua ngumi kali akiwa katika mazoezi ya ubondia. Kisha akafyatuka kama kondoo akamkung’uta kichwa cha kifuani Malle. Malle akayumba yumba lakini hakuanguka. Akatokwa na yowe kubwa la maumivu huku akitokwa pia na matusi ya nguoni. Akajaribu kujirusha tena kwa mguu wa kulia, Husna hakukwepa badala yake alitega mikono tena akawa amepangua pigo lile. Wakati huu gari ya akina Fonga ilikuwa inapita mbele yao barabarani. Malle alitaka kuikimbilia ile gari lakini akanaswa miguu yake na msichana wa ajabu aliyekuwa mbele yake, akapiga mweleka na yule binti hakufanya jitihada za kumkabili akamsubiri ainuke. Malle aliaminikabisa akaiamua kumkabili binti yule kwa kutumia kisu chake ambacho kilikuwa mahali fulani mwilini kwake ataweza kumshinda vibaya lakini alichokuwa akihofia ni kuufanya ule umati uliokuwa ukishabikia ugomvi ule kulibadili tukio hili la ugomvi wa kawaida na kuwa ugomvi ambao polisi walitakiwa kupewa taarifa. Shida kuu ya Malle ilikuwa kuonana na mtu ambaye macho yake yalimueleza kuwa alikuwa ni Fonga. Malle alitaka kujiaminisha kwanza kama kweli ni yeye ajue kipi cha kufanya, kwani baada ya tukio la kumuua huyo Fonga,vijana hawa walitakiwa kwenda mahali alipokuwa amefichwa Betty na kisha kumuacha huru. Sasa huyo Fonga yu hai tena!! Malle aliduwaa. Uwezo wake wa kurusha mateke ukaathiriwa na tukio hilo hivyo kumpatia nafasi Husna kupangua kirahisi. Lakini kitendo cha kupigwa ngwala na kisha kutua chini kwa aibu kulimkasirisha sana na hata aliposimama tena imara mambo yalibadilika. Alirusha mateke kwa kasi kubwa, Husna alijaribu kuyapangua lakini safari hii mateke manne yaliuchakaza uso wake. Walevi walishangilia mpambano ule huku wakipewa onyo wale wote waliotaka kuachanisha!! Wote walijua ni mpambano wa kawaida tu na mshindi atapatikana kisha kila mmoja ataondoka zake. Malle alirusha konde la mkono wa kuume lililokuwa na ujazo mkubwa, lengo likiwa kumyamazisha binti yule na kisha atimue mbio kama ataweza kuliwahi gari aliloamini ndani yake alikuwamo Fonga. Malle alijipongeza kwa onyo alilompa Rambo kuwa asipige risasi yoyote ile. Kwani bila onyo lile bila shaka Rambo angekuwa amezua balaa tayari. Ngumi ile nzito ilipokelewa katika namna ambayo ilileta msisimkokuitazama. Husna badala ya kukwepa, alijirudisha nyuma kidogo kishaakakikutanisha kichwa chake na ngumiile. Kaa!! Ukasikika mlio, Malle alikuwa amepata hitilafu katika vidole vya mkono wake. Wakati akijichua huku uso wake ukiwa umetawaliwa na mikunjo ya hasira likatokea tukio ambalo ilikuwa bahati ya Husna kuliona. Yule mwendawazimu, muhanga wa pigo la Husna alikuwa akihaha huku na kule, mara akainama na kunyanyuka na kitu ambacho kilibadili eneo lile badala ya kuwa uwanja wa mapigano ukageuka kuwa uwanja wa damu. Rasi mwendawazimu alikuwa ameokota bunduki ambayo Husna aliipiga kikumbo kisha ikaruka mbali kutoka mikononi mwa Malle. Walevi hawakuzisikia kelele ambazo walinzi walikuwa wanapiga, Malle naye maumivu ya mkono yalikuwa yamemvuruga akili yake. Husna akawahi kujitupa pembeni kabla mwendawazimu Rasi hajafanya tukio la kutisha ambalo lilifanana kabisa na filamu za mapigano. Rasi alianza kufyatua risasi hovyo. Mbaya zaidi bunduki ile haikuwa katika mfumo wa kiwambo cha kuzuia sauti. Hivyo kila mlio ulisikika barabara na kuwachanganya watu. Baada ya dakika saba kimya kikatanda, damu ikiwa imetapakaa. Sinza ilikuwa kimya!!! Kila mmoja akiwa na hofu tele juu ya mfululizo wa matukio wa siku hiyo. Ni polisi pekee walikuwa wanaranda huku na kule katika doria kali kabisa.

    *****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    WAKATI Fonga na wenzake wakiwa katika simanzi na kuamini kuwa Husna aliuwawa katika shambulio lile, mwanadada huyu aliitazama taarifa ya habari asubuhi na kuushuhudia mwili wa Malle yule adui yake mkubwa ukiwa una madoa mawili katika kifua chake. “----- angeniua jana alivyonibadilikia dah” alisema kichovu Husna kisha akavuta shuka na kujifunika tena.

    TAARIFA hiyohiyo ilipokelewa jijini Dar es salaam, kwa namna ya kipekee. Mzee mmoja wa makamo alichukua simu yake upesi na kupiga simu kwa muheshimiwa Beka. Alitaka kumuuliza nini kimetokea, hasahasa baada ya kuona katika runinga kijana wa mzee Beka waliyemzoea kwa jina la Rasi akiwa amefungwa pingu na taarifa ikidai kuwa anahusika katika mauaji yale japokuwa alitazamika kama mtu mwenye wazimu uliokolea kichwani mwake. Mzee huyu aliona ni vyema kumuuliza muhusika moja kwa moja. Ama! Beka hakuwa akipatikana katika namba zake zote, akajaribu kumpigia kimada wake wa siri lakini bado majibu yalikuwa yaleyale kuwa Beka hakuwa akifahamika ni wapi alipo. Mzee huyu akakumbuka kuwa mzee Beka alivyomuomba nyumba yake kwa ajili ya kumtia mtu adabu alikuwa hana utaratibu wa kutumia vijana wengine tofauti na wale vijana wake wa kazi. Sasa vijana hao wapo matatani, mmoja ameuwawa na mwingine eti! Amekumbwa na wazimu na amehusika katika mauaji ya kutisha Sinza!! Ilishangaza!! Mzee yule akapata hofu kuwa huenda maadui wa mzee Beka ambao alikuwa amewakomoa kwa kumteka mtu wao walikuwa wamemzidi nguvu. Na kama ni hivyo basi mzee Beka popote alipo lazima kwa namna yoyote ile atakuwa amewatajia wababe hao mahali ambapo amemuhifadhi mateka wake. Na kama ikibainika kuwa nyumba hiyo ni ya kwake mzee huyo basi wale watu wabaya wangeweza kumgeukia na yeye. Mzee huyu akaamua kuchukua maamuzi ya kumuhamisha mateka huyo kabla mambo hayajaharibika. Mateka ambaye hakuwahi kumuona hapo kabla, na hakuwa na haja ya kumtambua kwani haikuwa mara ya kwanza kwa wazito hao kuwatia adabu watu wanaotaka kuwasumbua katika namna hiyo ya kuteka. Kwa sababu alikuwa ametingwa na shughuli za bunge na siku hiyo alitakiwa kuchangia hoja, alichukua simu yake ya mkononi. Aweze kuwasiliana na mtu ambaye anaweza kusimamia jambo hilo kwa niaba yake kwani baada ya muda kidogo alitakiwa kukwea pipa kuelekea Dodoma!! Akampigia mwanaye mpenzi. Isayah Akunaay. “Son! Goodmorning!!” akasalimia mzee Akunaay Zingo. “Morning Daddy!!” alijibu Isaya. “Naomba umtafute Joseph, nahitaji umpeleke katika nyumba yangu ya Chamanzi. Kuna jambo nahitaji kumuagiza achukue pale na hajawahi kufika. We si unapakumbuka babaa eeeh!!” mzee Akunaay alimwambia kwa sauti ya upole kabisa kijana wake!! Isaya akakubaliana na mzee wake. Simu ikakatwa. Kisha mzee Akunaay akampigia Joseph. Kijana wake mtiifu, akamueleza hali halisi juu ya hatari iliyokuwa mbele yao. Hivyo akatakiwa kumwamisha upesi iwezekanavyo huyo mateka ambaye hakumjua jina wala jinsia. Joseph akatii!! Akapewa maelekezo juu ya eneo ambalo ataupata ufunguo wa ziada wa nyumba ile. Laiti kama mzee Akunaay angetambua kuwa ni Betty ndiye mateka bora angekwenda mwenyewe!! Na laiti angetambua mambo yaliyojiri usiku uliopita maeneo ya Sinza, basi ni heri angeachana na kikao cha bunge na kutafuta suluhu mapema. Lakini hakuyajua haya.

    Akunaay anamuingiza Isaya katika jambo zito tena lenye utata!!



    RISASI iliyopita jirani kabisa na sikio lake iliacha mvumo wa aina yake ambao hadi wakati ule kunapambazuka alikuwa anausikia mvumo ule. Mvumo wa ajabu! Alipoukumbuka mvumo ule akajihisi kijasho chembamba kikimtoka, kwa mara ya kwanza Rambo akakiri kuwa harufu ya kifo ni ya aina yake na wala haipendezi hata kidogo. Kifo kisikie kwa jirani yako!! Usife wewe. Rambo alijisemea huku akilipapasa sikio lake kwa mkono wa kushoto. “Hivi nini kilimsibu yule Rasi hadi kuamua kutufanyia vile, amemuua Malle. Ameua na watu wengine halafu sasa wanatangaza kuwa alikuwa na wazimu. Tangu lini Rasi akawa na wazimu? Tangu lini…yaani Rasi hata akivuta bangi vipi hachanganyikiwi wala hapotezi kumbukumbu, leo hii wanasema ana wazimu duh! Mbona kizaazaa.” Alisema kwa sauti ya juu kama kwamba anaongea na mtu ambaye atampatia jibu baada ya hoja yake hiyo yenye maswali mengi kwa mkupuo mmoja. Lakini la! Hakuna aliyemjibu. Hakika Rambo alikuwa amenusurika kutoka katika domo la mamba!! Almanusura mwendawazimu Rasi amfyatue katika dakika zake saba za kutawanya vichwa vya wasiokuwa na hatia na wengine wenye hatia. Risasi ilipita pembeni kidogo ya sikio lake na kisha kufyatua kibanda kilichokuwa nyuma yake. Rambo akawahi kukimbia kutoka katika eneo hilo, sasa yupo katika nyumba ya kulala wageni yenye hadhi ya chini kabisa akiwa anajiuliza maswali kadhaa baada ya kupata taarifa juu ya utata wa Rasi mwendawazimu muuaji. Rambo hakutaka kumuamini mtu yeyote, kama Rasi kweli ni mwendawazimu kama wanavyosema wao basi wazimu wake ukitulia lazima tu atawataja wenzake, na yeye Rambo aikuwa mwenzake. Bingwa wa mapambano ya kutumia viungo vya mwili akalegea na kuwa mdogo kabisa kisha akajutia kujiingiza katika kazi hiyo haramu. Lakini majuto pekee yalikuwa hayatoshi. Rambo alitakiwa kufanya jambo upesi sana ili aweze kulikimbia jiji la Dar es salaam kabla hayajasambazwa matangazo kuwa anatafutwa kwa udi na uvumba!! Rambo akajipekua mifukoni mwake na kujikuta na pesa isiyozidi shilingi elfu kumi za kitanzania. Kiunoni aliichimbia vyema bastola yake iliyokuwa na risasi za kutosha. Kwa pesa aliyokuwa nayo asingeweza kulikimbia jiji. Hivyo kwa udi na uvumba alitakiwa kupata pesa ya upesi sana kabla siku hiyo haijamalizika. Angeweza kwenda benki kuchota pesa za kutosha lakini alihofia kitu kimoja tu, kuwa alitakiwa kurejea katika chumba alichopanga maeneo ya Mburahati ili aweze kuchukua kadi yake ya benki. Rambo hakuwa tayari kwa karata hii, ilikuwa mojawapo ya karata ngumu kabisa na hatari. Rambo akasimama akajitoa tongotongo katika uso wake kisha akaufungua mlango na kutoka nje. Shati lake lisilochomekewa liliificha bunduki yake. Alipofika nje alinunua kofia aina ya pama, akajifunika kichwa chake. Kisha akapanda daladala iliyokuwa imesheheni abiria. Akaning’inia mlangoni. Safari ya kuelekea Mbagala!! Rambo aliweka ulinzi wa hali ya juu ili hiyo banana banana isijekumuumbua na bunduki yake kiunoni. Safari ya Mbagala pekee haikuwa hitimisho. Alichukua gari nyingine dogo kwa safari ya kuelekea Chamanzi. Ni huku alipaona kuwa mahali sahihi kabisa kwa maamuzi aliyokuwa amechukua.

    Akiwa ameufunika uso wake katika namna ileile aliifikia nyumba ambayo Betty alikuwa amehifadhiwa. Bunduki yake haikuwa mbali na kama lingetokea lolote lile angeweza kuitumia. Rambo hakutaka kupoteza zaidi ya dakika kumi katika jingo lile. Alipanga kufika na kuzichukua pesa zilizotengwa kwa ajili ya chakula na usafiri wa hapa na pale wakati wote ambao Betty atakuwa amehifadhiwa. Kwa mahesabu ya haraka haraka alikisia kuwa ni shilingi kuanzia laki tatu hadi laki nne. Kwa kiasi hiki angeweza kuukimbia mji hadi pale hali itakapotulia. Wakati akikadiria kuwa atatumia dakika kumi, alisahau kabisa kuwa ulipangalo wewe na mwenzako naye anapanga lake. Aliufikia mlango akapapasa juu na kuukuta funguo kama walivyouacha awali. Akatazama nyuma, mbele, kushoto na kulia, kisha akaufungua mlango. Akaingia kwa hatua za harakaharaka akiwa ameuweka mkono wake karibu kabisa na mahali ilipokuwa bunduki yake ili aweze kuanzisha kasheshe lolote iwapo tu utasikika mchakato wowote unaohatarisha usalama wake.

    Wakati akiufungua mlango wa mwisho ndipo akakutana na hekaheka nyingine. Alitilia maanani sana kungalia nyuma yake akiamini kama ni hatari basi upande ambao inaweza kutokea ni sehemu moja tu. Getini!! Akasahau kabisa kuwa adui anaweza kuwa akimngojea ndani ya nyumba. Rambo alilisahau hilo. Nyuma yake hapakuwa na hatari yoyote ile. Akaufungua mlango ukawa wazi huku macho yake yakiwa bado yanatazama mlangoni asijue kuwa kuna kiumbe kilikuwa kikingojea kosa kama hilo litokee, na kilikuwa kikimfuatilia kuanzia lipokuwa anaingia ndani. Rambo hakupata nafasi ya kupiga kelele wala kuitumia bunduki yake. Upande wa ubao ukatua katika paji la uso wake. Hili la kwanza lilimvuruga kidogo akayumba yumba kisha akajiachia tena likatua pigo la pili lililokuwa zito kuliko la awali. Rambo akalainika taratibu kisha akafanya jambo la mwisho kujaribu kuichukua bastola yake kiunoni lakini jitihada zake ziliishia mikono ilipofika kiunoni, giza likatanda. Macho kabla hayajafumba yakakutana na sura iliyoiva kwa hasira kabisa. Sura ya Betty. Mateka ambaye Rambo hakumuhofia hata kidogo!!

    Mpango madhubuti kabisa, Betty akajisifu kwa ujasiri aliouonyesha, akatoka katika nyumba ile upesi bila kuchukua kitu chochote kile cha ziada. Akauacha mwili wa Rambo ukitapakaa pale mlangoni katika namna ya kufurahisha kutazama iwapo ingekuwa ni filamu. Aliifuata njia ya vumbi asijue mahali alipokuwa ni wapi, akazidi kutembea hadi alipopishana na gari lililokuwa likienda kasi, likamtimulia vumbi wakati linasimama. “Mambo mrembo!!” kijana mmoja akamsalimia huku akionekana dhahiri kuwa akijibiwa atakachohitaji zaidi ya hapo ni mapenzi. Betty akageuka na kumkata jicho kali yule kijana aliyekuwa anaendesha gari lile. Kisha bila kusema neno lolote akazidi kukaza mwendo, alikuwa amevaa kandambili miguu ikiwa imepauka na nywele zikiwa zimevurugika. Gari ikatimua mbio huku akisikia vicheko kutoka katika gari. Ni hapa ndipo akatanabai kuwa dereva hakuwa peke yake. Ndani kulikuwa na mtu mwingine. Hakujali zaidi akaendelea kukaza mwendo bila kutambua yu wapi. Hatimaye akaifikia barabara ya lami!! Akaendelea kuifuata. ‘SHULE YA MSINGI CHAMANZI’ hatimaye akakisoma kibao kilichomuhakikishai kuwa bado yu katika jiji la Dar es salaam. Swali likawa je atatoka vipi na kuingia mjini hasahasa kwa mwanadamu pekee ambaye angeweza kumuamini kwa siku hiyo. Joyce Keto pekee!! Betty akajipima na kugundua kuwa alikuwa na nguvu bado mwilini mwake. “Samahani, nikienda huku mbele ni wapi?” Hatimaye Betty akamuuliza kijana aliyekuwa anajishughulisha na kushona viatu kando kando ya barabara. “Ukienda huku ni Mbande, na ukienda mbele zaidi utafika Mvuti, na huku ni Mbagala.” Alijibiwa huku kijana akiendelea kushona kiatu chake. Nguvu zilirejea tena baada ya kusikia Mbagala. Aliamini kwa kufanikiwa kufika Mbagala asingeweza kushindwa kumalizia safari yake ya kumtafuta Joyce na hatimaye kumshirikisha kila kitu kilichomkuta hadi hapo alipo. “Magari hayoo yanakufikisha Mvuti.” Fundi viatu alimwonyesha Betty gari lililokuwa likipita. Na kwa mara ya kwanza akamtazama vyema usoni. Alikuwa akivujwa jasho na uso wake ulikuwa na mashaka huku akiwa amekata tamaa. Betty akamtazama yule fundi, macho yao yakagongana. Betty akatokwa na kauli. “Hata hiyo nauli ninayo basi!!” lakini kauli hii haikutoka katika mdomo aliisema tu katika moyo wake!! Kisha akamshukuru yule fundi. Akatoweka kwa mwendo wa kawaida huku akionekana kuwa amechoka waziwazi. Fundi alimsindikiza kwa macho huku akimsikitikia! Aliendelea kumtazama hadi pale lilipopita gari aina ya Toyota Hilux katika mwendo mkali. Macho yake yakahamia katika gari lile. Kisha yaliporejea kwa yule dada, alikuwa amesimama na yeye akistaajabu gari lile lilivyokuwa katika mwendo mkali. Ya wanadamu mengi!! Alisema kisha akapuuzia kila kilchokuwa kinaendelea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Betty alistaajabishwa na mwendo wa gari lile ambalo awali lilimpita katika barabara ya vumbi. Na sasa limempita katika barabara ya lami. Akapuuzia pia na kuendelea na safari yake ndefu kwa mwendo wa miguu. Alitumia zaidi ya saa zima barabarani kuifikia Mbagala. Miguu ilikuwa inawaka moto na alikuwa kiu kikubwa cha maji. Lakini ni nani wa kukupa maji mjini bila kukufahamu, Betty akapiga moyo konde akaanza tena safari ya kuiacha Mbagala aweze kuitafuta Ubungo ambapo angeweza kukutana na Joyce iwapo ingekuwa kama anavyodhani. Betty hakuwa na mtu mwingine wa kumuamini katika jiji hilo. Safari ya mateso ikaanza tena, alipofika maeneo ya chuo cha uhasibu miguu ilikataa kabisa, asingeweza kuimalizia safari ya Ubungo. Hapa Betty akalazimika kuomba msaada kwa wanafunzi wa kike waliokuwa kituoni. Msichana msiuchana tu!! Akawezeshwa zaidi ya nauli!! Gari lilipokuja akapanda na bahati nzuri akapata siti. Kidogo akapata pumziko, akasinzia huku akimsisitiza kondakta akumbuke kumshusha wakifika kituo ambacho alikuwa anashukia. “Oyo!! River side hiyo dada.” Alishtuliwa Betty. Akajikongoja upesi akashuka. Kisha akavuka barabara ka kuanza kuitafuta nyumba aliyokuwa akiishi Joyce. Kutokana na foleni kubwa maeneo ya Tazara na Buguruni, muda ulikuwa umeenda sana na ilikuwa saa kumi na moja jioni. Betty hakujipeleka kwa Joyce mchana kweupe, alihitaji kulifikia eneo lile kigiza kikiwa kimetawala ili hata kama kuna tatizo aweze kuliepuka kirahisi. Tofauti na mchana kweupe. Majira ya saa mbili usiku alikuwa maeneo ya nyumba aliyopanga Joyce. Nyumba ilikuwa imefungwa, Betty akamkuta jirani mmoja nje, akamuulizia juu ya rafiki yake yule.

    “Ana muda hajaonekna tangu pavamiwe hapa…” alijibu yule jirani mgeni. Moyo wa Betty ukapasuka kwa mshtuko, kusikia habari ya kuvamiwa kisha Joyce haonekani tena. Ametekwa!! Aliwaza Betty, kisha akatoweka eneo lile. Sasa alikuwa amebaki na senti chache sana!! Na usiku ule angelala wapi hilo lilikuwa swali gumu kabisa. Akaamua kucheza pata potea!! Akatoweka na kuingia eneo la ndani la chuo kikuu cha Dar es salaam. Kigiza kilikuwa kimetanda tayari, na kwa muonekano wake alionekana waziwazi kuwa alikuwa amefikwa na jambo zito. Ule urembo wake ulikuwa umetoweka kabisa kutokana na uso kumvimba kwa taharuki, nywele zilizotimliwatimliwa kichwani nazo zilizidi kumfanya kituko. Kisha kandambili miguuni zikaupoteza ule u-Betty wake. Akilini alimuwaza Isaya tu!! Hakuna mtu mwingine tena ambaye angeweza kumsaidia katika hili. Japo hakutaka kuamini mtu mwingine zaidi ya Joyce Keto, kwa hapa alikuwa hana ujanja. Akaamua kujikabidhi kwa Isaya, iwapo tu atafanikiwa kumpata kwa usiku huo pekee.

    *****

    MZEE AKUNAAY alikosa utulivu kabisa alipokuwa katika kikao cha bunge. Alisimama kutoa hoja lakini alikuwa kama anayetetereka, kwa wale waliokuwa wanamfahamu waliinamisha vichwa chini pale alipotoa hoja za kizembe na kuzisimamia kana kwamba ni hoja zenye tija. Baada ya kuketi alifikia na ‘memo’ zaidi ya kumi zikimuuliza iwapo sawa kichwani. Huku nyingine tatu zikimuulizia muheshimiwa Beka maana bunge halikuwa na taarifa yoyote ile kuhusu kutokuwepo kwake bungeni siku hiyo. Memo hizo ndizo ziliiamsha akili yake na kugundua kuwa kuna jambo lilikuwa halijakaa sawa, nalo ni mkasa wa Beka kutokuwa bungeni na mkasa wa jijini Dar es salaam. Mzee Akunaay alianza kuona uzito wa jambo hilo, kuwa hata kama Beka atakuwa amefanya vitendo viovu basi ni yeye atakuwa wa kwanza kuhojiwa juu ya jambo hilo. Kufikia hatua hii mzee Akunaay hakuweza kusikia tena hekaheka za bunge zilivyokuwa zinaendelea. Na hata spika alivyosimamisha bunge kitu cha kwanza alipotoka nje ni kuwasha simu yake na kisha kuanza kusaka jina la mwanaye aweze kumuuliza iwapo alikuwa amefanikiwa kumfikisha kijana wake katika nyumba ile. Simu ya Isaya haikuwa ikipatikana, akaamua kumpigia Jose moja kwa moja. Simu ya Jose nayo haikuwa ikipatikana. Mzee Akunaay akashikwa na hasira na kusonya kwa nguvu. Mara wakafika wabunge wengine wawili. “Mheshimiwa hivi hizi tetesi za Beka kutekwa ni sahihi maana dah kila redio sasa inatangaza jambo hilo…” “Mh! Beka katekwa? Acheni utani!!” aliuliza naye kama mtu asiyejua lolote. “Katekwa ndio na wameuwawa watu, muhudumu wa hoteli amedai kuwa kuna polisi walimkamata. Lakini jeshi limesisitiza kuwa halihusiki hata kidogo” alijibu mbunge mwingine. Mzee Akunaay akajiunga katika mshangao lakini machoni akiwa ana hofu!! Akiwa bado hajapata mawasiliano na kijana wake Jose wala mtoto wake Isaya. Mara ikafuata taarifa nyingine ya kushtua kutoka kwa mkewe. “Nini kimetokea mume wangu?” aliuliza mama Isaya katika simu. “Mi mwenyewe hata sielewi Beka amekuwaje..” alijibu kwa masikitiko. “Sio Beka mume wangu, ni Jose…..Jose amekufa kufa vipi sasa…” “Jose amekufa, Jose huyu kijana wangu…..” “Ndio, amekufa sijui niseme wamekufa eti alikuwa na mwenzake maeneo ya Chamanzi. Kijana wako huna habari naye…” alijibu katika namna ya kumsuta mumewe.

    Mzee Akunaay akakata simu haraka. Hakutaka kusema neno lolote kwani tayari alikuwa amehamanika. Kifo cha Jose akiwa na mwenzake kilimaanisha kuwa aliyekufa mwingine ni mtoto wake mpenzi, Isaya. Hakika mzee Akunaay alikuwa amefikwa na mazito!! Akaziona waziwazi dalili za jina lake kuchafuka tena kuchafuka katika namna ya kuipoteza imani yake na kujijengea chuki miongoni mwa wananchi wa jimbo lake na wasiokuwa wa jimbo lake. Kichwa kilimuuma kwelikweli, licha ya kufikiria juu ya heshima yake kutoweka. Akakumbuka pia alitakiwa kukabiliana na msiba wa mwanaye mpenzi!!



    Wakati mzee Akunaay akiumiza kichwa chake juu ya tatizo lililokuwa likimkabili, na huku akijiuliza yu wapi mzee mwenzake na mbunge mwenzake. Beka!! Mzee Beka alikuwa akisota kujibu maswali ya mwanadada Joyce!! Joyce alikuwa amegeuka mbogo baada ya Beka kuthibitisha kuwa alimteka Betty ili aweze kupata penzi lake kwa wepesi. Hasiri zilimchemka Joyce na kujikuta akimvamia Beka asiyekuwa na meno mawili kinywani na kumzaba makofi mawili ya nguvu!! Joyce alikuwa na hasira mara mbili, kwanza alikuwa amedhalilishwa utu wake kwa kujikuta akigawa penzi kwa Beka na pili alikuwa amechukizwa na kitendo cha Betty kutekwa pasi na makosa yoyote. Mbaya zaidi huyu huyu Beka alimchezea shere, akampigia simu na kumwomba kiasi kikubwa cha pesa na kama hiyo haitoshi akacheza na akili yake kwa kuingia chumbani kwake na kuondoka na ule ujumbe hatari ambao ungeonwa na askari ungezua mshikemshike. Mambo haya yalimkera sana Joyce!! Fonga ndiye aliyewatenganisha wawili hawa. Akamchukua Joyce na kutoka naye katika chumba kile, Joyce aliyekuwa na hasira huku akitetemeka midomo alianza kunywea baada ya Fonga kuanza kumshutumu!! “Hivi Joy kweli nikawa nakueleza mambo mengi vile kuwa niachie mambo mengine lakini ukenda kwa Beka. Kwa hiyo ukaniona mimi sina maana kabisa labda ama!! Maana hadi sasa hivi sijui nini kilikupeleka kwa Beka. Ujue ulichofanya ni kama umalaya, ulijiuza Joy. Umejiuza kwa bei nafuu sana ujue. Halafu sasa huyo Beka ana maukimwi…” alimaliza Fonga kisha akampa mgongo Joyce ambaye alikuwa ameinama kwa aibu. Neno lililomshtua Joyce ni lile la mwisho, Fonga kumfananisha na Malaya. “Fonga!!” aliita, na sauti yake ikasikika kama anataka kulia ama ametoka kulia. Fonga akajifanya amenuna na anayehitaji kubembelezwa, lakini hakujua Joy ni msichana wa aina gani. “Nazungumza na wewe Fonga, tena nisikilize kwa makini. Usidhani nilivyokuvulia nguo zangu usiku ule uliponipatia pesa basi mimi ni mwepesi kiasi hicho unanisikia!! Nafanya kitu ninachojua kwa nini nakifanya, usinichukulie rahisi kiasi hicho Fonga. Na ujue kabisa kuwa bila tatizo hili nisingeingia katika mahusiano na wewe Fonga..i could never!! I swear Fonga umepata bahati ya mtende kunifanya ulivyonifanya Fonga. Leo hii unanifananisha mimi na Malaya!!! Unajua nimetoka wapi na Betty, unamjua Betty vizuri Fonga…..” alisita kidogo akapenga kamasi, sasa ilikuwa zamu ya Fonga kugeuka mwenyewe bila kulazimishwa akawa anamtazama Joy.

    “Fonga, wewe na yeyote yule ni uchafu tu linapokujua jina la Betty. Hakuna maana yoyote ile, ni kweli umenifanyia mengi na umeniokoa kwa mengi lakini kamwe usithubutu kunisema eti mimi ni malaya kisa tu kunikuta nikiwa na Beka!!

    Kisa tu nilikuchojolea nguo zangu Fonga. Fonga hujawahi kunikosea heshima kama leo Fonga, yaani wewe wa kunifananisha mimi na malaya…. Ni vile tu bado nakuhitaji Fonga, ni vile tu bado nauhitaji msaada wako Fonga naapa kuwa ningekuchukia moja kwa moja na usingenisikia kamwe. Unaniita malaya mimi?? Ok labda tuseme sawa mimi ni malaya, niache na umalaya wangu nilioufanya ili nipate kumwokoa rafiki yangu kipenzi. Wewe inakuuma nini? Inakuhusu nini au labda niseme hivyo….” Joyce akazidiwa na kilio. Fonga alikuwa ameingiwa na neno moja baada ya jingine na yalikuwa maneno msumari kweli, akaijutia kauli yake ile. Lakini hakuwa na nafasi ya kufanya marekebisho tena ni neno limemtoka mdomoni tayari. Angefanyua nini kama si kubembeleza??

    “Kidoti, nisamehe mpenzi wangu. Sikukusudia kukuita malaya, ni hasira zinazozaa hasara na hasara ndo kama hii, Joyce kama nilivyokueleza siku ya kwanza. Nakupenda sana, sitaki kujieleza zaidi kwa sababu ni penzi hili limenisababisha nitokwe na maneno hayo. Nisamehe Kidoti wangu!! Nitakupigania hadi mwisho, na sitajali kwa lolote lile ambalo limetokea…… Ujue nimeumia sana, huyu Beka alimuua Monica, mpenzi wangu wa kwanza kumtamkia kuwa nina nia ya kumuoa. Beka akatumia pesa zake kumlaghai Monica, akanipokonya tonge mdomoni. Akaniweka jela zaidi ya mwaka mmoja Joy, niliteseka sana Joy nilihangaika, sikuwa na kosa lolote nikasota rumande miezi minne na baada ya hapo miezi mingine tisa nikasota jela!! Joyce nilipotoka nikakuta wapo katika penzi motomoto, akampa zawadi ya ushindi katika yale mashindano yaliyonikutanisha na wewe Joy. Niliumia sana lakini ningemfanya nini mtu na pesa zake? Monica akanidharau kupindukia!! Akaniita mimi jambazi ninayeishi. Sikuwahi kumjibu lakini moyo uliniambia kuwa bado nampenda Monica…..huenda hata yeye alinipenda…” Fonga akanyamaza kidoto akaonekana kuwa katika hisi nzito sana. Kisha akaendelea, “Ni kweli Monica alikuwa akinipenda bado, mara yangu ya mwisho kumuona alikuja nyumbani kwangu akinililia, alinililia kuwa ameukwaa Ukimwi! Aliyemuambukiza ni Beka. Na kisha amemkataa kata. Nikamshauri Monica aende ustawi wa jamii, hilo lilikuwa neno langu la mwisho kwake na alinielewa sana. Lakini baada ya hapo sikumuona tena!! Baadaye nadhani unajua kilichotokea Joy!!.”

    “Si walisema Monica alijiua Fonga!!” Joyce alidakia.

    “Monica asingeweza kujiua kamwe. Hawezi kujiua….” Mara Fonga akafyatuka na kukimbilia kilipo chumba ambacho Beka alikuwa amefungiwa. Kiatu chake cha ngozi kikiwa kimetangulizwa mbele alimrukia Beka na kuutuliza mguu ule katika kifua cha Beka. Beka akarushwa nyuma na kujibamiza katika ukuta huku akitokwa na yowe kuwa na kisha damu nzito ikamtoka kinywani. Joyce alifika na kukuta tukio hilo likiwa limetokea tayari na sasa Fonga alikuwa akijandaa kumrukia tena Beka. Joyce akajaribu kumzuia lakini akaishia kusukumwa pembeni, Fonga alikuwa amekasirika sana.

    “We Ngedere!! Nauliza swali moja tu na unipe majibu upesi. Nani alimuua Monica….” Aliuliza. Beka akarembua jicho lake na kumtazama Fonga katika hali ya kuomba huruma, Fonga akajihesabia sekunde tano. Ilikuwa bahati kuwa Beka naye alishtukia kuwa Fonga hakuwa yule Fonga wa miaka iliyopita. Akawahi kujisalimisha

    “Nisamehe Fonga!! Ni kijana wangu nd’o alimuua. Sio mimi naapa!!” “Halafu mkasingizia amejiua sivyo..” alisema Fonga kisha akamrukia Beka, mikono miwili ikatua katika shingo ya mzee yule ambaye alikuwa mahututi. Midomo ikiwa imemuanguka na udenda uliochanganyikana na damu ukimwagika kwa fujo bila jitihada zozote za kuzuiliwa.

    “Fonga utamuua Fonga!!! Fonga hajatwambia Betty yupo wapi Fonga achaaa!!!” Joyce alilia akisisitiza, lakini Fonga hakuwa na habari, hasira ilikuwa imemtawala. Akazidi kuikaba shingo ya Beka.

    Wacha wee!! Mtu akikaribia kufa huwa anatumbua macho na kisha kujikuta ana nguvu kubwa sana ya kupigania roho yake. Beka akaanza kurusha miguu huku na kule akitapatapa. Fonga akiwa ameegemeza goti lake katika kifua cha Beka na mikono ikifanya jitihada katika kulikaba shingo. Joyce akajiziba macho yake, ulimi wa Beka uliotoka nje ulimtisha haswaa!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mara likatokea tukio la maajabu. Mlango ukapigwa teke na kikaingia kiumbe mfano wa mzuka kisijulikane wapi kilipotokea. Kisha kikawa kama kinapaa, na mwisho kikatua katika vita ya Beka na Fonga, mara Fonga akapiga yowe kubwa huku akiruka na kutulia pembeni akiugulia maumivu. Kile kiumbe mfano wa mzuka kilikuwa kimelala kifudifudi mbele ya mwili wa Beka. Fonga na Joyce wakabaki wameduwaa, Joyce akizidi kujibanza ukutani na Fonga akiwa anaugulia maumivu katika kona nyingine.

    Mara kile kiumbe kikasimama wima!!! Kilikuwa ndani ya mavazi aina ya baibui nyeusi, ikiambatana na nikabu. Ni macho pekee yaliyoweza kuonekana. Ilikuwa patashika!!

    Mara mlango ukavamiwa tena kwa fujo, Mark akajitupa ndani akiwa ametanguliza bunduki yake mbele. Kile kiumbe kilichovaa baibui ni kama kilikuwa kinatambua nini kitatokea. Kikajikunja na kuunda alama kama namba saba kisha kikajitanua na kutupa teke la punda aliyekosa shukrani.

    Doh! Teke likatua katika kifua cha Mark, bunduki ikaruka mbali. Mkunjo ule wa namba saba ukamkumbusha Fonga jinsi alivyojikunja na kisha kujitupa mtaroni akimpisha kijana aliyekuwa nyuma yake asambaratishwe na risasi kutoka kwa wafuasi wa Beka katika sekunde ileile ambayo yeye aliinama chini, ni mkunjo ambao ulimjia tu kwa uoga wa kukikabili kifo na pia kutimiza maneno yaliyosemwa na Malle, kuwa akisikia neno ‘maliza’ akimbie!!

    Malle alikuwa ameisalimisha roho yake!! Lakini sasa alikuwa marehemu. Wakati haya yakipita katika kumbukumbu za Fonga jinsi alivyokikwepa kifo kile cha kikatili kilichoondokana kichwa cha kijana asiyehusika, mara alimuona Mark akijitutumua na kisha kuchomoa kisu kidogo katika mifuko ya suruali yake. Ni hapo kile kiumbe kilipojifunua upesi upesi nikabu yake. Kila mtu akastaajabu ndani ya chumba kile. Mark akadondosha kisu chake kwa fadhaa. Aliyegawa kipigo kie ndani ya dakika chache sana alikuwa ni HUSNA NGUMI JIWE!! Binti alikuwa akitabasamu!! Kisha akakikuna kidogo kichwa chake ambacho alikitumia kumtandika Fonga.

    “umekomaa mgongo aisee, kidogo nipoteze fahamu ati!” alisema tena Husna, kauli hii ikawafanya watabasmu.

    “Hivi umenipiga na rungu ama!” Kwa mara ya kwanza Fonga naye akahoji, bado alikuwa amejikunja akiyasikilizia maumivu. Kauli hii ikawafanya waangue vicheko, kasoro Joyce tu ambaye alinyanyuka na kujiweka jirani kabisa na Fonga, kisha akamnong’oneza, “Fonga sahau yote yaliyotokea, nipo kwa ajiri yako!!!”. Fonga hakuamini kile ambacho Joyce alisema, maumivu yakasafiri kwa muda kidogo. Akatabasamu!!

    ****

    BETTY alisota akitembea kwa miguu, akiambaa kutoka chuo cha Ardhi na kuchepuka upande wa kushoto akaingia katika himaya ya chuo kikuu cha Dar es salaam, alipishana na wanafunzi mbalimbali wa kike na kiume.

    Waliongea na kucheka kivyao, lakini yeye hakuwa na cha kumfanya walau atabasamu. Alikaza mwendo na hatimaye akazifikia hosteli ambazo Isaya alikuwa anaishi, akaanza kupanda hatua moja hadi nyingine. Hatimaye akakifikia chumba cha Isaya kama hatua kumi hivi za umbali. Akashuhudia kundi la watu, wnaume wakiwa katika hamaniko lililochanganyikana na hasira!!

    Wakamuona!!

    “Nd’o haya mambo tumekataa unamuona….unamuonaa..” akasema mwanaume mmoja. Kisha wenzake nao wakavutika kujua anamaanisha nini. Duh! Usiombe kauli ya umoja ni nguvu ifanye kazi dhidi yako!!

    Wanaume wale takribani kumi na tano wenye hasira wakaanza kumsogelea Betty. Miguu ikamlegea, hakujua ni kitu gani wanamaanisha, na hakupata nafasi ya kuuliza kabla hajavurumishiwa ngumi nzito begani na makofi mawili shavuni.

    “Mnatuletea umalaya wenu hapa…haya unajibu swali moja tu kisha unaweza kutoweka ama la!!” mwanaume aliyeonekana kuwa na sauti kupita wote alisema. Kisha akauliza, “unasoma kozi gani? Usiku huu unamtafuta nani? Na kitambulisho chako kipo wapi?” Betty akachanganywa na yale maswali, hakujua lolote kuhusu kozi, hakuwa na kitambulisho chochote lakini alijua kuwa alikuwa akimtafuta Isaya.

    Kigugumizi kikamkamata, na hapo akazidisha hasira katika kundi lile.

    “Mnatuletea….” Alisema mwanaume mmoja huku akizivuta nywee za Betty, “….mambo yenu ya kimalaya huku watu tunatafuta elimu.” Alimaliza kwa kumzaba kofi kali usoni. Maumivu yakatambaa kwa kasi, chozi likamtoka katika jicho moja. Betty akatambaza macho yake huku na kule, mara akamuona mwanaume pekee ambaye alikuwa ameikamata roho yake mkononi, hakika roho yake ilikuwa mikononi mwa kijana mwingine. Macho yalimuona lakini alishindwa kulikumbuka jina lake, kipigo kikawa kinaendelea pasi na sababu.

    “Yaani nawaambia roho yake mpaka itulie nanyi mtyakuwa mmekoma Malaya nyie.” Mwanaume yule mwenye sauti kuu alisema, Betty akashindwa kuelewa, roho ya nani itulie!!!

    Mungu wangu! Asiwe Isaya baba, iweke huruma yako kwangu mimi mkosefu eeh baba!! Betty alifanya sala fupi kimoyomoyo.



    Maajabu! Mara akalikumbuka jina la yule kijana pekee ambaye alikuwa akimtambua katika kundi lile lililokuwa linamshambulia.

    Betty akajitetea kwa mara ya mwisho, akawasukuma vijna wawili waliokuwa wanamkabili, kwa sababu hawakutegemea shambulizi lile. Wakayumba, Betty akatimua mbio huku akilitaja jina la mwanaume yule.

    “Ramaaaaaaaa!!!” kijana mmoja alimsindikiza na teke zito la mbavuni ambalo lilimyumbisha lakini hakusimama, hatimaye akamfikia huyo Rama. Akamkumbatia kwa nguvu!!

    “Rama mimi Betty wa Isaya!! Mimi Betty..” alimwambia huku akigeuka kutazama vijana wawili aliowasukuma wakimfuata kwa hasira, mikanda yao mikononi.

    “Rama wazuie Rama wataniua hao.” Alisihi Betty huku akimtikisa Rama. Wakati vijana wale wanafika na Rama naye kumbukumbu zake zilifanya kazi!! Mwanya!! Mwanya wa Betty ukamkumbusha haswaa!! Alikuwa huyu huyu aliyevikwa pete na Isaya. Rama akautega mgongo wake kumkinga Betty huku akiwazuia waliotaka kumshambulia.

    Ilikuwa patashika na laiti kama Rama asingekuwa na mwili uliojengeka kimazoezi basi ingekuwa habari nyingine, Rama akapambana na hatimaye akasikilizwa!!

    Ni wakati akiendelea kumtetea kwa jitihada zote na huku akionekana kuzidiwa, ndipo akatokea mkombozi wa roho hii. Isaya.

    Rama akapiga kelele Isaya akamsikia na kutazama nini kinatokea, akasogea kwa kunyata kama anayengojea kujua nini kinatokea. Hapo Betty akachomoka mbio, akimuacha Rama. Isaya akaangusha simu yake chini, akamdaka Betty juu kwa juu. Sasa wale vijana wakabaki kutazama tukio hili katika namna ya kufurahia na kustaajabu!! Kumbe mpigwaji alikuwa ni mchumba wa mtoto wa mbunge!!!

    Zama hizo watoto wa vigogo walikuwa wakiogopeka sana hivyo, mtu mmoja baada ya mwingine waliohusika katika kumpiga binti yule wakatoweka bila kuaga. Isaya hakuamini kile alichokuwa akikiona mbele yake, Betty alikuwa amerejea mikononi mwake!!

    Akiwa hana majeraha makubwa, Isaya alimkokota Betty huku akiwa amemshika begani. Moja kwa moja hadi katika gari yake! Wakatoweka kwa ajili ya kwenda hospitali.

    “Mbona wametaka kuniua jamani, kuna nini kimetokea? Nikadhani umekufa Joram wangu” Betty aliuliza hatimaye juu ya kilichotokea huku akimuita Isaya kwa jina lake alilomtambulisha mara ya kwanza kabisa. Isaya akiwa katika usukani alimwezea Betty kwa ufupi juu ya mwanafunzi aliyechomwa visu mara nane katika mwili wake hadi kupoteza uhai kisa kikiwa mapenzi. Kitendo cha mauaji haya katika hosteli aliyokuwa anaishi Isaya kilizua hasira kwa wanafuzi na kisha kulipiza kisasi kwa wanawake wowote ambao hawaeleweki katika mazingira yale hasaha mida ya usiku.

    “Kwa hiyo wangeniua..” aliuliza kizuzu Betty. Isaya hakujibu.

    “Yaani nilipata simu basi nikakupigia lakini sikukupata!” alisema Betty katika namna ya kulalamikia.

    “We acha tu ni stori ndefu, hata sasa hivi sipatikani vilevile!! Nitakusimulia….Bett nini kilitokea kwani?”

    “Nadhani sina jibu sahihi hadi sasa lakini nilitekwa Isaya!! Nilitekwa bila kujua kosa langu.” Alijibu Betty. Wakati huo walikuwa wameifikia hospitali ya Amana Buguruni. Mazungumzo yakakatishwa! Betty akajieleza kwa daktari, akapatiwa matibabu ya awali ambayo hayakuwa makubwa sana. Na usiku huo huo akaruhusiwa kuondoka. Isaya akamwendesha hadi Magomeni, wakafanikiwa kupata chumba katika hoteli ya kifahari.

    Ni heri usiku huu usingekuwepo!! Ni heri hata wawili hawa wasingekutana tena!!!

    ****

    MZEE AKUNAY alikuwa mwingi wa hasira wakati anashuka katika ndege ya kampuni inayomilikiwa na serikali. Kama ni matusi alikuwa ametukana yote, kisa kikiwa kuhairishiwa safari ghafla na muda kusogezwa mbele. Ilikuwa saa mbili usiku akalikanyaga jiji la Dar es saalam. Akiwa ameuvuta mdomo wake vile vile aliwasha simu yake na kujaribu kupiga namba ya Isaya lakini kama alivyokuwa Dodoma bado namba ya Isaya haikuwa ikipatikana. Wakati ananung’unika mara ikaingia simu kutoka kwa mkewe. Akapokea upesi amsikilize alikuwqa na taarifa gani mpya.

    “Uwiiii!! Baba Isaya, Isaya wangu mieeee…..Isaya wangu uuuwi.” Alianza kwa kulia mke wa mzee Akunaay.

    “Isaya amekuwaje eeh!! Mama Isaya.” Aliuliza mzee Akunaay huku akiwa anatetemeka, kilio cha mkewe kilimaanisha kuwa taarifa juu ya Isaya ni mbaya sana.

    “Mwanangu Isaya wamemuua uuuuwi.” Alilia kwa sauti ya juu mama Isaya. Mzee Akunaay japo jambo hilo aliliwaza hapo kabla lakini sasa liimwingia akilini vizuri. Akakiri kuwa yu katika wakati mgumu zaidi. “Kuna nini mume wangu niambie kuna nini, mara Jose na sasa mwanangu Isaya uuuuwi!!” Mzee Akunaay alimjua mkewe vizuri jinsi anavyokuwa akipagawa, akaamua kukata simu na hakutaka kupokea tena simu ya mkewe. Alitaka kuhakikisha ni kipi kimetokea, aliamini kuwa Isaya atakuwa ameuwawa akiwa katika harakati za kumpeleka Jose kumtoa mateka wa mzee Beka. Kama ni hivyo basi ili kumridhisha mkewe na kumtuliza kidogo mzee Akunaay alitakiwa kufanya juu chini kumtia mikononi muuaji wa mtoto wake. Na aili amtie mikononi litakiwa kwanza kuhakikisha anazungumza na Beka!! Amweleze nini chanzo cha yote haya. Swali likaja, atampata wapi Beka ambaye hakuna mtu walau mmoja ajuaye wapi alipo. Beka akiwa amechanganyikiwa akiwa ndani ya teksi ya kukodi, folenbi kubwa ikiwa imetanda. Akaanza kuwaka.

    “We jamaa mpuuzi sana sasa unajua kabisa Tazara mida hii huwa kuna foleni we unaileta tu gari huku, kwani njia ya Machimbo huijui ama!!” alimuwakia dereva wa taksi.

    “Mzee sasa Machimbo kufanyaje tena? Si tunaenda Ubungo ama sikukusikia?” dereva alijitetea. Majibu ya dereva ndo yakamfanya Akunaay aamini kuwa uchizi ulikuwa unamuandama. Aibu zikamshika akini hakuwa tayari kujishusha, akakaa kimya. Baada ya masaa mawili, majira ya saa nne usiku walikuwa ndani ya hosteli ya Mabibo. Mzee Akunaay akajutia kutokuwa karibu na mwanaye katika suala la elimu yake, sasa hakuwa akijua mwanaye kama alikuwa anaishi Mabibo ama anaishi ‘Main campus’.

    Huu nao ukawa mtihani. Wanafunzi walikuwa wengi mfanowe utitiri. Angeanzia wapi kumuulizia Isaya na kumpata kirahisi. Ndi walikuwa wakimfahamu baadhi ya wanafunzi lakini, wengi hawakujua alikuwa akiishi hosteli za chuo ama alikuwa akiishi nje katika nyumba za kupanga!! Laiti kama Mzee Akunaay angekuwa karibu na mwanaye na kumfahamu vyema huenda angeweza kuikoa roho hii….roho iliyohisiwa kufa kabla haijafa kweli! Lakini hakuwa karibu na mwanaye!!! ….. Akashusha pumzi na kisha kujikaza na kusema maneno kadhaa ya kuisindikiza roho ya marehemu peponi.

    Akunaay alikuwa katika wakati mgumu sana wa maisha yake!! Akaondoka zake na kutafuta hoteli akajipumzisha huku akingoja skendo magazetini kuhusu yeye na Mzee Beka na kisha ausome kwa uchungu msiba wa mwanaye katika magazeti hay ohayo.

    “Wajinga wanaweza hata kuandika kuwa nahusika kumuua mwanangu!!!! Yaani wamepewa uhuru sana hawa watu.” Alijisemea. Akajifunika shuka na kuanza kuutafuta usingizi. Akiwa ndani ya shuka akamkumbuka Inspekta X, huyu alikuwa mtu wao wa karibu yeye na Beka na aliwasaidia katika mambo mengi sana ya kiujanja ujanja. Mzee Akunaay akaona heri ajisalimishe kwake. Akampigia simu.

    INSPEKTA aliisikia simu ile ikiita, akiwa usingizini. Akapapasa na kuipokea bila kujua nani mpigaji. Akaisogeza sikioni.

    “Al Jazeera hapa.” Sauti nzito yenye mikwaruzo ya usingizi ilijitambilisha.

    “Aaah muheshimiwa!! Umenitupa sana siku hizi mzee wangu..” aijibu kwa uchangamfu huku akikaa kitako, usingizi ukiyakimbia macho yake na uzembe ukiukimbia mwili wake.

    “Majukumu tu! Sasa X umesikia juu ya jamaa chizi aliyefanya mauaji!!” aliuliza mzee Akunaay kwa jina la uficho Al jazeera.

    “Aaah hiyo ipo kituoni kwangu mbona. Si yule wa Sinza hotelini Rombo.” Alijibu X.

    “Yeah huyo huyo…sasa bwana X, wewe mwenyewe utajua kipi cha kufanya. Lakini hali ipo hivi. Huyo jamaa akirejewa na akili zake za kawaida. Mdogo wako naingia matatani.” Alijieleza kwa upole. X akaduwaa leo hii Jazeera anajiita mdogo wake!!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Una maana gani mkuu.” “Namaanisha hivi kuna maelezo yake yanaweza kunifunga mimi. Ni mbaya sana akishajieleza.” “Kwani alikuwa kijana wako.”

    “Hapana alikuwa kijana wa George Bush. Si unajua tena mimi na Bush letu moja.” Aliendelea kujibu kinyonge. X akastaajabu!! “Aisee!! Hapo sasa naanza kuelewa. Doh! Sasa tunafanyaje.” X aliuliza swali.

    “Bwana inspekta mimi nimekimbilia kwako, kama ningejua la kufanya si ningekuwa nimefanya kaka. Sema nilichowaza ni aidha huyo bwana awe chizi milele ama la asitoe maelezo kabisa, awe kimya!!” Alilamika Jazeera huku akitoa mawazo yake. “Basi kesho nitakupa majibu. Nadhani vizuri tukionana.” “Halafu kuna jingine ambalo ikiwezekana hata usiku huu lingefanyika ingekuwa bora.” “Jambo gani tena!!” “Kuhusu Geore Bush!!” “Amekuwaje?” “Umsake umuue…usiku huu huu!!” “Whaat!! Jazeera yaani nimuue Beka ama!!” alijichanganya akataja jina halisi lakini hata Jazeera hakushtuka. “Mbunge wa kawaida na waziri nani mkubwa.” “Waziri!!” “Basi ingeshangaza Bush kukutuma kuniua mimi na sio wewe kushangaa mimi kukuagiza kumuua Bush….” “Al-Jazeera naomba tukutne kesho tuzungumze…’ “Inspekta X acha upuuzi, nakwambiua mtafute leo ummalize, amemuua mtoto wangu unaniambia ulale mpaka kesho mambo ya kishenzi na kihanithi umeyaanza lini wewe!!!” aling’aka Mzee Akunaay. “Haya bosi! Naanzia wapi sasa mimi.” “Wewe na mimi nani alisomea mambo ya kipelelezi X, mbona unanikosea heshima leo. Si unajua mimi ni mwalimu tu!! Maswali gani hayo waniuliza sasa.” “Najua lakini walau dondoo muhesimiwa.” “Mchezo wa hapo Rombo green, Kimara kwa kijana wake mmoja, Magomeni kwa huyo anayeitwa chizi Rasi, na Chamanzi katika nyumba yangu. Huko ndipo Beka amemuulia kijan wangu!! Amka sasa tafadhali.” Alimaliza na kuamrisha. Inspekta X akajutia kuwa anakula pesa za bwelele kutoka kwa watu wazito, sasa zilikuwa zinamtokea puani. Akatakiwa kuiacha shuka na kuingia mtaani kuwatumikia majangili hao. Bunduki yake ndogo kiunoni, pingu yake ya siri, na kisu chenye sumu. Inspekta X akaingia kazini! Usiku wa saa tano!! **** HUSNA ngumi jiwe, akiwa bado amesimama katikati ya chumba kile aliyatawala maongezi. Akajieleza kwa kifupi sana jinsi alivyokabiliana na kijana wa Beka kabla hajajitokeza yule kijana aliyeitwa rasi mwenye uchizi na kuanza kufyatua risasi hovyo. “Nikakimbilia Sinza huko Madukani, nikachuku chumba nikalala zangu nd’o nakuja kuona taarifa ya habari asubuhi juu ya mauaji pale hotelini. Nikauchuna ndani ya chumba tena asubuhi ile nikaongeza muda wa kuendelea kukitumia chumba, hapo nikiwa nimejipanga kutoweka usiku. Hakika usiku nikaondoka kama naenda kununua maji. Hiyo ikawa kwaheri. Kufika hapa naingia chumbani hata kabla sijatulia nikmsikia huyu manzi anapiga kelele. Nikanyata na kuchungulia namkuta jamaa anataka kumuua mtu wetu….” Akasita akamgeukia Fonga. “Sasa wewe ungemuua tungefaidika nini unadhani. Kama ishu ingekuwa kumuua si tungemmaliza kulekule hotelini. Yaani watu tumekwepa risasi huko halafu we unataka kukitia mchanga kitumbua chetu!!” alimfokea Fonga, na hakuonekana kuwa na utani hata kidogo. Fonga akainamisha uso wake chini sasa akawa ametambua kwa nini dada yule alimtandika kichwa kikali namna ile, kichwa kilichokatisha azma yake ya kumuua Beka kwa mikono yake. Fonga akataka kujieleza, Husna akamkatisha. “Oya! Washkaji eeeh!! Huyu ----- atatufia hata kabla hatujapata tunalohitaji mwisho tutaingia gharama tena kutafuta mahali pa kumtupa.” Alisema Husna. Mark akatikisa kichwa kuunga mkono, Joyce naye vile vile. Husna akamsogelea Beka akamnyanyua kichwa chake kilichokuwa kimeinama kama kisichokuwa na uhai. “Mzee, ninakuheshimu sana nd’o maana nilikuwa nakufungulia bia zako huku ukinishika matako sawa!!” aianza hivi, kisha akaendelea, “nahitaji nawe uniheshimu katika hili, sharti langu ni moja tu, kila swali lijibiwe kwqa ufupi na kwa wakati! Na sidhani kama umesahau kuwa huna meno mawili kinywani, kwa hiyo kama unahitaji yaendelee kupukutika…aah sio kupukutika, safari hii nakuua. Ukiona kichwa change kinakuja sehemu yoyote katika mwili wako ‘shahadia’ upesi maana utakufa, hakika utakufa!!” Husna alimkoromea Beka huku akimkumbusha juu ya sala ya kushahadia inayotumika kwa dini yake pindi kifo kikikukaribia. Inaamika kuwa ukifanikiwa kuitaja sala hii, unafutiwa dhambi zako baada ya umauti. Akatulia kwa dakika zipatazo mbili, hakuna hata mtu mmoja aliyekohoa. Kisha akamnong’oneza kitu Mark. Mark akajibuluza akafika mbele ya Beka. “Betty yupo wapi.” Akauliza. “Chamanzi!!” alijibu upesi Beka. “Kwanini ulimteka??” “Hilo amelijibu tayari..” Fonga alidakia. “Nyumba ile inalindwa na nani?” “Hakuna mlinzi ni nyumba ya mbunge mwenzangu hakai mtu pale.” Alijieleza kwa kirefu huku uteute wenye damu ukiwa unachuruzika. “Hakai mtu, kwa hiyo umetudanganya kuwa mateka yupo huko. Beka nitakupasua!! Nitakuchanachana Beka.” Husna aliingilia mazungumzo na kumchimba mkwara Beka. “Nisamehe nimejichanganya tu…yupo kule Betty.” “Na tusipomkuta!!!” “Yupo ninao uhakika huo, kama hayupo nifanyeni chochote kile. Yupo kule Betty. Funguo za chumba chake najua mimi tu zilipo.” Alijitetea na kueleweka. Wakati akina Fonga wakidhani mambo hayo yatafanyika siku inayofuata, Husna hakuwa na mtazamo huo, yeye aliwabadili wenzake na mpango wote ukatakiwa kuwa usiku uleule. “Lakini jamani nioneeni huruma, mimi nitawapa pesa yoyote mtakayotaka, msiniharibie tu mtaani nitaupoteza ubunge wangu jamani, nitafungwa mimi eeeh.” “Beka hatuna nia ya kukuharibia cha msingi timiza yote tutkayohitaji, tunaanza na Betty kisha pesa.” Mark alimjibu. Husna alitabasamu kusikia pesa hatimaye imezungumzwa. Husna akisaidiana na Fonga walimsafisha Beka kiasi fulani, kisha wakampitisha kwa njia ya uwani. Akatupwa katika gari. Safari ya kuelekea Chamanzi. Ilikuwa ni saa tano na nusu usiku!!



    MUDA ule ambao inspekta X akiingia kazini usiku ule. Isaya na Betty walikuwa hawajalala bado. Walikuwa wakiulizana maswali ya hapa na pale. Betty akielezea tukio lake la kutekwa na watu asiofahamu nia yao. Isaya akatamani kuwasha simu yake na kumwelezea baba yake juu ya tukio la kupatikana kwa Betty lakini alihofia kuwa hakutimiza matakwa ya mzee wake ambaye alikuwa na kawaida ya kutopenda maneno mengi zaidi ya vitendo. “Yaani ningekuwa sijazingua hapa ningempigia mzee na angetupatia ulinzi wa hali ya juu si unamjua tena mzee.” “Umemzingua nini tena!!” “Ujue tuna nyumba yetu huko Mbagala mbele huko aliniagiza nimpeleke mtu fulani sasa mimi nikawa na vipindi darasani. Nikamuagiza jamaa yangu mmoja hivi ampeleke. Sasa hadi sasa hivi hapatikani kwenye simu wala nini, sijui kama Alifanikiwa kufika ama alipotea. Nd’o maana hapa nimezima simu ili mzee asije kuniumbua.” Alisema Isaya kisha akaiwasha simu yake!!! Akatafuta jina la Kindo. Akapiga lakini bado Kindo hakuwa akipatikana. “Duh bado hapatikani!! Bila majibu ya Kindo hapa siwezi kuongea lolote na mzee wangu namjua yule!!” alimaliza Isaya kisha akaizima tena ile simu yake. Sasa akamgeukia Betty.

    Ubaya wa chumba! Chumba kikiwa na jinsia mbili tofauti. Chumba kikiwa na giza huondoa kabisa dhana ya urafiki kati ya mwanamume na mwanamke, giza likikitawala chumba huzitawala pia akili za wahusika. Baada ya maongezi yoyote yale likikosekana jipya basi hufuta stori za mapenzi. Kama chumba kimekaliwa na wapenzi wa siku nyingi waliozoeana, baada ya maongezi hukumbatiana na kusinzia. Lakini kama ni wageni, baada ya maongezi ni vitendo!! Isaya alikuwa mgeni kwa Betty!! Betty naye alikuwa mgeni kwa Isaya, lakini kimtazamo walitofautiana sana, Isaya akitamani ngono kwa siku lakini baada ya hapo mapenzi kama kawaida na Betty akiendelea kuwa ubavu wake. Betty alijilazimisha ngono ilimradi tu atimize azma yake ya kukusanya pesa!! Hilo lilikuwa ni wazo kuu kabla hayajatokea hayo yote yaliyotokea. Lakini baada ya kutekwa kisha kurejea uraiani kwa kujikomboa mwenyewe, aliporejea mtaani anakuta taarifa mbaya juu ya rafiki yake kipenzi, jambo hili likambadilisha uelekeo kidogo wa kufikiri. Kama Joyce Kidoti hayupo mjini maana yake kwa namna yoyote ile anamuhitaji sana Isaya katika kila kitu kabla hajajipanga tena kimashambulizi ama kusalimu amri na kulikimbia jiji maana tayari alikuwa anazungukwa a watu wabaya. Alipojiaminisha kuwa Isaya anahitajika katika maisha yake, kwa roho safi kabisa akamfuta katika orodha ya watu walistahili kuuwawa kisa ni wanaume wenye tamaa. Maelezo ya Isaya juu ya harakati walizopitia na baba yake katika kumsaka baada ya kutekwa ziliikonga nafsi yake, kisha akakiri Isaya alikuwa tofauti na wanaume wengine!! Isaya hakustahili kufa!!

    Wakati akiwaza haya, Isaya alikuwa amejikita katika kuzipapasa sehemu sisimuzi katika mwili wa Betty, Betty akatambua kitu ambacho Isaya alikuwa anahitaji. “Isaya baba, una mpira!!” alimuuliza kwa sauti ya kubembeleza huku akimtazama macho yake yaliyolegea. Isaya alitia huruma, uso wake ukafedheheshwa na swali lile. Ni kweli hakuwa na kinga!! “Nenda ukachukue kinga mume wangu!! Nipo katika siku zangu za hatari sana. Leo siku ya kumi na moja Isaya.” Alidanganya Betty ilimradi amuokoe Isaya iwapo tu kinga itasaidia kweli kukinga virusi. “Lakini baby mimi si….aaah yaani kwani kuna nini?” alijiuauma Isaya. “Mimba Isaya, siku ya kumi na moja nimekwambia yaani hii ni mimba bila chenga zozote.” Alisisitiza Betty, wakati huo alikuwa yu uchi wa mnyama tayari. Isaya hakutaka kumkera Betty, akavaa suruali yake akatoka nje. Na baada ya dakika tano akarejea akiwa na kinga. Taa ikazimwa tena!! Betty akauacha upande uliobaki wa jitihada kwa muumba!! Kama kinga itazuia kweli sawa na isipozuia basi Isaya naye ataingia rasmi katika orodha!! Orodha ya wafu wanaoishi!! Kiza kilipotanda, ni kitanda pekee kikabakia kuwa shahidi wa yote yaliyotokea. Labda kingekuwa kinaweza kuongea kingesema ukweli siku ukweli ulipohitajika kuwekwa hadharani. Lakini kitanda hakiwezi kusema!! Haya yalitokea saa sita na dakika kadhaa usiku!!

    **** JOYCE angeweza kuachwa nyumbani kama si tabia yake ya kuwa king’ang’anizi. Fonga alishauri abaki waende wao kumaliza kipande cha shughuli iliyobakia lakini zile hisia za kwamba hakuna mtu mwenye uchungu na Betty kama alivyo yeye zikampelekea kuandamana na timu nzima, sasa ndani ya gari, Mark alikuwa anaendesha, Fonga upande wa kushoto, kamanda Husna ‘ngumi jiwe’ akiwa nyuma upande wa kushoto, katikati alikuwa Beka na kulia kwake akaketi Joyce. Safari ya kuelekea Chamanzi. Njia nzima barabara ilikuwa wazi, magari yalionekana kwa nadra sana hivyo hawakuhangaishwa na sehemu hata moja. Beka alikuwa kimya, akisota kila gari ilivyokuwa inapiga mabonde kutokana na mwendo mkali na usiokuwa wa kistaarabu wa Mark. Wakaifikia Mbagala, hapa sasa Beka akaanza kutoa maelekezo jinsi ya kuifikia nyumba ambayo Betty yu ndani yake. Walipobakiza mita kadhaa kuweza kuifikia nyumba, Fonga akahamia siti ya nyuma akamkamata Beka vizuri. Joyce mapigo ya moyo yalikuwa juu sana akiwa na matamanio ya kumuona tena Betty na kumthibitishia kuwa anampenda sana. Huenda mapigo ya moyo ya wakati huu yalikuwa ya kawaida kuliko yaliyotokea baada ya dakika kadhaa mbele. Geti la nyumba ile halikuwa limefungwa, lilikuwa limeegeshwa tu. Wakasukuma na kuingia ndani, Beka akaongoza njia mpaka ndani. Hapo hakuna mtu ambaye alikuwa na hofu yoyote juu ya uwezekano wakuwa wanafuatiliwa ama la!! Giza liliwapa amani. Hapakuwa na mtu ndani!! Beka akaelekeza funguo za chumba alichokuwa anafungiwa Betty. Hakika funguo zilikuwepo, chumba kikafunguliwa!! Joyce akawa na kiherehere akachungulia ndani mapema, taa ilipowashwa akitarajia kukutana na sura ya rafiki yake, akakutana na chumba kitupu!! Maajabu!! Si yeye tu aliyestaajabu, hata Beka alistaajabu. Ni kitu ambacho hakikutarajia hata kidogo. “Kwa hiyo tunatania Beka!!” Fonga alihoji kwa ghadhabu kubwa. “Naapa kwa majina ya mitume yote, binti alikuwa humu. Na fungu ndio hiyo jamani.” Alijitetea mheshimiwa Beka. Mark akageuka na kumnasa kofi usoni!! Beka akalia kama mtoto mdogo huku akiendelea kujitetea kwa juhusi zote. Beka alikuwa amefikwa!

    Wakapiga hatua kuingia ndani ya chumba. Ni hapa ndipo ikaja ponapona kidogo ya Beka!! Joyce akaiona kanga ya Betty ambayo aliondoka nayo nyumbani siku ya mwisho. Akaikimbilia na kuikwapua kisha akaanza kulia. Mark akamuonya kuwa ule ni usiku na hawajaenda kuomboleza pale. Fonga akamkata jicho kali Mark, Mark akaelewa maana yake!! Kuonekana kwa kanga ile kukarejesha imani kwa Beka kuwa alikuwa anasema ukweli kuhusu uwepo wa Betty pale ndani. Mark alipotazama darini aliona kifuniko cha silingibodi kilikuwa kimeng’olewa!! “Na hapo tundu la nini?” Beka akatazama kisha akaelezea hisia zake kuwa ni aidha Betty ametoroshwa ama ametoroka. Kwa fadhaa timu nzima ikatoka nje na kusimama uwani, wakimpa vitisho kadha wa kadha Beka.

    Kutokea kona nyingine mbili gizani viwiliwili vitatu tofauti vilikuwa katika mawindo. Kiwiliwili kimoja kikiwa na silaha mkononi wakati kiwiliwili cha pili kikiwa na silaha kiunoni, kiwiliwili cha tatu kikiwa tupu bila silaha.

    JAMBAZI ama muharifu yeyote hupenda kuishi kwa wasiwasi na uvumilivu!! Wasiwasi humfanya asimuamini mtu yeyote hata kama ni mwema, hii humfanya kuwakwepa maadui zake mapema. Uvumilivu huu humfanya kupata kile anachokitarajia!! Hata kama ni kwa kuchelewa kiasi gani. Rambo hakuwa muharifu mgeni bali mzoefu. Hivyo kauli mbiu hizi aliishi nazo. Baada ya aibu ya kupigwa na Betty hadi kupoteza fahamu alijiweka katika tahadhari kubwa, watu wa kwanza kuwasambaratisha walikuwa Jose na Kindo. Vijana alioamini kuwa ni askari wapelelezi. Hawa aliwafyatua risasi kisha kuwatia katika gari na kuwatupa jirani na nyumba ya mzee Akunaay aliyokuwa amehifadhiwa Betty ambaye alitoroka kishujaa. Baada ya tukio hilo la kuwawahi wawili wale Rambo alirejea tena mchezoni. Siku hiyohiyo baada ya miili ile kugundulika ndipo Rambo akagundua kuwa hisia zake kuwa walikuwa ni ma askari hazikuwa sahihi. Jose alikutwa na vitambulisho vya kazi. Ni hapa Rambo alipoamua kujipa uvumilivu!! Asingeweza kuukimbia mji na shilingi chache wakati anayo bunduki inayoweza kumpatia pesa nyingi hasahasa akifanikiwa kumpata Beka. Rambo akaamua kuwa na subira, akajiundia makazi yake katika kijiwe cha jirani tu na nyumba ya Akunaay. Huku alikuwa macho kutazama nani anaingia na nani anatoka. Usiku alikuwa anajichanganya na vijana wa sungusungu wakizunguka pamoja. Hawakujua kama mwenzao yupo katika windo lake. Hatimaye ukafika usiku wa mvumilivu hula mbivu!! Akaona gari maeneo ya nyumba ile. Wakashuka watu kadhaa, kwa mbali akamuona mzee wake wa kazi na bosi wake. Beka!! Akajipongeza kwa uvumilivu. Sasa alikuwa akijiandaa kichwani mwake juu ya aina gani ya shambulio anaweza kulifanya.

    Wakati yeye akiwaza haya, Inspekta X alikuwa akipuliza moshi wa sigara yake juu ishara ya furaha. Baada ya kukosa mambo ya msingi kutoka katika nyumba waliyokuwa wakiishi akina Rasi na kwingineko kwa Rambo, sasa aliukuta uhai katika nyumba ya mzee Akunaay. Akaaka kumpigi simu mzee yule lakini akaona hapakuwa na haja sana kwa sababu hata jambo la kumwambia lilikuwa halijapatikana. Akaitoa Bunduki yake akaikoki vyema kisha akaibusu baada ya kuwa ameiweka katika kiwambo cha kuzuia sauti. Roho ya mbunge Beka ilikuwa mikononi mwa Inspekta X na ilikuwa halali yake kutokana na maelezo ya mzee Akunaay. Akaombea amkute Beka hapo ili aweze kumaliza kazi upesi kisha arejee kitandani.

    upande wa tatu ulikuwa ukiduwaa, kiwiliwili hiki kilikuwa kimejinyoosha chini na kulingana na urefu wa majani yaliyokuwa eneo lile. Hakikufurukuta hata kidogo bali kugeuza macho kutazama upande alipokuwa Rambo na kisha kurejesha kwa Innspekta. Mapigo ya moyo yakamwenda mbio, afadhali asingeiona bunduki ya inspekta, lakini ilikuwa hivyo kuwa anakaribia kupambana na mtu mwenye silaha. Kitu kingine hakujua kama wawili wale walikuwa na jambo moja la kufanya pale ama kila mmoja katika mawindo yake. Hili nalo lilimuumiza kichwa zaidi. Alitamani kama ingekuwa ndani ya uwezo angewapa taarifa kule ndani juu ya hatari inayowazunguka, lakini asingeweza kuiweka roho yake rehani kwa kusimama na kukatiza katikati ya windo la wanaume wale asiowafahamu. Kama basi angekuwa nyuma ya mmoja wao basi angejirusha na kumtandika kichwa cha ‘umauti’, kichwa kimoja kinachoondoka na uhai ama kutia uchizi. Lakini hakuwa karibu nao kabisa. Kwa mara ya kwanza katika siku hizo mbili za mapambano Husna ngumi jiwe akajikuta yu matatani na uoga ukimtawala!! Ni kweli alijipongeza kwa kuyaheshimu mawazo yake na kuamua kushuka kutoka ndani ya gari kabla haijafika eneo la tukio kisha kumwachia Fonha jukumu la kumkamata Beka . Hakika mawazo yalikuwa sahihi, kwani alikuwa akitazamana na pande mbili ambazo hazikuwa zikihusiana nao hata kidogo. Lakini mawazo hayo hayo yasingeweza kuwaangamiza maadui zake, hapa sasa alihitaji silaha ama msaada wa aina yoyote ile. Alipogeuza macho kwa yule mtu mwingine ambaye hakuonekana kuwa na Bunduki. Huko napo akakutana na hofu nyingine, hata upande wa pili pia palikuwa na silaha. Bunduki mbili dhidi ya mikono mitupu!! Mkojo wenye kiherehere ambao huja wakati wa mshtuko ukamvamia Husna, akajaribu kuubana ikashindikana. Jemedari wa kike, mtaalamu wa vichwa vya kutia uchizi, mwanamama mwenye ngumi yenye uzito na ugumu wa jiwe akajikojolea!!! Si hatari hii?? Sio mshikemshike hapa?? Haya ya jasiri kujikojolea yalitokea Saa nane usiku!!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Licha ya kujikojolea lakini alikuwa makini na macho yake kutazama pande zake mbili hatarishi!! Jicho lake likatazama jinsi kijana wa upande mmoja jinsi alivyokuwa anatokomea. Walau Husna akaipata afueni, kupambana na mmoja halikuwa tatizo kubwa sana. Angeweza kumuhimili. Akavuta sekunde kadhaa akiwa ametulia palepale chini ili aweze kuiruhusu akili yake kufanya maamuzi ya nini kifuate tofauti na kuendelea kulala chini.

    MLIO wa bunduki ni kitu cha ajabu sana, kama hujawahi kuusikia kabla inaweza kupigwa mbali na wewe lakini ukahisi imelikosakosa sikio lako ama imekupiga mgongo!! Husna naye hakuwa mwenyeji sana katika milio ya bunduki! Usiku ule maeneo ya Rombo katika mkasa ule ilikuwa mara yake ya kwanza kukumbana na bunduki. Sasa alikuwa ameusikia mlio tena kwa mara nyingine. Akiwa pale chini alijkunja zaidi, sasa kijasho kikaanza kumtoka na uoga wa waziwazi ukichukua hatamu. Lakini mkojo haukutoka tena!! Mara ukasikika tena mlipuko mwingine wa risasi. Jicho lake likamuona yule kijana aliyekuwa amebakia katika upeo wa macho yake akihaha na kuduwazwa na hali ile iliyokuwa inaendelea Hapa ndipo akagundua kuwa watu wawili aliowaona katika kona mbili tofauti hawakuwa na ushirika wa aina yoyote ile. Hivyo kulikuwa na makundi ya aina tatu nje ya ile nyumba! Hilo lilikuwa wazi lakini tatizo likaja katika nia!! Hakujua kama kila kundi lilikuwa na nia moja! Yule bwana anayehaha alipotoweka, Husna naye akaanza kujivuta katika majani kwa kutumia tumbo ili aweze kutambua milipuko ile ilitokea wapi na kwa nini, mashaka yake yalikuwa juu ya yule bwana aliyetoweka wa kwanza!! Sasa atakuwa amemlipua nani? Eeh Mungu saidia asiwe Beka!! Aliomba Husna huku akiwaza pesa. Mara akamuona mwanaume mmoja akiwa anatimua mbio kuelekea upande alipokuwa yeye, alipomtazama vizuri alimtambua kuwa ni askari kutokana na mavazi yake!! Mikononi alikuwa mtupu!! Husna akatabasamu na kumhesabia hatua. Moja, mbili tatu!! Kisha akajirusha na kumchota ngwara ya nguvu. Akaangukia katika tuta. Akajiviringisha na sasa alikuwa amemkaba koo huku wote wakiwa wamelala. Kabla hajafanya lolote, mara akatokea yule kijana aliyetoweka awali, alikuwa ameshika bunduki huku akiangaza huku na huko. Bila shaka alikuwa akimfukuzia yule kijana ambaye sasa alikuwa amemkwida. Husna aliendelea kutulia tuli katika giza lile lililomficha!! Na yule kijana aliendelea kuhaha akiangaza huko na huku nakujiuliza yule mtu amepotelea wapi. Mara akaanza kupiga hatua kuelekea katika shamba lile huku akitumi mwanga hafifu kutoka katika simu ya mkononi. Kimbembe!! Husna akalegeza ile kabali aliyokuwa amemwekea afande!! Akatamani kusimama atimue mbio lakini alielewa kwa kufanya hivyo ni kujitoa sadaka na kufyatuliwa risasi na kupoteza uhai bila kufikia lengo. Kitu ambacho kilimuumiza sana. Akaendelea kutulia na yule bwana mwenye bunduki akiendelea kukaribia eneo walipokuwa, bunduki mkononi simu mkononi kwa ajili ya mwanga!! Husna alikuwa amefikwa na akakiri kuwa mbio za sakafuni zilikuwa zimeishia ukingoni!!!

    ILIVYOKUWA UPANDE MWINGINE!!

    Rambo aliendelea kutulia kwa dakika zaidi katika kona yake akilikagua eneo kabla hajaamua kuvamia. Alijinyoosha viungo vyake na kujiweka tayari kunyumbulika iwapo yatatokea mapambano yoyote yale ya ana kwa ana. Baada ya pale akahama upande ili aweze kuliona geti vizuri. Huku ndipo akaona kitu cha ziada. Difenda ya polisi!! Ilikuwa imepaki mita nyingi kidogo kutoka katika ile nyumba ya Beka. Mapigo ya moyo ya Rambo yakaenda kasi zaidi ya awali, akatambua kuwa alikuwa katika vita kubwa ya kumpata Beka akiwa hai. Lakini hakutakiwa kukata tamaa huenda hiyo ilikuwa nafasi pekee ya kumpata Beka akiwa hai. Akaiweka sawa bunduki yake isionekane na kisha akajitembeza kama msamaria mwema akipiga mluzi akapita jirani na ile gari ya polisi. Alipoipatiliza akatupa jicho ndani ya gari akaona vijana watatu. Nyuso zao zikiwa hazipo kikazi kabisa walionyesha uchovu, wawili walivaa sare za kazi huku mmoja akiwa amevaa kiraia. Hakwenda mbali zaidi akarejea akiwa amebadilika, bunduki yake ikiwa tayari kwa kutupa risasi. Haswaa alifanya hivyo lakini hakuwahi sana kufikiri kuwa hakuwa ameiweka katika kiwambo cha kuzuia sauti. Mlio mkubwa ukatoka wakati akisambaratisha kifua cha askari mmoja, hapakuwa na muda wa kujirekebisha akalazimika kuendelea kuitumia ikiwa hivyohivyo akarusha risasi ya pili ikalivunja bega la askari mwingine!! Akageuka huku na kule kumtafuta askari mwingine wa tatu lakini hakumuona, akasubiri kutokea ndani ya jingo labda kuna askari wengine watafanya majibizano ya risasi lakini pakawa kimya. Na ndipo akausikia mchakato katika majani, akawa mwepesi kuhisia, na alikuwa sahihi kabisa. Akaona vazi la kiaskari bila kofia likichikichia kichakani nyuma ya nyumba. Akatimua mbio kumkimbilia. Alipokata kona, hakuona mtu…akaamini yu katika kichaka kilekile…sasa ananyata akiwa na simu yenye mwanga hafifu na bunduki mkononi!!

    Husna alikuwa akimwona Rambo lakini yeye alikuwa hajawaona bado, labda kwa sababu tuta lile liliwameza. Lakini alikuwa akielekea huko huko!! Husna alikuwa anajiuliza askari wamefikaje katika tukio hili walilolifanya ghafla, Rambo naye alijipamaswali mengi iwapo Beka tayari yupo chini ya ulinzi ama vipi. Sio wao pekee waliokuwa wakijiuliza maswali, hata Inspekta X ama kwa jina la uhalisia Abrahiman Ndayanse alikuwa katika sintofahamu!!!

    *****

    SIMU iliendelea kuita sebuleni wakati yeye akiwa chumbani. Akapiga kite cha ghadhabu na kulaumu simu isiyokuwa na uhai na tabia zake za kufanya mwanadamu kuwa kama mtumwa. Inapiga makelele lazima uifuate. Alikuwa na haki ya kulalamika bwana huyu maana alikuwa katika faragha na mkewe ambaye alikuwa ametoka safari. Walikuwa na siku nyingi tangu wawe katika hali hiyo ya faragha!! “Mume wangu huwezi kujua anataka nini…kila apigaye simu ana sababu..” Mama Vicky alimweleza mumewe huku akivutavuta ndevu zake. “Ah Ah mama Vicy sababu nyingine za kipumbavu…angalia saa ngapi hapo..saa nne inaelekea saa tano.” Aling’aka mzee huyu kama vile aliyekuwa anapiga alimsikia. Simu ikakoma kuita, lakini hazikupita sekunnde nyingi ikaanza kuita tena, mkewe akachukua upande wa kanga akajistiri, kisha bila kumuaga mumewe ambaye alikuwa amechukia kukatishwa faragha yake. “Izime kabisa hiyo simu au iweke sailensi!!” alimalizia mzee yule maneno yale wakati huo mkewe alikuwa ametoweka tayari. Mara mlio wa simu ile uliokuw ukisikika kwa mbali ukaanza kuongezeka na kuzidi kumtia kero bab mwenye nyumba. Mlango ukafunguliwa na mkewe akaingia na simu ikiwa inaita!! “Shemeji yako jamani!!” alimwambia huku akimnyooshea mkono ili achukue simu. “Nani? Mama Saidi” alifanya kubashiri mke akatikisa kichwa kuashiria kuwa amepatia kabisa. “Yaani kama nilijua huyu mama Saidi yeye huwa hana cha hu ni usiku wala mchana upo kazini yaani yeye huwa ni kupiga tu hovyo simu, yaani huyu shemeji yangu huyu elimu yake haijamkomboa kabisa, haiwezekani mtu uwe na digrii unapiga piga simu usiku. Na hii sio mara ya kwanza yaani mamam Said huyu. Mama Said aaargh…..hapa najua tu tayari mume wake amemchanganya..yaani hawa ni watu wazima lakini hovyoo” Baba Vicy alizidi kuwaka. Hatimaye simu ikakatika. “Basi mume wangu, yaani simu ndo useme maneno yote haya. Hebu pokea umsikilize usiwe hiuvyo mtu wa kulaumu wakati hakuoni.” Mkewe alimsihi na hapo simu ikaanza kuita mara ya tatu. “Halow!” alikoroma katika simu iliyowekwa katika spika za nje. “Shem weeee!!! Shem mimi nitakufa kwa presha mimi!!!” “Ama!! Kelele, ni nini sasa!!” alikaripia. “Shem weee!! Ino..Ino ataniua mimi Inoo” sauti ya mwanamke katika simu iliendelea kulia. Mikono ya baba Vicky ilikuwa ikitetemeka kwa hasira kutokana na kilio cha yule mama kwenye simu, mwanaume huyu mchapakazi alikuwa hapendi mambo ya kuzungukazunguka. “Ino amefanya nini?” alijikaza akauliza bila kuonyesha jazba. “Uwiiii!! Ino ameondoka Ino…Ino kapigiwa simu na wanawake wake huko Inooo uwiiiii Ino ataniua mimi….Ino simpi nini Ino weeeee!” mama Saidi aliendelea kufanya ngonjera zake. Mtu na mkewe wakimsikiliza kisha bila kuambiana wakatazamana na kisha kutabasamu!! “Shem!!...” “Bee shem weee!” alijibu. “Nieleze bila kupiga kelele Ino ameenda wapi na amepigiwa simu na nani?” “Shem wee!! Ino amepigiwa simu na hawara zake huko. Ametoka sasa hivi!!” “Na unataka nifanye nini kwa muda huu labda.” “Umzuiee ataniua mimi!!” alijibu bila kufikiri yule mama. “Ama!! Yaani mimi nimelala namzuiaje sasa shem!” alihoji kwa ghadhabu ya wazi wazi. “Uwiiiiii nafwaaaa mieee nafwaaa uwiii mwana wa Mwakyusaa weeee….uwiiiii” kilio kikali kutoka kwa mama wa kinyakyusa kikashika hatamu katika simu. “Baba Vicky hebu ongea naye vizuri shemeji yako, unadhani mtu mzima anaweza kujiliza maksudi kwenye simu!! Eeh!!” Mke alimkaripia kistaarabu mumewe kwa kunong’ona!! Nano likamuingia mzee. Akairudia simu yake. “Shem! Basi nyamaza, nasimamia hilo jambo naagiza vijana wangu wafuatilie wajue ni wapi alipoenda sawa!!” “Haya shem weeee! Ino weee!” alikubali mama yule na kilio kikiishia ishia. Alipokata simu bwana huyu alibofya namba nyingine kisha sasa hakuzungumza kama baba Vicy tena!! “Kituo cha polisi Magomeni usalama! Fuatilia nyendo za Inspekta Inocent Abrahman Ndayanse, ametoka kwake si zaidi ya robo saa iliyopita. Nahitaji kupewa taarifa kwa kila hatua anayopitia over!!” aliamrisha Mkaribu mkuu wa polisi ama kwa kimombo ‘Assistant Super Retendant’ bwana Seba ama akiwa nyumbani na mkewe baba Vicy!! Waliopokea taarifa hii walikuwa vyeo vya chini na hata huyo Inspekta alikuwa na cheo cha chini yake!! Wakatii amri haraka iwezekanavyo. Wakafanikiwa kumnasa katika mtego akiwa anaiacha nyumba yake akichukua taksi. Bahati ilikuwa upande wao, walimtambua yule dereva wa taksi. Wakamtumia kutoa uelekeo wa wapi wanaelekea. Hatimaye wakafika Chamanzi katika uwanja wasiojua nini kinaendelea!! Wakiwa na masalia ya uchovu wanashtuliwa na milio ya bunduki!! Askari mmoja anapoteza uhai palepale, mwingine anavunjwa bega. Mmoja bado alikuwa katika mapambano!! Lakini katika kabali ya uhakika kutoka kwa mwanadada Husna ngumi jiwe!! N a zaidi ya hapo kuna bunduki inawasogelea iwamalize!! WAKATI vijana hawa ambao kama isingekuwa amri ya mkuu huyo wasingetoka kituoni, sasa wakiwa katika utata. Mama Saidi alikuwa akijaribu kulivuta shuka na kujifunika vizuri akingojea majibu kutoka kwa ‘Assistant Super Retendant’ Seba. Amani kidogo iliutawala moyo wake, wivu ukatulia kwa muda akaamini kuwa kila kitu kitaenda sawa!! Hakujua mumewe alikuwa nje kwa jina la Inspekta X na alikuwa akifuatilia mambo ambayo ni ‘X’ tupu, magumu kuelezeka. Laiti kama angeyajua haya labda lingekuwa jambo la kwanza kumueleza Seba akalisimamia. Lakini mama huyu wa kinyakyusa aliwaza wivu tu wa kimapenzi si jingine!! Asubuhi taarifa ilikuwa nyingine kabisa!! Kutoka kwa mtu yuleyule! Ikaamsha taharuki nyingine.

    ****

    Uvumilivu na uanaume halisi ulioonyeshwa na Isaya kwa kukubali kutumia kinga usiku ule akiwa na Betty, ulimgusa haswa binti huyu. Alijiuliza maswali mengi sana juu ya tabia za wanaume kupenda kuwa ving’ang’anizi bila kuhofia afya zao ama kumuonea huruma mwanamke ambaye tendo mnafanya wote lakini mimba anaibeba mwenyewe. Mwanaume hupenda kujali masilahi yake, yeye apate tu starehe na hajali kuhusu usalama wa mwanamke. Lakini kwa Isaya ilikuwa tofauti. Isaya alionyesha ukomavu na uelewa!! Laiti kama ningekuwa mzima! Huyu alikuwa mwanaume sahihi wa kunioa na kuzaa nami. Alijisemea Betty wakati akimfikiria Isaya. Katika kuwaza haya akaamua jambo moja la mwisho katika jiji ambalo tayari lilikuwa limemgeukia na kujiundia maadui!! Betty akawa amefikia uamuzi wa kurejea kijijini Ukala. Aliamini kuwa akiwa na shilingi milioni tatu hadi tano atayaendesha maisha yake bila wasiwasi wowote na akajipa moyo zaidi kuwa anaweza kufanya harakati za ukombozi hukohuko Ukala. Jambo ambalo aliamua kulifanya ni kuunda uongo ambao atamweleza Isaya ilimradi waweze kuachana kabla Ukimwi wake haujaamka tena. Alitamani sana kumwambia ukweli juu ya afya yake lakini akahofia mapokeo yanaweza kuwa mabaya na akakosa anachokihitaji. Betty alihitaji Isaya ampatie kiasi kikubwa cha fedha kabla hajaamua kutoweka jijini. Akapanga kucheza na akili ya Isaya itakapofika asubuhi. Akamtazama Isaya alivyosinzia, akatikisa kichwa cha masikitiko. Kisha na yeye akasinzia hivyohivyo. Ilipofika asubuhi habari ilikuwa nyingine kabisa!! Ukazuka utata!! Huku kila nafsi ikipagawa!!



    RAMBO aliendelea kunyata huku akiwa makini kabisa na mazingira yale, kila mtikisiko hata wa jani aliutilia shaka na mapema kujikuta amegeuka huku bunduki yake ikiwa tayari kukohoa na kisha kuondoka na uhai wa mtu iwapo ingemlazimu kufanya hivyo!! Alizidi kupiga hatua kuelekea ule upande ambapo akina Husna walikuwa pamoja na yule askari aliyemkimbia. Husna alifumba macho huku akisubiri lolote kutokea maana ni kama vile hakuwa na ujanja wa ziada, kwa mtindo ambao Rambo alikuwa akiutumia kunyata kwa namna yoyote ile angesimama kumkabili angeishia kumeza risasi na kuachia uhai. Husna akaendelea kuwa mtulivu, sasa hakuwaza tena kuhusu yule askari na badala yake alifikiria tu kuhusu maisha yake ambayo yalikuwa hatarini. Kufumba macho hakuona tena kama ni suluhu, akafumbua ili aone huenda yule adui alikuwa amebadili uelekeo. Ni hapo alipokutana na ndoto ya ajabu ambayo ilimpa uhai tena. Kutoka katika ukuta uliokuwa unaizunguka nyumba ile alikutana na kiumbe kikiwa kinaelea angani huku kikiwa kimetanguliza mguu wake mbele. Kiumbe kile na mguu wake mbele kikatua katika mkono wa yule adui!! Bunduki ikamtoka mkononi huku na yeye akiyumbishwa. Mark kazini!! Husna akatabasamu baada ya kumuona bosi wake akiwa amefanya jambo la muhimu huenda kupita yote tangu siku hiyo ya ajabu ianze asubuhi.

    Rambo aliyumba na kuanguka chini, Mark akadhani kuwa adui yake ni dhaifu kiasi kile. Akatembea kimajivuno kuifuata bunduki ile, hakujua yule bwana pale chini ni bingwa wa mapigano ya ana kwa ana. Ni hapa alipochotwa ngwara kali, ikamtupa chini. Akili ya Mark ikashtuka na kukiona kifo kikijongea. Hakumpa adui nafasi ya kuifikia bunduki ile na yeye akajihami akiwa amelala kifudifudi aligeuka ghafla, giza likamsaidia kumhadaa adui yake, akarusha kile ambacho alikuwa amekikamata mkononi kama silaha ya mwisho. Akarusha!! Huku akiamini kuwa akimkosa tu huo nd’o mwisho wake kwani hakuwa na mbinu nyingine ya kumkabili na kumzuia asiiwahi bunduki ile. Wacha wee!! Likatua katika uso wa Rambo. Lilikuwa mfano wa jiwe lakini ni dongo gumu kutoka katika kipande cha ardhi. Lilipotua katika uso wa Rambo likapasuka na kuingia machoni. Acha Rambo apagawe!! Mark akapata fursa ya kuonyesha umahiri wake wa kupigana dhidi ya kipofu wa muda!! Akamvamia adui yake na kumpiga teke la mbavuni, akayumba kushoto, wakati adui asiyeona akidhani atapigwa tena katika upande mwingine wa mbavu, Mark alitupa ngumi nzito katika taya za Rambo, ilikuwa ngumi kali haswa! Rambo akiwa mwanaume jasiri akajikuta akitokwa na kilio kikubwa! Aliumizwa hakika. Rambo kajaribu kutapatapa huku na kule iwapo ataweza kumpata Mark kwa hisia lakini ilikuwa kazi bure, Mark alifanya mtindo wa kudonoa. Anapiga kisha anasogea mbali, anapiga kushoto anajibanza kulia!! Hatimaye akaiokota bunduki ile. “Wewe ni nani? Swali moja jibu moja!!” aliamrisha Mark! “Steven!” alijibu kwa jeuri Rambo huku akianza kidogo kupata uwezo wa kuona kidogo sana. “Ulikuwa unatafuta nini huku!” “Nakutafuta wewe!!” aliendeleza jeuri huku akiwa na nia na majibu yake. “Umenijulia wapi mimi na nani alikwambia nipo huku.” Alikoroma Mark. “Mama yako mzazi.” Rambo aligandamiza zaidi huku akiamini kuwa Mark akiendekeza hasira tu basi atajutia. Na aliamini kuwa hawezi kumuua kizembe hadi atambue ni nini alifuata kule. Kweli jibu lile likamchefua Mark. Akataka kumfyatua yule kipofu wa muda lakini akaona hicho kitakuwa kifo chepesi sana. Akamvamia ili ampige na kitako cha bunduki. Ni kosa hilo ambalo hungojewa na maadui wengi katika mapambano, mpinzani ukasirike ili ufanye ujinga!! Mark akapiga hatua mbili pekee, hatua za mwisho za kutamba. Rambo akatumia uwezo wake mdogo wa kuona, akafyatuka teke lenye nguvu zote, likatua katika shingo ya Mark. Akapepesuka huku akitokwa na yowe la uchungu na hofu. Kisha miguu miwili ikapaa hewani na kutua katika kifua chake, akatua chini kama mzigo. Husna aliyekuwa anaufurahia mchezo ule akiwa na mateka wake ambaye kwa sasa alisahau kumtilia maanani, alishtushwa na shambulizi lile. Hakika lilikuwa shambulizi kali mno. Akataka kupiga kelele na kwenda kumsaidia Mark lakini na yeye akkutana na jambo linalofedhehesha, wakati akimlaumu Mark kwa kujisahau na yeye alisahau kuwa alikuwa amejisahau muda mrefu. “Upo chini ya ulinzi!!” alikutana na kauli ile, alipojitazama mkono wake akakutana na pingu!! Balaa jingine, yaani alinogewa kutazama mpambano hadi akafungwa pingu katika mkono wake bila kujua!! Maajabu. Akataka kumrukia kichwa cha ghadhabu yule askari pale chini lakini wakajikuta wote kwa pamoja wapo kimya tena na wakiingiwa hofu!! “Wote mtulie kama mlivyo!! Atakayetikisika tu napasua kichwa chake…haya sogea hapo katikati kuku nyie” sauti ya amri ikasikika. Mtutu mwingine wa bunduki, na kundi jingine la watu. Husna akawatambua wote, Fonga, Joyce na mzee Beka. Walikuwa wamepatikana siku hiyo!!! Mark akasimama mikono juu, Rambo naye mikono juu!! Inspekta X akatawala uwanja huu wa mapambano akiwa na mateka watano. Tofauti na wengine waliokuwa wanahitaji mali, inspekta X yeye alikuwa anatimiza matakwa ya bwana Akunaay. Matakwa ya kumuua Beka!! Lakini kwa sababu Beka alikuwa na watu wengine ambao wanaweza kuleta usumbufu baadaye akaamua kuwaunganisha wote ili awatokomeze na kuondoa ushahidi. Inspekta hakuwa na utani na hakupenda usiku ule aendelee kupoteza muda na maswali na majibu kwa sababu hakuyahitaji. Beka hakuwa akiamini hata kidogo kama yule aliyewateka ni kijana ambaye huwa wanamtumia katika kuzipata taarifa za siri ambazo zina manufaa kwao. Sasa alikuwa amewateka!! Mwanzoni alidhani kuwa huyu bwana alikuja kumwokoa lakini alipowaamuru wote kutembea mikono ikiwa juu ndipo imani ikaanza kutoweka. Rambo naye alishangazwa na uwepo wa inspekta yule eneo lile, tena akiwa upande wa tatu yaani hajulikani ni wa upande wa adui ama mwenzao. “Beka usinilaumu mimi muheshimiwa lawama zako huko uendako zitupe kwa Akunaay. Mimi natimiza wajibu tu kama ambavyo nakutimizia wewe unaponihitaji!!” alizungumza Inspekta X huku akiwa makini na kila mmoja. Beka akaduwaa kusikia kuwa rafiki yake wa karibu kabisa nd’o ameagiza hayo!! Si Beka pekee aliyekuwa akishangaa bali hata Joyce naye alikuwa anashangaa kusikia jina la Akunaay. Hili lilikuwa jina la baba yake Isaya! Mwanaume ambaye alikuwa akimpenda. Ina maana baba yake Isaya anafanya mamb haya pia!! Sasa anahusika vipi katika mpango huu!! Joyce alijiuliza katika nafsi yake huku akiwa anatetemeka na mikono ikiwa juu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mark alikuwa mkimya, lile pigo lililoiathiri shingo yake lilikuwa limemvuruga haswa, hakuwa anaweza kugeuka vizuri. Lakini alijilazimisha na hatimaye akaiona bunduki ya yule mpinzani wake katika mapambano. Maamuzi ya ghafla yakapenya katika kichwa chake, akadhani mtekaji ambaye ni kama alikuwa anaongea na Beka pekee atakuwa amejisahau kabisa. Akajirusha ili aweze kuichukua bunduki ile. Lakini hata kabla hajaifikia akarushwa juu zaidi. Alipotua chini alikuwa tayari kwa kuzikwa iwapo ndugu zake watautambua mwili wake katika gwaride la utambuzi!!

    “Nimeanza na huyo. Na ninapenda kuwakumbusha kuwa sijawahi kurusha risasi yangu kimakosa ninapoamua kuua!!” alitisha Inspekta. Mateka wote wakawa katika kitete, mwenzao mmoja alikuwa amekufa tayari. Joyce akiwa na begi dogo mgongoni, akajutia kujiingiza katika safari hii ambayo alizuiwa kabisa asijihusishe nayo. Sasa alikuwa anakufa bila kujua hatma ya Betty, jambo hili lilimuumiza sana. Mtekaji alizidi kuzunguka kwa madaha akiwazunguka mateka wake. “Rambo!! Si makosa yangu bwana!! Nami nimeagizwa ili maisha yaendelee bwana” alisema Inspekta huku akimtzama Rambo, sasa alikuwa na bunduki mbili. Moja mkononi na nyingine kiunoni!!

    Sasa alikuwa upande ambao Husna na yule askari walikuwa!! Husna kwa kushuhudia kifo cha Mark alikuwa amejitoa muhanga kimawazo kuwa na lolote litakalolazimika kuwa liwe!! Iwapo tu atapata nafasi, akafikiria kuwa ni jambo la aibu sana kukosa yote. Amkose Beka na pesa zake, kisha awapoteze na jamaa zake wote tena akishuhudia kwa macho wanavyouwawa. Alimtazama askari yule kwa jicho la kuibia na kumuona akitokwa jasho jingi huku jicho likiwa limemtoka haswa. Ni kama kuna kitu alikuwa anakiona mbele yake na hakutaka kuamini. Husna akajipima nguvu zake na kugundua kuwa alikuwa imara na angeweza kufanya kitu ambacho alikikusudia! Mkono mmoja ukiwa umefungwa pingu na mwingine ukiwa huru hilo halikuwa tatizo kwake. Tatizo alikuwa ni yule askari mwenye umbo dogo tu! Ghafla akagundua kuwa askari yule si tatizo na badala yake anaweza kuwa faida kubwa kwake. Kadri Inspekta alivyoendelea kutamba na yeye Husna akili za kumtumia askari yule zikaongezeka. Kwa sababu kijana alikuwa ametaharuki hakutambua nia ya Husna alipojitikisa. Lakini alishtukia alipokabwa shingo yake kwa nguvu zote akajaribu kutikisika haikuwezekana. Inspekta alipowapa mgongo kabisa, Husna akatumia nguvu zake zote akamnyanyua askari yule na kumrusha hewani katika upande mwingine. Askari yule akapiga kelele kubwa ya hofu, lakini kama alivyosema Inspekta kuwa huwa hana mazoea ya kupiga risasi kisha akamkosa mtu!! Hata huyu naye alifika chini risasi yenye nguvu ikichimba shingo lake. Mauti yakamkuta akiwa chini!! Husna akasubiri kama kitatokea kilichopita katika akili yake. Ama hakika binti huyu alibarikiwa machale!! Inspekta alianza kurudi kinyume nyume Bunduki yake ikiwaelekea mateka wake mgongo wake ukiwa umeelekea alipo Husna!! Akazidi kupiga hatua ili aufikie mwili wa yule Askari kijana aweze kujua nini kimejiri. Hili lilikuwa kosa kubwa, kujisogeza karibu na Husna!!! Husna hakungoja nafasi ya pili maana isingetokea tena. Sasa alikuwa katika tuta ambapo ilikuwa ngumu kabisa kumuona, akapapasa huku na kule akakutana na jiwe, akalirusha upande wake wa kulia. Inspekta akahisi kitu, akaanza kutembea huku akizidi kutoa maonyo na akijitamba kuwa bunduki yake inasafiri umbali wa mita mia nane hivyo asithubutu mtu kutikisika. Wakati huo mateka walikuwa wamempa mgongo. Akapiga hatua kufuata kishindo kilipotokea, akalifikia tuta ambalo HUsna alikuwa amejilaza. Akalivuka. Mgongo wake ukawa jirani na Husna!! Husna anataka kitu gani zaidi ya hicho?? Huenda kilikuwa kichwa kikali na cha hasira kupita vyote alivyowahi kupiga. Na huenda kichwa cha mwisho kabisa kukipiga katika maisha yake. Husna alikivuta kutoka mbali na kukiachia katikati ya mgongo wa inspekta X. “Ka!!” mlio huo ukasikika…. Bila kupiga kelele zozote zaidi ya kukohoa kidogo Inspekta na bunduki zake mbili alilainika na kutua chini kama mzigo. Husna alikuwa amempiga katika uti wa mgongo!! Sehemu hatari kabisa katika mwili wa mwanadamu. “Joyceeeee!!!! Towekaaa!!” alipiga kelele Husna. Joyce akageuka bila kujua nani anamuita, Fonga akaitambua sauti. Ilikuwa sauti ya jemedari Husna ngumi jiwe. Na mara akaingia katika uwanja wakamuona hadharani. “Timkieni huku kuna njia, hakuna kugeuza kishanuka hapa.” Aliamrisha Husna. Fonga akamkamata Joyce mkono na kuanza kutimua mbio!! “Sasa vipi kuhusu Betty jamani!!” alilalamika Joyce. Husna akamtukania tusi zito kwenda kwa mama yake aliyemzaa. Joyce akataka kumkabili Husna lakini Fonga akawahi kumvuta mkono wakakimbia. Husna akiwa amemsahau yule mwanaume aliyemwagiwa michanga machoni, alimvagaa Beka. Sasa alikuwa anataka pesa!!! Kumbe lao moja Rambo naye anataka pesa!! Wakati akina Joyce wakitegemea kuwa Husna anakuja nyuma yao. Huku nyuma ukazuka upinzani ambao ulikuwa mkali kupita yote katika riwaya hii. Rambo alikuwa anaweza kuona sasa, Husna alikuwa na hasira na mafanikio ya ghafla ghafla. Wote wawili wakiamini kuwa kumpata Beka nd’o mafanikio yao. Nani ampate na nani asimpate! Rambo akaweka kauzibe kwa mwanamke huyu aliyewaokoa kutoka katika kifo!! Rambo akamzuia asimchukue Beka. Husna akalazimisha, ni katika kipindi hiki, Beka akawekwa kando kisha uwanja ukatawaliwa na wababe wawili. Husna ngumi jiwe na Rambo mtaalamu wa mpigano ya ana kwa ana. Rambo hajui lolote kuhusu Husna lakini Husna alikuwa amemuona Rambo wakati anapigana. Rambo akampuuzia Husna akamfuata ili amnase vibao viwili na kumwacha akilia hapo. Lakini alichokutana nacho ni fedhea kubwa. Husna ambaye mkono wake ulikuwa bado na pingu aliurusha mkono ule. Pingu ikatua katika taya ya Rambo, akalia kwa uchungu lakini akaendelea kushambulia kitoto sana. Akidhani Husna ni mwanamke kama wanawake wengine. Mpaka alipopokea ngumi yenye uzito wa haja ndipo akatambua kuwa alikuwa anapambana na kiumbe hatarishi. Rambo akapiga hatua nyuma na kujipanga vyema kimapambano. Akarusha teke kali, Husna akaudaka mguu wake kisha akamzoa ngwara, akatua chini kama mzigo! Husna hakufanya juhudi za kumvamia ili wapambane akiwa amemkubatia kwa chini alimuacha anyanyuke. Rambo akasimama wima akiwa na hasira akarusha ngumi nne mfululizo. Moja tu ndo ilimchana Husna juu ya jicho. Nyingine tatu alizipangua kama awezavyo kufanya katika mazoezi yake ya ubondia. Rambo akafyatuka na teke la kuzunguka, hapa Husna akakosa umakini teke likambabatiza begani akayumba lakini hakuanguka, akajipanga na kusimama wima kisha akaanza kunesanesa kibondia akimlia taiming Rambo aweze kujiingiza hovyo kutane na balaa. Alichezesha miguu yake huku na kule binti huyu, alifurahisha kumtazama hakika!! Rambo akakunja ngumi kisha akamrukia Husna kwa kutumia goti lake, Husna akamkwepa bila kujihangaisha kumpiga pigo la mgongo japo alikuwa anaweza. Hilo lilikuwa kosa. Rambo akarusha pigo ambalo Husna alikuwa analitambua lakini hakuwa amejiandaa. Teke la ‘shukrani ya punda’..likatua moja kwa moja katika mbavu za Husna, akaugulia maumivu makali. Rambo akatambua hilo na kuanza kujinufaisha na hali ile, anamzuga Husna kam anapiga ubavu wenye maumivu, Husna akiyumba anapokea ngumi usoni, anazugwa tena anapokea teke miguuni. Husna akajaribu kujirudisha mchezoni lakini haikuwezekana. Jicho moja halikuwa na uwezo tena wa kuona damu ilikuwa imeliziba kabisa. Ni hapa ambapo likatokea kosa jingine lililoumaliza mchezo katika namna ya kutamanisha kutazma tena na tena. Rambo baada ya kuona kuwa Husna hana ujanja kabisa alijiamua kufanya shambulizi lake la mwisho, kama alivyomshambulia marehemu Mark alitaka pia kummaliza Husna. Akajirusha teke la kuzunguka ambalo lengo kuu ni kumvunja shingo Husna. Kama bahati vile Husna akaudaka mguu wa Rambo, hivyo akabaki amesimamia mguu mmoja. Bahati nyingine, jicho moja lililoweza kuona likashuhudia nyeti za Rambo, nguo yake ilikuwa imepasuka katikati ya mapaja. Ni hapa Husna alipotokwa na ile ngumi yake matata ambayo ilimpa jina la Husna ngumi jiwe wakati yupo gerezani. Ngumi iliyowatisha manyampara wa kike!! Ngumi iliyokuwa ikimpa heshima. Ngumi jiwe!! Akiwa ameushikilia mguu vilevile aliachia ngumi ile moja kwa moja kwenye korodani za Rambo. Yowe kubwa likamtoka Rambo wakati akijirusha na kutua chini, safari hii Husna hakungoja asimame! Akamrukia kwa miguu yake miwili, akatua tena katika nyeti. Husna akafanya kitendo ambacho kila mwanaume anatambua kuwa hawezi kukihimili kikitokea!! Akaanza kumsigina Rambo kwa kutumia kisigino chake katika nyeti zake, Rambo akapoteza fahamu!! “UPO CHINI YA ULINZI TULIA HIVYO HIVYO!!” wakati Husna akiamini amemaliza kazi alisikia sauti ikimuamrisha!! Akatulia tuli. Mapigo ya moyo yakiwa juu, damu nayo ikizidi kumtiririka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog